Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hassan Elias Masala (17 total)

MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwa na zoezi la utafiti katika Kata ya Nditi, Wilayani Nachingwea linalofanywa na kampuni tofauti:-
(a) Je, nini hatma ya utafiti huo wa muda mrefu ambao unaleta mashaka kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo?
(b) Je, wananchi wa maeneo jirani wanaweza kuruhusiwa kufanya shughuli za uchimbaji mdogo ili waweze kunufaika badala ya kuwa walinzi na vibarua?
(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta watafiti zaidi katika maeneo mengine ya Wilaya hizo kama Kiegei, Marambo, Nditi na kadhalika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa eneo la Nditi lililoko Wilaya ya Nachingwea limefanyiwa utafiti wa madini kwa muda wa zaidi ya miaka minane sasa, hasa madini ya nickel katika eneo la Ntaka Hill. Leseni ya utafutaji ya PL Namba 4422/2007 ilitolewa tarehe 7 Aprili, 2007 kwa kampuni ya Warthog Resources ambayo inatoka Australia ambayo kwa sasa inaitwa Nachingwea Nickel Limited.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mwaka 2007 hadi mwaka 2014 kampuni hii imetumia zaidi ya dola za Marekani milioni 36 na kugundua mashapo ya madini ya nickel takribani tani 356,000 na ya shaba tani 76,000 na upembuzi yakinifu unaonesha mashapo yanatosha kuchimba kwa mgodi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuendelea kuanguka kwa bei ya nickel kwenye Soko la Dunia kumesababisha kampuni kutoanzisha mgodi wa uchimbaji mapema. Kampuni inakusudia kuanzisha mgodi huo mara baada ya bei ya nickel kuimarika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kifungu Namba 14 cha Sheria ya Madini ya 2010, kinamzuia mtu yeyote asiye na leseni halali ya kuchimba madini, kufanya hivyo. Namuomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu tushirikiane kuelimisha wananchi ili kutovamia maeneo kuchimba madini kiholela bila kuwa na leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Lindi kuna kampuni 98 zenye jumla ya leseni 213 za utafutaji mkubwa wa madini. Madini yanayofanyiwa utafiti ni pamoja na nickel, dhahabu, graphite, gypsum, manganese pamoja na beach sands.
Sehemu kubwa ya maeneo aliyotaja Mheshimiwa Mbunge, ya Kiegei, Marambo na Nditi ni baadhi ya maeneo ambayo leseni hizi za utafutaji zipo. Tunashauri pia wananchi wa maeneo hayo watumie fursa ya uwepo wa makampuni haya kushirikiana nayo katika shughuli za utafiti. Aidha, Wakala wa Jiologia Tanzania (GST) wanaendelea kufanya utafiti wa madini katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya Nachingwea.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza maji ya mradi wa Mbwinji kwenye Vijiji vyote vinavyozunguka mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Maji safi wa Msasi-Nachingwea kutoka chanzo cha Mbwinji unahudumia wakazi wapatao 188,250 wa Miji ya Masasi na Nachingwea pamoja na baadhi ya Halmashauri za Wilaya ya Masasi, kama vile Nachingwea na Ruangwa. Zaidi ya shilingi bilioni 40 zimetumika katika ujenzi wa mradi huo ambao ulizinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 24 Julai, 2014.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha huduma ya maji katika Wilaya za Masasi, Ruangwa na Nachingwea, Mamlaka ya mradi wa Kitaifa wa Masasi - Nachingwea (MANAWASA), inakusudia kufanya upanuzi wa miundombinu ili kuunganisha vijiji vingi vikiwemo vijiji vya Mtepeche, Naipanga, Chemchem, Mailisita, Mkotokuyana na Nampemba vya Wilaya ya Nachingwea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kutekeleza miradi ya upanuzi wa miundombinu ya usambazaji maji kupitia katika Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Masasi-Nachingwea na itaendelea kutenga fedha zaidi ili kupanua huduma ya upatikanaji wa maji katika Miji ya Masasi na Nachingwea pamoja na vijiji vyake.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH (K.n.y MHE. HASSAN E. MASALA) aliuliza:-
Redio ya Taifa (TBC) haisikiki Wilayani Nachingwea, pamoja na kuwepo kituo cha kurusha matangazo katika eneo la Stesheni.
