Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. David Mathayo David (25 total)

MHE. SHALLY J. RAYMOND (K. n. y MHE. DKT. DAVID M. DAVID) aliuliza:-
Je, mradi wa maji tambarare ya Mwanga na Same hadi Korogwe umefikia hatua gani na wananchi wategemee utakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa kupeleka maji katika Miji ya Mwanga na Same pamoja na Vijiji vya Wilaya ya Mwanga, Same na Korogwe vilivyopo kandokando ya bomba kuu. Mradi huu utakapokamilika unatarajia kuhudumia watu 456,931. Ujenzi wa mradi huo umegawanywa katika awamu mbili. Awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa chanzo cha maji, mitambo ya kusafisha maji na miundombinu ya kusafirisha na kusambaza maji katika miji ya Mwanga na Same. Awamu ya pili inahusisha ujenzi wa miundombinu ya kupeleka maji katika vijiji 38 vilivyo kandokando ya bomba kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza imepangwa katika loti tatu. Utekelezaji wa loti ya kwanza unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, ujenzi wa mtambo wa kusafisha maji na kulaza bomba la urefu wa kilomita 12.8 kutoka kwenye chanzo hadi kwenye matanki ya kituo cha kusukuma maji Kisangara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, loti ya pili inahusu ujenzi wa miundombinu ya kupeleka maji katika Mji wa Mwanga ambao upo katika hatua ya manunuzi. Tayari zabuni zimetangazwa ili kumpata mkandarasi mwenye sifa. Aidha, fungu la tatu la ujenzi wa miundombinu ya kupeleka maji katika Mji wa Same utekelezaji wake unaendelea na mkandarasi yupo katika hatua ya maandalizi ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa mradi wa Same - Mwanga - Korogwe awamu ya kwanza unatarajiwa kukamilika Disemba, 2019. Ujenzi wa awamu ya pili ambayo inahusisha kupeleka maji katika vijiji vilivyo kandokando ya bomba kuu haujaanza kutokana na ukosefu wa fedha. Serikali inaendelea kutafuta fedha za utekelezaji wa awamu hiyo.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-
Vijiji 48 vya Jimbo la Same Magharibi vyenye zaidi ya kaya 2,943 havijapatiwa umeme wa REA japokuwa vina mahitaji makubwa ya umeme.
Je, ni ipi ratiba ya kuwasambazia umeme wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi kabambe wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu umeanza nchi nzima tangu Machi, 2017. Mradi huu unajumuisha vipengele vya miradi vitatu vya Densification, Grid Extension pamoja na Off Grid Renewable.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zitakazofanyika ni kuongeza wigo wa usambazaji umeme katika vijiji, vitongoji vyote, taasisi za umma na maeneo ya pembezoni ambayo hayajafikiwa na miundombinu ya umeme, ikiwa ni pamoja na visiwa.
Mradi wa REA Awamu ya Tatu utakamilika mwaka 2020/2021. Vijiji vya Jimbo la Same Magharibi vitapatiwa umeme kupitia mradi huu wa REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivyo itahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 67.81. Ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 261, ufungaji wa transfoma 43 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja 2,457.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii itagharimu shilingi bilioni 10.8.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-
Mkomazi Game Reserve (sasa Hifadhi ya Taifa Mkomazi) ilianzishwa kabla ya Uhuru wakati tukiwa na idadi ndogo ya watu na mifugo.
Je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa kusogeza mipaka ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi ili wananchi wa Kata za Visiwani, Mji Mdogo wa Same na Vumari wapate maeneo ya kuishi, kilimo na ufugaji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa Mkomazi imetokana na kupandishwa hadhi kwa Pori la Akiba la Mkomazi – Umba kupitia Tangazo la Serikali Namba 27 la mwaka 2008. Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ilirithi mipaka ya lililokuwa Pori la Akiba la Mkomazi – Umba mipaka ambayo ilitambulika kisheria kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 275 la mwaka 1974.