Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Lameck Okambo Airo (11 total)

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI (K.n.y MHE. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-
Serikali chini ya uongozi wa Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ilitangaza Jimbo la Rorya kuwa Wilaya mpya na sasa ina miaka saba tangu kutangazwa na hitaji kubwa la kwanza ni kutekeleza ahadi ya Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na kurudiwa tena kuahidiwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano za kujenga kwa lami barabara ya kutoka Mika - Utegi - Shirati - Kirongwe yenye urefu wa kilometa 58, kwa kuzingatia umuhimu wake kwamba ni kiungo kati ya Tanzania na Kenya kupitia Rorya, itainua pato la Halmashauri kupitia ushuru wa mpakani na tarafa tatu kati ya nne kupata urahisi kuingia nchi jirani ya Kenya kwa ukaribu zaidi kuliko kutumia barabara ya kwenda Sirari:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hii ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Wilaya ya Rorya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mika – Utegi – Shirati – Ruariport/Kirongwe, yenye urefu wa kilometa 58 ni muhimu kwa Wilaya ya Rorya kiuchumi na kijamii, kwani inaunganisha Wilaya ya Rorya na Wilaya nyingine za Mkoa wa Mara pamoja na nchi jirani ya Kenya. Kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii, Serikali ilianza kuijenga kwa awamu kwa kiwango cha lami barabara kutoka Mika – Ruariport au Kirongwe tangu mwaka wa fedha wa 2009 - 2010. Hadi sasa kipande cha barabara chenye urefu wa kilometa 7.5 kwenye barabara hii kimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami. Aidha, sehemu iliyobaki itaendelea kujengwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-
Usambazaji wa umeme kupitia REA ulikusudiwa kufikishwa kwenye vijiji na senta 54 kwenye Awamu ya II na ingewezesha upatikanaji wa umeme asilimia 25-30, kwani upatikanaji wa umeme kabla ya mpango huo ulikuwa ni asilimia 5 na kwa kuzingatia mahitaji makubwa ya umeme kwa maendeleo ya wananchi wa Rorya umeme wa asilimia 25 bado ni wa chini na hata hivyo bado mradi unasuasua:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza kasi ya usambazaji umeme katika Wilaya ya Rorya?
(b) Je, ni lini Mpango wa REA II utakamilika na kuanza REA III?
(c) Je, REA III ina vijiji na senta ngapi ndani ya Wilaya ya Rorya?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa REA Awamu ya II kwa Wilaya ya Rorya ulitarajia kufikisha huduma ya umeme katika vijiji 44. Mradi huu upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo ujenzi wa njia kubwa ya umeme msongo wa kilovoti 33 na ufungaji wa transfoma umekamilika kwa asilimia 95 na wateja zaidi ya 300 katika vijiji 16 wameunganishiwa umeme kwa sasa. Ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa muda uliopangwa, Serikali imeongeza kasi ya usimamizi wa karibu pamoja na kumwelekeza Mkandarasi Derm Electric kukamilisha kazi hizo kwa wakati.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa REA, Awamu ya II utakamilika mwishoni mwa Juni, 2016. Vijiji vitakavyobaki katika REA Awamu ya II vitaunganishiwa umeme kupitia REA Awamu ya III itakayoanza Julai, 2016.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Rorya, vijiji vipatavyo 56, sekondari nne na kanisa moja vinatarajiwa kupatiwa umeme katika Mpango wa REA Awamu ya III.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-
Wilaya ya Rorya ilianzishwa mwaka 2007, ina ukubwa wa kilometa za mraba 9,345 na idadi ya watu wapatao 400,000, lakini inakabiliwa na tatizo la uhaba wa watumishi katika Mahakama ya Mwanzo ya Kineri, Ryagoro, Obilinju na Shirati. Hadi sasa Wilaya ya Rorya inatumia Mahakama ya Wilaya ya Tarime inayosababisha kesi kuchelewa kusikilizwa kwa wakati.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Mahakama ya Wilaya kwenye Jimbo la Rorya?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, natambua kuna upungufu wa watumishi katika Mahakama za Mwanzo zilizotajwa kwenye swali hili ambapo kuna upungufu wa watumishi takribani tisa wakiwemo Mahakimu na Wasaidizi katika Mahakama hizo. Katika mwaka huu wa fedha 2016/2017, Mahakama imejipanga kupeleka watumishi hao katika mahakama hizo hususan Mahakama ya Mwanzo ya Nyaburongo ambayo inahitaji Hakimu. Mahakama ya Mwanzo ya Kinesi ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja kwa sasa haitumiki kutokana na uchakavu wa miundombinu yake ambayo itafanyiwa kazi katika mipango ya ukarabati ya baadae.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Rorya umewekwa katika mpango mkubwa wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya mahakama kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, katika mwaka wa fedha huu, Mahakama imepanga kujenga Mahakama ya Wilaya Bunda na Mahakama Kuu - Mara.
