Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Eng. James Fransis Mbatia (30 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami nitoe mawazo yangu kwenye Mpango ulioko mbele yetu, hoja iliyoko mbele ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa siha njema ya kusimama kwenye Bunge hili. Nawashukuru wapigakura wa Jimbo la Vunjo walionichagua kwa zaidi ya asilimia 72 ya kura zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango uliopo mbele yetu unatakiwa ujibu yafuatayo:-
(1) Unakuzaje uchumi wa Taifa letu?
(2) Unasaidiaje vijana wetu kupata ajira?
(3) Ujasiriamali wa Taifa hili utaongezeka kwa kiasi gani?
(4) Sekta mbalimbali katika Taifa letu na hasa sekta binafsi Mpango huu utaishirikisha kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza na hilo kwa sababu Taifa letu hapa tulipofikia sasa Serikali ya Awamu ya Tano siyo kwamba imeanza sifuri. Serikali zilikuwepo za tangu Awamu ya Kwanza mpaka sasa, lakini Taifa letu limekosa itikadi. Leo hii hatuna itikadi ya Taifa ya kutuonesha kwamba itikadi yetu ni nini na malengo yapo namna gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano nieleweke vizuri, wakati wa Mwalimu Nyerere tulikuwa na itikadi ya ujamaa, lengo likiwa ni kujitegemea na mifumo yetu yote, sekta zetu zote zilikuwa zinatekeleza itikadi ya ujamaa, lengo likiwa ni kujitegemea, lakini leo hii ukiangalia Mpango huu una-address au unatoa mwelekeo gani wa kuonyesha itikadi ya Taifa letu ni ipi kama ipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme itikadi ya Awamu ya Tatu ilikuwa ni uwazi na ukweli, ndiyo itikadi au ya Awamu ya Nne labda maisha bora kwa kila Mtanzania au ya Awamu ya Tano useme hapa kazi tu je, hiyo ndiyo itikadi. Tunatakiwa tuwe na itikadi ya Taifa, vyama vishindane kwenye msingi ile ambayo tumekubaliana ya Kitaifa. Kwa mfano, kwenye sekta ya elimu, siyo kwenye sekta ya elimuWaziri aliyekuwepo ndiyo aamue namna ya kuindesha sekta hiyo, tuwe tumekubaliana Kitaifa, sekta ya elimuinaongozwa hivi kwa miaka kumi au ishirini ijayo. Kwa hiyo, yeyote atakayeingia pale ataongoza kwa misingi ambayo imewekwa. Lakini hebu tuangalie muda tunaoupoteza kwenye kugombana, akiingia huyu anabadilisha, akiingia huyu anabadilisha na ni kuvuruga tu Taifa la Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuwe na maono ya miaka ishirini au thelathini ijayo, lakini siyo kwamba tunakosa mifumo na hasa ile mifumo inayolinda utu wa mwanadamu, inayokuza utu wa mwanadamu, mifumo hiyo ni ya elimu, mifumo hiyo ni ya kiutamaduni, mifumo hiyo ni yetu sisi kama Taifa ambayo inakuza zaidi utu wa mwanadamu, thamani ya utu wa mwanadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasoma Netherlands miaka ya 2007/2008, Bishop Acronson anakwambia maendeleo ya Netherlands yamepatikana kwa kasi kwa miaka 64 kwa sababu ya maelewano ya Kitaifa na kutambua utu wa mwanadamu upo namna gani, kutambua uhai wa mwanadamu upo namna gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii hapa Watanzania sisi sote ni watoto wa mama Tanzania, lakini kama sisi sote ni watoto wa mama Tanzania kwa nini tunabaguana? Kwa nini tunajenga misingi ya kulipasua pasua Taifa la Tanzania? Kwa nini tunajenga misingi leo hii Tanzania ni moja, anasema huyu wa Kusini, huyu wa Kaskazini, huyu wa Mashariki huyu wa Magharibi, ni kwamba tumekosa mifumo inayojali utu kwamba huyu Mtanzania ana haki kama Mtanzania mwingine, kama ni mifumo ya utawala bora, mifumo ya utawala wa kidemokrasia inalinda haki za wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesomea mambo ya majanga, yapo majanga ya aina kuu tatu na zaidi ya asilimia 95 ya majanga yote yanasababishwa na binadamu. Kuna known knowns risk, known unknowns risk and unknown unknowns risk ambazo ni acts of God, lakini hizi known known risk tunazisababisha sisi binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majanga kusipokuwa na utulivu kwenye Taifa, kwa mfano, mwaka 2013 Taifa lilikuwa limekwishaanza kupasuka misingi ya udini, waislamu na wakristo, Taifa litaongozwaje, kuuawa kwa viongozi wa dini, Taifa litaongozwaje, mipango itatekelezwaje, lakini tulipokaa watu ambao ni chini ya 100 Taifa lilitulia, Mheshimiwa Lukuvi alikuwepo kwenye mazungumzo yale tuliyojifungia watu chini ya 100 Taifa likatulia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi tukiwa na meza ya maridhiano, uundwaji wa dola siku zote duniani ni meza ya maridhiano, sisi sote ni Watanzania tuheshimiane na tukubaliane. Yanayotokea Zanzibar tusione kwamba ni mambo madogo, la hasha, ni mambo makubwa sana, yanayotokea Zanzibar leo hii tujue kwamba Tanzania tunaihitaji dunia kuliko dunia inavyoihitaji Tanzania. Narudia, Tanzania inaihitaji dunia kuliko dunia inavyoihitaji Tanzania. Leo hii Tanzania hatuwezi tukawa ni kisiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mipango tunayopanga hapa ni lazima tu-address suala la utawala bora na kwa kuwa tumekubaliana kwenye mfumo huu na Tanzania sisi siyo kisiwa je, duniani, let us think globally but act locally. Kama hatuwezi tuka-address kwamba dunia hii ambayo imeshakuwa leo hii ni kijiji, akili zetu zinajishusha kwamba dunia imekuwa ni kijiji kwa kasi ya maendeleo ya kasi ya sayansi lakini leo hii tunarudi hapa kuanza kuulizana wewe wa Kaskazini, wewe wa Kusini, wewe wa Mashariki, wewe wa Magharibi, wewe Mzanzibari, wewe Mbara tunaliua Taifa la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipokubali kwamba umoja wa Taifa la Tanzania ndiyo utakaoweza kulea kizazi hiki na vizazi vijavyo, tutakuwa tunajimaliza wenyewe. Sisi Wabunge majukumu yetu ya kwanza kwa Taifa tunalileaje Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo rasilimali nyingi tu za Taifa hili, nendeni kwenye ripoti ya kutekeleza Mpango huu na hili nitoe nasaha kwa Mawaziri, kuna baadhi ya Mawaziri wanasema tu sijui ili waonekane kwenye runinga, wanasema ohh, tunaweza tukajitegemea kwa rasilimali zetu sisi wenyewe, mtapata wapi fedha Serikali ya kujenga reli ya kati kwa standard gauge kwa rasilimali zetu sisi wenyewe humu ndani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono kabisa kujenga reli ya kati na matawi yake yote kwa kuwa ndiyo langu kuu la uchumi wa Taifa la Tanzania. Tuimarishe Bandari ya Dar es Salaam, tuunganishe na mitandao ya reli, Taifa hili uchumi wake utakwenda kwa kasi kubwa sana. Tusianze kugombana na Kagame na Uhuru Kenyatta wametuamsha, tuwachukulie positively katika kujenga Taifa letu. Tusianze kulalamika lalamika tu hapa ohh, Kagame anatuzidi kete, Kenyatta, kwanza hata lugha hizo ni kwamba umeshindwa kufikiria. Nimeshawahi kusema kuna nguzo kuu sita za umaskini wa fikra ambazo ni ya kwanza, majungu; ya pili fitna; ya tatu umbea; ya nne kusema uongo; ya tano kujenga chuki na ya sita uvivu wa kufikiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, let us think big positively Taifa letu hili tutalipeleka mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Vunjo tunategemea sana sekta ya utalii, Tanzania ni ya pili kwa vivutio vya utalii duniani lakini Tanzania inashika nafasi ya 110 kati ya nchi 133 kwa…
Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, utambulisho wa mwanadamu ni utu wake! Je mifumo yetu ya elimu inajali utu wa mwanadamu? Utu ndiyo msingi mkuu wa haki za binadamu. Lengo la nne la maendeleo endelevu ya dunia linasema ensure inclusive and equitable, quality education and promote lifelong learning opportunities for all; elimu shirikishi, sawa, bora kwa wote! Meli ya elimu Tanzania inazama, sisi tunaosafiri ndani ya meli hiyo hatujitambui, both quality and quantity of education are being eroded. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania pole pole tunaondolewa kwenye mkondo muhimu wa maendeleo. Leo ni Ijumaa, Mtume Muhammad (S.A.W.) anasema “mwenye kutaka akhera na asome, mwenye kutaka dunia na asome, na mwenye kutaka vyote na asome! Elimu ni kitu chake kilichompotea Muislam, popote akipatapo na akichukue”
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma Biblia Takatafu Mithali 4:13, “Mtafute sana Elimu usimuache aende zake, yeye ndiyo uzima wako” popote umtafute! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeanza na hayo kwa sababu leo hii tunazungumzia ada elekezi. Ada elekezi maana yake nini? Serikali iingie kwenye ushindani, wala sio suala; ada elekezi, mabasi ya njano, kodi zisizotabirika kwenye sekta ya elimu! Mambo haya tuliongea na Mheshimiwa Rais Mstaafu wakati tunachangia BAKWATA mwaka juzi, shule ya Sekondari Al-Haramain pale Dar es Salaam na tukakubaliana kimsingi kodi kwenye sekta ya elimu ziondolewe, elimu ni huduma sio mambo ya kutoa kodi kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii niyapongeze Mashirika ya Dini kwa kazi nzuri wanayofanya na hasa Dayosisi ya Moshi, Askofu Fredrick Shoo, Askofu Isaack Amani na kazi wanazofanya zote hizo wanafanya kwa niaba ya Serikali wakiwepo Sekta Binafsi. Kwa hiyo, haya mambo ya ada elekezi na nini naomba wala tusipoteze muda, badala yake Serikali itoe ruzuku kwenye Mashirika ya Dini, kwenye Sekta Binafsi, wayape nguvu ili waweze kutoa elimu, Taifa letu likielimika, Taifa linafaidika kwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto za Walimu, mafao yao, Walimu kukaa mbali na familia zao na wewe umelisemea vizuri sana, tunaomba watu wote waje karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, deni la Walimu sio suala la kuzungumzia tena! Leo hii Wizara ya Elimu inalijua vizuri. Juzi nilikuwa natoa vyetu, ukitoa vyeti leaving certificate vimeandikwa TAMISEMI, Academic certificate, Wizara ya Elimu, sasa watu hawa wanajichanganya, ni vitu gani vya ajabu sana! Jina la Wizara yenyewe, danadana tangu tumepata uhuru mpaka leo hatujui hata jina la Wizara ni kitu gani. Waziri akiingia kwenye Wizara ndiyo mfumo yaani Waziri ndiyo mfumo, aliyofanya Shukuru Kawambwa umekuja kuyapindua yote, utakayofanya sasa hivi wewe akija mwingine anayapindua yote, akija mwingine anayapindua yote, hili linakuwa tatizo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya BRN yamekwenda wapi leo hii? Yaani ni vitu vya ajabu tu! Miaka kumi mambo hayaeleweki. Jimbo la Vunjo tuna shule za msingi 128, shule 102 ziko hoi bin taabani, je, ni karne ya kuzungumzia mambo ya mifumo ya vyuo? Nilikuwa nasoma mitaala ya elimu ya awali, naunga mkono wale wote waliozungumzia walemavu. Ukisoma lile lengo la 326 kuhusu madarasa ya vyuo na namna ya walemavu kuweza kupata haki zao, leo hii ziko kwenye hali gani? With due respect hali inazidi kuwa mbaya, mbaya, mbaya! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vitabu; Sera ya vitabu ya mwaka 91; Sekta ya Binafsi waandikie vitabu, Taasisi wakague vitabu, EMAC imevunjwa hapa Bungeni tarehe 5 Juni, 2013, siku ya Jumatano, Bunge hili tumevunja EMAC, nani anahariri vitabu leo hii? Afadhali magazeti yanahaririwa vizuri kuliko vitabu vya shule za msingi na nitatoa mfano hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo tulilonalo hapa ni itikadi zetu za siasa na Mwenyezi Mungu atatulaani kwa hilo. Tulikuja hapa mwaka 2013 na hoja ya elimu, ninayo hapa! Yote tunayozungumza kwenye Bunge hili nimeisoma hii jana mpaka saa nane na nusu za usiku, yamo humu ndani, lakini itikadi zikaingia hapa, mpaka na Kiti kikaingia kwenye mambo ya itikadi, tukashindwa Wabunge kuisimamia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu leo jioni Wabunge wachukue nafasi yao ya kuisimamia Serikali wakati wa Kamati ya Matumizi kama Serikali hii haitashika adabu! Naomba sana with due respect, ninayo kwa mfano Mheshimiwa Ndalichako, Sera ya Elimu hii hapa! Iliyozinduliwa mwaka jana na Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, imetumia zaidi ya bilioni 50, ukisoma ukurasa wa 22 inaelezea mtaala unafundishwa elimu ya msingi, yaani mtaala unafundishwa! Ukisoma ukurasa wa 27 unasema mtaala ni mwongozo mpana, hata hawajui maana ya mtaala ni nini, Sera ya Elimu hapa!
Mheshimiwa Naibu Spika, nakala hizi zililetwa mezani hapa mwaka 2013. Nikahukumiwa kwamba nimesema uongo, wanaonesha kwamba ni Taasisi ya Elimu Mitaala ya 2005, lakini hapa hapa Mungu si Abdallah sio Athumani, leo hii mmeweka kwenye website yenu toleo la 2007, leo hii mmeweka kwenye website yenu! Yaani kwamba Serikali ilidanganya Bunge hili kuleta mitaala ya uongo ya kugushi ndani ya Bunge hili! Tunamdanganya nani? Huwa tunamdanganya nani? Tanzania ni yetu sote, leo hii ndiyo mitaala iliyo kwenye Website yenu. Hii mitaala mliyoenda, anakiri Bhalalusesa - Kamishna wa Elimu na ulikuwa kwenye ile Kamati kwenye Bodi ya Spika, Bhalalusesa umenisikitisha sana Kamishna wa Elimu – umesema uongo kwenye mitaala hii hapa na evidence zote ninazo. (Makofi)
Mitaala ya elimu ya msingi Bhalalusesa unasema mmefanya editing, lakini hebu nikuambie, malengo ya elimu Tanzania, lengo la tatu, sentensi moja ina „na‟ „na‟ „na‟ mara saba, mtaala wa elimu wa shule ya msingi hapa. Malengo ya 2020 - 2025 ukisoma hata copy and paste mtaala wa shule ya msingi na awali ni tofauti, ku-copy tu lengo la elimu! Malengo ya elimu Tanzania leo hii, mtaala wa awali ni tofauti na ya sekondari, ni tofauti na ya diploma ni tofauti na Walimu, tunamdanganya nani? Ku-copy mitaala ya elimu nchini, mtaala mmoja ni tofauti na mwingine. Mtaala wa awali yako 10, mtaala huu mwingine yako mengi tu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimetoka Vunjo, kwa sababu ya muda tunazungumzia vitabu, vitabu ninavyo hivi hapa! Ukisoma kitabu cha juzi hiki hapa nimechukua Vunjo, kina mhuri wa EMAC japo tulishaivunja EMAC! Angalia ukurasa wa kule mwisho jedwali, juzi nimekikuta shule ya msingi Kochakilo, 2X7=15! Hii hapa! Nimeichukua!
Mheshimiwa Naibu Spika, chukua kitabu cha hisababti darasa la kwanza, pale mwanzoni kabisa wanasema namba nzima ni moja hadi 99, hiki hapa! Hii ndiyo sumu tunayowalisha Watanzania leo hii. Ukiangalia cha Kiingereza, chapter four ndiyo inaanza na a,e,i,o,u wakati huku mwanzoni wanaanza na sentensi, vitu vya ajabu tu! Ukisoma cha Kiswahili cha ajabu, usiku nilikuwa nasoma kitabu cha sayansi, kitabu cha sayansi, hapa tunatukana watoto huku, ukurasa wa 67 tunafundisha watoto wa miaka minane namna ya kujamiiana, mambo ya ngono, ndiyo maadili tunayowafundisha watoto wetu leo hii na imewekewa mihuri ya EMAC. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hoja ya elimu nilisema nini? Tulisema, ukiangalia mambo yote, angalia hisabati, angali akila kitu, ukiangalia vitabu vyote hivi hapa, nimechukua vichache tu lakini jana usiku nikasema ; Ewe Mungu tunapeleka wapi Taifa hili. Tulisema udhaifu uliopo katika sekta ya elimu unahusiana na mfumo wa utoaji wa elimu, ndicho kirusi kilichoambukiza udhaifu kwenye sekta nyingine zote katika Taifa letu. Sababu ya msingi ya kusema mambo yote, maendeleo ya Taifa lolote, kijamii, kiteknolojia, kiuchumi na kisiasa ni tunda la mfumo wake wa elimu. Uhai wa taifa lolote lile hutegemea wingi wa matumizi ya wananchi wake walioelimika na mwisho tulisema hapa hapa kwamba; elimu ndiyo mapigo ya moyo ya Taifa letu, mapigo ya moyo yakienda kinyume na asili yake, uhai huweza kupotea, tunao wajibu wa kutunza uhai huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa namwomba sana Rais Mheshimiwa Magufuli afumue Wizara yote ya Elimu. Kama kuna ufisadi wa kupita ni Wizara ya Elimu na watendaji wa Wizara ya Elimu, hasa Taasisi ya Elimu yaani ndiyo hovyo kupindukia ndani ya Taifa la Tanzania. We are eroding our education, tunaua Taifa letu, tunambabaisha nani? Tunamdanganya nani? Labda tuondoe Hansard, tufungiane humu ndani, wenyewe tu tuondoe na media, tuelezane ukweli wa Taifa hili, la sivyo tunaangamiza Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nahitimisha. Mtume Muhammad anatuasa anasema: “Ukiona uovu unatendeka, zuia, ukishindwa kuzuia, kemea, ukishindwa kukemea onesha basi hata chuki” na Zaburi moja inasema…
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Mbatia! Nilikuwa nasubiri umalizie sentensi
MHE. JAMES F. MBATIA: … inasema: “Kheri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki…… (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kuchangia kuhusu mtaala wa elimu ya msingi katika ukurasa VIII. Serikali imekiri kuwepo na mtaala uliokuwa ukitumika mwaka 1997. Je, Serikali inaweza kuleta nakala ya mtaala huo hapa Bungeni, kwani nimeutafuta bila mafanikio wakati ni mali ya umma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, malengo ya maendeleo ya milenia ya mwaka 2002, yaliyotajwa katika ukurasa wa pili yalizingatiwa vipi katika kutayarisha mtaala wa elimu ya msingi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwaje Mashirika ya Dini yanahusishwa katika tathmini ya mtaala wa elimu ya msingi, lakini sio katika kutathimini mtaala wa elimu ya awali na Serikali za Mitaa kuhusishwa katika tathmini ya mtaala wa elimu ya awali lakini sio katika mtaala wa elimu ya msingi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo ya elimu ya Tanzania katika mtaala wa elimu ya msingi, ukurasa nne ni tofauti na yale yaliyoainishwa katika mtaala wa elimu ya awali katika ykurasa wa tatu na nne, kulikoni?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Vunjo maeneo mengi hayana maji safi na salama toshelezi. Mfano ni Kata za Mwika Kusini, Makuyuni, Kahe Mashariki, Kahe, Kirua Kusini, Kilema Kusini, Momba Kusini na Kirua Magharibi. Sehemu nyingine tajwa hapo juu, miundombinu ya maji ni ya zamani sana, ni chakavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Momba Kusini walishirikiana na Mbunge, wameanza utaratibu wa kitaalam wa kuwa na andiko ambalo linakadiria mahitaji ya takriban shilingi milioni 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tumekubaliana kila kaya kuchangia sh.10,000/= lakini chanzo cha fedha hizi hazitoshelezi. Je, Serikali itasaidia kiasi gani katika mradi huu kama kichocheo? Kutoka chanzo cha maji ya uhakika kimepatikana Kisumbe, Mamba (South Water Supply System from Kisumbe Spring). Nashauri elimu shirikishi kwa wananchi namna bora ya kuyatawala, kuvuna/kuyasimamia na kuyatumia maji.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti iliyoko mbele yetu imeingia katika migogoro mingi tu, hii bajeti ya mwaka huu. Kwanza nianze na suala la madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1633 Kanisa Katoliki lilimdhalilisha na akafungwa mwanasayansi mmoja anaitwa Galileo kwa sababu ya kwamba alisema dunia inazunguka jua. Baada ya miaka 350 Vatican tarehe 30 mwezi wa kumi siku ya Ijumaa mwaka 1992 waliomba dunia radhi na walimuomba mwanasayansi huyu radhi, kwa sababu ni mfumo, uwajibikaji wa pamoja. Zaidi ya miaka 350 Galileo aliombwa radhi na Vatican. Sioni kwa nini tunaona aibu Serikali kuomba radhi Watanzania kuhusu suala la madini, kwa sababu ukiangalia tangu mwaka 1994 mpaka leo hii sheria na mikataba ni uwajibikaji wa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi ukasema kwa sababu Serikali ilikuwani ya mwaka 1995 ni tofauti na Bunge hili, hata Bunge la 2015 watu walifukuzwa Bungeni huku kwenye masuala ya Sheria za Gesi pamoja na Mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kushabikia tu hapa ndani; mwaka 2002 nilikwenda Harare, tulikuwa Zimbabwe, kwenye mgogoro huu huu wa mapambano ya kiuchumi. Vita vya kiuchumi ni vibaya sana, kweli kweli! lakini lazima tuwe wakweli. Wakati wa malumbano wakaanza kusema kwamba kuna watu wengine wanaitwa wametumwa na wazungu, wengine wamefanywa nini, leo hii Zimbabwe haina hata sarafu yake, Zimbabwe imeangamia kabisa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa vita hii; na nipende kuweka wazi Kambi ya Upinzani hakuna Mbunge hata mmoja kutoka Kambi ya Upinzani anayepinga wizi wa dhahabu ya Taifa la Tanzania, hayupo. Tunaangalia maslahi mapana ya mama Tanzania na msimamo wa Kambi ya Upinzani, wezi, wizi wa rasilimali za Taifa tuzishughulikie sote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini haya yakifikiwa lazima tukubali historia tulitoka wapi, tunajifunza kwa historia na kwa kuwa sasa Serikali iliyoko madarakani imelitambua hilo, tuko tayari kabisa kabisa kushirikiana kwa hili. Tuko tayari kabisa kabisa kupambana vita hivi endapo tutaacha kuwa na propaganda za kisiasa ambazo hazilisaidii Taifa la Tanzania. Tanzania ni yetu sote, Tanzania si mali ya kikundi cha watu wachache, tubishane kwa hoja, lakini yale mambo ya msingi Mheshimiwa Waziri yenye maslahi mapana kwa Tanzania tuyazingatie sote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo leo hii tutarudi kwenye makosa yale yale ya mwaka 1997, 1998 na mwaka 1997 nilikuwa kwenye Bunge hili, mwaka 1998 nilikuwa kwenye Bunge hili, sheria zilivyoletwa wengine wakabaguliwa tutarudi back to square one. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme na nirudie tena na Watanzania watusikie vizuri kabisa, mapambano haya tuliyaanzisha na kwa kuwa wenzetu mlio wengi mmekubaliana na sisi, tuko tayari kuungana na nyie kwa sauti moja endapo tutaacha propaganda na tuwe tayari kushugulika kweli kweli tushirikishane kweli kweli kwa maslahi mapana ya Tanzania. Si mtu yeyote ajitokeze aseme kwamba hili ni langu, hili ni langu, kuna msaliti, kuna huyu, hapana! Tunatahadharisha tu and it’s better to be pro-active rather than being reactive. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tukiangamia, tunaangamia sisi sote, Watanzania wanaoumia wanaumia wote, watoto wanaokosa huduma wanakosa wote. Waliouwawa migodini haikuchagua huyu ni wa CCM huyu ni wa Upinzani, huyu ni wa nani, tuliumia sisi sote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo vita hivi vituunganishe kama Taifa la Tanzania lakini tuwe wakweli wa dhati kabisa tushirikiane, tuungane kwa pamoja, tutavusha Taifa la Tanzania. Wengine wakionekana wasaliti, wengine hapana ni wa kudandia, wengine ndiyo wenye akili zaidi kuliko wengine tunaliangamiza Taifa la Tanzania, tutarudi kama mambo ya Zimbabwe, tusiruhusu masuala ya Zimbabwe yaje Tanzania na Bara la Afrika unaona tunavyochezewa. Tuanze kufikiria zaidi miaka 10, 20, 30 ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama yale tuliyozungumza mwaka wa 1997, 1998 yangezingatiwa leo hii tungekuwa tumepiga hatua mbele.

Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini amejibu hapa, amesema hata mrahabatunaopata tofauti na kwenye dhahabu ni asilimia tatu na almasi asilimia tano na ni kwa mujibu wa Sheria na kwa mujibu wa mikataba. Sasa tuunganike sote, tuone Taifa linavyoibiwa kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo, ningependa kulitahadharisha Bunge na leo ni siku ya Ijumaa. Mtume Muhammad aliwahi kuwausia waumini wake, maarifa ni kitu chake kilichompotea muumini, popote akipatapo na akichukue. Hili suala la madini lazima Wabunge wapewe semina kwanza, kwamba uchumi wa madini ukoje, biashara ya madini ikoje. Tupewe semina kwanza tujue duniani biashara hii ikoje, tukifanya mabadiliko ya sheria kwa mhemko tulionao tutatandikwa kweli kweli kwa sababu tutafanya ni ushabiki kabla hatujajua mambo haya na tukubali huyu ana taaluma hii, huyu ana taaluma hii, tuwe na taaluma shirikishi, tushirikiane pamoja kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ili tuweze kutoka hapa, tuwe na mifumo endelevu ambayo inahimili. Leo hii yuko Rais Magufuli, kesho atakuja Rais mwingine, lakini kuna mifumo ambayo ni ya Kikatiba. Tukawa na Katiba mpya ambayo Rais yeyote yule anayekuja lazima ataheshimu katiba, sheria na taratibu, tutasonga mbele tukitoka hapa tulipo kwa sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema haya kwa nia njema kabisa kabisa. Bila kupata elimu ya kutosha ya uchumi wa madini tutapata matatizo makubwa sana na lazima tukubali kushiriki kwa pamoja tutafute suluhisho ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine, Bunge letu hili huwa tunashabikia vitu ambavyo hatuvijui, Mithali 18:13 inasema kujibu au kushangilia kabla ya kusikiliza ni upumbavu na jambo la aibu. Sasa tusije tukaanza kujishangilia, kujidhalilisha sisi wenyewe tunamdanganya nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ushabiki huu ambao unaendelea kwenye Bunge letu. Tunaona mambo ya ajabu ajabu ambayo yanaendelea kwenye Bunge letu, niombe tena chonde chonde; kwa mfano tuko kwenye viwanda viukuze uchumu wetu lakini viwanda tulikuwa navyo. Viwanda vilishabinafsishwa na kwenye zoezi la kubinafsishwa hata sisi wengine tuliumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi nimeshtakiwa Mahakama Kuu nadaiwa dola milioni moja kwa ajili ya mambo ya ubinafsishaji, Dkt. Mwakyembe anajua ile kesi ya NBC nashtakiwa mimi na wanaotushtaki ni hao hao wa upande mwingine ambao ndiyo wanashirikiana na hao kutudhalilisha kwa sababu ya kulitetea Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri nakuomba angalia sana Sekta ya Madini, angalia Uvuvi. Ukiangalia tozo zilizoko kwenye sekta ya madini, tozo zilizoko kwenye masuala ya uvuvi wa bahari kuu tukiwekeza vizuri kwenye sekta ya madini tukaondoa kodi zisizo na tija kwenye sekta ya madini, tukaondoa tozo zilizoko kwenye sekta ya madini ambazo ziko karibu kodi na tozo zaidi ya 57, tutavutia watalii kutoka milioni moja kwenda kwenye milioni mbili. Tutoke kuwa niexpensive destination hapa Tanzania utalii peke yake utaendesha uchumi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunashika nafasi ya 110 kati ya Mataifa 133 katika ushindani wa utalii na mapato ya utalii; lakini ni wa pili katika vivutio vya utalii duniani. Let us think big, let us think globally and act locally. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukubali kwamba Taifa hili tukiwekeza vizuri kwenye madini, kwa mfano hata kwenye uvuvi, bahari kuu ina kilometa za mraba 230,000; mapato gani tunayopata kwenye uvuvi? Nendeni mkasome ile na Mheshimiwa Waziri wa Fedha tulikuwa wote pamoja kwenye ile ripoti ya kutafuta vyanzo vipya vya mapato.

