Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka (3 total)

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu ya Waziri Mkuu kuonesha kwamba hiyo sera bado ipo. Kwa uzoefu wangu, utekelezaji wa sera hiyo haupo. Nina mifano, nchi za jirani anapokuja mwekezaji kuwekeza katika nchi hiyo huwa anaruhusiwa kuja na watu watano tu kutoka nchini kwake, tofauti na ilivyo hapa nchini kwetu. Wawekezaji wa kwetu hawana hiyo sera; hawana limit ya kuweka wafanyakazi kutoka nchini kwao. Ndiyo hiyo inayosababisha sasa hivi viwanda vingi vinaendeshwa na wageni wakati sisi wenyewe Watanzania tunapoteza ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushahidi huo ninao kwa sababu nimefanya kazi kwenye sekta ya watu binafsi siyo chini ya miaka 30 mpaka naingia hapa Bungeni. Tumeshaona wafanyakazi wengi wako zaidi ya miaka 20 wafanyakazi wa nchi za nje. Ukiwauliza vibali vyao havieleweki na wengine kama wanakuja Wakaguzi, wanafungiwa kwenye ma-godown, huo ushahidi ninao.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, nipe kauli yako, ni lini Serikali yetu itaweza kufuatilia hili suala ili kuzalisha ajira kwa watu wetu? Lini itaweka sheria kwa wawekezaji kwamba wanahitajika walete wafanyakazi wangapi kutoka kwenye nchi wanazotoka?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimhakikishie kwamba jambo hili tunalisimamia tena kwa ukaribu zaidi. Sera aliyoitaja ya nchi za nje ndiyo sera yetu nchini kwamba mwekezaji yeyote anayekuja kuwekeza nchini iwe ni kiwanda au sekta ambayo inahitaji utalaam, tumeruhusu watumishi watano, ndio ambao wanaruhusiwa kuingia kufanya kazi nchini. Sekta zote ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania, tumeweka utaratibu na tunasimamia kwamba sekta zote hizo zitafanya kazi na Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna eneo ambalo linalalamikiwa, basi Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane, kwa sababu sekta ya kazi iko ofisi kwangu. Nina Naibu Waziri anayeshughulikia ajira na kazi na nina Katibu Mkuu. Kwa hiyo, ni rahisi pia kufuatilia maeneo hayo ili tuone kwamba tunafungua nafasi hizo kwa Watanzania badala ya kuwa tunajaza raia kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado Serikali hii haizuii mashirika ya nje au wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza nchini, lakini lazima wanapofika Tanzania wataendelea kufuata sheria na sisi Serikali tutasimamia sheria hiyo kuwa inatumika ili kufungua nafasi kwa Watanzania.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kukamilika kwa daraja la Mto Kilombero ni wazi kwamba sasa Mkoa wa Morogoro unafunguliwa kibiashara. Nini mipango ya Serikali kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Lindi kwa barabara inayopitia kutoka Liwale kuelekea Morogoro? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kiongozi wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa ni moja kati ya ahadi yake ya kuhakikisha barabara kutoka Ilonga hadi Liwale inashughulikiwa. Ahadi hiyo tumepewa na nimhakikishie kwamba tutaishughulikia hadi tuikamilishe katika kipindi hiki cha miaka mitano.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, ahsante kwa majibu yanayotia matumaini, lakini umeainisha kwamba tatizo kubwa tulilonalo ni tatizo la vyanzo vya maji. Je, Serikali haioni sasa imefikia wakati wa kuvuna maji ambayo maji mengi kwa mfano, wakati wa masika kama sasa hivi, maji mengi yanapotea hakuna namna yoyote ya kuvuna hayo maji ili iwe ni chanzo mbadala cha maji?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya mipango ambayo tunayo ni ya uchimbaji wa mabwawa kwenye maeneo ambayo tunadhani tunaona kwamba kuna utiririshaji wa maji hasa msimu wa mvua.

Pili, tumeendelea kutoa elimu kwa Watanzania kuzitumia mvua na maji ambayo yanatiririka, kuweza kuyaweka pamoja ili yawe akiba yetu ya kuweza kupata maji na kusambaza kwenye vijiji. Mpango huo upo pia hata kwenye bajeti umeona mipango wa uchimbaji mabwawa maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Kuchauka, wewe unatoka Liwale ni jirani yangu na ninapafahamu Liwale, iko miradi mingi sana tu ya kuchimba mabwawa, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba juzi nilikuwa nazungumza na Mkurugenzi wako akiripoti kwamba kuna mvua nyingi, mabwawa mengi yameharibiwa, kwa hiyo tuahitaji tena kutenga fedha za kutengeneza mabwawa yako pale, jambo hili nalo tunalifanya karibu maeneo yote ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika nasihi na ninatoa wito kwa Halmashauri zote za Wilaya nchini kuhakikisha kuwa tunatumia vizuri mifereji iliyopo na mvua ambazo sasa zinaisha mwishoni, pia hata msimu ujao wa mvua kuweza kujenga mazingira ya kukusanya maji yanayotiririka, wenye nyumba za bati na nyumba zote watumie mvua hizi kupata maji na kuyaweka mahali ili tuweze kuyatumia kipindi cha ukame, kwa kufanya hilo tutakuwa tumepunguza ugumu wa upatikanaji wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaahidi Waheshimiwa Wabunge na Watanzia wote Serikali itaendelea na mipango yake ya kuhakikisha kwamba tunamtua ndoo Mama ili aweze kufuata maji kwa umbali mfupi na hasa ule umbali ambao tumejiwekea kwenye sera wa usiozidi mita 400. Ahsante