Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Sikudhani Yasini Chikambo (13 total)

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Tunduru inayohudumia majimbo mawili ina tatizo la gari kubebea wagonjwa ambapo gari lililopo ni moja na linaharibika mara kwa mara.
Je, ni lini Serikali itapeleka gari jipya katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassini Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imetenga shilingi milioni 141 kutokana na mapato ya ndani ili kununua gari la wagonjwa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Tunduru. Vilevile katika mwaka huo zimeombewa shilingi milioni 300 kupitia maombi maalum ili kununua magari mawili kwa ajili ya vituo vya afya, ili kuboresha mfumo wa rufaa kwa wagonjwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha magari hayo yanapatikana kwa ajili ya huduma za afya.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-
Miradi ya Maji ya Benki ya Dunia nchini imekuwa ikisuasua sana na hata ile iliyokamilika maji yamekuwa yakitoka wakati wa mvua tu.
Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi inayosuasua ikiwemo ile ya Wilaya ya Tunduru?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassini Chikambo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza programu ya maendeleo ya sekta ya maji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo. Kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi katika Jimbo la Tunduru kama ilivyo pia katika maeneo mengine nchini ilitokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha pamoja na kutopatikana kwa vyanzo vya maji vya uhakika katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Spika, katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Programu ya Maendeleo Sekta ya Maji, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ilipanga kutekeleza jumla ya miradi kumi na moja, kati ya hiyo, miradi minne ya vijiji vya Nandembo, Nalasi, Lukumbule na Amani ujenzi wake unaendelea na miradi minne katika vijiji vya Majimaji, Muhuwesi, Nakapanya na Mchoteka haikupata vyanzo. Aidha, mradi wa Mbesa umesimama baada ya Halmashauri kuvunja mkataba wa mkandarasi kutokana na kutokishi taratibu za kimkataba na tayari taratibu zinaendelea kumpata mkandarasi mwingine.
Mheshimiwa Spika, miradi yote ambayo haikupata vyanzo itapewa kipaumbele katika Awamu ya Pili ya utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji iliyoanza mwezi Januari, 2016.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika, mwezi Agosti, 2016 Wizara imetuma kiasi cha shilingi milioni 147.4 kwa Halmashauri ya Tunduru na Serikali itaendelea kutuma fedha kwa kadri zitakavyopatikana. Upungufu wa maji kwenye miradi iliyokamilika hususan wakati wa kiangazi umesababishwa na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu. Wizara inashauri tuendelee kuihamasisha jamii katika uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia nyumba za makazi Askari Polisi na Magereza katika Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma?
(b) Je, Serikali imejipangaje kufanya ukarabati kwa nyumba za askari zilizopo Wilayani Tunduru ambazo kwa muda mrefu hazijafanyiwa ukarabati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa nyumba za makazi, maafisa na askari, Serikali imeendelea na utekelezaji wa mpango wa kujenga nyumba mpya kwenye baadhi ya magereza nchini kwa kutumia fedha zinazotengwa katika fungu la bajeti ya maendeleo kila mwaka. Kwa kutambua uhaba na uchakavu wa nyumba za Askari Polisi na Magereza, Serikali ina mpango wa kuwajengea askari nyumba 9,500 nchi nzima ikiwemo kwenye Gereza la Wilaya ya Tunduru pamoja na nyumba 4,136 kwa upande wa polisi, ikijumuisha Wilaya ya Tunduru.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo la uchakavu wa nyumba za makazi za maafisa na askari, Serikali itaendelea kuzifanyia ukarabati nyumba za Askari Magereza na Polisi nchini zikiwemo za Wilaya ya Tunduru kwa kutenga bajeti ya ukarabati kwa kila mwaka wa fedha kutegemeana na bajeti itakavyoruhusu.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo la uagizaji wa dawa za kilimo na mifugo ndani ya nchi zisizokidhi vigezo na bei ya dawa hizo zinaongezeka siku hadi siku na kufanya wakulima na wafugaji wadogo kukosa maendeleo.
(a)Je, Serikali inachukua hatua gani za kuhakiki dawa hizo kabla hazijaingia nchini?