Sasa tuwe tunaanza mapema kutengeneza na tuwe na muendelezo wa bajeti hizi ya mwaka 2015, 2016 ninazo zote hapa 2017. Angalia hata deni la Taifa, limetoka trilioni 35, likaenda 39 leo hii ni trilioni 50.8. Tanzania tunazidi kwenda kusiko, lazima tuwe na bajeti ambazo ni endelevu kwa maslahi mapana ya Taifa la Tanzania. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, na vyanzo hivi vipya vya mapato tushirikiane sote. Kwa sababu tukisema tu deni la Taifa himilivu, watoto wetu na vizazi vijavyo vitakuja kututandika makaburi yetu viboko kwa sababu tulikuwa hatuwezi tukafikiri vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana Mwenyezi Mungu akubariki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo endelevu yanahitaji umoja wa Kitaifa (ushindi ni ushirikiano). Tarehe 21 Februari, 2018, Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) tulifanya mashauriano ya pamoja kati ya Viongozi Wakuu wa Dini na Viongozi Wakuu wa Vyama vya Siasa lengo likiwa kushauriana maudhui yaliyo kwenye lengo la 16 la Malengo Endelevu ya Dunia (Amani, Haki na Ujenzi wa Taasisi Imara). Tulikubaliana kwamba kuna umuhimu wa kuendelea na mashauriano haya kwa kushirikisha Serikali kwa kuwa mapendekezo yetu yameshafikishwa Serikalini, ni vyema mashauriano haya yakafanyika haraka iwezekanavyo kwani kuna viashiria vya wazi vya kuvunjika au kutoweka kwa amani yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, naikumbusha Serikali kwamba dunia ya leo ni meza ya mazungumzo. “Meli ya amani inazama nasi wasafiri tukiwa ndani.”
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa heshima kubwa kabisa hili ni Bunge na tukishatamka Bunge Tukufu linatakiwa lioneshe utukufu wake.
Hii si sehemu ya matusi na ukisoma Zaburi 1:1 inasema “Heri watu wale wasiokwenda katika shauri la wasio haki, wala hawakusimama katika njia ya wakosaji, wala hawaketi barazani pa watu wenye mzaha.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi tukafanya Bunge hili ni sehemu ya mzaha wakati kuna issues serious za kitaifa za kuzungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli ukishaitwa Mbunge halafu unaleta matusi ya nguoni ndani ya Bunge, si jambo la heri kabisa kwa yeyote yule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa heshima kubwa kabisa, sisi ni watu wazima, tuheshimiane, tusikilizane. Pia ukisoma Mithali 18:13 inasema:-

“Kujibu kabla ya kusikiliza ni upumbavu na jambo la aibu”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kujibu kabla ya kusikiliza ni upumbavu na jambo la aibu na hii ni Mithali 18:13. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite kwenye mchango wangu, baada ya kusema hayo, ni angalizo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wahandisi katika Taifa letu wanafanya kazi nzuri na niwapongeze sana na hasa Mhandisi au Meneja wa TANROAD wa Mkoa wa Kilimanjaro, tunashirikiana naye vizuri, anafanya kazi vizuri na tunamtia moyo na tutaendelea kufanya naye kazi vizuri. Hata hivyo, niwatahadharishe tu Wahandisi kwamba taaluma ya uhandisi duniani leo ni taaluma shirikishi. Huwezi ukajiita mimi ni engineer kwamba basi ile taaluma yako huwezi ukashirikisha wengine la hasha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na hilo kwa sababu ukiangalia adui mkubwa wa barabara leo hii ni maji; na mwaka jana nilisema tena namna gani Wizara hii inashirikiana na TAMISEMI na kutoa elimu ya kutosha namna ya uhifadhi mzuri wa barabara zetu na hasa kwenye suala la drainage system. Kwa sababu tunakubali Serikali haina fedha za kutosha kwa ajili ya maintenance ya barabara, sasa Local Government wanasafisha namna gani hii mitaro, kilimo cha matuta, mmomonyoko unavyotokea, maporomoko yanavyotokea barabara zetu zinaharibika kwa haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kilimanjaro uko kwenye mwinuko wa hali ya juu, hali ya barabara sio nzuri. Changamoto kwa wahandishi wetu, kwamba ni namna gani wanakuja na ubunifu mpya wa kupata material mpya ambayo inatumika kwenye hizi barabara badala ya kuweka kokoto zile zile au moram ya aina ile ile, lazima kuja na material nyingine labda moram mnachanganya na lime au moram mnachanganya na material mengine kwa ajili ya muda na uimara wa barabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasahau kuna barabara moja tuliomba, barabara inayoenda Kilema Hospitali ambayo ni hospitali ya wilaya. Barabara hii inahudumia watu wengi, tunaomba ipewe nafasi. Milioni mia mbili ishirini iliyopewa barabara hii kusema ukweli na ina kilomita zaidi ya 13, hazitatosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni zungumze suala la ujumla la miradi hii hasa sekta ya ujenzi. Nikizungumzia miradi ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa mfano na Dodoma nayo imeshaambukizwa na majiji mengine. Ukiangalia Master Plan ya Mkoa wa Dar es Salaam, ukizungumzia magari yaendayo mwendo kasi, Dar es Salaam Rapid Transport (BRT). Mradi ule wa Reli wa Dar es Salaam, flyovers, suala la usafiri wa majini kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo, boti ya Bagamoyo sijui imeishia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara za kutoka Dar es Salaam – Chalinze – Morogoro ambapo watu wamevunjiwa nyumba zao. Benki ya Dunia imesitisha, hakuna fidia na maumivu ni makubwa. Mambo hayo ya kujenga mambo ya namna hii si mema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upanuzi wa Julius Kambarage Nyerere International Airport, ring roads za kutawanya traffic katika Jiji la Dar es Salaam na miradi mingine mingi. Hainiingii akilini nikizungumza masuala ya majanga leo hii; mafuriko Dar es Salaam ni majanga makubwa lakini juzi tumeshuhudia pale Jangwani wanakoegesha au depot ya Dar es Salaam Rapid Transport. Serikali inawezaje ikasema watu watoke mabondeni na wao wakaenda wakawekeza pale? Future Plan iko wapi, UDA waliweza kujenga Ubungo walijenga Kurasini UDA wakati wa Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamata walijenga kule barabara ya Nyerere lakini leo hii depot ya Jangwani mafuriko yaliyotokea juzi mradi huu mkubwa uliowekezwa pale, nguvu iliyowekezwa pale, investment iliyowekezwa pale, nani anawajibika kwa kushauri ujinga huo wa depot ya Dar es Salaam Rapid Transport? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema kwa pamoja kwa sababu zaidi ya asilimia 96 ya majanga ya dunia hii yanasababishwa na binadamu. Najua Wahandisi wengine wanafanya kazi vizuri tu; lakini wanasiasa wanaingilia Wahandisi, matamko ya kisiasa; huku wamenipa kura wasibomolewe na huku hawajanipa kura wabomolewe. Sasa mambo ya namna hii, Tanzania ni yetu sote, hatuwezi kuangamia kwa ajili ya kukosa maarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia miradi hii ukisema ni ipi ya PPP, ukiangalia ni miradi ipi ya BOT ni investor gani ambaye ni makini serious investor atawekeza Dar es Salaam, huku kuna reli inayojengwa kwa standard gauge sawa tunaunga mkono itoke Dar es Salaam na isafirishe abiria kwa kasi kuleta Morogoro. Dar es Salaam Chalinze mradi huo, magari yaendayo kwa kasi, je, wanakaa pamoja na kuratibu miradi hii yote kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Dodoma imeanza tena, ukifika St. Gasper traffic imeanza, asubuhi na jioni, mvua ikinyesha Dodoma mafuriko yameanza area D na maeneo mengine. Sasa future plan yetu tuna design namna gani? Hii miradi return period yake tunaifanya kwa kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya ni majanga na ni majanga makubwa kweli kweli. Kwa mfano, ukisoma ile taarifa ya CAG na hili ni janga la kitaifa, ni janga pia la 1.5 trillion. Ukichukua majimbo yote ya uchaguzi Tanzania yako 264 ukigawanya kwa kila kilomita moja ya lami ya shilingi milioni mia saba kila jimbo la uchaguzi lingepata zaidi ya kilomita 8.12 za lami nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya ni vema tukayasimamia vizuri kwa sababu kashfa juu ya kashfa hakuna mwendelezo hakuna sustainability. Sasa sustainability haitakuwepo tukitoka kwenye ule mradi wa kutoka Dar es Salaam Bagamoyo Boat kashfa, sasa hivi kashfa nyingine ATCL, nayo tumeona matatizo yakijitokeza sasa hivi, kashfa juu ya kashfa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu, maandiko matakatifu yanasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Haya tunayoyasema; Isack Newton anasema katika kila kani mkabala kuna kani mrejeo sawa na kinyume na anasema vile kwa sababu lazima kukubali mawazo mbadala tushirikiane vizuri, tufanye kazi vizuri, kwa kuwa Tanzania ni yetu sote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tusipokuwa makini tukafuta Katiba, tukafuata sheria, tukafuata taratibu, Bunge likajua nafasi yake, a democratic principle inayosema no taxation without representation. Ndiyo maana Wabunge tuko hapa kwa ajili ya kuisimamia na kuishauri Serikali, kuangalia kodi za Watanzania zinatumika vizuri la sivyo Bunge hili litakuja kuhukumiwa kwa nini haya yanatokea kwa kiasi hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri, ukiangalia ule Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, lift pale tu ni tatizo lift. Wagonjwa wanatoka na ndege huko wananyanyuliwa na viti kana kwamba wananyanyuliwa kwenye machela wanawabeba mzoba mzoba. Watu wa nje wanatuonaje. Hilo lilinikumba mimi mwenyewe mwaka juzi tarehe 2 Disemba, mwaka juzi. Juzi tarehe 30 Ijumaa Kuu uwanja ule lift zilikuwa hazifanyi kazi. Yaani tunaonekana ni watu wa ajabu lift tu Uwanja wa Ndege wa Kimataifa hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lazima tu-think dunia wanatuonaje. Waziri with due respect, kazi yote mnayoifanya ni kazi kubwa, miaka miwili mmepewa zaidi ya trilioni tisa katika miundombinu ya nchi hii, lakini ni namna gani tunaipa kipaumbele miradi yetu ya sekta ya ujenzi, mawasiliano na uchukuzi. Kupanga ni kuchagua, sasa sisi tunapanga vipi? Kama tunasema sungura ni mdogo, basi twende kwenye idea ya concept mpaka formalization.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Serikali kwamba lazima tukubali taaluma za watu lazima ziheshimike. Pia naomba Wahandisi wasikate tamaa, waendelee kushauri vizuri na sisi wanasiasa tupate takwimu kutoka kwao ili tuweze tukazungumza na kuwasimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubongo wa mtoto ni very delicate, ili nieleweke vizuri nitatumia mfano wa yai la kuku.

Yai la kuku ukiliwekea joto stahiki utapata kifaranga, kitakuwa kuku na baadae litataga, lakini ukiwekea joto ambalo ni la juu sana yai hilo litaiva na likiiva linaliwa na itakuwa mwisho wake, lakini ukiwekea joto lingine yai hilo hilo unaweza ukariharibu au kulidumaza. Huu ni mfumo unaokufa au unaodumaa utakuwa na deterioration or stagnation katika system. Naomba tusiue au kudumaza akili za watoto wetu, lulu zetu, zawadi ya mama Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza na hilo kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba, tumeamua kupitia Wizara yetu ya Elimu kukumbatia ujinga ambao ndiyo umesababisha umaskini, maradhi, rushwa na mambo mengine katika jamii ya Tanzania. Imeandikwa kwamba watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa yaani mfumo endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema watu wanaagamia, ukichukua vitabu kwa mfano, nilikuwa nasoma hivi vitabu vilivyofanyiwa maboresho sasa. Ukisoma kitabu cha darasa la pili unaambiwa unganisha sauti za herufi, tangu lini ukaunganisha sauti za herufi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, consonant a, e, i, o, u hata kuiandika ni tatizo. Hivi vilivyofanyiwa maboresho vinavyosambazwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuimba kwenye Bunge hili, ukiangalia kitabu cha darasa la tatu cha Kiingereza vinavyosambazwa sasa kina makosa lukuki. Unawezaje ukaanza na alphabet unit ya tatu wakati unit ya kwanza unaanza na sentensi, nimetaja machache tu. Vitabu vyetu hivi havina majina ya Wahariri, vina maudhui mabovu na vinakiuka hata sheria na maadili vinaonesha ukatili, tangu lini polisi akawa ni mzungu na wanatesa watu, kwa nini vitabu hivi vilivyofanyiwa maboresho? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shule binafsi. Shule binafsi ni wadau muhimu sana katika elimu ya Taifa letu la Tanzania. Wengi wetu ni zao la shule binafsi hata Marais wastaafu Mzee Nyerere, Kikwete, Mkapa na Rais wa sasa Magufuli ni zao la shule binafsi na hasa mashirika ya dini. Mimi mwenyewe ni-declare ni zao la hizi shule binafsi. Leo hii kama siyo shule binafsi tuorodheshwe Wabunge humu ndani ya Bunge wangekuwa kwenye hali ya namna gani? Shule binafsi nyingi hata zilizotaifishwa kwa mfano shule ya Pugu, Ihungo, Umbwe, Peramiho, Masasi, Minaki, Weruweru, Kilakala nitaje chache tu na vyuo vya ualimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kilimanjaro una shule 314, mwaka jana kidato cha nne wamekuwa wa kwanza Kitaifa niwapongeze sana, niipongeze shule ya Anuarite ambayo ipo Jimboni Vunjo ambayo imekuwa ni shule ya tano kati ya shule kumi bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikopo ya vyuo vikuu inakuwa na ubaguzi wa hali ya juu sana. Ninapende kuuliza na Serikali inijibu vizuri student unit cost mfano mwanafunzi anayesoma Shahada ya Kwanza ya Udaktari pale KCMC Serikali inachangia kiasi gani na mzazi/mwanafunzi anachangia kiasi gani. TCU inalazimisha chuo kile waweze kuchangia shilingi 3,100,000; je, vyuo vingine vya tiba wanachangia kiasi gani ili kuwe na standard ambayo inaeleweka badala ya kupiga huku na kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matatizo mengi, Mzee Nyerere amesema nina kitabu chake hapa na nimesoma, ukisoma hotuba ya Mwalimu Nyerere ya mwaka 1967 anasema elimu yoyote iwe ya darasani au isiyo ya darasani ina shabaha yake, shabaha yenyewe ni kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine maarifa na mila za Taifa kwa kuandaa vijana wake tayari kuchukua nafasi zao katika kulitumikia na kuliendeleza Taifa. Mzee Mkapa amesema elimu yetu tunahitaji mjadala wa Kitaifa na Mzee Kikwete naye ametamka, nani atamke zaidi mpaka tuhakikishe kwamba tunaangamiza elimu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme the way forward, tukubali elimu yetu tupo kwenye janga ni maafa na ukiwa na maafa naomba tusiwe na tofauti za kiitikadi humu ndani, tusimame sote kwa pamoja na Mheshimiwa Waziri yote tunayoyasema uyachukulie very positive kwa ajili ya kujenga Taifa, Wizara, watoto wetu na kizazi chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu tuwe na mjadala mpana wa Kitaifa, hata urejee hoja yangu niliyoitoa humu Bungeni ya tarehe 31 mwaka 2013. Mjadala huu tukiwa nao tuwe na matokeo ya muda mfupi, kwa mfano matokeo ya muda mfupi.

Kuhusu shule binafsi kwa nini Wizara ya Fedha ianze kwenda kwenye majengo, mabwalo, mabweni, kumbi, waanze kutoza kodi ya majengo, kodi za ardhi na viwanja vya michezo. Hilo wala halihitaji mjadala ni suala la muda mfupi jadilini Serikalini ondoa zote wala usijadili, ada za mitihani ondoa wala msijadili masuala kama haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chonde chonde suala la kusimamia ubora wa elimu Tanzania, tuwe na chombo kimoja cha kusimamia standard ya elimu Tanzania na hili lisichukue muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunaihitaji dunia kuliko dunia inavyoihitaji Tanzania, tupende tusipende. Tuone kwa wenzetu karne hii ya sayansi na teknolojia, sayansi ni maarifa na teknolojia ni namna gani ya kutumia ya kutumia yale maarifa, duniani wenzetu wanafanya nini ili tuweze tukaondoka hapa Tanzania badala ya kila siku kulia. Lengo la nne la maendeleo endelevu ya dunia linasema elimu shirikishi, sawa, bora kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni miundombinu ya binadamu, ukombozi wa mtoto wa kike ni elimu, lakini nimefanya utafiti miaka ya 1978 ndiyo tatizo la lishe lilianza Tanzania kwa kasi kubwa na zaidi ya asilimia 42 ya Watanzania walikuwa na tatizo la lishe kwenye shule zetu. Kwa hiyo, kunakuwa na intellectual disability ya hali ya juu sana. Unaweza kuona labda hata wengi walio madaktari, wahandisi na hata miongoni mwetu miaka ya 1978 hiyo hatujapata lishe vizuri labda ndiyo maana tunashindwa kufanya maamuzi yaliyo sahihi katika mazingira ya ajabu tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba chonde chonde walemavu wetu, kuna shule ya walemavu pale Moshi ya Kanisa Katoliki ipo Kimashuku ambapo Kanisa Katoliki wanajenga shule nzuri tu pale lakini wamewekewa vikwazo kwa kuwekewa vigezo vingi na ni shule kwa ajili ya walemavu, sasa tunafanya mambo gani ya namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisema kwa uangalifu kabisa, unajua Mzee Mwinyi alinifundisha namna ya kuhifadhi. Kwa mfano, nilivyosoma darasa la kwanza, Sister Benedicta na Sister Protasia walikuwa wananifundisha wananiambia ukitaka kumjua Yesu ni kujua elimu na tulikuwa tunaimba hivi tunasema: “Wa rohoni ndiye mwalimu kwake ni hunifumbulia, kukujua nipe elimu, Yesu mwema nijalie, eeh Yesu wataka nikupende.” Yaani mwanafunzi unahifadhi kwa sababu ya ubongo wa mtoto na unajua umuhimu wa elimu katika Taifa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtume Muhamad anasema nini ukitaka akhera usome, ukitaka dunia usome, elimu ni kitu chake kilichompotea muislam popote akipatapo na akichukue. Baba Askofu Mstaafu Dkt. Shoo anatuambia hivi: “Matendo yetu mema tunayoyafanya hapa duniani ni sauti huru na hai miili yetu ikiwa kaburini.” Leo hii tunamsikiliza sana Baba wa Taifa yupo kaburini lakini kazi nzuri aliyoifanya ya elimu kwa Taifa letu. Sasa nani tena aseme ili tuweze tukaelewa (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaishauri Wizara chonde chonde, hapa tulipofika sasa kwa nini tusifundishe watoto wetu; “a, e, i, o, u hizi ni herufi kuu, tamka kwa sauti kuu, ndiyo a, e, i, o, u; na jicho eee, kama mpira ooo, ni kikombe uuu” tunakuwa very focused ili watoto wetu na bongo zao zilivyo delicate waweze kuelewa badala ya kuwarundikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, michezo na sanaa kwa sababu ya muda nitashindwa kurudia. Michezo na sanaa mtoto wa darasa la kwanza michezo na sanaa unamsaidia nini kwenye KKK! Anatakiwa kusoma, kuhesabu na kuandika. Sasa unamrundikia masomo yote na vitabu vyote hivi, huyu mtoto atafanyaje? Tumesema mara nyingi, angalia sera hii ya elimu ya mwaka 2014 iliyozinduliwa na Rais Kikwete ile siku ya Ijumaa tarehe 16 Februari, 2015 yapo mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachopenda kuomba baada ya kuizindua hii Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 haviendani vitu hivi. Sasa haya mambo ya kushindana huku shule binafsi huku hivi hapana. Hebu tuje pamoja kama Taifa na rai yangu kwa Bunge hili kwenye suala la elimu tuondoe itikadi... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, elimu shirikishi na endelevu ni muhimu kwa wananchi juu ya namna bora ya kuvuna, kutawala na kutumia maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naambatisha maombi ya mahitaji ya maji katika Jimbo la Vunjo yaliyofanyiwa uchambuzi wa kitalaamu. Mahitaji haya ni vijiji vipatavyo 37.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwanza nianze kabisa kusema kwamba naunga mkono taarifa ya Kamati, hii taarifa ni nzuri sana na imewasilishwa kitaalamu kweli kweli, niwapongeze Wanakamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utalii atika Taifa letu, kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2012 mpaka 2015/2016 utalii ulikuwa unakuwa kwa takribani asilimia 13.98 lakini mwaka 2016/2017 utalii umeshuka mpaka asilimia 3.3. Hii inatokana na kutokutekelezwa kwa sheria, matamko ya ajabu ajabu, kutokutabilika kwa kodi, sijui tunaenda wapi? Kwa sababu utalii 2013/2014 ulikuwa umekuwa kwa asilimia 17.5 na mwaka huu wanasema asilimia 17 lakini Serikali hii ilisema utalii ifikapo 2020 utakuwa umekuwa kwa asilimia 30 lakini badala yake umeshuka mpaka asilimia 3.3; kulikoni Serikali ya Awamu ya Tano? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mazingira rafiki ya utalii; nilishawahi kusema tena hapa na narudia, Tanzania tunahitaji dunia kuliko dunia inavyoihitaji Tanzania. Ukiangalia kodi katika sekta ya utalii ziko zaidi ya 57, lakini kodi hizi kila kukicha kodi. Dubai juzi wametangaza ufutaji wa kodi kwenye sekta ya utalii na pia wanatoa viza kwa foreigners kwa zaidi ya miaka kumi katika ku-invest seriously kwenye utalii, lakini hapa kwetu kutoa kibali cha foreigner kwenye utalii ni dola 4,000 na ni kwa miaka miwili mpaka miaka minne. Sasa kupanga ni kuchagua, je vivutio vya utalii tunavifanyaje?

Mheshimiwa Spika, Mapato Yanayotokana na Utalii. Kati ya fedha zinazopatikana kutokana na utalii, na Waziri wa fedha alikuwa hapa; kwa mfano takribani dola za Kimarekani bilioni 10 utalii peke yake inachangia asilimia 25 takribani dola za Kimarekani bilioni 2.3, inafutiwa na bandari transit goods bilioni mbili, dhahabu bilioni 1.6. Kwa hivyo hawa giant watatu ni zaidi ya asilimia 61 ya mapato yote ya fedha za kigeni. Tanzania miaka miwili, mitatu iliyopita tulikuwa wa pili kwa vivutio vya utalii duniani kati ya nchi 133, lakini kwenye miundombinu ya utalii tunashika nafasi ya 110 kati ya nchi 133.

Mheshimiwa Spika, sasa utalii maana yake ni nini? Tutafikiaje watalii 8,000,000? Kwa mfano utafiti ulikuwa umefanyika, lazima tuwekeze kwenye miundombinu ya utalii, lazima tuwekeze seriously na tuamue kwamba kwenye sekta hii ya utalii, kwa sababu kwa mfano TANAPA leo hii, Ngorongoro na wale wengine wote. Inakuwaje Serikali inachangia Mfuko Mkuu wa Serikali na Serikali hiyo hiyo inachukua corporate tax kwenye mashirika?

Mheshimiwa Spika, kwa mfano fedha ambazo zimepatikana TANAPA kwa mwaka 2017/2018 zilikuwa ni takribani shilingi bilioni 214, Ngorongoro yenyewe ni shilingi bilioni 104. Mwaka huu tunategemea TANAPA yenyewe wapatikane shilingi bilioni 292.8 Ngorongoro shilingi bilioni 156. Sasa lakini miundombinu ya utalii ipo hoi bin taabani.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia huwezi ukatangaza, Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake amesema wameweka mpango mkakati wa TBC kutangaza utalii. TBC itamtangazia nani duniani? Ningetaka nisikie kwamba katika kutangaza huku, mashirika kama CNN, BBC, Voice of America, Aljazeera, India, China, Sky News na mengineyo mengi ndio wanaotangaza utalii. Utafiti umeonesha tukiwekeza vizuri kwenye utalii, kwa miaka mitatu/minne tutakuwa tunapata dola za Kimarekani bilioni 16.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwa kiasi kikubwa kwa mfano TANAPA kati ya hifadhi 16 hifadhi tano zinatoka Serengeti, Mlima wa Kilimanjaro, Tarangire, Manyara, Arusha. Kwa miaka kumi mfululizo kwa mfano, Mlima wa Kilimanjaro peke yake uliliingizia taifa hili fedha shilingi bilioni 471.5; uendeshaji ulikuwa shilingi bilioni 67.5 miradi katika vijiji ambavyo vinazunguka mlima huo ambavyo vilikuwa 88 zilikuwa shilingi bilioni 8.2 ambayo chini ya asilimia 0.48 ilhali sera inasema ni asilimia 7.5. Tukiendelea namna hii ni kwamba tunaua utalii wetu sisi wenyewe.

Mheshimiwa Spika, utalii Kaskazini kwa mfano, kuna tamko lililotolewa kwamba watu wa Kaskazini wasubiri kwanza, nilisema eeh Mwenyezi Mungu atujaalie, nilitumia Zaburi ya 141:3. Nilisema Mwenyezi Mungu awasaidie viongozi wa Taifa hili walinde vinywa vyao na awe mngojezi pa midomo mwao kabla hawajatamka. Huwezi ukaligawa taifa kwa kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fedha za kigeni asilimia 25 zinatoka Kaskazini au zaidi ya asilimia 98 zinatoka Kaskazini. Nakubali Ruaha na sekta nyingine zote lakini kwenye classification theory ya kawaida tu, aliye class A unaendelea ku-maintain kubaki class A wakati unamnyanyua na huyu mwengine aweze kufika class A. Huwezi ukasema kwamba huyu wa class A unamwambia stop, unamshusha tuu aende chini, thinking ya wapi hii?

