Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Vedasto Edgar Ngombale Mwiru (16 total)

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini siyo kweli kwamba katika Wilaya ya Kilwa kuna wakulima wanaingilia maeneo ya wafugaji na kama hivyo ndivyo, Mheshimiwa Waziri anao uwezo wa kunitajia vijiji vitano ambavyo kuna migogoro ya wakulima kuingilia maeneo ya wafugaji, hiyo ni moja.
Mbili, kwa kuwa, mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Kijiji cha Ngea haukutenga eneo kwa ajili ya wafugaji na kwa kuwa, Mkutano Mkuu wa Kijiji cha Ngea, ulishaamua wafugaji waondoke na kupata baraka za uongozi wa Wilaya. Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kuona athari ambazo wakulima wamezipata lakini athari za hifadhi za misitu pamoja na Bwawa la Maliwe?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kusema kwamba hizi ni taarifa ambazo tumezipata, nikuhakikishie ndugu yangu Ngombale mimi niko tayari kwanza kufika Kilwa. Katika sehemu yako na pili naomba nikuhakikishie kwamba, nitafika Kilwa, siyo kwa ajenda hii tu ya wakulima na wafugaji peke yake hapana! Kuna mambo mengi ya kimsingi ya kuweza kuyafuatilia kule Kilwa ambapo ofisi yangu ina kila jukumu la kufanya hivyo ili wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Spika, lakini suala zima la vijiji nikutaarifu kwamba, katika miaka ya nyuma kulikuwa na Mkuu mmoja wa Wilaya pale alikuwa anaitwa Nurdin Babu, katika hiki Kijiji cha Ngea ulichokizungumza japokuwa mwanzo wafugaji walikataliwa lakini baadaye Mkuu wa Wilaya alipokwenda kufuatilia baadhi ya wananchi walisema hapana, tunahitaji wafugaji waendelee kuwepo.
Kwa hiyo, kwanza kuna changamoto kidogo katika maeneo yetu, lakini kubwa zaidi haya yanatokea ni nini mara nyingi sana wakati mwingine hata hawa Viongozi wetu wa Vijiji inakuwa ni tatizo, mwanzo wafugaji walikataliwa walipoingia pale, lakini baada ya kukaa muda fulani tayari sasa kukawa na mgogoro mpaka Mkuu wa Wilaya pale aliingia site na wananchi wamesema bwana sisi hapa hatuna matatizo kwa sababu wafugaji wamechimba kisima hapa, sisi tunaishi vizuri, Mkuu wa Wilaya nenda, leo hii suala hili limekuja! Hata hivyo, nimesema ngoja niyachukue haya kwa sababu lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanaishi katika hali ya usalama. Hii migogoro mwisho wa siku inahatarisha maisha ya wananchi wetu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, hivyo nayafanyia kazi ndugu yangu, wala usipate hofu.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa vita ya Majimaji au harakati za awali za kudai uhuru wa Tanganyika zilitokana na chokochoko na misingi imara ya kukataa kuonewa na kudai uhuru kulikofanywa na majemedari wetu wakati wa vita vya Majimaji. Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga barabara hii ili kuwawezesha Watanzania kwenda katika eneo hilo wakajifunze namna gani nchi yetu ilivyojengwa katika misingi ya kudai haki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa kuwa barabara hii haipitiki kabisa Serikali ina mpango gani wa kuweka lami katika sehemu korofi kwa mfano mlima Ndundu, Mlima Ngoge pale Chumo, Mlima Kinywanyu na Mlima Karapina pale Kipatimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba umuhimu wa barabara hii na Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba sehemu hii ndiyo chemichemi za harakati ya ukombozi wa nchi yetu. Naomba nikiri kwamba, kuna maeneo mengi sana ya kijiografia ambayo wakati wa uhuru kama Tanzania tulipokuwa tunaenda katika mchakato walishiriki kwa kiwango kikubwa sana katika kufanikisha uhuru wa nchi yetu, nawapongeza sana ndugu zetu wa Kilwa katika hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakiri wazi kwamba kwa sababu umuhimu wa barabara hii kama nilivyosema awali katika jibu langu, tukirejea tena marejeo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi, lengo lake kubwa ni kuhakikisha wananchi wanafikiwa wa maeneo mbalimbali. Mheshimiwa Ngombale tutafanya juhudi siyo hapo Kilwa tu, isipokuwa maeneo mbalimbali. Ndiyo