Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Leah Jeremiah Komanya (64 total)

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye kutia moyo wananchi wa Wilaya Meatu. Mradi huu ni wa muda mrefu wa mwaka 2009, yapata sasa miaka sita, wananchi walitoa eneo hilo na kuacha kufanya shughuli zao pasipo malipo, matokeo yake bwawa hilo limekuwa likijaa na kusababisha uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na mmomonyoko wa udongo. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie Wizara katika mpango mkakati wake wa mwaka 2016/2017, imepanga ni lini mradi huo utakamilika na uanze kutumika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, nimekuwa nikishuhudia miradi kama hii, Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kuchimba mabwawa, lakini yamekuwa hayakidhi mahitaji kama ilivyokusudiwa, kwa mfano mradi wa maji Mjini Mwanuhuzi, naomba Serikali iniambie je, inaniahidi nini kukamilisha mradi huo na kuusambaza katika Vijiji vya Jinamo, Paji, Mwanjolo, Koma na Itaba?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ameuliza ni lini bwawa la Mwanjolo litakamilika; katika bajeti yangu ambayo nitawasilisha hapa Bungeni muda siyo mrefu, tumeliwekea bwawa hili mpango wa kuweza kulikamilisha, kwa hiyo, tutaleta maelezo na kazi ambazo zitafanyika ili tulikamilishe bwawa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu mradi wa maji anaoelezea, lini tutakamilisha katika vijiji vingine; mambo yote haya tumeyaweka kwenye mpango, kwanza tunakamilisha miradi yote ambayo inaendelea iliyokuwa kwenye program ya maji awamu ya kwanza, halafu tunaingia awamu ya pili. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge nia ya Serikali ni kwamba, miradi yote ambayo ipo tutaikamilisha na tutakwenda kuikagua kuhakikisha kwamba inafanywa jinsi inavyotakiwa. Ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la usambazaji wa umeme lipo pia katika Wilaya ya Meatu. Wilaya ina vijiji 109 lakini ni vijiji 21 tu, sawa na asilimia 19 vilivyopatiwa umeme. Ni lini Serikali itavipatia umeme vijiji vilivyosalia?
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba katika maeneo aliyoyataja ni vijiji 21 tu vimepatiwa umeme, na ninadhani anazungumzia eneo la Meatu; na vijiji takribani 105 havijapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama nilivyosema kwamba ugawaji wa umeme unakwenda kwa awamu. Tumemaliza awamu ya pili ambayo imehusisha vijiji vingi sana, na awamu ya tatu inakwenda sasa kumalizia kwenye vijiji vyote vilivyobaki nchi nzima. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, vijiji 100 vilivyobaki, pamoja na maeneo ya vitongoji ambavyo pia hajayataja nimhakikishie kwamba yote yatapata umeme kunzia mwaka 2017, 2018 hadi 2019.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na majibu ya Naibu Waziri. Wilaya ya Busega, Itilima na Kituo cha Polisi cha Mwandoya kilichopo Jimbo la Kisesa katika Wilaya ya Meatu, Askari wa Jeshi la Polisi wanaishi katika mazingira magumu. Nikisema mazingira magumu namaanisha hata zile nyumba za wananchi ni za shida sana kupatikana kwa ajili ya kupanga. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri katika mikoa aliyopanga kutembelea yuko tayari kutembelea Mkoa wa Simiyu ili aweze kujionea namna Askari wa Jeshi la Polisi wanavyoishi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Wilaya ya Meatu ilianzishwa mwaka 1986 na majengo hayo yalijengwa mwaka 1999, yapata sasa ni miaka 17. Majengo hayo yameanza kuchakaa na kuoza, lakini kwa mujibu wa majibu ya Naibu Waziri, nimeona hata kwenye ule mgawo wa nyumba 4,136 majengo hayo hayamo. Je, Serikali sasa haioni haja ya kukamilisha majengo hayo na kuweza kuyanusuru?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, kwamba niko tayari kutembelea Wilaya ya Busega? Jibu, niko tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba, katika mradi wa nyumba 4,136, Wilaya ya Busega na Itilima haimo. Ukweli ni kwamba, katika Mkoa Mpya wa Simiyu katika mradi wa nyumba 4,136 tunatarajia kujenga nyumba 150. Sasa nadhani sasa hivi kwa concern ambayo ameonesha Mheshimiwa Mbunge, tujaribu kuangalia sasa katika mgawo wa nyumba 150, tuhakikishe kwamba, zinakwenda katika Wilaya ya Busega na Itilima ili kukabiliana na changamoto kubwa ya makazi ambayo Mheshimiwa Mbunge amelizungumza na sisi tunalifahamu.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba niulize maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa makazi haya ya watu wenye ulemavu yako ndani ya Halmashauri, je, Serikali sasa haioni haja Halmashauri ikatenga bajeti ndogo ili iweze kusaidia upatikanaji wa chakula ili wananchi hao wawe na uhakika wa kupata chakula badala ya kusubiri msaada kutoka kwa mwananchi mmoja mmoja? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na jitihada za Serikali za kupambana na mauaji haya. Je, sasa naomba Serikali inihakikishie ina mkakati gani wa haraka kuhakikisha watu hawa wanahudumiwa na vitendo hivi vinakoma ili wananchi hawa waweze kuungana na ndugu zao na jamii ili waweze kushirikiana katika shughuli mbalimbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Halmashauri, ni kweli, kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu labda nifafanue kwanza; jukumu la kwanza la kumlinda mtu mwenye ulemavu linaanzia kwenye familia baadaye taasisi, Serikali kwa upande wa Halmashauri ni sehemu ya mwisho kwenye makazi kwa sababu msisitizo uko katika kuishi katika hali ya kuchangamana na wengine na kweli Halmashauri zinaagizwa kuhakikisha kwamba zinatenga bajeti kwa ajili ya kutoa misaada maalum hasa ya makazi na chakula kwa wale wanaohitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni jambo ambalo liko wazi kisheria, na tayari Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikitoa maagizo hayo na kwa kutumia fursa hii niwakumbushe wote wanaohusika na Wabunge pia kwa sababu ni Wajumbe katika Mabaraza ya Madiwani ambayo yanahusika kupanga bajeti ya Halmashauri mbalimbali kuhakikisha kwamba wanasimamia bajeti katika Halmashauri zao ili kuhakikisha kwa mba watu wenye ulemavu wanapewa kipaumbele katika masuala mbalimbali si tu ya makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu jitihada maalum, niseme tayari kumekuwa kuna jitihada mbalimbali na hata juzi tu nafikiri, siku ya Ijumaa kwa wale wanaosikiliza habari walisikia kuhusu hukumu nyingine ambayo ilitolewa na Mahakama Kuu - Kagera kwa watu waliofanya tukio mwaka 2008, majina yao siyakumbuki, lakini hizo hukumu zimetolewa na nafikiri katika mwaka huu kumekuwa kuna hukumu zaidi ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba makosa ya mauaji kwa sababu yana adhabu kubwa, kifo ushahidi wake inabidi uwe watertight kwa maana hiyo huwezi pia wakati mwingine ukaharakisha kutoa hukumu kwa sababu wengine wanasema kwa lugha ya kingereza justice rushed is justice buried na kuna changamoto zingine pia katika kesi hizi. Kuna baadhi ya watu hasa ukizingatia baadhi ya matukio yamekuwa yanafanywa na watu wa karibu katika familia, kumekuwa kuna ugumu wa kupata ushahidi kwa haraka, lakini niseme tu jitihada zinaendelea na zipo ambazo zimefanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa yote kama nilivyosema, suluhisho la kudumu ni katika kubadilisha tabia na ndio maana siku zilizopita chache katika wiki ya vijana Serikali ilianzisha mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba elimu inatolewa ili tatizo hili liishe na nina imani hili tatizo litakwisha ndani ya muda mfupi.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika,
nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa, zana alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri zinatumiwa zaidi na wanaume na zinarahisisha zaidi kazi kwa
wanaume, hususan, kwenye kaya zenye uwezo. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa zana ambazo zitamrahisishia mwanamke kulima mwenye kipato duni kama ninavyomwona mwanamke aishiye Mkoa wa Simiyu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imekusudia kutoa ajira zaidi. Kwa kupitia malighafi za mazao, si tu ajira zitatoka katika viwanda bali pia katika mazao ambayo yatauzwa na wakulima. Je, Serikali
ina mkakati gani wa kuhakikisha inatoa mbegu ambazo zitaleta tija katika kilimo cha mtama na alizeti katika Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, jitihada mbalimbali ambazo Serikali inachukua kuboresha kilimo za kugawa na kuleta zana za kilimo zinawasaidia wakulima wote wakiwemo na wanawake. Tunaamini kwamba tukiweza kuwa na zana za kilimo za kisasa, wanufaika wa kwanza watakuwa ni wanawake kwa sababu wao hasa ndio kwa kiasi kikubwa
wanajihusisha na kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile Wizara kupitia Mfuko wa Pembejeo imeweka utaratibu wa kuweza kukopesha zana za kilimo kwa bei nafuu na wanawake kwa kupitia vyama vya ushirika lakini vikundi mbalimbali ni wanufaika wakubwa wa huduma hii. Vilevile Wizara kwa kupitia Benki
ya Maendeleo ya Kilimo inatoa mikopo kwa ajili ya pembejeo. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge aweze kuwasiliana na sisi ili kuwaunganisha akinamama wakulima
wa Simiyu ili waweze kupata huduma hii.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kugawa mbegu za mtama na alizeti, katika mwaka wa fedha unaokwisha na hasa baada ya changamoto ya mvua kutokuwa nzuri, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iligawa zaidi ya mbegu milioni 14 za mtama. Vilevile tumegawa mbegu za alizeti kwa wakulima mbalimbali nchini wakiwepo na wakulima wa Mkoa wa Simiyu.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali yenye mikakati mizuri. Naomba nitumie muda wangu kuuliza swali moja tu la nyongeza. Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mwanuzi Wilayani Meatu inasuasua kwa kuwa chanzo chake cha bwawa kimejaa matope na kuathirika na mabadiliko ya tabianchi sambamba na chanzo cha New Sola Zanzui kilichopo Wilaya ya Maswa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira imefanikiwa kupata sh. 230,000,000,000 ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutoa maji Ziwa Victoria na kuyaleta Mkoa wa Simiyu na usanifu bado unaendelea. Je, Serikali haioni haja katika usanifu huo ikajumuisha kupeleka bomba kuu katika Makao Makuu yote ya Mkoa wa Simiyu ikiwemo Wilaya ya Meatu na Maswa kwa awamu ya kwanza kwa sababu Wilaya hizi zimeathirika kiasi kikubwa na ukame na ziko katika phase two na fedha ya phase two haijapatikana?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia na kuuliza swali na kwa umakini anaouonesha katika kufuatilia shida za maji za wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpe habari njema kwamba baada ya kupatikana sh. 250,000,000,000 siyo 230,000,000,000 za awamu ya kwanza sasa tunaanza utaratibu wa kupata fedha nyingine zaidi za awamu ya pili ambazo zitapeleka maji sasa katika maeneo yote aliyoyataja pamoja na mkoa mzima na mikoa mingine ambayo inakabiliwa na ukame mkubwa unaotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo, Serikali inatamka rasmi kwamba, inatambua changamoto ya maji na ina mipango ya kuyapeleka kwa wananchi wote wanaokabiliwa na ukame katika eneo hilo kwa kupitia mradi huu. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara imeanza kutekeleza ujenzi wa Bwawa la Mwanjolo, lakini mapungufu yaliyopo katika mkataba huo ni mabirika ya kunyweshea mifugo; je, Serikali haioni haja ya kuongeza mabirika ya kutosha ukizingatia Ukanda huo una ng’ombe wengi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sisi tunatambua ya kwamba mifugo ni maisha yetu na ufugaji ndiyo maisha yetu. Nataka nimhakikishie kwamba wao kupitia Halmashauri waibue miradi hii na sisi katika Serikali tutahakikisha kwamba tunawaunga mkono ili kusudi jambo hili linalohusu malisho na maji kwa ajili ya mifugo tatizo hili liweze kuisha.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi nzuri za Serikali, takwimu zinaonyesha kuwa, asilimia 60 ya wagonjwa wanaohudumiwa Hospitali ya Ocean Road wanatoka Kanda ya Ziwa, lakini katika huduma zinazotolewa kwa sasa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando zipo changamoto kubwa ikiwemo uhaba wa fedha wakati wa ku-service ile mashine. Hospitali yenyewe haijitoshelezi na kusababisha huduma hiyo kusitishwa wakisubiri fedha na kuendelea kuleta usumbufu kwa wagonjwa katika Hospitali ya Ocean Road. Je, Serikali haioni haja ya kupeleka ruzuku ya kutosha katika kitengo cha saratani kilichopo Bugando?
Swali langu la pili, tafiti zinaonesha kuwa maji yaliyoachwa kwenye gari lililopo kwenye jua na yakakaa kwa muda mrefu katika vyombo vya plastiki inaonyesha inapopata joto kuna chemical zinatoka kwenye plastiki aina ya dioxin ambazo zinaonyesha kuna uwezekano wa kupata saratani hususani saratani ya matiti. Je, Wizara ina mikakati gani ya kutoa elimu kwa wananchi?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwanza kuhusu ruzuku kuongezwa kwa ajili ya kituo cha tiba ya saratani kilichopo Kanda ya Ziwa kwa maana ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando ndiyo kwanza kimeanza kufanya kazi, kwa hiyo, tunatarajia uwepo wa changamoto mbalimbali ambazo zitajitokeza mpaka pale ambapo kita-stabilize. Kwa hivyo, ninaomba niichukue hii kama changamoto na tutatazama changamoto hii inasababishwa na nini ili wakati wa mchakato wa bajeti inayokuja, tuone ni kwa kiasi gani tunahitaji kuongeza ruzuku kwenye kituo hiki ili kiweze kutoa huduma bora zaidi katika mwaka wa fedha unaokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la pili ambalo linahusu plastics ambazo zinatumika kuwekea maji ambayo yakikaa kwenye jua kwa muda mrefu inasemekana yanaweza yakasababisha saratani, hili ni jambo ambalo limekuwa likisemwa kwenye mitandao mara nyingi lakini halina ukweli wowote ule na naomba niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wote kwamba Serikali iko makini na haiwezi kuruhusu kitu chochote kile ambacho kinauzwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu na kikawa na madhara kikaingia kwenye soko, kwa sababu tunafanya uchunguzi pia tunafanya udhibiti wa bidhaa zote ambazo zinaenda kutumika kwa wananchi kupitia taasisi yetu ya Tanzania Foods and Drugs Authority (TFDA) - (Mamlaka ya Chakula na Dawa) ambapo mambo yote haya yakisemwa ama yakizungumzwa kwenye jamii huwa tunayafanyia utafiti wa kimaabara na hatimaye kuthibitisha kama yana ukweli ama hayana ukweli ndani yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili analolisema Mheshimiwa Komanya tulikwishalifanyia kazi na tukabaini ni uzushi na halina ukweli wowote ule na kwa hivyo hakuna sababu ya kuendelea kuwatia wasiwasi wananchi.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii. Serikali katika kutatua upatikanaji wa maji hasa kwenye maeneo kame vijijini, imekuwa ikihamasisha kujenga miundombinu ya uvunaji wa maji kwa kutumia mapaa ya nyumba za Serikali, Asasi za Umma na nyumba za watu binafsi; na pia imekuwa ikitoa miongozi katika Halmashauri kutunga Sheria ndogo kwa ajili ya uvunaji wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nimekuwa nikishuhudia uvunaji huu wa maji ya mvua katika paa, ukivunwa kwenye mabati yaliyopakwa rangi. Naomba niambiwe kama kuna matatizo yoyote yanayopatikana kutokana na maji yaliyovunwa toka kwenye mabati yaliyopakwa rangi.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Komanya, ameelezea vizuri kabisa kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba Halmashauri zinaweka Sheria ndogo ndogo na zinapitisha michoro kwenye ujenzi wa nyumba kuhakikisha kwamba kila nyumba inakuwa na kisima cha kuvuna maji kutoka kwenye mapaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la msingi ni kuhusu yale mabati yenye rangi. Mheshimiwa Mbunge nakushukuru kwa swali lako zuri. Rangi ikipakwa, baada ya siku 90 process ile ya oxidation inaondoa kabisa kemikali katika rangi,
kwa hiyo, baada ya miezi mitatu hata ukivuna yale maji yanakuwa hayana madhara ya aina yoyote. Kwa hiyo, wala hakuna wasiwasi wowote.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, hiyo elimu wale waopaka hizo rangi wanapewa kweli? Kama mvua ikinyesha kabla ya miezi mitatu!
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Nielekeze Wakurugenzi kwamba wasimamie, kwasababu nchi yetu imegawanywa na katika mgawanyo huo, utawala uko katika Halmashauri na Halmashauri ina wataalam wote. Kwa hiyo, Wahandisi wote walio katika Halmashauri wasimamie suala hili la upakaji rangi kwenye mabati. Ni kweli upakaji rangi umekuwa unafanyika kwa jinsi mtu anavyopata hela yeye mwenyewe, lakini naomba kupitia Halmashauri, basi elimu itolewe kwamba rangi nayo ina sumu ila baada ya muda fulani ile sumu inaondoka. Kwa hiyo, elimu hii itolewe kwa wananchi pale ambapo wananchi wanataka kupaka rangi katika maeneo yao. Utaratatibu ndivyo ulivyo kwamba unapotaka kufanya ukarabati wa aina yoyote kwenye nyumba ni vyema uombe kibali ili uwe na usimamizi unaofaa.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii.
Matatizo ya Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mpwapwa yanafanana na matatizo ya Mamlaka ya maji ya Mji wa Mwanuhuzi. Mradi wa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Mwanuhuzi ulikamilishwa mwaka 2009 na ukakabidhiwa katika Mamlaka ya Maji Mwanuhuzi. Mradi huu ulilenga kusambaza maji katika vijiji Nane lakini ni vijiji Vitatu tu vilisambaziwa maji; na kusababisha qubic mita za ujazo wa maji, ambayo yanatumika ni moja ya tatu tu, na hivyo gharama ya uendeshaji katika Mamlaka ya maji kuwa juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishiriki katika Bajeti ya mwaka huu...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, naomba uulize swali tafadhali.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri haikuwa na fedha kwa ajili ya upanuzi wa mradi huu, kwa sababu fedha iliyokuwepo ilikuwa ni kwa ajili ya Mkandarasi mshauri wa vijiji 10;
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kusambaza maji katika vijiji vilivyobaki vya Bulyanaga, Mwambegwa, Mwagwila, na Mwambiti ili wananchi waweze kunufaika na mradi huu.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze yeye ni Mama anajua matatizo ya maji, kwa hiyo ufuatiliaji wake ni kwamba unamgusa moja kwa moja. Ametoa taarifa kwamba kuna mradi ulikamilika lakini umehudumia vijiji vichache. Mheshimiwa Leah Komanya, naomba sana ushirikiane na Halmashauri; kwa sababu mwaka huu tumetenga fedha kwa kila Halmashauri, kuhakikisha kwamba hayo maeneo ya vijiji yaliyokuwa yamekosa kupata maji basi muhakikishe kwamba nayo yanapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kama kuna tatizo la utaalam, Mheshimiwa Komanya, naomba utakapokuwa umefika kule na mmepata shida ya wataalam basi tuwasiliane ili tuweze kushirikiana kuleta wataalam atuweze kufikisha huduma hiyo hapo. Suala la nyongeza ni kwamba hii Mwanuhuzi iko Mkowa wa Simiyu, na Mkoa wa Simiyu tuna mradi mkubwa ambao utachukua maji kutoka ziwa Victoria, usanifu sasa umekamilika; na wakati wowote tutakamilisha taratibu ili kuhakikisha kwamba Mkoa wote wa Simiyu sasa tatizo la maji tunaliondoa.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada nzuri zinazofanywa na Jeshi la Polisi pamoja na wadau mbalimbali kuhusu kutoa elimu kuacha imani potofu na mila dhidi ya ukatili unaofanywa kwa watu wenye ualbino.
