Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Sikudhani Yasini Chikambo (37 total)

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naitwa Chikambo siyo Chikabo.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba ikumbuke kwamba Wilaya ya Tunduru tumeendelea kukiamini Chama cha Mapinduzi kwa kutoa kura nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikumbuke kwamba wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2014 alitoa ahadi za kutoa magari ya ambulance katika vituo vya afya vya Nalarasi,Nakapanya na Matemanga. Kwa hali ile ile ya kuendelea kukiamini Chama cha Mapinduzi. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie ni lini sasa ahadi hiyo itatekelezwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba ahadi hii imetolewa na Mheshimiwa Rais aliyepita na ahadi hii ni ahadi ya Serikali na ndiyo maana nimesema katika mchakato huu sasa hivi kuna gari la wagonjwa, bajeti imetengwa kwa ajili ya kupelekwa. Umesema maeneo mbalimbali ambayo Mheshimiwa Rais mstaafu alitoa ahadi hiyo, hii ni ahadi ya Serikali na ninajua wazi katika mkoa ule kwa sababu una vipaumbele vingi sana. Siyo ahadi hiyo peke yake, Mheshimiwa Mbunge ameniambia kwamba mpaka walikuwa na ahadi ya Mkoa mpya wa Selous tunayajua hii kama Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu maeneo haya yana vipaumbele maalum naomba nikwambie kwamba ahadi ya Serikali iko palepale katika mchakato tulioondoka nao tutahakikisha kwamba ahadi ya Mheshimiwa Rais inatekeleza ili mradi wananchi wapate huduma bora.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Tatizo la kusumbuliwa akina mama lishe limekuwa kubwa sana katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu. Siyo siri, tunapozungumzia mama lishe, sana tunawagusa akina mama na wale wajasiriamali wadogo wadogo. Wewe, mimi na Waheshimiwa Wabunge wote tutakuwa mashahidi kwamba hawa akina mama ndio wapigakura wa Chama cha Mapinduzi. Ni nini sasa agizo la Serikali kuhakikisha hawa akina mama lishe wanatengewa maeneo maalum ya kufanyia biashara zao katika Halmashauri zote ndai ya nchi yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli akina mama lishe wakati mwingine wanapata changamoto kubwa sana. Kibaya zaidi ni pale utakapoona Mgambo anakwenda kuchukua jungu la mama lishe halafu wanakusanyika pembezoni wanakwenda kula kile chakula cha mama lishe. Hili jambo linakera sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana siku moja nilipokwenda katika Soko lile la Ilala pale nilitoa maelekezo kwamba tuone jinsi ya kuwarasimisha vizuri tuwaweke katika utaratibu mzuri. Hilo ni moja.
Sehemu nyingine hata wakati mwingine kunaweza kuwa na utaratibu mzuri, Halmashauri zimejenga vibanda kwa akina mama lishe, lakini kuna baadhi ya watumishi wasiokuwa waadilifu, wanatumia vile vibanda wanakodisha akina mama lishe kwa pesa kubwa sana. Jambo hili tumelikemea pale Ilala na sehemu mbalimbali, lakini suala la upangaji wa haya maeneo ni kama nilivyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba ndugu zangu, Waheshimiwa Wabunge, tushirikiane na Halmashauri zetu, tutenge haya maeneo, tuyaweke vizuri ilimradi kwanza wale akina mama waliokuwa wanafanya kazi zao katika maeneo ya jua; waliokuwa wanafanya kazi zao katika maeneo yasiyo rafiki; bajeti zile zikifika katika mwaka huu wa fedha tutakaokuja nao, katika Ofisi ya Rais TAMISEMI ambao ndiyo jukumu letu kubwa kuzisaidia Halmashauri, hatutasita kuipa mipango ili kipaumbele ilimradi hawa akina mama waweze kupata fursa ya kufanya kazi zao katika mazingira rafiki; kwa sababu hata katika suala zima la afya itasaidia kupambana na magonjwa ya kipindupindu.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Sikudhani, naomba nikwambie kwamba nitashirikiana na wewe na ninajua kwamba Tunduru ndiko unakotoka, kule bainisheni hilo, tutaweka kipaumbele ilimradi wananchi waweze kupata fursa na akina mama wapate fursa nzuri za kiuchumi.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mwaka 2011/2012 Bunge hili liliazimia kuanzisha Mabaraza ya Ardhi matano. Miongoni mwa Mabaraza hayo ni pamoja na Wilaya ya Tunduru kuanzisha Baraza la Ardhi lakini mpaka sasa hivi tunavyozungumza Wilaya ya Tunduru katika Baraza lile la Ardhi bado halina Mwenyekiti, Mwenyekiti ni lazima atoke Songea aje Wilayani Tunduru. Ni lini sasa Serikali itachukua hatua ya kuona kuwa tunapata Mwenyekiti ambaye atakuwa anashughulikia migogoro ya ardhi iliyopo Wilayani Tunduru? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza swali lake liko nje na lile swali la msingi lakini kwa sababu ameuliza naomba tu nitolee maelezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa bajeti ya Wizara tulitoa orodha ya Halmashauri zote au Wilaya zote ambazo Mabaraza mapya yanakwenda kuanzishwa na yalikuwa ni Mabaraza 47 ambayo yamepangwa, lakini kwa kuanzia tukasema ni Mabaraza matano. Kesi yake katika Jimbo lake analolisema tunaitambua lakini kulingana na ule ufinyu wa bajeti iliyopo tumeshindwa kuwa na Wenyeviti wa kutosheleza Mabaraza hayo ambayo tutakwenda kuanzia nayo. Ndiyo maana tulisema tumeomba ombi maalumu kwenye Wizara ya Utumishi ili kutupa kibali tuweze kupata Wenyeviti tuwasambaze katika maeneo yote ambayo hayana Mabaraza na ambako kuna matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo, pale ambapo tutapewa kibali hicho, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwenye Baraza analolizungumzia ambalo halina Mwenyekiti kwenye Jimbo lake basi tutampatia. Kwa sasa bado tunasubiri kibali kutoka Wizara ya Utumishi.
MHE. SUKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ifahamike kwamba pesa hizi zinatengwa kwa ajili ya kusaidia vikundi vya wanawake na vijana na hasa wale wanaojiunga kupitia makundi mbalimbali. Kwa bahati nzuri nimekuwa Diwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru vipindi vinne. Pesa hizi hata kama zikitengwa katika Halmashauri nyingi nchini, kunapojitokeza jambo la dharura kwenye Halmashauri, pesa hizi zimekuwa zikitumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sasa Serikali itoe tamko kupitia Halmashauri zetu nchini, kunapojitokeza Halmashauri imekiuka utaratibu wa kutekeleza pesa hizi kuwafikia akina mama ni hatu gani sasa zitachukuliwa kwa Halmashauri ambazo zitashindwa kutekeleza? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba kiufupi tu niseme ifuatavyo; sasa hivi ni marufuku kwa Halmashauri yoyote asilimia kumi iliyotengwa kutowafikia vijana na kina mama na ninasema hivi sitanii.
