Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Aida Joseph Khenani (35 total)

MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-
Suala la madai ya walimu nchini limekuwa ni tatizo sugu hususan kwa walimu wa shule za msingi na sekondari. Je, Serikali imechukua hatua gani ili kumaliza tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kulipa madeni yasiyo ya mishahara na mishahara kwa walimu walioko katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kila yanapojitokeza na kuhakikiwa. Aidha, mwezi Oktoba, 2015 Serikali ililipa madeni ya walimu yanayofikia shilingi bilioni 20.125 na mwezi Februari, 2016 imelipa jumla ya shilingi bilioni 1.17 ya madeni ya walimu nchini. Katika fedha za madai ya walimu zilizolipwa Oktoba, 2015 Mkoa wa Arusha ulipelekewa jumla ya shilingi milioni 504.6 ambapo kati ya hizo Halmashauri ya Wilaya ya Meru ilipokea jumla ya shilingi milioni 27.6 ambazo zilitumika kuwalipa walimu 716.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inaendelea kukusanya madeni mapya ya walimu ambapo hadi tarehe 19 Aprili, 2016 madeni yasiyo ya mishahara yanafikia kiasi cha shilingi bilioni 17.5 kwa shule za msingi na sekondari wakati madeni ya mishahara yakifikia shilingi bilioni 49.8.
Mheshimiwa Naibu Spika, madeni haya yatafanyiwa uhakiki na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kisha kuwasilishwa Hazina ili yalipwe.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-
Toka imetangazwa kuwa elimu ni bure walimu wengi wanaofundisha elimu ya awali (chekechea) wameondoka katika shule walizokuwa wanafundisha na kuanzisha vituo vyao sababu ni kutolipwa.
Je, Serikali haioni hili ni tatizo kwa wanafunzi hao ambao wanahitaji msingi mzuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA TAMISEMI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa viti Maalum kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Spika, walimu walioondoka katika shule walikuwa wanalipwa kupitia michango ya wazazi ambao wengi wao hawakuwa na sifa ya kufundisha wanafunzi wa elimu ya awali kwa maana ya kuhitimu Daraja la IIIA.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa, walimu wote wanaopangwa kufundisha shule za msingi mongoni mwao wapo ambao wanapangwa kufundisha darasa la elimu ya awali kwa sababu ya mafunzo wanayopata vyuoni yakijumuisha mbinu za ufundishaji wa elimu ya awai. Vyuo vyote vya ualimu wa shule ya msingi vinatoa mafunzo ya ualimu ngazi ya stashahada ya elimu ya awali. Hadi mwaka 2016 wapo walimu wa daraja la kwanza, IIIA wapatao 191,772 ambao kati yao walimu wenye ujuzi wa kufundisha madarasa ya elimu ya wali ni 10,994.
MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI) aliuliza:-
Kumekuwa na hali ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na
mgambo na askari polisi wanapotekeleza maagizo ya Serikali dhidi ya wafanyabiashara wadogo wadogo hususan mama lishe, bodaboda pamoja na machinga. Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya hali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge
wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mgambo wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria
ya polisi wasaidizi ya mwaka 1969 kwa kuzingatia sheria hiyo, Halmashauri
zimeruhusiwa kuajiri askari ngambo kwa ajili ya kusaidia usimamizi wa Sheria
Ndogondogo za Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, askari mgambo anayefanya kazi katika
Halmashauri anawajibika kuzingatia sheria za nchi pamoja na sheria ndogo
ndogo zilizotungwa na Halmashauri. Jukumu lao kubwa ni kulinda mali za
umma, kulinda usalama wa wananchi pamoja na kutekeleza maelekezo
yatakayotolewa na Halmashauri kwa wakati wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgambo hawaruhusiwi kwa mujibu wa sheria
kuchukua au kuharibu mali za wananchi. Kufanya hivyo ni ukiukwaji wa sheria
za Serikali, na Serikali haitasita kuchuakua hatua kwa vitendo hivyo. Aidha,
naomba kutumia fursa hii kuzikumbusha Halmashauri zote kutenga maeneo
maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ili biashara hizo zifanyike katika
maeneo yaliyotengwa rasmi na kuacha kufanya shughuli hizo katika hifadhi za
barabara na maeneo mengine yasiyoruhusiwa.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:- Kumekuwa na bidhaa fake katika nchi yetu na zinagundulika zikiwa zimeingia nchini. Je, Serikali haioni kuwa kugundua bidhaa hizo zikiwa ndani ya nchi zinakuwa tayari zimewaathiri wananchi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge, kugunduliwa kwa bidhaa fake au bandia zikiwa ndani ya nchi zinakuwa tayari zimewaathiri wananchi. Ili kukabiliana na tatizo la bidhaa hizo kuingia nchini na kuleta madhara kwa watumiaji Serikali kupitia Tume ya Ushindani (Fair Competition Commission) kwa kushirikiana na wamiliki wa nembo za bidhaa mbalimbali imekuwa ikitekeleza mikakati ya kuhakikisha bidhaa fake haziingii nchini. Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kwa lengo la kuwafahamisha wananchi madhara ya bidhaa bandia kiafya, kiuchumi na kimazingira na jinsi ya kutambua bidhaa bandia. Elimu hiyo hutolewa kupitia warsha, makongamano, maonesho ya biashara, vyombo vya habari kama redio, luninga, mitandao ya computer na magazeti. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika njia za kuingizia bidhaa, ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Viwanja vya Ndege vya JK Nyerere, KIA na mipaka inayopitisha bidhaa kutoka nje ya nchi kwa wingi. Pia, kaguzi za kushitukiza hufanyika katika maduka na maghala yanayohisiwa kuhifadhi na kuuza bidhaa bandia kinyume na Sheria ya Alama za Bidhaa ya mwaka 1963 na marekebisho yake ya mwaka 2012. Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali inadhibiti uingizaji wa bidhaa bandia nchini kwa kuimarisha ukaguzi wa bidhaa nje ya nchi kabla ya kuingizwa nchini (Pre Shipment Verification of Conformity Standard). Kuendelea kuajiri wataalam zaidi na kufungua vituo vya ukaguzi wa ubora wa bidhaa katika mipaka zinapoingilia bidhaa kutoka nchi nyingine. Mipango hiyo inahusu mipaka ya Horohoro, Holili, Namanga, Sirari, Mutukula, Kabanga, Rusumo, Tunduma na Kasumulo. Aidha, Fair Competition Commission hushirikiana na taasisi za Serikali hususan Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), TBS, Jeshi la Polisi, Serikali za Mitaa na wananchi wenye mapenzi mema ili kufanikisha ukaguzi na uteketezaji wa bidhaa bandia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itaendelea kuwachukulia hatua wale wote watakaohusika na uingizaji wa bidhaa bandia, ikiwa ni pamoja na kuteketeza bidhaa hizo au kuzirejesha zilikotoka.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-