(a) Je, ni tatizo gani linasababisha kutosikika kwa Redio ya Taifa katika Jimbo la Nachingwea?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kukifanyia ukarabati kituo cha kurushia matangazo Nachingwea ambacho pia ni chanzo cha ajira kwa wakazi wa jirani na kituo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, matangazo ya Redio ya Taifa katika Jimbo la Nachingwea yalikuwa yakisikika maeneo yote ya Wilaya ya Nachingwea na Mikoa ya Kusini kwa ujumla kupitia mtambo wa masafa ya kati (medium wave) wa kilowati 100 ambao tangu tarehe 01/01/2012 haufanyi kazi kutokana na uchakavu. Kwa hivi sasa eneo la Nachingwea Mjini ndilo linalopata matangazo ya Taifa kwa kutumia mitambo miwili midogo ya redio, FM ya watt 230 (TBC- FM) na watt 100 TBC-Taifa, ambayo imefungwa katika kituo cha redio kilichopo eneo la Songambele.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali, ni kufunga mitambo mpya na ya kisasa ya FM yenye nguvu kubwa ya kilowati mbili pale fedha zitakapopatikana.
Mtambo huo utakuwa na uwezo wa kurusha matangazo yatakayowafika wananchi sehemu mbalimbali. Ufungwaji wa mitambo hiyo utaenda sambamba na ukarabati wa majengo ya mitambo, Ofisi na miundombinu mbalimbali ya kituo cha Nachingwea.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Nachingwea ni miongoni mwa Wilaya chache zilizo na historia ndefu katika kusaidia nchi nyingi za Afrika kupata uhuru; kwani wapiganaji wengi wa nchi hizo walihifadhiwa kwenye Kambi ya Ukombozi Farm 17 iliyopo Nachingwea:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhifadhi na kuendeleza maeneo ya Kambi ya Farm 17 hata kama yamegeuzwa kuwa Sekondari ili kuwa maeneo ya kihistoria na kuweza kuwavutia watalii?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzishawishi nchi zilizonufaika na Kambi ya Farm 17 kama Msumbiji na Zimbabwe ili ziangalie kwa karibu kambi hiyo kwa lengo la kuhifadhi kumbukumbu muhimu zilizopo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO – (K.n.y WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala Mbunge wa Jimbo la Nachingwea kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Farm17 ni miongoni mwa maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika katika harakati za ukombozi. Serikali kwa kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo Sanaa na Vijana imeanzisha mradi ujulikanao kama Road to Independence kwa lengo la kutunza kumbukumbu za historia ya ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo Farm 17. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itashirikiana na Wizara hiyo katika kuhakikisha kuwa eneo hili linatunzwa ipasavyo ili kuvutia watalii wakaolitembelea. Aidha, tunapenda kuushauri uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea kusaidia shule ya sekondari Farm 17 kuendeleza uhifadhi wa miundombinu ya kihistoria iliyopo shuleni hapo ili kutunza historia hiyo muhimu ya ukombozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haina mpango wa kuzishawishi nchi zilizopata hifadhi ya wapigania uhuru hapa nchini, kusaidia juhudi za uhifadhi wa maeneo hayo kwani nchi zenyewe zina hiari ya kuona umuhimu huo kwani lengo la Serikali ilikuwa ni kusaidia harakati za ukombozi kwa nchi husika.
Barabara ya Masasi – Nanganga – Nachingwea

(a) Je, Serikali ina mpango gani juu ya ujenzi wa barabara ya Masasi – Nanganga – Nachingwea, yenye urefu wa kilometa 91 kwa kiwango cha lami?