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ni sehemu muhimu ya mfumo wa kiikolojia na toshelezi kwa idadi ya wanyamapori waliopo hifadhini kujipatia mahitaji yao ikiwemo malisho, maji na maeneo ya mazalia hivyo kufanya hatua za kupunguzwa kwa eneo kusababisha athari hasi ikiwemo baadhi ya wanyamapori kutoka nje ya hifadhi kwa ajili ya kujitafutia mahitaji yao muhimu na hatimaye kusababaisha kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na wanyama pori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 hairuhusu kufanyika kwa shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ikiwepo kilimo, ufugaji na uchimbaji madini. Hivyo, kutokana na sababu hizi za msingi za kiuhifadhi, kwa sasa Serikali haioni haja ya kusogeza mipaka ya hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, isipokuwa kwamba Serikali itaendelea kupokea kutoka kwa wananchi na wadau wengine maoni yatakayozingatia matakwa ya sheria na taaluma ya uhifadhi. (Makofi)
MHE. MATHAYO D. MATHAYO aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuongeza ukwasi katika benki na kwa wananchi wa kawaida ili washirikiane na Serikali katika kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja, kaya na taifa kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mathayo David Mathayo, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufikia malengo ya Serikali ya kuimarisha uchumi na kudumisha utulivu wa mfumuko wa bei, Benki Kuu hutekeleza Sera ya Fedha inayolenga kudhibiti ukwasi ili uendane na mahitaji halisi ya uchumi. Kati ya Julai, 2016 na Julai, 2017 kiwango cha ukwasi katika mabenki kwa ujumla wake kiliongezeka kutoka asilimia 35.53 hadi asilimia 38.41 kwa mtiririko huo. Kiwango cha ukwasi wa asilimia 38.41 ni kizuri zaidi katika uchumi ikilinganishwa na kiwango cha chini cha asilimia 20 kinachotakiwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuimarika kwa ukwasi kwa mwaka 2017 kunatokana na hatua mbalimbali za kisera zinazochukuliwa na Benki Kuu. Miongoni mwa hatua hizo ni kutoa mikopo ya muda mfupi kwa mabenki, kununua fedha za kigeni katika soko la jumla la fedha za kigeni (Interbank Foreign Exchange Market) na kushusha riba inayotozwa kwa benki za biashara na Serikali wanapokopa Benki Kuu kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12 mwezi Machi, 2017 na kutoka asilimia 12 hadi asilimia tisa mwezi Agosti, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine iliyochukuliwa na Benki Kuu ni pamoja na kushusha kiwango cha sehemu ya amana ambayo mabenki yanatakiwa kuhifadhi Benki Kuu kutoka asilimia 10 hadi asilimia Nane (8) kuanzia mwezi Aprili, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Benki Kuu, hali ya ukwasi katika sekta ya fedha, hususan benki ni nzuri na hakuna vihatarishi vya kuleta madhara hasi katika uchumi wetu. Aidha, Benki Kuu itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha masoko ya fedha kwa lengo la kuhakikisha kwamba, yanaendeshwa kwa ufanisi na ushindani na hivyo kusaidia kuongeza ukwasi miongoni mwa mabenki na taasisi nyingine za kifedha.
MHE. COSATO D. CHUMI (K.n.y. MHE. DKT. DAVID M.
DAVID) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu za mkononi katika kata za Jimbo la Same Magharibi hususani Kata za Msindo, Mshewa, Mhuzi, Vumari, Vuudee, Tae, Suji, Gavao, Saweni na Ruvu Jiungeni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Kata za Vumari, Suji na Ruvu Jiungeni vitafikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia utekelezaji wa mradi wa Kampuni ya Simu ya Viettel. Utekelezaji wa mradi chini ya Kampuni ya Viettel unapaswa kukamilika mwezi huu wa Novemba, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Vijiji vya Kata za Mhezi, Msindo, Mshewa, Vuudee, Tae, Gavao na Saweni vinafanyiwa tathmini na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na vitaingizwa katika orodha ya miradi ya mfuko itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa pesa.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-
