Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joseph Roman Selasini (31 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi, ingawa ndiyo nimeingia, lakini niseme kidogo, nisije nikakosa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Rais na kabla sijasema chochote kuhusu maudhui ya hotuba hii, nimefurahishwa na jambo moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mmoja kati ya Wabunge wa upande huu tulioanzisha mageuzi miaka 20 plus iliyopita na tulipoanza kuna Mzee mmoja anaitwa Ndimara Tegambwage, aliandika kitabu kinachosema kwamba Upinzani Siyo Uadui.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema hilo kwa sababu, baada ya kupitia hotuba ya Mheshimiwa Rais, nimegundua kwamba mambo mengi ambayo tumeyasema kwa muda mrefu Mheshimiwa Rais ameyazingatia katika hotuba yake na jambo hili linanifurahisha sana, linaonesha kwamba alah, kumbe sisi sote ni Watanzania na kwamba mawazo tunayoyatoa huku, siyo mawazo mabaya, ni mawazo ya kuisaidia nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukuke nafasi hii kuwaomba viongozi wengine, Mheshimiwa Nape yupo pale, Mheshimiwa Jenista na wengine, muige mfano wa Rais, siyo kwamba kila kinachosemwa upande huu ni kitu kibaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, mimi nitachangia mambo matatu; la kwanza ni viwanda. Wazo la kufanya nchi yetu kuwa nchi ya viwanda ni wazo ambalo limechelewa sana. Mwalimu Nyerere alijitahidi, enzi za Mwalimu Nyerere tulikuwa na viwanda karibu katika kila zao, katika kila sekta, lakini bahati mbaya ndiyo hivyo viwanda vikachukuliwa, wengine wakavifisadi, wengine wakaviua na kadhalika. Sasa wazo hili, nadhani ndiyo wazo pekee ambalo litaisaidia nchi hii, kwa sababu ukiangalia sasa hivi ni bidhaa chache sana ambazo tunauza nje na kwa sababu hiyo, hata upatikanaji wa fedha za kigeni, unakuwa wa shida, ndiyo maana hali yetu ya uchumi inayumba mara kwa mara, dola inayumba mara kwa mara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri ambao ningependa kutoa, maana yake Mheshimiwa Rais amesema kwamba, atajitahidi kufanya nchi yetu iwe nchi ya viwanda, lakini ningefurahi zaidi kama mwelekeo ungeanza kuonekana, kwamba ni viwanda vipi tunaanza navyo ili watu waandaliwe. Tusije tukaanzisha viwanda halafu matokeo yake tukauwa kilimo. Kama tunaanza viwanda ambavyo vitawasaidia watu wetu kujiandaa ili malighafi za hivi viwanda zitoke hapa hapa, litakuwa jambo bora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu ukiangalia sasa hivi watu wanatoka vijijini, vijana wanatoka vijijini wanakuja mijini kuja kubangaiza na wanafanya hivyo kwa sababu kilimo sasa kinaanza kudharauliwa. Kijana anaona akifika mjini akishika soksi mbili,
tatu akizitembeza, anarudi kijijini anaonekana ni wa maana zaidi kuliko wale aliowaacha vijijini.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tuangalie vile viwanda ambavyo vitawafanya wakulima waweze kupata hamasa ya kuweza kuandaa malighafi kwa ajili ya viwanda vyenyewe ndiyo tuanze navyo. Nami nasema kwamba, Mheshimiwa Rais, pamoja na Serikali yake, kama mtajitahidi kuanza kufufua Viwanda vya Nguo, Viwanda vya Pamba, kwa sababu tunajua hapo nyuma jinsi Urafiki ilivyovuma, jinsi Mwatex ilivyovuma na viwanda vingine na mkifanya hivyo ni kwamba mnawahamasisha wakulima wa pamba kulima zaidi na vilevile kuweza kuona manufaa ya kilimo kwa sababu pamba yao itapata soko hapa hapa, pamoja na viwanda vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kwa sababu najua muda ni mchache, nisemee kuhusu maji. Utagundua na sidhani kama kuna Mbunge atasimama hapa bila kusemea suala la maji. Ningeomba sana suala la maji liwekewe kipaumbele kikubwa sana kwa sababu ndilo
suala ambalo linawatesa watu wetu ukiacha na mambo mengine. Pale Jimboni kwangu shida ya maji ni kubwa kuliko ambavyo mtu unaweza ukaelezea na hasa inapokuja wakati wa kilimo.
Ilisemwa hapa Bungeni kwamba sasa hivi mvua zinanyesha, lakini kwa experience ya pale Rombo maji yote yanakwenda nchini Kenya. Kule wameweka utaratibu wa kuyazuia. Matokeo yake kiangazi kikija, wale wa Kenya ndiyo wanatuuzia mboga na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishasimama hapa Bungeni mara nyingi nikiomba kwamba, jamani wale wanaohusika na Wizara ya Maji, sisi tuna makorongo mengi sana pale Rombo, tusaidieni tuweze kuzuia yale makorongo ambayo yanapitisha maji mengi sana wakati wa masika ili baadaye wakati wa kiangazi yatusaidie. Yatatengeneza hata ajira kwa vijana wetu, vijana watalima mbogamboga, vijana watalima kilimo cha msimu wa kiangazi na kwa sababu hiyo tutapunguza umaskini wa hali ya juu sana miongoni mwa vijana wetu na tutatengeneza ajira miongoni mwa vijana wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Ziwa pale linaitwa Ziwa Chala, lile Ziwa niliomba hapa nikaambiwa yale ni maji ya Kimataifa, ni maji ya Kenya na Tanzania, kwa hiyo, utaratibu utafanyika ili tuweze kupata maji yale yatumike pia na kwa watu wangu pale Rombo. Sasa cha kushangaza watu wa Kenya wanatumia maji ya lile Ziwa, lakini sisi tunahangaika na uhaba wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana katika hii mipango mizuri ambayo Rais ameeleza kwenye kitabu chake itufikishe maeneo kama hayo, mahali ambapo tunayo maji, maji ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia na maji ya Ziwa Chala ni maji ya Mlima Kilimanjaro.
Theluji ile pale Kilimanjaro inapoyeyuka imetengeneza underground rivers ambazo zinakwenda mpaka pale Chala. Sasa wenzetu wa Kenya wanayatumia sisi tunabaki tunayaangalia. Kwa hiyo, wakati tunapoendelea kutengeneza sera zetu, mipango yetu kufuatana na hotuba hii ya
Mheshimiwa Rais, naomba sana maeneo kama hayo yaangaliwe. Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize tu kwa kurudia ule wito wangu kwamba, jamani wote tunajenga nchi, nchi yetu hii ya Tanzania, kwa hiyo, mawazo ambayo yanatoka pande zote tuyapokee na tuyafanyie kazi, badala ya kupigana vijembe.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi uliyonipa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, kama ulivyosema asubuhi, muda mrefu sikuwa hapa Bungeni kwa sababu nilikuwa na kesi ya uchaguzi. Namshukuru Mwenyezi Mungu amenirejesha Bungeni salama na nawashukuru wananchi wangu wa Rombo kwa kuniunga mkono wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sikuwepo, iko michango mingi sana ambayo ilitolewa hapa Bungeni tangu wakati wa kuchangia mpango na kadhalika, basi kama nitarudia kwenye eneo ambalo wenzangu waliligusa naomba ionekane tu kwamba nami nataka niweke rekodi katika mambo yaliyotokea katika Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ambalo ningependa nilizungumze ni ujumbe ambao nimetumwa na wapiga kura wangu na baadhi ya viongozi hasa viongozi wa dini tuliokutana kwenye mazishi, akaniomba nikifika Bungeni niuseme, nao ni kuhusu matangazo haya kutokwenda hewani kama ilivyokuwa zamani. Wamenituma niseme ifuatavyo: kwamba Bunge kuna kujichanganya kwa hali ya juu ambapo watu wanahoji, Bunge hili lina wasomi au sote tumegeuka kuwa vilaza? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanasema hivi, mwanzoni ilisemekana Bunge ndilo linalohusika na kuzuia matangazo, lakini kadri siku zilivyokuwa zinakwenda, Serikali imejitokeza kuwa msemaji wa Bunge. Sasa wanashangaa, ni Bunge au ni Serikali? Katika Serikali kuwa msemaji wa jambo ambalo wanasema linahusu Bunge, Waziri wa Habari anasema kwamba hili linatokana na gharama, lakini Waziri Mkuu anasema ni ili wananchi wafanye kazi.
Mheshimiwa Spika, sasa wananchi wanajiuliza, hivi hii Serikali ni moja? Mambo yanaamuliwa kwenye Baraza la Mawaziri au mnaamulia kwenye chai? Kwa hiyo, wananchi wanataka kujua, jambo hili hatma yake ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nami nataka niwaambie kuna faida kubwa ya kukaa nje ya Bunge, Mbunge wakati Bunge linaendelea.
Mheshimiwa Spika, nataka niishauri Serikali, msifikiri jambo hili linawaletea umaarufu, linawachanganya kweli kweli kwa sababu wananchi walichoshikilia ni kwamba mnazuia wananchi wasione kile ambacho wanapaswa kuona kwa sababu mnaogopa kukosolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nami ninachokiona ni kwamba yako mambo Bungeni hapa yanafanyika mazuri na Wapinzani, yanafanyika mazuri na upande mwingine, ni kwa sababu gani mnakataa wananchi wasipate haki yao ya kuona nini kinachoendelea? Kama sasa hivi katika bajeti hii, wananchi wanauliza, wao wanalipa kodi; Bunge hili la bajeti ndilo linalogawa mafungu ya zile kodi zao, kwa nini mnawakimbiza kulipa kodi lakini wasiwe na haki ya kuangalia ile kodi yao inavyogawanywa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni muhimu tuseme ili ibaki kwenye rekodi, kwa sababu tumekuwa tukiwashauri, lakini hamtaki kupokea ushauri, nitoe mfano wa ushauri ambao tumekuwa tukiwapa. Tarehe 27 Mei, 2015 katika Bunge hili Mheshimiwa Esther Matiko alishika shilingi katika Wizara hii kuhusu boti ya Dar es Salaam Bagamoyo.
Mheshimiwa Spika, alichosema Mheshimiwa Esther wakati ule ndicho CAG ambacho sasa hivi ame-confirm kwamba boti ile ilikuwa chini ya kiwango, kwamba gharama za kununua boti ile zilikuwa kubwa. Sasa sisi hatushauri kwa maslahi yetu, tunashauri kwa maslahi ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, umezuka mtindo katika Bunge hili Wizara ya Uchukuzi ikiguswa kwa sababu, Rais alikuwa Waziri hapa, kuna hisia za kuzuwiazuwia Wizara hii watu wasiseme maneno! Hatusemi kwamba, Rais akiwa Waziri alifanya ufisadi, inawezekana ni Katibu Mkuu, inawezekana ni watu wake! Na sisi tunamwambia kwa sababu, ya umahiri wake wa kutumbua atumbue hawa ambao walihusika katika kuharibu fedha za wananchi. Hili ni jambo ambalo kila mtu mwenye akili na anayeipenda nchi ataniunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukitoka huko nenda kwenye barabara zetu. Mheshimiwa SavelinMwijage amezungumza hivi hakuna mtu anayeiona barabara ya Chalinze – Vigwaza mpaka Mlandizi? Hii barabara Mawaziri wanapita, Rais anapita na kila mtu anapita! Hivi haiingii kwenye fikra kwamba, hapa ni ufisadi umefanyika? Hapa ni wizi umefanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa haya yanazuiwa na yanapozuiwa mnafikiri kwamba, ni kusaidia Serikali, hapana! Serikali inaumizwa kwa kiasi kikubwa sana. Ujenzi wetu wa barabara lazima uangaliwe, kuna ufisadi na wizi mwingi sana unatokea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna barabara ya kutoka Mwika – Mkuu kwenda mpaka Tarakea, Jimboni kwangu; ile barabara haina miaka mitatu, leo kuna mashimo! Sasa hivi tumeanza viraka, ni nini kimetokea? Feeder roads hazijatengenezwa! Kuna eneo moja linaitwa Mengwe, Keni na Mkuu; zile feeder roads tuta la barabara liko juu mtu anapanda na pikipiki kule haoni gari linapita kule! Matokeo yake watu wanauawa kila siku!
Mheshimiwa Spika, nilisema mwaka jana na mwaka huu nasema tena! Isifikiriwe kwamba, Serikali itapendwa kwa kuambiwa halafu haitekelezi! Ninyi mmeficha wananchi wasitusikie, sisi haya tunakwenda kuwaambia! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, barabara ile ilijengwa na Wakandarasi wawili. Mkandarasi wa kwanza alipeleka vifaa akaviweka kwenye eneo la kiwanja cha michezo cha watoto wa shule pale Mengwe, mpaka leo hii miaka 10, matingatinga yako pale! Magari yanaozea pale! Watoto hawana mahali pa kuchezea! Tumeshahangaika kila mahali yale yaondolewe, hayaondolewi! Sasa mimi sijui Serikali ya Hapa Kazi Tu ningefikiria kwamba, haya mambo ambayo yamelalamikiwa miaka iliyopita ndio ingeyachukua sasa iyafanyie kazi.
Mheshimiwa Spika, kuna eneo katika barabara hiyo, wamejenga mto unapita juu ya barabara, Kikelelwa kule! Sasa hivi hapa jinsi mvua zilivyonyesha, maji yote yanaenda kwenye majumba ya watu. Watu wanateseka! Tumesema na tunaendelea kusema. Sasa huwezi hata siku moja ukawaridhisha wananchi wakati kero zao hazishughulikiwi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua muda unaniishia, lakini niseme sisi tumepata mafuriko mwaka huu kule Rombo. Kati ya mtandao wa barabara za Halmashauri, kilometa 285, kilometa 167.7 zimebomoka zote. Fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Halmashauri katika bajeti ya 2015/2016 mpaka robo tatu ya mwaka wa fedha tulikuwa hatujapata hata shilingi moja! Naiomba Serikali ituletee hizo fedha kwa sababu, sasa hivi wananchi katika vijiji vyote, katika Kata zote hakuna jinsi, barabara zimevunjika na kwa hiyo, wanategemea sana wapate fedha hizi ili waweze kurekebisha barabara maisha ya wananchi yaende kama ambavyo wanataka yawe.