Mheshimiwa Spika, kweli nimeshangaa sana, Taifa hili ni moja na ndiyo maana Mathayo 5:9 wanasema heri wapatanishi wanakuwa wana wa Mungu. Tunakuwa ni kitu kimoja, roho ya umoja Baba wa Taifa uliyoijenga ndani ya Taifa hili, Taifa hili ni moja. Watu wengine wa kutoka Kaskazini sasa hivi wanaanza kuonekana kama si watu wa Tanzania, hapana. Mama tibaijuka ameongea vizuri, yaani tumeanza kugawana kwa misingi ya kikabila, ukanda, taifa letiu linakwenda wapi? Tanzania ni yetu sote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusipoangalia tunakokwenda; nilisoma Kumbukumbu ya Yoshua bin Sira leo asubuhi, anasema kama huna macho yaani huna mboni ya jicho basi huwezi kuona na kama huna ufahamu huwezi kuwa na hekima. Wimbo wetu wa Taifa unazungumzia hekima, umoja na amani, ni rai yangu kwa viongozi wa taifa hili wazingatie wimbo wa taifa kwenye ile hekima, umoja na amani ili tuweze kukuza utalii vizuri ndani ya Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hoteli za Tanzania ziko hoi, nimeangalia hotuba ya mwaka jana inaonesha idadi ya hoteli tulizokuwa nazo na huduma za hoteli ziko 1,424 vitanda 35,000 ambapo ni sawa sawa tu na vilivyopo mji wa Mombasa peke yake. Sasa tunasisitiza kukuza utalii hapa kwetu, lakini tunapoanza kusema angalia ufukwe wa Bahari ya Hindi una kilometa 1,424. Serengeti peke ake ina kilometa za mraba 14,750 Masai Mara ina 1,510 ambayo inaingia mara kumi ndani ya Serengeti, lakini Masai Mara inashindana na hizi 14,750, tunafikiriaje sisi? Lazima tufikiri seriously.

Mheshimiwa Spika, suala la vigingi, nilienda kule Ngarenanyuki na Momela. Hiyo bila hata ya ubishi wowote. Nimekwenda binafsi mpaka Makanisa ya KKKT yamefungiwa ndani, shule zimefungiwa ndani, watu wamepigwa makanisani, mambo gani haya? Nchi hii ya utawala wa sheria?

Mheshimiwa Spika, na mwaka huu tunatimiza miaka 70 ya tamko la ulimwengu na haki za binadamu ambalo lilianzishwa tarehe 10/12/1948 siku ya Ijumaa, lakini mpaka sasa miaka 70 tunapiga watu mpaka tunaingilia kwenye makanisa wanakosali Jumapili!

Mheshimiwa Spika, nilikwenda mwenyewe Momela mpaka wazee wanajificha ndani ya kanisa ndiko wanatupa chakula kule Ngarananyuki? How? Why? This is not possible.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani ndani ya nchi hii hiii? Halafu Serikali iko kimya kwenye ukiukaji huu mkubwa? Ndiyo maana Tanzania leo hii tunashika nafasi ya 153 kati ya nchi 156 kwenye happiness index, yaani sisi tuko na Burundi, tuko na Yemeni tuko na wapi huku, si unajua, hata Somalia wametupita kwenye ukiukwaji wa haki za binadamu. How? Nchi gani? With due respect hapana hatuwezi tukakubali, Taifa hili tuwekeze akili zetu vizuri, tuangalie tunataka kufanya nini.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye miundombinu kwa nini tusiwakubalie ngugu zetu wa TANAPA na wengine wote, Ngorongoro na wengine, badala ya ule mfuko wa kuweka Serikali Kuu, japo ipo kwa mujibu wa sheria? Tuwekeze kwenye miundombinu ya utalii, miaka miwili, mitatu, minne, mitano, ijayo tayari tuna-double tunachopata au mara tatu; utafiti wa World Bank wamesema ni dola za Kimarekani bilioni 16 kama tukiwekeza vizuri.

Mheshimiwa Spika, mbuga nyingine za Ruaha, Katavi, kote huko tuzinyanyue lakini zinyanyuke kwa Serikali kukiri kuwekeza vizuri. Tukiwekeza kwenye utalii vizuri ndani ya Taifa hili litatoka, angalia hata kwenye ajira, utalii peke yake ni direct ni ajira zaidi ya 500,000 kati ya ajira 2,500,000.

Mheshimiwa Spika, sasa kila siku tunasuasua tunaongea lungha hii hii kwa nini hatufanyi maamuzi? Kwa nini hatukubari kwamba Tanzania yetu hii Mwenyezi Mungu alivyotujaalia Tanzania hii ilivyo nzuri, kwa mfano pale kwetu, ninakotokea, Jimbo la Vunjo, lango kuu la kuingia Mlima Kilimanjaro, kwa miaka kumi yale mapato ambayo yamepatikana pale, ukiangalia vile vijiji viko hoi bin taabani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna chuki imejengeka kati ya askari wa kulinda mbuga na raia. Kwa mfano vijiji vya Mshiri, Kijiji cha lyasongoro, vijiji vyote ambavyo vinazunguka, Kirie kote huku wanaonekana kama ni adui badala ya kuwa ni rafiki; na haya ni matatizo ya chuki tuu zinazojengwa. Sasa tujenge mahusiano yaliyo mema na yawe mema kweli kweli.

Mheshimiwa Spika, tulikwenda huko na Naibu Waziri wa Utalii kabla hajabadilishwa akaona matukio ya utesaji wa hali ya juu. Sasa naamini TANAPA, General ni mtu makini sana lakini nadhani kuna vurugu zinaingilia katikati ambazo si nzuri. Tutumie lugha iliyo nzuri ili tuhakikishe haya yote tuliyonayo ni kwa maslai mapana ya mama Tanzania ambayo ni yetu sote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupanga ni kuchagua, wenzetu wa Kenya ukiangalia walivyowekeza, ukisoma hata kwenye website, nilikuwa nasoma leo asubuhi, kwa miaka mitano ijayo utaona wanataka wafikie wapi kwenye utalii utaona hapa kwetu tunasuasua, ni blaa blaa tu tunafanya.

Mheshimiwa Spika, tuiwezeshe Wizara kwa mfano, Wizara imeomba bajeti hapa shilingi bilioni 115, lakini ukiangalia mapato tuu yanayotokana haya maduhuli yanayotiokana Wizara inayochangia ni shilingi bilioni 623.5.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, Mwenyezi Mungu akubariki sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami nichangie Taarifa ya Kamati mbili zilizoko mbele ya Bunge letu. Nitaanza tu kwa kukumbusha wajibu wetu sisi Wabunge. Wakati wa Taarifa za Kamati Bunge wajibu wake namba moja ni yale majukumu kwa Taifa; tunaacha tofauti zetu nyingine zote; na ndiyo wajibu wa kuisimamia Serikali vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taarifa ya Kamati ya Miundombinu, mimi ni Mjumbe. Taarifa yetu tunazungumzia kuhusu suala la bandari. Ukiangalia bandari zetu hasa Dar es Salaam na wale wengine wote wanaosimamia, kwenye maoni yetu ya Kamati tumeeleza namna gani ilivyo bora watu wetu kupata elimu au weledi katika Mataifa mbalimbali. Sasa nilikuwa najaribu kuangalia kwetu sisi Tanzania ambao kati ya nchi 38 za Afrika ambazo wana bandari, Tanzania tupo kwenye hali gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari zetu; nasisitiza, bandari zetu tukijilinganisha na bandari nyingine Afrika, Bandari za Egypt katika mambo ya Container Terminal ina uwezo wa container 2,900,000, Durban 2,600,000, Tangier Morocco 2,500,000 na Dar es Salaam 501,000. Kwenye mizigo, Bandari ya South Africa ni tani milioni 72, Mombasa tani milioni 31, Dar es Salaam tani 13,800,000 kwa mwaka. Ukiangalia kwenye region yetu hii, East Africa yote na Central Africa, Mombasa ndiyo wanaongoza. Sasa hapa ni kwa nini tunafikia kwenye hali hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasema kwa nini tumefikia kwenye hali hii, hebu tuangalie hapa Tanzania uwezo wetu wa forex. Utalii kwa takwimu za Benki Kuu za mwezi Novemba ni bilioni 2.4, asilimia 28; dhahabu, US Dollars bilioni 1.5, asilimia 17.6; bandari, transit goods, bilioni 1.23, asilimia 14.5; mazao yote ya kilimo ni dola milioni 883 ambayo ni asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia bandari yetu ambalo ndilo lango kuu la uchumi, ambapo tunategemewa na Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, DRC Congo, Malawi, hata mpaka na Sudan; uwezo wa bandari yetu huwezi ukasema unawekeza, lazima ziende sambamba. Bandari na reli lazima ziendane sambamba, upende usipende. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkakati wa bandari na iko kwenye Taarifa ya Kamati yetu, huwezi ukaweka vinginevyo kabla hujaangalia mzigo mkubwa wa bandari unapatikana wapi? Kwa hiyo, kipaumbele cha kiuchumi lazima kabisa bila kumung’unya maneno lazima tungewekeza kwenye tawi la Tabora, Kigoma, Uvinza na Msogati. Ambapo sasa ukiunganisha na bandari yetu ya Dar es Salaam ndiyo unaweza ukasema sasa hapa uchumi wako unaenda barabara, badala ya kuanza mambo mengine labda ya kisiasa na mambo ya namna ambayo hayawezekani kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nazungumzia bandari? Sisi ukanda wetu una urefu wa kilometa za bahari 1,424 na strategically tungetumia bandari yetu tu, forex ambayo mwaka jana, kwa takwimu za BoT, dola bilioni 8.5 tungezipata zote kutoka Bandari ya Dar es Salaam. Leo hii Bandari ya Dar es Salaam kama tulivyosema hapa ni asilimia 14 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijui tunafikiriaje? Lazima tuangalie hata washindani wetu wa Afrika, wakati sisi tunazungumzia mambo ya 20 equivalent units za mambo ya container, ukizungumzia Shanghai peke yake ni zaidi ya milioni 40 wakati sisi ni 501,000. Sasa radical change katika uchumi itakuwaje kama hatuwezi tuka-think globally na tukauza dhahabu in lacal solution? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kuangalia bandari za Afrika. Kuanzia South Africa mpaka Na. 13, unaenda South Africa, unaenda Egypt, Nigeria, Morocco, Algeria, Congo, Kenya, Ivory Coast, mpaka Na. 13 wala huioni Tanzania tuko wapi? Sisi tuko hoi bin taaban. Kwenye mizigo kwa mwaka ni tani milioni 13.8.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuwekeza vizuri katika Bandari ya Dar es Salaam kwenye wharfage badala ya Serikali au Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa maana ya Hazina kuchukua zaidi ya bilioni 400 wangewaachia bandari wawekeze serious kwenye bandari ili bandari zetu ziweze kuwa na nguvu za kutosha katika kutekeleza wajibu wake. Vile vile tumezungumzia bandari za nchi kavu miaka nenda rudi, miaka nenda rudi, songa, panda hivi and so forth, waende wakajifunze duniani wanafanyaje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia bandari nizungumzie kidogo barabara za Jiji la Dar es Salaam, barabara za Jiji la Dar es Salaam ni zaidi ya miaka kumi sasa na iko ukurasa wa 38, tumezungumzia suala la muda unaopotea barabarani, suala la mafuta, suala la msongo wa mawazo (stress) na suala la uchafuzi wa mazingira. Tulipozungumzia Dar es Salaam mpaka nakumbuka taarifa ya Chenge one na mkakati tufanye nini? Tukaja na mawazo na Serikali ikaja na MV Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirisha watu kwa njia ya maji, naomba niiulize Serikali leo MV Dar es Salaam ipo wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ingesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa msongamano katika Jiji la Dar es Salaam na ingesaidia kuzuia uchafuzi wa mazingira na muda wa kufanya kazi ambapo kila siku msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam unagharimu Taifa hili zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni nne kwa utafiti uliofanyika takribani miaka kumi iliyopita tangu mwaka 2009. Sasa Mheshimiwa Januari Makamba na mkakati wake wa mazingira na nini ile MV Dar es Salaam ipo wapi? Ili iweze kufanya kazi kwa mujibu na taratibu zinazosaidia, ni Serikali hiyo hiyo moja. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila utaratibu)

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ipo Dar es Salaam sawa kama ipo wapi basi tuhakikishe kwa sababu gani? Usafiri ulio rahisi kuliko mwingine wowote na unarahisisha ni usafiri wa majini na utasaidia katika mikakati ya namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusu barabara zetu ambazo nimezungumzia za Dar es salaam lazima kuwepo na mkakati madhubuti zile by pass, flyovers kuahakikisha tunaondoa na kuwekeza kwelikweli kwa sababu pale ndiyo lango kuu la uchumi ndiyo uchumi wetu zaidi mapato yetu ndani asilimia karibu takribani 80 tunapata katika Jiji la Dar es Salaam sasa either you like or not lazima tufanye hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la hizi barabara ambazo zinasaidia katika maendeo mbalimbali huwezi katika karne hii tukaanza kuzungumzia kabla hatujaunganisha barabara za Mikoa ya Katavi - Kigoma, Katavi - Tabora, Kigoma - Kagera, Njombe - Makete na Mbeya kwa pamoja ili kuhakikisha nchi nzima miji yote mikuu imeunganishwa kwa barabara za lami na ni sera ya Serikali kuhakikisha kipaumbele kinawekwa kwenye barabara zote kwenye miji yote mikuu kuhakikisha imeunganishwa kwa lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nizungumzie kidogo kuhusu Kamati ya Viwanda na Biashara, ule ukurasa wa 80 ambao unazungumzia mazingira ya kufanya biashara yaliyo rafiki, tukiri kwamba private sector ni engine ya uchumi wetu, lakini leo hii mazingira ya wafanyabiashara na Kamati imeandika hapa katika ukurasa wa 80 yamekuwa ni magumu kwelikweli na yamekuwa ya hofu. Sasa tutapata wapi fedha kama tunafanya wafanyabiashara ni washindani wa Serikali, badala ya Serikali kuwawezesha wafanyabiashara kujenga mazingira rafiki ya kikodi, kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji, kujenga mazingira rafiki na wakitoa kauli watoe kauli, kwa mfano, niulize lile suala la refundable, zile fedha billion 32 kwenye viwanda vya sukari hasa viwanda vya soda, mbona hawajarudishiwa kodi yao? Naomba warudishiwe fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maduka ya fedha za kigeni Mkoa wa Arusha amesema Mheshimiwa Lema hapa yapo kwenye hali mbaya na zile fedha zao mlizochukua Benki Kuu muda umetosha, warudishiwe fedha zao immediately ili wafanyabiashara hawa waweze kuendelea kufanya shughuli zao, kama wana makosa waelezwe hayo makosa na kama wameshafanya ukaguzi wao wazirudishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Arusha katika uchumi, utalii, tumekubaliana hapa forex kwenye utalii ni zaidi dollar billion 2.4 ambayo ni sawa na asilimia 28 ya fedha zote za forex ni za utalii na Jiji la Arusha ni la utalii. Sasa forex mnafunga, sasa tumlilie nani na watu wafanye nini? Sasa kama tukifanya maamuzi ya namna hii ya kupararazi forex katika Jiji la Arusha ambayo ndiyo radical change, this is very unfortunately. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe kwamba wakati wa Kamati za Bajeti kama zinarudia kwa sababu wa muda, sisi Wabunge jukumu letu namba moja ni kuhisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi, kwa sababu sisi tumekuja hapa ili kuweza kusimamia kodi za wananchi, sisi tumekuja hapa kwa ajili ya wananchi ambao ni walipakodi, wajibu wetu namba moja ni kuisimamia Serikali, kuishauri Serikali, kuweka kando tofauti ya vyama vyetu vya siasa ili kuona Taifa letu linapewa kipaumbele na wajibu wa Mbunge namba moja ni kwa Taifa lake, Taifa lake, Taifa lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna ubishi leo hii huu ukurasa wa 80, unasema mazingira ya kufanya biashara yamekuwa magumu na ugumu huo kwa kiasi kikubwa unasababishwa na uwekezaji wa Sheria mbaya za kodi na kwa kuwa hali hiyo imepelekea baadhi ya wafanyabiashara kuendelea kufunga biashara zao ambao hali hii haitoi tafsira nzuri kwa ustawi wa Tanzania, lakini pia wawekezaji nchini. Sasa niiombe Serikali na niishauri kwa nia ya dhati kabisa, mkinena maneno myasimamie maneno yenu, mkisema ni mazingira rafiki, kweli yaonekane rafiki, kama ni kodi kwenye biashara kwa mfano kwenye utalii kuna kodi zaidi 50, yatakuwaje mazingira rafiki na mazingira wezeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihitimishe kwa kusema na kuomba tena chonde chonde, tujaribu kuangalia tusiangalie humu ndani tukapongezana humu Tanzania, tujiangalie Afrika tupo kwenye position gani? Kidunia tuko kwenye position gani, elimu ya teknolojia dunia hii na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani sisi tuko kwenye position gani? Tukiweza ku-think global and have a local solution, naamini tutafanya radical change kuondoa hali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi na mimi nitoe mawazo yangu kwenye hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa leo ni Sokoine Day, alikuwa kiongozi mashuhuri kwa Taifa letu, ni siku ya kumkumbuka miaka 35. Mwenyezi Mungu amrehemu na tutekeleze yale mema aliyofanya kwa Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraharaka nianze na TARURA. Nimpongeze Mtendaji Mkuu wa TARURA kwa kazi nzuri kubwa anyoifanya kwa Taifa letu na TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Moshi wanafanya kazi nzuri. Nachowakumbusha tu ni ahadi za Mheshimiwa Rais kwa barabara za Himo Mjini pamoja na barabara ya Kilema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Vunjo lina barabara zenye kilometa 389.3, TARURA walifanya kazi hii ya kupima, nawapongeza sana, wakishirikiana na Vunjo Development Foundation (VDF) na barabara hizi zitagharimu shilingi bilioni 12.7, wananchi wameanza kuchanga wenyewe, Mbunge nimenunua mashine, Serikali imeahidi kutoa shilingi milioni 200 kwenye mradi huu kwenye barabara walizoweka kwenye kitabu, naipongeza Serikali. Hata hivyo, shilingi milioni 200 kati ya shilingi bilioni 12.7, naomba waongeze fedha hizi. Waliotengewa shilingi milioni 200 ni barabara ya Chekereni - Kahe ambayo tunashukuru lakini ni kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni elimu msingi, nimeuliza swali asubuhi, naomba tu kujua na tulitendee Taifa haki, hapa tuna Sera ya Elimu na inafafanua vizuri maudhui ya Sera ya Elimu na elimu msingi ni ipi na elimu sekondari ni ipi. Je, Taifa hili leo hii linaongozwa na Sera ipi ya Elimu kuandaa Taifa kwa miaka 30, 40 au 50 ijayo? Nitazungumzia zaidi wakati wa bajeti ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongele kuhusu ikama ya watumishi. Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kuna upungufu wa walimu 379, shule zingine zina walimu wawili, watatu na sekta ya afya pia ina matatizo makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tuko na wenzetu wenye albinism, niwapongeze kwa kazi nzuri wanayoifanya na mwaka huu ni wa kudumisha, kutetea na kulinda utu, heshima na mahitaji msingi ya watu wenye ulemavu. Nikiangalia bajeti iliyoletwa hapa bado walemavu wetu hatujaweza kuwaweka kwenye hali ya utu wao, heshima yao na mahitaji msingi yao ili na wao wajione ni binadamu. Sisi ambao tunajiona tuna akili nzuri na tumekamilika tunawaita walemavu lakini kwa kiasi kikubwa ukiangalia sisi tunaowaita walemavu ulemavu wetu wa fikra ni mkubwa kuliko ulemavu wao wa viungo vya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimponge sana Dkt. Reginald Mengi na Taasisi yake ya kutetea na kukuza utu wa walemavu. Dkt. Mengi anafanya kazi nzuri sana na niiombe Serikali imuunge mkono. Tulikuwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais tarehe 17 mwezi uliopita na Naibu Waziri, dada yangu Mheshimiwa Stella Ikupa katika shughuli ya kuwajengea utu walemavu, kwa hiyo wapewe nafasi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa kwenye mkutano wa Dkt. Martin Fatael Shao, Askofu Mstaafu naye amefanya utafiti kwenye sekta ya afya na watoto na imeonekana shule zetu haziko vizuri. Kwa kuwa nina ripoti yake hapa, nampongeza Askofu huyu kwa kazi nzuri anayofanya kwa walemavu, shule za msingi, elimu ya afya na kitabu hiki nitakiweka Mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka niingie kwenye utawala bora. Ndugu Isaac Newton anasema katika kila kanimkabala kuna kani iliyo mrejeo sawa na kinyume. Viongozi wowote wale hawaokotwi kwenye majalala viongozi huandaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1995 wewe ulikuwepo Bungeni, alikuwepo Mheshimiwa Mzee Lubeleje, Mheshimiwa Ndassa na Mheshimiwa James Mbatia kati ya Wabunge wote waliopo sasa, tulikuwa wanne. Wakati huo tulivyokuwa Bungeni ukiwa Mwanasheria Mkuu viongozi waliandaliwa kwa kupewa semina na kuelezwa jukumu la kwanza la Mbunge ni kwa Taifa lake; la pili kwa Jimbo lake la Uchaguzi; la tatu kwa chama chake cha siasa; na la nne kwa dhamira yake binafsi. Sasa hapa Bungeni leo hii watu wanachukulia mambo personal kana kwamba issues ni personal, sisi tunapita tu, tuijenge nchi yetu, wanasema great minds discuss ideas, Taifa hili ni letu sote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilibahatika kuongea na Mheshimiwa Rais kwa mapana sana tu tukakubaliana Taifa hili likiharibika au likienda mrama tunaangamia sisi sote, halichagui huyu ni wa chama gani, kwa hivyo, tuitazame nchi yetu. Let us think positive and big, let us think big yaani tufikiri kwa mapana tu, nchi yetu miaka 50 itakuwa kwenye hali gani. Kapteni Mstaafu Mheshimiwa Mkuchika unakumbuka mwaka 1992, 1995 ukiwa DC wa Ilala wakati tunaanzisha mfumo wa vyama vingi tulikuwa tunakuja ofisini kwako, tulikuwa tunaongea tuwe na Taifa gani baada ya miaka 25, miaka 30 ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nimesema hayo? Nimesema hayo kwa sababu nimeisoma hotuba ya Mheshimiwa Kapteni Mheshimiwa Mkuchika, ukiangalia Taasisi ya Kupambana na Rushwa kazi walizonazo hapa ni zaidi ya 10 au 15 kama sijakosea lakini ukiangalia bajeti yao ni ndogo kweli kuweza kuzama mpaka chini. Kauli mbiu ya taasisi hii nilikuwa nao wiki iliyopita kwenye semina na dada yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, Naibu Waziri pale TAKUKURU, tulitoa rai, huwezi ukasema unazuia, unapambana halafu ndiyo unaelimisha, hapana. Nilitoa rai siku ile kwamba tuanze na kuelimisha kwanza madhara ya rushwa. Tukishaelimisha ndiyo tutaenda sasa na hayo mengine ya kuzuia na kupambana, tuelimishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusiseme hapa kwamba kesi ziko 476 na nyingine zinaongezeka tujenge mazingira kesi zipungue zaidi kwa sababu ya watu kujua madhara na kujielimisha zaidi badala ya kufikiri kwamba zitaongezeka.tuwekeze kwenye kuondoa maovu zaidi kwenye jamii badala ya kufikiria maovu yataongezeka kwenye jamii. Hii ni namna ya jamii kujitambua na kwa moyo wa dhati kabisa nimpongeze CP Diwani Athumani na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuweza kupambana na rushwa katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hii ukiangalia kwenye uongozi baada ya rushwa, unaona wamepewa majukumu nane ambako tungewekeza zaidi kwenye taasisi ukurasa ule wa 80, tulishakubaliana tangu mwaka 2002 na Komredi Mangula, Katibu Mkuu wa CCM, wakati huo tuko kwenye TDC, nimpongeze sana Nsanzugwanko waanzilishi wa TDC (Tanzania center for Democracy) tulikubaliana Taifa liandae viongozi. Ukiangalia ma-RC, ma-DAS na ma-DED wetu wanaibukaje, vetting yao ikoje katika utumishi wa umma wa Tanzania ili waweze kuwa ni endelevu katika kutekeleza majukumu yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwa ma-DC na Ma-RC wetu, tumpongeze Kapteni Mheshimiwa Mkuchika uliwahi kuzungumza hapa, wanaandaliwaje, wanapikwaje ili waweze kutekeleza majukumu ipasavyo? Kwa hiyo, wasiibuke tu kila mtu na mambo yake, huyu anasema hili, yule anasema lile, kwa kweli tukiangalia kama wataendelea kufanya wanavyofanya tutakuwa hatulitendei Taifa letu haki. Mheshimiwa Mwenyekiti,

Mheshimiwa Mwenyekiti, rasilimali kubwa kuliko zote duniani leo hii ni rasilimali watu (umoja) na utawala bora is a collective approach inaanzia kwangu, kwako, kwa jamii nzima, kwa familia baadaye kwa Taifa. Mwalimu alikuwa anajua kwamba Taifa analipeleka wapi ndiyo wanafunzi tukawa tunaimbishwa kama kasuku ahadi za mwana-TANU, unaambiwa binadamu wote ni ndugu zangu, unajua kuwa huyu ni ndugu yangu; unambiwa rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala sitatoa rushwa, tulikuwa tunapata Taifa ambalo linaendelea, ni shirikishi, la wote kwa kuwa nchi hii ni yetu sote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kujitambua ni jambo muhimu sana na inatupasa sisi sote kwa pamoja kujua utawala bora ni wa pande mbili; anayeongoza na anayeongozwa, is a collective approach. Huwezi ukauchukulia utawala bora kwa yule tu anayeongoza. Ukikubali mawazo mbadala ukawa na utulivu; nimeona hata hapa Bungeni, unakuta Mbunge anaongea, mwingine amemwingilia, mwingine amefanya hivi. Hata Maandiko Matakatifu yanasema kujibu kabla ya kusikiliza ni upumbavu na aibu kwako ambaye hujataka kusikiliza. (Makofi)

Tusikilizane, tuvumiliane, tuwe na lugha ya staha. Taifa hili ni letu sote. Tukiwa na mawazo mapana namna hiyo, ninaamini hapa tulipo leo hii tutatoka na Tanzania ya leo, nani mwenye kujua kesho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji Taifa endelevu kwa maslahi mapana ya mama Tanzania. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya Elimu. Sekta ya Elimu kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu, Kitaifa inatakiwa kuwa na mifumo mitatu, yaani formal, non-formal and informal education.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera zetu za elimu, zinadhihirisha hilo kwani watoto wetu huondolewa mikononi mwa wazazi yaani hasa mama zao na kupelekwa shuleni chini ya walezi wengine yaani walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu ndiyo walezi wa Taifa, hoja kwa kielelezo humu ndani Bungeni hata Serikalini zaidi ya theluthi moja ni Walimu, nitatoa mfano, Serikalini na humu Bungeni, Mwalimu John Joseph Pombe Magufuli, Mama Janet Magufuli, Mwalimu Jenista Mhagama, Mwalimu Kilagi, Mwalimu Kabudi, Mwalimu Mwakyembe, Mwalimu Joyce Ndalichako, Mwalimu Susan Lyimo, Mwalimu Salma Kikwete, Mwalimu Profesa Mbarawa, Mwalimu Philipo Mpango, Mwalimu Grace Tendega, Mwalimu Shamsi Vuai Nahodha. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mwalimu Haonga.

