Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Martha Jachi Umbulla (25 total)

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa kususua kwa barabara ya hizi za Busokelo inafanana sana na kusuasua kwa ujenzi wa barabara ya kutoka Dodoma kwenda Babati na hasa kipande cha Mayamaya kwenda Bonga, naomba kujua Serikali inasema nini kuhusu changamoto hiyo kubwa ambayo imechukua muda mrefu na ahadi ilikuwa mwisho wa mwaka 2015 kumalizika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba barabara ya Busokelo na anayoongelea zinafanana, lakini hii ilikuwa inaongelea matengenezo na hiyo nyingine inaongelea ujenzi. Namwomba Mheshimiwa Mbunge, anafahamu kuna Mbunge ameleta swali kuhusiana na hii barabara. Ni hivi karibuni tu tutapata taarifa kamili na tutalijibu swali linalohusiana na barabara hii ndani ya Bunge hili linaloendelea.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Nishati ya umeme ni nishati muhimu sana hasa kwa maendeleo ya elimu. Hivi sasa sekondari zetu nyingi za kata, hasa kwa mikoa ya pembezoni kama Manyara na kwingineko hakuna umeme kabisa. Je, ni kwa nini usambazaji huu wa umeme vijijini unaofanywa na REA usilenge kwanza sekondari hizi za kata ambazo zina hali mbaya na ambazo zinahitaji kuboreshwa kielimu na kuboreshewa mazingira ya kusoma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumebaini kwamba taasisi nyingi za jamii kwenye kuunganishiwa umeme zimekuwa zikisahaulika. Hata hivyo, niseme kipaumbele cha REA Awamu ya II, kipaumbele cha REA Awamu ya III itakayaoanza vinalenga sanasana kwa kuanzia kuzipatia umeme taasisi za jamii zikiwemo shule, zahanati na taasisi nyingine, hilo ni la kwanza. Niombe sana Wabunge tushirikiane sasa na wataalam wetu wa REA na TANESCO huko vijijini kuwaelekeza wanapoanza kazi waanze na taasisi za jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe tu kuwaambia Waheshimiwa Wabunge, vipaumbele kwa kawaida kabla ya matumizi ya nyumbani tunaanza na taasisi za jamii. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutatembea na wewe kama ambavyo huwa unatembea siku zote, tutembee kwa karibu ikiwezekana siku nzima Mheshimiwa Mbunge, tuongelee hospitali yako ambayo haijapata umeme tuipelekee umeme kwa haraka iwezekanavyo. Naomba uvumilie tukitoka hapa, Mheshimiwa Naibu Spika naomba unipe fursa ya kukaa na Mheshimiwa Mbunge, tukitafakari namna ya kupeleka umeme kwenye maeneo aliyozungumzia.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo hayajaweza kutia matumaini makubwa, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitenga fedha kwa bajeti ya 2015/2016 kwa ajili ya miradi ya kipaumbele na ya kilio cha muda mrefu cha wananchi hususani mradi wa maji katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Haydom ambayo inatumikia mikoa zaidi ya minne ikiwepo Manyara, Singida, Simiyu na kwingineko na ambayo hadi leo haijakamilika kutokana na kukosa fedha lakini pia ikiwepo na bwawa la maji la Dongobeshi ambacho ni kilio cha muda mrefu. Hata Mheshimiwa Rais alipopita wakati wa kampeni walimpa mabango na ni kilio cha muda mrefu kweli kweli na sasa mkandarasi ameacha hiyo kazi kwa sababu pia hajalipwa fedha zake. Je, nini kauli ya Serikali kuhusu miradi hii ya kipaumbele cha wananchi na kilio cha muda mrefu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, miradi ya maendeleo ambayo inatengewa fedha kwa kipindi kilichopita huwa zile fedha zinakwenda kwenye dharura nyingine ambazo zinapangwa na Serikali kuliko fedha kwenda kwenye miradi iliyokusudiwa kama ilivyoidhinishwa na Bunge. Je, Serikali ina mikakati gani sasa kwa bajeti ya 2016/2017 kuhakikisha kwamba fedha zote zinakwenda kwenye miradi yenye kilio cha muda mrefu cha wananchi kuliko kwenda kwenye miradi ya dharura kama ambavyo ilikwenda kwenye miradi ya maabara kipindi kilichopita?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya maji ya Dongobeshi pamoja na bwawa la Dongobeshi, ni kweli kwamba miradi hii ilitambuliwa katika programu ya kwanza ya maendeleo ya sekta ya maji ambayo ilianza mwaka 2006/2007 na imekamilika mwaka 2015. Ilianza kutekelezwa na iko katika hatua mbalimbali lakini kutokana na matatizo kidogo ya fedha basi miradi hiyo haikukamilika kwa wakati. Tayari tumeshaanza kupeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo ya Dongobeshi na katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha na tumeelekeza kwamba kwanza lazima tukamilishe miradi ambayo ilikuwa inaendelea ndiyo tuanze miradi mingine mipya. Kwa hiyo, tutahakikisha tunashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba tunakamilisha miradi hii na hasa ule ambao utakuwa unapeleka maji kwenye Hospitali Teule ya Dongobeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni kweli kabisa kuna miradi mingi ya kipaumbele ambayo ilishindwa kupelekewa fedha katika awamu iliyopita lakini Mheshimiwa Mbunge wewe mwenyewe ni shahidi kwamba mwaka 2015 Serikali ilikuwa na majukumu mengi sana na yalikuwa ni majukumu yale ya muhimu kama vile suala la uchaguzi, kulikuwa na suala la kutengeneza Katiba, hivi vitu ni vya muhimu, ndiyo uhai wa nchi kwa hiyo fedha ilipelekwa kwenye maeneo haya. Nikuhakikishie kwamba kwa sasa majukumu hayo yameshakamilika na tayari tumeongeza ukusanyaji wa fedha. Kwa hiyo, miradi yote ambayo ilikuwa imeainishwa na kupewa kipaumbele tutahakikisha kwamba inakamilishwa.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa maeneo yaliyotajwa kwenye swali la msingi, Naberera iko Simanjiro na Kibaya iko Wilaya ya Kiteto na ni maeneo yanayozalisha sana mahindi hapa nchini, kwa hiyo, ni maeneo muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu, lakini hakuna barabara hata moja inayounganisha hata na Makao Makuu ya Mkoa ambayo ni Babati na barabara zake ni za vumbi na hivyo zinaharibika sana kwa ajili ya kubeba mahindi nyakati za mvua.
