Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Shally Josepha Raymond (19 total)

MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Ushirika hususani wa mazao hauna maendeleo mazuri na umekuwa ukisuasua kwa sababu mbalimbali.
(a) Je, ni vigezo gani vinatumika kupima na kutathmini maendeleo ya ushirika?
(b) Je, ni hatua zipi zinachukuliwa na Serikali kuboresha mazingira ya ushirika kukua?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kupima na kutathmini maendeleo ya ushirika nchini, Serikali inatumia vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ongezeko la idadi ya Vyama vya Ushirika vinavyoandikishwa na idadi ya wanachama kwenye vyama hivyo; idadi ya wananchi wanaopata huduma za kijamii na kiuchumi kupitia Vyama vya Ushirika nchini; uzalishaji na mauzo kupitia Vyama vya Ushirika; mitaji ya Vyama vya Ushirika na Vyama vya Ushirika vinavyouza mazao yaliyoongezwa thamani.
Pia uwekezaji wa Vyama vya Ushirika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii mfano, huduma za kifedha, shule na majengo ya vitega uchumi; ajira kupitia Vyama vya Ushirika pamoja na thamani na idadi ya mikopo inayotolewa kwa wananchama wake katika kutatua matatizo ya kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vingine ni pamoja na kupima ufanisi wa uendeshaji wa shughuli za Vyama vya Ushirika kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Vyama vya Ushirika ikiwemo kupitia Ukaguzi wa mara kwa mara wa nje (external audit) kila mwaka.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha mazingira ya ukuaji wa sekta ya ushirika nchini. Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini kwa lengo la kuijengea uwezo wa kiutendaji ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya Maafisa Ushirika katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya na kuendeleza kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu watendaji wa Serikali, Wajumbe wa Bodi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika kwa kushindwa kusimamia sheria katika kutekelza majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine zinazochukuliwa ni pamoja na kutoa elimu na kuendelea kuboresha mifumo ya masoko hususan wa Stakabadhi Ghalani; kuendelea kuviwezesha Vyama vya Ushirika kuzitambua kwa kuzihakiki mali zao na kuweka mikakati ya kuziendeleza mali hizo kwa manufaa ya wanachama; kuimarisha usimamizi na ukaguzi katika Vyama vya Ushirika kuzitambua kwa kuzihakiki mali zao na kuweka miakkati ya kuziendeleza mali hizo kwa manufaa ya wanachama; kuimarisha usimamizi na ukaguzi katika Vyama vya Ushirika.
Pia kuwajengea uwezo wanachama; kusimamia upatikanaji wa viongozi waadilifu na wawajibikaji wanaozingatia madili na misingi ya ushirika na pia kushirikisha Wizara za Kisekta na wadau mbalimbali katika kuhamasisha na kuendele za ushirika.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Kuna miundombinu ya kusambaza maji safi na salama iliyokamilika lakini inatoa huduma chini ya kiwango cha ujenzi wake (below design and built capacity).
(a) Je, ni miradi mingapi ya maji safi na salama inayotoa huduma chini ya uwezo wa usanifu na ujenzi wake kutokana na vyanzo kupungua au kukauka maji?
(b) Je, ni hatua zipi zinachukuliwa kuepusha miradi mingine kukumbwa na matatizo kama hayo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, miradi iliyosanifiwa na kujengwa inaweza kutoa huduma ya maji chini ya kiwango kutokana an sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa miundombinu iliyojengwa, ongezeko la matumizi, uharibifu wa miundombinu, kupungua au kukauka kwa vyanzo vya maji kunakoweza kusababishwa na uharibifu wa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabia nchi. Kwa takwimu hivi sasa jumla ya miradi 114 nchini kote imebainika kutoa huduma ya maji chini ya kiwango tofauti na ilivyosanifiwa.
Mheshimiwa Spika, ili kuepusha miradi mingine kukumbwa na matatizo kama hayo, Wizara imeandaa na inatekeleza mkakati wa kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji wa mwaka 2014 na mpango wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi wa mwaka 2013 ili kuhakikisha vyanzo vya maji vinakuwa endelevu.