Wananchi wengi Sumbawanga hawana hati miliki; aidha, kumekuwa na changamoto nyingi katika kupata hati hiyo hali inayowafanya wananchi kukata tamaa.-
Je, ni gharama kiasi gani zinazohitajika ili kupata hati miliki?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida hati miliki za ardhi hutolewa kwa utaratibu wa mwombaji kuchangia gharamaza upatikanaji wa hati husika. Utaratibu huu umetokana na matakwa ya Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 95 ambayo inaelekeza kuwa ardhi ina thamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za kupata hati miliki hutofautiana kutokana na thamani ya ardhi katika eneo linaloombewa hati, ukubwa wa eneo na matumizi yanayokusudiwa katika eneo husika. Kwa mantiki hiyo, gharama za kupata hati miliki hutofautiana kwa kuzingatia vigezo hivyo. Gharama zinazotakiwa kulipwa wakati wa umilikishaji ardhi ni kama ifuatavyo:-
Ada ya upimaji;
(ii) Ada ya uandaaji wa hati ambayo ni shilingi 50,000 ni fixed;
(iii) Ada ya usajili wa hati;
(iv) Ushuru wa stempu;
(v) Gharama za upatikanaji ardhi;
(vi) Ada ya mbele (premium) ambayo ni asilimia 7.5 ya thamani ya ardhi; na
(vii) Ada ya ramani ndogo (Deed Plan) ambayo ni shilingi 20,000 nayo ni fixed.
Mheshimiwa Naibu Spika, ada ya upimaji, usajili wa hati, ushuru wa stempu na gharama za upatikanaji ardhi hutegemea ukubwa na thamani ya ardhi katika eneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwa na uwiano wa gharama za umilikishaji wa ardhi nchini, Wizara imeandaa na kusambaza mwongozo wa ukadiriaji wa bei za viwanja kwa Halmashauri zote nchini. Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini hazina budi kuzingatia mwongozo wa bei elekezi za viwanja uliotolewa ili kuwawezesha wananchi kupata hati miliki kwa gharama nafuu zaidi.
MHE. AIDA J. KHENAN aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani kwa vijana wanaomaliza shule za msingi, sekondari na vyuo kwa kuwawezesha kujiajiri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inayo mikakati mbalimbali ambayo inawezesha vijana wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya mikakati inayotekelezwa mahsusi kwa ajili ya vijana wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari ni kama ifuatavyo:-
Ni kutekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi nchini, ambapo kupitia programu hii tumeanzisha utaratibu maalum wa kutambua ujuzi uliopatikana kupitia mfumo usio rasmi na kuurasimisha kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wale walio tayari kuhitaji na kuwapa vyeti vinavyotambulika. Utaratibu huu unawapa fursa vijana wetu kuendelea na mfumo rasmi wa mafunzo na pia kutambulika na waajiri au watoa kazi.
Ni kuhamasisha vijana wanaomaliza shule za msingi na sekondari kujiunga katika vikundi vya kuzalisha mali na kusajiliwa rasmi kupitia Sheria ya Usajili wa NGO’s . Hadi sasa jumla ya vikundi vya vijana vya uzalishaji mali 10,200 vimekwishakusajiliwa.
Aidha, ipo mikakati ya kuwawezesha wahitimu wa vyuo kujiajiri na kuajiriwa ambayo ni pamoja na:-
– Ni kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo inawezesha vijana wahitimu wa vyuo kupata ujuzi wa kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa. Programu hii inatoa mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wahitimu (internship) ili kuwapatia uzoefu wa kazi.
– Serikali imerahisisha utaratibu wa uundaji wa makampuni kupitia BRELA hivyo vijana wengi wanaomaliza vyuo kuweza kuanzisha makampuni na biashara zinazoweza kuajiri vijana wengine.
Mheshimiwa Spika, pia ipo mikakati inayowawezesha wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kujiajiri ambayo ni:-
(a) Serikali imeendelea kuimarisha utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao unalenga kuwasaidia vijana wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kuweza kujiajiri kwa kuwapa mikopo ya mashati nafuu na mafunzo ya ujasiriamali. Katika kipindi cha mwaka 2013/2014 hadi mwaka 2016/2017 Serikali kupitia Mfuko wa Mendeleo ya Vijana imetoa mikopo ya masharti nafuu ya shilingi bilioni 5.8 kwa vikundi vya vijana 6,076 vyenye wanachama 30,380 katika Halmashauri za Wilaya 157 kupitia SACCOS za vijana.
(b) Serikali kupitia Halmashauri zinatenga maeneo kwa ajili a vijana wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kufanya shughuli za uzalishaji mali ili kujipatia ajira. Katika mwaka 2016, jumla ya hekta 271,882 zilitengwa kwa ajili ya shughuli za vijana.
MHE. AIDA J. KHENAN aliuliza:-
Mara kwa mara Serikali imekuwa ikishindwa kesi mbalimbali Mahakamani:-
Je, Serikali imefanya uchunguzi na kujua sababu za kushindwa kesi mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n. y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge hakutaja aina ya kesi anazomaanisha katika swali lake, nianze kwa kufafanua kwamba, kuna aina mbalimbali za kesi au mashauri yanayofunguliwa Mahakamani na Serikali au dhidi ya Serikali. Mfano, mashauri ya jinai, madai, katiba, uchaguzi na kadhalika. Kwa ujumla mashauri hayo hufunguliwa kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, vilevile Halmashauri, Mashirika ya Umma, Taasisi, Wakala wa Serikali na Idara za Serikali zinazojitegemea zinayo mamlaka ya kuendesha na kusimamia mashauri yanayofunguliwa dhidi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mashauri yote yanayofunguliwa na Serikali au dhidi ya Serikali yamekuwa yakiendeshwa kwa weledi na pale inapostahili Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekuwa ikiratibu uendeshaji wa mashauri hayo na takwimu zetu zinaonesha mashauri mengi Serikali inashinda. Kwa mfano, kati ya mashauri 53 ya kupinga Uchaguzi wa Ubunge yaliyofunguliwa Mahakamani baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, Serikali ilishinda mashauri 52 na kushindwa shauri moja tu na katika mashauri 199 ya kupinga Uchaguzi wa Madiwani, Serikali ilishinda kesi 195.