(b) Je, Serikali ina utaratibu gani wa kudhibiti bei hizo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, lenye sehemu a na b kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, udhibiti wa ubora na usalama wa dawa na viwatilivu vinavyoingia nchini na ambavyo vipo katika soko unafanywa na Mamlaka mbalimbali za Serikali kama vile Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwa upande wa dawa za mifugo na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kitropiki (TFRI) kwa upande wa viuatilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza jukumu hili Mamlaka hizo zina mifumo ya udhibiti katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, usajili wa dawa zinazoingia nchini; dawa zote na viuatilifu vinavyoingia nchini zinatakiwa kwanza ziwe zimesajiliwa na mamlaka hizo ili kujihakikishia ubora, usalama na ufanisi kabla hazijaingia katika soko la Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wa viwanda vinavyotengeneza dawa; ukaguzi huu hufanywa na mamlaka hizo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa vinazingatia viwango vya uzalishaji bora wa dawa (good manufacturing practice).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wa kufuatilia dawa katika soko (post marketing surveillance) hufanyika ili kuhakikisha kuwa dawa zilizopo katika soko zinaendelea kuwa na ubora ule ule kama wakati ziliposajiliwa. Sampuli mbalimbali za dawa huwa zinachuliwa katika soko na kupelekwa maabara kwa ajili ya kuzipima kwa minajili ya kudhibiti na kuthibitisha ubora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa bei za dawa na viuatilifu zinapangwa na nguvu ya soko lakini Serikali imeondoa ushuru wa forodha na VAT ili kumpunguzia mkulima mzigo wa bei. Aidha, Serikali inaendelea kuzipitia tozo na ada mbalimbali katika sekta ya kilimo na ikionekana inafaa ziondolewe ili kuongeza unafuu kwa mkulima.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-
Ukosefu wa nyumba za walimu maeneo ya vijijini husababisha walimu kuhama maeneo hayo na hivyo kupelekea upungufu mkubwa wa walimu. Aidha, Halmashauri nyingi zikiwemo za Mkoa wa Ruvuma hazina uwezo wa kujenga nyumba za walimu kwa kutumia fedha za ndani.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga nyumba za walimu wa shule za msingi vijijini ili kuweka mazingira rafiki ya kufanyia kazi kwa walimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa upo upungufu wa nyumba za walimu nchini. Nyumba zilizopo kwa ajili ya walimu wa shule za msingi ni 41,321 wakati mahitaji halisi ni nyumba 222,115 hivyo kuna upungufu wa vyumba 179,794 sawa na asilimia 81. Mkoa wa Ruvuma una upungufu wa nyumba 5,470 za walimu wa shule za msingi.
Mheshmiwa Naibu Spika, Seriakli ina mikakati mbalimbali ya kuboresha utoaji wa elimu Nchini ikiwemo kutenga fedha za ujenzi wa nyumba za walimu. Kwa mwka wa fedha 2017/18 Seriakli imetenga jumla ya shilingi bilioni
• kwa ajili ya uejzi wa nyumba 1,669 za walimu wa shule za msingi nchini. Mkoa wa Ruvuma umetengewa shilingi milioni 470 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 30 za walimu wa shule za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuendelea kujenga nyumba za walimu kadri fedha zinavyopatikana kwa lengo la kuboresha mazingira na makazi kwa walimu. Ujenzi wa nyumba za walimu ni jukumu la wadau wote kuanzia Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, wananchi kwa ujumla, hivyo natoa wito kwa wadau wote walimu kuchangia ujenzi wa nyumba za walimu.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuanzisha miradi ya maji mikubwa na midogo na mingine imekabidhiwa kwa wananchi lakini haitoi maji.
Je, Serikali inaweza kueleza ni miradi ipi ya maji mikubwa na midogo iliyokamilika na isiyokamilika katika Mkoa wa Ruvuma na Wilaya zake zote?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naomba Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassini Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Ruvuma una jumla ya Halmashauri nane ambapo katika utekelezaji wa Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Serikali imetekeleza miradi katika vijiji 230 kwa Mkoa wote wa Ruvuma ambapo miradi katika vijiji 94 imekamilika na inatoa huduma ya maji. Miradi mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji katika Halmashauri zote za mkoa huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Mkoa wa Ruvuma umetengewa kiasi cha shilingi bilioni 18.44 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi, ukarabati, usanifu, usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maji.
Aidha, Serikali itaendelea kutatua tatizo la maji safi na salama kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuibua miradi mipya kwa kubaini vyanzo vya maji na kujenga miundombinu ya maji katika Wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma sambamba na mikoa mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa maji mijini, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetekeleza miradi ya uboreshaji wa huduma ya maji katika Miji ya Songea, Namtumbo, Mbinga na Tunduru. Hadi kufikia mwezi Machi, 2018 miradi hiyo imekamilika kwa wastani wa asilimia 97 na imegharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.6. (Makofi)
MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO (K.n.y. MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO) aliuliza:-
Kuna upungufu wa magari katika Vituo vya Polisi Mkoa wa Ruvuma. Yaliyopo sasa ni mabovu kabisa na hayafanyiwi matengenezo kutokana na ukosefu wa fedha.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka magari kwenye vituo hivyo?
(b) Je, ni lini Serikali itapeleka pesa kwenye vituo hivyo kwa ajili ya matengenezo ya magari na mafuta ya magari hayo ili polisi waweze kufanya kazi zao kwa wakati?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassini Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, kama lilivyoulizwa kwa niaba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Ruvuma una jumla ya magari 33 na kati ya hayo magari 24 ni mazima yanafanya kazi na magari tisa ndiyo mabovu. Aidha, Jeshi la Polisi hufanya mgao wa magari katika mikoa na vikosi kwa kuzingatia vigezo mbalimbali kama kiwango cha uhalifu katika eneo husika, hali ya jiografia, idadi ya watu na mahitaji ya kiutawala ambapo katika mwaka 2015 Mkoa wa Ruvuma ulipokea magari 11. Hivyo, mpango wa kupeleka magari katika Mkoa wa Ruvuma utategemea upatikanaji wa magari mapya na mahitaji kulingana na vigezo vilivyoainishwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitenga na kupeleka mgao wa fedha katika Jeshi la Polisi kila mwezi ambapo fedha hizi hugaiwa na kupelekwa mikoani kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya jeshi ikiwemo operation, matengenezo ya magari na mafuta kwenye vituo vya polisi. Aidha, utaratibu ulipo sasa kila Mkoa unapelekewa fedha kwa ajili ya matengenezo na mafuta kila mwezi kupitia kasima ya mikoa. Ni kweli kuwa magari mengi kwa sasa yamekuwa ni ya muda mrefu hivyo huhitaji matengenezo ya mara kwa mara ambapo Jeshi la Polisi linahitaji kufanya matengezo kwa magari yanayoharibika kwa kutumia fedha zinazopelekwa na kuwashirika wadau wa ulinzi na usalama katika maeneo husika.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-
Baadhi ya Mahakama za Mwanzo kama vile Matemanga, Napakanya na nyingine nyingi ni chakavu na hazipati fedha kwa ajili ya ukarabati hali inayosababisha Mahakimu na watumishi wengine kufanya kazi katika mazingira magumu sana:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa Mahakama hizo?
NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mbunge kuwa kwa baadhi ya maeneo watumishi wetu wanafanya kazi katika mazingira magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tunduru ina jumla ya Mahakama za Mwanzo tisa ambazo karibu zote majengo yake ni ya zamani sana na mengi yakiwa ni yale yalioachwa na mkoloni. Kati ya Mahakama za Mwanzo tisa zilizopo, majengo ambayo angalau yana hali nzuri ni matatu tu, ya Nandembo, Mlingoti na Ndesa. Mengine yaliyosalia yakiwemo ya Matemanga na Nakapanya ni chakavu sana, hayafai kukarabati na hivyo yamepangwa kujengwa upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa ujenzi wa mahakama, Mahakama ya Mwanzo Nakapanya na Mahakama ya Wilaya ya Tunduru zimepangwa kujengwa mwaka 2019/2020 kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-
Katika Wilayani Tunduru kulikuwa na Kambi ya Jeshi ambayo pamoja na mambo mengine ilishughulika na ulinzi katika Vijiji vya Wenje na Makande vilivyopo mpakani na Nchi ya Msumbiji:-
i. Je, Serikali halioni haja ya kurudisha Kambi hiyo ya Jeshi Wilayani Tunduru?
ii. Kambi iliyokuwepo ilikuwa na hekta za ardhi zisizopungua 18,000, je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza maeneo hayo ambayo sasa yamekuwa vichaka?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Wziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Chikambo kama ifautavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Ulinzi wananchi wa Tanzania liliweka kituo cha ulinzi cha Kombania ya sita ya 691 kikosi cha Jeshi (06/691 KJ) katika eneo la Chitanda, Wilayani Tunduru. Kutokana na sababu ambazo zilikuwa za msingi kwa wakati huo kituo hicho kilifungwa na eneo hilo likarudishwa rasmi kwa uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Tunduru mwaka 1998. Aidha, mwaka 2006 eneo hilo liliombwa upya na JWTZ kwa uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya kuendelea kulitumia katika kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu katika eneo hilo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na Makao Makuu ya Jeshi linaandaa mpango kwa kutumia wataalam wake kuwatuma kwenda Wilayani Tunduru kwa kushirikiana na uongozi wa Wilaya ya Tunduru kutathmini na kulipima upya eneo hilo na kulifanyia mchakato wa kulimiliki kwa misingi ya sheria za ardhi zilizopo.
MHE. DAIMU I. MPAKATE (K.n.y. MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO) aliuliza:-

