Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka (46 total)

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza ni kwamba hili bwawa lilitengenezwa maalum kwa ajili ya wafugaji kutokana na kwamba walihamishwa kutoka mbuga ya wanyama ya Mkomazi, na kazi ya pili ilikuwa uvuvi, ya tatu ilikuwa yale maji yanayo-spill over ndiyo yaende kwa wakulima. Tatizo ni kwamba huu mradi wote umegeuzwa kwamba unalenga wakulima zaidi kuliko wafugaji, matokeo yake nina wasiwasi kwamba hata Mtaalam (Consultant) mwingine akipatikana wa kutengeneza huu usanifu atakosea, kama alivyokosea mara ya kwanza ambapo huu mradi ulipotangazwa zile Terms of Reference hazikueleweka. Matokeo yake yalivyoenda UN Capital Development Fund, yakarudi kwamba haikukidhi matakwa ya ule mradi ungetengenezwaje. Sasa ninavyoliona hapa litarudia tena, because focus pia imebadilika kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, swali langu ni hivi huoni ni wakati muafaka sasa mradi huu ukasimamiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili pia tupate technical assistance ya kusaidia ku- frame huu mradi vizuri? Because kuharibika kwa huu mradi, I mean kujaa tope ni kwamba wafugaji walikuwa wanaleta ng‟ombe kwenye bwawa na hili bwawa ni kubwa sana, square kilometer kuna takwimu mbili, inaonesha 32 square kilometers, nyingine inaonesha square kilometers 24, ni mradi mkubwa sana. Kwa hiyo, ninachoomba au ninachoshauri ni kwamba huu mradi haionekani kwamba unatakiwa uendeshwe au usimamiwe na Wizara ya kilimo ili uweze kupata technical assistance inayotakiwa?
Swali la pili, sasa hivi wananchi wanapata shida sana, wanaolima hapa, licha ya kwamba mbolea na msaada wa kitaalam unakosekana, lakini ndege aina ya kweleakwelea, wanavamia sana mashamba ya wakulima na sasa hivi ndiyo kipindi ambacho mpunga wa eneo lote hilo la kwanzia Maore, Ndungu, Kihurio mpaka Bendera, linavamiwa na hawa ndege waharibifu. Je, Serikali inaweza kusema nini kuhusu kutatua tatizo la kuua hawa ndege waharibifu? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, ombi lake ni kwamba anataka bwawa lile lisimamiwe na Serikali Kuu badala ya Halmashauri. Naomba niwahakikishie, mwaka jana kwenye Bunge la Kumi tulipitisha Sheria ya Umwagiliaji na tukaanzisha Tume ya Umwagiliaji, Tume hii ndiyo itakayosimamia ujenzi wa mabwawa yale makubwa ambayo yataongeza eneo la umwagiliaji. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mbunge suala la utaalam lipo katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuhakikisha mabwawa haya yatatengenezwa inavyotakiwa, kwa hiyo usiwe na wasiwasi.
Swali la pili kuhusu ndege, hilo nafikiri labda Waziri wa Kilimo yupo hapa, anaweza akajibu. Ahsante sana.

