Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi (16 total)

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Pale Musoma Mjini tumekuwa na tatizo la maji kwa muda mrefu na bahati nzuri tumepata mradi ambao tulitegemea toka mwaka jana ungekuwa umekamilika na watu wameanza kupata maji. Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha kwamba mradi huo umekamilika kama ilivyokuwa ahadi yake ya toka mwaka jana?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeanza kupata fedha, kwa hiyo, wakati wowote ule tutatuma fedha na kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha tutakuwa tumekamilisha mradi huo.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, namshukuru Naibu Waziri na mimi nakubaliana naye alivyosema kwamba barabara ile ina umuhimu mkubwa hasa ukilinganisha kwamba kuna uzalishaji wa samaki katika eneo hilo, lakini vilevile ni eneo ambalo linapita nchi yetu ya jirani.
Sasa ukiangalia toka 2009 hadi leo, zaidi ya miaka mitano ni kilometa 7.5 peke yake ndiyo barabara iliyowekewa lami, napenda kufahamu Serikali itakuwa tayari kwa mwaka huu kutenga fedha kwa ajili ya hicho kipande cha barabara ili kiweze kujengwa zaidi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba ikumbukwe kwamba mbali na ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali ambayo yako katika mpango lakini kutokana na umuhimu Mheshimiwa Rais mwaka jana tuliweza kumpa maombi maalum hasa kwa pale Musoma Mjini, tulimpa ombi la barabara ya kutoka Bweri - Makoko ambapo kipande kile zipo sekondari zisizopungua 14, je, Serikali sasa itakuwa tayari kutimiza ahadi hiyo kuanzia mwaka huu wa fedha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yake yote mawili yanaongelea kutenga fedha kwa mwaka huu wa 2016/2017 kwa ajili ya kuendelea kujenga ile barabara ya Mika – Utegi – Shirati - Kirongwe pamoja na hii barabara aliyoiongelea ya Bweri - Makoko. Naomba kumuahidi kwamba hivi sasa tunavyoongea, wataalam wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, sekta ya ujenzi, wapo katika hatua ya mwisho ya kuangalia katika haka kasungura kadogo tulikokapata ni wapi tutenge kiasi gani. Kwa hiyo, naomba asubiri Bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano itakapokuja itatoa majibu sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pengine moja ningependa kusisitiza, mahitaji ya ujenzi wa barabara ni makumbwa sana sehemu mbalimbali za nchi na priority (kipaumbele) kwa mwaka ujao wa fedha ni kukamilisha miradi ya muda mrefu ili kuondokana na gharama za makandarasi wanazotudai kutokana na kuchelewa kukamilisha miradi. Hivyo, tutahakikisha kwamba barabara zile ambazo zimeanza muda mrefu lazima kwanza zikamilike kabla hatujaingia katika eneo jipya.
MHE.VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, na ameendelea kusema hapa kwamba hii michango tunahitaji kuendelea kuwahamasisha wananchi ili waweze kuchangia. Lakini ukiangalia kwa mapungufu tuliyokuwanayo kwa maana ya madawati, vyumba vya madarasa pamoja na maabara; ni mapungufu makubwa sana na kwa sababu wananchi wengi wanaamini kwamba michango ni hiari kama alivyosema Naibu Waziri, hatuoni kama tutashindwa kutekeleza azma yetu ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanaweza kupata elimu bora kwa sababu wanafunzi wengi wataendelea kukosa vyumba vya madarasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunatambua kwamba wazazi pamoja na shughuli kubwa wanazozifanya pamoja na kujenga hostel, lakini bado ukiangalia wale wanafunzi wa kike zile gharama zote za kuwasomesha kwenye zile hostel bado ni gharama za wazazi. Ni kwa nini Serikali isikubali kugharimia hizo gharama za hostel baada ya kuwa hizi hostel zimejengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mathayo kwa sababu katika rekodi pale juzi juzi ameweza kushiriki utoaji