Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Abdallah Ally Mtolea (2 total)

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami kwa niaba ya wananchi wa Temeke niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunatambua kwamba mmiliki wa ardhi ya nchi hii ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kimsingi Serikali imekuwa iki-enjoy mamlaka hayo kwa kuchukua baadhi ya maeneo kwa ajili ya kukaribisha uwekezaji. Hili ni jambo zuri sana kukaribisha uwekezaji. Isipokuwa inasahau kitu kimoja, pale ambapo inawakaribisha hao wawekezaji, haizifanyi Halmashauri husika kuwa sehemu ya uwekezaji ule kwa maana ya uanahisa. Je, Serikali yako imejipangaje sasa kubadilisha mwelekeo huu ili kila unapowekwa uwekezaji ile Halmashauri iwe sehemu ya mwanahisa?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mtolea, Mbunge wa Temeke kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu imefungua milango kwa wawekezaji nchini kuwekeza kwenye sekta mbalimbali kulingana na matakwa ya mwekezaji. Uwekezaji huu unafanywa na unajikuta upo kwenye mamlaka zetu za Halmashauri ya Wilaya, Manispaa na maeneo mengine. Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kama Serikali imejipangaje na Halmashauri hizi kuweza kunufaika na uwekezaji huu?
Mheshimiwa Spika, ni kweli. Sasa uwekezaji huu uko wa aina mbili; kuna uwekezaji ambao tumeutaka upitie kwenye Taasisi yetu ya Uwekezaji (TIC) ambapo TIC inayo Benki yake ya Ardhi na kwa kuwa ardhi ni ya Serikali, kwa hiyo TIC tumeweza kuwapa ardhi ambapo wao sasa wakipata mwekezaji mkubwa, wanaweza kwenda kuwekeza mahali. Kwa uwekezaji huu, wanapokwenda kuwekeza kwenye eneo lolote lile Halmashauri ndiyo ambayo itakuwa imetoa ardhi hiyo lakini kupitia TIC na uwekezaji huo, Halmashauri wanaweza kunufaika kwa tozo ya ile ardhi.
Mheshimiwa Spika, pia Halmashauri inaweza kunufaika pia kwa mwekezaji huyo kushiriki kikamilifu kwenye mipango ya maendeleo ya Halmashauri kwa kuchangia shughuli za maendeleo kwenye maeneo yale. Pia kama kuna tozo nyingine na manufaa ya uwepo wa mradi wenyewe kama kuna bidhaa zinatengenezwa tunatarajia eneo hilo linaweza kunufaika kwanza kwa gharama nafuu kupitia uwekezaji ule.
Mheshimiwa Spika, uwekezaji mwingine ni ule ambao Halmashauri yenyewe inakuwa na Benki yake ya ardhi ambayo inaamua sasa kutafuta wawekezaji ili kufanya maendeleo. Hii inanufaika zaidi kwa sababu kwanza atapata tozo ya ardhi, lakini pili, naye anaweza kuwa ni sehemu ya mwanahisa wa mradi wenyewe kulingana na utaratibu atakaotumia; lakini atanufaika na manufaa yale yote ambayo nimeyataja kwamba mwekezaji anatakiwa atambue kwamba yeye yupo pale na wananchi waliopo maeneo yale watanufaika kupitia mradi wake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namna ambavyo Serikali tunasimamia jambo hili, kwanza tunahakikisha wawekezaji tunawatambua na uimara wao, ubora wao katika uwekezaji na tunawaunganisha na maeneo hayo ili waweze kujenga mshikamano katika kuwekeza ili pia na yeye aweze kupata security na Halmashauri kwenye maeneo hayo ziweze kunufaika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, uwekezaji wa aina mbili; uwekezaji ambao wananufaika zaidi ni ule ambao Halmashauri yenyewe imetengeneza mpango wa matumizi ya ardhi lakini wametenga maeneo ya uwekezaji ili mwekezaji anapokuja, anakwenda kuwasiliana na Halmashauri. Kwa hiyo, pale wana-negotiate, wanaweza kukubaliana yale mambo ya msingi ili kuweza kupata tozo mbalimbali ikiwemo na Halmashauri yenyewe kutumia ardhi yake kuwa mwanahisa wa ardhi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utakuta kuna tofauti kati ya ardhi inayomilikiwa na TIC, Taasisi ya Uwekezaji ambayo inakwenda kumpeleka mwekezaji ili awekeze chini ya Taasisi ya Uwekezaji na ile ardhi ambayo mwekezaji anakwenda kwa uwekezaji chini ya Halmashauri yenyewe. Kwa hiyo, maeneo haya yote utofauti wake ni kama ambavyo nimeweza kuutofautisha na namna ambavyo unaweza kunufaika.