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, hilo swali la ndege waharibifu nimeshalipokea pia swali la aina hii kutoka kwa Mheshimiwa Elibariki Kingu, Mbunge makini wa kutoka Jimbo la Singida Magharibi, kuna ndege waharibifu wa aina hiyo hiyo. Niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge kwa maeneo hayo ambayo yamepata uharibifu wa aina hiyo, nimewaelekeza wataalam wangu ili waweze kutumia utaratibu ambao Serikali huwa inatumia wa kutumia ndege kwenda kushughulika na ndege waharibifu wa mazao katika maeneo hayo husika.
Kwa hiyo, kama kuna eneo lingine ambalo Wabunge hawakupata fursa ya kuuliza lina matatizo ya aina hiyo, naomba baada ya kuahirisha Bunge nipate taarifa za aina hiyo ili niweze ku-communicate na wataalam wangu waweze kuchukua hatua zinazostahili.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa vile swali la Mheshimiwa Kabongo limefanana na matatizo yaliyoko katika Mbuga za Wanyama za Mkomazi; na kwa vile nilishaongea na Waziri wetu wa Utalii, kaka yangu Mheshimiwa Profesa Maghembe kwamba tembo wanatoka Mkomazi National Park wanaingia kwenye Loresho tulilowatengenezea wafugaji na inaharibu sana sehemu hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa TANAPA tuliwaeleza tatizo hili na kwamba watusaidie kuboresha intake ili maji yawe mengi wakati wanatafuta jinsi ya kuwapelekea tembo wale maji. Je, Waziri anaweza kunisaidia kueleza atachukua hatua gani ya dharura kuhakikisha kwamba yale maloresho na tenki letu la intake lililoharibiwa na tembo na wanyama wengine linaboreshwa ili wafugaji waendelee kupata maji wakati wanatafuta jinsi ya kusaidia wanyama hawa? Ahsante.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, tutachukua hatua mbili. Kwanza ni kuhakikisha kwamba tunaongeza upatikanaji wa maji katika eneo ambalo hao tembo wanatoka kule kwenye National Park na pia tutafanya ukarabati wa maeneo ambayo yameharibiwa katika vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, kwa kweli nasikitika sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, najua hizi habari alipewa akiwa ofisini kwake.
Mheshimiwa Spika, hii guest house anayoizungumzia kwanza imepitwa na wakati sana, imejengwa miaka 56 iliyopita, lakini ambacho kimempita asione ni kwamba kituo hiki ni kikubwa sana na ni kizuri sana, kina eneo takribani zaidi ya heka tatu, kina mandhari mazuri sana, kina majengo mengine yote ya maabara, nyumba ya daktari, nyumba ya manesi na wodi za wagonjwa.
Sasa swali langu ni kwamba, je, kwanza Naibu Waziri atakuwa tayari tuende akajiridhishe kwamba jibu lake hili ambalo alizungumza kana kwamba kuna nyumba tatu tu, halitoshelezi maana ya kuwa na kituo kama hiki?
Pili, nataka Waziri aniambie kutokana na kwamba kituo hiki sasa hivi hakitumiki vizuri kama kituo cha utafiti kwa vile inaweza kuisha mwaka, miaka miwili hakujafanyiwa utafiti hata mtu mmoja; je, haoni kwa nini kituo hiki kiongezewe kiwe kituo cha afya ili pale watakapopenda kufanya utafiti wafanye, lakini kwa vile kuna majengo ambayo Serikali imetumia hela nyingi sana kukitengeneza na mandhari mazuri na kuna mlinzi, kuna gardener, kuna msafishaji, kuna tv, kuna maji, kuna umeme lakini kituo hiki sidhani hata hiyo guest house inapata watu wawili kwa mwezi maana mwenyewe nilienda nikalala pale kujiridhisha.
Mheshimiwa Spika, naomba Naibu Waziri aniambie; je, Serikali iko tayari kukifanya kituo hiki kiwe Kituo cha Afya ili kisaidie Kata tatu za Vuje, Maore na Bombo ambazo zina wananchi zaidi ya 50,000 ukichukulia kwamba Jimbo langu ni kubwa sana na ukichukulia kwamba jiografia ya kwangu ni mbaya sana na vituo vipo viwili tu na viko mbali mno? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka kwa maswali yake mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, majibu ya Serikali kwa swali lake la kwanza kwamba Waziri atakuwa tayari kwenda kukitembelea kituo hiki, ndiyo tupo tayari na baada ya Bunge hili tutakwenda na tutamtaarifu Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hili aongozane na sisi tutakapokwenda kukitembelea kituo hicho.
Mheshimiwa Spika, jibu la pili ni kwamba ninachokiona Mheshimiwa Kaboyoka ana uchu wa kupata kituo cha afya zaidi kuliko matatizo yaliyopo pale kwenye Kituo hiki cha Utafiti cha Gonja. Sasa mahitaji ya vituo vya afya huwa yanaibuliwa na wananchi kwenye Halmashauri yao wenyewe. Ninamshauri Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Watendaji kwenye Halmashauri yake na wananchi kwenye Halmashauri yake waweze kuanzisha mchakato wa namna ya kupata Kituo cha Afya kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kwamba kituo hiki kimekaa kwa muda mrefu na kwamba hakitumiki, hapana siyo kweli. Nakubaliana na yeye kimejengwa zaidi ya miaka 50 iliyopita lakini mwaka 2007/2008 kituo hiki kilifanyiwa ukarabati mkubwa kwa ajili ya maandalizi ya utafiti wa mabadiliko ya prevalence ya ugonjwa wa malaria ambao unaendana na tabia nchi. Wakati mchakato wa kuanza utafiti ule ikaonekana kwamba prevalence ya malaria imeshuka kwa kiasi kikubwa katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na kwa maana hiyo utafiti ule haukuendelea. Kwa sasa utafiti mwingine unaendelea kwenye kituo kile unaendeshwa na Taasisi yetu ya Utafiti ya NIMR kupitia kituo chake cha Amani kilichopo Tanga kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Muhimbili kuhusiana na namna ya kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano katika kufikisha ujumbe unaohusiana na kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI.
Kwa hiyo, siyo kwamba kituo kile hakitumiki, kituo kile kinatumika kwa matumizi yake ya awali ya utafiti, kama nitakapokitembelea kutakuwa kuna haja ya kuangalia namna ya kuweza kukifanya kitoe huduma nyingine mbali na zile huduma mahsusi tutashauriana ndani ya Serikali kuona kama tunaweza tukalichukua wazo hilo.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Kabla ya swali langu la nyongeza, nataka nieleze masikitiko yangu makubwa
kwa jinsi aliyempa Mheshimiwa Waziri taarifa hii alivyoipotosha. Mheshimiwa
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi namheshimu sana na inabidi kueleza
ukweli kwamba upotoshaji huu, itabidi huyu aliyempa hizi taarifa za uwongo amchukulie hatua. Kwa mfano, hapa ilipoandikwa kwamba, TANAPA
wakishirikiana na WOYOGE Trust Fund wameshajenga birika ni uwongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza na-declare interest, hii WOYOGETrust
fund mimi ndiyo Mwenyekiti wake. Huu mradi mwaka jana nilimuuliza Waziri wa
Maliasili na Utalii, kwamba wanyama wale wameharibu sana miundombinu
ambayo nilikuwa nimewasaidia wananchi kule kwa ufadhili wa Ubalozi wa Japan
na Waziri akakubali kwamba watarekebisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, basi
nimwambie tu kwamba, Waziri amepotoshwa maana TANAPA hawajaja kujenga
chochote kwanza ndiyo naambiwa mradi umeenda kwenye Bodi na kwamba
hata haujapitishwa. Wamempotosha sana.
Swali langu la nyongeza ni kwamba je, Waziri haoni kuna umuhimu wa
kuweka kituo cha artificial insemination, kwa kuzingatia kwamba madume
yanayopelekwa kusaidia wafugaji yanakufa, maana wafugaji wanayaswaga
nayo yale yanataka yafanyiwe zerograzing? Naomba ajibu swali hilo.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika,
kuhusu taarifa tulizotoa kupishana na taarifa aliyonayo yeye, niko tayari kukaa
naye kuangalia kwa nini yeye ana taarifa tofauti na ile ambayo tunayo kama
Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu artificial insemination ningependa
kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari huduma za artificial insemination
zinatolewa karibu kabisa na Jimboni kwake akifika tu kituo cha Tengeru, huduma
hizi zinaweza kupatikana vilevile niko tayari kukaa naye na kumwelekeza zaidi
namna ya wafugaji wake watakavyoweza kunufaika na huduma hii.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwa vile tatizo la Rungwe ni sawasawa na tatizo linalowapata wakulima wa tangawizi wa Jimbo la Same Mashariki na kwa vile wakulima hao walipata tatizo kubwa tangu walivyosaidiwa na SIDO mpaka leo kiwanda hakifanyi kazi na wameshauriwa kwamba waunde Kampuni na LAPF wamekuwa tayari kusaidia kuingia
katika Kampuni hiyo. Je, Wizara inawezaje kuwasaidia hawa wakulima ili wasije wakaingia tena katika tatizo walilolipata ambalo mpaka leo kiwanda hakijaweza kufanya kazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, Serikali au Wizara iko tayari kukutana na Mheshimiwa Mbunge pamoja na wakulima wa tangawizi ili kuangalia namna gani bora wanaweza wakatumia hicho kiwanda kwa manufaa yao na hivyo kuondokana na matatizo ambayo yameshatokea huko nyuma.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kweli nimesikitishwa sana na majibu wa Waziri ambaye naamini ni msomi na najua ni mtaalam wa mambo ya maji. Nimesikitika sana, kwanza mradi huu ambao uligharamiwa na Serikali ya Japan ulipelekwa Wizarani tangu 2012. Mwaka jana mwezi Novemba nikamwona Waziri nikamweleza, akaniomba nilete ile proposal na maombi nikampelekea.
Mheshimiwa Spika, licha ya kwamba hata hakunipa majibu, nashangaa leo akisema bwawa hili ni dogo ambalo
gharama zake 2012 ilikuwa milioni 800 na linahudumia wananchi ambao ni zaidi ya 40,000. Hata hivyo, kibaya zaidi amejichanganya tena na huo mradi wa Kalema dam ambao mwenyewe mwaka jana tukiongea juu ya bwawa hili. Nilimweleza wazi kwamba hawa UN-CDF wamekuwa tayari kulihudumia bwawa hili, nilichokuwa nimekosa kwenye Halmashauri ilikuwa utaalam.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Umoja wa Mataifa, wamekuwa tayari na Serikali ya Norway imeonesha kwamba
iko tayari kusaidia mradi huu, leo anajichanganya hapa na kusema anarudisha Halmashauri. Mradi huu wa Kalimawe ni square kilomita 24; Je, hilo ni bwawa la kati? Hapo nilikuwa nazungumzia masikitiko yangu. Swali langu ni kwamba kama Waziri aliona hili lingerudishwa kwenye Halmashauri, kwa nini hakunijibu hivyo, tangu mwaka jana Novemba?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Wizara hii kutokana na ripoti ya Mkaguzi wa Ufanisi katika Ujenzi wa Miradi ya
Maji Mijini, imeonesha uzembe mkubwa sana na upotevu mwingi wa hela za miradi, kiasi kwamba naamini ndio
maana wanashindwa hata kujenga miundombinu ya kumwagilia maji ili wananchi wetu, wakulima waweze
kuvuna….
Mheshimiwa Spika, nauliza je, kama Wizara inaona haiwezi kufanya mambo ya umwagiliaji badala yake walijua kuchakachua tu miradi ya maji, kwa nini wasiachie kazi hiyo au watumishi wake wakafukuzwa?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge
kwamba jinsi tunavyojibu maswali haya inategemea na namna ulivyouliza. Wewe umeuliza kwamba hili bwawa
umeleta maombi kwa muda mrefu, sasa na sisi tunatengeneza majibu kulingana na swali ulilouliza. Kwa hiyo,
hatujafanya uzembe wa aina yoyote katika kujibu.
Mheshimiwa Spika, pia naomba nimpe taarifa pia kwamba miradi hii ya mabwawa ya umwagiliaji ilikuwa ina
wafadhili mbalimbali ikiwepo JICA ndiyo walioweza kufadhili. Hatukuwa tumeiweka katika mipango ya bajeti ya Serikali ambayo sisi tunasimamia moja kwa moja. Sasa maombi yake tumesema kwamba sasa tunafanya mapitio, siyo kwa bwawa lake tu yako mengi nchi nzima, ili tuweze kuona ni namna gani tutayashughulikia.
Mheshimiwa Spika, pia swali la nyongeza la pili, kwamba kuna mradi ambao una uzembe, ambao haridhiki na utekelezaji wake. Naomba atuletee ili tuweze kuona nini kifanyike na kama kuna watu waliofanya uzembe basi
tuwachukulie hatua.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, mwaka jana mwezi Julai tulikwenda na Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA kutembelea vyanzo vya maji kutoka Milima ya Shengena ambayo inatiririsha maji mengi ambapo yanapita siyo mbali sana na hifadhi hii ya Mkomazi kwa upande wa Same Mashariki. Naye akaridhia kwamba kweli yale maji yangeweza kuchukuliwa na kusaidia sana ambapo yatakuwa ni maji ya kudumu kuliko haya mabwawa ambayo yanakauka mara kwa mara. Sasa nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, kitu gani kimefanya ule mpango usitekelezwe na badala yake wanakwenda tena kuchimba mabwawa wakati tumeshaona mabwawa kwanza ni hasara kubwa na pili maji yake yanakauka kila mara? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Waziri yuko tayari kutuma wataalam wake wakatembelee tena hii mito hasa Mto wa Hingilili ambao ndiyo unashusha maji mengi na kulinganisha na tathmini yake na kuchimba mabwawa ni ipi rahisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la kwanza, anatoa taarifa juu ya ziara yake na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka za Hifadhi za Taifa Nchini (TANAPA) kwenye Milima ya Shengena ambapo analiambia Bunge lako Tukufu kwamba waliweza kuona uwezekano kwamba eneo lile ni chanzo cha maji ambacho kingeaminika zaidi na kwa hiyo anataka kujua kwa nini Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii isingetumia chanzo kile badala ya vyanzo hivi ambavyo tumevieleza hapa vya kutumia maji kutoka ardhini.
Mheshimiwa Spika, masuala haya ambayo ni ya kisayansi msingi wake mkubwa ni utafiti na baada ya ziara anayoizungumzia, kilichofanyika ni kuangalia faida na hasara yaani cost benefit analysis na baadaye gharama za kuweza kutekeleza mradi ule wa kujenga miundombinu na kukusanya maji kutoka kwenye Milima ya Shengena na kuyafikisha kwenye maeneo yanayohitajika, katika hatua za awali, ilionekana kwamba gharama zake kwa sasa hivi hayawezi kuwa yanaweza kumudu kibajeti kuliko kujenga kisima au visima hivi tulivyovieleza hapa sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kuwa hicho ni chanzo ambacho ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kingeweza kuwa ni cha kuaminika na cha kudumu zaidi lakini kikwazo ni suala la uwezo wa kibajeti hatujafunga hilo dirisha. Hilo dirisha bado liko wazi lakini tusingeweza kukaa sasa kusubiri kufanya jambo kubwa na la gharama kubwa badala ya kufanya lile linalowezekana kwa sasa hivi.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge akubaliane na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwamba kwa sasa tutaendelea kutumia njia hii ya visima vifupi na visima virefu wakati tukiwa tunaangalia uwezo wa kibejati utakapokuwa umepanda basi tutatekeleza lile la pili.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwa kweli linamezwa na swali la kwanza kwa sababu alitaka kujua kama tunaweza kutuma wataalam kwenda kuangalia ile mito ambayo iko kule na kuweza kuona kama inaweza kutumika kama vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Spika, jibu lake ni lilelile tu kwamba katika mito anayoitaja hata kama tukienda sasa hivi itakuwa ni suala la kulinganisha gharama na kwamba Wizara imeona hatua hizi zinazochukuliwa kwa sasa hivi ni za mpito ambazo zinaweza kushughulikiwa na uwezo wa kibajeti uliopo, lakini njia zile nyingine za kudumu zaidi za muda mrefu zitaangaliwa hapo baadaye baada ya uwezo wa kibajeti kuwa umepanda.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba niulize swali dogo tu kuhusiana na idara hii ya maendeleo ya jamii.