Je, Serikali ina mikakati gani sasa kwa umuhimu nilioutaja kuhakikisha kwamba angalau kuna barabara hata moja inayounganisha maeneo hayo muhimu kwa uchumi na Makao Makuu ya Mkoa wa Babati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, labda unipe fursa, katika swali lililopita nilisema barabara inayoanzia Kilindoni na wakati huo tunaongelea mawasiliano kati ya Mafia na Kisiju. Sikuongelea barabara kutoka Kilindoni kwenda Kisiju. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye kumbukumbu, Hansard nadhani zitakuwa zimesema sahihi. Nilikuwa naunganisha usafiri kati ya Mafia na Bara, Kisiju wakati huo tunaongelea barabara ya Kilindoni inayoanzia Kilindoni, ambayo sasa amesema inaishia Rasinkumbi na hiyo barabara tumeanza kuijenga. Nilitaka tu niliweke sawa ili liweze kueleweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuje kwenye barabara ya kutoka Naberela hadi Kiteto. Naomba kuchukuwa fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikai hii ya Awamu ya Tano tuna dhamira ya dhati ya kuhakikisha Mkoa wa Manyara nao unaingia katika ramani ya barabara za lami ukiacha ile Barabara Kuu ambayo inatoka Arusha kupitia Babati na kuja Singida. Nako huko tunaingiza katika ramani ya barabara za lami. Nimhakikishie kwamba hii barabara ambayo nilijibu katika swali langu la msingi kwamba, tunaanza kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, hii inayopita Kiteto kwenda Arusha na inayounganisha Mkoa wa Dodoma, hiyo nao ni sehemu ya kuhakikisha Mkoa wa Manyara tunaufungua katika kuuwekea barabara ya lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika miaka hii mitano tutafanya kazi ya uhakika kuhakikisha eneo hili tunaliweka sawa na tunajenga baadhi ya barabara ambazo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi tulishaainisha.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa umuhimu huohuo wa wanawake wa Mkoa wa Morogoro kupata mikopo kutoka Benki ya Wanawake, Mkoa wetu wa Manyara, wanawake wengi ni wa kutoka jamii ya wafugaji na jamii ya wafugaji hawana elimu pana ya kukopa katika vyombo vya benki hasa tutakapokuwa tumefikiwa na Benki ya Wanawake. Je, Wizara ina mkakati gani kuhakikisha kwamba inaandaa mafunzo ya ujasiriamali pamoja na elimu ya uelewa ili wanawake wa jamii ya kifugaji nao waweze kunufaika na Benki ya Wanawake?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tuna changamoto ya kuwafikia wanawake ambao wako katika jamii za wafugaji lakini pia wanawake wenye ulemavu. Kwa hiyo, ni jambo ambalo tayari nimeshatoa maelekezo kwa Benki ya Wanawake kwamba wakati tunapotoa huduma zetu pia lazima tuwe na huduma maalum kwa wanawake walio pembezoni ikiwemo walio katika jamii za wafugaji. Pia nimeshatoa maelekezo kwa Benki ya Wanawake, tuwe na huduma mahsusi kwa ajili ya wanawake wenye ulemavu na nataka kumthibitisha Mheshimiwa Umbulla na Waheshimiwa Wabunge wanawake wengine ili msiweze kusimama tena kuuliza maswali ya nyongeza kwamba kuwawezesha wanawake kiuchumi ndiyo kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano, tunapozungumzia masuala ya usawa wa jinsia, tutajikita tu katika kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii imetokea kutokana na takwimu ambazo tunazo kwamba, kwa mfano wanawake ambao wanatumia huduma mbalimbali za benki ni asilimia 51 ukilinganisha na wanaume wanaotumia huduma za benki ni asilimia 63. Kwa hiyo, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa sababu ni Mjumbe wa High Level Panel on Women’s Economic Empowerment (Jukwa la Kimataifa la Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi), ameanzisha jitihada mahsusi za kuhakikisha kwamba wanawake wa Tanzania hasa walio vijijini wanafungua akaunti katika benki mbalimbali nchini, ameanza na akaunti inayoitwa Malaika Account. Lengo la Mama Samia pia ni kutoa elimu kwa wanawake ili waweze kujua masuala mbalimbali ya ujasiriamali na kauli mbiu yake anasema „usinipe samaki nipe nyavu na elimu ili niweze kuvua‟. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, tunaamini kupitia yeye tutaweza kuwafikia wanawake mbalimbali hasa walio vijijini.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zote za Serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi vijijini zinapita kwenye Halmashauri za Wilaya na katika vikao vya Halmashauri za Wilaya hasa Kamati hiyo ya Fedha na Mipango Wabunge wa Viti Maalum hawashiriki na ndiyo watu wenye dhamana na maendeleo ya wanawake.
Kwa kuwa sheria hiyo iliyotungwa ambayo inawakataza Wabunge wa Viti Maalum kuingia kwenye Kamati hizo ilitungwa zamani sana kabla hata utaratibu wa Ubunge wa Viti Maalum haujaanza bali kulikuwa na Wabunge wa Majimbo na Wabunge wa Kuteuliwa na Rais; na kwa kuwa mwaka jana kwenye Bunge la Kumi, Mheshimiwa Mwanri aliyekuwa Naibu Waziri alipokuwa anajibu swali hapa Bungeni, alitueleza kwamba sheria hiyo ni kandamizi na tunahitaji kuileta hapa Bungeni ili tuirekebishe Wabunge wa Viti Maalum washiriki.
Je, Serikali italeta lini hiyo sheria ili Wabunge wa Viti Maalum waweze kushiriki katika Kamati hii muhimu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Halmashauri zetu za Wilaya hasa kwa Mkoa wetu wa Manyara zinatenga asilimia kumi za fedha kwa ajili ya miradi ya wanawake. Utaratibu na mfumo wa utoaji wa fedha hizo kwa ajili ya miradi ya wanawake hauko vizuri na kuna upotevu mkubwa sana wa fedha hizo za Serikali.
Je, ni kwa nini Madiwani wa Viti Maalum wakisaidiana na Wabunge wao wasisimamie kikamilifu utoaji na urejeshaji wa fedha hizo ili ziweze kuwafikia walengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali kila kitu kipo kwa mujibu wa sheria na kanuni zake. Katika jibu langu la msingi katika eneo la pili nikasema mchakato unaweza ukaendeshwa kwa kuwashirikisha wadau. Hili la kuwashirikisha wadau kama nilivyosema lina umuhimu mkubwa sana. Katika maeneo mengine kwa mfano nikichukua Jimbo langu mimi la Kisarawe, Mbunge wangu wa Viti Maalum anaingia katika Kamati ya Fedha na sehemu zingine wanaingia katika Kamati hii, ina maana hivi sasa katika zile nafasi mbili Mwenyekiti anaweza akateua Mbunge wa Viti Maalum kuweza kuingia pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kusimamia fedha ni wajibu wa Madiwani na Wabunge wahusika katika eneo hilo. Kwa upana wa jambo hili, ndiyo maana nimesema wadau lazima washirikishwe. Kuna baadhi ya Majimbo, mfano Jimbo la Ilala, lina Wabunge wa Majimbo watatu, lina Madiwani wa Viti Maalum wasiopungua watano, kwa hiyo ukiangalia hapo, ndiyo maana nasema lazima wadau washirikishwe kuona jambo hilo linakaajekaaje na kuangalia ni jinsi gani tutafanya Kamati ya Fedha iweze kufanya vizuri. Kwa mfano, kwa hali ya sasa hivi ukisema Jimbo la Ilala Wabunge wote wa Viti Maalum waingie katika Kamati ya Fedha mtapata sura hapo, ndiyo maana nasema lazima sheria hiyo tuitazame kwa upana na wadau washiriki kila mmoja katika eneo lake kuangalia jinsi gani tutafanya, hilo ni jambo la msingi lakini kwa sasa hivi sheria inasimama hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu asilimia tano ya akina mama na siyo ya akina mama peke yake, ni ya vijana na akina mama. Jambo hili nililisema katika vikao mbalimbali kwamba jukumu la Kamati ya Fedha ni kuhakikisha kwamba fedha zinazokusanywa kutoka own source ziweze kuyafikia yale makundi ya akina mama na vijana. Kwa bahati mbaya hata katika kaguzi mbalimbali zilizopita hili ni miongoni mwa eneo lenye changamoto kubwa na ndiyo maana tumetoa maelekezo kuhusu suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema agenda ya kuhakikisha akina mama na vijana wanapata fedha hii ni yetu sote. Ndiyo maana bajeti ya mwaka huu criteria tuliyotumia kuhakikisha Halmashauri zote zinatengewa bajeti ni kuhakikisha kwamba wanatenga asilimia tano ya vijana na akina mama na walemavu watakuwa katika mchakato huo. Kwa hiyo, hili ni agizo la jumla kwamba kwa vile bajeti tumeipitisha basi kila Halmashauri ihakikishe inasimamia asilimia tano za akina mama na tano za vijana ziweze kuwafikia walengwa.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Taasisi nyingi za fedha zinawakwepa wakulima na wafugaji kuwapatia fursa za mikopo, lakini nashukuru katika maelezo yake sasa hivi amefafanua hasa kwa wakulima. Sasa je, Serikali ina mikakati gani hasa kuwapa wafugaji mikopo ili waweze kuendeleza mifugo yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema kilimo na mikopo iliyopo, pamoja na fursa zingine tunamaanisha vilevile ufugaji pamoja na uvuvi si kilimo cha mazao pekee.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya kutia matumaini, naomba kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kiteto kwa sehemu kubwa inakaliwa na jamii ya wafugaji ambao shule haijawa kipaumbele sana, hasa kwa watoto wa kike. Kwa sehemu kubwa ukombozi mkubwa ni kuwa na shule za bweni ambako wasichana wanaweza wakabaki shuleni badala ya kurudi nyumbani kukwepa kuolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachosikitisha ni kwamba kuna baadhi ya sekondari za kata tena za muda mrefu zenye mabweni, kama sekondari ya Ndedo na Lesoit ambazo ni za bweni na zina wasichana wengi wa Kimasai, lakini inasikitisha kwamba hizo shule za kata hadi leo hazina umeme. Na sio hizo shule tu hata Kituo cha Afya cha Osteti ambacho kinasaidia sana huduma za afya kwa akina mama hakuna umeme.
