Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Martha Jachi Umbulla (13 total)

MHE. FLATEI G. MASSAY (K.n.y. MHE. MARTHA J. UMBULLA) aliuliza:-
Ujenzi wa senta ya Michezo ya riadha katika Mkoa wa Manyara hususani Wilaya ya Mbulu imekuwa ni kilio cha muda mrefu kwa viongozi na wananchi wa eneo husika kutokana na vijana wengi kuwa na vipaji katika mchezo wa riadha na michezo mingine:-
(a) Je, ni lini Serikali itasikiliza kilio cha muda mrefu na kujenga senta ya michezo ya riadha Mkoani Manyara ili vijana wengi wenye vipaji waweze kunufaika?
(b) Je, Serikali haioni kuwa kwa kujenga senta ya michezo Manyara itaweza kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana wa Mkoa huo na maeneo jirani kama Singida, Arusha na Dodoma ambako kuna vipaji hivyo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Manyara na Wilaya zake una vijana wenye vipaji vya riadha na michezo mingine. Aidha, Serikali inatambua pia umuhimu wa kuwa na kituo kikubwa cha michezo hasa ya riadha ambacho pamoja na mambo mengine kitasaidia kuibua, kukuza na kuviendeleza vipaji vya vijana ikiwa ni pamoja na kuwapatia ajira vijana mkoani humo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Massay, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mkoa wa Manyara imepanga kujenga kituo cha michezo cha mkoa mara baada ya kukamilisha mazungumzo na kukubaliana na wananchi wanaomiliki ardhi katika eneo ambalo mkoa wamekubaliana. Aidha, kwa kipindi hiki ambacho uongozi wa mkoa hauna kituo cha michezo, mkoa umepanga kutumia kambi ya michezo ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwa muda, wakati wanasubiri kupatikana kwa eneo la kudumu la mkoa. Hii ni kutokana na sababu kuwa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ina hosteli na viwanja vya michezo vya kutosha.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kujengwa kwa kituo hiki katika mkoa kutaongeza ajira, kutapanua shughuli za kibiashara na hata kukua kwa uchumi wa Mkoa wa Manyara. Serikali inaendelea na mazungumzo na wananchi wamiliki wa eneo husika, yakikamilika na pesa zikipatikana ujenzi wa kituo hiki cha michezo utaanza.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Pamoja na juhudi kubwa ya Serikali ya Awamu ya Nne katika kutekeleza
ahadi ya miradi katika Ilani ya Uchaguzi bado haikuweza kukamilisha ahadi
zote ilizotoa:-
Je, Serikali ya Awamu ya Tano ina mpango gani wa kukamilisha ahadi za
miradi iliyoachwa na Serikali ya Awamu ya Nne bila kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba uniwie radhi huenda sauti
yangu leo ikaonekana nene kuliko kawaida lakini sina haja ya kumtisha mtu
yeyote. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu,
napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti
Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Nne kupitia Ilani yake ya
Uchaguzi ya mwaka 2010-2015, iliahidi kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta
za uzalishaji, miundombinu na huduma za kiuchumi, huduma za jamii na
uendelezaji wa wananchi kiuchumi. Miradi iliyopangwa kutekelezwa katika
sekta hizo ilijumuisha miradi ya muda mfupi na muda mrefu. Kulingana na aina
ya miradi, muda unaotumika kukamilisha miradi umekuwa ukivuka awamu moja
kwenda awamu nyingine ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha ahadi za utekelezaji wa miradi ya
uchaguzi ya mwaka 2010 inakamilika na kuendelea na miradi ya Ilani ya
Uchaguzi ya mwaka 2015, Serikali ya Awamu ya Tano tayari imezindua Mpango
wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Pia kupitia Bunge imekamilisha kupitisha
Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017 ambayo asilimia 40 itaelekezwa katika
miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali kupitia mipango na sera
mbalimbali za utekelezaji wa kibajeti itahakikisha kuwa miradi iliyoachwa na
Serikali ya Awamu ya Nne inaendelea kutekelezwa, na miradi ya Kiilani ya
Uchaguzi ya Awamu ya Tano nayo itatekelezwa.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Kamati za Fedha za Mipango za Halmashauri za Wilaya ni Kamati muhimu sana kwa Wabunge wote kushiriki bila kujali ni wa Viti Maalum au wa Jimbo kwa sababu zinashughulika na masuala ya fedha, bajeti na mipango ya miradi ya maendeleo; na kwa muda mrefu sasa Wabunge wa Viti Maalum wamekuwa wakiomba kuondolewa kwa sheria kandamizi na ya kibaguzi ya kuwazuia kushiriki katika Kamati hizo:-
(a) Je, Serikali iko tayari kusikiliza kilio cha Wabunge wa Viti Maalum ili kuwaruhusu kushiriki kwenye Kamati hizo?
