Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Emmanuel Papian John (3 total)

MHE. EMMANUEL P. JOHN aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaongeza gari la wagonjwa na mafuta ili kufanya huduma za kliniki katika maeneo hayo pamoja na huduma nyingine kuwaokoa kina mama na watoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Papian John, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto inayo magari mawili ambayo yamekuwa yakitumika kubeba wagonjwa waliopewa rufaa ya matibabu. Magari haya pia hutumika katika huduma ya mkoba za kliniki za Afya ya Uzazi na Mtoto (RCH) kwa lengo la kuwaokoa akina mama na watoto. Katika Mpango wa Bajeti ya mwaka 2016/2017, Halmashauri haikuweka kipaumbele cha ununuzi wa gari la wagonjwa kutokana na ukomo wa bajeti. Tunaishauri Halmashauri iendelee kutumia magari mawili yaliyopo huku ikijipanga kuweka kipaumbele cha ununuzi wa gari kwa mwaka wa fedha 2017/2018
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bajeti ya mwaka 2015/2016, Halmashauri hiyo ilitengewa shilingi 43,283,040 kwa ajili ya mafuta ya gari na hadi sasa fedha zote zimeshapelekwa. Changamoto ya kijiografia ndiyo inaonekana kuwa tatizo linalosababisha bajeti iliyotengwa kutokidhi mahitaji.
MHE. EMMANUEL P. JOHN aliuliza:-
Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi huko Kiteto baina ya wakulima na wafugaji:-
(a) Je, ni lini Serikali itaipatia Kiteto Mahakama ya Baraza la Ardhi ili kesi nyingi ziweze kusikilizwa hapo Kiteto?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kupima ardhi yote ya Kiteto ili kila mtu afahamu mipaka ya eneo lake ili kuepusha mwingiliano wa maeneo usio wa lazima, itafanya hivyo lini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 231 la Mheshimiwa Emmanuel Papian John, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu naomba nifanye sahihisho dogo kwenye jibu la msingi isomeke mwaka 2015/2016 na siyo 2016/2017 kama ilivyoandikwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu sasa Wabunge wafahamu kuwa lengo la Serikali la kuunda Mabaraza ya Ardhi katika kila Wilaya ni kusogeza huduma za utatuzi wa migogoro karibu na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara iliahidi kuunda Mabaraza nane likiwemo Baraza Nyumba katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kiteto ametoa jengo ambalo tayari limeshafanyiwa ukaguzi ili kubaini mahitaji. Wizara imekwisha nunua samani za ofisi na hata sasa inaendelea na taratibu za upatikanaji wa watendaji. Taratibu hizo zitakapokamilika baraza litaanza kazi mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, Novemba, 2014, kikosi kazi cha kushughulikia mipaka ya maeneo katika Wilaya ya Kiteto kiliundwa. Kikosi kazi hicho kilijumuisha wataalam kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI; Ofisi ya Takwimu; Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wataalam kutoka Halmashauri ya Kiteto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zilizofanyika zilikuwa ni kurekebisha mipaka ya vijiji 10; Kijiji cha Loltepes, Emart, Enguserosidan, Kimana, Kinua, Nhati, Nemalock, Ndirigishi, Krashna na Taigo) katika eneo lililokuwa limegombewa kuzunguka hifadhi ya Emboley Murtangos kukamilisha mipango shirikishi ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 10 ni pamoja na kupima mashamba 2,110 katika vijiji vitatu, Kijiji cha Loltepes mashamba 385; Kimana mashamba 1,250; na Nemalock 475 na kutoa elimu iliyolenga kutatua migogoro ya ardhi katika Wilaya ya Kiteto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii ni kazi endelevu na itakamilika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. EMMANUEL P. JOHN aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya NARCO (Hogoro) Kibaya – Olkesimeti – Oljoro - Arusha kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Papian John Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa ujenzi wa barabara ya NARCO (Hogoro) hadi Kibaya – Olkesumeti - Oljoro hadi Arusha yenye urefu wa kilomita 450 uko katika hatua ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na maandalizi ya nyaraka za zabuni. Kazi hiyo inafanywa na Mtaalam Mshauri M/S Cheil Engineering Co. Limited wa Korea Kusini akishirikiana na Inter-Consultant Ltd wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtaalam Mshauri tayari amewasilisha taarifa ya awali (Draft Final Report) mwezi Julai mwaka 2019 kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kupatiwa maoni kuhusu mapungufu ambayo tayari ameagizwa kuyafanyia kazi. Taarifa ya Mwisho ya Usanifu (Final Design Report) inatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa Septemba, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya usanifu kukamilika na gharama kujulikana, Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.