Katika bajeti ya mwaka huu kila Halmashauri imepitishwa bajeti yake mara baada ya kutenga ile asilimia kumi; kwa hiyo Mkurugenzi yeyote na Kamati ya Fedha watakaposhindwa kutimiza wajibu huu wa Serikali, tutahakikisha Halmashauri yao tutaiwajibisha kwa sababu imeshindwa kutimiza matakwa halisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo tumepitisha katika bajeti ya mwaka huu wa fedha.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Kwa kweli ni miongoni mwa Mawaziri ambao wanatoa majibu ambayo hayana ukakasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo naomba niulize swali dogo la nyongeza. Pamoja na maboresho hayo lakini kumekuwa na malalamiko kuhusu wale wapagazi kunyanyasika kwa kulipwa kiwango kidogo. Je, ni lini Seikali itaweka utaratibu wa kuboresha maslahi yao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sikudhani Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum kutokea Mkoa wa Ruvuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimesema kwenye majibu yangu ya swali la msingi, kwamba tutaboresha hali za wafanyakazi wanaotoa huduma kwenye sekta ya utalii kwa ujumla wake na wapagazi ni sehemu yao. Watalii wakifika kufanya utalii katika nchi yetu mojawapo ya vitu vitakavyofanya wao wanaofika kwanza waendelee kubaki kwa muda mrefu zaidi lakini pia kuweza kuvutia watalii wengine kuja ni pamoja na aina ya huduma wanazozipata na huduma hizo zinatolewa na wale ambao wamepewa fursa hiyo na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuboresha mazingira ya watenda kazi hawa ni jambo la msingi na Serikali inalizingatia ili kwa kufanya hivyo tuweze kuvutia watalii zaidi na wakija waweze kukaa kwa muda mrefu zaidi kwa ajili ya tija ya mapato kwenye sekta ya utalii.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuchelewa kukamilisha kwa miradi ya maji ya vijiji vya Nandembo, Nalasi, Lukumbule na Amani; je, Serikali haioni kwamba kuchelewa kukamilisha miradi hiyo kutaongeza gharama ya miradi?
Swali la pili, katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji amesema vijiji vya Majimaji, Muhesi, Nakapanya na Mchoteka utekelezaji wake haukufanikiwa kutokana na kukosa vyanzo. Je, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha vyanzo vinapatikana na utekelezaji huu unaanza mara moja kwa sababu jambo hili ni la muda mrefu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza amezungumzia Serikali haioni kwamba kuchelewa utekelezaji wa miradi kuna ongeza gharama; ni kweli ukichelewa utekelezaji wa mradi gharama inaongezeka kwa sababu kuna mabadiliko ya bei ambayo yanatokana na vifaa vya ujenzi, lakini pili wale wakandarasi wanaojenga wameajiri watu wao ile gharama ya mishahara muda unakuwa mrefu, kwa hiyo ni kweli kabisa kwamba kuchelewa kunaongeza gharama ya miradi. Kuchelewa kwa miradi kunatokana na matatizo ambayo yanajitokeza katika mkataba siyo kwamba ni suala ambalo linapangwa na binadamu basi tu ni kwamba, kwa mfano tunachelewa kwa sababu katika utekelezaji wa hii miradi tunasaidiana na wadau ambao ni marafiki zetu ambao wanatusaidia katika utekelezaji wa miradi sasa hela ikichelewa kupatikana basi kwa vyovyote vile lazima mradi uchelewe.
Mheshimiwa Spika, wakati mwingine tuna-design mradi kumetokea mabadiliko ya tabianchi yanayosababishwa na binadamu vyanzo vinakosa maji kwa vyovyote mradi ule lazima utachelewa.
Swali lake la pili amezungumzia suala la vyanzo, ni kwamba Serikali kwa sasa tayari kwa miradi ambayo haikupata vyanzo study zinaendelea kuhakikisha kwamba miradi hiyo inapata vyanzo na lazima vyanzo vipatikane ili tuweze kukamilisha utekelezaji wa hiyo miradi.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza ifahamike kwamba Wilaya nyingi zilizopo Mkoani Ruvuma zipo mpakani, kwa mfano Wilaya ya Nyasa inapakana na Malawi, Wilaya ya Tunduru inapakana na Msumbiji. Kuwa na makazi bora ya polisi katika maeneo haya kutahamasisha polisi wetu kuishi katika makazi salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri ameeleza kuna nyumba 9,500 zinategemewa kujengwa nchi nzima. Napenda kujua kati ya nyumba hizo ni ngapi zitajengwa Mkoani Ruvuma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, pale Wilayani Tunduru kulikuwa na jengo ambalo lilikuwa linatumiwa na Askari Polisi wanapokuja kuhamia, jengo lile liliungua moto. Jengo lile lilikuwa linasaidia sana na hasa kwa askari wa kike kupata makazi pale wanapokuja kuhamia. Naomba kujua Serikali imejipangaje katika kuhakikisha jengo lile linajengwa tena ili liwasaidie askari wale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na nyumba ngapi zinatarajiwa kujengwa Mkoa wa Ruvuma ni 320.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na jengo hilo ambalo amelizungumza tunachukua concern yake tuone ni hatua gani tutachukua ili kuweza kulifanyia ukarabati ikiwezekana katika bajeti zinazofuata.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Spika ahsante kwa kunipa nafasi. Tatizo la ujenzi wa barabara lililopo Mpanda hadi Uvinza halina tofauti na tatizo la ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami lililopo Mbinga hadi Nyasa. Barabara ile iliahidiwa na Serikali kwamba itajengwa, napenda kujua ni lini sasa ujenzi ule utaanza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Chikambo, kama ambavyo nilimweleza alipofika ofisini mbele ya Waziri wangu akifuatilia utekelezaji wa barabara hii akiongozana na Mheshimiwa Stella Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kwamba barabara hii inaanza kujengwa mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu kwamba tumechelewa katika taratibu za Procurement kwa sababu nafahamu fedha zinazotarajiwa kujengea barabara hii zinatoka African Development Bank na kwamba wao wana utaratibu wao wa Procurement, ni lazima tuufuate. Tumechelewa lakini tutahakikisha mara tutakapokamilisha taratibu za Procurement barabara hiyo itaanza kujengwa.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ambayo yametolewa kuhusiana na suala la kuhamisha watumishi katika Halmashauri zetu lakini suala hili limekuwa sugu sana. Ukiacha hao walimu ambao wamewazungumzia lakini wapo pia wauguzi, watendaji wa kata na vijiji. Mimi kama Mbunge au Diwani naweza kwenda kwa Mkurugenzi nikamuambia Mtendaji huyu simtaki mpeleke katika kijiji au kata nyingine bila kujali stahiki zake. Ni nini sasa kauli ya Serikali kuhusu watumishi hawa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, alichosema Mheshimiwa Sikudhani ni kweli na hili sisi viongozi tunatakiwa tujitathmini kwamba wakati mwingine una interest zako binafsi unasababisha mtu fulani ahame kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine bila kujua kwamba unalimbikiza madeni katika maeneo hayo. Bahati mbaya sana wakati mwingine Mkurugenzi akikataa ndiyo unaanza bifu (kutokuelewana) naye kuanzia hapo kwamba Mkurugenzi huyu hatufai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba utaratibu wa kuhamisha kama alivyozungumza Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Boniface Simbachawene ni lazima uendane na bajeti iliyokuwepo. Vilevile si vyema kwa viongozi wowote kuwaweka katika mazingira magumu watumishi hawa na kuwa-frustrate kwa kuwahamisha bila sababu yoyote. Tunasema jambo hilo likome na lisiendelee katika Halmashauri zetu kwa sababu halileti afya kwa watumishi wetu ndani ya nchi yetu.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini napenda afahamu kwamba tunapozungumzia wazabuni tusisahau kwamba tunawazungumzia wafanyabiashara. Mara nyingi kama walivyosema wenzangu wafanyabiashara hawa wanapata pesa zao kutoka kwenye mabenki lakini maelezo yake anasema kwamba wale ambao hawajalipwa watalipwa pindi Serikali inapopata pesa. Napenda kujua ni lini? Ni vizuri jambo hili sasa likawekewa mkakati.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu inatambua umuhimu wa kuwalipa wazabuni hawa lakini kama alivyosema Mheshimwa Naibu Waziri wa TAMISEMI kwamba sasa hivi tuliji-engage kwenye kuyahakiki madeni haya. Waheshimiwa Wabunge, naomba niwaambie jambo moja kwamba Serikali ina nia njema. Tulipokea madeni haya kwa ajili ya shule tu ya shilingi bilioni 21.64 baada ya uhakiki tumekuta ni shilingi bilioni sita tu ambazo ni halali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndiyo maana Serikali inaomba muda maalum ili tuweze kumalizia uhakiki. Hii itasaidia Serikali kulipa yale madeni ambayo ni halali kwa ajili ya wazabuni waliotoa huduma na siyo kuwahi kulipa wakati kuna vitu vingine vya kufanya na tutajikuta tunalipa madeni hewa. Tunasisitiza dhamira ya Serikali ni njema na tutalipa madeni yote yale ambayo ni halali tu.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nilipenda niseme kama ifuatavyo:-