(b) Je, Serikali iko tayari kufuta sheria hiyo kandamizi na yenye ubaguzi ambayo haina tija na hasa ikizingatiwa kuwa ilitungwa mwaka 1998 wakati ambao Ubunge wa Viti Maalum bado haujaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Halmashauri wametajwa katika kifungu cha 75(6) cha Sheria, Sura 287 ya Mamlaka za Serikali za Wilaya na kifungu cha 47(4) cha Sheria Sura 288 ya Mamlaka za Miji. Kwa mujibu wa sheria hizo mbili, Wajumbe wa Kamati hawatazidi theluthi moja (1/3) ya Madiwani wote isipokuwa Kamati ya Fedha na Mipango ambayo Wajumbe wake ni wale wanaoingia kwa nyadhifa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa Wajumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango umefafanuliwa katika Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa kila Halmashauri ambapo Wajumbe wake ni Mwenyekiti au Meya wa Halmashauri ambaye atakuwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti au Naibu Meya wa Halmashauri, Mbunge au Wabunge wa Majimbo wanaowakilisha majimbo katika eneo la Halmashauri, Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Halmashauri na Wajumbe wengine wasiozidi wawili watakaopendekezwa na Mwenyekiti/Meya kisha kupigiwa kura na Baraza la Halmashauri mmoja kati yao awe mwanaume au mwanamke. Hivyo, ili Wabunge wa Viti Maalum waweze kushiriki kwenye Kamati za Fedha tutahitaji kubadili sheria kwanza ili pendekezo hilo liweze kutekelezeka.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyoelezwa katika sehemu (a) ya jibu hili, Wajumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango wataendelea kuwa ni wale waliotajwa katika Sheria na Kanuni za Mamlaka za Serikali za Mitaa hadi hapo sheria itakapofanyiwa marekebisho kwa kushirikisha wadau mbalimbali.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Pamoja na juhudi za Serikali kupeleka huduma za umeme vijijiji vya Wilaya ya Kiteto hasa Kata za Lengatei, Kijungu, Magungu, Songambele, Ndedo na Makame, hawajafikiwa kabisa na utaratibu huu wa REA.
Je, Serikali itapeleka lini umeme katika vijiji vilivyotajwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya kata za Lengetai, Kijungu pamoja na Magungu, kama ambavyo amerekebisha Mheshimiwa Mbunge, pamoja na Songambele, Ndedo na Makame vitapatiwa umeme kupitia mradi kabambe wa REA Awamu ya Tatu unaoanza kutekelezwa mwezi Disemba, mwaka huu. Ujenzi wa mradi huu utaanza Disemba kama nilivyosema mwaka huu na utakamilika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020. Aidha, vijiji vya kata za Lengatei vikiwemo Ilala, Kijungu, Lesoit pamoja na kijiji cha Magomeni pia vitapatiwa umeme kupitia mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme kwenye Wilaya ya Kiteto itahusisha ujenzi wa njia ya msongo wa kilovolti 33 yenye urefu wa kilometa 810. Ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolti 0.4 yenye urefu wa kilometa 1,725 ufungaji wa transfoma 343 za ukubwa mbalimbali, lakini pia kuwaunganishia wateja wa awali umeme 10,800. Kazi hizi zitaanza mwezi Disemba mwaka huu na kukamilika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020. Gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 51.