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama takwimu zinavyoonesha si kweli kwamba, Serikali imekuwa ikishindwa kesi mara kwa mara. Hata hivyo, katika nchi yoyote inayozingatia uhuru wa Mahakama na utawala wa sheria, Serikali haiwezi kushinda kila shauri hata kama haistahili. Ni kweli kuna baadhi ya kesi ambazo Serikali inashindwa, sababu zinazosababisha Serikali kushindwa baadhi ya mashauri ni pamoja na namna ushahidi ulivyokusanywa na vyombo vya Serikali, kutokupatikana mashahidi muhimu, mashahidi kutokutoa ushahidi uliotegemewa, baadhi ya Taasisi, Mashirika ya Umma na Idara za Serikali kutoishirikisha mapema ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, zinapofungua au kufunguliwa mashauri Mahakamani, namna ushahidi unavyochukuliwa Mahakamani, mashahidi kula njama na kutoa ushahidi unaoathiri mashauri ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa ikiwemo kuhakikisha kuwa, mashahidi muhimu wanapatikana, kuwaandaa ipasavyo mashahidi kabla ya kutoa ushahidi, kujiandaa vema katika kila shauri, kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi ipasavyo, kushirikiana na vyombo vya Upelelezi kama TAKUKURU na Jeshi la Polisi katika maeneo yanayosababisha ushahidi kuwa hafifu na kurekebisha kasoro hizo, kukata rufaa na kuendelea kuzishauri taasisi za Serikali kutoa taarifa mapema kwa Mwanasheri Mkuu wa Serikali katika kila shauri lililofunguliwa Mahakamani, ili kwa pamoja kuangalia namna ya kulinda maslahi ya Serikali katika shauri husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kupitia Bunge hili sheria zinazosimamia Mashirika na Taasisi za Serikali zimekuwa zikirekebishwa na kuweka masharti yanayompatia Mwanasheria Mkuu wa Serikali haki ya kuingilia kati shauri lolote lililofunguliwa dhidi ya Serikali au Taasisi ya Umma kwa lengo la kulinda maslahi ya Serikali.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na watumishi waliokumbwa na sakata la vyeti fake?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako kuwa Serikali imeshatoa vibali vya kuajiri watumishi 15,000 ili kuziba pengo lililosababishwa na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti. Vibali kwa ajili ya watumishi hao vimetolewa katika ngazi ya Wizara, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na waajiri wote wameendelea kujaza nafasi hizo.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia imetoa vibali vya ajira kwa mamlaka zote za Serikali za Mitaa Kumb. Na. CFC.26/ 205/01/PF/91 cha tarehe 22 Agosti, 2017 na kibali kingine cha tarehe 12, Machi, 2018 kuziba nafasi zote za Watendaji wa Vijiji na Mtaa zilizoachwa wazi kutokana na zoezi la kuhakiki vyeti kwa kuajiri watumishi wapya.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa kutambua umuhimu wa kuajiri watumishi wa kada mbalimbali, Serikali imetoa vibali vya kuajiri watumishi 22,150 wakiwemo watumishi wa kada za ualimu 6,840, fundi sanifu wa maabara za shule 160, kada za afya 8,000, wahadhiri wa vyuo vikuu 624 na watumishi 6,526 wa kada nyingine.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-
Katika Hospitali ya Rufaa ya Rukwa kumekuwepo na tatizo la wanawake wajawazito na waliojifungua kulazwa katika kitanda kimoja.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo hilo katika hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Watoto, naomba kujibuswali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge, Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na changamoto ya akina mama wajawazito na waliojifungua kulala katika kitanda kimoja inayochangiwa na ufinyu wa nafasi katika jengo la wazazi lililopo kutokana na ongezeko la idadi ya watumiaji wa huduma hizi hasa kwa kuwa hospitali hii ilianza kama kituo cha afya mwaka 1974. Vilevile tatizo hili linachangiwa na ukosefu wa Hospitali za Wilaya katika Halmashauri za Kalambo na Sumbawanga hali inayosababisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kuhudumia wateja wote wanaotoka kwenye halmashauri zote mbili.
Mheshimiwa, Mwenyekiti, Wizara imeweka mikakati ya ufumbuzi wa changamoto hii kama ifuatavyo:-
a) Kupitia Mpango Kabambe wa Hospitali wa mwaka 2017/2018 yaani Comprehensive Hospital Operation Plan, Wizara imekamilisha ukarabati wa wodi mbili na hivyo kuongeza nafasi ya vitanda kwa ziada 20 ambavyo tayari vinatumika na hivyo, kupunguza msongamano uliokuwepo.
b) Serikali inafanya ujenzi na upanuzi wa miundombinu katika vituo vya afya sita ambavyo ni Mazwi, Nkomolo, Kirando, Mwimbi, Legezamwendo na Milepa ndani ya Mikoa hii. Kupanua wigo wa kujifungua kwa njia ya upasuaji. Hatua hii itapunguza tatizo la akina mama wajawazito wengi kupewa rufaa kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
c) Serikali kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imetenga jumla ya shilingi bilioni 100.5 katika mwaka 2018/2019 kwa ajili ya upanuzi wa Hospitali za Halmashauri 67 ambapo kila moja imetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.5. Halmashauri za Mkoa wa Rukwa zinatarajiwa kunufaika na fedha hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matarajio yangu kwamba Serikali kupitia mikakati hii itatoa tatizo la msongamano wa akina mama wajawazito waliojifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Rukwa.
MHE. DESDERIUS J. MIPATA (K.n.y. MHE. AIDA J. KNENAN) aliuliza:-
Kila mwaka kuna wanafunzi wanaoendelea na masomo (waliofaulu) na waliofeli wengi hubaki nyumbani kwa kukosa fedha na sifa za kuendelea na masomo:-
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwasaidia wanaoshindwa kuendelea na masomo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka Serikali huwapima wanafunzi kupitia Mitihani ya Taifa inayosimamiwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) baada ya kumaliza elimu ya msingi na elimu ya sekondari, ambapo wale waliofaulu huendelea na masomo katika ngazi inayofuata. Kwa wanafunzi ambao hawakufaulu mitihani ya kidato cha nne na cha sita, wanaruhusiwa kufanya tena mitihani kama watahiniwa wa kujitegemea (Private Candidates).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima vipo vituo vinavyotoa masomo ya elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi, kwa kusoma masomo ya kidato cha kwanza na pili kwa mwaka mmoja na kufanya mtihani wa maarifa unaofahamika kama (Qualifying Test) na endapo mwanafunzi atafaulu ataruhusiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne kama mtahiniwa binafsi. Katika programu hii, walengwa 10,420 wamesajiliwa katika mwaka 2017; kati yao 6,074 ni wanawake na 4,346 ni wanaume. Aidha, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima huandaa na kuendesha programu za elimu mbadala kwa vijana na watu wazima kulingana na mahitaji yao. Programu hizo hutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kama vile ujasiriamali, stadi za maisha, ufundi wa awali na programu za kisomo cha kujiendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia VETA inatoa mafunzo ya ufundi stadi kulingana na mahitaji ya soko la ajira ambapo jumla ya wanachuo 35,000 wanahitimu kila mwaka katika vyuo 732 vilivyosajiliwa na VETA nchi nzima. Mafunzo wanayopata yanawasaidia wahitimu kuwa na stadi za kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri katika sekta rasmi na isiyo rasmi. Aidha, Serikali inaendelea kuviimarisha Vyuo 55 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) ili viweze kuongeza wigo wa kudahili wanafunzi katika nyanja mbalimbali za mafunzo na hivyo kutoa fursa zaidi kwa wanafunzi wanaoacha masomo kwenye mfumo rasmi wa elimu.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI) aliuliza:-