Je, ni lini Serikali itaanzisha database ili kuwepo na takwimu kwa jinsia na umri ambazo zitasaidia kuhakiki mauaji na ukatili ambao haukuripotiwa? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Leah kwa kulileta swali hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali tunazo taarifa za masuala ya sensa ya watu aliowaongelea, ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi, kwa sababu tuna taratibu za kupata taarifa kufuatana na mfumo wa Kiserikali. Kwa ajili ya mambo ya kiusalama huwa hatupendi kuziweka wazi kwamba huyu yuko wapi na anafanya nini, lakini tunachofanya ni kuimarisha ulinzi kwa ajili ya kuwahakikishia usalama wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitangazie tu Bunge lako Tukufu kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita hakukuwepo na tukio lolote lililojitokeza linalohusisha kitendo cha kikatili kwa ndugu zetu wenye ulemavu. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kupambana na vitendo vyote vya kikatili likiwemo jambo hili alilolisemea Mheshimiwa Mbunge. Kanzidata hiyo ipo na ilishazinduliwa tayari kama nilivyotangulia kusema. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, Mheshimiwa Rais alipotembelea Mkoa wa Simiyu mapema Januari, 2017 baada ya kuona maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa, kwanza hakuridhishwa na bajeti iliyotengwa ya shilingi bilioni 38 ya kujenga Hospitali ya Mkoa. Hivyo, akasema hospitali hiyo ijengwe kwa shilingi bilioni 10 na kwamba akatoa ahadi zitolewe shilingi bilioni 10 ili mwaka 2019 aje kuzindua hospitali hiyo. Mpaka sasa ni jengo la OPD tu ndilo lililokamilika na 2017 mpaka leo hakuna fedha yoyote iliyoletwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, naomba commitment ya Serikali kuhusiana na ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, swali langu dogo la pili; tunayo Hospitali Teule ya Somanda, hospitali hiyo ina changamoto. Madaktari wanaohitajika ni 22, waliopo ni wanane, lakini hao wanane hawana examination room, hamna Mganga wa Usingizi wala hakuna casuality room.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha hospitali hiyo teule ya mkoa ili wananchi wa Mkoa wa Simiyu wasihangaike kwenda Mkoani Mwanza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa maswali mawili ya Mheshimiwa Leah Komanya; na nimpongeze kwa kufuatilia afya na maendeleo ya wananchi wa Simiyu.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu kwamba, Mheshimiwa Rais mwishoni mwa mwaka 2017 alikabidhi hospitali zote za rufaa za mikoa ambazo zilikuwa zinasimamiwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuja katika Wizara ya Afya. Na sisi ndani ya Wizara ya Afya tumeshajipanga kuhakikisha kwamba hospitali hizi tunazihudumia na kuzisimamia kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti kama nilivyosema katika jibu langu la awali.
Mheshimiwa Spika, niendelee kusema tu kwamba ahadi ya Mheshimiwa Rais ni commitment, nasi ndani ya Wizara tutaendelea kuisimamia kuhakikisha kwamba fedha hizo zinapatikana kwa malengo ambayo yamekusudiwa, baada ya kufanya tathmini ya kina kuangalia mahitaji halisi ya Hospitali hii ya Simiyu.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, swali lake la pili lilikuwa ni kuhusiana na watumishi. Katika mwaka wa fedha uliopita, Serikali iliajiri watumishi 3,152 ambao tuliwagawa katika mikoa mbalimbali. Tunatambua bado tuna changamoto kubwa sana ya watumishi na tunatarajia kwamba Serikali itatoa kibali hivi karibuni na Mkoa wa Simiyu utazingatiwa katika mahitaji yake.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali kwamba asilimia 40 ifanye kazi ya uhifadhi. Vile vile kwa mujibu wa waraka asilimia 60 inatakiwa iende katika vijiji vinavyopakana na hifadhi ambavyo ni Mwambegwa, Mwanyaina, Mwagwila, Semu, Nyanza, Matale na vingine vingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2016/2017 vijiji vile havikupelekewa hela na asilimia 40 haikufanya kazi ya uhifadhi na hivyo kuipelekea Idara ya Wanyamapori kushindwa kununua silaha kwa ajili ya kukabiliana na wanyamapori. Je, Serikali haioni sasa ipo haja ya zile fedha zikapelekwa moja kwa moja katika vijiji na asilimia 40 ikapelekwa katika Pori la Akiba kuliko kupelekwa Akaunti ya Amana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, asilimia 44 ya kilometa za mraba ya Wilaya ya Meatu ni hifadhi. Halmashauri imepata ugumu katika kukabiliana na ujangili, uhifadhi wa maliasili na uvamizi wa wanyamapori kwa sababu ina changamoto ya vitendea kazi. Je, Serikali iko tayari kuipatia gari Wilaya ya Meatu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Leah kwa jinsi ambavyo amekuwa akifanya kazi na kufuatilia masuala mbalimbali yanayohusu Jimbo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali asilimia 60 zinazobaki kule kwenye Halmashauri kwamba ziende kwenye vijiji kama alivyosema, ni wajibu kila Halmashauri zinazopata mgao huu ile asilimia 60 inatakiwa iende katika vile vijiji vinavyozunguka hifadhi, kwa sababu zinatakiwa zitumike katika kuleta maendeleo ya vijiji vile vinavyohusika. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuziomba Halmashauri zote nchini kutekeleza hilo agizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusu maombi ya gari, naomba nichukue nafasi hii kusema kwamba ni kweli kabisa kumekuwa na changamoto katika lile eneo na Wizara yangu inazo taarifa za kutosha. Tutalifanyia kazi maadam amelileta, tutaona pale hali itakaporuhusu kifedha tutawapelekea gari lile ambalo litawasaidia katika shughuli hizo. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa daraja la Sanjo katika Mto Simiyu na kilometa 4 za lami Mjini Mwanhuzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Komanya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi za Viongozi Wakuu zipo nyingi na kuna baadhi ya maeneo ambapo ahadi zinaendelea kutekelezwa na maeneo mengine tunaendelea na utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunatekeleza. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika kipindi hiki cha miaka mitano tutahakikisha sehemu kubwa ambazo viongozi wameahidi tunaendelea kutekeleza. Kikubwa tu ni kwamba kila wakati tunaendelea kufanya uratibu ili kuhakikisha hizi ahadi zinatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira. Maeneo haya nina interest ya kuyatembelea, nitatembea pia niweze kuona hili daraja alilolitaja pamoja na mipango mizima ya kuhakikisha kwamba ahadi zinatekelezwa, lakini kikubwa tunaboresha miundombinu ya barabara maeneo yote.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali inapeleka fedha Halmashauri kulingana na makusanyo lakini kumekuwepo na malimbikizo ya madeni yanayotokana na stahiki za watumishi kama gharama za mazishi, matibabu yasiyo ya Bima za Afya, gharama za kufungasha mizigo kwa wastaafu, masomo na likizo. Je, ni lini Serikali italipa madeni ya mwaka 2016/2017 yaliyohakikiwa na kuwasilishwa Januari, 2018? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali ilipunguza ruzuku ya matumizi ya kawaida kutoka asilimia 100 kwenda asilimia 40, mafungu niliyoyataja yanaonekana kuelemewa. Je, Serikali haioni ipo haja ya kufanya mapitio katika mafungu niliyoyataja na kuweza kuyaongezea bajeti? Mheshimiwa Spika, ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Komanya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza la kulipa madeni ambayo yameshahakikiwa, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali yetu imekuwa ikilipa madeni yote ambayo yamehakikiwa kwa ajili ya watumishi wetu. Kama ambavyo nimekuwa nikiliarifu Bunge lako Tukufu ni mwezi Aprili tu Serikali yetu ililipa zaidi ya shilingi bilioni 43 kwa ajili ya madai mbalimbali ya watumishi wetu katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuongezewa kwa bajeti katika mafungu aliyoyataja Mheshimiwa Leah Komanya, napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba katika mafungu ambayo tunayapa kipaumbele kuyapatia fedha za ruzuku ni Mafungu ya Utawala ambayo ndiyo yanashughulikia haya matatizo aliyoyasema kama gharama za mazishi na gharama za uhamisho. Kwa mfano, kwa mwaka huu 2017/2018 tuliomaliza tulikuwa na bajeti ya Sh.27,447,000,000. Kati ya hizi shilingi bilioni 27, Serikali yetu ilipeleka shilingi bilioni 22 kulingana na mahitaji yaliyoletwa kutoka kwenye Halmashauri zetu ambayo ni zaidi ya asilimia 90 ya bajeti ambayo ilikuwa imepangwa. Hili lilikuwa ni Fungu la Utawala ambalo ndilo linaloshughulika na madai mbalimbali aliyoyataja Mheshimiwa Leah Komanya.
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo tunatoa kipaumbele kupeleka fedha za ruzuku ni katika Fungu la Elimu ambapo Serikali yetu imekuwa ikiajiri Walimu na tunahakikisha Walimu wetu wanalipwa pesa zao kabla hawajafika kwenye vituo vyao vya kazi au wanapofika tu kwenye vituo vyao vya kazi. Kwa mfano, kwa mwaka 2017/ 2018 tulipanga kupeleka shilingi bilioni 116 na tukapeleka zaidi ya shilingi bilioni 111 kulingana na mahitaji yaliyoletwa kutoka kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba tunajua umuhimu wa mafungu haya na tunayapa kipaumbele katika kuyapelekea fedha za ruzuku.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mazingira ya Mkoa wa Simiyu yanafanana na mazingira ya Mikoa ya Kati kwa zao la alizeti lakini wakulima wa Simiyu wamekuwa wakilima zao hili kwa kubahatisha mbegu za alizeti zisizo na tija ukilinganisha na Mikoa ya Kati. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuleta mbegu zenye tija ikiwemo na kutoa elimu kwa wakulima wa Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa majibu yangu ya swali la msingi nilizungumzia mikakati iliyopo kwa Shirika letu la ASA, TOSKI na TARI. Mbegu zipo na nawaelekeza watu wa ASA wapeleke mbegu kule kwa Mheshimiwa Mbunge ili mbegu hizi zipatikane kwa gharama nafuu kwa hii mbegu aina ya Record. Pia kuna makampuni binafsi ambayo yamethibitishwa na Taasisi yetu ya Kudhibiti Ubora ya TOSCI yanauza mbegu kihalali nayo nayaomba yapeleke mbegu katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge ili wananchi wapate mbegu kwa urahisi zaidi.
MHE. LEAH. J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona kupitia mradi wa uwekezaji katika sekta ya kilimo (DASP) Serikali ilitumia shilingi bilioni 1.1 fedha za Benki ya Maendeleo ya Afrika kutekeleza mradi wa umwagiliaji katika kijiji cha Mwagwila Wilayani Meatu, lakini mradi huo ulitelekezwa.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipo tayari tutaongozana naye.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kutokana na mwamko uliopo wa wananchi kujiunga na vikundi vya ujasiriamali pamoja na VICOBA lakini wananchi wamekabiliwa na kutokuwa na uwezo wa uzalishaji. Tatizo hili linachangiwa na kutokuwepo na Maafisa Biashara wa kutosha katika Halmashauri zetu na kuwajengea uwezo wananchi. Halmashauri zote nchini zina Afisa Biashara mmoja au wawili au hakuna kabisa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaajiri Maafisa Biashara wa kutosha? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema katika mazingira ya sasa kuna vikundi vingi vya uzalishaji mali, kuna VICOBA na shughuli nyingi za kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Dkt. Kalemani na timu yake kueneza umeme vijijini na kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Profesa Mbarawa na timu yake kujenga barabara na sisi kupitia TARURA kujenga barabara za vijijini, fursa nyingi sana zinajitokeza. Kwa hiyo, kuna kazi kubwa sana iliyoko mbele yetu ambayo tunahitaji kuifanya kupitia kada hizi za Afisa Biashara, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Wachumi. Serikali itahakikisha kwamba wanapatikana wa kutosha ili kusudi wananchi wahudumiwe vizuri. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu inapaswa kunufaika na miradi ya maendeleo inayotokana na ujirani mwema, Outreach Department kutokana na Serengeti National Park na Ngorongoro Conservation; lakini ni zaidi ya miaka kumi haujawahi kutekelezwa mradi wowote.
Je, ni lini sasa Halmashauri ya Meatu italetewa miradi ya maendeleo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba taasisi zetu zote zinazohusika na masuala ya uhifadhi zinao mpango madhubuti kabisa wa kuhakikisha kwamba zinachangia katika miradi mbalimbali ya vijiji vile vinavyozunguka katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wilaya ya Meatu nina uhakika kabisa kwamba imetengewa kiasi cha fedha ambazo zitatekeleza miradi mbalimbali ya vile vijiji vinavyozunguka katika maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa tukifanya hivyo, kwa mfano, takribani kuanzia mwaka 2004 mpaka 2016 jumla ya shilingi bilioni 17.2 zimetumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya vijiji vinavyozunguka hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nina uhakika na Wilaya ya Meatu ni mojawapo ambayo imefaidika na itaendelea kufaidika. Na mimi naomba tuwasiliane baadae ili tuone kwamba imetengewa kiasi gani katika mwaka unaofuata.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Serikali. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa fedha za mafunzo zimekuwa zikibaki kila mwaka kutokana na wawezeshaji kutoka Vyuo vikuu Vya Tanzania; fedha hizo zimekuwa zikibaki kwa sababu wakati wa kutekeleza, wawezeshaji kutoka Vyuo Vikuu wamekuwa na programu nyingine katika vyuo vyao. Je, Serikali haioni ipo haja ya kutengeneza TOT wa Mkoa ili hata kama mradi utakapokwisha wanafunzi waendelee kupewa mafunzo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya mimba katika Mkoa wa Simiyu bado ni kubwa. Kwa mwaka 2017 wanafunzi 37 wa Shule za Msingi walipata ujauzito; 2018 wanafunzi 38; halikadhalika katika Sekondari kwa mwaka 2017 wanafunzi 159 walipata ujauzito; na mwaka 2018 wanafunzi 153.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchungu huo mkubwa wananchi waliamua kuanzisha ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Mwanjoro: Je, Serikali ipo tayari kuunga nguvu za wananchi waliofikisha jengo usawa wa boma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Leah Komanya kwa kuendelea kutaka watoto wa kike wapate elimu nzuri na juhudi hizi za kuunga mkono Serikali ambazo imeziweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anasema kuna fedha zinabaki kwenye programu hii. Ni kweli katika mazingira mbalimbali fedha inaweza kubaki, lakini maelekezo ya Serikali ni kwamba fedha ikibaki, wahusika wanapewa taarifa kwenye Wizara na inapangiwa majukumu mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mawazo Mheshimiwa Mbunge aliyotoa ni mazuri, tuyapokee; kuandaa TOT ili programu itakapoisha wawezeshwe watu wa eneo husika kwani itapunguza gharama, wenyewe kwa wenyewe watafundishana kwa lugha zao za nyumbani, hii kazi itaenda vizuri. Kwa hiyo, tunapokea wazo hili, tunalifanyia kazi. Ni wazo jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, anazungumza habari ya mimba na kuunga mkono juhudi za kujenga mabweni. Utakumbuka tangu juzi mpaka jana kumekuwa na mjadala katika Bunge hili Tukufu la kumalizia maboma ya madarasa lakini pia na mabweni na Vituo vya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba kazi hii inatekelezwa na Serikali inaunga mkono juhudi za wananchi, tunafanya mpango, tukipata fedha tutaweka nguvu katika maeneo hayo. Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa ambayo imepewa miradi mingi ya kuwezesha watoto wa kike wasome, kujenga madarasa, matundu ya vyoo na mabweni. Jambo hili tunalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba katika programu ijayo, fedha ikipatikana tutatoka hapa kuunga mkono nguvu za wananchi katika kumalizia mabweni ambayo wananchi wamechangia wenyewe.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nilikuwa na maswali madogo mawili ya nyongeza. Ni hatua zipi zilizochukuliwa kwa Wakurugenzi walioshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji mapato; kuchangia asilimia 40 katika miradi ya maendeleo; na kuchangia asilimia 10 kwa akina mama, watu wenye ulemavu na vijana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, katika nafasi za Wakuu wa Idara zilizo wazi Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha zinajazwa na watumishi wenye sifa za kuwa Wakuu wa Idara ili kuwepo na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za maendeleo ukizingatia Serikali inapeleka fedha nyingi sana katika miradi ya maendeleo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Leah Jeremia katika swali lake, anataka kujua ni hatua gani zimechukuliwa kwa Wakurugenzi na Watumishi wengine ambao wameshindwa kupeleka asilimia 40 na asilimia 10 kama ambavyo ndivyo ilivyo maelekezo ya Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba hata hivi karibuni Mheshimiwa Waziri wa Nchi alitoa taarifa ya tathmini ya makusanyo ya Halmashauri mbalimbali na Halmashauri ya kwanza mpaka za mwisho zimetajwa na alitoa muda ambao Halmashauri watachukua hatua kurekebisha mapato hayo na kila Mkurugenzi amepaswa kujieleza na kuonesha mikakati hiyo. Kwa hiyo, hatua zinachukuliwa na wana maelekezo mahususi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni kweli kwamba kuna fedha zimetengwa asilimia 40 ili ikaendeshe miradi ya Halmashauri. Tumetoa maelekezo, sisi viongozi wa Wizara hii, sisi Manaibu wenzake na Watendaji wengine, tukifanya ziara kwenye Halmashauri zetu, pamoja na kwenda kukagua fedha kutoka Serikali Kuu, ni lazima pia kila Halmashauri itupeleke kwenye mradi mmojawapo ambao ni own source; fedha ambazo wamekusanya kutoka kwa wananchi, zimefanya miradi? Hii ni ili tuwe na connection kati ya fedha ambayo inatolewa kama kodi, lakini pia na miradi ya maendeleo, kweli jambo linafanyika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni kweli kwamba kuna maeneo mengi wako Wakuu wa Idara na Vitengo wanakaimu na tumetoa maelekezo kufanyike utaratibu, wale ambao wana sifa wathibitishwe kazini na wale ambao hawana sifa waondolewe ili tuwe na watu ambao kimsingi wana uwezo wa kufanya maamuzi. Kwa sababu ni kweli kwamba kama mtu anakaimu, wakati mwingine amekaimishwa na Mkurugenzi, akipingana naye katika mambo fulani, anamwondoa anamweka mtu mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunataka watu wawe na uwezo, wakaelezee Idara, wawe na mipango na pia waweze kubuni kwa sababu ofisi ni ya kwake..