MHE. MARTHA J. UMBULLA Aliuliza:-
Kulingana na takwimu za mwaka 2010 Mkoa wa Manyara unaongoza kwa mila potofu ya ukeketaji wa wanawake kwa asilimia 71 hapa nchini hali inayotisha na kuhatarisha maisha ya wanawake.
(a) Je, Serikali katika kufanya utafiti imebaini ni Wilaya zipi na vijiji vipi vinaongoza?
(b) Je, hali hii na mila hii potofu imesababisha athari na vifo kiasi gani mkoani Manyara?
(c) Je, Serikali ina mikakati gani ya dharura ya kukabiliana na mila hii potofu ili kuondoa kabisa athari za ukeketaji?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII JINSIA NA WAZEE NA WATOTO Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, lenye vipengele (a),(b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utafiti uliofanya na Serikali katika Mkoa wa Manyara, imebainika kuwa ukeketaji upo vijijini kwa asilimia 100. Wilaya karibu zote zinajihusisha na vitendo hivi hasa Wilaya ya Hanang. Makabila yanayofanya ukeketaji katika wilaya hiyo ni Wairak, Wabarbaig na Wanyaturu hasa katika maeneo ya Kata za Balanglalu na Basutu.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, athari zinazotokana mila hizi potovu ni kubwa sana kwa wanawake hususan wakatiwa kujifungua. Kwani huweza kusababisha ulemavu wa kudumu; vifo kutokana na kutokwana damu nyingi; maumivu makali kupatwa na ugonjwa wa fistula na wakati mwingine kupata madhara ya kisaikolojia. Ni vigumu kutambua vifo vinavyotokana na ukeketaji kwani hufanyika kwa siri katika jamii hiyo.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetunga sheria mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hili. Hata hivyo, tunaamini kuwa sheria peke yake bila elimu kwa Umma haziwezi kumaliza tatizo hili. Ndiyo maana tunawawatumia Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii ili kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kuondokana na mila za tamaduni hizi.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Kwa muda mrefu mawakala wanaosambaza pembejeo wamekuwa wakihujumu wakulima kwa kutowafikishia kabisa au kuwaletea pembejeo ambazo siyo sahihi na kinyume na maelekezo ya Wizara husika:-
(a) Je, Serikali ilishughulikiaje malalamiko ya wakulima wa Wilaya ya Simanjiro?
(b) Je, Serikali imechukua hatua gani kwa mawakala wasio waaminifu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2013/2014 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara ilipokea malalamiko kutoka kwa wakulima wa kijiji cha Narakauo kuhusu hujuma ya matumizi mabaya ya vocha za pembejeo za kilimo. Halmashauri ya Wilaya iliunda Kamati ya ufuatiliaji na uchunguzi ili kushughulikia malalamiko hayo. Baada ya uchunguzi ilibaini kuwa kijiji cha Narakauo hakikupelekewa mbolea za kupandia na kukuzia na kasoro zingine za utendaji zilizofanywa na Mwenyekiti wa Kamati ya Vocha na Afisa Mtendaji wa Kijiji. Hatua zilizochukuliwa baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya Kamati Teule ni pamoja na watendaji wa zoezi hilo kufikishwa katika vyombo vya sheria, katika maana ya Polisi na TAKUKURU kwa uchunguzi zaidi, hadi sasa vyombo hivyo vya dola havijatoa taarifa ya matokeo ya uchunguzi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali ya Wilaya iliamua kuwa mawakala walioonekana kushiriki katika ubadhilifu huo hawataruhusiwa kutoa huduma ya kusambaza pembejeo za ruzuku katika Wilaya hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro imezuia malipo ya mawakala hao pamoja na kuwaondoa katika orodha za mawakala wanaosambaza pembejeo Wilayani humo.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Vifo vya akinamama na watoto kwa takwimu za hivi karibuni Mkoani Manyara vinatisha:-
Je, Serikali inatoa kauli gani ya mwisho ili kukabiliana na janga hili ikiwepo kuimarisha Vituo vyote vya Huduma ya Mama na Mtoto Vijijini bila kujali uwezo wa wanawake kulipia au kutolipia huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO aliuliza:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha kwanza cha Wizara ni kuhakikisha afya ya Watanzania wakiwemo akinamama na watoto inaboreshwa. Hivyo basi, ili kukabiliana na janga hili, Serikali imeweka mikakati ifuatayo kama ilivyoanishwa kwenye Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya wa Nne, Mpango Mkakati wa Pili wa Kuongeza Kasi ya Kupunguza Vifo Vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto na Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, kama ifuatavyo:-