Idadi ya watu nchini inazidi kuongezeka sambamba na ongezeko la mahitaji ya ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji ili kuendeleza shughuli zao kwa tija na kuwaondolea adha wanazozipata?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu ufugaji bora na uzalishaji wa malisho kupitia mashamba darasa ili kuwajengea uwezo wa kufuga kwa tija pamoja na kuendeleza malisho katika maeneo yaliyotengwa. Lengo la kutoa elimu hii ni kuhakikisha wafugaji wanaachana na ufugaji wa kuhamahama na kutulia kwenye eneo moja lenye malisho yaliyoboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya mashamba darasa 265 yameanzishwa katika Halmashauri mbalimbali nchini ambapo wafugaji wanaweza kujifunza jinsi ya kuzalisha mbegu na malisho bora ya mifugo ili kuongeza upatikanaji wa uhakika wa mbegu na malisho ya mifugo. Aidha, katika mwaka wa 2018/2019, Serikali imeongeza hekta 2,500 katika mashamba yake kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu za malisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imepanga kutoa mafunzo rejea kwa wafugaji na Maafisa Ugani nchi nzima juu ya ufugaji bora unaozingatia ukubwa wa ardhi iliyopo. Mafunzo hayo tayari yameanza kutolewa katika Halmashauri ya Simanjiro, Mkoani Manyara na Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, Mkoani Tabora na kuendelea kutolewa kwa awamu katika Halmashauri zote nchini. Aidha, Serikali imeendelea na juhudi za kuwasaidia wafugaji kukabiliana na tatizo la maji kwa ajili ya mifugo kwa kuchimba malambo 1,381 na visima virefu 103 katika Halmashauri mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Mawaziri nane iliyoundwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kutafuta suluhu ya migogoro ya matumizi ya ardhi iliyoko nchini tunaamini itakuja na mapendekezo chanya ambayo yatapelekea kuondoa migogoro na adha zinazowakabili wafugaji na wakulima nchini.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-