Mpango huo unatekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa kutoa elimu kwa wananchi ambao wananchi wanahamasishwa kutokufanya shughuli za kibinadamu katika umbali usiopungua mita 60 kutoka kwenye mito na vijito na mita 500 kutoka kwenye bwawa na kuondoa watu wote wanaofanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya vyanzo vya maji na maeneo oevu kwa maeneo hayo kupandwa miti rafiki kwa ajili ya kurejesha uoto wa asili.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Halmashauri zina wataalam wa kusimamia na kutekeleza mipango yao na zina uwezo kisheria kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo, elimu, afya, maji kilimo na ardhi pasipo kuingiliwa. Viongozi na Watendaji wa Serikali ngazi za Mkoa na Wilaya huambiwa watawajibishwa kufikia malengo mathalani, katika ujenzi wa maabara, madarasa na kutengeneza madawati:-
Je, mipaka ipi ni ya kinadharia (theoretical) na ipi inatekeleza (practical) kiutendaji na uwajibikaji kati ya viongozi wa Serikali Kuu na Halmashauri za Majiji, Miji na Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Joseph Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ugatuzi wa madaraka ya kisiasa, fedha na utawala kutoka Serikali Kuu kwenda kwa wananchi kupitia Serikali za Mitaa umetokana na mahitaji ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 145 na 146. Madhumuni ya ugatuzi ni kuwapa wananchi kupitia Mabaraza yao ya Madiwani, uwezo wa kufanya maamuzi kulingana na mahitaji yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali za Mitaa zimeundwa kwa mujibu wa Sheria Na.7 (Mamlaka za Wilaya) na Sheria Na.8 (Mamlaka za Miji)kwa malengo ya kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma mbalimbali za jamii kwa wananchi pamoja na kusimamia ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sheria kuweka utaratibu wa Serikali za Mitaa kujiamulia mambo yake kupitia vikao rasmi, hazijapewa uwezo wa kukataa maelekezo ya Serikali Kuu. Kwa mujibu wa Sera ya Maboresho ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1998, Serikali Kuu ina majukumu ya kutunga sera, kutoa miongozo ya namna bora ya kutekeleza sera, kuandaa mikakati ya kitaifa, kuweka mazingira bora ya utekelezaji wa sera kwa kuzipatia Serikali za Mitaa rasilimali watu, rasilimali fedha na baadhi ya vitendea kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuweka viwango vya utekelezaji, kufuatilia utekelezaji ili kujiridhisha kuwa miongozo na viwango vinazingatiwa na kuchukua hatua dhidi ya utekelezaji usioridhisha inapobidi hasa inapobainika matumizi yasiyo sahihi ya fedha ikiwemo viwango duni vya miradi visivyolingana na thamani ya fedha iliyotumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali Kuu huwakilishwa na viongozi wa Mikoa na Wilaya katika kusimamia utekelezaji wa sera na miongozo, Viongozi Wakuu wa Serikali ngazi ya Mikoa na Wilaya hutekeleza majukumu yao ya kisheria ya kuziwezesha Serikali za Mitaa kutimiza majukumu yao kikamilifu ikiwemo kutekeleza maagizo halali na ushauri wa viongozi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikibainika kiongozi wa Mkoa au Wilaya ameshindwa kutimiza wajibu wake na hivyo kusababisha Mamlaka ya Serikali za Mtaa zisitimize vizuri majukumu yao, Mamlaka ya uteuzi huchukua hatua za kiutawala. Napenda kusisitiza kwamba Katiba, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi zikirejewa vizuri hakuna mgogoro wowote wa kimipaka wala kiutendaji utakaodhihiri.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Kuna ongezeko la bidhaa bandia na zisizo na viwango zinazoingizwa nchini, miongoni mwa bidhaa hizo ni pembejeo za kilimo, madawa ya mifugo, dawa za binadamu, vyakula, vinjwaji, vifaa vya nyumbani na kadhalika.
(a) Je, ni hasara gani imepatikana kwa mwaka mmoja uliopita kutokana na bidhaa hizo kuingizwa nchini na kutumiwa na wananchi?
(b) Je, ni hatua gani zinachukuliwa kukomesha bidhaa hizo kuingia nchini hasa maeneo ya vijijini ambako uelewa wa watumiaji ni mdogo na maafisa wadhibiti ni wachache?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Ushindani (FCC) na kwa kushirikiana na wamiliki wa nembo za biashara, inaendelea kudhibiti bidhaa bandia zisiingie nchini ili kuhakikisha ushindani wa haki katika biashara. Katika kipindi cha Januari hadi Disemba, 2016 Tume ya Ushindani ilikamata bidhaa bandia zenye thamani ya shilingi bilioni 18.67. Bidhaa hizo zilikamatwa kwenye kaguzi za bandarini, vitengo vya makontena (ICDs) na katika masoko.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 hadi Machi, 2017, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na Taasisi nyingine waliteketeza bidhaa mbalimbali zenye thamani ya shilingi bilioni 2.4. Bidhaa hizo ni pamoja na nguo, nyama na sausage, vilainishi vya injini, battery za magari na za solar 1,430.
