Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Issaay Zacharia Paulo (67 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, nimpongeze sana Mheshimwa Rais na kumuombea kila lililo jema katika maisha yake. Nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na juhudi zake na Baraza la Mawaziri kwa ujumla. (Makofi)Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwatake Wabunge wetu wote tuendeshe siasa za kistaarabu na siasa za utashi mwema. Tumekuja huku Bungeni tukiwa na nia njema ya kuzungumza matatizo wa wananchi wetu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwanza kuipongeza Serikali kwa Mpango wake wa bajeti wa mwaka huu 2016/2017 ni mpango mzuri kwa kuwa unagusa maisha ya Watanzania na hasa hasa kupeleka fedha nyingi katika ngazi za chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuzungumzia mambo machache. Kwanza, nizungumzie eneo la miundombinu. Kwa kweli tumekwama sisi Wilaya ya Mbulu katika ile barabara ya Magara, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na Wizara yake watuonee huruma waangalie ule mlima na jinsi ambavyo nguvu ya Serikali inahitajika sana. Kwa kweli katika mwaka huu wa bajeti nashukuru kwa nia njema ya Serikali kwa kutenga fedha za bajeti katika ule mpango wa kujenga bwawa la umwagiliaji kule kwetu na ile barabara pia kwa ajili ya mlimani kuna nia njema hadi sasa tuendelee kuona ni namna gani tunakusanya mapato ili tuweze kutatua tatizo hili la jumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili nizungumzie jinsi ambavyo tunaweka vipaumbele katika ule utatuzo wa kero za wananchi. Kwa kawaida mtu hawezi kutambua juhudi za aliyeko kwenye uendeshaji wa chombo, mara nyingi mtu mwingine huwa haoni kama anayeendesha chombo anaendesha vizuri. Mimi niseme tu kwamba jitihada hizi ni kubwa na juhudi za Rais ni kubwa na ndiyo maana anaamua kupeleka fedha kwenye yale maeneo nyeti inapobidi na ambayo ndiyo kero kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali iendelee na kasi yake iliyoanza nayo, iendelee kufanya kazi zake kwa juhudi zote, iendelee kuona mawazo yote tunayochangia katika hii bajeti ni kwa namna gani yanaingia katika mpango wetu na yaweze kutatuliwa pale inapobidi. Si kwamba tunashindwa kutekeleza miradi, ni uwezo wetu lakini pamoja na makwazo mbalimbali. Niitake Serikali iangalie kwa dhati kabisa eneo la majanga. Eneo la majanga na dharura kwa maana ya maafa ya mvua, njaa, magonjwa na maafa mengine yoyote yanakwamisha mipango ya bajeti kwa kila mwaka kwa sababu yanajitokeza baada ya sisi kupanga mipango. Kwa hiyo, niitake Serikali ione ni kwa namna gani inatazama maeneo yanayoweza kuzuilika katika majanga yanayotokea. Mara nyingi tumepata majanga makubwa lakini yanatokea baada ya Serikali kupanga bajeti.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa bajeti ulioisha tulikuwa na dosari nyingi kwenye miradi mingi kwa kukosa fedha. Kwa hiyo, naiomba Serikali kwa kadiri inavyowezekana ione ni namna gani basi hata ile miradi iliyokwama inaingizwa kwenye mpango wa bajeti. Kwa sababu katika ngazi za chini huwa wao bado wanategemea mpaka Juni 30 ile miradi itapata fedha lakini nikitazama naona miradi mingi itakosa fedha na isipohamishiwa katika mwaka wa fedha unaokuja basi ile miradi itakuwa imesahaulika na ni miradi viporo na haitaweza kukamilika kwa namna yoyote ile kwa sababu itakwama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza bajeti au mpango wa maendeleo wowote ni mpango endelevu unaotekelezwa kwa awamu na unapofika ukomo wa muda uliotarajiwa maeneo yote ambayo hayakufanikiwa hayana budi kuhamia kwenye ule mpango mpya unaoendelea. Kwa hiyo, kila mtu au kila mdau wetu atazame, tuunganishe nguvu katika kukusanya nguvu kwa wadau wa maendeleo, Serikali kama Serikali na wananchi wetu huwa wana mchango mkubwa katika eneo hilo kwa kutoa michango yao ya hali na mali katika kuchangia shughuli za maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulianza na mambo mengi sasa hivi tunakejeliwa na shule za kata lakini bado zimeendelea kufanya vizuri na tulikuwa na tatizo la madawati limeendelea kutatuliwa. Kwa kawaida isingekuwa rahisi kila mtu atambue mchango wa Rais kwa sababu hapa tunatofautiana kiitikadi na ndiyo jitihada zinakwamishwa. Kwa hiyo, wote kwa pamoja tuunge jitihada za Rais na Waheshimiwa Mawaziri wala msikwazike nendeni kwenye Majimbo, kama nilivyowaalika kwenda Jimbo la Mbulu Mjini nendeni bila kunitafuta mimi, hamna sababu ya kunitafuta mimi Mbunge niko wapi, jitihada kubwa inahitajika kutoka kwao wao waende kwa wakati na waweze kutusaidia katika ile hatua nzuri wanayotarajia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala lingine la shilingi milioni 50 zinazolalamikiwa. Bado ni mapema sana, ndiyo tumeanza mwaka wa bajeti ya Serikali. Huu ni mwanzo wa kujadili bajeti ya Serikali na jinsi tunavyojadili hii, matokeo yake na changamoto zake baadaye ni sisi ndiyo tutakwenda kujadili kama Wabunge kwa niaba ya wananchi. Wananchi wana haiba na hamu kubwa ya kuona kwamba matatizo yao tunayajadili bila kupoteza muda na bila kuendeleza propaganda za kukwazana na porojo katika ukumbi huu wa mjadala wa matatizo ya wananchi kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kuzungumzia maeneo machache katika bajeti hii ambayo yanahitaji kutazamwa sana. Moja ni yale yaliyoguswa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa sababu Ilani hiyo ndiyo imeweka ahadi kwa wananchi na wananchi wanategemea ahadi yao itatekelezwa kwa jinsi ambavyo viongozi walioomba kura walisema na jinsi ambavyo Ilani imetafsiriwa kwao. Eneo hili linahitaji kutazamwa ni namna gani Ilani na zile ahadi za Rais zinaingizwa kwenye mipango ya mwaka hadi mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais alipokuwa Jimboni Mbulu aliahidi lami kilometa tano, naomba basi Serikali kila mwaka iweke utaratibu wa kutatua ahadi yake hiyo. Aliweka ahadi ya kuweka zege mlima Magara na daraja la Magara na pia barabara ya Mbuyuni - Magara - Mbulu ipate lami. Kwa sababu eneo hilo kwa jiografia ni hatarishi na kila kiongozi aliyeenda Mbulu ilikuwa hatuna sababu ya kumpitisha huko lakini ndiyo barabara pekee inayotuunganisha sisi na Babati kama makao makuu ya Mkoa na ndiyo inayotuunganisha sisi pia na mji mkubwa wa kibiashara wa Arusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa ujumla niseme bajeti ni nzuri, naunga mkono hoja na naomba Serikali isimamie utekelezaji wa bajeti kwa kuzingatia vipaumbele na kwa jinsi ambavyo bajeti hii itagusa maisha ya mwananchi wa chini ili mwisho wa siku matokeo mazuri ya hapa kazi tu yaonekane.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyoongoza nchi hii, lakini pia na Baraza zima la Mawaziri, tunawaomba nendeni mkamwambie Mheshimiwa Rais asilegeze uzi. Nchi yetu hii inahitaji mwendo wa Rais sasa, si lelemama na maneno mzahamzaha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaanza na hatua ya kwanza kumuomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, naomba mfumo wetu wa ukusanyaji wa mapato utazamwe. Nchi yetu bila mapato ya kutosha kutoka ndani ya nchi hatuwezi kufika mahali popote. Sasa hivi mfumo unaotumika unagandamiza sana wale walipakodi kulingana na mfumo na utaratibu unaotumika. Mimi ninaomba basi, tufanye utaratibu wa Serikali kutazama upya mfumo mzima wa ukusanyaji wa mapato yetu ya Serikali ili walau walipakodi wawe marafiki wa Serikali na wavae moyo wa uzalendo katika kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kutazama upya ahadi za Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ameahidi mambo mengi sana na kama hatutaweka kwenye utaratibu ule wa kawaida wa kuangalia ni namna gani zile ahadi zake zinaanza kutekelezwa kwa awamu kila mwaka ili ziweze kuingia kwenye mfumo wa bajeti ya Serikali, hatuwezi kufika mahali popote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo. mimi naona kama kule kwetu Mbulu ahadi zote alizoahidi bado hazijatekelezwa, tunandelea kusubiri Serikali itekeleze kwa sababu tayari viashiria vimeonekana. Naipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo tayari wametangaza tenda ya Daraja la Magara na mwaka huu wa fedha ambao tuko nao watatekeleza ahadi hiyo ya Rais ili kujibu kiu na matarajio ya wananchi wa Mbulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara ya lami aliyoahidi kule Mjini Mbulu, naona tender pia imetangazwa. Tunaishukuru sana Serikali kwa jinsi ambavyo tender ya ahadi ya Rais kilometa tano pale Mjini Mbulu imetangazwa, na ni imani yangu kuwa itatekelezwa katika mwaka huu wa bajeti kwa kadri ambavyo imetangazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani tunaweza kuzungumza mambo mengi sana, lakini bila pesa, bila nchi kuwa na uchumi, hata tukiongea namna gani mafanikio yetu hayatafika mahali popote. Kwa hiyo, katika eneo hili la ahadi za Mheshimiwa Rais, ni imani yangu kuanzia mwaka huu wa fedha tunaouendea kila mahali pataguswa ili iingie kwenye mfumo wa utekelezaji wa bajeti ya Serikali na iweze kutekelezwa. Mheshimiwa Rais ameahidi mambo mengi na kwa kadri alivyoahidi si rahisi kutekeleza kwa mwaka mmoja, lakini kwa kuwa Serikali ni endelevu na ina miaka mitano, ni imani yangu itatekeleza ahadi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kadri walivyoongelea kilio kikubwa cha bei ya mazao ya wananchi. Kwa sasa wananchi wanahangaika kutafuta masoko yao. Tuone Serikali itumie wataalam na mifumo mbalimbali na marafiki zetu ili kuona ni namna gani tunapata bei nzuri ya mazao ya wananchi ikiwemo mifugo na mazao yanayotokana na kilimo ili kuwezesha mwananchi wa chini kupata uchumi unaoweza kumudu mahitaji na matarajio ya nchi na katika kujihudumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ninapenda nizungumze kwa ufupi sana kutokana na muda ni eneo la miradi ya maendeleo. Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alianzisha mpango kabambe wa ujenzi wa maabara katika Halmashauri mbalimbali nchini. Hivi sasa bado baadhi ya maeneo mengi kwenye ujenzi wa zile maabara hakujakamilika na wananchi wamechanga vya kutosha. Tunaomba fedha hizi za ukamilishaji wa maeneo ya viporo ya maendeleo zingeweza kutafutwa kwa kila mwaka kwa awamu ili miradi ile ya maabara iweze kutekelezwa na iweze kufanya vizuri kwa maana ya kuwahudumia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la elimu tunaomba Wizara ya Elimu iangalie upya mfumo wa wakaguzi wa elimu katika nchi yetu. Wakaguzi wetu wa elimu mara nyingi wanapata wakati mgumu wa kukosa vitendea kazi na fedha za kuwawezesha ili waweze kutekeleza matakwa yale ya kukagua kiwango cha elimu, ubora wa elimu na hali yao ya kutekeleza mipango ya kazi kwa kuwa tunawalipa katika mishahara na kwa kuwa wao tayari tumewaajiri. Mfumo huu ungewekwa kama mfumo ule wa ukaguzi kitaifa kwa maana ya CAG hata kwa Taifa letu huu ukaguzi wa elimu ungejengewa mfumo mzuri kutoka ngazi ya Taifa mpaka kwenye Halmashauri zetu ungeweza kufanya vizuri na kuweza kujenga utaratibu unaofaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viporo vingi na kwa kweli kwa kadri ambavyo Serikali imefanya kazi katika mwaka huu mmoja tu wa Serikali wa 2016/2017 kazi nyingi sana zilifanyika na inaonekana tukiendelea kutafuta Wakala wa Maji, tukaendelea kutafuta na mawakala wengine, tukatafuta fedha kwenye vyanzo vya ndani vikaungana na fedha za wabia wa maendeleo, basi tunaweza tukafanya vizuri zaidi ili tuweze kukamilisha miradi iliyokusudiwa na kutoa huduma stahiki kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi niombe utaratibu wa upelekaji wa fedha za miradi ya maendeleo katika mwaka huu ulioisha wa 2016/2017 haukuweza kukaa vizuri kwa sababu fedha zilikuwa zinapelekwa, lakini hazilingani na asilimia. Tunaomba fedha za miradi ya maendeleo zitolewe kwa asilimia, kama Halmashauri ilikusudiwa bilioni 50 basi kama tunatoa asilimia 30, iwe ni asilimia 30 kwa namna ambavyo kila Halmashauri inapata kwa sababu yule aliyepangiwa fedha nyingi atapata asilimia 30 na yule ambaye fedha zake kwa mpango wa maendeleo si nyingi atapata zile asilimia 30. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nimemfuatilia Mheshimiwa Rais kwenye ziara yake siku moja, alitoa taarifa ya kwamba fedha za miradi ya maendeleo zimetolewa kwa asilimia 90, naomba tusimdanganye na kumpotosha Mheshimiwa Rais kumpelekea utaratibu wa taarifa isiyo rasmi, tuwe tunapeleka kile halisi ambacho tumepeleka kwa sababu tunaingia mgongano kati yetu sisi na wananchi kwamba zile fedha zimepelekwa wapi, mbona kwenye taarifa ya Rais zimepelekwa zote ama zimepelekwa asilimia
90. Mambo kama haya yanaipa mkanganyiko mamlaka ya kuchaguliwa kwa maana ya Waheshimiwa Madiwani, Waheshimiwa Wabunge na hata viongozi wengine, lakini pia na watendaji wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuliongelea ni eneo hili la uadilifu, uwajibikaji kwenye mifumo ya Serikali; bado kuna baadhi ya watendaji Serikali hawajabadilika. Tunaomba Serikali itazame upya watendaji wake wote kwa kila Wizara ili wabadilike, wawajibike kwa wananchi, watoe kauli nzuri kwa wananchi, waweze kuwahudumia wananchi na waweze kujitambua kwamba wao wana dhamana kama ambavyo wamekabidhiwa na watumie lugha nzuri wanapowahudumia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika ofisi nyingine majibu wanayopewa watumishi wadogo na wananchi hayalingani kabisa na Serikali ya Awamu ya Tano. Ninaomba sana kama itawezekana Serikali ifungue macho, hasa wale wenye mamlaka ya kusimamia rasilimali viongozi na rasilimali wananchi ili watu ambao wanawajibu wananchi wetu vibaya kwenye ofisi za Serikali, ambao hawataki kuwajibika waweze kuchunguzwa na waondoke kwenye mfumo mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili nalizungumza kwa sababu unapoona huku juu Serikali inafanya kazi vizuri sana, kule kwenye maofisi bado kuna watu wamekaa kwenye ma- bench hawawajibiki, kutoa file meza moja kwenda meza ya pili inachukua mwezi mzima, hii inatukatisha tamaa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naishukuru sana Serikali kwa jinsi ambavyo imeweka nia ya dhati ya kufanya mapitio ya barabara ya Karatu – Mbulu hadi kule Haydom kwa ajili ya kufungua wananchi wa Wilaya ya Mbulu ili waweze kuungana na wananchi wengine kwa mfumo wa barabara ya lami kwa maana ya kuwaunganisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana, itachochea uchumi kwa Wilaya ya Mbulu na Wilaya za Karatu na Wilaya nyingine za kule Mkalama na Shinyanga kwa sababu ukanda huu wa juu wa bonde la ufa ni kama umezungukwa na uzio ambao umefungwa moja kwa moja na Ukanda wa Bonde la Ufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kuchukua saruji ya Dangote, kama unataka kupeka Mbulu ni lazima kwanza iende Singida, halafu Itoke Singida ije Mbulu. Kwa hiyo gharama yake ni tofauti kabisa na maeneo mengine katika Tanzania yetu kwa kuwa barabara ni ya udongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukienda kule Tanga ukachukua saruji kule ukataka kuleta hiyo saruji, ni lazima iende kwanza Mto wa Mbu, ije Karatu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: …ije Mbulu. Kwa hiyo tunaomba sana barabara hii ni ya muhimu sana…
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii muhimu sana kuweza kuchangia mada yetu iliyopo mezani.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Kazi anayofanya ni kubwa nasi Bunge tuendelee kumsaidia. Nichukue nafasi hii pia kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati waliochakata taarifa hii hadi leo hii tunapojadili hapa kwenye Bunge hili kwa ajili ya kuweza kupata maamuzi na mwelekeo sahihi kwa Taarifa ya CAG.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia sana CAG kwa sababu amefanya kazi kubwa. Taarifa yake ina zaidi ya kurasa 1,000. Ukipita, hakuna sehemu iliyo nzuri na muhimu na ambayo inaweza ikatia matumaini kwa Watanzania. Kwa kweli taarifa hii iko kwenye mitandano kwa Karne hii ya 21 ni taarifa muhimu sana. Watanzania wengi wanasoma siyo kwamba ni sisi tu tulioko hapa Bungeni, kwa kuwa wao pia wanasoma, wanasubiri mustakabali wa maamuzi yenye tija na malengo sahihi kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yapo mambo ya msingi sana japokuwa taarifa hii imeletwa kwetu kama Muhimili wa Bunge, kama chombo cha wananchi na kwa kuwa Watanzania wengi wanaisoma na kwa kuwa, Taarifa ya CAG inapokuja Bungeni, CAG ameshahangaika sana, tuna kila sababu ya kumpongeza kwa sababu mpaka ije kwetu ameomba vielelezo vyenye kumpa matumaini kwamba hoja hizi zinajifuta, zina usahihi na matumizi sahihi ya fedha zilizotajwa katika kurasa zote za taarifa ya CAG.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo basi, kwa kuwa alikuwa ameomba nyaraka za kuweza kuthibitisha matumizi sahihi na ikashindikana, hatimaye wakati anafunga taarifa zake amekuja kukitaka chombo hiki cha wananchi Bunge na Muhimili wa Serikali waweze kujadili na kuona maoni yake yanafanyiwa kazi. Kwa miaka kadhaa tukiwa Wabunge tumekuta taarifa za CAG zinapokuja zinajadiliwa hapa Bungeni na hatimaye hatua zinazochukuliwa zinakuwa pengine hazikidhi na kutosheleza yale matakwa sahihi ya Watanzania na malengo wanayokusudia. Nitazungumzia mifano michache.

Mheshimiwa Spika, CAG anapotoa taarifa hapa yeye ameshachambua vya kutosha hivyo. Mimi siungani na wale wanao sema kwamba tuunde chombo kifanye utafiti tena. Tunachotarajia ni kwamba baada ya taarifa hii sisi kuijadili na kuisoma na kuona madudu yalivyo, matatizo yaliyojitokeza na matumizi mabaya ya fedha za umma; lengo letu kama Bunge, ninalishauri Bunge letu nakulishawishi, kwamba pengine sisi, kwa sababu wananchi wana matumaini kwetu, tuwe na maamuzi ambayo yatatoa matumaini kwao. Kwanza kuwawajibisha wale wote waliohusika kwenye taarifa hii na ambao wanaichezea mali ya umma.

Mheshimiwa Spika, vipo vyombo vya kutosha katika nchi hii kuchukua nafasi kuchambua taarifa hizi kuleta baadhi ya taasisi ambazo tayari ama wahusika wa ngazi mbalimbali wamehusika kwa namna moja au nyingine kutufikisha hapa tulipo. Kwa sababu hizi ni kodi za Watanzania na Watanzania wanataka huduma na viongozi wa nchi kama Rais na waandamizi wengine wote wanahangaika kutafuta namna ambavyo matatizo ya Watanzania yanatatuliwa; hivyo kuna kila sababu ya sisi kama Bunge kuweza kufikia maamuzi magumu kwa ajili ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa nini ninasema hivyo? labda nizungumze mifano michache. Mfano wa kwanza ni fedha za COVID 19. Tulisubiri magari ya ambulance tunakaribia mwaka, fedha hizo hazijaleta magari ya ambulance. Kichwani kwangu au kwenye mawazo yangu nawaza kwamba hata hizi fedha pengine za kununua hayo magari ingekuwa ni watu wanafanya mchezo wa Pwagu na Pwaguzi wanaweka kwenye akaunti ya deposit leo hii ina shilingi ngapi? Kwa nini manunuzi yanachukua muda mrefu kiasi hiki? Hatuoni kuwa kiasi cha fedha kilichotarajiwa kununua mitambo ya magari ya ambulance machine za X-rays na mitambo mingine ya kuchimba maji na mitambo mengine kwa manunuzi ya Umma yamechukua muda mrefu kiasi kwamba kuna mchezo wa kuchelewesha huduma kwa Watanzania?

Mheshimiwa Spika, hali hii inafanya Watanzania kutokuwa na imani na Bunge hili na kutuelewa vibaya. Kwa hiyo mimi nilikuwa nashukuru kama Mawaziri watakuja hapo, kila Waziri kwa kadri ya sekta anazosimamia na Wizara anayoisimamia aje na maelezo mahususi yatakayo wapa Watanzania Imani; kwanza ya kuchukua hatua lakini la pili kwa nini tunafika hapo, majibu yake yaweze kuridhisha Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo; kadri ambavyo CAG kila siku analeta taarifa hapa na sisi kila mwaka taarifa inapokuja tunakuwa tunachangia kwa kukwepa kwepa madhara yake ni kuwa tunamkatisha tamaa CAG na watendaji wake wote hadi ngazi ya chini. Kwa sababu yeye anafanya kazi ngumu na kazi ya kwenda kupekua watu na kazi ya kuleta taarifa hapa ni kazi ngumu, kazi ya kwenda kuandaa taarifa yenye ufafanuzi, wa kina na yenye kurasa zaidi ya elfu ni kazi ngumu.

Mheshimiwa Spika, wakati fulani, nchi hii ilipoingia kwenye tumbua tumbua hatukuielewa. Mimi nadhani hatukuielewa, sababu za kutumbua tumbua ilikuwa ni kwa kuwa wale waliokuwa wanapaswa kuchukua hatua hawakuchukua hatua kwa wakati unaofaa na kwa hivyo basi yule ambaye anamamlaka aliona ni nafuu nianze na yule aliyekaribu na mimi ili wale wengine waanze kuhofu kwamba kumbe mimi nisipochukua hatua kwa wakati basi wale wengine watachukua hatua na mimi naweza kufikiwa na janga hilo.

Mheshimiwa Spika, tutaishukuru sana Serikali, hasa Mawaziri, watakapo kuja, kwa sababu hivi punde tutahitimisha hoja hii, hivyo waje na kauli. kwa kwanza kuliomba Bunge maeneo ambayo wao wanahitaji msaada kwa Bunge, ushauri au hatua za kuchukua ili ziridhiwe kupitia sheria tulizopitisha. Pili, kuona ni kwa namna gani tatizo hili halijirudii. Tuanze na taasisi kadhaa ambazo kwa miaka mitatu taarifa zao zilikuwa chafu kupitia kwa Mkaguzi wetu (CAG), ili sisi pia kama Bunge tunapochukua hatua au tunapowapa wao nguvu kama Serikali basi nchi ipate unafuu na mafanikio wa yale ambayo Watanzania walio wengi wanatarajia.

Mheshimiwa Spika, hali nyingi zinajitiokeza kwa sababu ya uzembe, uadilifu na utimizwaji wa wajibu na majukumu. Haiwezekani tunachukua watendaji wabovu tunawazungusha kwenye nchi. kwamba anahama taasisi moja Kwenda nyingine ama halmashauri moja kwenda nyingine. Matatizo makubwa yanaendela katika nchi wakati nchi inawasomi wa kutosha. Ndani ya hiyo taasisi ambayo tunawahamisha hao watendaji wabovu, kuna watendaji wazuri lakini hawapewi nafasi kwa ajili ya kulindana pengine au kujenga mfumo ambao ni dhaifu katika nchi na mfumo ambao hauna tija kwa Tanzania nchi yetu. Na sisi ipo siku ama kupitia dhamana zetu tulizopewa tutalaumiwa na kulaaniwa; au kupitia nafasi zetu kwa wananchi, wananchi watakosa imani kwetu sisi kama Bunge na Serikali yao.

Mheshimwa Spika, kwa nini nasema hayo? fedha nyingi ukizijumlisha unafika mwisho hazijumlishiki, fedha ambazo tayari zimekosa matumizi na hazijaenda kutoa huduma.

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mimi nilikuwa naomba nimpatie taarifa Mheshimiwa mzungumzaji kwamba anayosema ni sahihi. Nafikiri sisi kuhangaika na wale watendaji kule chini ni sawasawa na kufukuzana na nyuki. Sisi watu wetu ni hawa Mawaziri na Watendaji wengine Wakuu Serikalini.

SPIKA: Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, unapokea taarifa hiyo?

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, mimi naipokea kwa mikono miwili (Makofi). Nchi hii ina mihimiri, mimi nikupongeze sana, sisi kubebeshwa mzigo kuhangaika kule chini, mimi naungana na mtu aliyenipa taarifa. Si muda wetu sasa hivi, sisi ni chombo na chombo hiki, kiungo chetu ni Serikali na Mawaziri, wao wachukue hatua, na wao wakichukua hatua nchi inapata unafuu.

Mheshimiwa Spika, kwa nini tunasema hivyo? Taarifa hii imechakatwa na kule halmashauri ilikotoka kuna mtu anaitwa mkaguzi wa ndani, na mkaguzi wa ndani atatakiwa apeleke vielelezo kwa wale ambao anawataka walete vithibitisho kwa ajili ya taarifa zenye utata. Kwa hiyo unapoenda kwenye ngazi ya halmashauri kwenye taarifa za halmashauri huko, zile halmashauri zinazofanya vibaya zilishapewa muda wa kupeleka nyaraka za utetezi ili mwisho wa siku hoja zao zifutwe. Hadi tunaletewa huku, walishashindwa, hawakupeleka.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hawakupeleka Mkaguzi Mkuu (CAG) hawezi kuacha kazi yake, ni lazima alete taarifa yake kwetu sisi kama Bunge na chombo cha wananchi na muhimiri Serikalini kuelezea hali halisi ya taasisi zilivyo. Kwa hiyo kule zilishadaiwa zifutwe kwa nia ya kwamba nyaraka zipelekwe lakini zimeshindikana, hapa zimekuja mahakamani ili zihukumiwe, kwa sababu umepewa nafasi ya kutetea hukutetea umepewa muda hukutumia vizuri. Sasa ni wakati wa chombo hiki kuamua ili Watanzania wapate amani.

Mheshimiwa Spika, si kwamba tuna chuki sana na Mawaziri lakini kadri unavyochelewa kuchukua hatua basi tatizo linakuwa…

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka nimpe taarifa mzungumzaji, kwamba ukweli sasa hivi inatakiwa tuchukue maamuzi magumu. Nitatoa mfano kidogo 2018, tuliingiziwa pesa za ujenzi wa Kituo cha Afya Nyang’wale tarehe 26 Mwezi wa 6, kufikia tarehe 1 mwezi wa 7 milioni 400 zikawa hazijulikani zilikokwenda, na hadi leo hii watu hao wako mtaani wanaendelea na shughuli zao kama kawaida. Nilikuwa nataka kumpa taarifa Mheshimiwa.

SPIKA: Mheshimiwa Zacharia Issaay, umepokea taarifa hiyo?

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, kwa mikono miwili. Fedha milioni 400 anazozizungumza mtoa taarifa ni kodi za Watanzania; na fedha hizo kwa kuwa hazionekani ziliko halafu bado wale watu wako wanaendelea; na tunatunga sheria hapa za utakatishaji wa fedha, matumizi mabaya ya fedha na Sheria nyingine nyingi kama vile za manunuzi halafu hatuzisimamii. Tunaendelea kupiga kelele na kodi za Watanzania zinatumika kulipa vikao hivi vya Bunge na gharama za uendeshaji wa Bunge, je tunaitendea haki nafasi yetu kweli?

Mheshimiwa Spika, mimi nadhani pamoja na sababu nyingi zilizowasilishwa na Waheshimiwa Wabunge, mimi niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge, katika kipindi hiki cha kujadili taarifa hii tumetendea haki nafasi zetu kwa hali ya juu sana. Hii ni kwa sababu sisi ndio tunaosubiriwa tuseme ili nchi ipone, na sisi ndio tunasubiriwa tuseme kwa niaba ya Watanzania milioni 60. Tunakwenda wapi kama endapo tunaanza kukwepa maamuzi magumu ambayo yataisafisha nchi na yataiweka nchi mahali pazuri?

Mheshimiwa Spika, mimi niwaombe Wabunge wenzangu tuungane kwenye hoja hizi na tutazame kwa kina maslahi mapana ya taifa letu, tuweze kuzungumza tukiwa Wabunge kama sehemu ya Watanzania na hatimaye maazimio tunayoazimia hapa kwa kuzingatia Sheria na Kanuni zetu za Bunge na Sheria nyingine za nchi yaweze kuwa na tija na kuhakikisha nchi yetu inapata ahueni na mafanikio ya maendeleo yanapatikana.

Mheshimiwa Spika, mengi yatazungumzwa lakini hatima yake, tunapo kwepa maamuzi magumu yote tuliyo yazungumza hayatakuwa na tija. Ili yale tuliyazungumza yawe na tija, na taarifa zimeletwa hapa na zimeeleza madudu ya kila sehemu, tuchambue kadhaa tuchukue hatua, tuweze kunoa Sheria inasema nini na wajibu wetu ni nini ili hatimaye nchi iweze kubadilika. Vinginevyo, kila mwaka CAG atahangaika kuleta taarifa hapa, taarifa zake atakazoleta hapa, hatutampa matumaini na hatutaona kama ni sehemu muhimu, na mwisho wa maamuzi yetu yatadharauliwa na Watanzania milioni 60.