Je, ni lini Naibu Waziri sasa atachukua jukumu la makusudi kutembelea Wilaya ya Kiteto, hasa maeneo haya niliyoyataja, ili kujionea mwenyewe jinsi ambavyo sekondari hizo hazina walimu na hata maabara tulizojenga hazitumiki kwa ajili ya kukosa umeme?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba ku-declare interest kwamba nimetoa mikopo kwa takribani miaka 20 sasa katika Mkoa wangu wa Manyara. Uzoefu unaonyesha kwamba ufanisi mkubwa kwa kurejesha mikopo kwa wanawake na vijana ni katika vijiji vile vyenye umeme wa uhakika. Je, nini kauli ya Serikali kabla ya kutoa hizo shilingi milioni 50 katika maeneo haya ya wafugaji na mikoa ya pembezoni kuhakikisha kwamba vijiji hivyo vitakuwa na umeme kabla ya kusambaza hizo fedha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Mradi wa REA Awamu ya Pili ulipokamilika maeneo mengi sana ya taasisi hayakupatiwa umeme. Nitoe rai tu kwamba, REA Awamu ya Tatu inayoanza sasa itaweka kipaumbele sana kupeleka umeme kwenye taasisi za umma ikiwemo shule, sekondari, pamoja na taasisi nyingine. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Umbulla kwamba, shule ya sekondari ambayo ameitaja Lesoit pamoja na shule ya Ndedo pamoja na Kituo cha Afya cha Osteti vitaanza kabisa kupelekewa umeme kwenye mradi wa REA Awamu ya Tatu unaoanza hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nimpongeze tu Mheshimiwa Mbunge, amekuwa akifuatilia sana masuala haya, lakini nimhakikishie mbali na vituo vya afya kwa sababu viko vingi. Viko vituo vya afya katika eneo lake la Njiapanda ambako pia kuna kituo cha afya kitawekewa umeme, lakini kuna eneo la Songambele halijawekewa umeme pamoja na vituo vingi sana ikiwemo na vijiji vya katikati na vyenyewe vitapatiwa umeme katika REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda kutembelea, kwa ridhaa yako, mara baada ya Bunge tufuatane na Mheshimiwa Mbunge moja kwa moja ikwezekana tuanze kukaa hata kabla ya kuanza kutembelea maeneo yake.
Kuhusiana na vijiji ambavyo vitapewa mikopo au ruzuku ya shilingi milioni 50 kupata umeme. Tutaanza kuvipatia umeme, tutakaa na wenzetu wa TAMISEMI ili kusudi shilingi milioni 50 zisiende bure, ili waanze kutumia umeme mara watakapoanza kupata pesa hizo.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Mimi nina swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa suala la rasilimali watu katika Wizara ya Elimu hasa kwenye vyuo vyetu na hata shule za sekondari bado ni changamoto kubwa na kwa kuwa hali hii inasababisha pia baadhi ya Waratibu wa Elimu kupangiwa masomo ya kufundisha sawasawa na Walimu wengine hali inayopelekea kuona kwamba ni kazi iliyopo nje ya job discription zao. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja sasa ya kufikiria kwa kuwa hiyo ni kazi ya ziada basi waweze kupewa posho ya ziada hawa Waratibu wa Elimu kuliko hali ya sasa ambayo wanafundisha kama Walimu wengine lakini hawana nyongeza ya mishahara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kulitambua hilo ndiyo maana sasa hivi Serikali imeamua kuweka posho ya madaraka ambayo mwanzoni haikuwepo. Kwa kipindi kilichopita tumelipa takribani shilingi bilioni 15 kwa ajili ya posho ya madaraka. Kwa hiyo, jambo hili Serikali tumelizingatia, tunalifanyia kazi na hivi sasa watumishi wale kutokana na jukumu hilo wana posho maalum kila mwezi, kuanzia Walimu Wakuu wa Shule za Msingi, Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari halikadhalika Waratibu wa Elimu wa Kata katika maeneo yetu.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa juhudi yake kubwa, amekuja mara nyingi katika Mkoa wetu wa Manyara kutatua kero mbalimbali za wananchi hasa katika sekta ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba kutoa masikitiko yangu kwamba sijaridhika na majibu ya Serikali katika swali langu hili la namba 94.
Kama tatizo liko kwa asilimia 100 katika mkoa, ina
maana kwamba lazima kwa utafiti uliofanywa na Serikali kuna vigezo vilivyoonyesha kwamba lazima kuna takwimu ambazo zinaonyesha asilimia 100 imetokana na vitu gani, hasa vifo na adhari mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu (b) ya swali langu nilitaka kupata idadi ya vifo, siyo sababu zinazosababishwa na ukeketaji kwa sababu hizo tunazijua. Nilitaka kupata takwimu ni vifo kiasi gani na maeneo gani ili sisi viongozi wa Mkoa wa Manyara tuweze kupambana, tuongeze juhudi ya
Serikali kapambana na janga hili ambalo liko kwa asilimia 100 katika mkoa wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, nini kauli ya Serikali kufuatana na hali hii mbaya katika mkoa wetu wa Manyara?
Swali la pili, kwa maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, amesema tunatumia Maafisa Maendeleo ya Jamii na Afisa Ustawi wa Jamii ili kutoa elimu kupambana na janga hili, lakini Maafisa Maendeleo ya Jamii na Afisa Ustawi wa Jamii wako siku zote na hali imefikia asilimia 100.
