Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hamidu Hassan Bobali (11 total)

MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Mkoa wa Lindi unapakana na Bahari ya Hindi na hivyo vijana wengi hujishuhulisha na shughuli za uvuvi ili kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga Chuo cha Uvuvi Mkoani Lindi ili kuwaongezea vijana hao ujuzi wa kazi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inatambua umuhimu wa kuwafundisha vijana mbinu sahihi za kufanya shughuli za uvuvi, kilimo na ufugaji. Hivi sasa Wizara kupitia Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (Fisheries Education and Training Agency – FETA) imeanzisha Chuo cha Uvuvi Mikindani, Mtwara kwa lengo la kusogeza huduma ya mafunzo ya uvuvi kwa wananchi wakiwemo vijana walioko Ukanda wa Kusini mwa Tanzania, ukiwemo Mkoa wa Lindi.
Ni mategemeo yetu kuwa mafunzo ya muda mfupi; wiki mbili hadi miezi mitatu yataanza kutolewa mwaka huu kwa kudahili wanafunzi 40 na yale ya muda mrefu ya stashahada yataanza mwaka 2017/2018. Ujenzi wa chuo hiki unaendelea ambapo hadi sasa madarasa mawili na karakana imekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) utaanza kutoa mafunzo ya uvuvi katika Chuo cha Mikindani, Mtwara muda mfupi mwaka 2016/2017 na yale ya astashahada na stashahada yataanza mwaka 2017/2018.
MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Wakulima wengi Mkoani Lindi wameamua kujikita katika zao la ufuta ambalo ndilo zao la biashara:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wakulima hao kupata pembejeo kupitia Mfuko wa Pembejeo.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Bobali Mbunge wa Mchinga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa zao la ufuta ambalo linalimwa kibiashara katika Mikoa ya Kusini yaani Lindi, Mtwara na Ruvuma na maeneo mengine tangu mwaka 1940. Mikoa hiyo huzalisha zaidi ya asilimia 75 ya ufuta wote unaozaishwa hapa nchini. Ufuta, hutumika kama chakula kwa binadamu, na vilevile hutumika kama chakula kwa mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la ufuta hustawi zaidi kwenye ardhi yenye rutuba ya asili na kwamba kiasi kidogo cha mbolea ya chumvichumvi, kinahitajika ndiyo maana wakulima hupendelea zaidi kulima kwenye ardhi mpya kwa kila msimu. Hata hivyo, ili kupata mavuno mengi, inahitaji kiasi kidogo cha mbolea za kupandia na kukuzia, na hivyo kulingana na hali ya udongo katika eneo husika kunahitajika mbolea .
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mpango wake wa ruzuku kwa wakulima inaangalia uwezekano wa kuongeza mazao mengine ikiwemo ufuta pale bajeti itakaporuhusu. Hata hivyo, kwa kuwa wakulima wa Mkoa wa Lindi wameamua kulima ufuta kama zao lao la bishara, Serikali inawashauri Wakulima wa Mkoa wa Lindi kupitia kwenye vikundi vyao vya ushirika kuomba mikopo kwenye Mfuko wa Taifa wa Pembejeo ili kuweza kujihakikishia upatikanaji wa pembejeo na kwa namna ya soko huria.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:-
Jimbo la Mchinga na Mtama linaunda Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na ukubwa wa Halmashauri hii ni kikwazo cha kuwafikia wananchi kwa urahisi katika kuwapelekea huduma za jamii.