Serikali iliahidi katika bajeti ya 2012, 2013 na 2014 kujenga Malambo, Majosho na Kisima kirefu kwa ajili ya wananchi na Wafugaji wa Kata ya Ruvu katika Jimbo la Same Magharibi:- Je, ni lini ahadi hiyo itakamilishwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshiniwa David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia bajeti yake na program mbalimbali imeendelea kukarabati na kujenga miundombinu ya maji ya mifugo kwa kutumia vipaumbele kama maeneo yenye mifugo mingi na yale ambayo yanapokea mifugo wakati wa kiangazi. Kupitia utaratibu huo Wizara imeweza kujenga mabwawa na malambo katika Wilaya za Kiteto, Kilindi na Ngorongoro. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2013/2014, Wizara ilitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa malambo katika Wilaya ya Same na Wilaya nyingine.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Wizara haikupatiwa fedha kwa ajili ya kufanya kazi hiyo. Mwaka 2015/2016, wataalam wa Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Same waliainisha eneo la Kijiji cha Ruvu, Kata ya Ruvu kwa ajili ya ujenzi wa lambo. Mwaka 2017/2018, Wizara imetenga fedha kwenye bajeti yake kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji kwenye baadhi ya Wilaya ikiwemo Wilaya ya Same.
Mheshimiwa Spika, naendelea kuzishauri Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kutenga fedha kupitia bajeti zao kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji ya mifugo kama malambo, mabwawa na visima virefu ili kupunguza kero ya upatikanaji wa maji kwa mifugo hasa wakati wa kiangazi. Aidha, Wizara itaendelea kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa kujenga na kukarabati miundombinu ya maji ya mifugo kutegemeana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-
Mkomazi Game Reserve (sasa Hifadhi ya Taifa Mkomazi) ilianzishwa kabla ya Uhuru wakati tukiwa na idadi ndogo ya watu na mifugo.
Je, Serikali haioni kwamba sasa ni wakati muafaka wa kusogeza mipaka ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi ili wananchi wa Kata za Visiwani, Mji Mdogo wa Same na Vumari wapate maeneo ya kuishi, kilimo na ufugaji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa Mkomazi imetokana na kupandishwa hadhi kwa Pori la Akiba la Mkomazi – Umba kupitia Tangazo la Serikali Namba 27 la mwaka 2008. Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ilirithi mipaka ya lililokuwa Pori la Akiba la Mkomazi – Umba mipaka ambayo ilitambulika kisheria kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 275 la mwaka 1974.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi ni sehemu muhimu ya mfumo wa kiikolojia na toshelezi kwa idadi ya wanyamapori waliopo hifadhini kujipatia mahitaji yao ikiwemo malisho, maji na maeneo ya mazalia hivyo kufanya hatua za kupunguzwa kwa eneo kusababisha athari hasi ikiwemo baadhi ya wanyamapori kutoka nje ya hifadhi kwa ajili ya kujitafutia mahitaji yao muhimu na hatimaye kusababaisha kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na wanyama pori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 hairuhusu kufanyika kwa shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ikiwepo kilimo, ufugaji na uchimbaji madini. Hivyo, kutokana na sababu hizi za msingi za kiuhifadhi, kwa sasa Serikali haioni haja ya kusogeza mipaka ya hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, isipokuwa kwamba Serikali itaendelea kupokea kutoka kwa wananchi na wadau wengine maoni yatakayozingatia matakwa ya sheria na taaluma ya uhifadhi. (Makofi)
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. DKT. DAVID M. DAVID) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka waganga, watumishi wa afya pamoja na vitendea kazi katika zahanati za Same Magharibi zilizojengwa kwa ushirikiano wa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt.David Mathayo, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua tatizo la upungufu wa watumishi wa sekta ya afya katika Jimbo la Same Magharibi, ambapo mahitaji ni watumishi 867 lakini waliopo ni 287, upungufu ni watumishi 585.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imepeleka watumishi wapya 10 wa sekta ya afya katika jimbo hilo. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, Halmashauri ya Wilaya ya Same imeomba kibali cha kuajiri watumishi wapya 104 wa sekta ya afya ambao watapangwa katika vituo vyenye upungufu mkubwa wa watumishi.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-