Kwa kuwa, idara hii ya maendeleo ya jamii ni muhimu sana katika Vijiji, Kata na Halmashauri zetu kwa ujumla, lakini unakuta idara hii haijaimarishwa na kwa muda mrefu Maafisa Maendeleo wamekaa katika sehemu moja kwa miaka mingi na bila nyenzo za kufanyia kazi. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuimarisha kitengo hiki na kuwasaidia Maafisa Maendeleo ya Jamii ili wafanye kazi yao ambayo sasa hivi tunavyoingia katika viwanda ndio watasaidia sana kuhamasisha wananchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua mchango mkubwa wa Maafisa Maendeleo ya Jamii hususan katika kuhamasisha na kufua hali ya wananchi kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya hapo awali ni kwamba Serikali inatambua suala hili na kupitia Sera ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1997, tumesisitiza kwanza kuweka msisitizo katika masuala mazima ya udahili; pili. kuweka msukumo sasa katika kupitia Serikali kuu na katika Halmashauri zetu kuweka msisitizo katika kuhakikisha kwamba Maafisa Maendeleo ya Jamii wanapata kipaumbele na wanaajiriwa ili waweze kwenda kuhudumu katika Halmashauri zetu. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba Naibu Waziri aliombe Bunge lako Tukufu radhi kwa kulidanganya. Amesema Tarafa ya Gonja ina Kituo cha Polisi cha Daraja B, naomba afanye home work, tarafa hii mimi ndiyo natoka na hakuna hata Kituo cha Daraja C, sasa hicho cha Daraja B amekitoa wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, hata huko anakosema kipo Kituo cha Daraja C, iko nyumba haijawahi kuwekwa polisi hata siku moja. Naomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri aeleze Bunge lako Tukufu kwa nini anatoa taarifa za uongo ambapo hata wananchi katika Jimbo langu watashangaa kwamba hicho kituo Daraja B, kiko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, Waziri atakumbuka kwamba nimeshawaandikia Wizara yao barua mara mbili kuomba kituo hiki kilichopo Maore, Tarafa ya Ndungu ambacho kimejengwa mwaka 1959, kimechakaa ceiling board zimedondoka, vigae vilivyowekwa hata kabla ya Uhuru vimebomoka hata OCS hana mahali pa kukaa kufanyia kazi, aseme lini Serikali itaweza kukarabati kituo hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili amesema Polisi wanafanya doria kwenye Jimbo hili, atajua kwamba Polisi wa Kituo cha Maore chenye Daraja B kama anavyosema kipo Tarafa ya Ndungu hawana hata matairi kwenye magari yao, usafiri wao ni wa shida, sasa hiyo doria wanaifanyaje? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilichokieleza katika majibu yangu ya msingi, nilieleza kwamba kulingana na maeneo ambayo walileta maombi ya ujenzi wa vituo katika Tarafa ya Gonja kwamba kuna Kituo cha Daraja B sio C. Katika Tarafa ya Mamba nilichokisema ni kwamba wananchi wametoa eneo, kwa hiyo tupo katika mchakato wa ujenzi wa kituo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kituo cha Maore ni kweli Mheshimiwa Mbunge aliwahi kuwasilisha barua yake kwa Mheshimiwa Waziri kuhusiana na ukarabati wa kituo hiki na barua yake tunaifanyia kazi na pale uwezo utaruhusu basi tutafanya marekebisho ya kituo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na ubovu wa magari kwa ajili ya doria, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba natarajia muda siyo mrefu kufanya ziara katika Jimbo lake nitamwomba na yeye kama atakuwa na nafasi tuambatane ili tukaone changamoto hizo. Tatizo la usafiri katika nchi yetu ni kubwa sana, kwa hiyo itategemea uzito tutakavyoona katika eneo hilo kulinganisha na maeneo mengine katika nchi nzima tuone uwezekano wa kusaidia usafiri ili waweze kufanya kazi zao vizuri hasa maeneo ya milimani ambapo hakuna mawasiliano mazuri ya usafiri.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa vile swali langu ni sawa sawa na hali halisi iliyoko Mbagala, ningependa nimuulize Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwamba jimbo la Same Mashariki limekuwa na shida sana ya walimu, tuna kata moja ya Bwambo, shule ya Changuruwe imekuwa na walimu wawili tangu darasa la kwanza mpaka la saba kwa muda mrefu sana na kilio hiki hakijaweza kusikilizwa na kufanyiwa kazi. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kunisaidia ni lini atanipa walimu tuongezee hii shule ambayo wanabidii sana lakini kwa walimu wawili hata ungefanya nini hawawezi kutosheleza kusaidia wanafunzi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge nikupe pole katika hilo. Nilivyofika katika Mkoa wa Kilimanjaro, miongoni mwa Mikoa ambayo ina walimu wengi ni Mkoa wa Kilimanjaro. Kwa hiyo, nitumie fursa hii sasa kumuagiza Afisa Elimu wa Mkoa, haiwezekani walimu wote wakajazana Moshi Mjini, wakati wananchi wa Same hawana walimu. Nimuagize Afisa Elimu wa Mkoa wa Kilimanjaro, shule zinapofunguliwa ahakikishe shule ambayo Mheshimiwa Mbunge ameianisha katika Halmashauri ya Same amepeleka walimu wa kutosha, la sivyo tutamuona kwamba hatoshi kusimamia eneo hilo la elimu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri, uvunaji wa miti hata baada ya kukomaa unakatazwa; na kwa kuwa Jimbo la Same Mashariki hakuna hata vitalu vya miti. Je, ni namna gani Serikali itahakikisha kwamba kunaanzishwa vitalu ili wananchi waweze kupata miche ya kuweza kupanda kwenye maeneo yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Same Mashariki wengi walihamasishwa na walipanda miti mingi na wengi walichukua mikopo ili wapande miti kwa biashara, lakini inapofika wakati wa uvunaji wanahangaishwa sana na Halmashauri hata pale Wizara ilipotoa maagizo kwamba waruhusiwe kuuza miti yao. Je, Mheshimiwa Waziri anatoa tamko gani hasa kwa Halmashauri ya Same ili wajue kwamba Wizara ina msimamo gani juu ya suala la wananchi waliopanda miti yao waweze kuivuna na kuiuza kibiashara? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kaboyoka katika swali lake la kwanza, anataka kujua ni namna gani Serikali itawawezesha wananchi wa kule Same Mashariki kuwa na vitalu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali lililotangulia, katika mkakati wa upandaji miti Kitaifa, kila Halmashauri ya Wilaya imepangiwa kupanda miti kwa wastani wa miti milioni mbili kila mwaka. Nasema ni wastani, kwa sababu itazingatia ukubwa wa Halmashauri, idadi ya watu, hali ya hewa ya Halmashauri inayohusika, kuona maeneo rafiki ambayo miti inaweza kupandwa. Kwa hiyo, ziko Halmashauri nyingine zitapanda miti zaidi ya hiyo, Halmashauri nyingine zinaweza zikapanda miti pungufu ya hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, uwepo wa vitalu vya miti ni suala ambalo litafanyika baada ya kazi ya mkakati huu kuwa imefikia katika Halmashauri hiyo na kwa hiyo, mtaweza kupata ushauri kutoka Wizarani chini ya mkakati huo nilioutaja ili muweze kuoneshwa ni maeneo yapi, ya ukubwa gani muweze kuwa na vitalu vya kuweza kupanda miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili la Mheshimiwa Kaboyoka, anataka tamko kuhusiana na miti ambayo inakatwa kwenye maeneo ambayo ni ya miti ya kupandwa ukilinganisha na hatua za udhibiti kwa mujibu wa sheria ambayo inazuia ukataji miti hovyo ambayo inaendana na uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu nimshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba ni jukumu la Serikali sasa kuweza ku-balance na tunaposimamia ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo mkaa na matumizi mengine, hatutakataza matumizi ya miti halali ambayo imepandwa kwa njia halali, isipokuwa usimamizi wake unaendana na upataji wa vibali mahususi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Taasisi chini ya Wizara zilizoko katika Halmashauri hiyo zitaweza kutoa utaratibu ambao chini ya utaratibu huo miti halali iliyopandwa kwa madhumuni hayo ikiwa imekidhi vigezo vya kisayansi kama vile kukomaa na mambo mengine, utaratibu huo hauwezi kuzuiliwa.
Mheshimiwa Mbunge, ufafanuzi zaidi kuhusiana na suala hili unaweza ukapatikana wakati wowote ule baada ya session hii.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kama Mheshimiwa Waziri atafuatilia na naamini ataunda hiyo Kamati maana najua bado mazingira ni machafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza ni kwamba; kwa kuwa hii mito mikubwa minne ya Yongoma, Saseni, Hingilini na Nakombo imejaa magogo ambayo yameletwa kutoka misituni na hivyo kufanya maji yatuame na yasiwafikie watu walioko mabondeni.
Je, Waziri atatusaidiaje au Serikali itatusaiaje kufundisha wananchi na kuwapa vifaa ili waweze kufanya usafi wa ile mito yaani Kiingereza wanaita dredging ili watoe yale magogo ili maji yaweze kufikia wananchi walioko bondeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba Mito ile ya Hingilini, Saseni, Yongoma pamoja na Nakombo ni kweli imeathiriwa na shughuli za kibinadamu yakiwemo hayo mdgogo aliyoyasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kifupi tutauma tena timu ya wataalam ili waende waone ukubwa wa lile tatizo na baada ya kuona ukubwa wa lile tatizo watatupa taarifa ambayo tutawashirikisha wananchi wenyewe katika maeneo yale ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha juu ya matatizo haya ambayo yanafanyika katika vyanzo vya maji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Kaboyoka usiwe na wasiwasi na kama utakuwa tayari kuambatana na mimi nitakapokuja kule, mimi nitakuwa tayari pia kuambata na wewe, ahsante sana.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunikumbuka maana mara nyingi sikumbukwi kwenye maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu liko sawasawa na la Mheshimiwa Mwalongo, ni kwamba kwenye Jimbo langu la Same Mashariki unakuta kata na vijiji hazina Watendaji, badala yake wanatumiwa Maafisa Ugani na wala wao hawana mafunzo ya kufanya kazi za utendaji. Ni lini Jimbo la Same Mashariki litasaidiwa ili tupate watendaji ambao wanakidhi hadhi ya kazi hiyo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Naghenjwa Kaboyoka, Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika nchi tuna tatizo kubwa la Watendaji hasa ngazi ya Watendaji wa Kata na Vijiji. Maeneo/halmashauri nyingi zina upungufu mkubwa sana wa Watendaji wa Kata na Watendaji wa Vijiji. Kwa hiyo, kutokana na upungufu huo wamekuwa wakitumika maafisa, wakati mwingine Maafisa Elimu wa Kata, Maafisa Ugani, Maafisa Kilimo wanakaimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa suala hili kwa sababu tunaliweka katika utaratibu wa kuomba vibali vya utumishi, napenda kuahidi nchi nzima kwamba suala hili litakuwa limekwisha ifikapo mwaka 2020.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunikumbuka ingawa ulitaka tena unifute.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwulize Waziri wa Maji kwamba Jimbo la Same Mashariki lina mito mingi ambayo inatumika kwa umwagiliaji wa mpunga na tangawizi, lakini maji hayo yanapungua kila kuitwapo leo.
Je, Wizara ina mkakati gani wa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira ili wapate fedha ya kusaidia kutunza vyanzo vya maji ya mito hii mikubwa iliyoko katika Jimbo la Same Mashariki? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli na napenda kukubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba tumekuwa na vyanzo vingi sana katika nchi yetu, lakini kiukweli ukipita maeneo mbalimbali kuna baadhi ya vyanzo vimekauka, vingine vimefikia hatua hata kupotea, ni kwa sababu tu moja, ni mabadiliko ya tabia nchi, lakini pili, shughuli za kibinadamu, watu kulima karibu na vyanzo vya maji, wengine kufanya suala zima la ufugaji na wakati mwingine hata shughuli za uchimbaji madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu ya Maji tuna mabonde, kazi yao kubwa sana ni kusimamia rasilimali za maji ili ziweze kuwa endelevu. Kingine tunapokea ushauri kuweza kushirikiana na wenzetu hawa wa mazingira katika kuhakikisha tunavilinda na kuvitunza vyanzo vya maji viwe na faida ya sasa na vizazi vijavyo. Ahsante sana.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya CAG iliyoishia Juni, 2017 imeonesha kwamba katika kaguzi zilizofanywa hasa katika Shirika la RAHCO ilitumia shilingi bilioni 20 kufanya upembuzi yakinifu wa miradi minne, lakini shilingi bilioni 20 zimepotea kutokana na kwamba miradi hiyo haikutekelezwa au haitekelezeki.
Je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba kuna harufu ya ufisadi katika miradi hii minne ambayo ametumia shilingi bilioni 20 wakati ikijulikana miradi hii haiwezi kufanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, imeonekana Wabunge wengi walikuwa wamelalamikia miradi ambayo inafanywa chini ya viwango ikitekelezwa na Wizara za Maji na Wizara za Ujenzi hasa TANROADS na kwamba pesa nyingi inatumika kwenye upembuzi yakinifu lakini nakuta miradi hiyo haifanywi.
Je, Serikali inakubaliana nami kwamba kuna sababu ya kumwomba Mheshimiwa Spika aunde Tume ya Kibunge ambayo itachunguza haya yote kwamba inakuwaje ifanywe miradi ya upembuzi yakinifu, lakini miradi hiyo haitengewi hela mwaka hadi mwaka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza kwamba kwenye upembuzi yakinifu wa NAFCO kwamba kulikuwa na ufisadi. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi ni kwamba hizi ni taarifa za kisekta na zinafanyiwa kazi na Wizara husika za kisekta. Inakuwa ni ngumu kwa mimi kusema kulikuwa na harufu ya ufisadi kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge amelitamka hili ndani ya Bunge lako tukufu; Serikali yetu ni moja, tunalifanyia kazi kuona jambo hili linafanyiwa kazi kabla ya kukiri aidha kulikuwa na ufisadi au hakukuwa na ufisadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, nimesema kwenye jibu langu la msingi Serikali yetu hufuata Katiba, Sheria, Kanuni zikiwemo Kanuni za Bunge lako tukufu na hivyo Serikali haina mamlaka ya kulipangia Bunge nini cha kufanya. Kama Bunge lako tukufu litajiridhisha kuna umuhimu wa kuunda Tume kwa ajili ya kazi hiyo anayopendekeza Mheshimiwa Mbunge, Serikali yetu iko tayari kabisa kuona hilo linatekelezwa kwa sababu ni majukumu ya Bunge kusimamia Serikali yetu. Ahsante.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Bunge lako lilipitisha hapa kwamba kilimo cha umwagiliaji ndiyo tu kinachoweza kutoa umaskini katika nchi hii. Kwa kuwa Jimbo la Same Mashariki tumepeleka maombi yetu yana miaka 16 sasa ya kujengewa miundombinu kupitia Bwawa la Yongoma kwa ajili ya umwagiliaji. Je, Waziri anaweza kuniambia lini Bwawa hili la Yongoma litajengwa ili tukuze kilimo cha umwagiliaji? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inakamilisha stadi ya mpango kabambe kwa ajili ya suala la kilimo cha umwagiliaji. Mpango ambao ukishakamilika utaainisha maeneo yote tutakayotekeleza miradi ikiwemo pamoja na kutumia Bwawa la Yongoma. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami nataka niombe tu kwamba Kituo cha Afya cha Kata ya Vunta, Tarafa ya Mamba Vunta kimepandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya takriban miaka 10 iliyopita, lakini hakijafunguliwa rasmi kutokana na kwamba kilikuwa hakijapata ukarabati unaofaa.
Mheshimiwa Spika, pamoja kwamba tunashukuru Serikali ilipeleka Ambulance, namwomba Mheshimiwa Waziri kwamba ni lini Kituo hiki kitafunguliwa rasmi ili kitambulikane kwamba kweli ni Kituo cha Afya cha Tarafa ya Mamba Vunta yenye kata tano? Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kwa sababu kuna sifa ya zahanati kupanda kutoka zahanati kuwa kituo cha afya, naye mwenyewe amekiri, ingekuwa vizuri baada ya kutembelea eneo hilo ambalo mimi nipo tayari, ili tukaone kama kweli inakidhi haja ya kuwa Kituo cha Afya itakuwa ni furaha kwangu mie kuhakikisha kwamba inapata hadhi ya kuwa Kituo cha Afya kwa mujibu wa kukidhi vigezo ambavyo vimewekwa ili kiweze kuwa Kituo cha Afya.

