Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Kemirembe Rose Julius Lwota (16 total)

MHE. KEMIREMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Nashukuru kwa maelezo mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nasikitika kusema hajajibu swali langu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mkoa wa Mwanza wanapata taabu kwa vipimo vya x-ray na CT-Scan na inawabidi waende kwenye Hospitali za Private ambazo ni gharama kubwa sana kufanya vipimo hivi. Swali langu: Je, ni lini Serikali itanunua machine ya CT-Scan na x-ray kwa hospitali yetu ya Mwanza ya Sekou Toure?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kemirembe, Mbunge wa Viti Maalum, Mwanza kama fuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, alichojibu Mheshimiwa Naibu Waziri kinabaki kuwa ni sahihi. Tuna mradi wa Orion kwa ajili ya kununua vifaa tiba na kuvisimika katika hospitali zote za Rufaa nchini ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure, Mwanza. Tumepata fedha, juzi Mheshimiwa Rais katika ile fedha ya kufanya Semina Elekezi kwa Mawaziri shilingi bilioni 2.8 itatumika kwa ajili ya kununua vifaa hivi. Tulikwama muda mrefu kwa sababu hiyo fedha haijapatikana. Fedha imeshatolewa. Kwa hiyo, lini? Tayari, anytime, soon, tutaweza kusimika hivi vifaa katika Hospitali za Rufaa zote za Mikoa Tanzania.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Kemirembe tunakuomba sana, tunajua wananchi wanatumia gharama kubwa kufanya hivi vipimo katika hospitali binafsi na lengo letu ni kuwapunguzia mzigo Watanzania. Hili tunalifanya kabla ya mwaka huu wa fedha wa 2015/2016 haujaisha.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo kubwa sana la maji Wilayani Misungwi kwenye Kata za Mbarika, Nyangomango na Iyerere ambako chanzo cha maji cha Ziwa Viktoria kinapita maji yaendayo Shinyanga na Kahama. Je, ni lini Serikali itapitisha maji kwenye vijiji hivi ambavyo vinayaona maji tu yanapita, lakini wao hawana maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ilikamilisha mradi wa kutoa maji Ziwa Viktoria kupeleka Shinyanga. Katika bajeti inayokuja ambayo Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji ataisoma, tumetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha upelekaji wa maji kwenye vijiji ambavyo vimepitiwa na hilo bomba kuu lakini havikuweza kupatiwa maji katika hiyo Programu ya Kwanza. Hii itakwenda sambamba na huu mradi ambao unaanza Shinyanga kuelekea Wilaya za Nzega na Mkoa wa Tabora na kwenda Igunga. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi, tunalifahamu hilo, sehemu zote ambazo hazijapatiwa maji kupitia mradi huo tutahakikisha kwamba tunaongeza vijiji ikiwemo vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge umevitaja.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo kubwa la vifaa hivyo kwenye Hospitali hii ya Wilaya ya Nyamagana, na ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ya mwaka 2013. Sasa je, ni lini vifaa hivi vitaletwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Nyamagana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana inahudumia wananchi zaidi ya 300,000 kwa hiyo inaelemewa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza inafika mahala inashindwa kutoa huduma stahiki. Pamoja na hayo, Halmashauri ya Jiji imejitahidi na kuongeza jengo la wodi ya wanaume na watoto ambayo hazikuwepo. Je, Wizara inampango gani wa kutusaidia ili wodi hizi ziweze kukamilika? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nadhani ni mara ya pili Mheshimiwa Kemi anauliza swali la sekta ya afya katika Mkoa wa Mwanza, kwa hiyo nimpongeze sana kwa kuona kwamba suala la afya ni muhimu sana. Lakini katika suala zima la ni lini x-ray italetwa, nimesema hapa kwamba kila kitu ni budgeting na bajeti ya mwaka huu tumetenga karibuni milioni 133. Lengo kubwa ni kwamba x-ray iweze kununuliwa na iweze kufika. Jukumu letu kubwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI ni kuhakikisha kwamba pesa hizo mwaka huu wa fedha zinapatikana ili ahadi aliyoweka Mheshimiwa Rais iweze kutimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kujengwa kwa wodi pale, nipende kusema kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI itashirikiana na ninyi watu wa Mwanza kuhakikisha wodi ile inafanya kazi. Sambamba na hilo nipende kuwashukuru wenzetu wa Vodacom ambapo juzi kupitia vyombo vya habari nimeona wanafanya usaidizi mkubwa sana katika hospitali ya Sekou Toure pale Mwanza. Lengo letu ni kwamba wadau wanaoshiriki kama kama hivi na sisi Serikali tunasaidia kwa kiwango kikubwa kupeleka huduma za afya kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Kemi kwamba Serikali itaungana na watu wa Mwanza, itaungana na Bwana Mabula, Mbunge wa Nyamagana na ninyi Wabunge wa Mwanza wote kuhakikisha suala la afya katika mkoa wa Mwanza, kwa sababu ni Jiji kubwa inaimarika vizuri kutokana na population kubwa iliyokuwepo katika eneo hilo.