Mheshimiwa Spika, la mwisho, yapo maeneo korofi maana maendeleo yakija yanakuja na tabu zake; yapo maeneo korofi ambayo tulishaomba yawekewe matuta. Kwa mfano, kuna eneo moja linaitwa Mamsera, juzi nimerekodi mtu wa 22 kuuawa kwa sababu ya speed kubwa.
Mheshimiwa Spika, nimekwenda TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro mara chungu nzima, Baraza la Madiwani, Halmashauri iliyopita na hii ya sasa hivi wamekwenda wameomba jamani pale pawekwe matuta watu wanakufa! Hivi ndiyo niseme kwamba, Serikali inapenda kusikia watu wake wanauawa?
Mheshimiwa Spika, juzi uso kwa macho, nimeona mweyewe mtu wa 22 ameuawa! Eneo la Tarakea, eneo la Kikelelwa, eneo la Keni, ni maeneo ambayo ni korofi! Mimi ni mmoja kati ya watu ambao tunapinga matuta, lakini wakati mwingine lazima tuyaombe kwa sababu ya wakorofi wachache. Naomba sana Waziri awaagize watu wa TANROADS Mkoa wa Kilimanjaro waweke matuta eneo la Mamsera, eneo la Keni, eneo la Holili na eneo la Tarakea.
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, moja kati ya vitu vinavyochangia hizi barabara kuharibika, niliwaambia yapo magari yanabeba pozzolana kutoka Holili na mengine yanabeba mizigo mizito yanapita kwenye ile barabara inakwenda Kenya, wekeni mizani hata ya kamba! Ni leo, ni kesho, ni leo, ni kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ya Awamu ya Nne imekwenda imekuja sasa Serikali ya Hapa Kazi Tu, wekeni basi hiyo mizani! Huu nao ni ushauri tunawasaidia kwa sababu, ile barabara inavunjika. Barabara zinatengenezwa kwa pesa nyingi, lakini wakorofi wachache wanasababisha zivunjike. Sasa tuseme namna gani, ili mtuelewe? Maana tukisema kwa kutetea rasilimali hamuelewi! Tukisema kwa kelele mnasema sisi tunapayuka, tunapiga kelele.
Mheshimiwa Spika, naomba sana kwamba, haya niliyoyasema Wizara iyafanyie kazi. Nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu wa Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ya mwanzo kuchangia hoja hii. Kwanza niseme kwamba, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya LAAC na kwa sababu hiyo mengi nitakayozungumza yatahusu maoni na mapendekezo ya Kamati yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusema tu kwamba, matatizo mengi ambayo tumeyaona katika ukaguzi yanafanana kwa halmashauri zote. Nipende kuzungumza zaidi maeneo yanayohusu fedha za Serikali ambazo zinapelekwa katika Halmashauri zetu. Karibu halmashauri zote nchini, zinakabiliwa na tatizo la kutopata fedha za maendeleo kutoka Hazina kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo hili ni kubwa kiasi kwamba, karibu katika halmashauri zote, kuna miradi ya maendeleo au haijakamilika au iko nusunusu na kwa kweli karibu halmashauri zote zina madeni yanayotokana na wakandarasi kutolipwa fedha zao kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kucheleweshwa kwa fedha hizi kwenda kwenye halmashauri, hakuna sababu yoyote ambayo katika ukaguzi tumeambiwa, ambayo Hazina wanazieleza halmashauri na ndiyo maana tungependa kusikia kama Bunge, Waziri wa Fedha atuambie tatizo linaloikumba Hazina kutopeleka fedha kwa wakati kwenye halmashauri ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya Halmashauri kuna matatizo makubwa sana ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo. Tatizo la maji ambalo Wabunge wote tunalizungumza, kiini chake ni kwamba, baadhi ya miradi inayosimamiwa na Halmashauri haitekelezeki kwa sababu ya madeni. Siyo hilo tu, tatizo ambalo tunalipata la ukarabati wa miundombinu ya elimu, ukarabati wa barabara na kadhalika linatokana na shida hii hii ya Hazina kutopeleka fedha kwa wakati. Kwa hiyo ili kuzisaidia halmashauri zetu, ni lazima utaratibu uangaliwe wa kusaidia hizi halmashauri ziweze kutekeleza bajeti zake kwa Hazina kupeleka fedha kwa wakati katika halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine ambalo ni kubwa na linakabili halmashauri zote ni Maafisa Masuuli kuhamisha fedha za miradi ya halmashauri bila kufuata taratibu za fedha. Tatizo hili ni kubwa zaidi, kw sababu maagizo ya Viongozi Wakuu na Viongozi wa Mikoa na Wilaya yanakwenda kwa Wakurugenzi wakati kukiwa hakuna fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili naomba nilieleze, halmashauri nyingi zimekuja mbele yetu, zimekumbana na tatizo hili, lakini ukiwauliza watakwambia tulikuwa tunatekeleza agizo la Rais kutengeneza madawati. Tumehamisha, tulikuwa tunatekeleza agizo la Rais, kujenga maabara. Maagizo haya yamesababisha uchochoro mkubwa sana wa wizi wa fedha za umma. Kwa sababu sasa fedha zinahamishwa bila utaratibu, bila kibali, bila maombi maalum, lakini ikuliza unaambiwa tulikuwa tunatekeleza maagizo ya kiongozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maagizo ya Mheshimiwa Rais, inavyoelekea na Marais wengine huko Mikoani, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na wenyewe wameingia katika utaratibu huu huu wa kutoa maagizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo linalokumbwa zaidi na uchotaji wa fedha hizi ni asilimia 10, fedha zinazopaswa zitengwe kutokana na own source ya Halmashauri kwa vijana na akinamama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, agizo hili la kutenga asilimia 10 kwa ajili ya akinamama na vijana ni agizo zuri na lengo lake lilikuwa ni kuwasaidia akinamama na vijana kuweza kujiajiri. Vijana wengi wanaotoka vijijini kuja mijini wanakuja kwa sababu katika vijiji hawana kitu cha kufanya, wanajua kwamba, kule mijni ndiyo kuna kila kitu. Sasa kila Afisa Masuuli anayeulizwa ni kwamba, fedha za Mfuko huu wa Vijana na Akinamama zimekwenda kujenga maabara, zimekwenda kutengeneza madawati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kushangaza ziko Halmashauri ambazo zimetekeleza agizo hili bila kutumia fedha hizi. Kuna Halmashauri ambazo Wakurugenzi wake wamewahamasisha wananchi wamechanga kuku, mazao, wametekeleza agizo hili. Zile halmashauri ambazo Wakuu wake wamekaa hawatafakari, hawafanyi utaratibu wa ubunifu wa namna ya kutekeleza agizo hili ndiyo kwa kiasi kikubwa akinamama na vijana wa maeneo hayo, fedha zao zimechukuliwa kwa ajili ya kutekeleza haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kuna halmashauri nyingi ni maskini kwa maana zile fedha zenyewe haziwatoshi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yao ya maendeleo na kwa sababu fedha kutoka Hazina haziji wanaingia kwenye ushawishi wa kutumia hizi fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tukasema lazima tuangalie utaratibu mwingine wa namna ambavyo fedha hizi vitawafikia akinamama na vijana kwa sababu lengo la kuwafikia akinamama na vijana bado lipo na litaendelea kuwepo na tunasema lazima miradi hii iboreshwe ili vijana wapate namna ambavyo wanaweza kujiajiri. Kwa sababu tunavyoona ni kwamba, uwezo wa Serikali hata na wa sekta binafsi kuwaajiri vijana wote na akinamama wote ni mgumu. Kwa hiyo, kama Serikali itaimarisha huu Mfuko kwa ajili ya kuwawezesha hawa vijana ni jambo jema, tena ni jema kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo fedha zinatumika vibaya ni ile asilimia 20, ambayo inatokana na kufutwa kwa vile vyanzo vya mapato ambavyo halmashauri zote zilikuwa zinatumia. Fedha hizi zinatoka Hazina moja kwa moja zinakwenda halmashauri ili halmashauri izitumie kwa ajili ya kupeleka kwenye kata na kwenye vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri nyingi fedha hizi haziendi vijijini na wote tunafahamu jinsi ambavyo Viongozi wetu wa Vijiji, Viongozi wetu wa Kata wanavyofanya kazi katika mazingira magumu. Sasa hata hizi fedha ambazo Serikali kwa makusudi mazima iliamua ili kuwasaidia hawa ili kuweza kufanya kazi vizuri hazifiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hii asilimia 20 hakuna utetezi, vitabu vyote tulivyokagua, Hazina wanapeleka hizi fedha, lakini hizi fedha zikifika kwa Wakurugenzi wanazitumia jinsi ambavyo wao wanaona inafaa. Ndiyo maana kama umesikia hotuba yetu tumependekeza kwamba, Serikali itafute njia nyingine ya kupeleka hizi fedha zisipitie kwa Wakurugenzi ikiwezekana ziende moja kwa moja kwenye kata au ziende moja kwa moja kwenye vijiji, kama vile fedha kwa ajili ya elimu zinavyokwenda kwenye shule zinazohusika moja kwa moja.Vinginevyo, hili tatizo litaendelea kusumbua na wananchi hawatapata faida na hizi fedha hata kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la mwisho, ambalo ningependa kulizungumza, ni kuhusu Sheria ya Manunuzi. Hili tumelipigia kelele katika Bunge lililopita na hata katika Bunge hili tumeendelea kulizungumza, ni vizuri Sheria ya Manunuzi ikaletwa kufanyiwa mapitio. Kwa sababu mpaka dakika hii kuna vifaa ambavyo vinaweza vikanunuliwa kwa bei ya soko lakini kwa sababu tu kwamba mkandarasi ametafutwa, bei ya vile vifaa inabadilika inakuwa mara mbili au mara tatu ya bei ya vifaa ambavyo viko sokoni, kwa hiyo, eneo hili linaziumiza halmashauri. Fedha ambazo zingeweza zikafanya kazi kiwango cha kuridhisha zinapunguzwa kutokana na matumizi mabaya ya Sheria ya Manunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni ushauri wa Kamati kwamba, kwa sababu eneo hili litaendelea kusumbua, ni vizuri Sheria ya Manunuzi ikaangaliwa ili vile vifaa ambavyo vinaweza vikanunuliwa kwa bei ya soko, sheria ielekeze ili kupunguza mianya ya wizi inayotokana na matumizi mabaya ya hii sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ni pendekezo; tumeongea na Wakurugenzi wetu na tulichogundua ni kwamba Wakurugenzi wengi sasa hivi ambao tunaongea nao, hawa wapya, maana huu ukaguzi ni ukaguzi uliotokana na hesabu za 2012/2013 – 2013/2014, sasa tutakwenda kwenye ukaguzi wa mwaka 2014/2015 na 2015/2016, ni vyema TAMISEMI ikaangalia uwezekano wa kukaa na hawa Wakurugenzi kuwapa kama semina hivi. Hili tumelisema sana, naomba lisibezwe, Wakurugenzi wengi tuliokaa nao uwezo wao ni mdogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashauri kwa nia nzuri, uteuzi umeshafanyika, sisi hatuna mamlaka ya kuwaondoa lakini tunawashauri, hawahawa mliowateua kama mnaona wanafaa vizuri, lakini tafuteni namna ya kuwapa semina, namna ya kuwaongoza ili waweze kujua namna ya kutenda kazi, kwa sababu Wakurugenzi wengine hata taratibu za namna ya kuendesha Serikali hawajui, kwa hiyo ni kwa nia nzuri tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vinginevyo, ukaguzi unaokuja tunakwenda kuona hoja nyingi zaidi za ukaguzi kwa sababu ndogo tu kwamba, Wakurugenzi hawana uwezo wa kusimamia halmashauri a, wengine wako rigid hawataki kusikiliza ushauri kutoka kwa wakuu wa idara waliowakuta pale, wengine wanafikiri wanajua zaidi kuliko wale waliowakuta, wengine walikuwa wanaendesha NGOs zao huko sasa wamekuja kwenye utumishi wa Serikali wanafikiri uendeshaji wa halmashauri ni sawasawa na uendeshaji wa NGOs zao kumbe ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, sisi tunawashauri kwa nia njema kabisa ni vizuri TAMISEMI wafanye semina ya hawa Wakurugenzi waweze kuongezewa uwezo wa kufanya kazi zao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na naunga mkono hoja zilizotolewa na Kamati zetu za Fedha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie katika hoja hii iliyo mezani kwetu. Hata hivyo, kabla sijachangia, nataka nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na daima nitaendelea kumshukuru kwa uponyaji ambao amefanya kwa Mheshimiwa Tundu Lissu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu wale waliobahatika kumwona Mheshimiwa Tundu Lissu siku ambayo watu wasiojulikana walikuwa wamedhamiria kudhulumu maisha yake, wataamini kabisa kwamba uponyaji wake ni mpango wa Mungu. Ndiyo maana kwa kweli binafsi nikisikia tukio la kuumizwa Tundu Lissu likiongelewa kwa dhihaka, kejeli, dharau kwa kweli linanikasirisha kupindukia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi baada ya Waziri Mkuu kujibu vizuri swali la Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Mlinga alikuja na mwongozo na uliojaa kejeli. Mwongozo ule ulimhusisha Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na mauaji ya albino, jambo hili halikubaliki. Ombi au pendekezo la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kwa Serikali kuhusisha Wachunguzi wa Kimataifa ni pamoja na baadhi ya matendo ambayo yamekuwa yakitokea katika nchi hii na kufumbiwa macho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wanakumbuka na sisi tunakumbuka kwamba, Mheshimiwa Goodluck Mlinga alihusishwa na kumuua mpenzi wa mpenzi wake.

