Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hassan Selemani Kaunje (6 total)

MHE. HASSAN S. KAUNJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wa eneo hili la bahari unaendana na shughuli za wavuvi na Lindi kuna wavuvi. Nilipenda niulize nini msimamo wa Serikali kuwasaidia wavuvi wa Lindi kuhusiana na kodi mbalimbali ambazo ni kero kwao? Vilevile wana mpango gani wa kuwasaidia zana za uvuvi ili waweze kuleza pato katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli watu wa Lindi shughuli zao kubwa sana hasa wale wa ukanda ni uvuvi na siyo watu wa Lindi peke yake isipokuwa hata Kanda ya Ziwa na maeneo mbalimbali ambao wanaguswa na vyanzo vya maji. Wengi wao wana tatizo kubwa za tozo za kodi za aina mbalimbali ambazo zinawakabili kiasi kwamba shughuli zao zinakwama. Ndiyo maana katika nyakati mbalimbali hapa nimekuwa niki-refer aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Kilimo aliyezungumzia suala la kupitia hizi kodi mbalimbali, lengo kubwa ni kupunguza hizi tozo mwisho wa siku wananchi wa kawaida ambao wavuvi wa Lindi waweze kupata fursa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge tuwe na subira, Serikali inafanya mchakato huu mpana katika suala zima la kilimo, mifugo na uvuvi ambapo inaonekana kwamba mvuvi mwingine akitoka halmashauri moja kwenda halmashauri nyingine anatakiwa alipe kodi. Kwa hiyo, Serikali inaangalia haya yote kwa kina lengo kubwa ni kuliboresha eneo hili mwisho wa siku wananchi wa eneo lako la Lindi wataweza kupata fursa sana katika suala zima la shughuli zao za uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo la pili la jinsi gani ya kuboresha suala zima la uvuvi, niki-refer tena katika Wizara ya Kilimo na Mifugo, wakati waki-submit hapa bajeti yao mwaka huu, walizungumzia wazi mkakati wao mpana wa kuwasaidia wavuvi hasa wale wa kandokando ya bahari na katika maziwa kwa kuangalia jinsi gani watapewa nyenzo ambazo zitasaidia katika suala zima la uvuvi. Hata hivyo, tulipopitisha bajeti ya TAMISEMI tulisema kuna zile asilimia tano za vijana na akina mama, katika maeneo mengine hasa ya uvuvi, halmashauri katika mipango yao iweze kuona jinsi gani ya kutumia five percent ya vijana na akina mama kuwasaidia wavuvi wa maeneo hayo ili waweze kushiriki katika shughuli za kujenga uchumi wa nchi yao.
MHE. HASSAN S. KAUNJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwanza kwa majibu ya ziada ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali langu la msingi ilikuwa ni lini, kwa maana ni mwaka gani katika miaka hii mitano au bajeti ipi hizi program za Maendeleo ya Sekta ya Utalii Kusini zitaanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa maana ya vivutio alivyovitaja, sambamba na vivutio vingine vya fukwe za Kisuele na Mitema ambazo ni bora kuliko zote katika ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki, kuanzia Somalia mpaka South Africa: Je, yuko tayari kuviwekea vipaumbele katika kuvitangaza kupitia taasisi zake zinazotangaza utalii wa nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Kaunje, kwa namna ambavyo ameanza kwa kasi kubwa kuweza kutetea eneo la Kusini ili utalii sasa uweze kuelekea upande wa ukanda huo, kwa maana ya Southern Circuit badala ya hali ambayo iko hivi sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la lini; nimezungumzia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwenye jibu langu la msingi, lakini pia nimetaja mradi wa Regrow ambao nilisema na wenyewe ni mradi ambao unakwenda kuboresha utalii katika ukanda wa kusini. Sasa kuhusu lini, nataka kusema, kuhusu mradi wa Regrow tayari mradi huo umeshaanza na uko katika hatua za awali na miradi mingine ambayo itakuwa inaunga mkono jitihada za utalii kusini itaweza kupangwa katika bajeti zijazo, wakati kwa sasa hivi tunatekeleza mradi huu wa Regrow ambao wenyewe tunautekeleza kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fukwe za Mitema na nyinginezo kuweza kupewa kipaumbele, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, kwamba Mikoa ya Lindi na Mtwara ina utajiri mkubwa sana wa fukwe za bahari, tofauti na maeneo mengine ambako kuna fukwe za Maziwa; Lindi na Mtwara kuna utajiri mkubwa sana wa fukwe za bahari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano, ambao unaanza na mpango huu wa mwaka wa kwanza wa 2016/2017, hatua ya kwanza tunayokwenda kuifanya ni kutembelea maeneo hayo yote na kuweka matangazo ya kutosha ili kuweza kuwavutia wawekezaji mbalimbali kuweza kuboresha miundombinu katika maeneo hayo ili fukwe hizo ziweze sasa kushiriki katika Sekta ya Utalii kwa tija zaidi.