Serikali iliahidi katika Bajeti ya mwaka 2012/2013 kujenga malambo, majosho na kisima kirefu kwa ajili ya Wananchi wafugaji wa Kata ya Ruvu Jimbo la Same Magharibi?

Je, ni lini ahadi hiyo itakamilishwa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mhe. Dkt. David Mathayo Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia bajeti yake pamoja na program mbalimbali imeendelea kukarabati na kujenga miundombinu ya maji ya mifugo katika maeneo mengi ya ufugaji hapa nchini ili kupunguza tatizo la maji hasa wakati wa kiangazi kikali. Katika Mwaka huu wa Fedha 2019/2020 Wizara imetenga fedha Jumla ya shilingi 700,000,000 kwa ajili ya kujenga visima kumi na kukarabati mabwawa kumi katika mikoa kumi Tanzania Bara. Katika utekelezaji wa mpango huo, kisima kimoja kinatarajiwa kuchimbwa katika Wilaya ya Same, hususan Kata ya Ruvu ili wafugaji waweze kupata maji kwa ajili ya mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha 2019/2020 Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kukarabati majosho 161 nchi nzima ili kudhibiti magonjwa yaenezwayo na kupe, mbung‟o na wadudu wengine. Mpaka sasa, majosho 46 yamekamilika, majosho 95 ukarabati unaendelea na majosho 20 ukarabati bado haujaanza. Aidha Wizara imejenga josho moja la kisasa Wilayani Bariadi. Pia Halmashauri mbalimbali zinakarabati majosho 288 na zinajenga majosho mapya 84. Kwa Halmashauri ya Same josho moja linakarabatiwa na Wizara katika Kata ya Ruvu-Muungano na matatu yanakaribatiwa na Halmashauri yaliyopo kwenye vijiji vya Mwembe, Bangalala na Mkonga. Mikakati ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya mifugo inaendelea kadri fedha zinapopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Napenda kuchukua fursa hii kutoa rai kwa halmashauri zote hapa nchini ikiwemo Halmashauri ya Same kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kujenga, kukarabati na kuendeleza miundombinu ya mifugo katika maeneo yao kwa kutumia fedha zinazopatikana kutokana na makusanyo ama tozo za mifugo.
MHE. ANNE K. MALECELA (K.n.y. MHE. DAVID M. DAVID) aliuliza:-

Je, ni lini Serikali kwa kushirikiana na Mashirika ya Simu itawapelekea huduma ya simu wananchi wa Kata za Msindo Mshewa, Mhezi, Vumari, Vudee, Tae, Suji, Gavao, Saweni na Ruvu Jiungeni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano Kwa wote imetoa ruzuku kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano katika Wilaya ya Same ambapo wakazi zaidi ya 13,531 wamefikiwa na huduma za mawasiliano katika Kata za Bombo, Maore, Mshewa, na Ruvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kufikisha huduma za mawasiliano nchi nzima. Kwa upande wa Same Magharibi, Serikali iliviainisha Vijiji vya Kata za Vumari, Suji na Ruvu Jiungeni ili kuangalia mahitaji halisi ya mawasiliano na hatimaye vimeingizwa katika orodha ya vijiji vya zabuni ya Awamu ya Nne. Zabuni hiyo ilitangazwa tarehe 18 Julai, 2019 ambapo mwisho wa kurudisha vitabu vya zabuni hiyo ni tarehe 3 Oktoba, 2019, ikifuatiwa na tathmini ya zabuni husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Mshewa imefikishiwa huduma za mawasiliano ambapo minara miwili (2) ya tigo imejengwa na kuihudumia kata hii. Pamoja na jitihada hizi na uwepo wa minara hii baadhi ya maeneo ya kata hii yanaonekana kuwa na changamoto za mawasiliano. Kata hii itafanyiwa tathmini zaidi ili kubaini maeneo mahususi ambayo bado yana changamoto ya mawasiliano ili yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasialiano kwa wote (UCSAF) imevipokea vijiji vya kata za Msindo, Mhezi, Vudee Tae, Gavao na Saweni na itavifanyia tathmini kuangalia mahitaji halisi ya mawasialiano na kasha kuviingiza katika orodha ya vijiji vya zabuni zitatazotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha hususani katika mwaka wa fedha 2019/2020.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID Aliuliza: -

Upatikanaji wa maji katika Mji mdogo wa Same ni asilimia 34; na mradi mkubwa wa maji Same – Mwanga – Korogwe umechelewa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa: -

(a) Je, ni kitu gani kilichochelewesha mradi huo na ni hatua gani zimechukuliwa kwa watu waliohusika na ucheleweshaji huo?