T A A R I F A . . .

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia na huo ni mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu. Gazeti la Dira liliandika vizuri sana kwamba mpenzi wako alikusaliti, wewe na kundi la vijana wenzako mkaenda kumuua, limeripotiwa Polisi, limeripotiwa kwenye magazeti na hujakanusha hadi hivi leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeiomba Serikali katika uchunguzi wa nani walihusika kutaka kudhulumu maisha ya Mheshimiwa Tundu Lissu, huyu ambaye alikwishatajwa kwamba alihusishwa na mauaji uchunguzi uanzie kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwenda kwenye hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo napenda kulizungumza ni kushauri Kiti chako. Jana kuna mwenzetu mmoja katika mchango wake alihusisha Bunge hili na ubaguzi. Namshukuru sana senator Ndassa kwa jinsi alivyojenga hoja yake asubuhi na kututahadharisha kwamba tusije tukaigawa nchi kwa sababu ya hisia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hili kwa sababu nakuomba kama ikikupendeza Hansard ya jana ya hotuba ya Mheshimiwa Musukuma iangaliwe kwa sababu…

TAARIFA . . .

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi sijapewa taarifa na kwa sababu hiyo naomba niendelee kukushauri. Nashauri ile hotuba yake iangaliwe kwa sababu ndani ya ile hotuba kuna maneno haya ambayo ni maneno mabaya kama yataachwa kwenye ile hotuba kwamba, wakati mnakula vizuri sisi tulikuwa kimya sasa zamu yetu mnapiga kelele. Naomba kama haya maneno yako kwenye Hansard yaondolewe kwa faida ya vizazi vijavyo. Haya maneno siyo mzuri, haya maneno ni mabaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa niingie kwenye Mpango. Mimi simlaumu Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa hoja yake aliyoileta Mezani kwa sababu wajibu wetu ni kumshauri ili baadaye atuletee Mpango. Namshukuru pia Spika kwa jinsi alivyotuweka sawa asubuhi. Mheshimiwa Mpango yuko hapa kutusikiliza ili tumsaidie aweze kuchukua hoja zetu, baadaye azifanyie kazi ili tuweze kuwa sasa na Mpango wenyewe. Mimi ninachoelewa kilicho mbele yetu ni Mapendekezo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuzungumza kuhusu gesi ambayo nchi hii inayo. Kamati ya Bajeti ilipata bahati ya kwenda Mnazi Bay na Msimbati. Gesi tuliyonayo ni nyingi kwelikweli, ni nyingi sana lakini hatuna uwezo wa kutumia robo tatu ya gesi tunayozalisha. Kinachotokea ni ukiritimba wa TPDC kwa sababu M&P ambao wanazalisha hii gesi wanaiuza kwa TPDC na wanaiuza kwa TANESCO Mtwara na ukiritimba huo unafanya sasa ile gesi isilete faida yoyote katika nchi.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba kama mikataba ambayo Serikali iliingia na M&P ikirejewa vizuri ile gesi inaweza ikauzwa kwa makampuni mengine, inaweza ikauzwa kwa watu binafsi. Kwa kufanya hivyo uko uwezekano hata wa kupunguza mafuta ya mitambo ambayo tunaagiza kutoka nje, mafuta ya magari tunayoagiza kutoka nje na kuokoa pesa nyingi sana za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mataifa mengi sasa hivi yenye gesi magari yake yanatumia gesi. Gesi inatumika majumbani, hakuna sababu yoyote ya kutojengwa kwa vituo vya kuuzia gesi kama vile vituo vya petrol na diesel na kufanya magari yetu yakatumia gesi. Ni kitu kidogo sana tu kwa sababu katika gari utahitaji kuwa na mtungi tu kwa ajili ya gesi na kwa sababu hiyo tutaokoa pesa nyingi sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali ifanye kila linalowezekana ili gesi ambayo inazalishwa kwa wingi itumike katika uendeshaji wa magari na maeneo mengine na ikiwezekana TPDC sasa iweze kutoa master plan ya namna ambavyo gesi hiyo itafika katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Mikoa ya Kaskazini, Mikoa ya Nyanda za Juu hata na Mikoa ya Kusini ili tuweze kuokoa uharibifu wa mazingira na vilevile tuweze kuokoa pesa nyingi sana za kigeni ambazo zinatumika kwa ajili ya kuagiza mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumza ni kuhusu kilimo chetu. Zamani kahawa, pamba, mkonge, pareto na kadhalika ni mazao ambayo yalikuwa yanatuingizia fedha nyingi sana za kigeni lakini sasa hivi maeneo ambayo yalikuwa yanalima pamba zamani pamba hailimwi tena kwa sababu wakulima wanakata tamaa, maeneo yaliyokuwa yanalima kahawa hivyohivyo na kadhalika na kadhalika. Sasa tunazungumza habari ya Tanzania ya viwanda lakini Tanzania ya viwanda itapatikana namna gani kama hatuwezi kuwahamasisha wakulima wetu tukapata malighafi. Naomba mpango utakapokuja uje na mkakati mahsusi kabisa wa namna ambavyo tutabadilisha kilimo chetu kiwe cha kisasa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kulikuwa na ule mpango wa SAGCOT ambao ulikuwa ni mradi mkubwa kabisa. Niseme wazi kabisa kwamba sipingani na mradi wa Stiegler’s Gorge wala siko kwenye hoja ya UNESCO na mambo mengine, lakini nataka kusema wataalam wametafakari namna gani mradi wa Stiegler’s Gorge na mwingiliano wa ule mkakati wa SAGCOT labda pengine ule mkakati umefutwa au namna gani. Kwa sababu yako mazao madogo madogo ukiacha haya mazao makubwa ya biashara ambayo yanaweza yakaibadilisha nchi hii. Tunaweza tukauza nje mananasi, maembe, nyanya na kadhalika na matokeo yake hivi ndiyo vitu vidogo ambavyo vinaweza vikafanya watu wa kawaida kuonekana kwamba Serikali inawajali na kipato chao kinaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kuhusu ujenzi wa reli yetu, hili ni wazo ambalo hakuna mtu hata mmoja ambaye anaweza akalipinga, tunahitaji reli kutoka Dar es Salaam kwenda Isaka, Kigoma, Karema, Tanga na Moshi. Hoja ni hii tutaweza kwa pesa zetu? Naomba Serikali iseme fedha za kujenga reli hii tunazipataje? Hizi fedha shilingi trilioni 16 kwa ajili ya ujenzi wa reli kuzibeba peke yetu kama nchi maana yake ni kuacha shughuli nyingine za huduma kwa jamii, ni lazima zitaathirika.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo nasema kama walivyosema wenzangu tusione aibu hata siku moja kushirikisha private sector. Wako watu duniani kama Serikali ikidhamiria miradi hii mikubwa tunaweza tukaingia nao ubia ikafanywa vizuri kabisa. Kwa sababu hii reli lazima iwe ya kibiashara kama sisi tutaamua kukopa reli ifike mpaka hapa Dodoma halafu tushindwe kuiendeleza lazima kama nchi tutafakari hizi fedha tutazirejesha namna gani kwa sababu ikifika Dodoma itakuwa ni ya huduma tu haitaweza kuwa ya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima Mpango utakapokuja Waziri Dkt. Mpango atuambie ni maeneo gani ambayo yanaweza yakanyanyua uchumi ambayo tunaweza tukashirikiana na private sector. Eneo kwa mfano la ujenzi wa barabara, wamesema wenzangu wengine Mheshimiwa Adadi amesema kuna barabara nyingine ambazo Serikali haihitajiki kujenga sasa, kuna watu binafsi wanaweza wakajenga halafu wakaingiza road toll. Kwa hiyo, hii sheria ya PPP tusiiweke tu kwenye vitabu, tuangalie namna ambavyo itafanya kazi kwa manufaa ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kulisema kuhusiana na hilo, tusiwanyanyapae wafanyabiashara. Wafanyabiashara wanalalamika na wanalalamika kwa sababu inaonekana kana kwamba Serikali inataka kurudi katika ukiritimba wa Serikali yenyewe kufanya biashara. Miradi ya ujenzi sasa inakwenda JKT inarudi Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuhakikishe kwamba tunai-boost private sector kwa sababu Serikali ndiyo yenye pesa ifanye ubia na private sector ili wananchi waweze kunufaika kwa sababu private sector kwa kiwango kikubwa ndiyo inayotoa ajira kwa watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami namshukuru Mungu kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja hii. Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora, yapo malalamiko mengi kuhusu utendaji wa baadhi ya Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi na kadhalika kuhusu namna wanavyotekeleza majukumu yao. Baadhi yao bado wanafanya kazi kinyume na sheria za nchi, wanatoa matamko yanayogongana na maamuzi ya viongozi wengine wa Kitaifa. Kiburi hata cha kukataa kutekeleza maagizo ya Mawaziri na ubabe wa hali ya juu kwa wananchi. Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, moja, utaratibu wa kuwapata viongozi vetting uimarishwe. Mbili, kuwepo semina za mara kwa mara kuwakumbusha na kuwaimarisha. Tatu, kuwaondoa katika utumishi wale ambao hawataki kubadilika. Taifa liwe na benki ya watumishi badala ya utaratibu wa sasa, yaani viongozi waandaliwe mapema. Mheshimiwa Mwenyekiti, niandike kuhusu usalama wa raia, katika siku za hivi karibuni hofu imetanda miongoni mwa wananchi kutokana na maiti zinazookotwa maeneo mbalimbali ya nchi. Wananchi wanaotekwa majumbani mwao usiku bila maelezo. Baadhi ya wananchi kupigwa risasi hadharani na matamko ya vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi wa wananchi. Mazoea ya matukio haya, vyombo vya dola kutotoa wajibu kutasababisha chuki hata baadaye kisasi na hivyo kuvuruga amani ya nchi. Nashauri matukio haya yachunguzwe kwa kina na majibu ya uhakika yatolewe kwa wananchi na kwa familia za wahusika. Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, elimu, ipo haja ya Taifa kujadili kwa kina kuhusu mfumo wetu wa elimu. Sasa hivi nchi inasisitiza sana mfumo wa uchumi wa viwanda. Kama elimu yetu haitaelekezwa kwenye lengo hilo tutashindwa kufikia lengo. Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri turudishe elimu ya kujitegemea kwa vijana wetu wote kuanzia shule za msingi. Pili, nashauri vyuo vya VETA viimarishwe na wilaya ambazo vyuo hivyo havipo utafutwe uwezekano wa haraka wa vyuo hivyo kujengwa. Vijana wafundishwe kujifunza sio kwa ajili ya kuajiriwa bali elimu iwasaidie kujipatia ajira na kuchangia katika mkakati wetu wa viwanda. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na nchi jirani ina mkakati wa kuboresha mipaka yetu. Hatua hiyo imewafanya wananchi kuwa na hofu. Katika mpaka wa Tarakea Wilayani Rombo, wananchi wameishi katika mpaka hata kabla ya uhuru. Taarifa walizonazo ni kwamba wakati wa kunyoosha mpaka huo wataondolewa bila fidia yoyote. Naomba Serikali kutoa tamko kuhusu jambo hili ili kuwatoa wananchi hofu na kama itawaondoa ione uwezekano wa kuwalipa fidia. Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji nchini ni kubwa sana. Hata hivyo, tuna maji mengi sana katika maziwa na mito yetu. Wilaya ya Rombo ni mojawapo kati ya wilaya zenye tatizo kubwa sana la maji. Ukanda wa chini katika wilaya yetu ndio unaoathirika zaidi. Hata hivyo, tunashukuru kwa miradi inayoendelea. Pamoja na hayo, tunaomba vyanzo vya maji kutoka vijito toka Rongai vinavyotiririsha maji kuingia Kenya vitumike. Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba na tunarudia ombi hili kwamba makorongo katika mito yetu ya msimu izuiwe ili kujenga mabwawa ambayo yatatumika kuhifadhi maji ya mvua. Matumizi ya maji ya Ziwa Chala ambayo tuliambiwa ni ya Kimataifa ili hali wenzetu wa Kenya wanayatumia. Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, ajira kwa vijana sasa ni bomu kubwa katika nchi yetu. Vijana wengi wamemaliza elimu kuanzia msingi hadi vyuo vikuu. Hata hivyo, ni wazi Serikali haiwezi kuajiri vijana wote. Kama nchi ni muhimu kuliangalia tatizo hili kwa kina. Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo mifuko mbalimbali ya kuwasaidia vijana. Vile vile kuna asilimia kumi za vijana, wanawake na walemavu katika halmashauri. Utaratibu unaotumika katika kutoa pesa hizi ni wa upendeleo na kibaguzi na halmashauri hazipeleki pesa hizo ipasavyo. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri ianzishwe benki maalum kwa ajili ya kuweka pesa hizi ili zitolewe kwa utaratibu na masharti maalum. Itungwe sheria ili kuwabana Wakurugenzi kutoa pesa hizi. Wakurugenzi ambao hudharau kutoa pesa hizi wachukuliwe hatua za kinidhamu. Mkakati wa kuwatafutia vijana maeneo maalum ya kilimo uimarishwe. Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wa Rombo wana vikundi ambavyo kama wangepewa ardhi wako tayari kwenda sehemu yoyote katika Jamhuri ya Muugano kwa ajili ya kilimo. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naomba kumpongeza Waziri Mkuu na watendaji wake na naomba kuwasilisha.