Mheshimiwa Spika, nahitimisha kwa kuunga hoja mkono kwa asilimia mia moja, mchano wangu uishie hapo.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nichukue nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii, lakini pia nichukue nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini kwa kunichagua kuwa Mbunge wa Jimbo lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii pia, pamoja na Mpango huu tunaojadili wa Bajeti, nami nitoe mchango wangu kwa sehemu ambayo naiona katika Mpango huu. Kwanza napenda kuishauri Serikali katika ukusanyaji wa kodi. Ifike mahali sasa tukusanye kodi kwenye viwanda, tukusanye kodi kwenye makampuni makubwa, bandarini na tuwe na lengo kubwa la kukusanya kodi kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, hatua hii ya Mpango huu wa Bajeti wa mwaka huu unakabiliwa na changamoto kubwa huko mbele. Kwa hivyo, tusipokusanya kwa kiwango kikubwa mapato ya Serikali, Mpango huu unaweza kuwa mzuri sana kama ulivyowasilishwa kwetu sisi, lakini hatimaye usiwe na matumaini na mafanikio mbele ya safari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango huu ninaoutoa katika kukusanya mapato ulenge zaidi yale makundi makubwa ya walipakodi kuliko wale wananchi wa ngazi za chini na wafanyabiashara wa ngazi za chini. Ifike mahali sasa tujijengee dhana ya udhibiti wa mapato ya Serikali na jinsi ambavyo wananchi wana hamu kubwa ya kupata huduma bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kutokana na muda, ni eneo la elimu bure. Nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Mheshimiwa Rais kwa kutoa elimu bure. Naomba nishauri mambo machache.
Katika eneo hili sasa Serikali ije na mpango wake wa kuajiri nafasi zile za wazi katika Serikali ikiwemo zile za wale vijana wanaofanya vibarua katika shule hizi za sekondari ili gharama ipungue kwa mwananchi, lakini pia namna ya kupunguza zile gharama zilizobaki. Hadi sasa bado kuna michango mikubwa katika eneo hili la elimu ya sekondari na elimu ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iweze kuona ni namna gani inajaza nafasi za wahudumu, wapishi, walinzi na pia nafasi za kupunguza gharama zile zinazotokana na mwananchi ili wanafunzi wengi wapate elimu hii na kwa nafasi yao wapate kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo linalohitaji kuboreshwa zaidi. Katika mchango wangu naomba kuishauri Serikali.
Kwanza ichukue nafasi kubwa ya kuweza kuanzisha Vyuo vya VETA, lakini pia Vyuo vya Ufundi Stadi vilivyopo katika Wilaya na kwenye Majimbo yetu, vibadilishwe kuwa Vyuo vya VETA haraka ili vijana wetu wengi wapate hatua ya kuwa na nafasi ambayo vijana wanapata ujuzi na ufundi stadi na kuweza kuajiriwa na hatimaye kumudu changamoto zitakazotukabili katika uanzishaji wa viwanda.
Eneo la viwanda, naomba basi niishauri Serikali, eneo hili la viwanda, tuweze kufanya utafiti kama Serikali, tuone kiwanda gani katika kanda ipi, rasilimali gani inahitajika na ipo katika eneo hilo ili kupunguza gharama na viwanda hivyo viweze kuwa na tija na kwa hivyo tunapofanya hivyo tunapunguza gharama kubwa ya uendeshaji wa Serikali katika kuanzisha viwanda na kuleta tija zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, nitoe angalizo pia katika eneo hili, ni eneo ambalo linatupa kazi kubwa kwenye madeni ya Serikali. Jimboni
kwangu, nichuke nafsi hii kukuomba sana. Serikali ina madeni makubwa sana, isifumbie macho. Madeni ya maji, madeni ya maabara, madeni mengine mengi ya barabara, lakini wakati huu Mpango umewasilishwa kwetu ni mpango mzuri, tutashindwa kutekeleza kule mbele ya safari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali, wakati wa sasa hadi kufikia bajeti, ikusanye orodha kubwa na takwimu kubwa ya madeni ya Serikali ya miradi iliyoanzishwa. Kama Jimbo ninalotoka, madeni ni zaidi ya shilingi bilioni tatu kwa Mradi wa Maji wa Benki ya Dunia. Fedha zinazodaiwa na wakandarasi kwa ajili ya malipo yao, wale waliokamilisha kazi na wale ambao wamefikia hatua mbalimbali, ni zaidi ya shilingi milioni 700, lakini hata kama tumekuja na Mpango mzuri mbele ya safari tutakuja kuhitilafiana na hatutakuwa na tija katika hii mipango mizuri kama hatutaweza kuona ni kwa namna gani madeni ya maji, barabara, maabara zilizoanzishwa na wananchi kwa kiasi kikubwa sana na sasa hata umeme vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo ninalotoka mimi, umeme umekwenda kwa vijiji takriban tisa au kumi, huku Waziri anatupa matumaini makubwa sana. Naomba kama itawezekana maeneo haya ambayo tayari Serikali imekuwa na madeni makubwa, yawekwe kwenye Mpango huu wa sasa ili yaweze kutatuliwa na wananchi waweze kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona ni jambo jema kama tutakuwa tunakamilisha miradi na inatoa huduma. Miradi ya aina hii iko mingi, kwa mfano, tulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Rais katika barabara ya Magara inayounganisha Mji wa Mbulu na Mji wa Arusha na Mji wa Babati kwa maana ya Makao Makuu ya Mkoa, Babati na Makao Makuu ya Mkoa wa Arusha. Kilometa 13 za ahadi ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete imewekwa kilometa moja na nusu hadi leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Magara katika barabara hiyo, ambayo imepoteza maisha ya Watanzania wa Wilaya ya Mbulu na Wilaya ya Babati Vijijini, haikuwekwa hadi leo, kutoka ahadi ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete, ahadi ya Mheshimiwa Mkapa na leo ahadi ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli na ni kilometa hiyo yenye mazingira magumu na hatarishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapanga mipango, ikifahamu kwamba ahadi za Mheshimiwa Rais ni moja ya utatuzi wa kero za wananchi. Pale ambapo Rais anafanya ziara, anapokutana na changamoto ya kero zao anawaahidi. Kufanyike utaratibu wa kuratibu ahadi za Mheshimiwa Rais. Iwekwe kwenye Mipango ya Serikali, ili Serikali kila wakati na kila mwaka katika bajeti yake, iweze kutatua. Barabara hii ya Magara, ambayo ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi, nashangaa kama tena leo, tunatafuta fedha za usanifu kwa ajili ya Mlima Magara na Daraja la Magara, wakati Serikali imetumia pesa nyingi kufanya usanifu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii, ahadi nyingi za Rais ziwekwe katika bajeti hizi na Mlima Magara usipowekwa kwenye bajeti ya mwaka huu, natoa angalizo kwamba sitakuwa tayari kupitisha Mpango wa Bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii pia kuzungumzia eneo la kero ya akinamama, wauza matunda, mbogamboga, ndizi, waendesha bodaboda, kodi hizi ziondolewe, ni kero. Haya ni makundi madogo, hayana uwezo wowote na hali hii inawasababishia mazingira magumu ya kufanya kazi zao. Naomba nitoe mchango huu kwa kuishauri Serikali itazame kwa jicho la huruma makundi haya ambayo tayari ni makundi ya jamii. Yanafanya shughuli hizi, wana mapato madogo, hawa watazamwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitoe angalizo kwa jinsi tunavyopoteza muda wetu katika ukumbi huu. Mara nyingi tumekuwa wa kuzomeana, mara nyingi tumekuwa wa mipasho, mara nyingi kiti chako kimeshindwa kulinda kikao na kwa mara nyingi tunashindwa kupata nafasi ya kutoa michango yetu. Tunaminywa katika dakika hizi mnazotupa kwa sababu ya mipasho, mizozo na migongano ya kisiasa yasiyo na tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu, miaka mitano ni kama mshale wa saa na Rais alisema tupunguze mipasho, mizozo na vijembe. Sasa Bunge hili, takriban muda wote tuliotumia ndani ya ukumbi huu, tumetumia muda mwingi vibaya na kwa hivyo hasara hii ni kubwa kwa Bunge, ni kubwa kwa Serikali, tunagharamikiwa kwa kodi za Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uongozi wa Bunge, kutoka kwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti, watusimamie ipasavyo kwa kulingana na kanuni zetu humu ndani. Ili haki itendeke kwa kila mmoja wetu kukosolewa, kurekebishwa na kuadhibiwa ikibidi. Kwa sababu tusipofanya hivyo, tutafanya makosa makubwa na mbele ya safari tutaleta uvunjifu wa amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo imefika mahali, unafika mlangoni unaambiwa uvue mkanda. Hii ilikuwa jeshini, ilikuwa magerezani, sio huku. Huku ni eneo la heshima, tunatakiwa tujiheshimu na wale wenzetu wanaotuhudumia watuheshimu na hata kiti chako kiti kwa jinsi ambavyo tunafanyiwa, sio vizuri na sio itifaki ya Bunge. Naomba nafasi hii itumike vizuri, tusikejeliane na yeyote yule ambaye hataki kuheshimu kwa kweli tunakoseana.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Issaay muda wako umekwisha.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nafasi hii ni ndogo sana na ni ya hasara kwetu sisi na tunaminywa. (Makofi)
MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimwa Issaay.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami naomba nitoe sehemu ya mchango wangu kwenye Mpango huu. Kwanza nachukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa mchango wake wa kuitetea nchi hii katika kufanikisha azma nzima ya kuwaletea maendeleo Watanzania wote. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania tumwombee aweze kufanya kazi hii na tuweze kusogea kutoka hatua hii tuliyonayo tuweze kwenda mbele. (Makofi)
Pili, nachukua nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri kwa kazi kubwa wanayofanya. Nawaalika njooni Mbulu, msinitafute mimi, nendeni Mbulu. Mnahitajika sana. Mbulu tuna mahitaji makubwa, tuna kero nyingi. Nakupongeza sana Mheshimiwa Lukuvi kwa jinsi ulivyoshughulikia suala lililokaa miaka 10, sasa limetatuliwa, Wanambulu wana amani, wanakuombea. Waheshimiwa Mawaziri wengine baada ya Mkutano huu tunawaomba njooni Mbulu mtusaidie kwa jinsi ambavyo tuna matatizo mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuungana pia na Waheshimiwa Wabunge wote na kuwashukuru kwa jinsi walivyochangia Mpang huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tusimamie mapato. Azma nzima ya Rais wetu kusema Tanzania inastahili kusaidia siyo kusaidiwa, ni ya kweli kabisa. Tusimamie mapato, tusimamie huu Mpango, ifike mahali Mpango huu uletwe tena mbele yetu, tuujadili jinsi ambavyo unahitaji kurekebishwa na kuondoa dosari zinazokinzana na mafanikio ya Mpango huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa mpango wowote unapoletwa mbele ya Bunge hili tukiujadili, tukaupitisha, baadaye ukirejeshwa tunaweza kufanya marekebisho yanayohitajika katika Mpango kwa kufanyia utafiti kupitia kwa wataalam wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalopenda kulizungumzia ni mahitaji makubwa ya wananchi kuliko uwezo wa Serikali. Hii itaondolewa pale ambapo mahitaji makubwa yanatokea ya kutazama tena upya Mpango huu ili uweze kuleta tija katika huduma za umma na sehemu mbalimbali kwa jinsi ambavyo umewasilishwa kwetu na Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana Waziri wa Fedha na wadau wote waliohangaikia Mpango huu ambapo ni dira ya Taifa letu kwa mmwaka huu katika kuleta maendeleo kwa Watanzania wote. Umuhimu mkubwa wa Mpango huu unamgusa kila mdau hasa yule wa chini. Kwa jinsi ambavyo tunahangaika wakati wote na Bunge letu linahangaika na sisi Wabunge kule Majimboni tumeahidi mambo makubwa sana, rai yangu kwetu sote ni kila mmoja atimize wajibu wake katika Mpango huu na aone ni kwa jinsi gani atahangaikia suala hili ili pengine Mpango huu kwa miaka mitano uweze kutoa matokeo makubwa sana yenye kuweza kufanyiwa kazi hasa katika maeneo yenye changamoto nyingi ambapo kwa namna yoyote ile kila mmoja wetu anastahili kutimiza wajibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuone changamoto inayotokana na pato la Taifa kuwa dogo na jinsi ambavyo mahitaji yanakuwa makubwa, mengine yanaingia baada ya mahitaji ya dharura kutokea kama vile mafuriko, baa la njaa na mambo mengine kama magonjwa. Kwa hiyo, tunapopanga mpango tukienda miaka mitano bila kuwa na muda wa tathmini na muda wa kati na muda mrefu wa kuutazama Mpango huu umekinzana na mambo gani katika kufanikisha jambo lile ambalo limetokea na yale yaliyotokea katika Mpango, kwa kweli tunahitaji sana Bunge lipate kutazama upya na vikao vya tathmini vifanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia eneo la Mkoa mzima wa Manyara jinsi ambavyo hatuna kiwanda, hatuna reli, hatuna pia miundombinu ya barabara ambazo zinaunganisha mkoa wetu hasa eneo la juu la bonde la ufa ikiwemo Wilaya ya Mbulu na Wilaya nyingine ya Hanang jinsi ambavyo tunahangaika kutafuta namna gani tunaweza tukanufaika na hali hii ya miaka mitano katika kufanikisha azma hii, ambapo kila mwananchi anahitaji afanikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, kwa jinsi ambavyo tunahangaika na kwa jinsi ambavyo mahitaji ni makubwa, basi rasilimali zile nyingine za miundombinu zinavyotekelezwa, kwa mfano, miundombinu ya vyuo, viwanda na miundombinu ya mbalimbali, tupate na sisi tulio pembeni na tulioko juu ya bonde la ufa hasa maeneo magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi nalilia barabara ya Mbuyuni - Magara – Mbulu. Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi na Wizara yake waje Mbulu waone jinsi tunavyoteseka na barabara hiyo ambayo ina jiografia ngumu na wananchi wanapoteza maisha mara nyingi, lakini barabara hiyo na udogo wake, haishughulikiwi. Tunaomba katika hii miaka mitano ufumbuzi wa barabara ile ya Karatu - Mbulu - Haydom na hii ya Mbuyuni – Magara – Mbulu na ile ya Dongobesh - Manyara kule Manyara – Dongobesh - Babati ipate basi namna ya kufanyiwa utatuzi ili wananchi wakae kwa amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa eneo hili unahitaji wadau wakubwa wa maendeleo, tusiisahau sekta kubwa binafsi ambayo ndiyo mhimili unaochochea maendeleo kwa nchi yetu hasa katika viwanda na katika ulipaji wa kodi na jinsi ambavyo Serikali inahitaji mapato ili iweze kutatua changamoto na matatizo ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niweze kuzungumza eneo hili kwa kufanya maandalizi ya Wataalam, miundombinu na fedha kwa ujumla katika ushauri wa jumla, lakini tusisahau kutoa nafasi kubwa katika uwekezaji kwa wazawa wa nchi yetu. Eneo hili linahitaji sana Watanzania ambao wataendesha shughuli nzima ya uzalishajii katika Sekta ya Viwanda na sekta mbalimbali ili tuweze kupata manufaa makubwa na Watanzania waweze kumiliki uchumi wa nchi kwa manufaa yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa sekta hii binafsi, unahitaji zaidi uchocheaji na uwekezaji katika wale wazawa ambao wanahitaji kufanya hivyo na kufanikiwa katika hali sahihi. Katika eneo hili la kukejeli kutumbua majipu; kutumbua majipu tuendelee kutumbua majipu kwa sababu ndio waliotufikisha katika hii hali ambayo tunakuwa tegemezi sana. Ili tuepukane na utegemezi ni lazima tusimame imara katika kuhakikisha eneo hili tunafanikiwa kwa jinsi ambavyo tunaweza tukaenda mbele katika ile hali ya kudhibiti ubadhirifu, ufisadi, hujuma za nchi na mambo mbalimbali. Kwa ujumla Mheshimiwa Rais ana azma nzima, Wabunge tuwe na azma nzima na Mawaziri mpate nafasi pekee ya kumpa ushirikiano Mheshimiwa Rais wetu ili tuweze kufanikiwa.
Kwa hivyo basi, katika harakati za pamoja, ushirikiano wa jumla unahitajika. Wanaokejeli shughuli za utendaji wa Serikali kwa sasa katika muda huu mfupi ni kama wameanza vibaya. Hatuna sababu yoyote ya kukejeli Serikali, bado ni mapema sana. Safari hii tunayoanza ni ya miaka mitano; tuko ndani ya miezi mitatu, minne, mitano hadi sita, tukianza kukejeli, matokeo yake ni hatujajua chombo hiki kinaendaje na kwa jinsi gani tunahitaji mafanikio na siyo kukejeliana au kukatishana tamaa katika mwelekeo wa Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa nafasi ya pekee katika Mpango mwingine utakaowasilishwa hapo baadaye, tutazame upya hali ya Watanzania kwa jinsi ambavyo wanahitaji ushuru na kero mbalimbali ya tozo uondolewe kwa Watanzania wadogo. Wafanyabishara wadogo wana wakati mgumu! Tunapohitaji kuwadai ushuru na tozo mbalimbali, wao wanahitaji zaidi waweze kufanya mambo yao ya biashara ndogondogo ili wakue waje kwenye hatua ya wafanyabishara wa kati. Kwa hiyo basi, eneo hili litazamwe, lakini katika ile hali ya kulisaidia kundi hili la walioko chini sana katika maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango mkubwa unaotolewa na Mawaziri, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge kwa ujumla, unaweza kuchochea mafanikio makubwa na Mungu akitujaalia katika miaka hii mitano, Tanzania itasonga mbele na itakuwa nchi ya pato la kati na Watanzania wengi watanufaikia mapato ya nchi yao na watafurahia mafanikio ya nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nachukua hatua za makusudi kabisa za kututaka sisi Wabunge wote bila kujali itikadi; tumetoka kwenye Vyama mbalimbali, Majimbo mbalimbali lakini sisi wote ni Watanzania, tumeletwa na Watanzania katika Ukumbi huu ili tuweze kuzungumzia matatizo ya Watanzania, haijalishi ni wa eneo gani, lakini lengo kubwa ni kwa namna gani tunafanikiwa kutatua matatizo ya Watanzania wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa yote lakini niseme kwa ujumla naomba ushirikiano kwa Waheshimiwa Wabunge wote. Hata huyu anayekejeli Serikali ataihitaji Serikali hii imhudumie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na ahsanteni kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuwapongeza viongozi wetu kuanzia kwa Mheshimiwa Rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli. Nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri Mkuu Mheshimiwa Majaliwa na Baraza zima la Waheshimiwa Mawaziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii pia kuwapongeza viongozi wetu wa Bunge letu kuanzia kwa Mheshimiwa Spika, kwako wewe Mheshimiwa Naibu Spika na Wasaidizi wote wa Bunge. Naendelea kumwomba Mungu aijalie nchi yetu amani, mshikamano na utulivu; kwake yeye yote yawezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali ya Awamu ya Nne kwa mpango wake wa Wakala wa Umeme Vijijini. Kwa kweli kazi iliyofanyika ni nzuri sana na inatia moyo. Nachukua nafasi hii kumpongeza sana Profesa Sospeter Muhongo kwa moyo wake wa kujituma kwa nia njema ya kuwa mzalendo na moyo wa kupenda kuifanya nchi yetu kuwa ya umeme hadi 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii pia kuwaombea wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini kuanzia Taifa mpaka ngazi ya chini. Mungu awape uzima na maisha marefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mbulu katika mpango wa REA Awamu ya Kwanza na ya pili, imebahatika kupata umeme katika Majimbo yote mawili, vijiji 18 kati ya 123. Hivyo naomba sana Wizara hii iwatendee haki wananchi wa Mbulu. Maombi yangu ya kumwomba Mheshimiwa Waziri afanye ziara Wilayani Mbulu kutembelea miradi ya REA Awamu ya Kwanza na pili ili kujiridhisha na hali mbaya ya miradi hiyo hususan Vijiji vya Jaranjar Kata ya Tlawi na Guneneda Kata ya Tlawi na Kata ya Ayamohe.
Mheshimiwa Naibu Spika, barua yangu yenye dodoso la vijiji 33 niliyotuma kwa Mheshimiwa Waziri mwezi Februari, 2016 ifanyiwe kazi kwa kuwa Mbulu tumepunjika sana. Kwa Wilaya ya Mbulu imepata vijiji 18, naomba nijibiwe kwa barua ni lini Mheshimiwa Waziri atafanya ziara Wilayani Mbulu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri elimu itolewe na ngazi zote za TANESCO katika maeneo ambayo umeme unatarajiwa kutolewa au kupelekwa kwa wadau/wananchi wa maeneo husika. Wizara itoe elimu kwa wachimbaji wadodo wadogo wa madini ya dhahabu katika Kata za Nahasena, Aehandu ili kuondoa mgogoro katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria za kupata mrabaha katika machimbo kati ya HLW na wachimbaji itazamwe. Elimu itolewe kwa watumiaji wadogo wa umeme majumbani kwa kuondolewa kwa VAT na Service Charge ili kuleta hamasa ya matumizi makubwa ya umeme. Pia, watendaji wachache waliopo katika ngazi za Wilaya wadhibitiwe wanaotumia urasimu, ubabaishaji kwa wateja wanaohitaji kuunganishwa na umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira mazuri ya Tanzania katika kutumia umeme wa gesi yaandaliwe kwa kufanya tafiti za kitaalam ili umeme huu wa gesi uwe na tija kwa uchumi wa nchi yetu. Watazania wahamasishwe kutumia gesi kwa matumizi ya majumbani ili kupunguza matumizi makubwa ya mkaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri EWURA iwe na sekta mbili; moja, isimamie maji na nyingine isimamie mafuta na nishati ili kuleta tija.
Pia, utafiti ufanyike haraka kama Tanzania tumenufaika na asilimia nzuri ya mrahaba katika upatikanaji wa madini nchini. Pia, Sekta ya Mafuta itazamwe upya ili VAT irudishwe katika mafuta kuongeza mapato ya Serikali kwa kuwa mwenye kuhitaji mafuta ana uwezo, kwa hiyo, anastahili kulipa kodi.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. ZACHARIA P. ISSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali ifuatavyo:-
(i) Serikali itazame upya bei za gesi asilia kwani kwa sasa ni ghali ukilinganisha na maisha ya Mtanzania;
(ii) Serikali ifanye mapitio maeneo yenye makazi ya wananchi kwa wale wanaoishi karibu na vyanzo vya maji na maeneo ya miinuko katika nchi yetu. Mfano; wananchi hao wanaweza kufanya shughuli rafiki wa mazingira;
(iii) Serikali iangalie uwezekano wa kunusuru maeneo yenye uoto wa asili ili kuwa endelevu kwa kizazi kijacho;
(iv) Serikali itoe Waraka kwa DC’s (District Commissioner) na DED’s (District Executive Director) nchini kuhusu upandaji wa miti na mashindano ya Kaya kwa Kaya,
Kijiji kwa Kijiji, Kata kwa Kata na Wilaya kwa Wilaya na mwisho Kitaifa. Siku ya Mazingira ifanyike na kutoa zawadi;
(v) Taasisi mbalimbali ziwe na bustani za miche kama kitovu cha utoaji wa..
(vi) Tunaomba Serikali itusaidie kunusuru Maziwa madogo ya asili katika Mkoa wa Manyara; Ziwa Basutu katika Wilaya ya Hanang; Ziwa Tlawi katika Wilaya ya Mbulu; Ziwa Manyara katika Mkoa wa Arusha Wilaya ya Monduli na Ziwa Babati katika Wilaya ya Babati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa inayofanyika kwa kila sekta katika nchi yetu. Kwa kweli ni kazi nyingi zimefanyika na ina matokeo chanya kutatua matatizo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze ndugu yangu Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima kwa kazi kubwa wanayoifanya, wamejitahidi kufanya kazi kubwa na sekta hii sasa inaelekea pazuri na mafanikio yanaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaona eneo kubwa kwenye eneo hili la hotuba yake pamoja na bajeti aliyoiwasilisha tunao wajibu mkubwa kwanza wa kutazama ikama ya watumishi, hali yetu siyo nzuri kwa Maafisa Ugani, na hatuwezi kufanikiwa bila kuwa na wataalam, rasilimali mbalimbali pia vifaa na vitendea kazi pamoja na fedha kwa ujumla. Kwa hiyo naona kuna umuhimu mkubwa kwa sababu eneo lenyewe kwa mfano, Jimbo la Mbulu Mji lina watumishi Watano tu lakini lina Kata 17, lina Vijiji 34 na mitaa 58. Eneo kubwa la Jimbo langu wengi ni wakulima na wafugaji, wale wafugaji wana mifugo, kwa hiyo tatizo kubwa tulilonalo hatuna wataalam. Pia na najua siyo Idara yake yeye lakini wana jukumu kubwa la kuangalia idadi iliyoko kwa watumishi walioko ili tuone namna gani basi wale wachache wanaweza wakahudumia Watanzania na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kufanikiwa au kupata mafanikio bila kuwa na wataalam hao, vitendea kazi na rasilimali nyingine pia tuje na mpango kabambe, wafugaji wanahama sana, wanahama sana mifugo wanapata matatizo, mifugo yao wananyang’anywa, wanakamatwa misituni, siyo kwamba wanaingia kwenye misitu kwa nia mbaya ni kutokana na majanga ya ukame yanayoikabili ulimwengu kwa ujumla lakini pia mabadiliko ya tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili Mheshimiwa Waziri kama hatutakaa chini tutapata tatizo kubwa sana kwa ajili ya wananchi wengi na hasa wafugaji hao wanapopoteza mifugo yao na mwisho wa siku wale wa misitu wanavyowakamata wananauza bila hata kuangalia pande zote mbili na athari zinazotokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuona tunajipangaje kwa hali tuliyoona Afrika Mashariki kwenye majanga yale ya ukame mifugo imekufa sana kutokana na mabadiliko ya tabianchi, kwetu tuna kazi kubwa ya kubadilisha koo za mifugo, kupunguza idadi ya mifugo wengi wa kienyeji, kuja kwenye ufugaji wa tija pia kuangalia ufugaji unakuwa na tija na mifugo wanaopungua wale wanakuwa bora zaidi kulingana na mahitaji ya wakati wa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu kabisa tatizo hili la wingi wa mifugo litazidi kuongezeka kama taarifa yake ilivyosema leo, kama hatutachukua jukumu la kuwa na mashamba darasa ya kupunguza idadi ya mifugo pia unenepeshaji na namna ya kubadilisha koo za mifugo basi moja kwa moja tatizo hilo litakuwa kubwa kwa nchi yetu na mwisho wa siku umaskini utakuwa unaendela kukabili kundi hili la wafugaji ambao ndiyo kundi kubwa na mifugo hawa tunawategemea kwa namna mbalimbali kama ambavyo tunajua katika maisha yetu ya kila siku na ndiyo uchumi na maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kumkumbusha Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Rais katika ziara yake Mkoani Manyara, aliagiza maziwa yale ya Babati, Tlawi kule Mbulu na Bassotu aliagiza wataalam waende kuangalia namna ya kunusuru yale mabwawa kwa ajili ya shughuli za uvuvi lakini pia uwepo wa rasilimali hiyo. Timu yako ilikuja tunakupongeza sana, ilifanya kazi nzuri sana, ilitembea na wataalam wa Wilaya zetu lakini taarifa ile nadhani sasa ni karibu miezi Sita hazijaweza kurudi kwetu, nakuomba Mheshimiwa Waziri ile taarifa ifanyiwe kazi ili iweze kurudi na tuweze kujua matokeo ya ile taarifa ili tuweze kufanikiwa kwa jinsi ambavyo tunaweza tukaona ina tija na wananchi wetu wakapata mrejesho, wajibu wa wananchi ni nini kwenye ile taarifa au wajibu wa wataalam ni nini na wajibu wa Wizara ni upi, ili kuweza kulinda hizi rasilimali zilizoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza pia Serikali kwa kupeleka pikipiki, tumepeleka pikipiki kwa Maafisa Ugani wa mifugo, ingawa upelekeaji ule haukuwa mzuri kwa sababu mwenye watumishi Watatu alipelekewa pikipiki Tatu, mwenye watumishi Ishirini alipelekewa pikipiki Ishirini. Hii ilitokana na idadi ya watumishi walioko lakini haijaangalia rasilimali mahitaji yalivyo, ukubwa wa eneo na jinsi ambavyo kundi hili la wafugaji linavyohudumiwa na ni kubwa kiasi gani. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri kuna mambo mawili kwenye zoezi hili, kwanza ni kuendela kuona namna ya kuweza kupeleka pikipiki zaidi kwenye yale maeneo ambayo bado hayajapata pikipiki, kwa mfano, mimi nimepata tatu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uwezeshaji wa mafuta, Maafisa wetu tumewapelekea pikipiki Mheshimiwa Waziri hawana uwezo wa kupata hayo mafuta ya kuhudumia wananchi, kwa hiyo tuangalie utaratibu gani tunaweza tukafanya ili tuweze kuona pikikpiki hizo zinakuwa na tija kwa manufaa ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kuishauri Serikali kuona utaratibu wa namna gani tunapoanzisha mizani kwenye masoko. Mheshimiwa Waziri amebainisha kwenye hotuba yake kwamba sasa mifugo watauzwa kwa kilo minadani. Je, ni kwa kiasi gani mazingira hayo ya minada na masoko kwenye maeneo yetu tayari yana miundombinu ya kilo? Ili kusiwe eneo moja tu tunatoa huduma hiyo kwa kilo ama soko linaendeshwa kwa vipimo lakini eneo jingine halina miundombinu, pengine timu ingepita nchi nzima au wangeomba taarifa wao kama Wizara ili waone basi maeneo gani hawana mizani na nini kifanyike ili eneo hili la miundombinu ya mizani liweze kupatikana na kwa wingi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine kwa namna ya pekee ninaiomba Serikali itupatie fedha Milioni 130 niliandika barua Halmashauri ya Mji wa Mbulu kujenga masoko Milioni 130, wakati tunapeleka bajeti ile Milioni 130 wakawa wameiondoa. Mheshimiwa Waziri wewe mwenyewe unakumbuka nimekuja ofisini mara kadhaa, nilipokuomba uliniambia nikuandikie barua, nikakuandikia barua ya hali halisi ya Mji wa Mbulu na Halmashauri ya Mji wa Mbulu kwa sababu tayari tuna Kata Kumi ziko Vijijini na hatuna majosho. Kwenye ile barua ulinijibu kwamba itafanyiwa kazi, kwa hiyo naomba Wizara yako itazame upya uataratibu wa ujenzi wa majosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule ujenzi uliotumika kipindi kilichopita na ukarabati wa kipindi kilichopita haukuwa na tija sana kwa sababu ilionekana ukarabati wa majosho ulikuwa unasimamiwa na Wizara na fedha nyingi hazikuwa zimetoa matokeo chanya kwa maana ya thamani ya Shilingi, kwa hiyo ni jukumu letu wote kuona kwamba walau fedha zile zilizotengwa kwa ajili ya miundombinu ya majosho zinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchimbaji wa mabwawa. Sababu kubwa ya mifugo kuhama kwanza ni kuwa wengi halafu hawana tija wingi wao kwa mfugaji, pia ukosefu wa malisho na maji. Sababu hiyo inahitaji miundombinu ya mabwawa, kwa hiyo nafikiri kama inawezekana Mheshimiwa Waziri maeneo maalum yaainishwe kwa ajili ya kuchimba mabwawa pia ufugaji uwe wa kupunguza mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwenye Halmashauri zetu tuna vituo tumejenga nadhani miaka kumi ya huduma za mifugo na kilimo, vituo hivi kwa sasa havitumiki hasa kwenye Jimbo la Mbulu Mji. Utatumiaje vituo sita wakati wewe huna wataalam lakini pia dhana nzima ya kuanzishwa kwake ilikuwa ni namna pekee ya vituo hivyo vitoe elimu kwa wafugaji na semina kwa wafugaji pia na namna ya uzalishaji na uboreshaji wa wafugaji. Kwa hiyo, mimi nadhani kuna haja ya ile miundombinu kutumika, inazidi kuchakaa kama kwenye Jimbo langu inafika karibu sita haitumiki kwa sasa na tulijenga kwa gharama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwenye mpango huu kabambe wa sekta yako ya mifugo basi na eneo hili lifanyiwe kazi ili vituo vile vipate wataalam ambao ni wabobezi lakini pia wamesomea hiyo fani, watatoa elimu kwa wafugaji na wakati fulani semina mbalimbali na huduma za mifugo zinapatikana kwenye yale maeneo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa Zacharia Issaay.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Nakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti, basi mengine nitandika kwa maandishi naunga hoja mkono kwa asilimia 100.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja ya makadirio ya Wizara ya Ardhi. Kwanza nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake kwetu sisi sote na Taifa letu kwa ujumla maana yeye ndiye anayewezesha haya yote na uwepo wetu sisi lakini na baraka zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kumwombea na kumshukuru sana Hayati Baba wa Taifa Mheshimiwa Julius Kambarage Nyerere ambaye Serikali yake ya Awamu ya Kwanza iliona jambo hili la ardhi ya Tanzania kuwa mali ya Serikali ya Tanzania kinyume na nchi zinazotuzunguka. Hii imefanya thamani ya ardhi yetu kuwa mali yetu kama Watanzania lakini pia kutokuwa na mkanganyiko wa muingiliano kwa kuwa umilikishwaji wake unatolewa kwa Watanzania kwa dhamana ambayo Serikali inayo ili sisi wote kama Watanzania tuwe wapangaji kwenye ardhi. Kwa sababu tunaona migogoro mingi na umilikaji unaotumika katika baadhi ya nchi ambao unamilikiwa na watu kutoka nje na wageni na unao leta mkanganyiko kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza pia Mheshimiwa Rais. Zipo kazi nyingi sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amejitahidi katika Serikali ya Awamu ya Sita na Serikali zote zilizopita kwa jinsi ambavyo nchi yetu inakwenda mbele na tunasonga mbele katika muundo wa Serikali, lakini kwa maendeleo na huduma kwa wananchi. Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi kubwa sana. Hatutaweza kupata muda wa kutosha kuzungumzia jambo hili tukiwa humu, niwaombe Wabunge wenzangu wote tuwe wakalimani wa kwenda kuyazungumza hayo kwa wananchi na kutafsiri kwa wananchi wetu. Ushahidi kila Mbunge anao kwenye Jimbo lake na katika eneo lake kwa jinsi ambavyo Serikali imejitahidi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi pia kwa Wizara, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji kwa sababu tunajua mapungufu hayataisha, lakini tunaona hatua zinavyochukuliwa na tunavyojaribu kusonga mbele na kupata mafanikio kupitia Wizara hii. Zipo changamoto nyingi lakini kwa ujumla nchi haijengwi siku moja. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu tunampongeza Waziri na timu yake na wale Mawaziri waliopita, Mbulu Mji tumepewa fedha za upimaji na umilikishwaji lakini kupima, kupanga na kumilikisha. Ni fedha ya maoteo inayotolewa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza zoezi hili la upimaji wa mipango miji. Zoezi hili la upimaji mipango miji na fedha hizi hazina riba, ni fedha zinazotolewa na Serikali na baadaye tunarudisha bila riba, lakini imefanya tatizo kubwa la ujenzi holela wa miji yetu kupungua kwa sababu kadri tunavyopima tunaondoa mgogoro wa upimaji, lakini pia tunaondoa mgogoro ambao unazalishwa na kesi za muingiliano na kesi za kunyang’anyana ardhi baina ya wananchi na wananchi, ama taasisi; ama mtu na mtu hali ambayo inaifanya na kuipeleka mipango miji, lakini na umilikaji wa ardhi kuwa na hatua nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi zilipotolewa katika Halmashauri mbalimbali na Mbulu ikiwemo imekumbwa na changamoto nyingi sana na changamoto kubwa ni uhaba wa watumishi. Unakuta kwenye Halmashauri moja Afisa Ardhi ni mmoja, Afisa Mipango Miji ni mmoja lakini wanaohitajika kwenye zoezi zima wanaweza kufika kumi na ilipofika hapo halmashauri nyingi zilitafuta makampuni kwa njia ya tender ama kwa njia ya nukuu za bei, lakini zile kampuni zilizopatikana kwa namna moja au nyingine hazijatusaidia kwa jinsi inavyopasa na jinsi ambavyo manufaa na matokeo mazuri ya zoezi hili au ya fedha hizi zinapatikana katika halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano fedha nyingi zinakwenda kwenye ukodishaji wa vifaa, kulipa wataalam lakini pia na uandaaji wa mipango kitu ambacho kinafanya eneo hili la upimaji kukosa mafanikio makubwa. Rai yangu hapa ni kwamba pengine Serikali katika mipango yake ya mwaka huu na miaka inayokuja iangalie zile kada muhimu sana za ajira katika Wizara hii ya Ardhi ili utekelezaji wa Serikali ipate ufanisi na mafanikio zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu huu wa watumishi katika Sekta ya Ardhi unakwaza shughuli nyingi. Kwa hiyo, tusipouondoa ina maana huna rasilimali watumishi lakini pia na ufanisi unatarajiwa ili kufikiwa katika hatua inayofaa. Mara nyingi fedha hizi zinapotolewa elimu kwa wananchi ni ndogo sana kwa wale wanaosema upimaji umekuwa na gharama kubwa tatizo kwenye upimaji sikuona kwa upimaji ushirikishi kwa sababu gharama zinazotolewa kupima viwanja ni gharama zinazotekelezeka, tatizo kubwa ni uhamasishaji, tafsiri ya mwanzo kwa wananchi katika elimu kwa jinsi ambavyo tunataka eneo hilo liwe kwenye mipangoo miji na liweze kupimwa na kupatiwa michoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa sasa nataka kuishauri Serikali, twendeni kwa pamoja kama Wizara tuone utatuzi wa jambo hili unafanyika ili kuondoa matatizo makubwa kwa sababu tayari shule zilizopimwa, taasisi zingine zilizopimwa lakini pia maeneo ya miji yaliyopimwa yana dosari mbalimbali na kwa zoezi lolote lile linalofanyika lazima lifike muda tufanye tathmini na changamoto zilizoko na mafanikio yaliyopatikana ili zoezi lililotarajiwa liweze kufanikiwa na kupata mafanikio mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hivi kwa sababu fedha hizi kwa kadri zilivyotolewa kuna migogoro, unakuta Wilaya na Wilaya kuna migogoro, Mikoa na Mikoa kuna migogoro na Mkoa wa Manyara una migogoro ya ardhi kwa kiasi kikubwa sana hasa hasa hizi za mipaka ya maeneo ya utawala, lakini pia migogoro ya taasisi na taasisi lakini pia na migogoro ya mtu na mtu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali walitupa Baraza la Ardhi kule Dongobesh, lakini hata hivyo msaada wa lile baraza utapatikana na utatoa tija endapo ardhi hii itapimwa, lakini pia mipaka ya kila mmoja ikaainishwa na zoezi hili likafanikiwa ili kuondoa kesi nyingi na malalamiko mengi kwa wananchi.

Kwa hiyo, naiomba Serikali eneo la Mkoa wa Manyara, ukienda Wilaya ya Simanjiro ni migogoro isiyoisha. Nikupongeze Mheshimiwa Waziri na timu ya Mawaziri imeenda mara kadhaa, Wilaya ya Kiteto ni migogoro isiyoisha Wilaya ya Babati ni migogoro isiyoisha, Wilaya ya Mbulu ni migogoro isiyoisha. Niombe tathmini ya ile timu ifanyike, mrejeshio upelekwe kwa wananchi baadae, na tafsiri ya Sheria zitakazokuja baadae zitolewe kwa wananchi kwamba baada ya mapendekezo yaliyotolewa fikra za wananchi wale, mrejesho wa wananchi upatikane na tuweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze eneo la mabaraza ya ardhi; Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Dongobesh Mheshimiwa Waziri anahudumia mabaraza mawili, kwa hiyo kesi nyingi huwa zinakwama pale Dongobesh kwa ajili ya kwamba anakuwa anahudumia Wilaya nyingine kule Ngorongoro na huku anahudumia Mbulu.

Nilikuwa naomba kwenye bajeti hii kama itawezekana baadhi ya mabaraza yaliyo anzishwa yapate Wenyeviti wake ili walau kupunguza msongamano wa kesi katika maeneo mengi na hili tuweze kupata manufaa ya wananchi kuhudumiwa kwa wakati, lakini pia kutokinung’unikia chombo hiki ambacho kinatarajiwa kutoa utatuzi wa matatizo hayo yaliyoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi sana yanahitaji kufanyiwa kazi katika sekta ya ardhi na kwa sababu hiyo eneo la Wizara hii tunaishukuru Serikali imeitengea fedha kwa yale mapungufu yanayoonekana basi Mheshimiwa Waziri mimi nikupongeze, lakini pengine Serikali ione kwa umuhimu fedha inazotenga kwenye Wizara hii ipeleke kwa kiasi kilichopendekezwa ili kutatua matatizo ya wananchi katika eneo hili la ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo mahususi yatolewe na Wizara kwenda kwenye Halmashauri zetu. Shule za msingi, taasisi za dini, shule za sekondari, na maeneo mengine na mipaka ya vijiji yakipewa kipaumbele ina maana tunaenda chini kwa kadri ambavyo kila eneo tunakwenda kupima na kuonesha mipaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna zoezi linalolalamikiwa kwenye KKK; zoezi la KKK limekumbwa na tatizo, mwanzoni wakati tunakwenda kwa wananchi tunasema tunakuja kupima, halafu tunakuja na umilikishwaji. Katika hatua ya umilikishwaji hatufiki tunaishia kupima na kuweka beacon, kampuni zile zinaondoka, zikiondoka maeneo yale yaliyowekwa alama yanabaki kukosa alama za kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nilikuwa nashauri, kuliko kuchukua eneo kubwa la upimaji lenye kupigwa nondo bila beacon na ambalo halipewi hatimiliki, mimi nadhani ni muhimu tukapima eneo dogo tukakamilisha zoezi letu, lakini kwa tafsiri ya makubaliano ya pamoja kati ya Halmashauri zetu na wale wanopimiwa ili wapate hati na tujue zoezi la eneo hilo limekwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu zile kampuni zikiishaondoka unakuta zile beacon baada ya muda hazina alama kwa sababu ni nondo zilipigwa, alama zile zinafutika, awamu nyingine tunaenda tena kupima yale maeneo na zile kampuni kwenye usimamizi na maombi ya fedha zilishaomba kwamba watamaliza mchakato wote na kila aliyepimiwa atapewa hati ili fedha zile ziwe na tija na manufaa kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza suala la Mabaraza ya Ardhi; Mabaraza ya Ardhi katika meneo mengi yanakaa kwa muda mrefu. Swali langu kwa Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay na muda wako umekwisha.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie nashukuru sana na naunga hoja mkono kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Niungane na Wabunge wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa rehema zake, baraka zake lakini kama Taifa kwa jinsi anavyotulinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais kuna mambo mengi tunampongeza kwa ajili ya Serikali kutekeleza mambo mengi, ukiacha Wizara moja moja, kwa ujumla katika nchi yetu twendeni kila Mbunge kwenye Majimbo yetu tukaeleze yale mafanikio ya Serikali ili agenda hii ya kumpongeza Rais iwe agenda yenye mashiko na inayoonesha taswira nzuri kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza kwa sehemu kidogo Mheshimiwa Waziri lakini pia nimweleze duku duku na maeneo ambayo ninadhani pengine kupitia ujumbe wangu huu yataboreshwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na eneo la Mbulu Mjini, Jimbo la Mbulu Mji ina mitaa 58, Kata sita za mji, vijiji 34 na Kata 10 ziko vijijini. Siyo kama tunavyozungumza Mbulu Mji kama Mji, Mbulu Mji una sura mbili, nianze na sura ya eneo la mji na kwa sababu hali hii ipo katika maeneo mengine hata kwa Majimbo yetu kwa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Mbulu Mji wale wa pale katikati utakuta yuko ndani ya kilometa moja kutoka katikati ya mji lakini hajafungiwa umeme lakini amemaliza wiring na yuko ndani ya mita 30 ya nguzo. Hapa ushauri wangu ni kwamba niungane na mwenzangu Mheshimiwa Francis Isack alivyozungumza, twendeni tukafanye tathmini ya maeneo ya miji yetu na hali ya uhitaji wa umeme na wale waliofanya wiring, hapa tunatafutiana ajali za kisiasa kwa sababu moja kwa moja wananchi waliofanya wiring leo unapowaambia waunganishiwe umeme kwa shilingi 320,000 wakati shilingi 27,000 ingeunganisha wao wana matumizi makubwa lakini pia wako ndani ya mji kwa maana ya ndani ya kilometa moja ama mbili. Hali hii itaifanya matumizi makubwa ya umeme kupatikana lakini na uzalishaji kuja juu na kwa vyovyote wananchi wale watakuwa wamefunga umeme huu katika majumba yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuelimishane au tuambizane na tutazame kwa sura tofauti kila Mbunge kwenye eno lake, kwa hali ya uchumi wa wananchi wetu ni mwanancni gani ana uwezo wa kulipa shilingi 320,000 akafanya wiring tena kwa shilingi 320,000 na mambo mengine, umeme wenyewe kwenye jengo hilo moja shilingi 700,000? Hii ni hali ambayo kwa vyovyote haiwezekani Mheshimiwa Waziri, utakapokuja pale toa kauli kama Serikali eneo hili la uunganishwaji wa umeme wa awali Serikali ije na njia mbadala ya kuunganisha umeme kwenye makazi ya watu kwa maeneo ya mjini na vijijini kwa sababu eneo hili la mji zamani wakati wanafanya wiring wananchi walitegemea sana kwamba eneo hili wanaunganishiwa umeme kwa shilingi 27,000 wao wanapata gharama ya kufanya wiring kwa maana ya kufanya uunganishaji wa waya kwenye majengo yao ili wapate huduma ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la vijijini kwa Mbulu Mji utakuta kijiji cha mwisho kilometa 40, ndani ya kijiji hicho tunapopeleka kilometa mbili, kwenda kwenye vitongoji utakuta kitongoji kutoka katikati ya kijiji ni kilometa 20 ama 15 tena, kwa hiyo, nguzo za kwenda huko ni nyingi. Mimi ushauri wangu kwenye eno hili nilikuwa naangalia tunapoanza kuweka umeme kwenye maeneo ya vijijini tuangalie utaratibu ambao utashika kaya nyingi na nyumba nyingi ili ziingizwe kwenye mfumo huu wa kuunganisha umeme. Eneo hili la vijijini ndiko waliko wananchi wengi, matumizi yao siyo makubwa, wao sana sana watatumia umeme kwa taa, kuchaji simu na huduma zingine ndogo ndogo lakini mambo ya friji na mambo ya mitambo mingine haitakuwepo sana zaidi ya mashine za kusaga na vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa nafikiri kama inawezekana eneo hili litazamwe na Wizara. Mheshimiwa Waziri timu yako imepita mara nyingi na mara nyingi umetuletea mipango hii ya vipaumbele kwenye vikao vyetu vya bajeti, kwa bahati nzuri baadhi ya maeneo mengi Serikali imejitahidi kuangalia ni namna gani umeme unakwenda. Kwa hiyo Jimbo langu la Mbulu Mji, vijiji vyote umeweka nguzo, vingine vina miezi miwili, vingine miezi mitatu, vingine sita umeme haujawaka. Hali ambayo nguzo zile zinazidi kuoza, mimi nilikuwa nafikiri uwekaji wa nguzo utegemeane na waya na vifaa vingine ambapo ukisimika nguzo hizo, walau umeme unawaka kwenye hicho kijiji ili unahamia kijiji kingine kuleta sura ya matumizi lakini na pia sura ya kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati uliosahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeruka maeneo mengi ya taasisi za umma, migodi, pampu za maji, taasisi binafsi na mashirika ya umma, nadhani kuna haja ya kufanya tathmini upya ili hayo maeneo ya taasisi za umma yakiwemo makanisa na taasisi zingine na shule lakini pia na visima na maeneo mengine ya muhimu kama migodi tukaona namna ya uunganishwaji wa umeme. Mimi kule kuna wachimbaji wadogo wako mwaka wa 10 nadhani wanachimba lakini umeme haujafika mpaka leo, wakisubiri umeme waunganishiwe na kule kuna uzalishaji mkubwa.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hizi zingeachwa kwanza ili tuokoe muda.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Issaay taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kuchauka.