Kimeshapandishwa? Kama tayari kimeshapandishwa, maana yake kuna baadhi ya taratibu ambazo hazijafuatwa. Naomba tukishamaliza hiki kipindi cha maswali na majibu, nipate fursa ili tuweze kuongea na DMO tujue hasa nini ambacho kimetokea kama tayari kimeshapandishwa, lakini hakiwi treated kama Kituo cha Afya.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niseme tu kwamba kwa kuwa Serikali imeonekana inapeleka pesa kidogo sana ya maendeleo kwenye sekta hii ya kilimo hasa katika jimbo langu na kwa hiyo Maafisa Ugani wanakuwa wanakosa kazi za kufanya. Je, Serikali haioni ni kupoteza hela za Serikali kama watazidi kuongeza waajiriwa wakati hawana kazi za kufanya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; ni wazi kwamba Maafisa Ugani hawa wanaopelekwa kwenye vijiji hawajawahi kufanyiwa semina, wengine wana miaka kumi, wala orientation ya kwamba kazi ambazo wanatakiwa wazifanye kwa kipindi hiki ni nini na kwa kuwa ukijua kwamba kozi wanazochukua haziko specific kwenye mazao yale, mtu ametoka kulima korosho leo anapelekwa kwenye ndizi, hajui hata kutengeneza migomba.
Je, Serikali haioni kwamba haijawatendea haki maafisa ugani hawa wanaopelekwa vijijini bila kufanyiwa semina na orientation za kuwafanya waelewe kile wanachotakiwa kufanya katika vijiji au kata zile pamoja na kwamba pia hawana vitendea kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza amesema kwamba Serikali inapeleka bajeti ndogo, nimwambie tu kwamba bajeti inayopelekwa na Serikali Kuu katika Halmashauri ni sehemu ndogo tu ya bajeti ya jumla ambayo Halmashauri inatakiwa ifanyie kazi. Maana yake kule kuna bajeti ya ndani inaitwa own source budget. Kwa hiyo hakuna sababu yoyote inayokubalika inayomfanya Afisa Ugani yeyote aseme kwamba ameshindwa kwenda kijijini eti kwa sababu ya bajeti ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili amesema kwamba kuna Maafisa Ugani wamepelekwa kule lakini hawana ujuzi na mazao husika. Sisi Serikali tunachokifanya tunapeleka Afisa Ugani ambaye amesomea Sekta ya Kilimo, Sekta ya Mifugo kwenda kufanya kazi za ugani katika Halmashauri fulani, sasa akikuta kule kuna zao fulani mahususi ni kazi yake kujiridhisha kupitia tena, kudurusu documents mbalimbali zinazohusu zao hilo mahususi ili awe vizuri kitaaluma na kiuendeshaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakubaliana naye kwamba mtu ambaye amesoma general agriculture akienda kwenye zao la tumbaku specific atalazimika kukosa baadhi ya utaalam katika zao lile, ni kweli, lakini tunawahimiza kwamba lazima wahakikishe kwamba wanalifahamu hilo zao vizuri na waweze kuwashauri wakulima vizuri kwa sababu wao ni wataalam wa kilimo. Kama mimi ni mchumi lakini nilisoma shule ya kilimo nakumbuka masomo ya kilimo wakati ule, je mtu ambaye amesoma cheti au diploma au ana degree ya kilimo, lazima atakuwa anajua vizuri zaidi. Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze pia na mimi kujibu swali la mama yangu, Mheshimiwa Kaboyoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba na mimi niongezee hapo kidogo kwamba sisi kama Wizara ya Kilimo kupitia vyuo vyetu vyote vya mafunzo nchini, swali ambalo na mimi niliweza kulijibu jana, ni kwamba tumefanya mpango mkakati hata wale Maafisa Ugani ambao pia bado hawatoshelezi na tumesema wasikae ofisini, lakini tuna mpango mkakati kama Wizara ya Kilimo kuhakikisha kwamba tunawajengea uwezo hata wale ambao Maafisa Ugani wako maofisini ili waweze kutoa mafunzo kwa wakulima kuendana na mazao ambayo yapo katika hayo maeneo. Naomba kuwasilisha.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Kwa kuwa Bwawa la Yongoma, katika Mto wa Yongoma lilikuwa-designed na Serikali ya Japan kupitia JICA tangu 2012; na kwa kuwa mwaka huu 2018/2019 liliwekwa kwenye bajeti kwamba lijengwe, Serikali inatoa tamko gani kuhusu ujenzi wa bwawa hili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Kaboyoka. Kubwa ambalo nataka niseme ni utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha. Nia ya Serikali bado ipo pale pale, na sisi kama Wizara tunaendelea kuhakikisha fedha hizi zinapatikana ili bwawa lile liweze kujengwa na wananchi waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu swali vizuri na naishukuru Serikali kwa jitihada zake zinazoelekezwa Hangang’ hasa ziwe Bassotu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, ni kweli visima vimechimbwa, lakini nafikiri ni Wilaya ya peke yake ambayo zimewekwa solar ambazo hazina betri na ni Wilaya ambayo temperature yake iko chini kwa hiyo maji hayapatikani kila wakati. Sasa nataka kujua wakati kwingine kunawekwa solar za betri kwa nini Wilaya ya Hanang’ katika visima mbalimbali vilivyochimbwa kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri hawakuweka betri hizo na hasa Masakta ambapo ilipangiwa shilingi bilioni 1.2 mpaka leo tatizo liko palepale?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Wilaya ya Hanang’ iko kwenye bonde la ufa na kwa hivyo kuna joto chini, kwa hiyo kupata maji kwenye visima ni ngumu sana. Sasa nataka Mheshimiwa Naibu Waziri anieleze kama bwawa linalotakiwa Dirma linachimbwa na bwawa la Gehandu na Gidahababieg linachimbwa kusudi tatizo hilo la ujumla la Hanang’ liweze kukabiliwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana mama yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu kwa kazi kubwa anayofanya. Ni miongoni mwa wamama ambao wamejitoa kupigania suala zima la maji katika jimbo lake la Hanang.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la kwanza la changamoto ya betri, nimuagize Mhandisi wa Maji wa Mkoa wa Manyara afuatilie kwa haraka ili changamoto hizi tuweze kuzitatua kwa haraka ili wananchi wake waendelee kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yenye ukame au yaliyopitiwa na bonde la ufa, uchimbaji wa visima imekuwa ni changamoto kubwa sana, mfano Dilma. Sisi kama Wizara ya Maji tumeona haja sasa ya kuchimba mabwawa. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo katika uchimbaji wa mabwawa ili wananchi wake waweze kupata huduma hii muhimu na kuweza kumtua mwanamama ndoo kichwani. Ahsante sana.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Hali ya Jimbo la Same Mashariki na Shule za High School haiko tofauti sana na ile ya Kigoma Kusini. Serikali ilishatupa hela ya kujenga bweni la wasichana ili Kidato cha Tano kianze na bweni hilo la kuchukua wanafunzi 80 limeisha. Sasa hivi wananchi wameshatengeneza matofali na wanaanza ujenzi wa kupandisha madarasa mawili ili Form Five ianze. Je, Serikali inaweza kutusaidia katika vile vifaa kama mabati na kumalizia umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama ambavyo umesema, tunaposema Serikali inamalizia maboma, tumepiga mahesabu maana yake ni pamoja na kumalizia majengo yenyewe, kuezeka kuweka madirisha na kuweka madawati ndani ya vyumba vile. Tumekadiria karibu shilingi milioni 12,500,000/= kila boma moja kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tumeshapeleka fedha mwezi wa Pili kama nilivyosema, ambapo sasa tunarajia watakuwa wanaendelea kumaliza, kwenye bajeti hii pia kuna mpango wa kupeleka fedha za kumalizia maboma ya Shule za Msingi na Sekondari. Kwa hiyo, nimtie moyo Mbunge kwamba tutapeleka fedha hizo. Hayo aliyozungumza ya umeme na miundombinu mingine itazingatiwa katika kurekebisha. Hiyo ni nchi nzima kwenye Majimbo yote. Ahsante.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Same Mashariki lina tatizo kubwa sana la huduma za afya. Kituo kilichokuwa kimeitwa Kituo cha Afya Vunta kwenye Tarafa ya Mamba Vunta ilikuwa ni ghala la mazao kikapandishwa hadhi lakini hakina hadhi hata ya kuwa dispensary, Tarafa ya Gonja haina hata zahanati wala kituo cha afya cha serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kuiomba Serikali kwamba kwa muda mrefu nimeenda kuongea na Serikali kuhusu kuboresha angalau basi Hospitali ya Gonja Bombo ambayo Serikali kupitia KKKT wanasaidia watu wa Tarafa hii ya Gonja na ya Mamba Vunta kupata huduma katika hospitali hii.

