Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. John John Mnyika (12 total)

MHE. JAMES F. MBATIA (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:-
Pamoja na kuwa karibu na Makao Makuu ya TANESCO, baadhi ya maeneo ya Jimbo la Kibamba hayana umeme na yale yenye umeme kiwango chake hupungua na kuongezeka (low voltage and fluctuation):-
(a) Je, Serikali inaweza kuwasilisha orodha ya maeneo yasiyo na umeme katika Kata za Saranga, Mbezi, Msigani, Goba , Kwembe na Kibamba, na lini maeneo hayo yatapatiwa umeme; (TANESCO)?
(b) Je, Serikali ina inachukua hatua gani kuondoa tatizo la kupungua na kuongezeka kwa umeme katika Kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John John Mnyika, Mbunge wa Kibamba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, orodha ya maeneo yasiyo na umeme katika Kata ya Saranga, Mbezi, Msigani, Goba, Kwembe pamoja na Kibamba ni kama yafuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kata ya Saranga ni Saranga Ukombozi na Nzasa na yanatarajiwa kupatiwa umeme mwezi Mei mwaka huu; Kata ya Msigani na Marambamawili inatarajiwa pia kupata huduma za umeme mwezi Aprili, mwaka huu; Kata ya Goba na Kata ya Goba Mpakani inatarajiwa pia kupata umeme mwezi Septemba, mwaka huu; Kata ya Kwemba ni King‟azi „B‟ itakayopatiwa umeme mwezi Septemba, mwaka huu; na Kisokwa ambalo limeombewa fedha kwenye bajeti ya TANESCO mwaka 2016/2017.
Pia Kata ya Mbezi ni Kibesa inayoombewa fedha katika bajeti ya TANESCO ya mwaka 2016/2017; na Msumi ambalo inapatiwa umeme mwezi Mei, mwaka huu; na katika Kata ya Kibamba maeneo yote yamefikiwa na umeme wa huduma iliyopita.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na tatizo la kupungua na kuongezeka kwa umeme katika Kata hizo, ukarabati wa miundombinu unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia mwezi Februari, 2016 na pia unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2016.
Kazi zitakazohusishwa na ukarabari huo ni pamoja na kuongeza njia ya umeme toka njia moja hadi njia tatu, yaani (upgrading), lakini kufunga nyaya zenye uwezo mkubwa wa kuondoa tatizo la kupungua kwa umeme chini ya utaratibu unaoitwa re-conductoring. Aidha, kutakuwa na ufungaji wa transfoma kubwa na kuondoa ndogo ili kukidhi mahitaji ya umeme katika maeneo husika.
MHE. ESTER A. BULAYA (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:-
Mabaraza ya makundi maalum ya kijamii kama wanawake, vijana, wazee, watoto na walemavu ni vyombo muhimu katika kuwaunganisha kimaendeleo:-
(a) Je, ni lini Serikali itawasilisha taarifa ya tathmini ya utendaji wa Mabaraza ya Watoto na Walemavu?
(b) Je, Serikali imefikia hatua gani katika kuwezesha kufanya kazi kwa Baraza la Vijana la Taifa baada ya sheria yake kupitishwa?
(c) Je, ni lini Serikali itawezesha kuundwa kwa Baraza la Wanawake la Taifa ili kuwaunganisha katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali namba 87 la Mheshimiwa John John Mnyika, Mbunge wa Kibamba, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu imeanza kufanya tathmini ya utendaji wa Mabaraza ya Watoto ngazi za Kata, Wilaya, Mkoa na Taifa katika mikoa sita ya Tanzania bara. Lengo kuu la tathmini hii ni kubaini hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa malengo ya Mabaraza kama ilivyokusudiwa katika uanzishwaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi hili litakamilika mwezi Mei, 2016. Mara baada ya kukamilika kwa zoezi hili, Wizara itaandaa ripoti ambayo itaonesha matokeo ya tathmini ya utendaji wa Mabaraza hayo katika ngazi zote na kuiwasilisha kwa wadau kwa mujibu wa taratibu za uendeshaji wa Baraza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Taifa la Ushauri la Watu Wenye Ulemavu lilizinduliwa tarehe 1 Novemba, 2014. Kutokana na ufinyu wa bajeti, Baraza hili lilifanya kikao chake cha kwanza tarehe 14 na 15 Januari, 2016.