Sasa je, Serikali ina mikakati gani ya ziada ili kupambana na tatizo hili specifically kwa Mkoa wa Manyara ili na sisi Manyara tubaki salama?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII JINSIA NA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Namshukuru Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, kwa maswali yake ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu yetu ni kwamba
kwanza, asilimia 100 siyo kwamba ni watu wote. Ni kwamba tatizo hili lipo zaidi Vijijini kuliko maeneo ya Mijini, lakini kiwango hasa cha kitakwimu kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na
National Bureau of Statistics ni kwamba katika wanawake 100 wa Mkoa wa Manyara, basi wanawake 71 wamekeketwa. Idadi ya vifo hatukuweza kupata takwimu za idadi yake kwa
uhakikika kwa sababu vitendo vya ukeketaji vinafanyika gizani, vinafanyika kwa siri na utamaduni umebadilika, badala ya kuwakeketa kipindi kile cha usichana mdogo, sasa hivi wanakeketa watoto wachanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mbinu mpya
ambayo wamegundua, wanawakeketa watoto wakati wakifanya tohara kwa watoto wa kiume. Kwa hiyo, wanawachanganya, inakuwa kama ni sherehe ya tohara inayokubalika kisheria kwa watoto wa kiume wanawaunganisha na watoto kike. Kwa hiyo, kuna mbinu nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kujibu maswali yake, najibu tu yote kwa pamoja mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi akizungumza hapa, aligusia Legal Anthropology. Sisi kwenye tiba tunazungumzia Medical Anthropology, sasa tunapo-approach tatizo pamoja na kuwa na sheria, pamoja na kuwa na mambo mengine, hatuwezi kujikita kwenye sheria peke yake, ni lazima tuitazame jamii nzima holistically, lazima tuitazame jamii nzima kwa ujumla wake. Tuzitazame mila na desturi za jamii husika, tutazame namna ya kupenya kwenye hiyo jamii ili kuufikisha ujumbe wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa msingi huo, tumekuja na mkakati mpya sasa wa kutumia mbinu inaitwa kwamba alternative right of passage. Kwa sababu kwenye mila za kukeketa, imebainika kwamba ni lazima zifanywe na jamii
zinazofanya mambo hayo kwa sababu wanataka kuwagraduate watoto wa kike kutoka kwenye status ya usichana na kwenda kwenye status ya uanamke. Sasa kama wasipokeketwa, wanaume wanakataa kuwaoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili ku-address hili tatizo, huwezi kutumia sheria peke yake, ni lazima uelewe sababu hizo na sasa mbinu yetu mpya ya ARP (Altenative Right of Passage) tunaitumia kwa maana ya kuyafikia viongozi
wa kimila na watu mashuhuri kwa jamii husika ili kufikisha ujumbe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo namshauri Mheshimiwa Martha Umbulla na viongozi wote wa kimila na Kiserikali katika Mkoa wa Manyara kuanza kuhamasisha jamii yao kuachana na mila hizi kwa hiari na kwa kuwaelewesha kuliko kutumia zaidi nguvu. Ahsante.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mara nyingi Jeshi la Polisi linapohitajika kuwahi kwenye matukio ya kuwalinda raia na mali zao wanapata shida sana ya kuwahi kwenye matukio hayo kutokana na matatizo waliyonayo kwenye magari yao, magari mengi yanakosa matairi, mafuta na ni mabovu, tatizo hilo ni karibia nchi nzima lakini nazungumzia katika Mkoa wangu wa Manyara. Je, Serikali ina mpango gani mahsusi kabisa wa kuhakikisha kwamba magari ya Jeshi la Polisi yanakuwa na vifaa hivyo muhimu ili kuhakikisha kwamba ulinzi wa raia na mali zao unakuwa wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba tuna changamoto ya upungufu wa vitendea kazi kwa ujumla katika Jeshi letu la Polisi na hii inatokana na ufinyu wa bajeti tulionao. Tutajitahidi katika bajeti ya mwaka huu kuongeza fedha kwa ajili ya matumizi kwa Jeshi la Polisi ili tuweze kukidhi mahitaji hayo, siyo tu kwa Mkoa wa Manyara pia kwa nchi nzima kwa ujumla wake.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba pia nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, nina maswali madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, wakulima hasa wa jamii ya wafugaji wanapopelekewa pembejeo kwa maana ya mbegu, mbolea na madawa, pale ambapo hawana maelekezo mazuri ya uelewa wanazikataa pembejeo hizo na hivyo kuwanufaisha wale mawakala kwa kujinufaisha kuziuza tena.
Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha kwamba wanapowapelekea pembejeo wakulima wa jamii ya wafugaji na wengineo ambao hawana uelewa mzuri wanawaelekeza vizuri ili waweze kunufaisha kilimo chao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Tarafa ya Dongobesh katika Wilaya ya Mbulu kwa msimu uliopita hawakupelekewa kabisa mbolea na mbegu na dawa kwa ajili ya pembejeo za kilimo kwa msimu uliopita. Nini kauli ya Serikali pale ambapo inatokea tatizo kama hilo hasa tukiwa katika harakati za kuboresha kilimo tunakoelekea kwenye Tanzania ya viwanda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba jamii za wafugaji lakini vilevile Watanzania walio wengi/wakulima hawana ufahamu mzuri kuhusu umuhimu na namna ya kutumia mbolea kwa ajili ya kuendeleza kilimo chao. Katika kushughulikia changamoto hii Serikali imekuwa ikiimarisha huduma za ugani ili wananchi waweze kupata elimu na ufahamu mzuri ili waendelee kutumia mbolea kwa namna inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa - Halmashauri zetu, tunaendelea kutoa miongozo ile vile kutoa elimu kwa Maafisa Ugani ili waweze kutoa taarifa sahihi na elimu inayotakiwa kwa ajili ya wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile katika kuhakikisha kwamba huduma za ugani zinaendelea kuboreshwa, Wizara yangu imebuni Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDPII) ambao utekelezaji wake unaanza katika mwaka wa fedha na moja kati ya masuala yanayotiliwa mkazo sana ni masuala ya ugani na tunategemea kuendelea kuimarisha vituo vya rasilimali za kata (World Resource Centre) ili ziendelee kutoa teknolojia muhimu ya kilimo na elimu ili wananchi waweze kuweza kutumia mbolea na kufanya kilimo ambacho kinakuwa na tija zaidi.
Pia Wizara kwa sasa imejipanga kutumia huduma za ugani mtandao (E-extension services) ili iwe rahisi hata kwa kutumia tu simu za mikononi wananchi waweze kupata taarifa muhimu kuhusiana na namna ya kutumia mbolea lakini vile vile kuhusiana na taarifa zingine muhimu za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la nyongeza
la pili kuhusiana na kata ya Dongobesh kutopata pembejeo katika msimu uliopita, nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika msimu uliopita siyo maeneo yote nchini yalipata pembejeo za kilimo zile za ruzuku, kwa sasa Wizara imejipanga ili makosa kama haya na upungufu kama huu usitokee tena, kuhakikisha kwamba mbolea inapatikana dukani kama CocaCola.