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali ambayo yatakuwa na afya katika Ushirika wetu. Hata hivyo, bado kuna upungufu kwenye kaguzi zinazofanywa katika Vyama vya Ushirika. Mkaguzi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) anakagua na ripoti yake inapelekwa kwa Vyama vya Ushirika hivyo kuwepo kwa mgongano wa maslahi. Je, Serikali haioni ni muda muafaka Vyama Vikuu vya Ushirika vikakaguliwa na Mkaguzi wa Mkuu wa Hesabu za Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Chama cha Ushirika Nyanza, SHIRECU na SIMCU vina mali nyingi na Serikali inafanya juhudi ya kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa vinu vya kuchambulia pamba. Nimeshudia Naibu Waziri akifanya ukaguzi wa vinu hivyo kujiridhisha na kuona hali halisi. Hata hivyo, tukumbuke katika maeneo hayohayo kuna vinu vya kuchambulia pamba vinavyomilikiwa na watu binafsi wanaofanya biashara kwa faida hivyo kuwepo na ushindani. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Vyama vya Ushirika vinajisimamia na kuwa endelevu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Komanya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama Serikali nikiri kumekuwa na udhaifu katika mfumo wa Ushirika na ndiyo maana Serikali imeamua kufanya mapitio makubwa ya Sera pamoja na Sheria ya Vyama vya Ushirika. Kama alivyosema kuhusu suala la COASCO na kushauri kwamba CAG akague Vyama Vikuu vya Ushirika; kwa mujibu wa sheria, CAG anakagua fedha za umma zinazopitishwa na Bunge, Vyama vya Ushirika ni private entity kwa muundo wake, ni vyama vya hiari.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika mapendekezo tunayokuja nayo ili kuifanya COASCO iwe na taasisi nyingine inayoifanyia oversight, bado ndani ya Serikali tunaangalia ni namna gani tutaifanya COASCO iweze kufikia malengo tuliyonayo ya kuweza kusimamia Vyama vya Ushirika na kuwa na nguvu ambayo tunaitarajia. Ni kweli sasa hivi wakifanya ukaguzi, taarifa pamoja na kuipeleka kwa Mrajisi lakini vilevile wanaipeleka kwa wanachama husika wa Chama cha Ushirika. Hii imekuwa ikileta matatizo na pale ambapo kunakuwa na viongozi wasiokuwa waaminifu huweza kutumia nafasi hiyo vibaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwa sasa COASCO wanafanya kazi nzuri, kwa miaka hii miwili wame-produce report ambayo imeweza kutuonyesha taswira ya Vyama vyetu vya Ushirika vina hali gani na sisi kama Wizara tumeanza kuchukua hatua. Kutokana na report hiyo, tumeona upungufu ambao unatulazimu sisi kama Serikali kuja na mabadiliko katika muundo wa Ushirika na namna ambavyo COASCO itafanya kazi na pale ambapo tunaamini kwamba kuna umuhimu wa kumuingiza CAG hatutasita kuchukua hatua hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Nyanza, SIMCU na SHIRECU; moja, ni sahihi kwamba ginnery nyingi na miradi mingi iliyokuwa chini ya Ushirika imefeli. Nini tunafanya kama Serikali? Tumepitia ginnery zaidi ya nane na tumeshazifanyia feasibility study ili kuweza kuziinua zikiwemo ginnery za Chato, Mbogwe, Kahama (KACU), Lugola na Manawa. Ginnery hizi tumezipitia na kuziangalia kama zinaweza kuanza kufanya biashara. Taarifa hii imeshakamilika, tunaifanyia kazi tukishirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini muundo wa uendeshaji tumesema clearly kwamba ginnery hazitaendeshwa na Wenyeviti wa Vyama vya Ushirika. Ginnery zitakuwa ni business entity zinatazoendeshwa na professional people ambao watazisimamia kibiashara ili ziendeshwe kibiashara. Mara nyingi tumekuwa tukitoa mifano, Kampouni kama Vodacom, Airtel na multi-nation zingine, shareholders hawaendeshi wana contract management na hiyo ndiyo model tutakayotumia kuendesha ginnery hizi ili ziweze kujiendesha kibiashara, hatutaziendesha kama taasisi za huduma.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Katika Mkoa wa Simiyu tayari mbegu za pamba zimeshaanza kusambazwa na kupata mbegu za pamba kwa wakulima mpaka uzinunue. Wapo baadhi ya wakulima bado hawajalipwa pamba na wanunuzi; je, Serikali inawasaidiaje ili wakulima hao waweze kupata mbegu za pamba?