maana Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilikuwa ikifanya mikakati katika maeneo mbalimbali, tulianza hasa katika miji tumeenda katika halmashauri, lengo letu ni kwamba maeneo mbalimbali yaweze kufikika chini ya miradi yetu ambayo sasa hivi tuna mradi wa TSP Project ambayo inahusisha ujenzi wa miundombinu ya barabara za lami katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili litakuwa katika mpango wetu, mkakati mpana wa kuhakikisha Halmashauri nyingi zinafikiwa na haya ni mambo ambayo tunayafikiria, ndiyo maana hata ukiangalia bajeti yetu ya mwaka huu tuna bajeti takribani ya bilioni 43 kwa ajili ya kuondoa vikwazo, lakini bilioni zaidi ya 200 kwa ajili ya kuhakikisha Halmashauri ziweze kufikiwa vizuri. Kwa hiyo, ni mambo ambayo Serikali yetu inayaangalia na ndani ya miaka mitano tuna imani tutafanya mambo makubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lile la kuhusu sasa vile vipande korofi ikiwezekana viwekewe lami na najua Halmashauri ya Kilwa jinsi gani jiografia yake ilivyo na wakati mwingine malori yanashindwa kupanda. Tutawaelekeza wenzetu wa TANROAD ambao tunashirikiana nao kwa karibu zaidi na barabara takribani kilomita 48 zinahudumiwa na TANROAD, tutahakikisha Serikali inayapa kipaumbele yale maeneo korofi ambayo mvua ikinyesha barabara hazipitiki kwa kuyafikiria kwa jicho la karibu zaidi.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Katika jibu lake la msingi Mheshimiwa Waziri anasema kwamba, ndiyo kwanza wameanza ukarabati wa mitambo ile, nilifanya ziara mwezi wa Saba na nikakutana na Meneja na akanieleza kwamba, ukarabati umefanyika, lakini bado kuna tatizo kila inapofika saa tano ya usiku mashine zile hujizima na baada ya saa nane ndiyo huweza kuwaka tena. Nahitaji kufahamu ukweli ni upi, maelezo ya Mheshimiwa Waziri au yale aliyonipa Meneja wa kile kituo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; bado kuna tatizo kubwa na hasa la kiufundi. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri anieleze kwamba, mkandarasi aliyetumika kufanya ukarabati ule ni yule aliyeelekezwa na mtengenezaji wa mashine au hawa wenzetu wa Magomeni? Mheshimiwa Naibu Waziri kama yuko tayari kufuatana nami kwenda kuangalia namna ya kutafuta suluhu ya tatizo lile? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nitoe ufafanuzi mzuri wa matatizo ya umeme kule Kusini. Ukweli ni kwamba, umeme Mikoa ya Lindi na Mtwara una matatizo na matatizo ni ya kiufundi. Ilikuwa ni kampuni ya ARTMUS iliyopewa jukumu la kusambaza umeme huko, ilijenga miundombinu ya msongo mdogo wa kilovoti 33; ukizitoa Mtwara ziende mpaka Masasi, Nachingwea, ukweli ni kwamba umeme unakuwa na matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kinachofanyika sasa hivi ambacho Mheshimiwa Naibu Waziri ameongea ni kweli kwamba, TANESCO inarekebisha hizo njia, zitajengwa sasa badala ya kilovoti 33 ni kilovoti 132 double circuit (njia mbili) za kuleta umeme mwingi zaidi. Kwa hiyo, hiyo kazi nadhani itakamilika mwisho wa mwaka huu, lakini nimemtuma mtu aende Mtwara kwa sababu, Mbunge wa Mtwara aliniuliza, nimemtuma Engineer aende alete jibu kabla ya Jumatano wiki ijayo. Kwa hiyo, jibu kamili mtalipata kama mradi unaendelea vizuri, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili kutatua hili tatizo, kama anavyosema Mheshimiwa, Somanga Fungu, lazima tukiri mitambo ya Somanga Fungu ina matatizo. Siyo Somanga Fungu tu ni kitu ambacho lazima tuwe wakweli tukifanyie kazi, kwa nini mitambo yetu inavyoanza kazi, ikifika miaka miwili tu inakuwa na hitilafu! Hicho kitu ni lazima tukifanyie kazi ni cha kitaalam; Somanga Fungu ilifungwa baada ya miaka miwili ikaleta matatizo. Ule wa Nyakato Mwanza umefungwa baada ya miaka miwili una matatizo! Mtambo wa Ubungo baada ya miaka miwili una matatizo, hivi ni vitu ambavyo lazima tuviongee kwa uwazi kuliko kuvificha, kuna tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Somanga Fungu ukweli ni kwamba, yule na nadhani Mbunge yuko makini sana alikuwa anauliza swali la kututega sisi; ukweli ni