Mheshimiwa Spika, shirika pia lilifanya ukaguzi wa mabati na kutekeleza mabati 84,000 ambayo hayakukidhi viwango. Aidha, takriban lita 94,869 za vilainishi vya injini, na katoni 200 za bendera za Taifa zilirudishwa nchi zilikotoka. Vilevile aina 11 za pombe kali katoni 123,942 zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki vilizuiliwa kuingia sokoni na kurudishwa katika nchi zilikotoka.
Mheshimiwa Spika, Tume ya Ushindani na TBS zinafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi nyingine katika kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kudhibiti bidhaa zinazopitia katika mipaka na nchi jirani, kufuatilia ubora wa bidhaa hafifu na bandia na kuziondoa katika soko. Ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa taasisi hizi, Serikali inongeza ajira za watumishi, kufungua vituo vya ukaguzi wa bidhaa katika mipaka yote na kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kama vile luninga, redio na magazeti na kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalma kuzuia magendo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote tushirikiane kupambana na bidhaa bandia na zisizokidhi viwango. Adui namba moja wa viwanda ni bidhaa bandia na zile zisizokidhi viwango.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
(a) Je, Serikali inazo takwimu za kuaminika za vijana waliohitimu vyuo mbalimbali ambao hawajaweza kujiajiri au kuajiriwa;
(b) Je, ni taaluma zipi zina fursa nyingi za zipi zina fursa chache za kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu?
(c) Je, kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita ni ajira ngapi zilipatikana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Joseph Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali ina takwimu sahihi na za kuaminika za vijana waliohitimu vyuo mbalimbali, lakini hawajaweza kujiajiri au kuajiriwa ambazo hutumika katika kupanga na kutathmini utekelezaji wa programu zinazohusiana na masuala ya ajira. Takwimu hizo huptikana kupitia tafiti za nguvu kazi na tafiti za hali ya ajira na mapato zinazofanywa na ofisi ya Taifa ya Takwimu, pamoja na zinazofanywa na Taasisi za Elimu, kama vile Tracer Studies. Kwa mujibu wa utafiti wa nguvu kazi nchini, vijana 65,614 ambao ni wahitimu wa vyuo mbalimbali hawakuwa wamejiajiri wala kuajiriwa mwaka 2014.
(b) Mheshimiwa Spika, taaluma zenye fursa nyingi za kuajirika ni pamoja na fani za afya ya binadamu zikiwemo utabibu, uuguzi, ufundi sanifu wa maabara, ualimu na ufundi. Aidha, taaluma zenye fursa chache za ajira ni pamoja na masomo ya utawala, biashara na rasilimali watu. Napenda kuchukua fursa hii kuwashauri wanafunzi kusoma masomo ya sayansi kwa kuwa yana fursa nyingi zaidi za ajira hususani wakati huu ambao Taifa linaelekea kuwa nchi ya viwanda.
(c) Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuanzia mwaka 2015 hadi 2017/2018, jumla ya ajira mpya 1,336,957 zilipatikana kama ifuatavyo:-
Kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Serikali ajira 593,986, sekta binafsi ajira 571,073 na Serikalini ajira 171,898. (Makofi)
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
Kuna miradi ya umwagiliaji iliyogharimu fedha nyingi kuijenga lakini inatumika chini ya uwezo na usanifu (below designed capacity) kwa sababu mbalimbali.
a) Je, ni Halmashauri ngapi zina fursa ya kilimo cha umwagiliaji na zimewekeza kwa kiwango cha kutosha kwenye miundombinu ya umwagiliaji?
b) Je, kuna mpango wowote unaotekelezwa wa kuwapata wataalam wa umwagiliaji katika muda mfupi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri zote nchini zina fursa ya kilimo cha umwagiliaji na Halmashauri hizo zimeweka katika mipango yake ya maendeleo miradi inayofaa kuendelezwa kuwa kufuata vipaumbele. Skimu za umwagiliaji zimejengwa katika Halmashauri mbalimbali nchini, lakini kutokana na kukosekana kwa fedha baadhi ya skimu hizo ujenzi wake haukukamilika. Kwa sasa Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japani (JICA) imefanya mapitio ya Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa Taifa ulioandaliwa mwaka 2002. Mapitio hayo yataainisha maeneo yote yanayofaa kwa umwagiliaji katika kila Halmashauri na mikoa yote nchini. Mapitio hayo yanatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kufanya mawasiliano na Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kupata kibali cha kuajiri wataalam wa kutosha katika fani ya umwagiliaji. Pamoja na hayo, Halmashauri ambazo hazina wataalam wa umwagiliaji zinashauriwa kuajiri wataalam wa fani hizo.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-