MHE. HASSAN S. KAUNJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nisikitike tu kwamba jibu lake haliendani na uhalisia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhalisia uliokuwapo Lindi ni kwamba takwimu za watu wanaokadiriwa 100,000 ni wa Jimbo la Lindi Mjini. Vilevile nimkumbushe Naibu Waziri katika mchakato wa bajeti iliyopita ya mwaka jana kwamba maafisa wa Halmashauri walishakaa vikao tofauti na maafisa wa Wizara yake katika kuangalia uwezekano wa kubadili bajeti kutokana na idadi ya watu. Sasa anaposema kwamba idadi ya wakazi wa Lindi na akitumia takwimu za wapiga kura ni sahihi nakataa kukubali jibu lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali ya nyongeza kama tu Mheshimiwa Naibu Waziri na Wizara yake walikubali kwamba idadi ya watu wa Lindi ni kidogo na hivyo watafanyia kazi mchakato wa kuongeza bajeti katika bajeti inayokuja, je, yuko tayari kuthibitisha hilo au kulifanyia kazi hilo kwa bajeti inayokuja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kutokana na idadi ya watu kutotumika idadi stahiki katika Jimbo la Lindi imepelekea huduma za afya kupelekwa katika kituo kimoja tu cha afya katika Lindi Mjini na hivyo kupelekea shida kubwa kwa watu wa Lindi.
Je, Mhehsimiwa Waziri anayehusika yuko tayari kuiboresha hospitali inayotoa huduma ambayo inaendeshwa na Jeshi la Polisi Lindi ili kuweza ku-accommodate matatizo ya afya ya wananchi waJimbo la Lindi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiiwa Mwenyekiti, kwa swali la kwanza ambalo anasema kwa bajeti inayokuja, naomba nilikumbushe Bunge lako tukufu kwamba Bunge hili lilipitisha sheria ya takwimu Machi, 2015 ambayo inatoa mamlaka kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuratibu takwimu zote rasmi. Na kwa Serikali tunachofahamu ni kwamba idadi ya watu wa Lindi Mjini ni ambao wametajwa na kwa makadirio ya mwaka 2016, idadi ya watu Lindi Mjini ni 85,871 hiyo ndio takwimu rasmi inayotambulika na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu swali la pili, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge swali hili tutakaa pamoja na Waziri wa Afya na Waziri wa TAMISEMI tutalifanyia kazi kuona hospitali hii inaboreshwa.
MHE. HASSANI S. KAUNJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naibu Waziri yuko tayari kuwaambia wananchi wa Lindi kumwambia Mbunge wao na Mheshimiwa Rais kwamba ahadi ya Mheshimiwa Waziri wake ya kwamba mradi huu utakamilika tarehe 3 Julai, 2017 kwamba, itatekelezwa kama walivyoahidi? Swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri awe tayari kuweza kunifikishia salamu zangu za pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu na yeye mwenyewe kwa kuweza kukamilisha mradi mwingine pacha na huo wa kijiji cha Chikondi. Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kunifikishia salamu zangu hizo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Mheshimiwa Mbunge, ahadi ya Mheshimiwa Waziri itatekelezwa na nikwambie tu kwamba ni siku kumi tu zimepita nimeenda Lindi, nimeenda kukagua ule mradi, nimekuta vifaa vyote vilivyokuwa vinatakiwa kwenye mradi vimewasili na tayari kuna kundi kubwa ambalo liko pale linafunga na mabomba yaliyobaki yanakamilishwa na eneo ambalo kutokana na mvua kubwa mabomba yalifumuliwa, linarekebishwa. Kwa hiyo, uwe na uhakika kabisa kwamba maji yatatoka na inawezekana hiyo tarehe 3 au kabla ya tarehe 3 Julai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, Mheshimiwa Mbunge, Waheshimiwa Wabunge wamecheka, hawakujua wewe una maana gani? Ni kwamba baada ya ziara ya Mheshimiwa Rais, tuliamua kuchimba kisima kingine ili kuongeza uwezo wa upatikanaji wa maji Lindi na kisima kile tayari kimekamilika, na mimi mwenyewe nimeenda kukagua juzi. Tumekuwa na matatizo kidogo yaliyokuwa yamejitokeza kuhusiana na ukataji wa huduma ya umeme kwenye mitambo, ambapo jana tumekaa nao kikao; tunatarajia kulikamilisha mapema. Kwa hiyo, Mheshimiwa nikuhakikishie kwamba huduma ya maji Lindi inafika na Mheshimiwa Waziri yupo humu ndani, ameshasikia salamu zako. Nakushukuru sana.