wa mifuko 200 ya cement kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika eneo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefika pale Musoma Mjini, nimeweza kutembelea nimeona kazi kubwa anayofanya. Kwa hiyo, imani yangu kwa ile kazi unayoifanya na nadhani mnataka mjenge takribani vyumba karibuni 200 vinatakiwa vikamilike ndani ya mwezi Machi, naomba tuwaunge mkono kwa sababu mnafanya kazi njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kusema kwa mkakati huu tutashindwa, naomba nikuhakikishie ndio maana mwaka huu tunakamilisha vyumba vingi kwa kutenga karibu shilingi bilioni 29, na ndugu zangu Wabunge naomba niwaambie huku site tunakotoka sasa hivi ukienda huko utakuta kazi kubwa sana ya ujenzi wa madarasa inaendelea. Naamini katika muda huu ambao tuko hapa Bungeni, Mbunge mwingine akirudi katika site kwake atakuta kwamba kuna madarasa mengine katika eneo lake hata alikuwa hajatarajia yameshakamilika. Hii yote ni juhudi ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niwahakikishie Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tutajitahidi kuhakikisha azma ya Serikali kuwapatia wananchi wake elimu bora inafanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala zima la zile hostel zilizojengwa changamoto ni kubwa sana, katika suala la vijana hasa watoto wetu wa kike kwamba ikiwezekana kwamba zile hostel zilizojengwa Serikali igharamie. Naomba niseme hili ni wazo ngoja tutalifanyia kazi, kwa sababu kugharamia hostel zote Tanzania ni bajeti kubwa sana na hizi zimejengwa makusudi ni hostel za kata ziko katika maeneo yetu. Lengo ni mtoto anaenda shuleni na kurudi lakini kwa sababu changamoto ya uzito kwa wanafunzi ni vyema tujenge hostel nasema tuendelee na mpango huu wa sasa pale Serikali kwa kushirkiana na wadau mbalimbali itakavyoona kwamba nini tufanye, lengo ni kuboresha wananchi katika kata zetu tutafanya hivyo kwa kadri inavyowezekana.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kule Musoma nako tumekuwa na tatizo kubwa sana la nyumba za askari na kwa bahati nzuri Serikali iilisikia kilio chetu. Hivi ninavyozungumza ni zaidi ya miaka mitatu sasa kuna jengo kubwa la ghorofa ambalo limejengwa pale Musoma Mjini. Cha kushangaza mpaka leo askari wetu hawajakabidhiwa. Nataka kujua Serikali inasubiri nini kukabidhi jengo hilo ili liweze kusaidia kuondoa ile adha kubwa wanayopata maaskari wetu?
Waheshimiwa Wabunge linapofika suala la maslahi ya askari, robo ya tatu ya Bunge huwa wanasimama kutaka askari wetu wapewe maslahi hayo. Nitakapokuwa nakutana nao nitawaambia kwamba Wabunge huwa wanawasemea ili mnapopita majimboni wawape ushirikiano. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu jengo la Mara, kuna hatua za ukamilishwaji ambazo ndiyo zilikuwa zinafanyika kutoka kwa mkandarasi wetu. Ni moja ya majengo ambayo yapo kwenye hatua za ukamilishwaji na yatakapokuwa yamekamilika yatakabidhiwa ili askari wetu wasipate shida hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wengi mlikuwa bado mnafuatilia, nimeshazunguka mikoa yote kasoro mikoa minne na kwa Mheshimiwa Sikudhani nitafika, bado Ruvuma, Njombe, Songwe, Geita pamoja na Singida. Nimetambua ukubwa wa tatizo hili na sisi ndani ya Serikali tunaendelea kuwasiliana kuweza kuhakikisha kwamba tunalibeba kwa ukubwa wake na hivyo tutalifanyia kazi ili kuweza kupatikana jawabu la kudumu linalohusu makazi ya askari wetu ili waweze kuendana na hadhi ya kazi wanazozifanya.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kilimo cha mabondeni ni kilimo ambacho ni cha asili na kimezoeleka na wananchi, hasa wa Mikoa ya Iringa, Njombe, Songea na kinajulikana kwa jina la ukulima wa vinyungu, sasa hivi kimezuiwa kutokana na kuzuia uharibifu wa vyanzo vya maji; na kwa kuwa, kilimo hicho ndiyo kimekuwa kikitumika kwa muda mrefu.