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kumekuwa na uharibifu mkubwa sana wa barabara ya Mkoa wa Mwanza hususan barabara ya Mwaloni iendayo kwenye Soko la Kimataifa la samaki, Mkuyuni, Kiseke, Nyamongolo Bulale na Kishiri. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kutengeneza barabara hizi, zenye umuhimu wa kiuchumi kwenye Jimbo la Ilemela na Nyamagana?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayoiongelea ni barabara yetu sote; sisi Ujenzi na TAMISEMI; na kwa sasa iko chini ya TAMISEMI, lakini kazi tunaifanya kwa pamoja. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, katika swali aliloliuliza kwamba tutafanya kazi kwa pamoja kati ya TANROAD Mkoa pamoja na wenzetu wa Halmashauri tuiangalie hii barabara ambayo inagusa eneo nyeti na muhimu la uvuvi ili tuweze kuiweka katika hali ambayo wavuvi wetu watapata fursa nzuri ya mawasiliano.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ila nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Naibu Spika wote tunafahamu tatizo la maji na tunajua kabisa maji ni uhai na hakuna Mbunge hata mmoja humu ndani ambaye tutamsimamisha ambaye Jimbo lake halina tatizo la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika ifike mahali kama Serikali tuwe na vipaumbele vichache ambavyo tutaweza kuvitekeleza kiuhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, katika
mradi huo wa Nyamazugo - Buchosa mradi huo wa maji unapita katika vijiji vya Isenyi, Nyamabanda na Nyanzenda ambapo ndiyo chanzo cha maji kinaanza na unaenda kutekelezwa kwenye vijiji vingine zaidi, swali langu, ni lini Serikali itafikisha maji katika vijiji hivi vichache ambavyo maji yanapita na kwenda kutekelezwa kwenye vijiji vingine?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Wilaya ya Sumve kwenye vijiji vya Kadashi na Isunga kumekuwepo na mradi wa maji ambao umekaa unasuasua kwa miaka mingi. Je, ni lini Serikali itamaliza mradi huu wa Wilaya ya Sumve? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya Mbunge ni kwamba kuna chanzo cha maji lakini kuna vijiji jirani ambapo maji yanatoka kwamba kwa mujibu wa design vijiji
vile vitakosa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tufanye rejea ya Mheshimiwa Waziri wa maji kwamba na Waziri wa Nishati na Madini kwamba kwa mkakati wa Serikali ya hivi sasa ni kuhakikisha kwamba maeneo yote ambayo vyanzo vinapatikana basi vitapewa kipaumbele jinsi gani kuweka design kama mwanzo vilisahaulika kuweka utaratibu wa
kuweka design nzuri ya kuhakikisha maeneo yale ambayo vyanzo vinapatikana yaweze kupata maji.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba nikuhakikishie kwamba Serikali hii itafanya kila liwezekanalo wananchi wa eneo lako lile lazima wapate maji kutokana kwamba lazima Serikali iweze kuwahudumia wananchi wale, lakini siyo hivyo tu, na wao watasaidia kuweza kulinda vizuri
chanzo cha maji katika eneo lile. Lakini katika eneo la Sumve ni kwamba kuna mradi wa maji lakini mradi huu unaonekana kwamba haujakamilika, ni commitment ya Serikali na
naomba tufahamu, siyo mradi huo peke yake karibu kuna miradi mingi sana ilianza kutekelezwa lakini mingi ilisimama huku nyuma naona flow ya fedha lilikuwa siyo nzuri, lakini hivi sasa kwa Seriakli ilivyojipanga ni kwamba mradi sasa hivi
mkandarasi akikamilisha kazi, aki-submit certificate maana yake certificate inalipwa na mkandarasi anaendelea kufanya kazi. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie kwamba Serikali itajitahidi kwa kadri iwezekanavyo miradi yote ambayo ilikuwa ime-stuck sasa wakandarasi waweze kutimiza wajibu wao, wakamilishe ile miradi, wa-raise certificate zitalipwa ilimradi lengo la miradi iweze kukamilika na miradi hiyo iweze
kuwapata wananchi.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ila nina swali dogo moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuliona hili na siku ya Mei Mosi ametoa tamko watumishi wote watakaohamishwa vituo vyao walipwe fedha zao kabla ya uhamisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna baadhi ya watumishi wengi tu ambao wamehamishwa kwenye vituo vyao vya kazi, wameenda kwingine na hawajalipwa fedha zao za uhamisho mpaka leo. Kuna baadhi ya taasisi hata waliohamishiwa hapa Dodoma Makao Makuu hawajalipwa fedha zao mpaka leo.