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua tatizo hilo alilolisema Mheshimiwa Leah Komanya, ni kweli kampuni binafsi na ningeomba kupitia Bunge Watanzania wote wakaelewa; walionunua pamba sio Serikali ya Jamhuri ya Muungano, walionunua pamba ni kampuni binafsi za Watanzania, lakini tunafahamu kwamba Watanzania wote hawajalipwa wanaodai kampuni hizi. Mpaka sasa wameshalipa bilioni 417, wakulima wanadai bilioni 50. Tarehe 14 tutakutana na wanunuzi ili kulitatua tatizo la wao kumalizia kulipa kwa wakulima ili wakulima waweze kupata fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo vilevile makampuni yaliyopewa haki ya kusambaza mbegu bora katika maeneo ya wakulima wa pamba nao tutakutana nao ili kutengeneza utaratibu ambao hautowalazimisha wakulima wanaodai kulazimishwa kulipia mbegu ya pamba. Tutatengeneza utaratibu ambao utamfanya mkulima kama anaidai kampuni kampuni hiyo impe mbegu wakati anamlipa atakata gharama yake ya mbegu alizompatia. Kwa hiyo tarehe 14 tutamaliza tatizo hili na hili halitakuwa tatizo tena muda mfupi ujao.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa namna anavyozifikia Halmashauri zetu na kutoa maelekezo namna ya kuitekeleza mahitaji ya watu wenye ulemavu. Nilikuwa nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mkakati wa kuanzisha kanzidata nilitaka kufahamu ni utaratibu gani unaotumika kuwapata wahitimu wenye ulemavu ili waweze kuingizwa katika kanzidata?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili katika Halmashauri zetu kuna vikundi vya wajasiriamali wenye ulemavu wakiwepo mafundi selamala, lakini wameshindwa kupata masoko katika ofisi za umma. Nilitaka kufahamu Serikali ina utaratibu gani wa kuwasaidia kupata masoko ili waweze kukuza mitaji yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA A. IKUPA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ninaomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Leah Komanya Mbunge wa Viti Maalum, pia nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Leah kwa jinsi ambavyo amekuwa akihakikisha kwamba watu wenye ulemavu Mkoani Simiyu wanaenda vizuri. Nilienda ziara Mkoani Simiyu tulikuwa naye na kuna mambo niliahidi na niliweza kutekeleza pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza ameuliza kwamba ni utaratibu gani ambao Serikali tunautumia kuwapata wahitimu hao wenye ulemavu na kuweza kuwaingiza kwenye kanzidata yetu.

Awali ya yote tuliweza kuviandikia vyuo vyote vya elimu ya juu pamoja na vyuo vingine ambavyo vinatoa mafunzo kwamba watu wenye ulemavu wanapohitimu basi Ofisi ya Waziri Mkuu kuna kanzidata ambayo tunawaingiza na kuweza kuwapatia ajira. Lakini njia nyingine ambayo tumekuwa tukiitumia ni watu wenye ulemavu mara nyingi wamekuwa wakipiga simu na wakija ofisini wao wenyewe physically kwa ajili ya kutafuta ajira. Kwa hiyo, wanapokuja pale ofisini tunapata zile details zao na kuweza kuwaingiza kwenye kanzidata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiongee tu kwa kifupi kwamba kanzidata hii imekuwa na manufaa makubwa, hata mwaka jana tuliweza kupata walimu ambao waliajiriwa pale nafasi za ajira zilipotangazwa kupitia kanzidata hii. lakini pia sasa hivi tuna programy ya internship kwa vijana na tunaposema vijana ni pamoja na vijana wenye ulemavu na tunaposema vijana ni pamoja na vijana wenye ulemavu. Kupitia kanzidata hii tumepata wahitimu wenye ulemavu zaidi ya 100 ambao watanufaika nah ii program ya internship. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza kwamba ni kwa jinsi gani Serikali inafanya kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanapata masoko ya bidhaa zao, tumekwisha kuzielekeza Halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya biashara za watu wenye ulemavu, lakini pia masoko ambayo yamekuwa yakiandaliwa sasa hivi tumesisitiza kwamba miundombinu ni lazima iwe rafiki kwa watu wenye ulemavu, lakini pia ndani ya hayo masoko wahakikishe kwamba kunakuwa na maeneo ambayo ni maalum kwa ajili ya watu wenye ulamavu. Mikakati ya Serikali iko migni lakini kwa ufupi ni hiyo. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru shule ya wasichana Nyalanja yenye kidato cha tano na sita ina mchepuo mmoja tu lakini inayo madarasa sita zaidi ya miaka mitano hayatumiki.

Je, Serikali haioni haja ya kutupatia bweni kwa ajili ya kuongeza mchepuo mwingine?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna miundo mbinu kama hiyo, naomba nilichukue jambo hilo kwa sababu hivi sasa ukingalia tuna vijana wengi sana ambao kwa kweli ufaulu umeongezeka. Kwa mfano mwaka huu tuna vijana zaidi laki moja plus ambao wote wanatakiwa wape nafasi kwa ajili ya kidato cha tano na kuendelea. Kwa hiyo, kama kuna fursa kama hiyo ya madarasa yapo tutaangalia nini tufanye ikiwezekana tukatafute fedha kwa haraka tuongeze pale bweni kwa ajili kuhakikisha kwamba tunaongeza mchepuo mwingine vijana wengi wa kitanzania waweze kupata nafasi.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na kadhia hiyo, Serikali imekuwa ikichukua muda mrefu sana kulipa fidia na kifuta machozi lakini gharama hiyo pia haiakisi gharama ya uharibifu unaofanywa.

Je, Serikali ipo tayari kubadili kanuni zake kwa kuongeza gharama za kifuta machozi?

Mheshimiwa Spika, binafsi nimekuwa nikichukua hatua ya kumpigia simu Meneja wa TAWA Maswa Game Reserve lakini amekuwa haonyeshi ushirikiano wowote.

Je, Serikali ipo tayari kuwapatia mizinga wananchi katika vikundi katika Kata ya Lukungu, Mwakiloba, Kilejeshi na Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu ili kuweza kukabiliana na tatizo la tembo hao?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ni kweli yamekuwepo malalamiko ya muda mrefu ya kiwango kidogo cha kifuta machozi na kifuta jasho ambayo yamekuwa yakitolewa na Wizara yangu. Lakini nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara yangu inapitia upya viwango hivyo, na mara itakapokamilisha tutatangaza na kuwajulisha waathirika tumefanya marekebisho na nina imani ingawa haiwezi kulipa thamani halisi ya maisha ya mtu na mazao yaliyoharibika lakini itakuwa imeongeza kiwango ambacho tumekuwa tukitoa kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili nimefahamu kuwa Mheshimiwa Leah Komanya amekuwa akipiga simu mara kwa mara kutetea wananchi hasa wakati mazao yanapokuwa yamefamiwa na wanyama. Nimhakikishie tu kwamba huyu afisa ambaye hatoi ushirikiano tutampa maelekezo, lakini nitoe maelekezo kwa maafisa wetu nchi nzima kuhakikisha wana-respond haraka sana wanapopata taarifa za uwepo wa wanyama.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sasa hivi wanyama hawa wameongezeka baada ya kudhibiti ujangili kwa kweli limekuwa ni tatizo lipo nchi zima. Kwa hiyo, niwaelekeze maafisa wanyamapori popote pale walipo kuhakikisha kwamba wana wajibika haraka wanapopata taarifa hizi ili kuweza kutoa ushirikiano kwa wananchi. Na nimhakikishi tutawasiliana ili tuweze kuona namna watakavyoweza kutoa mizinga hii ya nyuki katika maeneo ya vijiji hivi.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Asilimia 10 ya EP4R inayotolewa kwa ajili ya msawazisho wa ikama, imekuwa siyo suluhu katika Mkoa wa Simiyu kwa kuwa walimu wengi sana wamekuwa wakihama. Walimu 60 wanahama kwa robo moja katika Wilaya ya Meatu na watano ndio wanahamia. Je, Serikali haioni haja ya kuwa na mkakati ili walimu wanaoajiriwa wakabaki kuitumikia Halmashauri angalau kwa miaka mitano kabla ya kuruhusiwa kuhama?

Mheshimiwa Spika, ni dhahili kwamba, siyo wasichana wote hupata hisia (pre-menstrual syndrome) kabla ya kuanza hedhi na wakati huo hakuna mwalimu yeyote wa kike ambaye anaweza kutoa msaada. Je, Serikali haioni haja ya kuwapatia Waheshimiwa Madiwani wanawake elimu ya hedhi pamoja na afya ya uzazi angalau mara moja kwa mwaka ili kwa kushirikiana na Wabunge wanawake, angalau tuwe tunatoa elimu ya uzazi kwa watoto wetu wa kike? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wa Viti Maalum wote kwa kuzingatia mambo ya wanawake na hasa waschana katika shule zetu ili kuimarisha afya zao.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anapendekeza kwamba walimu ikiwezekana wakae miaka mitano ili waweze kuhudumia katika maeneo haya. Ndiyo maana Mheshimiwa Waziri Mkuu alishatoa maelekezo katika Ofisi ya Rais TAMISEMI kwamba walimu wote kwa ujumla pamoja na wahudumu wengine wa afya, tunaandaa mfumo wa kisayansi ambao utakuwa unaweza kuonyesha kama mwalimu anataka kuhama kutoka point ‘A’ kwenda point ‘B’ ikiwa tunaweza kuangalie ile ikama.