MHE. JAMES F. MBATIA: Ndiyo na Mwalimu Haonga. Nikitaja kwa uchache, hapa ni Mwalimu, Mwalimu, Mwalimu. Nenda kwa Makatibu Wakuu, Katibu Mkuu Akwilapo Mwalimu, dada yangu Semakafu Mwalimu, wote ni Walimu, Walimu. Mama aliye na mtoto mchanga asipopata mahitaji msingi hawezi kumnyonyesha ipasavyo mwanaye, rai yangu, tumuenzi Baba wa Taifa hili, kwa kuwapatia Walimu wetu upendeleo wa makusudi katika mishahara yao na stahiki zao. Msemo wa hakuna mwingine kama mama, kwa heshima tuseme Tanzania hakuna mwingine kama Mwalimu, kwani sisi sote humu ndani ni zao la Walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu, Mwalimu John Joseph Pombe Magufuli, rai yangu kwake, awe mstari wa mbele kesho Mei Mosi, awe wa kwanza kuongeza mishahara ya Walimu na stahili zao kwa upendeleo wa makusudi, kwa kuwa Walimu ndiyo sekta kuu ya uzalishaji katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulinde uhuru na heshima ya Taifa letu, yaani Tanzania kwa kuwapatia walezi wetu, Walimu mishahara na stahiki zao zenye kukuza na kuhifadhi utu wao ili waweze kuwa na furaha ya ndani, wawe na uwezo na utu na rai ya kufundisha. Tutoke kule kwenye asilimia 60 ya Walimu sasa hivi ambao hawataki kufundisha warudi kwenye ari yao, warudi kwenye taaluma yao waweze kufundisha na kulilea Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza na hilo kwa sababu naiangalia elimu ya Tanzania kwa miaka 25 ijayo, miaka 30 ijayo. Ukisoma hotuba ya Kambi ya Upinzani, nimeisoma yote kwa makini ifikapo mwaka 2036 tutakuwa na Watanzania zaidi ya milioni 90. Mwaka 2045 tutakuwa na Watanzania zaidi ya milioni 120, je critical mass ya Watanzania, critical thinkers ya Watanzania watakuwa kwenye hali gani kama hatuondoi itikadi zetu, hatuondoi tofauti zetu tukajikita kwenye kuiangalia Tanzania miaka 30, miaka 50 ijayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bora, sawa na shirikishi kwa wote, mfumo wetu rasmi wa elimu wa sasa, kwa mfano Sera ya Elimu ya mwaka 2014 elimu msingi, ukiangalia na mitaala yake. Mitaala ya darasa la saba tayari imeshafundishwa darasa la nne, la tano na la sita. Ukiangalia Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, kwa nini hatukubali kuwa na mfumo ambao ni shirikishi, ni sawa, na ni elekezi kwa wote, badala ya kila Waziri anayekuja anakuja na mfumo wake na matamko yake ambayo tunaharibu elimu ya Taifa la Tanzania, lazima tuiangalie Tanzania kwa miaka zaidi ya 50 ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kwenda Finland, Finland, kwa nini hata mwaka jana, wameweza kuwa ni watu wa kwanza duniani kwa watu wao kuwa na raha? Waliandaa mifumo yao ya elimu yenye kujenga utu wa binadamu kwa zaidi miaka 40 iliyopita. Wakasema Taifa letu, tunataka liwe na uelewa wa namna gani, Taifa letu watu wake wajitambue namna gani, Taifa letu tushirikishane namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bahati mbaya sana hapa tunazungumzia formal education, lakini non formal and informal education tunaiweka kwenye hali ya namna gani. Uandaaji wa sera hizi, Daktari ndiyo ukienda hospitalini anakwambia wewe umeugua kitu gani na unatakiwa utibiwe namna gani? Leo hii, ukija kwenye Sera zetu za Elimu mitaala yetu inatengenezwa na watu wengine, ambao sio wale walezi, Walimu ambao wangekuwa ni shirikishi wa kutosha kwa sababu wanajua athari za watoto. Ukija hata kwenye lishe yetu, siku 1,000 za kwanza, yaani miaka miwili na miezi tisa, watoto wetu wanapokosa lishe ya kuweza kujenga vizuri uwezo wao, kwa mfano jana niliona mtu mmoja, mvua imenyesha, lakini kwa sababu yeye ameshazoea kwamba lazima kila siku aamke na amwagilie bustani, mvua huku inanyesha na huku anamwagilia bustani. Unakuta tayari ana udumavu wa akili kwa sababu alikuwa amezoea tu na unajua kwamba ni mtu mwenye akili nzuri tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, so we must think big, and think global namna gani tunawaacha, tunawakuza watoto wetu, namna gani tunawapa Walimu wetu ambao ndiyo walezi wakuu wa Taifa letu, waweze kuliangalia Taifa, waweze kuwa na utulivu, waweze kulea watoto wetu. Kwa sababu kama mama wewe, unamtoa mtoto wako unamkabidhi Mwalimu, ni kwamba umemwamini zaidi huyu Mwalimu kuliko hata wewe mzazi, kuliko hata mfanyakazi wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dada yangu Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako alikuwa Taasisi ya Elimu, alikuwa Baraza la Mitahani, ametoka huko amepewa dhamana hiyo, anaacha legacy ya namna gani kwa Taifa la Tanzania kwamba umeanzisha mfumo huu, tunaiona Tanzania ya miaka 50, tunaiona Tanzania ya miaka 30 yenye uelewa wa hali ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Naibu Waziri, Mheshimiwa Ole chonde chonde, tuache tofauti zote, tuwe na utulivu wa ndani, tukubali bila shaka, ukitaka kuliangamiza Taifa lolote lile anza kuua mifumo yake ya elimu inayolinda utu wa binadamu. Sasa hapa kila siku tunapiga kelele, hili, limetokea hivi, hili limetokea, tunakuwa negative, negative, let us think positive, think globally, think big and tuione Tanzania ya miaka 50 ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la vitabu, leo hii Taasisi ya Elimu, inachofanya na vitabu, kwa mfano tangu mwaka 2014 vitabu vya darasa la sita, vitabu vya darasa la saba, viko, havionekani, viko wapi? Tunasema vinaandaliwa, vinaandaliwa, niombe chonde chonde wawachukue akina Mzee Walter Bugoya, tuachane na tofauti zetu. Tuseme yaliyopita, yamepita si ndwele tugange yajayo, wawachukue akina Mzee Mture Elibariki, wanavyo vitabu vingi tu. Wazungumze nao, wawe na partnership, washirikiane nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule binafsi naupongeze Mkoa wa Kilimanjaro, ambao unaongoza na nimekuja kufanya utafiti kwa nini unaongoza?. Utaona shule nyingi ni za binafsi ndizo zinazoongoza, sasa Serikali badala ya kupambana na hizi shule binafsi ionekane ni washindani, wawe na ubia nao wawe ni washirika wenzao, hata kuwapatia ruzuku kwa sababu wanaelimisha Taifa kwa niaba ya Watanzania wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo niombe Walimu tulioko humu ndani, na asilimia 35 ya shule za Sekondari za Mkoa wa Kilimanjaro ni Shule binafsi na niwapongeze sana na Shule za Walimu wa Vunjo. Nikiangalia Ikama ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi tunazungumzia Walimu, Ikama ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, shule za Sekondari za Serikali zina upungufu wa Walimu 685. Shule za Msingi zina upungufu wa Walimu 376, sasa licha ya kazi kubwa wanayofanya Walimu hawa na wa Vunjo kule Halmashauri ya Moshi na sehemu nyingine Tanzania nzima, ni namna gani tunawapa uwezo, shule unakuta ina Walimu wawili au watatu, sio Wabunge tuje hapa tuongee basi tumeondoka. Wakati wa kupitisha bajeti, Wabunge tuoneshe nafasi yetu kwa mujibu wa Katiba tuiambie Serikali hapana, ukiwekeza kwenye akili ya mwanadamu ndiyo miundombinu mikubwa yenye rasilimali kuu, kuliko raslimali nyingine yoyote ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuipe Wizara hii bajeti ya kutosha, tufikiri vizuri, tuisimamie Serikali, la sivyo, watoto wetu miaka 20 ijayo, miaka 30 ijayo watakuja kuona kizazi hiki ni kizazi cha ajabu kweli, kwa mfano Joseph Roman Selasini hapa, Mbunge wa Rombo, baba yake alikuwa ni Mwalimu na aliwanasihi vizuri familia yao na unaweza kuona wamefika wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi baba yangu alikuwa Mwalimu na unaweza kuona nimekuwa ni zao la namna gani, sasa hebu jamani tuache tofauti zetu, tulikumbuke Taifa letu, tumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wote humu ndani tukisema Tanzania, tunasema hakuna mwingine kama Mwalimu, tukisema Tanzania tunarudia hakuna mwingine kama Mwalimu, tukisema Tanzania tunasema hakuna mwingine kama Mwalimu. Tukisema mlezi wa Taifa la Tanzania, tunasema ni Mwalimu, mlezi wa Taifa la Tanzania tunasema ni Mwalimu, mlezi wa Taifa la Tanzania, tunasema ni Mwalimu. Sekta inayozalisha kuliko zote ni Wizara ya Elimu, sekta inayozalisha kulko zote ni Wizara ya Elimu tuache tofauti nyingine zote tukubali sote kwa pamoja, Taifa hili ni letu sote tulinyonyeshe Taifa hili, tumnyonyeshe mama Tanzania kwa kuipa upendo Sekta ya Elimu, ili Sekta ya Elimu iweze kuwa na utulivu wa ndani, iweze kuwa na furaha, inyonyeshe watoto wa Tanzania ili Mwalimu wetu aweze kuwa nambari moja katika Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii, kwanza kabisa niwapongeze Kamati zote mbili Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Kamati ya Nishati na Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nishauri tu kwamba nimesikiliza mijadala tangu asubuhi ili mijadala yetu iweze ikawa na afya tuzingatie misingi ya utu wakati tunajadili, misingi ya kuwa na utulivu wa fikra, msingi wa rasilimali muda baadaye rasilimali fedha kwa muda utakaotumia katika mijadala yetu. Na wazo zuri ni wazi zuri usiangalie limetoka upande upi. Tujadili pamoja, tufakari pamoja na hatimaye tushauri pamoja. Hii italeta tija na itatusaidia sana kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu tukigawanyika na yote mazuri ambayo tunayazungumza ambayo nimeyasikia hapa na mengine yanaonekana basi kauli zetu kwa sababu sayansi nilishawahi kusema tena narudia sayansi ambayo imekuwa duniani kwa miaka
300 hivi inaonesha hisia kunuia na kutenda kwa mwanadamu hasa zile nguvu zinazotoka kwenye moyo wake zinaitwa magnetic force hasa spoken words maneno yanayotumika neno likishatoka limetoka na kipaji chetu cha kusikiliza.

Mheshimiwa Spika, nimeanza na hilo kwa sababu dunia ya leo tunaenda kwenye artificial intelligence. Kwenye diplomasia ya kiuchumi kwenye artificial intelligence yaani mashine zimeanza kufikiri kama binadamu, mashine zimeanza kutoa majawabu kama binadamu na kwenye logic naaanza kufikiria na kwenye logic unaenda kwenye tautology, wale waliosoma hesabu, if and only if na kwenye tautology unaongea nini na nani mahali gani wakati gani halafu hii halafu inaenda kwa kasi kubwa sana. Unaongea nini narudia unaongea nini na nani, mahali gani, wakati gani, halafu hii halafu ndio iliyo nzito zaidi kuliko yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwenye artificial intelligence tunaangalia dunia na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje yupo hapa. Kwenye diplomasia ya kiuchumi wakati Taifa hili linaasisiwa Mwalimu Nyerere alianza na kanuni ya utu, binadamu wote ni ndugu zangu, hakusema Afrika wote ni ndugu zangu, alisema binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.

Sasa tukishasema binadamu wote ni ndugu zangu tuchunge sana ndimi zetu hasa kutoa lugha ambazo zinaudhi wengine, tunatoa lugha ambazo zinadhalilisha wengine na hili ni kwetu sote tu. Kwa mfano tukitoa lugha za kukebehi na kujadili mataifa mengine tuangalie lengo la kumi na saba la malengo endelevu ya dunia linazungumzia global partnership, linazungumzia ushirika wa kidunia halizungumzii ushindani wa kidunia. Leo hii tuko humu ndani tunazungumza ushindani wa kivyama badala ya kuzungumza ushindani wa Taifa katika ushirika wa dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati wa mijadala kama hii na sisi tunaisimamia na kuishauri Serikali. Niishauri tu Wizara ya hasa Mambo ya Nje kwenye suala la global partnership ili yale malengo kumi na sita na lile la kumi na saba la global partnership badala ya kusema mimi unasema sisi, badala ya kusema yangu unasema yetu. (Makofi)

Sasa katika misingi hiyo umimi huu au ubabe huu hautatusaidia sana, lugha ni lugha tu nafasi yetu Tanzania katika mahusiano ya kimataifa, diplomasia yetu ya kiuchumi katika mataifa mengine, tunashauriana namna gani, tunasikilizana namna gani, kwa sababu mataifa yetu ni mataifa huru (a sovereign state). Unakaaje na wenzako kama wametoa kauli mnazungumza kwa lugha ya staha badala ya kutoa lugha tu, labda wakoloni hawa, mabeberu hawa, wamefanya hivi hata tukipiga kelele sana wao wanajibu kwa vitendo na tukiri kwenye artificial intelligence leo hii wenzetu wanaenda kwenye mashine za namna hiyo wakati sisi bado tuna upungufu hata kwenye shule zetu za miundombinu ya vyoo kwa takribani asilimia 60.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo we must think big and we must think globally while we want to have a local solution. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye diplomasia ya kiuchumi kwa mfano nilibahatika mwaka juzi kwenda Israel, tulialikwa na Chuo cha True Man Institute kwenye masuala ya ushirikiano kati ya Afrika na Israel. Waisraeli leo hii wanavuna maji yaliyo safi na salama kwa kutumia hewa angani, lakini dunia ya leo zaidi ya watu bilioni moja hawana maji safi na salama. Sasa ni namna gani mahusianao yetu kwenye hii free market ya dunia ya leo mahusiano yetu ya kuweza kuvuna rasilimali hii knowledge hii katika kuisaidia taifa letu la Tanzania tukiwa wamoja.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano wakati wa Mwalimu mahusiano kati ya Wapalestina na Waisraeli mwaka juzi tulipokuwa kwenye hicho chuo cha True Man Institute tulikuwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani akina Poel, wakina Mheshimiwa Raila Odinga, Balozi mmoja wa Israel aliwahi kuwa Kenya akiwa anashughulikia Afrika Masharikia akasema uso mzuri hauitaji urembo. Nanukuu maneno yake; “uso mzuri hauitaji urembo.” Maana yake nini kwamba chema chajiuza, kibaya chajitembeza. (Makofi)

Sasa tukifikiri tukiwa na utulivu mzuri tu, tukaangalia sisi sasa tunatumia namna gani nafasi hii kuvuna teknolojia hii, kuweza kuona namna gani inatusadia katika maji, basi Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje inashirikiana na zile Wizara nyingine zinazohusika tunasimama wote kwa pamoja kama Taifa kwa sababu hili lina maslahi kwa wote kama ni maji ni yetu sote katika majimbo yetu, kama ni suala la umeme ni letu sote katika majimbo yetu, kama ni suala lolote lile sote tunasimama kama Taifa na vita hivi vya kiuchumi tutavishinda tukiwa wamoja kama Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo tunakumbuka Zimbabwe ilivyokuwa kwenye hali n zuri tu mwaka 2002 nikiri nilienda Zimbabwe tulitumwa na Rais Mkapa kuangalia uchaguzi wa Zimbabwe, lakini walikuwa wamegawanyika. Tulienda Bulawayo tukaenda Tumbuiza, tukaenda Harare mpaka Victoria Falls sasa wanatumia nafasi ya mgawanyiko ndani ya Taifa ili kutugawa. Sasa tusijaribu kuona kwamba tunafanya tu upande mmoja tufikiri kwa pamoja, tuwe na utulivu kwa pamoja, tuone ni namna gani ya kuweza kuvuka katika hali ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishauri Kamati na niiombe Kamati na hasa ya Mambo ya Nje ukiangalia Taifa la India leo hii na teknolijia yao ya afya na vijana wao wanavyojitahidi kwenye afya namna gani mgogoro ulioko kati ya India na Pakistan hasa mambo ya Jammu na Kashmir. Kwa sababu kila mara India wanauliza wao wanataka wafanye mazungumzo yao, sasa Tanzania sisi tunasimamia wapi kwenye mahusiano yetu kati ya Pakistan na India hasa masuala ya Kashmir, halafu tunakuwa na msimamo gani ili sisi wote tunaweza tukafaidi yale mengine ambayo ni makubwa badala ya kutoa lugha tu ambazo sio nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nizungumzie kidogo masuala ya usalama katika Taifa letu. Yako haya mambo yanayoendelea kwenye Taifa letu hata juzi yalitokea mauaji huko Kilimanjaro ambayo lazima tujiulize sote na tutafakari kwa sote kwa pamoja. Nimejaribu kujiuliza maswali yafuatayo kwenye suala la ulinzi na usalama wa taifa letu. Kwanza nitoe tena pole kwa vifo vilivyotoke kule, lakini kwenye masuala ya hivi vikundi mbalimbali tujiulize je, kuna matatizo au vikwazo au changamoto gani katika jamii yetu labda ya kikatiba, kisheria husika na kanuni zake, jamii kujitambua, mifumo yetu ya kitaasisi hasa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama mfano public order (usalama wa raia), public health (masuala ya afya), peace (suala la amani ya Taifa), crowd management na disaster preparedness endapo jambo lolote lile linatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na tujiulize kama taifa na hasa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa nini haya yote na matakwa yake ya kisheria yanatokea mambo ya namna hii, je, ni maadili yetu ya kitaifa yamemomonyoka, je, elimu ya kimungu ndani ya madhehebu yetu yenyewe yako katika misingi ya namna gani.

Mheshimiwa Spika, tukiwa na tafakuri ya kina sote kwa pamoja tunaamini kwamba tutabaki kuwa pamoja na wakati wa mijadala hasa wakati huu tunashauri Serikali, tunashauriana Wabunge na hasa Kamati tuhakikishe kwamba kipindi cha mwaka kama hiki sisi kama Wabunge yale majukumu makuu manne ya Mbunge tunasimamia kwanza jukumu la kwanza ambalo ni kwa Taifa lako, la pili kwa jimbo lako la uchaguzi yale ya vyama na mengine unaweka pembeni Taifa linakuwa pamoja tunashiriki pamoja, tunajadiliana pamoja, taifa letu litasonga mbele na tumpe upendo mama Tanzania kwa maslahi ya wote.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi uliyonipa. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Miswada iliyoko mbele yetu. Nimwombe Mwenyezi Mungu anijaalie nichangie Miswada hii, nikifanya rejea ya dunia ilivyo na sisi hapa Tanzania tunataka kufanya nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na ule wa Mamlaka wa Hali ya Hewa; kuna mambo ya msingi ambayo tunatakiwa kuyazingatia wakati tunatengeneza au tunatunga sheria hizi, kwani sisi Tanzania sio kisiwa na kuna mambo hayo makuu ya msingi (The four core elements) katika masuala haya ni suala la scope, time, cost and quality. Tukiweza kuangalia hili jambo kwa ukubwa wake na tukaona hali halisi ya nchi duniani ilivyo leo, namna gani wenzetu wanafanya duniani leo, zile nchi ambazo wana teknolojia ya kisasa leo, wanaazimaje takwimu au taarifa zilizo sahihi za hali ya hewa (weather forecast). Baada ya hapo tukafanya integration kwetu sisi hapa nyumbani, je mamlaka au Serikali inao uwezo kweli wa kusema wenyewe watadhibiti taarifa za hali ya hewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tukiuliza leo rejea ya takwimu tulizonazo hapa nchini Tanzania za Mamlaka ya Hali ya Hewa kama miaka 100 au 200 iliyopita hatuna, tunaweza tukawa na za kuanzia miaka ya sabini hapo na kuendelea, lakini wenzetu wanazo takwimu kuanzia miaka 1800 na wanaangalia return period yaani wanaangalia ni muda gani labda tukio fulani linaweza likatokea, labda ni la maafa au ni tukio la namna gani linaweza likatokea kutokana na uzoefu wa huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano unasema mafuriko yametokea, utabiri wa hali ya hewa lakini precision, reliability, efficiency ya mamlaka husika na uwezo walionao wa kuweza kutoa hizo takwimu ambazo ni sahihi, relative to na hali inavyobadilika duniani leo, inabidi mamlaka hii iweze kukubali namna ya kuwezesha zile four core elements nilizozisema za integration, human resource, communication and risk management. Yaani ile engineering perspective, how we can make integration in able to archive the four core elements of integration, human resource, communication and risk management. Ukiangalia sasa hawa ni authority, je, Kitengo cha Kupambana au Kujikinga na Majanga Tanzania, kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2015, kina uwezo gani na kinafanya kazi gani leo hii ili hali ya hewa inayotabiriwa hapa nchini Tanzania iweze kwenda sambasamba na takwimu hizi za mamlaka ya hali ya hewa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwekeze zaidi kwenye kutoa elimu hata kuangalia namna gani Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa maana ya Wizara hii inashirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kuhakikisha kwenye shule zetu watu wanapata elimu na umuhimu wa utabiri wa hali ya hewa. Ile awareness, watu wetu kujitambua na kuona umuhimu wa hali hiyo, nilisema nitazungumzia kwa mapana yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kwa nini hapa kwetu Tanzania vyombo vyetu vya habari au mamlaka inavyotabiri na hoja kwa kielelezo labda nilieleweke vizuri, nitatoa mfano wa tarehe 16 Januari, siku ya Jumatano lilipotokea tatizo hapo Dumila Morogoro. Mvua ilivyonyesha nyingi, daraja linakatika asubuhi ni watu gani waliotoa zile taarifa kwamba daraja linaleta matatizo linaweza likaangamiza maisha ya Watanzania, walikuwa ni watu wa bodaboda, watu wa kawaida tu pale Dumila. Je, takwimu zilikuwa zimetolewa na watumiaji wa barabara wakapata taarifa kwamba hali hiyo itatokea ambayo ni precision isiyokuwa na uwalakini wa aina yoyote ilikuwa haipo. Ndiyo maana unakuta hata wataalam wetu humu ndani hawana ile reliability (kuaminika) kwa takwimu za hali ya hewa za Tanzania, wanaamua kutafuta takwimu za hali ya hewa za wxmax.africa.com ambazo ziko reliable zaidi kuliko takwimu zetu za humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikitokea labda hata tishio kama la ukanda wa bahari, bahari yetu ina urefu wa kilomita 1,424 ambayo ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu lakini ni namna gani watu wote wa Pwani wanapata taarifa zilizo sahihi? Watu wetu wote wanaoishi Ukanda wa Pwani kuanzia Mtwara mpaka Tanga kutokana na tabia nchi ni kwa jinsi gani wanaweza kila siku kupata elimu? Ndiyo maana nimesema elimu, elimu, elimu ni muhimu katika kushughulikia suala la hali ya hewa na hasa wavuvi wetu wa baharini, kwenye bahari kuu na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Muswada wa pili, suala la Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini. Ni kweli kwamba usafiri wa ardhini na hasa hapa kwetu Tanzania njoo kwenye reli na barabara na mamlaka hii sasa tunatoka kwenye SUMATRA tunaitenganisha tunakuja kwenye mamlaka kamili ya ardhini, design ya barabara zetu, barabara zetu zina design speed ya kilomita 80 kwa saa lakini magari tunayoyatumia mengine ni ya kilomita 240 kwa saa. Kwa sababu hili jambo ni pana lazima wakati mwingine kuangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize kwa mfano, kwa nini Ujerumani hawana limit speed na rate of accident Germany ni tofauti na ya kwetu Tanzania, relative to. We must think globally but we must have a local solution how we can deal with these things, unless otherwise maisha ya wetu itakuwa ni matatizo. Kwa nini leo hii usafiri wa mabasi usiwe ni saa 24 inakuwa ni wa mchana tu, tuko kwenye karne gani ya ujima hii? Hatuwezi tukawa na uwezo mpana, gari inatoka Kigoma inafika hapo Morogoro inazuiliwa kwa sababu haiwezi kusafiri labda baada ya saa 4.00 za usiku au ni saa 6.00, tuone namna bora ya kutumia barabara hata tulizonazo kwa kuongeza mambo makuu mawili na la tatu ni sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kwenye engineering perspective ya suala la time, quality and cost, sasa hivi kuna suala la integration, chochote kinachokubalika ni efficiency and reliability. Efficiency, ufanisi na kuaminika, ni sawasawa hata na binadamu tu. Nikimuamini Mwenyekiti ile trust, ukimuamini inachukua muda kujenga ule uaminifu na kuaminiana lakini is a matter of seconds kuondoa ule uaminifu (trust) na kwenye biashara hii iko hivyohivyo. Mamlaka imeandaaje rasilimali watu na inapewaje uwezo na Serikali kuwekeza kwenye uwezo wao waweze kuiona dunia ili usafiri wetu uweze kuwa wenye tija, wa kukuza uchumi wetu, wa kuhakikisha kwamba Tanzania tunaingia kwenye ushindani na tuko kwenye ushindani wa ukwelikweli, ni lazima sasa sheria hizi tunazozitunga ziweze kukuza zaidi utu wa mwanadamu, ziweze zikamfanya Mama Tanzania akawa na upendo zaidi ili kizazi chetu hapa Tanzania tukasema kweli tuko katika ushindani wa usafiri wa namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mamlaka hii inayoanzishwa ili iweze ikatoa ufanisi, ni ushauri kwa Serikali, wakati wa kutengeneza Kanuni, tukubali kutumia wataalam na wataalam waachwe wafanye kazi yao, wanasiasa kwa mfano, lile janga lililotokea pale Morogoro, nimeshashuhudia mengi tu la Morogoro, Dar es Salaam na Pwani huko unakuta kwa kiasi kikubwa wataalam wanaogopa kufanya maamuzi mpaka wasubiri wanasiasa ndiyo wawaongoze namna ya kufanya maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile ya tarehe 16 niliishuhudia mwenyewe, wataalam wako pale lakini hawafanyi maamuzi mpaka wasubiri Kamati za Ulinzi na Usalama, maisha ya mwanadamu hayawezi yakasubiri maamuzi ya kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ile empowerment yaani kuangalia zile taratibu tu na elimu ya kuelimishana vizuri. Tuangalie vizuri namna gani ya kuweka kanuni zetu, namna gani sheria hii inaendana na zile kanuni zetu na ni namna gani wenzetu duniani wanavyofanya. Vilevile ni namna gani masuala haya yote tunaya-integrate kwa pamoja ili usafiri wetu wa ardhini na sasa hivi tuna standard gauge, barabara zetu watumiaji wote kwa pamoja bila ubaguzi wa namna yoyote namna gani tutawezesha kutoa elimu kwa watumiaji kwenye magari yetu ili tuone akina mama wajawazito, walemavu na watoto wa shule wanapewa kipaumbele, ni suala la elimu, elimu, elimu. Suala la kuangalia ni kuhakikisha utu wa mwanadamu tunau-integrate namna gani katika masuala haya ya usafiri ili sheria hii tunayotunga iweze kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sheria isiwe ni adhabu. Kwa mfano, kuweka adhabu ya asilimia 1.5, adhabu ya vifungo vikubwa vya miaka miwili, tutoe elimu zaidi badala ya kuweka adhabu. Tuone wasafirishaji wa mabasi waonekane ni sehemu ya kuisadia Serikali kwa kuwapatia incentive zaidi na hata ruzuku ya namna gani ya kuendesha kwa sababu wanatoa huduma iliyo bora kwa ajili ya Taifa na siyo kuwakomoa au kuwabambikizia kesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ni nani anakagua mabasi, hivi ni Polisi, ni Mamlaka au ni nani? Unakuta Mamlaka wanakagua lakini akitoka hapo Polisi wameingiana wakati hawana taaluma hiyo. Kwa hiyo, hata Traffic Police Ordinance au Traffic Act ni lazima iangaliwe na hii ya Mamlaka ili migongano isiwepo tuweze kupata dira sahihi ya usimamizi huu tunaousubiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe chondechonde, naunga mkono Muswada huu waziwazi kabisa kwa sababu ni Muswada wenye maslahi mapana kwa nchi yetu ya Tanzania, naunga Miswada yote mikono wa Hali ya Hewa na huu na kwa lengo la kuifanya Tanzania iwe sehemu salama na nzuri zaidi ya kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa muda huu, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini wa Mwaka 2018
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Miswada iliyoko mbele yetu. Nimwombe Mwenyezi Mungu anijaalie nichangie Miswada hii, nikifanya rejea ya dunia ilivyo na sisi hapa Tanzania tunataka kufanya nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na ule wa Mamlaka wa Hali ya Hewa; kuna mambo ya msingi ambayo tunatakiwa kuyazingatia wakati tunatengeneza au tunatunga sheria hizi, kwani sisi Tanzania sio kisiwa na kuna mambo hayo makuu ya msingi (The four core elements) katika masuala haya ni suala la scope, time, cost and quality. Tukiweza kuangalia hili jambo kwa ukubwa wake na tukaona hali halisi ya nchi duniani ilivyo leo, namna gani wenzetu wanafanya duniani leo, zile nchi ambazo wana teknolojia ya kisasa leo, wanaazimaje takwimu au taarifa zilizo sahihi za hali ya hewa (weather forecast). Baada ya hapo tukafanya integration kwetu sisi hapa nyumbani, je mamlaka au Serikali inao uwezo kweli wa kusema wenyewe watadhibiti taarifa za hali ya hewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tukiuliza leo rejea ya takwimu tulizonazo hapa nchini Tanzania za Mamlaka ya Hali ya Hewa kama miaka 100 au 200 iliyopita hatuna, tunaweza tukawa na za kuanzia miaka ya sabini hapo na kuendelea, lakini wenzetu wanazo takwimu kuanzia miaka 1800 na wanaangalia return period yaani wanaangalia ni muda gani labda tukio fulani linaweza likatokea, labda ni la maafa au ni tukio la namna gani linaweza likatokea kutokana na uzoefu wa huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano unasema mafuriko yametokea, utabiri wa hali ya hewa lakini precision, reliability, efficiency ya mamlaka husika na uwezo walionao wa kuweza kutoa hizo takwimu ambazo ni sahihi, relative to na hali inavyobadilika duniani leo, inabidi mamlaka hii iweze kukubali namna ya kuwezesha zile four core elements nilizozisema za integration, human resource, communication and risk management. Yaani ile engineering perspective, how we can make integration in able to archive the four core elements of integration, human resource, communication and risk management. Ukiangalia sasa hawa ni authority, je, Kitengo cha Kupambana au Kujikinga na Majanga Tanzania, kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2015, kina uwezo gani na kinafanya kazi gani leo hii ili hali ya hewa inayotabiriwa hapa nchini Tanzania iweze kwenda sambasamba na takwimu hizi za mamlaka ya hali ya hewa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuwekeze zaidi kwenye kutoa elimu hata kuangalia namna gani Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa maana ya Wizara hii inashirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa lengo la kuhakikisha kwenye shule zetu watu wanapata elimu na umuhimu wa utabiri wa hali ya hewa. Ile awareness, watu wetu kujitambua na kuona umuhimu wa hali hiyo, nilisema nitazungumzia kwa mapana yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia kwa nini hapa kwetu Tanzania vyombo vyetu vya habari au mamlaka inavyotabiri na hoja kwa kielelezo labda nilieleweke vizuri, nitatoa mfano wa tarehe 16 Januari, siku ya Jumatano lilipotokea tatizo hapo Dumila Morogoro. Mvua ilivyonyesha nyingi, daraja linakatika asubuhi ni watu gani waliotoa zile taarifa kwamba daraja linaleta matatizo linaweza likaangamiza maisha ya Watanzania, walikuwa ni watu wa bodaboda, watu wa kawaida tu pale Dumila. Je, takwimu zilikuwa zimetolewa na watumiaji wa barabara wakapata taarifa kwamba hali hiyo itatokea ambayo ni precision isiyokuwa na uwalakini wa aina yoyote ilikuwa haipo. Ndiyo maana unakuta hata wataalam wetu humu ndani hawana ile reliability (kuaminika) kwa takwimu za hali ya hewa za Tanzania, wanaamua kutafuta takwimu za hali ya hewa za wxmax.africa.com ambazo ziko reliable zaidi kuliko takwimu zetu za humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikitokea labda hata tishio kama la ukanda wa bahari, bahari yetu ina urefu wa kilomita 1,424 ambayo ni baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu lakini ni namna gani watu wote wa Pwani wanapata taarifa zilizo sahihi? Watu wetu wote wanaoishi Ukanda wa Pwani kuanzia Mtwara mpaka Tanga kutokana na tabia nchi ni kwa jinsi gani wanaweza kila siku kupata elimu? Ndiyo maana nimesema elimu, elimu, elimu ni muhimu katika kushughulikia suala la hali ya hewa na hasa wavuvi wetu wa baharini, kwenye bahari kuu na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Muswada wa pili, suala la Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini. Ni kweli kwamba usafiri wa ardhini na hasa hapa kwetu Tanzania njoo kwenye reli na barabara na mamlaka hii sasa tunatoka kwenye SUMATRA tunaitenganisha tunakuja kwenye mamlaka kamili ya ardhini, design ya barabara zetu, barabara zetu zina design speed ya kilomita 80 kwa saa lakini magari tunayoyatumia mengine ni ya kilomita 240 kwa saa. Kwa sababu hili jambo ni pana lazima wakati mwingine kuangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize kwa mfano, kwa nini Ujerumani hawana limit speed na rate of accident Germany ni tofauti na ya kwetu Tanzania, relative to. We must think globally but we must have a local solution how we can deal with these things, unless otherwise maisha ya wetu itakuwa ni matatizo. Kwa nini leo hii usafiri wa mabasi usiwe ni saa 24 inakuwa ni wa mchana tu, tuko kwenye karne gani ya ujima hii? Hatuwezi tukawa na uwezo mpana, gari inatoka Kigoma inafika hapo Morogoro inazuiliwa kwa sababu haiwezi kusafiri labda baada ya saa 4.00 za usiku au ni saa 6.00, tuone namna bora ya kutumia barabara hata tulizonazo kwa kuongeza mambo makuu mawili na la tatu ni sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kwenye engineering perspective ya suala la time, quality and cost, sasa hivi kuna suala la integration, chochote kinachokubalika ni efficiency and reliability. Efficiency, ufanisi na kuaminika, ni sawasawa hata na binadamu tu. Nikimuamini Mwenyekiti ile trust, ukimuamini inachukua muda kujenga ule uaminifu na kuaminiana lakini is a matter of seconds kuondoa ule uaminifu (trust) na kwenye biashara hii iko hivyohivyo. Mamlaka imeandaaje rasilimali watu na inapewaje uwezo na Serikali kuwekeza kwenye uwezo wao waweze kuiona dunia ili usafiri wetu uweze kuwa wenye tija, wa kukuza uchumi wetu, wa kuhakikisha kwamba Tanzania tunaingia kwenye ushindani na tuko kwenye ushindani wa ukwelikweli, ni lazima sasa sheria hizi tunazozitunga ziweze kukuza zaidi utu wa mwanadamu, ziweze zikamfanya Mama Tanzania akawa na upendo zaidi ili kizazi chetu hapa Tanzania tukasema kweli tuko katika ushindani wa usafiri wa namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mamlaka hii inayoanzishwa ili iweze ikatoa ufanisi, ni ushauri kwa Serikali, wakati wa kutengeneza Kanuni, tukubali kutumia wataalam na wataalam waachwe wafanye kazi yao, wanasiasa kwa mfano, lile janga lililotokea pale Morogoro, nimeshashuhudia mengi tu la Morogoro, Dar es Salaam na Pwani huko unakuta kwa kiasi kikubwa wataalam wanaogopa kufanya maamuzi mpaka wasubiri wanasiasa ndiyo wawaongoze namna ya kufanya maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ile ya tarehe 16 niliishuhudia mwenyewe, wataalam wako pale lakini hawafanyi maamuzi mpaka wasubiri Kamati za Ulinzi na Usalama, maisha ya mwanadamu hayawezi yakasubiri maamuzi ya kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ile empowerment yaani kuangalia zile taratibu tu na elimu ya kuelimishana vizuri. Tuangalie vizuri namna gani ya kuweka kanuni zetu, namna gani sheria hii inaendana na zile kanuni zetu na ni namna gani wenzetu duniani wanavyofanya. Vilevile ni namna gani masuala haya yote tunaya-integrate kwa pamoja ili usafiri wetu wa ardhini na sasa hivi tuna standard gauge, barabara zetu watumiaji wote kwa pamoja bila ubaguzi wa namna yoyote namna gani tutawezesha kutoa elimu kwa watumiaji kwenye magari yetu ili tuone akina mama wajawazito, walemavu na watoto wa shule wanapewa kipaumbele, ni suala la elimu, elimu, elimu. Suala la kuangalia ni kuhakikisha utu wa mwanadamu tunau-integrate namna gani katika masuala haya ya usafiri ili sheria hii tunayotunga iweze kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sheria isiwe ni adhabu. Kwa mfano, kuweka adhabu ya asilimia 1.5, adhabu ya vifungo vikubwa vya miaka miwili, tutoe elimu zaidi badala ya kuweka adhabu. Tuone wasafirishaji wa mabasi waonekane ni sehemu ya kuisadia Serikali kwa kuwapatia incentive zaidi na hata ruzuku ya namna gani ya kuendesha kwa sababu wanatoa huduma iliyo bora kwa ajili ya Taifa na siyo kuwakomoa au kuwabambikizia kesi.


Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ni nani anakagua mabasi, hivi ni Polisi, ni Mamlaka au ni nani? Unakuta Mamlaka wanakagua lakini akitoka hapo Polisi wameingiana wakati hawana taaluma hiyo. Kwa hiyo, hata Traffic Police Ordinance au Traffic Act ni lazima iangaliwe na hii ya Mamlaka ili migongano isiwepo tuweze kupata dira sahihi ya usimamizi huu tunaousubiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe chondechonde, naunga mkono Muswada huu waziwazi kabisa kwa sababu ni Muswada wenye maslahi mapana kwa nchi yetu ya Tanzania, naunga Miswada yote mikono wa Hali ya Hewa na huu na kwa lengo la kuifanya Tanzania iwe sehemu salama na nzuri zaidi ya kuishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa muda huu, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu kwa niaba ya wananchi wa Vunjo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara ya kwanza nachangia kwenye Mkutano huu wa Bunge, nipende tu kusema kwamba haki ya kuwa na fikra tofauti na mwenzio ni haki ya msingi, ni haki ya kuzaliwa, ni haki ya Kikatiba na tusijengeane chuki binafsi kwa sababu hizi ni kazi za Watanzania tu tunazifanya. Masuala ya chuki binafsi hayana nafasi hapa tunapita tu na Tanzania ina umri mrefu kuliko sisi binadamu. Kwa hiyo, kujengeana chuki binafsi hapa siyo jambo la kheri wala halitatujengea mambo yote ya udugu wetu na mambo ya msingi kwa maslahi binafsi ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wajibu wa Bunge letu ni kuisimamia na kuishauri Serikali. Wajibu wa Bunge letu kwa niaba ya wananchi kwa kuwa wananchi ndiyo walipa kodi na rasilimali za Taifa zinazotumika na Serikali, tunasimamia Serikali kwa niaba ya wananchi na kuna kanuni inayosema hakuna haja ya kulipa kodi kama hakuna uwakilishi (no taxation, no representation). Sisi Wabunge tukiwa ndani ya Bunge hili, tukiwa tunasema mambo hata kama hayapendezi lakini mgongano wa fikra unaleta tija. Hata mwanasayansi mmoja Isaac Newton katika kanuni yake ya tatu anasema katika kila kani mkabala kuna kani iliyo mrejeo sawa na kinyume. Tukiwa na mawazo mapana Serikali hii ya Awamu ya Tano itafanya kazi yake vizuri ya kuhudumia Watanzania kwa maslahi mapana ya wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na usafirishaji, hii Tanzania ni kubwa. Afrika Mashariki kabla haijaingia Sudan ya Kusini, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi ni asilimia 48 tu ya eneo lote la Afrika Mashariki, Tanzania ina eneo la kijiografia zaidi ya asilimia 52. Katika hali hiyo tufanyeje? Lazima tukubali kwenye vipaumbele tuanze kuwekeza kutokana na kasi ya mabadiliko ya sayansi ya teknolojia duniani na suala la kuunganisha bandari zetu na reli na hasa reli ya kati ambayo ndiyo lango kuu la uchumi na kuwa na reli ya kisasa (standard gauge), hili sio suala tena la kupiga danadana. Suala la Serikali kutumia resource zake kwenye bajeti hii shilingi trilioni moja kujenga standard gauge labda ungesema ni upembuzi yakinifu na mambo mengine. Dunia ya leo nenda hata Marekani, nenda Ulaya, Mheshimiwa Waziri ametembea na anaijua dunia na ningependekeza hata Kamati mbalimbali za Bunge ziende nje ya Tanzania wakapate exposure ili waweze kuishauri vizuri Serikali, tuone wenzetu duniani wanafanyaje, wakiwekeza kwenye akili ya mwanadamu mambo mengine yote yanaenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri suala la reli ya kati Serikali ikope na hii kazi ifanyike ndani ya mwaka mmoja, miaka miwili au mitatu suala hili tuachane nalo tufanye mambo mengine makubwa zaidi. Tukisema tunatafuta resource zetu wenyewe hatuwezi tukajenga hii reli ya kati. Angalia wenzetu wa Kenya wameshaanza kuanzia Mombasa, wameshafika Nakuru, Naivasha sasa wanakimbilia Nairobi wakiwa na lane hii moja ya reli sisi bado tunapiga danadana ya maneno tu, mara ratili kumi, mara ratili pound ngapi hapana hatuwezi tukafika huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, bandari zetu tulizonazo, jana kwenye maoni ya Upinzani nilizungumzia kuhusu Bandari ya Mtwara nayo ikapewa kipaumbele chake ukilinganisha na Bandari ya Dar es Salaam.
Tumezungumzia masuala ya malori zaidi ya 5,000 mpaka 6,000 kwa mwezi pale Kurasini ni suala la kufanya maamuzi tu Bandari ya Kavu ya Soga ipo pale fanya maamuzi, mwekezaji yupo tunasonga mbele lakini ni danadana mwakani tunarudia kwenye maneno hayo hayo hatuna nafasi ya kufanya mambo ya namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara zetu, sisi Wabunge wakati tunatoka Dar es Salaam tunaona eneo la Chalinze lilivyoharibika, ni matuta matupu. Eneo lile anatoka Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na amejenga barabara nyingi tu ndani ya Taifa hili tunasemea vitu gani vya ajabu hapa? Angalia barabara za Gairo hapo, tupo kwenye hali gani na tunapita sote pale tunaona. Kwa nini barabara hizi zinaharibika kiasi hicho? Ni kwamba zaidi ya asilimia 99.43 ya usafirishaji wetu wa mizigo unatumia barabara. Sasa tunafanya mambo ya vicious cycle of poverty, unazunguka pale pale barabara, barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wengine wanasema bandua lami weka lami, kuna suala la classification theory! Labda niwaombe watu wa TANROADS na Wahandisi na ikupendeze Mheshimiwa Waziri Wabunge tupewe semina kuhusu ujenzi wa barabara unakuwaje ili tuwe na fikra pana za kuweza kutoa michango yetu iweze ikasaidia vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ijikite kwenye kutoa huduma za elimu, afya, maji, haki, mahakama na nyinginezo lakini masuala ya ujenzi wa barabara, ujenzi wa reli na bandari duniani leo ni suala la kutafuta wawekezaji, ni sekta binafsi inapewa kipaumbele katika maeneo haya. Serikali tena mnaanza kurudi kule ambapo tumeshatoka tutakuwa tunapiga danadana tu.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge tunamchanganya hata Waziri. Jana hapa Mbunge mmoja alitoa mchango kuhusu reli akashangiliwa sana, mwingine akasema kuhusu viwanja vya ndege akashangiliwa sana, sasa Waziri achukue lipi, awekeze kwenye reli au awekeze kwenye viwanja vya ndege au basi tu tunafanya kama ngoma za kuigiza hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri TANROADS kwamba maji ni adui mkubwa wa barabara. Tulivyofundishwa masuala ya asphalt na bitumen kwenye ujenzi wa barabara maji ni adui mkubwa wa barabara. Sasa Serikali kuu inashirikianaje na Serikali za mitaa ili TANROADS kwa kushirikiana na Halmashauri kuona namna gani tunaishirikisha jamii ili tuweze kufungua mitaro yetu vizuri, kuwa na kilimo cha matuta, kilimo cha kingamaji, hasa maeneo ya miinuko ili iweze ikawa ni shirikishi kwa wote, la si hivyo hili tunalofanya hapa barabara zetu zinaharibika kila siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee nimpongeze Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kazi nzuri anayoifanya na unyenyekevu na upole wake na tarehe 13 tulishiriki naye kwenye kongamano la pamoja la namna ya kujikinga na maafa (risk management) katika Mkoa wa Kilimanjaro.
Wataalamu wetu wakati mwingine tunawalaumu kutokana na mashinikizo tunayowapa sisi viongozi wa kisiasa halafu wanashindwa kufanya kazi zao vizuri. TANROADS kusema ukweli wanafanya kazi nzuri kuna wachache hawafanyi kazi vizuri, sasa wale wachache wasifanye wale wengi wakalaumiwa bure. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mawasilianio, kodi zisizotabirika, sisi ni wa pili baada ya Gabon kwa kodi nyingi na zisizotabirika kwenye sekta ya mawasiliano hasa kwenye sekta ya simu. Tuwe na mifumo endelevu na mipana ya miaka zaidi ya 100 ijayo ili tuweze kuhakikisha kwamba Tanzania tunayoihitaji ya miaka 150 ijayo inakuwaje, tuweze kushindana na wenzetu duniani. Tusipofanya hivyo tutakuwa hata kwenye ukanda wa Afrika Mashariki tutakuwa nyuma. Kwa mfano Bandari ya Dar es Salaam ndiyo inashika mkia katika ukanda wa Afrika Mashariki, tusijilinganishe na tunachopata sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naomba zile barabara za ahadi za Rais ziweze kupewa kipaumbele, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kutoa mchango kwenye hoja hii iliyoko mbele ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri inaonesha kwamba Wizara yake au sekta ya utalii inaingiza asilimia 25 ya fedha zote za kigeni katika Taifa hili, kwa hivyo ni sekta nyeji. GDP - Pato la Taifa katika utalii, na hii ni zaidi ya miaka mitatu iliyopita tunataka atupe takwimu za sasa, ni asilimia 17.5, ya leo ikoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Tanzania ni ya pili kwa vivutio vya utalii duniani baada ya Brazil. Tumekaa na sekta ya utalii wakati Mheshimiwa Chenge akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, tukafanya michanganuo mingi na tukatoa ushauri kwa Serikali namna bora ya kuweza kuweka mazingira mazuri na rafiki na yenye kuvutia ili tuweze tukaingia kwenye ushindani hasa wa soko la utalii duniani. Ukizungumzia Serengeti, ina kilometa za mraba zaidi ya 14,000 tukishindana na Masai Mara ambayo ina kilometa za mraba 1,400, ukizungumzia Mlima Kilimanjaro, ukizungumzia Ukanda wa Bahari ya Hindi kilometa 1,424, unataja vingi tu lakini Tanzania inashika nafasi ya 110 kati ya nchi 133 kwenye mazingira rafiki na mapato katika sekta ya utalii, huu ni uendawazimu, yaani kwenye mtu mwenye akili nzuri unaona kabisa hatuko serious. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka na wewe Mwenyekiti tulikuwa pamoja kwenye Kamati ya Chenge One kuhusu sekta ya utalii wakati tunatafuta vyanzo vipya vya mapato. Leo hii kulikoni sekta hii, nimesoma hotuba ya Waziri, TANAPA mchango wake kwenye maendeleo ya jamii ni one billion, wakati ukiangalia kwa mfano Mlima Kilimanjaro peke yake mapato yake ni zaidi ya bilioni 60 kwa mwaka ambayo ni asilimia 34 ya mapato yote ya sekta ya utalii. Lakini ukiangalia mazingira yanayozunguka Mlima Kilimanjaro, likiwepo Jimbo la Vunjo, hali ya vijiji ambavyo viko karibu na mlima huo hali yake ni hoi bin taabani. (Makofi)
Leo hii Mbunge unaambiwa uchangie kujenga shule, changia madawati, changia huduma sijui za nini hii haiwezekani wakati vivutio tunavyo, fedha zipo. Hii ni Serikali naamini ni endelevu ya chama hicho hicho. Serikali iliyopita Waziri mwenye dhamana alikubali kwenye Bunge hili kwamba angalau asilimia 25 ya mapato yanayotokana na hifadhi hizi yaweze kuhudumia maeneo ambayo yako karibu na hifadhi hizi, ambapo ukiwa karibu na waridi unanukia waridi. Sasa leo hii ukiangalia maeneo haya yako hoi bin taabani lakini mapato haya je, leo hii Wizara yake inaendeleza ile sera ambayo ndiyo nilikuwa nataka iwe endelevu katika kuhakikisha tunapata mapato au laa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri inajichanganya, ukisoma ukurasa wa 87 unasema mwaka 2014 walipata bilioni nne kutokana na kodi ya vitanda kwa watalii ambayo ni dola moja na nusu kwa kila kitanda kwa usiku. Ukisoma ukurasa wa 127 mwaka 2014 watalii waliolala watalii hotelini ni 1054 na wastani wa kukaa hotelini siku kumi, ukizidisha unapata zaidi ya shilingi bilioni 31 na sio bilioni nne ambazo zimeandikwa hapa na ni takwimu zinazotoka hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri tu Wizara hii ili iweze ikawa ni endelevu lazima kuwe na mazingira rafiki kwa wawekezaji hasa wazawa kwenye sekta ya utalii. Ukiangalia kodi ambazo Serikali inatoza kwenye sekta ya utalii na hasa tour operators ni zaidi ya 40. Tumeimba, tumeimba, tumeimba! Ajira zinazotolewa vijana kwa mfano kule Marangu kule ambao wanaelekea Mlima Kilimanjaro hawa ma-tour guiders hali ya maisha waliyonayo ambayo ni hoi bin taabani hakuna sera ya kuweza kuwalinda vijana hao. Kama sekta ya utalii umesema indirectly inatoa ajira zaidi ya milioni moja, je wale ambao wanazalisha katika sekta hii hali yao inakuwa ya namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ada hizi, tozo hizi, leseni hizi ambazo wewe unamkamua ng‟ombe tu huna namna bora ya kuweza kumlisha huyo ng‟ombe ili aweze kutoa maziwa zaidi; angalia utalii wa Kusini ulinganishe na utalii wa Kaskazini na kama huu utalii wa Kaskazini unazalisha zaidi unasaidiaje utalii wa Kusini ili kweli kama sisi ni wa pili kwa vivutio vya utalii tuweze tukafaidika na rasilimali hii badala ya danadana ambazo tunapiga kila siku hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia viwanja vya ndege kwa mfano cha Musoma kiko kwenye hali gani? Angalia kiwanja cha ndege cha Iringa kiko kwenye hali gani? Angalia viwanja vya ndege vya kusini kwa mfano Masasi pale ile air strip iko kwenye hali ya namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri tu Serikali iangalie upya tozo na ada na leseni katika sekta hii ili kujenga mazingira rafiki na endelevu, na hizi fedha zinazotokana na tozo zirudi sasa kwenye sekta yenyewe na hasa kujenga miundombinu ambayo itakuwa ni rafiki na tuweze tukazalisha zaidi. La sivyo huwezi ukakamua tu wakati hutengenezi hali ya ulinzi na usalama kwenye mbuga zetu na kwenye mazingira ya utalii; hali ya miundombinu ya vyoo na hali ya maji, hali ya barabara na hali yote ya mazingira ambayo ni rafiki katika sekta ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwa wanyapori. Vitalu zaidi ya 50 vimerudishwa. Mwaka 2008/2009 Serikali ilikuwa inapata zaidi ya dola milioni 20 kwa mwaka kutokana na uwindaji. Leo hii mazingira yamekuwa tofauti kwenye soko la ushindani, mwaka jana Serikali imepata dola milioni nne tu kutoka dola milioni 20 miaka minane iliyopita. Sasa hapa tunaenda mbele tunarudi nyuma? Na hapa kwenye ukurasa wa 36 tunawapongeza TANAPA, ndio wanafanya kazi vizuri, Mlima Kilimanjaro uhifadhi umekuwa wa kwanza kivutio katika Bara la Afrika lakini je, mazingira yale yanatuweka kwenye mazingira gani ambayo leo tunaweza tukasema kweli Tanzania au wanaozunguka mazingira hayo ni rafiki na ni endelevu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe kupitia kwako kwenda kwa Serikali kwamba waangalie tena, narudi tena, kodi hizi, tozo hizi na ukiangalia wawekezaji wazawa kwenye sekta ya wanyama pori ambao ndo tungewasaidia zaidi ya asilimia 90 wameondoka wamefilisika, jiulize kwa nini? Kwanini hamkai nao? Kwanini hamzungumzi? Kwa nini hatujengi mazingira rafiki? Huwezi ukakaa mahali ukajifungia, watu wachache wanafanya maamuzi kwa wale wawekezaji ambao ndio wangesaidia taifa letu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe Tanzania yetu hii tuna haki nayo sote kwa pamoja. Mawazo mazuri ni mawazo mazuri tu hata kama yangekuwa yametoka kwa shetani. Ukisoma taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuna mawazo lukuki ambayo yataisaidia sana Serikali. Ukisoma taarifa ya kamati hasa ukurasa wa 12 na 13 ni mawazo mazuri kweli kweli lakini mbona tunarudia kauli zile zile miaka nenda rudi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nishauri kwamba yafaa Mheshimiwa Waziri afanye semina na Wabunge wote, Wabunge wampe mbinu mpya, mawazo mazuri, fikra mpya za kisasa za kuhakikisha Wizara hii miaka mitano ijayo tunatoka hapa tulipo kwenye asilimia 17 ya DGP twende hata asilimia 30 mpaka asilimia 50 tuendane na kigezo cha sisi kuwa wa pili kwa vivutio vya utalii duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Mwenyezi Mungu akubariki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE: JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwa haraka tu nianze kwa kutoa pole kwa wale wanafunzi wetu wa Lucky Vincent na Jimbo Vunjo

tulikuwa na wanafunzi wawili ambao ni Irene pamoja na Marioni walikumbwa kwenye mkasa huu. Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi. Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa la elimu nchi hii au tatizo kubwa la Taifa letu linaanzia Bungeni hapa. Suala la GPA unakumbuka mwaka 2013, Serikali ilivyoleta hoja ya kuondoka kwenye madaraja kuja kwenye GPA, Bunge hili likashangilia kweli kweli, likapitisha GPA. Baada ya miezi michache wakatoka kwenye GPA wakaja kwenye madaraja, Bunge hili hili likashangilia kweli kweli. Sasa tusitumie wingi wa itikadi zetu kuua Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na hiyo kwa sababu tangu tumepata uhuru, Serikali hii ni mwendelezo. Nimemsoma Eliufoo, hotuba yake hii hapa ya tarehe 11 Machi, 1967. Ukimsoma Eliufoo akiwa Waziri wa Elimu na akitoa ripoti ya Elimu ya mwaka 1966, zaidi ya miaka 50 iliyopita anazungumzia bodi ya kusimamia viwango vya elimu nchini Tanzania, wakati huo Mwalimu Nyerere alikuwa na Itikadi ya Ujamaa, lengo likiwa ni kujitegemea. Kwa hiyo, elimu ilikuwa inatolewa kwa misingi ya lengo la kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nimefanya utafiti, nitampatia na ripoti ya Eliufoo ambayo najua hana, ambayo ina zaidi ya miaka ambayo sijui kama ulikuwa ameshazaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli inaleta uchungu mkubwa sana kwa sababu kila Waziri anayeingia kwenye Wizara, yeye ndio sera, yeye ndio mitaala na yeye ndio kila kitu. Kama Bunge hili tulishangilia GPA, akaja Waziri huyu akabadilisha akaja kwenye madaraja tukashangilia; hivi tupo wapi? Reasoning power yetu ipo wapi? Kufikiri kwetu yamkini kuko wapi? Ndiyo sababu tunafika mahali kama Bunge haliwezi likasimamia Serikali vizuri hatuwezi tukafikiri vizuri, hatuwezi tukaiongoza Serikali vizuri, tutaendelea kupata matatizo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema no research, no data, no right to speak. Mwaka 2013 kwenye Bunge hili, Mheshimiwa Waziri wa Elimu alisema ataleta ripoti ya Sifuni Mchome, alisoma kauli ya Serikali Bungeni na tukashangilia, hii hapa; mpaka leo hii ripoti ya Mchome hatuna na wakati huo wanafunzi zaidi ya asilimia 65 walikuwa wamepata daraja sifuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wakati Waziri wa Elimu anajibu hoja Bungeni hapa, ninayo majibu yake. Serikali ni hiyo hiyo moja, kwa sababu tangu tumepata uhuru Serikali ni hiyo hiyo moja. Waziri wa Elimu akiwa anajibu tarehe 01 Februari, 2013, siku ya Ijumaa, Mheshimiwa Waziri alitamka Bungeni hapa kwamba yale yote tuliyoyapendekeza yatatekelezwa na akasema Serikali itaunda Tume ya Kudumu ya Elimu nchini ya kupambana na matatizo yote na akaweka neno “education quality assurance and control.” Bunge hili hili! Kwa hiyo, hapa tunapoteza muda tu. Tunaongea, tukishafungasha makabrasha kesho kutwa, tumeondoka, hakuna wa kufuatilia, hakuna tathmini inayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 tulizungumzia kuhusu vitabu, mwaka 2015 tumezungumza, miaka mitano mfululizo tumezungumza udhaifu wa Sekta ya Elimu na tukaambiwa kuwa vile vilikuwa vya EMMAC. Mheshimiwa Mulugo amemaliza kuzungumza, alikuwa Naibu Waziri, waliivunja EMMAC hapa tarehe 5 Juni, 2013. Sasa udhibiti wa vitabu ukapelekwa Taasisi ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli leo hii Mheshimiwa Mama Ndalichako, Serikali ya Awamu ya Tano, wanaandika vitabu, kitabu cha Kiingereza Darasa la Tatu, hapa juu penyewe tu pameandikwa I learn English Language, ndiyo imekuwa ithibati. Hapa Kazi Tu! Serikali ya Awamu ya Tano “I learn English Language,” ndiyo fedha tunazopitisha Bunge hapa ndiyo zinaandika vitabu hivi, “I learn English Language.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu katika chapter one, mwanafunzi anaanza kusoma sentensi, “good morning; thank you; good morning dear mother; good morning, lakini unaenda mpaka chapter five ndiyo wanaanza kusoma a, e, i, o, u. Niliwahi kuimba hapa na leo narudia tena. Tuliwahi kusema kwamba mtoto anaanza kusoma a, e, i, o, u hizi ni herufi kuu tamka kwa sauti kuu ndio a, e, i, o, u na kikombe u, u, u kama jicho e, e, e mwenye mpira o, o, o ni kikombe u,u,u! (Makofi)