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, yenye dhamana ya kushughulikia watu wenye ulemavu itafanya tathmini na kutoa taarifa baada ya kumalizika kipindi cha mwaka mmoja baada ya Baraza hili kuanza kufanya kazi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lilipitisha rasmi Sheria Na. 12 ya uundwaji wa Baraza la Vijana la Taifa yaani The National Youth Council, 2015 na kusainiwa na Mheshimiwa Rais tarehe 22 Mei, 2015. Hivi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu ipo katika hatua ya kutunga kanuni za utekelezaji wa sheria hii kwa mujibu wa kifungu Na. 27 cha Sheria, ili kuwezesha uundwaji wa Baraza kuanzia ngazi ya Kata hadi Taifa. Aidha, Wizara inatarajia kanuni hizi kukamilika mwaka huu wa 2016 ili Baraza lianze kufanya kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo na vijana.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwepo kwa jitihada za wanaharakati, wanazuoni na watafiti katika kusaidia kuundwa kwa chombo cha kuwaunganisha wanawake kwa lengo la kuimarisha juhudi zao katika mapambano ya kulinda haki zao na kuleta usawa wa kijinsia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa kutambua jitihada hizo Serikali imepanga kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kujadili na kutoa maoni kuhusu haja ya kuwepo kwa Baraza la Wanawake Tanzania ambalo litasaidia kulinda maslahi na haki zao kwa mujibu wa sheria na kuleta usawa wa kijinsia.
MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:-
Wananchi wa Mloganzila waliopisha ujenzi wa MUHAS hawakulipwa fidia ya ardhi au angalau “mkono wa kwaheri” na wapo wenye madai ya „kupunjwa‟ fidia ya maendelezo:-
(a) Je, ni lini wananchi hao watapewa malipo yao kama Serikali ilivyoahidi?
(b) Je, ni kwa namna gani Serikali imeshughulikia madai ya mapunjo ya fidia ya maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Mnyika, Mbunge wa Kibamba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya kuwalipa fidia ya hisani au mkono wa heri iliyotolewa na Serikali mnamo tarehe 20 Mei 2015 italipwa baada ya kupata fedha. Malipo haya hayajafanyika kutokana na ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia ililipa kiasi cha Sh. 8,067,904,700 kwa ajili ya fidia ya maendelezo katika ardhi kwa wananchi 1,919 katika kipindi cha mwaka 2008 mpaka 2010. Aidha, mwaka 2011 Serikali ilitenga kiasi cha sh. 1,610,374,700 kwa ajili ya fidia ya wananchi 619 waliosalia. Fedha hizi zililipwa kama fidia ya maendelezo kwa wananchi waliokuwa wamewekeza ndani ya shamba ambalo lilikuwa mali ya Serikali. Serikali haidaiwi mapunjo kwa kuwa fidia ilishalipwa kwa mujibu wa Sheria.
MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:-
Serikali inapaswa kuharakisha upimaji wa ardhi na utoaji wa hati za viwanja katika Jimbo la Kibamba ili kuepusha makazi holela.
(a) Je, ni maeneo gani ambayo hayajapimwa na lini yatapimwa?
(b) Je, kuna mpango gani wa kupunguza gharama na muda wa upimaji na utoaji wa hati ili kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa huduma tajwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Mnyika, Mbunge wa Kibamba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Kibamba, maeneo ambayo bado hayajapimwa yapo katika kata za Manzese, Mabibo na baadhi ya sehemu katika Kata za Ubungo, Mburahati, Kimara, Saranga, Goba, Mbezi, Kibamba, Kwembe na Makuburi. Tayari upimaji unaendelea katika Kata ya Kimara ambapo viwanja 3,196 vimepimwa. Taratibu zinakamilishwa ili kuwapimia wananchi 186 waliolipia gharama katika kata ya Kibamba ambao unahusisha upimaji wa maeneo ya huduma za umma 123 katika Manispaa ya Ubungo. Aidha, upimaji umepangwa kufanyika katika Kata za Mbezi, Msigani, Goba na Kwembe kupitia kampuni binafsi zilizoidhinishwa na Serikali ili kuharakisha zoezi hilo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, viwango vya gharama
za upimaji vinavyotumika sasa vipo kwa mujibu wa sheria ambavyo vilipangwa kwa kushirikisha wadau mbalimbali na kwa kuzingatia matumizi ya zana za kisasa za upimaji ikiwemo mifumo ya kijiografia na kompyuta (Geographical Information System). Matumizi ya mifumo hiyo imerahisisha zaidi upimaji ambapo ramani za hati (deed plan) katika Manispaa ya Ubungo zimeongezeka na kufikia hati 1,000 kwa mwezi.
MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:-
Eneo la hifadhi ya barabara ya Morogoro katika Jimbo la Kibamba ni pana kuliko barabara kuu nyingine nchini na inaingia katika makazi ya asili ya wananchi.
(a) Je, ni lini Serikali itawalipa wananchi fidia kwa ardhi ya asili ya tangu kabla ya uhuru ambao walihamia wakati wa vijiji vya ujamaa?
(b) Je, ni lini Serikali itawasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria husika ili eneo la hifadhi ya barabara iwiane na barabara kuu nyingine nchini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa John John Mnyika, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Barabara ya mwaka 1932 (The Highway Ordinance Cap.167) kifungu namba 52 eneo la hifadhi ya barabara ya Morogoro kuanzia maili 10.02 yaani kilometa 16 kutoka Posta ya Zamani mpaka maili 23.12 yaani kilometa 37 ni futi 400 ambazo ni sawa na takribani mita 120 kila upande kutoka katikati ya barabara. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia TANROADS imeweka nguzo za kuonesha mipaka ya eneo la hifadhi ya barabara katika eneo tajwa na maeneo mengine nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya barabara ya Morogorio kati ya kilometa 16 na kilometa 37 iko ndani ya Jimbo la Kibamba ambapo hifadhi ya barabara ni mita 120 kila upande kutoka katikati ya barabara. Hivyo Serikali haitalipa fidia kwa mwananchi yoyote wa Jimbo la Kibamba aliyejenga au aliyefanya maendelezo yoyote ndani ya eneo la hifadhi ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haina mpango wa kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ili kufanya eneo la hifadhi ya barabara Morogoro liwiane na barabara kuu nyingine nchini kwa kuwa eneo la hifadhi ya barabara ya Morogoro lililotengwa linahitajika kwa ajili ya upanuzi wa barabara ili kuwaiana na mahitaji ya sasa na ya miaka ijayo.
MHE. JAMES F. MBATIA (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:-
Jimbo la Kibamba linapaswa kuhudumiwa kwa sehemu kubwa na maji ya kutoka mtambo wa Ruvu Juu:-
(a) Je, ni maeneo gani mpaka sasa yana shida kubwa ya maji na lini maeneo hayo yatapata huduma kamili ya maji?
(b) Je, ni kwa nini miradi mikubwa ya maji imechelewa kukamilika kinyume na ratiba iliyotolewa na Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John John Mnyika, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yanayohudumiwa na mtambo wa Ruvu Juu ni pamoja na Mlandizi, Visiga, Misugusugu, Kongowe, Picha ya Ndege, Tumbi, Pangani, Kibaha, Maili Moja, Kiluvya, Kibamba, Kwa Yusufu, Mbezi, Makabe, Msakuzi, Malamba Mawili, Msigani, Matosa, Kimara, Kibangu, Makuburi, Tabata, Segerea, Kinyerezi na Kipawa. Maeneo yote haya yataanza kupata maji baada ya kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa mfumo wa kusambaza maji ambao unaendelea kutekelezwa na kampuni ya Jain Irrigation Systems Limited. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingine mikubwa inachelewa kukamilika kutokana na sababu mbalimbali ambazo ni pamoja na kuchelewa kwa upatikanaji wa fedha za ujenzi, ugumu wa upatikanaji wa maeneo ya ujenzi wa miradi, changamoto za kiufundi na kuchelewa kuwasili kwa mitambo na vifaa kutoka nje ya nchi kwa miradi yenye kuhitaji mitambo hiyo. Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto hizo. Kwa sasa utekelezaji wa miradi mingi mikubwa unaenda vizuri.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:-
Ujenzi wa barabara za mzunguko/mchepuko kwa kiwango cha lami ni muhimu katika kupunguza msongamano kwenye barabara kuu ya Morogoro.
(a) Je, ni lini barabara ya Tangibovu – Kibaoni – Goba – Mbezi – Malamba Mawili – Kinyerezi utakamilika?
