Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zainabu Nuhu Mwamwindi (14 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi jioni ya leo niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, tingatinga letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba nianze kama Waheshimiwa Wabunge wenzangu walivyoanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mungu mwenye rehema ambaye ametuwezesha leo na mimi Zainabu Mwamwindi kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano nawakiilisha wazazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Ni hotuba ambayo ilikuwa ina mashiko mazuri na makubwa sana, ni hotuba ambayo ilisheheni kila kitu na ni hotuba ambayo siyo tu kwamba sisi Wabunge wa CCM ndiyo tunaipongeza au tunasema kwamba ilikuwa ni hotuba nzuri bali ndiyo ukweli uliojitokeza siku Mheshimiwa Rais alipokuja kutufungulia au kutuzindulia Bunge letu la Jamhuri ya Muungano. Hotuba hii siyo sisi tu, hotuba hii kuanzia wale wengi wanaoishi vijijini waliipongeza sana. Pia wasomi baadhi yao waliipongeza hotuba hii lakini na wale ambao wanaishi mjini nao pia waliipongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwenye macho haambiwi tizama na mwenye masikio haambiwi sikia, Mheshimiwa Magufuli Watanzania kumchagua hatukufanya kosa. Pia niseme tu kwamba Watanzania kukichagua Chama cha Mapinduzi ndiyo usahihi wenyewe, ni chama
ambacho wamekiona kina sera nzuri, Ilani inayotekelezeka lakini pia ndiyo Chama kinachosema ukweli, hilo ni sahihi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Katika hotuba yake, aliongea kwa uchungu na Wabunge wengi wamechangia sina sababu ya kurudia lakini niseme yako mambo muhimu ambayo alikuwa ameyakazia sana, alikazia sana suala la maji.
Kule Tosamaganga, Kata ya Kalenga ambayo ina vijiji vitatu na vitongoji sita ule mradi wa maji ni wa mwaka 1974 miundombinu imechakaa. Nitoe ombi kwa Serikali ya CCM, Serikali sikivu, Serikali ambayo ina huruma na wananchi isaidie mradi huu. Tosamaganga ni sehemu ambayo imetoa viongozi wengi sana ambao wanalitumikia taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1974 wakati mradi wa maji unawekwa kule Tosamaganga ulizingatia uwepo wa watu waliokuwepo kwa wakati ule. Sasa Tosamaganga imekuwa na idadi kubwa sana ya watu hivyo maji hayatoshelezi kutokana na wananchi kuongezeka kwa kiwango kikubwa. Tosamaganga pia ina shule nyingi sana ambazo watoto wanasoma pale. Imezungukwa na mito lakini kuna mlima mkubwa, watoto wanashuka kwenda kufuata maji kule wengine wanatumbukia. Hivi karibuni amekufa mtoto mmoja wa kiume anaitwa Onesmo kwa sababu alikuwa amekwenda kufua siku ya Jumamosi, kwa bahati mbaya nguo yake ikateleza kwenye maji wakati anaifuatilia akazama kwenye maji. Kwa hiyo, bomba za Tosamaganga pamoja na vijiji vyake maji hayatoki kabisa. Kwa hiyo, namuomba Waziri wa Maji uiangalie Tosamaganga kwa jicho la huruma, maji yale hayatoshelezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikuombe Mheshimiwa Waziri, kule Unyangwila na Irangi, wale watu wameanza wao kwa nguvu zao kuchimba mtaro kwa ajili ya kutafuta maji na wameshafikisha kilomita tatu na nusu lakini hawajui watapata wapi mabomba na maji kwenda
kuyafikia ni kilomita sita na nusu. Mheshimiwa Waziri nakuomba katika ufalme wako iangalie Tosamaganga na Kalenga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati akiwa Mbunge Marehemu Dkt. William Mgimwa, alikuwa ameahidi kupeleka gari la wagonjwa katika Hospitali ya Ipamba, ni Hospitali Teule ya Wilaya ya Iringa. Hospitali ile ni kubwa kwani inatoa huduma kwa wananchi wanaotoka maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Iringa na pengine hata Mikoa ya jirani lakini cha kusikitisha hakuna gari la wagonjwa. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Afya, hebu tazama Hospitali Teule ya Ipamba ili waweze kupatiwa gari la wagonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara yangu ya kwanza leo nimeshuhudia Mbunge akilidanganya Bunge Tukufu. Mbunge wa Iringa Mjini amesimama hapa kwa kujiamini kabisa, akizungumzia habari ya Iringa Mjini yeye kama mwakilishi wa wananchi wa Iringa.