Mheshimiwa Spika, la pili, ni kwamba, tunavyozungumza hapa, mwezi huu mwanzoni, tumepeleka fedha za EP4R, motisha kila Halmashauri. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge wakafuatilie fedha zimeenda katika Halmashauri zao na kwenye majimbo yao, Halmashauri zote nchini zimepelekewa fedha hizi za ku-balance ikama, vilevile na fedha za kumalizia maboma ya shule za msingi. Naomba mkasimamie ili zifanye kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, nitasikitika sana kama kuna shule ambayo ina walimu katika Halmashauri yake, tumepeleka fedha za ku-balance ikama halafu bado iendelee kubaki shule moja ambayo haina mwalimu wa kike, itakuwa ni bahati mbaya; na kwa kweli Mkurugenzi huyo, au Afisa Elimu wa Mkoa na viongozi wa mkoa huo watakuwa hawakuitendea haki Serikali. Maelekezo ni kwamba, fedha iliyopatikana wazingatie kuhamisha walimu wa kike, wahakikishe kila Halmashauri ina mwalimu wa kike. Kwa sababu unakuta Halmashauri mbalimbali zina walimu wengi katika maeneo mbalimbali. Tulipeleka fedha ili mwalimu akihamishwa asianze kulalamika. Hili nadhani lizingatiwe na lifanyiwe kazi. Waheshimiwa Wabunge, tusaidiane kufuatilia hili ili liweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, hoja ya miaka mitano kuelekeza, ziko taratibu mbalimbali za Utumishi wa Umma, hizo ndizo zinazingatiwa. Hata hili la kuzuia kwa muda, kimsingi tumezuia kwa sababu baada ya malalamiko mengi, kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema kwamba kuna maeneo walimu wanafika. Hata juzi tumeajiri walimu, walipaswa kuripoti tarehe 21 mwezi huu ndiyo ilikuwa waripoti kama ajira ndiyo tupange, lakini wameshaanza kuomba uhamisho. Hata kuripoti hajaripoti, hajapewa hata namna ya ajira, hajaanza kulipwa mshahara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukizuia ajira kunakuwa na malalamiko mengi sana kwamba watu wanaonewa, lakini kimsingi matatizo hayo ndiyo tunayazingatia. Kwa hiyo, tunaomba walimu waendelee kubaki maeneo yale na uhamisho umeendelea kusitishwa mpaka tutakapokamilisha mfumo ili tuweze kumhamisha mwalimu tukijua kwamba eneo analotoka au kwenda haliathiri sana utoaji wa elimu katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anashauri kwamba Waheshimiwa Madiwani wa Viti Maalum wapewe semina hii ili waweze kusaidia na Waheshimiwa Wabunge. Hili jambo tunalipokea, lakini ukweli ni kwamba elimu hii ya uzazi inatolewa; ni elimu endelevu, inatolewa kwa wazazi wenyewe, kwa wanafunzi wenyewe, kwa walimu wa kike na wa kiume. Pia Mheshimiwa Waziri wa Afya alishauri juzi hapa; na hata akina mama katika nyumba zetu, unaweza ukamlea mtoto vizuri zaidi, kwa sababu unakaa naye muda mwingi zaidi ili kusaidia kuboresha mambo haya. Tunaupokea ushauri huu, tutaona utakapofika wakati muafaka tuufanyie kazi. Ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali, bado malipo ya mishahara na makato kwa watu ambao sio Watumishi wa Umma bado yanaendelea kulipwa kulingana na hoja za Mkaguzi CAG. Kwa mfano 2017/2018 shilingi milioni 207.3 zililipwa. Je, ni kwa nini Wizara ya Fedha inachelewa kukamata yaani ku-hold makato yaliyolipwa kwa Taasisi mbalimbali na kusimamisha makato ya mishahara kwa kiwango sawa na watumishi wasiostahili kulipwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; je, Serikali inachukua baada ya muda gani kuweza kuhuisha taarifa za watumishi ili waweze kushughulikiwa haraka kwa kuondolewa katika Mfumo wa Malipo ya Mishahara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba nami nijibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Komanya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kama Serikali tulifanya HR Audit kwa Watumishi wote wa Umma wakiwepo na hawa wa TAMISEMI zaidi ya 197,000 mwaka ule wa 2016, lakini watumishi wote wale wanaoacha kazi, waliofukuzwa kazi, waliofariki, hawasalii kabisa kwenye Payroll ya Serikali. Naomba niliambie Bunge lako Tukufu na Watanzania wote kwamba kama Serikali sasa hivi tumeboresha Mfumo wa Utumishi na Mishahara kiasi cha kwamba hatutatumia tena ile Lawson Version 9 ambayo tulikuwa tunatumia, tuna Mfumo wetu wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, taarifa zozote zinazotoka kwa waajiri wote, kama ziko sahihi zinatolewa siku hiyo hiyo ikiwepo pamoja na malipo ya madai yote. Kwa hiyo, nawataka waajiri wote nchini kuhakikisha kwamba wanatuletea taarifa ambazo ni sahihi na kwa wakati na kutokana na mfumo wetu huu mpya ambao tunauanza mwezi ujao, basi taarifa za watumishi wote zitatolewa siku hiyo hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Mradi huu ulizinduliwa mwaka 2009 na baadaye ulikabidhiwa katika Mamlaka ya Maji Mwanhuzi lakini ulipokabidhiwa usambazaji wa maji haukufanyika kama ulivyokusudiwa. Nataka kujua Serikali ina mkakati gani kuhakikisha vitongoji vya Mwambegwa, Bulianaga, Jileji na Vibiti vinasambaziwa maji ikiwemo kujengewa tanki kupitia Wakala wa Maji Vijijini?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba maji ya Bwawa la Mwanyahina yamefikia kiwango cha mwisho, yakitibiwa hayawezi kutakasika na wananchi tumekuwa tukiwatumainisha kuhusu ujio wa mradi wa wa maji wa Ziwa Victoria. Nataka kujua Serikali katika utekelezaji wake wa hatua za awali umefikia hatua zipi? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Komanya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Ziwa Victoria tayari utekelezaji wa awali unaendelea. Vilevile ili kuendelea kuhakikisha vijiji hivyo alivyovitaja vinaendelea kupata huduma ya maji wakati tukisubiri mradi ule wa muda mrefu tayari wataalam wetu wameweza kufanya usanifu na kuweza kuweka mkakati wa kuchimba visima 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tayari visima vitatu vimechimbwa na viwili angalau vimeonyesha kwamba vina maji ya kutosha. Pale Mwandoya lita 40,000 kwa saa itaweza kupatikana katika moja ya visima ambavyo vimechimbwa.

Vilevile Mwankoli kisima kimeweza kupatikana chenye uwezo wa kutoa maji lita 8,500 kwa saa. Kwa hiyo, Wizara itaendelea kuhakikisha kuona kwamba maeneo yote tunayashughulikia na maji yanapatikana bombani.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Meatu liko nyuma katika utekelezaji wa umeme wa REA, kwa kuwa ni asilimia 46 tu ndiyo iliyotekelezwa. Je, Serikali haioni haja ya kupeleka kwanza kwenye kata saba ambazo hazijafikiwa kabisa ambazo ni Kata ya Mwamalole, Mwamanongu, Mwabuzo, Imalaseko, Kimali na Mbushi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika maswali mengine yaliyotangulia, Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na TANESCO na REA tunapeleka umeme na tumejipanga kupeleka umeme katika maeneo ya vitongoji na vitongoji hivyo ndimo kata zinapopatikana, ndimo vijiji vinapopatikana na wilaya inahudumia maeneo hayo hayo. Kwa hiyo katika awamu ya tatu, mzunguko wa pili, hatujabaguwa nani aanze na nani afuate tutakwenda kwa pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme katika awamu hii ya tatu, mzunguko wa pili, tumefanya mambo mawili ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na uhakika wa kupeleka umeme katika maeneo yote kwa wakati mmoja. Jambo la kwanza tulilolifanya tumegawa kazi kidogo kwa wakandarasi wachache wachache kuhakikisha kwamba basi mkandarasi anakuwa hana kazi kubwa za kufanya na hivyo kushindwa kumaliza kazi yake kwa wakati katika eneo alilopewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili tulilolifanya, tumehakikisha kwamba tunapeleka wasimamizi katika maeneo hayo ya kanda na kwenye mikoa ambayo yatakuwa yanatokea REA kwenda kuhakikisha kwamba wale wakandarasi tuliowapeleka wanafanya kazi.

Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Leah kwamba katika kipindi hiki cha REA awamu ya tatu, mzunguko wa pili, ataona matunda makubwa na mafanikio makubwa ya upelekaji wa umeme katika maeneo yote ya vijiji na vitongoji tuliyokuwa nayo.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Changamoto zilizopo Jimbo la Lushoto zinafanana kabisa na zilizopo Jimbo la Meatu kwa kuwa ni Kituo cha Mwanhuzi pekee kilichoongezewa miundombinu ambacho pia kinatumika kama Hospitali ya Wilaya.

Je, Serikali haioni haja ya kuongeza miundombinu katika Kituo cha Afya Bukundi ili kukabiliana na wagonjwa ambao pia wanachangizwa na wagonjwa kutoka Wilaya ya Mkalama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Bukundi katika Jimbo la Meatu ni muhimu sana na kwa bahati njema nakifahamu vizuri nikiwa nimefanya kazi huko kama Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Nafahamu kwamba tunahitaji kukiboresha na kukitanua kituo kile ili kiweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi kwa sababu kipo pembezoni sana na eneo lile kuna umbali mkubwa sana kufika kwenye vituo vingine vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge Leah Komanya kwamba Serikali inatambua umuhimu huo na mipango inaendelea kufanywa kutafuta fedha. Mara fedha zikishapatikana tutahakikisha kituo hicho ni miongoni mwa vituo ambavyo majengo yake yatakwenda kupanuliwa ili kiweze kutoa huduma bora zaidi za afya.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Wananchi wa Jimbo la Meatu wapo wanaotembea hadi kilometa 40 kwenda tu kufuata huduma za afya katika zahanati. Je, ni lini Halmashauri ya Wilaya ya Meatu italetewa fedha za kukamilisha maboma katika ule utaratibu wa kukamilisha maboma matatu kwa mwaka 2020/ 2021?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Leah Komanya kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwasemea wananchi wa Meatu, lakini pia kuhakikisha miradi ya huduma za afya inakamilishwa na kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Jimbo la Meatu ni jimbo kubwa na wananchi wanafuata huduma za afya mbali kutoka kwenye makazi yao. Ndiyo maana Serikali imeweka mpango wa maendeleo ya afya msingi kuhakikisha tunajenga zahanati katika kila kijiji, vituo vya afya katika kata ili kusogeza huduma hizi kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie kwamba katika mwaka huu wa fedha 2020/2021, Serikali ilitenga shilingi bilioni 27.75 na tayari imekwishatoa shilingi bilioni 23 katika majimbo na wilaya zipatazo 133 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma matatu kwa kila halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimhakikishie kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha, Juni 30, Jimbo la Meatu pia litakuwa limepata fedha zile shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma hayo. Hili ni sambamba na majimbo na halmashauri zote ambazo bado hazijapata milioni 150, shughuli hiyo inaendelea kutekelezwa na kabla ya Juni 30, fedha hizo zitakuwa zimefikishwa katika majimbo hayo.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuongeza vijiji tisa ambavyo viliachwa katika mzunguko wa pili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Mzunguko wa Pili wa REA Awamu ya Tatu, Serikali imetenga wigo mdogo wa kusambaza umeme katika vijiji ambao ni kilometa moja.

Je, Serikali haioni namna ya kuongeza wigo kutokana na mtawanyiko wa jinsi vijiji vyetu vilivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kukatika katika kwa umeme katika Jimbo la Meatu na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kumeathiri utekelezaji wa shughuli za maendeleo za wananchi: Je, ni lini kituo cha kupoozea umeme kitakamilika katika Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba katika upelekaji wa umeme kwenye maeneo yetu hatuwezi kufika katika maeneo yote kwa wakati mmoja. Ni kweli kwamba wigo uliopo hautoshelezi mahitaji tuliyokuwa nayo kwa sababu mahitaji ni makubwa kuzidi uwezo tuliokuwa nao.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba mara kwa mara tumekuwa tukiongeza wigo kwa maana ya kupanua scope ya kazi ambayo tunakuwa tumempa mkandarasi kulingana na mahitaji ya eneo husika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Leah, ambaye amekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa masuala ya umeme ya Jimbo lake, kwamba tutakapokwenda katika utekelezaji, tutaongeza wigo kama ambavyo tayari tumeongeza wigo wa vijiji tisa ambavyo Mheshimiwa Waziri amevitaja hapo kuhakikisha kwamba tunawafikia wananchi wote kuwapelekea umeme.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili; ni kweli Mkoa wa Simiyu unapokea umeme kutoka maeneo matatu; Mwanza, Shinyanga (Ibadakuli) na Bunda. Umeme huo unakuwa siyo wa uhakika kwa sababu unasafiri umbali mrefu. Hivyo Serikali imechukuwa jitihada za kuamua kujenga kituo cha kupooza umeme pale Imalilo katika Mkoa wa Simiyu ambacho kitagharimu takribani shilingi bilioni 75 na ujenzi wa transmission line ya kilometa 109 kutoka Ibadakuli (Shinyanga) mpaka pale Imalilo.