Kumekuwa na utaratibu wa Serikali kuchukua maeneo kwa wananchi na kuahidi kuwalipa, lakini huchukua muda mrefu kuwalipa.

Je, Serikali haioni kuwa kufanya hivyo ni kuwanyima wananchi haki yao ya msingi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ulipaji wa fidia hufanyika kwa mujibu wa Sheria Namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria Namba 5 ya mwaka 1999. Sheria hizi zinaelekeza kwamba pindi Serikali au mamlaka nyingine inapotwaa maeneo ya wananchi, wanatakiwa kulipa fidia stahiki, kamili na kwa wakati. Pamoja na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999 Serikali ilitunga Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini Namba 7 ya mwaka 2016 ambayo imeelekeza kuwa pindi uthamini unapofanyika waliothaminiwa mali zao wanapswa kulipwa ndani ya miezi sita. Baada ya miezi sita tozo yaani prevailing interest rate in commercial banks inapaswa kuongezwa kwenye malipo ya madai ya fidia husika. Aidha, baada ya kupita kwa kipindi cha miaka miwili toka uthamini wa awali ufanyike, sheria inaelekeza pia, uthamini wa eneo hilo utafanyika upya.

Mheshimiwa Spika, licha ya taratibu za ulipaji wa fidia kuwekwa wazi katika sheria, kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi katika maeneo mbalimbali kuhusu ucheleweshaji wa malipo ya fidia. Katika kutatua changamoto hizo Wizara imeandaa mwongozo unaozitaka taasisi zote zinazotaka kuchukua mali za wananchi kuwasilisha uthibitisho wa uwezo wa kulipa fidia kabla ya kuidhinishiwa kwa taarifa za uthamini wa mali unaotarajiwa kuchukuliwa. Aidha, mwaka 2016 Wizara ilizindua Mfuko wa Fidia ya Ardhi utakaosaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijitokeza katika ulipaji wa fidia. Mfuko huo umepewa jukumu la kuratibu malalmiko ya ulipaji fidia na kusimamia malipo yote ya fidia yanayofanywa na watu au taasisi binafsi, ili kuhakikisha kuwa viwango vinavyotumika ni vile vilivyokubaliwa kwa wakati huo.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kuwa changamoto ya ucheleweshaji wa malipo ya fidia imepatiwa ufumbuzi kwa kiasi kikubwa. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa changamoto hii inafikia mwisho ili kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa wananchi.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, kwa nini Serikali inatenga na kutumia fedha kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, tuna majibu yake. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba nimjibu Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, madhumuni ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kama ilivyotajwa kwenye Katiba, Ibara ya 146(2)(a) mpaka (c) ni kuimarisha demokrasia na kutumia demokrasia katika kuharakisha maendeleo. Katika kutekeleza jukumu hili muhimu, viongozi wanaoongoza vyombo vya Serikali za Mitaa huchaguliwa kwa njia ya kidemokrasia kupitia uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika ngazi ya vijiji, mitaa na vitongoji.

Mheshimiwa Spika, uchaguzi wa Serikali za Mitaa unahitaji rasilimali fedha ili kuwezesha upatikanaji wa mahitaji mbalimbali kwa ajili ya uchaguzi ikiwemo vifaa vya uchaguzi yani masanduku, lakiri, fomu na kadhalika. Pamoja na vifaa hivyo, zipo gharama mbalimbali zinazohusiana na uendeshaji wa uchaguzi huo ikiwemo mafuta ya magari, matengenezo ya magari na posho mbalimbali kwa ajili ya watu watakaoshughulikia mchakato mzima wa uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, vilevile zipo taratibu za kisheria ambazo zinapaswa kufuatwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kama vile kutoa matangazo ya Kiserikali yanayohusu uchaguzi, kufanya vikao mbalimbali na wadau wa uchaguzi, kuhakiki maeneo au majimbo ya uchaguzi na kuandaa Daftari la Wapiga Kura, kuratibu shughuli hizo zote zinahitaji rasilimali fedha. Hivyo, kukamilisha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni lazima Serikali itenge fedha za kugharamia shughuli hizo, kama ilivyo kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, kwa sasa Tanzania ina aina ngapi za madini?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Tanzania ina aina mbalimbali za madini ambayo kijiosayansi yamegawanyika katika makundi matano ambayo ni; madini ya metali kama vile dhahabu, madini ya fedha, chuma, shaba, risasi, aluminum, nickel, niobium, bati na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, yako pia aina nyingine ya madini, ambayo ni madini ya vito (gemstones) ambayo ni pamoja na madini ya Tanzanite, almasi, rubi pamoja na mengineyo

Mheshimiwa Spika, kundi la tatu ni la madini ya viwandani, ambayo yanaintwa industrial minerals kama vile kaolin, mawe ya chokaa, jasi, phosphate pamoja na chumvi na na mchanga wa ufukweni.

Mheshimiwa Spika, madini ya ujenzi ni kundi lingine la madini ambayo ni madini ya nakshi kama vile mawe, kokoto, udongo wa mfinyanzi, mchanga na mawe ya nakshi. Aidha, yapo pia madini ya nishati kama vile makaa ya mawe, gesi na uranium.

Mheshimiwa Spika, madini haya ni muhimu katika kujenga uchumi wa viwanda na kuongeza mchango wa uchumi kwa madini katika Pato la Taifa. Madini haya ni muhimu katika maendeleo ya wananchi kwa kuwa yanatumika katika shughuli mbalimbali za ujenzi, viwanda, mapambo na kuleta fedha za kigeni nchini.
MHE. MARY D. MURO (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENAN) aliuliza:-

Je, ni lini Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) litajenga nyumba za bei nafuu ambazo wananchi wenye hali ya chini wataweza kununua?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekuwa likitekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba kwa kufuata Mpango Mkakati wa Miaka 10 unaoanza 2015/2016 - 2024/2025. Pamoja na Shirika kutekeleza mpango mkakati huo, Shirika limekuwa na miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa kipato cha chini wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za nyumba hizo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo gharama kubwa ya kununua ardhi, riba ya mikopo na gharama za uwekaji wa miundombinu katika maeneo ya miradi. Ili Shirika liweze kujenga nyumba za gharama nafuu hususani kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini, mamlaka husika zinatakiwa kuwezesha upatikanaji wa ardhi, uwepo wa miundombinu ya umeme, maji, barabara na riba nafuu ya mikopo ya taasisi za fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika ziara Mkoa wa Mtwara aliagiza kuwa Halmashauri zote nchini zitoe ardhi kwa Shirika la Nyumba la Taifa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na pia taasisi zinazohusika na miundombinu ziweke miundombinu hiyo kwenye maeneo ya miradi ya shirika ili kupunguza gharama ya nyumba hizo. Kufuatia utekelezaji wa maelekezo hayo, bei ya nyumba katika baadhi ya miradi imeshuka kwa kiasi kikubwa. Mfano, bei ya nyumba katika mradi wa Chatur, Wilaya ya Muheza imeshuka mpaka shilingi milioni 24.6 ikilinganishwa na bei ya miradi ya awali mfano Ilembo, Katavi ambayo ilikuwa inauzwa milioni 30.6; Mlole Kigoma milioni 34.2; na Mtanda, Lindi milioni 33.6. Tunatoa rai kwa Halmashauri zingine za Miji na Wilaya kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais ili waweze kujengewa nyumba za gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi, shirika linadhamiria kujikita zaidi katika ujenzi wa nyumba za kupangisha ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wasio na uwezo wa kununua nyumba. Kwa kuanzia nyumba hizo za kupangisha zitajengwa katika Jiji la Dodoma eneo la Chamwino ili kukidhi mahitaji yaliyopo hususan kwa watumishi wa Serikali.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Kumekuwa na matamko na makatazo mbalimbali juu ya wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shuleni:-