Amezungumzia mradi wa maji wa Iringa Mjini na kujidai kwamba Iringa Mjini maji yanapatikana kwa kiwango cha asilimia 98 lakini akasema Iringa kuna barabara za lami, akaenda mbali zaidi akasema taa Iringa Mjini zinawaka bila shida barabarani. Mheshimiwa Mbunge
amelidanganya Bunge lako Tukufu. Naomba tumwogope Mungu, Mchungaji Msingwa ni Mchungaji na nafikiri ana hofu ya Mungu lakini anapozungumzia vitu hata anaposema tunajikomba ndiyo tuna haki sisi tumsifu Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Iringa Mjini mpaka sasa maji ni asilimia 95, ni mradi ambao ulianzishwa na Mheshimiwa Monica Mbega wakati wa kipindi chake na hata wakati wa uzinduzi wa mradi huu alikuja Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne. Mbunge wa Iringa Mjini, Mheshimiwa Peter Msingwa hakushiriki katika uzinduzi wa mradi huu kwa sababu mradi huu alikuwa hautaki na hakuukubali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili la barabara vilevile Mheshimiwa Msigwa amezikuta barabara za lami zikiwa tayari zipo. Ni mradi uliotoka Serikali Kuu na siyo yeye. Taa za barabarani ni package ya mradi wa barabara…
NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa Mwamwindi naomba ukae.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. ZAINAB N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu na Makatibu wote wa Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni barabara itokayo Iringa Mjini kwenda Ruaha National Park. Barabara hii ni muhimu sana kwa watalii, naomba ipewe kipaumbele kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, natanguliza shukrani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZAINAB N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kukushukuru wewe mwenyewe binafsi kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia leo katika Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, ambaye ameniwezesha leo nami niweze kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli; nampongeza Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu; nampongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa na timu yake yote ya Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo wanatukonga nyoyo zetu Watanzania, wametuonesha umahiri wao na kwamba wana ari kubwa ya kulitumikia Taifa na wananchi wote wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna moja au nyingine, naitumia nafasi hii pia kuwashukuru wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wamechangia mimi uwepo wangu au wamerahisisha mimi Zainab Mwamwindi kuwepo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Nawashukuru kwa namna ya pekee na nasema Mungu awabariki sana, ahsanteni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inahitaji kwenda kwa kasi na ari kubwa. Tunasema tunahitaji Tanzania yenye viwanda. Kilimo kinatajwa kama uti wa mgongo wa nchi yetu na kinatajwa kwa sababu ya kwamba hakuna hata mmoja kati yetu Wabunge wa Jamhuri ya Muungano ambaye hatujui kwamba bila kilimo nchi haitasonga mbele. Ni lazima tulime na tuweze kupata mafanikio mazuri, lakini pia ndoto yetu ya kuwa na viwanda vingi itatokana na uzalishaji mali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natokea Mkoa wa Iringa. Mkoa wa Iringa kuna Kiwanda kikubwa cha Karatasi cha Mgololo. Kiwanda kile kinazalisha karatasi, lakini namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho yake, atueleze au awaeleze wananchi wa Tanzania kwamba ni kwa nini Kiwanda cha Mgololo kinachotengeneza karatasi soko lake halipo lakini pia karatasi zake hazipatikani sokoni na hata kama zitapatikana, karatasi zake huwa ghali sana? Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Mwijage naomba atusaidie sisi wananchi, ni kwa nini Tanzania hii tunatengeneza karatasi lakini kwa bahati mbaya sana karatasi zile zikipatikana bei inakuwa ghali kuliko zile ambazo zinaingizwa kutoka nchi za nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie suala la kinu cha kusindika au kusaga sembe kilichoko Manispaa ya Iringa. Ni kiwanda ambacho kinasaga sembe. Inawezekana kikawa ni kiwanda pacha, kinahusiana na kilimo vile vile. Kiwanda kile kilikuwa kinafanya kazi vizuri sana huko nyuma wakati wa NMC lakini mara baada ya Shirika la NMC kufa, kiwanda kile sasa kimekuwa hakifanyi kazi kama ambavyo inatakiwa. Pia kuna vijana wetu na akinamama pia wapo ambao nao walikuwa wanapata ajira na wengi wao wakiwa ni akinamama ambao ndio wanaotunza familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana, naomba Mheshimiwa Waziri, atusaidie katika kiwanda hiki, Serikali iweke mkono wake kwa asilimia mia moja ili iweze kuwakomboa wananchi wa Mkoa wa Iringa ambapo wananchi wa Mkoa wa Iringa hasa ni wakulima wa mazao ya mahindi, wanazalisha mahindi kwa kiwango kikubwa sana, lakini mara nyingine tunakosa soko la kupeleka mahindi, tukauze wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, Serikali itie mkono wake kwa asilimia mia moja katika kiwanda kile ili tuweze kukuza ajira kwa vijana wetu, lakini pia wakulima wa Mkoa wa Iringa na mikoa jirani waweze kunufaika na kiwanda kile kwa kuuza mahindi yao pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mama. Vazi la mwanamke yeyote wa Kitanzania ni Kanga. Namwomba Waziri wa Viwanda atusaidie sisi wanawake wenye maumbile kama mimi, tumekuwa sasa hatuvai kanga, kwa sababu Kanga zinazidi kuwa ndogo siku hadi siku na akinamama wamenituma nije niseme katika Bunge lako hili. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri, kanga zilizopo sasa zinatosha kuvaa wasichana wadogo na Tanzania hii wanawake wameshiba, wako vizuri, wanahitaji kuvaa kanga wapendeze watoke katika shughuli mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, hilo aliwekee kipaumbele sana maana wanawake ndiyo jeshi kubwa na tegemeo la Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile ni mara yangu ya kwanza leo kuchangia, naomba kusema naunga mkono hoja ya Waziri wa Viwanda na Biashara. Nasema ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inahitaji kwenda mbele kwa kasi. Ni jambo linalofahamika duniani kote kuwa tofauti muhimu ya nchi tajiri na masikini ni uzalishaji bidhaa za viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kimetajwa kuwa ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu; kilimo hakiwezi kustawi bila ya viwanda. Wakati Serikali imelivalia njuga suala la viwanda hapa nchini, naomba kuishauri Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kutazama nyuma wapi tulikwama kama Taifa na wapi tulipo na changamoto ipi tunazokabiliana nazo. Kwa mfano, mimi nimetoka Iringa ambako kuna kiwanda kikubwa cha karatasi kilichopo Mgololo Wilayani Mufindi. Namwomba Waziri wakati wa majumuisho anisaidie kuwaeleza Watanzania, ziko wapi karatasi za Mgololo katika soko? Kwanini zikipatikana bei yake huwa ghali kuliko karatasi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinu cha kusaga unga Iringa Mjini kilikuwa chanzo muhimu cha ajira na soko la uhakika la zao la mahindi Mkoani Iringa na mikoa jirani. Mheshimiwa Waziri pamoja na kuwa na ulinzi, kinu hicho kipo katika sekta pacha ya kilimo na viwanda, tunaiomba na kuishauri Serikali kuhakikisha kuwa kinu hicho kiwe katika asilimia mia moja ya uzalishaji ili kukuza ajira na uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake amebainisha kuwa Sekta ya Viwanda ni msingi wa maendeleo wa Sekta ya Kilimo umetueleza kuwa asilimia 99.15 ya viwanda vyote nchini ni viwanda vidogo sana na viwanda vidogo Iringa kama ilivyo baadhi ya Mikoa nchini kama vile Tanga, Morogoro na kwingineko, kuna uzalishaji mkubwa wa matunda ambayo mengi huishia kuoza mashambani kwa kukosekana kwa viwanda vidogo vya kati katika maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kuhusishwa kwa viwanda vidogo hasa katika maeneo ya uzalishaji ni ukombozi mkubwa kwa wakulima ambao wengi wao ni wanawake. Ufufuaji na uanzishaji wa viwanda utakuwa na maana endapo Wizara husika itaweka vipaumbele, kwani mwisho wa siku tunachotaraji ni kuwepo kwa viwanda vyenye tija. Tunapofufua kiwanda cha mbolea tutakuza ajira na kupunguza gharama za pembejeo kwa wakulima na kuongeza uzalishaji mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiona ari na hamasa kubwa aliyonayo Mheshimiwa Waziri ya kuhakikisha kuwa Tanzania ya viwanda inawezekana. Wanawake wa Tanzania vazi lao ni khanga, naomba kushauri kwamba kifufuliwe Kiwanda cha Mutex na Urafiki.