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nimuulize swali Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika Serikali ya Awamu ya Nne nchi hii ilitumia mabilioni ya fedha kuzunguka nchi nzima kwa ajili ya kukusanya maoni ili kuandaa Katiba Mpya na hii ilikuja baada ya kugundua kwamba Taifa hili linahitaji Katiba Mpya ili kutibu changamoto nyingi ambazo zinaikabili katika maeneo mbalimbali ikiwemo kulinda rasilimali, uwajibikaji, haki za binadamu, tunu za Taifa na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Nne kwa kuanzisha mchakato ule, pamoja na changamoto ambazo zilijitokeza baadaye.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali ya Awamu ya Tano toka imeingia madarakani, leo miaka miwili tayari imepita haijafanya jambo lolote la kuendeleza mchakato ule ili zile ndoto za Watanzania za kupata Katiba Mpya ziweze kutimia. Zaidi tumekuwa tukisikiliza kauli mbalimbali za kwenu viongozi na za viongozi wa Chama chenu cha Mapinduzi ambazo hazioneshi nia ya kukamilisha mchakato huo wa Katiba Mpya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba awaambie Watanzania leo, nini mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kutimiza ndoto za Watanzania kupata Katiba Mpya?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mtolea, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali ya Awamu ya Nne ilianza mchakato wa Katiba Mpya na kupitia hatua zote za kuunda Tume, ikapita kukusanya maoni na sisi kama Waheshimiwa Wabunge tulikuwa miongoni mwa Wajumbe ambao tulishiriki katika kuweka misingi ya Katiba hiyo. Suala la Katiba Mpya linahitaji gharama kubwa ya fedha na zinatokana na mapato yanayokusanywa ndani ya nchi lakini kila mwaka wa fedha una vipaumbele vyake na sisi tumejikita katika kutoa huduma za jamii kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukishuhudia Watanzania wanahitaji maji kwenye vijiji, kumekuwa na mahitaji ya huduma za afya, tunahitaji kuimarisha elimu, miundombinu, ili kuwawezesha Watanzania kuendelea na maisha yao. Katiba ni mwongozo ambao unaelekeza mambo kadhaa. Sasa hivi tunayo Katiba ambayo pia ina miongozo ile ile ingawa tumekusudia kuibadilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunayo Katiba inaendelea na miongozo ipo, na haya ni mapendekezo ya kufanya marekebisho ya maeneo kadhaa; lakini mchakato wake kwa sababu unahitaji gharama kubwa na kipaumbele cha Serikali ni kutoa huduma ya jamii kwa Watanzania; kwanza tumeanza kuimarisha makusanyo ya ndani ili tuweze kumudu kutoa huduma za wananchi, Watanzania. Pale ambapo tutafikia hatua nzuri ya mapato huku tukiendelea kutoa huduma hiyo na matatizo haya yakipungua kwa kiasi kikubwa, tutakuja kuendesha mchakato huo pale ambapo inaonekana tunaweza tukaufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua hayo yote lakini pia tumeona muhimu zaidi tuanze na huduma za jamii ili Watanzania waendelee kufanya kazi zao za kuboresha uchumi wao ili wapate nafasi ya utulivu waje waangalie jambo lingine, kwa sasa tutatumia Katiba iliyopo. Ahsante sana.