(b) Je, ni lini ujenzi kwa kiwango cha lami kwa barabara nyingine za mzunguko/mchepuko katika Jimbo la Kibamba utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John John Mnyika, Mbunge wa Kibamba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam na kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mnamo mwaka 2010 ilianza kutekeleza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara za pete (ring roads) na zile za mchepuo.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zinazojumuishwa kwenye mpango huo ambazo ziko katika Jimbo la Kibamba ni barabara za Bunju ‘B’ – Mipiji Magohe – Victoria – Kifuru hadi Pugu Kilitex yenye urefu wa kilometa 33.7 na barabara ya mchepuo ya Tangibovu – Goba – Mbezi Mwisho – Msigani
– Malambamawili – Kifuru – Kinyerezi hadi Banana, yenye urefu wa kilometa 26.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara ya mchepuo kuanzia Tangibovu – Goba – Mbezi Mwisho – Msigani – Malambamawili – Kifuru – Kinyerezi umetekelezwa kama ifuatavyo:-
(i) Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara yenye urefu wa kilometa 16 kuanzia Tangibovu – Goba – Mbezi Mwisho umekamilika mwaka 2016;
(ii) Ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara yenye urefu wa kilometa nane kuanzia Msigani – Kifuru – Kinyerezi umekamilika mwaka 2017; na
(iii) Ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara yenye urefu wa kilometa mbili kutoka Mbezi Mwisho hadi Msigani pamoja na barabara ya kuingia na kutoka kwenye Kituo cha Mabasi Mbezi unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara ya Bunju ‘B’ – Mpiji Magohe – Victoria – Kifuru hadi Pugu Kilitex yenye urefu wa kilometa 33.7 ambayo inapita kwenye Jimbo la Kibamba utaanza mara baada ya usanifu kukamilika na fedha za ujenzi kupatikana.
MHE. JULIUS K. LAIZER (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:-
Barabara za pete (ring roads) na barabara za mchepuo (feeder roads) ni muhimu katika kupunguza msongamano na matatizo ya miundombinu kwa wananchi:-
(a) Je, Serikali itakamilisha lini ujenzi wa barabara hizo zilizoanza kujengwa katika Jimbo la Kibamba?
(b) Je, Serikali itaanza lini ujenzi wa barabara ambazo zimetajwa katika mipango ya Serikali lakini hazijaanza kujengwa mpaka sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John John Mnyika, Mbunge wa Kibamba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mkakati wa kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam, Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mnamo mwaka 2010 ilianza kutekeleza ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara za pete (ring roads) na barabara za mchepuo (bypass).
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zilizoingizwa kwenye mpango huo ambazo ziko kwenye Jimbo la Kibamba na hatua za utekelezaji wake uko katika hatua mbalimbali ni kama ifuatavyo:-
Barabara ya Bunju B – Mpiji Magohe – Victoria – Kifuru hadi Pugu yenye urefu wa kilometa 33.7 (outer ring road); barabara ya Mbezi –Msigani –Malambamawili – Kifuru – Kinyerezi – Banana (sehemu ya Kinyerezi – Mbezi – Malambamawili – Kifuru) yenye urefu wa kilometa 10; na barabara ya Tegeta – Kibaoni – Wazo Hill -Goba – Mbezi/ Morogoro Road yenye urefu wa kilometa 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambazo ujenzi kwa kiwango cha lami umekamilika ni sehemu ya barabara ya Mbezi – Msigani – Malambamawili – Kifuru – Kinyerezi – Banana kuanzia Msigani – Kifuru yenye urefu wa kilometa nane na barabara ya Tegeta Kibaoni – Wazo Hill – Goba Mbezi/ Morogoro road sehemu ya Goba Mbezi/Morogoro Road yenye urefu wa kilometa saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ambazo ujenzi wa kiwango cha lami unaendelea ni barabara inayoanzia Msigani mpaka Mbezi yenye urefu wa kilometa mbili zikiwemo barabara za kutoka na kuingia kwenye kituo cha mabasi ya Mbezi na barabara nyingine ni Goba – Madale yenye urefu wa kilometa tano. Barabara ambayo usanifu wake bado unaendelea ni barabara ya pete (outer ring road) ya Bunju B – Mpiji Magohe – Victoria – Kifuru hadi Pugu yenye urefu wa kilometa 33.7.
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:-