Afya za wanawake wengi vijijini zinaathiriwa na moshi wa kuni wanazopikia kwenye majiko ya mafiga matatu ambayo yanatumia kuni nyingi na hivyo kuchochea kasi ya ukataji miti:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa matumizi ya majiko ya mafiga matatu kote nchini?

(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka wa kuondoa majiko hayo kwenye shule zote za msingi na sekondari?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, matumizi ya tungamotaka hususan kuni na mkaa kama chanzo cha nishati ya kupikia hapa nchini yanakadiriwa kufikia asilimia 85. Matumizi ya tungamotaka ikiwemo mafiga matatu husababisha madhara ya kiafya kutokana na kuvuta hewa chafu inayotokana na kuni na mkaa kwa watumiaji pamoja na uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji wa miti.

Mheshimiwa Spika, kupitia Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015, Serikali imekuwa ikihamasisha matumizi bora ya nishati ikiwemo teknolojia zinazopunguza gesi ya ukaa na matumizi makubwa ya kuni na mkaa kwa kutumia majiko banifu. Aidha, Serikali imekuwa ikihamasisha kuacha matumizi ya nishati mbadala wa kuni na mkaa katika kupikia gesi na mitungi (Liquefied Petroleum Gas), bayogesi, vitofali vya mabaki ya tundamotaka na majiko ya nishati jua.

Mheshimiwa Spika, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini pamoja na jukumu la kusambaza umeme vijijini inasaidia usambazaji wa teknolojia bora za kupikia hususan katika taasisi za Umma nchi nzima zikiwemo Shule, Magereza, Kambi za Wakimbizi na Zahanati.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Elimu ya Msingi ni muhimu kuwawezesha wahitimu kuzalisha na kuwapatia stadi za maisha lakini wapo wahitimu wa Elimu ya Msingi, Sekondari na Vyuo wasioweza hata kuanzisha bustani za mboga mboga na matunda:-

Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha elimu inayotolewa inamwezesha mhitimu kupata ujuzi na stadi za maisha ili aweze kujiajiri?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuwawezesha wanafunzi kupata stadi za maisha na kuzalisha limezingatiwa katika mitaala ya ngazi mbalimbali za elimu hapa nchini kwa lengo la kumwezesha mhitimu kupata ujuzi na stadi za maisha ili aweze kujiajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuwawezesha wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kupata stadi za maisha na ujuzi ili waweze kuzalisha, Serikali imehuisha mitaala ya Elimumsingi kwa lengo la kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa stadi mbalimbali za maisha. Kwa mfano, katika shule za msingi, somo la Stadi za Kazi linawajengea wanafunzi stadi za ujasiriamali na hivyo kuwandaa kujiajiri kwa wale watakaoishia ngazi hiyo ya elimu. Kwa upande wa shule za sekondari stadi za ujasiriamali kama vile, kuweka malengo, kuwasiliana na uthubutu zimezingatiwa kwenye mitaala.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imewezesha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 54 kutoa maarifa na ujuzi wa ufundi katika fani mbalimbali kwa wahitimu wa Elimumsingi ili waweze kuzalisha kama vile ushonaji, ufundi umeme, uashi na uselemala. Pia, Serikali imeendelea kujenga uwezo wa walimu wa ufundi katika vyuo hivyo ili kuboresha ujuzi wao katika nyanja mbalimbali za kiujuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizi za Serikali, jukumu la kufundisha wanafunzi stadi za maisha ni la jamii nzima. Hivyo, naomba kutoa rai kwa wazazi/walezi na jamii kwa ujumla kuwapa nafasi watoto wetu kufanya kazi mbalimbali za nyumbani kulingana na umri wao ili kusaidia kuwafundisha kwa vitendo.
MHE. SHALLY J. RAYMOND Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzalisha mbegu bora za kuku wa kienyeji na kuhakikisha zinawafikia wafugaji wa kuku katika Mkoa wa Kilimanjaro kwa bei nafuu ya ruzuku na kwa wakati?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwanza nimshukuru Mungu sana kwa kutupa uzima sisi wote na kutulinda, lakini kwa vile ni mara ya kwanza na mimi nasimama mbele ya Bunge lako tukufu, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kunipa nafasi ya kuweza kuendelea kuhudumu kwenye Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuku wa asili ambao yeye ameita kuku wa kienyeji, hususan katika uzalishaji na lishe bora kwa watumiaji. Wizara kupitia taasisi yake ya utafiti TALIRI Kituo cha Naliendele, Mtwara inaendelea kufanya utafiti wa aina ipi ya kuku wazazi wa asili watakaotumika kuzalisha vifaranga hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa imesajili makampuni mawili ya AKM Glitters Company, Dar es Salaam na Silverland Poultry Company iliyoko Iringa, kuanzisha mashamba ya kuku wazazi ili kuzalisha vifaranga vya kuku chotara aina ya kuroila na sasso, ambao wanauzwa kwa bei ya ruzuku ya shilingi 1,400 kwa kifaranga cha sasso na shilingi 1,500 kwa kifaranga cha kuroila.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge tunamshauri, kama Wizara, awasiliane na mawakala zaidi ya 15 waliopo mkoani kwake ili waweze kumhudumia pale inapohitajika.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-

(a) Je, ni matukio mangapi ya moto yametokea kwenye Shule na masoko katika kipindi cha miaka mitano iliyopita?