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami namshukuru Mungu kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora, yapo malalamiko mengi kuhusu utendaji wa baadhi ya Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi na kadhalika kuhusu namna wanavyotekeleza majukumu yao. Baadhi yao bado wanafanya kazi kinyume na sheria za nchi, wanatoa matamko yanayogongana na maamuzi ya viongozi wengine wa Kitaifa. Kiburi hata cha kukataa kutekeleza maagizo ya Mawaziri na ubabe wa hali ya juu kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, moja, utaratibu wa kuwapata viongozi vetting uimarishwe. Mbili, kuwepo semina za mara kwa mara kuwakumbusha na kuwaimarisha. Tatu, kuwaondoa katika utumishi wale ambao hawataki kubadilika. Taifa liwe na benki ya watumishi badala ya utaratibu wa sasa, yaani viongozi waandaliwe mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niandike kuhusu usalama wa raia, katika siku za hivi karibuni hofu imetanda miongoni mwa wananchi kutokana na maiti zinazookotwa maeneo mbalimbali ya nchi. Wananchi wanaotekwa majumbani mwao usiku bila maelezo. Baadhi ya wananchi kupigwa risasi hadharani na matamko ya vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi wa wananchi. Mazoea ya matukio haya, vyombo vya dola kutotoa wajibu kutasababisha chuki hata baadaye kisasi na hivyo kuvuruga amani ya nchi. Nashauri matukio haya yachunguzwe kwa kina na majibu ya uhakika yatolewe kwa wananchi na kwa familia za wahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, elimu, ipo haja ya Taifa kujadili kwa kina kuhusu mfumo wetu wa elimu. Sasa hivi nchi inasisitiza sana mfumo wa uchumi wa viwanda. Kama elimu yetu haitaelekezwa kwenye lengo hilo tutashindwa kufikia lengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri turudishe elimu ya kujitegemea kwa vijana wetu wote kuanzia shule za msingi. Pili, nashauri vyuo vya VETA viimarishwe na wilaya ambazo vyuo hivyo havipo utafutwe uwezekano wa haraka wa vyuo hivyo kujengwa. Vijana wafundishwe kujifunza sio kwa ajili ya kuajiriwa bali elimu iwasaidie kujipatia ajira na kuchangia katika mkakati wetu wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na nchi jirani ina mkakati wa kuboresha mipaka yetu. Hatua hiyo imewafanya wananchi kuwa na hofu. Katika mpaka wa Tarakea Wilayani Rombo, wananchi wameishi katika mpaka hata kabla ya uhuru. Taarifa walizonazo ni kwamba wakati wa kunyoosha mpaka huo wataondolewa bila fidia yoyote. Naomba Serikali kutoa tamko kuhusu jambo hili ili kuwatoa wananchi hofu na kama itawaondoa ione uwezekano wa kuwalipa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji nchini ni kubwa sana. Hata hivyo, tuna maji mengi sana katika maziwa na mito yetu. Wilaya ya Rombo ni mojawapo kati ya wilaya zenye tatizo kubwa sana la maji. Ukanda wa chini katika wilaya yetu ndio unaoathirika zaidi. Hata hivyo, tunashukuru kwa miradi inayoendelea. Pamoja na hayo, tunaomba vyanzo vya maji kutoka vijito toka Rongai vinavyotiririsha maji kuingia Kenya vitumike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba na tunarudia ombi hili kwamba makorongo katika mito yetu ya msimu izuiwe ili kujenga mabwawa ambayo yatatumika kuhifadhi maji ya mvua. Matumizi ya maji ya Ziwa Chala ambayo tuliambiwa ni ya Kimataifa ili hali wenzetu wa Kenya wanayatumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, ajira kwa vijana sasa ni bomu kubwa katika nchi yetu. Vijana wengi wamemaliza elimu kuanzia msingi hadi vyuo vikuu. Hata hivyo, ni wazi Serikali haiwezi kuajiri vijana wote. Kama nchi ni muhimu kuliangalia tatizo hili kwa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo mifuko mbalimbali ya kuwasaidia vijana. Vile vile kuna asilimia kumi za vijana, wanawake na walemavu katika halmashauri. Utaratibu unaotumika katika kutoa pesa hizi ni wa upendeleo na kibaguzi na halmashauri hazipeleki pesa hizo ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri ianzishwe benki maalum kwa ajili ya kuweka pesa hizi ili zitolewe kwa utaratibu na masharti maalum. Itungwe sheria ili kuwabana Wakurugenzi kutoa pesa hizi. Wakurugenzi ambao hudharau kutoa pesa hizi wachukuliwe hatua za kinidhamu. Mkakati wa kuwatafutia vijana maeneo maalum ya kilimo uimarishwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wa Rombo wana vikundi ambavyo kama wangepewa ardhi wako tayari kwenda sehemu yoyote katika Jamhuri ya Muugano kwa ajili ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naomba kumpongeza Waziri Mkuu na watendaji wake na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu na ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kwanza kuchangia katika hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijatoa mchango wangu, niseme tu kwamba Mheshimiwa Rais alipochagua vijana kuongoza katika sehemu mbalimbali, nadhani kusudio lake lilikuwa vijana waoneshe uwezo kwa sababu ya ujana wao, uwezo wa kufikiri, kukimbia na kutenda kwa haraka. Ni kwa sababu hiyo nataka niwapongeze Mawaziri hawa watatu; Mheshimiwa Jafo pamoja na wenzake Mheshimiwa Kandege na Mheshimiwa Kakunda kwa kazi wanayofanya. Wizara hii ni kubwa sana, lakini kwa muda mfupi wameweza kukimbia nchi nzima na kufanya hayo mengi waliyoyafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme tu kwamba kwa mara ya pili leo hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani imekosekana. Sasa jambo hili siyo afya kwa Bunge na wala siyo rekodi nzuri ambayo inaandikwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri Uongozi wa Bunge uchukue hatua dhidi ya jambo hili, kwa sababu jambo hili likiendelea linafedhehesha demokrasia ndani ya Bunge na vizazi vijavyo vitatuona kwamba tumeweka precedent mbaya sana katika nchi yetu na Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa napenda sana nizungumze suala la elimu. Suala la elimu sasa ni jambo ambalo linazungumzwa na wengi katika nchi yetu na miezi michache iliyopita, Mheshimiwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alitoa rai lifanyike kongamano kwa ajili ya kujadili elimu ya nchi hii ambayo inaporomoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami leo ningependa kusema kwamba ni lazima elimu yetu tuibadilishe tujikite kwenye elimu yenye ujuzi kwa watoto wetu; elimu yenye malengo ambayo itawezesha watoto wetu wakimaliza hata primary school wajue kwamba ni nini ambacho wameandaliwa kwenda kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wahenga wenzangu ndani ya Bunge, wanakumbuka kwamba baadhi yetu tulimaliza darasa la saba tukiwa tuna ufundi wa namna fulani. Tulikuwa tunajua kutengeneza meza, bustani mbalimbali, masweta, mashuka na kadhalika, lakini leo hii mtoto anamaliza darasa la saba hajui chochote. Hata kilimo ambacho anaambiwa akafanye hajui, mtoto anamaliza form four hajui chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana turejee kwenye elimu ya zamani ya kujitegemea. Nasema tuache kuendesha elimu kwa matamko. Siku chache zilizopita, tumesikia habari ya kuondolewa michango mbalimbali kwenye mashule; ni sawa kuna michango ambayo ilikuwa inakera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nazungumza sana kuhusu mchango wa chakula mashuleni. Upo utafiti unaosema kwamba akili za watoto wetu zimedumaa kwa asilimia 42 kwa sababu ya lishe duni. Hii vile vile inatokana na elimu tunayowapa. Zamani tulikuwa tunalima bustani tunakula mboga mashuleni; tulikuwa tunafuga sungura, tunakula sungura mashuleni; tulikuwa tunafuga kuku, tunakula mayai shuleni; na tulikuwa tunafuga ng’ombe tunakunywa maziwa shuleni. Sasa ni mdudu gani aliyeingia katika nchi yetu akaondoa mambo haya katika Shule za Msingi matokeo yake watoto wetu sasa tunawadundulizia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iangalie uwezekano wa kuwapa watoto wetu wote chakula. Wale ambao mmesoma zamani mtakumbuka jinsi Mwalimu Nyerere alivyoenda kwa Rais J. F. Kennedy wakati ule tukapata shayiri na maziwa watoto wakasoma, kiwango cha elimu kilipanda namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ni huduma. Pamoja na kwamba tunajenga standard gauge, reli; tunanunua ndege na kadhalika, kama hatutaangalia tukahudumia elimu yetu sawasawa, Taifa hili litakwenda kuangamia. Mifano tunayo, sasa hivi bajeti inajadiliwa katika nchi zote za Afrika Mashariki. Ukienda Kenya wanajadili kuhusu ajira kwa vijana na akinamama, wanajadili habari ya uwekezaji katika assembling ya viwanda vya magari. Ukienda Uganda wanajadili habari ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tupo katika Bunge, Watanzania wanajadili habari ya watoto waliotelekezwa. Ni kwa sababu akili zetu tumezi-corner kwenye kujadili vitu vidogo vidogo badala ya kujadili issues kubwa za kuisaidia nchi yetu. Kwa hiyo, naomba kabisa Wizara iangalie namna ya kututoa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nizungumze habari ya asilimia kumi ya wanawake na watoto. Naunga mkono yale yaliyosemwa na Kamati yangu, lakini tumekuwa tukiwalaumu Wakurugenzi hapa. Hawa Wakurugenzi, leo nataka niseme kwamba Wakurugenzi katika nchi yetu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana na sababu ni kwamba fedha za kuendesha Halmashauri hawapati. Matokeo yake wanaangalia ile asilimia kumi ndiyo inayowasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna Halmashauri ambazo hazilipi posho kwa Madiwani; na sababu ni kwamba fedha ambazo walikuwa wanategemea kwenye vyanzo mbalimbali, Serikali Kuu imechukua, yaani ni kana kwamba hawa Wakurugenzi wamefungwa mikono na miguu halafu wanaambiwa wakimbie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, pamoja na utekelezaji wa hayo Kamati iliyosema, lakini ni lazima Serikali iangalie uamuzi wake wa kuzinyang’anya hizi Halmashauri vyanzo vyake vya mapato. Ni kweli asilimia kumi inasaidia, katika Jimbo langu najua. Jimboni kwangu Warombo ni watu wanaohangaika dunia nzima wamo, Halmashauri zote Tanzania Warombo wapo kwa sababu wamezoea hivyo. Wangepata hizi pesa, zingewasaidia zaidi. Kwa hiyo, naunga mkono itungwe sheria, lakini pia iwepo akaunti maalum ambapo hizi pesa zitaingia ziweze kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kuhusu TARURA. Naunga mkono TARURA kwa sababu hapo nyuma fedha za barabara zilikuwa zinagawiwa kisiasa. Diwani anataka barabara yake anakwenda ana-influence kule, inajengwa. Diwani ambaye hawezi kufanya hivyo, anashindwa. Sasa nasema tu kwamba ili kuondoa malalamiko TARURA ishirikishe Halmashauri kwa kutoa taarifa mbalimbali ya kazi wanazofanya ndani ya Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuwe na Bodi ya TARURA ngazi ya Wilaya na bajeti ya TARURA iongezwe kutoka asilimia 30 ya Mfuko wa Barabara sasa, angalau ifike asilimia 50 na uanzishwe mfuko wa matengenezo ya barabara ya dharura kwa sababu barabara hizi za za vijijini ni tofauti na zile barabara kuu. Hizi za vijijini zinaharibika mara kwa mara mvua inaponyesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumze kuhusu utawala bora. Tumeshuhudia ugomvi na kutoelewana katika Halmashauri mbalimbali kati ya Wakurugenzi, Madiwani pamoja na Watendaji wengine. Tunaiomba Serikali kwa mara nyingine itafute namna ya kuondoa hii migogoro, kwa sababu kwenye migogoro kazi haiwezi kufanyika. Wakurugenzi ambao wanafikiri wanataka kufanya siasa, wanafikiri wanataka kuua Wabunge, ni vizuri Serikali iwa- identify wakae pembeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni kwa Halmashauri zote, unakuta Wakurugenzi wamekaa pale, Mkurugenzi wa Halmashauri X ana uhusiano na Mkurugenzi wa Halmashauri Y huko, wanachoreana namna ya kupata Ubunge, matokeo yake wanaingiza migogoro katika Halmashauri, Halmashauri haziendi kwa sababu huyu ana tamaa. Wachunguzeni ili iamuliwe, kama wanataka kufanya siasa, wafanye siasa. Vinginevyo tunao wajibu kabisa wa Kimungu wa kuhudumia watu wetu na siyo kuvutana kwa ajili ya nani awe nani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, yapo maagizo yanayotolewa na viongozi wetu. Kwa mfano, Mawaziri wetu wametoa maagizo kuhusu Halmashauri ya Tunduma kwa barua mara mbili, Mkuu wa Wilaya hatekelezi, Mkurugenzi hatekelezi, Madiwani na Halmashauri iliyochaguliwa na wananchi haifanyi kazi na haikai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unashindwa kuelewa, hii dharau ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kwa Mawaziri wetu inatoka wapi? Kwa sababu Waziri anamwakilisha Rais na Waziri anapotamka maana yake anaangalia sera, sheria na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie viburi vya baadhi ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Watendaji ili Halmashauri zetu ziweze kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna kamata kamata ya...