Je, matamko na makatazo hayo yamesaidia kwa kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali naomba kutumia nafasi hii kuwatakia vijana wetu 947,221 wanaofanya mitihani yao ya darasa la saba, naomba niwatakie kila la kheri na Mungu awaongoze katika mitihani yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, matamko na makatazo kuhusu wanafunzi wanaopata ujauzito yanatokana na Kanuni za Elimu za Mwaka 2002, Kanuni Na. 4 ya Sheria ya Elimu ya Mwaka 1978, Sura Na. 353 inayobainisha makosa ya wanafunzi shuleni. Aidha, yanazingatia marekebisho ya Sheria ya Elimu Na. 25 ya Mwaka 1978 yaliyofanyika mwaka 2016. Katika marekebisho hayo, mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari atahukumiwa kifungo cha miaka 30 jela. Sheria hii pia inatoa adhabu kwa mtu yeyote anayesaidia mhalifu aliyempa mwanafunzi mimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria na makatazo hayo yamesaidia jamii kufahamu umuhimu wa kulinda hadhi na usalama wa mtoto wa kike. Pia, imesaidia kujua adhabu kwa mtu yeyote anayempa mwanafunzi mimba ambapo kesi zimefunguliwa na baadhi ya wahusika wamehukumiwa kifungo kwa kosa hilo. Aidha, elimu, matamko na sheria vimesaidia kupunguza mimba za wanafunzi kwenye maeneo mengi nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka mikakati ya kupunguza changamoto kwa watoto wa kike ikiwa ni pamoja na kujenga mabweni na hosteli katika maeneo ambayo wanafunzi wanalazimika kutembea umbali mrefu. Aidha, Serikali pia imeweka mpango wa kusaidia wasichana wanaoacha shule kwa sababu mbalimbali ili waweze kuendelea na masomo. Mpango huo ni kutoa elimu kupitia Vyuo vya Elimu Nje ya Mfumo Rasmi vinavyoratibiwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Waziri pamoja na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC).

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano wa kuwalinda watoto wa kike na kuhakikisha kuwa taarifa zinatolewa kwa mamlaka husika ili kuhakikisha kuwa mtu yeyote anayemsababishia mtoto wa kike kukosa elimu anakumbana na mkono wa sheria.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, kuna utaratibu wowote wa kuajiri watu wote waliohitimu Vyuo na kukidhi vigezo vya kuajiriwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani Mbunge wa Viti maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mrefu Serikali imekuwa Mwajiri Mkuu, wa Wahitimu wa Vyuo mbalimbali kutoka katika soko la Ajira nchini. Ajira hizi zimekuwa zikitolewa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya raslimali watu katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi mbalimbali za Serikali kwa kuzingatia ikama na bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kugharamia ajira mpya katika Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, Serikali ilianzisha Sekretarieti ya ajira katika Utumishi wa Umma, kwa lengo la kuratibu mchakato wa ajira katika Utumishi wa Umma kwa uwazi na ushindani kwa njia ya usaili wa nadharia na vitendo pale inapobidi. Hivyo, wahitimu wanaofaulu usaili ndiyo wanaokidhi vigezo vya kuajiriwa na huwa wanaajiriwa kwa kada zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Duniani kote, Serikali siyo mwajiri pekee wa wahitimu wa vyuo mbalimbali vya elimu, kwani pamoja na kuajiriwa Serikalini, wahitimu hao huajiriwa pia katika Sekta binafsi, Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali, Asasi za Kiraia na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, wahitimu wengine huamua kujiajiri wenyewe na hivyo kutoa mchango wa maendeleo kwa Taifa kwa njia moja au nyingine. Aidha, kuhitimu Elimu ya juu, siyo kigezo pekee cha kuwezesha muhitimu husika ila sifa na ushindani wa kutosha ili kuweza kuajiriwa na Serikali. Hivyo, Serikali haina utaratibu wa kuajiri wahitimu wote wa vyuo vya Elimu ya juu nchini. Ahsante.
MHE. AIDA J. KHENAN aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha kwenye kivutio cha maporomoko ya Kalambo?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maporomoko ya Mto Kalambo yapo katika Msitu wa Hifadhi ya Mazingira Asilia Kalambo yenye ukubwa wa hekta 41,958. Hifadhi hii ni muunganiko wa misitu miwili; Msitu wa Mto Kalambo na Msitu wa Hifadhi wa Maporomoko ya Mto Kalambo. Kutokana na kuwepo kwa maporomoko hayo, eneo hili lina bioanuai nyingi. Kwa kuzingatia umuhimu wa eneo hilo, mwaka 2019, Serikali ilipandisha hadhi msitu huo kwa Tangazo Na. 127 kuwa Msitu wa Mazingira Asilia.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), mwaka 2016 ilianza kuboresha miundombinu katika Maporomoko ya Kalambo ili kuwezesha watalii kuvifikia kivutio husika kwa urahisi, ikiwa ni pamoja na kujenga ofisi sita, kutengeneza njia za kutembelea wageni (walk trail) na kujenga ngazi katika maporomoko ya Mto Kalambo ambapo hadi sasa takribani ngazi zenye urefu wa mita 450 zimekamilika.

Mheshimiwa Spika, aidha, kazi ya ujenzi iliyoanza mwaka 2018 ambayo inahusisha ujenzi wa jengo la ofisi, ngazi zenye urefu wa mita 514, vyoo na geti inayofanywa na kampuni iitwayo Green Construction Limited inaendelea kufanyika katika maporomoko hayo na kazi hii inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu wa 2020.

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha mazingira ya utalii katika eneo hilo, Serikali itahamasisha sekta binafsi ili zijengwe nyumba za kulala wageni, kumbi za mikutano na eneo la kuhifadhi wanyamapori hai (zoo) ili kuweka mazingira rafiki kwa watalii.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI) Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapelekea wakulima pembejeo kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kurudi tena ndani ya Bunge. Pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani yake kwangu.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali huratibu mahitaji, upatikanaji, usambazaji, matumizi na kuhakiki wa ubora wa pembejeo za kilimo ili ziweze kufikishwa kwa wakulima kwa wakati zikiwa na ubora stahiki. Katika kutekeleza jukumu hilo, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati. Mikakati hiyo, ni pamoja na kupata mahitaji halisi ya pembejeo za kilimo kutoka kila Mkoa kabla ya msimu wa kilimo kuanza, kuwasiliana na makampuni ya pembejeo na kuyahimiza kusambaza pembejeo hizo mapema kulingana na mahitaji ya kila Mkoa kabla ya msimu wa kilimo.