Je, kwa nini Serikali isiigawe Halmashauri hii ili kuwa na Halmashauri mbili yaani Mchinga na Mtama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uanzishwaji wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa unazingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 145 na Ibara 146 na Sheria ya Serikali za Mitaa, Mamlaka ya Wilaya, Sura Namba 287 kifungu cha 5 ambazo kwa pamoja zinampa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kuwa na Madaraka ya kuanzisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kusudio la kugawanya Halmashauri ni lazima likidhi vigezo vinavyowekwa kwa kuzingatia taratibu zilizopo ikiwa ni pamoja na kujadiliwa kwenye vikao vya kisheria, ikiwemo Mkutano Mkuu wa Vijiji, Kamati za Maendeleo za Kata, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC), Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) na baadae huwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais – TAMISEMI inatambua kuwa suala la kugawa Wilaya ya Lindi liko katika majadiliano kupitia vikao vya Halmashauri; hatua hizo zitakapokamilika Serikali itatuma wataalam kwa ajili ya kuhakiki vigezo vinavozingatiwa kabla ya kugawa Halmashauri husika.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:-
Mkoa wa Lindi umekuwa na shule chache za Kidato cha Tano na cha Sita, matokeo yake vijana wanaofaulu Kidato cha Nne kuingia Kidato cha Tano hupangiwa shule za mbali:-
Je, ni kwa nini Serikali isifanye utaratibu wa kufanya Shule ya Sekondari Mchinga kuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi Kidato cha Kwanza hadi cha Sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uhitaji mkubwa wa Shule za Sekondari Kidato cha Tano na Sita katika Wilaya ya Lindi, tayari Halmashauri ya Wilaya ya Lindi imependekeza Shule ya Sekondari ya Mchinga kuwa ya Kidato cha Tano na Sita. Hata hivyo shule hiyo ina upungufu ukosefu wa mabweni, matundu ya vyoo, jiko na bwalo la chakula. Halmashauri imeelekezwa kuweka vipaumbele na kutenga bajeti kwa ajili ya kurekebisha upungufu wa miundombinu ili shule hiyo iweze kupata sifa ya kusajiliwa na kuwa ya Kidato cha Tano na Sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya upungufu huo kurekebishwa na kukamilika, Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, itatuma wataalam kwa ajili ya kukagua vigezo vilivyozingatiwa ili shule iweze kupandishwa hadhi kuwa ya Kidato cha Tano na Sita na endapo itaridhika itatoa kibali. Aidha, Shule za Sekondari za Kidato cha Tano na Sita ni za Kitaifa na kwa mantiki hiyo, zinapokea wanafunzi waliohitimu na kufaulu Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne kutoka nchi nzima.
MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Gereza la Kingulungundwa lililopo Wilayani Lindi linakabiliwa na uhaba mkubwa wa Nyumba za Askari na miundombinu mibovu:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha makazi ya Askari katika Gereza hilo?
(b) Gereza hili lipo umbali wa kilometa tatu kutoka barabara kuu inayotoka Dar es Salaam kwenda Lindi, lakini wakati wa masika, barabara hiyo haipitiki kwa gari kutokana na kujaa tope na maji. Je, Serikali haioni kuwa kukosekana kwa mawasiliano ya barabara kutoka Gerezani ni jambo la hatari?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafahamu kuwa lipo tatizo la uchakavu na upungufu wa nyumba za Askari wa Jeshi la Magereza nchini na hali hiyo inatokana na baadhi ya nyumba kujengwa kabla ya uhuru ama katika maeneo mengine ambapo zilijengwa kwa matumizi ya muda wakati ikisubiri ujenzi wa nyumba za kudumu na za kisasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya nyumba za Askari Magereza hivi sasa ni nyumba 14,500 wakati zilizopo ni nyumba 4,221, hivyo kuwepo kwa upungufu wa nyumba 10,279 ambao unasababisha baadhi ya Askari kuishi nje ya Kambi. Kwa sasa Serikali ina mpango wa kuwajengea Askari Magereza nyumba 9,500 na mara baada ya mpango huo kukamilika tunategemea kumaliza kero za makazi ya Askari Magereza nchini likiwemo Gereza alilolitaja Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imeendelea na mpango wa kuzifanyia ukarabati mkubwa baadhi ya nyumba kwenye baadhi ya Magereza na kujenga nyumba mpya. Ni nia ya dhati ya Serikali kuendelea kuboresha nyumba za Askari nchini zikiwemo za Gereza la Kingulungundwa kwa awamu. Kwa sasa, Jeshi la Magereza linajenga nyumba 320 za Maafisa na Askari hapo Ukonga na fedha ambayo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshatoa ni shilingi bilioni 10 na shilingi bilioni tano tayari zilishatolewa kwa ajili ya ujenzi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba barabara inayotoka barabara kuu ya Dar es Salaam kuelekea Gereza la Kingurungundwa imekuwa haipitiki kwa gari wakati wa masika. Kimsingi barabara hiyo ipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Lindi vijijini na ndiyo yenye jukumu la kuifanyia matengenezo barabara hiyo kwa kuwa haiishii Gerezani tu, bali inaendelea kwenye vijiji vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza limeshafanya mawasiliano na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Vijini ili barabara hiyo iweze kutengenezwa na kuepusha adha inayojitokeza wakati wa masika.
MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Sekta ya uvuvi bado haijatumika kikamilifu kulipatia Taifa pato na kuwaondoa Watanzania hususani wavuvi katika dimbwi la umaskini.
(a) Je, ni lini Serikali itaweka jitihada za kusaidia wavuvi hasa wale wanaojihusisha na uvuvi wa Bahari Kuu?
(b) Je, ni lini Serikali itatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wavuvi wadogo wadogo ili waweze kuvua katika Bahari Kuu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya Uvuvi nchini kwa kutekeleza mikakati yenye lengo la kuendeleza wavuvi nchini ili waweze kupata ajira, lishe, kipato na kuchangia katika Pato la Taifa. Kwa mwaka 2016 sekta ya Uvuvi imechangia asilimia 2.0 katika Pato la Taifa na imekua kwa asilimia 4.2.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jitihada za kuwasaidia wavuvi wadogo hususani wale wanaojihusisha na uvuvi wa Bahari Kuu Serikali imeanza kuweka vifaa maalum vya kuvutia samaki (Fish Aggregating Devices - FADs) ili kuwasaidia wavuvi kupata samaki wengi na kutumia muda mfupi katika uvuvi. Hadi sasa jumla ya FADs 77 za mfano zimewekwa katika maeneo mbalimbali. Vilevile Serikali imetoa mafunzo kwa wavuvi wadogo ili waweze kuvua katika Bahari Kuu ambapo hadi sasa jumla ya wavuvi 150 wakiwemo 83 wa Ukanda wa Pwani ya Bahari wa Hindi.
• Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo inatoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wakulima wakiwemo wavuvi na wafugaji ili waweze kununua zana bora za uvuvi. Aidha, Serikali imeanzisha Dirisha la Kilimo katika Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB). Mikopo hiyo inatolewa kupitia vyama vya ushirika ambayo pamoja na majukumu mengine inatoa pia mikopo ya masharti nafuu kwa watu wanaojishughulisha na sekta za kilimo, mifugo na uvuvi. Ili kuweza kukidhi masharti ya kupata mikopo hiyo, Serikali inaendelea kuwahamasisha wavuvi kujiunga katika Vyama vya Ushirika vya Msingi wa Wavuvi ili kuwa na nguvu ya pamoja na kuweza kukopesheka.
MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Kumekuwa na Maswali yaliyokosa majibu stahiki kila mara kuhusu suala la mabaki ya mjusi (Dinosaur) yaliyopo Ujerumani, kila linapoulizwa au kuchangiwa hapa Bungeni:-
(a) Je, ni nini kauli ya mwisho ya Serikali kuhusu faida ambayo wananchi wa Mkoa wa Lindi na Tanzania kwa ujumla watanufaika kutokana na mabaki hayo?
(b) Je, kwa nini Serikali isishauriane na Serikali ya Ujerumani kuboresha barabara na huduma za maji katika Kijiji cha Manyangara katika Kitongoji cha Namapwiya, ambapo mabaki ya mjusi huyo yalichukuliwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maswali kuhusu mijusi mikubwa (Dinosaria) iliyochimbuliwa katika Kilima cha Tendaguru, Mkoani Lindi, nchini Tanzania kati ya mwaka 1909 hadi mwaka 1913 na kupelekwa katika Makumbusho ya Elimu Viumbe ya Berlin, nchini Ujerumani, yamejibiwa kwa miaka mingi na wakati tofauti Bungeni ambapo Serikali imekuwa ikitoa ufafanuzi uliokidhi haja katika mazingira yaliyokuwepo wakati maswali hayo yanajibiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika siku za hivi karibuni Wizara yangu imefuatilia suala hili kwa umakini mkubwa kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kujiridhisha kama ifuatavyo:-
(a) Wazo la kuwarudisha dinosaria nchini halina tija kutokana na changamoto za kiteknolojia na gharama, ikilinganishwa na faida za kuchukua hatua hiyo.