(b) Je, ni lini Serikali italipa fidia wananchi wanaotakiwa kupisha ujenzi wa barabara hiyo hasa ikizingatiwa kuwa tathmini imeshafanyika muda mrefu?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekwishakamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 91 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Kazi za usanifu zimekamilika mwezi Septemba, 2015. Aidha, kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Nanganga.
Mheshimiwa Naibu Spika, zoezi la tathmini kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaoathirika na kazi ya ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea – Nanganga limekamilika na ulipaji wa fidia kwa wananchi hao ili kupisha ujenzi utaanza mara baada ya fedha kupatikana.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwamilikisha na kutoa Hati za Kimila kwa wananchi wa Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nachingwea ina jumla ya vijiji 127, hadi kufikia mwaka 2007 vijiji 104 vilikuwa tayari vimefanyiwa upimaji. Kati ya hivyo 104, vijiji 99 tu ndiyo vilikuwa vimepata vyeti vya vijiji na hapo vijiji 22 ndiyo vilikuwa vimewekewa mpango wa matumizi bora ya ardhi. Mwaka 2009 Vijiji vya Mbondo, Nakalilonji na Nahimba vilikuwa katika mchakato wa kuandaliwa Hati Miliki za Kimila pamoja na ujenzi wa Masijala ya Ardhi kwa ufadhili wa MKURABITA ambao haukukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa kukamilisha wananchi na kutoa Hati za Haki Miliki za Kimila ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Ardhi Na. 5 ya mwaka 1999 na Kanuni zake. Hati na Haki Miliki za Kimila siyo tu zinawahakikishia wananchi usalama wa miliki zao bali pia huwawezesha wananchi kuzitumia kama dhamana za mikopo pale wanapohitaji kukidhi vigezo vya mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi zinazofanywa na Halmashauri mpaka sasa ni kutenga fedha katika bajeti zao ili kukamilisha zoezi la utoaji wa hati 1,170 ambazo hazikukamilishwa na MKURABITA. Aidha, Halmashauri imejiwekea mkakati wa kutayarisha hati nyingine 1,170 na kuzigawa kwa wananchi wa Vijiji vya Mbondo, Nakalonji, Nahimba na Namatunu ifikapo 2017. Jukumu la Halmashauri za Wilaya ni kutenga fedha katika bajeti zao ili kuwezesha utoaji wa hati za haki miliki za kimila kwa kufuata sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza Ofisi ya Mbunge wa Nachingwea kwa kuwezesha pia kufanikisha zoezi la uandaaji wa Hati Miliki za kimila katika Kijiji cha Namatunu kwa kutumia fedha za Mfuko wa Jimbo ambapo mpaka sasa jumla ya hati 66 zimeandaliwa. Nitoe rai kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kutenga fedha katika bajeti zao ili wananchi wote wenye uhitaji katika Halmashauri zetu waweze kupata haki ya kumiliki ardhi zao ili kuinua pia vipato vyao.
MHE. HASSAN E. MASSALA aliuliza:-
Wilaya ya Nachingwea ina ardhi ya kutosha lakini vijana wengi bado wanakabiliwa na tatizo la ajira:-
Je, Serikali inatoa kauli gani kuwasaidia vijana hawa kujikwamua kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya Serikali katika kuwasaidia vijana wa Nachingwea kujikwamua kiuchumi ni pamoja na kufanya yafuatayo: Kuwashauri vijana wa Wilaya ya Nachingwea kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali na kubuni miradi mbalimbali ya uchumi katika nyanja za kilimo, ufugaji na viwanda vidogo vidogo vya usindikaji wa mazao ya kilimo. Hii itasaidia kutengeneza nafasi za ajira kwa vijana na kuwakwamua vijana katika lindi ya umaskini wa kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kwamba mpango huu unafanikiwa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira inaendelea kutekeleza mikakati ifuatayo:-
(a) Kuhakikisha Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea zinatenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za kiuchumi za vijana.