Mheshimiwa Spika, wakulima kupitia Vyama vyao vya Ushirika wanahimizwa kuainisha na kuwasilisha mahitaji ya pembejeo mapema kwa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) ili waweze kununua mbolea wanazohitaji kwa wakati kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa pamoja ambao katika mwaka 2020, wakulima wa Mikoa kama Iringa, Mbeya waliingiza mbolea moja kwa moja kutoka kiwandani katika nchi za Morocco na China. Aidha, Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya uzalishaji na uagizaji na uthibiti wa mbegu bora na viuatilifu nchini ikiwemo kuhamasisha uzalishaji wa pembejeo hizo ndani ya nchi ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara wa pembejeo kujenga maghala makubwa kwa ajili ya kuhifadhi pembejeo hususan katika maeneo yenye mahitaji makubwa ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati wote. Utekelezaji wa mpango huu ulianza mwaka 2019 ambapo Wadau wa Maendeleo wakiwemo African Fertilizer and Agribusiness Partnership waliwezesha ujenzi wa jumla ya maghala 12 mwaka 2019 yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya tani za mbolea 50,000 katika Mikoa ya Kilimanjaro, Morogoro, Arusha, Iringa, Rukwa, Njombe na Songwe. Aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha pembejeo nchini ili kuongeza upatikanaji wake kwa wakati na bei nafuu kwa wakulima.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA (K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI) Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapelekea wakulima pembejeo kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kurudi tena ndani ya Bunge. Pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa imani yake kwangu.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali huratibu mahitaji, upatikanaji, usambazaji, matumizi na kuhakiki wa ubora wa pembejeo za kilimo ili ziweze kufikishwa kwa wakulima kwa wakati zikiwa na ubora stahiki. Katika kutekeleza jukumu hilo, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati. Mikakati hiyo, ni pamoja na kupata mahitaji halisi ya pembejeo za kilimo kutoka kila Mkoa kabla ya msimu wa kilimo kuanza, kuwasiliana na makampuni ya pembejeo na kuyahimiza kusambaza pembejeo hizo mapema kulingana na mahitaji ya kila Mkoa kabla ya msimu wa kilimo.

Mheshimiwa Spika, wakulima kupitia Vyama vyao vya Ushirika wanahimizwa kuainisha na kuwasilisha mahitaji ya pembejeo mapema kwa Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA) ili waweze kununua mbolea wanazohitaji kwa wakati kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Mbolea kwa pamoja ambao katika mwaka 2020, wakulima wa Mikoa kama Iringa, Mbeya waliingiza mbolea moja kwa moja kutoka kiwandani katika nchi za Morocco na China. Aidha, Serikali inaendelea kuboresha mifumo ya uzalishaji na uagizaji na uthibiti wa mbegu bora na viuatilifu nchini ikiwemo kuhamasisha uzalishaji wa pembejeo hizo ndani ya nchi ili kukidhi mahitaji ya upatikanaji kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara wa pembejeo kujenga maghala makubwa kwa ajili ya kuhifadhi pembejeo hususan katika maeneo yenye mahitaji makubwa ili kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati wote. Utekelezaji wa mpango huu ulianza mwaka 2019 ambapo Wadau wa Maendeleo wakiwemo African Fertilizer and Agribusiness Partnership waliwezesha ujenzi wa jumla ya maghala 12 mwaka 2019 yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya tani za mbolea 50,000 katika Mikoa ya Kilimanjaro, Morogoro, Arusha, Iringa, Rukwa, Njombe na Songwe. Aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha pembejeo nchini ili kuongeza upatikanaji wake kwa wakati na bei nafuu kwa wakulima.
MHE. AIDA J. KHENANI Aliuliza:-

Utaratibu unaotumika sasa kuwakopesha matrekta wakulima unawasababishia hasara kwa kuwa wanatozwa riba kubwa: -

Je, kwa nini Serikali isibadili utaratibu huo ili kuleta tija?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya pembejeo na zana za kilimo ikiwemo matrekta kwa wakulima hutolewa kupitia mifumo mbalimbali. Mojawapo ya mifumo hiyo ni kupitia Sekta Binafsi ambapo kampuni zinazofanya biashara ya pembejeo na zana za kilimo hutoa mikopo kwa wakulima mmoja mmoja ama kupitia vikundi. Aidha, mfumo mwingine ni kupitia Taasisi za Serikali kama Mfuko wa Taifa wa Pembejeo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ambazo hutoa mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa wakulima ukilinganisha na kampuni binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwepo kwa mifumo hiyo, baadhi ya wakulima hushindwa kupata mikopo ya pembejeo kutokana na riba kubwa na masharti mengine yanayotolewa na watoa huduma. Kutokana na changamoto hizo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeanza kuwatambua watoa huduma wote wanaotoa mikopo ya pembejeo za kilimo ikiwemo matrekta ili kujua aina ya huduma na mikopo inayotolewa kwa wakulima pamoja na riba wanazotoza. Hatua hiyo itasaidia kutambua changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi ikiwemo kupunguza riba, kuweka utaratibu unaomuwezesha mkulima kurejesha mkopo kulingana na mapato ya mkulima kwa msimu wa kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za Kilimo pamoja na Benki ya Maendeleo ya Kilimo zinaendelea kutoa mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa wakulima, ambapo zinatoza mikopo ya zana za kilimo ikiwemo matrekta kwa wastani wa riba ya asilimia 6 hadi 10 kulingana na aina ya mkopo. Lengo la jitihada hizo ni kuwawezesha wakulima kupata zana bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji na tija. Katika mwaka 2020/2021 hadi Februari Mfuko wa Taifa wa Pembejeo umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 959,500,000. Kati ya mikopo hiyo, mikopo ya matrekta makubwa 16 yenye thamani ya shilingi 729,000,000.00 imetolewa. Aidha, Benki ya Maendeleo ya Kilimo imetoa mikopo ya matrekta makubwa 62 yenye thamani ya shilingi bilioni 5.6.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ili kuongeza matumizi ya zana bora za kilimo na kuongeza tija katika kilimo, Serikali imepanga kuhamasisha Sekta Binafsi kuanzisha vituo vya kutoa huduma za kukodisha zana za kilimo kwa lengo la kusogeza huduma za upatikanaji wa zana za kilimo kwa wakulima na kupunguza matumizi ya jembe la mkono kutoka asilimia 53 ya sasa hadi kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
MHE. AIDA J. KHENANI atauliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza changamoto ya maji katika Wilaya ya Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenan, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika; hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Nkasi ni wastani wa asilimia 48. Katika kutatua changamoto ya huduma ya maji, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Wilaya ya Nkasi imeendelea na ujenzi wa jumla ya miradi 12 ambayo ni Kirando, Kabwe, Kisula, Isale, Mpasa, Matala, Kantawa, Sintali, Chonga, Kate, Mtambila na Katongolo ambapo itakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mradi wa uchimbaji wa visima virefu sita umekamilika katika vijiji vya Ntumbila, Kachehe, Itindi, Lyazumbi, Nkomo II na Milundikwa. Ujenzi wa miundombinu ya usambazaji utafanyika katika mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo utahusisha matanki matatu ya maji yenye ukubwa wa lita 90,000 na lita 45,000 na vituo vya kuchotea maji 23.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mji wa Namanyere, Serikali inaendelea na uboreshaji wa huduma ya maji kwa kutumia chanzo cha maji cha bwawa la Mfili ambapo kazi mbalimbali zitafanyika ikiwemo ufungaji wa pampu mbili katika bwawa la Mfili, ulazaji wa bomba kuu umbali wa kilomita 3.9, ulazaji wa mabomba na ujenzi wa tanki la lita 500,000 la kuhifadhi maji. Kazi hizo mradi zinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai, 2021.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, kwa nini wazazi wanachangishwa michango ya kuchangia elimu wakati Serikali inasema Elimu kwa Shule ya Msingi na Sekondari ni bure?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Waraka wa Elimu Na.5 wa mwaka 2015 iliamua kutoa elimumsingi bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne. Uamuzi huo ulijielekeza katika kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 ambayo ina lengo la kuhakikisha watoto wote wa Kitanzania wenye rika la elimumsingi wanapata elimu bila kikwazo chochote ikiwemo ada au michango. Aidha, Serikali ilitoa Waraka wa Elimu Na.3 wa mwaka 2016 kuhusu utekelezaji wa elimumsingi bila malipo. Waraka huu unafafanua maana ya elimumsingi na kuainisha majukumu ya kila kundi linalohusika katika utoaji wa elimumsingi bila malipo na kuweka utaratibu wa utekelezaji wake.