(Hapa Mheshimiwa Mbunge aliimba wimbo wa a,e,i,o,u)

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo Kiingereza, chapter five ndiyo wanaanza kuimba a, e, i, o, u, njoo kwenye kitabu cha Darasa la Kwanza cha Kiswahili, yaani ukienda kitabu cha Darasa la Kwanza cha Kiswahili kilichopitishwa mwaka huu na Serikali hii ya Awamu ya Tano kimeandikwa taja majina ya wanyama, “yawanyama” ni neno moja. Ndiyo maana leo hii Wizara inamdhalilisha Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais yupo kwenye TV kila siku anasema “ka ta umeme,” neno moja. Yaani hata silabi haipo, “ka ta umeme,” yaani na watoto wetu ndiyo wanayojifunza “ka ta umeme,” ambayo ni silabi. Sasa quality Assurance and control, iko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Education Act ya 1962 section (3) inazungumzia namna ya kuhakikisha bodi inaweka vigezo gani, marupurupu ya Walimu, marupurupu ya Wafanyakazi, namna ya kuweka mishahara, allowance na kila kitu. Naomba urejee kwenye Education Act section (3) State of Education, inaeleza vizuri kabisa; “there-is hereby established a body to be known as the Unified Teaching’ Service…” na mengine yanaendelea, sitayasoma kwa sababu ya muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema nitampatia Mheshimiwa Waziri hii ripoti ya Eliufoo sasa ya 1967.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mengi ambayo tunayasema hapa, tunasema kwa nia njema kwa kuwa tunalitakia Taifa hili mema, lakini Serikali ambayo inaingia madarakani hata hamfanyi rejea kukaa ofisini, mwenzako amekukabidhi nini, inakuwa ni matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye vitabu sasa hivi, mbili ni namba shufwa au siyo namba shufwa; au mbili ni namba tasa au siyo namba tasa? Kuna mgogoro wanasema mbili siyo namba tasa; ndio sumu tunayolisha watoto wetu leo. Sifuri gawanya kwa sifuri wanasema ni sifuri, wakati haigawanyiki. Namba yoyote ikigawanywa kwa sifuri haigawanyiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa matatizo tuliyonayo, kwa mfano Jimbo la Vunjo, tuna Shule za Msingi 128 lakini Mwalimu mmoja kwa uwiano wa wanafunzi 61, Mwalimu mmoja kwa uwiano wa mkondo mmoja na nusu mpaka miwili, yaani hata miundombinu yenyewe, Kitaifa standard ni Mwalimu mmoja kwa wanafunzi wangapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Walimu wa Sayansi mliowaajiri tarehe 18 Aprili, 2017 hawajapewa fedha yoyote ya kujikimu na hili wala siyo la Vunjo tu, hata kule Rungwe nimepata taarifa zao, Bunda nimepata taarifa zao, Halmashauri ya Moshi nimepata taarifa zao, kote huko ni matatizo makubwa. Sasa kulikoni? Tufanye nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta binafsi, kwa nini hatuweki mazingira rafiki ya kuvutia kwa sekta binafsi yaweze kuwekeza vizuri elimu? Kuna tozo na kodi zipatazo zaidi ya 15 kwenye elimu, nani alisema elimu ni biashara katika nchi hii? Katika karne hii ya Sayansi na Teknolojia kodi 15 kwenye Sekta ya Elimu; tozo na kodi, yaani tumekosa vyanzo vingine vya mapato mpaka tunaenda kufanya elimu kwamba ni biashara!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea namna hii, mazingira ya walemavu wetu, tukienda kwenye TEHAMA, elimu ya juu yaani yapo mambo mengi. Wakati huo wa Mwalimu, walipoamua kutengeneza Taifa lenye skills, uwezo na ujuzi walijenga ile shule ya Galanos, Ifunda na Kibaha, kwa ajili ya michepuo ya kilimo na ufundi na wakajenga shule ya Wasichana ya Bwiru na shule ya sekondari ya Moshi kwa ajili ya mchepuo wa biashara, yaani unakuwa na elimu unajua unafanya nini lakini lengo lake miaka mitano, kumi, 20 ikoje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Mheshimiwa Waziri na ulikuwa kwenye sekta hii, hata tukisoma ripoti mbalimbali, ripoti hii hapa wakati huo ukiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na unajua ile ya mwaka 2010 ikatoka Juni, 2011 unaijua vizuri. Sasa haya mambo ya trial and error maana yake nini? Why? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie na nipendekeze tena kwa sababu naona muda wangu imebaki dakika moja, nasema kwamba elimu ndiyo mapigo ya moyo ya Taifa letu, mapigo ya moyo yakienda kinyume na asilia yake uhai huweza kutoweka. Tunao wajibu wa kuokoa uhai huu kwa sababu maendeleo ya Taifa lolote lile na jamii yake ni tunda la mfumo wa elimu. Lazima tujenge mifumo ya elimu inayojali utu wa mwanadamu, inayokuza utu wetu kwenye utamaduni wa Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipatia nafasi hii nami nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii au hoja tuliyonayo mezani. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwamba nilikuwa na afya iliyotetereka kwa takriban miezi sita iliyopita, lakini sasa naendelea vizuri na ndiyo maana nimeweza kusimama kwenye Bunge hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze moja kwa moja kwenye barabara za Jimbo la Vunjo. Mwaka 2016 Mheshimiwa Waziri aliniahidi kuhusu barabara ya Kawawa - Nduoni mpaka Marangu Mtoni. Barabara hii ina kilometa 29, imeshajengwa zaidi ya nusu kwa upande wa Kawawa –
Nduwoni kuna bado kilometa 4.8 na mwaka 2016 mliahidi kwamba kilometa hizo zitaingizwa kwenye Bajeti ya mwaka huu. Kwa bahati mbaya sana hizo kilometa 4.8 nimejaribu kukagua kila mahali japo sikuwa kwenye Kamati, mpaka sasa hazikuweza kuingizwa kwenye Bajeti ya mwaka huu. Naomba majibu sahihi, ahadi ya Mheshimiwa Waziri hii itatekelezwa vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya Kilema Road kwenda Hospitali, tunashukuru angalau zile kilometa mbili zimejengwa lakini hazijakamilika vizuri, ambapo zilikuwa ni eneo korofi sana. Ahadi ya Rais wakati wa uchaguzi aliahidi kwamba barabara ya Kilema kilometa 13 itajengwa yote kwa lami na siyo eneo lile ambalo ni korofi tu. Pia barabara ya Mabogini kwenda Kahe mpaka kutokea Chekereni ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Barabara za Himo Mjini ni ahadi za Mheshimiwa Rais, kwamba zote zitajengwa ili Mji Mdogo wa Himo uweze kufanana na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 nilishauri, maeneo yenye milima au maeneo yenye miinuko kwa mfano Mkoa wa Kilimanjaro, barabara zinajengwa lakini sehemu ya kutolea maji (drainage system) na maji ni adui mkubwa wa barabara. Namna gani Wizara yake na Serikali za Mitaa wanashirikiana pamoja ili Serikali za Vijiji wawe wanasafisha hiyo mitaro mara kwa mara? Kwa sababu wasipofanya hivyo, hili jukumu la Serikali Kuu, hawawezi kutekeleza wao wenyewe na mkikaa pamoja, tukishirikiana pamoja na Serikali za Mitaa wakahimiza hasa vijijini ili isafishwe hii mitaro barabara zitadumu zaidi, kwa sababu maji ni adui mkubwa wa barabara na uharibifu huu wa barabara kwa kiasi kikubwa tunazungumzia ujenzi wa barabara kitaalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumzia vizuri Mbunge aliyemaliza sasa hivi, Mheshimiwa Chenge. Ni namna gani tunafanya maintenance ya barabara? Namna gani kwenye mikataba yetu tuna-include local component capacity basic ya Wahandisi wetu ili hawa wakubwa wakishaondoka waweze ku-maintain barabara hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mikubwa kwa mfano ya reli ya kati ni namna gani tunaweka Wahandisi local component tuwanjengee uwezo wale wakiondoka waweze ku-maintain barabara hizo? Namna gani tunaiwezesha TANROADs? Nawapongeza sana TANROADs kwa kazi kubwa wanayofanya na hasa Mkoa wa Kilimanjaro, nawapongeza kweli kweli, wanafanya kazi nzuri ya kitaalam na ya kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Engineer wa TANROAD wa Mkoa wa Kilimanjaro na timu yake anafanya kazi nzuri na Ma-engineer wote kwa kweli wanafanya kazi nzuri. Ni namna gani tunawawezesha, tunawapa capacity ya kutosha ili waweze kuhakikisha miundombinu hii inaendelea kuwepo? Ni namna gani sasa hivi tunajenga reli ya standard gauge? Ni namna gani tunaandaa wafanyabiashara na namna gani ya kupitisha mizigo kwenye reli ukilinganisha na kwenye barabara, kwa sababu uharibifu wa barabara hizi ambazo zimefunguka karibu nchi nzima, uharibifu wake unakwenda kwa kasi kubwa? Angalia mvua zilivyonyesha sasa hivi barabara zinavyoharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la environmental impact assessment ambalo kwa kiasi kikubwa nimeisoma kwenye hoja ya Mheshimiwa Waziri, sioni likiwekewa kipaumbele cha kutosha. Nitatoa Mfano ili nieleweke. Ukiangalia upanuzi wa Airport ya Dodoma, suala la environmental impact assessment lilizingatiwa kiasi gani? Angalia uharibifu mkubwa uliotokea kwa binadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mwingine nieleweke. Barabara inayopita Serengeti iliyokuwa ijengwe, dunia ilipiga kelele kuhusu kusumbua wanyama wa Serengeti. Je, usumbufu wa binadamu ukoje? Miundombinu sawa ijengwe vizuri, lakini suala la kukuza utu na kuzingatia maadili ya uharibifu wa mazingira nao upewe kipaumbele cha kutosha, ambapo nikiangalia kwenye hoja ya Mheshimiwa Waziri, sioni suala la environmental impact assessment na mitigation missions zake ziko kubwa kiasi gani? Au utazingatiwa kiasi gani ili miundombinu hii iendane sambamba na inclusiveness ya wote ambao ni watumiaji wa barabara hizo?
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za Taifa letu la Tanzania, zipo kwenye classification mbalimbali zikiwepo barabara za Mkoa wa Kilimanjaro. Tusipozingatia kilimo cha matuta katika Mkoa wa Kilimanjaro, uharibifu wa udongo wakati wa mmomonyoko ambao ukija kwenye barabara unaharibu barabara hizo. Sasa ni namna gani sheria zetu, kanuni, tamaduni na mila zetu zinaweza kulinda barabara hizi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tusipoweza kuzingatia tamaduni, tukawa ni copy and paste ilimradi tumeona mradi fulani huko Ujerumani au huko Japan tukauleta hapa kwetu, wakati component ya maintenance na kutunza miundombinu hii hatujaizingatia vya kutosha, tutapata matatizo makubwa sana mbele ya safari. Tutakuwa na miundombinu ambayo iko kwenye class A, lakini namna gani ya kui-maintan ibaki class A itakuwa ni shida ili ile ya class B iende kwenye class A, class C iweze ikafanya hivyo, lakini hapo unaweza kukuta ule uelewa wa ujenzi wa miundombinu tunaendelea kusema, hii ndio class E iende class A, wakati ya class A bado inaendelea kuwa na uharibifu mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, angalia barabara inayotoka Morogoro kuja Dodoma, barabara zinazotoka Dar es Salaam kuja Dodoma, angalia barabara sasa zinazojengwa za Dar es Salaam ambayo ni maendeleo mazuri tu, lakini ni namna gani ya kuhifadhi barabara hizo, namna gani ya kuzingatia wale wote ambao watatumia barabara hiyo? Ninachozungumzia hapa, narudi kwenye central education; elimu kwa matumizi ya barabara, elimu kwa matengenezo ya barabara, elimu kwa ujenzi wa barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, angalia uwanja wa Airport. Nitatoa mfano nieleweke vizuri. Ukiangalia Airport ya Amsterdam, ndege zote zinazoruka pale, wakazi wa Aalsmeer wote imebidi wapewe compensation ya kutosha na ujenzi wa nyumba zao za sasa hivi lazima uzingatie masuala ya sound proof ili waweze kuishi vizuri katika nyumba hizo. La sivyo, miaka 10 mpaka 20 ijayo, japo tunazingatia kwenye miundombinu, tusipofikiri kwa mapana kitaalam, tutapata shida kwa ajili ya kutokutoa haki kwa uhalisia wa binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujue leo hii duniani, uharibifu mkubwa zaidi ya asilimia 96 unafanywa na binadamu. Sasa kama unafanywa na binadamu, zile known-known risk, know- unknown risk and unknown-unknown risk ambazo ni act of God; lakini kuna nyingi hapa ambazo tunasema ni act of God while is not an act of God! Ni uzembe wetu tu sisi binadamu, ndiyo tunaosababisha mambo ya mafuriko, hatuna mitaro mizuri na matatizo mengine. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Waziri lakini namwomba, chonde chonde!
Mheshimiwa Naibu Spika, nihitimishe kwa kusema tena kwamba barabara za Bunju ambazo Mheshimiwa Waziri aliahidi mwaka 2016 ahakikishe zinapewa kipaumbele ili tuweze tukazungumza vizuri na ukizingatia kwamba mimi ni Shadow Minister wa Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyezi Mungu akubariki, ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Afya na nguvu ni bora kuliko dhahabu; mwili wenye nguvu ni bora kuliko utajiri mwingi. Joshua Bin Sira 30:13. Hakuna utajiri ulio bora kuliko afya ya mwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeanza na hayo kwa sababu hatuwezi tukazungumzia maendeleo ya aina yoyote kama hatuwekezi ipasavyo kwenye afya ya binadamu. Lengo la Tatu la Maendeleo Endelevu ya Dunia yanazungumzia afya bora kwa rika zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya afya ya Tanzania ikoje? Hali ya afya ya hapa kwetu Tanzania kwa kiasi kikubwa ambapo tuko zaidi ya watu milioni 50 inatisha. Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha ifikapo mwaka 2030 zaidi ya Watanzania 85,000 watafariki kwa magonjwa ya moyo; Watanzania 42,000 watafariki kwa magonjwa ya saratani; na Watanzania 68,000 watafariki kwa magonjwa haya ya ajali. Sasa tujiulize tunashindaje changamoto zote hizi? Tufikiri globaly na tu-act locally tutaweza namna gani kupambana na changamoto hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, magonjwa ya moyo, magonjwa ya kansa, magonjwa ya figo, mashine kwa mfano ya kusafisha damu kwa kiasi kikubwa mashine hizi ziko Dar es Salaam zaidi na ni ghali sana. Kwa mfano sindano moja wakichomwa ni shilingi 67,000 unaandikiwa sindano 12, huyu Mtanzania hata wa kipato cha kati ataweza kumudu kiasi gani? Tujiulize ile linear accelerator kwa ajili ya magonjwa ya kansa ambayo tumeimba kwa zaidi ya miaka kumi ifungwe pale Ocean Road ni lini itafungwa? Tumekuwa tukizungumzia uwekezaji kwenye sekta ya afya kwamba Hospitali za Apollo kutoka India watakuja kuwekeza hapa Tanzania ili kusaidia foreign kuwekeza kwenye sekta ya afya ili kuwe na ushindani hali ikoje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikiri hivi karibuni nilikuwa natibiwa Hospitali ya Zydus kule India. Ni hospitali ya watu binafsi ina vitanda zaidi ya 550, ina vitanda vya ICU 162 na ina mashine za kisasa ukilinganisha na sisi kama Taifa la Tanzania. Hospitali za namna hii namna gani tunafanya mazungumzo nao kwa sababu penda tusipende dunia leo imekuwa ni kijiji, kama hapa kwetu Tanzania hatujitoshelezi tunaweza tuka-source hata wenzetu wa nje wakawekeza kwetu hapa Tanzania. Kwa sababu leo hii sekta ya afya ina upungufu wa wataalam zaidi ya 58% na Afrika Mashariki hapa Kenya, Uganda na Tanzania, Tanzania tunashika nafasi ya chini sana katika kuwa na watalaam wa kutosha katika sekta ya afya. Sasa changamoto zote hizi tunashiriki namna gani kuziondoa? Ndiyo maana nimesema afya ya mwili ni bora kuliko utajiri mwingine wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa kawaida kabisa wakati ilivyotokea kikombe cha babu, ni Watanzania wangapi waliokimbilia kwa babu, ni Watanzania wangapi waliopoteza maisha kwenda kwa babu na namna gani Serikali ilijitoa kwenye sera yake ikaenda ikawekeza miundombinu kwa babu na Serikali karibu yote ikahamia kwa babu kwa ajili ya matibabu kwa babu? Sasa unaweza kuona tu kwamba Watanzania wengi ni kwamba afya, afya, afya ziko katika hali ambayo siyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa mfano watalaam mabingwa kutoka nje wanaokuja hapa nchini, kupata vibali tu vya kufanya kazi (working permit), inachukua miezi sita mpaka minane lakini unawapa kwa muda wa miaka mwili tu! Sasa wale mabingwa hawawezi wakasubiri muda wote huo. Badala ya kuwapa miaka miwili wape basi hata miaka mitano au zaidi ili kuwapa confidence ya kuwekeza katika sekta ya afya. Hata tukijiuliza miaka 10 iliyopita ni mabingwa au ni taasisi ngapi za kidunia zimewekeza vizuri katika sekta ya afya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nikienda Vunjo, Hospitali ya Kilema nimeizungumzia na hata leo asubuhi nimeizungumzia. Tukiangalia Hospitali ya Kilema ina zahanati zaidi ya 13 za Maua, Makomu, Womboni, Mboni, Mbahe, Rauya, Arumeli, Uparo, Mawanjeni, Uchira, Miwaleni, Iwa na Yamu lakini Zahanati ya Miwaleni imefungwa moja kwa moja haina hata wataalam.