(b) Je, ni lini sasa mradi utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema yote ambayo amenijalia hata siku ya leo nami nimekuwa mmoja wa Wabunge katika Bunge hili Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyoonyesha juu yangu kwa sababu Bunge la Kumi na Mbili ni Bunge ambalo hakika Wabunge wote wako imara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuwashukuru sana wanawake wa Mkoa wa Mbeya kwa kunipa imani kubwa na kuona naweza kuja kuwawakilisha na kulisukuma gurudumu la maendeleo. Nakushukuru wewe binafsi Naibu Spika kwa sababu nawe ni mpiga kura wangu halali na mwaminifu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kushukuru familia yangu, hasa mume na baba yangu mzazi pamoja na watoto wangu waliofanikisha kuwa hivi nilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mhe. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Mradi Mkubwa wa Maji wa Same-Mwanga-Korogwe kwa gharama ya shilingi bilioni 262. Mradi huu unahusisha ujenzi wa miundombinu ya chanzo cha maji, ulazaji wa bomba kilomita 71, vituo vya kusukuma maji 3 na matanki 7 yenye ujazo kuanzia lita laki tatu hadi milioni tisa na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji kilomita 204. Katika utekelezaji mradi huu mkataba wa mwisho ulitarajiwa kukamilika Machi, 2021. Hata hivyo, kumekuwepo na kasi ya utekelezaji usiyoridhisha hadi Serikali imefikia hatua ya kusitisha mikataba na wakandarasi mwezi Desemba, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inafanya juhudi kuhakikisha taratibu za kupata wakandarasi wapya wa kumalizia kazi za mifumo ya umeme na ulazaji wa bomba kuu kilomita 34.

Aidha, kazi za ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji zinatekelezwa na wataalam wa ndani wa Wizara wakishirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kumtumia mkandarasi wetu Seprian Lwemeja.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatarajia mradi huu ukamilike Desemba 2021 na utanufaisha wananchi wapatao 438,820 kwa Mji wa Same-Mwanga pamoja na vijiji 38 vya Wilaya ya Same, Mwanga na Korogwe. Awamu ya kwanza itahudumia wananchi 168,820 katika miji ya Same na Mwanga. Awamu ya pili ambayo utekelezaji wake utaanza mwaka wa fedha 2021/2022 utanufaisha wananchi 270,000 katika vijiji vilivyo eneo la mradi ambapo Wilaya ya Same ni Hedaru, Mabilioni, Gavao, Makanya, Mgwasi, Bangalala, Chanjo, Mwembe, Njoro, Majengo, Bendera, Mkonga, Ijinyu na Mgandu; Wilaya ya Mwanga ni Kifaru, Kiruru Ibwejewa, Kisangara, Lembeni, Kivegere, Mbambua, Kileo, Kivulini, Kituri na Mgagao; na Wilaya ya Korogwe ni Bwiko, Mkomazi, Nanyogie, Manga-Mtindilio na Manga-Mikocheni.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID Aliuliza:-

Je, ni lini utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne ya kujenga Daraja la Mto Pangani mpakani mwa Wilaya za Same na Simanjiro utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Pangani umekatisha kwenye kipande cha barabara ya Same – Ruvu – Mferejini chenye urefu wa kilomita 34.2. Barabara hiyo inaunganisha Kata za Same na Ruvu katika Wilaya ya Same na sehemu ya mto inayopendekezwa kujengwa daraja ina upana wa mita 70. Sehemu hii haipitiki kwa sasa kutokana na kukosekana kwa daraja la kuunganisha Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya ya Simanjiro Mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais-TAMISEMI kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekuwa ikikihudumia kipande cha barabara hiyo kwa kufanya matengenezo kwenye maeneo korofi ambapo katika mwaka wa fedha 2018/2019 kiasi cha shilingi milioni 48 kilitumika. Aidha, katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 kiasi cha shilingi milioni 63 kimetengwa kwa ajili ya matengenezo ambapo kwa sasa mkandarasi anaendelea na matengenezo ya kipande cha kilomita 7.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umepanga kufanya usanifu wa daraja ikiwa ni pamoja na kipande cha barabara yenye urefu wa kilomita 34.2 kwa upande wa Same hadi kufikia eneo la Mto Pangani panapohitajika kujengwa daraja ili kuunganisha Wilaya za Same na Simanjiro. Serikali itatoa kipaumbele cha ujenzi wa daraja na miundombinu ya barabara hiyo muhimu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID Aliuliza:-

Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi huchangia Pato la Taifa kutokana na shughuli za utalii.