(b) Kusimamia utekelezaji wa utoaji wa mikopo kwa vijana ya 5% ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
(c) Kukopesha vikundi vya vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili kuchochea upatikanaji wa mitaji ya kuendeshea shughuli za kiuchumi za vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii adhimu kumwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa yeye ni kijana na amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya vijana kitaifa na kimataifa, basi tushirikiane kwa pamoja kuwaongoza vijana wa Wilaya ya Nachingwea katika kubuni miradi mbalimbali yenye tija ili kuwakwamua vijana wa Wilaya ya Nachingwea katika suala zima la ukosefu wa ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kauli ya Serikali ni kuendelea kuunga mkono jitihada zitakazofanywa na vijana wa Nachingwea na nchi nzima kwa kusaidia upatikanaji wa mitaji na mikopo kupitia Mifuko ya Uwezeshaji ya Serikali na pia kwa kuwashirikisha wadau wapenda maendeleo ya vijana kuwasaidia vijana kujiinua kiuchumi.
MHE. HASSAN E. MASALA Aliuliza:-
Barabara ya Nanganga – Nachingwea – Masasi imeshafanyiwa upembuzi yakinifu toka mwaka wa 2015/2016.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MWASILIANO
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ilikamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Nanganga. Aidha, katika mwaka wa 2017/2018 Wizara imeomba kutengewa shilingi bilioni 3.515 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hiyo.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Huko Nachingwea kulikuwa na viwanda viwili vya kukamua ufuta na korosho ambavyo vimebinafsishwa kwa muda mrefu lakini wawekezaji hawajaviendeleza hadi sasa hivyo kupunguza ajira na mzunguko wa fedha:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani juu ya wawekezaji waliopewa viwanda hivyo viwili?
(b) Kama wawekezaji hao wameshindwa kuendeleza viwanda hivyo, je, Serikali ina mpango gani na viwanda hivyo hasa ikizingatiwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeonesha nia ya kufufua viwanda nchini?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kuona kuwa viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinafanya kazi na kuchangia katika uchumi kupitia uongezaji thamani mazao ya kilimo, ajira na mapato ya Serikali. Katika kutekeleza azma hiyo, juhudi zimefanyika kuhamasisha wawekezaji ili kufufua viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo havifanyi kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Nachingwea, mafanikio yaliyopatikana kiwanda hicho kiliingia makubaliano ya awali (MoU) na Kampuni ya Sunshine Industry ya China mwezi Machi, 2017 ya kufufua kiwanda husika kwa utaratibu wa kujenga, kukimiliki, kuendesha na kuhamisha (Build Own Operate and Transfer). Usimikaji mitambo unaendelea na uzalishaji unatarajiwa kuanza mwezi Septemba 2017.
Mheshimiwa Spika, kiwanda cha kukamua ufuta au Kiwanda cha Mafuta ya Ilulu Nachingwea kilianza uzalishaji mwaka 1989 na mwaka mmoja baadaye kilisimamisha uzalishaji hadi kilipo binafsishwa kupitia ufilisi tarehe 14 Mei, 1997 kwa Kampuni ya Murzah Oil Mills iliyokuwa inamilikiwa na Marehemu Abbas Gulamali. Hati miliki ya Kiwanda alikabidhiwa mnunuzi mwaka 1999. Kufariki kwa Mheshimiwa Gulamali kuliathiri sana juhudi za kufufua kiwanda hicho.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo zoezi la ukarabati mitambo ili kuendelea na uzalishaji wa mafuta ya kula lilishindikana kutokana na uchakavu wa mitambo. Hivyo, mwaka 2009 familia ya marehemu Gulamali ilibadilisha shughuli ambapo kwa kushirikiana na Kampuni ya JAKAS Cashewnuts Factory ya Mtwara ilianza kubangua korosho hadi mwaka 2014 ubanguaji uliposimama kutokana na matatizo mbalimbali yakiwepo kujiondoa kwa Kampuni ya Olam kwenye shughuli za ubanguaji na biashara ya korosho kwa vile ndiyo ilikuwa ikigharamia shughuli za ubanguaji na kununua korosho zilizokuwa zikibanguliwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeipa Ofisi ya Msajili wa Hazina maelekezo ya kuchambua Mkataba wa Mauzo ya mali ya Kiwanda cha Mafuta ya Ilulu kwa Kampuni ya Murzah Oil Mills na kujadiliana na familia ya Marehemu Gulamali ili kukubaliana jinsi ya kuhakikisha mali za kiwanda hicho zinatumika kuchangia katika uchumi kupitia ajira na mapato ya Serikali. Ofisi ya Msajili wa Hazina inaendelea na jukumu hilo.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
• Je, Serikali kupitia REA III ina mpango gani wa kusambaza umeme katika kata zilizobaki Wilayani Nachingwea?