(i) Kufuatilia vifo vyote vitokanavyo na uzazi na kuvitolea taarifa kila robo mwaka ili kuongeza uwajibikaji na kugundua ukubwa wa tatizo katika kila Halmashauri nchini;
(ii) Kupandisha hadhi asilimia 50 ya vituo vya afya
na kuviwezesha kufanya upasuaji wa kutoa mtoto tumboni. Hadi sasa vituo 159 vinatoa huduma ya upasuaji wa matatizo yatokanayo na uzazi pingamizi ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa damu. Kati ya hivi, vituo 106 ni vya Serikali hii ni sawa na asilimia 21 ya vituo vya afya vya Serikali 484;
(iii) Kuanzisha Benki za Damu katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi yenye idadi kubwa ya vifo vitokanavyo na uzazi. Hadi sasa benki zimeanzishwa katika Mikoa ya Mara, Kigoma, Simiyu na Geita. Hii ni katika kuimarisha upatikanaji wa damu kwenye vituo vya kutolea huduma ya upasuaji;
(iv) Kuanzisha Mpango wa Kifuko chenye Vifaa Maalum kinachohitajika wakati wa kujifungua ambacho mama mjamzito atapewa kuanzia wiki ya 28 ya ujauzito anapohudhuria kliniki;
(v) Kutoa huduma ya Mkoba kwa wajawazito hadi wiki sita baada ya kujifungua na kwa watoto chini ya miaka mitano kwa kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii;
(vi) Kuwajengea uwezo watoa huduma wa afya kwa kuwapatia mafunzo ya huduma muhimu wakati wa ujauzito, stadi za kuokoa maisha kwa matatizo ya dharura yatokanayo na uzazi;
(vii) Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itashirikiana na wadau kuboresha upatikanaji wa vifaa, vifaa tiba na vitendanishi;
(viii) Kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii na kwa mwaka 2015/2016 watoa huduma 917 walipatiwa mafunzo jumuishi ya afya ya uzazi na mtoto. Hii ni katika kuhakikisha huduma ya afya ya uzazi inakuwa endelevu ili kuifikia jamii; na
(ix) Kuendelea kuelimisha jamii na hasa vijana kuhusu afya ya uzazi na kutilia mkazo juu ya lishe bora kwa kutumia vyombo mbalimbali vikiwemo redio, luninga na simu za kiganjani.
Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuomba ufadhili wa wadau mbalimbali ili kusaidia kujaza pengo la uhitaji wa ambulance. Kwa kutekeleza haya, tunaamini kwamba vifo vya wanawake wajawazito, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano vitaendelea kushuka kwa kasi.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Barabara ya kutoka Kibaya, Wilayani Kiteto kwenda Ranchi ya NARCO iliyoko Kongwa inaharibiwa na magari makubwa yanayobeba mahindi kutoka Kiteto kwenda soko maarufu la Kibaigwa, Kongwa na Serikali ilishaahidi kuijenga kwa kiwango cha lami. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Arusha – Kibaya – Kongwa ina urefu wa kilometa 430. Barabara hii inaunganisha Mikoa ya Arusha, Manyara na Dodoma, na lengo la Serikali ni kuijenga kwa kiwango cha lami. Barabara hii itakapokamilika itarahisisha usafirishaji wa mazao na mifugo katika Mikoa ya Arusha, Manyara na Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017 na 2017/2018 Serikali imetenga jumla ya shilingi 1,350,000,000 kwa ajili ya kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii. Aidha, mnamo tarehe 21 Aprili, 2017 Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imesaini mkataba na Mhandisi Mshauri Kampuni ya Cheil Engineering Company Limited kutoka Korea ya Kusini ikishirikiana na Kampuni ya Inter-consult ya Tanzania kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kuikamilisha katika kipindi cha miezi 21.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya usanifu itakapokamilika na kujua gharama halisi za mradi Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii, ili iendelee kupitika kwa urahisi wakati tunaendelea na maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ngazi ya Mkoa ya Haydom inahudumia wananchi wengi lakini inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi, madaktari wakiwemo Madaktari Bingwa pamoja na ukosefu wa maji.