(b) Je, uchunguzi uliofanyika ulibaini vyanzo vya moto huo ni nini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2016 hadi 2020 ilipokea taarifa 175 za matukio ya moto kwenye Shule na taarifa 55 za matukio ya moto kwenye masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika chunguzi na tafiti mbalimbali za vyanzo vya matukio ya moto katika masoko na mashuleni, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilibaini vyanzo vya moto kuwa ni migogoro baina ya wanafunzi na menejimenti za shule, lakini matumizi ya umeme yasiyo sahihi, uhalifu, uchomaji wa makusudi (hujuma), hitilafu za umeme, uchakavu wa mifumo ya umeme na uzembe wa kuacha moto kwenye majiko ya mkaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kudhibiti matukio hayo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea na mikakati ya kuzuia majanga ya moto kwa kufanya ukaguzi wa majengo na kutoa ushauri na mapendekezo ya kitaalam, yakiambatana na utoaji wa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto na pia kusisitiza kuwepo kwa vifaa vya awali vya kuzimia moto yaani (fire extinguishers) na vifaa vya kung’amua moto yaani (fire detectors) na uwepo wa Walinzi katika maeneo husika. Nakushukuru.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Je, ni lini makubaliano ya kibiashara yatafanyika baina ya taasisi za Umma na makampuni binafsi yanayolima kahawa Mkoani Kilimanjaro ili kuzalisha miche bora yenye ukinzani dhidi ya magonjwa na kuigawa kwa wakulima bila malipo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa miche bora ya kahawa hufanyika kupitia wakulima binafsi, vikundi vya wakulima, Vyama vya Ushirika, Taasisi ya Utafiti ya TaCRI na mikataba baina ya TaCRI na kampuni binafsi au shirika.

Mheshimiwa Spika, kutokana na gharama kubwa ya uzalishaji wa miche hususani pale ambapo hakuna ufadhili maalum wa taasisi au shirika, kumekuwepo na utaratibu wa wakulima kuchangia gharama kidogo ili kuwa na uzalishaji endelevu na upatikanaji wa miche bora.

Mheshimiwa Spika, mathalani wakulima hutakiwa kuchangia kiasi cha shilingi 100 kwa kila mche sawa na asilimia 10 ya gharama halisi ya mche. Kati ya Julai, 2016 mpaka 2021 TaCRI imezalisha jumla ya miche 2,308,606 ambayo imeendelea kusambazwa Mkoani Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, TaCRI imekuwa ikiingia mikataba ya kuzalisha miche bora yenye ukinzani dhidi ya magonjwa na kuisambaza kwa wakulima kadri ya mahitaji. Mikataba hiyo ni pamoja na uzalishaji wa miche 100,000 uliofanyika kati ya mwaka 2018 na 2019 ambapo TaCRI ilishirikiana na Ushiri AMCOS ya Wilayani Rombo kuzalisha miche hiyo.

Mheshimiwa Spika, TaCRI kati ya mwaka 2016 na 2019 ilishirikiana na Taasisi za Hivos na Solidaridad kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa miche bora ya kahawa ambapo jumla ya miche 890,677 ilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima katika Wilaya za Same, Mwanga na Moshi.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Je, ni Mikoa ipi inaongoza kwa mafanikio katika kampeni ya kuwabadili wakulima kutoka kwenye kilimo cha kujikimu na kulima kibiashara na ni mikoa ipi bado inasuasua?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampeni ya kilimo biashara hapa nchini ilianza katika mazao yenye asili ya biashara ambayo ni pamoja na pamba, korosho, kahawa, pareto, chai, tumbaku na mkonge ambapo uhamasishaji wake ulifanyika kwa kuanzisha Vyama Vikuu vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa inayolima mazao ya kibiashara ni pamoja na Mwanza, Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Mtwara, Lindi na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Ruvuma, Mbeya, Songwe, na Iringa. Kufuatia kazi kubwa iliyofanywa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika utoaji wa elimu ya kilimo biashara na utafutaji wa masoko ya mazao, wakulima katika mikoa hii wamebadilika na kwa sasa wanalima kilimo cha kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa ambayo ilikuwa nyuma katika kutekeleza dhana ya kilimo biashara ilikuwa ni pamoja na mikoa ya Rukwa, Katavi, Kigoma, Dodoma, Singida, Morogoro, Manyara na Njombe. Mazao makuu katika mikoa hii ni yale ya nafaka, mikunde na mazao ya mafuta ambayo yalikuwa yakilimwa zaidi kwa ajili ya usalama wa chakula. Hivyo, kutokana na elimu ya kilimo biashara ambayo imekuwa ikitolewa kwa Maafisa Kilimo na wakulima katika mikoa hii, wakulima wengi wamebadilika na wanalima mazao kwa kuzingatia mahitaji ya soko.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Je, ni programu zipi zinatekelezwa kuvuna maji ya mvua na asilimia ngapi ya Wananchi hutumia huduma hiyo?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilibuni Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) inayotekelezwa nchini kote kuanzia mwaka 2006 hadi 2025. Programu hiyo inatekelezwa kupitia Programu ndogo tatu ambapo pamoja na mambo mengine, programu hizo zinazingatia uvunaji maji ya mvua kwa kuelekeza ujenzi wa mabwawa makubwa, ya kati na madogo na pia, uvunaji wa maji ya mvua kwa kutumia mapaa ya nyumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia programu hizo, mabwawa yamejengwa na kukarabatiwa kwenye maeneo mbalimbali nchini na katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa mabwawa ya ukubwa wa kati na madogo katika wilaya 16, ujenzi wa mabwawa ya kimkakati ya Farkwa na Kidunda na usanifu wa ujenzi wa mabwawa katika Wilaya 24. Aidha, Serikali ilitoa mwongozo wa Uvunaji wa Maji ya Mvua kupitia mapaa ya nyumba kwa watu binafsi na taasisi za Umma na kwa sasa miundombinu hiyo inaonekana katika maeneo mbalimbali nchini. Serikali itatafiti kufahamu ukubwa wa matumizi ya teknolojia hiyo nchini.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Je, ni kiasi gani cha ngozi kinazalishwa kwa mwaka mzima na kutumika nchini na kiasi gani ghafi kinauzwa nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inazalisha wastani wa vipande milioni 13.6 vya ngozi kwa mwaka. Kati ya vipande hivyo, milioni 4.2 ni vya ng’ombe, vipande milioni 6.9 ni vya mbuzi na vipande milioni 2.5 ni vya kondoo. Kwa sasa, tunavyo viwanda vitatu vinavyofanya kazi ya usindikaji wa ngozi katika hatua ya kati (wet blue) na hatua ya mwisho (finished leather).