TAARIFA . . .

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, bila shaka umenilindia muda wangu, sasa hii siyo nafasi yako ya kujitetea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, sasa hivi kumekuwa na matamko mbalimbali na ya ajabu ya kuhatarisha usalama wa nchi. Yupo mtu mmoja anaitwa Cyprian Musiba, anaita mkutano na Vyombo vya Habari anaanza kushukutumu baadhi ya Viongozi na kutoa maagizo, kwamba ningekuwa mimi ningeua hata 200. Juzi Maaskofu wamezungumza, anaitisha Vyomb vya Habari, anasema ningeua hata 200. Hivi nchi hii si Usalama wa Taifa wapo, nchi hii si ina dola? Hivi huyu mtu mnamkalia kimya ina maana mnamtuma? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi watu wanapotea, sasa hivi watu wanauawa, mtu anasimama hadharani anasema ningekuwa ningeua 200, ningekuwa ningeua 300, halafu anaangaliwa tu hivi na anaandika kwenye gazeti lake. Wakati Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, shemeji yangu, unafungia magazeti kwa sababu mbalimbali, huyu anatoa matamko kwenye hilo gazeti lake kwamba ataua, atakamata, atafanya nini! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho amenitaja mimi kwamba ni mmoja kati ya majasusi wa CHADEMA. Nataka niwaambie, kwa sababu watu wamepotea hapa watu wameuawa hapa, Serikali mnamsikia Ndugu Musiba mnakaa kimya, hamumchukulii hatua, mimi nataka nijenge hoja kwamba Serikali mnawajua wauaji, kwa sababu Musiba anawatamka hamchukui hatua, ni mtu wenu. Vinginevyo, njooni hapa mtuambie huyu Musiba ni nani na mchukue hatua dhidi yake. Vinginevyo, kujenga nyumba ni jambo gumu lakini kuibomoa ni kwa siku moja; (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa hili waasisi walilijenga kwa nguvu, kwa shida kubwa, lakini watu kama akina Musiba kwa sababu ya kutafuta political mileage, wanalivunja. Kwa sababu kama ataniua mimi, mimi nina ukoo wangu, mimi nina ndugu zangu, nina rafiki zangu, hicho kisasi mtakibebea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Ardhi. Awali ya yote niseme kwamba Bunge hili liliunda Kamati Teule kwa ajili ya kuchunguza migogoro ya ardhi na kwa bahati nzuri, nilikuwa miongoni mwa Wabunge walioteuliwa na Mheshimiwa Spika wa Bunge la Kumi kuingia kwenye Kamati hiyo kwa ajili ya kazi mahususi ambayo Bunge liliagiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumpongeza Waziri Lukuvi pamoja na wasaidizi wake, kwa sababu kadri ninavyofuatilia utendaji wao ni kwamba yale mapendekezo ya ile Kamati Teule yanaendelea kutekelezwa hatua kwa hatua. Moja kati mapendekezo tuliyotoa ni kwamba Wizara ijaribu kuzi-coordinate Wizara zinazoshughulika na masuala ya ardhi; Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maji, ili kuweza kuratibu vizuri matumizi ya ardhi yetu maana yake tuligundua kila Wizara inafanya mambo yake kuhusu masuala haya ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiona ni kwamba, hili linafanyika na mambo yanakwenda vizuri. Vilevile tulitoa pendekezo kwamba, lazima watumishi wa Wizara hii wapewe nafasi ya kwenda kujifunza, kwa sababu migogoro ya ardhi haipo Tanzania peke yake, iko nchi nyingi. Nchi zetu za Afrika Mashariki na Kati, migogoro hii ni mingi sana na wenzetu kwa mfano, Ethiopia wamejaribu kuitatua kwa namna ambavyo imeleta muafaka kati ya wakulima na wafugaji. Kwa hiyo, tulipendekeza watumishi hawa wapewe nafasi ya kwenda kujifunza namna wenzao walivyotatua migogoro hii na kuleta amani katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo lingine ambalo tulitoa ni hili ambalo linazungumzwa sasa hivi kuhusu upimaji wa ardhi. Migogoro haiko kwa wakulima na wafugaji peke yake au kwa wakulima na hifadhi peke yake au na wawekezaji peke yake, lakini hebu tazameni; ukitoka Dar es Salaam kuja Dodoma, sasa miji hii inaungana, maana yake kuna ujenzi holela wa ovyo ovyo tu. Dar es Salaam imeshaungana na Chalinze; Chalinze imeshaungana na Morogoro; Arusha imeungana na Bomang‟ombe; Bomang‟ombe imeungana na Moshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiachia hali hii iendelee, maana yake ni kwamba huko tuendako Taifa hili litakosa ardhi ya kilimo, kwa sababu kila anayefikiria kuweka jengo lake analiweka mahali popote anapotaka. Ni matumaini yangu kwamba Mheshimiwa Lukuvi hili atalizingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na upimaji, Wizara ilikuwa na mfuko maalum ambao ulikuwa unazisaidia Halmashauri kukopa ili kuweza kufanya upimaji katika Halmashauri zao. Ulikuwa unaitwa Plot Development Revolving Fund.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi watu wa Rombo tulipeleka maombi yetu Wizarani kwa ajili ya kukopa fedha hizi ili tuweze kufanya upimaji, mpaka leo hatujajibiwa na nadhani pengine Mfuko umekufa. Nadhani hiki kilikuwa kitu kizuri. Wizara iangalie namna ya kuboresha huu Mfuko ili Halmashauri ziweze kukopa fedha kwa ajili ya kusaidia kupima katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, ni hiki kilio cha kila Halmashauri kirejeshewe mapema ile retention wanapokusanya kodi ya ardhi. Mara nyingi inachelewa, sasa matokeo yake ni kwamba zile Ofisi za Ardhi katika Halmashauri zinakuwa kama zimefungwa miguu na mikono, hazina nyenzo, hazina fedha, kwa sababu hiyo upimaji unakuwa ni mgumu sana na utekelezaji wa majukumu yao pia unakuwa ni mgumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo, nizungumze kidogo kuhusu Jimbo langu. Katika Jimbo langu kuna eneo la Ziwa Chala. Hili ni ziwa pekee katika Afrika kama siyo dunia. Ni ziwa pekee ambalo maji yake hayajachafuliwa kwa asilimia 85. Sasa hivi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinafanya utafiti wa namna tabianchi ilivyobadilika kwa miaka 500,000 iliyopita kwa kutumia lile ziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sijui Halmashauri au Wizara, ilikwenda ikakabidhi watu iliyowaita wawekezaji eneo la lile ziwa na kuwamilikisha. Pamoja na hayo, ardhi inayozunguka lile ziwa ni ardhi ambayo wananchi wa Kata ya Holili, Chala, Mamsera, Ngoyoni na Mengwe walikuwa wamemilikishwa zamani na iliyokuwa inaitwa Land Board. Sasa wananchi wa Kata hizi wanazuiwa kwenda kwenye maeneo yao, wanapigwa, wanadhalilishwa na wenzao wawili matajiri ambao ni Warombo kule kule waliokwenda kumleta Mzungu wakamweka pale kwa kigezo kwamba ile ardhi ni mali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Wizara kwa sababu waliopewa hiyo ardhi walikuwa viongozi katika Serikali ya Chama cha Mapinduzi, mwone kwamba jambo kama hili linawachafua. Kata nilizotaja ni karibu tano, wazee wanapigwa, akinamama wanapigwa na watu wachache waliopewa ardhi yao wanadai kwamba ni mali yao. Naamini Mheshimiwa Lukuvi kwa kasi aliyoonesha na kwa usikivu alioonesha, nami niseme ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, siyo dhambi kumpa pongezi Mheshimiwa Lukuvi. Siyo dhambi hata kidogo, kwa sababu hata mimi binafsi niseme tu kwamba, kuna mambo aliyonitendea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilidhulumiwa kiwanja Tegeta tangu mwaka 1994. Nimekwenda kwenye haya mnayoita Mabaraza za Ardhi, nimehangaika sikupata haki yangu; lakini Mheshimiwa Lukuvi ameingia, haki yangu nimepata. Sasa ndiyo maana nasema siyo dhambi kama jambo zuri likifanyika lisemwe. Nami ningesema na wengine waige mfano wa Mheshimiwa Lukuvi wa kutatua mambo kwa haraka. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba hata hili la Ziwa Chala Mheshimiwa Lukuvi atalifuatilia na alitatue kwa masilahi ya watu wangu wa Rombo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hilo tu, pale Tarakea kuna kiwanja cha vijana cha kucheza mpira, watu wamefanya siasa tu, wakampa mfanyabiashara mmoja anaitwa Maulidi, kajenga hapo jengo lake. Sasa kwa uhaba wa ardhi tuliyonao Rombo, vijana wetu hawana mahali pa kuchezea, lakini tajiri kaweka jengo pale, liko limesimama naye anatumika kwa ajili ya kukisaidia Chama chenu kwenye kampeni, anatoa pesa za kampeni. Matokeo yake kwa kuwa anatoa pesa za kampeni, hakuna mtu anayemgusa. Ni imani yangu kwa kasi hiyo hiyo pia Mheshimiwa Waziri atakwenda pale aangalie jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kata ya Mengwe, hili nililisema kwenye Wizara ya Ujenzi, tuna kiwanja pia cha watoto cha kucheza mpira. Wameweka hapo matingatinga tangu mwaka gani sijui, yako pale, vijana hawana mahali pa kuchezea, hebu Mheshimiwa Lukuvi aangalie namna ya kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niseme tu, Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla tuna matatizo makubwa sana ya ardhi. Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro nao ni Watanzania, nimesikia tukizungumza hapa kuhusu mashamba ambayo Serikali inayarejesha kwa wananchi. Naomba kama unaweza ukawekwa utaratibu hata wananchi wa maeneo ambayo ni highly populated kama Rombo, vijana wana moyo wa kufanya kazi ya kilimo, lakini hawana maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana hawa wapo tayari kwenda kwenye maeneo mengine ya nchi ambayo wakipewa ardhi kwa utaratibu fulani wanaweza wakaendeleza kilimo. Nami niko tayari kuwaorodhesha vijana kama hao na kuwapeleka ofisini kwa Mheshimiwa Waziri ili kama kuna shamba fulani la Serikali watalitoa, basi na wale vijana wanufaike kwa sababu nao ni Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kujua, huu utaratibu wa kupima ardhi ambazo tunapata hati zile za kimila, sijui namna gani, kwa mashamba ya kimila kama ya Kilimanjaro, vile vihamba ambavyo vina makaburi, tunaambiwa hatuwezi kukopa kwa sababu mashamba yetu yana makaburi, upimaji wake unafanyika namna gani. Sisi tutakosa hiyo haki kwa sababu siyo dhambi sisi kuzika kule kwenye vihamba vyetu, ni kwa sababu ya ukosefu wa ardhi. Mheshimiwa Waziri aangalie namna ya kutusaidia ili wale wananchi waweze kupata manufaa ya ardhi yao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi, na kwa kweli hii ni nafasi ambayo nilikuwa naisubiri kwa hamu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie mambo mawili ambayo yanaendelea katika Jimbo langu. Mwaka 2011 nilisimama katika Bunge hili nikasema Jimbo la Rombo halina hifadhi ya wanyama, nilisema hivyo kwa sababu tembo kutoka Kenya, Mbuga ya Tsavo pamoja na Amboseli walileta maafa makubwa sana katika Jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, karibu vijiji 20, Kata ya Holili, kijiji cha Kidondoni Kata ya Chana, kijiji cha Ngoyoni, kijiji cha Ngareni, Shimbi Kati, Kiraeni, Msaranga, Mahorosha, Leto, Urauri na Rongai, mazao ya wananchi yaliliwa na tembo, wananchi waliuawa na wengine wakapata vilema vya kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi ya fidia yalipelekwa Wizarani kuanzia mwaka 2012 hadi leo hakuna majibu, hakuna chochote. Ninaiomba sana Wizara ishughulikie jambo hili kwa sababu ni kero na wananchi wamejenga chuki kubwa kati yao na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iliahidi kutujengea vituo vya kudhibiti wanyama pori. Iliahidi kutujengea vituo vitatu, kimoja Ngoyoni, kituo cha pili Mahorosha na kituo cha tatu Kikelelwa, hadi sasa ni kituo kimoja tu kimejengwa. Naomba Wizara ifanye jitihada za kuhakikisha kwamba vituo vingine viwili vimekamilishwa na ninapenda nimsikie Waziri wakati anafanya majumuisho ili kero hii iishe moja kwa moja kwa wananchi wa Rombo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kero nyingine ambayo ningependa kuizungumza ni uvamizi wa nyani kutoka mlima Kilimanjaro. Kijiografia, Mlima Kilimanjaro wote uko katika Jimbo la Rombo, pamoja na kwamba mlima huu unahudumiwa na Halmashauri zote ambazo zinazunguka ule mlima. Mlima Kilimanjaro ukiungua ni wananchi wa Rombo wanaswagwa kwenda kuzima moto mlimani. Wapo waliovunjika, wapo waliokuwa vilema kwa sababu ya kwenda kuzima moto, wanachoambulia ni nusu mkate kwa kila anaekwenda kuzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lucy Owenya amezungumza hapa imefika wakati Mheshimiwa Maghembe, wananchi wa Rombo na Halmashauri zinazozunguka Mlima Kilimanjaro tunataka mrabaha kama wenzetu wa madini wanavyopata. Vinginevyo tumedhamiria safari hii mlima ukiungua hatuzimi, mje mzime wenyewe. Kwa sababu mlima unaingizia TANAPA zaidi ya shilingi bilioni 60 kwa mwaka, lakini hakuna ambacho Halmashauri hizi hususan watu wangu wa Rombo wanakipata zaidi ya vilema ambavyo vinatokana na maporomoko wakati wanaenda kuzima moto mlimani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kama vile haitoshi mlikuwa mmetupa half mile kwa ajili ya akina mama kwenda kukata kuni pamoja na majani mkijua kabisa kwamba Jimbo la Rombo ardhi yetu ni ndogo na kwa sababu hiyo hatuna maeneo ya kuswaga wanyama wetu, wanyama wetu tunawaweka ndani.
Kwa hiyo, eneo lile mlitupa, tulikuwa tunapata majani pamoja na kuni, sasa taabu tunayoipata ni kwamba wananchi ambao wanaishi karibu na eneo hili, vijiji vya Masho, Maharo, Mokara, Ubaa, Mashuba, Kirwa, Katangara, Lesoroma wanapata shida mbili; shida ya kwanza ni kwamba kila wanapolima nyani wanatoka mlimani wanakula mahindi yao yote na mwaka huu wameshindwa kulima kwasababu ya shida ya nyani, KINAPA hawataki kutuwezesha ili kupambana na wale nyani. Shida ya pili ni akina mama ambao wanakwenda kwenye ile half mile kwa ajili ya majani na kuni kinachowapata ni kwamba wanatandikwa viboko, wengine wanabakwa, wengine wananyang‟anywa vifaa vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme mwaka jana askari wa KINAPA waliwakamata akina mama wafuatao, Ndugu Selfina Mtengesi Luka wa Kitongoji cha Mori, Ndugu Fabiola Joseph, Ndugu Rose Luka, Ndugu Witness John, Ndugu Rafia Makongoro wa Kitongoji cha Kimongoni, wakawalaza chini na kuwatandika viboko. Ninaiambia Serikali tabia hii ya askari wenu kupiga wananchi hovyo hovyo, mnawakomaza na mnaleta matatizo katika nchi kwa sababu itafika mahali watasema hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba wakati wa kufanya mjumuisho aibu hii ambayo imetokea Rombo ya akina mama ambao hawajawahi hata kupigwa na waume zao wanaambiwa walale chini, watandikwe viboko vya makalio katika Serikali hii ambayo tunasema ni Serikali yenye amani na utulivu, uniambie ni hatua gani zitakazochukuliwa, kwa sababu ikiendelea hivi itafika mahali sisi tutasema hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiondoka kwenye masuala yanyohusu Jimbo langu, ni kwamba tunazungumza habari ya utalii lakini kuna mambo mengi sana katika nchi yetu ambayo tungeweza tukayatumia yakatuletea uchumi mzuri tu. Kamati ya Bajeti chini ya Mheshimiwa Chenge mwaka jana nakumbuka tulienda Dubai kwa ajili ya semina wakatucheka, wakatuambia mnahangaika na vitu chungu nzima, utalii peke yake ungefanya Tanzania ikawa kitu cha ajabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza habari ya Serengeti, habari ya Mlima Kilimanjaro na kadhalika, mbona kuna vitu vingi vinapotea? Mimi nashangaa watu wanakuja kutalii Bungeni hapa, nashangaa. Kila Halmashauri TANAPA ingeweza ikaamua kujenga makumbusho katika kila Halmashauri watu wakaenda kujifunza habari ya vita ya Maji Maji, watu wakaenda kujifunza kwa mfano pale Kilwa pana handaki linakwenda mpaka Mombasa, linafukiwa tu. Pale Rombo kuna Kata inaitwa Keni, kuna handaki Machifu walichimba zamani linatoka Keni linaenda mpaka Wilayani, yanafukiwa tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa walivyotumia wazee wetu akina Mirambo, akina Mkwawa, akina Mangi Mareale, vinapotea mnaona tu, hakuna mtu anayejali ajenge makumbusho avihifadhi viweze…
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa niseme mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Utawala na TAMISEMI na kwa sababu hiyo naunga mkono taarifa ya Kamati yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, mimi niko hapa mbele ulizoea kumwona Mbowe pale na Lissu hapa na wengine, sasa nipo peke yangu hapa kwa muda mrefu, kweli naumia na hivi nichukue nafasi hii kuwapa pole wenzangu Lissu, Mbowe na Matiko na kuwaombea Mwenyezi Mungu kwamba mitihani inayowakabili, basi waipokee na Mwenyezi Mungu ajalie siku moja tuweze kuwa pamoja tena hapa na najua itakuwa hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nichangie kwenye utawala bora na nitazungumza kuhusu sheria mbili ambazo naona ni muhimu katika kipindi cha sasa nizizungumze. Sheria ya kwanza ambayo ningependa nizungumze kidogo ni The Regional Administration Act, 1997 ambayo ndio inawapa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa mamlaka ya kuweza kuwaweka kizuizini Watanzania kwa masaa 24 au 48.