Mheshimiwa Spika, kituo hiki tayari kilizinduliwa na Mheshimiwa Waziri. Ujenzi wake ulizinduliwa tarehe 3 Machi, kwa kuweka jiwe la msingi na tunatarajia kwamba mwezi Julai tutakuwa tayari tumekamilisha taratibu za manunuzi na kufikia mwishoni mwa mwaka ujao Desemba, kituo hicho kitakuwa kimekamilika chenye kuweza kusafirisha msongo wa kilovoti 220.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mkoa wa Simiyu utakuwa una uhakika wa umeme kwa sababu umeme mkubwa utakuwa unapoozwa pale na kusambazwa katika maeneo yote ya Mkoa wa Simiyu na hivyo tatizo la kukatika katika kwa umeme litakwisha. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushuru na ninaishukuru Serikali kwa kuleta shilingi milioni 51 kwa ajili ya kulipa fidia na kifuta machozi.

Je, ni lini Serikali italeta muswada Bungeni wa kuongeza viwango vya kifuta machozi pamoja na fidia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na watumishi wa Idara ya Wanyamapori Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ambao ni wawili tu wameelemewa kutokana na upungufu wa vitendea kazi.

Je, Serikali haioni kwa kipindi hiki cha miezi miwili watumishi wa TAWA wakawepo doria wakati wa usiku ili kusaidiana na wananchi wanaokesha ili wananchi waweze kuvuna mazao yao katika kipindi hiki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Uatlii naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nianze na hili la pili; ninaomba nimuahidi Mbunge na Wabunge wengine wote ambao wana changamoto ya tembo kwamba kipindi hiki ambacho ni cha mavuno, askari watasimamia zoezi mpaka pale ambapo wananchi watatoa mazao yao na hili litaanza kuanzia sasa. Nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge hili tutalitekeleza sisi kama Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili la kwanza ambalo alisema kuleta muswada wa kuongeza kifuta machozi na kifuta jasho kwa wale ambao wameathirika na wanyama wakali hususan tembo; nimelipokea lakini wakati huo huo Serikali inaendelea kuangalia tathmini ya namna ya kufanya, lakini wakati huo huo tunaangalia nchi zingine wamefanyaje.

Mheshimiwa Spika, suala hili kwenye nchi za wenzetu/ majirani zetu ambao wana changamoto kama hii, wao liliwashinda wakaamua kuachana na mambo ya kifuta machozi kwa sababu kadri changamoto inavyozidi kuongezeka, ndivyo gharama zinavyozidi kuongezeka. Serikali ya Tanzania kwa kuwathamini wananchi wake iliona bora iweke hili eneo ili angalau wananchi waweze kufaidika. Kwa hiyo, tunalipokea lakini tutaenda kulichakata na tuone faida na hasara kwa pande zote mbili, ahsante. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Serikali iliahidi kujenga kiwanda cha kusindika chumvi Ziwa Eyasi, Nyalanja katika Jimbo la Meatu; je, ni lini Serikali itatekeleza hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba tunahamasisha ujenzi wa viwanda mbalimbali hapa nchini ikiwemo viwanda ambavyo vinachakata chumvi. Katika jimbo la Mheshimiwa Komanya katika Halmashauri ya Meatu Serikali iliahidi kujenga kiwanda kwa ajili ya kuchakata chumvi iliyopo katika Mkoa huo wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali kama Wizara tulipata andiko kutoka kwenye Halmashauri ya Meatu na andiko hilo tunalifanyia kazi. Lakini pia tunajua kwamba kuna taasisi moja ya Nutrition International ambayo yenyewe tayari imeshaanza kuongeza thamani chumvi inayochimbwa pale ambayo kweli soko lake lipo katika nchi za Rwanda na Burundi na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba sisi Tanzania ambao ndio tuko kwenye Ukanda huu wa Pwani pamoja na Kenya, ndio wenye deposit kubwa za chumvi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa hiyo, ni vyema sana na sisi kama Serikali tumelitambua hilo kutumia soko hili ili tuweze kuzalisha chumvi nyingi zaidi, tuweze kuuza katika masoko ambayo yanatuzunguka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutakamilisha hilo, na Serikali inaendelea kulitekeleza andiko hilo ili angalau tuweze kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho kwa kuwavutia wawekezaji wengi zaidi, lakini pia na taasisi za Serikali ambazo zinaweza zikafanya uwekezaji katika eneo la Meatu. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa kuonesha nia ya kuanza kuijenga hii barabara kwa sababu ni ahadi ya muda mrefu iliyoko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipande cha kilometa 74 ipo mito minne ya Itembe, Chobe, Lyusa na Nkoma ambayo imekuwa inakwamisha kuleta tija ya daraja la Sibiti lililogharimu shilingi bilioni 34.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutembelea kipande hicho na kuweza kuishauri Serikali kuanza kujenga madaraja kwa fedha iliyotengwa mwaka huu wa fedha unaoanza? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika barabara inayoiunganisha daraja la Sibiti kilometa 25 ambayo pia imetengewa fedha iko juu ya mbuga kali sana. Kujenga barabara hii inatakiwa ianze katika kipindi cha kiangazi. Ni nini kauli ya Serikali kuhusu kuianza barabara hii kama ilivyotengewa fedha mwaka 2021/2022? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Meatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Leah Komanya kwamba yale ambayo tumejadili sana ulivyokuja ofisini bado yanabaki kuwa hivyo hivyo na nitaendelea kuyaeleza hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Daraja la Sibiti ambalo lina barabara ya maingilio yenye urefu wa kilometa 25 nataka nimhakikishie Mheshimiwa Komanya na wananchi wa Meatu kwamba tayari mkataba umeshasainiwa na muda wowote barabara yenye urefu wa kilometa 25 unaanza kujengwa, lakini hautajengwa kwamba ni kilometa nusu Simiyu na nusu Singida bali tutajenga zaidi upande wa Singida ambako ndiko kwenye bonde kubwa kuhakikisha kwamba barabara hiyo inapitika.

Kwa hiyo, tayari muda wowote barabara itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ambayo pia ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu madaraja aliyoyataja naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Meatu niko tayari kwenda kuyakagua kwa sababu ni barabara ambayo imeongelewa sana, lakini nimhakikishie kwamba tayari tumeshafanya design, kwa hiyo, kinachotegemewa sasa hivi ni kupata fedha ili tutakapoanza ujenzi basi tutasubiri pia na tutategemea ushauri wake pengine ikiwezekana tuanze kwanza kujenga madaraja hayo kabla ya kujenga barabara. Kwa hiyo, nitakuja kama alivyoshauri. Ahsante sana.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Shule ya Sekondari Ngh’oboko Halmashauri ilishajenga majengo ya kidato cha tano na sita, madarasa manne yakiwa na ofisi tatu na vyoo 16 vya ndani. Je, Serikali iko tayari kujenga bweni na kukamilisha bwalo ambalo liko usawa wa Hanam likiwa na store ili shule hii iwe na kidato cha tano na sita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Mbunge hili ombi lake ameshalileta ofisini kwetu na nimeshalikabidhi kwa wataalam waweze kuangalia kwamba wanaweza kusaidia nini. Maombi aliyoyaainisha hapo ni bweni na bwalo, kwa hiyo, nilishalikubali tangu jana alipokuwa ameniletea yale maombi. Kwa hiyo, nimwambie tu kwamba aondoe wasiwasi, Serikali chini ya Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu itafanya hii kazi na tutaifungua hiyo shule ili wanafunzi waanze kusoma.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa barabara ya Mwanuzi hadi Mwabuzo, kilometa 42 imekuwa ni barabara muhimu kutokana na wafanyabiashara wanaotoka Wilaya ya Meatu na Maswa kwenda Igunga kufanya biashara na hata magari ya kusafirisha pamba. Kikao cha DCC kilipeleka maombi Mkoani na RCC walishapeleka Wizarani. Je, Serikali haioni haja ya kuipandisha barabara hiyo kuwa ya TANROADS? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kipande cha Mwabuzo – Igunga, kilometa 36 kimekuwa ni cha muhimu kutokana na biashara inayofanyika hadi mabasi saba yanapita katika barabara hiyo na wakati wa masika yanalazimika kupitia Shinyanga mpaka Igunga, kilometa 300. Je, Serikali haioni haja ya kuifungua barabara hiyo kutoka Mwabuzo kilometa 36 hadi daraja la Manonga kilometa 36? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba nitoe maelezo ya maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jeremiah ambayo yameulizwa kwenye Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja walipeleka maoni yao katika ngazi ya wilaya kama utaratibu ulivyo, yamefika kwenye ngazi ya mkoa wakajadili kwenye RCC yao na sisi Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi tumeshatuma watalaam wetu katika eneo hilo, ma-engineer wameenda wametafuta tafuta taarifa mbalimbali. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avute Subira, watalaamu wetu walete majibu yale, halafu kama itakidhi vigezo barabara hiyo itapandishwa hadhi na kuhudumiwa na TANROADS ili iweze kutengenezwa na ipitike wakati wote.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; barabara yake ya pili ambayo ameizungumza, tumeipokea kwa uzito tutaifanyia kazi, tuombe ushirikiano ili barabara hiyo iweze kufanyiwa matengenezo ya kudumu na wananchi wa eneo hilo waendelee kupata huduma muhimu kwa njia ya barabara. Ahsante. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi na Serikali ya Kijiji ya Mwambiti iliyopo Jimbo la Meatu katika Halmashauri ya Meatu imeridhia kutoa eneo lake la ekari mia moja bila fidia kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha VETA; Je, Serikali ipo tayari kupokea hati hiyo ya kieneo ili kukabiliana na vijana wanaokosa fusa zinazotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Komanya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa hatua hiyo nzuri waliyoichukua ya kutafuta eneo na tayari wameshaandaa mpaka Hati na Wizara tuko tayari kupokea hati hiyo. Kwa sababu wameshapiga hatua moja mbele kwa kupata eneo na tayari wameshatafuta Hati tunaamini katika mchakato unaokuja pindi Serikali itakapopata fedha ina maana atakuwepo kwenye mgawo wa awamu hiyo.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Serikali isiiondoe Wilaya ya Meatu kuchukulia umeme katika Kituo cha Mabuki, Mwanza, chenye umbali wa kilometa 200 ikairejesha Wilaya ya Meatu ilikokuwa mwanzo inachukulia Ibadakuli, Shinyanga, umbali wa kilometa 100 ili kuondoa tatizo la kukatikakatika kwa umeme, ambalo linasababishwa na umeme kusafiri umbali mrefu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuweka eneo moja kupata umeme kutoka sehemu nyingine ni jambo la kitaalamu na sio kwa kuangalia umbali peke yake, lakini pia na uwezo wa kituo fulani kuhudumia watu wetu walioko jirani, lakini naomba nikiri kwamba, nachukua jambo hilo na nitaenda kuliwasilisha kwa wataalam ili walichakate na kuona kama kwa sasa tunaweza kuhama kutoka upande hu una kwenda kwingine, kwa ajili ya kuboresha huduma hii. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Rais na Wizara kwa kuidhinisha na kutekeleza mradi wa dharura katika Mji wa Mwaluzi siku si chache wananchi wataanza kunufaika na Mto semu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto zilizoainishwa katika majibu ya Serikali ninamuomba Mheshimiwa Naibu Waziri afike Jimbo la Meatu katika Bwawa hilo ilia one hizo adhan a kuchukua hatua za haraka ili kunusuru bwawa hilo lililogharimu Shilingi Bilioni 1.8 bila kunufaisha wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mradi huu ulitekelezwa na Wizara, RUASA Wilaya kwa mwaka uliotajwa tayari mipango mingine imewekwa. Je, ukarabati huu utafanywa kwa ngazi ya Mkoa au ngazi ya Wizara? Ninakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninapenda kupokea pongezi na kwa hakika tuna kila sababu ya kuendelea kumuombea Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameitendea haki hii Wizara ya Maji. Tumeendelea kupata fedha na ndiyo maana tunaona kila kona miradi ya maji inaendelea kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, kufika Meatu ni moja ya taratibu zangu za kazi, naomba nikupe taarifa Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wabunge wote wanaotoka Mkoa wa Simiyu ratiba yangu ni kuanzia tarehe 25 mwezi huu kuwa Simiyu hivyo tutafika maeneo haya yote korofi ili kuona tunafanya kazi kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na ukarabati tutafanya kwa kushirikiana na watendaji wetu ambao wapo katika Mkoa ule na Wizara hatuna pa kukwepea ni lazima tuwajibike katika hilo. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Msingi wa uanzishwaji wa maboma ya zahanati ulitokana na uliokuwa mradi wa uendelezaji wa mitaji katika Serikali za Mitaa. Hivyo katika Bunge la Kumi na Moja, lilitaka Serikali kukamilisha maboma hayo baada ya mradi huo kwisha. Je, Serikali haioni haja ya kupeleka mwongozo wa matumizi ya fedha katika fedha za kukamilisha maboma ya zahanati? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, takribani ni miaka miwili sasa Serikali imepeleka fedha 2021/2022: Je, Serikali iko tayari kufanya sensa ya kuangalia fedha zilizopelekwa kukamilisha maboma, zinaendana na maboma yaliyokamilishwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilipeleka mwongozo wa namna ambavyo fedha zinazopelekwa kwa ajili ya kukamilisha maboma ya zahanati Shilingi milioni 50 kwa kila boma zinatakiwa kutumika na kukamilisha maboma yale. Moja ya maelekezo ilikuwa ni kwamba, boma ambalo linaombewa fedha, Shilingi milioni 50 lazima liwe limefika hatua ya renter, siyo msingi au chini ya renter. Hesabu zilifanywa kwamba Shilingi milioni 50 ipelekwe kwenye jengo ambalo limefikia hatua ya renter linakamilika na kuanza kutoa huduma za afya mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kila inapopeleka fedha, inapeleka na mwongozo, na pia tunafuatilia kuona utekelezaji wa miradi hiyo kwa mujibu wa mwongozo uliopelekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na kufanya tathmini kama fedha ambazo zilipelekwa kwa ujenzi wa maboma zimekamilisha; katika mwaka wa fedha uliopita zaidi ya maboma 555 yamelekewa Shilingi milioni 50, lakini zaidi ya asilimia 85 mpaka Juni mwaka huu yalikuwa yamekamilika, na yako hatua za mwisho za kusajiliwa. Tunaendelea kufanya tathmini kuhakikisha fedha hizo zinaleta tija kwa wananchi.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kilomita 25 kwa kiwango cha lami katika maingilio ya Daraja la Sibiti kwa kuwa bajeti yake imetengwa mwaka huu wa bajeti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunategemea kujenga barabara za maingilio zenye urefu wa kilometa alizozitaja kama 23. Barabara imeshakamilika na tuko mbioni kwa muda wowote tutakapokuwa tumekamilisha fedha kwa sababu tunaendelea na hiyo mipango ya kuhakikisha kwamba maingilio yale yanajengwa kwa kiwago cha lami. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango upo, tumeahidi na tutautekeleza kadri fedha zitakapopatikana, kama si mwaka huu basi mwaka wa fedha tutakaouanza.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati zilizojengwa miaka ya 2000 vyumba vyake havikidhi hadhi ya kujifungulia kinamama kwa kuwa ni vidogo na vingine ni mfano wa corridor limewekwa pazia tu.

