Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Munde Abdallah Tambwe (5 total)

MHE. MUNDE T. ABDALLAH aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora inakabiliwa na kero mbalimbali kama vile ukosefu wa madaktari bingwa wa watoto, akina mama, mifupa, na kadhalika; ukosefu wa vifaa muhimu kama vile ECG machine, CT-Scan, MRI machine, ukosefu wa huduma za ICU pamoja na kwamba lipo jengo zuri lakini halina vifaa vya huduma za dharura:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kutatua kero hizi zinazokabili hospitali hii kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua changamoto ya Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Serikali imewapeleka masomoni Madaktari Bingwa wawili akiwemo Daktari wa Upasuaji na Daktari wa Watoto. Aidha, Mkoa katika bajeti ya mwaka 2015/2016 imeomba kibali cha kuajiri Madaktari Bingwa wanne ili kuboresha utoaji wa huduma ya afya. Kwa sasa hospitali hiyo inatumia Madaktari Bingwa watano kutoka China wanaojitolea ambao wamebobea katika maeneo ya tiba, upasuaji, huduma za uzazi, watoto na huduma ya masikio, pua na koo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa vifaa, Serikali imepanga kusimika vifaa vya kuangalia mwenendo wa afya ya wagonjwa (patient monitor), vifaa vya uchunguzi wa tiba vikiwemo ECG, CTG, Pulse Oxymeter na Oxygen Concentrator katika hospitali zote za ngazi ya mkoa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora. Mpango huu unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha 2015/2016 na unahisaniwa na Uholanzi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Aidha, Serikali ina mpango wa kuweka huduma ya MRI kwenye Hospitali za Rufaa za Kanda na Taifa ambapo kwa mwaka 2015/2016, huduma hii itasimikwa katika Hospitali ya Kanda ya Bugando ambayo inahudumia pia wakazi wa Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Mkoa wa Tabora umeingia makubaliano na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), ili kuweza kukopeshwa vifaa muhimu, hususan kwa ajili ya huduma za dharura (ICU).
MHE. MUNDE T. ABDALLAH aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango mkakati gani kupitia diplomasia ya uchumi na nchi ya China kuunganisha wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa ili kuingia ubia wa kuimarisha viwanda vidogo na vya kati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munde Abdallah Tambwe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba nchi yetu ni miongoni mwa nchi nne Barani Afrika ambazo Serikali ya China imezichagua kuwekeza viwanda vyake katika miaka mitatu ijayo (2016 mpaka 2018). Kufuatia uamuzi huo Majimbo mawili ya China ya Jiangsu na Zhejiang yamekwishaelekezwa kuwekeza nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya China imeanzisha Mfuko Maalum wa Fedha kwa ajili ya kuwezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati wa Afrika kupata mitaji maalum. Mfuko huo umewekwa katika Benki ya Maendeleo ya China na tayari umetengewa dola za Kimarekani bilioni tano. Serikali imekwishaanza mazungumzo na benki hiyo kwa ajili ya kuwezesha mabenki nchini yaweze kukopa fedha hizo ili hatimaye yaweze kuwakopesha wajasiriamali wetu wanaotaka kuwekeza kwenye sekta ya viwanda kwa kushirikiana na wenzao wa China.
Mheshimiwa Spika, tarehe 22 Agosti, 2016 Wizara yangu iliitisha kikao cha pamoja kati ya Benki ya Maendeleo ya China na mabenki ya Tanzania ili kupewa utaratibu wa namna ya kupata fedha za mfuko huo. Matarajio yetu ni kwamba, mabenki hayo yatakidhi vigezo vya kuchukua fedha kutoka katika Mfuko huo wa China, ili Watanzania waanze kupata mitaji mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Spika, ubalozi wetu nchini China mara kwa mara umekuwa ukiwashawishi wafanyabiashara wa China waje kuwekeza nchini na mara kadhaa umeandaa ziara za makampuni mbalimbali ya China kuja nchini kuonana na Kituo chetu cha Uwekezaji (TIC).