Mheshimiwa Mwentekiti, sasa ni namna gani tunawekeza akili na fikra zetu ili bajeti ya Wizara hii iweze kutosheleza mahitaji. Nikiri bajeti ya Wizara hii ni kidogo mno katika kutekeleza majukumu yote katika sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya mwanadamu na utu wa mwanadamu ni afya kwanza. Mwanadamu aliyeshiba vizuri na mwenye afya nzuri, na nikupongeze Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu na Naibu wako kwa kazi kubwa mnayofanya lakini bajeti yenu kidogo mno. Katibu Mkuu atadaiwa huku na kule, Dkt. Mpoki, anafanya kazi nzuri tu lakini sasa afanyeje wakati bajeti ni kidogo kiasi hiki? Kwa hiyo, tujifikirie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge, tumepewa mamlaka na Katiba ya kuisimamia na kuishauri Serikali. Tukiacha tofauti ya itikadi zetu hapa tukaamua kuisimamia Serikali vizuri, tunaweza tukapangua hata bajeti hii tukaiongezea Wizara ya Afya bajeti zaidi ili binadamu aweze kushiba vizuri, binadamu aweze kuwa na uelewa vizuri na aweze kuondokana na haya matatizo ambayo ni makubwa katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto ya miundombinu katika Hospitali ya Kilema pamoja na Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi. Tuna changamoto ya uzio kwa mfano pale Mawenzi na miundombinu yote ile ni chakavu. Pale Kilema hatuna Kitengo cha ICU, ujenzi wa jengo la utawala ni matatizo, uzio wa hospitali ni matatizo, nyumba za watumishi ni matatizo, marupurupu kwa watumishi kwa ujumla wake ni matatizo wanafanya kazi katika hali ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba chonde chonde tuangalie ni namna gani Wizara inashirikiana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kuwa na mawazo mapana zaidi na kuangalia wenzetu duniani wanafanya nini ili tuweze kuondokana na changamoto hizi tukawekeza vya kutosha katika sekta hii ya afya ambayo ni duni kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujifunze kwa wenzetu duniani na tuangalie wanafanya nini, kwa sababu kila mtu hapa atazungumzia Jimbo lake la uchaguzi, atazungumzia sehemu yake, bajeti ni kidogo, lakini Wabunge tunayo nafasi, tunayo nguvu, tunao uwezo wa Kikatiba wa kuweza hata kupangua bajeti hii, kwa sababu bajeti kubwa haijasomwa na wakati wa kukaa na Serikali ili Wizara hii ikaongezewe bajeti ili performance ya Watanzania katika Wizara ya Afya iweze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, chonde chonde niombe tena, Serikali inaweza ikafanya maamuzi kwenye miundombinu, barabara, reli na mengineyo wakawekeza zaidi kwenye private sector, lakini fedha tunazopata ndani tukawekeza zaidi kwenye ile miundombinu inayokuza utu wa mwanadamu zaidi. Kwa mfano, afya, elimu ambayo ndiyo kipaumbele namna gani wataalam wetu wa humu ndani tunawapa haki zao, stahili zao, watumishi wetu. Madaktari wetu wa humu ndani wako kwenye hali gani, Wakunga wako kwenye hali gani, wauguzi wako kwenye hali gani, vituo vyetu vya afya viko kwenye hali gani. Kwa mfano, pale Vunjo Kituo cha Afya cha Kirua, Kituo cha Afya cha Mwika na Hospitali ya Marangu vile vituo vyote vya afya na zahanati zote zinazotoa huduma wanatoa huduma nzuri sana lakini katika mazingira magumu sana.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali za Rufaa kwa mfano, KCMC, Bugando angalia Hospitali ya Muhimbili kweli tunazungumza kwamba hali ya Muhimbili bado ni tete sana angalia wagonjwa wanalala ndani wane, watano wajawazito hawa zaidi ya wawili watatu, wengine wako katika hali ambayo siyo nzuri sana tuwe wa kweli. Unaweza ukasema hapana, lakini ukienda Hospitali ya Mwananyamala, Temeke haziridhishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaomba chonde chonde Wizara hii naomba iongezewe bajeti ili iweze ikatoa huduma yake kwa kukuza utu wa mwanadamu. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kwenye cover la juu kabisa ukurasa ule wa kwanza, anaonyesha binadamu wa kale walioishi zaidi ya miaka milioni 3.6. Kulikuwa na hoja hapa ya nembo ya Taifa. Nembo ya Taifa (Uhuru na Umoja) ni alama za Taifa. Hatuhitaji mpaka watu wafe ndio tuanze kuwakumbuka kwenye mambo mazuri waliolifanyia Taifa. Huyu Mzee Francis Maige Ngosha, aliye-design hiyo nembo ya Taifa na anaishi bado na yuko kwenye hali hoi bin taabani maisha yake. Naipongeza sana kituo cha ITV Ndugu Godfrey Monyo jana alivyoonyesha tukio la mzee huyu. Tuitake Wizara ya Maliasili na Utalii ni nembo ambayo ni kielelezo cha Taifa, waagize mara moja Mzee huyu ajengewe makazi mazuri na apewe matibabu kwa ajili ya kuendeleza vigezo vya Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Wizara hii uwezo inayo ni sehemu ya mali kale na Mzee huyu amefanya kazi kubwa tuachane na Urasimu Serikalini, Wizara yake ina uwezo na Mzee huyu yupo Jimboni kwako wamjengee makazi ya kisasa, wampe matibabu mazuri ili mzee huyu aweze kufaidi akiwa hai asisubiri mpaka afe ndio tuanze kusema mazuri ya kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema ya kupongeza ITV kwa tukio la jana la Francis Maige Ngosha na kazi nzuri aliyoifanya, sasa niombe nizungumzie sekta ya utalii kwa ujumla wake. Ningeomba nianze na maswali, je, Tanzania tunashika nafasi ya ngapi sasa baada ya takribani miaka kumi mfululilizo kwa vivutio vya utalii duniani. Tunashika nafasi ya ngapi kwenye yale mataifa 133 ambayo tunajiwekea kwenye vigezo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, akishatujibu wakati wa kuhitimisha, atueleze kwamba kwenye miundombinu na ushindani kwenye sekta ya utalii, Tanzania tumewekeza kiasi gani ili kushindana na nchi wenzetu kwa sababu Tanzania tuliokuwa tunashika namba mbili baada ya Brazil tulikuwa tunashika nafasi ya 110 kati ya nchi 133 kwenye miundombinu na ushindani wa utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pato letu la Taifa sasa hivi asilimia 17.5 inatokana na utalii. Miaka zaidi ya mitano iliyopita tulikuwa ni asilimia 17 hiyo hiyo miaka minne/mitano iliyopita 17.5. Lakini Serikali walitamka Bungeni hapa mwaka 2014 kwamba ifikapo mwaka 2020 sekta ya utalii itaingizia Taifa hili Pato la Taifa kwa mwaka walikuwa wana malengo ya zaidi ya asilimia 30. Sasa mbona mfululizo tunabaki kwenye tarakimu hiyo hiyo asilimia 17.5 na mapato ya fedha za kigeni zaidi ya asilimia 25, lakini ili uweze kumkamua ng’ombe vizuri inabidi umlishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya utalii ina kodi nyingi za kero, ina tozo nyingi za kero na sasa hivi kuna kodi na tozo zaidi ya 57. Mimi natoka kwenye eneo la utalii, ukiangalia wanaohudumia watalii, ukiangalia watu wa kati, Makampuni yanayofanya kazi ya utalii, kodi zilizopo ni kero kweli kweli na tozo. Yasiwe ni maneno yangu, kwenye hoja ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 98 katika changamoto anazozungumza katika sekta ya utalii ni pamoja na huduma hafifu zinazotolewa kwenye sekta ya utalii. Gharama za juu za huduma ya utalii, anasema gharama za juu, anakiri kwamba Tanzania is the most expensive destination katika region hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Tanzania tuko expensive kodi hizi, tozo hizi ndizo zinazosababisha nchi yetu tunazidi kuondoka kwenye asilimia 17.5 ya Pato la Taifa kwa sababu tunaendelea tu kukusanya kukusanya wakati ng’ombe huyu hatumlishi. Hatuna mazingira rafiki, hatuna mazingira mazuri tunayoweka kwenye sekta ya utalii. Wekeza kidogo usiangalie kuvuna leo hii, wekeza vizuri, wekeza vizuri tuwe na washindani. Leo hii Afrika ya Kusini, Zambia, Mozambique, Mauritius, Botswana, Namibia wanatushinda kwa kasi kubwa na Kenya walikuwa na mgogoro na hali yao ya ulinzi na usalama, lakini na wao wanakuja kwa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serengeti eneo lake ni zaidi ya kilometa za mraba 14,750; Masai Mara wana kilometa za mraba 1,510 lakini wanashindanaje na sisi, vivutio vyote tulivyonavyo hivyo, ufukwe wa bahari ambao ni kilometa 1,424; sisi ni kwamba bado tunaendelea kupiga danadana hatufanyi maamuzi, na kama ukiondoa kodi hizi, tozo hizi kwa mfano, concession fee, mtalii akitaka kuja nchini anamkataba wa zaidi ya mwaka mmoja, miwili, mtiatu kabla. Lakini hapo hapo unataja kwamba kuanzia labda mwezi wa saba, concessional fee inatoka dola 25; dola 20 mpaka dola 50. mtalii wa namna gani atakuja kwenye nchi ambayo ni expensive kiasi hichi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima kujenga mazingira rafiki, mazingira mazuri, mazingira ambayo yanakubalika. Kwa mfano, Tarangire kule na Manyara, sasa hivi mnatoka kwenye dola 15 mnaenda mpaka dola 35, watalii wa namna gani watakuja namna hii. Concession fee kwa mtalii kwa siku tano ni dola 635 ukiweka na VAT ndani yake ni zaidi ya dola 700, utaenda sehemu ambayo ni rahisi na yenye mazingira mazuri ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili utalii wetu kweli uweze ukawa na maana hata suala la single entry kwenye sekta hii ya utalii, anaingia mbugani anataka kutoka, akae kwenye hoteli zilizoko karibu na maeneo ya mbugani, arudi tena wakati wa jioni angalau akaone wanyama wametulia, lakini una mdai tena. Hii inaingiaje akilini, jenga mazingira mazuri, let us think globaly but act locally. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipojenga mazingira mazuri, hata Sera yenyewe ya Utalii wa Taifa ya mwaka 1999 na mazingira yake yote hayo, kwa mfano, Mlima Kilimanjaro, lango kuu la kuingia Mlima Kilimanjaro linapita Marangu katika Jimbo la Vunjo, vijiji vinavyozunguka Mlima Kilimanjaro maeneo ambayo wanatakiwa kuwa rafiki, sekta hii inahudumia namna gani vijiji hivi viweze vikaonekana kweli mazao ya Mlima Kilimanjaro katika sera, kama ni asilimia 10; ni asilimia 20 ya mapato yale yanabaki pale kujenga mazingira rafiki na mazuri katika sekta hii ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukiyazungumza haya kwa mfano suala la park fees, VAT kwenye park fees, kwa nini uweke VAT kwenye park fees kama umeshaweka VAT kwenye usafiri, umeshaweka VAT kwenye malazi ondoa VAT kwenye park fees ili mazingira haya yaweze kuwa rafiki kwa vivutio vya utalii, la sivyo tutakuwa tunapiga danadana hapa hapa asilimia 17.5. Tufanye maamuzi ya kuweza kuweka Tanzania kuwa ni sehemu rafiki Tanzania ni sehemu yenye kuvutia watalii, Tanzania ni sehemu yenye miundombinu mizuri ya utalii, Tanzania ni sehemu ambayo yanajenga mazingira rafiki na Bodi ya Utalii ipewe madaraka ya kutosha. Bodi ya Utali na vile vyama vinavyozunguka waweze kukaa pamoja washirikishwe vizuri. Suala hili liwe ni inclusiveness, washirikishwe vizuri kutoa mawazo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano nimesoma hotuba hii yote Tanzania Tour Operators (TATO) ambapo kwenye hotuba wala hawakujulikani kana kwamba wanafanya kazi katika Taifa la Tanzania. Sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri maeneo yote ya Tanzania ambayo yanazungukwa na mbuga hizi yajengewe mazingira rafiki. Walikuwa wanazungumza Selous jana, mbuga ya Selous ambayo ni kubwa hata wanafunzi wetu kwenye vitabu vya shule hawafundishwi kwamba Tanzania tuna national park kama maeneo ya Selous, Tanzania wanafundishwa kuna Serengiti, Mikumi, Manyara na Ngorongoro, je, mbuga kama za Selous, Ruaha ziko nyingi tuu vivutio viko vingi tuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuvitangaze hivi tuwekeze kweli kweli, fedha hizi za maendeleo zilitengwa kwenye bajeti ya Wizara hii kwa ajili ya kutangaza na kuvutia utalii Tanzania ni kidogo mno. Wekeza vizuri na wewe umekili kwamba bajeti ya utalii ni kidogo kwenye hotuba yako ukurasa wa 98, sasa kama bajeti ya utalii na utalii huo huo unaleta mapato, mapato haya Serilkali ifikilie kwa mapana tuwekeze ipasavyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Ninaamini nina dakika kumi za kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii. Kwanza kabisa nianze na maswali kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua tu, Serikali uwekezaji wake katika sekta ya afya ni asilimia ngapi? Sekta binafsi uwekezaji wake katika afya kwa ujumla wake ni kiasi gani na ndani ya sekta binafsi, mashirika ya dini yanachangia huduma ya afya kwa kiasi gani? Ni kiasi gani kuna ubia kati ya Serikali na sekta binafsi? Kuna ubia kiasi gani kati ya mashirika ya dini na Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu lengo la nne la Malengo Endelevu ya Dunia inazungumzia afya bora kwa wote ifikapo mwaka 2030. Nawapongeza wataalam wetu katika sekta ya afya, Waziri, Katibu Mkuu Dkt. Mpoki, wataalam; akina Profesa Mseru, akina Dkt. Janabi na wenzao, KCMC, Bugando na wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwe wakweli tu, katika Taifa letu, sekta ya afya japo wanafanya kazi kubwa na juhudi kubwa hatujawawezesha sekta hii kibajeti waweze wakatekeleza majukumu yao inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali yetu iko kwenye hali hii, basi inabidi kuweka vivutio rafiki, mazingira rafiki, hata tukaangalia motisha kwa sekta binafsi tuweze kupata wawekezaji wakubwa wanaoaminika waweze wakasaidiana na Serikali katika sekta ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kufanya utafiti nimeona ni Aga Khan peke yake ambayo imeweza kuwekeza zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa sasa kwenye sekta ya afya.

Wako wapi wawekezaji wakubwa kama Aga Khan wawekeze ili afya ya Mtanzania, utu wa Mtanzania ukaweza kupata nafasi yake? Duniani kukoje, nikiangalia namna gani tunaweza tukafanya a medical tourism katika maeneo fulani hapa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natoka Vunjo, pale Vunjo tuna Hospitali ya Kilema ya Kanisa Katoliki, ubia na Serikali; tuna Hospitali ya Marangu ya KKKT; Kirueni wanaanzisha hospitali yao kule Mwika ambapo wana vifaa vya kisasa; wana MRI na CT Scan, lakini hawana majengo ya kutosha. Vifaa hivi wamepata Canada, Serikali ishirikiane nao ili hata watu waweze kutoka nje kuja kutibiwa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale kuna kupanda Mlima Kilimanjaro; hali ya uokoaji wa wapanda Mlima Kilimanjaro, miundombinu rafiki tunaifanyaje? KCMC iko pale, tunatokaje ndani ya box ili tuweze kusema eneo fulani tunatengeneza a medical tourism na facilities za kutosha zipo na tukaacha ku-export au kwenda kutafuta huduma za afya nje ya Watanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hayo kwa sababu ukiangalia huduma zinazotolewa hapa kwetu Tanzania, na mimi ni mhanga, Mheshimiwa Waziri unajua hilo. Ni kwamba inabidi tujitoe na tufikiri kwa mapana kwamba namna gani uhai wa mwanadamu; nimesoma kitabu cha Biblia Takatifu leo asubuhi Yoshua bin Sira ule mstari wa 16:30 inasema: “Hakuna utajiri ulio bora kuliko afya ya mwili na hakuna furaha iliyo bora kuliko furaha moyoni.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia Tanzania leo hii tumewekwa wapi kwenye happiness index? Tumewekwa pamoja na Yemen, Syria na Burundi. Tumeshika nafasi ya 153 kati ya nchi 156. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa lazima tutoke tufikiri kwamba kwa nini hatuna furaha moyoni kwenye mambo ya ustawi na kwenye afya zetu? Tukiangalia, Watanzania ni wagonjwa kiasi gani kwenye utafiti? Wataalam wetu tunawasaidia kiasi gani? Kama huyu ni daktari, unamwezesha namna gani? On call allowance, risk allowance, huduma nyinginezo ambazo madaktari wetu hawazipati, waka-concentrate kwenye kutibu tu na masomo yao ya sayansi yalivyo magumu? Unakuta daktari wetu huyu anafuga kuku, huyu ana bar, huyu anaenda kutafuta income nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni namna gani tunawaheshimu madaktari wetu? Kwa mfano, daktari ana kitambulisho chake, akipita polisi anamsimamisha, umeongeza speed, amwambie ninawahi kwenda kutibu, polisi anamwachia. Huwezi ukamweka daktari kwenye kundi moja na walevi. You cannot do things like that. (Makofi)

Mjeshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima tufikiri kwa mapana, ni namna gani tunawapa incentives madaktari wetu waweze kufanya research. Wizara yako inatuonesha, kuna upungufu wa wataalam zaidi ya asilimia 50 katika sekta ya afya. Wauguzi, Manesi, Madaktari wenyewe, Madaktari Bingwa na kwingineko. Namna gani tunafanya in training na out training? Nitoe mfano, think globally.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi uliopita nilikuwa Zydus Hospital; imeajiri watu wauguzi wake pamoja na madaktari zaidi ya 1,200; lakini wanaotibiwa pale kila siku, wanaoingia na kutoka pamoja na waliolazwa na madaktari wote kwa pamoja ni zaidi ya watu 5,000 kwa siku. Ni shirika kubwa ambalo limewekeza kweli kweli. Serikali ya India imeshirikiana nao namna ya kutoa huduma iliyo bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna mtaalam mmoja anaitwa Dkt. Daria Singh, anaweza akafanya operesheni nne kwa siku moja ya knee replacement na accuracy asilimia 100. Anafanyaje? Ni kwamba huyu amewezeshwa vizuri, amefikiri vizuri, anajua kazi yake anaifanyaje. Sasa hebu tujiulize hapa kwetu, kulikoni? Kuna nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni vyema Mheshimiwa Waziri tukafanya in training na out training, yaani tukaomba wataalam kama hawa wa Zydus Hospital wakaja kutusaidia kufundisha humu ndani, na sisi tukaenda tukasoma kule kwao. Wataalam wetu tukafanya programu ambazo ni exchange program na tukaweka mazingira yaliyo rafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuje kwenye vitendea kazi. Kwa mfano, Waheshimiwa Wabunge hapa leo hii wanazungumzia X-Ray kwenye mikoa. Kweli hii ni karne ya kuzungumzia X-Ray, CT Scan na MRI? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulizungumzia na Serikali imeahidi miaka nenda rudi kuhusu linear accelerator kwa ajili ya wagonjwa wa kansa; mpaka leo hii hakuna linear accelerator nchi hii. Tulikuwa tunamsifia sana Dkt. Janabi na wenzake hapa, mambo ya Cardiac Cath. Lab.; Tanzania tunazo tatu tu, ambapo tuna population ya watu zaidi ya milioni 50 compared na wenzetu wa Kenya wanazo Cardiac Cath. Lab. zaidi ya tisa. Wako kwenye hali bora kuliko sisi katika mazingira haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukimsoma Yoshua bin Sira sura ya 30:17 inasema: “Afadhali kifo kuliko maisha ya taabu na pumziko la milele kuliko ugonjwa wa kudumu.” Ukijaribu kuangalia ni kwa nini anasema hivi?

Mheshimiwa Naibu Spika, tujiulize kweli afya zetu, ilivyotokea kikombe cha kwa babu kinatibu, karibu nusu ya Serikali yote ilikimbilia kwa babu kwa sababu unaweza kuona afya yako siyo nzuri. Sasa tunafanyaje? Miundombinu ile tuliyopeleka kule, tunaiwezeshaje sekta hii ya afya ili afya za Watanzania ziwe bora? Tuwe wakweli kwamba afya za Watanzania ziko hoi bin taabani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Bima ya Afya hospitali nyingine zinakataa, hasa hospitali za watu binafsi kwa sababu haitoshelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nayapongeza sana mashirika ya dini. Niwe mkweli kabisa! Nawapongeza sana KKKT, Wakatoliki pamoja na BAKWATA kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuwekeza kwenye sekta ya afya. Sasa tuwape lugha nzuri, tushirikiane nao vizuri; wao wana mtandao mkubwa duniani waweze kuleta ile technology na ile misaada tukashirikiana kwa pamoja, kwa kuwa dunia yetu hii ni kijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba chonde chonde, inaonesha hata kwenye kitabu chako na kitabu cha Kamati kuhusu lishe, hali ya Tanzania lishe siyo nzuri. Hili tatizo la lishe lilianza tangu miaka ya 1978 pale...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi wanapostaafu hawapatiwi haki zao stahiki kwa wakati. Kwa mfano, waliostaafu mwaka 2017 mwishoni wanatakiwa wahame kwenye nyumba za Polisi kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muundo wa Jeshi letu la Polisi kuwa chini ya Wakuu wa Mikoa na wa Wilaya (Kamati za Ulinzi na Usalama) linawaweka katika hali ngumu kiutendaji (Rejea Ibara ya 147 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Himo kinafanya kazi kubwa (huduma eneo la mpakani na nchi jirani), hawana vitendea kazi vya kutosha hasa magari; Ofisi ni ndogo na ni chakavu; makazi yao hayatoshelezi na chakavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, weledi wa Jeshi letu la Polisi uwekwe msisitizo hasa mahusiano na jamii (elimu endelevu)
Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwanza, Tanzania tumebahatika kuwa kwenye eneo zuri sana la vivutio hivi vya utalii. Ukiangalia ikolojia yetu Tanzania na ukiangalia vivutio vya utalii Tanzania na tukijilinganisha na dunia sisi tuko kati ya wale watano bora duniani kwenye vivutio vya utalii. Kwa mfano, ukiangalia GDP ya Taifa letu na ukiangalia fedha za kigeni za Taifa letu leo utalii unaongoza nchi yetu hii kwenye fedha za kigeni. Kwa takwimu za mwaka jana zilikuwa ni shilingi bilioni 2.4 ambayo ni asilimia 28 ya fedha zote za kigeni zinatokana na utalii.

Mheshimiwa Spika, sasa utalii huu unawezeshwa na zile hifadhi zetu za Serengeti ikiongoza, KINAPA, Tarangire, Manyara, Arusha na Ngorongoro pia. Tunahitaji Wizara ikawa na vision yenye mwelekeo au mpango mkakati sahihi. Watuambie ule mpango mkakati wa 2022 umefikia wapi ili ku-double GDP na forex kwenye utalii? Kwa mfano, Southern Corridor, Ruaha, Mikumi na kwingine, hizi hifadhi tano ambazo ndiyo zina break even, ambazo zinazalisha zile nyingine na TANAPA wanafanya kazi nzuri sana chini ya Jenerali Waitara kama Mwenyekiti wa Bodi, Allan Kijazi - Mkurugenzi wa Bodi, kwa kweli nawapongeza sana TANAPA kwa kazi kubwa sana wanayoifanya, wanafanya kazi kubwa sana na nzuri katika Taifa letu lakini tujiangalie kidunia miundombinu hii ya utalii ikoje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa takwimu za mwaka juzi tunaonekana kwenye ushindani wa miundombinu ya utalii zikiwepo barabara zetu, viwanja vyetu vya ndege, vyuo vinavyohudumia watalii, hoteli kwa pamoja tunashika nafasi ya 110 kati ya nchi ya 133. Sasa ni namna gani tunaimarisha hii miundombinu kwenye hifadhi zetu iweze kwenda sambamba na kuhakikisha tuna- double GDP na forex yetu na kuhakikisha hifadhi zote hizi mpaka za Moyowosi anazosema Mheshimiwa Nsanzugwanko na Tanzania yote Mwenyezi Mungu aliyotujalia mambo haya yanakuwa ni endelevu. Tukiwekeza vizuri hapa, hata sekta nyingine zikisuasua lakini hii Mwenyezi Mungu aliyotupatia tuhakikishe inakwenda kwa kasi kubwa. Kwa hiyo, tuwekeze miundombinu ya kutosha kwenye sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ile asilimia 10 ambayo TANAPA wanachangia kwenye Mfuko Mkuu basi iondolewe moja kwa moja irudi kwenye miundombinu ya utalii. Vilevile Southern Corridor ambayo imeshaanza tusiiachie katikati na hizi nyingine zote ambazo zimeletwa kwa Azimio hili tuziangalie ili Tanzania iwe ni sehemu nzuri na salama kwa vivutio vyetu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa muda ulionipatia. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza siku ya leo.

Mheshimiwa Spika, nitajikita zaidi kwenye Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na mapendekezo yao na ushauri wao ni mzuri sana, nawapongeza Kamati. (Makofi) Mheshimiwa Spika, kwa kiasi kikubwa wamefafanua baadhi ya malengo na mwelekeo wa elimu yetu Tanzania. Lengo la Nne la Maendeleo Endelevu Duniani ni elimu bora, sawa, shirikishi kwa wote. Tunajiuliza leo hii, je, Sera yetu ya Elimu Tanzania na mitaala, muhtasari na vitabu vinaakisi mahitaji ya kusudio hili au lengo hili la dunia? Je, mahitaji ya msingi ya wanafunzi wetu, marupurupu ya walimu wetu, mazingira rafiki katika shule zetu, yanaweza yakaakisi lengo
hili la dunia?

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu ukiangalia Sera yetu ya Elimu ya sasa hapa Tanzania na Mheshimiwa Waziri aliwahi kusema hapa Bungeni kwamba ina matatizo, tunajiuliza leo hii Tanzania tunafuata sera ipi ya elimu? Ni Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 au ni Sera ya Eimu ya mwaka 1995? Hii ni kwa sababu Sera ya Elimu ya sasa inasema elimu msingi ni miaka sita baadaye miaka minne lakini kuna pre-primary ambayo inakuwa ni miaka 11. Leo tunafata Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, kwa hivyo elimu yetu inakuwa haina mfumo ambao ni shirikishi, bora na unaelekeza usawa kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu tumekuwa tunafanyia elimu yetu sample na majaribio ya mara kwa mara, kwa mfano, suala la Big Results Now, ninayo nakala yake hapa, ukiangalia yaliyokuwa yameainishwa humu ndani yalikuwa ni mazuri sana. Hata hivyo, kisoma taarifa hii ya Katibu Mkuu ya utafiti ya Wizara ya Elimu, ambayo ilikuwa inaeleza elimu yetu kwa miaka mpaka 2024, ukurasa ule wa pili inasema, tatizo kubwa tulilonalo katika elimu yetu ni masuala ya kimfumo, kuna upungufu mkubwa wa kimfumo. Ni Wizara inasema yenyewe. Ukienda mbele zaidi ukurasa wa 62 inasema: “Usimamizi na uendeshaji wa elimu, uliotajwa kwa kiwango kikubwa, ni chanzo cha matatizo ya elimu Tanzania.”

Mheshimiwa Spika, sasa hii ni Serikali yenyewe inasema hivyo, leo hii tunajiuliza, hivi kweli mfumo wetu wa elimu, taarifa ya Serikali za Mitaa hapa, ya Mheshimiwa Rweikiza ameiwasilisha vizuri; hivi masuala ya kisera, kimuundo, kiuendeshaji yako TAMISEMI au yako kwenye Wizara yenyewe ya Elimu? Je, Waziri wa Elimu au Katibu Mkuu wa Elimu na Katibu Mkuu wa TAMISEMI wanaingilia vipi katika usimamiza wa Maafisa Elimu katika ngazi za Mikoa, ngazi za Halmashauri na Wilayani na kwingineko?

Mheshimiwa Spika, tatizo hili kwa kiasi kikubwa, ndiyo maana maandiko matakatifu yanasema, watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Ninasema hivyo kwa sababu, ukiangalia Tanzania ya leo, product ambayo tunazalisha sasa hivi; ukichukua Elimu ya Msingi, Sekondari, mpaka Vyuo Vikuu, kwa mwaka tunazalisha watu zaidi ya 1,200,000. Ifikapo miaka kumi ijayo, tutakuwa na vijana zaidi ya milioni 12, hawajui waende wapi, kwa sababu elimu yetu haimfanyi huyu kijana akawa mbunifu, awe skilled akajua kabisa ninamaliza elimu kwa kiwango hiki, naenda wapi.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu ni mara nyingi na nime-check kwenye Hansard ya Bunge ya mwaka 2013, niliwahi kusema kwamba udhaifu ulioko katika Sekta ya Elimu hapa Tanzania ndiyo unaosababisha tabia ya Watanzania walio wengi wa kutokujiamini katika kufanya majukumu yao, kupotea kwa mila na desturi za Kitanzania, kumomonyoka kwa uadilifu miongoni mwa wafanyakazi wetu, kuporomoka kwa uwajibikaji, yako mengi ambayo yaliainishwa.

Mheshimiwa Spika, athari zake sasa nini? Zinasababisha nini katika elimu yetu? Athari zake ni pamoja na ugumu wa elimu yenyewe, huduma mbovu zinazotokea katika sekta mbalimbali, viwango duni vya ubora wa bidhaa hii inayozalishwa hapa Tanzania, uharibifu wa mazingira yetu, udhaifu katika kukabiliana na majanga ya aina mbalimbali hata namna gani tunasimamia TEHAMA yetu.

Mheshimiwa Spika, hii ripoti ukiisoma tufanye nini kwenye utafiti ili tujue tunaenda wapi, ukurasa wa 55 unasema, nchi za Afrika zimekubaliana kwamba 1% ya GDP yake iwekezwe kwenye utafiti, lakini taarifa ya Kamati inaonyesha hapa inasema ni asilimia 0.034 ndiyo inayotolewa kwenye utafiti, ambapo kutokana na GDP yetu utafiti peke yake, COSTECH wangetakiwa wapate one point two trillion kwa sababu ndio tunajijua tunataka twende wapi; lakini leo hii, wanapata shilingi bilioni 40 tu. Kwa hiyo, hapa kitakwimu ni kwamba tunaiua elimu yetu sisi wenyewe.

Mheshimiwa Spika, sasa ukiangalia Vyuo Vikuu, mathalan, nilikuwa naangalia kwenye utafiti, ukiangalia Vyuo Vikuu 28,000 duniani, kwenye Ranking Web of Universities; 28,077. Tanzania tuko wapi? Tanzania kitakwimu kati ya Vyuo Vikuu 28,000 mpaka 10,000 hapo katikati, Tanzania ndiyo tunaingia hapo kwenye University zetu tano tu. Tuko kati ya 5,000 mpaka 10,000. Ni kwamba sasa tuko kwenye dunia gani Tanzania? Yaani katika 5,000 bora hatumo duniani.

Mheshimiwa Spika, naomba tu kwa unyenyekevu mkubwa, Vyuo vyetu Vikuu ukiangalia mfumo wenyewe wa utoaji mikopo, hauoani na mikopo inarudishwa. Je, ule utaratibu ambao tulishawahi kuusema Benki, tukawa hata na Benki ya mikopo, watu wanaenda kukopa kule kwenye Benki moja kwa moja na mkaweka mfumo wa namna gani wa kurudisha hizo fedha ili mikopo yetu iweze ikawa ni endelevu umefikia wapi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ubunifu uko wapi? Vyuo Vikuu vya Umma viko hoi bin taaban. Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tangu mwaka 2014 wale wanataaluma; kinaidai Serikali zaidi bilioni 16.1 na Wahadhiri hao, Wanataaluma wako kwenye hali ambayo ni ngumu sana, ambayo inaleta matatizo.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa ajira, zimefanyika teuzi mbalimbali kutoka kwenye Vyuo Vikuu, replacement yake ikoje? Ndiyo maana unakuta Vyuo Vikuu vyetu leo hii zaidi ya watu wenye umri wa wanataaluma Wahadhiri wenye miaka 70 na kuendelea, bado wanapewa ajira za mikataba katika Vyuo Vikuu na efficiency inakuwa kwenye hali ya namna gani?

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mazingira, kuna mtaalam mmoja aliwahi kusema kwenye dunia ya leo “with technology things are changing faster than we can imagine, knowledge is for free for those who loves it, an educated person is the one who loves knowledge and seek it.”

Mheshimiwa Spika, nimelisema hilo kwa sababu kama hatutakubali, tukarudi miaka ya 1980 ambako kwenye Kamisheni ya Jackson Makwetta, ambayo alipendekeza tufanye nini Tanzania; na mpaka miaka 13 baadaye ndiyo ikatoka sera ya kwanza ya mwaka 1995.

Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa kabisa, niiombe Serikali ya Awamu ya Tano, Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli, aunde Kamisheni ya Elimu Tanzania kabla ya Taifa letu la Tanzania halijaangamia. Kamisheni ya Elimu ambayo itatuambia sisi humu ndani tunataka nini, Kamisheni ya Elimu itakayojadiliana kama Watanzania tunataka mfumo wa namna gani vijana wetu wajiendeleze; Kamisheni ambayo tutajua duniani kuko namna gani; Kamisheni itakayotuonyesha mfumo wetu wa elimu uwe namna gani; Kamisheni ambayo itatuonyesha Tanzania ya leo tunataka iende upande gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kumalizia kwa maneno ya Yeremia 22:29 inasema, “Ee nchi, nchi, nchi lisikie neno la Bwana.”