Ili kuharakisha upimaji na urasimishaji wa ardhi na makazi, Serikali iliruhusu kampuni binafsi kufanya kazi hiyo katika maeneo mbalimbali.

(a) Je, ni lini kampuni zinazofanya kazi hiyo zitatoa hati za ardhi au leseni za makazi kwa wananchi?

(b) Je, ni vikwazo gani vinakabili zoezi hilo na Serikali inachukua hatua gani kuviondoa ili kuzisaidia kampuni hizo kumaliza kazi hiyo kwa haraka?

(c) Je, ni lini Serikali itakamilisha mpango kabambe (masterplan) mpya ya Jiji la Dar es Salaam ili uwe dira katika upangaji, upimaji na urasimishaji?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Mnyika, Mbunge wa Kibamba, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, umilikishwaji wa ardhi hufanywa kwa mujibu wa Sheria Na.4 ya mwaka 1999 ambayo inampa Kamishna wa Ardhi mamlaka ya kutoa hati au leseni za makazi. Hivyo, lengo la kusajili makampuni ya upangaji na upimaji ardhi ni kuongeza kasi ya upangaji na kupima ardhi nchini lakini hati miliki za ardhi hiyo hutolewa na Kamishna baada ya mwananchi kulipa gharama za umilikishaji zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kimingi kwa sasa hatuna kikwazo au vikwazo vinavyokabili zoezi la urasimishaji ardhi nchini zaidi ya changamoto ya mwitikio mdogo wa wananchi katika maeneo mbalimbali. Awali zoezi hili lilikuwa linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa ramani za msingi (base maps), uhaba wa vifaa vya kisasa vya upimaji, matumizi ya teknolojia duni, baadhi ya wananchi kutokuwa tayari kulipia gharama ya ardhi kwa ajili ya miundombinu na uelewa mdogo kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuondoa changamoto hizo, Serikali iliweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa picha za anga katika Jiji la Dar es Salaam na KIbaha na kuandaa ramani za msingi (base maps) mpya za mwaka 2016, ununuzi wa vifaa vya kisasa vya upimaji, kuongeza mtandao wa alama za msingi za upimaji yaani control points, usimikaji wa mfumo wa ILMIS kwa ajili ya kurahisisha umilikishaji na uhamasishaji wa wananchi kuhusu zoezi la urasimishaji.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, rasimu ya mwisho ya mpango kabambe ya Jiji la Dar es Salaam imekamilika na nakala za kielektroniki za rasimu hiyo zimesambazwa kwa wadau kwa ajili ya kupitia na kutoa maoni yao. Aidha, rasimu ya mpango huo imewekwa kwenye tovuti ya Wizara www.lands.go.tz ili kwezesha wadau kutoa maoni yao. Kwa sasa Mtaalam Mwelekezi anafanya mawasilisho ya rasimu hiyo katika mikutano ya hadhara (public hearing) katika Mamlaka zote za Upangaji za Jiji la Dar es Salaam ili kuapata maoni ya wananchi.
MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:-

Tarehe 4 Februari Serikali ikijibu hoja binafsi kuhusu upatikanaji wa maji iliahidi kuwa ifikapo mwaka 2016 matatizo ya maji yangekuwa yamemalizika katika Jiji la Dar es Salaam:-

(a) Je, ni kwa nini ahadi hiyo haijatekelezwa kwa wakati?