Je, Serikali haioni kuwa umefika wakati wa kuukarabati Uwanja wa Ndege wa Same Mjini ili ndege ndogo na za kati ziweze kutua kuleta watalii wa ndani na nje ya nchi katika Hifadhi ya Mkomazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ushauri wa Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kuhusu ukarabati wa Kiwanja cha Ndege cha Same, Serikali itaangalia uwezekano wa kukifanyia ukarabati kiwanja hicho kwa kadri ya upatikanaji wa fedha ili kuongeza Pato la Taifa kupitia sekta ya utalii. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH A. TADAYO K.n.y. MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-

Idadi ya watu wa Same imekuwa ikiongezeka tangu tupate Uhuru na mpaka wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi upo kilometa tatu kutoka Same Mjini. Wanyamapori na hasa tembo wameonekana Same Mjini mara nyingi.

Je, ni lini Serikali itafikiria kuweka upya mipaka mipya ya hifadhi ili kutoa maeneo kwa ajili ya makazi ya watu na shughuli nyingine za kijamii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Makao Makuu ya Hifadhi ya Taifa Mkomazi yapo eneo la Zange lililopo umbali wa kilometa sita kutoka Same Mjini. Wanyamapori hususan tembo wanaoonekana karibu na Mji wa Same mara nyingi ni wale wanaotoka katika maeneo ya Ruvu na Simanjiro kuelekea Hifadhi ya Taifa Mkomazi na wale wanaotoka katika Hifadhi ya Taifa Tsavo West nchini Kenya kupitia Ziwa Jipe na Kijiji cha Toloha katika Wilaya ya Same. Ikumbukwe pia kuwa maeneo mengi ambayo wananchi wanaishi kwa sasa yalikuwa yanatumiwa na wanyamapori kama mapito (shoroba) kuelekea maeneo ya Ruvu na Simanjiro.

Mheshimiwa Spika, kuendelea kumega eneo la hifadhi kwa kuweka mpaka mpya wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi siyo suluhu ya mgogoro huo kwa sababu eneo hilo litaendelea kuwa makazi na mapito ya wanyamapori. Hata hivyo, katika kudhibiti wanyamapori hao, Serikali itaendelea kuimarisha mikakati inayotumika ambayo ni pamoja na kuendelea kutoa mafunzo kwa wananchi ya mbinu za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu ambapo mafunzo hayo yanaendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Pia kuimarisha, kuendeleza tafiti na kutumia mbinu mbalimbali za udhibiti na ufuatiliaji wa tembo. Mbinu hizo ni pamoja na mikanda ya elektroniki (collaring) kwa ajili ya kufuatilia makundi ya tembo ambayo ni korofi na kufundisha na kuviwezesha vikundi vya wananchi kwa ajili ya kufuatilia maeneo walipo tembo.

Mheshimiwa Spika, pia matumizi ya ndege zisizokuwa na rubani, matumizi ya pilipili, matumizi ya mizinga ya nyuki na matumizi ya vilipuzi na vifaa vyenye mwanga mkali; lakini pia kutengeneza minara ya kuangalia mbali katika maeneo yanakabiliwa na changamoto ya tembo kuingia. La mwisho ni kuhamasisha wananchi kutoa taarifa mapema pindi wanyamapori ikiwemo tembo wanapoonekana kwenye maeneo ya makazi au mashamba.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa rai kwa wananchi wote wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa Mkomazi waendelee kusimamia mipango ya matumizi ya ardhi iliyowekwa pamoja na kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto za wanyamapori wakiwemo tembo pindi zinapojitokeza katika maeneo ya makazi ya watu na shughuli nyingine za kijamii.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -

Wananchi wa Wilaya ya Same bado wanaendelea kutaabika sana kwa kukosa huduma bora za afya kwenye Hospitali ya Wilaya licha ya ahadi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa ya ujenzi wa hospitali mpya ya Halmashauri ya Wilaya ya Same.

Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa ikizingatiwa kuwa eneo la ujenzi wa hospitali hiyo tayari limeshatengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya nchini zikiwemo Hospitali za Halmashauri. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni 55.7 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali 68 za Halmashauri zilizoanza kujengwa katika mwaka wa fedha 2018/2019. Pia Serikali imetenga shilingi bilioni 11.4 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Hospitali 27 za Halmashauri zilizoanza kujengwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 na shilingi bilioni 14 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali 28 za Halmashauri katika Halmashauri 28 ambazo hazikuwa na Hospitali za Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa Hospitali kongwe 43 za Halmashauri ambazo zina uchakavu wa miundombinu ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Same. Kupitia Programu ya Ujenzi na Ukarabati wa Vituo vya Kutolea Huduma za Afya nchini; Hospitali hizo zitaanza kujengwa upya kwa awamu kuanzia mwaka wa fedha 2022/ 2023. Ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -

Barabara ya Mlimani kutoka Mwembe – Mbaga hadi Mamba - Myamba ni kero kubwa kwa wakazi zaidi ya 150,000 katika Majimbo ya manne; Same Magharibi na Same Mashariki ambapo zaidi ya 70% ya wakazi wake wanaishi milimani.