Je, Serikali haioni haja zahanati hizo za zamani kukajengwa wodi ya akina Mama ili kuendana na sera ya afya ya kinamama baada ya kujifungua wapumzike Saa 24? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ndiyo maana nimesema Serikali imeanza na imegundua tatizo hilo kwamba lipo na ndiyo maana kumekuwa na marekebisho yanayoendelea kwenye vituo mbalimbali. Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika harakati za kupunguza vifo vya akina Mama na Watoto hayo anayoyasema yamezingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona kuna fungu maalum kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI, limekuwa likipelekwa kwa ajili ya kujenga hayo maeneo ya akina Mama kwa ajili ya kujifungulia.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naishukuru Serikali; mwezi Julai mwaka jana tumepokea shilingi milioni 192 kwa ajili ya uendelezaji wa shule hiyo kuwa kidato cha tano na sita. Ni lini Serikali itatuletea fedha kwa ajili ya kukamilisha bwalo na kujenga makataba ya high school?

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa fedha hizi zilikuja zikaanzisha majengo mapya na kuacha yaliyokuwepo. Ni lini Serikali itakamilisha nyumba nne za watumishi zilizopo pale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tulishaanza hatua ya awali na tumebakisha tu ujenzi wa bwalo pamoja na maktaba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa tutakapopata fedha za mradi ambayo tunayo sasa hivi, tutazitenga kwenye bajeti na kupeleka katika shule hiyo.

Mheshimiwa Spika, na kuhusu majengo mapya ni kwamba kwa sababu sasa hivi tuna miradi mikubwa miwili ya SEQUIP pamoja na BOOST ambapo sehemu ya fedha hizo ni pamoja na kumalizia majengo, kujenga majengo mapya, pamoja na nyumba za walimu. Tutafanya hivi mara tutakapopokea fedha hizo, ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA. Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali.

Kwa kuwa miundombinu iliyopo ni chakavu na ina hadhi ya kituo cha afya, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu imetenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kuanza miundombinu mipya.

Je, Serikali haioni haja ya kujenga miundombinu mipya inayokidhi hadhi ya Wilaya kwa kuwa hospitali hiyo ina eneo la hekari za ziada 17?

Mheshimiwa Spika, hospitali hii ina upungufu mkubwa wa watumishi kwenye eneo la wauguzi wenye degree na wenye weledi; mahitaji ni wauguzi 24 tuliye naye ni mmoja. Je, Serikali haioni haja ya kutuletea wauguzi wenye weledi ukizingatia tumejenga Jengo la ICU? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuwapongeza Halmashauri ya Meatu kwa kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kuendelea na ujenzi na ukarabati wa Hospitali ya Halmashauri ya Meatu, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imefanya tathmini nchini kote hospitali chakavu 50 ambazo zinaupungufu wa Miundombinu zimeanza kutengewa fedha shilingi bilioni 16.5 mwaka huu wa fedha, lakini hospitali 39 ikiwemo ya Meatu zinatengewa fedha kwa mwaka ujao wa fedha. Kwa hiyo nimhakikishie kwamba kazi ya ujenzi wa Majengo hayo itafanyika.

Mheshimiwa Spika, pili, ni kweli kwamba Halmashauri ya Meatu ni miongoni mwa Halmasahuri zenye upungufu wa watumishi. Hata hivyo Serikali kwenye mwaka wa fedha uliopita imeajiri jumla ya watumishi wa afya 10,462 na Halmashauri ya Meatu imepata jumla ya watumishi 104 wakiwemo wauguzi, lakini pia na madaktari na zoezi hili tutaendelea kulitekeleza kwa awamu, ahsante sana.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, ni kweli wiki moja iliyopita tumepokea Milioni 43 kwa ajili ya kuanza kazi zilizoainishwa hapo. Kutokana na umuhimu wa daraja katika mto huo uliosababisha Mheshimiwa Rais Samia Suluhu kuahidi daraja la juu mwaka 2015.

Je, Waziri uko tayari kufika katika Kijiji hicho ukajionea adha inayokata mawasiliano ya Kata Nne na Wilaya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Maafisa kutoka Wizara ya Ujenzi walifika kukagua hilo daraja pamoja na barabara. Ninataka kujua Je, ni lini Serikali itaipandisha hadhi hilo daraja kuwa TANROADS ili tuweze kupata fedha za kutosha kuihudumia barabara hiyo kutokana na umuhimu wa kiuchumi wa Wilaya ya Meatu na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya Mbunge wa Meatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niko tayari nitakwenda katika eneo lake kama alivyoahidi, kwa hiyo nitafika kwenda kujionea hiyo hali halisi anayoizungumza Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapokea maombi yote na tunatambua kwamba kuna maombi mengi sana ambayo Halmashauri na Mikoa kupitia Bodi ya Barabara yameyafikisha kwa ajili ya kupandishwa hadhi. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kuyafanyia kazi na mara watakapokuwa wamemaliza kujiridhisha maana yake barabara hizo zitapandishwa hadhi. Kwa hiyo, siyo kwamba Serikali inapuuza ni kwa sababu tunafanya tathmini tunaangalia uwezo wa kifedha ili kazi hiyo inapokamilika maana yake na hizo barabara iweze kutengenezwa kulingana na hiyo hadhi.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Utekelezaji wa ujenzi wa vyoo shuleni kupitia program ya usafi wa mazingira inazingatia uwepo wa maji. Je, ni upi mkazo wa Serikali katika uvunaji wa maji katika majengo ya Serikali zikiwemo shule zetu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara itaendelea kuhakikisha shule zote zinapata maji safi na salama pamoja na vituo vya afya. Lengo ni kutimiza kauli ya maji ni uhai na maji yatazingatiwa kufika na Waheshimiwa Wabunge niwatoe hofu, shule zote katika majimbo yetu zitafikiwa na huduma ya maji safi na salama.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nusu ya Wilaya ya Meatu imepakana na Hifadhi ambazo ni Ngorongoro, Serengeti na Maswa Game Reserve. Je, ni lini Serikali itaendelea kunufaisha miradi katika Wilaya ya Meatu, miradi ile ilikuwa inatolewa na ujirani mwema kutokana na utalii unaofanywa katika Hifadhi ya Serengeti na Ngorongoro ikiwemo ujenzi wa mabweni?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimwambie tu kabisa Mheshimiwa Mbunge kwamba, asiwe na wasiwasi na niendelee kumpongeza kwa sababu wananchi wanaozunguka yale mapori ya akiba tunatambua umuhimu wa namna ya kunufaika na CSR. Hata hivyo, kwenye eneo hili Mheshimiwa Leah amekuwa akileta maombi katika ofisi zetu, lakini tutambue tu kwamba katika kipindi cha miaka miwili hii iliyopita tulikuwa tuna changamoto ya UVIKO 19 ambapo hifadhi zetu ziliathirika sana. Hivyo Serikali ilichukua jukumu la kuzisaidia hizi hifadhi ili ziweze kujiendesha.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumeshaanza kuimarika vizuri, CSR zitarudi kama ilivyokuwa mwanzo na pengine zaidi hasa ukizingatia Royal Tour imeibua mambo mengi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami kilometa 25 katika maingilio ya Daraja la Sibiti ili kunusuru mmomonyoko kwa kuwa barabara iko juu ya mbuga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Daraja la Sibiti linatakiwa kujengwa approach roads, yaani barabara za maingilio kilometa 25. Taratibu za kumpata mkandarasi ambaye atajenga zinaendelea. Hata hivyo bado katika hii barabara ndiyo barabara ambayo mpango wa EPC+F barabara ndefu pia itapita hapo. Ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali kwa kutambua uwepo wa maboma nchini.