Viwanda vilivyopo vimesababisha wanawake wengi sasa hawavai khanga kwa sababu ukubwa wa khanga kiurefu na upana ni mdogo sana. Namtakia kila la kheri Mheshimiwa Waziri na timu yake Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyeniwezesha na kunipa afya njema na uzima wa kuniwezesha leo hii nichangie kwa maandishi katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya utalii ni moja ya sekta muhimu sana na kwa hakika ni sekta ambayo ikipewa msukumo wa nafasi ya kipekee, italiongezea Taifa letu fedha nyingi. Mbuga zetu za hifadhi ambazo ni vivutio vya watalii zinahitaji kuwekewa mazingira mazuri ambayo yatawavutia watalii, naomba nitoe mifano miwili ya mbuga za Ruaha na Saadani, barabara ya kutoka Iringa Mjini kwenda Mbuga ya Ruaha siyo ya kiwango cha lami, na vivyo hivyo barabara itokayo Tanga kwenda Pangani hadi Saadani ni mbuga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii naiomba Serikali iangalie kwa jicho la kipekee kama biashara nyingine zilivyo na ushindani, Serikali iongeze kasi katika kuutangaza utalii wetu. Bodi ya Utalii ishirikiane na wadau mbalimbali wa sekta binafsi kufanya jitihada hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, kwa hotuba nzuri yenye kuonesha mwelekeo, nampongeza pia Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara na nawatakia kila la kheri, wasonge mbele na kasi hii ya hapa kazi tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja mia kwa mia.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali yangu kwa jitihada inazoendelea kuzifanya katika kuboresha sekta ya afya nchini. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa utendaji wake mzuri uliotukuka kwa kuisimamia vizuri Ilani ya CCM. Nampongeza pia Mheshimiwa Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na Mawaziri wote wakishirikiana na watendaji, wanafanya na kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake Dkt. Hamisi Kigwangalla nawapongeza sana kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kutekeleza majukumu yao katika Wizara hii, hongereni sana.