Je, ni lini barabara hiyo yenye urefu wa Km 120 itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami nyepesi (Surface dressing) ili kufanikisha shughuli za maendeleo katika Wilaya ya Same?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mwembe – Myamba hadi Ndungu ni barabara ya changarawe yenye urefu wa kilometa 90.19. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Aidha, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022, Serikali imetenga shilingi milioni 1,848.97 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hiyo. Vilevile, ujenzi wa Daraja la Yongoma lililokatika wakati wa msimu wa mvua umekamilika kwa gharama ya shilingi milioni 453. Ahsante. (Makofi)
MHE. ESTHER E. MALLEKO K.n.y. MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -

Je, ni lini Benki Kuu itaweka utaratibu mzuri kwa Serikali na taasisi zake kuweka fedha katika Benki za biashara ili kuwa na mzunguko mzuri wa fedha?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa sasa wa Serikali na taasisi zake kutunza fedha za Benki Kuu ni mzuri na wa uwazi zaidi kwa kuwa unachochea ukuaji wa huduma jumuishi za kifedha. Aidha, mfumo wa sasa unaiwezesha Serikali kusimamia kwa ufanisi utulivu wa uchumi jumla, hususan sarafu yetu na mfumuko wa bei nchini ambao ni msingi wa ukuaji endelevu wa uchumi jumuishi. Vilevile, utaratibu wa sasa unatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, Sura ya 197. Ahsante sana.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -

Je, ni lini BOT itashusha riba inapokopa kupitia Hati Fungani kufikia asilimia 10 ili wananchi waweke fedha kwenye Benki za Biashara?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, viwango vya riba za hati fungani vilifanyiwa marekebisho mwezi Aprili 2022 ambapo hati fungani ya miaka 25 ilishuka kutoka asilimia 15.95 hadi 12.56; Miaka 20 kutoka asilimia 15.49 hadi 12.10; Miaka 15 kutoka asimilia 13.5 hadi 11.15; Miaka 10 kutoka asilimia 11.44 hadi 10.25; Miaka saba kutoka asilimia 10.08 hadi 9.48; Miaka mitano kutoka asilimia 9.18 hadi 8.6; na miaka miwili kutoka asilimia 7.82 hadi 7.6. Riba za hati fungani zilishushwa ili kuendana na riba za soko na pia wananchi waweze kuweka fedha zao kwenye benki za biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, wastani wa riba za hati fungani za Tanzania zipo chini ikilinganishwa na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afika Mashariki. Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa riba za hati fungani za Serikali na kuchukua hatua stahiki ili kutoathiri akiba za fedha katika benki za biashara, ahsante.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatoa vibali vya kuajiri Walimu wa kutosha kukabiliana na ongezeko la Wanafunzi na Wahitimu wangapi wapo kwenye soko la ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 Serikali imetoa kibali cha nafasi 10,003 za ajira kwa Walimu. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imepanga kutoa kibali cha ajira kwa nafasi 30,000 zikiwemo nafasi za Walimu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu wahitimu waliopo kwenye soko la ajira, ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, kuanzia mwaka 2016 hadi Desemba, 2020 jumla ya wahitimu ni 248,379. Idadi hii inajumuisha Walimu wa Astashahada, Stashahada na Shahada na kati ya wahitimu hawa wameajiriwa na Serikali na wengine Sekta Binafsi.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -

Je, ni kero zipi za Muungano zimetatuliwa na zipi zimebaki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa Serikali za pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimejadili na kuzipatia ufumbuzi jumla ya changamoto 22. Baadhi ya changamoto hizo ni: -

(i) Gharama za Kushusha Mizigo Bandari ya Dar es Salaam kwa Mizigo inayotoka Zanzibari;