TAARIFA

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mchangiaji amesema kwamba kweli kunatakiwa umeme ufikishwe kwenye baadhi ya taasisi, kwa mfano kwenye nguzo na hii minara ya simu, minara ya simu mingi inaendeshwa kwa ma-generator kwa hiyo mimi nilifikiri kwamba ingetoka sera kabisa kwamba, pamoja na kwamba unapozungumzia taasisi tuzungumzie vilevile kwenye minara ya simu kote kufikiwe na umeme.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Zacharia taarifa unaipokea.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea ni ufinyu wa muda tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia eneo hili la kukatia kwa umeme na migao ya umeme. Hili ni janga na hii ni ajali ya kisiasa pia. Wabunge Majimboni hatukai, umeme unakatika wananchi wanatulalamikia, umeme unakuwa wa mgao, wananchi wanatulalamikia, tuangalie mgao huu namna ambavyo tutaupunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbulu Mji linaongoza kwa mgao wa umeme na kukatika kwa umeme, nafikiri kama inawezekana sababu zitolewe mapema na wananchi wajiandae kwa sababu umeme ni uchumi, umeme ni huduma, umeme pia unaleta mafanikio kwa wananchi kufanya shughuli zao kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili litazamwe ili ukataji wa umeme na mgao upungue, tumekuwa na matatizo makubwa kwenye eneo hili hasa kwa mwaka huu tulionao pengine ni umeme ulikuwa mdogo kutokana na mabadiliko ya tabianchi lakini pia na hali ya maji kwenye mabwawa, tuangalie pia utaratibu wa kuzalisha umeme kwa njia ya upepo. Eneo hili la Kanda ya Kati tunao uwezo wa kuzalisha umeme wa upepo. Tafiti zilishafanyika, Serikali iangalie utaratibu sasa wa kuzalisha huo umeme ili uweze kunufaisha wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuangalie utaratibu huu wa nauli. Mheshimiwa Waziri ruzuku ya Serikali tumeweka kwenye mafuta, Serikali tunaishukuru kwa kuweka ruzuku ya fedha kwenye ununuzi wa mafuta, hali hii haijapunguza mpaka leo. Wakati tunaweka ruzuku lita ya mafuta ilikuwa shilingi 3,350 saa hizi lita ya mafuta ni shilingi 2,930. Kuna tofauti ya karibu shilingi 500 kwa lita lakini nauli haijapungua. Tutazame eneo hili kama sababu zinatosha za gharama za nauli kubaki pale halafu huku tumeweka ruzuku ya Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ni eneo ambalo tunapenda kuishauri sana Serikali itoe fedha za Wizara hii kadri ambavyo zimeombwa na Mheshimiwa Waziri na Wizara yake ili walau mgongano huu wa kulia umeme na kuomba umeme mara kwa mara upungue, kwa sababu yale yaliyowekwa kwenye vipaumbele hivi na Mheshimiwa Waziri viweze kutekelezwa na ili vitekelezwe ni fedha tulizoomba Serikali ijitahidi namna ya kutoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ingawa siyo kwa umuhimu, ninaomba basi hali hii ya baadhi ya maeneo kwenye mji, Mheshimiwa Waziri tuma timu, fanya ziara mahususi na wewe kwenye maeneo ya Miji kama Mbulu na vijiji vyake. Ninawapongeza Waheshimiwa Mawaziri tuliyowaambia Mbulu Mji una maeneo mawili na maeneo hayo mawili kwa ujumla yameweza kutembelewa na kila Wizara iliona jitihada zake na kuongeza fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga hoja mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Awali ya yote, naungana na Wabunge wenzangu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyetujalia kuiona siku ya leo na baraka zake kwa nyakati tofauti tofauti. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu maisha yetu ni rasilimali na hazina anayotujalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mji, nathibitisha kabisa kwamba mambo mengi niliyokuwa nimeahidi kwenye uchaguzi, yametekelezwa kwa asilimia kubwa sana. Nampongeza Mheshimiwa Rais, Mawaziri, kuanzia kwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wote. Kwa sababu mwaka jana 2022, wakati tunahitimisha Bunge la Bajeti nilikuwa nimesema nashika shilingi ya Mheshimiwa Waziri Mwigulu, akanitania siku moja akasema, “kwa umri wako ukishika Shilingi na hurudishi itakuaje?” Nikawa nacheka. Kwa maana ya kuona kwamba ninahofia yale mambo ambayo tuliyaandika kwenye bajeti na hayatatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa staha na furaha kubwa kwa niaba ya wananchi, naipongeza sana Serikali kwa sababu kazi kubwa imefanyika, na pia ndani ya mwezi huu wa Sita nadhani, kuanzia tulipoanza hili Bunge letu la Bajeti mpaka sasa, Jimbo la Mbulu Mji limepokea fedha nyingi sana kutoka Serikalini. Fedha zilizopokelewa, nyingine hata hazikuwa kwenye mpango ule wa awali, zilikuwa zinazokuja kama fedha za kimkakati kwa ajili ya kutatua matatizo ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa sababu Mbulu Mji, sisi wananchi wake kama Halmashauri, tunakusanya mapato madogo sana, lakini mahitaji yetu ni makubwa sana Serikalini, kiasi kwamba wakati fulani unajiuliza, sasa hayo tutayatatuaje? Kwa hiyo, natuma ujumbe huu kwa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri wote kuwashukuru sana. Kwa sababu kila sekta katika mwaka huu wa bajeti ni takribani karibu Shilingi bilioni saba au nane zimepelekwa kwenye Jimbo la Mbulu Mji, katika robo hii ambayo tunamaliza sasa kama dakika za mwisho za kumalizia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Makamu wa Rais kwa ziara anazofanya katika majimbo yetu. Pia, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ya hivi karibuni kule Jijini Arusha katika halaiki ya kanisa kwa ajili ya kuelezea hali halisi ya taharuki ambayo Watanzania wanaichukulia kwa hatua ya tofauti zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kutoa mchango wangu mchache sasa. Kwanza niungane na Wabunge wenzangu ambao walikuwa wanaipigia kelele dhana hii ya kuondoa au kupunguza kodi kwa bidhaa ya mafuta kutoka nje, na bidhaa nyingine, lakini tunataka kuingiza bidhaa hiyo, kupunguza na kujenga soko la ndani. Niseme tu kwamba, nchi yoyote ni lazima ijenge uchumi wake wa ndani ili iweze kwenda mbele, kwa sababu nchi nyingi zinajenga uchumi wa chini na uchumi wa kati na baadaye inaenda kwenye uchumi wa kuuza nje na pia kujenga uwezo wa wananchi katika rasimali walizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naungana na Wabunge wenzangu kwamba eneo hili la kupunguza kodi kwenye bidhaa za nje pengine itaua viwanda vya ndani na mwisho wake wananchi wetu watashindwa katika uzalishaji. Kwa sababu hali ya uzalishaji itatofautiana na ile ya kipato wanachopata hasa kwenye sekta ya kilimo na sekta zingine kwa ajili ya kupungua kwa gharama kubwa na uchumi kushuka na bidhaa zetu kushindwa kushindana na bidhaa zinazotoka nje. Kwa hiyo, rai yangu hapa ni kwamba tuangalie kwa umakini sana eneo hili na pia kulinda viwanda vya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita lile la miaka mitano, kwenye Halmashauri tulikuwa na viwanda vya ndani kama 100. Vile viwanda vilishafika hatua ya kuchakata na kufungasha malighafi za ndani, na pia viwanda vile vilikuwa vinatoa ajira kwa wananchi wa chini, wale waliioko kwenye majimbo. Vimekuja kufa kwa ajili ya matatizo ya wataalam na uelewa mdogo wa usimamizi, kutokana na kwamba hatukua na muundo mzuri. Hapa ushauri wangu ni kwamba tuangalie muundo wa SIDO na taasisi nyingine zitakazolinda viwanda vya ndani hasa hizi ndogo ndogo ambazo zinafungasha mazao ya wananchi. Pia kule kuna ajira za muda za wale wanaofanya vibarua, na pia maisha ya wananchi wetu yanaendelea na huduma za familia zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nashauri kama itawezekana, tuijengee uwezo SIDO, na tuwe na matawi ya SIDO kwenye wilaya zetu ili kuvilea viwanda vidogo vya chini kwa ajili ya kujenga uwezo wa wananchi. Tunapozungumza uwezo wa wananchi, tunachukua kundi kubwa la viwanda vidogo vidogo ambavyo watafanyakazi, watarudi makwao, lakini Maisha yao yanaendelea, wanasomesha watoto na pia wanapata huduma ya kila siku kupitia familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza sana Serikali kuondoa kodi. Miaka miwili iliyopita nilikuwa nimeuliza swali hapa Bungeni kwa ajili ya vijana wa vyuo vya chini na vyuo vya kati kuwa na gharama kubwa ya kuwasomesha, na vijana wengi wanashindwa na familia nyingi zinalemewa kwa ajili ya gharama. Kwa sababu tulikuwa tunakuta mwanafunzi anayesoma pengine Shahada ya Chuo Kikuu anasoma kwa gharama sawa na yule ambaye anasoma chuo cha cheti, wakati mwananchi yule anayemshomesha yule, gharama ile ilikuwa hailingani na kipato chake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunamshukuru Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ajili ya kuondoa ada hizi na gharama hizi katika baadhi ya vyuo. Rai yangu hapa ni kwamba tuangalie vyuo vingine pia ambavyo kwa uwezo wetu tukijijenga, tuweze kuwaweka na kundi hilo la vyuo vya cheti na vyuo vingine ili kujenga uwezo wa watendaji au watumishi ama wataalamu wa ngazi hizi za chini. Kwa sababu hata kufa kwa viwanda ni pamoja na hawa wataalamu wa ngazi za chini wanakuwa wachache. Kwa hiyo, tatizo hili ni kubwa kwa kadiri mnavyoona. Kwa vyovyote vile, hapa tunamwondolea mwananchi gharama kubwa. Alishamsomesha mtoto shule ya kata na sasa anaenda kwenye chuo kwa ajili ya kumjengea uwezo ili aweze kukabiliana na hali ya ulimwengu unaokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu haya ni majumuisho, katika taarifa yetu ya bajeti kuu, tumeongelea eneo hili la wastaafu. Wastaafu wa zamani pensheni yao ni shilingi 100,000 kwa mwezi. Yaani bima anayotakiwa ahudumiwe kwa maisha aliyonayo, inaweza kuwa shilingi 600,000, lakini yeye kwa mwezi anachopata ni shilingi 100,000 au shilingi 150,000. Nadhani Serikali itazame vizuri, iangalie namna gani watumishi hawa waliotumikia Taifa letu tunawaangalia ili nao basi wasiombolezee Serikali yetu, lakini pia wawe na amani wanapoelekea katika uzee wao na waweze kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niongelee eneo la kuongeza ukusanyaji au utaratibu wa ukusanyaji wa mapato. Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kwenye kuhitimisha, angetuambia sisi Wabunge basi, kwa Serikali na taasisi za umma, ni lini siku ya mwisho ya matumizi ya mashine za POS kukusanya fedha za Serikali? Kwa sababu huko ndiko ambao fedha nyingi tunashindwa kukusanya na pia kuingia kwenye mfumo wa Serikali, kujenga uchumi wa nchi yetu na pia mapato yetu kuwa halisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna fedha mbichi zinazopotea katika corridor hiyo au katika muundo huo na tutakapotoa tamko; kwa sababu kama tunafanya mambo makubwa sana hayo, tukumbuke kuwa hata na hilo la POS linawezekana kwa nchi yetu. Tutafute muundo wa maeneo yote hayo ambayo yanakusanya mapato ya Serikali, yawe yanaingia kwenye mfumo na kuweza kuwa na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni kwamba bado tunahitaji kujenga uwezo wa wakusanyaji, kwa maana, kuna wilaya zetu nyingi hazina majengo ya wakusanyaji kwa maana ya TRA. Pia katika halmashauri hatuna Maafisa ambao wanaweza kukidhi haja na kujaza nafasi hizo ambazo ni muhimu sana katika makusanyo ya Serikali. Nilikuwa nafikiri hilo litatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwamba tumehangaika sana, hatuwezi kuwaajiri hawa vijana waliomaliza chuo, hawa ambao tayari wengine ni wa certificate wengine ni wa diploma, wengine ni wa degree. Serikali ione kwamba namna pekee ya hawa vijana kupata ajira ni kuangalia sheria za sekta binafsi za ajira, na maslahi katika sekta binafsi kwenye ajira, na pia namna ambavyo tutachochea kupitia viwanda ambavyo tutakuwa navyo ndani ya nchi na vijana wataajiriwa kutokana na taaluma zao ili kuondoa mzigo mkubwa uliopo kwa Serikali. Kwa sababu kwa vyovyote vile, mbele ya safari Serikali haitaweza kubeba jukumu hili la kuwaajiri hao vijana, kwa sababu kila mwaka wanamaliza masomo yao na wanapomaliza wanaiangalia Serikali kama baba yao ili iweze kuwaajiri na hawataajirika kwa sababu ya uchache wa nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mwaka wa fedha unaokuja tuone namna ya kuajiri zile takwimu ambazo tumeziombea kwa ajili ya kupunguza idadi kubwa ya hao vijana. Tunajua hatuwezi kuajiri mara moja, lakini angalau tutafute madirisha ya kuajiri. Hata katika nchi zinazotuzunguka kwa uhusiano mzuri tulionao, basi tuwe na sehemu hiyo ya kulielezea jambo hili katika sura ambayo inaweza ikaleta tafsiri nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali, siyo kuilaumu tu; hata kwa hii hatua iliyoichukua ya mazao, kwa maana kuna muundo rasmi unaoandaliwa ili kuona kwamba angalau hata kama tutauza mauzo nje, Serikali itapata kodi, na pia hatutauza yote baadaye tukabaki na njaa ambayo ni janga la Taifa na mwisho wa siku haitawezekana. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri aliyekuwa anatoa tafsiri hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni Mamlaka ya Chakula na Lishe, kwa maana ya hasara inayotokea katika nchi yetu ni kubwa sana, kwa sababu ya uteketezaji wa bidhaa bandia na bidhaa ambazo zinazoingizwa nchini na tunazotengeneza kama bidhaa feki. Nilikuwa nashauri, kama itawezekana, tutazame muundo wetu wa kudhibiti uingizaji na utengenezaji wa bidhaa bandia, kwa sababu wanaoathirika sana sio wahusika, ni wale wafanyabiashara wa kawaida na wanapokamatwa kwa kukutwa na hiyo bidhaa, wanapata hasara kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muundo wa taasisi hii tukiutazama na namna ambavyo utaweza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nitachangia mengine kwa maandishi kwa sababu nina mambo mengi sana niliyaorodhesha katika mchango wangu wa leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na ninaunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kwanza kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa jinsi anavyofanya kazi kubwa ya kulitumikia Taifa letu na hususani katika kukemea yale yote ambayo yanakinzana na matakwa ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kumpongeza sana mpendwa ndugu yetu Mheshimiwa William Lukuvi kwa kazi kubwa aliyofanya kule Mbulu. Nampongeza sana namwombea kwa Watanzania wote na kazi anayofanya kwa nchi yetu ni kubwa kwa dakika hii ya sasa na jinsi ambavyo ardhi ni eneo lenye matatizo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwanza kuiasa Serikali, mara nyingi tumepata matatizo mengi hasa yale yanayotokea baada ya wananchi kujenga, wananchi wanapimiwa na Maafisa wa Serikali katika maeneo ya hifadhi na maeneo ambayo hayafai kwa makazi, baadaye Serikali inaenda kubomoa bila hata fidia. Naiomba Serikali ianze kuainisha maeneo yote ambayo hayafai kwa matumizi mbalimbali ya wananchi wetu yakiwemo yale ya mikondo ya maji na yale ambayo ni hatarishi kwa maisha yao ili kuepuka hasara kubwa na matatizo mbalimbali yanayotokea baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuwataka watu wa barabara na wale wengine wote wanaotumia ardhi, kwa sababu mara nyingi sana tumekuwa na tatizo la kubomoa majengo baada ya wananchi kujenga na wanapata madhara makubwa hasa ya kiuchumi. Kwa hiyo, ningeiomba Serikali iainishe hata yale ya barabara. Tumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais alipokuwa Waziri wa barabara aliweka alama X kwenye mtandao wa barabara zote nchini na kwa hivyo nyumba nyingi hazikujengwa hadi sasa na zile zilizokuwepo zinaendelea kuchoka lakini pia ione umuhimu wa kufidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kuongelea eneo hili la fidia, wananchi wengi wanapata hali siyo nzuri kutokana na kwamba baada ya mtu kujenga anabomolewa jengo, madhara ni makubwa sana na kwa hivyo niitake Serikali iwe inaangalia madhara makubwa yanayompata Mtanzania wakati wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la Watumishi wa Serikali. Wote tunafahamu kuwa wale waliojenga kwenye mikondo ya maji na waliojenga kwenye barabara walipimiwa na watumishi wa Serikali ambao ni wataalam, haijalishi ni mtaalam wa aina gani lakini alienda kumpimia yule mtu. Leo hii tunapofika hatua ya kwenda kubomoa yale majengo bila fidia bila hali ya kuangalia ni kwa namna gani mwananchi yule anadhurika, hatuwatendei Watanzania haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji wengine wamegawa plot mara mbili kwa Mtanzania mmoja, hali inayoleta migogoro mikubwa kati ya mtu na mtu au taasisi na taasisi. Naomba Serikali iangalie ni kwa namna gani inajitahidi kuona athari za namna hizi zinachukuliwa hatua za kimsingi na zile za mpango mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kuwepo na mpango kabambe wa wananchi kupata hati miliki. Hati miliki itaondoa mgogoro mkubwa wa ardhi kwa asilimia kubwa nchini. Iwezekane basi hata namna ya wananchi na Serikali yao kuingia ubia, zipi gharama za Serikali na ipi gharama ya mwananchi ili apate hatimiliki katika ardhi anayomiliki sasa. Kumekuwa na tatizo kubwa la kesi nyingi za ardhi kubadilishwa kutoka kesi ya ardhi kwenda kuwa kesi ya jinai kwa ajili ya uelewa mdogo wa wananchi. Naiomba Serikali itafute njia mbadala ya kuondoa tatizo hili kwa kutenga fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Wizara hii ilipowasilishwa imekuwa ni bajeti ndogo kuliko tulivyotarajia. Tulitarajia tungekuwa na mpango kabambe wa wananchi kupata hatimiliki, lakini kwa ubia wa gharama kati ya Serikali na wao ili kuwezesha wananchi kumiliki ardhi yao na kuondoa migogoro mikubwa inayotokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inabidi kukemea hii hali ya rushwa kwenye Mabaraza ya Ardhi. Maana siyo kwamba Wapinzani wakizungumza mambo yote ni ya uongo, mengine ni ya ukweli lazima tutazame na tuone tunafanyaje wakati inapobidi. Serikali isione tu kwamba hali ya kuachia vyombo vya kiutendaji ni hali ya kawaida, inaendesha inavyotaka, inaendesha kwa mfumo huu wa kidikteta, inaendesha kwa mfumo wa rushwa na wakati huo huo wananchi wanaumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niitake Serikali kutazama upya watumishi wote au watendaji wote wa Mabaraza ya Ardhi na matendo yao na kuona ni namna gani wale ambao hawafai kabisa na wanatumia madaraka yao vibaya wanaondolewa kwenye system ya utendaji wa chombo hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika hali hii wananchi wengi wanashindwa kutetea haki yao kutokana na uelewa mdogo wa kisheria. Uelewa wa kutetea haki yao na pale wanapotaka kutetea haki yao wananchi wengi hawana uwezo na kwa hivyo wanashindwa kutetea haki yao lakini hali hii inasababisha madhara makubwa kwa wananchi kukosa haki yao na hatimaye kubaki na hali ya sintofahamu na kupoteza haki yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naitaka Wizara iwe na mpango kabambe wa kuona maeneo yenye matatizo ya ardhi au migogoro ya ardhi, basi wanafanyiwa utaratibu wa kuanzishiwa Mabaraza ya Ardhi yakiwemo yale ya Wilaya kwa ajili ya kupunguza umbali mkubwa na gharama kubwa wanayopata wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wana kipato kidogo, hawawezi kuweka Wakili, hawawezi kwenda kwenye Mahakama ambayo iko mbali na makazi yao na kwa hivyo hawana uwezo wa kutetea haki yao ya kimsingi na wanaacha inapotea bure. Kama itawezekana pia kuwe na utetezi wa Wanasheria wa Halmashauri kutetea kesi zinazoingiliana na zile za Halmashauri na Halmashauri nyingine au kijiji na kijiji kingine kwa ajili ya utatuzi wa kero hizi na migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwa sababu muda huu ni mdogo, nimwombe Mheshimiwa Waziri alituahidi kule Mbulu kuanzishwa kwa Baraza la Ardhi Wilayani Mbulu. Namwomba sana katika bajeti hii haionekani, lakini sisi tayari tumetimiza wajibu wetu tutamwandikia barua Wabunge wote wa Majimbo mawili, Baraza hilo kwa mwaka huu lazima liwepo awe na majibu wakati wa kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nimtakie kazi njema Mheshimiwa Lukuvi, niwatakie Watanzania wote utashi mwema wa kuiona nchi yetu inakwenda vizuri na niwashukuru sana kwa jinsi ambavyo Baraza letu la Mawaziri linafanya vizuri sana na wanajitahidi, kukejeliwa ni jambo la kawaida, tunaongezewa speed, tuwe na speed kali sana. Ahsanteni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, kukejeliwa ni kuongezewa mwendo wa safari, nawashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana. Na mimi naomba nitoe mchango wangu mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niamze kwa masikitiko katika Wizara hii. Kama ambavyo wenzangu wameongea kama pato la Wizara hii ni shilingi bilioni moja, na sisi Watanzania tunapigwa bakora, wananchi wanaenda kwenye msitu wanapigwa bakora, ifike mahali tuone basi kile kinachopatikana kina tija kiasi gani. Ninaomba sheria ya Wizara hii iwekwe mbele ya Bunge hili tuipitie upya yote tuangalie upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria nyingi za Wizara hii zimekuwa kandamizi na hii inaipelekea jamii yetu kupata matatizo mara nyingi hasa wale wanaokaa na kukutana na mazingira yale ya hifadhi. Kwa hiyo, naomba sheria itazamwe upya mbele ya Bunge hili ili tuione jinsi ambavyo inaenda na wakati wa sasa na pia ni sheria yenye manufaa kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ninaomba basi pia tutazame, muone jinsi ambavyo fidia inayotolewa ni ya ajabu sana. Mwaka jana kabla ya mwezi Oktoba tembo walitoka Msitu wa Marang wakaenda mpaka kwenye Wilaya yangu ndani ya Jimbo langu wakaua watu watatu hadi mazishi hakuna mtu wa TANAPA aliyekuja. Kama anaweza kutoka tembo mpaka kilometa 40 au 30 akamuua mtu na bado sisi tunakaa huku tunazungumza mjadala wa bajeti ya Wizara hii tunakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inaelekea pabaya, inaonesha tembo ndio wana thamani kuliko binadamu. Na mimi nikuombe wewe na Serikali kwa ujumla jinsi ambavyo tunapata madhara makubwa ya tembo hawa wanaotoka msitu wa Marang katika Jimbo langu na wanakula mazao ya watu mashambani huku wanaua wananchi, hakuna hatua inayochukuliwa tulipowaita TANAPA hawakuja mpaka siku ya tatu, hatimaye tembo wanaua watu watatu kwa siku tofauti. Tuangalie sana upana wa jambo hili, kama ambavyo wananchi wanapata madhara na pia fidia hakuna hatushiriki kwenye mazishi, tunapata matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla kabisa tutazame jinsi ambavyo sheria ipo nyuma ya wakati, sheria ipo nyuma ya maisha ya wanadamu wetu na haiwatendei haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu wa kawaida akiingia msituni katika misitu ya Marang huko Jimboni kwangu, Waziri afahamu hili, mtu wa kawaida akipita kwenye msitu au akakutwa kwenye msitu hana kitu chochote anapigwa na askari; sisi bado tunaanza kupiga meza tunafurahia Wizara hii. Kama ni hiyo shilingi bilioni moja iondolewe kwenye bajeti upatikanaji wa huduma upungue kupitia fedha hizo ambazo mnatarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasikitika sana kama askari alieenda shule aliyepata taaluma anaanza kumpiga badala ya kumpeleka mbele ya sheria tunakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamsikitikia sana Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ambavyo watu wake wamekuwa wa ajabu. Tuliendesha operation tokomeza ikazalisha mambo ya ajabu sana na Watanzania wengi wakafa bado Bunge halijaanza kutazama jambo hili leo bado askari wanapiga wananchi wetu. Ninamuomba Waziri, nilimuomba mara nyingi afanye ziara kwenye Jimbo langu awasikilize wananchi, aje na karatasi nyeupe wananchi waandike mambo waliyofanyiwa na kama Rais anatumbua atumbue kuanzia kwa Waziri mpaka kwa watendaji wengine wote. Nimekasirika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, wananchi wangu wamedhurika na pia kama ambavyo tukio linatokea Waziri ni mzito kufika, watendaji ni wazito kufika, hatimaye wananchi wanawekwa njia panda. Mimi siko tayari kuungana na hii Wizara, nipo kinyume kabisa. Nimtake Waziri apange ziara na apange ratiba ya vikao vya ujirani mwema kote Tanzania kwenye mazingira ambayo kuna hifadhi hizi ili kila mara kwa kila robo tuone wananchi wamefanyiwa nini. Hifadhi hizi zilikuwepo kabla TANAPA hawajaja, jamii walilinda, walihifadhi ndiyo maana hifadhi ziko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasikitika sana; mimi ni wa CCM habari ya CCM hapa hakuna, hapa tuzungumze uchafu. Bila ziara, askari wanatoka kwenye msitu wanaenda kukamata wananchi, wanawapiga wananchi bado mnasema eti tunafanya vizuri, hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; vikao vya ujirani mwema vimeachwa kwa sababu matendo yao hayafanani na hali halisi ya Watanzania na haki za binadamu. Nimekasirishwa sana, kijiji cha Tawi nilikotoka mimi tembo wameuwa watu wawili kilometa 50; kama hatuwezi kuwarudisha tembo msituni tuna sababu gani sasa ya kupiga makofi eti kushabikia hii Wizara? Halafu mtu wa Mbulu anafuata fidia Dar es Salaam; aliwe shamba fidia Dar es salaam, fidia yenyewe shilingi laki moja. Anakwenda tena anakufa mtu fidia sijui shilingi laki tano Dar es Salaam; hivi kutoka Mbulu kwenda Dar es Salaam na kuishi kwenye gesti na hoteli na nini ni shilingi ngapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni shilingi ngapi zinapotea? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushiriki wa TANAPA kwenye misiba inayotokana na wanyama iwekwe kwenye sheria, migogoro itatuliwe haraka; migogoro inaaachwa mpaka wananchi na TANAPA wanaingia uadui, tunapata uadui. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchimbaji wa madini msitu wa Marang. TANAPA wanachimba madini kwenye msitu, mwananchi akiingia anakamatwa na anauawa. Kama Usalama wa Taifa wapo, wale watu watatu waliokufa kule Magara fanyeni uchunguzi walikufa kwa ajili ya nini. Wananchi wanasema walikufa kwa sababu walikwenda kuiba madini, Kaizer akienda kuiba madini ndipo anauawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri afanye ziara, aende msitu wa Marang, Jimbo la Mbulu, aende Yaeda Chini. Yaeda Chini usiku hutatoka, majangiri ni bunduki zinatembea utafikiri hii ni nchi ya vita. Habari ya u-CCM mnayoleiteta hapa ni ya kazi gani kama mambo ni ya hovyo hovyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaitaka Serikali hii ijiangalie upya!, Serikali hii ijiangalie upya. Kama watu wanauawa kwa ajili ya kwenda kuchimba madini na TANAPA wanachimba; ninakutaka Waziri, nenda kwenye msitu wa Marang ukachukue hatua ya wale wanaochimba msitu wa Marang na wa Manyara, watoke wale TANAPA na wao wasichimbe, hawana sababu ya kuchimba pale. Mali zinazokamatwa zinakuwa miradi ya watu. Mali inakamatwa, mbao inakamatwa inauzwa, ni miradi ya watu, mnasema tunapata shilingi bilioni moja ya kazi gani? Shilingi bilioni moja itatufikisha wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba sana, na ninaitaka Serikali; kazi ya Bunge ni kuibana Serikali, na wewe Waziri tunaanza na wewe. Tuanze na wewe na wewe uwabane walio chini yako. Mtu yeyote wa CCM achukue hatua juu yangu kama anaweza. Kama ni namna hii... (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nani alikuja kwenye kampeni wakati tunafanya kampeni? Kila mmoja alitetea kiti chake ndiyo maana tuko huku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kura zangu zilipungua kule Daudi, Gehandu, Marang kwa ajili ya mtindo huu huu wa kuleana.
MWENYEKITI: Ahsante, ahsante
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza kwa kunipa nafasi hii ili nitoe mchango wangu lakini pia niweze kuipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo imetoa bajeti ya tofauti ya trilioni saba. Hiki ni kiwango kikubwa sana kwa nchi yetu kama ambavyo tutafikia haya malengo na kwa vyovyote mafanikio yatakuwa makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mchango mdogo wa kuishauri Serikali. Kwanza tusimamie mapato ili tuweze kufanikiwa katika hali hii ya ukusanyaji. Nilikuwa nategemea pengine tukusanye mapato kwenye forodha, viwanda na pia tuweze kukusanya kwenye makampuni makubwa. Eneo hili tukifanikiwa tukafika hiyo asilimia mwaka huu ni dhahiri kwamba tumefaulu kwa kiasi kizuri na mwakani ni mlango wa kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie eneo la CAG. Hawa wakaguzi wanafanya kazi katika mazingira magumu sana kwa sababu Mkurugenzi anayekaguliwa ndiye anayemwezesha. Nashauri kama itawezekana kitengo hiki cha ukaguzi kiweze kujitegemea katika nchi yetu kutoka ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya ili tuweze kufikia malengo mazuri. Kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamelalamikia sana hela ndogo ya CAG, kwa kweli kama hatujaweza kumwezesha CAG katika dhana nzima ya fedha, watumishi na dhana nzima ya vitendea kazi kwa vyovyote vile tunachokifanya hakipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri kule chini tuna mambo mengi sana. Kuna ya maabara, zahanati pamoja na nyumba za Walimu yameachwa. Kila mwaka tumeshindwa hata kutatua baadhi ya yale maboma. Kwa hiyo rai yangu kwetu sote ni kwamba, fedha zilizoombwa na Halmashauri hizi zifikishwe katika ngazi hizo za Halmashauri na tuweze kufuatilia. Kwa sababu hiyo tunaweza tukafika na huduma itatolewa katika ngazi hiyo ya chini na kutatua kero kwa ngazi ya Jimbo. Kwa jinsi ambavyo miradi mingi ni viporo hata miaka mitano ya sisi Wabunge inaweza kwisha hatujatatua hata kitu kimoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama ambavyo nilizungumzia hilo, naomba utoaji wa fedha zile ambazo zinapelekwa kwenye ngazi za chini ziweze kufanya vizuri. Pia nchi yetu imekuwa na hali mbaya ya bidhaa feki. Hizi tumebaki kuteketeza kwa sababu tayari baada ya muda tunaona zimeshaingia nchini, ziko ndani ya soko, kwa hiyo kiwango hiki kinaathiri sana uchumi wa jamii na kwa hivyo hali hii inawafanya wananchi washindwe kuelewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kama itawezekana wale wanaodhibiti na kuangalia ubora wa bidhaa zinazoletwa kutoka nje na zile za ndani waweze kuwa makini kuangalia ni kwa namna gani ambavyo bidhaa hizi zinadhibitiwa ili zisiwe zinavuruga soko kwa sababu tunapokwenda kuchoma au kuteketeza ni tayari wananchi wanapata hasara kubwa kiuchumi na pia wanadhurika kiafya, kwa sababu kuna madhara ya afya na kuna madhara ya kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika ngazi hii ya Halmashauri tungeomba ikafanye semina ya Waheshimiwa Madiwani. Miradi mingi ya ngazi za chini Waheshimiwa Madiwani hawawezi kutambua na kujua miradi hii na thamani yake kifedha. Kwa hiyo, tukiweka fedha za semina na fedha za uwezeshaji katika zile Kamati, hasa Kamati ya Uongozi ni imani yangu kwamba watatusaidia sana katika kukagua miradi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia bado hatujanufaika katika rasilimali gesi na mafuta kwa kuwa labda ni mwanzo, lakini naomba kwa mwaka unaokuja pia tuone ni namna gani tunanufaika katika rasilimali hizi za gesi na matuta kwa kiwango kizuri ili nchi yetu iweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji wanalalamika, ifike baadae huko tufike na wao tunawawezesha, tukikusanya hela vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, si vibaya tukawa na chombo kinachofuatilia ukusanyaji wa mapato katika Taifa letu. Ukusanyaji huu wa mapato sio ukusanyaji mzuri kwa sababu kwa vyovyote vile kuwaachia tu TRA wao ndiyo wakusanye na hatuwezi kubaini na kufanya utafiti kwa vyovyote hatutafika. Nashauri tuwe na chombo kinachoweza kufuatilia ukusanyaji wa mapato ili kiwe kinaielekeza Serikali kufanya kile kinachowezekana. Kwa hiyo, kwa vyovyote vile mara nyingi Serikali yetu imekuwa na wakati mgumu pale ambapo mifumo ya bajeti inapokusanywa na baadaye katika matumizi, hatuna vipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kuwe na uwiano wa vipaumbele vya matumizi ya bajeti kwa pale ambapo pesa hizi zimepatikana katika Central Government na Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi nilipokuwa kule ngazi za Halmashauri nilikuwa nafikiri huku kuna neema, nimekuja huku vilio ni balaa. Kwa hiyo, naomba kama itawezekana kwa vyovyote ngazi hizi za chini ziweze kuletewa hela kwa kuwa wao ndiyo walio karibu sana na wananchi wetu na kwa vyovyote wasingeweza kufanya kazi hiyo na wasingeweza kuona.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naishauri Serikali iweze kuratibu ahadi za Mheshimiwa Rais ili kwa mwaka tujue ni ahadi ngapi tumetekeleza na ahadi zipi zimebaki na kupitia Mbunge wa Jimbo na Serikali tuone basi yale yatakayotatuliwa chini ya uwezo wa Serikali yanapata kutatuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vyovyote vile katika hali hii ya nchi yetu kutafuta mapato na tunatoka trilioni 22 tunaenda 29 ni kiwango kikubwa sana na hali hii itatufikisha mahali pazuri jinsi ambavyo fedha hizi zikipatikana zitatatua kero za wananchi. Sisi tunaotoka kwenye Majimbo tuna wakati mgumu sana. Wakati wa kuomba kura unasema jamani nitajenga daraja, baadaye uchaguzi ukiisha daraja linakuwa kubwa na uwezo wa kujenga lile daraja unakosekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri kuhusu fedha za maji. Miongoni mwa maswali mengi yaliyoulizwa na Waheshimiwa Wabunge ni juu ya miradi mingi ya maji nchini. Nizungumzie uzoefu wa Jimbo la Mbulu au majimbo yote mawili ya Mbulu. Wataalam wanateua wazabuni ambao hawana fedha, hawana uwezo na kwa hivyo baadaye wale wazabuni wanashindwa kutekeleza ile miradi na tusitarajie kwamba hiyo miradi ya maji itakamilishwa kwa Juni, 30 hii siyo rahisi hata siku moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwa vyovyote Serikali iratibu, ipitie miradi upya, itoe maelekezo kwa ngazi za Halmashauri ili waweze kuvunja mikataba inapobidi, kwa sababu katika Jimbo la Mbulu tuna miaka miwili wananchi hawajapata huduma, lakini pia miradi imetelekezwa. (Makofi)
Kwa hiyo, nashauri, Serikali itoe maelekezo ipitie upya mikataba iweze kuondoa ile mikataba ili wananchi wapate huduma stahiki. Nia hiyo ya Serikali kusema tunalipa kile kilichokamilika ni utaratibu mzuri wa Serikali, lakini kama hawawezi kufika na hawawezi kutekeleza ungefanyaje? Kuna miradi toka mwaka 2013 haijakamilika mpaka leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante nashukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali kupitia upya sheria mbalimbali, naomba Serikali itafute utaratibu wa kila Tarafa nchini kuwa na Mahakama za Mwanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kupata wazee wa Mahakama uboreshwe. Hivi sasa wazee wengi wa Mahakama wanakaa muda mrefu bila kuteuliwa kwa kuzingatia jinsia na kutoka Kata au Tarafa kulingana na idadi yao, hata hivyo uteuzi haushirikishi Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi baadhi yake yamejihusisha na rushwa kiasi kwamba wapokea huduma toka Mabaraza mbalimbali nchini yanakosa imani.
Kwa sasa kuna haja ya ufafanuzi wa Wizara kuhusu masuala mbalimbali ya wananchi kufahamu utaratibu wa kupata haki zao mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Wakuu wa Wilaya ndiyo Wenyeviti wa Kamati ya Maadili ya Mahakama. Kuna haja ya kuwa na ratiba ya vikao vya Kamati hiyo muhimu kwa ustawi wa Mahakama nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya Maadhimisho ya Mahakama nchini itumike kuwa siku ya wapokea huduma kutoa mawazo yao kuhusu huduma hiyo ili Watendaji wa Mahakama waweze kujijua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa malipo ya Wazee wa Mahakama utazamwe ili kuleta tija, kwa sasa wazee wengi wanalalamikiwa kujihusisha na rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwe na kipindi cha kuwahabarisha umma kuhusu huduma ya Wasaidizi wa Kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isaidie kutoa fedha za ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mbulu na Jengo la nyumba ya Hakimu wa Wilaya. Kwa sasa majengo yaliyoko ni chakavu sana, hayafai kwa matumizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Wilaya ya Mbulu yenye Kata thelathini na tano ina Mahakama moja ya Wilaya na Mahakama za Mwanzo tatu lakini Mahakama za Mwanzo haina Mahakimu wa kutosha na kesi nyingi huchelewa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba Waziri mwenye dhamana afanye ziara Wilayani Mbulu na kuona changamoto ya Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha mchango wangu kwa sekta ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia kwa Mheshimiwa Rais, Waziri na Naibu wake na watendaji wote.