Je, Serikali ili kuwanufaisha wananchi wa vijiji vya Lukani, Kihesa Mgagao, Lulanzi, Idete, Kimala, Boma la Ng’ombe, wameweka mikakati gani mbadala kuhakikisha kwamba hawa wananchi wanaendelea kulima kilimo kisasa? Imejipangia mikakati gani? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa lazima tukubaliane kwamba ili tuwe na maji endelevu ya kuweza kuwatosheleza Watanzania ni lazima tutunze vyanzo vya maji. Katika utunzaji wa vyanzo vya maji, kuna watu ambao kwa miaka mingi kama anavyosema wamekuwa wanalima kilimo cha vinyungu; maana yake wanalima kwenye vyanzo vya maji. Sasa mikakati ya kuweza kuwatafutia shughuli mbadala ni lazima muwe shirikishi kati ya Halmashauri na Serikali. Haiwezi kuwa Serikali tu inawapelekea kwamba mtafanya hiki, kwa hiyo, ni lazima iwe shirikishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakwenda kukaa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo tuweze kuona shughuli nyingine ambayo wanaweza wakafanya nyingine tofauti na uharibifu wa vyanzo vya maji. Kulingana na sheria yetu, ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji, haturuhusiwi kufanya kazi yoyote, kufuga mifugo au kulima ili tuwe na maji na rasilimali ya kutosha kuwapelekea Watanzania.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba umeme wa REA ni wa vijijini, lakini yako maeneo ya mjini ambayo yana maeneo mengi na makubwa ya vijijini. Nashukuru kwamba REA wameweza kutupatia umeme katika mitaa michache kama ya Nyabisare pamoja na kule Bukanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, kwa kuwa, maeneo mengi ya taasisi yako kwenye hizo kata za pembezoni, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba REA wanaweza kutupatia umeme katika maeneo yote hayo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa yako maeneo, najua Tarime mko wawili na kuna Musoma na Tarime lakini ki-TANESCO ni Tarime, hakuna shida Mheshimiwa, nimeshakuona Mheshimiwa Esther Matiko.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba, ukweli yako maeneo ambayo yako pembezoni ingawaje yanasemeka yako mjini. Tumeshakaa na Mheshimiwa Manyinyi, yako maeneo na hasa kwa taasisi za umma, taasisi zote za umma zitapelekewa umeme kupitia mradi wa REA.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini viko vijiji ambavyo itabidi tuviangalie, vile vijiji ambavyo vinaonekana viko mjini vitapelekewa umeme kupitia miradi ya TANESCO lakini vile vya vijijini kama ambavyo amesema Nyabisare na vingine, tutachambua ili kuona ni vijiji gani vipelekewe kwa Mradi wa REA. Vijiji vyote vya Miradi ya REA tumeshakabidhiwa, kwa hiyo, kwa Mheshimiwa Mbunge ambaye anaona kuna sehemu kuna utata ni vema tukae ili isionekane kijiji fulani kinarukwa.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Nadhani wote tunatambua umuhimu wa Wenyeviti wa Mitaa na kazi wanazozifanya, lakini kumekuwa na kilio cha muda mrefu sana kuhusiana na maslahi yao kwa kazi kubwa wanayoifanya. Je, Serikali sasa iko tayari kutenga bajeti kwa ajili ya kuwalipa mishahara Wenyeviti wa Mitaa pamoja na Madiwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili nililijibu takribani wiki mbili zilizopita na nikasema kwamba kwa jambo la kulipa mishahara utaratibu wa sasa ni kulipa posho. Pale Bunge litakapoamua vinginevyo, tutaangalia jinsi ya kufanya. Kikubwa zaidi ni kwamba tutaendelea na utaratibu huu, lakini tujue kwamba endapo jambo hili litaingia katika mshahara maana yake ni kuwa wage bill lazima itabadilika katika utaratibu wa kiserikali, ambayo vile vile ina changamoto yake. Kwa hiyo lazima tufanye analysis ya kutosha juu ya namna ya kufanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa utaratibu