Hata hivyo Watanzania wengi zaidi ya nusu ya wakazi wote nchini wanaishi vijijini. Hivyo basi tunapoimarisha huduma za afya katika maeneo vijijini tutawanusuru maisha ya watu wengi ambao ndio nguvu kazi ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuangali ikama ya watumishi wa sekta ya afya kwa lengo la kuondoa mlundikano wa madaktari na wahudumu wengine wa afya katika miji mikubwa na kuwapeleka maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna zahanati ambazo zikijengewa uwezo kama vile wa vifaa, majengo na wataalam zitapunguza mlundikano katika hospitali za Wilaya na Mikoa. Moja ya zahanati hizo ni zahanati ya Ulanga iliyoko Wilaya ya Iringa, Mkoa wa Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Waziri binti yangu mchapakazi, mbunifu na msikivu, uje kuitembelea zahanati hii iliyoko Kalenga ambayo ipo katika hali mbaya sana. Uchakavu wa majengo, miundombinu kama nyumba za watumishi, hata chumba cha wazazi, inasikitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie kwa kuipongeza tena Wizara kwa kazi kubwa ikiwemo kuikarabati Hospitali ya Mkoa wa Iringa na kuipandisha hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa, ila nashauri tena Wizara ikae na Wizara ya Mambo ya Ndani ili kurahisisha upanuzi wa hospitali hiyo kwa kuondoa Gereza la Iringa Mjini katika eneo lilipo hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuwa na afya njema na kushiriki katika Mkutano huu wa Saba wa Bunge la Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimpongeze Spika, Mheshimiwa Job Ndugai, Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashililah, Wenyeviti wa Bunge na watendaji wote wa Bunge kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa pamoja na Baraza lote la Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kuwaletea maendeleo wananchi katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Waziri, Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, Naibu Waziri, Mheshimiwa Injinia Ramo Makani na watendaji wote wa Wizara hii, mfano, katika kupambana na majangili katika hifadhi zetu, kuendelea kutatua migogoro kati ya hifadhi na vijiji vilivyo jirani na hifadhi na kutangaza utalii wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyoko umbali wa kilometa 130 kutoka Mjini Iringa ina sifa za kipekee kuliko mbuga zote nchini na katika Bara la Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sifa hii bado haijatoa tija inayostahili kwa Taifa. Miundombinu hasa barabara itokayo Iringa Mjini siyo rafiki kwa watalii wa ndani na nje ya nchi. Ujenzi wa barabara ya lami kutoka Iringa Mjini kuelekea mbugani hadi sasa uko katika kilometa zisizozidi 15 kutoka Iringa Mjini. Siyo rahisi kwa watalii wengi kuvutiwa na safari ya kilometa 115 katika barabara yenye vumbi hivyo tunakosa mapato mengi ambayo yangeweza kupatikana kwa kukosa wageni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, tunalo jengo la kumbukumbu ya Chifu Mkwawa (Mtwa) liko umbali usiozidi kilometa 3 kutoka Kijijini Kalenga, njia inayoelekea katika kumbukumbu hii haina lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, iboreshe uwanja wa ndege ili ndege kubwa na ndogo ziweze kutua na kuruka jambo ambalo litavutia watalii wengi. Aidha, ujenzi wa barabara ya lami kwenda Ruaha National Park uharakishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba TANAPA iendelee kusaidia maendeleo hasa katika maeneo ambayo vivutio vya utalii vinakopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi niungane na wengine katika kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayoendelea kuifanya. Nampongeza sana Mheshimiwa Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Injinia Stella Manyanya kwa hotuba nzuri ya Wizara hii, pamoja na watendaji wote wa Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumpongeza sana Rais wangu wa Awamu ya Tano Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kuleta mfumo wa elimu bila malipo. Mfumo wa elimu bila malipo umewakomboa wengi hasa waishio vijijini na kuongeza idadi ya watoto kupata elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Wizara pamoja na kazi nyingi nzuri na mipango ya Wizara inayoendelea, waingie shule ya msingi ya Kipera ambayo ina watoto wasiopungua 70 wanapata elimu maalumu, ni watoto wenye ulemavu na miongoni mwao wapo watoto wenye ulemavu wa ngozi (albinism). Mazingira ya ulinzi wa watoto hawa siyo rafiki, shule ipo pembezoni