(a) Je, Serikali itachukua hatua gani za dharura kutatua changamoto hizo?
(b) Kwa kuwa watumishi hawa wanafanya kazi katika mazingira magumu, je, ni kwa nini Serikali isiondoe kodi kwenye posho zao kama vile on-call allowance, hardship allowance na food allowance?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Haydom inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ina jumla ya watumishi 680 ambapo kati yao watumishi wa Serikali ni 156. Serikali imekuwa ikiisaidia hospitali kupitia Sera ya Ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) ambapo mpaka sasa imepeleka watumishi 156 wa kada mbalimbali wakiwepo madaktari 10 ambapo saba ni Madaktari Bingwa na watatu ni Madaktari wa Kawaida. Mbali na watumishi, Hospitali ya Haydom inapata ruzuku ya dawa kupitia MSD na ruzuku ya fedha za Busket Funds kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu. Hata hivyo, Serikali itaendelea kupeleka watumishi hasa madaktari na wauguzi kadri vibali vya ajira vitakavyokuwa vinapatikana.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Haydom inapata maji kutoka chanzo cha maji kilichopo umbali wa kilometa 20 katika Kijiji cha Binja, Kata ya Endamilay, Wilaya ya Mbulu. Hospitali hiyo inajitosheleza kabisa kwa maji hayo. Hata hivyo, maji haya yanapatikana kwa gharama kubwa kutokana na kukosekana kwa nishati ya umeme katika eneo husika, hivyo hospitali kulazimika kusukuma maji kwa kutumia mitambo ya dizeli (jenereta) inayotumia jumla ya lita 2,800 kwa mwezi sawa na shilingi 6,020,000/= ambayo ni sawa na shilingi 72,240,000/= kwa mwaka.
Kwa kuwa hivi sasa kupitia Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) inasambaza umeme katika maeneo mbalimbali yakiwapo ya Haydom inatarajiwa kuwa umeme huo utasaidia mradi wa maji wa Hospitali ya Haydom kupata huduma ya umeme na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji wa kutumia dizeli.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Haydom ina makundi mawili ya waajiriwa kama ifuatavyo; kundi la kwanza ni waajiriwa walioajiriwa na Hospitali ya Haydom moja kwa moja na hukatwa kodi ya mapato kama sheria inavyoelekeza; kundi la pili ni la waajiriwa waliajiriwa na Serikali lakini wanafanyakazi Hospitali ya Kilutheri Haydom, watumishi hawa wanalipwa posho ya kuitwa kazini baada ya masaa ya kazi (on-call allowance) na Hospitali ya Haydom na hii ndiyo sababu inayopelekea wakatwe kodi katika posho hiyo. Makato hayo yanatokana na Sheria ya Kodi ya Mapato (Income Tax) ya mwaka 1973.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-
Changamoto ya fedha za mikopo inayotolewa na Halmashauri za Wilaya kwa makundi ya wanawake na vijana nchini ni urejeshaji hafifu pamoja na kutorejeshwa kwa fedha hizo kabisa; kuna taasisi za fedha hapa nchini zinatoa mikopo kwa makundi tajwa hapo juu kwa ufanisi mkubwa na kwa uzoefu wa muda mrefu:-