Waheshimiwa Wabunge, wote mnakumbuka kauli maarufu ambayo Waheshimiwa Wabunge najua mnaipenda sana ya Mheshimiwa Mwigulu alipokuwa Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, hilo alilokuwa anasema limetima kuanzia msimu unaokuja mbolea ya DAP na UREA itapatikana nchi nzima kwa bei ambayo itakuwa na dira ili kuhakikisha kwamba hatutakuwa tena na upungufu na bughudha zingine ambazo zimekuwa zikitupata katika kusambaza pembejeo za kilimo. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ya jumla kuhusu swali hili. Pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa takwimu za vifo vya akinamama vinavyotokana na uzazi katika Mkoa wa Manyara vinaongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mfano, mwaka 2015 tulikuwa na vifo 38, mwaka 2016 vifo 49 na nusu mwaka tu ya 2017 tayari vifo 23.
Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake amesema wameanzisha Benki ya Damu katika Mikoa ya Geita, Simiyu, Mara na Kigoma na sijasikia Mkoa wa Manyara; na kwa kuwa pia amesema wamejengea uwezo Wahudumu wa Afya nchi nzima bila kutaja Manyara. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana nami kwenda katika Mkoa Manyara kuangalia hali hii ikoje ili kupatia ufumbuzi wa haraka janga hili katika mkoa wetu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vifo vingi
vya watoto wachanga vinatokana na kukosa na huduma upasuaji na huduma ya damu kwa ajili ya akinamama wajawazito; na kwa kuwa pia amesema kwamba wamewezesha vituo 159 nchi nzima bila kutaja katika hivyo 159 vingapi vipo Manyara na katika vituo vya afya 106 vilivyojengewa uwezo kwa njia ya mafunzo hajataja Manyara. Je, anaweza akaniambia kwamba hali ikoje katika kuwezesha vituo vya upasuaji katika mkoa wetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mama yangu mpendwa, Mheshimiwa Martha Umbulla kwa kufuatilia kwa ukaribu sana mambo yanayohusu Sekta ya Afya kwa Mkoa wa Manyara hususani mambo yanayohusu wanawake na watoto kwenye mkoa wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, halikuwa
swali per se, nikubaliane naye niko tayari kwenda Manyara wakati wowote atakapoona inafaa. Nimkumbushe tu kwamba toka nimeteuliwa kuwa Naibu Waziri nimeshafika Mkoa wa Manyara zaidi ya mara tatu na nimefika mpaka anapokaa yeye, jirani na nyumba anayoishi pale Dongobesh.
Mheshimiwa Spika, bahati mbaya yeye hakuwepo
lakini nimefika mpaka Dongobesh, nimefika mpaka kwenye kituo cha afya ambacho yeye Mbunge wa Viti Maalum na rafiki yangu Mheshimiwa Flatei Massay wanajenga na nikawapongeza sana kwa jitihada wanazofanya za kujenga kituo kile cha afya na kuleta hizi huduma za upasuaji karibu zaidi na wananchi wa Dongobesh. Niwashukuru kwa kunipa Uchifu wa pale Dongobesh na kunivalisha yale mavazi yenu ya kimila. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilipofika pale niliguswa na nikajitolea mimi mwenyewe bati 100 kwa ajili ya kuwasaidia kwenye jitihada hizo. Kwa hivyo, akiniambia specifically nitaje vingapi, sikumbuki ni vingapi tulivyonavyo pale, lakini nafahamu Mkoa wa Manyara wanafanya jitihada kubwa sana za kuboresha huduma za Mama na Mtoto hususani kwa kupandisha hadhi zahanati zao kwenda kwenye vituo vya afya na mimi mwenyewe nimefika pale nikashuhudia mradi wao huu wa pale Dongobesh.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, niruhusu tu nifanye utafiti nitampa majibu ya statistics anazozitaka baadaye kwamba ni vituo vingapi hasa. Hata hivyo, azingatie agizo ambalo nililitoa mimi mwenyewe nikiwa Mwandoya kwa Mheshimiwa Mpina, ambapo nilisema kwamba, Halmashauri zote nchini wahakikishe wanapandisha hadhi vituo vyao vya afya ambavyo vilikuwa havitoi huduma za upasuaji sasa vianze kutoa huduma za upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni. Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuna damu salama na kuna huduma za uchunguzi wa magonjwa katika ngazi ya kituo cha afya.
Mheshimiwa Spika, nilisema pia kwamba kama kuna kituo ambacho kitakuwa hakijakidhi matakwa haya ya sera, maana yake tutakishusha hadhi kiende kuwa zahanati badala ya kukiita kituo cha afya jina tu wakati hakitoi huduma za kituo cha afya. Nilitoa miezi sita ambayo inakwisha sasa hivi. Miezi hii mitatu inayofuata, natuma timu yangu ya wataalam kwenda kukagua kwamba ni Halmashauri zipi zimetekeleza agizo lile, agizo la Mwandoya. Ma– DMO, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya wote nchini wanajua.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, kituo ambacho kitakuwa hakijakidhi hayo masharti, nitakishusha hadhi. Kwenye lile agizo langu nilisema nitapeleka taarifa yangu kwa Mheshimiwa Rais mwenyewe kwamba hawa ndiyo wateule wake ambao wanakubaliana na vifo vya akinamama wajawazito kwa sababu hawataki kutekeleza agizo ambalo lingeokoa maisha yao. Nina uhakika Mheshimiwa Rais atachukua hatua. Nimejibu kwa upana ili kuwakumbusha.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu upasuaji, kwa sehemu nimelijibu. Kuhusu damu salama, kwa Mkoa wa Manyara kwa ujumla wake kwenye bajeti hii inayokuja, tumeweka kama Mkoa wa kipaumbele kwa ajili ya kuanzisha Benki Salama ile kubwa.