kabisa, huduma ya maji hakuna, ulinzi hawana, watumishi ni wachache sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii, kumpongeza sana Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako kwa kuipa fedha shule ya msingi ya Kalenga iliyoko Jimbo la Kalenga kiasi cha shilingi 241,000,000 kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo. Shule hiyo kwa hali iliyokuwa ingeleta maafa kwa watoto wanaosoma pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri azipokee salaam toka kwa wananchi wa kijiji cha Kalenga mahali shule ilipo pamoja na vitongoji vyake. Wanatoa shukrani nyingi kwa kupelekewa pesa hizo na mimi kama mdau wa Kalenga nasema ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuwa na afya njema na kushiriki katika Mkutano huu wa Saba wa Bunge la Bajeti. Nampongeza Mheshimiwa Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson; Wenyeviti wa Bunge, Katibu wa Bunge Dkt. Kashililah , pamoja na watendaji wote wa Bunge kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake; Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kasim Majaliwa pamoja na Baraza lote la Mawaziri, kwa kazi kubwa wanayofanya katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana tena sana Mheshimiwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi; Naibu Waziri, Mheshimiwa Angelina Mabula pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa na nzuri sana ya kuendelea kutatua migogoro ya ardhi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ziara aliyoifanya Naibu Waziri Mheshimiwa Angelina Mabula katika Mkoa wa Iringa na kutatua mgogoro uliokuwepo kati ya Manispaa na wananchi waliopo kwa maeneo waliyonunua kwenye Serikali ya Kijiji cha Igumbilo, Kata ya Igumbilo. Nashukuru sana mgogoro uliokuwepo unaelekea kumalizika kwa maelekezo sahihi aliyoyatoa au kuagiza Manispaa itekeleze, wananchi wamepatiwa viwanja katika maeneo yao, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Angelina Mabula. Ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wetu wa Iringa unaendelea kupanuka kwa majengo pamoja na idadi ya watu kuongeza bado ujenzi holela nao unaongezeka, nimwombe Mheshimiwa Waziri, Ndugu yangu Lukuvi atusaidie kupunguza eneo la mipaka ya Manispaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kuzirudisha nyumba za National Housing Serikali Kuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mungu aliyeniwezesha kutoa mchango wangu katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri pamoja na watendaji wote katika Wizara hii kwa kutekeleza vema majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kuishauri Serikali kwa jicho la huruma imtazame mkulima wa zao la mahindi. Mkulima huyu ameteseka sana, amelima kwa taabu lakini anapofika kuuza mahindi yake anapatiwa masharti na kuzuiwa kujitafutia masoko likiwemo la kufanya mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika mambo mawili yanayohusu Wizara hii ya Kilimo kuhusu zao la pareto. Inafahamaika kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu duniani zinazozalisha asilimia 90 ya zao la pareto. Kilimo cha zao hili katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania kimeweza kuwa mkombozi kwa wananchi kiuchumi na kukuza pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Wizara isimamie kwa ukaribu ustawi wa zao hili katika Mikoa inayolima na hasa kufanya tafiti mpya zitakazobainisha maeneo mapya ya uzalishaji na kuongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kukushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi na mimi leo niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Afya, Wizara nyeti, Wizara ambayo kwa kweli imeshika uhai wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Wabunge wenzangu kwa kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna ambavyo amejitoa muhanga kwa ajili ya Watanzania. Pia nimpongeze mama yetu Mama Samia Suluhu na yeye kwa kumsaidia kwa nafasi yake ya Makamu wa Rais. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri na Naibu Mawaziri wote kwa namna ambavyo kwa kweli wanafanya kazi na macho yetu yanaona na masikio tunasikia yale ambayo wamekuwa wanayafanya katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee sana ninaomba nimpongeze sana mwanangu Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Ummy Mwalimu na kweli wewe ni mwalimu, lakini niseme tu nitakuwa sijajitendea haki kama sitakupongeza kwa namna ambavyo kwa kweli umethubutu katika Wizara hii kama mama. Niseme tu kweli kwamba hujatuangusha sisi wanawake wenzio na tunazidi kukutia nguvu kwamba changamoto za kawaida kama binadamu na pale unapokosea Mungu anaona kwamba umekosea kwa bahati mbaya lakini nia na dhamira yako ya kweli katika nafasi hii tunaiona na tuseme tu Mheshimiwa Rais hajakosea kukupa nafasi. Pia nimpongeze Naibu Waziri na pia niwapongeze watendaji wote wa Wizara yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja asilimia mia kwa mia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM) ni mpango ambao umeelekezwa na Serikali kwamba kila kijiji kiwe na zahanati, kila kata iwe na kituo cha afya na kila Wilaya iwe na Hospitali ya Wilaya. Zahanati ya Kalenga kwa yeyote ambaye ameshafika Kalenga, na kwa namna ninavyoifahamu Kalenga zahanati ile ni kongwe, imejengwa kabla ya uhuru na haikujengwa purposely kwamba iwe zahanati kwa ajili ya kutoa huduma ya afya, ilikuwa ni shule ya msingi ambayo mimi kwa umri wangu nimesoma darasa la kwanza mpaka la nne, halafu shule ile ikahamishiwa baada ya Serikali kufuta shule za middle school ikahamia kwenye shule iliyokuwa inaitwa Kalenga Upper Primary School na ikawa zahanati ya kijiji cha Kalenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kalenga ni kijiji ambacho kina historia na ni kijiji ambacho viongozi wetu wakuu akiwemo aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Chifu Adam Sapi Mkwawa amezaliwa pale na amezikwa pale, lakini pia ni kijiji ambacho kina makumbusho ya Taifa letu. Kijiji kile kwa sasa ni kijiji mji na idadi iliyokuwepo wakati ule na sasa, idadi ya watu imeongezeka kuliko mara tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati ile kwanza majengo yake yalifanya kuchapiwa tu, kubadilishwa iwe zahanati lakini haina sifa wala hadhi ya kuitwa zahanati ya kijiji cha Kalenga. Kwa sababu dakika tano kwangu ni chache, mengine nitatoa kwa maandishi, nikuombe Mheshimiwa Waziri mwanangu Ummy ushirikiane na Wizara ya TAMISEMI angalau uitazame kwa jicho la huruma, wananchi wa Kalenga wana utayari wa kujenga kituo cha afya, wana eneo lao ambalo limezidi ekari 12 ambalo halina gharama ya Serikali kulipa fidia lakini pia wapo tayari wao kama wao kutumia nguvu zao kuweza kusimamisha kuanza kujenga pia wanaomba serikali pale watakapokwama iweze kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee sana katika Majimbo magumu ambayo ninayafahamu mimi ni Jimbo la Kilolo. Jimbo la Kilolo kuna shida, wao kutokana na miundombinu ya kwao pale wamekubaliana katika kila kata, vijiji vitatu viunganike vijenge kituo cha afya kimoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyeniwezesha kusimama na kuweza kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Naunga mkono maoni na ushauri uliotolewa na Kamati.

Mheshimiwa Spika, ili tuwe na utalii endelevu lazima tutunze vivutio vyetu. Mkoa wa Iringa ndio kitovu cha utalii katika Nyanda za Juu Kusini. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendeleza utalii kwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Spika, ninatambua mchango mkubwa wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa nchi yetu. Hifadhi ya Ruaha inayopakana na vijiji 21 vinavyofaidika na uhifadhi kupitia Mbomipa. Pamoja na hayo kuna vijiji ambavyo bado ni maskini sana na ndivyo vinavyotumika kwenye ujangili wa wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Rais amekubali kutujengea barabara kwa kiwango cha lami itokayo Iringa kwenda Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye urefu wa kilometa 130, ninaomba kuishauri Serikali kupitia Wizara hii wawe wanatoa elimu ya ujirani mwema, wasaidie kutoa elimu ya ujasiriamali kama ilivyo Hifadhi za Manyara na Ngorongoro ili kuweza kutengeneza soko la bidhaa za asili kwa kuwatengea eneo ili wageni wanapopita kuelekea hifadhi waweze kusimama na kununua bidhaa na wananchi hawa watafaidika moja kwa moja na kuwapunguzia umasikini.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie makumbusho ya Chifu Mkwawa ambayo yameachwa kwa muda mrefu na hivyo kuendelea kupoteza mapato ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kuona umuhimu wa kutembelea makumbusho ya Chifu Mkwawa. Ninaomba yaweze kuendelezwa ili wageni wanaopata nafasi ya kupumzika Iringa Mjini wapate fursa ya kutembelea makumbusho yetu na kuongeza kipato kwa Taifa na pia kuwanufaisha wananchi wa Kalenga.