Mheshimiwa Naibu Spika, ngozi zinazosindikwa katika hatua ya kati ni vipande 51,866 vya ngozi ya ng’ombe na vipande 262,229 vya mbuzi na kondoo. Usindikaji hadi hatua ya mwisho ni vipande 145,000 vya ngozi ya ng’ombe na vipande 259,000 vya ngozi ya mbuzi na kondoo. Pia, kuna wasindikaji wadogo wanaosindika na kutengeneza bidhaa za ngozi maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inauza nje ya nchi ngozi ghafi na iliyosindikwa hatua ya awali, wastani wa vipande 1,630,740 vyenye thamani ya Shilingi Bilioni 10.5 kwa mwaka. Ngozi hiyo, inauzwa katika nchi za Nigeria, Afrika ya Kusini, Ghana, Togo, Pakistan, Marekani, Italia, Dubai na China, ahsante sana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzalisha Mbegu bora za Parachichi aina ya Hass na kuzigawa kwa wakulima kwa bei nafuu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli miche ya parachichi katika baadhi ya maeneo imekuwa ikiuzwa kwa bei kati ya shilingi 5,000 hadi shilingi 6,000 ambapo baadhi ya wananchi wanashindwa kumudu, kwani ekari moja inahitaji miche siyo chini ya 70 na kwa ekari 10 utahitaji shilingi 3,500,000 kwa ajili ya miche tu iwapo bei ya mche ni shilingi 5,000.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia TARI inatarajia kuanza uzalishaji wa miche ya parachichi milioni 20. Miche hiyo itauzwa kwa bei ya ruzuku ya chini ya shilingi 2,000. Aidha, katika kudhibiti ubora wa wazalishaji binafsi, Serikali kupitia Taasisi ya Uthibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) imeanza usajili wa wazalishaji wa miche ya parachichi nchini. Pia katika kuhakikisha usimamizi bora wa zao hili, Serikali inatarajia kuzindua mwongozo wa uzalishaji wa zao la parachichi.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kujenga Mabwawa ya kuvuna maji ya Mvua pamoja na mifereji ya umwagiliaji ili kupunguza athari za mvua katika Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa ambayo ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua pamoja na ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji umeendelea ili kupunguza athari za mvua na kusaidia wakulima kujihakikishia kilimo cha mwaka mzima kupitia umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imekamilisha mapitio ya usanifu wa ukarabati wa Bwawa la Ikuini na taratibu za kumpata mkandarasi kwa ajili ya ukarabati wa bwawa hilo unaendelea.