Suala la uingizaji wa dawa za kilimo zisizokidhi vigezo limekuwa sugu katika nchi yetu. Hata hivyo Mheshimiwa Waziri ameeleza mamlaka mbalimbali ambazo zinahusika katika kuhakiki hizo dawa na uingizaji. Nilipenda kujua ni hatua zipi zimekuwa zikichuliwa kwa makampuni hayo ambayo yamekuwa yakileta dawa ambazo hazikizi vigezo; hasa kwa sabau zinaleta mzigo mkubwa kwa wakulima wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali inaendelea kupitia tozo mbalimbali katika sekta ya kilimo ili kuona uwezekano wa kuziondoa tozo hizo. Nilipenda kujua kwamba zoezi hilo la kupitia hizo tozo ambazo zimekuwa mzigo kwa wakulima wetu litaanza lini ili kuleta unafuu kwa wakulima wetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na uingizwaji wa dawa ambazo hazikidhi viwango ni kweli kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna changamoto hiyo. Hata hivyo Serikali imeendelea kudhibiti na kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha tatizo hilo linamalizika ili kuhakikisha kwamba wakulima wetu hawaathiriwi na viuatilifu ambavyo si salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya hatua ambazo tunazichukua ni kwamba pale tunapogundua, kwamba Kampuni fulani imeingiza dawa ambayo si sahihi, mara nyingi Kampuni ile inafutiwa leseni, lakini vile vile kama ni maduka tunayafunga, lakini tayari vile vile kuna kesi nyingi ambazo ziko Mahakamani kwa watu na Makampuni ambao wamebainika kuvunja taratibu za Kisheria kuhusiana na viuatilifu pamoja na dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana 2016 tulifanikiwa kukamata viuatilifu lita 14,600 ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa kawaida wa kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanapata viuatilifu na dawa salama. Ifahamike tu kwamba viuatilifu vingi ambavyo vinaingia ambavyo havikidhi viwango vingi vinatoka nje na hiviingizwi kwa utaratibu wa njia rasmi, zinapitia katika uchochoro, katika panya roads. Kwa hiyo, mara nyingi wahalifu kila wakati wanagundua njia mpya ya kuhakikisha kwamba wanakwepa mkono wa Sheria lakini Serikali imeendelea kuhakikisha kwamba kila wakati yule ambae anahusika anachukuliwa hatua za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na tozo, nafikiri Mheshimiwa Mbunge amekuwepo, kwa sababu sasa tunaendelea na mjadala wa Wizara yetu, kwamba tayari Wizara imependekeza kufuta tozo 108, tozo ambazo tunahakika zikifutwa zitamsaidia sana mkulima, mfugaji na mvuvi wa Tanzania katika kuendelea kunufaika na kilimo, ufugaji na uvuvi wao. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge aendelee kufuatilia kwa sababu tayari tumeishaondoa hizo tozo, lakini Wizara inaendelea kuongea na Wizara zingine ambazo zinasimamia baadhi ya tozo ili tuendelee kuziondoa au kuzipunguza.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Kwanza nianze kuwapongeza Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya, Mheshimwa Rais amewaona ninyi na sisi Wabunge wenzenu tuna imani na ninyi katika kutatua kero za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali la nyongeza. Wakati wa Kampeni za Uchaguzi Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliahidi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, barabara inyoanzia Wilayani Namtumbo katika vijiji vya Mtorapachani, Ligusenguse na kuelekea Mchoteka na Lasi hadi Tunduru. Naomba nijue ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwa ufupi kabisa tunaratibu ahadi zote za Mheshimiwa Rais, ahadi zote za Makamu wa Rais kwa maeneo ambayo yanahusu ujenzi wa barabara. Nimuahidi tu kwamba katika kipindi cha miaka mitano hivi zoezi hili litakuwa linaendelea kukamilisha barabara zote zilizoko kwenye ahadi, ahsante.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO:Mheshimiwa Naibu Spika,asante kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi kwamba ukosefu wa makazi bora ya walimu kunawakatisha tamaa walimu kuishi vijijini na mara kwa mara walimu wengi wamependa kuhama kutoka kwenye maeneo haya na kuhamia maeneo ya mijini ambako kuna makazi bora. Ukichukulia Halmashauri moja tu ya Tunduru mahitaji ni nyumba za walimu 1782; upungufu 1688 lakini Naibu waziri amesema ana mpango wa kujenga nyumba 30 katika mkoa mzima wa Ruvuma naona hii kasi ni ndogo nilipenda kujua Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha jambo hili tunalimaliza kwa haraka na ukizingitia sisi wote tumetokana na hao walimu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu langu la msingi nimeeleza kwamba ni wajibu wetu sisi Serikali Kuu Halmashauri pamoja na wananchi kwa ujumla tukizingatia kwamba upungufu huu ni mkubwa sana haitakuwa busara tukasema tunaiachia Serikali peke yake, tuna wajibu wa kuhakikisha kwamba tunashirikishana ili tatizo hili tulimalizekwa haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hii naomba nirejee kwa ruhusa yako jana wakati Mheshimiwa Gekul wakati anaomba Mwongozo kwa Mheshimiwa Spika alisema kwamba kuna barua (Waraka ambao umetolewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI) ukiwataka wananchi kwamba kuanzia sasa hivi ni wajibu kushiriki kuanzia mwanzo kwa maana ya msingi hadi kwenda kumalizia. Kabla Serikali haijaleta taarifa yake rasmi naomba niseme kwamba hakuna waraka kama huo ambao umepelekwa ni wajibu wetu sisi wananchi pamoja na Serikali kushirikiana ili kumaliza matatizo yanayohusu watumishi wa Serikali.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo Ngomalusambo Wilayani Mpanda la mradi wa maji kukamilika lakini hautoi maji halina tofauti na mradi wa maji uliopo Wilayani Tunduru Kijiji cha Nandembo. Mradi ule ulitumia mamilioni mengi ya shilingi lakini mpaka hivi tunavyozungumza wananchi wale hawapati maji. Napenda kujua ni nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha sasa huduma hiyo inapatikana ipasavyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuna sababu inawezekana mradi mwingine kwa mfano juzi juzi nilikuwa na ndugu yangu Kibajaji hapa katika Kijiji chake cha Manzase mradi umekamilika lakini tatizo kubwa lilikuwa ni suala zima la power, kwamba nishati ya aina gani iweze kutumika, kwa hiyo case by case hii miradi haitoi maji kwa sababu maalum. Inawezekana sehemu nyingine pampu hazijakamilika, hazijanunuliwa au mradi haufanyi kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa case ya Mheshimiwa Mbunge, sifahamu mradi huo ukoje. Jambo ninalotaka kulifanya tukitoka hapa naomba anipe takwimu halisi ni kitu gani kinachoendelea pale tutoe maelekezo ya stahili nini kinachotakiwa kufanyika, kwa sababu najua miradi hii inakwama katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo Mheshimiwa Sikudhani naomba anijulishe baadaye kuna kitu gani pale kinachoendelea, tutoe maagizo mahsusi katika suala zima la mradi tuweze kuwasaidia wananchi wake waweze kupata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo nilimwona Mheshimiwa Musukuma hapa akisimama kwa ajili ya mradi wake wa Changorongo, naamini alitaka kusimama kwa hoja hiyo. Mheshimiwa Msukuma kwa sababu tumekubaliana hapa miongoni mwa jambo tunalotaka kwenda kulifanya baada ya Bunge kutembelea ile shule ya msingi tutafika hapo kwa ajili ya kujibu lile swali kwa ajili ya wananchi wa Geita pale ambao muda mrefu tumewapigia kazi waweze kupata huduma inayostahili.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tafsiri ya swali langu, nilipenda kujua miradi ambayo inatekelezwa katika Mkoa wangu wa Ruvuma mimi kama mwakilishi wa mkoa ule, lakini majibu ya Mheshimiwa Waziri yameeleza kwamba kuna miradi ambayo inatekelezwa katika vijiji 230, vimekamilika vijiji 94.