Mheshimiwa Spika, nilipofika pale Manyara miezi sita iliyopita nilihakikisha wana damu ya kutosha, lakini niliona kuna RMO pale alikuwa anasinziasinzia hivi kutekeleza mpango huu, tulishauriana na wenzetu wa TAMISEMI na tulikwishamtoa.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru sana Serikali kwa juhudi kubwa ya kujenga barabara nyingi za lami hapa nchini, lakini naomba nioneshe masikitiko yangu kuhusu uwiano wa barabara za lami hapa nchini, kwa sababu, tunajua baadhi ya wilaya zina barabara za lami vichochorini hadi katika vijiji mbalimbali. Katika mkoa wetu wa Manyara, hususan Wilaya za Kiteto, Simanjiro na Mbulu, hakuna barabara ya lami inayounganisha Makao Makuu ya Wilaya na Makao Makuu ya Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, labda tukiacha Wilaya ya Hanang ambayo kwa bahati imepitiwa na Barabara ya kutoka Singida, Babati, Arusha, tunaomba kwa kuwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kuna barabara ambazo Serikali imedhamiria kujenga; kwa nini Serikali isiweke kipaumbele kuhakikisha kwamba, barabara zilizoko kwenye Ilani ya Uchaguzi kwa kulenga zile Wilaya ambazo hakuna barabara za lami zinazounganisha makao makuu ya mkoa na Makao Makuu ya Wilaya? Kwa nini isitoe kipaumbele ikajenga barabara za lami, hususan lami kutoka Wilaya ya Kiteto – Kibaya hadi Makao Makuu Babati? Lami kutoka Mbulu hadi Babati na lami kutoka Simanjiro – Orkesmet hadi Babati? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nilipokee hili suala la kuangalia uwiano kama ushauri, lakini yako mambo ambayo lazima tuyatazame wakati tunakamilisha ujenzi wa barabara, kwa sababu eneo hili analolizungumza Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba kuna uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na mifugo. Mimi nilipata brief ya mkoa juu ya network ya barabara za Manyara na niseme baada ya Bunge hili pia nitakwenda kwa ajili kuangalia miradi inayoendelea, lakini pia kuweza kuona siku za usoni tuweze kukimbizia hii barabara iweze kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikiri tu kwamba, Serikali ya Awamu hii ya Tano imefanya kazi kubwa, kwa sababu barabara za lami zilizotengenezwa katika kipindi cha miaka miwili zenye urefu wa kilometa 1,500 si haba, kiasi cha shilingi trilioni 1.8 kimetumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kukamilika kwa barabara hizi ni fursa pia, ya kwenda kushughulikia barabara nyingine ambazo tayari shughuli za upembuzi yakinifu zinaendelea, zitakapokamilika tuweze kwenda kujenga barabara hizi. Ahsante.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza naomba nimpongeze sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kuridhisha. Pia nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali yetu kwa kuipandisha hadhi Hospitali ya Haydom kuwa Hospitali ya Rufaa Ngazi ya Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na upandishwaji hadhi huko, ni kwa nini Serikali yetu isione umuhimu wa kuhakikisha kwamba inajenga miundombinu ya hospitali hii muhimu inayohudumia mikoa zaidi ya mitatu hasa katika suala la upatikanaji wa maji, jambo ambalo ni muhimu sana? Amekiri mwenyewe kwamba source ya maji sasa hivi ni umbali wa kilometa 25 kutoka hospitali kwa kutumia jenereta ambayo inakabiliwa na uharibifu wa mara kwa mara. Suala la REA Awamu ya Tatu linachukua muda mrefu, tungeomba Serikali ifikirie kupeleka umeme katika hospitali hii muhimu kabla ya hata REA kufikia eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, suala la income tax kwenye posho za watumishi wa Hospitali ya Haydom tayari ameshaonyesha kwamba kuna tabaka mbili ya watumishi katika hospitali hiyo, lakini ukweli na utafiti unaonyesha kwamba baadhi ya watumishi katika Hospitali za Wilaya na kwingineko katika nchi yetu hawakatwi kodi kwenye on-call allowances lakini hawa watumishi wa Haydom wanakatwa na hasa tukizingatia kwamba wanafanya kazi katika mazingira magumu sana. Tunaomba Serikali itoe kauli katika hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Umbulla, naomba kwa moyo wa dhati kabisa nimpongeze kwa jinsi ambavyo amekuwa akipigania wananchi wa mkoa wake lakini bila kusahau hata Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo jinsi ambavyo wamekuwa wakiipigania hospitali yao hii ya Haydom. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maswali yake ya nyongeza anasema kwamba ufanyike utaratibu wa haraka ili kuwezesha kupatikana umeme kabla ya REA.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, utaratibu wa haraka kabisa na chanzo cha uhakika ni kwa kutumia REA Awamu ya Tatu, nadhani ndiyo njia sahihi. Kwa taarifa tulizonazo Serikalini ni kwamba tayari mkandarasi yupo kule. Kwa hiyo, tuvute subira, kama mmesubiri muda wa kutosha, kipindi kilichobaki ni kifupi na tatizo hili litakuwa limeondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na watumishi ambao wameajiriwa na Hospitali hii ya Haydom kukatwa on-call allowance. On-call allowance inakatwa kwa sababu wao katika malipo ambayo wanafanya, wanajumuisha pamoja na mshahara wao na ukisoma ile Sheria ya Income Tax, unapotaka kukata kodi lazima utizame vyanzo vyote, ni tofauti na hawa wa Serikalini ambao allowance hizi huwa zinalipwa dirishani, hazisubiri mpaka kipindi cha kuja kulipa mshahara wa mwisho. Kwa hiyo, ni namna tu watakavyojipanga wakaji-adjust inawezekana kabisa wasikatwe hicho wanachokatwa. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona na namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa majibu yake kwa maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni vizuri tuweke rekodi sawasawa. Bunge hili kupitia Finance Act ya mwaka 2011 liliongeza misamaha kwa posho mbalimbali. Katika vitu vilivyoongezwa kwamba vitasamehewa kodi ya mapato ni allowance payable to an employee who offers intramural private services to patients in a public hospital and housing allowance, transport allowance, responsibility allowance, extra duty allowance and honoraria payable to an employee of the Government or its institution whose budget is fully or substantially paid out of Government budget subvention. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, allowances hizi ndizo zilizosamehewa kodi kwa mujibu wa sheria na TRA hiki ndicho wanachofanya. (Makofi)
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vifo vya wanawake wanapokwenda kujifungua katika mikoa yetu tunaposomewa, kwenye RCC bado iko juu sana na tena kwa muda mrefu sasa na hii ni kutokana na kukosa vifaa tiba, vitendanishi na huduma stahiki kwa ajili ya kujifungua. Je, sambamba na ukarabati wa zahanati na vituo vya afya sasa hivi kama mkakati wa Serikali, nini kauli ya Serikali hasa kutokana na vifo hivi, takwimu hizi ambazo zipo kwa muda mrefu, mama kwenda kujifungua anafariki?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwenye Bajeti ya mwaka huu ambapo tumetenga takribani shilingi bilioni 183, mahsusi kwa ajili ya kununua dawa na vifaatiba, nina hakika kwenye mwaka huu wa utekelezaji utakaoanza Julai Mosi, mambo yatabadilika sana kwenye sekta ya afya, hususan kwenye eneo la dawa, vifaa, vifaatiba na vitendanishi na hivyo nimtoe shaka Mheshimiwa Umbulla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla wake niseme tu kwamba matatizo na changamoto ambazo zinawapata akinamama wajawazito na watoto, kipindi kile cha puerperium cha kujifungua na cha kunyonyesha, yatatatuliwa tu endapo tutafanya mabadiliko makubwa kwenye mfumo mzima wa afya, hususani kuwekeza zaidi kwenye mfumo wa afya ya msingi, kwa maana ya kuziwezesha zahanati na vituo vya afya ziweze kufanya kazi ipasavyo.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hamasa kubwa kwa vijana waajiriwa katika shule zetu hasa za maeneo ya pembezoni pamoja na vituo vya afya na zahanati, ni kule kuwepo kwa mitandao ya simu na umeme wa uhakika, kwa kuwa vijana wetu kwa kweli wanapenda kutumia simu za mikononi katika mitandao hiyo kwa uhakika; na kwa kuwa maeneo yetu ya vijijini hasa katika Mkoa wetu wa Manyara na kwingineko maeneo ya pembezoni, huduma hiyo ya umeme na mitandao ya simu haipo.
Je, Serikali hasa Wizara ya Utumishi ina mikakati gani mahususi ya kuwa na mawasiliano ya karibu kuhakikisha kwamba katika maeneo ya pembezoni katika shule hasa za sekondari na vituo vya afya kunakuwepo na umeme ili kutia hamasa ya waajiriwa waendelee kuishi maeneo hayo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nipende tu kusema kwamba kwa utafiti uliofanywa na bodi yetu ya mishahara katika utumishi wa umma mwaka 2014/ 2015, moja ya changamoto ambazo zilibainika, kwanza katika mazingira haya magumu inategemeana na sekta kwa sekta maeneo mengine jiografia, hali ya miundombinu, huduma za kijamii zilizopo; lakini pia nafurahi kwamba ametaja suala zima la mitandao ya simu pamoja na umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipende kumuhakikishia tu kwamba kupitia ripoti ile ya utafiti tulitoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, lakini pia tumewasilisha katika Wizara husika ikiwemo Wizara ya Nishati na nyinginezo kuhakikisha kwamba wanapopanga mipango yao ya maendeleo basi wanatoa vipaumbele katika maeneo haya yenye mazingira magumu.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwanza mimi niishukuru Serikali kwa kujenga na kukamilisha barabara ya Dodoma hadi Babati kwa ufanisi na sasa inatumika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, cha kusikitisha ni kwamba vyombo vya usafiri kutoka Dodoma, Singida, Babati wanatoza nauli kiasi cha shilingi 17,000 hadi shilingi 20,000 na wanatoza kiasi hichohicho kutoka Dodoma kupita Kondoa kwenda Babati, umbali ambao ni sawa na Dodoma kwenda Iringa kwa gharama ya shilingi 8,000 hadi shilingi 10,000 tu.