Je, kwa nini Serikali isipitishe utoaji wa mikopo hiyo kwenye taasisi hizo zenye ufanisi wa muda mrefu na watalaam wa kutosha kama WEDAC ili kuepusha upotevu wa fedha za Serikali na mikopo kuwafikia walengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ilianzisha Mfuko wa Wanawake na Vijana baada ya kubaini kuwa wanawake na vijana wanashindwa kupata mikopo kutoka taasisi zingine za fedha ambazo zina masharti magumu. Lengo la kuanzishwa kwa mfuko huu ni kuondoa tatizo hilo ili kuwawezesha wanawake na vijana wengi kuendesha shughuli zao za kiuchumi ili kujikwamua na umaskini.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa taasisi zote za fedha hufanya biashara, unapoingia ubia na taasisi yoyote ya fedha lazima kuwepo na gharama za usimamizi wa mikopo hata kama masharti yatakuwa nafuu. Gharama hizo zinabebwa kwenye riba ukiacha masharti mengine kama dhamana na kadhalika. Kwa kuzingatia lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ambapo tunawalenga wananchi wa chini kabisa ambao hata uwezo wa kugharamia gharama za uendeshaji wa mifuko hiyo kwa wengine ni vigumu, ni vema mfumo wa uendeshaji uliopo na usimamizi chini ya Halmashauri ukaendelea kutumika.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge hili nawaelekeza Wakurungezi katika Halmashauri zote, kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na Vijana zinatolewa na kukopeshwa kwa vikundi hivyo kama ilivyoelekezwa katika mwongozo wa mipango na bajeti. Fedha hizo zitolewe kwa kadri mapato ya ndani yanavyokusanywa.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. MARTHA J. UMBULLA) aliuliza:-
Mazao ya pareto na vitunguu saumu yanalimwa Wilaya ya Mbulu na yana thamani na faida kubwa kwa wananchi.
Je, Serikali itakubaliana na mimi kuwa kuna haja ya kuanzisha viwanda vya kusindika mazao haya Wilayani Mbulu ili kuhamasisha kilimo cha mazao hayo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli mazao ya pareto na vitunguu saumu yanayolimwa katika Wilaya ya Mbulu yana thamani na faida kubwa kwa wananchi. Hivyo, Serikali inakubaliana na Mheshimiwa Umbulla kuwa kuna haja ya kuendelea kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vya kusindika mazao hayo Wilayani Mbulu ili kuchochea zaidi kilimo cha pareto na vitunguu saumu.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua faida zitokanazo na zao la pareto, Serikali iliamua kuanzisha Bodi ya Pareto kwa lengo la kudhibiti uzalishaji, usindikaji na biashara ya pareto nchini. Hivyo, kupitia Bodi ya Pareto na Kituo cha Uwekezaji Tanzania, Serikali itaendeleza juhudi za kuhamasisha uwekezaji kwenye viwanda vya kuengua na kuchuja pareto ili kuongeza thamani ya zao hilo na kuwanufaisha zaidi wananchi katika maeneo yanayolimwa pareto ikiwemo Mbulu.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa zao la vitunguu saumu, Wizara yangu kwa kupitia karakana za SIDO katika Mikoa ya Arusha na Kimlimanjaro zinatengeneza blenda ambayo inatumika kusaga zao hilo kuwa katika mfumo laini (garlic paste); teknolojia hii inapatikana kwa shilingi 1,800,000. Aidha, SIDO hutoa mafunzo kwa vikundi na watu binafsi juu ya usindikaji wa zao la vitunguu saumu katika mikoa inayolima zao hili.
Mheshimiwa Spika, hivyo, nashauri Mheshimiwa Mbunge afike ofisi za SIDO, Mkoa wa Manyara zilizoko Babati kwa ufafanuzi zaidi na hatimaye tuweze kushirikiana.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-

Uwanja wa Ndege wa Arusha ni muhimu sana kutokana na ukweli kuwa ni lango la kurahisisha watalii kuelekea kwenye Mbuga zetu za Wanyama na Hifadhi ya Taifa.