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunisikiliza.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Mpango uliopo mbele yetu. Nami nitachangia hasa ule ukurasa wa 11 na 12, idadi ya watu na mwenendo wa umaskini wa Taifa letu na viashiria vya umaskini kwa ujumla wake. Nimetafakari kwa kina baada ya kuusoma Mpango wote na huu wa miaka mitano nikarejea kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwamba Mpango huu umejikita zaidi kwenye Dira ya Maendeleo ya 2020-2025, Malengo Wndelevu ya 2020-2030 na Mpango huu wa miaka mitano na huu wa sasa kuanzia 2016/2017-2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere alituasa na imekuwa ni msingi wa kimaadili wa Taifa letu kwa baadhi ya wosia mbalimbali za Mwalimu Nyerere. Kati ya maneno ya Mwalimu Nyerere ni kwamba, siyo maneno, falsafa ya Mwalimu Nyerere ni kwamba ili tuendelee (maendeleo) Mpango, unatengeneza Mpango wako ili uendelee vizuri tunahitaji watu, tunahitaji ardhi, siasa safi na uongozi bora. Uongozi ukisoma kwenye malengo endelevu ya dunia ni uongozi shirikishi. Mpango unaanzia chini unaenda juu lakini kwingine maeneo mbalimbali unakuwa vice versa, unaweza ukaenda horizontal, au unaweza ukatoka juu ukaenda chini lakini hasa kushirikisha watu wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wetu ili ufanikiwe lazima msingi uimarike zaidi, hata nyumba yako ukijenga ili iweze ikasimama imara msingi ni jambo muhimu kuliko jambo lingine lolote. Msingi ulio imara katika kuhakikisha Mpango huu unafanikiwa inaelezea hapa katika mambo matatu inasema suala la usalama, amani, ulinzi na utengamano wa kijamii. Utengamano wa kijamii, jamii inapokuwa pamoja inafikiri pamoja, inashirikiana pamoja kwa sababu maendeleo ni yao. Dunia ya leo mpango au jambo lolote lenye tija limewekewa vigezo vikuu vinne, kigezo cha kwanza ni kukuza utu wa mwanadamu, utu! Kigezo cha pili ni utulivu wa fikra (piece of mind); kigezo cha tatu ni rasilimali muda; na kigezo cha rasilimali fedha. Unaweza ukakopa fedha, deni la Taifa limefikia trilioni 52.3 sawa na utazilipa kesho lakini huwezi ukakopa rasilimali muda, muda ukishaondoka umeondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 2002 tukiwa viongozi wa vyama tulisema ili tushirikiane na Serikali yetu vizuri, Mzee Mangula akiwa Katibu Mkuu wa CCM lazima tuandae Chuo cha Kitaifa cha Kuandaa Viongozi. Viongozi hawaokotwi kwenye majalala, viongozi huandaliwa. Naona hata debate inayoendelea sasa hivi ya namna gani ya umoja wa Kitaifa ukizingatia kwenye wimbo wetu wa Taifa ambao tayari tulishaandaliwa, je tunautumiaje. Kutumia hekima, umoja na amani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye malengo endelevu ya dunia imeelezea kwanza lengo la kwanza namna ya kuondokana na umasikini, la pili linazungumzia kuhusu njaa, la tatu linazungumzia ustawi wa jamii na afya na afya ndiyo rasilimali kubwa, utajiri mkubwa kuliko wote wa binadamu. Ukisoma Yoshua Bin Sira, Sura ya 30:16, utajiri mkubwa kuliko wote kwa mwanadamu ni afya yake. Halafu unaenda ya nne inayozungumza nini, elimu bora, sawa, shirikishi kwa wote (quality) ili jamii iweze ikajitambua vizuri. Ukienda ya tano unazungumzia akinamama, usawa wa jinsia na unajua kama rasilimali na hasa akinamama ukiwapa uwezo zaidi ile electromagnetic force inayotoka kwenye mioyo yao ni tofauti na ya wanaume na hii ni sayansi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sayansi iliyofanyika miaka 300 iliyopita inajaribu kuchambua hisia ambazo zimekuwepo ulimwenguni zaidi ya miaka 5,000 iliyopita kabla ya Kristo kuhusu electromagnetic force ya hisia, kunuia na kunena. Hisia, kunuia na kunena (electromagnetic force). Hata sauti za akinamama zinavyozungumza tu ni tofauti na za wanaume hasa kwenye ile nguvu ya mioyo yao namna ya kuifanya jamii iweze ikashiriki maendeleo yao pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwetu huu ni mwaka wa takribani wa 57 wa uhuru, rasilimali viongozi iko wapi? Huwezi ukasema kazi waliofanya labda Baba wa Taifa, akaja Mzee Mwinyi, akaja Mkapa, akaja Mheshimiwa Kikwete, na sasa hivi tunaye Mheshimiwa Magufuli, ni uongozi shirikishi na uongozi endelevu wa pamoja. Rasilimali viongozi ukiangalia hata debate inayoendelea, majibu yanayotoka kuhusu umoja wa Kitaifa yanatolewa majibu badala ya kutolewa majawabu yaliyo sahihi kwa ajili ya mustakabali wa Taifa letu. Najiuliza kwa mfano, mimi Mbunge wa Vunjo, Mbunge wa Vunjo maendeleo nayaangalia pale kijijini kwangu namna gani ile jamii naishirikisha kwenye msaragambo, kwenye mitaro yao, kwenye masuala yao ya elimu, masuala yao ya afya, namna gani wanashiriki kwenye maendeleo yao endelevu ya kila siku ambayo ni jamii inakaa pamoja wanaona fulani ndiyo anayefaa kutuongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mimi Mbunge wa Vunjo niliyepata kura 73% ya wapiga kura wote pale Vunjo, yaani wagombea wote wa Chama cha NCCR Mageuzi ambao tulishawaingiza wamesajiliwa 1,008 hakuna mwenye sifa hata moja wameondoa wote, wote, kwamba hawafai na ni halmashauri yote ya Wilaya ya Moshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hayo maendeleo endelevu shirikishi ambayo Mbunge yuko tofauti na Madiwani, Madiwani wako tofauti na Wenyeviti wa Vijiji. Hayo maendeleo tusilichukulie hili jambo ni jepesi jepesi, soma lengo la 16 la malengo endelevu ya dunia. Linasema ili ku- transform the world lazima kuwe na justice, piece and strong institutions, tuwe na haki, amani na mifumo imara na endelevu. Siyo majibu yanayotoka hapa, unachonuia ile electromagnetic force. Tulichukulia amani ya Taifa letu, amani ya Mama Tanzania na leo ni Ijumaa, Mtume Mohammed (Swalla Allah Alayh Wasalaam) anatuhusia, ukiona uovu unatendeka zuia, ukishindwa kuzuia kemea, ukishindwa kukemea onesha basi hata hasira, onesha basi hata chuki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe tu Serikali kwa nia njema na Mpango huu ulivyoeleza, ili uweze ukawa endelevu na nzuri tukubali kuridhiana Taifa hili ni letu sote. Vyama vya Siasa ni vikundi tu katika jamii lakini vyama vya siasa vitasambaratika lakini Tanzania itabaki kuwa hii moja. Mama Tanzania apewe upendeleo na tumrutubishe zaidi aweze kunyonyesha kizazi hiki na vizazi vijavyo, amani yetu ipewe kipaumbele kuliko kitu kingine chochote. Tunazungumzia umasikini huku, watu wanakata mashamba unasikia mahindi yamekatwa, chuki inajengeka na mahali penye chuki panakuwa na woga na mahali penye woga amani inatoweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba chonde chonde, ili haya yote tuweze tukayafanyia kazi vizuri na yakawa ni shirikishi kwa wote bila migongano ya aina yoyote, niombe viongozi, siasa safi na uongozi bora, ukimsoma kiongozi, usome Yakobo 3:18 anakuambia “Amani ni tunda la wapenda amani wanalolifia”, na hiyo mbegu ni ipi! Mbegu yenyewe ni ipi, ni haki na uadilifu, haki na uadilifu. Sasa tuone kizazi hiki tunarithisha nini vizazi vijavyo ili Mpango wetu huu wa kuondoa umaskini huu kila Mtanzania ashiriki. Let say, pale Vunjo kwa mfano, wanamchukia Mbatia, ana sura mbaya, hawamtaki na nini, lakini kumchukua Mbatia kusisababishe wana Vunjo wasishiriki kwenye maendeleo ya Taifa lao la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maneno yanayosemwa tusiyachukulie wepesi wepesi, TCD ilipoanzishwa na Mzee Mkapa ilikuwa ni ya kuleta jamii kwa pamoja. Vyama vilivyo na wawakilishi Bungeni, tukae, tuzungumze, tuishauri Serikali na Katiba yetu. Wabunge tukae tuishauri Serikali, tuisimamie Serikali vizuri……

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, kwanza nitoe pole kwa shule ya Wasichana ya Ashira Mabweni yao yameungua moto jana na wanafunzi zaidi ya 100 hawako kwenye hali nzuri na eneo hili linapakana na Mlima Kilimanjaro kwa hiyo, niombe na TANAPA pia waweze kuangalia ni namna gani tunaweza tukashirikiana katika kurudisha hadhi ya shule yetu ya Ashira ili iweze kuwa kwenye hali nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pongezi kwa TANAPA kwa kazi nzuri wanayoifanya na ujirani mwema wa vijiji 88 vya Mkoa wa Kilimanjaro kupitia KINAPA wamefanyakazi nzuri na wameshirikiana na Vunjo development foundation (VDF) pamoja na Ofisi ya Mbunge tumeweza kutengeneza barabara zaidi ya kilometa tisa kwa hivyo niwapongeze sana TANAPA kupitia Mkurugenzi wake Kijazi na Mwenyekiti wa Bodi Gen. Waitara na wote pamoja na Sakayo Mosha sekondari imejengwa vizuri, Zahanati ya Kitoo wanafanyakazi nzuri na mtu akifanyakazi nzuri yapasa kumpongeza, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tabia yetu sisi Watanzania kwenye sekta ya utalii badala ya kuuza utalii au kuuza huduma tunauza neno “samahani”. Huduma vigezo vyetu au uwezo wetu wa kutoa huduma unavyokuwa chini badala ya kuona namna gani ya kuboresha kutoa viwe kwenye standard tunatoa neno “samahani” hasa kwenye mahoteli yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitasema kwanini nasema hivyo; kwanza sekta ya utalii ndiyo sekta kuu inayoongeza fedha za kigeni hapa Nchini. Asilimia 25 ya forex yote inatokana na utalii sasa tusiangalie ugali wa leo tu, nitumie lugha rahisi, tuangalie kesho. Nasema hivyo kwa sababu ukiangalia bajeti ya Wizara hii ni bilioni 120, fedha za maendeleo ni bilioni moja tu za ndani za nje ni bilioni 47.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiangalia maduhuli na mwaka jana niliomba tena, ukiangalia maduhuli yanayotokana kwa mfano na TANAPA peke yake mwaka jana ilikuwa zaidi ya bilioni 292. Unamlisha Ng’ombe vizuri ili umkamue vizuri na aweze kukuletea tija zaidi. sasa kwa kweli bajeti ya Wizara hii ni kidogo sana. Kwa mfano, Bosi ya utalii, Jaji Thomas Mihayo ambaye ni Mwenyekiti na wenzake wanafanyakazi nzuri lakini tunawawezesha kiasi gani waweze wakatangaza utalii wetu? Fedha zinazotolewa kwenye kutangaza utalii, kwa mfano, tukijifunza kwa wenzetu wa Kenya ni zaidi ya Dola milioni 100 yaani zaidi ya bilioni 200 yaani fedha zote za bajeti ya Wizara hii hazitoshelezi kuutangaza utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pengine nipendekeze tu; maduhuli yanayotokana na Wizara hii Serikali ione umuhimu wa kuacha ndani ya Wizara angalau kwa miaka mitano ili Wizara iweze ikakua na GDP yake iweze ikakua ili Taifa liweze likavuna zaidi kutokana na hali ya namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, viko vigezo vingi ambavyo vinarudisha nyuma utalii wetu. Kwa mfano, work permit za expert kama kuna wafanyakazi 100, wafanyakazi wawili ambao ni experts au wataalam kwanini wasipewe mazingira rafiki ya kuweza kufanyakazi vizuri. Ubora wa vyakula vyetu, kwa mfano, lile katazo la vyakula vya mifugo au maziwa kutoka Kenya, kodi nyingi nyingi tuangalie ushindani zaidi kwenye standardization, standards zetu tuziboreshe zaidi ziashindane badala ya kuwelka restrictions ambazo siyo rafiki, utitiri wa kodi. Nipongeze Kambi ya Upinzani wameandika vizuri utitiri wa kodi uliopo, Kamati nayo imeandika vizuri pia, tuangalie utitiri mwingi sana kwenye kodi katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna matamkao yanayotolewa, Serikali ikitoa matamkoa iangalie sana. Kwa mfano, matamko ya magonjwa kama ya Dengue ambayo watalii wanaibebaje kwamba Tanzania tayari yote ina magonjwa ya namna hiyo wanaogopa hata kuja Tanzania. Hata hii mifuko ya plastic namna gani wanafanya package, restrictions ziko namna gani, tamko la Serikali liko namna gani kwa hivyo matamko haya tunayoyatoa lazima yaangalie kwa mapana yake, utalii Kusini na mazingira, UNESCO wako kwenye position gani tunaitangaza namna gani Dunia kwenye mambo ya namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu ukiamua kupanga vizuri, kwa mfano, Kilimanjaro marathon wakati wa low season ukaipanga kama ni package moja ya kuanzia unawaambia watalii wanakuja wanaanzia Arusha kwenye kuangalia wanyama Serengeti, wanakuja kwenye Kilimanjaro marathon, wanatoka kwenye Kilimanjaro marathon kwenye kukimbia huko wanakwenda Zanzibar (Zanzibar music festival) kwenye raha huko, wanakuja Dar es salaam, Dar es salaam wanaangalia biashara na Mji ulivyo, wanakwenda mbuga za Saadani-Bagamoyo kwahivyo inakuwa ni package moja na ukiipanga vizuri ni taaluma tu yaani inakuwa ni tourist plan ambayo ikiipanga as a tour moja faida yake ni kubwa kwa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, wataalam wapo, tuwawezeshe watalaam wetu waweze kuzifanya hizi tour zikaweza kuwa na hii route ikawa na manufaa na maslahi mapana kwa Taifa. Kwa mfano, kipindi cha low season, kwa mfano, Easter time ukasema wiki mbili nzima ni za plan nzima ambayo ina-compensate sio ina compensate ile zitakwenda sambamba na high season, ukimaliza kipindi cha Easter high season nayo inakuja kwa hivyo unakuta mwaka mzima utalii na tuweke priority kutokana na vivutio vyetu vya utalii. Kipaumbele kwenye eneo hili kwa ukubwa wake kiko hivi, kipaumbele kwenye eneo hili kiko hivi, eneo hili la kutangaza vivutio vile tulivyonavyo yaani kwa lugha nyingine niseme we must organize what we have and plan for it, tu-plan, tu- organize, turatibu, tuweze kuelekeza na kuweza kutawala vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia watu kwa mfano, European wana-route zao wanazi-plan vizuri unaanzia Belgium, unakwenda France, unakwenda Spain, unakwenda Germany wanakuwa ni package moja sasa hapa kwetu na vivutio vingi hivi tulivyonavyo vya utalii yata-stick big. Mheshimiwa Waziri naujua uwezo wako na mmetulia vizuri sana kwenye Wizara sasa hivi nikupongeze kwa hilo na ubinifu washirikishe wadau walio wengi, tuishirikishe Dunia, tushirikishe wawekezaji kwenye sekta hizi kwa sababu uwekezaji kwenye utalii pamoja na communication kwenye utalii ni watoto pacha, wanarandana, wanaingiliana sasa namna gani unachukua wataalam hawa, kwa mfano, Makampuni ya humu ndani tukatumia…

Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja namalizia sekunde 30; Makamouni ya huku ndani yakatmika vizuri katika kuwekeza na kutangaza utalii badala ya Makapuni ya humu ndani kutumika na watu wa nje zaidi tuyawezeshe Makapuni ya ndani na wao waweze kuwekeza vizuri katika sekta hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana Mwenyezi Mungu akubariki.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru naamini nina dakika 10 tafadhali sana.

Meshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi uliyonipatia. Bara la Afrika ukisoma report ya Thabo Mbeki ya mwezi Machi, 2014 aliyowasilisha kwa Mawaziri wa Fedha wa Bara la Afrika. Bara la Afrika kwenye Illicit Financial Flows kila mwaka tunapoteza zaidi ya dola bilioni 50, hasa nchi zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya fedha hizo asilimia 65 zinatokana na hizi biashara za madini ambazo siyo za wazi, mikataba ambayo ni ya hovyo hovyo kama tuliyonayo hapa nchini kwetu Tanzania, ambayo tumeingia wakati wote, sasa swali ninalojiuliza sisi na hasa Bunge hili, Je tunalitendea haki Taifa letu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivyo kwa sababu na hii naisema kwa pande zote, uwezo wetu wa ku-debate mambo ambayo ni ya msingi kwa Taifa la Tanzania, uwezo wetu wa kufikiri utu wa mwanadamu, utu wa Mwafrika kuuweka mbele kuliko kitu kingine chochote, uwezo wetu wa kutuunganisha pamoja, tukianza kushutumiana hapa unaruhusu hao mabeberu watumie upande wowote na utalipasua Taifa la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilihusika kwenda Zimbabwe mwaka 2002, tulitumwa na Rais Mkapa, zile lugha za kibaguzi zilizokuwa zinatokea na tulikuwa na Mzee Mheshimiwa Ngombale Mwiru, Mheshimiwa Janguo, Mbunge wa Kisarawe; Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi na wengine. Mpasuko uliokuwa umetokea Zimbabwe leo hii hawana hata currency yao, tukiangalia Venezuela Taifa lile limesambaratika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mambo kama haya inatupasa sote kwa pamoja kuweka maslahi ya Mama Tanzania mbele na tuwe kitu kimoja bila kubaguana, badala ya kila mtu kusema hili langu, langu wakati Taifa hili ni letu sote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Profesa Kabudi wewe ni Mwalimu wa Sheria, Montevideo Convention kitu cha kwanza rasilimali kubwa kuliko zote duniani ni watu, watu na kati ya zile tabia kuu nne ya kwanza ni watu, ardhi, utawala na mahusiano, lakini watu tunawapata kwenye wimbo wetu wa Taifa kwenye Hekima, Umoja na Amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi watu wa Taifa la Tanzania takribani milioni 55 na maliasili zetu zote hizi, tunatakiwa kuwa na sauti hii moja, kwa maslahi ya wote, bila ubaguzi wa aina yoyote. Sasa huu Muswada ambao uko mbele yetu, najiuliza kweli maswali mengi sana, tangu tumeanza kulumbana hapa, huyu lile ambayo hailisaidii Taifa. Je, tunajitambua? Je, tunataka kukumbata giza au mwanga?

Mheshimiwa Naibu Spika, naona katika Miswada hii tunataka kukumbatia mwanga, sasa mwanga huo kwa maslahi ya wengi ya pamoja sasa tunashirikiana vipi badala ya kushutumiana shutumiana tu na kupoteza muda wa Bunge na kupoteza rasilimali za Taifa badala ya sisi kujijua kwamba mikataba hii ikifanyika vizuri, tukiruhusu wawekezaji wakaja hapa, tukiangalia wananchi wa kwetu, kwa mfano, Mheshimiwa Waziri amesema kwenye hii Kifungu cha 11 ile mikataba itaangaliwa kuanzia huko nyuma itafunguliwa yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo Commision ya akina Mheshimiwa Thabo Mbeki wanasema; Illicit financial flow zote zinazofanyika Afrika zinafanyikia hasa kwenye mikataba. Commission ya Thabo Mbeki ya 2014, kwa kiasi kikubwa ile asilimia nyingine 30 ndiyo mambo ya dawa ya kulevya na kutakatisha fedha, lakini asilimia tano ni rushwa, uadilifu integrity ya watawala integrity ya viongozi integrity ya watu wetu ambayo wanasimamia mikataba hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge kuna kauli mbiu inayosema pamoja tutashinda na tukisema pamoja tutashinda hata kama unanichukia mimi angalia Taifa achana na James Mbatia.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami nitoe mchango wangu kidogo katika Muswada ulioko mbele yetu. Nilikuwa najaribu kutafakari tu kwa ujumla, au nitoe mawazo yangu ya ujumla kuhusu Muswada huu wa Maji, inaonekana kwamba bado tatizo hili la ukosefu wa maji litakuwepo kwa sababu tumeanza mwisho badala ya kuanza mwanzo. Ni namna gani tungetakiwa kuanza na vyanzo vya maji, uvunaji wa maji, usimamizi wa maji, baadaye matumizi ya maji. Ukisoma lengo la sita la malengo endelevu ya dunia linasema to ensure availability and sustainable management of water and sanitation for all na ifikapo mwaka 2030, yaani miaka kumi na moja kuanzia sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tuna vyanzo vingi vya maji, Tanzania tuna baraka ya kupata mvua nyingi, namna gani tumeanzia hapo uvunaji, vyanzo ili ile miundombinu sasa ya usambazaji wa maji, iweze kuendelea na namna gani ya kuyaweza kuyasimamia haya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia suala la gharama, suala la ubora na suala la muda, je, Serikali na Kamati yetu ya Maji, best practice ya namna ya usambazaji wa maji na Miundombinu yake, sisi hatuko kwenye kisiwa, ni namna gani wameweka utafiti wa kutosha wakiiangalia dunia na maji na namna gani Sheria hii inaweza ikaakisi au ika-address tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tutakuwa tunafanya labda, trial and error hatujaweza kuangalia matatizo yaliyo makubwa ya maji katika Taifa letu; na ni kwa nini wakati vyanzo tunavyo na maji tunayo ya kutosha, ni namna gani tunaangalia bajeti yetu, kwenye Mfuko Mkuu kwa ajili ya uhai wa binadamu na kukuza utu wa binadamu kwenye maji? Pia, ni namna gani kwenye karne hii tunazungumzia usimamizi wa maji katika Taifa letu na matumizi ya maji au tunaweka tu sheria na mifumo, lakini mifumo ambayo ni endelevu kwa kiasi gani, katika nchi hizi za maziwa makuu na Tanzania tukiwemo, tusingelikuwa kwenye karne hii, tunaweka utaratibu wa kisheria wa namna gani ya kutoa hizi adhabu ndogondogo, badala ya kuwekeza kwenye elimu ya kujitambua na thamani ya maisha kwenye maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu maji, tunasema ni uhai, maji ndio utu wa mwanadamu, maji ndio kila kitu, sasa ni kwa kiasi gani tumewekeza kwenye utafiti na bajeti ya Serikali ikaenda kwa kiasi kikubwa kwenye utafiti, utafiti,
utafiti tukaondokana na tatizo hili la maji na kwa kiasi kikubwa lingekuza Uchumi wa Taifa letu, kuanzia kwenye domestic water use na kwenda kwenye mambo mengine ya matumizi ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu, ukiangalia kwa mfano raslimali watu na kwenye sasa, miundombinu ya maji, kama Muswada unavyojaribu kuielezea hapa, je, tunaanza kuweka miundombinu au kuweka mifumo ya kisheria kabla hatujaandaa watu wenye knowledge ya kutosha ya kuweza kuyasimamia hayo maji. Au tunataka tukifika 2030 yaani miaka kumi na moja ijayo Tanzania tutazungumza vipi, katika yale malengo endelevu ya dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hivyo kwa sababu ukiangalia kifungu cha 48 ambacho Mheshimiwa Antony Bahati Calist Philomena Komu, amekileta hapa, kwamba kwenye amendments zake na anaishauri Serikali Madiwani ambao ni Serikali zetu za Mitaa, ambapo wao, ndio wanawakilisha wale watumiaji wa maji kuanzia kwenye Kamati zao za Maendeleo za Kata, ndio wenye taarifa sahihi na bila kuwa na taarifa sahihi, huwezi kwenda kwenye ku- plan, ku-organize, ku-coordinate, ku-direct na ku-control.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, naomba wakati wa amendments naomba kabisa kwenye sheria hii, japo imeanza kwa huku, ile amendment ya Mheshimiwa Komu ikubalike ili Madiwani waweze kuwa na taarifa sahihi hata kama ni Wataalam waweze waka-plan vizuri na ule utaratibu mwingine wote wa kuweza kuishauri Mamlaka ya kutumia maji iweze ikafanikiwa na kufanya checks and balance yaani wawe na planning, waweze ku-organize, ku-coordinate, ku- direct na ku-control ili utawala huo au matumizi haya ya maji yaweze kwenda kwa utaratibu unaofaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kifungu cha 63 na 64 Serikali ina amendments za Serikali, pale penye eneo la adhabu ya milioni tano wamesema zianzie laki tano, lakini zisizidi milioni 10, wamebadilisha tu wakaenda from milioni tano kwenda kwenye laki saba lakini zinaenda kwenye milioni 10. Hebu tujiulize; mtu anatumia maji na utaratibu wa matumizi ya maji, labda ni kwenye domestic use je, definition inasema nini kwenye misuse of water? Kwa sababu ukisema misuse ya maji, wewe labda unayatumia kama domestic use kwenye bustani, kwenye matumizi labda ya mifugo au unayatumia namna gani kwa ajili au kwenye yale mahitaji ambayo ni muhimu na unayahitaji wewe, halafu unaenda kwenye adhabu au wale watu wenye Mamlaka, sasa hapa panahitajika ufafanuzi, yaani definition ieleweke vizuri ya misuse maana yake nini kwenye Kifungu hiki ambacho nimekisema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia vijijini kwa ujumla, tumeona karibu asilimia 16 ya bajeti ya watu wa vijijini wanatumia kwenye maji, lakini nilikuwa najaribu kuangalia takwimu inaeleza kwamba kwenye Sub-Sahara African milioni ya watu ambao wako Kusini mwa Jangwa la Sahara, wanatumia maji kwa ajili ya binadamu na vyanzo hivyo hivyo vinatumika na mifugo au vinatumika na wanyama au vinakuwa polluted. Sasa ni kwa namna gani sheria zetu hizi zinaweka kwenye utafiti wa kutosha kwa sababu wakitumia maji na mifugo ndio vyanzo vya magonjwa mengine ambayo yanaleta athari kubwa katika kukuza uchumi, yanaleta athari kubwa kwenye afya ya binadamu na matatizo mengine kama hayo ambayo nimeyaelezea hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye ile Ibara ya 66, namna gani tuna-harmonize Vyama vyetu vya Watumiaji wa Maji, ziko Mamlaka ndogondogo za Watumiaji wa Maji, naweza nikajaribu kuangalia kwa mfano pale Moshi, MWUA na vile vyama vingine labda Kiliwater, Kirua Kahe na wengine, namna gani wana-harmonize kwa pamoja ili hawa RUWASA waweze kufanya nao kazi isije ikatokea migongano, ni nani anawajibika kwa nani katika kuleta matumizi yaliyo bora na matumizi ambayo siku ya mwisho yule mtumiaji au mlaji au huyu mwanadamu yaweze kumletea tija yenye uwezo ulio mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania yetu tuna tatizo la maji haya ambayo tunayazungumzia hapa. Ni mapendekezo yangu kwenye Muswada huu pamoja na kwa Serikali kwa ujumla na zile Sheria nyingine za Maji zilizopo, tujitahidi kwa uwezo mkubwa kuweka utafiti na kuweka malengo, tuone ndani ya miaka mingine kumi ijayo, sio lengo tu kufikiwa mia kwa mia au tisini kwa ngapi, ni namna gani tunaangalia kwa miaka hamsini ijayo kwa ajili ya maendeleo endelevu ya maji na maendeleo endelevu ya kukuza utu wa Watanzania kwa ujumla hasa katika sekta ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, niiombe Serikali yetu, suala la maji sio la suala la trial and error, sio suala la kusubiri mpaka wakati bajeti, Wabunge tuweze tukaona labda chukua fedha hapa weka hapa, fanya hivi, fanya hivi, kama wameweza ku-concentrate kwenye miundombinu kwa mfano ya barabara, miundombinu ya reli, tuone maji ni zaidi ya miundombinu mingine yoyote kwa ajili ya kumwezesha huyu mama hasa ambao ndio wazalishaji wakuu katika Taifa la Tanzania, hasa kuwapunguzia ule muda ambao wanapoteza kwenye kutafuta maji, wakiweza kupata maji ya kutosha na uchumi wa Taifa utaongezeka, tija ya Taifa itaongezeka na Tanzania tunaweza tukaongelea Tanzania ya haki ya viwanda vya vya kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa kunipatia muda.