kwamba, aliyetengeneza ile mitambo na anayefanya repair sasa hivi ni watu tofauti, huo ukweli lazima tuukubali. Sasa tunachofanya ni kwamba, ukweli wamefanya rapair ya Somanga Fungu hatuna sababu ya kufunga safari kwenda kule kuthibitisha kwa sababu kazi yenyewe haijakamilika. Kwa hiyo, hakuna kujiridhisha, tunajua kazi haijakamilika, kwa hiyo tungoje ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la Somanga Fungu kulitatua na Mikoa ya Kusini ni kuingizwa kwenye gridi ya Taifa. Kwa hiyo, fedha zimepatikana na TANESCO wameanza kujenga miundombinu ya msongo mkubwa kutoka Somanga Fungu, kuunganisha na Kinyerezi, tunataka iwe ya kilovoti 400, walikuwa 200 nikasema hapana, tumezowea tunafanya vitu kidogo baada ya muda tena matatizo! Kwa hiyo, watapeleka kilovoti 400 kusudi ule umeme wa Somanga Fungu na wa Mtwara ukiingia Somanga Fungu unaweza kwenda Kinyerezi na nyie mkipata matatizo mnaweza mkapata umeme kutoka kwenye gridi ya Taifa.
Waheshimiwa Wabunge, hili tatizo linatatuliwa tulieni tu, halitachukua muda mrefu. (Makofi)
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri, lakini pia kukishukuru Kiti chako kwa sababu swali hili nililileta kwa mara ya kwanza halikupata majibu muafaka ya Serikali. Kwa majibu haya kidogo napata faraja kwamba ndugu zangu wale wa Kilwa watakwenda kupata fidia kutoka Serikali ya Ujerumani chini ya usimamizi wa Serikali ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri pia Serikali katika suala hili kwamba wenzetu wa Kenya waliendesha mchakato wa kudai fidia za waathirika wa Vita ya Maumau na Serikali ya Uingereza ikatoa fidia kwa waathirika wale. Kwa hiyo, nishauri Serikali nayo ikajifunze kutoka Kenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa kuwa historia ya Vita ya Majimaji imechanganywachanganywa na kuvurugwa; na kwa kuwa Taifa hili limedanganywa eti kwamba Kinjekitile Ngwale ndiyo kiongozi wa Vita ya Majimaji. Ukweli ni kwamba Kinjekitile Ngwale siyo kiongozi wa Vita ya Majimaji na kiongozi wa Vita ya Majimaji ni Sikwako Mbonde na majemedari wake Ngumbalio Mandai, Lindimio Machela, Ngumbe-kumbe Mwiru na wengine. Serikali iko tayari sasa kufanya utafiti wa kihistoria ili basi kuwaeleza Watanzania ukweli wa jambo hili? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa misingi hiyo ya kuchanganya historia ya Vita ya Majimaji, sherehe za kumbukumbu za Mashujaa wa Vita ya Majimaji kila mwaka zinafanywa Majimaji Songea badala ya kufanywa Nandete Kipatimu. Serikali iko tayari kuhamisha sherehe zile kutoka Majimaji Songea kwenda Nandete Kipatimu ambako ndiko chanzo cha Vita ya Majimaji?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nikubaliane naye kuhusu ushauri anaoutoa kwamba Tanzania ikajifunze kutoka Kenya kwa sababu Wakenya waliweza kudai fidia ya Vita vya Maumau na waliweza kupata fidia hiyo, tunakubaliana naye na tutafanya hivyo ili tuweze kujua wenzetu wanafanyaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili la kufanya utafiti wa kihistoria ili kupata ukweli wa vita hii na uongozi wake na kadhalika nao ni ushauri mzuri, tunaupokea tutafanya kazi hiyo. Sasa ni hapo baada ya kupata ukweli huo, ndiyo hilo swali lake la tatu litaweza kupata jibu muafaka. Kwa sababu siwezi kulijibu sasa mpaka pale historia itakapopatikana na ukweli ukajulikana ndipo tutaweza kulizungumza hilo swali lake la tatu.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri katika jibu lake la msingi amesema kwamba vijiji vya Mkarango na Nandete katika kata ya Kipatimu na vijiji vya Kata ya Kinjumbi na Kibata vitapata mawasiliano katika mradi utakaokamilika ifikapo Novemba, 2017; sasa tunazungumza ni mwezi Mei. Nataka nijue tu, je, programu ya utekelezaji wa miradi hiyo umeshaanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kumekuwa na utaratibu kwa kampuni moja kujenga minara ya simu, baadae makampuni mengine kuja kufunga mitambo yao ya mawasiliano. Nataka nijue katika kata ya Chumo pana kampuni imejenga mnara wa simu na kuna kampuni moja tu ya Vodacom ndiyo imefunga mitambo yake ya mawasiliano.