(a) Je, ni lini Serikali itapanua na kuboresha uwanja huo ili kuwezesha Watalii wengine kutumia ndege zetu na nyingine kutua Arusha kwa urahisi?

(b) Je, Serikali haioni kuwa Uwanja wa Ndege wa Arusha ungetumika kimkakati kukuza Sekta ya Utalii nchini na kuongeza pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Wziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeendelea kukikarabati Kiwanja cha Ndege cha Arusha ambapo mwaka huu wa fedha 2019/2020 kazi ya kuboresha maegesho ya magari, kukarabati barabara za viungo zimeshaanza na ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Taratibu za kumpata Mkandarasi kwa kazi ya kurefusha barabara ya kuruka na kutua ndege kutoka mita 1640 za sasa hadi mita 1840 sambamba na ujenzi wa eneo la kugeuzia ndege yaani (Turning pads) zinaendelea. Ujenzi huu utawezesha ndege kubwa aina ya Bombardier Q 400 za ATCL kutumia kiwanja hiki.

Aidha, mipango ya kuweka taa za kuongezea ndege kwenye uwanja huo utawekwa kwenye mwaka wa fedha 2020/2021.
MHE. MARTHA J. UMBULLA aliuliza:-

Mwaka 2012 Mahakama ilitoa hukumu kuwa wakulima na wafugaji wote waondoke ndani ya Hifadhi ya Jamii ya Emborley Murtangos iliyoko Wilayani Kiteto lakini baadhi ya wananchi walipinga amri hiyo na kuendelea kufanya shughuli zao na kusababisha mgogoro baina ya wakulima na wafugaji:-

(a) Je, Serikali imeshughulikia kwa kiasi gani mgogoro huo uliodumu kwa miaka 8?

(b) Je, Serikali ilichukua hatua gani kuwadhibiti na kuwaadhibu waliokiuka amri hiyo?

(b) Je, nini kauli ya Serikali juu ya matumizi ya Hifadhi hiyo ili kumaliza mgogoro huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kibali chako, naomba kabla ya kujibu swali la msingi la Mheshimiwa Mbunge, uniruhusu niwapongeze na kuwashukuru sana Kamati za Mitihani ya Darasa la Saba ngazi ya wilaya na mikoa, walimu wetu, wanafunzi, wazazi na wadau wote wa elimu Tanzania kwa juzi na jana kumaliza zoezi la mitihani ya darasa la saba. Taarifa njema ni kwamba mitihani hiyo imetoka salama hakuna mtihani uliovuja. Tnawashukuru sana Kamati na hasa Baraza la Mitihani, Wizara ya Elimu na TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014/2015, Serikali iliunda Kikosi Kazi cha wataalamu kutoka Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mipango na Fedha (Ofisi ya Taifa ya Takwimu), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto kwa lengo la kuhakiki mipaka ya hifadhi, kupima na kuweka alama za mipaka na kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo. Baada ya kufanyika kwa kazi hiyo, eneo la hifadhi lilibaki na ukubwa wa hekta 75,394.6 kutoka hekta 133,333 za awali na kusajiliwa kwa namba 79667.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuwaondoa wananchi wa makundi ya wakulima na wafugaji wanaondelea kuingia kwenye hifadhi. Kuanzia mwaka 2014-2019, wananchi 49 wamefikishwa mahakamani kwa kukiuka amri ya Mahakama na makubaliano ya matumizi ya ardhi yaliyoidhinishwa.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Hifadhi ya Emborley Murtangos litabaki kuwa eneo la hifadhi ya jamii kwa kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi kama ilivyoidhinishwa na kwa kuzingatia maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa. Aidha, hali ya ulinzi na usalama katika eneo hilo itaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha panakuwepo na amani na utulivu wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazielekeza Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya kuchukua hatua stahiki pale inapobainika ukiukwaji wa matumizi ya ardhi kwenye eneo la hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.