(b) Je, ni Mitaa ipi katika Jimbo la Kibamba maji hayatoki na ni lini DAWASA itahakikisha maji yanatoka katika maeneo hayo?

(c) Je, Serikali iko tayari kuwasilisha katika kila Mkutano wa Bunge Taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini kama ilivyokubali katika Bunge la Kumi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Myika, Mbunge wa Jimbo la Kibamba, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam yanapata maji kama Serikali ilivyoahidi kupitia Bunge lako Tukufu baada ya kukamilisha miradi mikubwa ya maji ambayo ilikamilika mwaka 2016. Serikali inatambua kuna baadhi ya maeneo ya jiji hilo hayajapata maji kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la watu na ukuaji wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na upatikanaji wa maeneo ya kupitisha miundombinu ya miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 80 ya wakazi wa Jimbo la Kibamba wanapata huduma ya maji. Maeneo ambayo hayapati maji kwa sasa ni maeneo ambayo yapo kwenye miinuko mikubwa. Ili kuhakikisha wananchi wote wa Jimbo la Kibamba wanapata maji, hasa wanaoishi katika miinuko mikubwa, Serikali inaendelea na ujenzi wa matenki katika eneo la Msakuzi Kusini na Maramba Mawili Juu kwa lengo la kuhakikisha wananchi wote wa Jimbo hilo wanapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi Kiti kilishalitolea mwongozo suala hili katika Mkutano wa Pili, Kikao cha Tisa kilichofanyika tarehe 5 Februari, 2016. Katika mwongozo wa Kiti ilielekezwa kama ifuatavyo; naomba kunukuu; “Bunge la Kumi na Moja litakuwa linaweka utaratibu wake wa namna bora kufikisha maelezo kwa Waheshimiwa Wabunge kwa nyakati tofauti.”

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. JOHN J. MNYIKA aliuliza:-

Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliwahi kupewa jukumu la nyongeza la kusimamia kura ya maoni ya mabadiliko ya Katiba kwa Sheria iliyotungwa na Bunge kwa kutumia Ibara ya 74(6)(e) ya Katiba ya Nchi:-

(a) Je, ni kwa nini Ibara ya 74(6)(e) isitumike ili Uchaguzi wa Vitongoji, Vijiji na Mitaa wa Mwaka 2019 usimamiwe na Tume ya Taifa ya Uchaguzi badala ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI)?

(b) Je, ni kwa nini Serikali haijatekeleza makubaliano na Vyama ya mwaka 2014 ya kuwezesha Uchaguzi wa Vitongoji na Mitaa kutumia Daftari la Wapiga Kura lililoboreshwa badala ya Orodha ya Wakazi?

(c) Je, ni hatua gani Serikali imechukua kuhakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019 unakuwa huru na wa haki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa John John Mnyika Mbunge wa Kibamba lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi yaliyoainishwa katika Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kusimamia uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na kutekeleza majukumu mengine yoyote kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge. Jukumu la kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa si miongoni mwa majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa Katiba isipokuwa ni jukumu la Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288. Hivyo, masharti ya Ibara ya 74(6)(e) ya Katiba hutumika tu pale ambapo kuna Sheria iliyotungwa na Bunge inayoipatia Tume ya Taifa ya Uchaguzi majukumu mengine.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kueleza, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi haina Mamlaka ya kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kutokana na msimamo huo wa Kikatiba uchaguzi wa Serikali za Mitaa hauwezi kutumia daftari la kudumu la wapiga kura kwa kuwa daftari hilo lipo chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha 12 cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343. Kwa msingi huo, makubaliano yoyote yaliyowahi kufanyika kuhusu matumizi ya daftari la kudumu la wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa yanapaswa kuzingatia masharti ya Kikatiba na sheria za nchi.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unakuwa huru na haki Serikali imeandaa Kanuni na Miongozo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019 ambazo zimezingatia maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali wa uchaguzi vikiwemo vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu Tanzania pamoja na asasi za kiraia.
MHE. SAED A. KUBENEA (K.n.y. MHE. JOHN J. MNYIKA) aliuliza:-