Je, ni lini makampuni ya Airtel na Tigo yatakuja kufunga mitambo yao ya mawasiliano, ili kutanua wigo wa mawasiliano kwa wananchi wa kata ya Chumo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kutokana na jibu la msingi kwamba ifikapo Novemba mwaka 2017, mwaka huu tulionao kwamba, miradi ambayo inaendelea itakuwa imekamilika. Kwa msingi wa jibu hilo ni kwamba, programu hii inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la pili, amesema kwamba, kuna Kampuni ya Viettel imetajwa, lakini kuna Kampuni ya Vodacom, kuna Kampuni za Tigo, umeona kampuni moja ipo pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala moja dogo
Mheshimiwa Mbunge, ni suala la fizikia nyepesi tu kwamba hii minara inafanya kazi kwa kutegemea mawimbi na mawimbi ya Vodacom, mawimbi ya Airtel, minara ya Airtel, mawimbi ya Viettel ni mawimbi yanayotegemeana, kwa hiyo, kukishakuwa na Mnara mmoja wa Vodacom
unarahisisha pia Mnara wa Viettel kuja kujengwa pale. Kwa hiyo, ukishatangulia mnara mmoja, basi tarajia kabisa kwamba, na minara mingine na makampuni mengine yatakuja kuwekeza kwa sababu kumeshakuwa na urahisi wa kuwepo mawimbi katika lile eneo.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa
Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa chanzo cha umeme pale Somanga Fungu kinashindwa kufanya kazi vizuri na kupelekea matatizo makubwa ya umeme kwa Wilaya ya Kilwa na Rufiji kwa sababu ya mitambo ile kuchelewa kufanyiwa ukarabati na kwa kuwa sasa tatizo hilo linaendea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itatuunganisha watu wa Kusini na Gridi ya Taifa kwasababu sasa umeme imeshafika pale Kilwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge Ngombale kwamba mitambo ya Somanga Fungu inatarajia kufanyiwa ukarabati hivi karibuni na kampuni ya RENCO ya Italy. Na Serikali kupitia TANESCO wameshasaini mkataba na ukarabati huo utakamilika Desemba, 2018 ambapo mitambo itakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 7.5 na matumizi ya Kilwa ni megawati tatu. Kwa hiyo naomba nimtaharifu kwamba hilo linafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza ni lini…
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejikita kwenye kutoa misaada midogomidogo kwa wavuvi kama vile engine na nyuzi za kushonea nyavu za wavuvi. Je, Serikali iko tayari kuwakopesha wavuvi wa Kilwa zana za kisasa kama vile boti kwa ajili ya vikundi hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, Serikali au majibu ya Waziri yameshindwa kuthibitisha kama yamewasaidia wavuvi wa Kilwa kupata zana hizo za kisasa na inawezekana kabisa wavuvi wa Kilwa hawana taarifa yoyote kuhusiana na utaratibu huu. Sasa Serikali au Waziri anaweza kunithibitishia kwamba katika hizo mashine zilizobaki wavuvi wa Kilwa wanakopeshwa mashine hizo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ipo tayari kuwawezesha wavuvi wa Kilwa? Ndiyo, Serikali ipo tayari kuwawezesha wavuvi wa Kilwa kupitia vikundi vyao. Tena na hapa naomba nimuelekeze tu kwamba vikundi hivyo vinaweza vikatumika hata vile vya BMU (Beach Management Unit) na mashine hizi bado zipo, tunawakaribisha Waheshimiwa Wabunge wote ambao watahitaji mashine hizi wafuate utaratibu kupitia kwa Maafisa Uvuvi wetu ambapo watapeleka kwa Mkurugenzi na baadae maombi yale yatafika Wizarani katika Idara yetu ya Mafunzo na Elimu ya FETA kwa ajili ya kuweza kuwapatia wavuvi wetu ili waweze kufanya uvuvi wenye tija.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi. Kilwa ni miongoni mwa eneo ambalo mifugo inakuja kwa wingi na Serikali haijaandaa kabisa miundombinu. Serikali ina mpango gani kutujengea malambo Kilwa ile mifugo iliyopo pale iweze kupata afya inayostahili? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaanza na kisima kimoja mwaka huu ujao wa fedha kwa Mheshimiwa Mbunge.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nimeyasikia na naomba anisikilize kwa makini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba eneo hilo la Tarafa ya Kipatimu lina zaidi ya wakazi 60,000, hatuna kituo cha Polisi, jitihada hizo zimefanywa na wananchi, nikiwemo na Mbunge, nimetoa mifuko 100 ya saruji ku-support na wananchi tayari wamefyatua matofali, tunayo matofali, lakini shida kubwa tunayopata ni ushirikiano kutoka kwa ofisi yake ya Mkoa ambayo mpaka sasa tumehitaji kupata ramani imekuwa shida, tumehitaji kupata mchanganuo imekuwa shida. Je, sasa Mheshimiwa Waziri yuko tayari kunipatia ramani na mchanganuo wa ujenzi ule ili ujenzi uweze kuendelea kwa sababu wananchi wana ari kubwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza kwa mchango wake katika kufanikisha ujenzi wa kituo hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ramani na ushirikiano mwingine nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba atapata. Naomba tu baada ya maswali tukutane ili niweze kumpa utaratibu huo namna gani ambavyo anaweza akapata ushirikiano huo, naamini kabisa inawezekana tu tatizo ni mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida Vyombo vyetu vya Dola, kwa maana ya Jeshi la Polisi, vimekuwa vikipenda sana kufanya kazi karibu na wadau mbalimbali ikiwemo Wabunge na wamekuwa wakitoa ushirikiano wa haraka. Kwa hiyo, nadhani kama kulikuwa na changamoto ya mawasiliano, basi baada ya maswali nitakuwa tayari kumsaidia kufanikisha hilo kwa haraka. (Makofi)
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa iliingia mkataba na wenzetu wa DDCA kwa ajili ya kuchimba visima virefu toka mwaka 2017, lakini mpaka sasa mradi huu haujatekelezwa. Ni lini DDCA watatekeleza mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, lakini kubwa nampongeza Mheshimiwa Mbunge, Wizara yetu ya Maji jukumu letu ni kuhakikisha wananchi wanapata maji. Sisi Wizara ya Maji siyo Wizara ya ukame nawaagiza ndugu zangu wa DCAA kuhakikisha miradi hiyo wanachimba kwa haraka ili wananchi wako wapate maji safi salama na yenye kutosheleza.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuwapongeza community redio ya Mashujaa FM kwa kufanya coverage kwa niaba ya TBC.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Serikali ilitenga hiyo bajeti ya kujenga mtambo Nangurukuru, mwaka 2017/2018 na hii 2018/2019 imerudia kuwa inaendelea kutenga bajeti bila ya utekelezaji. Sasa nini commitment ya Serikali katika bajeti ya mwaka huu kwa sababu inaonekana kana kwamba Serikali haina nia thabiti ya kujenga mtambo huo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa TBC ndio chombo cha Taifa na kina jukumu la kutoa mawasiliano kwa wananchi, kutokana na kusua sua kwake Mheshimiwa Waziri haoni kwamba wanawakosesha haki wananchi wa Kilwa kupata habari? Lakini pia…
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ameonesha wasiwasi kwamba TBC inasuasua katika utekelezaji wa usikivu hususan katika Wilaya yake ya Kilwa. Kwanza napenda kutumia nafasi hii kumtoa hofu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kwanza, wote tunafahamu kwamba katika bajeti ya fedha ya mwaka WA 2017/2018 Serikali ilitenga shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kuboresha usikivu wa TBC na fedha hiyo ilishatolewa yote. Katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga bajeti ya shilingi bilioni tano. Kwa hiyo tuna imani kabisa fedha hiyo itatolewa yote kwa sababu imekuwa ni mpango wa Serikali na tumeona kabisa Serikali ina commitment na ndiyo maana katika fedha zote ambazo zinatengwa zimeendelea kutolewa kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, kwamba TBC kusuasua kwake kunawakosesha haki wananchi, nimtoe hofu kama ambavyo tumejibu katika jibu letu la msingi, kwamba katika mwaka huu wa fedha wa 2018/2019 Serikali kupita shirika lake la TBC imejipanga kujenga mnara mpya wa kurushia matangazo yake katika eneo la Nangurukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaamini kabisa na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mimi kama Naibu Waziri pamoja na Waziri wangu tutawasimamia katika mwaka huu wa fedha kuhakikisha kwamba mtambo huo unajengwa, ili basi wananchi wa Kilwa waweze kupata haki yao ya kuweza kupata habari, ahsante.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mheshimiwa Ngombale na siyo Mheshimiwa Katani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali mwaka huu ilijielekeza kwamba sisi wa zao la ufuta tutatumia Stakabadhi Ghalani…
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mheshimiwa Vedasto Ngombale sio Mheshimiwa Katani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Katani hayupo kwa leo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru baada kuwa sasa umetambua jina langu vizuri. Ninachosema ni kwamba Serikali ilielekeza mwaka huu katika zao la ufuta utaratibu wa manunuzi utafanyika katika Mfumo wa Stakabadhi Ghalani na kwamba mikoa yote inayolima ufuta itatakiwa kuingia katika mfumo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa ninavyozungumza ufuta umeshakuwa tayari na kuna baadhi ya mikoa tayari wameshaanza kuuza katika mfumo holela na Serikali iko kimya haijasema chochote. Naomba kufahamu, je, tutaingia katika mfumo wa Stakabadhi Ghalani au tutaendelea katika utaratibu ule ambao tulikuwa tumeufanya mwaka jana? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni kweli kwamba, ufuta ni moja ya zao ambalo Serikali ilidhani na inatarajia kuliweka kwenye Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, lakini ili uingie kwenye huo mfumo yako maandalizi ya msingi ambayo lazima yafanyike vinginevyo mfumo hautafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachofanya sasa hivi tunakamilisha hayo maandalizi, tutakuwa na mkutano wa wakuu wa mikoa yote inayolima ufuta ili tujiridhishe kwamba maandalizi hayo yako in place tuweze kuanzisha mfumo wenyewe.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Vipo vijiji vingine. Ukiacha Mtepera na Zinga, kuna Vijiji vya Miguruo na Ngarambi, navyo vinapakana na Pori la Akiba la Selous. Ni lini zoezi hili litafanyika katika vijiji hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, uhamishaji umefanyika, wananchi wana uelewa wa mipaka yao kwa kutumia alama zile za asili kama milima na mabonde. Kwa mfano, katika Kijiji cha Zinga pale pana mlima mkubwa unaitwa Nandanga, sasa Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana nami ili kwenda kurekebisha mipaka ile kwa kuzingatia alama zile za asili kama milima na mabonde?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Vijiji vya Miguruo na Ngarambi, zoezi hili tutalifanya wakati tukipitia upya. Zoezi la kwanza lilikuwa ni kuweka alama kulingana na GN inavyosoma, lakini kuna maeneo mengi ambayo tuligundua yana migogoro. Kinachofuata sasa ni kupitia upya kuangalia ni maeneo gani ambayo migogoro ina faida kwetu au kwa wanakijiji na tutaangalia namna ambavyo tunaweza tukaisuluhisha. Kwa hiyo, tutakapoanza zoezi hili ambalo tunakwenda kulifanya, tutapita katika vijiji hivi viwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili; ni kweli kwamba alama nyingi ambazo zimetumika kama mipaka ya vijiji zilikuwa ni alama za asili; miti mikubwa, labda mto fulani, alama ambazo zimekuwa zikitoweka. Kwa hiyo, tumepata taabu katika kuelewa mipaka ya vijiji na pia mipaka ya mapori haya ya akiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Ngombale kwamba nitakuwa tayari kuambatana naye ili kwenda kuona hizi sehemu zenye mgogoro.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti,swali la kwanza, jokofu hilo la Hospitali ya Kinyonga halifanyi kazkwa sasa na Hospitali hii ya Kinyonga ipo sambamba kuelekea Mikoa ya Kusini. Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga jengo hilo kwa haraka sambamba na kuleta jokofu lenye uwezo la kuhifadhi zaidi ya mwili mmoja ili kuendana na chochote kinachoweza kutokea ili kukidhi haja hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali inampango gani kukarabati Kituo cha Afya Njinjo ambacho hali yake kwa sasa ni mbaya sana? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ngombale Vedasto,kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, leo asubuhi kabla sijaingia hapa Bungeni nimefanya utaratibu wa kuwasiliana na Halmashauri na nina taarifa njema, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge leo tarehe 2 Mei, halmashauri inaingia mkataba na mdau wa Pan Africaambao wamekubali kujenga jengo la kisasa kwa ajili ya chumba cha kuhifadhia maiti, lakini kwa makubaliano kwamba na halmashauri nao watatununua jokofu la kisasa ili liweze kumudu hali ya uhitaji wa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anaomba ukarabati waKituo cha Afya cha Njinjo, naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunafanya ukarabati katika vituo vyote vya afya vile vile vilivyojengwa zamani, ili viwe na mwonekano wa sasa. Naye atakiri kwamba, katika nafasi aliyopata kutembelea vituo vya afya ambavyo tunavijenga sasa hivi tumevijenga vizuri, hali kadhalika hata hospitali za wilaya za zamani tungependa zikarabatiwe ziwe na muonekano wa kisasa kama kwa Hospitali ya Kilwa ya mwaka 1965, kwa vyovyote vile hata hali yake hailingani na hadhi ya hospitali ya Wilaya.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mradi wa Mingumbi – Miteja ambao umekamilika, Kijiji cha Njia Nne ambacho kimepitiwa na mradi huo hakikupata maji: Je, Serikali sasa iko tayari kusambaza maji kwa Kijiji hiki cha Njia Nne ili kuondokana na tatizo la maji ambalo liko pale?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; mwaka 2017, Wakala wa Serikali (DDCA) ilifanya mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kuchimba visima virefu 21, lakini mpaka sasa wamechimba visima vitatu tu katika vijiji 18. Sasa je, DDCA iko tayari kuchimba visima virefu hivyo, au nini sababu zilizowafanya DDCA wasichimbe visima virefu katika Vijiji vya Nampunga, Chumo, Mtondo wa Kimwaga, Nandembo, Kibata, Kinjumbi, Somanga na Marendego?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anafahamu nia ya Serikali yetu. Zaidi ya shilingi bilioni 4,668 ziliwekezwa pale katika kuhakikisha tunatekeleza Mradi wa Maji wa Mingumbi na Miteja katika jitihada za kutatua tatizo la maji. Nataka nimhakikishie kwamba nia ya Wizara yetu ni kuhakikisha Watanzania wanapata maji safi na salama. Tutafanya extension ili wa Kijiji kile cha Njia Nne nao waweze kupata maji safi na salama katika kuhakikisha tunamtua mwana mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la uchimbaji wa visima, tulitenga kiasi cha shilingi milioni 456 katika kuhakikisha zaidi ya vijiji 19, ikiwa Kilwa Kusini na Kilwa Kaskazini vinapata huduma ya maji. Tuliwapa kazi hiyo DDCA, wamefanya kazi, lakini kulikuwa kuna ucheleweshaji mkubwa. Sisi kama viongozi wa Wizara tumeshamwondoa Mkurugenzi yule wa DDCA maana yake kulikuwa na ucheleweshaji. Yote hii ni kuweka mtendaji ambaye ataendana na kasi ya kuhakikisha tunatatua tatizo la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Ngombale, sisi kama Wizara ya Maji tutahakikisha kwamba visima vilivyobaki vinachimbwa kwa wakati na wananchi wake waweze kupata maji safi na salama.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Serikali ina mpango gani wa kutenga pesa kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa barabara ya kutoka Njia Nne - Kipatimu (km 50)? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la rafiki yangu Mheshimiwa Ngombale ,kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza mara nyingi juu ya barabara hii. Niombe tu tuwasiliane ili tuone kwa sababu kwenye Mipango Mikakati yetu katika Wizara tumeiweka katika Mpango ili tuweze kuendelea na hatua ya ujenzi wa lami. Kwa hiyo, tuonane na Mheshimiwa Mbunge ili nimpe taarifa za kukutosha ili aweze kutoa maelezo mengi kwa wananchi wake. Ahsante.