Mheshimiwa Spika, naomba pia Serikali imalize mgogoro uliopo kati ya familia ya Mkwawa kuhodhi Makumbusho haya ya Taifa.

Mheshimiwa Spika nashukuru, naunga mkono hoja, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ZAINAB N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha na mimi kutoa mchango wangu kwa maandishi katika Wizara hii nyeti ya TAMISEMI. Nianze kwa kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Nampongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kujitoa kwake mhanga kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu kwa namna ambavyo amekuwa anafanya kazi usiku na mchana kumsaidia Mheshimiwa Rais. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri wote pamoja na watendaji wote kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nampongeza sana Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Seleman Jafo pamoja na Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Josephat Kandege na Mheshimiwa Joseph Kakunda wanafanya kazi kweli bila kuwasahau watendaji wote wa Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua na kuzithamini kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kufika kuwaelekeza na kuwaongoza Watanzania katika uchumi utokanao na viwanda. Viwanda ni matokeo ya mambo mengi moja ya mambo yatakayowawezesha Watanzania kuumiliki na kuuendesha uchumi wa viwanda ni elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira bora ya kufundishia na kujifunza ni suala lenye umuhimu wa kipekee kwa wakufunzi na wanafunzi. Nafahamu wakati mwingine rasilimali fedha huwa chache lakini niombe Wizara ya TAMISEMI iangalie kwa jicho la kipekee Shule ya Sekondari ya Kalanga. Shule hii ina uchakavu mkubwa mno wa majengo kiasi ambacho Walimu, wafanyakazi na wanafunzi wakiyaona mawingu yenye dalili ya mvua mawazo yao yote hujielekeza katika kufikaria usalama wao pindi mvua itakaponyesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee niiombe Wizara iinusuru shule hii. Pili, naomba niishauri Serikali katika eneo hili la uimarishaji miundombinu ya shule, Serikali iangalie uwezekano wa kutenga na kutumia fedha nyingi katika mambo machache kwa mwaka husika na kisha kuhamia katika masuala mengine. Nionavyo mimi hali hii itaweza kutatua changamoto nyingi za jambo moja kwa kipindi kimoja cha bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri Jafo apatapo nafasi aje atembelee Shule hii ya Sekondari ya Kalanga iliyopo katika Kijiji cha Kalanga ambayo iko umbali wa kilomita saba tu kutoka Iringa Mjini na itampa fursa pia ya kujifunza mengi ikiwemo utajiri uliolala wa historia ya Wahehe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mchango wangu kwa maandishi katika wizara hii. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wake wote kwa kazi nzuri sana wanayoifanya na kuitendea haki wizara hii ambayo ni muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Prof. Joyce Ndalichako anastahili pongezi kubwa kwani mwenye macho haambiwi tazama na mwenye masikio haambiwi sikia. Changamoto nyingi zilizokuwepo zimepungua kwa kiwango kikubwa lakini pia elimu imeboreka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri na kubwa ambazo zimekuwa zikifanyika bado kuna changamoto ambazo zinaweza kuboreshwa mfano kurudisha michezo, kilimo na mchakamchaka mashuleni haya huko miaka ya nyuma yalikuwepo na matokeo mazuri yalionekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara sasa iandae mfumo mzuri wa kuwaandaa wanafunzi kisaikolojia kwani wanafunzi wengi wanaomaliza akili yao ni kupata ajira ambazo kupatikana si rahisi sana kiasi kwamba akikaa miaka mingi nyumbani bila kupata ajira anakata tamaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba katika mchango nitoe salamu kutoka kwa wananchi wa Kalenga walionituma nimfikishie salamu za kushukuru sana Waziri wa Elimu Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako kwa kuikumbuka shule ya msingi Kongwe ya Kalenga kwa kuwajengea maboma mawili ya madarasa yenye madarasa manne na uzio wa kuizunguka shule na matundu 16 ya vyoo pamoja na kukarabati nyumba za walimu ambazo zilikuwa zimechakaa kabisa na kushindwa kukaliwa na walimu hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu sikivu kuwapatia Wizara ya Elimu pesa yote iliyoombwa katika bajeti yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.