Bado tatizo la kupungua na kukatika kwa umeme bado linaendelea na baadhi ya maeneo hayajafikishiwa umeme mpaka sasa.

(a) Je, ni kwanini matatizo ya kukatika au kupungua kwa umeme katika Jimbo la Kibamba halijapatiwa ufumbuzi kinyume na Serikali ilivyoahidi?

(b) Je, ni maeneo gani katika Jimbo la Kibamba mpaka sasa TANESCO haijafikisha umeme na lini yatafikiwa?

(c) Je, kuna mkakati gani wa kupunguza gharama za wananchi kuunganisha umeme au kuwarejeshea wanapovuta wenyewe umbali mrefu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa John John Mnyika, Mbunge wa Kibamba lenye sehemu (a) (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la kukatika kwa umeme katika Jimbo la Kibamba linatokana na zoezi la kuhamisha miundombinu ya umeme ili kupisha upanuzi wa barabara ya Dar es Salaam - Morogoro. Kwa sasa tatizo hilo limepungua, baada ya zoezi hilo kukamilika kwa asilimia 97 na itakamilika mapema mwezi Juni, 2019. Hali ya upatikanji wa umeme katika Jimbo la Kibamba imeimalika kutokana na kukamilika kwa kazi ya kubadilisha nguzo mbovu na kukata miti kwenye mkuza wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 kutoka Ubungo hadi Kibamba. Vilevile kupitia TANESCO imetenga shilingi bilioni 5 kwenye bajeti ya 2018/19 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mloganzila, Luguruni, chenye uwezo wa MVA 90, kituo hiki kitasambza umeme katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Kibamba, ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Mloganzila na hivyo kutatua tatizo la ongezeko la mahitaji ya umeme katika Jimbo la Kibamba.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Kibamba kuna baadhi ya maeneo ya ambayo hayajapatiwa huduma ya umeme ikiwa ni pamoja na maeneo ya Kibesa, Kisopwa, Kipera, King’azi, Msumi na baadhi ya maeneo ya Mpigi na Kwembe. Katika bajeti ya mwaka TANESCO ilienga shilingi bilioni 3.78 kwa ajili ya kupeleka umeme katika maeneo ya Kwembe kwa Tendwa, Kwembe Kipera, Mbezi Luis, Kibwegere, Msakuzi, Mpigi CCM ya Zamani, Kibamba Delini, Mpiji, Kwembe, Msumi na King’azi. Kazi ya kupeleka umeme katika maeneo haya inaendelea na itakamilika mwezi Septemba, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yaliyosalia ya Kibesa, Kisopwa na Kipera, yatapatiwa umeme kupitia bajeti ya 2019/20.

(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Mwezi Desemba, 2013, Serikali kupitia EWURA ilipunguza gharama za kuunganisha umeme kutoka shilingi 385,682, hadi 272,000 kwa wateja wa njia moja wa mjini, aliye ndani ya mita 30 ikiwa ni punguzo la asilimia 30. Kanuni za Sheria ya Umeme Kifungu 131 ya mwaka 2008 zilizotangazwa katika gazeti la Serikali Na. 63 la Tarehe 4 Februari, 2011 zinaelekeza TANESCO na mteja kukubaliana namna ya kurejeshwa kwa gharama zilizotumika kujenga miundombinu ya umeme kama TANESCO haitakuwa na uwezo wa kibajeti kwa wakati huo kumfikishia mteja huduma ya umeme.