(ii) Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia; na

(iii) Utaratibu wa Vikao vya Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Kushughulikia Masuala ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, changamoto zote zilizopatiwa ufumbuzi zimefafanuliwa kwa kina na zinapatikana katika tovuti ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja zilizobakia kutatuliwa ni nne ambazo ni: -

(i) Mapendekezo ya Tume ya pamoja ya Fedha;

(ii) Usajili wa Vyombo vya Moto;

(iii) Uingizaji wa Sukari katika Soko la Tanzania Bara; na

(iv) Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na Hisa za SMZ zitakazokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Mwembe – Mbaga hadi Mamba kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mwembe – Mbaga hadi Mamba ambayo inaitwa Mwembe – Myamba – Ndungu yenye urefu wa kilometa 90.19. Baada ya usanifu kukamilika Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kutatua tatizo la uhaba wa maji tambarare ya Same wakati ukisubiriwa Mradi wa Maji wa Mwanga – Same hadi Korogwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wakati utekelezaji wa mradi mkubwa wa Same – Mwanga – Korogwe unaendelea na unaotarajia kukamilika mwezi Juni, 2024 na kunufaisha baadhi ya maeneo ya Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto ya maji kwa wananchi wa Wilaya ya Same. Mathalani katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imekamilisha miradi ya maji katika Vijiji vya Kirinjiko, Mabilioni Kijomo na Gunge na tayari inatoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi. Aidha, visima vitatu vimechimbwa katika eneo la Mahuu kwa ajili ya kuhudumia eneo la Same Mjini ambapo kwa jumla vina uwezo wa kuzalisha jumla ya lita 720,000 kwa siku.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka huu wa fedha 2023/2024, Serikali itafanya utafiti wa maji chini ya ardhi pamoja na kuchimba visima virefu viwili katika maeneo ya Same Mjini na Kijiji cha Marondwe, Njoro ili kuongeza vyanzo zaidi vya maji. Utekelezaji wa visima hivyo unatarajiwa kuanza mwezi Januari, 2024 mara baada ya uchimbaji kukamilika na maji kupatikana.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-

Je, ahadi ya Serikali ya kusambaza umeme wa REA III katika vijiji 48 vya Jimbo la Same Magharibi na vitongoji vyake imefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Same, Vijiji 91 kati ya 100 tayari vimepelekewa umeme na vijiji tisa vilivyobaki vitapelekewa umeme ifikapo mwezi Desemba, 2023.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kuanza ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme katika vitongoji 2,034 nchini kwa gharama ya shilingi bilioni 377.05 ambapo vitongoji 15 katika Jimbo la Same Magharibi vitapelekewa umeme. Serikali itaendelea kupeleka umeme kwenye vitongoji 162 vilivyobaki kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha, nakushukuru.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-

Je, nini mpango wa kuajiri waganga, watumishi wa afya na kupeleka vifaatiba kwenye zahanati na vituo vya afya nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoa vibali vya ajira kwa watumishi wa kada ya afya ili kupunguza uhaba wa watumishi uliopo. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Ofisi ya Rais, TAMISEMI, iliajiri watumishi 7,732. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 tayari Serikali imeajiri watumishi 5,319 wa kada za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi bilioni 69.95 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba. Kati ya hizo, shilingi bilioni 7.1 ni kwa ajili ya hospitali 71 za Halmashauri, shilingi bilioni 47.7 ni kwa ajili ya vituo vya afya 159 na shilingi bilioni 15 ni kwa ajili ya zahanati 300. Hadi kufikia mwezi Aprili 2023 jumla ya shilingi bilioni 58.85 zilikuwa tayari zimetolewa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya vifaatiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 116.92 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA K.n.y. MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-

Je kwa nini Serikali haitengi fedha za TARURA kwa kuzingatia jiografia, ukubwa wa eneo na mazingira ya Wilaya au Jimbo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA ZA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, TARURA inaendelea na zoezi la uandaaji wa formula itakayotumika kwenye ugawaji wa rasilimali fedha zinazohitajika kwenye ujenzi na matengenezo na miundombinu ya barabara kulingana na mahitaji ya eneo husika. Formula itazingatia ukubwa wa mtandao wa barabara (road network), thamani ya miundombinu ya barabara iliyopo (asset value), hali ya barabara (road condition), wingi wa magari (traffic volume), idadi ya wakazi (population), mazingira (geographical terrain), kiwango cha mvua (annual rainfall) na kilimo (agriculture potential).