Sasa ni lini Serikali italipa fedha za watumishi hawa waliohamishwa na hawajalipwa fedha zao za uhamisho? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa concern ya Mheshimiwa Mbunge na siku zote maswali yake yamekuwa yakigusa wananchi wake na hasa watumishi, nakupongeza sana Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi yetu ilifanya zoezi la uhakiki wa madeni kwa sababu tuna Halmashauri mpya nyingi sana zimeanzishwa. Kwa mfano, siku nilivyofika pale Busega au kwa mtani wangu Tabora Vijijini kwenye Halmashauri mpya ya Isikizya, nimekutana na watumishi wakilalamikia suala hili la madeni. Ndiyo maana ofisi yetu tukafanya uhakiki wa madeni na tumeyawasilisha Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunazunguka maeneo mbalimbali tumekuta baadhi ya Halmashauri tayari madeni haya yameshaanza kulipwa. Kwa hiyo, kwa sababu uhakiki ulishafanyika na taarifa iko Hazina tufanye subira na wengine wameshaanza kulipwa na madeni yao yote yatalipwa kwa sababu Serikali haitaki kuona haki za watu zinadhulumiwa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Naibu Waziri Mheshimiwa Selemani Jafo kwa majibu mazuri, lakini pia Mheshimiwa Kemilembe kwa swali zuri ambalo kusema ukweli linawagusa watumishi wengi na hasa wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tabia za Wakurugenzi wa Halmashauri kuwahamisha na hasa walimu kwa kuwakopa gharama ambazo wangepaswa kuwalipa kwa ajili ya usumbufu na gharama za uhamisho.
Nilisema hapa Bungeni hadi tarehe 30/04/2017 wanapaswa kuwa wamewalipa walimu waliowahamisha. Hili nililisema si kwa madeni ya nyuma sana ya uhamisho maana yale yote tulishayapeleka Wizara ya Fedha kwa ajili ya kulipwa, lakini kuna uhamisho uliofanyika kati ya mwezi Januari hadi Machi wa kupanga ikama za walimu. Deadline imefika na kuanzia sasa Wizara yangu itachukua hatua kwa wale wote ambao hawajawalipa walimu waliowahamisha. Haiwezekani Serikali tunapambana kupunguza madeni lakini wako watu wengine ni viwanda vya kuzalisha madeni yasiyokuwa na sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kusema ukweli suala hili tumelitilia msisitizo mkubwa lakini pia Serikali ipo katika mchakato wa kuandaa fedha kwa ajili ya kupanga hizi ikama kwa nchi nzima kwa Halmashauri zote. Zoezi hili litaenda sambamba na malipo ya moja kwa moja kwa watumishi watakaohamishwa kwa sababu ni haki yao ya msingi ya kiutumishi.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kumekuwa na tatizo kubwa sana na uhaba mkubwa wa dawa ya morphine kwenye hospitali zetu ambayo inapelekea wagonjwa hususani wa cancer kuteseka na maumivu makali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu, je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuweka dawa hii ya morphine kwenye list ya dawa muhimu au National Essential Drug List ili ziweze kupatikana kirahisi na kuwaponya maumivu wagonjwa hawa wa cancer? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwamba dawa ya morphine iwekwe kwenye Essentials Medicine List ni kitu ambacho katika hali ya sasa ya nchi yetu hatuwezi kukikubali kwa sababu ni katika dawa ambazo ziko controlled na kwamba ili kuzitoa ni lazima kuwe kuna ujuzi fulani unaohitahijika kuwepo katika kituo hicho ndipo mtu aweze kuruhusiwa kutoa dawa hiyo. Ndiyo maana inatolewa kwa kibali maalum, inatunzwa kwa kibali maalum na hatuwezi kubadilisha hilo kwa sababu dawa ya morphine ina madhara kama ikiwa administered na mtu ambaye hata ujuzi wa namna ya kuitunza na namna ya kui-prescribe.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri inaonyesha dhahiri kabisa kwamba Serikali inabagua maeneo ambayo hayana Hospitali za Wilaya. Kwa mfano, Wilaya ya Sengerema kuna hospitali moja ya mission inahudumia wananchi wote wa Wilaya ya Sengerema na kuna ombi ambalo limetolewa na wilaya yetu miaka minne iliyopita la kujenga Hospitali ya Wilaya Sengerema ya Serikali.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ombi hili na kujenga Hospitali ya Wilaya ili kuweza kuweka huduma ya vifaa tiba na dawa katika Wilaya yetu ya Sengerema? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishe tu kwamba Serikali haibagui Wilaya yoyote ile dhidi ya Wilaya nyingine kwa sababu Wilaya zote hizi mwisho wa siku ndiyo zinaunda nchi yetu Tanzania. Kwa hivyo, tunatoa huduma sawa kwa maeneo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuhusu hospitali ya Sengerema, nimefika kwenye hospitali ile na nimeshuhudia maendeleo makubwa yanayofanywa kwa ushirikiano baina ya mission, Mheshimiwa Mbunge, rafiki yangu na Mwenyekiti wangu wa Bunge Sports Club Mheshimiwa Ngeleja pamoja na Halmashauri yake na wadau mbalimbali wakiwemo Vodacom Foundation na kuna miradi mizuri inayoendelea katika Wilaya ya Sengerema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kujenga Hospitali ya Wilaya nimshauri Mheshimiwa Mbunge akishirikiana na Mheshimiwa Ngeleja kwa pamoja kwenye vikao vyao vya Halmashauri waweke kipaumbele cha kuanzisha mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Nina uhakika Mheshimiwa Jafo anasikiliza vizuri hapa atashirikiana nao kuwapa ufundi na sisi tutawapa ufundi, lakini pia ikibidi kama kuna rasilimali fedha tutawasaidia. Hata hivyo, uamuzi wa kwanza uwe ni wao wenyewe kuweka kipaumbele cha kuanzisha Hospitali ya Wilaya, lakini kwa sasa inaonyesha wameridhika na huduma zinazotolewa na Hospitali ya Mission.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tatizo kubwa sana la wavuvi, hasa wa Kanda ya Ziwa na wa Ziwa Victoria kuchomewa nyavu zao na kusababishiwa hasara kubwa sana na Serikali. Ni lini sasa Serikali itatoa maamuzi ya kukataza nyavu hizi kutengenezwa kwenye viwanda ili wananchi wetu wasiendelee kupata hasara ya kuchomewa nyavu zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali itaendelea kutoa elimu ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata kujua nyavu gani ambazo haziruhusiwi na nyavu gani ambazo zinaruhusiwa.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia sheria zetu za uvuvi tutaendelea kushirikiana na wavuvi wetu na jamii yote ya wavuvi ili kuhakikisha kwamba zile nyavu zisizoruhusiwa hatutaziacha, lakini nyavu zinazoruhusiwa ambazo zipo katika vipimo vya kisheria zitaendelea kutumika. Vilevile kuwahamasisha wawekezaji zaidi waweze kutengeneza nyavu zinazoruhusiwa kwa ajili ya kulinda mazingira yetu.