• Je, nini mpango wa Serikali kutatua tatizo la kukatikakatika kwa umeme Wilayani Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, nimshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa imani yake na nikushukuru wewe pia Mheshimiwa Spika kwa uongozi wako.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote visivyo na umeme vinapata umeme kupitia mradi kabambe wa kupeleka umeme vijijini Awamu ya Tatu (REA III) unaotegemewa kukamilika mwaka 2020/2021. Mradi huu utajumuisha vipengele vitatu vya Densification, Grid Extension na Off-Grid Renewables. Mkoa wa Lindi chini ya Mradi wa Uendelezaji wa Gridi mzunguko wa Kwanza unatekelezwa kwa muda wa miezi 24 na Kampuni ya State Grid & Technical Works Ltd. Katika Wilaya ya Nachingwea Mpango wa Awamu ya Tatu utavipatia umeme vijiji 30. Kazi za utekelezaji wa mradi zilianza mwezi Julai, 2017 na zitakamilika Juni 30, 2019. Aidha, vijiji vilivyobakia vitapatiwa umeme katika mzunguko wa pili wa REA III utakaoanza Aprili, 2019 hadi Disemba 2021.
Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme mzunguko wa kwanza itajumuisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 380, ufungaji wa transfoma 180, ujenzi wa njia za msongo wa kilovoti 0.4 zenye urefu wa kilometa 360 na uunganishaji wa wateja wapatao 5,710 katika Mkoa mzima wa Lindi. Aidha, kwa Wilaya ya Nachingwea jumla ya wateja wapatao 1,200 wataunganishwa. Mkandarasi anaendelea na upimaji wa njia za umeme ambapo amefikia asilimia 30 na kazi za upimaji zitakamilika mwishoni mwa Novemba, 2017. Gharama za miradi hiyo ni jumla ya shilingi 24,636,112,764.82 na dola za Kimarekani 5,657,471.30 pamoja na VAT.
(b) Mheshimiwa Spika, umeme unaotumika katika Wilaya ya Nachingwe unatoka katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia kilichopo Mtwara Mjini ambapo njia ya kusafirisha umeme kutoka Mtwara ina urefu wa kilometa 210 na pia hugawa umeme katika maeneo ya Mkoa wa Mtwara kabla ya kufika Nchingwea. Hivyo, pakitokea tatizo lolote mwanzoni au katikati ya njia basi, umeme hukatika katika maeneo mengi ya Mkoa wa Lindi, ikiwemo Nachingwea. Ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali kupitia TANESCO imejenga njia mpya ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Mtwara hadi Mnazi Mmoja, Lindi na kujenga kituo cha kupoza umeme chenye uwezo wa MVA 20, 132/33kV ambapo ujenzi wake umekamilika na mradi mzima umegharimu jumla ya shilingi bilioni 16.