wa sasa hivi tutaendelea kwa mujibu wa sheria inavyozungumza. Bunge litakapoamua hapo baadaye tutaenda na maamuzi hayo ambayo Bunge litakuwa limeamua hapo baadaye.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Serikali kwa maana ya TAMISEMI wametoa muongozo katika makusanyo yale ya Halmashauri kwa maana ya kwamba asilimia 60 zinapaswa kwenda kwenye maendeleo, asilimia 20 zinapaswa kwenda kwenye kata, asilimia 10 zinapaswa kwenda kwa vijana na wakina mama, kwa hiyo Halmashauri inabakia na asilimia 10 peke yake ambayo ndiyo sasa ilipe mishahara na kuendesha Halmashauri. Je, kutokana na hali hiyo ni kwanini sasa hawa Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wasilipwe moja kwa moja kutoka Serikali Kuu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ukiwaangalia
hao Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wanayo majukumu mengi na makubwa kwa hiyo hata wakati mwingine wanashindwa kutekeleza majukumu yao kutokana na tabu walizonazo hasa hasa za usafiri. Je, Serikali sasa imejiandaaje kuhakikisha kwamba nao inawawezesha kupata usafiri ili waweze kutekeleza majuku yao ya kila siku?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ni kwamba kwanini sasa hawa Wenyeviti wasilipwe moja kwa moja kutoka Serikali Kuu na msingi umesema kwamba kwa sababu kulikuwa na suala zima la mgawanyo wa zile fedha kwamba asilimia 60 ziende katika maendeleo;
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipowasilisha bajeti yetu mwaka Mheshimiwa Waziri alitoa ufafanuzi hapa kwa kina kwamba hili limeonekana kwa sababu lilikuwa hoja ya msingi ya Waheshimiwa Wabunge, ndiyo maana tumetoa maelekezo. Mheshimiwa Waziri alizungumza wazi hapa kwamba fedha hizi sasa zitagawanyika tofauti, kwamba kwa baadhi ya Halmashauri hasa zile ambazo uwezo wake ni mdogo, sasa asilimia 60 zitakwenda katika matumizi haya mengine na asilimia 40 itakwenda katika maendeleo, huu ndio ufafanuzi kulingana na bajeti ya mwaka huu tuliyoipitisha hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo, lengo letu kubwa katika dhana ya ugatuaji wa madaraka ni kutafuta jinsi ya kufanya katika kuongeza nguvu za Halmashauri za kuweza kukusanya mapato. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mathayo tutaendelea kulisimamia hilo, lakini kubwa na la msingi ni jinsi ya kufanya katika kukusanya vizuri mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja ya pili, kuhusu vyombo vya usafiri; ni kweli, tukiangalia viongozi wetu wana changamoto kubwa ya usafiri, kwa sababu kama Madiwani wanafanya kazi kubwa, lakini hili naomba tulichukue sisi Serikali kwa sababu ni jambo ambalo naona ni la msingi hapo baadaye kwa kupitia Halmashauri zetu ni kwa jinsi gani tutafanya kupitia mifuko mbalimbali ili aangalau kuwezesha Waheshimiwa Madiwani waweze kupata vyombo vya usafiri. Hata hivyo jambo hili tutashirikishana vizuri kupitia katika Serikali zetu za Mitaa.