MHE. KEMIREMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhimu wa daraja hili na kuagiza lijengwe haraka iwezekanavyo. Pamoja na hayo, kumekuwa na tatizo kubwa sana ambalo linatengeneza usumbufu mkubwa sana kwa wananchi kutokana na ubovu wa meli zilizopo. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kurekebisha vyombo hivi wakati tunasubiri ujenzi huo wa daraja? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu mara nyingi tumezungumza juu ya changamoto mbalimbali ambazo zinawapata wananchi ambao wanavuka kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu tunafuatilia sana matatizo ambayo yapo hapa kutokana na hivi vivuko vipo, najua vipo vivuko vikubwa vitatu lakini iko changamoto ambayo vikiharibika vinasababisha usumbufu mkubwa sana kwa wananchi wa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu matatizo haya pia yanachangiwa na wananchi wenyewe. Nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge tushirikiane kuwaomba sana wananchi katika maeneo haya hasa wavuvi, wanavua katika maeneo haya ya kivuko, matokeo yake zile nyavu zinanaswa na vivuko hivi na mara nyingi inasababisha uharibifu wa vivuko hivi ambavyo vinafanya kazi pale. Kwa hiyo, niombe tu wananchi tushirikiane na tusimamie jambo hili ili wananchi wasije wakaendelea kuvua maeneo haya ya karibu ili vyombo hivi vifanye kazi kwa efficiency. Kwa hiyo, nasisitiza tu kwa upande wa wenzetu wa TEMESA, wasimamie vizuri wakati harakati za ujenzi wa kivuko zinaendelea. Baada ya ujenzi naamini kwamba usumbufu utakuwa umeisha lakini pia itachangia sana katika ukuaji wa uchumi wa maeneo hayo na Tanzania kwa ujumla.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kumekuwa kuna hamasa ya uhamasishaji mkubwa sana kwa wananchi wetu kujiunga na vikundi hivi ili waweze kupata mikopo hii asilimia 10 kutoka kwenye Halmashauri zetu, lakini kiuhalisia Halmashauri nyingi mikopo hii haitoki. Nataka kujua, Serikali ina mpango gani wa kuwezesha Halmashauri zetu ili mikopo hii iweze kutoka na akinamama, wazee na watoto waweze kupata mikopo hii kama inavyoonekana? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, swali hili limekuwa likijirudia mara kwa mara na majibu ambayo tumekuwa tukitoa, tumekuwa tukielekeza kwamba wakati tunakuja kuhitimisha bajeti kuna kipengele ambacho kitaingizwa katika Finance Bill ambacho kitamlazimisha kila Mkurugenzi kuhakikisha kwamba pesa hizi zinatengwa na zisipotengwa sheria zitachukuliwa ili kutoa adhabu kwa wale wote ambao hawatatimiza takwa hili la kisheria. Kwa sasa hivi, imekuwa ni kama option lakini tutakuja na kipengele ambacho kitamlazimisha kila Mkurugenzi a-make sure kwamba pesa hizi zinatengwa.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Nyakato Steel – Igombe, kilometa 18 na Barabara ya Mwaloni – Kirumba, kilometa 1.2 zimekuwa zikisuasua na ujenzi wake kwa muda mrefu sana. Mheshimiwa Angeline Mabula, amekuwa akifuatilia barabara hizi kwa muda mrefu lakini bado hatujapata majibu sahihi ya Serikali. Ni lini sasa barabara hizi zitakamilika na wananchi wa Mkoa wa Mwanza, hususan Wilaya ya Ilemela waweze kupata barabara safi na salama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua changamoto za barabara za Ilemela, nami nimekwenda, nimeona. Nitoe tu maelekezo na wito kwa Mameneja wetu kule kwenye Mkoa wa Mwanza kwamba wasimamie kwa ukaribu nami nitakwenda kuhakikisha kwamba maeneo haya; na yapo maeneo siyo haya tu aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge, yapo maeneo mengi kwenye Jimbo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Angeline Mabula kwa sababu amekuwa akifuatilia sana, ilinichukua siku nzima, mtandao ni mkubwa sana kwenye Jimbo lake, mjini lakini…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, majibu mazuri na muhimu, fanya ziara naye.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, nitakwenda.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli suala hili la matibabu bure limekuwa na changamoto kubwa sana mpaka kuna baadhi ya vituo na hospitali wakina Mama wajawazito wanambiwa waende na mabeseni, pamba na hata mikasi.