Mheshimiwa Spika, kwa taarifa zilizopo TIC wameendelea kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa ambao makampuni mbalimbali ya China yameingia ubia na Watanzania kuanzisha viwanda nchini. Mfano mzuri ni ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuzalisha nondo na bidhaa za chuma kinachojengwa Kibaha, Mkoani Pwani kwa ubia kati ya Watanzania na Wachina. Kiwanda hicho kitakapokamilika kitazalisha ajira nyingi kwa ajili ya vijana wa Kitanzania.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH aliuliza:-
Pamoja na jitihada za Serikali na mmiliki wa Kiwanda cha Nyuzi Tabora (TABOTEX) ambazo zimewezesha kiwanda hicho kuwa katika hali ya kufanya kazi bado kiwanda hicho kinakabiliwa na ukosefu wa soko la bidhaa zake:-
Je, ni kwa nini Serikali isikipatie kiwanda hiki hadhi ya EPZ ili kipate vivutio vitakavyokiwezesha kupata ushindani katika masoko ya nje?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda cha Nyuzi cha Tabora kilisajiliwa na Serikali tarehe 17 Agosti, 1977 kwa lengo la kusokota nyuzi za pamba ili kuuza kwenye viwanda vya nguo vya ndani ya nchi na ziada kuuzwa nje ya nchi. Kiwanda hiki kilianza kazi rasmi tarehe Mosi Januari, 1990 kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni 6.22 kwa mwaka na kuajiri zaidi ya watu 1,000. Kiwanda hiki baadaye kilibinafsishwa kwa mtindo wa kuuza mali (disposal of assets) kupitia Loans and Advances Realization Trust (LART) hadi mwaka 2004 kilipopata mnunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnunuzi huyo Ms Rajan Indusrties alinunua kiwanda hicho kwa thamani ya dola milioni 1.5 ambapo baadaye pia alishindwa kuendesha kiwanda hicho. Mwezi Julai hadi Septemba, 2017 alijitokeza mwekezaji na kufunga mitambo midogo na kwa ajili ya kutengeneza kamba na vifungashio kwa mazao kama tumbaku na korosho. Aidha, ameanza mchakato wa kufufua kinu cha kuchambulia pamba cha Manonga ambacho Rajan ni mmiliki mbia na chama cha Igembensabo Corporation Union kwa asilimia 80 na mwenzake asilimia 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kiwanda kusajiliwa chini ya Mamlaka ya EPZ nawashauri wawekezaji wawasiliane na EPZA. Hata hivyo, ili kiwanda kiweze kusajiliwa chini ya mamlaka ya EPZ kinatakiwa kukidhi vigezo vifuatavyo:-
• Kuwa na uwekezaji mpya ikiwa ni pamoja na mashine;
• Kuwa na mtaji usiopungua dola za Kimarekani milioni 500;
• Kuwa na uhakika wa soko la nje;
• Kuuza asilimia 80 ya bidhaa zake nje ya nchi; na
• Kuwa na uhakika wa kutoa ajira mpya zisizopungua 500 tofauti na ajira zilizopo sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nawashauri wawekezaji kupitia vigezo hivyo kutathmini na hatimaye kuwasilisha maombi ya kusajiliwa kwenye mamlaka ya EPZ.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanzisha Chuo Kikuu katika Mkoa wa Tabora hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa huo hauna Chuo Kikuu hata kimoja cha Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kuna marekebisho madogo sana nadhani atakuwa aliyapata Mheshimwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munde Abdallah Tambwe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kutokana na gharama kubwa ya uwekezaji inayohitajika katika kuanzisha vyuo vikuu, ni vigumu kwa sasa Serikali kuanzisha Chuo Kikuu katika Mkoa wa Tabora. Hata hivyo, katika Mkoa wa Tabora kuna Tawi la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambacho ni cha Serikali, pia kuna Chuo Kikuu cha Theophil Kisanji Kituo cha Tabora na Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo. Uwepo wa Vyuo hivi na hasa vyuo binafsi ni matokeo ya Serikali kutekeleza sera ya ushirikishwaji wa Sekta binafsi kutoa elimu ya juu nchini
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kutoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza na kushirikiana na Serikali katika kuanzisha Vyuo Vikuu katika program za vipaumbele vya Taifa kama vile Uhandisi, Teknolojia, Afya, Kilimo na Ualimu wa Sayansi na Hisabati na maeneo mengine ambayo yataonekana yanafaa.
MHE. MUNDE A. TAMBWE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Manispaa ya Tabora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Munde Abdallah Tambwe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Manispaa ya Tabora hupata huduma za afya kupitia kwenye zahanati 22 zilizopo kwenye Wilaya hii. Kwa kuwa zahanati inatoa huduma za magonjwa madogo (minor illness), wananchi wa Manispaa ya Tabora hupata huduma kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete. Hata hivyo, Hospitali ya Mkoa kwa sasa imeelemewa na wagonjwa wengi, hivyo manispaa imeona ni vyema ianzishe ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ulianza mnamo tarehe 19/10/2015 kwa kuanza na jengo la OPD kwa gharama ya shilingi milioni 150 chini ya mkandarasi HERU Construction Company Limited ambapo hadi sasa sehemu ya msingi, nguzo, ngazi na slabu vimekamilika kwa asilimia 100, mkandarasi ameshalipwa jumla ya shilingi milioni 145.7 kwa fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Manispaa ya Tabora imetenga shilingi milioni sabini kwa ajili ya ujenzi wa jengo la OPD katika hospitali hiyo. Vilevile Ofisi ya Rais, TAMISEMI itahakikisha inatoa kipaumbele kwa Manispaa ya Tabora katika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya mara fedha za awamu ya pili zitakapo patikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI inasisitiza kuhakikisha fedha za miradi zinazopatikana zilenge katika ukamilishaji wa miradi iliyopo badala ya kuibua miradi mipya; kwa mfano fedha za Local Government Capital Development Grand (LG- CDG) milioni 483.5 kwa mwaka 2017/2018 ambazo zilitolewa maelekezo kwamba zitumike katika kukamilisha miradi iliyokwishaanzishwa.