Kwanza, kuongeza bajeti ya Wizara kwa zaidi ya mara kumi; kuendelea kutoa vifaa tiba vya hospitali na vituo vyake yaani vitanda, magodoro na kadhalika; kutoa ajira ya madaktari wawili katika hospitali ya Wilaya ya Mbulu na kwingineko katika Wilaya za nchi yetu na kugawa pikipiki katika Halmashauri zetu nchini, naomba katika mgao ujao Halmashauri za Wilaya ya Mbulu wapewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iboreshe mfumo wa utoaji na upokeaji wa dawa katika hospitali za Wilaya vituo na zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wajumbe wa Bodi ya Afya ya Wilaya na Bodi ya Vituo vya Afya na Kamati ya Afya ya Zahanati wapatiwe semina ya majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iondoe mpango wa kila Halmashauri za Wilaya kukamilisha kituo kimojawapo katika vituo vilivyoko kwa mwaka ili kuweka nguvu mahali pamoja hali itakayosaidia kuwa na vituo vitano kwa miaka mitano. Hivi sasa fedha za bajeti hugawanywa na Madiwani kiasi kwamba hakuna mafanikio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ijitahidi kulipa madeni ya watoa huduma wa zabuni za chakula katika Halmashauri ya Mbulu, ni zaidi ya miaka saba sasa madeni hayo hayajalipwa. Japokuwa Serikali imesitisha watoa huduma ya chakula kwa wanafunzi wa chuo na huduma ya wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Mbulu ni taasisi kongwe kwa umri wake, kwa hiyo ninaomba Serikali yetu ione utaratibu wa kukarabati majengo ya hospitali hiyo. Naomba Serikali itusaidie kupata gari la ambulance kwani kwa sasa gari lililopo ni chakavu sana na wagonjwa wa rufaa ya kwenda Haydom ni kilometa 100, rufaa ya kwenda hospitali ya KCMC ni kilometa 360. Hivyo, naomba Serikali ituonee huruma kwa kutupa gari kwa ajili ya maisha ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Februari 2017 nilifanya kikao cha watumishi wa afya hususani wale walioko katika Hospitali ya Wilaya, katika kikao hicho watumishi walitoa kilio cha kukosa kwa muda mrefu fedha zao za on call allowance(malipo ya posho ya masaa ya ziada), naomba Waziri wetu baada ya bajeti atoe kauli ili watumishi wawe na amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naendelea kusema kuna umuhimu mkubwa wa dawa za Serikali kuwekewa alama kwa ajili ya kupunguza uvujaji wa dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iwaajiri watumishi wa afya, bado tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi wa afya katika Hospitali ya Wilaya, vituo na zahanati katika Halmashauri za Vijiji hali inayopelekea huduma za afya kuwa hafifu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itazame upya mfumo wa TFDA ili kupunguza uharibifu wa rasimali za umma kwa ajili ya afya ya mlaji. Mfano, simu fake, viroba na kadhalika, hali inayosababisha kudhoofisha uchumi wa jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho katika Hospitali ya Wilaya ya Mbulu kuna chuo cha PHN. Tunaomba Mheshimiwa Waziri wetu wa Afya aweze kufanya ziara katika chuo hicho na hospitali hiyo. Hata hivyo, kuna jengo lililokuwa linajengwa na Serikali Kuu, jengo hilo lililojengwa chini ya kiwango, hivyo chuo chetu kinafanya kazi katika mazingira magumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja .
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Awali ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoongoza nchi yetu na kwa jinsi anavyosimamia utendaji wa Serikali tangu aingie madarakani. Ni kiongozi wa mfano na katika mifano yake halisia ameweza kuipeleka nchi na kuweza kuongoza na kutoa dira sahihi kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue pia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kufika wakati huu wa sasa sisi Wabunge wote. Pia nichukue nafasi hii kwa niaba ya Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote na mimi mwenyewe, wana-Mbulu na Watanzania kwa ujumla kutoa pole nyingi kwa ndugu zetu, marafiki na jamaa wote waliopatwa na hali mbalimbali ya kupoteza ndugu zao katika nyakati tofauti kwa matukio ambayo hatujaweza kuyazoea. Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki nchi yetu tuweze kupata hatua nyingine nzuri kwa baraka zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Baraza la Mawaziri, Mheshimiwa Spika, wewe mwenyewe na watendaji wote wa Serikali kwa jinsi ambavyo wanajitahidi kutekeleza majukumu yao na kuwapa Watanzania fursa sahihi na nia njema ya kuweza kufanikisha malengo mahsusi kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kutoa mchango mchache ambao natarajia kuzungumza katika Bunge hili kwa nafasi hii ya viwanda. Kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kuiasa Serikali; uanzishwaji huu wa viwanda tunaouanzisha hivi sasa ningependa kushauri Serikali ijikite katika hali halisi ya kila Kanda kuwa na kiwanda ili maendeleo yetu yaweze kuendana na sehemu mbalimbali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa kuna baadhi ya maeneo yatakuwa yamekosa fursa ya kupata viwanda kutokana na hali halisi ya jiografia, rasilimali zilizoko na fursa nyingine za hali ya kupatikana kwa malighafi. Niseme tu kwamba kwa namna yoyote ile tufanye pia utafiti katika nchi yetu ili pia tuweze kuona ni maeneo gani kwa nchi yetu yanaweza kuwa na malighafi ili yale maeneo ambayo hayatapata uwekezaji wa viwanda na fursa za kujengewa viwanda basi waweze kuzalisha na kupata fursa ya kuwa na malighafi ambayo itaendeleza nchi yetu katika hali hii ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo yetu iboreshwe katika uzalishaji na uingizaji wa bidhaa. Nizungumze tu kwamba tukio lile la kuondolewa kwa simu feki katika nchi yetu liliumiza Watanzania wote, Watanzania walikuwa wanahangaika, wakapata simu, wakawa wanamiliki lakini mwishoni tukajikuta simu nyingi zinazomilikiwa hazitaweza kukidhi haja. Pamoja na pombe zingine zilizofutwa katika ile hali ya kawaida ambayo ilionekana si nzuri kwa matumizi ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii ambayo tusipoidhibiti katika uanzishwaji wa viwanda hivi na tusipoboresha mfumo wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini, tutakuta tumeanzisha viwanda vingi lakini bidhaa ambayo inazalishwa itakuwa ni bidhaa ambayo pia Watanzania watakuwa wametumia katika hali ambayo si sahihi. Hivi sasa si kweli, hata tuliotumia simu na wale Watanzania wote na waliotumia viroba na pombe mbalimbali na madawa lazima wamedhurika. Si rahisi kwa mara moja tukatambua madhara yake ni kwa kiasi gani, lakini ni vizuri tutakatazama upya mifumo yetu, tukafanya vizuri na tukaweza kuona viwanda vyetu vya ndani vinahimili mashindano au ushindani wa bidhaa kutokana na ubora unaotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi bila viwanda haitawezekana, lakini kuwa na viwanda bila kuwa na watu wenye taaluma ni kazi moja ngumu pia. Nitoe rai kwa Serikali, tuweze kupitia vyuo vyetu vya VETA, vyuo vya ufundi stadi kuandaa watumishi wa kada za kati na kada za chini ili waweze kupata nafasi za ajira na waweze kunufaika kama watumishi katika viwanda ambavyo tunatarajia kuanzisha. Bila kuwa na Watanzania hawa wenye taaluma ya chini na ya kati, basi viwanda tutakavyoanzisha vitakuwa vinamilikiwa na watu wa nje na pia tutakuwa tunatafuta watumishi wa kada za chini kutoka nchi zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, niweze kusema tu kwamba, kwa ujumla usimamizi wa kodi haujakaa vizuri kwenye viwanda ingawa suala hili ni la Wizara ya Fedha. Viwanda vyetu vingeweza kuzalisha bidhaa nzuri zenye kuhimili ushindani zikaingia kwenye mfumo na mfumo wa ukusanyaji wa kodi ukatazamwa, basi Tanzania ingeweza kuwa nchi ya mfano katika kukusanya na nchi ya mfano katika kuelekea uchumi kupitia viwanda ambavyo tutaanzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pengine utafiti ufanyike ili tujue ni maeneo gani yanakuwa na malighafi na maeneo gani yanaweza kuwa na fursa za uanzishwaji wa viwanda kutokana na rasilimali zitakazokuwepo katika maeneo hayo, pia katika yale maeneo ambayo kwa namna moja au nyingine tunaweza tukawa tumepata mwingiliano wa kiuchumi kwa maana ya yule anayezalisha, yule mwenye malighafi na yule mwenye kutokewa na fursa hii ya kupatikana kwa kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kusema kwamba, Watanzania si kwamba hawapendi mali inayozalishwa Tanzania, ni pale baada ya mtumizi anapoona mali au bidhaa iliyotoka nje ina thamani kubwa kuliko ile iliyoko nchini. Kwa vyovyote, lazima yule ambaye ananunua au mlaji au mtumiaji atakuwa na taswira nyingine tofauti ya kuona kwamba pengine ile ya nje ni bora zaidi kumbe hata sisi tuna bidhaa bora na nzuri zaidi, tatizo ni pale tu tunaposhindwa kudhibiti ubora unaotakiwa katika hali ya uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutazame pia wakati huu tunafufua viwanda, je, ni kwa kiasi gani tumefanya utafiti kwa nini viwanda hivi awali vilipotea au vilishindikana kuendeshwa au vilipata kukwama na hatimaye kushindwa kujiendesha? Kwa vyovyote vile bila utafiti, bila mapitio tunaweza tukaanzisha na mbele ya safari kukaja tena wimbi lingine la viwanda hivi kupotea na hatimaye nchi yetu kupiga mark time au kutokuwa na hatua ambayo si nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pengine kwa namna moja au nyingine naweza nikazungumza jambo lisiwafurahishe Watanzania. Tukiwa watu wa kuamini mambo mepesi, yasiyo na tija, ambayo hatuyafanyii utafiti, mambo ambayo rasilimali wataalam hawatumiki kama sehemu ya Watanzania waliopata fursa ya kupata taaluma hiyo, basi kwa vyovyote vile si rahisi tukawa na viwanda ambavyo ni endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza kwanza Mheshimiwa Rais na vilevile kuwapongeza Wizara kwa jinsi wanavyohangaika. Pia tunaomba sekta hii muhimu sana itakayoajiri Watanzania wengi, ipate fedha katika Bajeti ya Mwaka huu kwa asilimia 100 ili fursa hii ya viwanda kupanda na kupata nafasi nzuri, iweze kuwafikia Watanzania na Watanzania waweze kunufaika na fursa hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapitisha bajeti, mwakani tunatarajia kuona kwamba angalau kile tulichopitisha kuna asilimia pengine 100 au 80 kwenda mbele ipelekwe kwenye malengo mahsusi yaliyoanzishwa au yanayoanzisha viwanda ili tuweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, lakini nikitegemea yale yote yaliyokusudiwa yanapata fursa ya kutengewa fedha na kufanikiwa. Ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nitoe tu mchango wa kushauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, mfumo wetu wa kukusanya mapato hivi sasa si mzuri. Tungeweza kukusanya kodi na ushuru au nchi ingeweza kupata hela ya kutosha hasa katika viwanda kwa kudhibiti mianya na kuweka utaratibu mzuri wa ukusanyaji kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri mfumo mzima wa kusanyaji kodi utazamwe. Hivi sasa kodi zinalipwa katika utaratibu ambapo wale wanaolipa wanapangiwa kiwango kikubwa sana kutokana kwamba wengi wao huwa hawako kwenye mfumo ambao unaipa Serikali kodi. Ukusanyaji huu uungane na ule wa viwanda vikubwa sasa tunapata wakati mgumu pale ambapo mfumo wa ukusanyaji wa kodi ndani ya viwanda na makampuni haujakaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hivi sasa Watanzania wanaogopa sana kutumia mifumo hii ya kielektroniki katika kukusanya mapato. Mfumo huu ni mzuri, mimi ni mdau wake kwa takribani miaka 10, shida iliyopo ni uelewa kwa wafanyabiashara na wadau wanaopaswa kutumia mfumo huu ili nchi ipate mapato ya kutosha. Kwa hiyo, nashauri kama itawezekana kufanyike utaratibu wa mfumo huu na viwango vile vya kodi kupungua ili kundi kubwa la ukusanyaji wa mapato waweze kuingia katika utaratibu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, katika taarifa hizi tulizowasilishiwa, upelekaji wa fedha katika ngazi za Serikali za Mitaa hasa fedha za miradi ni mdogo sana. Tunapata wakati mgumu sana sisi Wabunge, bajeti hii tunapokaa hapa hatimaye tunapopitisha lakini mwishoni tunaenda kuwaambia wananchi malengo ya Serikali yetu au Serikali yao kuhusu miradi ya maendeleo. Sasa pale ambapo fedha za miradi ya maendeleo hazitapelekwa katika ngazi za Serikali za Mitaa miradi mingi ya maendeleo inakosa fedha na hatimaye sasa tunaingia mgogoro wa wachaguliwa na wananchi waliotuchagua lakini pia miradi mingi inakosekana na huduma inakuwa duni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upelekaji huu wa fedha ukisimamiwa kwa kuzingatia mpango mzima wa bajeti na kwa kuona kwamba umuhimu wa miradi ya maendeleo na uendeshaji wa Serikali unapelekewa fedha kwa vyovyote vile miradi mingi ya maendeleo itafanikiwa. Hivi leo hata tukipiga kelele kwa Waziri na timu yake bila pesa kupatikana nadhani Waziri hatabadilika kuwa fedha na hatutaweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne ni suala la Mfuko wa Maji. Naomba jambo hili litazamwe na namna pekee ya kuondoa kero ya maji nchini ni kutafuta mfumo mzuri wa kuona fedha za miradi ya maji zinapatikana kama ilivyo kwa Mfuko wa Mawasiliano na huu Mfuko wa Maji upate fedha za kutosha na pengine taarifa yetu iletwe baadaye ili tuweze kuona na kuishauri Serikali namna gani Mfuko huu wa Maji unapata fedha za kutosha ili miradi ya maji vijijini iweze kutatuliwa. Hivi sasa hali ni mbaya sana katika miradi ya maji na hasa miradi mipya na vile viporo lakini pia hali ni mbaya katika upatikanaji wa fedha na kwa vyovyote vile hatutafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, madeni ya watumishi na wazabuni wenzangu walishaongea sitaongelea, nashauri malipo ya wastaafu yawe na mfumo wa wazi ambao unaonesha dira sahihi na kiwango kizuri. Hivi sasa wastaafu wetu au watumishi wanapoelekea kustaafu wengi wao wanakata tamaa na kuona kwamba ni wakati mgumu sasa unakuja kwao. Pengine tuone namna ya kuboresha malipo yale ya wastaafu na utaratibu wa wazi ambao hauwabugudhi wala kuwatesa wale wastaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, tulifanya ziara mimi na timu yetu ya Kamati ya TAMISEMI, tulienda kule Njombe, jengo la Hospitali ya Mkoa wa Njombe ni kubwa na linajengwa kwa shilingi bilioni 3.2 mpaka kukamilika, lakini miradi kama hiyo katika mikoa mingine nchini na katika Wilaya zingine inajengwa kwa shilingi milioni karibu nane mpaka tisa na hata zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kuwe na mfumo na utaratibu unaoangalia matumizi ya fedha katika manunuzi ya umma na jinsi ya kutekeleza miradi kwa kuzingatia mfano wa Hospitali ya Njombe. Matumizi sahihi ya fedha yanaweza yakasaidia nchi pia kuona ni namna gani kile kidogo kinachopatikana kinakuwa na thamani katika utekelezaji wa miradi ya wananchi na miradi ya huduma na utoaji wa huduma Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, saba, ni Wakaguzi wa Ndani katika Halmashauri, wakaguzi hao mara nyingi wanafanya kazi katika utaratibu ambao sio mzuri. Nashauri Idara ya Ukaguzi wa Ndani katika Halmashauri zetu wapewe nafasi ya kuwa Idara inayojitegemea na Serikali ianzishe mfumo huu toka Taifa hadi Halmashauri ili wasiwe wategemezi kwa Wakurugenzi na watendaji wa Halmashauri kwa jinsi ambavyo wao ndiyo jicho la Halmashauri pale walipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nane, semina kwa Madiwani. Madiwani bila kufanyiwa semina wakapewa kazi ya kusimamia miradi ya maendeleo ni kazi bure. Nashauri Serikali ione umuhimu ya kutenga fedha kwa ajili ya semina za majukumu, wajibu na usimamizi na uendeshaji wa Halmashauri wao kama wawakilishi wa wananchi ili waweze kufanya kazi yao na kwa makusudi yaliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tisa, ajira Serikalini. Tunashindwa kuajiri watu sasa kwa sababu hata mfumo ule wa kuwastaafisha watu unakuwa si rafiki kwa wale wanaoelekea kustaafu na kwa hivyo hela hatuna hivyo vijana wengi wanakosa ajira. Ingewezekana tungepunguza hata umri wa kustaafu sasa lakini tuboreshe pensheni ya kustaafu ili kustaafu kuwe miaka 50 kwa hiari na lazima 55. Hali hii itafanya wastaafu waone wanalipwa pensheni inayolingana na maisha yao yajao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumi, kuimarisha Benki ya Kilimo. Hivi sasa tunazungumza suala zima la upatikanaji wa fedha, lakini bila kuboresha Benki ya Kilimo ambayo ndiyo itachukua wananchi wengi na watanufaika na huduma yake na kutazama utaratibu wao ulio rafiki katika kukopesha wakulima, kwa vyovyote si rahisi uchumi wa kawaida ukamfikia mwananchi na mzalishaji na mjenga uchumi wa nchi kwa kadri ambavyo inawezekana kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumi na moja, Tume ya Mipango iboreshwe, irudi Ofisi ya Rais kama Kamati ilivyoomba lakini ijengewe uwezo na iweze kuwa chombo/ taasisi inayoweza kushauri Serikali kuhusu uchumi wa nchi. Chombo hiki kikisimamiwa kikakaa vizuri kinaweza kitatufikisha katika hali ambayo itatujenga zaidi kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni misamaha ya kodi isiyo na tija. Hivi sasa si kweli kwamba misamaha yote ya kodi inayotolewa ina tija kwa nchi yetu. Kama itawezekana nashauri kuwe na chombo kinachosimamia mfumo huu na kutazama msamaha uliotolewa kwenye kampuni au taasisi fulani una tija kwa nchi, kizazi kijacho na uchumi wa nchi kwa siku za baadaye. Misamaha haiwezi kuepukika kutokana na hali halisi inayojitokeza, lakini si misamaha yote ina tija kwa hivi sasa. Naona jambo hili likitazamwa linaweza likajenga uchumi wa nchi lakini likaongeza pia mapato Serikalini na tutafanikiwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nichukue nafasi hii kwanza kuipongeza Serikali Baraza la Mawaziri na wataendaji wote Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mambo machache, kama ambavyo waheshimiwa wajumbe wenzangu wamezungumza kuhusu Wakala huyu wa Barabara Vijijini, naomba Serikali katika bajeti inayokuja ije na utaratibu wa kubadilisha hizi sheria za mgao wa fedha kwenye Mfuko wa Barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi za TARURA hazitoshi zilizokuwa zinatolewa. Kama ambavyo tunaona kwenye Wilaya tulizotokana na Halmashauri tulizotoka daraja la korongo moja halitoshi kwa fedha ambayo anapewa TARURA, sasa kwa kuwa maeneo ya vijijini yamekuwa na ongezeko kubwa na vyombo vya usafiri na mahitaji makubwa ya mtandao wa barabara tungeomba basi Wizara yetu na hata Serikali waone umuhimu wa eneo hili la wakala huyu TARURA kuongezewa fedha za mfuko wa barabara zinazomilikuwa na Serikali za Mitaa maeneo ya mijini na vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la ahadi za Rais. Mheshimiwa Rais sasa tuna miaka miwili na zaidi tangu uchaguzi mkuu umepita. Alihaidi ahadi nyingi za bara bara katika maeneo mengi ya vijijini. Kwa mfano katika jimbo langu la Mbulu Mjini alihaidi barabara ambayo haipo kwenye mtandao wa TANROADS. Sisi Wilaya tukasubiri TANROADS atakuja kutekeleza hiyo ahadi ya kilometa tano ya lami. Kumbe barabara alizoahidi sasa hivi mmiliki na msimamizi na mtekelezaji ni TARURA. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI akija wakati anatoa mrejesho aone umuhimu wa kuona barabara zile ambazo zimeahidiwa na Mheshimiwa Rais kwenye mtandao wa barabara ambao TARURA atahudumia kwenye bajeti hiituanze utekelezaji wake, kwa maana ya kuzitengea fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira, Serikali ilikuwa na nia njema ya kutaka kuajiri pengine nafasi kama 50,000 hivi katika mwaka wetu huu ambao umebaki miezi minne. Basi hata kabla ya mwaka huu kuisha tuone ni namna gani nafasi kadhaa zitaajiriwa ili kupunguza hii gap kubwa ya mahitaji makubwa ya ajira. Tuna nafasi nyingi kwenye Serikali za Mitaa hasa za Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata, walinzi na wapishi na watu mbalimbali ambao ni kada mbalimbali katika nafasi za ajira. Kwa hiyo, nafasi hizi zingeajiriwa hata sehemu ili kupunguza ukubwa wa tatizo hili kama ilivyo sasa hivi na hali hii itasaidia ni kwa namna gani walau tunapata watu ambao watakuwa watenda kazi katika Mamlaka za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la upelekaji wa fedha za mradi ya maendeleo. Nilikuwa namuuliza Mkurugenzi wa kwetu, fedha hadi sasa kiasi kilichopelekwa ni kidogo sana nilikuwa naomba basi fedha za mradi ya maendeleo hata kwa hii robo iliyobaki ipelekwe kwa kiasi kizuri ili kupunguza hali hii ya ukosefu wa fedha za miradi ya maendeleo kwenye ngazi za Halmashauri. Kwa sasa tuna mahitaji ya miradi ambayo tumeahidi kwa wananchi lakini bado hatujapata nafasi ya kupeleka fedha kwa kiasi kizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekta ya miundombinu kwa ajili ya ujenzi holela mijini, katika Kamati yetu tulikuwa tumependekeza Serikali ione umuhimu wa kuandika waraka kwa Serikali za Mitaa kwenye Halmashauri ili na wale Maafisa Mipango Miji na Wakurugenzi wadhibiti ujenzi holelea unaoendelea kwenye maeneo ya miji yetu ili kuepuka gharama kubwa ya uvunjaji wa majengo hapo baadaye. Kwa vyovyote vile nimuombe Mheshimiwa Waziri, nampongeza sana Mheshimiwa Jafo, Wakurugenzi wanapokuja kwenye Kamati yetu safari hii waje na utaratibu wa kiasi gani walitoa fedha za asilimia 10 ya akina mama kwa mwaka huu wa fedha ili tuone ni kwa namna gani jambo hilitunalozungumza muda mrefu limetekelezwa kwa kiasi na linaweza kuwa na dira nzuri katika utekelezaji ule wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mahakama, tumekuwa na mahitai makubwa ya mahakama, tumekuwa na hali ngumu ya wananchi kufuata huduma ya mahakama mbali. Tutafute ni namna gani walau kwenye tarafa tunakuwa na mahakama, kwa hivi sasa zinaemewa zaidi ya kilomita kama 50…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoiongoza nchi yetu na kwa hatua kubwa aliyoifanya katika kurekebisha mifumo mingi ya Wizara hii na sekta ya madini kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wetu wa Madini na Naibu wake wote wawili kwa jinsi wanavyotendea haki nafasi zao pamoja na watendaji wote wa Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kwa Wizara hii ni kama ifuatavyo:-

(a) Tunaomba sana Serikali itazame upya mikataba ya uchimbaji wa madini kote nchini ili kuona ni kwa namna gani nchi yetu inanufaika kupitia rasilimali hii ya asili kutoka kwa Mungu.

(b) Serikali itazame mpango wa kuwasomesha wataalam wabobezi wa sekta hii.

(c) Serikali ifanye mpango wa kutumia wataalam watakaobaini maeneo yalipo madini nchini hasa katika maeneo ya wachimbaji wadogo kote nchini.

(d) Kwa kuwa wachimbaji wadogo kwa sasa wanachimba kwa kubahatisha basi Serikali yetu itumie wataalam wake ili kurahisishia wachimbaji hao wadogo nchini kutumia njia bora.

(e) Kwa kuwa maeneo mengi nchini yanasemekana kuwa na leseni na kwa kuwa maeneo hayo yanashikiliwa na watu hao ambao hawachangii Taifa letu mapato ya uhakika basi Serikali ifanye mapitio au tathmini ili kuona njia bora na zenye manufaa katika kurekebisha suala hili.

(f) Nimuombe Mheshimiwa Waziri afanye ziara katika Jimbo la Mbulu Mjini kwenye machimbo ya Tsawa, Kata ya Gehandu, Mbulu Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho natanguliza shukurani zangu na naunga mkono hoja kwa asilimia 100.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kuanzia kwa Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Waziri wetu mama yetu mpendwa Ummy Mwalimu, Naibu Waziri Mheshimiwa Faustine Ndugulile na watendaji wote wa Wizara na ngazi zote kwa kutatua changamoto ya upungufu wa miundombinu ya majengo, dawa, vifaatiba na rasilimali watumishi kwa ujumla; kuendelea kuboresha sera yetu ya afya nchini na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM 2015 hadi 2020.

Aidha, naungana na Watanzania wenye nia njema pamoja na wananchi wa Jimbo langu la Mbulu Mjini kwa maombi na mapenzi makubwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kutoa ushauri wangu kwa Serikali kuhusu bajeti inayowasilishwa ya Wizara hii kwanza, kuendelea kutoa nafasi kubwa ya ajira kwa sekta hii ya afya kupitia mipango yetu ya ikama kila mwaka. Pili, kuongeza uwezekano wa mashine za x-ray katika Hospitali za Wilaya na vituo vya afya ili kuleta tija zaidi, tatu, kusimamia matumizi ya mashine za kielektroniki katika vituo vya afya, zahanati, hospitali za wilaya, rufaa kote nchini ili kuongeza mapato na nne, kusimamia mpango wa kila Mtanzania anaetaka Bima ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika tano, kufufua bodi za afya za zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya kulingana na muda wa ukomo wao wa uteuzi; sita, kuendelea kuhamasisha kliniki ya wanaume na wajawazito ili kujenga ushawishi wa uzazi wa mpango; saba, kuitaka MSD kutumia dawa zenye muda mrefu katika hospitali zetu; nane, kuona na kutathmini mpango wa PPP katika hospitali binafsi unanufaisha jamii au wapokee huduma kwa kiasi gani badala ya kuboresha hospitali zetu, hata hivyo, mpango huu wa ubia wa sekta binafsi haumpunguzii mpokea huduma gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kuna madeni makubwa ya malipo ya masaa ya ziada katika Halmashauri za Mji wa Mbulu, hospitali hiyo iliyokuwa ya Wilaya hapo awali inakabiliwa na upungufu wa watumishi hivyo basi naomba sana OC inayotolewa itumike kwa vigezo vya bajeti kinyume na matumizi mengine.

Pia naomba Serikali ione umuhimu wa kuona inafanya maandalizi ya watumishi wapya kwa vituo vya afya vya Daudi, Thawi na Dongobeshi kwani mahitaji hayo mapya ya miundombinu yanaweza kufanya majengo hayo yasitoe huduma. Kwa sasa hospitali ya Wilaya ya Mbulu iliyoko Mbulu Mjini inatoa huduma asilimia 30 kwa wananchi wa Jimbo la Babati Vijijini, Mbulu Vijijini na Karatu hivyo kupewa mgao wa dawa kwa kuangalia takwimu za sensa ya mwaka 2012 haitakidhi haja ya huduma bora. Hata hivyo Halmashauri ya Mji ya Mbulu kupitia Baraza la Madiwani walishatuma taarifa hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa idadi ya watoto walemavu ni kubwa, Serikali ione kila Halmashauri inateua shule moja ya msingi na sekondari na kufanya marekebisho ya miundombinu yake ili kundi hili lipate elimu kwa maisha ya baadae katika jamii yetu na kizazi kijacho.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa katika Hospitali ya Wilaya, baadhi ya vifaatiba havipewi vipaumbele mfano shule, blanketi, vifaa vya matibabu ya macho na meno kitendo kinachofanya wataalam hao kutokutoa huduma na katika vikao vya Baraza la Madiwani ukihoji wakati wa bajeti kauli ni kwamba ukomo wa bajeti hauruhusu, mfano ni Hospitali ya Wilaya ya Mbulu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho Mheshimiwa Waziri wa Afya nimemuomba atembelee Hospitali ya Wilaya ya Mbulu kwa kuwa ni mali ya Serikali na kwa kuwa tayari mwaka jana alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Hydom na kituo cha afya katika mwezi wa Juni. Pia ziara hii ni ahadi yake, Mungu akitujaalia hasa siku ya Jumamosi moja ili Jumapili Mheshimiwa awahi kwenye majukumu yake. Katika ziara hiyo aweze kutembelea Tarafa ya Nambis ambako tarafa hiyo haina kituo cha afya hata kimoja na ina akina mama wengi sana kwa maelezo nitatoa maelezo zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ninawatakia kazi njema na majukumu mema katika kutumikia Wizara hii muhimu sana kwa mustakabali wa maisha yetu na Taifa kwa ujumla. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Tano chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake za kuboresha huduma ya afya kote nchini hususan ujenzi wa miundombinu ya majengo nchini kote; kupunguza upungufu mkubwa wa dawa na vifaatiba kote nchini; kupunguza upungufu mkubwa wa watumishi wa kada za afya kote nchini; kupambana na maambukizi ya VVU nchini na mpango mkakati wake wa kuboresha sekta hii kila mwaka, hali inayowafanya wananchi kuwa na imani kubwa kwa Serikali yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara itazame upya mtawanyiko wa Madaktari katika Hospitali za Wilaya na Mikoa ili kuhakikisha angalau kila hospitali inapata mtaalam mmoja kwa kila kitengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali iangalie sera ya familia kutunza wazee na watoto kupitia familia zao badala ya kutelekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, maombi ya Hospitali ya Mji wa Mbulu kupatiwa gari la kusafirisha wagonjwa (ambulance) kwani gari lililoko limechakaa sana na wagonjwa wengi wanapata rufaa ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Haydom na KCMC Moshi nako ni mbali sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la Tarafa ya Nambis katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu haina hata kituo kimoja katika kata zote tano na ni mbali kutoka Hospitali ya Wilaya hali inayosababisha akinamama wajawazito kukosa huduma na kutembea zaidi ya kilomita 30 mpaka 40 kufika Mbulu Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba Mheshimiwa Waziri wa Afya afanye ziara katika Jimbo la Mbulu Mjini hususan Tarafa hiyo ya Nambis kwa kuwa alishaahidi kufanya ziara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Basi, naomba nitumie dakika kumi pia. Kwanza nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kutujalia nafasi hii ya uwepo wetu hapa na jinsi ambavyo ametulinda hadi leo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, natoa shukrani za dhati kwa Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kutoka kwake Rais, Makamu wake, Waziri Mkuu na Mawaziri wote kwanza kwa kazi kubwa wanayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitachangia kwa staha sana. Kwanza nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri zaidi ya 14 waliofika Mbulu, lakini walipita katika barabara ya Magara na leo daraja la Magara linajengwa kwa fedha nyingi za Tanzania. Pia barabara zote za TANROADs; nawapongeza Watendaji wote wa TANROADs kwa jinsi ambavyo wanahangaika katika barabara zetu za Wilaya ya Mbulu, wakati wote kunapitika na wanajitahidi kufanya kazi hii mara mbili kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nina maombi Serikalini. La kwanza, naishukuru pia kwa mnara kule Nambisi umefunguliwa, Tarafa ambayo haikuwa na mawasiliano toka zamani na sasa wananchi wa Tarafa hiyo wamepata mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mambo machache. La kwanza, naungana na Waheshimiwa Wabunge wote ambao walikuwa wanatetea fedha za Mfuko wa Barabara, TARURA wapewe asilimia 50 na Serikali Kuu 50, vinginevyo basi hata tutafute namna ya vyanzo vingine vya kusaidia TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu barabara zilizopokelewa na TARURA zimekuwa na jiografia ya maeneo magumu sana. Maeneo mengine ni yale yenye makorongo katika maeneo ya vijijini. Kwa mfano, kwenye Jimbo langu la Mbulu Mjini, kuna makorongo ambayo yanahitaji madaraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, korongo moja linaweza kuwa bajeti ya TARURA kwa Halmashauri yangu au kwa Jimbo langu la Mbulu Mjini. Sasa hawezi kufanya daraja au kivuko na maeneo hayo yamekuwa kikwazo katika huduma za jamii za afya, elimu na huduma nyingine za kijamii. Kwa hiyo, tunaomba sana, pengine ikiwezekana hata madaraja ya chuma kusaidia kwa namna gani kwa sasa maeneo haya kwa nchi nzima yanapata muunganiko wa kupata mtandao wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua nyingine pia, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kila mwaka ametupa kilomita moja ama mita 500 katika mlima Magara. Waheshimiwa Mawaziri, ni mashahidi waliofika Mbulu, waliopita barabara ya Magara. Barabara ile kwa jiografia haipo Tanzania nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri zile kilomita moja au moja na nusu unayotoa kwa kilomita kama 40 inaweza kuwa takriban miaka kadhaa, wananchi wale wasihudumiwe kwenye hilo eneo. Kwa hiyo, tunaomba kwa bajeti ya mwaka huu kwa fedha walizotenga japo ni kidogo lakini watupe; na mwaka unaofuata watupe hata angalau kilomita tano za mlima ili mlima ule uweze kupitika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom mpaka Sibiti. Majimbo yanayopitiwa na barabara hii ni zaidi ya sita. Tunaomba sana Serikali itusaidie ni kwa namna gani barabara hii inapewa fedha mara moja kwa ajili ya usanifu ulioandikwa kwenye kitabu hiki, lakini na baadaye mpango wake wa kufanyiwa kazi kwa kiwango cha lami. Barabara hii inatoa huduma kwa Majimbo yasiyopungua sita au saba. Pia ina miji midogo takribani kama arobaini na kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Wakurugenzi wa Benki ya Ujerumani walikuwa wanasema barabara hii ni barabara muhimu, inapita kwenye miji mingi na jamii nyingi. Kwa hiyo, tunaomba sana kwa jinsi ambavyo Mheshimiwa Waziri ameandika kwenye kitabu hiki, lakini hakuna fedha zilizowekwa zaidi ya kuwategemea wahisani wa KfW. Kwa hiyo, tunaomba ili mtandao wa barabara katika eneo hili la bonde na juu ya Bonde la Ufa kwa maana ya Karatu, Mbulu na Haydom uweze kupatikana kuunganisha mikoa kama mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba sana kama ambavyo nimezungumza, ni ahadi za Mheshimiwa Rais. Tuna miaka mitatu sasa, katika ahadi zile za Mheshimiwa Rais, kwa mtandao wa barabara za TANROAD na Serikali Kuu, watusaidie kutekeleza zile ahadi ili ziweze kupungua kwa maeneo yote ya nchi nzima na tunajua ni maeneo makubwa sana ambayo tayari yana matatizo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la minara. Sasa hivi kuna haja ya Mheshimiwa Waziri kufanya ziara kwa maeneo ambayo hajaenda, lakini pia kuchukua taarifa ya wataalam ambayo inaonesha ni maeneo gani hayana mawasiliano. Juzi Mheshimiwa Waziri alikuwa anatuhoji na kutuambia kila Mbunge yale maeneo ambayo yeye anaona ili alinganishe na yale ya Wizara kama yanafanana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapongeza sana kwa mpango huu wa kushirikishana mawazo na kupokea mawazo ya Waheshimiwa Wabunge. Hata hivyo, niseme tu kwamba kumekuwa na desturi ya taasisi hizi zinazoweka minara kuweka minara mahali pamoja katika ushindani ule wa kukimbilia eneo moja. Basi Serikali isiwe inaruhusu uwekaji wa hiyo minara kwa maeneo yale. Tunaomba sana katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia barabara za miji Mikuu kama Dodoma. Sisi tunaoishi katika eneo hili la Mji wa Dodoma kuja Bungeni imekuwa tabu sana na kwenda kwenye maeneo tunayoishi. Tunaomba hata uchongaji wa kawaida wa barabara za changarawe, maeneo yote ambayo hayajafikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hili kwa sababu siku moja nilikuwa nasafiri asubuhi lakini gari lilifunga njia nikawa nimechelewa usafiri ule wa kwenda na Waheshimiwa Wabunge wenzangu. Kwa hiyo, inaonekana kwamba barabara hizi za Dodoma zinahitaji upanuzi wa kina na namna ambavyo uchongaji utawekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili la Dodoma linahitaji sasa ongezeko la alama za wapita kwa miguu. Magari yamekuwa mengi, wapita njia wamekuwa wengi, tumehamia kwenye huu mji kwa wingi wetu. Kwa hiyo, kuna haja ya wataalam kupitia upya mfumo mzima wa barabara za Dodoma ili ziweze kuwekewa alama kwa jinsi itakavyowezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nimwombe sana Mheshimiwa Mbarawa, kama Waziri mwenye dhamana, naomba anisikilize; yeye na Naibu Mawaziri wote, Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii, aje Mbulu apite barabara ya Magara aone jinsi ambavyo barabara hii inahitaji sana jitihada za haraka za Serikali ili iweze kutafutiwa ufumbuzi hasa eneo la Mlima kwa kiwango cha zege kwa sababu ni hatari sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale Mawaziri waliopita kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri, wawe Mabalozi wetu wazuri kuizungumzia barabara hii ya Mbulu - Magara hadi Mbuyuni, kwa maana ya barabara ya Magara kwa sababu jiografia yake ni hatarishi na wananchi hawataacha kwa sababu ina ufupi wa kwenda Mkoani Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, eneo hili Mheshimiwa Waziri aji-commit wakati anatoa mrejesho wake, atueleze anakuja lini Mbulu ili aone jinsi ambavyo tuna mahitaji makubwa na jiografia yake haipo katika Tanzania nzima kwa sasa? Japokuwa eneo hili ni eneo fupi, lakini ni tete na hatarishi. Viongozi wote, Mawaziri wote wale 14 waliopita pale walikuwa wanasema Mheshimiwa Mbunge pole sana, kwa kweli hatukujua wakati wote ulikuwa unapiga kelele na kulalamika Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru kwa ujenzi wa daraja na hata kwa hizo kilomita chache wanazoweka Mlimani, ila watuongezee kwenye bajeti, ninyi Mawaziri na Naibu Mawaziri wake wote wawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tunaishukuru sana Serikali na tunawatakia kazi njema. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza niipongeze Serikali kwa kazi kubwa inayofanya. Pia nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote Serikalini kwa kazi kubwa wanayofanya. La kwanza nizungumzie kwamba katika Wizara ambazo zina changamoto lukuki katika nchi hii ni Wizara hii ya Mambo ya Ndani. Wabunge wenzangu wote wamezungumza suala la miundombinu ya majengo kwenye makazi ya askari, maofisi na hata magereza na vituo vya polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mwaka wa tatu sasa, changamoto ya Wizara hii haiwezi kutatuliwa kwa jinsi tunavyokwenda, hali ni ngumu sana, fedha ni kidogo. Tulifanya ziara Mtwara na Lindi tukakuta viporo vya miradi ambayo hata kwenye kitabu cha bajeti baadhi yake haikuwekwa. Sasa Waziri tungependa atuambie ile miradi tuliyotembelea japo yeye hakuja ni kwa namna gani Serikali sasa inatatua changamoto ya hizi Wizara kwenye miundombinu ya majengo yale kwa sababu tumeshawekeza na sasa hakuna utekelezaji wa ukamilishaji wa hiyo miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Rais kwa hela aliyotoa kwa ajili ya Makao Makuu Dodoma lakini fedha zile hazitasaidia kwenye miradi ambayo tumekagua. Wizara hii Jeshi la Zimamoto, Polisi na Magereza magari yake ni mabovu sana na hasa kwangu kule Mbulu, hayana matairi, hayana muda wa matumizi, muda wa matumizi wa hayo magari umeshakwisha. Kwa hiyo, Waziri aje atuambie ni kwa namna gani angalau tunakombolewa kwenye tatizo kama hili la ubovu wa magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba matumizi ya magari ya Serikali ni miaka mitano. Kwa hiyo, inapokuwa zaidi ya miaka mitano yale magari yanakuwa hayana tena hadhi ya matumizi katika utendaji wa Serikali na hasa askari. Magari ya askari ni magari yanayotakiwa yawe mapya, watakapoitwa mwendo wao ni wa kasi, wanakimbia, kuna roho za watu juu ya yale magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yanapokaa muda mrefu na yamechakaa, kule kwangu Wilaya Mbulu, magari yote matatu, majimbo yote mawili yamechakaa. Nimeomba miaka mitatu sasa na leo tunapitisha bajeti hakuna gari, lakini kwenye makazi, ni mahali gani tutakwenda, kule Mbulu tukienda Magereza haifai, imejengwa toka ukoloni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Wilaya hakifai, kimechakaa, majengo mengine yale ya makazi ya askari hayafai, wangeenda waandishi wa habari tungejificha. Nafikiri hata hayo yanayojengwa anzeni na Makao Makuu ya Maafisa wa majeshi yetu yaliyo chini ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, waende kwenye ngazi ya mikoa kujenga nyumba za Makamishna wa Mikoa, waende kwenye ngazi za Wilaya tupeleke tuanze kwenye ngazi za Wilaya tupeleke tuanze kwenye ngazi za maafisa ili hata wale askari wa kawaida wakipangisha, basi na yale majengo yafanane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Askari ni utii, askari ni uhodari, askari ni uaminifu wanatupigia saluti, wanampigia Waziri saluti, mtu yoyote saluti mwenye mamlaka kwake, siku moja na sisi huko tunakokwenda kwa Mwenyezi Mungu wao watapewa ufalme huo, tutawapigia wao saluti. Nadhani mambo haya sio mambo ya mchezo wakati fulani tunapoyaongea, yanahitaji sana kuangaliwa na kwa namna gani tunatatua basi hata kwa awamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia kuna askari wachache wanaochafua majeshi yetu ziara ya viongozi Waziri, Inspekta Generali, RPC akutane na baadhi ya viongozi na baadhi ya wanajamii na viongozi wa madhehebu ili masikio yake pia yapate kusikia eneo hili kuna matatizo gani, kukagua tu askari na kupita hakusaidii kuona sikio lako, kisogo chako kina kitu gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, kuna Wabunge wameongea mambo hapa, kama hayana ukweli wafute zile kauli. Mfano, Mheshimiwa Zitto anazungumza watu 68 wameuawa, watu mia tatu na kitu hawaonekani, aisaidie Serikali upelelezi kwa sababu sisi tunazungumza kwa niaba ya Watanzania, mambo haya yanapotosha umma . (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza ni kwamba, wakati huu ambapo tunaelekea kwenye kupitisha bajeti, mambo ni mengi, lakini tuyaweke kwenye vipaumbele, kuna baadhi ya mambo tumetembea sisi na Mheshimiwa Waziri, tumetembelea Wizara hii, tumeona mambo mengi sana, tumeona miradi viporo, tumeona hakuna namna ya utatuzi, basi tutafute njia mbadala ili tuweze kukamilisha hiyo miradi ambayo tulitarajia kwa namna ya pekee sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee nalipongeza Jeshi la Polisi kwa sababu kazi hii wanayofanya sio rahisi. Kama tunavyozungumza sisi ni kazi ngumu sana, unapolala yeye anakulinda na mali yako, unapoamka yeye anaendelea kukulinda, lakini mazingira yao hayafanani na kazi wanayofanya. Kwa hiyo, nadhani hatujawatendea haki askari wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umenipa dakika tano, ni ya kuishukuru Serikali, mimi nilitaka dakika 20 za kuizungumzia Wizara hii na kwa namna ya pekee nimwambie hatuwatendei haki askari. Mheshimiwa Mwigulu, yeye kama Waziri, ajitazame, atafakari maneno tunayoyazungumza hapa. Mengine yeye ni mtu mzima, aende kuyachambua kuna mambo ambayo yana ukweli kabisa na yafanyiwe kazi na yeye kama kiranja wa Wizara hii kwa nafasi yake anapaswa kuangalia Watanzania wanasema nini. Mengine yanasababishwa na askari kutokana na mazingira ya kazi yao. Kazi inapokuwa ngumu, mazingira yanapokuwa si rafiki, lazima mtu anashawishika kwenda kufanya mambo mengine ambayo hayana maana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, naomba watuangalie kwenye ngazi za wilaya, mikoa, na ngazi za Taifa ili tuweze kufanya kazi hii kwa weledi na askari wawe na amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuona siku hii ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa iliyofanya nchi nzima ikiwemo Jimbo la Mbulu Mji. Niseme tu kwa ujumla kazi zilizofanywa na Serikali hii ya Awamu ya Tano zipo katika ngazi mbalimbali na kwa nyakati tofauti. Watanzania wa leo wana masikio na macho na wanaona matokeo ambayo yanagusa zaidi maeneo ambayo pengine kwao yalikuwa tatizo kwa namna mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya afya ambayo ni muhimu sana lakini Serikali kwa jitihada mbalimbali imechukua hatua za makusudi kuboresha huduma ya afya kutoka kwenye miundombinu na huduma mbalimbali ikiwemo dawa na vifaa tiba lakini pia katika kila sekta kwa kazi hizi zimefanyika. Kwa namna ya pekee sana, tunampongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake lakini pia Baraza la Mawaziri kwa kuwa kila sekta imejaribu kufanya kazi. Nayazungumza haya kwa sababu yamefanyika katika Jimbo langu la Mbulu Mji na nchi nzima kwa ujumla kadri tulivyoona kwenye Kamati mbalimbali kwa kukagua miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwa uchache na umuhimu sana kuzungumzia eneo la ajira. Hali ni mbaya sana, tunaomba Serikali ifanye utafiti na ichukue hatua za makusudi kuona ni kwa namna gani vijana wote waliomaliza elimu yao katika vyuo mbalimbali wanaweza kutoa mchango wao kwa Taifa letu. Kadri nafsi za ajira zinavyokuwa chache basi sekta hii ambayo tunaiita ni sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kuchukua vijana wetu ambao wamehitimu. Tatizo tulilonalo ni kwamba vijana wengi wanakosa nafasi ya kufikiri kwamba sekta binafsi inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuwapatia Watanzania ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili ili kwa namna mbalimbali tutazame sheria za ajira na upungufu uliopo kwenye sekta binafsi katika suala la ajira kwa vijana. Vijana wengi wanaogopa kuajiriwa na sekta binafsi kutokana na mtazamo wao uliojijenga kwamba Serikali itawaajiri, kwa hiyo, sekta binafsi inaogopwa. Kwa hivyo, ni jukumu la Serikali kutazama upya suala la ajira pamoja na mazingira ya kustaafu kwani ndiyo yanaifanya jamii na vijana kuona kwamba wakiajiriwa katika sekta binafsi hawatakuwa sawa na wale walioajiriwa katika sekta za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nayasema haya? Kila mtu hapa tulipo anaogopa kustaafu, hata Wabunge tunaogopa kustaafu kwa sababu mazingira ya kustaafu baadaye siyo mazuri, kila mtu ana hofu hatma yangu itakuwaje baadaye nikishastaafu. Kwa hiyo, kuna haja ya kuangalia sheria na taratibu za ajira na mafao ya kustaafu katika sekta binafsi kwa sababu akiangalia kama baadaye akistaafu hali yake siyo nzuri, basi lazima kijana aanze kupata hofu na waweze kuogopa kuajiriwa katika sekta binafsi. Pengine haya yanatokana na mishahara midogo lakini pia mazingira ya kufanyia kazi yanakuwa siyo rafiki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima Serikali itazame pia shule zetu za sekondari na msingi ni namna gani tunabadilisha na kuingiza mitaala ya sekta za biashara, ajira na mafao baada ya kustaafu ili vijana wetu wasisome kwa dhamira au kwa nia ya kwamba hapo baadaye wataajiriwa na Serikali. Katika shule zetu za msingi lazima tuwe na mitaala ya kilimo na biashara na kufanya mambo haya kuwa rafiki kwa kijana wa Kitanzania. Sasa hivi vijana wana chuki kwetu sisi Wabunge wanaona kwamba hatuzungumzii suala zima la upungufu wa ajira katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya umma na sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uanzishwaji wa viwanda, tusipotafuta utaratibu na mazingira yanayoruhusu vijana waende kwenye ile hali ya kwenda kwenye viwanda, tutakujakuta tumeanzisha viwanda lakini vijana wetu hatukuwaandaa katika ile mitaala ya ajira kwenye sekta ya viwanda. Hii ni kwa sababu utakuta vijana wengi hawana mwamko wa kwenda vyuo vya ufundi, vyuo vya kati na vyuo vya ujuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapopata ajira kwenye viwanda au tunapoanzisha kiwanda tutajikuta kwamba vijana hawana uwezo na taaluma ya kuweza kujiingiza kwenye zile sekta za viwanda. Nadhani tutumie vizuri nafasi za Maafisa Vijana katika Halmashauri zetu na kuwe na forum za majadiliano katika ngazi ya wilaya na baadaye mkoa. Serikali ione utaratibu ambao utawezesha vijana kujadili masuala yao mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapungufu haya yanaweza kufanyiwa kazi na kuleta tija kwa sababu hata sasa sekta ya michezo hatujaitumia vizuri ikaonesha mchango wake katika ajira kwa Taifa letu. Nasema hivi kwa sababu kama ambavyo vijana wanafanya mazoezi ya mashindano ya shule za msingi na sekondari na mwisho mkoa, hakuna utaratibu wa kuwashika mkono kwa vile vipaji vyao vinapoibuliwa na kufika kwenye ngazi ya mkoa. Kwa sababu hiyo basi, tunayo sababu ya kuendeleza fursa zote zinazowagusa vijana ili waweze kujiendesha na kutambuliwa kupitia vile vipaji walivyozaliwa navyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunawaambia vijana waanzishe shughuli binafsi au wajiari, mazingira si rafiki sana kwa sababu kwanza hawana mitaji lakini hata akisema anaanzisha biashara uwezo wa kusimamia biashara hana kwa sababu yeye mwenyewe alitarajia aajiriwe Serikalini ama kwenye sekta fulani wakati anasoma, hakuwa amejiandaa kwa kujiajiri. Kujiajiri ni nafasi pana au namna ya kijana kujiajiri kunahitaji maandalizi toka mwanzo, amefanya mazoezi kama nchi nyingine huko duniani zinavyofanya kwamba anapokuwa na sura fulani basi anakuwa na nafasi ambayo ameifanyia mazoezi na mwisho wa siku akijiajiri ni nature aliyokuwa nayo toka mwanzo na hiyo inampeleka kufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili pia naomba kuishauri Serikali, kuna taarifa isiyo rasmi inatembea ambayo inasema kauli ile ya Rais ya kubadilisha Kikokotoo siyo waraka wa Serikali. Kama kuna hiyo kauli na kuna watu wanaitumia hiyo loophole tunawaomba watambue kauli ya mwenye nchi ni sheria, ni waraka huwa inatakiwa izingatiwe. Wastaafu wengi wanalalamikia jambo hili kwa maana ya kwamba bado hawajabadilishiwa, kwenye Jimbo langu kuna baadhi wamenipigia simu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Zacharia.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nitoe shukrani za dhati kwa Rais mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Awamu hii ya Tano, kupitia salamu zao kwangu mimi Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini. Kwa kweli ni Serikali iliyofanya kazi kubwa sana katika Tanzania hii na hasa nikizungumzia Jimbo la Mbulu Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipoingia Bunge hili nilikuwa mkorofi sana, nilikuwa nachangia vibaya pia, lakini nilikuwa nafikiri ni lini matatizo haya ya wananchi wa Mbulu yatatatuliwa. Yamefanyika kwa kasi kubwa sana. Nitoe salamu za shukrani pia kwa Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima, Naibu Mawaziri na watendaji wote Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa shukrani hizi kwa sababu kulikuwa na mambo magumu sana yalikuwa hayafanyiki, lakini sasa yanafanyika. Nashukru sana kwa timu hiyo kufanya kazi toka walivyoingia madarakani pamoja na TANROADS. Barabara za Halmashauri ya Mji wa Mbulu zilikuwa hazipitiki nyakati nyingi za mvua na akina mama walikuwa wanapata shida. Kwa sasa ni miaka mitatu barabara hizo zinapitika nyakati zote pamoja na mvua hizi ambazo zinanyesha za mwezi wa Nne hadi wa mwezi wa Sita; na ni historia kubwa kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na daraja la Magara. Natoa shukrani za dhati kwa Katibu Mkuu ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI. Daraja la Magara ni daraja lenye upana wa mita 84, siyo rahisi ingejengwa kwa sababu mbele ya hilo daraja kuna mlima ambapo wewe Mheshimiwa Naibu Spika, ulipita, mlima wenye kona 130, haupo Tanzania nzima kwa maeneo ambayo nimetembea, lakini leo hilo daraja linajengwa liko katika hatua za mwisho. Naishukuru sana Serikali, nasema ahsanteni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ule mlima uliokuwa umepanda siku ile ulipokuja Mbulu, sasa karibu robo yake au asilimia 30 ya mlima una zege. Kwa hiyo, usiposhukuru wakati fulani utaonekana na wewe huna shukrani na hutambui jitihada za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile mnara uliojengwa katika Tarafa ya Nambis ambako wamehangaika sana Wabunge wenzangu waliotangulia, lakini Tarafa hiyo ambayo ndiyo asisi ya kabila letu kule Nambis, sasa hivi kuna Halotel wananchi wanawasiliana. Naishukuru kwa dhati sana Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na maboresho yoyote yaliyofanyika katika Mji wa Mbulu hadi sasa yanayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije sasa kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Eng. Kamwelwe. Utakuwa Waziri wa kwanza kuweka historia katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu kwa kilometa hizo 50 unazofikiri za kutoka Mbulu kwenda Haydom.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna namna nyingine. Jimbo la Mbuli Mjini tunapakana na Jimbo la Karatu, tunapakana na Jimbo la Babati, tunapakana pia wakati fulani na Jimbo la Vijijini, lakini eneo hilo la kilometa kama 389 inayozungumzwa, eneo letu ndiyo tuko katikati tumezengukwa na ukanda wa Bonde la Ufa ambako hakuna njia nyingine zaidi kutokea Haydom kuja Mbulu ama kutokea Karatu - Mto wa Mbu kuja Mbulu. Kwa hiyo basi, hizo kilometa 50 ni muhimu sana, ni za thamani. Mheshimiwa Waziri tunakushukuru kwa mpango wako unavyofikiri wa hata hizo kilometa 50 ili baadaye tuunganishwe kutoka Karatu mpaka kule Shinyanga kutokana na umbali huu kupunguzwa kwa awamu kwa sababu ya uwezo wa Serikali yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme ninaishukuru pia Serikali na ninaiomba isibadilishe mpango wake huu wa usanifu wa barabara ya Mbuyu wa Mjerumani – Magara – Mbulu ambapo barabara hiyo inaunganisha Mji maarufu wa Arusha, lakini pia inaunganisha Makao Makuu ya Mji wetu wa Babati. Kwa hiyo, ni shukrani pekee tunazitoa, lakini pia tunaomba mpango huu uzingatiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba sana Wizara hii pia iangalie utaratibu wa kuweka minara ile iliyopanga katika bajeti ya mwaka huu unaoisha Juni katika Tarafa ya Nambis ambako tulipagiwa minara. Basi tunamwomba Mheshimiwa Waziri na timu yake utekelezaji wa ile minara ufanyike.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaomba watutumie wataalam wa viwanja vya ndege kwani Mkoa wa Manyara hauna uwanja wa ndege, kwa sababu sisi tulio juu ya bonde la ufa kwa maaana ya Mji wa Mbulu huwa usafiri wetu wa dharura ni mgumu. Kwa hiyo, hata tukipata uwanja wa ndege kule Babati, Manyara utasaidia kuunganisha mkoa wetu na mikoa mingine ya nchi kwa kadri ambavyo itawezekakana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hii ni kubwa, ukisoma kitabu cha bajeti kwa kadri ambavyo fedha hizi kidogo kidogo ambazo zimewekwa ili kutatua changamoto zilizoko, zipo jitihada kubwa zimefanyika katika kila Wizara katika Jimbo la Mbulu Mjini ndiyo maana wakati fulani nanyamaza, nasema nitoe tu salama za shukrani lakini zaidi kuomba omba Serikali ihakikishe basi ni kwa namna gani hatua hii inayokusudiwa ya barabara hizi za Dongobeshi - Dareda kupata usanifu na Mbulu - Magara - Mbuyuni kupata usanifu, lakini na hizo kilomita 50 za kwenda Haydom, ambapo itakuwa imepunguza, tutakuwa na kipande cha Mbulu kwenda Karatu na kipande Haydom kwenda Shinyanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, eneo hilo ni muhimu sana, naona anasemeshwa, lakini hili ni ombi kwa niaba ya Serikali na nasema Waziri huyu ni msikivu atakuwa ameweka historia, barabara hiyo inaweza ikaitwa kwa jina lake, ikaitwa Kamwelwe Road kwa sababu ilikuwa haipo, haipatikani, sasa angalau kuna dalili, tunaishukuru Serikali na tunamshukuru na Rais. Naomba Mheshimiwa Waziri afanye ziara alikataa kupita Magara, alisema kona hizo ni nyingi anaogopa, akapita Karatu, safari hii akija apite Magara ili aone huo mlima tunaoulalamikia na hiyo barabara ya Magara ilivyo ngumu na Wanambulu wakiililia wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumshukuru Mungu kwa majaliwa yake kwetu sote.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya katika kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Spika, aidha, nampongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kuzuia uuzaji wa Chakula/Nafaka ya chakula nje ya nchi kwa kuwa nchi yetu mwaka huu maeneo mengi yamekumbwa na ukame.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuishauri Serikali kuongeza Bajeti ya Wizara hii kutokana na kwamba sekta hii huchangia zaidi ya asilimia 25 ya Pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, upungufu wa maafisa ugani tunaomba sana Serikali iajiri maafisa ugani walau hata kwa ngazi ya Kata kote nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali ichukue hatua za makusudi kupata fursa ya kuokoa mauzo ya korosho ili hata hasara itakayotokea iwe ndogo. Sote tunafahamu lengo la Serikali lilikuwa ni kukomesha hujuma walizokuwa wanafanyiwa wakulima wa korosho.

Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu nia hiyo njema ya kumwezesha mkulima kupata faida kupitia kilimo cha korosho.

Msheshimiwa Spika, mwisho naomba Wizara kupita wataalam wake wafanye ziara katika Jimbo la Mbulu Mjini. Tulikuwa na bwawa la Tlawi, katika Kijiji cha Tlawi. Bwawa hili la Tlawi limefanyiwa usanifu wa kina mwaka 2005 na kuombewa fedha kuanzia mwaka 2009 mpaka sasa. Hata hivyo nampongeza sana Mheshimiwa Isack Kamwelwe alifanya ziara ya kutembelea eneo lililotarajiwa mwaka 2017 na kuahidi kulitafutia hela. Kwa kuwa bwawa hilo ni muhimu na wananchi wa Kijiji cha Tlawi tayari wamepeleka mawe lori hamsini (50) katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, naomba Mheshimiwa Waziri kama tulivyo kubaliana ufanye ziara kwa ajili ya ufumbuzi wa suala hilo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na ninaunga hoja asilimia 100 kwa maslahi mapana ya taifa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuipongeza sana Serikali yetu ya Awamu ya Tano kuanzia kwa Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli, Rais wetu, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Naibu Waziri na watendaji wetu wote wa Wizara na mashirika yote ya umma na wadau wote. Shukrani hizi ni kwa ajili ya utendaji wake wenye dira kwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nitoe mchango wangu wa ushauri kwa Serikali yetu.

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ione umuhimu wa kutupatia mtumishi (afisa wanyamapori) kwa Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Mnamo mwaka 2017 nilimuomba Mheshimiwa Waziri, Prof. Jumanne Maghembe kuhusu hali tete ya wanyama wakali waliopoteza maisha ya wananchi nane ndani ya miezi mitatu mwaka 2015. Nami niliandika barua Wizarani kuomba mtumishi walau mmoja, hata hivyo Halmashauri ya Mji wa Mbulu inapakana na Hifadhi ya Marang’, Manyara na Msitu wa Hifadhi ya NOWU, eneo lote hili lina wanyama wakali.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara iharakishe fidia kwa wananchi walioharibiwa mazao yao kwa miaka ya 2016, 2017 na 2018 ambayo taarifa ya tathmini yao iko Wizarani (TANAPA).

(c) Mheshimiwa Naibu Spika, sheria itazamwe kuhusu viwango vya fidia na kifuta machozi kulingana na viwango vya sasa.

(d) Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali itoe fedha zinazoombwa na Wizara kwa asilimia 100 ili kuwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naunga mkono hoja asilimia 100, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuwapongeza sana viongozi wetu wote, Mheshimiwa John Pombe Magufuli - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu - Makamu wa Rais, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu pamoja na wewe Mheshimiwa Spika wetu na waandamizi wengine wote kwa nafasi zao mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nawaomba sana Watanzania tuungane kwa pamoja kumwomba sana Mwenyezi Mungu aiepushe Tanzania na dunia nzima kwa janga hili la dunia, kwa kweli hakuna mbadala katika janga hili.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali ije na mkakati wa kuboresha kukabiliana na majanga kwa kutazama, kutathimini na athari za tabianchi kwa kutenga fedha, wataalam na vifaa ambavyo kwa matukio ya sasa hali hii ya maafa na majanga haiepukiki.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali kupitia Halmashauri iteue shule moja ya msingi na sekondari zenye mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu ili kupata fursa elimu kwa kuwa kwa sasa kundi hili halina mfumo rasmi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nawaambia wapinzani kuwa kila Mtanzania ameelewa Serikali ya CCM imefanya nini, kwa hiyo propaganda haina nafasi tena katika Serikali ya awamu ya tano, tukutane Oktoba kitaeleweka.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja asilimia 100.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli Rais kwa jinsi anavyoiongoza nchi yetu. Hata hivyo, Watanzania wanakiri kuwa Mheshimiwa Rais amechelewa kupokea uongozi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Medard Matogolo Kalemani Waziri wa Nishati, Naibu Waziri na waandamizi wake kwa jinsi wanavyotumikia nafasi zao. Aidha, tunawaombea utume mwema katika kutimiza majukumu yao kwa Taifa la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, nimesikitika kukosa nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara hii. Hoja yangu ni kutaka Mheshimiwa Waziri wakati wa kutupa hitimisho lake atuambie ni lini mradi wa REA III utafikisha umeme katika Makao Makuu ya Kata za Gunyoda, Muray, Silaloda, Gunyoda kwa kuwa mradi wa REA awamu ya kwanza ulifika Mbulu 2007 mpaka leo kuna vijiji 38 na kata tano ambazo bado line kubwa haijafika ukiacha vijiji vingi ambavyo umeme umepita bila kufika kwenye vitongoji.

Mheshimiwa Spika, naomba uchunguzi wa kina ufanyike katika mradi wa umeme wa REA 1 – II – III kuhusu idadi ya nguzo zilizopelekwa kwani wananchi wanalalamika kuwa ni nguzo nyingi zinazoletwa katika halmashauri ya mji wakati huo mradi hauendi wala kusambaa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Kalemani alitoa ahadi ya kupeleka umeme katika Kata ya Muray toka mwaka 2016 akiwa Naibu Waziri mpaka leo umeme haujafika. Hivyo tunaelekea uchaguzi, kauli ya Mheshimiwa Waziri ni kauli ya Mheshimiwa Rais, hivyo basi, naomba kauli ya Serikali vinginevyo nitashika shilingi ni lini umeme wa line kubwa utafika kwenye Kata za Muray, Gunyoda, Silaloda na Soheda kupitia Mradi wa REA III katika Jimbo la Mbulu Mjini.

Mheshimiwa Spika, la pili, Serikali ina mkakati gani wa kusambaza chombo cha Umeme Tayari (UMETA) ili kupunguza gharama kubwa ya nguzo, waya na kazi zingine katika maeneo ya vijijini kwani mahitaji ya umeme katika kaya za vijijini ni taa, kuchaji simu hivyo chombo hiki ni muhimu sana

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maeneo mengi ya REA awamu ya I – II – III yamerukwa katika Jimbo la Mbulu Mjini na kwa kuwa kuna shule nyingi za msingi, sekondari, Makanisa yaliyoachwa toka 2008. Nashauri ziara za viongozi wetu hususan Mawaziri inapotokea basi wawasiliane na Waheshimiwa Wabunge badala ya TANESCO kupanga ratiba ya ziara hizo ili Mbunge naye atoe ushauri wake kumsaidia Waziri.

Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa Mheshimiwa Waziri wa Nishati Mheshimiwa Medard Kalemani alikuja kuzindua Mradi wa Umeme wa REA Jimbo la Mbulu Mjini katika Kata ya Ayomohe 2018 mwezi Mei lakini mpaka leo hakuna majengo yaliyosambaziwa hali hii imewapa mshangao wananchi wa Kata ya Ayamohe, naomba Waziri afanye tena ziara mapema mwaka huu ili kuleta msukumo.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nachukua nafasi hii kuwaombea watumishi wetu wa TANESCO Mkoa na Wilaya ya Mbulu waliotangulia mbele za haki Mwenyezi Mungu awapokee katika ufalme wake usio na mwisho. Aidha, naomba Wizara iwateue watendaji wa nafasi hizo ili kuimarisha utendaji.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake mbalimbali sisi pamoja na Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano na Sita kwa jitihada kubwa iliyofanya katika sekta hii muhimu sana ambayo ndiyo uti wa mgongo kwa Watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbulu naungana na Watanzania wote kumwombea kwa Mwenyezi Mungu Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano, Ee Mungu umpokee mtumishi wako mwaminifu, mtiifu, mzalendo, mwana mapinduzi mahiri wa Afrika katika ufalme wako wa milele mbinguni, Amina.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hasan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuapishwa kupokea uongozi wa Taifa letu tuendelee kumwombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kumlinda na kumjalia baraka zake katika kutuongoza.

Aidha, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wetu wote wa Wizara hii kwa ngazi mbalimbali katika jitihada zao kutekeleza, kusimamia na kushauri kwa weledi mkubwa katika nyakati mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia hotuba ya mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii kupitia kwa Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti wa Kamati hii.

Mheshimiwa Spika, Serikali isimamie suala la ubora wa pembejeo, uwepo wa Maafisa Ugani na mashamba darasa kwa kila kijiji hususan mashamba ya taasisi na shule za sekondari za kata katika maeneo yanayofikika kwa urahisi ili kuwasaidia wakulima wengi ambao kwa sasa wanapata mavuno ya gunia tano mpaka kumi kwa ekari moja wakati wangeweza kupata hadi gunia 40 kwa pembejeo bora.

Mheshimiwa Spika, kimsingi hadi sasa wakulima wetu wengi bado hawajafikia kile kiwango cha kilimo cha kisasa chenye tija. Hivyo basi ni muhimu sana Serikali ione utaratibu wa uhamasishaji wa kilimo chenye tija, pamoja na kuangalia uwezekano wa Maonesho ya Nane Nane kwa ngazi ya Wilaya kwa kufanya mapitio ya gharama za kuwezesha ili kuondoa gharama zisizo na tija.

Mheshimiwa Spika, Serikali iajiri Maafisa Ugani walau kwa ngazi ya kata na kuwapatia walau pikipiki na mafuta kupitia Halmashauri ili waweze kupanga ratiba ambayo itakuwa wazi kwa wananchi kwenye vijiji vya kata husika kama ilivyo kwa kada zingine za watumishi.

Mheshimiwa Spika, Serikali iache utaratibu wa kuzuia mauzo ya mazao ya wakulima kwenye masoko ya nje kwa kuwa wakulima nao hulima kwa gharama kubwa. Hivyo basi kama sababu kubwa ya kufanya hivyo ni upungufu wa mazao hayo Serikali inunue kupitia wakala wake na baadaye iuze kwa bei mbili tofauti ya soko la ndani na nje kwa kuwa tunawakatisha tamaa wakulima wetu.

Mheshimiwa Spika, Serikali itazame upya majukumu ya msingi ya kada za kilimo na ushirika kwa ngazi za Halmashauri za Wilaya, Kata na Vijiji kwani kwa sasa kata hizi katika maeneo mengi nchini zinakosa tija katika kutoa huduma kwa wananchi utakuta Afisa Ugani yuko kwenye ngazi fulani lakini hana mpango kazi.

Mheshimiwa Spika, naunga hoja asilimia 100 na naomba kuwasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kutoa mchango wangu kwenye Bunge hili. Kwanza nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake kwetu sote na kwa Taifa na sisi Watanzania wote. Pia nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyoongoza Taifa letu toka kipindi kilichopita na sasa. Vile vile nawapongeza wachangiaji wote wa leo kupitia Muswada huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sitachangia mpango huu, naomba univumilie, nizungumze kama Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mji, lakini pia kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mchango wangu ni mdogo sana. Kwanza, ni namna gani ambavyo wananchi wangu wa Jimbo la Mbulu Mji wanapata tabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kigugumizi cha kuzungumza suala la Corona. Jimbo langu wamepotea nikiwa huku Bungeni kwa mwezi mmoja watu wengi kidogo. Ukanda ule ni wa baridi. Naomba niishauri Serikali, tumekuwa na matumizi ya dawa za asili, tumekunywa kama gongo, yaani tunakunywa tu bila kujua hali halisi ikoje. Ni kwa nini Serikali isichukue jukumu la kuchukua dawa zote za Waganga wa Asili ikapeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali halafu ikaja na kauli ya kutuambia angalau ni dawa zipi tuweze kutumia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu inaonyesha vifo vilivyotokea kwenye Jimbo langu, sehemu kubwa vina viasharia vya mtu kushindwa kupumua, maumivu ya kifua na hali kadhalika. Nimekwenda Jimboni, nikaja kwako mara kadhaa kuomba kibali, wakati mwingine nimetoroka hata bila kuja kwa sababu nakwenda Jimboni, narudi; nafika huku mtu wa karibu amefariki, narudi tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawapongeza sana Waganga wa Asili waliochemsha miti shamba wakanywesha Watanzania. Waheshimiwa Wabunge tuliokuwa na kigugumizi, asilimia kubwa tumeshakunywa; nami nimeshakunywa. Ni kwa sababu sikubaliani na chanjo ya watu wa Magharibi, lakini nakubaliana na naamini dawa za asili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inashindwa nini kutumia wataalam wa ndani na vyombo tulivyonavyo kufanya utafiti ili angalau hizi dawa za asili sehemu fulani tujue ina msaada? Kwa sababu Jimbo langu la Mbulu watu wanapata matatizo. Hata leo niliitwa kwenda kuzika mtoto wa Diwani, nikawaambia jamani, Bunge liko ukingoni, ninyi muendelee tu. Ukiuliza, dalili ni hiyo hiyo; na ukanda wetu una baridi. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, majaribio haya ya dawa za asili ambayo tunakunywa kutoka Bunge lililopita na Bunge hili la sasa, mimi nimekunywa, sijui wengine, lakini naona matokeo yake ni chanya katika kutatua tatizo hili. Je, ni kwa nini basi kama hatuna wataalam au vyombo tusiagize hata wataalam wa nchi nyingine na vyombo nchi nyingine tufanye utafiti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza haya kwa sababu nina machungu. Itafika mahali hata hao wanaotupima hapo getini, Manesi wanaotuhudumia hospitalini; juzi nilienda Benjamin Mkapa kupata vipimo nikaambiwa Mheshimiwa mitungi haitoshi. Mitungi ya oxygen Benjamin Mkapa haitoshi. Pia mashine za oxygen hazitoshi. Najua kuna watu watanielewa vibaya, wacha wanielewe vibaya, mimi nimepewa dhamana ya kuja kuzungumza hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao watumishi wa Afya hatujajiweka vizuri namna ya kuwalinda, namna ya wao kuwa na imani. Dawa hizi za mitishamba tunazokunywa ni ghali sana. Ni kati ya shilingi 30,000/= mpaka 50,000/=. Mwananchi wa kawaida hawezi. Je, haiwezekani Serikali ikachukua jukumu la kufanya utafiti angalau kwa dawa zetu? Siyo lazima sisi tuamini vitu vya watu wa ng’ambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naamini kabisa Tanzania tuna hazina kubwa ya dawa za asili. Tatizo letu ni namna ya kuzichambua ili tujue ni dawa gani zina mchango kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la Mbulu Mji lina Hospitali ya Mji ambayo iko katikati. Ina vituo vya afya lakini hawana mashine hiyo ya oxygen, hawana mitungi na watu wanakufa. Wanapokufa kwa ugonjwa huu pengine wa kifua au kushindwa kuhema, mashine hizo zingeweza kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki iliyopita sikupata kuchangia, nilikuwa naenda Jimboni nazika, narudi; nafika hapa, narudi naenda kuzika; ifike mahali niseme wazi tu kwamba hali halisi ikoje. Kwa Mbulu, ukanda ule ni wa bonde la ufa. Juu ya bonde la ufa kuna baridi sana. Mwezi wa tatu, wa nne, wa tano, wa sita na wa saba, mafua haya yatakuja tu na watu watapata shida.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Zacharia Issaay.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, lakini naomba mitungi hiyo ipelekwe katika Hospitali ya Mbulu na hospitali nyingine nchini na vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Polepole, alisema, Corona ataishi Tanzania kwa adabu na sasa anaishi kwa adabu, lakini kwa kutegemea dawa zetu tulizonazo na mifumo yetu tuliyonayo na maombi yetu tunayoomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa Serikali, hospitali za wilaya, vituo vya afya, wapelekewe hiyo mitungi isaidie.

MWENYEKITI: Ahsante sanaMheshimiwa.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, umenionea, sijamaliza dakika kumi.

MWENYEKITI: Ni dakika tano tano.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Ni tano?

MWENYEKITI: Eeh, ni tano.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono Mpango uliokuwa umejadiliwa na wenzangu. Ila hili ombi langu lifanyiwe kazi kwa nchi nzima. Tunalo tatizo, tusifiche.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili lipo tu, kwa heshima na taadhima nikwambie. Maana sisi tulioko huku tusifikiri siku moja hatutakuwa wananchi. Tutakuwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono Mpango wetu ulioletwa kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza niungane na Watanzania wote na Waheshimiwa Wabunge kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake kwetu sote. Nafasi hii ya pumzi na uhai ni rasilimali na rehema za Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru pia Serikali kwa kazi kubwa iliyofanya, Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi kilichopita kupitia sekta hii ya afya, kwa kweli kuna miradi mingi na mageuzi makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nije kwenye kuchangia hoja iliyopo mezani. Nizungumzie Bima ya Afya kama wenzangu walivyozungumza, Bima ya Afya ni changamoto, ni changamoto kweli kweli. Bima ya Afya ambayo mtumishi amekatwa fedha zake lakini anakwenda hospitalini hakuna dawa. Kama Bunge tunatakiwa kujitafakari, kujitathimini na nini angalau Serikali ichukue hatua za mahususi kwa ajili ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya afya ni sekta muhimu sana na ugonjwa hauna hodi, unapougua wala hakuna maandalizi yanayotokea. Kwa hiyo eneo hili lina changamoto, hakuna dawa na kwa wakati wowote ule mtu anapata madhara lakini akifika kwenye sehemu ya huduma hawezi kuhudumiwa kwa sababu wa ukosefu wa dawa na vifaa tiba. Kwa hiyo, nashauri kama itawezekana, kuna haja kubwa sana ya kufanya tathmini kwenye huduma ya afya na fedha nyingi zinatumika kwenye huduma ya afya kwa kulipia gharama ambazo hazina uhalisia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukienda sekta binafsi, huduma ambayo kwenye sekta ya Serikali unapata kwa laki moja au na laki na nusu; kwa sekta binafsi ni kati ya laki tano mpaka sita. Mifano ya wazi iko kwenye miwani, mifano ya wazi ipo kwenye vipimo na unasaini form, lakini wakati unasaini form ukilinganisha na huduma unayopata Serikalini kuna tofauti kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linahitaji Serikali itazame upya na ione uwiano au utofauti huu uliopo ni kwa kiasi gani tunaweza kuwa na tofauti ya kawaida. Sioni sababu za msingi za gharama hizo kuwa kubwa kwa sekta binafsi wakati kwetu sisi haipo. Ninavyoona ni vile kwenye vituo vyetu tunakosa kabisa huduma hizi na tunapokwenda sekta ya binafsi basi wao wana maamuzi yao binafsi juu ya utoaji wa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili lilitusumbua sana, kama alivyozungumza Mheshimiwa Abbas Tarimba, wakati wa uchaguzi hoja nyingi zilizopunguza kura za CCM ilikuwa huduma za afya; huduma ya afya kwa wenye bima, huduma ya afya kwa wananchi, huduma ya afya kwa wazee, huduma ya afya kwa watoto na huduma ya afya kwa mama na mtoto. Hapa tusipapase wala kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa. Tunalo tatizo kwenye huduma ya afya kwa sababu sera inazungumza tofauti na hali halisi iliyoko kwenye maeneo ya huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inatakiwa itazamwe kitaalam nini kifanyike, kwa mfano, kwenye jimbo la Mbulu Mji, tulikuwa na wakati mgumu sana wa kutetea kura za CCM kwa sababu ambulance ambayo inamsafirisha mgonjwa wa rufaa anayetoka Hospitali ya Mji wa Mbullu kwenda Haidom lazima awe na laki moja ya mafuta ya ambulance, vinginevyo mgonjwa huyu hata angekuwa amepata matatizo hasafirishwi haraka ili kuokoa maisha yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninachozungumza ni kwamba, wakati fulani tunapotoa huduma nadhani kuna haja ya kuwasikiliza wale wanaopokea huduma nao wanasema nini kuhusu huduma tunayotoa sisi kama Serikali. Kwa nini nazungumza hivi? Kijana anayepata ajali wa bodaboda, familia ya kwao unakuta haina uwezo ya kulipa hiyo ambulance kwa laki moja. Sasa mgonjwa huyu hatahudumiwa kwa wakati na kwa umuhimu ulioko ili aende kwenye kituo cha afya au kwenye hospitali ya rufaa ili aweze kuhudumiwa. Kwa hiyo, nadhani eneo hili litazamwe, Serikali haifanyi biashara inatoa huduma na kama tunatoa huduma kuna maeneo nyeti ya kutazama.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo la huduma ya mama na mtoto. Kuna ushahidi wa wazi hususani jimbo la Mbulu Mji, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wapokee taarifa hii nimeshawaeleza hata tukiwa wenyewe kwamba kuna haja kubwa ya kutazama upya Hospitali ya Mji wa Mbulu na huduma inavyotolewa. Tunalo tatizo unakuta akinamama wajawazito wanaingia kwenye gharama; analipia vifaa tiba pamoja na gharama mbalimbali ili aweze kuhudumiwa kwa ajili ya kujifungua salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ninayoyazungumza nina ukweli nayo, nimekwenda hospitalini mara kadhaa kuwauliza walioko kwenye huduma na wameniambia tunalo tatizo na wanasema nisiwe naondoka ondoka niwe nafika hospitalini kila siku. Sasa kwa kweli kazi Mbunge ni kukaa geti la hospitalini ama kwenye wodi ili kwa kuwa yupo ndio waweze kutoa huduma bora. kwa hiyo, nadhani hili jukumu ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ziara ya Kamati; Kamati zetu zinapopita, ziende basi kuwasikiliza pia wapokea huduma, wafanye hata namna ya kusikiliza wanaopewa huduma wanasemaje, kuliko kupita tu kukagua majengo ya hospitali, kukagua vitu mbalimbali, waende pia kwenye upande wa upokeaji wa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia vitambulisho vya wazee, wazee ndiyo waliolitumikia Taifa hili, naomba sana vitambulisho vya wazee walivyogawiwa havina huduma hospitalini, hakuna dirisha la wazee, hakuna afisa anayewashika mkono awapeleke wanapaswa kwenda wapi na kuangalia sehemu gani. Sisi kama Wabunge kuingia kwenye jengo hili kunatufurahisha sana, lakini tuangalie sana kuingia kwenye jengo hili ni kwa ridhaa ya wananchi walio wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba hata Wizara ya Waziri, wawe wanafanya vikao Waziri na Naibu Waziri, wasipite tu barabarani, wasikilize wananchi wanasema nini katika maeneo wanayofanya ziara ili wasikie huduma ya afya ikoje. Eneo hili ni muhimu sana, sisi Mbulu tuna vituo vitatu, tuna hospitali ya mji, hatuna gari la ambulance, hatuna mafuta, hata Nurse anataka alipiwe, tunakwenda wapi? Tunapokwenda ni wapi? Nadhani kuna maeneo tunakosea sana. Maeneo yetu ya kisera na maeneo ya wale wanaopokea huduma wanatushauri nini ili tukafanye vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa watumishi kwenye sekta hiyo umeathiri sana huduma bora kwa akinamama, watoto na wazee kwa sababu eneo lao halifikiwifikiwi zaidi ya wale wagonjwa ambao wanamwona Daktari na Muuguzi, lakini eneo hilo la wazee, eneo hilo la akinamama na watoto, eneo hilo la watu wa bima ambao ndiyo watakaohamasisha bima ipendwe nchini, halina watumishi kwa kiasi kikubwa sana katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo kwa uchache sana kutokana na muda ni eneo hili ambalo nataka kuwaeleza kwamba, wakati fulani tunapotoa huduma hizi za afya, sisi tuwe kama kioo au kama kauli nzuri kwa sababu unakuta Nurse aliyeko hospitalini badala ya kauli yake kuwa sehemu ya tiba, anakuwa sehemu ya kuongezea ugonjwa. Tatizo ambalo si nzuri sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imeshagonga.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nitashika shilingi. Naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ISSAAY Z. PAULO: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuungana na viongozi wa Taifa letu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake kwetu sote kama Taifa kupitia majanga mbalimbali hususan janga la corona, kimbunga cha jobo kule Mtwara na mengi kadha wa kadha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupokea uongozi wa Taifa letu. Hivyo tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu amjalie ulinzi na baraka katika kuongoza Taifa letu tuwe kielelezo mbele ya mataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge letu navipongeza sana vyombo vyetu vyote vya ulinzi na usalama, kama nchi siyo rahisi kutambua haraka kujua kazi kubwa ya vyombo vyetu vya ulinzi ndani ya nchi na nje ya nchini. Nayasema haya kwa sababu majeshi yetu ni nguzo ya tunu ya amani na utulivu ulioko nchini kwetu. Hivyo basi sisi kama Bunge tuwe mstari wa mbele tuwatetea kupata stahiki zao mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini nachukua nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 na 2020 kwa jimbo langu la Mbulu, hongereni sana wadau mbalimbali walioshiriki kwa kwa hali na mali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee naungana na Watanzania wote kumwombea sana Mheshimiwa Hayati John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano kwa kweli kama Taifa mchango wake tutaukumbuka daima. Ee Mwenyezi Mungu umpokee mtumishi wako mwaminifu, mzalendo, mtiifu mwana mapinduzi wa Afrika katika ufalme wako wa milele mbinguni, Amina.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha naungana na waheshimiwa viongozi wa Taifa letu, Bunge zima, Watanzania wote kwa ujumla kutoa pole nyingi kwa msiba wa kifo cha mpendwa wetu Mheshimiwa Hayati Khatib Said Haji, Mbunge wa Jimbo la Konde, Mwenyezi Mungu ampokee katika ufalme wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kutoa ushauri wangu kupitia bajeti hii ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa nikianza na kutokana na changamoto kubwa sana ya makazi ya askari, upungufu wa magari na vitendea kazi hivyo Serikali ijitahidi kupeleke fedha zote zinazopangwa kwenye bajeti zetu kwani hali ni mbaya sana ili majeshi yetu yatekeleze majukumu yao kwa weledi mkubwa kuendana na utandawazi mkubwa duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema hayo kwa sababu nimehudumu kwenye Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Serikali yetu haijafanikiwa kupeleka fedha za maendeleo kwa zaidi ya 50% zinazopangwa.