Je, Serikali haioni haja ya kutafuata programu nyingine ya kufanya maboresho katika Ofisi za Kata baada ya programu ya Ruzuku ya Uendelezaji Mitaji Serikali za Mitaa kukoma? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliridhia watendaji walipwe shilingi 100,000; je, Serikali sasa haioni yale malipo yao yakakatwa at source, yakalipwa na Hazina katika mapato ya Halmashauri kwa sababu yanapitia kwenye mfumo wa Treasury Single Account ili kuondokana na usumbufu unaotokana na ucheleweshwaji wa Watendaji wa Kata kupata yale mafao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Ofisi za Maafisa Watendaji za Kata, na pia Ofisi za Watendaji wengine wote wa Serikali katika Halmashauri zetu na ndiyo maana imeendelea kutenga fedha kwa awamu, kuhakikisha kwamba tunakamilisha majengo hayo na fedha hizo ni kupitia mapato ya ndani, na pia kupitia fedha za Serikali Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nachukua fursa hii kuwakumbusha na kuwasisitiza Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali Mitaa kote nchini kuweka kipaumbele katika bajeti za mapato ya ndani kwa ajili ya Ujenzi wa Ofisi za Kata na pia Ofisi za Vijiji na Ofisi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na posho za Maafisa Watendaji wa Kata shilingi 100,000, Serikali ilishatoa maelekezo, na ni wajibu wa Wakurugenzi kuhakikisha fedha za posho za Watendaji wa Kata zinawafikia kwa wakati bila ucheleweshaji wowote. Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutafuatilia kuhakikisha kwamba fedha hizo zinawafikia kwa wakati, ahsante. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa kuwasha umeme kwa wakati katika vijiji vya Jimbo la Meatu hususani kwenye kata ambazo zilikuwa hazijaguswa. Je, ni lini sasa Serikali itaanza kusambaza umeme wa ujazilizi katika vitongoji vyote vya Jimbo la Meatu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunashukuru kwa pongezi angalau kuna maeneo ambapo Mradi wetu wa REA III, round II umekamilika ikiwemo Mkoa wa Simiyu na tunaendelea kuhakikisha kwamba na maeneo mengine mradi unakamilika. Katika vitongoji kama nilivyotangulia kusema tayari tumepata fedha kwa ajili ya kuongeza wigo kutoka kilomita moja hadi kilomita tatu ambazo zitafika katika vitongoji vingi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali inatafuta fedha nyingi zaidi za kuweza kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote takribani 36,000 ambavyo vimebaki Tanzania visivyokuwa na umeme takribani shilingi 6,500,000,000,000 na tunaamini zitapatikana na umeme katika miaka minne, mitano au sita ijayo, vitongoji vyote Tanzania vitafikiwa na huduma ya umeme.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, ni lini Serikali itaendeleza Ujenzi wa skimu ya Kijiji cha Mwagrila baada ya kutumia shilingi bilioni 1.2 na haikuwa kwenye mpango wa Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tulituma watalamu kupitia skimu zote nchi nzima, zile ambazo zilikwama na zile ambazo zinahitaji marekebisho tumeishatengeneza picha nzuri ya kuzijua zote pamoja na hiyo ambayo ameitaja nataka nimtoe hofu ya kwamba ipo ndani ya mipango ya Serikali tutaitekeleza.
MHE. LEAH. J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa maboresho yaliyofanywa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kwa kuwa changamoto kubwa ya mkaguzi wa nje CAG katika POS ilikuwa ni matumizi ya fedha mbichi na kusababisha kushuka kwa mapato ya hamashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kufahamu je, mfumo mpya wa TAUSI unakwenda kukabiliana nayo vipi hii changamoto?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakusanya mapato wengi hawana taaluma. Nilitaka kujua mkakati wa Serikali wa kuajiri wahasibu wa kutosha katika halmashauri zetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la kwanza nianze kwa kusema changamoto kubwa ambayo ilikuwepo kwenye halmashauri zetu na hizi POS kuwa ziko offline ilikuwa ni uadilifu wa watumishi wetu. Tayari Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilichukulia hatua wale wote waliopatikana na hatia ya kucheza na POS hizi na hivyo kupotezea mapato halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna Dashboard hivi sasa katika mfumo mpya wa TAUSI ambapo katika halmashauri zote, Mkurugenzi ana uwezo wa kuona mapato yaliyokusanywa kwa wakati huo na kama kuna POS yoyote itakwenda offline basi nayo Mkurugenzi ataona. Hata hiyo, dashboard ile ile iko Mkoani na vilevile Ofisi ya Rais, TAMISEMI tuna uwezo wa kuona. Kwa hiyo, tumefanya maboresho makubwa sana na kuanzia tarehe 1 Julai ndio mfumo pekee ambao utatumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali la pili; la taaluma, Kuajiri watu wenye taaluma ya uhasibu. Hili tunalipokea na kadri ya uwezo wa Serikali wa kibajeti tutaajiri watu kuendana na taaluma ya uhasibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Je, Serikali iko tayari kujua sababu za kwa nini Kituo cha Afya cha Iramba Ndogo hakijakamilika ili kiweze kuchukua hatua na kunufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali iko tayari kufanya tathmini na kujua sababu zilizopelekea kituo hiki cha afya kutokamilika. Pia itachukua hatua za kisheria na za kinidhamu ikithibitika kuna baadhi ya watumishi ambao hawakufuata taratibu za fedha na kusababisha kituo kutokamilika, ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Nataka kujua kauli ya Serikali kuhusu kuporomoka kwa zaidi ya asilimia 50 kwa bei ya alizeti kwa wakulima na hali nchi ina upungufu mkubwa wa kujitosheleza katika uzalishaji wa mafuta ya kula?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli bei ya alizeti imeporomoka na imesababisha kuwakatisha tamaa wakulima, lakini sisi Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Fedha tumekaa chini na kuangalia namna bora ya kuweza kutatua changamoto hii ikiwemo kuangalia sera zetu za fedha na hasa katika kuliboresha eneo la kuongeza kodi kwa mafuta ambayo yanaagizwa kutoka nje ya nchi ili kuweza kuwalinda wakulima wetu wa ndani. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru hadi hapo ilipofikia ni kazi kubwa imefanywa na Serikali, Mheshimiwa Rais Samia alipita njia hiyo akaiona hiyo adha kwenye hilo daraja. Je, Serikali iko tayari kutoa kipaumbele kwenye mwaka ujao wa fedha kwa sababu Wilaya tumetenga hizo fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mvua inaponyesha Kata ya Mwabuzo, Mwamanongu, Imaraseko, Mwamalole hukata mawasiliano na Wilaya. Je, Mheshimiwa Waziri upo tayari kuja kuiona hiyo adha wanayopata Wananchi wa Jimbo la Meatu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali ipo tayari kutoa kipaumbele kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili ambalo Mheshimiwa Mbunge aliliuliza kwenye swali lake la msingi na tutaangalia kadri ya upatikanaji wa fedha kwenye mwaka wa fedha 2023/2024, kuona ni namna gani tunaweza kuanza na kama fedha basi zitakuwa hazitoshi katika mwaka huo wa fedha tutaenda kuona tunatenga fedha kwa ajili ya kutekeleza pia ahadi hii ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mwaka wa fedha 2024/2025.

Mheshimiwa Spika, nikijibu swali lake la pili la kama nipo tayari kuongozana naye kwenda kuona namna miundombinu ilivyoharibika katika maeneo haya ya Jimbo lake kule Meatu. Nipo tayari kuongozana nae na baada tu tukihitimisha Bunge hili la bajeti tarehe 30 Juni mwaka huu, mimi nipo tayari kupanga na Mheshimiwa Komanya ili tuweze kuelekea wote kule Meatu.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Je, Serikali imefanya tathmini kujua kama majukwaa ya wanawake yanaleta tija katika wilaya zetu?

NAIBU WAZIRI UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Komanya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukwaa haya ya wanawake katika mikoa yamekuwa na tija kubwa, kwa sababu ndio ambayo yamepelekea wanawake wengi kupata mikopo, lakini pia kuwa na elimu ya ujasiriamali katika maeneo tofauti tofauti. Changamoto tuliyonayo ni kuona sasa tunawezesha zaidi majukwaa haya ya wanawake ili kuweza kupata mikopo kwa wakati, lakini yenye kutosheleza mahitaji yao kadri ambavyo wanaomba. Kwa hiyo kuna tathmini ya kutosha ambayo tunaifanya ili kuona namna gani zaidi ya kuendeleza majukwaa haya ya wanawake katika mikoa.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza.

Shule husika ililetewa fedha shilingi milioni 80 kwa ajili ya kujenga bweni la watoto wenye mahitaji maalum, je, ni lini Serikali italeta fedha za kukamilisha bweni hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge. Mheshimiwa Komanya amekuwa akifuatilia sana shule hii ya Mwanhuzi na alinieleza nilipokutana naye ofisini kwamba ndipo alipotokea yeye kwenye kata hiyo na atahakikisha kwamba fedha hii shilingi milioni 348 inapatikana, kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Leah kwa hili.

Mheshimiwa Spika, nikijibu swali lake la nyongeza la bweni ambalo lilianzwa kujengwa katika shule hii hii ya Msingi ya Mwanhuzi. Serikali ilipeleka shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni kwa watoto wenye mahitaji maalum katika shule hii na sio shule hii pekee yake bali ilipeleka nchi nzima kwa ajili ya ujenzi wa mabweni haya, lakini baada ya kupeleka fedha hizi ujenzi ule haukukamilika na changamoto hii tunaifahamu na timu ya wataalam ilitumwa kwa ajili ya kufanya tathmini kwenye mabweni yote na mabwalo yote ambayo yalipelekewa fedha na hayakukamilika. Baada ya tathmini hiyo kufanyika sasa tupo katika mchakato wa kutafuta fedha kwa ajili ya kupeleka kukamilisha ujenzi wa mabweni haya na mabwalo haya. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Elimu bila malipo imeweza kuibua vijana wenye vipaji kutoka familia zenye mazingira magumu. Mfano, Bariadi mwaka juzi alitokea kijana aliyepata ‘A’ zote katika masomo yake. Wanafunzi hao wamekuwa wakipangwa shule maalum au shule zilizo mbali zaidi na kushindwa kumudu gharama za kusafiri na zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani wa kuwabaini wanafunzi wa aina hii ili waweze kuwasaidia na kutimiza ndoto zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tumekuwa tukiomba mabweni kwa ajili ya shule zetu za Kata na zinapokamilika shule hizi zinakuwa za Kitaifa. Je, Serikali haioni haja ya kuona kuwa na catchment area kama vile katika Mkoa au Wilaya kuwe na shule ya bweni ili tuweze kuwanusuru vijana wanaokatisha masomo kwa kutembea umbali mrefu. Kwa mfano, mwanafunzi anayetokea Lukale kilomita 40 kwenda Bukundi na kurudi kilomita 40? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwamba wanafunzi wote wenye vipaji Serikali inawazingatia, na inapotokea wanafunzi waliofanya vizuri kama huyo na bahati mbaya anakuwa ameenda katika maeneo ambayo hakustahili, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumefungua dirisha, mnatuletea hayo maombi na tunaweza tukafanya mabadiliko mengine. Kwa hiyo, hilo liko wazi na liko ndani ya uwezo wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ujenzi wa shule za bweni katika ngazi ya mkoa kwa kuzingatia hayo; umbali, mahitaji na vipaji, ndiyo maana kwa mwaka huu wa fedha na mwaka 2021, Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ameamua kujenga Shule za Kimkoa kwa wasichana. Mwaka 2021 tumeshapeleka fedha shule 10 na mwaka huu vile vile tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule nyingine 10 za kimkoa ambazo zitapokea wasichana wenye vipaji katika mikoa husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie tu kwamba lengo la Serikali litafikiwa na tunafanya hivyo kupunguza umbali pamoja na kuongeza tija ya elimu katika maeneo husika, ahsante. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Jengo linalotumika katika Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Meatu halikidhi hadhi kwa sababu lilikuwa ni Mahakama ya Mwanzo tukiwa Wilaya ya Maswa. Je, Serikali iko tayari kutujengea jengo jingine kwa kuwa eneo la kujenga Mahakama ya Wilaya tunalo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali iko tayari kujenga jengo la Wilaya kama tu wanaendelea kutumia majengo ambayo hayakuwa mahsusi kwa ajili ya Mahakama za Wilaya. Kama tulivyoeleza hapo mwanzo tayari wako kwenye mpango na tutakapowasilisha ofisini kwako na kuwatumia wao wataona kila mtu kwenye position yake Mahakama yake inajengwa lini. Asante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Jengo linalotumika katika Mahakama ya Wilaya katika Wilaya ya Meatu halikidhi hadhi kwa sababu lilikuwa ni Mahakama ya Mwanzo tukiwa Wilaya ya Maswa. Je, Serikali iko tayari kutujengea jengo jingine kwa kuwa eneo la kujenga Mahakama ya Wilaya tunalo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Leah Komanya Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali iko tayari kujenga jengo la Wilaya kama tu wanaendelea kutumia majengo ambayo hayakuwa mahsusi kwa ajili ya Mahakama za Wilaya. Kama tulivyoeleza hapo mwanzo tayari wako kwenye mpango na tutakapowasilisha ofisini kwako na kuwatumia wao wataona kila mtu kwenye position yake Mahakama yake inajengwa lini. Asante.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Kwa kuwa mradi huu ulitumia shilingi bilioni 1.2 na haukukamilika; je, Serikali haioni haja ya kuangalia kilichosababisha kutokukamilika ikiwemo halmashauri kutohusishwa kusimamia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa kuwa Wilaya ya Meatu hatujanufaika na Miradi ya Umwagiliaje je, Serikali pia ipo tayari kutupatia eneo la umwagiliaji katika Kata ya Mwamalole na Mwabuzo eneo moja ambalo tumelipa kipaumbele kama wilaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba tu nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na changamoto ambazo zilijitokeza awali na mapendekezo ambayo ameteyatoa sasa hivi tu miradi yote tunahakikisha kwamba inashirikisha watu wote ikiwemo halmashauri, Wabunge wa maeneo husika pamoja na Sekretarieti za Mikoa ili kuhakikisha kunakuwa na ufanisi katika kutekeleza. Kwa hiyo, tumelipokea hilo jambo na tutalifanyia kazi na hata hivyo karibuni tulikaa na Wabunge kuanisha kwenye maeneo ya miradi hiyo kuona namna gani watashiriki katika miradi yao.

Mheshimiwa Spika, la pili, kutoa kipaumbele katika maeneo ambayo ameyataja hapa ikiwemo Mwamalole. Kata ya Mwamalole nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imepanga kwamba maeneo yote yanayofaa kwa ajili ya umwagiliaji tutayafikia na tutajenga miradi kwa ajili ya Skimu za Umwagiliaji na Mabwawa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa Serikali imetenga fedha ya kujenga VETA katika bajeti inayoanza Julai, imetenga fedha ya kujenga VETA 36.

Je, Serikali inaweza ikawaambia nini vijana wa Meatu ambao tayari wameshaandaa eneo la kujenga VETA?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoanza kueleza kwenye majibu ya msingi kwamba Serikali ina sera ya kujenga chuo katika kila wilaya nchini. Katika bajeti yetu ya Serikali ni kweli tumetenga zaidi ya shilingi bilioni mia moja kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 36 au vyuo katika wilaya 36 nchini. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwa vile tutaweka vigezo vya namna gani zile Wilaya 36 tunakwenda kuzipata na kwenda kufanya ujenzi na kwa vile ujenzi unafanyika kwa awamu, nimhakikishie tu na niwahakikishie wananchi wa Meatu katika mgao huo ujao tuwahakikishie kwamba na wao Wilaya ya Meatu tutaweza kuzingatia ili tuweze kupata chuo katika eneo hilo. (Makofi)