Kumekuwa na wimbi kubwa la watoto wa mtaani ambao wanaishi katika mazingira magumu.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia watoto hao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, Mbunge Viti Maalum kutoka Mkoa wa Ruvuma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na wimbi kubwa la watoto wa mitaani ambao wanaishi katika mazingira magumu. Katika kipindi cha Januari hadi Disemba, 2019 jumla ya watoto 36,548 wakiwemo watoto wa kiume 17,894 na wa kike 18,654 walitambuliwa. Kati ya hao jumla ya watoto 1,178 walipatiwa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za afya, msaada wa kisaikolojia na jamii, msaada wa kisheria, kuunganishwa na familia zao na kuwapatia elimu ya ujasiriamali.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mpango wa kuwaunganisha watoto na familia na kuwatafutia malezi mbadala wale wasio na familia katika Mkoa wa Mwanza. Programu hii imeanza kutekelezwa mwezi Novemba, 2019 na inatarajiwa kufika mikoa yote ambayo ina wimbi kubwa la watoto wanaoishi mitaani.

Mheshimiwa Spika, mwisho nichukue nafasi hii kuikumbusha jamii kuwa jukumu la matunzo, malezi, ulinzi na usalama wa mtoto ni la familia na jamii kwa ujumla. Vilevile Mamlaka ya Serikali za Mitaa zinapaswa kusimamia Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 ili kuwawajibisha wazazi wanaotelekeza majukumu yao na badala yake wanawaacha watoto kuzurura mitaani.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuza:-

Serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa wafanyabiasha kupitia Baraza la Uwezeshaji:-

(a) Je, ni vigezo vipi vinatumika katika kutoa mikopo hiyo?

(b) Je, ni wafanyabiashara wangapi ambao wamenufaika na mikopo hiyo Mkoani Ruvuma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua tatizo kubwa la mitaji linalowakabili wananchi wa Tanzania na hasa wajasiriamali, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ilisaini makubaliano maalum na Benki ya TPB na Taasisi ya UTT Microfinance kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali. Chini ya makubaliano hayo, miongoni mwa vigezo vya msingi vilivyopaswa kuzingatiwa na waombaji ni kama ifuatavyo:-

(i) Wafanyabiashara wanapaswa kujiunga katika vikundi vya VICOBA au SACCOS kwa ajili ya kupeleka maombi yao ya mikopo;

(ii) Kikundi kinapaswa kuwa na usajili, Katiba na Sera za uendeshaji wa kikundi; na

(iii) Kikundi kinapaswa kuwa na Ofisi inayotambulika, uongozi, mfumo mzuri wa utunzaji wa kumbukumbu za kihasibu na akaunti ya benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi yanayokidhi vigezo husika hupelekwa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa ajili ya kuombewa dhamana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Agosti, 2016, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lilidhamini mikopo yenye thamani ya Sh.542,844,500 ambapo jumla ya wajasiriamali 729 wamenufaika na mikopo hiyo Mkoani Ruvuma kupitia Benki ya TPB. Aidha, Baraza lilidhamini pia mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa SACCOS mbalimbali mkoani humo kupitia Benki ya CRDB. Hata hivyo, Baraza limedhamini wajasiriamali katika mikoa mingine pia ndani ya nchi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Juni, 2019 kiasi kilichorejeshwa na wajasiriamali waliokopeshwa kwa dhamana kupitia Benki ya TPB ni Sh.430,292,635.60 sawa na asilimia 79.3. Hivyo, natoa wito kwa wakopaji waliosalia, kukamilisha marejesho ya mikopo yao ili Baraza liweze kuwahudumia wafanyabiashara ama wajasiriamali wengine wenye uhitaji.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-

Serikali ilivunja Bodi ya Korosho na majukumu yake sasa yanatekelezwa na Bodi ya Mazao mchanganyiko:-

Je, ni lini Serikali itachukua hatua ya kuunda tena Bodi ya Korosho na kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kama ilivyo kwa mazao mengine?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassini Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Korosho Tanzania imeanzishwa chini ya Kifungu cha 3(1) cha Sheria ya Tasnia ya Korosho Na. 18 ya Mwaka 2009. Majukumu ya Bodi ya Korosho ni kusimamia na kuratibu uendeshaji wa tasnia ya korosho nchini ikiwa ni pamoja na uzalishaji, usindikaji na biashara ya korosho. Aidha, Serikali kupitia Waziri wa Kilimo kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya Tasnia ya Korosho kutoa maelekezo na mwongozo maalum kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa tasnia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alitengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Korosho na kuivunja Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi tarehe 10 Novemba, 2018 kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa Bodi aliondolewa katika nafasi yake tarehe 26 Oktoba, 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, si kweli kwamba Serikali ilivunja Bodi ya Korosho na majukumu yake kutekelezwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko. Bodi ya Nafaka ilianzishwa kwa Sheria Na. 19 ya Mwaka 2009 na inaendelea kutekeleza majukumu yake ya Kisheria ambayo ni pamoja na kufanya biashara ya kununua na kuuza nafaka na mazao mengine ndani na nje ya nchi ambapo imepewa jukumu maalum la kununua korosho. Mnamo tarehe 15 Aprili, 2019 Waziri wa Kilimo alimteua Kaimu Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Korosho na Wajumbe wa Bodi nane (8) wameshateuliwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Bodi hiyo, inakamilisha muundo wake baada ya Mwenyekiti wake kuteuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakamilisha kuunda upya Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania. Uteuzi wa Wajumbe utatangazwa na Mamlaka za uteuzi muda mfupi ujao kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni zilizopo.