Pili, kutokana na vijana wengi kujiunga na JKT na baada ya kuhitimu wanarudi uraiani. Ni wakati sasa wa kuona kuwa na matawi ya SUMA JKT kwa ngazi ya mikoa ili kuchochea fursa za ajira kupitia matawi hayo. Kuna umuhimu wa kutoa maelekezo ya Serikali kuajiri vijana wote kwenye ulinzi katika taasisi za umma kama vile halmashauri, elimu, afya na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie umuhimu wa dhana ya uraia na uzalendo ambao ndiyo nguzo muhimu sana kwa kila Mtanzania ili kuwajengea vizazi vyetu na Watanzania kwa ujumla kwani ni dhahiri kuwa vijana wote wanaohitimu JKT hawataweza kupata nafasi za ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vijana wengi wanaojiunga na JKT toka awali hawajiandai kisaikolojia kuwa lengo lake ni kujiari hivyo ni muhimu toka mwanzo wa kujiunga vijana wetu waulizwe hulka yake ni nini katika kujiajiri kama sekta za kilimo, ufundi, ufugaji ili kubaini anapaswa kwenda kambi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naunga hoja mkono asilimia 100 na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuungana na viongozi wenzangu na Watanzania wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuijalia nchi yetu baraka katika ustawi wa kijamii, kichumi, kisiasa, kidiplomasia mbele ya mataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuapishwa kushika hatamu ya kuliongeza Taifa letu, Mwenyezi Mungu amlinde na kubariki kutuongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini naungana na Watanzania wote kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano katika uongozi wa Mheshimiwa Hayati John Pombe Magufuli, Rais wa Serikali yetu ya Awamu ya Tano, viongozi wake waandamizi, watendaji na wadau mbalimbali kwa jinsi walivyosimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2021 hususan sekta ya viwanda kama mhimili mojawapo uliotufikisha uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha kwa namna ya pekee naomba kumwombea Mheshimiwa Hayati John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Seikali ya Awamu ya Tano, Mheshimiwa Khatib Said, Mbunge wa Jimbo la Konde, Wahshimiwa Wabunge wenzetu na Watanzania wote waliotangulia mbele ya haki, Mwenyezi Mungu awapokee katika ufalme wake wa mbinguni, Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nitoe mchango wangu kupitia mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii, kwanza tunaiomba Serikali ifanye tathimini ya viwanda 100 kila Hamashauri zilizoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya TAMISEMI, kwani uwepo wa viwanda 100 ulikuwa chachu ya ajira kwa kila Halmashauri, japo kuna haja kubwa ya kuwa na Maafisa Biashara watakaosimamia, kushauri na kuratibu uendeshaji wa viwanda hivi ili kulinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ifanye mapitio ya mchakato wa uanzishwaji viwanda na biashara kwa kuondoa vikwazo, urasimu na vigezo ambavyo siyo rafiki katika uanzishwaji wa viwanda hapa nchini kwa kuwa suala la uwekezeji lina ushindani mkubwa sana duniani kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali ijitahidi kupeleka fedha zote zinazoombwa kwenye bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuleta ufanisi mkubwa katika sekta hii kushikilia uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwe mstari wa mbele kusimamia suala la ubora wa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kwa ajili ya kulinda afya ya watumiaji na kukidhi ushindani, bei, ubora na soko la ndani na nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isimamie suala la kuhamasisha matumizi sahihi ya blueprint kama dira katika kuhamasisha wawekezaji hali itakayochochea uanzishwaji wa viwanda kulinda uwepo wa Tanzania kudumu katika kundi la nchi za uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga hoja hoja asilimia mia moja, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia mada hii iliyoko Mezani.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuipongeza Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa utekelezaji wa miradi ya REA nchi nzima. kwa ujumla Serikali imefanya kazi kubwa kuanzia Serikali ya Awamu ya Tano na hii ya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri Kalemani na timu yake bila kinyongo kwa moyo mweupe maana kati ya miaka hii mitano iliyopita na kipindi hiki tulichoanza wamejitahidi sana kwenye miradi hii ya REA. Mimi niseme tu kwamba Waziri amejitahidi sana, ameenda kwenye Jimbo langu karibu mara tatu, nampongeza na kumshukuru na Mungu aendelee kumbariki. Mchango wake ulikuwa mkubwa kwa mimi kurudi hapa Bungeni kutokana na hii miradi aliyotekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nichangie kidogo kwenye Wizara hii. Kwanza mradi huu unaokuja tunauomba uanze na kata ambazo zimerukwa. Kuna kata ambazo aliahidi kule kwangu akiwa Naibu Waziri na baadaye Waziri; Kata za Murai, Silaloda, Masieda na Nasei.

Mheshimiwa Spika, eneo hili limetusumbua kwa sababu ya jiografia na umbali kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakandarasi mliowateua, niwapongeze wale waliowasiliana na Wabunge wao lakini nimewasiliana na Wabunge wa Mkoa wa Manyara kwa kweli, mkandarasi wetu hadi sasa hajaweza kuonesha utayari wa kuwasiliana na sisi ili tujue mipango yake anayokwenda kutekeleza ikoje. Hii itasaidia sana ikiwa Madiwani, Waheshimiwa Wabunge watafahamu jinsi ambavyo miradi hii itakavyotekelezwa ili baadaye tuwe kitu kimoja na hata tunapokwenda kwa wananchi tuwe na kauli ya pamoja tukijua utekelezaji wa mradi utaendaje.

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye utekelezaji pia wa Mradi wa Ujazilizi. Nina kata 17 ambapo saba ziko mjini na 10 ziko vijijini, lakini watu wa REA wanasema wewe wa mji huduma yako ni TANESCO na TANESCO hata miaka 10 hawataweza kupeleka umeme kwenye kata hizo kwa sababu, mbili hazikupelekewa umeme moja kwa moja Kata ya Silaloda, lakini pia na Kata ya Ilboru kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kama itawezekana, kata zile zilizoko pembezoni kwenye eneo la mji wangu au eneo la Mji wa Mbulu ziingie kwenye REA kwa sababu bado hazijafikiwa. Kama nilivyokudokeza Mheshimiwa Waziri, wewe ni msikivu na pia unatusikiliza sana huku Bungeni, lakini tuna hofu kidogo na utekelezaji wa ahadi zako unazotoa. Ukiwaagiza wao hawana majawabu na pia hawatekelezi kwa wakati, utakumbuka mwaka 2019 tulikwenda Mbulu, tulifanya ziara, ukaagiza umeme uende Gunyoda na Murai, lakini mpaka leo bado. Sasa kupitia hii REA inayoanza waanze na kata hizo ili wananchi wale waone ahadi ya Waziri ni ahadi ya Serikali na hiyo ahadi ya Serikali iweze kutoa matokeo chanya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kama kuna maeneo ya namna hii, kwa mfano kwenye Jimbo la Mbulu Mji kuna vijiji toka 2009/2010 wamepelekewa umeme kwa kaya kama 20 mpaka 50, kaya nyingine bado zinasubiri kwenye maeneo ya vijijini. Najua timu ya Wizara ilipita wakati ule ikatambua maeneo ambayo umeme haujapelekwa na ramani ilishachorwa basi waanze kwenye hivyo vijiji ambavyo vinahitaji ujazilizi kwa ajili ya kufanikisha jambo hili.

Mheshimiwa Spika, udhibiti wa magenge na kuchukua fedha za wananchi. Kumekuwa na tatizo kubwa wananchi wanahitaji umeme, wanaambiwa umeme utakuja, baadaye wanaambiwa hampo kwenye orodha. Kwa hiyo, kuna uchukuaji rejareja wa fedha kwa wananchi Sh.50,000, Sh.100,000, mianya ambayo sio mizuri sana kwa taswira ya Serikali yetu. Nashauri kama itawezekana watu hawa wadhibitiwe na TANESCO na mamlaka zilizoko na pia wananchi wahojiwe kwa nini nguzo tatu zilipelekwa kwa fulani ambaye yuko kijiji fulani badala ya ule mradi unaoendelea.

Mheshimiwa Spika, jambo hili ni la muhimu sana na kwa namna ya pekee nashauri kama itawezekana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Zacharia Issaay.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja kwa asilimia 100, tuko pamoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana na viongozi, Watanzania wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali za ustawi wa kijamii, kiuchumi, kidiplomasia na kisiasa. Kama Taifa tuendelee kusema ahsante sana Mungu wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini nachukua nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hasan, Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kwa kupokea uongozi wa Taifa letu kwa amani na utulivu. Ninamwombea baraka, ulinzi na mafanikio makubwa kwa Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Spika, aidha, nawaombea watendaji na wateule wote wa Serikali ya Awamu ya Sita, Mwenyezi Mungu awajalie mafanikio mema katika utume wao Taifa letu lipate kufikia malengo makuu.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana na Watanzania kuendelea kuwaombea Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano na Watanzania wote waliotangulia mbele ya haki kwa Mwenyezi Mungu awapokee katika Ufalme wake usio na mwisho. Kwa kweli kama Taifa mchango wake utakumbukwa daima. Kwa vielelezo hivi, Bwawa la umeme, SGR, Busisi Bridge, Bomba la Mafuta na mengine mengi sana.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii ya Nishati. Kwanza Wizara kupitia Mpango wa REA lll unaoendelea, ije na mkakati wa kuwatambua walengwa kwa kuwa wako wateja wengi sana waliofanya uwekaji wa waya katika makazi yao lakini umeme haujaunganisha.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ugumu wa utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Waziri katika Jimbo langu la Mbulu Mjini kupitia ziara zake mbalimbali katika Jimbo letu. Kwa kauli ya watendaji wa TANESCO na REA kuwa hawana fedha, mifano hiyo iko katika Kata za Murray 2016, 2018, Gunyoda, Nahasey 2018 hadi sasa umeme haujaenda, hali iliyotupa wakati mgumu kuomba kura za CCM wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba, 2020.

Mheshimiwa Spika, kutokana na maeneo mengi ya vijijini kuwa na uhitaji mkubwa wa nguzo na nyaya za umeme, Serikali iangalie uwezekano wa kufanya uhakiki wa maeneo hayo ili kupeleka kifaa cha utayari (UMETA) wakati majengo yakiendelea kuongezeka. Hivyo basi, naomba kauli ya Serikali kuhusu hali hii umeme kwamba utaenda lini?

Mheshimiwa Spika, mwisho, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini nachukua nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kulijaalia Taifa letu ustawi katika nyanja mbalimbali za kijamii, kiuchumi, kisiasa, kidiplomasia, hali inayotufanya kuwa kelelezo mbele ya mataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naungana na Watanzania wote kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kupokea uongozi wa Taifa letu, hakika tumekuwa kielelezo mbele ya mataifa, nawaasa Watanzania wenzangu tumpe ushirikiano wa dhati na kumwombea kwa Mwenyezi Mungu amjalie ulinzi, baraka na mafanikio katika kuliongoza Taifa letu Eeh Mungu mjalie baraka zako za milele.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Jemadari wa Afrika na Mwana Mapinduzi na Mzalendo wa kweli, Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, viongozi na watendaji wote kwa jinsi tulivyotekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa kiasi kikubwa. Hakika tumwombee Hayati Mheshimiwa John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Taifa mchango wake tuukumbuke daima, pamoja na viongozi na Watanzania wote waliotangulia mbele za haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kwa Wizara hii ya Fedha kupitia Taarifa ya Hali ya Uchumi yam waka 2021/2022; kwanza Serikali itazame upya mfumo wa kukusanya kodi ya mapato kwenye taasisi za fedha hususan mabenki na mawakala wao kwani mara nyingi unapotoa hela kwenye ATM mbalimbali utaona ujumbe wa maneno kuwa hakuna huduma kwa sasa kwani mfumo huu utaikosesha Serikali kupata mapato yenye uhalisia. Sote tufahamu kuwa upatikanaji wa tozo na kodi kwenye miamala ya fedha ukidhibitiwa vizuri na Serikali tutapata mapato mazuri kwa kuwa kiwango cha riba na tozo ni mkubwa katika taasisi hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TAMISEMI itazame mpango wa kutoa mafunzo ya Waheshimiwa Madiwani kufahamu majukumu yao katika kusimamia Halmashauri zetu nchini, kukusanya mapato ya ndani na matumizi ya mapato hayo, kushauri na kuhamasisha shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza sana Serikali Kuu kwa azma yake ya kulipa posho za Madiwani kupitia mapato ya Hazina hivyo basi kuna sababu mahususi za kutazama fedha zilizopangwa awali kupata miongozo yake kwa Waraka kutoka TAMISEMI ili mchanganuo wake uwasilishwe kwenye kikao cha Kamati ya Fedha ya mwezi Julai kwa waraka badala ya maelekezo kwa fedha zile nyingi ili sehemu itakayobaki isaidie kuchangia miradi ya maendeleo kwenye kata na vijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha Serikali iangalie kiwango cha posho ya vikao kwa Waheshimiwa Madiwani kwani kiasi cha shilingi 40,000 kwa Diwani wa Kata kuhudhuria kwa robo mwaka kwa kikao kimoja tu ni kidogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono kwa asilimia 100 na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, naungana na Watanzania wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa jinsi alivyoijalia nchi yetu baraka zake katika ustawi wa jamii, amani, demokrasia, uchumi, diplomasia ya mashirikiano na mataifa mengine.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ilivyotatua changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta za elimu, afya, maji, barabara na vitendea mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, aidha binafsi ninakupongeza sana kwa kuchaguliwa kwako kuwa Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwenyezi Mungu akujalie mafanikio mema.

Sasa naomba nitoe mchango wangu katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu; kwanza Serikali itazame kwa upana suala la kukabiliana na majanga kutokana na matukio mbalimbali kwa kuja na mkakati wa kukabiliana na matukio yanayojitokeza kama vile corona, moto, ukame, mafuriko, viwavi jeshi na milipuko ya magonjwa, kwa kuandaa rasilimali wataalam fedha na vitendea kazi.

Mheshimiwa Spika, pili, Serikali ifanye tathimini ya kina kuhusu mafanikio ya viwanda 100 kwa kila Halmashauri ili kuleta tija zaidi kwenye ajira kama ilivyo kusudia awali; tatu, Serikali ifanye mapitio ya kina ahadi za viongozi wakuu wa Serikali walizotoa wakati wa uchaguzi na ziara wanazofanya mfano ni miaka saba sasa ahadi ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John P. Magufuli ya lami kilometa tano, Mbulu Mji ni kilometa 2.5 mpaka sasa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu. Nichukue pia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia kuona siku ya leo; lakini pia nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa inayofanyika kwenye Jimbo la Mbulu Mji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nianze na hoja chache. Mwaka huu wakati wa bajeti hii inayoendelea tuliletewa muhtasari wa mpango wa utekelezaji wa umeme vijini. Tulifurahishwa sana na huu mpango wakati ule ukiwa unaelezea jinsi ambavyo mpango huu utataekelezwa kwenye maeneo yetu, hasa miradi ya umeme. Tuna changamoto kubwa sana kule vijijini kwa sababu tunapofika muda fulani wa kuhitimisha Bunge hapa tunalazimika kwenda kule vijijini ili tuweze kuwaambia wananchi walau Serikali yetu ina mpango upi kwa upande wa kila sekta.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hoja yangu kubwa ni kwamba miradi hii ya REA Vijijini imekuwa michache na inasubiriwa sana na wananchi kwa jinsi ambavyo umeme ni nishati muhimu sana kwa maisha ya kila siku na kwa huduma mbali mbali za jamii. Kwa hiyo katika taarifa ambayo ninaijengea hoja muda huu ni taarifa ya utekelezaji wa mpango huu kwa sababu viko vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme hadi sasa kwenye maeneo mbali mbali hususan Jimbo lile la Mbulu Mjini. Jimbo la Mbulu Mji lina vijiji na mitaa. Eneo la vijijini kuna vijiji ambavyo na kata hadi sasa umeme haujafika lakini mkandarasi ana miaka miwili. Ni kwa kiasi gani tunafuatilia utekelezaji huu wa mpango wa umeme vijijini? Na kwamba unafanyiwa tathmini inapofika muda fulani na wakandarasai wanaopewa hii kazi na REA nao wanafuatiliwa ili walau wanachi wapate huduma kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa iliyowasilishwa ya mpango huu ilitupa matumaini kwa sababu katika bilioni 2.705 ya fedha za Wizara hii, kama tulivyoambiwa kwamba hela nyingi za miradi, kwa asilimia karibia 99, ilikuwa ya fedha za ndani; pengine tumekwama huko. Hata hivyo, sasa wananchi kule vijijini hawajapata umeme. Mimi nilikuwa naishauri Serikali, kabla hatujaenda kwenye bajeti ya mwaka unaokuja, huu wa 2023/2024 kwanza tujitathmini hao wakandarasi wamefanya kazi zao kwa kiwango kilichokusudiwa na mipango kazi yao ilienda vizuri? Na kama haikwenda vizuri basi tujitathmini na kuona namna gani tunachukua hatua sasa ya kubadilisha utararibu ule wa kazi zilizoko kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mkandarasi anatekeleza kwenye mikoa mitatu ndani ya miaka mitatu lakini hakuna eneo liliowasha umeme. Vilevile unakuta ni nguzo tu zimesimikwa, maeneo mengine hakuna nguzo na maeneo ya visima vya maji hakuna umeme, na maeneno mengine yanakosa umeme kwa sababu ya maeneo ya migodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikua naona kama inawezekana historia ya wakandarasi hawa itazamwe upya na hasa yule aliyepewa kazi Mkoa wa Manyara, kwa sababu bado tuna tatizo kwenye mkoa wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine, ni eneo la ujazilishi. Kwenye taarifa hii ya Wizara, nitampatia Mheshimiwa Waziri baadaye; kuna maeneo ambayo tulitegemea sana, maeneo ya ujazilishi yanapata miradi lakini kwa bahati mbaya miradi hii ya ujanzilishaji haijaanza hadi sasa. Kwa hiyo, mimi nadhani pia tujikite kwenye utaratibu wa ujazilishi kwa sababu katika kijiji unakuta kuna kaya 20. Kaya zingine zote takriban 200 na kitu hazina umeme kwa sababu hatujaweza kusambaza kwenye vitongoji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa kuwa mpango wetu wa awali huu wa mwaka 2022/2023 ulikuwa unagusa maeneo ya ujazilishi, na huu mradi wa ujazilishi uje vizuri kwenye mpango unaokuja ili tuweze kufanikisha adha hii na njia hii ya huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo la ruzuku ya Serikali kwenye mafuta. Tunaipongeza Serikali kwa mpango wake wa kuweka ruzuku kwenye mafuta, na tulitegemea itapunguza makali, na kwa sehemu imepunguza. Hata hivyo tunachoona mafuta yanaposhuka bei ya usafirishaji inabaki pale pale. Mafuta yanapopanda bei ya usafirishaji inabaki pale pale. Sasa hapo ndipo mwananchi mtumia huduma anajiuliza; ni kwa kiasi gani walau ruzuku yetu ya Serikali imekua na tija? Na kama ni kipindi cha tathmini hapo pia tunatakiwa tufanye tathmini ili tuweze kufanya utaratibu mzuri wa ruzuku uwe na tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kutokana na muda niseme pia, kwenye maeneo ya mijini na maeneo ya vijijini sasa hivi TANESCO wametowa utaratibu mpya wa umeme kwa 320,000 na umeme wa 27,000 ubaki kwenye maeneo ya vitongojini. Hata hivyo kwenye miji mingi, hasa Mji wa Mbulu, mitaa kumi ndiyo center ya mji, mitaa mingine 48 na vijiji 34 vilivyoko vijijini ni maeneno ya wananchi. Kwa hiyo, mimi nilikuwa nafikiri kwa kuwa tunajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere, na tuwaombee viongozi wetu walioanzisha wazo hili; tuone utaratibu wa maeneo ya vijijini ni kwa namna gani basi umeme ule wa vijijini unarudi katika kiwango cha 27,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jinsi tunavyokwenda kwenye baadhi ya mitaa na baadhi ya maeneo hata pembezoni mwa miji wananchi wengi hawataweza 320,000. Kwa hivyo kuna haja ya kuona kama tunajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere na eneo hili la ujazilishi na eneo hili la uunganishwaji wa umeme litazamwe katika mpango wa bajeti unaokuja, ili kufanikisha taarifa nzima ya utaratibu ambao unaweza ukasaidia wananchi hao ambao tayari wengi wao wamefanya wiring. Tayari wengi wao wana hamu ya kuunganisha. Hata hivyo, wiring tu laki tatu na kitu mpaka laki nne, ukichanganya na laki tatu nyingine na ishirini hizo ni laki saba. Kwa hali ya kawaida ya mwananchi wa kijijini au mwananchi anayetegemea hiyo nishati, kwa kweli hataweza kuunganisha umeme kwa jinsi ambavyo uwezo wa mwananchi ulivyo na hali halisi ilivyo na hatuwezi kuwa na manufaa kwa umeme huu ambao sahizi tunajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere. Lengo letu ni umeme uzalishe kwa kasi, lengo letu ni kuangalia kiasi gani wananchi wengi wanaunganisha umeme na wakishaunganisha umeme wanufaike na fursa hii ya kupata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika utaratibu huu wa kuangalia shughuli mbali mbali za miradi ya maendeleo tumekuwa na mipango mizuri sana, mipango ambayo tukienda kutafsiri kwa wananchi baadaye wanachi nao wanatuhoji mbona ule mpango wenu mlioutafsiri kwetu haujatekelezwa. Mimi nilikua nafikiri kama inashindikana wakati fulani tuanze na vipaumbele kama vinavyoainishwa kwenye Wizara mbali mbali na hasa hii Wizara ya Nishati ili mwisho wa siku tuweze kuona ni namna gani tunapata umeme kwa wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine; ni dhahiri wazi 2015 tulisema tutapeleka umeme kila kijiji na kila kitongoji 2020 kwenye…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa inayofanyika Serikalini ya kutatua matatizo ya wananchi. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Innocent Waziri wetu wa TAMISEMI na timu nzima Manaibu, Katibu Mkuu wa TAMISEMI na Mtendaji Mkuu wa TARURA pia na Watendaji wote wa Wizara hii walioko chini ya Wizara hii. Mimi ni Mjumbe wa Kamati kwa hiyo mchango wangu ni sehemu tu ya nyongeza kwenye taarifa ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali kwa mradi wa maboresho ya Miji Tanzania (TSCP) kwa Mji wa Mbulu ni mradi mzuri. Mradi huu ndiyo unakuja kugusa wananchi wa Mji wa Mbulu na Miji mingine nchini na kwa kuwa miradi hii inagusa soko, stendi, barabara za lami, dampo na machinjio, vyote vilivyotajwa kwenye mji wa Mbulu haviko. Kwa hiyo naishukuru sana Serikali. Rai yangu kwa Serikali ni kwamba waangalie Miji yenye changamoto nyingi ya miradi hii kwa maana ya kama Mbulu kwa sababu changamoto ni kubwa na inaweza ikagusa maisha ya mafanikio ya wananchi kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ni eneo la ufunguzi wa zahanati kwa kuwa dakika zenyewe ni chache niseme tu kwamba wananchi wana hamu kubwa na haiba kubwa ya kujenga miradi ya zahanati. Katika mji wa Mbulu tuna zahanati nne zilizo tayari kwa maana ya Halmashauri ya Mji wa Mbulu, lakini zahanati hizo zilianzishwa siyo mwaka huu zilianzishwa miaka minne iliyopita, kwa sababu hiyo basi, tungeiomba Wizara waangalie zahanati zote zilizo tayari kwa kuwa wameandika kwenye taarifa ya mpango wa bajeti basi ziweze kufunguliwa baada ya Julai ya mwaka huu kwa ajili ya mwaka huu wa bajeti ili tuweze kuona wananchi walioanzisha zahanati miaka saba, miaka tano, miaka nne basi waweze kuona manufaa ya miradi walioanzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyingine ni ahadi za Viongozi Wakuu hasa zinazogusa eneo letu la TARURA. Mheshimiwa Rais Hayati Magufuli aliahidi lami kilomita tano katika Mji wa Mbulu, hadi sasa ni kilomita 2.5 zinazotekelezwa inaonyesha kama vile chini ya mita 500 kwa mwaka kwa bajeti ya mwaka kwa barabara hizo. Kwa hiyo, sababu yake hapa ni kwamba Viongozi hawa Wakuu wanaporudi wananchi wanaanza kuhofu na kufikiri kwa nini miradi hii au ahadi hizi za viongozi wakubwa zinachelewa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani TARURA kupitia TAMISEMI waende waratibu upya ahadi za Viongozi Wakuu halafu baada ya hapo waweze kuweka kwenye vipaumbele kadri ya miaka inavyokwenda ili kuondoa madeni ya ahadi za viogozi wetu wa ngazi zile za nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni posho za Waheshimiwa Madiwani. Bahati nzuri mimi nilianza kuwa Diwani posho za 350,000 zilitolewa kwa miaka karibu 10 sasa na kwa kweli hali ni mbaya sana kwa Waheshimiwa Madiwani mimi niungane na wale Wabunge wenzangu waliozungumzia jambo hili kwa upana isitoshe hiyo hata posho za vikao wanapewa 40,000 wakati nikiwa Diwani posho ya kikao kimoja ilikuwa sitting ni 70,000 lakini wakati huo huo night za kutoka kwenda kwenye vikao ni siku tatu maana 65,000 x 3 = 195,000 + 70,000 sasa hivi ni 40,000 hata ungekuwa unaenda wapi na vikao vinapoisha Waheshimiwa Madiwani wanatembelea bajaji, wanatembelea boda boda wanalala katika mazingira magumu huko vijijini ndiyo wao wanasimamia shughuli za maendeleo na watendaji wanaosimamiwa wana mishahara mikubwa sana. Kwa hiyo siyo rahisi mtu anayesimamia watendaji wengine yeye anakuwa na posho kidogo kiasi hicho. Mimi ninafikiri ni muda muafaka wa sisi kutazama upya ili kuona ni namna gani kwa kadri ya mapendekezo ya Kamati yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji hawa ni watu muhimu sana nao tusiwaache kwa kweli, kwa sababu Mheshimiwa Waziri Innocent sina mamlaka ya kushika mshahara wako lakini hatutarajii kwamba mshahara wako unakwenda kushikwa kwa ajili ya jambo hili limezungumzwa kwa upana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo jingine ni kwamba naishukuru Serikali wameweka daraja la Unyoda lililokuwa kikwazo na limetenganisha Halmashauri mbili katika mpango. Ninaomba wasiondoe iendelee na baada ya Julai tuanze utekelezaji wake. Eneo jingine ni ukarabati wa shule kongwe nchini, Halmashauri ya mji wa Mbulu au Mji wa Mbulu ni Mji ulioanzishwa na wakoloni kwa takribani sasa shule asilimia 60 ya Mji wa Mbulu ni shule kongwe kwa sababu ndiyo Makao Makuu ya Wilaya ya Mbulu ambayo imezaa Karatu, imezaa Babati, imezaa Hanang na sasa Mbulu Vijijini. Kwa hiyo eneo hili nalo ni muhimu sana kwetu sisi tunaiomba Serikali iangalie kwa mapana yake namna ambavyo itaweza kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nichangie eneo la Milioni 500 kwa kilomita moja, Mheshimiwa Waziri na watu wa TARURA, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara kwenye Jimbo la Mbulu Mji alikuta mradi wa kilomita moja bado haujatekelezwa, ulitangazwa mara tatu hauna Mkandarasi, hebu tujiridhishe tatizo ni Watendaji hawatimizi wajibu wao, ama ni fedha hazitoshi za Milioni 500 kwa sababu kilomita moja ina mifereji, kilomita moja ina lami, kilomita moja ina taa za barabarani, kilomita moja kuna culvert huko huko tuangalie na kama tatizo siyo hilo basi hata sasa huo mradi ndiyo unaanza kutekelezwa utakamilika lini huu wa kilomita moja ili fedha hizi ziweze kutazamwa na ikidhi haja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla tunaishukuru Serikali kwa kazi kubwa inayofanya. Watutolee pia fedha za ukamilishaji wa miamala kwa ajili ya vituo vya afya ili walau miradi iendane na mwaka wa bajeti na tuweze kukamilisha miradi yetu kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri nyingi zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa Wahandisi kadiri tunavyopeleka fedha nyingi vijijini, fedha nyingi kwenye Halmashauri hatuna Wahandisi, mimi nadhani tufanye tathmini ya mapitio tuna Wahandisi wangapi wako eneo gani Halmashauri gani haina Mhandisi nini kifanyike kwa hatua ya dharura ili miradi iende kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana nimechangia kwa muhtasari kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati nayarudia kuyakumbusha yale tuliyojadili, naunga hoja mkono kwa asilimia mia moja, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii muhimu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kujaalia neema na baraka Watanzania. Aidha naungana na Watanzania kuipongeza sana Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu mpendwa kwa jinsi inavyotekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025 na kutatua kero ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nitoe mchango wangu kupitia hotuba ya Wizara na Kamati ya Katiba na Sheria; kwanza Serikali iangalie matumizi sahihi ya maadhimisho ya siku ya sheria kwa ajili ya kupata picha ya upande wa wapokea huduma ili kutathmini kwani kwa sasa jamii na wapokea huduma hawajafahamu kikamilifu maudhui ya maadhimisho hayo, hivyo basi kutafutwe muundo mzuri wa siku hiyo kuwa na tija nzuri zaidi ili kuleta ufanisi wa utendaji kazi na jamii kuwa na imani kwa mahakama kama mhimili wa kutoa haki kwa wapokea huduma za jamii na matumizi sahihi ya media, redio na mitandao ya kijamii.

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu itoe fedha za kujenga na kukarabati mahakama zote kongwe zilizojengwa toka enzi za kikoloni kwani kwa sasa hazifai kwa matumizi, mfano huo ni Mahakama ya Wilaya ya Mbulu, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri atembelee na maeneo mengine nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali ijitahidi kutoa fedha zinazoombwa kwenye bajeti kwani hadi mwezi Februari, 2022 ni kiasi cha asilimia 29.87 kilichotolewa ya maombi ya matumizi, kiasi hiki ni kidogo sana kulingana na malengo yaliyotarajiwa katika kutekeleza majukumu yake muhimu na katika maombi ya miradi ya maendeleo hadi Februari, 2022 ni asilimia 45.37; hali hii itaathiri mpango wa bajeti ya maendeleo ya mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, Serikali iandae kalenda ya vikao vya Kamati ya Maadili za Wilaya na Mikoa na kuwepo kwa wajumbe kutoka upande wa wapokea huduma ili kupata taswira ya upande huu. Aidha, ni muhimu sana kuangalia hadidu za ajenda Kamati ya Maadili za Mahakama.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuungana na viongozi wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake kwetu sote katika majanga mbalimbali na mafanikio katika nyanja za ustawi wa jamii, amani, uchumi, diplomasia na siasa za utashi mwema na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuungana na viongozi wenzangu wote kuwapa pole nyingi wale waliopoteza wapendwa wao katika kipindi chote hadi leo hii, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awapokee katika ufalme wake usio na mwisho mbinguni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha kwa namna ya pekee nachukua nafasi hii kuipongeza sana Serikali yetu ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano kwa jinsi inavyosimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 hadi 2025, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kazi iendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nitoe mchango wangu katika Wizara hii muhimu kwa ustawi wa uchumi wa Taifa letu. Serikali yetu ifanye mapitio ya blueprint ili kutathimini wawekezaji wa ndani na nchi ya nje kwa ajili ya kuona inatoa hamasa kwani changamoto kubwa inayosababisha nchi yetu kutokuhimili upandaji wa bidhaa na mfumuko wa bei ni uchache mkubwa wa viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi za ndani mfano wa wazi ni mafuta ya alizeti, sukari, kahawa na mengine, lakini husafirishwa nje ya nchi na baadaye kurudishwa ndani ya nchi baada ya kuchakatwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu ihamasishe uwepo wa wawekezaji wakubwa wa viwanda vya dawa, pembejeo za kilimo na uchimbaji wa mafuta na gesi kwani matukio ya janga la corona na vita vya Urusi na Ukraine na mengine mengi iwe ishara kwa Taifa letu kujifunza athari za majanga katika uchumi wa Taifa letu na kuepuka uagizaji mkubwa wa bidhaa zinazoweza kuzalishwa ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha nadhani ni wakati muhimu sana Wizara yetu ione kupata tathimini ya viwanda vidogo 100 vilivyoanzishwa kwa kila Halmashauri kwani bado kwenye maeneo ya vijijini kuna malighafi nyingi za kutengeneza na kuchakata na kufungasha bidhaa za matumizi za majumbani kama subuni ili kupunguza mahitaji madogo madogo na kuchochea ajira mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja kwa asilimia mia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, naungana na Watanzania wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake katika Taifa letu kwa jinsi alivyotuvusha kupitia changamoto mbalimbali kama vile janga la Corona, mafuriko, mioto, ajali mbalimbali na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wetu mpendwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoiongoza nchi yetu na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Profesa Mkenda, Waziri wa Wizara hii; Mheshimiwa Omary Kipanga - Naibu Waziri wa Wizara hii; pia nampongeza Mheshimiwa Sodoyeka Katibu Mkuu wa Wizara hii; Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara hii; Wakurugenzi na watendaji wote wa Wizara hii kwa jinsi mnavyoitumikia Wizara hii hongereni sana Mwenyezi Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nitoe mchango wangu kupitia hotuba ya mapendekezo ya Wizara hii muhimu sana kwa ustawi wa Taifa letu; kwanza naipongeza sana Wizara kwa mpango wake wa kufanya mapitio ya sera yetu ya elimu ili kuendana na mahitaji muhimu kwa wakati uliopo na ujao, na mchakato wa kuchukua maoni ya wadau mbalimbali kuhusu mtaala wa elimu yetu ili kumwezesha Mtanzania kukabiliana na mazingira ya karne ijayo katika dunia hii.

Mheshimiwa Spika, Serikali itusaidie kuanzisha Kitengo cha Elimu Maalum kila halmashauri kwenye shule moja ya msingi katika tarafa ambayo iko katikati ya kila halmashauri mfano huo uko kwenye Halmashauri ya Mji wa Mbulu Shile ya Msingi Endagikort ambayo ina wanafunzi zaidi ya 30.

Mheshimiwa Spika, napongeza pia hatua ya Wizara kumtuma Mkurugenzi wa Elimu Maalum Dkt. Matonya kuitembelea Shule ya Msingi Endagikort, asanteni sana.

Ninaomba Wizara itusaidie kurasimisha kitengo hicho na kujenga bweni la kulala wanafunzi wa elimu maalum. Hivyo basi wakati tukielekea huko tusisahau kuona elimu ya vyuo vya ujuzi hasa vyuo VETA na FDCs mitaala yake kufanyiwa mapitio ili kumwezesha mhitimu kufika chuo kikuu kwa ngazi za kuhitimu secondary school, cheti cha ufundi, diploma hadi shahada.

Mheshimiwa Spika, kwa moyo wa dhati ninaiomba sana Serikali itoe fedha za awamu ya pili kukamilisha ujenzi na ukarabati wa majengo ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi - Tango FDC Mbulu kwa kuwa ujenzi wa awamu ya pili ulishakamilika kwa kiwango cha juu sana, kwani Tango FDC ilijengwa miaka 60 iliyopita hivyo majengo mengi ni chakavu sana na hatarishi kwa matumizi.

Mheshimiwa Spika, kwenye mitaala ya elimu ya msingi na sekondari tusisahau kuingiza masomo ya maarifa ya jamii, kilimo, mifugo, biashara kwani zaidi ya 50% ya vjana wetu wahitimu wa kidato cha nne ndiyo Watanzania wa kawaida ambao hawataweza kwenda kwenye elimu ya juu kwa hiyo, maarifa na ujuzi watakayopata kwa ngazi hizo za msingi na sekondari inayowaweka kwenye hali ya kukabiliana na changamoto za kukabiliana na maisha ya kawaida.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja 100%.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niungane na Wabunge wenzangu na Watanzania wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake kwetu sote.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili; nimpongeze sana Mheshimiwa Rais. Zipo sababu za msingi za kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu ya mikopo hii ambayo juzi tumepata ya COVID-19 kwa sababu imegusa mpaka mwananchi yule wa chini na tumepata miundombinu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zile sababu zinapopingana na mikopo hii ni sababu za kiuelewa tu kwa sababu kila mtu hapa anadaiwa na kila Taifa linadaiwa. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais na aendelee kutafuta fedha zaidi ili kutatua matatizo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nikupongeze Profesa na timu yako, Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii pamoja na Watendaji wote kwa jinsi ambavyo mnaihudumia Wizara hii na kwa jinsi ambavyo mnaitendea haki. Hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza pia Wizara kwa mapitio ya sera na mitaala kwa wakati wa sasa. Elimu yetu ya sasa ni lazima iendane kukidhi matakwa ya wakati wa sasa na wakati ujao. Sera iweze kufanya mapitio kwa wadau wote ili kupata mawazo mazuri na namna ambavyo itakidhi haja pengine kwa miaka 50 ama pengine hata 100 kwa huko tuendako.