MHE. KISWAGA B. DESTERY (K.n.y. MHE. LAMECK O.
AIRO) aliuliza:-
Wananchi wa Kata ya Koryo kwa kushirikiana na Mbunge wao na wananchi wa Rorya wanaoishi Mwanza, Arusha na Dar es Salaam wamejenga wodi ya akina mama na watoto pamoja na kununua jokofu lakini mapungufu yaliyopo sasa ni Jengo la upasuaji.
Je, Serikali sasa haioni ipo haja ya kusaidia jengo hilo pamoja na vifaa vyake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA
SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 mradi uliidhinishiwa shilingi milioni 30 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo la upasuaji. Fedha zote zimepokelewa na tayari Halmashauri imeanza taratibu za kumpata mkandarasi. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 25 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa jengo hilo.
KITETO Z. KOSHUMA (K.n.y. MHE. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-
Wavuvi wa Wilaya ya Rorya wanaovua katika Ziwa Victoria wamekuwa wakitekwa, kunyang’anywa nyavu zao pamoja na injini za boti. Aidha, majambazi wanaofanya vitendo hivyo hutumia silaha nzito na inasemekana ni wanajeshi kutoka Uganda.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongea na Serikali ya Uganda ili kukomesha uvamizi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwepo na matukio ya uporaji wa nyavu na injini za wavuvi katika Ziwa Victoria. Uporaji huu unafanywa na wahalifu ambao bado Jeshi la Polisi halina ushahidi kuwa wanatoka ndani au nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na matukio ya uhalifu ikiwemo uporaji wa nyavu na injini za wavuvi katika Ziwa Victoria, Serikali kupitia Jeshi la Polisi ina mikakati ya kununua boti zenye uwezo na zenye mwendo kasi mkubwa. Boti hizi zitasaidia askari polisi kufanya doria za mara kwa mara na kufika kwenye matukio haraka. Aidha, Serikali inashirikiana na nchi jirani katika udhibiti wa pamoja kwa matukio ya uhalifu wa majini.
MHE. BONIPHACE M. GETERE (K.n.y. MHE. LAMECK O. AIRO) Aliuliza:-
Wakati Rais akiwa kwenye ziara Wilayani Rorya aliahidi ujenzi wa Daraja la Mto Mori linalounganisha Tarafa ya Suba Luoimbo na Nyancha, lakini kwenye bajeti ya mwaka 2016/ 2017 ujenzi wa daraja hilo haukuwepo.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga daraja hilo ili kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mto Mori unapita katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na Rorya hali inayosababisha kuwepo kwa uhitaji wa madaraja mawili ili kurahisisha usafiri katika maeneo hayo mawili. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kupitia Mfuko wa Barabara imetengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Mto Mori kwa upande wa Tarime. Taratibu za manunuzi zinaendelea, ili kumpata mkandarasi wa kujenga daraja hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Rorya usanifu wa awali umefanyika ili kujua gharama za ujenzi wa daraja hilo ambazo zinakadiriwa kuwa shilingi milioni 300. Halmashauri ya Wilaya ya Rorya imepanga kuweka kipaumbele na kutenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 ili kukamilisha ujenzi huo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE (K.n.y MHE. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-
Katika mpaka wa Tanzania na Kenya uliopo Wilayani Rorya, kuna Ofisi za Uhamiaji na Customs za nchi yetu zipo kwenye makontena.