Je, Serikali iko tayari kurekebisha hitilafu hiyo ili wajasiriamali wetu sasa watoke Babati asubuhi kuja kufanya ujasiriamali katika Jiji la Dodoma kwa ufanisi na kwa nauli nafuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia suala la nauli kwa wananchi kwa ujumla lakini pia kwa kufanya mchanganuo ambao nimemsikiliza hapa.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba pale nauli zinapopanda zinawiana na ubora au ubovu wa barabara. Kwa hiyo, yaweza kuwa labda watumiaji wa barabara hiyo walikuwa wamekariri nauli kubwa wakati barabara haikuwa nzuri.
Kwa hiyo, nizichukue pongezi zake lakini hili suala tutalifanyia kazi, ziko mamlaka zinazoshughulika na masuala ya nauli ili waweze kuona stahili kamili ya nauli katika barabara hii Mheshimiwa Mbunge aliyoitaja ili tuweze kuchukua hatua zinazostahili. (Makofi)
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kama lilivyo suala la madini katika Jimbo la Mbogwe, Mkoa wetu wa Manyara maeneo mengi yana madini kulingana na utafiti uliofanyika. Hivi sasa uchimbaji huo unafanywa kiholela na sina hakika kama Serikali ina mkakati wowote ama ina taarifa na suala hilo. Je, Serikali sasa iko tayari kutupa takwimu ama hali halisi ya madini yaliyoko katika Mkoa wetu, Wilaya za Mbulu, Simanjiro na Kiteto?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felister Bura, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Bura atakumbuka kwamba wakati tunawasilisha bajeti yetu pamoja mambo mengine tulitoa machapisho na majarida mbalimbali ambayo ndani yake yalikuwa yanatoa takwimu kwa ujumla kwenye sekta ya madini kwa kila Mkoa, Wilaya na maeneo mbalimbali. Naamini Mheshimiwa Bura akienda kukapitia kale kakijitabu atapata taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hili jambo lingine ambalo ameeleza juu ya wananchi kuchimba kwenye maeneo mbalimbali kwenye Mkoa Manyara. Niseme kwamba Serikali inazo taarifa za wachimbaji wadogo kuvumbua. Mara ugunduzi unapotokea, kazi yetu ya kwanza ni kupeleka usimamizi ili kudhibiti usalama lakini vilevile kudhibiti mapato ya Serikali. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Bura ugunduzi wowote unaotokea katika Mkoa wa Manyara tunafahamu na tayari kuna usimamizi ambao unafanywa na Ofisi zetu za Madini kwenye Kanda pamoja na Mikoa.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza na mimi nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya na kwa majibu yake mazuri.
Kwa kuwa umeme wa REA kwa sehemu kubwa inapopita katika Wilaya zetu za Mkoa wa Manyara zikiwepo Mbulu vijijini, zinapita katika barabara kuu na kuacha pembeni taasisi muhimu kama shule, zahanati na nyinginezo:-
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba umeme huu sasa ujaribu kwenda vijijini zaidi ili iweze kunufaisha shule za sekondari, zahanati na taasisi nyingine muhimu na huko ambako kuna wananchi walio wengi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Umbulla ambapo kwa kweli ameuliza swali la msingi, lakini tangu mwanzo baada ya kubaini changamoto ya REA I na REA II tumetoa maelekezo. REA Awamu ya Tatu taasisi zote za Umma alizozitaja ziwe zipaumbele. Kwa hiyo, naomba niendelee kusisitiza kwa wakandarasi, wasimamizi wa miradi yote, Mikoa na Wilaya walitekeleze hilo kwa wakati na kwa usimamizi wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ili Wabunge wasiendelee kuuliza swali kama hili, ni kwamba densifications awamu ya pili inaanza hivi karibuni katika mikoa 11. Densification hii maana yake ni ujazilizi, yale maeneo ambayo yamerukwa yatapatiwa umeme katika awamu inayoanza mwaka 2018/2019. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa sababu mmeshapitisha bajeti, msiwe na wasiwasi.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa walengwa wa mikopo hii ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri zetu wanapewa kwa makusudi ya kufanya biashara ili waweze kuzirejesha baada ya kupata faida. Je, walengwa hawa ambao ni wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wametayarishwa kwa kiasi gani ili waweze kuelewa masharti ya mikopo hiyo, aina ya biashara wanazopaswa kufanya, lakini zaidi sana elimu ya ujasiriamali kwa sababu mwishowe watahitajika kurejesha kwa faida? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kutokana na majibu ya Naibu Waziri kwamba malengo ya kutoa mikopo hii ni kuwapa watu wa hali ya chini sana katika nchi yetu; na kwa kuwa kuna baadhi ya kaya maskini hapa nchini ambazo zinaongozwa na wanaume pia ambao wanahitaji msaada, je, Serikali ina kauli gani kuhusu kaya hizo ambazo zinaongozwa na wanaume ambao wanahitaji pia kupata msaada kutokana na asilimia 10 ya mapato ya halmashauri zetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala zima la elimu, ni ukweli usiopingika, maana wanasema kwamba, ‘mali bila daftari hupotea bila taarifa,. Ni wajibu wa Maafisa Ushirika na Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha kwamba watu wetu wanapata elimu juu ya kuanzisha biashara na namna nzuri ya kuweza ku-keep record ili wajue hicho kiasi ambacho wanakopa kinatumikaje ili waweze kurejesha kwa wakati kitumike kwa wengine.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla yeye mwenyewe amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba elimu inatolewa. Si elimu tu peke yake lakini amekuwa akisimamia mfuko ambao umekuwa ukifanya vizuri katika eneo la Mkoa wa Manyara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili, ni imani yetu kwamba pale ambapo unamwezesha mama unaiwezesha familia. Ni matarajio yetu kwamba akina mama katika mikopo hii wanayopata hawawaachi waume zao pembeni, kwa hiyo tunakuwa tunaiwezesha familia kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba pale ambapo kuna ushirikiano kati ya baba na mama hakika familia hiyo husimama. Ni matarajio yetu kwamba baada ya kuwatosheleza akinama tutatizama pia upande wa akina baba kama haja itakuwepo.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Ni azma ya Serikali kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa na Wilaya mbalimbali. Mkoa wetu wa Manyara ambao una Makao Makuu Babati hakuna barabara ya lami inayounganisha Wilaya za Kiteto na Simanjiro na nyakati zingine hazipitiki kutokana na hali mbaya ya barabara hizo kuwa za vumbi na kwa kuwa iko kwenye Ilani kwa muda mrefu. Je, ni lini Serikali sasa itaunganisha barabara kutoka Simanjiro na Kibaya kuja Babati kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nilihakikishie Bunge Tukufu kwamba utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi unaendelea ambayo imeelekeza ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami; na hasa hasa nikitaja barabara ambayo inatoka Kilindi inapita Kiteto inakuja mpaka Dodoma huku Kondoa ambayo ni barabara kumbwa sana itaanza kutengenezwa hivi karibuni chini ya usimamizi wa Wizara ya Ujenzi. Hii barabara ya kutoka Babati kwenda mpaka Simanjiro na ile aliyoitaja nyingine tunaziangalia kwa karibu sana na ndiyo maana matengenezo yake huwa ni ya uangalizi wa juu kabisa chini ya usimamizi ya Mkuu wa Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wake umepelekea barabara hizo kuimarika na kwa sasa zinapitika muda wote wa mwaka isipokuwa matengenezo madogo madogo kama kuna mvua kubwa sana. Kwa hiyo nimhakikishie kwamba utekelezaji utafanyika, naomba tu wananchi wawe na subira.