Je, ni lini Serikali itapeleka angalau Madaktari basi wakasaidie kuboresha huduma hii ili akina mama wajawazito wasife wakitembea umbali mkubwa zaidi ya kilometa 15 mpaka 30 kufuata huduma katika Tarafa ya Ndungu ambayo kituo kipo bondeni na Tarafa hizi zote kubwa ziko milimani ambapo hata barabara zetu ni mbaya sana?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuunga mkono juhudi za wananchi pale ambapo wanaanzisha ujenzi wa maboma ya zahanati Serikali kupitia Halmashauri imekuwa ikichangia kukamilisha yale maboma lakini sambamba na hilo tumefanya maboresho makubwa sana ya vituo vya afya takribani kati ya vituo zaidi ya 500 ndani ya nchi yetu, zaidi ya 300 na tumeweza kuvifanyia maboresho kuweza kutoa huduma za dharura za kumtoa mtoto tumboni.

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo, Serikali katika mwaka huu wa fedha mabao unakwisha tumejielekeza nguvu katika kujenga hospitali za Wilaya 67 na lengo ni kusogeza hizi huduma za fya karibu zaidi na wananchi.

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo, katika maeneo ambapo hatuna Hospitali za Wilaya tumekuwa tunafanyakazi kwa karibu sana na hizi hospitali ambazo ziko katika taasisi za kidini ambazo kwa jina zimekuwa zinaitwa DDH na tumekuwa tunawapatia rasilimali fedha kwa ajili ya dawa pamoja na watumishi. Kwa hiyo, sisi tuko tayari kama Serikali tukipata maombi mahususi kuhusiana na hii Hospitali ya DDH ambayo nimekuwa nimeiongelea kama kuha hitaji la rasilimali watu tuko tayari kuweza kushirikiana nao kwa ajili ya lengo la kutoa huduma kwa wananchi wa Same Mashairiki.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu yaliyotolewa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza ni kwamba kutokana na utafiti uliofanyika kuangalia uwepo wa jasi katika Kata ya Bendera na Makanya umechukua muda mrefu, je, Serikali haioni umuhimu kusaidiana na Wizara ya Madini ili watume wataalamu wakafanye utafiti wa kina kujua kuna-deposit kiasi gani ili hata TIC wakiwa na nyaraka hizo iwe rahisi kwa mwekezaji kujua kwamba kuna potential ya kuwekeza katika eneo hili? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, awali yote kwanza nichukue nafasi hii kupongeza sana uongozi wa Wilaya ya Same kama nilivyoeleza awali kwa kuweza kutenga eneo hili la uwekezaji zaidi ya ekari 4000

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niweze kujibu swali dogo nyongeza la Mheshimiwa Kaboyoka, kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ukiangalia kwa takwimu za uzalishaji za hivi sasa kwa Makanya peke yake uzalishaji ni zaidi ya takriban tani 145,000 na kwa upande wa Bendera ni takriban tani 25,200. Vilevile ukiangalia kwa takwimu tulizonazo kwa TIC nchi nzima tumeweza kusajili zaidi ya miradi 78 ambayo inahusika na uzalishaji wa cement na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na jasi. Kwa hiyo, ukiangalia inathibitisha kabisa kwamba kweli Wilaya ya Same inahitaji mwekezaji.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa hitaji la kufanya utafiti, tutaendelea kushirikiana na Wizara ya Madini kuweza kuona ni kwa namna gani tunaweza kuharakisha kufanya utafiti ili kuweza kujua rasilimali iliyoko pale kwa kujua tani ni ngapi ili kuweza kuwa na uhakika hata mwekezaji anapokuja basi ijulikane ataweza kuzalisha kiasi gani lakini vilevile uhai wa migodi ile pia ni kwa miaka mingapi. Nishukuru sana kwa kufuatilia na nishukuru kwa namna ambavyo mmekuwa mkishirikiana pia na Mheshimiwa Kilango na uongozi mzima wa Wilaya ya Same.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kweli jibu limekuwa la ujumla sana nipende tu kusema kwamba Kata za Bendera, Ndungu, Kihurio zina ukame mkubwa sana na hata hivi tunavyoongea hakuna hata msitu mmoja ni Kata ya Maore tu ambayo ina kamsitu kadogo kaasili.