Mheshimiwa Spika, majukumu ya jamii na wananchi kuhusu michango yamebainishwa kwenye Waraka wa Elimu Na.3 wa mwaka 2016. Waraka unaeleza kuwa Kamati za Shule au Bodi za Shule zitashirikisha jamii katika maazimio na maamuzi ya masuala mbalimbali yanayohusu maslahi na maendeleo ya shule hususan uchangiaji wa hiari na kuwasilisha maamuzi hayo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ili kupata kibali. Hivyo, uchangiaji katika elimu unaoruhusiwa ni wa hiari na hauhusishi wanafunzi kuzuiwa kuhudhuria masomo.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, Serikali imesaidia mikopo kwa vikundi vingapi vya wavuvi Wilaya ya Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025 Ibara ya 43(h) inaelekeza Serikali ihamasishe uanzishaji na uimarishaji wa vikundi na Vyama vya Ushirika vya Msingi vya Wavuvi wadogo kwa lengo la kuwapatia mitaji, ujuzi na vifaa pamoja na zana za uvuvi. Katika kutekeleza ahadi hiyo, Serikali imefanya yafuatayo: -

(a) Imeendelea kuhamasisha wavuvi kujiunga kwenye Vyama vya Ushirika vya Wavuvi ambapo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya wadau 16,733 kutoka halmashauri 21 nchini wamepatiwa mafunzo hayo ikiwemo halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ambapo hadi sasa jumla ya Vyama vya Ushirika 146 vya Wavuvi vimeundwa.

(b) Serikali imeendelea kuwezesha wavuvi kupitia Vyama vya Ushirika vya Wavuvi kwa kuvipatia injini za boti, ambapo kwa sasa Serikali ipo kwenye mchakato wa kuvipatia injini za kupachika Vyama vya Ushirika vya Wavuvi kumi kikiwemo Chama cha Ushirika Kabwe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, ahsante.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza changamoto ya maji katika Jimbo la Nkasi Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama katika Wilaya ya Nkasi ni wastani wa asilimia 52.2. Katika kutatua changamoto ya huduma ya majisafi na salama katika Jimbo la Nkasi Kaskazini, Serikali imeendelea na utekelezaji wa miradi minne ambayo ni Kirando, Namanyere, Matala na Katongolo. Miradi hii imepangiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba, 2021.

Mheshimiwa Spika, aidha, kuanzia mwezi Januari, 2022 Serikali itaanza utekelezaji wa miradi ya maji katika Vijiji vya Korongwe, Lyazumbi, Masolo, Mpata, Isale na Kakoma na utekelezaji wa miradi hiyo umepangwa kukamilika mwezi Oktoba, 2022. Kukamilika kwa miradi hiyo, kutawanufaisha wananchi wapatao takribani 97,000.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mji wa Namanyere, Serikali inaendelea na uboreshaji wa huduma ya majisafi na salama kwa kutumia chanzo cha maji cha Bwawa la Mfili. Ujenzi wa mradi huo unahusisha kazi za ujenzi wa chanzo, ufungaji wa pampu mbili zenye uwezo wa kusukuma lita 80,000 za maji kwa saa, ulazaji wa bomba kuu kilometa 3.9, ulazaji wa bomba la kusambaza maji kilometa 6.4, ujenzi wa tanki la lita 500,000. Ujenzi wa mradi huo umepangwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba, 2021.

Mheshimiwa Spika, aidha, kupitia mradi wa Maziwa Makuu wa kutumia Ziwa Tanganyika, Serikali imekamilisha usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni ya kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Tanganyika. Kupitia mradi huo, vijiji 32 vya Halmashauri ya Nkasi vinatarajiwa kunufaika.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya Polisi katika maeneo ya mpakani wilaya ya Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya mpakani mwambao mwa Ziwa Tanganyika katika Wilaya ya Nkasi kuna vituo vitano vya Polisi vya daraja C, ambavyo ni kituo cha Wampembe, kituo cha Namansi, Kipili, Kilando na Kabwe. Vituo hivi vinatoa huduma kwa wananchi kwa saa 24. Pia kuna tarajiwa kujengwa kituo kingine cha Polisi cha Daraja C katika eneo la Mpasa. Vituo vyote hivyo vinakidhi mahitaji ya kutoa huduma katika eneo la mpakani kando ya ziwa Tanganyika katika Wilaya ya Nkasi. Aidha, Serikali imepanga kuimarisha huduma kwenye vituo hivyo kwa kuvipatia usafiri stahiki hatua kwa hatua kulingana na upatikanaji wa fedha. Nakushukuru.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka usafiri wa majini Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. FREDY A. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali katika bajeti ya mwaka huu wa 2022/2023 imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa meli mbili mpya, chelezo na ukarabati wa meli za Mv Liemba na MT. Sangara ili kuboresha hali ya usafirishaji katika Ziwa Tanganyika. Kati ya meli zitakazojengwa, moja ni ya kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo na ya pili ni ya kubeba mabehewa na malori yenye uzito wa tani 3,000.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) inaendelea na mchakato wa ununuzi wa Wakandarasi wa kutekeleza miradi hiyo.
MHE. VINCENT P. MBOGO K.n.y. MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuwapatia Wananchi maeneo ya kulima kutoka kwenye mapori na Hifadhi ambazo hazina wanyama kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nkasi ni mojawapo ya wilaya zitakazonufaika na uamuzi wa Baraza la Mawaziri wa kumega maeneo ya hifadhi kwa ajili ya shughuli za wananchi ikiwemo kilimo, ufugaji na makazi. Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi unatakiwa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya hekta 10,828 zimependekezwa kumegwa kutoka Msitu wa Hifadhi ya Lowasi unaopakana na Pori la Akiba la Lwafi kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji na makazi.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itasambaza maji katika Wilaya ya Nkasi kutoka Ziwa Tanganyika?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kutumia Maziwa Makuu kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio karibu na vyanzo hivyo ikiwemo wananchi wa Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imeanza kutumia Ziwa Tanganyika kuwanufaisha wananchi wa Wilaya ya Nkasi ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imekamilisha miradi ya maji ya Kirando, Kamwanda, Mkinga na mradi wa maji Kabwe.