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa kusambaza umeme maeneo mengi katika nchi yetu lakini najua kipaumbele moja wapo cha Serikali ni kulenga zile Taasisi zenye kutoa huduma za jamii kama shule, zahanati nakadhalika. Shule ya sekondari ya Bama iliyoko Kata ya Nangwa Wilayani Hanang licha ya kuomba kwa muda mrefu hadi leo juhudi za kuomba huo umeme haujazaa matunda. Ni nini tatizo ambalo linasababisha sekondari hiyo isipate umeme hadi leo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake la nyongeza Mheshimiwa Martha. Kwanza nimpongeze kwa sababu amefuatilia sana kuhusu shule hii, lakini nieleze tu shule hii ipo karibu sana na umeme takribani nusu ya kilomita na tumekuwa tukifuatilia sana halmashauri ile iweze kulipia ili umeme uweze kuingia kwenye hiyo shule ya sekondari. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nashukuru sana kwa kukumbushia hili lakini na mimi nitoe maelekezo wa Mkurugenzi wako na Mwenyekiti wa Halmashauri alipe gharama za kuunganishiwa umeme ili shule hiyo ipate umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kwa Waheshimiwa Wabunge kwa niaba ya Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri zote nchini wahakikishe wanatenga fedha mahususi kwa ajili ya kuingiza umeme kwenye Taasisi za Umma, hapa tuna maana shule, vituo vya afya, zahanati na Taasisi nyingine. Imekuwa ni changamoto kubwa sana tunapokwenda maeneo yale unakuta shule ipo karibu umeme lakini halmashauri haijalipia. Basi nitoe rai hiyo ili wafanye hivyo ziweze kuunganishiwa umeme na shule ambazo ziko mbali hata kama kijijini hatujapeleka umeme sisi tutapeleka umeme mahususi kwa ajili ya hizo shule za sekondari na vituo vya afya. (Makofi)
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwanza nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa ajili ya kununua ndege nyinghi ili kiinua na kuboresha uchumi wan chi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa kazi kubwa anayofanya ameshafika Manyara mara kadhaa kutatua kero za sekta yake. Nina maswali mawili, kwa kuwa Serikali imeainisha kwenye Mwongozo wa mpango 2020/2021 kwamba itaboresha viwanja kadhaa vya ndege hapa nchini, lakini katika orodha hiyo kwa bahati mbaya sijaona uwanja wa ndege wa Arusha kulingana na umuhimu wake.

Je, Serikali ina mkakati gani sasa kwa umuhimu ambao tumeutaja wa uwanja huo kuboresha uwanja huo ili kukuza uchumi wa nchi yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa manufaa ya kuwa na ndege nyingi ni ndege hizo kutumika. Sasa kwa kuwa pia uwanja huu uko katikati ya mikoa mingi ikiwepo Mkoa wa Manyara, Mkoa wa Singida, Mkoa wa Simiyu, Mkoa wa Mara na hata Mkoa wa Dodoma.

Je, Serikali ina mkakati gani ili kuboresha uwanja huo na wananchi walio wengi wa mikoa tajwa waweze
kuhamasika kutumia usafiri wa ndege ili kutumia ndege zetu ambazo zinatosheleza hapa nchini kwa sasa hivi?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Arusha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipongeze majibu ya Naibu Waziri, ni kweli tumeweka bajeti kwa ajili ya kuendelea kuimarisha uwanja wa ndege wa Arusha na kama alivyozungumza tumeshaweka tender na bajeti hii ambayo sasa hivi mpango Waheshimiwa Wabunge mnaongea tutaweka bajeti kwa ajili ya kuurefusha. Na maana yake ni nini, katika kiwanja ambacho kinaongoza kuwa na ndege nyingi kiwanja cha Arusha ni cha tatu, kinarusha kwa siku zaidi ya ndege 125.

Kwa hiyo, ni biashara kubwa ndiyo maana tunataka Bombardier iende ikatue pale. Kwa hiyo, mpango wa kuboresha upo ili hiyo Mikoa ambayo umeitaja nayo iweze kufaidi kutumia usafiri wa ndege na tutaendelea kufanya hivyo Mheshimiwa Mbunge.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nami nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ya kina. Nachukua nafasi hii pia kuipongeza sana Serikali, hasa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais wetu, John Pombe Magufuli kwa jinsi ambavyo inashughulikia kwa ukamilifu migogoro mingi ya ardhi hapa nchini na hususan katika Mkoa wetu wa Manyara. Hapa pia nimpongeze sana Mheshimiwa RC wetu, Alexander Mnyeti na ma-DC wote wa mkoa huu kwa sababu migogoro hii sasa hivi inaenda ikipungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina swali moja tu la nyongeza. Hivi karibuni Mheshimiwa Rais wetu ametoa tamko kwamba kuhusiana na migogoro hii ya ardhi ya wananchi kuvamia maeneo mbalimbali kwa ajili ya makazi, kwa ajili ya kilimo na ufugaji yapatiwe ufumbuzi haraka ili kuleta utulivu na amani kwa wananchi katika maeneo mbalimbali:-

Je, Serikali imeweza kushughulikia kwa kiwango gani matatizo haya ya migogoro ya wananchi tukijua kwamba kule Manyara kuna mgogoro unaofukuta kule vilima vitatu kuhusiana na wananchi kukosa amani na kuvamia maeneo kwa ajili ya makazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naomba nipokee pongezi zangu kwa niaba ya Wizara na pongezi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Nampongeza Mheshimiwa Mbunge Umbulla kwa kutambua kazi kubwa inayofanyika na Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Alexander Mnyeti na Wakuu wenzake wa Wilaya, Wakurugenzi wote pamoja na Watumishi wa Serikali katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mheshimiwa Rais kwa mapenzi na ukarimu alionao kwa Watanzania aliamua kuunda kikosi kazi cha Waheshimiwa Mawaziri wanane, wamezunguka maeneo yote yenye migogoro, Wakuu wa Mikoa wameshirikishwa, Wakuu wa Wilaya wameshirikishwa, taarifa zikakusanywa. Kazi hii imeshafanyika, sasa wameandaa ripoti wamempelekea mwenye mamlaka ili aweze kuangalia na kutoa maelekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Tanzania kwamba, Mheshimiwa Rais dhamira yake ni kuondoa migogoro kati ya wananchi na wakulima, wakulima na wafugaji, ili kazi iendelee kuwa nzuri sana. Tumpe muda alifanyie kazi, kama ambavyo alikuwa na nia njema ya ku- control migogoro hii, tuwe na amani kwamba, migogoro itaisha na wananchi wetu watafurahi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.