(b) Tanzania iendelee kusisitiza kupata manufaa kutokana na uwepo wa dinosaria wake huko Berlin, Ujerumani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia majadiliano bya kina yaliyohusisha pia wataalam waliobobea katika masuala ya malikale kutoka pande zote mbili, imekubalika kama ifuatavyo:-
i. Serikali ya Ujerumani itendesha shughuli za utafiti zaidi huko Tendaguru na katika maeneo jirani, ili kuwezesha uchimbuaji wa mabaki ya dinosaurian wengine yanayoaminika kuwepo katika maeneo hayo.
ii. Serikali ya Ujerumani itawezesha kuanzishwa kwa kituo cha makumbusho, ili shughuli za utalii zifanyike katika eneo hilo na kuvutia watalii kutoka nchini na nje ya nchi.
iii. Serikali ya Ujerumani itafadhili zoezi la uimarishaji idara inayohusika na malikale katika Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam na kuwezesha upatikanaji wa watalaam wa kutosha wa fani husika, ili kuendeleza utalii wa malikale nchini. Hivyo, uboreshaji wa barabara na miradi ya maji anaouzungumzia Mheshimiwa Mbunge utakuwa sehemu ya mafanikio ya shughuli za utalii katika eneo linalozungumziwa.
MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Je, Serikali imefanya tathmini juu ya ubora na changamoto zilizopo katika shule za sekondari za kata nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la kitafiti la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 ni kipindi ambacho tafiti, tathmini, mikakati na mipango mingi katika sekta ya elimu, ikiwemo Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP) inayotekelezwa kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi (MMEM) kuanzia mwaka 2000 na Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES) kuanzia mwaka 2004 ilianzishwa.
Mipango hiyo ndiyo chimbuko la maamuzi ya kuanzisha Shule ya Sekondari kila Kata ili kuhakikisha watoto wengi zaidi waliokuwa wanakosa nafasi za masomo ya sekondari, licha ya kufaulu mitihani ya darasa la saba kwa sababu tu ya uchache wa shule wanapata nafasi hizo. Hadi mwezi Oktoba, 2017 tulikuwa na shule za sekondari za kata 3,103 zilizokuwa na wanafunzi 197,663 ambapo kama zisingekuwepo wangeikosa elimu ya sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini mbili za Serikali zilizochambua kwa kina sekta ya elimu kupitia Tume ya Profesa Mchome ya mwaka 2013 iliyochambua sababu za ufaulu hafifu wa wanafunzi kwenye mitihani ya mwaka 2012 ya kidato cha nne na Kamati kuhuisha na kuoanisha Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo mwaka 1996, Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu ya mwaka 1999 na Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Elimu ya Msingi mwaka 2007 iliyoongozwa na Mwalimu Abubakar Rajab mwaka 2013, ndizo zilizobaini na kuishauri Serikali kuanzisha sera mpya moja ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014.
Mheshimiwa Naibu Spika, sera mpya imetoa maelekezo mahususi kuhusu namna ya kuboresha elimu ya awali, elimu ya msingi, elimu ya sekondari, elimu ya ufundi na elimu ya juu. Mitaala imesharekebishwa, ikama, vifaa, samani na miundombinu vyote hivi vinaendelea kuboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa shule mpya, ujenzi wa madarasa, vyoo, maabara, mabweni, maktaba, nyumba za walimu, ofisi ya walimu, mabwalo na majengo ya utawala unaoendelea nchi nzima kwa kushirikiana na wananchi; kuboresha upatikanaji wa vitabu vya kiada na ziada katika shule za sekondari pamoja na juhudi za Serikali kuhakikisha walimu wa kutosha wanapatikana hasa wa masomo ya sayansi na hisabati, ni uthibitisho wa namna Serikali ilivyo na dhamira ya kuinua ubora wa elimu.
MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Wakati wa kampeni za Urais mwaka 2015 Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alifika Kijijini Nangaru katika Jimbo la Mchinga na kuahidi kupandisha hadhi Barabara ya Mtange – Chikonji – Nangaru kutoka hadhi ya Halmashauri kuwa barabara ya Mkoa:-
a) Je, ni lini barabara hiyo itapandishwa hadhi?