Kukamilika kwa miradi hiyo kumeboresha hali ya upatikanaji wa huduma maji Wilayani Nkasi kutoka asilimia 47 hadi asilimia 53.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali itaendelea na usanifu wa miradi ya maji kupitia chanzo cha Ziwa Tanganyika kwenye vijiji 10 vya Kilambo, Kala na Tundu Kata ya Kala, Izinga, Mwinza na Wampembe Kata ya Wampembe, Ninde, Kisambala na Namasi Kata ya Ninde na Mandakerenge Kata ya Kipili. Vilevile, katika mwaka 2022/2023, usanifu utafanyika kwa ajili ya kupeleka maji Mji wa Namanyere pamoja na vijiji vilivyoko kilomita 12 kila upande ambapo bomba kuu litapita. Usanifu huo unatarajiwa kukamilika katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/2023 na baadaye ujenzi utaendelea.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, kwa nini wanufaika wa TASAF wasilipwe mkononi badala ya kupewa kwa njia ya simu na benki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu Swali lililoulizwa na Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwaka 2019 Serikali ilifanya majaribio ya mfumo wa kieletroniki wa malipo kwa walengwa katika mamlaka za utekelezaji 19. Baada ya majaribio, mwaka 2020 mfumo wa malipo kwa njia ya kielektroniki ulipitishwa rasmi na walengwa kuanza kutumia mfumo huo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inakiri kutokea changamoto katika baadhi ya maeneo ya utekelezaji. Hivyo utaratibu wa malipo kwa sasa upo katika njia tatu; kwa njia ya simu, akaunti ya benki na njia ya malipo ya fedha taslimu.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huu ni uchaguzi wa mnufaika mwenyewe atumie njia gani kadri ya mazingira yake. Aidha, naomba kutoa rai kwa Mheshimiwa Mbunge tusaidiane kuelimisha walengwa juu ya njia hizi kuu tatu za malipo.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia Wavuvi wa Ziwa Tanganyika zana za uvuvi za kisasa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto za wavuvi zilizopo ikiwemo ukosefu wa zana za kisasa za uvuvi. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga fedha kwenye programu maalum ya mikopo wenye masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kupitia dirisha la extended credit facilities (ECF) kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi boti za kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza mpango huo, Serikali inakamilisha taratibu za kutoa boti 158 kwa mkopo kupitia Benki ya Kilimo (TADB) kwa Vyama vya Ushirika 45, Vikundi vya Wavuvi 71 na watu binafsi 43. Aidha, katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika jumla ya Vyama vya Ushirika vinne, Vikundi vinne na watu binafsi watano wanatarajiwa kunufaika na mikopo wa boti hizo usiokuwa na riba.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali kupitia TADB inatoa mitaji kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ili kuboresha shughuli zao za maendeleo. Aidha, Serikali inawahimiza wavuvi kujiunga katika vikundi na kuanzisha vyama vya ushirika vya msingi, SACCOS na VICOBA ili waweze kukopesheka na kuweza kununua zana na vyombo bora vya uvuvi.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa semina elekezi kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya mara kwa mara kuhusu utawala bora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa mafunzo elekezi kwa viongozi wa ngazi mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeendelea kutoa semina elekezi kwa viongozi wanaoteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Katika kipindi cha mwezi Februari hadi Agosti, 2023, Serikali ilitoa mafunzo elekezi kwa viongozi wa ngazi ya Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala wa Wilaya ambapo agenda moja wapo ilikuwa ni ya utawala bora.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, ni kwa nini Wananchi wanaotumia Bima ya Afya wanalalamika kuhusu huduma wanazopatiwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umekuwa ni nguzo muhimu katika uboreshaji wa huduma za Afya Nchini ambapo Taasisi Binafsi za Afya pamoja na Vituo vya Huduma za Afya vya Serikali vimeonekana kutoweza kujiendesha bila uwepo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kutokana na Watanzania wenye uwezo wa kulipa fedha taslimu kuwa wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 70 ya mapato ya vituo vya huduma za Afya vya Serikali pamoja na binafsi vinategemea Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri hayo kumekuwepo na changamoto za kimiongozo ambapo dawa chache zilikuwa zinatolewa katika zahanati na vituo vya Afya. Serikali imefanya maboresho kwa kuongeza idadi ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba ambapo kwa ngazi ya zahanati imeongeza kutoka aina 254 hadi 451 na kwa ngazi ya vituo vya Afya toka aina 414 hadi 828.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, kwa nini Vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo mpakani mwa Ziwa Tanganyika havina Usafiri wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mahitaji ya vyombo vya usafiri vya uhakika katika kudhibiti uhalifu maeneo ya mpakani mwa ziwa Tanganyika. Kwa dhamira ya kuimarisha upatikanaji wa usafiri, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kununulia magari na pikipiki ambapo mchakato unaendelea. Pindi yatakapofika, pikipiki na magari hayo yatagawiwa wilaya zote zikiwemo zilizopo mpakani mwa ziwa Tanganyika. Pia katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.5 za kununulia boti 10 kwa ajili ya doria baharini na kwenye maziwa. Baada ya kununuliwa, boti hizo zitagawiwa kwenye maeneo yenye changamoto za uhalifu ikiwemo Ziwa Tanganyika, nashukuru.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: -

Je, mchakato wa mradi wa kutoa maji Ziwa Tanganyika umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kutumia chanzo cha Ziwa Tanganyika kuwapatia wananchi wa Mkoa wa Rukwa huduma ya majisafi na salama. Usanifu kwa ajili ya kuwapatia wananchi maji katika vijiji 40 vya pembezoni mwa ziwa umekamilika na tayari wananchi kwenye vijiji tisa wanapata maji na miradi inaendelea kutekelezwa kwenye Vijiji vilivyobaki hatua kwa hatua. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itaajiri mtaalam mshauri kwa ajili ya kufanya usanifu wa miradi ya maji kupitia chanzo cha Ziwa Tanganyika ili kunufaisha maeneo mengi zaidi Mkoani Rukwa.
MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga soko la kisasa la mazao yatokanayo na uvuvi Wilayani Nkasi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI, alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenani, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kujenga na kuboresha miundombinu ya uvuvi ikiwemo mialo na masoko katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa upande wa mwambao wa Ziwa Tanganyika unaojumuisha Wilaya ya Nkasi shughuli za uvuvi zinafanyika katika mialo ipatayo 239. Kati ya mialo hiyo, Serikali iliboresha mialo minne ya Kibirizi, Ikola, Muyobozi na Kirando katika Wilaya ya Nkasi ambapo Mheshimiwa Mbunge anawakilisha. Aidha, Serikali imejenga na kuboresha masoko mawili ya samaki ya Kibirizi na Kasanga Wilayani Sumbawanga. Pia kwa sasa Serikali inaendelea na jitihada za kuupandisha hadhi mwalo wa Kirando uliopo Wilaya ya Nkasi ili uweze kufikia hadhi ya kuwa soko la kisasa la samaki na mazao ya uvuvi. Ahsante.