Mheshimiwa Spika, kabla sijasema hayo kwa sababu mimi ni muhenga, nimekaa nimeona utawala tangu Awamu ya Kwanza mpaka sasa ni kwamba zamani kulikuwa na utaratibu mzuri wa kuwapata viongozi hawa; Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa. Zamani kulikuwa na promotion walikuwa promoted kutoka kwenye miongoni mwa Makatibu Tarafa au Maafisa Ustawi wa Jamii na kadhalika. Sasa siku hizi wanapatikana namna gani sielewi, kwa sababu inavyoelekea wengi uzoefu wa kazi hiyo hawana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwa kweli Mzee Mkuchika Waziri amejitahidi sana kuwafunda na Katibu Mkuu TAMISEMI aliyestaafu Mzee Iyombe naye alijitahidi sana kuwafunda, lakini mambo haya yanaendelea na nayasema kwa sababu ni mambo ambayo yanaweza yakaleta chuki miongoni mwa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sheria ile kifungu cha 7(2) na 15(2) pia vinaweka masharti ya namna viongozi hawa wanavyopaswa watumie ile sheria. Kwamba ili kumweka mtu ndani, Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa masharti manne lazima yazingatiwe. Jambo la kwanza, ni lazima kuwe na kosa la jinai; jambo la pili, kosa hilo lifanyike mbele ya kiongozi; jambo la tatu, kosa liwe linatishia na jambo la nne, kuwe hakuna njia nyingine yoyote ya kufanya zaidi ya kumweka ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wananchi, viongozi hata na wawekezaji wamekuwa wakikamatwa kwa chuki. Mfano mdogo sana Iringa, waliwekwa ndani Diwani mwanamama Celestina Johansen kwa kosa ambalo lilifanywa na halmashauri kwa kuagiza nyumba ya mkazi mmoja ikavunjwe, mama kwa sababu ni Diwani wa eneo lile Mkuu wa Mkoa akaamua awekwe ndani kwa kosa ambalo sio la kwakwe. Mkuu wa Mkoa huyu huyu juzi alimkamata mwekezaji mmoja kwa kutolipa Cess, lakini polisi walivyochunguza wakagundua kwamba yule mwekezaji hana kosa lakini ameshawekwa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huko Ukonga pia Diwani Nancy Disunte naye alikwishawekwa ndani. Hai ndio usiseme, ni kila kukicha Madiwani wanawekwa ndani, Arumeru Mheshimiwa Diwani Elisa Mungure, Mbozi Mheshimiwa Pascal Haonga. Juzi Mkuu wa Mkoa wa Mara alimweka ndani Diwani wa Kata ya Mwema kisa alikunja nne akiwa kwenye mkutano wake.