Mheshimiwa Spika, umeme utapozwa katika msongo wa kilovoti 33 na kusafirishwa kwenda katika Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na badae Liwale. Ujenzi wa njia ya msongo wa kilovoti 33 ya Wilaya ya Ruangwa unategemewa kuanza Januari, 2018 baada ya kupatikana kwa fedha za utekelezaji. Pamoja na ujenzi huo, ukarabati wa miundombinu iliyopo unaendelea ili kuboresha mfumo mzima wa usambazaji katika Wilaya ya nachingwea na Lindi kwa ujumla.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Je, ni nini kauli ya Serikali katika kushughulikia tatizo la migogoro ya mipaka katika Kambi za JKT Nachingwea na Kikosi Namba 41 Majimaji na vijiji vinavyozunguka Kambi hizo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inatambua kuwepo kwa migogoro katika maeneo mbalimbali kati ya Kambi za Jeshi na vijiji jirani au maeneo yaliyotwaliwa na Jeshi kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya 41 KJ (Majimaji) ilipimwa mwaka 2005, wananchi waliokuwepo wakati wa upimaji idadi yao walikuwa 61. Katika Kambi ya 843 KJ ya JKT iliyopo Nachingwea mwaka 2009 Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea ilichukua jukumu la kuainisha mipaka kati ya Kambi hiyo na Kijiji cha Mkukwe. Wananchi waliokuwa ndani ya Kambi wakati wa kubaini mipaka hiyo walikuwa ni kaya tisa.
Mheshimiwa Spika, mwaka huu wa fedha 2018/2019 Wizara yangu imetenga bajeti kwa ajili ya uthamini na kulipa fidia kwa wananchi wanaostahili. Baada ya uthamini, wananchi wenye stahiki ya malipo watalipwa fidia zao kwa mujibu wa sheria na kanuni za fidia za ardhi zilizopo.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani juu ya wawekezaji walioshindwa kuendeleza Viwanda vya Kukamua Mafuta vya Ilulu na Kiwanda cha Mamlaka ya Korosho Wilayani Nachingwea?
NAIBU WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba Serikali inafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kuwa waliobinafsishiwa viwanda wanatimiza wajibu wao ipasavyo na kwamba viwanda hivyo vinafanya kazi kama ilivyokusudiwa kwa mujibu wa mkataba wao na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kiwanda cha Mafuta Ilulu, kiwanda hicho kiliuzwa kwa njia ya ufilisi. Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikimfuatilia mwekezaji ili kiwanda kilichonunuliwa kichangie katika uchumi wa Taifa letu. Kutokana na ufuatiliaji huo, tarehe 6 Juni, 2018, mmiliki wa Kiwanda cha Mafuta cha Ilulu, alitoa taarifa rasmi kurejesha kiwanda hicho cha Serikalini kwa kuwa ameshindwa kukiendeleza. Taratibu za kisheria zinafuatwa ili kukamilisha makabidhiano hayo rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Msajili itaendelea kuona matumizi bora zaidi ya kiwanda au eneo hilo. Aidha, kwa upande wa Kiwanda cha Korosho Nachingwea, kilibinafsishwa kwa kuuza hisa asilimia 100. Hivyo, uendeshaji wote wa kiwanda upo chini ya mwekezaji binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda kinaendelea na zoezi la kufunga mitambo ya kubangua korosho na sehemu ya maghala inatumika kuuzia na kuhifadhia korosho za wakulima na wanunuzi. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinakamilisha ufungaji mitambo na kuanza uzalishaji haraka ifikapo msimu ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilikuwa nimeahidi hapo awali, narudia kusema tena mara baada ya Bunge hili nitatembelea viwanda vyote vilivyobinafsishwa Mkoani Lindi na Mtwara pamoja na maeneo mengine kwa ajili ya ufuatiliaji na tathmini ya viwanda hivyo.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea – Ruangwa - Nanganga utaanza kufanyika kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Masasi – Nachingwea - Ruangwa hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 145 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS).