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kunisaidia kujua miradi hiyo ipo katika maeneo gani? Mimi kama mwakilishi wa wanawake wa Mkoa wa Ruvuma nipate kujua ni ipi inatekelezwa ili nilete msukumo katika Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, ipo maradi miwili sugu ambayo inatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru. Kuna Mradi wa Mtina na Mradi wa Matemanga. Miradi hii ni ya muda mrefu sana na ilitakiwa iwe imekamilika. Hivi ninavyozungumza, Halmashauri imesitisha mikataba ya wale wakandarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama inavyofahamika ni kwamba tafsiri ya wananchi ni kuona miradi inakamilika na inatoa maji. Je, nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha miradi hii inakamilika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyowapigania wananchi wake, Mwenyezi Mungu ambariki sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wangu aliniagiza kwenda Mkoa wa Ruvuma kufanya ziara na kuangalia hali ya upatikanaji wa maji. Pamoja na kuangalia, nilijiridhirisha kupita katika Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma, lakini kuna kazi kubwa sana inayofanyika katika vijiji mbalimbali. Moja, Ngunguru, Mbesa, kuna Chandarua, Jeshini na Muungano, yote kuna sehemu ya utekelezaji wa miradi ya maji. Kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge anataka kujua vijiji vyake kwenye utekelezaji wa maji, nipo tayari baada ya Bunge nimpe nyaraka hii ambayo imeidhinisha vijiji vyote ambavyo utekelezaji wa maji upo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, kumekuwa na kusuasua sana kwa miradi ya maji kwa mfano Matemanga. Mimi Naibu Waziri nilifika pale kuona hali ya upatikanaji wa maji, lakini tumekuja kujifunza kwamba pamoja na Serikali kupeleka fedha, lakini kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa sana wakandarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya sababu ni watu kupeana kazi kishemeji shemeji au kiujomba jomba. Kwa hiyo, kwa kuwa kazi ya Waziri au kazi ya Wizara yetu ni kuhakikisha wananchi wanapata maji, tumeiomba Halmashauri isitishe mkataba na yule mkandarasi, watafute mkandarasi mwingine haraka ili wananchi wale waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Miongoni wa vitu vya afya ambavyo vilipangiwa kupatiwa pesa Mkoani Ruvuma ni pamoja na Kituo cha Afya Namtumbo na Mkasali. Naishukuru Serikali vituo hivyo vimepata pesa. Hata hivyo, kipo Kituo cha Afya cha Matemanga ambacho kilipangiwa kupatiwa pesa kwa ajili ya ukarabati, lakini pesa ile mpaka sasa haijaenda. Ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na hiyo pesa ya ukarabati wa vituo vya afya? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yale ya awali. Naomba kumpa comfort kwanza mtani wangu Mnyamwezi. Mheshimiwa Ntimizi wiki iliyopita alikuja ofisini kwetu pale kwa ajili ya vituo vya afya vitano vilivyoanzishwa katika mchakato wa ujenzi wa na tumewapa commitment kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI itahakikisha kwamba ina- support ndani ya mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuhusu suala la Matemanga, tayari naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ndani ya wiki hii tu-cross-check accounts zetu kule katika halmashauri yetu, tutakuwa tumeshaingiza hizo fedha tayari kwa ajili ya kuhakikisha kituo kile kinakamilika. (Makofi)
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayolima zao la korosho na yapo maeneo mengi ambayo ni rafiki kwa ujenzi wa viwanda vya korosho ikiwemo Wilaya ya Tunduru na Namtumbo ambapo zao la korosho linalimwa katika Wilaya hizo.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha tunajenga viwanda katika maeneo hayo ili wakulima sasa waweze kubangua korosho zao katika Wilaya hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi kwanza nampongeza Mheshimiwa Chikambo, lakini pia nawapongeza wote wanaofuatilia suala hili la korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa rai kwa sisi sote ambao tuko hapa na Watanzania wengine ambao watafanikiwa kuwafahamu wanaohitaji kuwekeza katika viwanda vya korosho; tafadhalini Tanzania ni katika nchi ambayo inatoa korosho bora sana. Hali kadhalika kupitia SIDO tunatengeneza viwanda vidogo vidogo vya kuweza kuendeleza ubanguaji au viwanda vya korosho. (Makofi)
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Hii asilimia 10 ambayo tunaizungumza ni ile inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri. Sote tutakuwa mashahidi kwamba ziko Halmashauri hazina uwezo wa kukusanya vyanzo vya mapato, wana vyanzo vidogo na vile vyanzo vingine vimechukuliwa na Serikali Kuu. Hii inasababisha kushindwa kutenga hii asilimia 10 kwa ajili ya wanawake, vijana na walemavu. Ni nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha tunazipa uwezo Halmashauri ili ziweze kutenga hizi pesa kwa ajili ya kukopesha wanawake, vijana na walemavu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumetoa maelekezo kwamba Halmashauri zote zifanye mapitio ya vyanzo vyao vya mapato ili kuhakikisha kwamba wanaongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na pili ni kwamba hata kama wamekusanya shilingi 10; asilimia 10 iko pale pale. Asitoe vigezo kwamba eti kwa sababu amekusanya mapato kidogo, basi atenge hiyo asilimia 10. Asilimia 10 ni ya kisheria na kwa mujibu wa maelekezo. Kwa hiyo, hata kama amekusanya 100 asilimia 10 iko pale pale.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyoelezwa kwenye swali la msingi kwamba wananchi 803 wa Kata za Matogoro na Seedfarm wanadai fidia ya kiasi cha shilingi bilioni 1.9, lakini majibu ya Serikali wamesema katika mwaka wa fedha 2017/2018 watalipa, mimi nafahamu mwaka wa fedha 2017/2018 unaishia hivi karibuni watalipa milioni 500. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kiasi hiki kilichobaki kinalipwa kwa wakati?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa malipo haya yamechelewa; Je Serikali haioni kwamba iko haja ya kuwalipa wananchi hawa pamoja na fidia kwa kuwa jambo hili limekuwa la muda mrefu? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WA WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nitumie nafasi kumpongeza dada yangu Sikudhani Chikambo pamoja na Mheshimiwa Mbunge wa Songea Mjini kwa namna wanavo wapigania wananchi wa Majimbo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara ya Maji kwa kuona wananchi wale wametoa eneo kwa ajili ya chanzo cha maji, Wizara yetu ikaona haja ya kulipa. Nadhani kabla ya bajeti hii kuisha tutawalipa fedha zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kiasi kilichobakia nitumie nafasi hii kwanza kulipongeza Bunge lako Tukufu kwa kutuidhinishia Bajeti yetu ya Maji na katika fedha zile kiasi ambacho kilibakia tumeshawatengea fedha wananchi wa Songea. Kikubwa nimwombe Mheshimiwa Mbunge akawasimamie wananchi wake waende kuzitumia fedha zile vizuri, badala ya kwenda kuongeza familia nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji hatuko kwa ajili ya kuwadhulumu, kikubwa fedha hizi zitatoka kwa wakati katika kuhakikisha tunawalipa fidia wananchi wake. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Sisi sote tunafahamu kwamba mahakama ni chombo cha kisheria ambacho kimekuwa kikitoa haki na kuleta amani katika maeneo mbalimbali kwa mujibu wa sheria. Je, Serikali haioni kuchelewa kuweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi kwa watumishi wa mahakama wakiwemo Mahakimu ni kudhoofisha hali ya utendaji kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika jibu la Mheshimiwa Waziri la msingi amekiri kama mahakama hizo ni chakavu na majengo mengi ni yale yaliyoachwa na Mkoloni, je, ni nini tamko la Serikali la kuharakisha ujenzi wa mahakama hizo sambamba na ujenzi wa nyumba za Mahakimu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inatambua changamoto iliyokuwepo katika ujenzi wa mahakama na kwa muda wote tumeendelea kutenga fedha kwenye bajeti zetu kuhakikisha kwamba tunakabiliana na changamoto hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa Wizara tumeamua kushirikiana na Baraza la Nyumba la Taifa na Chuo Kikuu cha Ardhi ili kupitia ujenzi wa nyumba za mahakama na ofisi za mahakama kwa kupitia teknolojia mpya ya moladi tuweze kuzifikia mahakama nyingi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tunajenga mahakama nyingi kadri iwezekanavyo na hii itatokana na upatikanaji wa fedha. Uzuri tunayo teknolojia mpya ya moladi, naamini tutawafikia wananchi wa Tunduru na wao wapate huduma hii ya mahakama. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini iko miradi mingi ya maji ya umwagiliaji katika Mkoa wangu wa Ruvuma ambayo haijakamilika ikiwemo miradi ambayo iko katika Vijiji vya Legeza Mwendo, Misiaje na Kitanda Wilayani Tunduru. Miradi hii ilitakiwa ikamilike kupitia mpango wa ASDP Awamu ya Kwanza, lakini mpaka leo haijakamilika kwa ukosefu wa fedha.