Je, ni lini Serikali sasa itaona umuhimu wa kuweka angalau fedha kidogo za kuchangia akina mama wajawazito ili waweze kupata huduma bora? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, huduma kwa ajili ya akina mama wajawazito ni bure na sisi kama Seriakli tumekuwa tunaendelea kuwekeza sasa hivi takribani akina mama milioni mbili wanajifugua kwa mwaka ndani ya nchi yetu na sisi kama Serikali kupitia Bajeti hii ya dawa, vifaatiba na vitendanishi tumejaribu sana kuhakikisha vifaa vya kujifungulia vinakuwepo, tumehakikisha kwamba chanjo kwa ajili ya watoto tunakuwa nazo, dawa zote za muhimu kwa maana dawa za kupunguza upungufu wa damu kwa akina mama yale madini ya iron pamoja na phera sulfate pamoja na folic acid tunakuwa nazo, dawa za kuongeza uchungu oxytocin tunakuwa nazo na dawa za kupunguza kifafa cha mimba tunakuwa nazo. Kwa hiyo, ni sehemu chache sana ambazo tunapata malalamiko kama hayo na mimi kama Naibu Waziri nimetembelea sehemu mengi sana basi ni sehemu nyingi vifaa vya kujifungulia tunavyo na sisi kama Serikali tunavyo kupitia Bohari yetu ya madawa.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Katika Wilaya ya Kwimba, Kata za Bugando, Mkalalo na Mwabomba kumekuwa na tatizo kubwa sana la mawasiliano na ni la muda mrefu. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka mawasiliano kwenye Kata hizo za Wilaya ya Kwimba ili wananchi hao waweze kufaidika na mawasiliano ya nchi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kemilembe, Mbunge wa Viti Maalum, Mwanza, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Kemilembe kwa jinsi anavyofuatilia masuala ya mawasiliano kwa Mkoa Mzima wa Mwanza ambapo kwa kweli muda mwingi sana amekuwa akifuatilia maeneo mbalimbali ya Mkoa huo. Kuhusu Wilaya ya kwimba ni kweli Mheshimiwa Kemilembe alikuja akaniletea barua kuhusu kata ambazo alizitaja. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Kemilembe na Mbunge wa Kwimba kwamba tayari zabuni kuhusu kata alizozizungumza zimewekwa kwenye kitabu maalum ambapo anaweza akaja mezani kwangu kuangalia. Awamu ya tano tutahakikisha kata zote zilizobakia ambazo hazijapata mawasiliano zinapata mawasiliano.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mtakubaliana nami kwamba kuna mstari mdogo sana kati ya uzima na afya ya akili. Katika nchi ambazo tafiti zimefanyika kwa mfano Marekani inaonyesha katika kila watu wanne mmoja ana tatizo la afya ya akili, Uingereza katika kila watu watano mmoja ana tatizo la afya ya akili, Australia katika watu 6 mmoja ana tatizo la afya ya akili.

Mheshimiwa Spika, nadhani wewe mwenyewe unaweza kuwa shahidi hata humu ndani wakati mwingine unajiuliza tuko salama kiasi gani. Nataka kufahamu je, Serikali yetu imefanya tafiti ya kujua ni idadi gani ya watu ambao wameathirika na ugonjwa wa afya ya akili Tanzania? Na kama tayari tafiti zimefanyika matokeo yake yakoje?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kemilembe Lwota Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Mwanza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli changamoto za afya ya akili zinazidi kuongezeka na ndio maana Shirika la Afya Duniani sasa hivi linaweka msukumo mkubwa katika kuliangalia suala la afya ya akili. Takwimu zake ziwezi nikazipinga, ni kweli takribani karibia asilimia moja ya katika jamii yetu ya Tanzania tunaamini kwamba wana tatizo l a afya ya akili.

Kwa hiyo hata hili alilolisema, kwamba hata humu ndani inawezekana na sisi ile asilimia moja tuna changamoto kama hizo. Sisi kama Serikali bado hatujafanya utafiti wa kina wa kuangalia ni uzito wa jambo hili likoje aina gani ya magonjwa ya akili ambayo tunayo ndani ya nchi yetu. Tunalipokea hili Mheshimiwa Mbunge na tutaenda kulifanyia kazi.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA: Mheshimiwa Spika, ahsante nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, suala la ajali za bodaboda siyo kwa Mkoa wa Mara tu, ni Tanzania nzima kwa ujumla wake. Bodaboda hawa wengi wao wanakata third part insurance ambayo kimsingi inatakiwa iwasaidie pale wanapopata matatizo lakini kiuhalisia insurance hii haiwasaidii chochote bodaboda hawa wanapopata matatizo.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kukaa na hawa watu wa insurance ili baadhi ya fedha inayotozwa/ wanayolipa hawa watu wa bodaboda iweze kwenda kwenye Halmashauri zetu ili waweze kupata msaada kwenye hospitali ambapo hospitali hizi ndiyo zinawapokea na kuwatibu watu hawa? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, wazo lake linafikirika na kwa hiyo basi tunalichukua, tulitafakari.