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali moja la nyongeza. Ni ukweli usiopingika kwamba ufugaji wa samaki ni zao linaloweza kuleta matokeo ya haraka kwanza si katika tu suala la ajira lakini vilevile katika kipato cha mfugaji hata yule mwenye kipato cha chini. Hata hivyo, liko tatizo moja kubwa sana la chakula cha samaki. Taasisi nyingi zikiwemo hizi zetu za Serikali ambazo zinaonesha utafiti wa ufugaji wa samaki wanakuonesha kwamba samaki hasa aina ya tilapia anapaswa afugwe ndani ya miezi sita awe ameshafikia uzito usiopungua nusu kilo kwa kula chakula chenye formula hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza unapokuja kwenye hali halisi wale samaki wanalishwa zaidi mpaka wakati mwingine mwaka mmoja pasipokufikia uzito ule. Kutokana na hali hiyo wakulima au wafugaji wengi wanakata tamaa katika hili zoezi zima la ufugaji wa samaki. Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kuhakikisha utafiti madhubuti unafanyika ili ile formula inayotolewa iweze kuleta tija kwa wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba udhaifu umeonekana kwa samaki wetu wanaofugwa hasa hao tilapia ambapo kutokana na chakula wanacholishwa wanachukua muda mrefu lakini ukuaji wao wa kuweza kufikia nusu kilo na sentimeta 50 ili waweze kuvuliwa umekuwa sio wenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili la ufugaji wa samaki kwa maana ya aqua culture katika nchi yetu ni jipya. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, sasa tunayo Kurugenzi mahsusi kabisa inayohusika na jambo hili la aqua culture na kupitia tafiti zetu mbalimbali za TAFIRI na vyuo vyetu vingine tunafanya jitihada za kuhakikisha tunaondoa tatizo hili la chakula cha mifugo hii ya samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wafugaji wote wa samaki nchini kwamba, baada ya muda siyo mrefu watafiti wetu hawa watabaini na kugundua lishe iliyo bora zaidi ili kuweza kukidhi mahitaji ya soko na mahitaji ya wafugaji wetu. Waendelee kujiandaa na kuendelea kuhamasishana katika ufugaji wa samaki, tatizo la chakula cha mifugo hii ya samaki litakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa pale kwenye Mji wetu wa Musoma tatizo la nyumba za polisi limekuwa ni tatizo kubwa na kwa muda mrefu. Na ninakumbuka kuanzia mwaka 2006 nimekuwa nikipiga kelele hapa Bungeni na bahati nzuri Serikali yetu sikivu ikakubali na ikaanza kujenga pale jengo na kufikia mwaka 2014 likawa limekamilika zaidi ya asilimia 85, lakini cha ajabu Serikali imeshindwa kutoa fedha za kulimalizia, matokeo yake wameanza kuiba milango, masinki na vitu vingine.
Je, Serikali sasa ni lini itatoa fedha ili ujenzi huu uweze kumalizika na wale askari waweze kuihsi vizuri?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru babu yangu Mheshimiwa Veda Mathayo kwa swali lake alilolileta. Nilishafika kwenye jengo hilo analoliongelea na kwa kweli limeshakamilika kwa kiwango kikubwa. Na sisi kama Wizara tunajipanga kuhakikisha kwamba, katika mwaka wa fedha huu fedha zitakazopatikana na ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo ambayo yameshafikia hatua nzuri, likiwepo hilo pamoja na maeneo mengine yanakamilishwa.
Kwa hiyo, punde fedha zitakapopatikana tutatoa kipaumbele kwa majengo haya ambayo yameshafikia hatua nzuri, ili yaweze kukamilishwa na askari waweze kuhamia. (Makofi)
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi niweze kusema kuuliza swali moja la nyongeza.
Tunatambua kwamba katika kupambana na uvuvi haramu hawa Beach Management Units wamekuwa wakisaidia sana, lakini kwa bahati mbaya sana walikuwa hapati kipato cha moja kwa moja, kwa hiyo wakati mwingine wanageuka wao nao kushiriki katika uvuvi haramu.