Je, ni nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha tunapeleka fedha za kukamilisha miradi hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze mama yangu Mheshimiwa Chikambo kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini kikubwa kama nilivyoeleza tumekuwa na miradi mingi ambayo haijakamalika, nasi kama Serikali tumeona haja ya haraka ya kuunda Tume.
Namwomba sana Mheshimiwa Mbunge, subira yavuta heri. Heri itapatikana pindi Tume itakapotuleta majibu ya haraka nasi tutaweza tukakamilisha. Ahsante sana.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini naomba niulize swali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo migogoro inayoendelea baina ya vijiji vyetu na hifadhi zetu, ikiwemo Hifadhi hiyo ya Selous ambayo muuliza swali ameizungumza, lakini pia ipo migogoro baina ya kijiji na kijiji, hii inapelekea wananchi wengi kukosa amani.
Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kumaliza migogoro hii katika nchi yetu ili wananchi waendelee kuishi kwa amani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kumekuwa na changamoto, kumekuwa na migogoro mbalimbali katika maeneo mbalimbali yanayopakana na hifadhi. Lakini naomba nitumie nafasi hii kumueleza Mheshimiwa Mbunge kwamba kuanzia mwaka wa fedha 2018/2019 yaani Julai, Wizara kwa kushirikiana na taasisi zetu za Hifadhi za Taifa tutahakikisha kwamba vijiji vyote vinavyozunguka maeneo ya hifadhi vinapimiwa na vinaondokana na matatizo ambayo yapo katika yale maeneo. Kwa sababu tumetenga fedha kwa ajili ya hiyo kazi kwa hiyo vijiji vyote vitapitiwa.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali maji ya Benki ya Dunia, viko vijiji ambavyo vilikuwepo kwenye mpango kikiwemo kijiji cha Nakapanya, Majimaji, Muwesi na Mchoteka. Vijiji hivi viliwekwa kwenye mpango na ilionyesha kwamba pesa yake ipo lakini majibu ya Serikali walisema kwamba vyanzo havijapatikana. Nini sasa kauli ya Serikali katika kuendelea kufanya utafiti ili wananchi wale wafaidike na huo mradi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana lakini nampongeze Mheshimiwa Mbunge, siyo mara yake ya kwanza kuulizia kuhusu suala zima la maji. Kama fedha zipo, namwomba sana Mhandisi wa Maji wa eneo hilo afanye kazi. Unapokuwa Mhandisi wa Maji, jukumu lako ni katika kuhakikisha wananchi wanapata maji. Sisi kama Wizara ya Maji tuko tayari hata kutoa watalaam wetu katika kuhakikisha wanatafuta vyanzo vya maji ili wananchi wake waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote kwanza napenda sana nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo ynanaleta matumaini kwetu na kwa wapiga kura wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015 kulitolewa ahadi na Mheshimiwa Makamu wa Rais ya kujenga barabara inayoanzia Wilaya ya Namtumbo - Lusewa – Mchoteka - Nalasi kwa kiwango cha lami. Ni nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha tunatekeleza ahadi hii kabla ya mwaka 2020 wakati wa uchaguzi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sikudhani Yassini Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitembelea maeneo haya nikitokea Nakapanya kuja Tunduru. Natambua pia ile kiu ya wananchi wa Tunduru ili kuweza kupita kwenye barabara hii kutoka Namtumbo - Lusewa - Nalasi lakini nia yao twende kuunganisha na wananchi wa Msumbiji. Najua katika Mto Ruvuma maeneo haya ya kutoka Nalasi tunahitaji kuwe na kivuko.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimhakikishie tu kwa ujumla wake kwamba barabara hii iko kwenye mpango na hata kwenye bajeti kuna kiasi cha fedha kimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara hii. Vilevile nimhakikishie pia tutakapokamilisha Daraja la Ruhuhu kile kivuko ambacho muda mwingi tumezungumza tutakipeleka eneo hili ili wananchi wa Nalasi na majirani zao waweze kuvuka kwenda Msumbiji. Ahsante sana.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Jeshi la Wananchi liliweka kambi katika Vijiji vya Wenje na Makande kwa ajili ya kuimarisha ulinzi katika mipaka yetu na kama inavyofahamika kwamba Wilaya ya Tunduru ni miongoni mwa Wilaya zilizoko mpakani mwa Msumbiji. Je, Serikali haioni sasa wakati umefika wa kurudisha kambi katika maeneo yale ili kuendeleza ulinzi kama ilivyokusudiwa awali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hivi karibuni Serikali imetangaza halmashauri ya mji katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru; kutangaza halmashauri ya mji ni wazi kwamba tunaongeza maeneo ya utawala. Kuongeza maeneo ya utawala ni wazi pia kwamba idadi ya watu inaongezeka. Je, nini sasa kauli ya Serikali katika kuandaa mpango huo rasmi wa kukabidhi maeneo yale ya Kitanda katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili wananchi sasa wapate kuyaendeleza maeneo yale? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa anafuatilia sana jambo hili. Niseme tu Mikoa ya Kusini ikiwemo Mtwara na Ruvuma, Kamati za Ulinzi na Usalama zilishafanya maombi ya uimarishwaji wa masuala ya kiulinzi mpakani. Kwa kuwa wamefanya maombi hayo, mawasiliano yanaendelea kufanyika kuona namna bora ya kuimarisha ulinzi huko mipakani. Jambo litakalokuwa limeamuliwa Kamati za Ulinzi na Usalama pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa kuwa wanafuatilia wataweza kujulishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili aliloliuliza, nisema tu kama ambavyo nimejibu kwenye jibu la msingi kwamba Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Jeshi la Wananchi watatuma timu ya wataalam. Wakishamaliza kufanyia vipimo kwa kushirikiana na halmashauri wataweka matumizi bora ya ardhi na kuweza kukidhi kile alichokisemea kuhusu ongezeko la watu pamoja na uwepo wa halmashauri ya mji.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo yamekuwa yakileta matumaini kwetu na kwa wapiga kura wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niulize swali. Wananchi wa Wilaya ya Nyasa waishio kando kando ya Ziwa Nyasa katika Vijiji vya Mkiri, Ngumbo na Ndumbi wana tatizo la kupata maji safi na salama. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wananchi wale wanapata maji safi na salama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri na nia njema ya wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa sisi kama Wizara yetu ya Maji tulishukuru Bunge lako Tukufu kwa kutuidhinishia fedha kiasi cha Sh.727,345,000,000; na utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha. Fedha hizi zipo nimwombe Mhandisi wa Maji ajipange sasa katika kuhakikisha wananchi wale wa vijiji ambavyo amevitaja Mheshimiwa Mbunge wanapata maji safi salama na yenye kutosheleza.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Wilaya ya Tunduru ni miongoni mwa wilaya kubwa ina kilometa za mraba 18,786 sawa na Mkoa wa Mtwara wenye wilaya sita. Je, Serikali haioni wakati sasa umefika wa kugawa wilaya hiyo kulingana na majimbo yaliyopo, kuna Jimbo la Tunduru Kusini na Jimbo la Tunduru Kaskazini maeneo hayo sasa yakapata wilaya? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpe taarifa tu kwamba Jimbo la Sikonge ambako mimi natoka lina kilometa za mraba 27,873 sasa yeye kilometa za mraba 18,786 anaweza akasubiri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape comfort wananchi wa Tunduru kwamba maeneo haya Serikali inafahamu kwamba ni makubwa, lakini kwa sasa hivi mzigo uliopo kwa Serikali ni kuhakikisha kwamba inaziwezesha wilaya mpya ambazo zimeanzishwa hivi karibuni, tuna wilaya kama sita ambazo zimeanzishwa hivi karibuni zipate majengo, vifaa vya uendeshaji, zipate watumishi, huo mzigo bado ni mkubwa sana na halmashauri mpya vilevile. Kwa hiyo, tukimaliza kuziwezesha hizi halmashauri mpya na wilaya mpya zikapata vifaa na majengo yakakamilika kabisa hapo ndiyo tutakuja kwa awamu nyingine sasa ya kuanzisha wilaya mpya na halmashauri mpya.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupunguza vifo vya akina mama wajawazito ni pamoja na uwepo wa vifaa vya kujifungulia katika hospitali zetu lakini mpaka hivi tunavyozungumza, ziko hospitali, zahanati na vituo vya afya akina mama wanatakiwa waende na mabeseni na mipira kwa ajili ya kujifungua. Ni lini tatizo hili litarekebishwa na Serikali yetu? Ahsante. (Makofi
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la dada yangu Mheshimiwa Sikudhani Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Ruvuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna changamoto ya vifaa mbalimbali lakini lazima tumshukuru Mheshimiwa Rais, tukumbuke hapa katikati aliweza kutoa vifaa kwa karibu Halmashauri zote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na uboreshaji wa vituo hivi vya afya 208 tunavyovijenga ambavyo jumla yake pamoja na vifaa itagharimu karibu shilingi bilioni 156, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote siyo muda mrefu sana vituo hivi vinavyokamilika, vifaa hivi tutavisambaza maeneo mbalimbali. Ni imani yangu kubwa kwamba tutapunguza kero kubwa sana katika suala zima la vifaa vya kujifungulia katika vituo vyetu vya afya na zahanati zetu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa Majibu mazuri. Pamoja na majibu yake, lakini naomba niulize swali la nyongeza. Katika kutekeleza mradi wa barabara kwa kiwango cha lami barabara ya Namtumbo - Tunduru – Tunduru – Mjini Nakapanya wananchi wale wamekuwa wakusubiri kulipwa fidia zao kwa muda mrefu. Je, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha wanalipwa na kuwaondolea adha hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chikambo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, mradi huu ulikopita wananchi walipwa fidia isipokuwa natambua tumezungumza na Mheshimiwa Chikambo, wapo wananchi wachache sana ambao walikuwa wana malalamiko yao, suala hili tunaendelea kulifuatialia, tukitatua tutawalipa hawa wachache kulingana na stahili zao.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na yenye kuleta matumaini kuhusiana na miradi hii ya umwagiliaji. Lakini pamoja na pongezi hizo mimi naomba niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, iko miradi ya kilimo cha umwagiliaji ambayo ilikuwa inaendelea katika Mkoa wetu wa Ruvuma ikiwemo mradi wa kilimo cha umwagiliaji uliopo Legezamwendo, Misyaje na baadhi ya vijiji vingine. Miradi hii imesimama kwa ajili ya kukosa pesa na nina uhakika tayari miradi hii ilishaanza. Kuendelea kuchelewa kupeleka pesa maana yake ni kuongeza gharama za mradi.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha tunapeleka pesa katika miradi hii ili kukamilisha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru, ni kweli kwamba kuna miradi mingi ambayo imeanza kujengwa na haijamalizika mpaka sasa na labda nilitaarifu Bunge lako rasmi; baada ya Tume hii ya Taifa ya Umwagiliaji kurudi Wizara ya Kilimo tuliweza kupita katika scheme karibuni zote nchini ili kuzingalia na namna gani na wataalam wetu na hiyo pia ndani ya Serikali kama mnakumbuka siku tatu zilizopita Mheshimiwa Waziri Mkuu amewasimamisha zaidi ya Wakurugenzi saba kwa ajili ya kupisha uchunguzi tufanye tathmini ya kina kuangalia matumizi ya fedha kwa sababu pesa zilikwenda nyingi, lakini matumizi yalikuwa ni mabovu sana.

Kwa hiyo siyo kila mradi ukikwama kumalizika ni kwa sababu kwamba pesa zilikosekana, lakini baada ya hiki chombo tulichounda sasa hivi, Tume tuliyounda sasa hivi kwenda kuchunguza mapungufu hayo ya ubora wa miradi, thamani ya miradi baadae tutakuja na taarifa rasmi na kujipanga namna gani tutakwenda kumaliza mradi huu.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza napenda nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo amekiri kwamba watoto wa mitaani wapo.

Mheshimiwa Spika, zipo sababu nyingi zinazosababisha uwepo wa wimbi kubwa la watoto wa mitaani ikiwemo na wazazi na hasa akinababa kutelekeza familia zao.

Je, Serikali inachukua hatua gani pindi inapowabaini wazazi wa aina hiyo, inawachukulia hatua gani katika kuhakikisha wanarudi katika familia zao na familia zinaimarika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali inatekeleza programu ya kuwaunganisha watoto na familia na kuwapa malezi mbadala na Waziri ameeleza kwamba programu hii inatekelezwa katika Mkoa wa Mwanza, tunayo mikoa 26; ni nini sasa mkakati wa Serikali wa kuhakikisha programu hii inafika katika mikoa mingine ikiwemo Mkoa wa Ruvuma ili wazazi na watoto waliopo katika maeneo yale wafaidike na programu hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuifanya, lakini kwa ufuatiliaji wa karibu sana kuhusiana na masuala ambayo yanahusiana na haki na ustawi wa watoto Tanzania. Nakupongeza sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa tumeona ongezeko la watoto ambao wanaishi na kuzurura mitaani na moja ya kisababishi ni hiyo sababu ambayo Mheshimiwa Mbunge ameisema, wazazi kutelekeza majukumu yao ya msingi ya kuwasimamia watoto hawa. Na ni kweli kwamba tuna Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 ambayo imetoa haki za msingi kwa mtoto. Na sisi Serikali kupitia Ustawi wa Jamii tumeendelea kuyashughulikia mashauri mbalimbali ya wazazi na hususan akinababa kutelekeza watoto na kuyapeleka Mahakamani kukazia hukumu.

Mheshimiwa Spika, tunatambua bado ipo changamoto ya wigo wa Maafisa Ustawi wa Jamii katika maeneo mbalimbali na sisi kama Serikali tunajaribu sana kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya Maafisa Ustawi wa Jamii katika maeneo mbalimbali. Lakini vilevile tunaendelea kutafakari kuhusiana na hizi adhabu ambazo tumeziweka, hususan pale ambapo mzazi kuna hukumu ya Mahakama, lakini wazazi wanaendelea kukaidi. Tunaangalia njia bora zaidi ya kuhakikisha kwamba zile adhabu zinawekewa msisitizo.