Swali langu la pili ni je, Serikali iko tayari kusaidiana na wanavijiji kutenga maeneo kisheria ambayo yatakuwa ni misitu ya vijiji badala ya kusema halmashauri inafanya wakati hatuoni kwamba sehemu hizi zinatendewa haki kwa kuotesha miti ambayo itapunguza ueneo wa jangwa katika eneo hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba zoezi hili limekuwepo la uhamasishaji wa upandaji miti na Wizara yangu ina mkakati wa katika mwaka 2016 – 2021 kupanda miti milioni mia mbili na themanini katika maeneo mbalimbali ya nchi. Tumechukua mapendekezo ya Mheshimiwa Mbunge kwenda katika eneo husika kwa kushirikiana na Serikali za vijiji ili vijiji vyenyewe vitoe ridhaa ya maeneo ambayo vinataka tuyatenge na kuyachukua na kuyaboresha kwa ajili ya misitu hiyo lakini uzoefu unaonesha sehemu nyingi ambazo tumekwenda baada ya kuyachukua maeneo haya na kuyaboresha wanavijiji tena wamerudi na kuyadai maeneo haya waweze kurejeshewa. Kwa hiyo, kama Mheshimiwa Mbunge yuko tayari kutoa ushirikiano Wizara yangu itakuwa tayari kutoa ushirikiano huo wa kwenda kuhamasisha upandaji miti katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini katika swali lake la pili tutatuma wataalam wetu katika Wizara yetu kwenda kuangalia uwezekano wa kuanzisha vitalu vya miti katika Kata hizo alizozitaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwanza napenda kusema kwamba Serikali imepotosha Bunge lako Tukufu kwa kusema uongo ambao haukubaliki. Je, Waziri anajua kwamba TAMISEMI chini ya Waziri Jafo waliunda Kamati ya Uchunguzi (fraud) mwaka 2018 na Kamati hii ilitoa mapendekezo kuonesha jinsi SIDO ilivyowaibia wakulima pamoja na Halmashauri ambayo haikufanya kazi yake vizuri kuwasahauri wakulima na michango ambayo ilitolewa na Rais wakati huo Kikwete, karibu shilingi milioni 300 haikutumika vizuri na akaomba hatua madhubuti zichukuliwe na SIDO ilipe hela zile za wakulima?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri ana habari kwamba kutokana na kutofanya kazi kwa mitambo ile ndiyo maana sasa hivi PSSF imenunua mitambo mipya na inaifunga kwa kuona kwamba mitambo ile iliyofungwa ilikuwa batili? Inakuwaje Waziri…

NAIBU SPIKA: Umeshauliza maswali mawili tayari.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kaboyoka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme hakuna uongo ambao umesemwa katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi kwamba SIDO baada ya kuingia mkataba ule na kuweza kufunga mtambo ule kulikuwa na changamoto mbalimbali na hasa kwenye upande wa ukaushaji katika mchakato ule. Baada ya kujadiliana na Halmashauri ya Same ikaonekana kwamba wakulima wale walikuwa hawaridhishwi na utendaji wa mitambo ile kwa hiyo SIDO ilishirikiana na mradi wa Market Infrastructure, Value Addition And Rural Finance - MIVARF kuagiza mtambo mpya ambao ulikuwa na gharama ya shilingi milioni 29 na SIDO walichangia katika mtambo huo mpya shilingi milioni 9 na ukafungwa kama nilivyosema tarehe 27/02/2015 na ukaendelea kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hasara au gharama ambazo zilikuwa zimeingiwa na wakulima wale baada ya kuwa mtambo ule haufanyi kazi vizuri, kama nilivyosema tunaielekeza SIDO waweze kufanya mashauriano na Halmashauri ili waone namna gani ya kuwafidia wakulima wale ambao walipoteza mazao yao kipindi kile ambapo mtambo ule ulikuwa haufanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtambo uliopo sasa hivi unafanya kazi vizuri na yeye atakuwa ni shahidi. Wakulima wale wameridhika na wanaendelea kufanya kazi zao za kuchakata zao la tangawizi.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika Bunge lililopita la Kumi na Moja, Bunge lako Tukufu lilielezwa kwamba Serikali imetenga shilingi bilioni 5 kuanza kuweka lami barabara ya kutoka Same Kisiwani - Mkomazi. Je, kazi hii itaanza lini? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Naghenjwa Kaboyoka, Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama Serikali ilivyoahidi kwamba imetenga shilingi bilioni tano kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Same Kisiwani, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba bado barabara nyingi hazijatangazwa na zitaendelea kutangazwa kadri tunavyokwenda na barabara nyingi tu zitatangazwa kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha. Pia tunategemea baada ya bajeti hii barabara hizo zitaendelea kujengwa ikiwa pengine ni pamoja na hii Same Kisiwani, itategemea na bajeti hii tunayoendelea kuipitisha itakavyokuwa imepita. Ahsante.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, shule hizi ziliahidiwa tangu 2019/2020 kwamba zingeanza high school; na madarasa yalishakamilika Shule ya Bombo na bweni lilikuwa ni moja tu ambalo lilikuwa lijengwe ili wavulana nao wapate nafasi. Cha kusikitisha ni kwamba sasa yamepelekwa tena mpaka Septemba 2022. Swali langu ni kwamba: Kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kuona kwamba high school ni muhimu sana katika shule zetu ili wanafunzi wetu waweze kuendelea na masomo ambayo yatawapa ujuzi zaidi katika maisha yao? (Makofi)

Swali la pili ni kwamba, kwa kuwa somo la Stadi za Kazi mashuleni linafanywa zaidi kinadharia: Je, Serikali ina mpango gani kuongeza nguvu katika kufanya masomo ya vitendo kusudi wanafunzi wanapomaliza shule wakaweze kujiajiri kwa kuzingatia kwamba Serikali haiwezi kuajiri wanafunzi wote wanaomaliza shule? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Naghenjwa amejaribu kuainisha, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kufungua shule hizo kama ambavyo ilikuwa imeahidi katika mwaka wa fedha 2019/2020? Nimweleze tu kabisa kwamba Serikali inafahamu umuhimu wa kuanzisha Kidato cha Tano na Sita katika shule hizo na ndiyo maana tumekuwa tukipeleka fedha kila mwaka ili kuhakikisha kwamba shule hizo zinakidhi vigezo vyote vinavyotakiwa. Kwa sasa kuna upungufu wa miundombinu ya msingi; madarasa bado hayajajitosheleza, hakuna maabara na hakuna maktaba katika maeneo hayo. Kwa hiyo, tunataka tukamilishe ili tuweze kuzifungua shule hizo zikiwa na vigezo vyote vilivyokamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili kuhusu stadi za kazi mashuleni kwamba wanafunzi kwa sasa wanasoma nadharia, nieleze tu kwamba Sera ya Serikali ni kuhakikisha kwamba stadi zote za kazi mashuleni wanafunzi wanafanya kwa vitendo. Ndiyo maana unaona katika mwaka uliopita 2020 kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, watoto waliomaliza Kidato cha Nne kwa mfano kwenye masomo ya sayansi hawakufanya ile alternative to practical, walifanya ile real practical kwenye mitihani yao.

Mheshimwia Naibu Spika, kwa hiyo, hii inaonesha tu kwamba nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaondoa hii dhana ya nadharia na ndiyo maana katika bajeti zetu unaona tumejenga maabara karibu katika shule zote nchini na tutahakikisha tutazikamilisha kwa wakati ikiwemo kuzipelekea vifaa. Ahsante.
MHE. NAGHENJWA L KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa katika mwaka wa fedha huu 2021 Serikali ilisema imetenga bilioni 5 kwa ajili ya kujenga barabara ya kutoka Same Kisiwani mpaka Mkomazi kwa kiwango cha lami. Je, fedha hiyo itatolewa lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kaboyoka Viti Maalum kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema fedha hii kwa kujenga kwa kuanza kwa kiwango cha lami Same hadi Mkomazi ambapo tumetenga bilioni 5 fedha itaanza kutoka mara bajeti itakapoanza kutumika ya mwaka 2021/2022, ahsante.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Kwa kuwa wananchi wa Tarafa ya Gonja katika Wilaya ya Same kwa takriban miaka kumi sasa wameomba kujengewa Bwawa la Yongoma ili lisaidie umwagiliaji katika Kata kame za Ndungu na Maore na design ilishafanywa na wajapan tangu 2012. Je, ni lini Serikali itajenga bwawa hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kaboyoka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika bajeti inayokuja mwaka 2022/2023 tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa 19, natumai pia na bwawa la Mheshimiwa litakuwemo ndani ya ujenzi huo. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumuuliza Naibu Waziri kwamba kwa kuwa barabara nyingi zilizoko chini ya TARURA, mifereji yake imejaa takataka, imeota majani na ni nyingi na hasa zile Mjini. Na kwa kuwa, tunajua kwamba TARURA ina upungufu wa wafanyakazi: -