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii, Serikali iliamua kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwe lengo la kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami, kazi ambayo ilikamilika mwaka 2018. Hivi sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Serikali inatafuta fedha za ujenzi wa barabara hii, itaendelea kutengewa fedha za matengenezo mbalimbali ili iendelee kupitika wakati wote ambapo katika mwaka wa fedha 2018/2019 jumla ya shilingi milioni 547.4 zimetengwa kwa ajili ya kuifanyia matengenezo barabara hiyo.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-

Je, nini mpango wa Serikali juu ya kuboresha jengo la Mahakama Wilayani Nachingwea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama ya Tanzania haipo katika mpango wa maboresho ya majengo ya Mahakama nchini, ambapo pamoja na mambo mengine imekusudia kusogeza haduma ya Mahakama karibu na wananchi. Ili kufikia lengo hilo, Mahakama imeendelea kutatua changamoto kubwa ya uhaba na uchakavu wa majengo kwa kuendelea na kukarabati majengo nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mahakama ya Tanzania inafahamu tatizo la uchakavu wa majengo mengi ya Mahakama nchini, ikiwemo jengo la Mahakama ya Wilaya Nachingwea. Katika kukabiliana na changamoto hii, Mahakama imeweka kipaumbele katika kuboresha na kujenga majengo ya Mahakama nchini kulingana na mpango mkakati wa miaka mitano ambao umeendelea kutekelezwa kwa awamu kutegemea na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge wa Nachingwea kuwa kutokana na uhitaji mkubwa wa rasilimali na rasilimali chache zilizopo, katika mpango mkakati wa miaka mitano, Mahakama iliamua kujipanga upya na kuweka vipaumbele ili kuhakikisha tunaondokana na changamoto hii. Aidha, tayari tathmini ya jengo la Mahakama Nachingwea imeshafanyika. Kimsingi jengo hili linahitaji kujengwa upya na siyo kufanyiwa maboresho. Aidha, baada ya tathmini hiyo kufanyika ujenzi wa jengo hilo umewekwa kwenye mpango wetu wa ujenzi wa Mahakama wa mwaka 2020/2021kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-

Kambi za Jeshi 41KJ, 452 Medium ni miongoni mwa kambi kongwe na zenye mchango mkubwa katika Ulinzi wa Taifa letu. Kutokana na ukongwe huo, kambi hizo zimechakaa miundombinu yake mfano shule na zahanati zilizopo kwenye kambi hizo:-

(a) Je, nini mpango wa Serikali juu ya kuboresha miundombinu ya Zahanati zilizopo kwenye kambi hizi?

(b) Je, nini mpango wa Serikali wa kuboresha miundombinu ya shule hiyo iliyopo kwenye kambi hizo?

(c) Je, nini mpango wa Serikali juu ya kuboresha miundombinu ya Medium Workshop hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Jeshi 41KJ na 451KJ ni miongoni mwa kambi kongwe na zenye mchango mkubwa katika ulizi wa Taifa letu. Kutokana na ukongwe wa kambi hizo, umepelekea kuchakaa kwa miundombinu ya zahanati, shule na medium workshops zilizopo huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshwaji wa miundombinu ya hospitali kuu ya kanda iliyopo chini ya kambi ya Jeshi la 41 KJ, umekamilika likiwemo jengo kuu la hospitali, wodi za wagonjwa, chumba cha kuhifadhia maiti pamoja na vitanda vya malazi na kujifungulia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo ni upungufu wa wataalam pamoja na madawa, ambapo kwa hatua za awali Jeshi la Wananchi wa Tanzania tayari limeshawaandikisha madaktari 300 ambao wamepelekwa Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli na wanatarajiwa kutawanywa katika hospitali na vituo vya afya mbalimbali nchini, ikiwemo hospitali kuu ya kanda iliyopo 41KJ. Changamoto ya upungufu wa madawa itashughulikiwa kadri ya fedha zinatakavyopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, 451KJ, ina kituo kidogo cha afya ambacho hutoa huduma ya kwanza kwa Maafisa, Askari, pamoja na raia waliopo jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule inayozungumziwa hapa ni Shule ya Msingi ya Maji Maji iliyopo katika Kambi ya Jeshi 41KJ. Kwa nyakati tofauti Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya shule za msingi zikiwemo shule zilizopo katika maeneo ya Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaendelea kufanya mawasiliano na Wizara yenye dhamana ya kusimamia Shule za Msingi (TAMISEMI) ili ione uwezekano wa kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya Shule ya Msingi Maji Maji iliyopo katika Kambi ya Jeshi 41KJ Wilayani Nachingwea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za bajeti zimekuwa hazitosherezi katika kufufua karakara hiyo, hivyo Jeshi la Wananchi Tanzania limeweka mikakati ya kufufua miundombinu ya karakana ili iweze kujiendesha kibiashara kwa ajili ya kulihudumia Jeshi na Wananchi kwa ujumla. Aidha, mchakato wa kuipeleka karakana hiyo katika ngazi ya VETA unaendelea chini ya Makao Makuu ya Jeshi.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-

Je, ni lini Barabara ya Masasi – Nachingwea – Nanganga itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Masasi – Nachingwea – Nanganga yenye urefu wa kilometa 106 ni barabara ya mkoa na inasimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Wizara yangu kupitia TANROADS iliifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao ulikamilika mwaka 2018. Baada ya kukamilika kwa usanifu huo, Serikali sasa inatafuta fedha kwa ajili ya kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-

Kwa muda mrefu sasa soko la zao la mbaazi limekuwa likisuasua:-

Je, nini mpango wa Serikali katika kukwamua wakulima wa mbaazi nchini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara imeandaa na kutekeleza mikakati ya muda mfupi na muda mrefu ili kutatua changamoto ya masoko ya zao la mbaazi na mazao mengine ya jamii ya mikunde. Mkakati wa muda mfupi ni pamoja na kutafuta masoko mbadala nchi za nje ambapo mbaazi ghafi zitauzwa. Jitihada hizo zimeanza kuzaa matunda mwezi Machi, 2019 kufuatia ziara ya Serikali kutafuta masoko ya mazao ya kilimo ikiwemo mbaazi katika nchi jirani za Malawi, Burundi, Congo DRC na Zambia. Katika ziara hiyo, nchi ya Malawi kwa mwaka huu imeonyesha uhitaji wa tani 7000 na taratibu za kuhakikisha order hiyo inatekelezwa zinaendelea.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa muda mrefu ni kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya kukoboa na kuongeza thamani mbaazi na mazao mengine jamii ya mikunde nchini. Tayari Serikali imefanikiwa kushawishi wawekezaji kuja na kuwekeza katika viwanda vya kuchakata na kusindika mbaazi na mazao ya jamii ya mikunde. Kampuni ya Mahashree Agro Processing Ltd kutoka nchini India inajenga kiwanda Mkoani Morogoro ambapo hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu, yaani mwezi huu unaaonza kesho, tunategemea kwamba kiwanda hicho kitaweza kuanza kazi.

Mheshimiwa Spika, kiwanda hicho kitakuwa kimeanza kufanya kazi na kitakuwa na uwezo wa kuchakata na kusindika tani 700,000 kwa mwaka. Aidha, viwanda vya Quality Pulse Exporters Limited kilichopo Dar es Salaam - SEZ (Agro Pulse Processing) ambacho wawekezaji wake wanatoka India na Kenya kwa sasa kinafanya kazi. Vilevile kuna kiwanda cha Samson Agro Export Limited nacho pia kinafanya kazi na wawekezaji wake ni kutoka India.

Mheshimiwa Spika, katika kukuza soko la ndani, naendelea kutoa wito na kuwakumbusha Watanzania kutumia mbaazi na mazao mengine jamii ya mikunde ikiwa ni moja ya mazao ambayo yana virutubisho muhimu kwa afya ya binadamu.