b) Je, ni kwa nini Serikali huchukua muda mrefu kutekeleza ahadi mbalimbali zilizotolewa na Mheshimiwa Rais wakati wa Uchaguzi Mkuu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mwasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka kuwa, mwezi Julai, 2017, Serikali ilianzisha rasmi Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza mtandao wa barabara za Wilaya. TARURA imeanzishwa kwa Sheria ya Wakala wa Serikali (The Executive Agency Act), Sura 245 kupitia Gazeti la Serikali, GN No. 211, la tereha 12 Mei, 2017. Lengo la uanzishwaji wa wakala huu ni kuhakikisha kuwa barabara za Wilaya zinapata msukumo wa usimamizi wa kutosha kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali imesitisha zoezi la upandishaji hadhi wa barabara za Wilaya kuwa za Mkoa kwa vile kuna Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ulioanzishwa mahsusi na kupewa jukumu la kusimamia na kuendeleza barabara za Wilaya nchini. Ni matumaini yangu kuwa mtaipa ushirikiano TARURA, ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kukidhi matarajio ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utekelezaji wa ahadi ya Viongozi Wakuu, ahadi hizi zinajulikana na zitaendelea kutekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:-
Kumekuwa na raia wengi kutoka Msumbiji katika Jimbo la Mchinga hasa Vijiji vya Kilangala B, Butamba, Mvuleni, Kitolambwani na Kikonde ambao wamekuwa wakishiriki uchaguzi katika nchi zote mbili Tanzania na Msumbiji.
(a) Je, raia hao ni Watanzania au wa Msumbiji?
(b) Je, Serikali imepitisha utaratibu wa uraia pacha na kuwapa watu maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa Tanzania. Aidha, Ibara ya 5(2) ya Katiba hairuhusu mtu mwenye uraia wa nchi nyingine (raia pacha) kushiriki katika shughuli za uchaguzi ikiwemo kupiga kura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ili mtu aweze kupiga kura lazima awe ameandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura lililoanzishwa chini ya ibara ya 5(3)(a) ya Katiba. Uandikishaji wa wapiga kura unapokamilika, daftari la awali huwekwa wazi kwa mujibu wa kifungu cha 24 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 ili kukaguliwa na wananchi. Kifungu cha 24(1) cha sheria hiyo kinatoa fursa kwa mtu aliyejiandikisha kuweka pingamizi dhidi ya mtu mwingine aliyendikishwa kwenye daftari ikiwa imebainika kuwa hana sifa ya kuandikishwa kwa kutokuwa raia wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hii, sheria zetu hazijaruhusu uraia pacha na hakuna watu maalum waliopewa uraia wa aina hiyo.
MHE. KIZA H. MAYEYE (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:-

Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni cha muda mrefu na pia kimetumika kuandaa viongozi wa nchi yetu na nchi jirani:-

(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kukipandisha hadhi Chuo hicho kuwa Chuo Kikuu?

(b) Je, kwa nini Serikali haipeleki fedha za maendelo katika Chuo hicho kama zilivyopangwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA - K.n.y. WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali Mbunge wa Mchinga, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni Taasisi ya Elimu ya juu iliyoanzishwa na Sheria Na.6 ya mwaka 2005. Chuo kinatekeleza majukumu yake makuu kuendesha mafunzo ya Kitaaluma katika fani ya Sayansi ya Jamii katika ngazi za Cheti, Stashahada, Shahada ya Kwanza na umahiri. Aidha, Chuo kinaendesha mafunzo ya Uongozi, Maadili na Utawala Bora, Mafunzo ya Elimu ya kujiendeleza, kinafanya tafiti na kinatoa ushauri kwa umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Serikali kwa sasa si kupandisha hadhi Vyuo vilivyopo, bali ni kuboresha mazingira ya Vyuo Vikuu vilivyopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu, kwa kuwa na vifaa vya kisasa na kuwa na Wahadhiri wengi zaidi wenye Shahada ya Uzamivu. Hatua hizo zitawezesha kuongeza nafasi za Udahili na kuimarisha ubora wa elimu itolewayo. Jitihada zinazofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ni pamoja na zifuatazo:-

(i) Kupata wataalam zaidi katika fani zenye uhaba ambapo Chuo kimepeleka wataalam 33 kwenda kusoma Shahada za Uzamivu; na

(ii) kuongeza miundombinu ya Chuo kama vile ujenzi wa vyumba vya madarasa na kumbi za mihadhara ambapo, ujenzi wa ukumbi wenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 330 kwa wakati mmoja umekamilika na kuzinduliwa tarehe Mosi Aprili, 2019.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikipeleka fedha za maendeleo katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kadri fedha hizo zinavyopatikana, mfano mwaka 2017/2018, Serikali ilitoa fedha zote zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maendeleo kiasi cha shilingi Bilioni 1 nukta 89 ambazo zilitumika kukamilisha ujenzi wa hosteli ya wanafunzi, ahsante.