MHE. HASSAN S. KAUNJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Waziri wa Maji, tulifanya ziara ya kukagua vyanzo vya maji katika eneo la Manispaa ya Lindi na kuna mradi mkubwa wa maji wa Ng‟apa, Lindi. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuniambia mradi ule utakamilika lini na wananchi wa Lindi wakaweza kupata maji ya kunywa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na nyaraka za kimkataba na utekelezaji unaoendelea, tunategemea mwezi Aprili mwaka huu wa 2017, mradi huo utaanza kutoa maji kwa ajili ya wananchi wa Lindi.
MHE. HASSAN S. KAUNJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri nina maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza Serikali ya Awamu ya Nne ilitoa ahadi ya kujenga kituo cha Afya katika kata ya Mnazi Mmoja. Ahadi hii ilikuwa ina inataka kutekelezwa na Serikali Kuu, mpaka tunapozungumza hakuna chochote kinachoendelea ikiwa ni mwaka wa saba sasa. Nini kauli ya Serikali kuhusu jambo hilo?
Swali la pili, wananchi wa Lindi tuliwahamasisha waanze kujenga vituo vya afya katika kata zao. Wamepata maelekezo kutoka TAMISEMI ya kwamba vituo hivyo visimame kujengwa kwa muda mrefu mpaka sasa. Nini kauli za Wizara dhidi ya watu wale ambao wameamua kujitolea kuweza kujenga vituo vile vya afya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya Serikali kama zilivyo ahadi zingine na nikifahamu sehemu ya Mnazi Mmoja ni juction ya population kubwa na imetolewa ahadi hii takriban miaka saba, nikijua kwamba kuna juhudi zimeshaanza pale. Naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali naomba ihamasishe Halmashauri yako muanze kuibua jambo hili vizuri halafu na sisi tutaliratibu vizuri. Naomba nikuambie Serikali itakupa ushirikiano wa kutosha lengo letu ni kwamba commitment ya Serikali ya ahadi zote zilizotolewa na viongozi wetu wa Kitaifa tunaenda kuzitekeleza.
Kwa hiyo, naomba nikusihi Mheshimiwa Mbunge katika mchakato huu bajeti utakao kuja sasa tuliweke hili vizuri ili na sisi tutalipa nguvu, lengo kubwa kituo cha afya tuweze kukitengeneza katika eneo lile. Jambo la hivi vituo vya afya vingine ambavyo wananchi wameanza ujenzi nikijua kwamba commitment ya Serikali ni kuwahamazisha wananchi katika suala zima la ujenzi wa afya. Kama vituo hivyo ni vipya vinaendelea basi naomba niseme kwamba tutaendeleza kuvihakikisha tunavipa nguvu. Lakini nikijua kwamba kuna utaratibu ambao wakati mwingine umejitokeza kuna utaratibu wa kubadilisha zahanati kuwa kituo cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Ofisi yetu sasa ilitoa maelekezo kama hizi zahanati tuziache ziwe zahanati lakini tujenge vituo vipya viwe vya afya. Lakini kwa sababu Bwana Kaunje jambo hili umelileta hapa naomba nikuhakikishie kwamba ofisi yetu itakupa ushirikiano wakutosha kuangalia scenario ipi iliyoko kwenye Manispaa ya Lindi tuweze kusaidiana kwamba wananchi waweze kupata huduma kutokana na hali halisi ilivyo pale kwako Lindi.