Je, Serikali haioni ni muhimu wakaishauri TARURA iingie mkataba agencies yoyote ambayo inaweza kusaidia kufanya usafi wa barabara hizi?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, wazo tumelipokea, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zipo taratibu wa barabara hizi kufanyiwa usafi. Usafi ni pamoja na kufyeka, kuondoa mchanga, ama kuzibua makaravati yanayokuwa yameziba, kazi hizi huwa zinatangazwa ambapo Wakandarasi wanaomba na kupewa hizo Kandarasi kwa ajili ya kufanya huo usafi. Kwa hiyo utaratibu upo na barabara hizo zinasafishwa kwa upande wa TARURA TAMISEMI wanasimamia kuhakikisha kwamba barabara zinasafishwa lakini kwa barabara za TANROADS ambazo zipo chini ya Wizara ya Ujenzi pia zinasimamiwa kuhakikisha kwamba barabara hizi hazizibi kwa sababu ya uchafu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitoe rai kwa watumiaji wa barabara kwamba sehemu kubwa ya kuziba hii barabara na uchafu wakati fulani ni kwa sababu ya kazi za kibinadamu ambazo watu wanafanya kazi kwenye hifadhi ya barabara na kusababisha tatizo hilo. Kwa hiyo, niwaombe wananchi kupitia nafasi hii kutokufanya kazi za maendeleo kwenye hifadhi za barabara kwa sababu zinazababisha barabara hizo kuziba. Ahsante. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza pia nikushukuru kwa kunipa nafasi kwamba swali hili lirudiwe leo kwa mara ya tatu.

Kwa kuwa, Kata ya Bombo lijenga Ofisi yake ya Kata na ikaweka nafasi ya Polisi pamoja na chumba cha mahabusu. Kwa kutambua kwamba hizi sehemu zote ulizoongelea ziko tambarare na hawa wakazi wa Kata Tisa zote wako milimani ambako usafiri ni shida sana. Je, Serikali haioni ianzishe kituo mnaita Police post ili angalau katika Kata hii ya Bombo kiwepo kusaidia wananchi walioko huko milimani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuwapongeza wananchi wa eneo hilo kwa kujenga jengo la utawala ngazi ya Kata na kutenga eneo kwa ajili ya huduma za Kipolisi. Nitumie nafasi hii kuelekeza Jeshi la Polisi hususani Mkoa wa Kilimanjaro kutembelea eneo hilo kuona kama ujenzi ule unakidhi kuwa Kituo cha Polisi basi huduma za kipolisi zianze kutolewa kwenye eneo hilo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu haya ambayo yanaleta faraja kwa watu wa Same, kati ya mtandao wote wa barabara hizi za Same za kilometa 874 asilimia 80 ya barabara hizo zina-connect watu wa milimani ambao wao ndio wakulima wengi na kule ndiko kwenye mvua kubwa ambazo hizi barabara huharibika mara kwa mara.

Je, Serikali itakubaliana na mimi kwamba wakati umefika sasa barabara hizo zitengenezwe kwa kutumia aidha mawe au zitumie zege hasa zile sehemu mbaya ili wananchi waweze kupeleka mazao sokoni kwa wakati wote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri maeneo ambayo ameyaainisha ya milimani katika Halmashauri ya Same na mimi nimefika na ninatambua hali ngumu ambayo wanapata wananchi wa maeneo hayo na Serikali tumepokea ushauri na tutashauriana katika ngazi za chini ili waweze kutekeleza sehemu ya mawazo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyatoa, ahsante sana.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata majibu ya swali hilo, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa utafiti uliofanywa na Tanzania National Carbon Center mwaka 2018 unaonesha kwamba mifugo ya kuchungwa – siyo ile ya kusafirishwa, ya kuchungwa inachangia asilimia 28 ya uharibifu wa mazingira. Je, Serikali ilitoa maagizo kwa halmashauri kwamba zitenge maeneo ya hao wafugaji ili wapate maeneo makubwa ya kufugia?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, ranchi zetu zilizopo Tanzania haziwezi kutumika kama mashamba darasa ya wale wakulima wetu wakubwa wasiojua faida ya ufugaji ambao siyo wa kuswaga?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninashukuru kwa maswali madogo mawili ya msingi ambayo Mheshimiwa ameyaeleza, nimhakikishie tu kwamba kwa sasa Serikali ina mpango wa kutenga maeneo na tumeanza kufanya hivyo, katika hatua ya awali mpaka sasa tumetenga hekta Milioni 3.38 ambazo zitachangia katika malisho na zimeelekezwa katika halmashauri za vijiji, lakini kutumia ranch kama eneo la mashamba darasa jambo hilo ndiyo lipo katika mkakati wa sasa na tumekuwa tukifanya hivyo katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, moja ya mipango mikubwa tuliyonayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni pamoja na hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameeleza. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka hapo awali tulikuwa na shule ambazo zilikuwa za wananfunzi wenye vipaji maalumu. Shule hizo zilikuwa Kilakala, Loreza, Tabora Boys, Mzumbe, Iliboru na kadhalika lakini hadi sasa hivi hatuzisikii hizo shule zikizungumziwa au tukipata taarifa kwamba performance yake ya vile vipaji vyao maalum vimetumikaje.

Je, Serikali ina mpango gani basi kuziimarisha hizo shule ilikusudi tuone kwamba huu mtaala ambao unatengenezwa sasa hivi wa mali utaweza pia kuwa na tija katika shule hizi maalum?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; tumeona nchi za wenzetu kama Japan na Uchina wanatilia sana mkazo kwenye kazi za stadi, na matokeo yake ni kwamba zile kazi zinazotengenezwa na wanafunzi zinauzwa wakati wakifanya mahafali ya shule na kuwaalika wazazi ili kusudi wanafunzi wale wapate morali kwamba kweli vile wanavyotengeneza vina maana na wawanye wengine wa shule nyingine wapate moyo kwamba kumbe hizi shule za ufundi zina maana.

Je, Serikali ina mpango gani pia kuanzisha utaratibu ambao hivi vifaa vinavyotengenezwa na wanafunzi hawa wanaokwenda kwenye hizi shule za amali zitakuwa zenye thamani ya kuweza kuuzika ili ziongeze kipato kwenye shule hizi wanazofanyia?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kaboyoka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli alichozungumza Mheshimiwa Mbunge. Nimuondoe wasiwasi, shule hizi bado zipo. Kwa upande wa wasichana ni kama alivyozitaja; tuna Shule ya Msalato hapa Dodoma tuna Kilakala ambayo ipo Morogoro. Pia tuna Tabora Girls ambayo ipo kule Tabora. Kwa upande wa wavulana tuna shule ya Kibaha Sekondari, tuna Mzumbe, tuna Ilboru pamoja Tabora Boys.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani jambo kubwa alilolizungumza ni kwamba hazisikiki. Tunaomba tuchukue ushauri wa Mheshimiwa Mbunge twende tukaimarishe ufundishaji. Hizi ni shule zetu ambazo tunasema ni maalum kabisa kwa ajili ya kupokea watoto wenye vipaji na vipawa mbalimbali. Tunaendelea kuzihudumia na kuziimarisha, lakini tunaomba tuchukue fursa hii, tubebe ushauri wako ili twende tukaziimarishe zaidi ili ziweze kujitangaza kama ilivyokuwa zamani, zilikuwa zinavuma sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili amezingumzia suala la zile study mbalimbali. Kwa vile tumesema kwamba sasa hivi tunafanya mapitio ya mitaala, mapitio ya mitaala hii itakwenda kuongeza baadhi ya masomo ambayo yatakwenda kufundisha sanasana stadi mbalimbali hasa kwenye skills.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia suala la kuongeza ubora wa vile vitu ambavyo vitakuwa vinazalishwa ili viende vikapate soko, kwa maana ya tuvibiasharishe iwe kama kitega uchumi cha chuo. Tunaomba tubebe ushauri huo; na kwa vile tunapitia mitaala tutakwenda kuchopeka baadhi ya kozi ambazo tutakwenda kuzungumza au tutakwenda kushughulikia zaidi zile study za mikono na kazi za mikono ambazo tutakwenda kuzipeleka sokoni kwa ajili ya kukuza na kuongea vipato na iwe kama miradi kwenye shule zetu.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa Serikali ilishachukua vipimo vya kujenga Bwawa la Iyongoma na bwawa hili ni muhimu sana kwa ajili ya kumwagilia Skimu ya Ndungu ambayo kwa muda mrefu imekuwa na matatizo: Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga bwawa hili?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo yeye mwenyewe amesema kwamba tayari kuna mipango inaendelea kuhakikisha tunalijenga hilo bwawa na wataalamu kama walishakuja kuangalia. Moja ya maeneo ambayo tutaangalia ni haya ambayo tayari yameshafanyiwa usanifu yakinifu ili yaweze kuanza kutekelezwa kadiri ambavyo tumepanga kwenye bajeti zetu za Wizara na kuhakikisha pia kama kuna miradi mingine ambayo itapelekea kukamilisha mabwawa haya nayo pia tutaangalia. Kwa hiyo, hili bwawa nalo litawekwa katika kipaumbele katika mipango ya Wizara, nakushukuru sana.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Shirika la CARMATEC limebobea katika kutengeneza mitambo ya biogas; je, Serikali inajishughulishaje na shirika hili karika mambo ya utengenezaji wa biogas?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa nchi ya China inaongoza kwa uzalishaji wa biogas kwa kiwango cha cubic meters 15,000,000 kwa mwaka; je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka wananchi wetu wakasome wapate ujuzi wa hali ya juu wa kutengeneza biogas; kwanza kwa sababu tunahitaji kufuga zaidi kisasa kuliko kuswaga ng’ombe; na pili itapuguza uharibifu wa mazingira kwa ajili ya mmomonyoko wa udongo unaoletwa na ng’ombe wengi ambao wanachungwa badala ya kufungwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Mbunge anataka kujua namna ambavyo Serikali na Wizara yetu inavyoshirikiana na mashirika haya ikiwa ni pamoja na wadau wetu wa China. Wizara imepokea ushauri huo wa Mheshimiwa Mbunge. Tutakwenda kulifanyia kazi jambo hili la mashirikiano yetu na kupeleka wanafunzi wetu kwenda kujufunza nchini China.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, jambo hili tumelichukua na ushauri huu tumeupokea na tutakwenda kulifanyia kazi.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza, kwa vile kumekuwa na malamaiko ya wananchi ambao wananyang’anywa mashamba yao halafu wanapewa hela. Katika harakati za kuhangaika kutafuta mashamba mpaka ile hela inaisha. Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kuelimisha wananchi kuhusu Sheria hii ili pale wanapopewa fedha waombe pia wapewe na shamba?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kutokana na kwamba ardhi kubwa ya Tanzania haijapimwa. Je, Serikali itakapowapa mashamba mbadala hawa wananchi walionyang’anywa itawahahikishiaje kwamba hawatahamishwa tena maana haya yameshatokea na wananchi wanahangaika sana katika kuji-establish mara ya tatu. Naomba nipate majibu.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa swali lake la kwanza kwamba tutoe elimu ya hii Sheria kwa wananchi ili waweze kupata fidia zote mbili kwa pamoja au kwa namna yoyote ile.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, suala la fidia linazingatia sana mazingira ya eneo ambapo mtu anafidiwa. Kwa hao wenzetu wa kulima kimsingi mamlaka za Mkoa huwa zinashirikishwa kwa karibu sana katika suala zima la namna ya kuwapa fidia ya maeneo mengine wale wananchi na kumekuwa hakuna matatizo makubwa sana. Usalama wa mashamba pale wanapofidiwa yale mashamba kwa vyovyote kama ni mkono wa Serikali umekwenda kuwaondoa pale. Yale mashamba mapya watakayopewa lazima yatolewe kwa utaratibu wa kupimwa na wapewe zile hati ambazo zitawasaidia kuwaweka kwenye usalama wa maeneo mapya waliyopewa.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kusimamia taasisi ndogondogo zinazoumiza wananchi katika mikopo yake kama hizi zinazojulikana kama kausha damu, komandoo, rusha roho na kadhalika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango na mikakati na ndiyo maana tumeanzisha sheria na taratibu kwa hiyo taasisi yoyote ambayo inaanzisha mikopo lazima ifuate sheria na taratibu na iwe imesajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali la nyongeza.