Mheshimiwa Naibu Spika, huku kila mmoja ana mawazo. Mimi nizungumzie hili suala la fikra ya Serikali kutaka kuondoa kada ya Maafisa Elimu Kata. Nadhani suala hili tulitazame kwa upana kabla ya maamuzi. Tunaweza kuwa na maamuzi tukafikiri kwa muda wa haraka yanatija lakini athari ziko. Kata moja ina shule mia na kitu, Maafisa kwenye Wilaya tunao wawili. Hivi ni kwa kiasi gani tunaweza tukawapanga wale Maafisa wa Elimu wa Wilaya wakasaidia kusimamia shule zaidi ya 100 ama shule takribani 100 na wale walioko kwenye hizo shule wakaweza kutoa tija na kutimiza majukumu yao bila usimamizi wa ngazi yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni tuliondoa Kada ya TRC’s hivi Vituo vya Ualimu. Muda mfupi baadae tukarudisha, nadhani kila jambo tunapoangalia tufanye tathmini lakini pia ushauri wangu kwa Serikali na hata Wizara kwenye Sera inayokuja kama kada hizi zilikosa majukumu na kazi za kufanya, basi tutazame majukumu ya kimsingi ya usimamizi wa kada hii na iwe imewekwa kwenye mitaala na kwenye Sera ya Elimu ili na wao tuone product yao au uzalishaji wako na ustawi wa eneo hili, kwa sababu siyo rahisi Walimu wa shule zote nchini wakafanya kazi bila usimamizi ambao ni wa utashi na kitaaluma na ambao unapimwa katika muda fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia mfumo ambao unatumika ingawa Wizara hii ni mtambuka na Wizara ya TAMISEMI. Kwa mfano, Watendaji Walimu Wakuu, Waratibu Elimu hawa TRC’s na Maafisa Elimu wa Wilaya, wanafanya vibaya kwenye eneo moja anapewa uhamisho kwenda kwenye eneo jingine wakati bado tuna rasilimali ya watendaji wazuri sana. Jambo hili ambalo baadae mwisho wa siku tunakuja kukuta alipokuwa amebomoa anakwenda kubomoa sehemu nyingine na yule ambaye anafanya vizuri kwenye eneo moja anahamishwa kwenda eneo jingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, badala ya kuwa na mfumo wa maboresho tunakuwa na mfumo wenye mkanganyiko wa Watendaji ambao tunawahamisha bila sababu za msingi badala ya kuwaondoa. Nadhani ifike mahali hatuoni haya, utendaji na usimamizi wa mtu ulingane na tathmini inayofanyika na mafanikio yanayopatikana kwenye nafasi ambayo ameteuliwa na mamlaka fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nimekupa jana mchango mkubwa sana wa maandishi, kutokana na muda huu wa dakika tano ambao siyo rafiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niseme kwamba twendeni kwenye eneo hili la chakula cha mchana shuleni. Bila kuwepo kwa chakula cha mchana kwenye Shule za Msingi, kuzungumzia eneo la ufanisi wa taaluma ni kazi bure. Kama ni kwenye eneo la mtaala tazameni kama ni Sheria au Kanuni itakayowataka wazazi kuhakikisha chakula cha mchana shuleni kwa wanafunzi ni lazima. Isiwe tena ni hiyari kama ilivyo kwenye maeneo mengi nchini na shule moja ya jirani inafanya vizuri na shule nyingine haifanyi vizuri, lakini shule hizo ziko kwenye eneo moja na mazingira yanafanana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo jingine ni semina za Kamati. Kamati za Shule tunapoteua, tunawateua kwa tabia zao, mienendo yao katika jamii, lakini baada ya kuwachagua hatuna namna yoyote ya kuwafanyia semina na namna yoyote ya mafunzo ili wajue majukumu yao na jinsi ambavyo wataisaidia jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nadhani kama inawezekana eneo hili pia la semina kwa Kamati za Shule ni muhimu sana ili kuleta uwiano mzuri na daraja zuri kati ya jamii yenye shule na shule yenyewe ili kupata ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango mwingine Mheshimiwa Waziri amezungumza kwenye hotuba yake. Miundombinu aliyozungumza ya nyumba za Walimu, majengo mengine. Mwalimu anakosa nyumba kwenye shule aliyopelekwa anatoka kilomita 10 ama kilomita tano kutoka mahali yalipo majengo ya kupangisha. Gharama tu ya kwenda kwenye hiyo shule na kurudi kwa mfano anakuja asubuhi kama ni 5,000/= ya bodaboda, mchana 5,000/= kwa ajili ya chakula, kurudi tena shuleni 5,000/=, kurudi tena nyumbani 5,000/=. Mshahara wa Mwalimu huyu unaisha kwenye gharama tu za kuhudumia nafasi yake bila kupata chochote na bila kuwa na manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka kuishauri Serikali, niungane na wale wenzangu wote waliozungumza namna ya motisha kwa Walimu na namna ya ruzuku ya ufundishaji kwa Walimu. Kada hii ya Ualimu vijana wetu wanaenda tu kwa sababu ya kupata ajira lakini kwa jinsi mazingira yake yalivyo na kama kuna kada zingine tunavyotoa motisha pengine kwa kazi zingine wanazofanya pamoja na zile za ajira na utumishi, tuna haja kubwa ya kuitazama upya ili kundi hili nalo tulione kwa moyo mkubwa na jinsi ambavyo kazi yao ya utume imetufikisha hapa tulipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la upungufu wa Walimu wa Sayansi limekuwa na athari kubwa sana. Vijana walioko Sekondari na hata wa Shule za Msingi wanashindwa kupata taaluma ya sayansi kwa majaribio na sayansi kwa kina kwa sababu Walimu hawa hatuwezi kuwaajiri kwa jinsi tunavyoona. Serikali itazame ni kwa namna gani walau hata shule moja inakuwa na Mwalimu wa Sayansi au hata wawili kwa sababu unakuta wanafunzi ni wengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jinsi ambavyo maeneo mengine yana Walimu wa Sanaa, tunakosa Walimu wa Sayansi muda mrefu. Katika migao ya Walimu wa Sayansi, tutazame eneo hili kwa sababu muda wa wanafunzi wetu shuleni huwa hausimami unakwenda na mwisho wa siku wanafanya mtihani na ndiyo maana tunakosa Walimu wengi wa Sayansi kwa jinsi ambavyo hali inakuwa ngumu sana ya kuwaajiri kwa wingi unaohitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Serikali ifanye tathmini ione namna gani sasa tunapata walau hao Walimu, hata kama siyo kwa kiasi kikubwa tuweze kupata eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni jinsi ambavyo matatizo ama mashtaka ya Walimu yanachukua muda mrefu sana. Unakuta Mwalimu ana mashtaka…

NAIBU SPIKA: Ahsante. Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, basi mchango wangu uungane na mchango ule wa maandishi. Naunga mkono hoja. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa kuandika jana na leo andika tena ni vizuri.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana na viongozi wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake kwetu sote, kwani tunajivunia kwa jinsi alivyotuvusha kwenye majanga mbalimbali kwa mfano corona na ustawi katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kidplomasia, kisiasa, amani, mshikamano wetu kitaifa, hongera sana mama.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kwa niaba ya wananchi wote wa Jimbo la Mbulu Mjini kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu mpendwa kwa jinsi anavyoiongoza nchi yetu na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM yam waka 2020/2025.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara na Mheshimiwa Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa jinsi mnavyoitendea haki Wizara hii kwanza kutusikiliza sisi wawakilishi wa wananchi na kutatua tatizo la maji kwa nchi nzima, hongereni sana.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nitoe mchango wangu kupitia hotuba ya Wizara hii, Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yako nzima naomba kukueleza masikitiko yangu kwa kuwa katika mpango wa bajeti mwaka 2016/2017 Halmashauri ya Mji wa Mbulu ilikuwa miongoni mwa miji itakayonufaika na mradi wa miji 28. Binafsi mimi nasikitika kwa sababu hata wakati tunaondolewa mimi kama mwakilishi wa wananchi sijashirikishwa, wakati Jimbo la Mbulu Mjini kuna kama 17 kata 10 eneo la vijiji 34 na kama saba yenye mitaa 58, hadi sasa ni kisima kimoja tu cha Bargish Antsi kilichimbwa 2016/2020. Hivyo basi kupitia kauli yako ya wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani. Tunaomba mturudishe kwenye miradi ya P4R kutokana na eneo hilo la vijiji 34 na kutuongezea fedha zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tuliwasilisha maombi yetu ya nyongeza ya fedha za miradi kutoka milioni 700 mpaka bilioni 1.5 lakini kiasi hicho hakipo kwenye mapendekezo bajeti ya mwaka 2022/2023 na document hizo ninazo kwenye tablet yangu. Ninapata wakati mgumu sana kushika shilingi yako, hivyo kwa heshima kubwa ninakuomba mdogo wangu kaa na timu yako kuona njia mbadala ya kunusuru hali hii, chonde chonde.

Mheshimiwa Spika, ninaiomba Wizara yetu hii iagize makusanyo ya mapato ya bili za maji katika maeneo yote ambayo tayari kuna DPS za maji nchini kwani hali hii itasaidia kudhibiti upotevu wa fedha za mauzo ya maji.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maji itazame utaratibu wa mapendekezo ya majina ya bodi za maji kwani kwa sasa mchakato wa wajumbe wawili wa bodi mpya kwa kila nafasi kwenye ngazi za Kata, Baraza la Madiwani na baada ya hapo Meneja wa RUWASA ngazi hiyo kuwasilisha ngazi ya Mkoa na Wizara kwa ajili ya kupata wajumbe mahiri katika kusimamia utoaji wa huduma bora za maji kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, mwisho, naomba kuwasilisha na naunga hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika Taifa letu nyakati zote kwa kutujalia amani, upendo, mshikamano na kutuepusha katika majanga mbalimbali makubwa nyakati zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa jimbo langu nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wetu wote kwa jinsi wanavyoliongoza Taifa letu na walivyosimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha mwaka 2020 – 2025, kwani kuna mafanikio makubwa sana katika nyanja za kidiplomasia, kiuchumi, maridhiano ya kisiasa, ustawi wa jamii na utatuzi wa kero mbalimbali kwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye sekta zote nchini. Aidha tunaendelea kuiombea nchi yetu baraka za Mwenyezi Mungu katika ulinzi, amani, mafanikio na mshikamano kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu Mheshimiwa Rais wetu, viongozi na watendaji wetu wote awajaalie mafanikio mbalimbali katika kuliongoza Taifa letu wakati wote wanapotekeleza majukumu yao wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia hotuba ya mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii ya Katiba na Sheria iliyowasilishwa katika Bunge letu hivi punde.

Pia Serikali iangalie mpango wa kufufua Mahakama za Mwanzo katika ngazi za tarafa ambazo zilianzishwa toka enzi za mkoloni ili kurahisisha wananchi kupata huduma za mahakama kwa ukaribu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iangalie uwezekano wa kujenga mahakama zote kongwe zilizoanzishwa toka enzi za mkoloni ambayo majengo yake yote ni chakavu sana kwa sasa, mfano wake ni Mahakama ya Wilaya ya Mbulu ambayo ilijengwa na mkoloni toka mwaka 1934 ambayo kwa sasa ni chakavu sana na iko ndani ya mita kumi ya hifadhi ya barabara kuu hali inayosababisha kelele nyingi sana za magari yanayopita wakati shughuli za mahakama zikiendelea na kuhatarisha usalama wa wananchi waliokuja kusikiliza mashauri ya ndugu zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi nawasilisha maombi mahususi Wizarani kutupatia fedha za ujenzi wa jengo hilo la mahakama katika bajeti hiyo na tayari uwanja umeshapatikana, pia nitashukuru sana kama Wizara itatuma wataalamu wa Wizara kuja kuona hali halisi ya jengo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iangalie utaratibu wa uteuzi wa wazee wa mahakama nchini kwa kuwekwa wazi kwa wananchi wa wanaopokea huduma katika eneo hilo na namna ya kuwahudumia kwani uwepo wao ni muhimu na kutaisaidia mahakama kutekeleza majukumu yake kwa uwazi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali itoe kwa asilimia 100% fedha za ujenzi wa mahakama zinazoombwa katika kila mwaka wa bajeti nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa 100% na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba niungane na wachangiaji wote walio mshukuru Mungu kwa majaliwa yake kwetu sote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya. Mimi nichangie tu mchango mdogo sana, la kwanza ni kwenye Bima ya Afya.

Mheshimiwa Waziri Bima ya Afya kwa baadhi ya hospitali imekuwa tatizo kubwa sana. Nadhani ni wakati muafaka wa kufanya tathmini kuongeza idadi ya watu tutakaowataka maoni yao kuhusu suala la Bima ya Afya.

Mheshimiwa Spika, Bima ya Afya huduma inayotoa Benjamin Mkapa, Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na baadhi ya hospitali hapa nchini inatolewa kwa hatua ya juu sana, lakini katika hospitali nyingi nchini Bima ya Afya inalalamikiwa sana. Nadhani ifike mahali sasa tuone kwamba namna ya Bima ya Afya ni pamoja na kuangalia utoaji wa huduma kwa wanachama wake na jinsi ambavyo kila hospitali nchini inakuwa na dirisha na Afisa anayehudumia pamoja na Daktari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda Benjamin Mkapa na ukaenda Hospitali ya Rufaa ya Dodoma wanao Madaktari waliopangwa kuhudumia watu wa Bima ya Afya, lakini katika hospitali nyingine wanachama wa Mfuko huu wa Bima ya Afya na Makundi yale mengine ya Bima ya Afya wanalalamika sana. Jukumu letu kubwa ni kusema yale ambayo ni mazuri na yale ambayo kidogo wapokea huduma wanalalamika. Mimi nadhani tuongeze wigo wa mikutano kwa mwaka kama mara mbili kwa wale wapokea huduma ili tujue wanasema nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni eneo la utendaji wa MSD. Kupitia Bunge hili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. MSD utendaji wao tumechoka, MSD nanunuzi yenyewe yanachukua miezi Sita, mifano hai ambulance tunazosubiri sasa ni miezi sita, lakini pia picha ya wazi ipo kwenye Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Tumeagiza jokofu ni miezi sita sasa, jokofu halijaletwa wananchi wanapata matatizo, tumehangaika vya kutosha.

Mheshimiwa Spika, hebu tuulizane kumbadilisha Mkurugenzi Mkuu inatosha Mheshimiwa Waziri? Kupitia ile ziara ya Waziri Mkuu hadi sasa, kwa nini tusiangalie kurudi kwenye suala la kuangalia upya mfumo mzima wa MSD na watendaji wake? Jambo hili linawaumiza watanzania walio wengi, kwa sababu tunaweza tukambadilisha Mkurugenzi Mkuu lakini MSD ikabaki na mfumo uleule ambao una matatizo. Nilitegemea baada ya ziara ya Waziri Mkuu, naamini Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya kazi kubwa sana Serikali haitachukua hatua. Lakini ni wapi tumepoteza hata ile sura ya kutumbua tumbua, tukatumbue tumbue huko huko MSD kwa sababu kuna matatizo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, katika hali ambayo tunafanya hii kazi ya kuwawakilisha wananchi, wananchi wanalamika kule, hiyo MSD yenyewe ukizungumza upande mmoja, Mbulu Mji hatuna ambulance, x-ray, mortuary. Hivi kweli Watanzania wa Halmashauri ya Mji Mbulu inazungukwa na eneo lote la vijijini, huduma ni pale katikati, vitu vyote hivyo havipo! Pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri tunakupongeza sana umefanya kazi kubwa sana ulipokuwa Wizara hii ndiyo maana Mheshimiwa Rais amekuona akakurudisha Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, hivi kweli watanzania wa Mji wa Halmashauri ya Mbulu Hospitali ya Mji wa Mbulu inazungukwa na eneo lote la vijijini huduma ni pale katikati vitu vyote hivyo havipo. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri tunakupongeza sana umefanya kazi kubwa sana ulipo Wizara hii ndio maana Mheshimiwa Rais amekuona akakurudisha Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nashauri kama itawezekana tuone utaratibu wa namna gani tunaweza tukatazama. Kama ni sisi tunashindwa kumudu huduma hizi za upatikanaji wa dawa na huduma zingine tukae chini tuangalie, ni utaratibu gani utakaowawezesha Watanzania kupata huduma ya dawa na huduma nyingine za matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ufunguzi wa zahanati. Halmashauri ya Mji wa Mbulu tayari tuna zahanati nne zilizo tayari zimeanzishwa kwa mchakato wa wananchi takribani miaka kama saba, nane, sita sasa hivi ziko tayari kibali tu cha kusajili zahanati hizi imechukua zaidi ya mwaka. Wananchi waliouza mali zao waliotumia nguvu zao wakajenga zahanati hizo wanasubiri huduma lakini huduma haziwafikii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani tuharakishe utaratibu huu wa mchakato wa kusajili zahanati na vituo vya afya ili walau, huduma za mwanzo zianze kutolewa tuweze kufanikiwa namna ambavyo tunaweza tukapata hali halisi ya mafanikio katika utoaji wa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi hawatuelewi kabisa wanapoona wamemaliza kujenga zahanati mwaka wa kwanza unakwisha mwaka wa pili unakwisha. Ninawaomba sana watu wa Wizara ya Afya na TAMISEMI kaeni pamoja mtufungulie hizo zahanati ili wananchi wapate huduma za mwanzo. Mwananchi analalamika anapotoka kwenye Kijiji kwenda kwenye Hospitali ya Mji kwa gharama pengine ya Shilingi 20,000 kwenda Shilingi 10,000 na kurudi Shilingi 10,000 lakini huko huko dawa anagharamikia nafuu angekuwa anapata hiyo huduma anayofuata pale alipo ili gharama za usafiri zisiwepo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni matumizi ya lugha ambayo hayaridhishi. Yapo matumizi ya lugha kwa baadhi ya watumishi wetu wa sekta ya afya hususani wale ambao tunawaita wakunga, wauguzi pamoja na madaktari. Lugha ya daktari ni sehemu ya tiba anapotumia lugha ambayo mgonjwa akifika anaongezeka ugonjwa ni shida sana. Mheshimiwa Waziri ninakuomba sana katika jambo kama hili tusione haya kuchukua hatua unapofanya ziara. Alikuja Naibu Waziri wa TAMISEMI Afya alikuta madudu kule Mbulu alipewa taarifa ambayo haina uhalisia, alipokwenda kwenye nyaraka inapishana na taarifa ambazo amepewa hadi leo hakuna hatua iliyochukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nadhani kama Waziri wa TAMISEMI amefanya ziara awasiliane na Waziri wa Afya hatua zichukuliwe mapema ili huduma ibadilike, lakini pia wananchi waone kuna mabadiliko baada ya maagizo ya viongozi wanaokuja. Mwisho niseme tu kwamba ninaomba sana Wizara ya Afya itembelee Hospitali ya Mji wa Mbulu ina matatizo nyinyi kama Wizara chukueni majukumu yaliyo yenu TAMISEMI kama Wizara itachukua majukumu yaliyo yao, ili kuona ni kwa namna gani walau Hospitali ya Mji wa Mbulu inakuwa sehemu ya kimbilio kwa huduma za afya kwa wakati wote katika hali ya kumhudumia mwananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala la Ambulance Mheshimiwa Waziri wa Afya Mheshimiwa Jafo alipokuwa Waziri nimeandika barua hakuna Ambulance iliyokwenda, nimeomba Ambulance hakuna Ambulance iliyokwenda, sasa hivi tena ni mwaka unakwisha. Jamani kama ni namna hii tungeelezwa lugha ya wazi tu kwamba Ambulance hizo hazipo, X-Ray hiyo haipo lakini pia tungeelezwa kama ambavyo dawa inakosekana. Mimi nilikuwa nashauri kwenye dawa tuna shida gani tusiweke alama kwenye dawa za Serikali kama tatizo ni wizi. Tuna ugumu gani wa kuweka alama ya Serikali kwenye dawa za Serikali ili upotevu wa dawa na wizi wa dawa…

SPIKA: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa. Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza niungane na wenzangu wote kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote niipongeze Serikali kuna kazi nyingi sana zimefanyika katika Jimbo la Mbulu Mjini, kazi kubwa ambayo ilikuwa imeshindikana kwa muda mrefu. Aidha nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu kabla ya wakati huu kulikuwa na miradi ambayo ilishindikana kwa muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue pia nafasi hii kuiopongeza Serikali kwa kazi kubwa iliyofanyika na naomba nichukue nafasi hii kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii. Kwanza Jimbo la Mbulu Mji Manyara kule lina sura mbili, kuna Vijiji na Mji. Eneo la vijiji ni Kata 10 eneo la Mji ni Kata Sita, katika hali kama hiyo kuna changamoto kubwa sana hasa kwenye upande wa watumishi. Wakati tunagawanyika mwaka 2015 Halmashauri ya Mbulu Mji ilipokea asilimia 40 ya watumishi, hadi tunapoongea sasa hivi hatujapata hata kujaza zile asilimia ambazo zilipungua kulingana na Mji kupokea asilimia 40 kwa 60. Kwa hiyo, tumeomba mara nyingi ajira za ujazaji ukiacha hizi ajira mpya.

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu ni mkubwa sana. Kwa mfano, kwenye eneo la Watumishi wa Kilimo wako Watatu badala ya 54. Katika hizo Kata za Vijijini kuna Vijiji 34. Katika Vijiji 34 vilivyoko watumishi hawa wa kilimo na mifugo walikuwa muhimu sana, kuna upungufu wa watumishi 54 wa kilimo na watumishi 52 wa mifugo, ukijumlisha ni watumishi 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilio changu ni kwamba nimeenda Wizara ya Utumishi mara nyingi, bahati mbaya

Mawaziri wamebadilika lakini ofisi ni ile ile. Nikitetea walau hizi nafasi za ujazaji zijazwe ili wananchi wangu wapate huduma bora kulingana na upungufu huu wa watumishi. Hizi ni kada mbili tu zina upungufu wa watumishi 100 sijaenda kwenye kada zingine. Mfano mwingine ni Vijiji na Mitaa tulizogawiwa 2014, kulikuwa na mahitaji ya Watendaji wa Vijiji na Mitaa zaidi ya 94 hadi sasa wamejaza nafasi za 30 tu na kila unapoenda unaahidiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu au hoja ya msingi zaidi ni kwamba hata yule aliyestaafu mshahara wake anapokea nani? Mheshimiwa Waziri kama alistaafu yuko kwenye mshahara na mshahara wake pengine ulikuwa unaweza kuajiri hata watumishi watatu, wanne, kwa maana ya yeye anaweza akawa anapokea zaidi ya Milioni Moja na watumishi wapya wanaoajiliwa kwa kada tofauti tofauti wanaweza kuajiliwa mpaka Watatu kwenye nafasi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu hapo ni kwamba hatuangalii data zetu kwa umakini na maeneo gani yanaathirika sana. Ukizungumza Maafisa hawa ambao ni ngazi za Kata na Vijiji wakakosekana moja kwa moja uwezo wa utendaji wa Serikali na utoaji wa huduma kwa Serikali unapungua kwa asilimia kubwa sana. Kwa hiyo, nilikuwa naona wakati fulani kibali hiki siyo hisani unapoona mtumishi wako amestaafu na kinaombwa mwezi wa Machi kila mwaka kwenye bajeti lakini hakuna kinachotokea. Ninaomba Mheshimiwa Waziri eneo kama hili linahitaji kibali cha ajira mbadala na kama Halmashauri ina Kata 17 ina Vijiji 34 ina Mitaa 58 wananchi wa eneo la Mbulu Mji, eneo la Mji ni ndogo. Eneo hilo la Mji lilichanganywa pamoja na eneo la vijiji, lengo kubwa lilikuwa kwamba kutokana na jiografia ilivyo, na kwa kuwa Halmashauri iligawanywa kwa lengo la kupeleka huduma karibu na wananchi, basi tusiwapeleke wananchi wale wa upande wa Vijijini waende Jimbo la Mbulu Vijijini ili wapokee huduma. Kwa hiyo naomba sana chonde chonde, nendeni kwenye data muangalie Halmashauri ya Mbulu Mji imeomba nafasi ngapi za ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo jingine naomba nichangie kwa upande huu wa wenzetu ambao wako katika eneo la TAKUKURU. TAKUKURU Wilaya ya Mbulu ina miaka zaidi ya 15 inapangisha jingo, TAKUKURU Wilaya ya Mbulu pia ina upungufu wa watumishi. Kwa hiyo kuna hoja nyingi za TAKUKURU katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu na Wilaya ya Mbulu hazifanyiwi kazi kwa wakati kulingana na wale watumishi walivyo wachache. Kama inawezekana hoja nyingi zinazokwama kwa ajili ya utekelezaji wa Maafisa, basi ngazi za Mkoa na ngazi zingine ziangalie namna ya kutatua tatizo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye ndege za Serikali. Duniani kote hakuna Serikali inaweza ikafanya biashara ika – perform au ikafanya ufanisi zaidi, ushauri wangu kwenye eneo hili la ndege za Serikali hasa za ATCL kwa maana zile zinazokodishwa kwenda ATCL basi Serikali ibinafsishe ili yenyewe ipewe gawio ama ipewe sehemu ya hisa, kwa sababu ni eneo ambalo limelalamikiwa sana na taarifa za CAG, kwamba zinaonesha zinaipa Serikali gharama kubwa na hakuna mafanikio zaidi. Kwa nini nazungumza hivi? Ninazungumza hivi kwa sababu ukiacha ndege za Viongozi wa Serikali hizi ndege zingine zote kwa kukodisha huwezi kupata mrejesho wa mafanikio ya mapato na ufanisi wa kiuchumi kwa maana ya uzalishaji. Kwa hiyo, eneo hili linahitaji zaidi sana lipate utaratibu wa kukodishwa ama wa kubinafsishwa kwa utaratibu wa wazi wa Serikali kusubiri gawio ama sehemu ya faida iliyotarajia kutoka mwanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni eneo la ajira. Vijana wengi wanatoka vijijini, wanakuja huku Makao Makuu ya Nchi kufanya usaili, kule wanakotoka wanakopa, wanapokuja huku wanapata gharama kubwa, ushauri wangu katika eneo hili Serikali iangalie utaratibu wa kuwezesha Sekretarieti ya Ajira kufanya usaili kikanda ili kupunguza gharama kubwa ambayo watoto wa wananchi na vijana wetu hawa wanapata gharama kubwa na kadri wananvyokuja huwa wanakosa kwa sababu nafasi tunazopata ni chache na hizo nafasi chache wanapokuja wengi baadae inageuka kuwa kilio. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wakati tulipitisha hapa Bungeni kikokotoo kwa Watumishi wa Umma. Wastaafu wamelalamikia sana eneo hili. Hata kama hatusikii, tuliona kuwa ni muhimu, Maazimio ya Bunge siyo Msahafu. Tutazame upya kilio cha wale wengi ambao ni Watumishi wa Umma, walishaitumikia nchi hii, na sasa wanalia kule. Hawa ni watumishi, waliitumikia nchi hii kwa uzalendo mkubwa sana, wanacholalamikia ni umri wa Mtanzania umeshuka. Kwa kuwa umri wa Mtanzania unashuka, na kikokotoo kile kinakuwa kidogo. Nadhani tuna jukumu kubwa la kutazama kama Bunge na kama Serikali, ili tuone hao watumishi na wastaafu wanachokizungumza katika ile hali ya uhalisia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na muda, naomba nizungumzie pia eneo lingine la TASAF.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali nzima ya Awamu ya Sita kwa jinsi walivyosimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020/2025. Kwa kweli kwa niaba ya wananchi wa jimbo langu la Mbulu Mjini napenda kuchukua nafasi hii kwa jinsi tulivyotatua changamoto nyingi zilizoshindikana kwa zaidi ya miaka 20 kwa kupatikana fedha za miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, mifano hiyo ni ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji la Endayaya Tlawi ambayo usanifu wake ulikamilika toka mwaka 2003 na sasa linajengwa kwa shilingi bilioni saba.

Pili, ujenzi wa barabara ya lami Karatu – Mbulu - Haydom ambayo ni ahadi ya Serikali ya Awamu ya Nne inayotekelezwa; tatu, ujenzi wa sekondari mpya katika Kata ambazo haziko, ujenzi wa vituo vya afya kikata; na nne, kupatikana kwa fedha za mfuko wa jimbo kwa ajili ya matengenezo ya barabara TARURA na fedha zingine nyingi.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia mpango huu wa mapendekezo ya Bajeti ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora; kwanza Serikali itazame upya mfumo wake wa kujaza nafasi wazi za watumishi wanaostaafu, kwa mfano halmashauri yangu ya Mbulu Mjini kuna watumishi wengi waliostaafu toka mwaka 2015; mpaka sasa hakuna kibali cha ajira mbadala iliyotolewa hali inayopelekea halmashauri kubakiwa na maafisa kilimo watatu badala ya 54 na maafisa mifugo, uvuvi na ushirika kubakiwa watano badala ya 52. Mbaya zaidi hivi karibuni kuna mtumishi wa ajira mpya aliyepangwa mpaka leo hajaripoti, kwa hiyo, halmashauri yetu ina upungufu mkubwa sana wa watumishi, Serikali ichukue hatua za haraka.

Mheshimiwa Spika, pili, Serikali iangalie upya utaratibu wa kuwaingiza walengwa wa TASAF hasa wale walioko kwenye maombi ya rufaa; tatu, Serikali iangalie uwezekano wa kuingiza somo la uzalendo kuanzia elimu ya msingi hali itakayowaandaa kizazi cha Watanzania kitakachokuwa na uzalendo mkubwa kwa nchi yao. Nasema hayo kwa sababu ukipitia taarifa nyingi za CAG ni wazi kuwa kizazi chetu kinazidi kupoteza maadili na uzalendo; nan ne, Serikali ijaze nafasi zinazokaimiwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na sekta zingine zijazwe au kuthibitisha wale wanaokaimu nafasi hizo haraka ili kuboresha utendaji na uwajibikaji kwa watumishi wetu.

Mheshimiwa Spika, tano, Serikali iangalie uwezekano wa muda mzuri wa Bunge kujadili taarifa ya CAG mara itakapokabidhiwa kwa Mheshimiwa Rais ili kuondoa hisia nyingi za wananchi kama ilivyo sasa kujadiliwa mwezi Novemba kila mwaka.

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake kwetu nyanja mbalimbali za ustawi wa kijamii, kiuchumi, kisiasa kidiplomasia na kutuepusha na majanga mengine mengi. Pia tunampongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa mambo mengi sana katika kuiongoza nchi yetu na utekelezaji wa Ilani ya CCM 2025, kwa kweli sisi kama Wabunge wa CCM tuna mengi ya kujivunia kupitia Rais wetu, tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu amjalie ulinzi, baraka na mafanikio katika utume wake kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Sekretarieti ya Ajira nchini ndiyo chombo pekee cha kufanya usaili wa ajira nchini ambapo nchi ina wahitimu wengi sana wanaotuma maombi ya nafasi ya ajira pindi tangazo litakapotolewa, Serikali iangalie uwezekano wa kuijengea uwezo wa fedha, magari na vitendea kazi mbalimbali ili usaili wa nafasi za kazi ufanyike kikanda hapa nchini kwa kuwa wanaofanikiwa ni wachache.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niongeze sehemu ya mchango wangu kupitia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Mbulu ni Wilaya kongwe hapa nchini, kwa sasa inakabiliwa na upungufu mkubwa wa miundombinu ya huduma hususan majengo ya taasisi mbalimbali, kwa hiyo toka mwaka 2005 serikali ilifungua ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mbulu, toka muda huo mpaka leo taasisi hiyo haina jengo la ofisi kwani walipangisha nyumba ya mtu binafsi ambayo ni ndogo sana na iliyojengwa kwa ramani ya makazi. Hivyo ninaiomba sana Serikali itujengee ofisi ya taasisi hiyo muhimu kwa maendeleo na ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie upya utaratibu wa kuongeza malipo ya pensheni ya kila mwezi kwa watumishi wastaafu wa miaka ya nyuma kwa kuwa kiasi kinacholipwa kidogo sana ambayo haiwezi kumpatia hata bima kubwa, sote tunafahamu kundi hili linakabiliwa na maradhi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia moa moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, naungana na Watanzania wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali za ustawi wa amani, kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiplomasia na mambo mengi katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini nachukua nafasi ya kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi/watendaji wetu wote Serikalini kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2025, kwa kweli kazi nyingi zimefanyika katika jimbo langu la Mbulu Mjini kwa kila sekta, hasa yale mambo mengi ambayo yaliyoshindikana muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii ya uwekezaji, viwanda na biashara. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na watendaji wake wote Wizarani na wadau wengine.

Mheshimiwa Spika, mimi mchango wangu ni kwamba tuangalie utaratibu wa kuhakikisha maafisa wetu wa biashara ngazi za halmashauri, mikoa tuwajengee uwezo wa kuwalea na kuwajengea uwezo wawekezaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, nasema hayo kwa sababu TAMISEMI ilipoagiza kila halmashauri nchini kuwa na viwanda 100 vingi viliyoanzishwa vilitoa ajira kwa vijana wengi, lakini hadi sasa ni vichache vinavyoendelea kufanya kazi na changamoto kubwa ni ukosefu wa wataalam washauri, mitaji ya kutosha na mazingira ya ukosefu walezi. Hivyo kuna haja kubwa kulinda na kuimarisha viwanda vidogo na vya kati kwa kuwa kundi kubwa la wananchi wataajirika kwa ajira ya muda na mikataba na wawekezaji wa viwanda vidogo watakuja kuwa wawekezaji wa ndani ambao mapato yao yataendeleza uchumi wa Taifa letu na mafanikio ya wawekezaji hawa wadogo watajenga miundombinu hapa hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, naunga hoja mkono kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali za ustawi wa kijamii, kiplomasia, kisiasa, amani na utulivu katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana na viongozi wenzangu wote kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali nzima ya Awamu ya Sita kwa jinsi ilivyotekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Kamati yetu na watendaji wake wote kwenye Wizara hii kwa ujumla. Kwa kweli mambo mengi yaliyoshindikana muda mrefu yamefanyika sana katika jimbo langu, kwa mfano mradi wa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Tlawi Endayaya katika Halmashauri ya Mbulu Mjini ulifanyiwa usanifu toka mwaka 2003 lakini tunashukuru Serikali sasa unajengwa kwa shilingi bilioni saba.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa daraja la Gunyoda ulikuwa kilio cha wananchi wa halmashauri ya Mbulu Mjini, Karatu na Mbulu Vijijini mwaka 1998 lakini sasa imejengwa kwa shilingi bilioni 1.4.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya lami kutoka Karatu, Mbulu Mji, Haydom, Sibiti mpaka Lalago mradi huu unaounganisha majimbo matano ya Karatu, Mbulu Mjini, Mbulu Vijijini, Mkalama na Meatu unajengwa na Kampuni ya Kichina sasa.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli kila sekta kazi kubwa sana imefanyika kwa lengo la kutatua kero za wananchi na maombi ya muda mrefu, hakika tuliadi wakati wa uchaguzi kupitia ilani yetu ya CCM na tumetekeleza.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi, Serikali iangalie utaratibu wa kuongeza bajeti ya Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi kama zinavyoombwa ili tuweze kuona tija ya uzalishaji katika Wizara hii muhimu sana kwani takwimu ya mifugo tulionao ni wengi sana, lakini tija ya kiuchumi ni ndogo sana.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie mpango kabambe wa mafunzo na mikopo kwa ajili ya vikundi vya wafugaji na wasindikaji wa mazao ya mifugo na uvuvi kwa lengo la kuleta mageuzi makubwa ili kuleta tija kubwa zaidi kiuchumi kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie wawekezaji wadogo watakaoanzisha ranchi ndogo ndogo na mabwawa ya kufugia samaki katika ngazi za tarafa na kata, hali hii itawabadilisha wafugaji wengi kuona umuhimu wa kufuga mifugo wachache wenye tija badala ya kuthamini idadi kubwa.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie matumizi sahihi na muhimu kwenye vituo vya mafunzo na zana za kilimo zilizojengwa toka mwaka 2013 kwa kuwapeleka wataalam na kuanzisha kalenda ya mipango kazi zao kulingana na maoni ya wafugaji na wavuvi. Wizara iangalie usimamizi na uendeshaji wa majosho ya mifugo na maeneo ya minada ya mifugo uwe chini ya Maafisa Ugani wa Mifugo badala ya kuziachia Serikali za Vijiji na Mitaa kwani tunazidi kusababisha uharibifu na kupoteza ukubwa wa maeneo.

Mheshimiwa Spika, mwisho naomba Wizara itoe fedha za ujenzi wa majosho kumi katika Halmashauri ya Mbulu Mjini kwenye Kata za Tlawi, Gunyoda, Gehandu, Bargish na Marang ambayo niliomba kwenye barua yangu kwa Katibu Mkuu mwezi Februari, 2023 kupitia maelekezo ya Mheshimiwa Abdallah Ulega, Waziri wa Mifugo kwangu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, niungane na Watanzania wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali sisi Watanzania wote na Taifa letu kwa ujumla, sisi kama Taifa hatuna cha kumlipa muumba wetu zaidi ya maombi na sala kila wakati.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana na wananchi wa Jimbo langu la Mbulu Mjini kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali nzima ya Awamu ya Sita kwa jinsi tunavyotekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa kila sekta, tuendelee kuiombea Serikali yetu amani, upendo, mafanikio na mshikamano kwa Mwenyezi Mungu wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa moyo wangu wa dhati nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa Waziri wetu wa Ujenzi, Naibu Mawaziri wote wawili, Mheshimiwa Balozi Asha – Katibu Mkuu Ujenzi, Mheshimiwa Joseph Migire, Katibu Mkuu - Uchukuzi, Naibu Makatibu Wakuu wote, Wakurugenzi wote wa Wizara, Ndugu Rogatus Mativila - Mtendaji Mkuu wa TANROADS na timu yake ya watendaji wote makao makuu na Meneja wa Mkoa wa Manyara kwa jinsi wanavyotekeleza majukumu yao na kutusikiliza changamoto zilizoko kwenye majimbo yetu na kuzitatua kwa kadri ilivyowezekana.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii muhimu sana kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambayo imewasilishwa katika Bunge letu na taarifa ya Kamati yetu ya kudumu ya miundombinu.

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu kupitia Wizara ya Fedha ijitahidi kutoa fedha za malipo ya wakandarasa wanaojenga miradi ya barabara na miundombinu mbalimbali ya ujenzi kwa wakati ili kuepuka gharama za malipo zinazoongezeka nje ya mikataba na wananchi kupokea huduma iliyotarajiwa kwa mujibu wa mikataba.

Pia Serikali iangalie utaratibu wa kuongeza bajeti ya dharura kwa Wakala wa Barabara TANROADS kwa ajili ya madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi hali inayofanya barabara nyingi kujifunga na kuleta adha kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, Serikali itusaidie mpango kabambe wa kujenga kilometa tano za zege katika barabara ya Mbuyu wa Mjerumani – Magara - Mbulu sehemu ya Mlima Magara kwa kuwa mpango wa zege katika eneo la Mlima Magara imekuwa ahadi ya viongozi wetu wakuu kutoka Serikali ya Awamu ya Nne, Tano na Sita. Hivyo basi eneo hilo ni hatarishi sana na matengenezo yake yamekuwa na gharama kubwa yasiyo na tija.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru sana Serikali yetu kwa mpango wa ujenzi barabara ya Karatu, Mbulu, Haydom, Maswa, Sibiti. Tunaiomba Serikali mkataba wake usainiwe haraka kwa kuwa ni kiu ya wananchi wa majimbo yote sita katika mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Simiyu mpaka Shinyanga. Mradi huu utagusa sana hisia ya wananchi walio wengi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, naungana na Watanzania wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali za ustawi wa kijamii, amani, upendo, mshikamano wakati wote tangu kuanzishwa kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, naungana na wananchi wote wa jimbo langu la Mbulu Mjini kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi na watendaji wote Serikalini kwa jinsi walivyotatua changamoto mbalimbali na utekelezaji wa Ilani ya CCM 2022-2025, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie mafanikio na baraka.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika kwa jinsi unavyoliongoza Bunge letu toka ulivyopokea majukumu yako, nawe Mwenyezi Mungu akujalie baraka na mafanikio pamoja na wananchi wa jimbo la Mbeya Mjini.

Mheshimiwa Spika, kwa moyo wa dhati nampongeza Mheshimiwa Jumaa Aweso – Waziri wetu; Mheshimiwa Maryprisca Mahundi - Naibu Waziri; Katibu Mkuu Engineer Nadhifa Kemikimba; Naibu Katibu Mkuu na watendaji wetu wote wa Wizara kwa ngazi zote. Kwa kweli jitihada zinaonekana japo kuna changamoto.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu; kwanza, Serikali iongeze jitihada za kutafuta fedha za kujenga miundombinu ya visima vyote vilivyotayari kuchimbwa katika maeneo mbalimbali kwani tayari tumemaliza uchimbaji wa visima saba katika jimbo langu la Mbulu Mjini yapata mwaka sasa, lakini hatujaweza kujenga matanki na kuweka mtandao wa mabomba kwenye vijiji, hali hii inawafanya wananchi kusubiri huduma ya maji kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, Serikali itazame upya suala la mchakato wa uteuzi wa bodi mpya ya maji kwenye mamlaka za maji za RUWASA Wilaya na Miji kwani maeneo mengi bodi humaliza muda wake, lakini ngazi hizo hazichukui hatua za mchakato wa uteuzi wa bodi mpya haraka.