Mheshimiwa Spika, lakini katika swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuna hii programu ambayo tumeianzisha ya kuwaunganisha watoto na walezi ama walezi mbadala ama wazazi mbadala. Hii tumeianza katika ngazi ya majaribio tutakapoona mafanikio na matunda ya programu hii, hapo sasa ndio tutakapoanza kwenda katika maeneo mengine ya nchi hususan majiji ambayo tuna changamoto kubwa ya watoto wanaozurura mitaani.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nimesikia vigezo ambavyo vinatumika katika kutoa mikopo. Pia nafahamu katika maeneo yetu tunavyo vikundi vya wajasiriamali vikiwemo vikundi vya VICOBA na SACCOS. Swali la kwanza, je, Serikali ina mkakati gani wa kufikisha elimu hiyo kwa walengwa na hasa walioko vijijini ili kuwawezesha wana VICOBA na SACCOS kunufaika na mikopo hii ambayo inatolewa na Baraza la Uwezeshaji? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nimekuwa nikisikia kwamba kuna Baraza la Uwezeshaji wa Taifa, napenda kujua haya Mabaraza yapo na ngazi za Mkoa, Wilaya na hadi ngazi za Kata ili wana vikundi wale waweze kuyatambua na kupata mikopo kupitia Mabaraza hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sikudhani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Sikudhani kwa jinsi ambavyo ameendelea kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wanapata manufaa ya yale yanayotendeka ndani ya nchi yetu. Mheshimiwa Sikudhani ni Mbunge wa Viti Maalum lakini tunaona anatetea wananchi kwa ujumla wake. Mheshimiwa Sikudhani, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nije kwenye maswali yake mawili ya nyongeza, ameuliza ni njia zipi ambazo Serikali inazitumia kuhakikisha kwamba elimu hii ya uwepo wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ama fursa ambazo zinazopatikana ndani ya Taifa letu inawafikia wananchi wetu. Serikali siyo kwamba ina mikakati bali imekuwa ikifanya kwa kutumia media, tumekuwa tukitumia media mbalimbali kuhakikisha kwamba taarifa hizi za uwezeshaji wananchi kiuchumi zinawafikia wananchi. Sambasamba na hilo Serikali kila mwaka tumekuwa tukitumia maonyesho mbalimbali ambapo katika mwaka wa fedha uliopita 2018 maonyesho haya yalifanyika Mkoani Mbeya lakini pia mwaka huu wa fedha maonyesho haya mwezi Oktoba yatafanyika Mkoani Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa tukifanya makongamano pamoja na semina mbalimbali. Katika makongamano haya tumekuwa tukishirikiana na Wakuu wa Wilaya kwenye Wilaya mbalimbali. Kupitia makongamano haya, tumekuwa tukienda na hii Mifuko yetu na kutoa elimu kwa wananchi wetu na wale ambao wanakuwa tayari basi wanapata mikopo palepale wakati wa maonyesho hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati mwingine tulio nao ni kwamba umeandaliwa Mwongozo wa kuipima Mifuko hii ni kwa jinsi gani inafanya kazi. Kipimo kimojawapo ni kuangalia ni kwa jinsi gani imetoa fedha kwa wananchi wetu au ni kwa kiasi gani imefikia wananchi wetu. Kwa hiyo, mikakati tuliyo nayo ndani ya Serikali ni mingi na Mwongozo huu utazinduliwa hivi karibuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ameuliza Mabaraza haya yako katika ngazi zipi. Mabaraza haya yako kwenye ngazi za Halmashauri kupitia Waratibu. Tuna Waratibu mbalimbali ambao wanaratibu masuala haya ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza napenda kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri; lakini kama ilivyoelezwa kwenye swali la msingi kwamba kumekuwa na malalamiko mengi katika Vituo vyetu vya Polisi pale wananchi wetu wanapokwenda kuhudumiwa katika maeneo yale:

Sasa je, ni mkakati gani wa Serikali katika kuhakikisha siku zijazo kunafungwa CCTV Camera katika hayo maeneo ili kuleta ushahidi katika yale matukio wanayofanyiwa wananchi pale? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninafahamu kwamba Serikali ina dhamira ya dhati katika kuhakikisha Jeshi la Polisi linafanya vizuri, lakini kama litafanya vizuri bila kutunza kumbukumbu haitasaidia. Ni lini sasa mkakati wa Serikali katika kuhakikisha matukio yote yanakuwa katika kumbukumbu ili linapohitajika jambo lolote kwa mtuhumiwa yeyote linapatikana kwa urahisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Sikudhani Chikambo kwa maswali yake mazuri. Nimhakikishie kwamba kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, ni kwamba dhamira hiyo Serikali kupitia Jeshi la Polisi ya kufanya maboresho katika mfumo mzima wa TEHAMA ikiwemo maeneo mawili ambayo ameyazungumza ya mifumo ya CCTV na kumbukumbu kwa kutumia teknolojia ya kisasa, dhamira hiyo ipo na pale ambapo bajeti itaruhusu, basi sisi tutakamilisha huo mpango.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa Mikoa ambayo imekuwa ikijishughulisha na kilimo cha chakula na biashara na kwa kufanya hivyo, wakulima wengi wanahitaji kupata mbolea kwa ukaribu.

Pamoja na maelezo mazuri ambayo yametolewa na Naibu Waziri, naomba Serikali ione sasa wakati umefika wa kuondoa hizo tozo zote kwa hao wafanyabiashara ambao watakuwa wamekidhi vigezo ili kuwaruhusu sasa waende wakafungue maduka huko vijijini ambako ndiko waliko wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya Mawakala ambao siyo waaminifu, wamekuwa wakiuza mbolea kinyume na bei elekezi na hii inapelekea kuwafanya wakulima wetu kununua mbolea na pembejeo kwa gharama ya juu sana. Je, Serikali inakuja na kauli gani kwa Mawakala ambao wamekuwa wakiongeza bei za pembejeo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chikambo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la tozo, Wizara ya Kilimo sasa hivi inapitia upya tozo na gharama mbalimbali ambazo zinaweza kupunguza na kurahisisha shughuli za biashara katika sekta ya kilimo. Kwa kuwa Serikali inakuja na Blue print nataka nimuombe Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla, huo utakuwa ni wakati mzuri sana wakati tunafanya mapitio ya Sheria ya Kurahisisha Mazingira ya Kufanya Biashara kuweza sote kushauriana na kuja na mwelekeo sahihi. Hata hivyo, katika mwaka wa fedha unaokuja, zipo baadhi ya tozo ambazo tutazileta Bungeni kwa ajili ya kuomba namna ya kuweza kuzibadilisha na kurahisisha mazingira ya kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la wafanyabiashara wasio waaminifu, nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa hatua alizochukua za kupita katika maduka na kuwakamata wafanyabiashara ambao wanakwenda kinyume na maelekezo ya Serikali. Kumekuwa na tatizo la wafanyabiashara wa viuatilifu na mbolea, kuhusu suala la bei elekezi, tumeagiza kwamba yeyote anayekwenda kinyume na maelekezo ya Serikali katika kuuza mbolea tofauti na bei elekezi, viongozi walioko katika ngazi za Wilaya na Mikoa waweze kuwakamata na kuwachukulia hatua na kuwapeleka katika vyombo vya Sheria kwa sababu hiyo itakuwa ni dhuluma na wizi kwa wakulima na ni jambo ambalo kama Serikali hatuwezi kuliruhusu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo, tunaendelea kusisitiza wafanyabiashara wote walioko katika sekta ya kilimo wanaouza mbolea na pembejeo na mbegu ambao wamekuwa siyo waaminifu kwa kuuza mbegu feki, kwa kutoa viuatilifu feki, Serikali inafuatilia kwa karibu. Tunatumia nafasi kuwaomba Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanakagua na nawataka wananchi wanaponunua wahakikishe wanaomba risiti ili watakapokutana na tatizo iwe rahisi sisi Serikali kuweza kuchukua hatua na kuwafuatilia na kuwapeleka katika vyombo vya sheria.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri na kazi nzuri ambayo inafanyika na Wizara hii. Pamoja na pongezi hizo naomba niulize swali la nyongeza, yako maeneo mpaka hivi tunavyozungumza yana tatizo la usikivu kwa upande wa TBC, yakiwemo maeneo ya Nyasa kule mipakani, baadhi ya maeneo katika halmashauri ya Wilaya ya Tunduru na hasa yale ya mipakani, badala ya kuwa na usikivu mzuri wa TBC sasa wanasikiliza redio za nje kama kule Nyasa.