Je, ni lini Serikali itaanzisha huu ufugaji wa samaki kwa njia ya cage ambao utakuwa unawapatia vile vikundi wa Beach Management Units kipato cha ziada ili waendelee kutunza maeneo yetu haya ya Uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue kwanza nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mathayo kwa sababu amekuwa mmoja kati ya Wabunge ambao wamejitahidi sana kuhakikisha kwamba wavuvi wao wanaingia katika ufugaji wa samaki vilevile uvuvi ambao ni endelevu, tunatambua jithata hizo zimezaa matokeo mazuri sana kwani katika eneo analotoka uvuvi haramu umepungua sana. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ufugaji wa samaki kwenye vizimba (cage culture) ni moja kati ya aina ufugaji wa sasa ambao Serikali imeamua kuhimiza wananchi wajihusishe nao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inachofanya ni kutoa elimu pamoja na kuweka mazigira wezeshi ambayo wavuvi mbalimbali wanaweza wakajihusisha katika cage culture kwa hiyo katika BMUs lakini vilevile kwa wavuvi mmoja mmoja kama kuna ambao wanataka kuingia katika ufugaji wa samaki katika vizimba Wizara yangu iko tayari kushirikiana na Halmashauri wanazotoka ili kutoa elimu ya njia sahihi ya kuweza kufanya ufugaji wa samaki kwenye vizimba.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nadhani Mheshimiwa Naibu Waziri analifahamu vizuri suala hili la Kiwanda cha Nguo cha MUTEX, wale watumishi ajira yao ilikoma toka mwaka 1984 na baadhi yao mafao waliyopaswa kulipwa ilikuwa ni zaidi ya Sh.400,000 ambazo wao walizikaa kwamba hayo mafao yalikuwa ni madogo. Tumehangaika na suala hilo kwa kusaidiana na Mheshimiwa Waziri na hatimaye Desemba mafao yao yakatoka badala ya kulipwa zaidi ya Sh.400,000 wamelipwa chini ya Sh.100,000. Kwa sababu suala hili limechukua muda mrefu sasa, je, Mheshimiwa Naibu Waziri sasa yupo tayari kufuatana nami twende tukakae na hawa watumishi ili hilo suala liweze kuisha?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ameomba kuogozana nami kwenda Musoma Mjini, naomba nimwambie baada ya Bunge hili kuahirishwa ziara yangu ya kwanza ni kwenda Msoma Mjini kukutana na wastaafu hawa.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili wale vijana wanaoishi kando kando wa ziwa waweze kuona umuhimu wa kutunza ziwa lao na kuzuia uvuvi haramu. Ni lini sasa Serikali itaweza kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia kujenga mabwawa kando kando ya ziwa pamoja na cage ziwani ili ziweze kuwasaidi hao vijana katika kujipatia kipato ili waweze kuona umuhimu wa kutunza ziwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kila moja amekuwa akishuhudia akina mama wengi wanao nunua samaki wakiwa wamenyanganywa kwenye madishi yao, hata wale waliokaanga samaki wao wanaouza sokoni ambayo hii kusema kweli wao si wavuvi, lakini wanakuja kunyang’anywa samaki wale ambao wameshawanunua. Waziri anatoa kauli gani kuhusiana na unyanyasaji huu ambao unandelea katika baadhi ya maeneo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, mkakati wa Serikali tulionao wa kuhakikisha tunapunguza nguvu ya uvuvi katika maziwa na kuepusha vijana na uvuvi haramu katika kuhamasisha kufanya ufugaji wa samaki; tunaomkakati sana. Hivi sasa ninavyozungumza, tumeshaanza mkakati huo katika Ziwa Victoria ambapo wako watu binafsi walioanza ufugaji wa samaki katika vizimba lakini vilevile na sisi kama Serikali tumejiandaa kuhakikisha tunatengeneza incubators, kwa maana ya vikundi vya vijana ambavyo vitakwenda kufanya shughuli ya utengenezaji wa mabwawa lakini vilevile utengenezaji wa cages kwa ajili ya ufugaji wa samaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Manyinyi ahakikishe anawaunganisha vijana wake kama nilivyotangulia kujibu katika swali la awali, wakae katika vikundi vya ushirika, nasi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tuko tayari kwenda kutoa elimu, lakini vilevile utaalam na kuhakikisha tunawasaidia vijana hawa kuwaongoza katika kufikia lengo sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni juu ya kauli gani tunatoa kwa ajili ya wale akina mama na wanawake wanaouza samaki katika mabeseni. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa tunalinda rasilimali za uvuvi. Katika lengo hilo, hatuko tayari kuona mwanamama anayefanya biashara ya uuzaji wa samaki katika mabeseni huko masokoni, anaonewa. Kama yuko Afisa wa Serikali anayekwenda kumsumbua na kumnyanyasa mwanamke anayeuza mafungu yake matatu, manne sokoni ya samaki, hii leo natoa kauli hapa katika Bunge hili Tukufu, jambo hilo ni marufuku. Kwa sababu lengo letu siyo kuangalia hawa samaki wanaowekwa katika mabeseni, lengo letu ni kutazama hasa kiini cha makosa haya yanayotokana na uvunjaji wa Sheria ya Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niwahakikishie tu akinamama wanaouza samaki nchini kote, wawe huru katika uuzaji wa samaki wao, wahakikishe kuwa wanapata kipato cha familia zao na kujenga Taifa letu.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika marekebisho ya Uwanja wa Ndege wa Musoma, nakumbuka Mheshimiwa Rais amefika pale mara mbili na mara zote ameahidi uwanja huo ujengwe kwa kiwango cha lami na uthamini umefanyika, sasa ni zaidi ya miezi sita. Nataka kupata kauli ya Serikali baada ya kuwa kuna sintofahamu, je, mpango wa kujenga uwanja huo upo au haupo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Manyinyi, Mbunge wa Musoma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Ndege wa Musoma uko kwenye mipango ya kupanuliwa na kuwekewa runway kwa kiwango cha lami na TAA. Hivi karibuni nilifanya ziara Mjini Musoma tukakuta kuna changamoto ya fidia ambapo kulikuwa kuna mvutano wa hapa na pale lakini kuna timu ya wataalam imetumwa pale kwa ajili ya kwenda kuhakikisha ile changamoto ya fidia ya shilingi bilioni tatu na milioni mia saba inatatuliwa ili tuweze kulipa fidia na upanuzi uweze kuendelea.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, mkwe wangu, kwa majibu mazuri aliyoweza kunipatia, lakini (a) kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kati ya watumishi 15,000 walioondolewa waligundua kwamba watumishi 4,160 waliondolewa kimakosa. Hawa ni wale waliopata nafasi ya kuja Dodoma, Utumishi na kwenda Dar es Salaam kwenye Tume. Wale ambao hawakuwa na uwezo, tafsiri yake ni kwamba wamebaki huko.

Sasa swali; ni lini sasa Serikali itaunda tume ambayo angalau itakwenda kila Halmashauri au Mkoani pale iwaite wale wote waliokumbwa na mkasa huu wa kupoteza ajira waje ili vyeti vyao viweze kuhakikiwa ili wale ambao hawakupata nafasi ya kuja waweze kurudi kazini?

Swali la pili; tunatambua kwamba wako watumishi ambao wamekaa au wametumikia nchi hii katika kipindi kirefu na wengine walibakiza tu mwaka mmoja wastaafu na kwa bahati mbaya wamekumbwa na huo mkasa; Serikali ina mpango gani angalau hata kuwapa kifuta machozi ili waende wakaanze maisha yao huko waliko kuliko kuwaacha kama ilivyowaacha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia sana suala la watumishi wa Umma, hususan wale ambao walikuwa wameandika taarifa zisizokuwa na ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kujibu swali lake la kwanza; kwanza kabisa naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge na kwa faida ya Watanzania wengine na Watumishi wa Umma wote kwamba Serikali ilishafanya zoezi la ufuatiliaji kwa zaidi ya asilimia 95 na hilo zoezi limeshakamilika. Wale watumishi wote ambao waliandika taarifa zao siyo sahihi katika personal records au kwenye OPRAS, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba kama walidanganya watakosa stahiki zao zote kwa sababu Kanuni ya Utumishi wa Umma, kile kifungu D.12 kinasema mtumishi yeyote ambaye anaandika taarifa za uongo hataruhusiwa kuwa Mtumishi wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali pia ilitoa msamaha hadi tarehe 31 Desemba, 2017, kwamba wale wote ambao walikuwa wamejiendeleza, basi walete taaifa zao kwenye Ofisi yetu ya Utumishi maana ilishatoa msamaha ili taarifa zao ziweze kuingia na waweze kurudi kazini. Kwa hiyo, zaidi ya watumishi 500 wamesharejeshwa na wale ambao walijiendeleza baada ya muda huo basi waweze kutuletea vyetu vyao tuweze kuhakiki na waweze kurudi kazini. Ahsante.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni kwa nini sasa hawa viongozi ambao mara kwa mara maana huwa tunashuhudia, kiongozi akifika mahali wanawapiga wakinyanyua mabango yao, wanapigwa, wanafukuzwa na kwa tamko hilo sasa ni kwa nini hawa viongozi wanaofanya mambo haya ya kunyanyasa wananchi wasichukuliwe hatua za kinidhamu?

Mhshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; mara nyingi huu utaratibu wa kutatua kero za wananchi, unakuta hata leo mfano Waziri wa TAMISEMI akifika pale ziko kero nyingi za wananchi yeye ndio anazitatua, au Waziri wa Ardhi akifika pale zinaonekana ziko wazi ambazo labda Mkurugenzi angeweza kuzitatua, lakini ameshindwa kuzitatua mpaka kiongozi afike pale. Hali hii sasa inaonesha dhahiri kwamba, leo baadhi ya kero nyingi zinaweza kutatuliwa tu pale ambapo viongozi wa Kiserikali au viongozi wakuu wanaenda pale. Serikali inao mpango gani wa kuhakikisha kwamba, hayo matatizo yanaisha na matatizo ya wananchi yanatatuliwa kule kwenye ngazi za wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MIAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge wa Musoma Mjini, ndugu yangu, kaka yangu Vedastus Mathayo Manyinyi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua ni kwa nini kuna baadhi ya watu wanazuia wananchi kutoa kero zao au kuonesha mabango ambayo yamejaa hisia za changamoto zao katika maeneo yao na amesema kwamba, wanapigwa. Tunachojua ni kwamba, Mheshimiwa Rais na viongozi wengine wakifanya ziara wamekuwa wakiruhusu maswali kujibiwa na wananchi kutoa kero zao. Tukumbushane kwamba, pia kwenye mikutano ile ambayo kiongozi hasa Mheshimiwa Rais anapokuwepo ni mkusanyiko mkubwa sana. Sasa wakati mwingine ni watu wa usalama wanaangalia mazingira yalivyo, bahati mbaya sana yale mabango hayaratibiwi, kwa hiyo, wao wanachukua tahadhari kwanza ya kiusalama halafu wakigundua kwamba, ni ya hoja genuine, wana lengo la kupeleka kero, inaruhusiwa na wamekuwa wakifanya mara kadhaa tumeshuhudia sisi wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nitoe wito kwamba, viongozi wetu hawa kwenye maeneo yetu ya mikoa na wilaya, tunao ugatuzi wa madaraka katika nchi hii kutoka ngazi ya kitongoji mpaka ngazi ya kitaifa na hii itaenda sambamba na kujibu swali lake la msingi, kimsingi Mheshimiwa Rais ameshatoa maelekezo, tumeeleza kwamba, viongozi wetu watoke ofisini, kama ni Mkuu wa Mkoa awe na utaratibnu wa kusikiliza wananchi wake katika eneo lake husika. Kwanza akutane na Wakuu wa Wilaya kwenye mkoa wake husika na watendaji wake, anapokea changamoto katika mkoa wake, wanaweka mikakati namna ya kutatua zile changamoto, halafu badae anafanya ziara kwenda kusaidia yale ambayo yameshindikana ngazi ya wilaya wasaidiane kama mkoa kuyamaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi maana yake ni kwamba, jambo ambalo lipo kwenye ngazi ya kitongoji limalizwe na viongozi wa kitongoji kwa tatizo husika. Jambo likitoka kwenye kitongoji kuja kwenye kijiji au mtaa liwe na uwezo huo walimalize, kwenye kata vivyo hivyo na kwenye ngazi ya wilaya na mkoa. Tukifanya kazi kwa pamoja kila mtu akaenda site, watu wasikilizwe, kero zitatuliwe, hakuna sababu ambayo itakuwepo tena Mheshimiwa Rais au Viongozi wa Kitaifa Mawaziri kwenda mahali mbalimbali kutatua kero.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nitoe wito kwa viongozi wetu kimsingi ni kuonesha kwamba, mtu huyo kwenye mkoa au kwenye kata ameshindwa kufanya kazi. Kama kuna changamoto inatolewa mbele kiongozi wa Kitaifa akiwa kwenye ziara wakati pale kuna mtu ambaye ni wa kisiasa mwakilishi, lakini pia kuna mtu ambaye ni mteuliwa wa Rais au mamlaka nyingine halafu kuna watendaji wa Serikali. Tukifanya kazi kila mtu kwa ngazi yake hii habari ya kupeana mabango wakati viongozi wamekuja haitakuwepo, tutakutana na viongozi watafanya mambo ya jumla makubwa ya Kitaifa na tutaenda na maendeleo yetu kama kawaida. Ahsante.