Kwa kuwa Serikali ina mpango wa kuendelea kuwapatia vijana wetu ajira; na kwa kuwa tumeona sehemu kubwa ya ranchi bado hazitumiki.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kugawia vijana wetu maeneo ya kufuga na wakawafundisha ufugaji bora ili waweze kuwekeza sawa na wale wenzetu katika sekta ya kilimo walivyofanya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, mpango tulionao sasa hivi ni pamoja na kuongeza maeneo na kugawa maeneo ambayo hayatumiki kwa vijana ambao sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumepanga kufanya hivyo katika mwaka wa fedha unaokuja. Kwa hiyo, liko kwenye mpango na tunakwenda kulitekeleza, ahsante sana.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kujua kwamba Wilaya ya Same ina madini mengi ya gypsum hasa kwenye Kata za Bendera na Makanya na kwa kujua kwamba gypsum inaweza kuwa na products nyingi ambazo zitatengeneza ajira kubwa katika viwanda hivyo. Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia wananchi wa Wilaya ya Same kupata wawekezaji ili waweze ku-process ile gypsum wa-add value? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Naghenjwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli moja ya maeneo ambayo tunayaangalia ni kuhamsisha uwekezaji katika sekta nyingi ikiwemo hii ya madini na hasa ya gypsum ambayo inatumika katika maeneo mengi kwenye ujenzi na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake najua ndio wanashiriki sana katika shughuli za kiuchumi kama nilivyosema tutaona namna ya kukaa na Mheshimiwa Mbunge ili tuone kama kunakuwa na andiko kwa ajili ya Wilaya ya Same ambayo litavutia mahususi uwekezaji wa viwanda katika sekta hii kwa maana ya kuzalisha gypsum na shughuli nyingine za kiuchumi au viwanda vingine katika Jimbo la Same.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nataka kumkumbusha tu kwamba, pamoja na kwamba nchi yetu kuwa na ukubwa wa eneo lenye square kilometer 947,300 eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta milioni 44 tu.

Je, Serikali haioni wakati umefika kuharakisha kutunga sheria itakayolinda eneo hili la kilimo ili lisije likavamiwa kwa shughuli nyingine? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuilinda ardhi kwa ajili ya kilimo. Kama nilivyosema hapa, tumeamua kupitia baadhi ya sheria ili mwisho wa siku tuje na sheria ambayo imekamilika. Nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaharakisha mchakato huu ili mwisho wa siku tupate sheria yetu ya kilimo, tutunze ardhi ya kilimo.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwanza namshukuru Naibu Waziri wa Kilimo kwa majibu yake mazuri aliyoyajibu kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, lakini nilichotaka kusema tu ni kwamba, Wizara ya Ardhi pamoja na Wizara ya Kilimo tumeshaanza mchakato wa kuyatambua yale maeneo ambayo yanafaa kwa kilimo. Kwa hatua ya kwanza itakayofanyika ni kuya-gazette ili yasiweze kuingiliwa na watu wengine. Kwa hiyo, stage nyingine itakayofuata ndiyo hiyo ya kutunga sheria ili kuyalinda kwa ajili ya uhifadhi wa kilimo. (Makofi)
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; Tarafa ya Gonja yenye kata nne na Tarafa ya Mambavunja yeye kata tano zote hizi zimekuwa hazina kituo cha polisi na kwa muda mrefu tumeomba mpaka wananchi wameweka nafasi za kwamba polisi wanaweza kuanzia pale na kuna sehemu za kujenga vituo vya polisi.

Je, lini Serikali itatusaidia kujenga vituo hivyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kaboyoka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua uwepo wa baadhi ya tarafa na kata zisizokuwa na vituo vya polisi na polisi wetu tunaowapanga mpaka kwenye ngazi ya kata wanatumia majengo ambayo huamuliwa na mamlaka zetu za Serikali za Mitaa. Nimuombe Mheshimiwa Kaboyoka kuwa na subira, tunavyoanza kutekeleza mkakati wetu wa kujenga vituo vya polisi mahala ambako hakuna kabisa vituo, zikiwemo tarafa alizozitaja huko Gonja. Nashukuru.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itakabidhi Mradi ulioko katika Kata ya Vuje, Wilaya ya Same, ambao ulianza tangu 2018 ambao uligharimu takribani Sh.1,300,000,000?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, miradi ikishakamilika ni wajibu wa Wizara kukabidhi kwa wananchi na unaendeshwa na vile vikundi vidogo vidogo ambavyo vinaundwa na wananchi. Kwa hiyo na mradi huu ambao umeshatumia fedha ya Serikali zaidi ya bilioni ni lazima nao uje ukabidhiwe kwa wananchi, ili lengo la kufikisha huduma ya maji kwa wananchi liweze kutimia.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali ya nyongeza. Kwa kuwa tafiti zimeonesha kwamba Gypsam au jasi inatoa mbolea ikichakatwa na kwa kuwa Wilaya ya Same ina jasi nyingi katika Kata ya Bendera na Makanya: Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka viwanda katika sehemu hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kaboyoka, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika malighafi ambazo zinatumika katika kuzalisha mbolea, mojawapo ni Gypsam, na kwa sababu Mheshimiwa Mbunge amesema kuhusiana na Jimboni kwake, Mkoani huko, basi tutaona namna gani ya kuvutia pia wawekezaji waweze kuona namna ya kutumia malighafi zilizopo pale ili kuanzisha viwanda vya mbolea kama ambavyo tunavutia maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.

Wilaya ya Same Jimbo la Same Mashariki kuna mito mikubwa mitatu ambayo inatitirisha maji bondeni ili wananchi watumie katika umwagiliaji wa mpunga kwenye Kata za Maore, Ndungu na ...

SPIKA: Swali?

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Tatizo hii mito imejaa magugu imejaa magogo. Je, Serikali iko tayari kusaidia mito hii isafishwe ili maji yatiririke kwa urahisi? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, ni jukumu la Serikali kusaidia maeneo mbalimbali na hata eneo hilo kifupi ni kwamba niwatume wataalam wangu kwenda kuangalia kufanya need assessment ya eneo lile, lengo ni kwamba tunapoenda kutafuta mipango ya kutafuta fedha na eneo hilo tuweze kulishughulikia maana yake sambamba na Ziwa Jipe ambalo liko katika Wilaya ya Mwanga kule katika Mkoa wa Kilimanjaro.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina swali la nyongeza; kwa kuwa Bwawa la Kalemawe lililopo Jimbo la Same Mashariki lililojengwa na wakoloni mwaka 1958/1959 limejaa tope sana na hili lilikuwa linasaidia sana wakulima wa kata ya Kalemawe, Kihurio na Bendera. Je, Serikali ina mpango gani kusaidia kutoa tope hilo ili ikusanye maji ya kuweza kusaidia kwenye kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaelekeza timu ya wataalam waende kuangalia eneo hilo ili wapate tathmini halisi na baadaye waweze kufanya utekelezaji katika eneo hilo.