Je, Serikali ina mkakati gani kupitia Wizara kuhakikisha maeneo yote sasa yanakuwa na usikivu mzuri ili wananchi waweze kuitumia fursa hii kupitia Shirika la TBC, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa maswali yake mazuri ya nyongeza, lakini kama ambavyo amezungumza sisi kama wizara tunatambua ni kweli kwamba tatizo la usikivu kwa baadhi imekuwa ni changamoto. Lakini Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kwamba kwa kipindi cha hii miaka minne ya utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Tano kazi kubwa sana imefanyika katika kuhakikisha kwamba tunaboresha masuala ya usikivu wa TBC katika nchi nzima ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tumeweza kufikia Wilaya 102, lakini wakati Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani tulikuwa tuna Wilaya 52 tu ambazo zilikuwa zinapata usikivu wa TBC. Lakini malengo ambayo tunayo kwa mwaka huu 2019/2020 kwa bajeti ambayo tayari tumeshaipitisha ni kuhakikisha ya kwamba tunaongeza Wilaya 15 kwa maana utoke Wilaya 102 tuweze kuwa na usikivu katika Wilaya 117.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie fursa hii kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge pamoja na watanzania nzima kwamba sisi kama Serikali tumejipanga katika kuhakikisha kwamba tatizo la usikivu wa TBC katika nchi nzima ya Tanzania linaboreshwa na niwahakikishie kwamba kwa sasa hivi TBC iko vizuri na tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa sababu imekuwa ikiongeza bajeti kila mwaka lakini lengo kuhakikisha ya kwamba tunaboresha usikivu TBC, ahsante.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri lakini pamoja na pongezi hizi naomba niulize maswali madogo mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni mkakati gani ambao umewekwa na Serikali wa kuwawezesha vijana kupata mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kujiajiri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tumekuwa tukishuhudia vijana wengi wanajishughulisha na shughuli za kilimo. Je, Serikali haioni kwamba iko haja sasa ya kuona wale vijana ambao wanajishughulisha na shughuli za kilimo waweze kupata mafunzo na kwa kuwa tunafahamu kilimo ni uti wa mgongo ili waweze kufanya kazi zao kwa umakini na waweze kupata tija? Ahsate.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Sikudhani Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nichukue fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo anafuatilia masuala ya vijana na akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la mkakati, ni kweli kwa kutambua kwamba ujasiriamali hivi sasa ni nguzo muhimu ya kumfanya kijana aweze kujiajiri, hivi sasa tumeshatambulisha mtaala wa ujasiriamali kuanzia ngazi ya chini mpaka elimu ya vyuo vikuu. Pia mkakati wa Serikali hivi sasa ni kuendelea kuwapitia wajasiriamali wote nchi nzima kwa kuwapa mafunzo katika kila Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, navyozungumza hivi sasa tumeshakamilisha mikoa zaidi ya 14 katika awamu ya kwanza na tutakwenda kumalizia awamu ya pili ambapo kila mkoa tumekutana na wajasiriamali zaidi ya 500 katika kuwapa elimu na ujuzi wa namna ya kuweza kufanya biashara zao.

Kwa hiyo, Serikali inatambua umuhimu huo wa wajasiriamali na ndiyo maana katika moja ya mkakati wetu ni kuwapa elimu na kuwasaidia pia kuweza kupata mikopo ya masharti nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu vijana kushiriki kwenye kilimo, Ofisi ya Waziri kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo tunao mkakati maalum wa kuwahusisha vijana katika kilimo ambao tumeanza kuutekeleza. Navyozungumza hivi sasa tunayo programu ya kilimo cha kitalu nyumba ambacho kitawafikia vijana 18,800 nchi nzima ambako kila Halmashauri nchi nzima vijana 100 watafundishwa kuhusu kilimo cha kitalu nyumba na vijana 20 watapata ujuzi wa kuweza kufundishwa kutengeneza green house. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba vijana wengi wa Kitanzania wanashiriki moja kwa moja katika uchumi wa viwanda kupitia sekta hii ya kilimo. Lengo letu ni kuwafikia vijana 47,000 katika mwaka huu wa fedha.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa moja ya majukumu ya Bodi ya Korosho ni kufanya biashara na kusimamia ubora wa korosho. Katika msimu wa 2018/2019 jukumu la kufanya biashara ya korosho lilifanyika na Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Je, Serikali imejipangaje katika kuhakikisha msimu wa 2019/2020 jukumu hili linafanywa na Bodi ya Korosho?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika msimu wa 2017/2018 Bodi ya Korosho iliingia Mkataba na vikundi mbalimbali kuzalisha miche ya korosho na kupitia Bodi ya Korosho walifanya mikataba na vile vikundi. Mpaka hivi ninaposimama hapa, baadhi ya vikundi havijalipwa fedha zao. Je, ni lini sasa Serikali itawalipa wanavikundi wale ambao walizalisha miche ya korosho na miche ilisambazwa katika mikoa mbalimbali ili wapate fedha zao kama sehemu ya wajasiriamali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, swali lake la kwanza anataka kujua kwamba jukumu mojawapo la Bodi ya Korosho ni kutaka kufanya biashara ya korosho. Nataka nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya kuwatetea wakulima wa korosho hususan watu wa Tunduru na Mkoa mzima wa Ruvuma na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu lake hili, kwanza nimwambie kwamba majukumu yake kama kwenye jibu langu la msingi nilivyosema hayajaondolewa kwenye Bodi ya Korosho kwa sababu bodi hizi zina majukumu mawili tofauti. Jukumu la kufanya biashara ni jukumu la Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ambalo sasa anaponunua korosho ni jukumu lao la kimsingi la kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Bodi ya Korosho ni kusimamia, ni waratibu, ni uratibu wa kusimamia biashara ya korosho na hili jukumu wanaendelea nalo kwamba wale waliobaki ambao menejimenti inaendelea kuratibu na mpaka sasa hivi inaratibu katika ubora wa biashara ya korosho pamoja na biashara nzima ya korosho na maandalizi ya msimu ujao wa korosho.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, anataka kufahamu kwamba ni kweli kwamba mwaka 2017, sisi kama Serikali tuko katika programu ya kuendeleza zao la korosho ya miaka mitatu ya kuzalisha miche milioni 10 na kuigawa kwa mikoa mbalimbali inayolima korosho. Ni kweli Serikali tuliingia mkataba kupitia halmashauri mbalimbali na vikundi mbalimbali kwa ajili ya uzalishaji huo wa miche na mpaka sasa kuna baadhi ya mikoa sita tumeshalipa. Baadhi ya mikoa mingine ipo kwa sababu kwamba ulipaji huu utalipwa baada ya kufanya uhakiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ile mikoa yote ambayo imelipwa, ile mikoa imemaliza uhakika na hii mikoa ambayo bado haijalipwa itamaliza uhakiki haraka iwezekanavyo ili kuweza kuwalipa kuendeleza zao letu la korosho.