Mheshimiwa Spika, Serikali iwe na ratiba ya ukaguzi wa tathimini ya kiufanisi wa utendaji, mapato na matumizi pamoja kuangalia mwongozo wa uendeshaji wa mamlaka za maji kama unakidhi haja na kutoa fursa ya maoni kama upande wa wapokea huduma wanaridhika.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie suala la upotevu wa maji kwenye mitandao ya mabomba kwa kulinganisha uzalishaji wa maji kutoka vyanzo mpaka ankara za malipo kwa watumiaji, kwenye suala la madeni mpango wa kuunganisha mfumo wa kulipa bill ya maji kwa kununua kwanza ili kufanikisha upunguzaji wa madeni.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maeneo mengi ya mji yanapokea wimbi kubwa la wananchi wengi wanahamia, Serikali iangalie upatikanaji wa vyanzo vikubwa vya maji badala ya kuchimba visima vingi kwenye eneo moja ilhali upatikanaji wa maji hauendani na wingi wa watu.

Mheshimiwa Spika, Serikali ijitahidi kutoa fedha zote zinazoombwa kwenye bajeti ya Wizara hii kwani kuna maeneo mengi miradi mingi imekwama kwa ajili ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Serikali itafute fedha za ujenzi wa majengo ya Ofisi za Mamlaka ya Maji RUWASA kwa ngazi ya Wilaya na mijini ili kupunguza gharama za uendeshaji isiyolingana na mapato halisi ya mamlaka mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali za ustawi wa kijamii, kiuchumi, kisiasa, kidiplomasia pamoja na mambo mengi sana katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuungana na wananchi wa jimbo langu la Mbulu Mjini kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali nzima ya Awamu ya Sita kwa jinsi anavyoliongoza Taifa letu na kutupatia fedha nyingi sana za miradi ya maendeleo kwani miradi inayotekelezwa hivi sasa ni mikubwa sana ambayo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Spika wetu, wewe mwenyewe Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge letu kwa jinsi mnavyoliongoza Bunge hili toka tulivyoanza, hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee nampongeza Mheshimiwa Nape Nnauye – Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Engineer Mathew Kundo - Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na watendaji wa Wizara na taasisi zilizoko chini ya Wizara hii muhimu kuendana na utendaji wao wa kila siku, hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kuishauri Serikali kupitia mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii muhimu sana kupitia hotuba ya Waziri na maoni na mapendekezo ya Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali iangalie utaratibu wa kuboresha minara yetu ya TTCL kwani tuna minara mingi ya TTCL ina uwezo wa chini kupokea usikivu wa mawasiliano hali ambayo inawafanya wananchi wengi kutokutumia mitandao yetu ya TTCL kuliko mitandao mingine ya simu. Hivyo basi ushauri wangu timu ya wataalam wetu wa Wizara wafanye tathimini ya minara yote ya TTCL kwa lengo la kufanya maboresho ya usikivu na kuleta ushindani na minara ya mitandao mingine kwa ajili ya kujibu kiu ya watumiaji wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kuwezesha masomo ya TEHAMA katika shule zetu za sekondari nchini hasa zile za A-level tunaiomba Wizara hii kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuzipatia shule hizi computers ili kuwezesha wanafunzi wetu wa shule za sekondari za kata waweze kijifunza TEHAMA na kushindana na wanafunzi wenzao wa shule binafsi na kuwajengea uwezo wa kufahamu kikamilifu matumizi ya TEHAMA kabla ya kuhitimu masomo ya sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali yetu idhibiti sms za utapeli zinaotumwa kupitia line za simu zetu za TTCL na matapeli kuomba hela kwa wananchi kwa kuwa hapo awali line za simu mitandao mingine zilikuwa zinatumika, ni dhahiri kuwa walifanya maboresho katika kukomesha tatizo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, naungana na Watanzania wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja za ustawi wa kijamii, kiplomasia, amani na utulivu na kutuepusha na majanga mbalimbali katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana viongozi wenzangu wote, wananchi wote wa Jimbo la Mbulu Mjini na wote wenye mapenzi, kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali nzima kwa jinsi tulivyotekeleza Ilani ya CCM yam waka 2020-2025, kwa kweli kwa miaka miwili sasa yapo mambo mengi sana yaliyoshindikana huko nyuma na sasa tayari yamefanyika.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Profesa Adolf Mkenda, Waziri na Naibu Waziri, Kamati yetu, Katibu Mkuu na watendaji wetu wote katika Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuishukururu sana Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kutupatia fedha za ujenzi wa mabweni mawili mwaka 2017 na 2018 katika Jimbo la Mbulu Mjini hivyo basi tunawaomba watusaidie ujenzi wa mabweni mawili katika Shule yetu ya Sekondari ya Kata ya Daudi (Marangw) kwa kuwa ni shule kongwe iliyoko maeneo ya wafugaji.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii muhimu sana ya elimu kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, Serikali itazame upya muundo wa ngazi za Wadhibiti Ubora wa Elimu kwani kwa sasa shule za sekondari nchini zimekuwa nyingi sana, hivyo basi kuwe na Wadhibiti Ubora wa Elimu ya Sekondari wawepo kwa ngazi ya kanda, mkoa na halmashauri kote nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie vigezo vya usajili wa vituo vya malezi ya watoto wadogo na elimu ya awali nchini hususan walimu wanaoajiriwa wengi wao hawana taaluma ya kutosha kwa ustawi wa Taifa unaanzia malezi na makuzi ya mtoto hivyo eneo hili ni muhimu liangaliwe vizuri.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie utaratibu wa kila halmashauri nchini kuwa na shule moja yenye kitengo cha elimu maalum kwani kuna kundi kubwa la watoto wenye mahitaji maalum ambao mazingira yao hayana huduma hiyo muhimu sana, kwa mfano Shule ya Msingi Endagikort katika Halmashauri ya Mbulu Mji ina wanafunzi zaidi ya 30 kwa miaka sita sasa hali inayofanya wanafunzi hao kusoma kwenye mazingira magumu sana, hakuna miundombinu ya madarasa, mabweni, vifaa vya kufundishia na walimu wa elimu maalum, ajira kutoka Serikalini.

Kwa hiyo, ninaomba Waziri wa Elimu afanye ziara mahususi katika Jimbo la Mbulu Mjini, kutembelea Shule ya Msingi Endagikort, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Tango FDC na Chuo cha Ukunga na Uuguzi Mbulu kwani maeneo hayo yana changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie utaratibu mzuri wa matumizi ya vituo vya walimu (TRC) kwenye tarafa zetu nchini kwa kujikita kwenye misingi yake ya kuanzishwa kwani kwa sasa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu na hayafanyiki na baadhi ya vituo havitumiki, hata hivyo uamuzi wa walimu waratibu kupangiwa vipindi vya kufundisha kwenye shule zilizoko karibu utasaidia sana kuongeza vipindi vya masomo kwa wanafunzi.

Mheshimiwa Spika, mwisho, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake kwetu sote na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, ninaipongeza sana Serikali yetu chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na viongozi wetu wakuu na watendaji wote Serikalini. Kwa namna ya pekee nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Stergomena Tax, Waziri wetu wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, pamoja na wakuu wote wa vyombo vya ulinzi kwa kuendelea kuitunza na kuilinda heshima ya kulinda mipaka ya Taifa katika nyanja za kitafa, kikanda na kimataifa. Rai yetu kwa vyombo vyetu waendelee kudumisha utii, uzalendo, ukakamavu, weledi na utaifa kwanza. Kwa kweli wanatuheshimisha mbele ya mataifa, hongereni sana Mwenyezi Mungu awabariki.

Mheshimiwa Spika, aidha niungane na Watanzania wote kukupongeza sana wewe Spika wetu na waheshimiwa Wabunge, viongozi wote waliochaguliwa na walioteuliwa kwenye nafasi zao mbalimbali tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu aweze kuwajalia kufanikisha majukumu yenu.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nitoe mchango wangu kupitia hotuba ya Wizara hii muhimu sana kwa mustakabali wa Taifa letu; kwanza kutokana na umuhimu wa ujenzi wa Makao Makuu ya JWTZ Kikombo, Dodoma, tunaiomba sana Serikali itoe fedha za kukamilisha ujenzi huo. Hata hivyo tunaipongeza sana Serikali kwa kutumia mfumo wa force account kwani kutokana mfumo huu umeisaidia sana Serikali kuokoa gharama kubwa za fedha katika ujenzi huo.

Mheshimiwa Spika, tunaishauri Serikali iangalie vyombo vyetu vingine vya ulinzi ili wawezeshwe kupata fedha za kutumia kujenga miradi ya maendeleo na miundombinu mingine kama vile magereza, vituo vya polisi, ofisi za mikoa na wilaya.

Pili, Serikali iangalie mpango wa kuwezesha upatikanaji wa fedha za kutosha, vitendea kazi, wataalam, kwenye mashirika ya NYUMBU, MZINGA na SUMA JKT ili mashirika hayo ambayo yana dira ya uzalishaji mali yaweze kutanua matawi ili kuongeza wigo wa ajira kwa vijana wote wanaomaliza mafunzo ya JKT na kuzalisha bidhaa ambayo zitakidhi haja kwenye masoko ya ndani ya nchi na nje.

Tatu, kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu katika mji wa Ddodoma hali itakayochochea mahitaji makubwa sana ya huduma za jamii hususan sekta ya afya, tunaiomba sana Serikali yetu ijitahidi sana kutoa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Jeshi hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, nne, kutokana na mabadiliko ya teknolojia kubwa sana duniani, tunaiomba sana Serikali iongeze bajeti ya Wizara hii katika nyanja za vifaa vya ulinzi na mafunzo ya muda mfupi, muda wa kati na mrefu ili kuongeza medani za kisasa zaidi katika ulinzi wa mipaka yetu na Taifa letu kikanda, kitaifa na kimataifa.

Mheshimiwa Spika, mwisho siyo kwa umuhimu naendelea kuvipongeza sana vyombo vyetu vya ulinzi katika utendaji wao.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali za ustawi kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana na wananchi wa Jimbo langu la Mbulu Mjini kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali nzima ya Awamu ya Sita kwa jinsi wanavyoliongoza Taifa letu na kutatua changamoto nyingi sana zinazowakabili wananchi hususan utekelezaji wa Ilani ya CCM yam waka 2020 - 2025 kwa kila sekta. Hivyo basi tuendelee kuliombea Taifa letu kwenye nguzo kuu ya amani, upendo, uchumi, baraka, utulivu, diplomasia ya kisiasa, na mshikamano kwa Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Spika, naomba nikupongeze wewe, Naibu Spika na Wenyeviti wetu wote kwa kuliongoza Bunge letu katika kuzigatia Kanuni za Bunge kikamilifu na kwa busara ya hali ya juu hongereni sana.

Mheshimiwa Spika, aidha, sisi Wabunge wako tunaungana wote kukuombea mafanikio mema katika nafasi unayogombea, Mwenyezi Mungu awe kiongozi katika kufungua mapito yako upate kuchaguliwa kwa maslahi makubwa ya Taifa letu.

Aidha, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa January Makamba, Waziri wa Nishati Naibu Waziri na watendaji wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia mapendekezo na maoni ya Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge na kupitia maoni ya Mheshimiwa Dunstan Kitandula, Mwenyekiti wa Kamati yetu na hotuba ya Mheshimiwa January Makamba Waziri wetu wa Nishati.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kuelezea hali halisi ya jiografia ya Jimbo la Mbulu Mjini; eneo la Mbulu Mjini tuna kata 17 kati ya hizo kata 11 ni maeneo ya vijiji na kata sita ni eneo la mitaa 58 ya miji. Hapa naomba kutoa maelezo ya hali ya uunganishaji wa umeme katika vijiji, mitaa na vitongoji. Ninaishukuru sana Serikali, tayari tumeweza kuunganisha laini kubwa kwenye makao makuu ya kila kata, kwa upande wa vijiji bado hatujaweza kuwasha umeme kwenye vijiji 11 hali inayowafanya wananchi kutopata huduma hii muhimu ya kuwaunganishia umeme. Mbaya zaidi katika maeneo mengi ya mitaa ya mji pembezoni kuna wateja wengi sana waliofanya kuunganisha waya kwenye majengo yao kwa lengo la kulipia shilingi 27,000 lakini wameshindwa kwa kuwa hawana uwezo huo wa kulipia gharama ya shilingi 320,000. Kwa hiyo, Serikali iangalie namna ya kuwaunganishia huduma ya umeme.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali; Serikali yetu iangalie kwa kina suala la kuunganisha umeme kwa shilingi 27,000 katika maeneo ya mitaa ya miji yenye sura ya vijiji ili kuwezesha wananchi hao wenye uhitaji mkubwa kupata huduma hiyo muhimu. Serikali iangalie upelekaji wa umeme kwenye vitongoji kwa kuangalia vipaumbele maeneo ya taasisi za Serikali, binafsi, migodi ya madini na makazi mengi ya wananchi ili kutumia fedha kidogo kunufaisha watumiaji wengi zaidi. Kwa kuwa maeneo ya vijijini majengo mengi yako mbali mbali Serikali iangalie kutafuta kile chombo cha Umeme Tayari (UMETA) ili kuwapatia wananchi hao ambao hatutaweza kuwaunganishia kwa muda wa miaka mitano ijayo kutokana na umbali kati ya makazi na makazi mengine.

Aidha, Serikali ijitahidi sana kutoa fedha za bajeti ya Wizara hii kama ilivyoomba kwenye bajeti hii ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vyote vilivyoainishwa kwenye mapendekezo ya Wizara na maoni ya Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ili kujibu kiu ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, katika muhtasari wa utambulisho wako wa wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara hii kuna nafasi nyingi za watendaji wakuu zinazokaimiwa, hivyo basi tunaiomba Serikali nafasi hizo zijazwe na watendaji wenye sifa stahiki ili kuleta ufanisi wenye tija kwa manufaa mapana ya Taifa letu.

Mwisho, naomba nitoe shukrani zangu kwa Mheshimiwa Waziri na watendaji wakuu wa Wizara yake kwa kutupatia mitungi 100 ya gesi ambayo itafanikisha kampeni ya kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na kupunguza athari ya mabadiliko ya tabianchi, hongera Mheshimiwa Waziri ubarikiwe.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuungana na viongozi wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake. Aidha, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wote na watendaji wote Serikalini kwa jinsi walivyosimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM yam waka 2020 – 2025; hongereni sana na Mwenyezi Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii muhimu sana kwa mustakabali wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunaiomba sana Serikali iiongezee bajeti ya Wizara hii kwani kuna mahitaji makubwa sana ya rasilimali watu, miundombinu, vitendea kazi na mahitaji makubwa ya kukabiliana na majanga ya ukame, magonjwa na upungufu wa maeneo ya malisho.

Pili, kwa kuwa sekta hii ya mifugo imekuwa na mchago mkubwa katika pato la Taifa na wafugaji wanakabiliwa sana na maeneo ya malisho ni wakati muafaka kwa Taifa letu kusimamia mkakati wa kubadilisha koo za mifugo kwani hatua hii itawafanya wafugaji kuwa na mifugo wachache na watakaohimilika kutunzwa, kuhudumiwa na kuongeza mapato kwa mfugaji na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kuondoa upungufu wa Maafisa Ugani Serikali iangalie utaratibu wa kuwaajiri na kuwapanga kulingana na wingi wa mafugo na kuwapangia majukumu ya kila siku kwenye vituo vya mafunzo kila kata na kijiji badala ya wao kutafutwa na wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo wengi wao hupenda kupangwa kwenye Makao Makuu ya Halmashauri hata kama wako wachache badala ya tarafa, kata na kijiji, hali inayowafanya mchango wao wa kitaalamu kutokuonesha matokeo makuu kwa Serikali na wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa minada yetu tunaishauri Serikali iweke mizani ya kupima mifugo kwani hakuna uhalisia wa pande zote mbili (muuzaji na mnunuzi) hivyo basi hapo ni lazima matumizi ya vipimo vitumike kuleta uhalisia kwa kuanza na minada mikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa sekta ya uvuvi Serikali itoe waraka wa maelekezo ya usimamizi kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa kuwatumia Maafisa Maliasili wa ngazi hizo katika kuzuia uvuvi haramu kwenye mabwawa na maziwa madogo kwani hakuna Maafisa Uvuvi wa kutosha na athari ni nyingi sana kutokana na uvuvi unaoendelea huko kwenye maziwa hayo kwa mfano Ziwa Tlawi Mbulu na Ziwa Babati na Basutu Hanang.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali za ustawi wa kijamii, kiuchumi, kiplomasia, kisiasa na mshikamano wa Taifa letu wakati wote.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuungana na wananchi wa jimbo langu la Mbulu Mjini kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Serikali nzima ya Awamu ya Sita kwa jinsi wanavyoliongoza Taifa letu na kutatua changamoto nyingi sana zinazowakabili wananchi hususan utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2025 kwa kila sekta, Mwenyezi awabariki sana.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mohamed Mchegerwa, Waziri wa Wizara hii, Naibu Waziri Mheshimiwa Mary Masanja na watendaji wakuu wote wa taasisi zilizo chini ya Wizara hii kwa jinsi wanavyotumikia nafasi zao.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson - Spika wetu, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge, Wajumbe wa Kamati hii, Katibu wa Bunge na watendaji wote wa Bunge kutokana na mipango yao mizuri ya kufanikisha maandalizi ya taarifa hii.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mchango wangu kwa kupitia hotuba ya mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii muhimu sana ya Maliasili na maoni ya Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge letu.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie uwezekano wa kuchimba mabwawa ya maji katika hifadhi zetu au kujenga mabwawa kwenye mito ndani ya hifadhi zetu, kwa sababu dunia inakabiliwa na mabadiliko ya tibianchi na ukame mkubwa hivyo basi tatizo la ukosefu wa upatikanaji wa maji katika hifadhi zetu siyo suala litakalopungua kwa haraka bali litazidi kuongezeka sana.

Mheshimiwa Spika, Serikali iajiri Maafisa Wanyamapori katika Halmashauri zote nchini ambazo zinapakana na Hifadhi za Taifa. Kwa kuwa kumeongezeka tatizo la wanyama wakali na waharibifu kutoka ndani ya hifadhi zetu na kwenda kwenye maeneo ya makazi ya watu na kupoteza maisha na kuharibu mali za wananchi, hali hii imekuwepo katika Halmashauri ya Mbulu Mji, ninaomba tupatiwe mtumishi huyu muhimu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kutowepo kwa mahusiano mazuri kati ya wananchi na askari wa hifadhi zetu hali inayosababisha athari nyingi ikiwemo vifo na kupoteza mali, naiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwepo kwa ratiba ya vikao vya ujirani mwema kila robo mwaka kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi zetu nchini kwa kuunganishwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na sisi Wabunge tushiriki kwa maslahi mapana ya Taifa letu kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie upya uhalisia wa sheria za fidia na kifuta machozi kwa wananchi wanaoathiriwa na wanyama wakali na waharibifu wa mazao yaliyoko mashambani na kwenye maghala yao hali ambayo imesababisha umaskini mkubwa kwa jamii.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara hii iangalie uwezekano wa kuwepo kwa kitengo cha kuratibu, kubaini na kutangaza vivutio kwenye tovuti za halmashauri ili kukuza na kuchochea utalii wa ndani na nje ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pia Wizara iangalie utaratibu mzuri wa kutoa michango ya miradi ya maendeleo kwa jamii katika huduma za sekta kwenye maeneo hayo ya hifadhi ambayo yanapakana na wananchi wetu ili kuongeza mahusiano na hamasa ya kuthamini uendelevu wa hifadhi za taifa letu.

Mheshimiwa Spika, naomba kukumbushia umuhimu mkubwa sana wa ziara ya Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri katika jimbo langu la Mbulu Mjini kwenye Kata za Gehandu, Bargish, Daudi na Marangw ambazo zinapakana na hifadhi ya Ziwa Manyara na Hifadhi ya Msitu wa Marang kwa ajili ya kufanya mikutano ya hadhara ya ujirani mwema na ufafanuzi wa sheria za hifadhi na kuhamasisha jamii kuwa sehemu ya walinzi na wahifadhi wa rasilimali hiyo muhimu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, naungana na Watanzania wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa baraka kwa kuijalia nchi yetu amani, utulivu, mshikamano, ustawi wa jamii na kutuepusha na majanga mbalimbali yanayotokea mara kwa kote duniani.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kwa niaba ya wananchi wote wa Jimbo la Mbulu Mjini kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan - Rais wetu mpendwa kwa jinsi anavyoiongoza nchi yetu na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020 – 2025.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waziri wa Wizara hii, Naibu Waziri wa Wizara, Mheshimiwa Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa jinsi mnavyoitendea haki Wizara hii kwanza kwa kutusikiliza sisi wawakilishi wa wananchi na kutatua changamoto mbalimbali tunazowasilisha kwenu, hongereni sana na Mungu awabariki.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naungana na viongozi wenzangu kutoa pole nyingi kwa familia zilizopata misiba mbalimbali ya kuwapoteza wapendwa wao kuanzia kwa viongozi wote, watendaji na Watanzania wote Mwenyezi Mungu atujalie hali ya ustahimilivu katika kipindi hiki, sote kwa pamoja tunaziombea roho zao kwenye ufalme wa mbinguni usio na mwisho.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia mapendekezo ya hotuba ya Wizara hii na taarifa ya Kamati yetu ya Bunge; kwanza tunaipongeza Serikali yetu kwa kutoa fedha za ndani kwa ajili mipango ya maendeleo. Hata hivyo kwa kuwa Wizara hii mpya tunaiomba sana Serikali iongeze bajeti ya Wizara hii kwa kuwa ina mahitaji makubwa ya miundombinu, watumishi na vitendea kazi mbalimbali na kuendelea kutumia utashi wa kushawishi kupata fedha za nje kwa wadau.

Pili, kwa kuwa Wizara imeundwa kuna umuhimu mkubwa sana kufanya mapitio ya sheria zilizoko na mpya ili kusimamia na kuwezesha utendaji wa Wizara yetu kukabiliana na masuala mbalimbali kama vile wingi wa watoto wa mitaani na ndoa zinazotelekezwa na haki za mirathi na wajane.

Mheshimiwa Spika, tatu, Serikali iwaelekeze asasi za kiraia wapitishe mipango kazi yao kwenye vikao vya Mabaraza ya Madiwani, DCC na RCC kwa ajili ya kupata vipaumbele na kufanikisha mahitaji muhimu na mtambuka katika maeneo hayo.

Aidha, Wizara iandae mafunzo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kwa ngazi za Kata na Wilaya katika ratiba zake kila mwaka. Pia Serikali iangalie uanzishwaji wa Mabaraza ya Wazee kwa ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Vijiji kurahisisha uratibu wa matatizo na changamoto mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, naunga hoja mkono asilimoa mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuungana na Watanzania wenzangu kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia baraka zake katika nyanja mbalimbali za ustawi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuungana na wananchi wa Jimbo langu la Mbulu Mjini kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi anavyoliongoza Taifa letu na Serikali yetu nzima ya Awamu ya Sita kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 & 2025 kwa kila sekta, Mwenyezi Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Pindi Chana - Waziri, Naibu Waziri na watendaji wakuu wa Wizara hii kwani kuna mafanikio makubwa sana katika Wizara hii muhimu kwa ajili ya kuibua vipaji vya Watanzania na kuchochea fursa ya ajira kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuungana na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wenzangu wote kuipongeza sana timu yetu ya Yanga kwa kweli wametuheshimisha mbele ya kimataifa hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kutoa mchango wangu kupitia hotuba ya mapendekezo ya bajeti ya Wizara hii muhimu ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, na maoni ya Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge, Serikali iangalie utaratibu wa kuweka kalenda ya mashindano mbalimbali za vipaji kupitia makundi kwenye ngazi za wilaya. Hata hivyo kuna vijana wengi walioko katika ngazi za shule zetu za sekondari na msingi nchini ambao wanakabiliwa na chagamoto mbalimbali katika kufikia ndoto zao mara nyingi. Kwa hiyo, kuna haja kubwa ya kuimarisha Kamati za Michezo ngazi za Wilaya na Mikoa ili kuelekeza mpango kazi zao kila mwaka na kushirikisha washiriki wa vipajj ngazi za chini ili kufanikisha mpango wa Taifa wa kuwa na washiriki wenye uwezo mkubwa kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iangalie uwezekano wa kila halmashauri nchini kuwa na walimu wa fani ya michezo ili kuendeleza vipaji kwa vijana wetu shuleni. Aidha, Serikali ielekeze halmashauri kama mdau wa sekta hii kutenga fedha za utamaduni, sanaa na michezo kupitia mapato yake ya ndani katika bajeti ya mwaka wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna umuhimu mkubwa sana katika Taifa letu wa kulinda, kuendeleza, kutunza na kustawisha lugha ya Kiswahili kuwa rasilimali tulizonazo kitaifa na kutumia kukipigania ukuaji wake Kimataifa na hapa tuna kila sababu ya kumkumbuka, kumuenzi na kumwombea Hayati Mheshimiwa Julius Kambarage Nyerere Baba wa Taifa letu kwa kutuunganisha sisi Watanzania kutumia lugha moja Kitaifa na kuwa nchi ya mfano Barani Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwe na data bank ya maeneo ya michezo nchini kuanzia ngazi za vijiji, wilaya, mikoa, na kuzipima na kuendeleza maeneo hayo. Nayasema hayo kwa sababu maeneo mengi yamevamiwa na kutumika kinyume na matarajio ya awali hali itakayohatarisha maendeleo ya sekta ya michezo nchini kutoweka na athari kwa kizazi kijacho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa michezo, utamaduni na sanaa ni fursa kubwa ya ajira nchini tunaiomba Serikali yetu iongeze bajeti ya Wizara hii na kutafuta wadau watakaotuunga mkono ili kupata mafanikio makubwa sana Kitaifa. Aidha, kuna haja ya kuendeleza miundombinu ya michezo nchini na kupangia matumizi kikanda na kimikoa ili kuchochea tasnia ya utamaduni, sanaa na michezo. Naomba pia Serikali yetu itusaidie kutuma wataalam wa Wizara kwa ajili ya kuendeleza na kukarabati Nyerere stadium iliyoko Jimbo la Mbulu Mjini, ni uwanja mkubwa katika mkoa wetu wa Manyara ili kupata mpango mkakati wa kuboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho siyo kwa umuhimu naomba kumkumbusha Mheshimiwa Waziri ombi langu la kuwa mgeni rasmi katika fainali ya Kombe la Mashindano ya Jimbo la Mbulu Mjini mwezi wa Julai 2023 ambayo kwa miaka saba sasa kombe hilo huanzia ngazi ya vijiji mwezi Aprili, ngazi ya kata mwezi Mei, ngazi ya tarafa mwezi Juni na kuhitimishwa ngazi ya Jimbo mwezi Julai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Mawaziri/Naibu Mawaziri waliotangulia kwa ushirikiano wao katika kuhitimisha kombe hilo kila mwaka kwa jinsi walivyoshiriki na kutambua mchango wa wananchi na wadau wa michezo katika Jimbo la Mbulu Mjini, asanteni sana, na karibuni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuungana na viongozi wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake kwetu sote, kwa jinsi alivyotuvusha kwenye majanga kama vile corona, ukame, mafuriko na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kwa niaba ya wananchi wote wa Jimbo la Mbulu Mjini kutoa pongezi za nyingi sana kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu mpendwa kwanza kwa kutunukiwa tuzo na kwa jinsi anavyotuwakilisha na kudumisha mahusiano na mataifa mbalimbali na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2020 - 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini nachukua nafasi hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango - Makamu wa Rais, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa – Waziri Mkuu, Baraza la Mawaziri na watendaji wote Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Balozi Liberata Mulamula Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Balozi Mbaruok Nassor Mbaruok – Naibu Waziri wa Wizara, Mheshimiwa Balozi Edward Sokoine - Katibu Mkuu wa Wizara, Mheshimiwa Fatma Rajabu Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nitoe mchango wangu kupitia hotuba ya Wizara hii; kwa kuwa suala la kutokujengwa na kuendelezwa limechukua muda mrefu tunaiomba Serikali itafute fedha za kujenga majengo ya ofisi za Balozi zetu na makazi ya watumishi hata kwa awamu, kwani Serikali inatumia gharama kubwa sana katika kupangisha majengo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie uwezekano wa kuwepo kwa maafisa wachumi wabobezi katika Balozi zetu na kama wapo watumike ipasavyo kwa kutangaza diplomasia ya uchumi na matumizi sahihi ya blue print na kutafuta fursa za mazao mbalimbali na bidhaa za nchi yetu katika masoko mataifa ya nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nchi yetu ina changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa ajira hapa nchini Serikali kupitia Balozi zetu ifanye uhamasishaji mkubwa sana makampuni ya nje kufungua viwanda vingi hapa nchini kwa kuondoa vikwazo na kuweka mazingira rafiki ili vijana wengi wa Kitanzania wapate ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hivi sasa kumekuwa na wimbi kubwa sana la kusafirisha mazao ya chakula kama vile mahindi, maharage na kadhalika kwenda nchi za Afrika Mashariki, kuna hatari kubwa sana ya Taifa letu kukumbwa na baa la njaa. Serikali itumie njia za kidplomasia kuzuia hali hii bila kuathiri mahusiano yetu na mataifa hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono kwa asilimia mia moja na naomba kuwaslisha.
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, naungana na viongozi wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake kwetu sote kwa jinsi anavyolijalia Taifa letu baraka zake kupitia majanga mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi na watendaji wengine wote Serikalini kwa jinsi wanavyosimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020 – 2025, hongereni sana.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara, Naibu Makatibu Wakuu, watendaji wote wa Wizara hii kwa utendaji wao uliotukuka, kwanza kutusikiliza na kufanyia kazi maoni yetu. Kwani ni ukweli usiopingika kuwa tatizo la ukosefu fedha na mahitaji ya ujenzi wa miundombinu ni changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao. Aidha, kwa namna ya pekee napenda kumpongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS nchini Engineer Rogatus na watendaji wake wa makao makuu, Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Manyara na watendaji wote wa TANROADS Mkoa kwa kuhakikisha barabara za Jimbo la Mbulu Mjini zinapitika wakati wote pamoja na jiografia yetu kuwa juu ya Bonde la Ufa.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mchango wangu kupitia hotuba ya Wizara hii; kwanza tunaishukuru sana Serikali kwa kutujengea Daraja la Magara kwani wananchi wa Wilaya ya Mbulu ni wanufaikaji wakubwa sana. Tunaiomba sana Serikali itusaidie kumwezesha kupata fedha za kuweka zege kilometa tano katika Mlima Magara Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara kwani tunatumia hela nyingi kuchonga na kuweka changarawe kila mwaka na pindi mvua ikinyesha mara moja tu barabara hiyo hujifunga bila usafiri na meneja wetu anatumia fedha nyingine zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa barabara ya Karatu - Mbulu, - Haydom – Meatu – Sibiti - Lalago kilometa 389 kwa kiwango cha lami tunaishukuru sana Serikali kwa hatua ya kumpata mkandarasi wa kilometa 25 kipande cha Mbulu – Garbabi. Hata hivyo tunaomba mkandarasi aanze kabla ya Julai, 2022. Serikali iharakishe mchakato wa manunuzi ya tender kwa kilometa 25 kipande cha Garbabi kilometa 25 Labay ili kujibu kiu na matarajio ya wananchi majimbo sita wanasubiri kwa hamu barabara hii.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mji wa Mbulu ni miongoni mwa miji mikongwe iliyoanzishwa na wakoloni nchini na kwa kuwa mji huu uko juu ya Bonde la Ufa na barabara zinazotuunganisha na miji ya Arusha na Babati zilizo fupi ni lazima upite Mbulu - Magara - Mbuyu wa Mjerumani kilometa 48 mpaka Arusha badala ya kupitia Karatu kilometa 228 na Mbulu - Kuta- Babati kilometa 68 badala ya 124 kupitia Dareda. Hivyo basi tunaiomba Serikali itupatie fedha za zege kilometa 13 kwenye maeneo hatarishi sana kwenye barabara hizo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha za kutosha katika Mfuko wa Barabara kwa mapato ya ndani na wafadhili, ni muhimu sasa Serikali ikae kikao cha pamoja na wachumi wabobezi wa ndani na Kamati ya Bajeti kwa haraka ili kupata vyanzo vipya vya mapato na kuleta mapendekezo ya Finance Bill kabla ya Bunge letu kuhitimisha ili kusaidia utatuzi wa jambo hili.

Mheshimiwa Spika, tunaishauri Serikali kwa kushirikiana na Wizara zingine mtambuka wakae kuangalia upya sheria za usimamizi na utunzaji wa barabara kukabiliana na uharibifu wa miundombinu na mwingiliano katika kushauri, kuelimisha na kuchukua hatua inapobidi.

Mheshimiwa Spika, mwisho ninaomba Mheshimiwa Waziri na Naibu Mawaziri wafanye ziara ya kutembelea barabara ya Mbuyu wa Mjerumani, Magara, Mbulu na Babati, Kiru, Mbulu kwani kwa heshima na staha siyo vizuri mimi kushika shilingi ya Mheshimiwa Waziri wakati hajui mazingira ninayoisemea. Kwani barabara hizo ni changamoto kubwa sana kwa wananchi wa Jimbo la Mbulu Mjini japo kuwa TANROADS Mkoa wa Manyara wamejitahidi sana japo kwa gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, naunga hoja mkono kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia amani, upendo, afya, mshikamano na utashi wa kisiasa katika Taifa letu. Aidha, tunampongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango - Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa usimamizi wao thabiti katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2022-2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Spika wetu, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote Serikalini kwa kuitumikia vizuri sana nafasi zao kikamilifu hongereni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali na Wizara waangalie upya wa kutafuta fedha zaidi katika kufanikisha mpango wa kupeleka umeme kwenye vijiji ambavyo bado hadi sasa line kubwa haijafika ili kurahisisha utekelezaji wa dhamira ya Serikali yetu na Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa malengo ya Serikali ya kupeleka umeme kila kijiji unasubiriwa na wananchi kwa hamu kubwa sana, na kwa kuwa bado kuna maeneo makubwa ambayo makandarasi tayari wamesimika nguzo zaidi ya miezi sita sasa, tunaiomba Serikali iwalipe makandarasi fedha zao kwa kazi ambayo tayari wamekamilisha ili waweze kuwasha umeme katika baadhi kwenye majimbo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mapendekezo ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati kiasi cha fedha zilizotengwa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili ni kidogo sana kulingana na mahitaji halisi ya mradi huu wa shilingi bilioni 1.240. Hivyo basi ni muhimu Serikali iangalie mpango mbadala wa kutafuta fedha zaidi, na mradi huu ni muhimu sana ukaanza kwenye vijiji ambavyo line kubwa ilishapita kwa zaidi ya miaka mitatu na maeneo yenye uzalishaji mkubwa kwa mfano taasisi za umma na binafsi, taasisi za dini, migodi, vijiwe vyenye biashara na maeneo ambayo yana uwezekano wa kuanzishwa viwanda vidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri kupitia hotuba yake aweze kutoa kauli ya Serikali kuhusu matumizi sahihi ya unit kwa watumiaji wadogo hususan umeme wa matumizi majumbani. Kwani eneo hilo lina mkanganyiko kati ya TANESCO na TRA, na wananchi wa kipato cha chini vijijini kuona tofauti ya umeme wa matumizi na ule wa kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho siyo kwa umuhimu, tunaiomba Serikali itume utafiti kuzalisha umeme wa upepo ili kuongeza vyanzo vya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuungana na viongozi wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa majaliwa yake kwetu sote, kwani tunajivunia kwa jinsi alivyotuvusha kwenye majanga mbalimbali kwa mfano corona na majanga mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kwa niaba ya wananchi wote wa Jimbo la Mbulu Mjini kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu mpendwa kwa jinsi anavyoiongoza nchi yetu na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020 – 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waziri wa Wizara hii Mheshimiwa Naibu Waziri wa Wizara na Mheshimiwa Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa jinsi mnavyoitendea haki Wizara hii; kwanza kutusikiliza sisi wawakilishi wa wananchi na kutatua tatizo la kuzuia ujenzi holela na kuleta kupanga, kupima na kumilikisha (KKK) kwa nchi nzima, hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee naungana na viongozi wenzangu kutoa pole nyingi kwa familia zilizopata msiba ya kuwapoteza wapendwa wao kuanzia kwa viongozi wote, watendaji na Watanzania wote, Mwenyezi Mungu atujalie hali ya ustahimilivu katika kipindi hiki, sote kwa pamoja tunaziombea roho zao kwenye ufalme wa mbinguni usio na mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nitoe mchango wangu kupitia hotuba ya bajeti ya mwaka 2022/2023 ya Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nachukua nafasi hii kuipongeza sana Serikali yetu kwa kuleta mpango wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika Halmashauri zote nchini na kuonesha mafanikio makubwa sana kukabiliana na kuzuia ujenzi holela na kurasimisha ardhi kuwa na thamani kubwa na miji itakayopangika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi kuna baadhi ya changamoto zinazozuia jitihada hizo zikiwemo upungufu mkubwa sana wa vitendea kazi, watumishi wa kada muhimu katika idara za Ardhi ngazi za Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba sana Serikali iwaajiri wataalam wa kada muhimu katika kufanikisha mpango huu muhimu sana kwenye bajeti ya mwaka huu. Tunashukuru sana Serikali kwa kuondoa baadhi ya maamuzi/hukumu katika Mabaraza ya Kata kwa kuwa baadhi ya walalamikaji na walalamikiwa kutokuridhika na maamuzi ya mabaraza ni muhimu sana Serikali kuwa na mfumo wa kuchunguza mabaraza yanayolalamikiwa hasa kwenye mashauri mengi yanayogusa Serikali za Vijiji, Halmashauri za Wilaya, taasisi za Serikali na watu binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza sana Serikali kwa mpango wake wa kutumia timu ya Waheshimiwa Mawaziri na watendaji kufanya ziara ya kutatua migogoro nchi nzima. Kwa hiyo ni muhimu sana kabla ya timu hiyo kuondoka wakatoa nafasi kwa waheshimiwa Wabunge wa maeneo hayo kama wawakilisha wa wananchi ili kupata na kuelewa historia na chimbuko lenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ijitahidi kukusanya mapato yake ya ndani kwa 100% ili kufanikisha lengo lake kwa mwaka wa bajeti kwani kiwango cha 42% kilichokusanywa mwaka 2021/2022 ni ndogo vinginevyo kufanyike mapitio ya kina kwenye vyanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho siyo kwa umuhimu tunaiomba sana Serikali ijitahidi kutoa fedha zinazoombwa na Wizara hii ili kufanikisha malengo kwani kiwango cha 51% kwa fedha zilizotolewa na Serikali 2022/2023 ni ndogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa silimia mia moja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia amani, upendo, afya, mshikamano na utashi wa kisiasa katika Taifa letu. Tunampongeza sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Isdori Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa usimamizi wao thabiti katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2022-2025.

Mheshimiwa Spika, tunawapongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote Serikalini, kwa kuzitumikia vizuri sana nafasi zao kikamilifu, hongereni.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nitoe mchango wangu kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii na taarifa ya Kamati iliyowasilishwa katika Bunge letu; tunaiomba Serikali itoe mpango kazi wa shughuli za michezo kwa Kamati za Wilaya na Mikoa ili kufanikisha uibuaji wa vipaji vya michezo kwa vijana wetu kutoka ngazi za shule za msingi, sekondari na wilaya ili kuwalea na kuendeleza vijana wetu katika ngazi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali iajiri maafisa michezo na utamaduni katika halmashauri zote nchini ili kufanikisha maendeleo ya michezo hapa nchini na pia tunaiomba Serikali ifanye utaratibu wa kuendeleza viwanja vya michezo kama vile uwanja wa michezo wa Nyerere Stadium, Mbulu kwa kuingia ubia na Chama cha Mapinduzi kwani hali ya hewa ya Mbulu ni nzuri sana kwa michezo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.