Je, ni lini Serikali itajenga majengo ya kisasa kwa ajili ya ofisi katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha na Mpango inatambua uwepo wa mahitaji ya ofisi ya kisasa katika Kituo cha Forodha kilichopo mpakani mwa Tanzania na Kenya, Wilayani Rorya Mkoa wa Mara. Kwa sasa Mamlaka ya Mapato Tanzania ipo katika hatua za kupata umiliki wa eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 22,933.5 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya ofisi. Mara hatua za umiliki wa eneo zitakapokamilika, Wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania itaanza taratibu za ujenzi wa ofisi na tuna uhakika tunaweza kuwa pamoja na ndugu zetu wa uhamiaji mara ofisi hizi zitakapokamilika na wao wakiwa wanashughulika na ujenzi wa ofisi zao.
MHE. BONIPHACE M. GETERE (K.n.y. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Rorya ilianzishwa mwaka 2007 na ina ukubwa wa kilometa za mraba 9,345 na idadi ya watu wapatao 400,000, lakini inakabiliwa na tatizo la uhaba wa watumishi katika Mahakama za Mwanzo za Kineri, Ryagoro, Obilinju na Shirati; hadi sasa Wilaya ya Rorya inatumia Mahakama ya Wilaya ya Tarime hali inayosababisha kesi kuchelewa kusikilizwa kwa wakati:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Mahakama ya Wilaya kwenye Jimbo la Rorya?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa Mahakama wa kujenga na kukarabati majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali, Mahakama ya Wilaya ya Rorya imepangiwa kujengwa katika Mwaka wa Fedha 2019/2020.
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO (K.n.y. MHE. LAMECK AIRO) aliuliza:-
Wilaya ya Rorya iliyoanzishwa mwaka 2007 sasa ina wakazi wapatao 400,000 na ina kata 26 na vijiji takriban 87 na ina vituo vya afya 4 lakini haina Hospitali ya Wilaya na wananchi wake hulazimika kutembea umbali wa takribani kilomita 30 kufuata huduma za afya Tarime na akina mama ambao ni asilimia 52 wanahitaji huduma ya hospitali kamili:-
Je, ni lini Wilaya ya Rorya itajengewa Hospitali ya Wilaya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 105 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya 67 hapa nchini ikiwemo Hospitali ya Rorya ambayo tumeitengea shilingi bilioni 1.5.
MHE. ALHAJ ABDALLAH M. BULEMBO (K.n.y. MHE. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-

Wakati wa ziara ya Kampeni za Uchaguzi Mheshimiwa Rais aliahidi kujenga daraja la kuunganisha Tarafa tatu za Luoimbo, Suba na Nyancha na tayari Halmashauri imeshapeleka makadirio Wizarani:-

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, daraja linalounganisha Tarafa za Luoimbo, Suba na Nyancha ni miongoni mwa ahadi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizozitoa maeneo mbalimbali nchini wakati wa Kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umefanya tathmini ya gharama za ujenzi huo na wamepata kiasi cha shilingi bilioni 1.15. Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hilo. Azma ya Serikali ni kuhakikisha ahadi hiyo pamoja na ahadi nyingine zilizotolewa na viongozi wakuu wa kitaifa zinatekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitao ijayo. Ahsante.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. LAMECK O. AIRO) aliuliza:-

Mheshimiwa Rais akiwa kwenye ziara ya kujinadi wakati wa kampeni Wilayani Rorya aliwaahidi wananchi wa Rorya kujenga barabara ya lami kutoka Mika-Utegi hadi Shirati;lakini hadi sasa ahadi hiyo haijatekelezwa:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lameck Okambo Airo, Mbunge wa Rorya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mika – Utegi – Shirati hadi Ruari Port ni barabara ya mkoa inayosimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara. Barabara hii ina urefu wa kilometa 48.73. Kati ya hizo, kilometa 40.13 zimejengwa kwa kiwango cha changarawe na kilometa 8.6 zimejengwa kwa awamu kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza maandalizi ya kuijenga barabara hii (km 48.73) kwa kiwango cha lami kwa kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kazi hiyo inafanywa na Makampuni ya Cordial Solution Ltd. na Atkins Tanzania Ltd yote ya Tanzania. Wakati makampuni hayo yakiendelea na kazi, yaliongezewa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya usalama na ulinzi kutoka Shirati – Masonga hadi mpakani mwa Tanzania na Kenya (km 16.4). Gharama ya kazi zote ni shilingi milioni 679.621 na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utaanza baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika na fedha za ujenzi kupatikana. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2019/2020, barabara hii ya Mika – Utegi – Shirati imetengewa shilingi milioni 630.148 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali.