Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Vedasto Edgar Ngombale Mwiru (15 total)

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-
Serikali katika awamu zote imekuwa ikiweka kipaumbele katika sekta ya Kilimo na Mifugo kwa umuhimu wake kwa maendeleo ya wananchi katika nchi yetu, lakini Wilaya ya Kilwa kama ilivyo katika maeneo mengine ya nchi yetu, imekuwa na migogoro inayotishia amani kati ya wakulima na wafugaji katika baadhi ya Vijiji vikiwemo vya Ngea, Kinjumbi, Somanga, Njianne, Namandungutungu na Matandu, kutokana na wafugaji kupitisha, kulisha, kunywesha na kuharibu mazingira katika mashamba ya wakulima na Hifadhi ya Misitu ya Vijiji kama Msitu wa Likonde, Mitarute na Bwawa la Maliwe katika Kijiji cha Ngea, ambacho hakipo katika mpango wa kupokea wafugaji:-
Je, Serikali inatoa wito gani kwa wafugaji wanaoruhusu mifugo yao kuwatia hasara na njaa wakulima na kuharibu mazingira ya baadhi, ili kuepusha uvunjifu wa amani ambao unaweza kutokea wakati wowote kuanzia sasa?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Wilaya ya Kilwa imekuwepo migogoro ya wafugaji na wakulima, hususan katika Vijiji vya Ngea, Kinjumbi, Somanga, Njianne na Namandungutungu. Ufuatiliaji umebaini kuwa sababu kubwa ya migogoro hii ni baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima na baadhi ya wakulima kuingia katika maeneo ya wafugaji. Hivyo, migogoro hiyo inatokea panapokuwepo mwingiliano baina ya makundi haya ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa vijiji 14 vya Wilaya ya Kilwa ambao uliainisha maeneo kwa ajili ya kilimo, ufugaji, biashara, makazi na uwekezaji. Licha ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kuandaliwa bado kumekuwa na tabia ya kutofuata sheria ya Ardhi Na. 13 na Na. 14 zote za mwaka 1999 na hivyo kusababisha mwingiliano usio wa lazima.
Mheshimiwa Spika, kutokana na tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji kuwa kubwa, ninawaagiza Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya, wote kuhakikisha kwamba suala hili linakuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa na utatuzi wake ufanyike kwa njia shirikishi. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa wale wote wanaokiuka Sheria, vikiwemo vitendo vya rushwa, hali ambayo imesababisha migogoro hii kuendelea kuwepo.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-
Moja ya matukio makubwa ya kihistoria katika nchi yetu ni vita ya Majimaji iliyopiganwa kati ya mwaka 1905 – 1907 kati ya Watanganyika na Wajerumani. Pamoja na kufahamu kwamba vita hivyo vilienea katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, lakini vilianza katika Kijiji cha Nandete, Wilaya ya Kilwa; Serikali inaonesha jitihada mbalimbali ya kuienzi historia hiyo, ikiwa ni pamoja na kujenga mnara katika Kijiji hicho:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza barabara ya kutoka Njianne hadi Nandete kwa kiwango cha lami ili kulifanya eneo hilo la kihistoria kufikiwa kwa urahisi na kuliongezea umaarufu kwa kutembelewa na watalii hususani wa kutoka Ujerumani jambo ambalo litaiongezea mapato Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa na Taifa kwa ujumla.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa kujenga barabara ya lami kwenda eneo hili la kihistoria ni la msingi, lakini kwa sasa wakati Serikali inajenga barabara kuu zote nchini kwa kiwango cha lami hasa zikiunganisha Makao Makuu ya Mikoa yote. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikitenga bajeti ya fedha kwa ajili ya matengenezo ili kuifanya ipitike wakati wote.
Kupitia Wakala wa barabara Mkoa wa Lindi, katika mwaka wa fedha 2015/2016, zilitengwa shilingi milioni 58.8 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kilomita 43 na matengenezo ya muda maalum kwa kiwango cha changarawe urefu wa kilomita sita, kwa jumla ya gharama ya shilingi milioni 192.3. Matengenezo ya barabara hii yameanza chini ya Mkandarasi Ungando Contractors Company wa Kibiti – Rufiji. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, barabara hii iko katika mpango wa kufanyiwa matengenezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kilomita 10 zinazohudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, katika mwaka 2015/2016, zimetengwa shilingi milioni 70 ambazo zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum kwa urefu wa kilomita nane. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, zimetengwa shilingi milioni 967.6 ambazo zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara katika Wilaya ya Kilwa.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano inakusudia kuifanya Tanzania kuwa ni nchi yenye uchumi wa viwanda, hivyo inahitaji kuwa na uzalishaji wa umeme wa uhakika. Hata hivyo, umeme unaozalishwa kwa kutumia gesi asilia pale Somanga Fungu unakatika mara kwa mara na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji:-
Je, Serikali inaweza kutuambia wananchi kiini hasa cha ukatikaji huo wa kila siku wa umeme unaozalishwa kutokana na gesi ya Songosongo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Somanga Fungu kilianza kuzalisha umeme mwaka 2010. Kituo hicho kina jumla ya mitambo mitatu ya kuzalisha umeme kiasi cha Megawati 7.5 kwa kutumia gesi asilia. Umeme unaofuliwa kutoka Somanga Fungu unatumika katika Wilaya za Kibiti, Kilwa pamoja na Rufiji. Kwa sasa mtambo mmoja wenye uwezo wa kuzalisha umeme Megawati 2.5 pia haufanyi kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukatika kwa umeme ni kweli kabisa kumekuwa na kukatika kwa umeme katika Wilaya za Kilwa, Kibiti pamoja na Rufiji kunakosababishwa na hitilafu katika mitambo ya kuzalisha umeme pamoja na miundombinu ya kusambaza umeme. Ili kukabiliana na changamoto hiyo tunaimarisha upatikanaji wa umeme katika wilaya hizo na Serikali kupitia TANESCO imeanza ukarabati sasa, ambao ni overhaul kabisa wa mitambo miwili ya uwezo wa kuzalisha umeme wa jumla ya megawati tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunafanya ukarabati na kufunga mtambo mwingine kwenye mtambo unaozalisha megawati mbili na kufanya sasa jumla ya gharama za marekebisho pamoja na kufunga mtambo kufikia bilioni tano. TANESCO inaendelea na ukaguzi, inafanya usafishaji na ukarabati wa mitambo hiyo ili kuwahakikisha wananchi wa maeneo hayo wanapata umeme wa uhakika.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:-
Napongeza jitihada za Serikali kwa kuanzisha mradi wa maji katika kijiji cha Mingumbi ambao utakapokamilika wananchi katika vijiji vya Mingumbi, Kilelima, Naipuli, Njia Nne, Tingi, Mtandago na Miteja kuondokana na tatizo la maji. Hata hivyo, tatizo la maji bado ni kero kubwa katika maeneo mengi ya Jimbo la Kilwa Kaskazini na Wilaya ya Kilwa kwa ujumla.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mradi mkubwa wa maji kutoka katika Mto Rufiji ambao upo jirani na Wilaya ya Kilwa kwa madhumuni ya kumaliza kabisa kero sugu ya maji inayowakabili wananchi wa Wilaya ya Kilwa.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ambapo ujenzi wa miradi umekamilika katika vijiji sita vya Kandawale, Mtandi, Ngea, Njinjo, Nanjilinji na Hanga. Ujenzi katika vijiji vya Mtandango na Mingumbi unaendelea na upo katika hatua mbali mbali, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga kiasi cha shilingi 785,924,000 kwa ajili ya kufanya utafiti, wa vyanzo vingine vya maji katika vijiji vya Lihimaliao, na Nainokwe ambavyo hapo awali vilikosa vyanzo, pamoja na kukamilisha miradi inayoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa muda mrefu, wa kumaliza kabisa kero ya maji, inayowakabili wananchi waishio maeneo yanayozungukwa na Mto Rufiji, ikiwemo Wilaya ya Kilwa. Serikali kupitia Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo wa Sekta ya Maji ambao umeanza mwezi Januari, 2016 itaangalia uwezekano wa kufanya utafiti wa mradi wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji kupeleka maeneo yote yanayozungukwa na mto huo, vikiwemo vijiji vya Wilaya ya Kilwa Kaskazini. (
MHE. HAMIDU H. BOBALI (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:-
Tanzania ni moja ya nchi duniani zilizoathirika kutokana na Tawala za Kikoloni na Vita vya Majimaji ni moja ya vielelezo vya athari hizo ambapo vita hivyo vilianza Wilayani Kilwa katika Kijiji cha Nandete mwaka 1905 - 1907:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha waathirika wa Vita vya Majimaji wanapata fidia kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Kijerumani?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, harakati za kupambana kivita dhidi ya ukoloni zilifanywa na Makabila mbalimbali hapa nchini ikiwemo Vita vya Majimaji na nyingine nyingi. Vita hivi vilifanywa na Watemi wa baadhi ya makabila wakiwemo; Mtemi Mirambo wa Tabora, Mtemi Mkwawa wa Iringa na Chifu Abushiri Bin Salim wa Uzigua, Tanga. Aidha, madhila ya ukoloni kwa wananchi ni mengi yakiwa ni pamoja na utumwa, ubaguzi wa rangi, ukandamizwaji na kuuawa kwa tamaduni zetu za asili. Pia, uporwaji wa mali zetu na ardhi bora za kilimo pamoja na mazuio ya kuendeleza vipaji vya teknolojia kama vile uundaji wa silaha. Haya ni baadhi tu ya madhila ya ukoloni. Makusudi ya vita vya watawala wetu wa jadi ilikuwa kupinga ukoloni na kutaka kujitawala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa harakati hizo za kivita za viongozi wa kijadi kwa pamoja zililenga kuwakomboa wananchi kutoka kwenye makucha ya ukoloni na kuleta uhuru kwa wananchi, siyo vyema kutoa madai ya fidia kwa jukumu hili la kizalendo lililotekelezwa na makabila mengi nchini mwetu. Badala yake madhila na athari ya Vita vya Majimaji yabaki kama sehemu muhimu ya kumbukumbu za ukombozi wa nchi yetu.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-

Tanzania ni moja ya nchi duniani zilizoathirika kutokana na Tawala za Kikoloni na Vita ya Majimaji ni moja ya vielelezo vya athari hizo ambapo vita hiyo vilianzia Wilayani Kilwa katika Kijiji cha Nandete mwaka 1905-1907:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha waathirika wa Vita vya Majimaji wanapata fidia kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Kijerumani?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, harakati za kupambana kivita dhidi ya ukoloni zilifanywa na makabila mbalimbali hapa nchini ikiwemo Vita vya Majimaji na nyingine nyingi. Vita hivyo vilifanywa na Watemi wa baadhi ya makabila wakiwemo Mtemi Mirambo wa Tabora, Mtemi Mkwawa wa Iringa na Chifu Abushir Bin Salim wa Uzigua Tanga. Aidha, madhila ya ukoloni kwa wananchi ni mengi yakiwa ni pamoja na utumwa, ubaguzi wa rangi, ukandamizwaji, uporwaji wa mali zetu na ardhi bora za kilimo pamoja na kuuawa kwa tamaduni zetu za asili. Haya ni baadhi tu ya madhila ya ukoloni. Maksudi ya vita za watawala wetu wa jadi ilikuwa kupinga ukoloni na kutaka kujitawala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ihakikishe kwamba Wajerumani wanawalipa fidia waathirika ni wazo zuri. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara yangu itaiandikia rasmi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili waangalie utaratibu bora wa kufikisha kwa wahusika madai haya.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-
Maeneo mengi ya Jimbo la Kilwa Kaskazini bado hayajapata huduma ya mawasiliano ya simu kama vile kata za Kibata, Kinyumbi, Kandawale na vijiji vya Nandete na Mkarango.
Je, ni lini Serikali itapeleka huduma hii katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya kata za Kibata, Kinyumbi, pamoja na vijiji vya Nandete na Mkarango kutoka katika kata ya Kipatimu, Jimbo la Kilwa Kaskazini vitafikishiwa huduma ya mawasiliano ya Kampuni ya Simu ya Viettel kupitia utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi unaotegemewa kukamilika ifikapo Novemba, 2017. Aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, itaainisha vijiji vya kata ya Mandawale na kuviingiza katika orodha ya miradi kwa ajili ya zabuni za siku za usoni kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ZUBERI M.KUCHAUKA (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuitangaza Wilaya ya Kilwa kuwa ni moja ya maeneo makubwa ya Kiutalii katika Kanda ya Kusini kwa kuzingatia historia yake, maajabu mbalimbali yaliyopo, fukwe, mapango, malikale, mbuga, mabwawa na utamaduni wake?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edger Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na hoja ya Mheshimiwa Mbunge kuwa Wilaya ya Kilwa ni miongoni mwa maeneo yenye fursa za uendelezaji utalii wa kihistoria na kiutamaduni yakiwemo magofu ya malikale yaliyopo eneo la Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ambayo ni maeneo yaliyopo kwenye orodha ya urithi wa dunia pamoja na vivutio vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuitangaza Wilaya ya Kilwa kuwa eneo muhimu la kiutalii Ukanda wa Kusini, Wizara imeandaa jarida la Karibu Kilwa (Kilwa District Heritage Resources); vipeperushi kama Welcome to Kilwa in Tanzania; ambavyo vinaonyesha picha na maelezo ya vivutio vya utalii vilivyopo Wilayani Kilwa na kuanzisha Kituo cha Taarifa za Kiutalii (Tourist Information Centre).
Mheshimiwa Naibu Spika, Jarida na vipeperushi hivi vinatolewa kwa wageni wanaotembelea Kilwa pamoja na kutumika kutangaza utalii wa Kilwa katika maonesho ya ndani, hususan maonyesho ya Saba Saba; Nane Nane na Maonyesho ya nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara kupitia Bodi ya Utalii na kwa kushirikiana na taasisi ya nchini Ufaransa imeweza kuandaa filamu maalumu ambayo inaitangaza Kilwa. Filamu hiyo ilizinduliwa rasmi mwaka 2016 na imetafsiriwa kwa lugha tatu za Kimataifa ambazo ni Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa. Filamu hiyo inapatikana kupitia mtandao, kwenye tovuti ya Bodi ya Utalii na kwenye wavuti ya YouTube.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-
Sekta ya Uvuvi ni moja ya maeneo ambayo Serikali ya Awamu ya Tano inayaona kuwa yanaweza kukuza uchumi kwa kuongeza Pato la Taifa, kupunguza umaskini na tatizo la ajira.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha wavuvi wadogo wadogo Wilayani Kilwa kwa kuwapatia zana za kisasa za uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuwawezesha wavuvi wadogowadogo wakiwemo wa Wilaya ya Kilwa kupata zana za uvuvi kwa bei nafuu ili kufanya uvuvi endelevu na wenye tija. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuondoa kodi kwa zana na malighafi za uvuvi zikiwemo engine za kupachika, nyuzi za kushonea, nyavu na vifungashio kupitia Sheria ya VAT ya mwaka 2007.
Vilevile kupitia Chapisho la Pamoja la kodi la Afrika Mashariki engine za uvuvi na malighafi zinazotumika kutengeneza zana mbalimbali za uvuvi na viambata vyake zimepewa punguzo la kodi ili kuwawezesha wavuvi kumudu bei za vifaa hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Programu ya Kutoa Ruzuku kwa Wavuvi, Serikali katika Awamu ya Kwanza ilinunua engine 73 na hadi sasa engine 49 zimelipiwa na kuchukuliwa na vikundi vya wavuvi vilivyokidhi vigezo vikiwemo vikundi 27 kutoka Ukanda wa Pwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia nafasi hii kuomba Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kuhamasisha wavuvi kujiunga kwenye Vyama vya Ushirika vya Msingi ili waweze kunufaika na fursa hii kama wavuvi wengine katika ukanda huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imeanzisha Benki ya Kilimo ambayo pamoja na masuala mengine inaweza kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa wavuvi ili kuboresha shughuli zao za kimaendeleo. Kutokana na kuwepo kwa benki hii na taasisi nyingine za kifedha, Serikali inaendelea kuhamasisha wavuvi kote nchini kujiunga katika Vyama vya Ushirika wa Wavuvi ili waweze kukopesheka na kuweza kununua zana za kisasa za uvuvi.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuitangaza Wilaya ya Kilwa kuwa ni moja ya maeneo makubwa ya Kiutalii katika Kanda ya Kusini kwa kuzingatia historia yake, maajabu mbalimbali yaliyopo, fukwe, mapango, malikale, mbuga, mabwawa na utamaduni wake?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edger Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na hoja ya Mheshimiwa Mbunge kuwa Wilaya ya Kilwa ni miongoni mwa maeneo yenye fursa za uendelezaji utalii wa kihistoria na kiutamaduni yakiwemo magofu ya malikale yaliyopo eneo la Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ambayo ni maeneo yaliyopo kwenye orodha ya urithi wa dunia pamoja na vivutio vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuitangaza Wilaya ya Kilwa kuwa eneo muhimu la kiutalii Ukanda wa Kusini, Wizara imeandaa jarida la Karibu Kilwa (Kilwa District Heritage Resources); vipeperushi kama Welcome to Kilwa in Tanzania; ambavyo vinaonyesha picha na maelezo ya vivutio vya utalii vilivyopo Wilayani Kilwa na kuanzisha Kituo cha Taarifa za Kiutalii (Tourist Information Centre).
Mheshimiwa Naibu Spika, Jarida na vipeperushi hivi vinatolewa kwa wageni wanaotembelea Kilwa pamoja na kutumika kutangaza utalii wa Kilwa katika maonesho ya
ndani, hususan maonyesho ya Saba Saba; Nane Nane na Maonyesho ya nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara kupitia Bodi ya Utalii na kwa kushirikiana na taasisi ya nchini Ufaransa imeweza kuandaa filamu maalumu ambayo inaitangaza Kilwa. Filamu hiyo ilizinduliwa rasmi mwaka 2016 na imetafsiriwa kwa lugha tatu za Kimataifa ambazo ni Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa. Filamu hiyo inapatikana kupitia mtandao, kwenye tovuti ya Bodi ya Utalii na kwenye wavuti ya YouTube.

MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-
Moja ya majukumu makubwa ya Serikali ni kulinda raia na mali zao kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama ikiwemo Polisi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukirejesha Kituo cha Polisi katika Tarafa ya Kipatimu Wilayani Kilwa ambacho kilihamishwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Kituo cha Polisi cha Kipatimu kilifungwa mwaka 1998 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa miundombinu na mahusiano mabaya kati ya raia na Askari kiasi cha kutishia usalama wa Askari na mali za Serikali zilizoko kituoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa wananchi wameona umuhimu wa kurejesha huduma za Polisi katika eneo husika ambapo wameanza ujenzi wa kituo kipya cha Polisi. Aidha, nimshauri Mheshimiwa Mbunge kuwasiliana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi ili kuona namna bora ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho.
MHE. VEDASTO EDGA NGOMBALE (KILWA KASKAZINI)
aliuliza:-
Kupata habari ni moja ya haki za Kiraia, TBC ni chombo pekee cha habari kwa sasa kinachowafikia wananchi wengi hususan wale wanaoishi vijijini lakini kwa muda mrefu sasa chombo hicho hakisikiki vizuri katika maeneo mengi ya vijijini vya Jimbo la Kilwa Kaskazini na Wilaya ya Kilwa kwa ujumla.
Je, ni tatizo gani linalosababisha chombo hiki kisisikike vizuri katika maeneo mengi ya vijijini?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edga Ngombale, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza kuchukua hatua mahsusi za kuboresha usikivu wa Redio katika Mikoa ya Lindi pamoja na Mtwara, ikiwemo Wilaya ya Kilwa kama ifuatavyo:-
(a) Mitambo ya kurushia matangazo iliyoko Nachingwea ya TBC Taifa imeongezewa nguvu kutoka watt 250 hadi watt 1,000 na ile ya TBC FM toka watt 150 hadi watt 1,000. Matokeo yake ni usikivu bora wa redio maeneo mengi ya Nachingwea, Ruangwa na sehemu za Wilaya ya Masasi.
(b) Mitambo miwili ya kurushia matangazo ya TBC Taifa na TBC FM imejengwa Mtwara, kila mmoja una ukubwa wa watt 1,000 na kuwezesha matangazo ya redio kuwafikia wananchi Mtwara Vijijini, Tandahimba pamoja na Lindi Vijijini.
(c) Hatua ya tatu ni ndani ya mwaka wa fedha 2018/2019 tuna mradi wa kujenga Mtambo mpya wa FM wa kurusha matangazo eneo la Nangurukuru ambao utaimarisha usikivu wa redio maeneo ya milima yaliyobaki.
MHE. VEDASTO E. NGAMBALE aliuliza:-

Hifadhi ya Akiba ya Selous imekuwa ikihamisha alama za mipaka na kuchukua eneo la ardhi ya vijiji katika Jimbo la Kilwa Kaskazini bila ya kushirikisha Serikali ya Vijiji:-

Je, Serikali iko tayari kusimamia Mamlaka ya Hifadhi hiyo kurudisha alama za mipaka katika maeneo ya awali ili kuepusha mgogoro unaoweza kutokea?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maliasili na Utalii inalo jukumu la kusimamia uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na misitu kwa kuzingatia uwepo wa mahusiano mazuri kati ya wananchi na maeneo yanayohifadhiwa. Jukumu hilo linatekelezwa kwa pamoja na mambo mengine kwa kutambua kulinda, kupitia upya na kuweka vigingi (beacons) katika mipaka ya Mapori ya Akiba, Hifadhi za Taifa, Hifadhi za Misitu na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iliagizwa kuweka vigingi kwenye mipaka ya hifadhi zote nchini kwa lengo la kuonesha mipaka kati ya hifadhi na vijiji ili kuepusha migogoro na uvamizi unaofanywa na wananchi na kusababisha malalamiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza maagizo haya, Wizara inafanya kazi ya kusimika vigingi kwenye mipaka ya mapori yote ya akiba likiwemo Pori la Akiba la Selous. Aidha, zoezi la upitiaji, uhakiki na usimikaji wa vigingi katika Pori la Akiba la Selou upande wa Kilwa Kaskazini limefanyika katika Kijiji cha Namatewa. Zoezi hili limefanyika kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya pamoja na Uongozi wa Vijiji kwenye maeneo hayo. Kazi ilifanyika kwa kutumia Tangazo la Serikali Na. 275 la Mwaka 1974 lililoanzisha pori hilo na ramani za vijiji husika kwa kushirikiana na Wapima wa Ardhi wa Wilaya zinazopakana na mapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya mpaka wa Pori la Akiba la Selous ambalo halijasimikwa vigingi upande wa Kilwa Kaskazini ni katika Vijiji vya Mtepera na Zinga Kibaoni. Hii ni kutokana na wananchi wa vijiji husika kutotambua ukomo wa mpaka kwa mujibu wa ramani za vijiji vyao wakidai eneo linalosalia ni la kijiji na siyo la hifadhi. Kwa mantiki hiyo, hakuna uhamishaji wa alama za mpaka uliofanywa kwa nia ya kuchukua eneo la ardhi la kijiji karibu na Pori la Akiba la Selous.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara zingine sita, imeelekezwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia upya maeneo yenye ubishani na migogoro ikiwa ni pamoja na vijiji na kuangalia mipaka ili kuondoa migogoro hiyo. Kwa sasa Wizara inaendelea kuweka utaratibu mzuri wa namna ya utekelezaji wa agizo hilo.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE aliuliza:-

Benki ya Dunia imefadhili miradi ya visima kumi (10) katika kila wilaya nchini:-

Je, Serikali imefanya tathmini kujua asilimia ya miradi iliyofanikiwa na ambayo haikufanikiwa; na kwa ile ambayo haikufanikiwa, Serikali haioni haja ya kuingiza fedha ili kukamilisha miradi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale, Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016, Wizara ya Maji ilifanya tathmini ya kina nchi nzima ili kujua idadi ya visima vyote vilivyochimbwa kwa Awamu ya Kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji katika Halmashauri zote Tanzania Bara. Idadi ya visima vilivyochimbwa ni 1,485. Kati ya hivyo, visima 990, sawa na asilimia 67 vilipata maji na visima 495 sawa na asilimia 33 vilikosa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo visima vyake vilikosa maji Serikali ilitumia vyanzo vingine mbadala kama vile chemchemi, mito, maziwa au kujenga mabwawa ili kuhakikisha maeneo yaliyopewa kipaumbele katika mpango wa vijiji 10 yanapata huduma bora ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali imeanzisha Mfuko wa Maji wa Taifa ambao unalipa miradi yote iliyochelewa kukamilika na miradi mipya inayoendelea kujengwa katika Halmashauri zetu. Lengo ni kuhakikisha huduma bora ya maji kwa kila mwananchi.
MHE. HAMIDU H. BOBALI (K.n.y. MHE. VEDASTO E. NGOMBALE) aliuliza:-

Zoezi la kupeleka mifugo Mikoa ya Kusini limeleta madhara makubwa kwa mazingira na wananchi kwa ujumla kwa sababu ya kukosa maandalizi kabla ya utekelezaji wake:-

(a) e, Serikali iko tayari kujenga Malambo ili kunusuru tatizo la maji kwa mifugo hiyo?

(b) e, Serikali iko tayari kuondoa mifugo ambayo ipo katika maeneo ambayo hayakupangwa kwa ajili ya mifugo kutokana na mipango ya matumizi bora ya ardhi katika Kata ya Mifola, Kandawale na Somanga?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu maswali ya Mhe. Vedasto Edgar Ngombale Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa ugetuaji wa Madaraka, kumradhi mnamo mwaka 2006 Serikali iliamua kuondoa makazi, shughuli za kilimo na za mifugo katika bonde la Ihefu ambalo lilikuwa linaendelea kukauka hivyo kuathiri upatikanaji wa maji ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji wa umeme. Kabla ya kuondoa mifugo katika maeneo hayo, Ofisi ya Makamu wa Rais ilifanya kikao na Wakuu wa Mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma kuwaomba waainishe maeneo ambayo yanaweza kutumika kupokea mifugo hiyo. Baada ya kikao hicho Wakuu wa Mikoa hiyo walionesha utayari wa kupokea mifugo katika Mikoa yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua iliyofuata ilikuwa ni kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi ya vijiji ambapo katika Mkoa wa Lindi jumla ya vijiji 69 vilitengeneza mpango wa matumizi bora ya ardhi, na jumla ya Hekta 215,343.34 zilitengwa kwa ajili ya malisho. Serikali pia ilijenga josho na kituo cha kupokea mifugo katika kijiji cha Marendego kilichoko Wilaya ya Kilwa ambapo mifugo ilikuwa inapokelewa na kupatiwa huduma za uogeshaji kabla ya kwenda kwenye vijiji vilivyoandaliwa kupokea mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mujibu wa Sera ya Ugatuaji wa Madaraka, wajibu wa kutoa huduma kwa wafugaji kama vile maji (ujenzi wa mabwawa na malambo) pamoja na majosho ni jukumu la halmashauri husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara iko tayari kushirikiana na halmashauri zenye changamoto kubwa ya ukosefu wa vyanzo vya maji kwa ajili ya mifugo kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Katika mwaka 2019/2020, Wizara imepanga kukarabati malambo 6 katika Mikoa ya Manyara, Pwani, Simiyu, Arusha, Geita na Tabora na kuchimba visima virefu 50 katika maeneo yenye mifugo mingi na yaliyotenga maeneo ya malisho ikiwemo Mkoa wa Tunduru- Ruvuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mujibu wa Sheria ya Matumizi Bora ya Ardhi Na. 6 ya Mwaka 2007, vijiji pia vinayo Mamlaka ya kutunga Sheria ndogo ya kusimamia utekelezaji wa mipango waliojipangia. Kwa sababu hiyo basi, vijiji husika vinao uwezo wa kuondoa mifugo katika maeneo ambayo hayakutengwa kwa ajili ya malisho. Hata hivyo, Wizara imeunda timu ya kutatua migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Aidha, Wizara iko tayari kutumia timu hiyo kwenda jimbo la Kilwa Kaskazini ili kushirikiana na halmashauri katika kutatua tatizo hilo.