Mheshimiwa Spika, aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bwawa la Boloti na Yongoma sambamba na mifereji itakayoweza kuhudumia takribani hekta 2,000 ndani ya Wilaya ya Same.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Je, maeneo mangapi yameshabainishwa kuwa ni vyanzo vya maji salama ardhini na hatua gani zinachukuliwa kulinda maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Bodi za Maji za Mabonde nchini na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ina jukumu la kutambua, kutunza, kuhifadhi na kuendeleza vyanzo vya maji vya juu ya ardhi na chini ya ardhi pamoja na kutambua uwezo wa chanzo na ubora wa maji yake. Hadi sasa vyanzo vya maji chini ya ardhi vilivyotambuliwa ni 152 na kati yake, vyanzo 30 vimewekewa mipaka na vyanzo 10 vimetangazwa kwenye gazeti la Serikali na hivyo kulindwa kisheria. Vilevile, Wizara inaendelea kufanya utafiti katika maeneo mengine 172 yenye maji chini ya ardhi ili kubaini uwezo wa chanzo na ubora wa maji yake.

Aidha, Serikali kupitia maabara za maji nchini hufanya ufuatiliaji wa mwenendo wa ubora wa maji chini ya ardhi kupitia visima vya uchunguzi vilivyochimbwa kwenye maeneo mbalimbali nchini. Sampuli za maji huchukuliwa kutoka visima hivyo na kufanyiwa uchunguzi na pale inapothibitika kuwepo kwa mabadiliko ya mwenendo wa ubora hatua stahiki huchukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na Serikali kulinda maeneo yaliyotambuliwa kuwa vyanzo vya maji chini ya ardhi ikiwemo kuyawekea mipaka na kuyatangaza kwenye gazeti la Serikali kuwa maeneo tengefu, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzani na uhifadhi wa maeneo husika.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -

Je, ni nyumba ngapi zinahitajika kwa Watumishi wa Umma waliopo Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEORGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimwa Mwenyekiti, ni kweli kuna uhitaji mkubwa wa nyumba za watumishi waliopo vijijini hususan watumishi wa kada ya elimu na afya. Hadi Mei, 2023, idadi ya nyumba za walimu zilizopo vijijini ni 55,097 wakati upungufu ni nyumba 255,097. Aidha, kwa upande wa watumishi wa afya, nyumba za watumishi zilizopo ni 7,818 na upungufu ni nyumba 15,272.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 kupitia Mradi wa SEQUIP, Serikali imekamilisha mchakato wa kujenga nyumba 212. Serikali itaendelea na jitihada za kukabiliana na upungufu wa nyumba za watumishi wa kada za elimu na afya hususan waliopo vijijini.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-

Je, kuna mipango gani ya kuweka mazingira wezeshi ya kupata mbegu bora za malisho kama Luseni pamoja na kuwezesha uzalishaji wa mitamba?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuimarisha mashamba yake ya kuzalisha mbegu za malisho kwa kuyapatia vitendea kazi na kuongeza ukubwa wa maeneo ya kuzalisha mbegu za malisho na malisho. Aidha, nitumie fursa hii kuendelea kuihamasisha sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa mbegu za malisho na malisho kibiashara ili kukidhi mahitaji ya ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uzalishaji wa mitamba, mpango wa Serikali ni kuendelea kuyaimarisha mashamba yake ya kuzalisha mitamba ya kituo cha kuzalisha mbegu za mifugo kwa ajili ya uhimilishaji cha NAIC- Arusha ili kuzalisha na kusambaza mitamba na mbegu bora za ng’ombe kwa gharama nafuu.