Mheshimiwa Spika, mambo haya sio mazuri na nayasema kwa dhati kabisa kwa sababu naipenda hii nchi. Kwa maana mambo haya yanaweka chuki miongoni mwa wale wanaowekwa ndani na tusisahau wale wana jamaa zao na chuki hii ikiendelea kuvimba itazaa kisasi, upendo kwenye jumuiya utakosekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali kwanza ifanye vetting ya kutosha kuhusu viongozi hawa, lakini pili iwape mafunzo ya kutosha kwa sababu haya wanayofanya mwisho wa siku ni Serikali inaaibika. Hii ni kwa sababu hawa wote na wengine sikupenda niwataje, wakienda mahakamani watashinda kesi zao.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema tangu mwanzo, utawala bora ni utawala wa sheria na sisi viongozi tunalumbana na mambo yaliyo chini ya sheria. Kwa mfano jana tulisikia hapa juu ya upelelezi wa kesi ya Mheshimiwa Lissu, Waziri alisimama hapa akaeleza lakini Waheshimiwa viongozi humu ndani wana sheria mko wengi sana.

Mheshimiwa Spika, kuna ya The Mutual Assistance in Criminal Matters Act ambayo ina uwezo kabisa ikitumika wa kuchukua maelezo popote na hatua zikachukuliwa. Lissu hawezi kushindwa kufuatwa Nairobi, Ubelgiji au popote alipo kwa kutumia sheria hii ambayo tuliitunga wenyewe hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tukitoa matamko ambayo yanakinzana na hii sheria, watoto wetu wanakuja kusoma Hansard, watoto wetu wanakuja kufanya mitihani yao kwa kufanya reference ya haya tunayosema tunaonekana sijui ni Wabunge wa namna gani. Kwa hiyo, ombi langu kwa viongozi wa nchi yetu na Wabunge wote kwa pamoja tufuate sheria ambazo tunazitunga hapa itatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika…

SPIKA: Mheshimiwa Selasini japo unamlaumu Waziri lakini kwa mfano dereva, kwa nini sheria hiyo ifuate si arudi tu aje atoe ushahidi?

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, wote hawa wawili wapo kwenye matibabu na wanaoweza kueleza kiwango cha namna miili yao imepokea matibabu ni Madaktari wao, lakini hii sheria Serikali, Wizara ya Mambo ya Ndani inaweza ikaitumia hata huyo dereva popote alipo akahojiwa.

SPIKA: Hao madaktari wameshaandika chochote kile kuleta huku?

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, lakini unaniwekea muda wangu eeh?

SPIKA: Muda wako nautunza kwa sababu…

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, ninachosema ili kuondoa hizi sintofahamu na kelele miongoni mwa jamii sheria hii ifuatwe popote pale walipo na haki itatendeka tu.

SPIKA: Lakini pia Madaktari si waandike ripoti ije?

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, sawa…

SPIKA: Mtunzieni muda wake, endelea Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza ni kuhusu uteuzi wa Wakurugenzi wetu. Zamani na nasema hili kwa sababu uliniweka kwenye LAAC katika kipindi chote cha Ubunge wangu kipindi kilichopita na tulipoanza Bunge hili uliniweka tena kwenye LAAC. Niligundua kwamba utaratibu uliokuwa unatumika ni kwamba Wakurugenzi walikuwa wanateuliwa miongoni mwa Wakuu wa Idara ambao tena wametumikia idara zao kwa sio chini ya miaka saba na kwa sababu hiyo Wakurugenzi walikuwa wana uzoefu mkubwa sana katika kazi zao, walizielewa halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, uteuzi ambao unafanyika sasa hivi tumewapata Wakurugenzi ambao sio wazoefu na matokeo yake imekuwa ni kama trial and error. Kwa mfano, Halmashauri ya Moshi (Moshi DC) miaka mitatu hii tayari imeshakuwa na Wakurugenzi watano na matokeo yake ni kwamba yaani ule utendaji unakuwa sio sawasawa na wengine ndio hawa tunaowasikia kwamba wanafanya kazi zao kibabe. Juzi tulisikia kwamba Mkurugenzi kapiga mtu risasi kanisani na mambo kama hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo hili pia ningeliomba Serikali iwe makini katika kuangalia kwamba ni nani tunawateua…

T A A R I F A

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, kabla sijaipokea nimweleze yeye kama Waziri anajua kwamba moja kati ya kazi za Bunge hili ni kumshauri Rais na kitu ninachofanya hapa ni kushauri. Kama yeye ni Waziri wa namna hii ina maana hamsaidii Rais, ndio maana anaogopa kumshauri. Mimi sijasema kwamba Rais apoke ushauri wangu, lakini ninachosema mamlaka za uteuzi zinazomsaidia Rais zihakikishe kwamba watu hawa wamekuwa vetted vizuri ili tupate watumishi wa kufaa katika kutumikia hii nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine la mwisho ambalo ningependa kuzungumza naona nimepigiwa kengele…

SPIKA: Ooh kengele ya pili imeshalia. Ahsante sana Mheshimiwa Selasini. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami nitoe maoni kwenye hoja iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kuna mahali tumekosea kwa sababu miaka ya nyuma tulikuwa tunafanya semina Wabunge wote tunapitishwa kwenye Mpango kabla hatujaanza kuujadili. Vilevile tulikuwa tunapewa walau ABCD ya tathimini ya Mpango uliopita na yote hiyo ni ili kujiweka sawa tu ili mjadala uweze kunoga vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, naomba nijadili kwa kuzungumzia mambo matatu. Jambo la kwanza ni kilimo. Miaka baada ya uhuru tulikuwa hatujaanza kuvuna madini katika nchi yetu na kwa sababu hiyo uchumi wa nchi yetu ulibebwa na kilimo. Mazao ya biashara wakati huo pamba, kahawa, korosho, katani, pareto na kadhalika ndiyo yaliyobeba uchumi wa nchi hii sasa mazao haya yanakufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sote tutakumbuka wakati wa Mwalimu katika maeneo ambayo mazao haya yalikuwa yanapatikana kwa wingi kulikuwa pia kuna viwanda vya ku-process mazao haya. Tulishuhudia Mwatex, Mutex, Coffee Curing kule Moshi na kadhalika sasa vyote hivi vimekufa na sijui nini kilitokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri kwa sababu asilimia 65 ya Watanzania wamejiajiri katika kilimo, basi huu Mpango uje na kitu tofauti kuhusu kilimo. Sote ni mashahidi kwenye bajeti tunayomaliza fedha zilizotengwa kwa ajili ya kilimo karibu Wabunge wote tulikuwa tunapiga kelele kwamba ziongezwe katika kilimo, ufugaji, na katika uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba fedha za kutosha zitengwe kwenye kilimo ili kuimarisha miundombinu ya kilimo. Ni muhimu sana tuone kuna mpango ambao uko wazi wa namna ambavyo nchi hii sasa tutakuwa na viwanda vya kutosha vya mbolea. Fedha za kutosha ziingizwe kwenye Mpango tuone ni namna gani sasa tunapata masoko ya ndani na hata ya nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema hivi siyo kwamba nabeza kazi ambayo imeshaanza kufanywa, kuna kazi inafanyika, lakini nachosema iimarishwe ili wakulima wawe na hakika ya kupata kipato cha kutosha na kizuri kutokana na jasho lao. Wewe ni shahidi mzuri sana na Waheshimiwa Wabunge jinsi tulivyohangaika hapa na mahindi, wakulima Sumbawanga, Mbeya na maeneo mengine walivyopata shida ya kuuza mahindi yao. Sasa hivi gunia la mahindi kwa mfano Kaskazini huku imevuka laki moja na kitu, wakati huo huo mahindi gunia yaliuzwa shilingi 20,000, shilingi 25,000 au shilingi 30,000. Sasa tutengeneze utaratibu ambapo kutakuwa hata na security kwa mkulima huyu ili wakati mazao yakipatikana kwa wingi awe na hakika basi baadaye kunaweza kukawa na nafuu na yeye akapata kipato cha kutosha kutokana na nguvu zake alizotia kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna soko nataka nilitolee mfano, kwa mfano soko la Kibaigwa hapa lilikuwa la Kimataifa watu walikuwa wanatoka Rwanda, Burundi na maeneo mengi ya nchi hii wanakuja kununua mahindi, alizeti na kadhalika lakini sa sahivi linaelekea kufa. Kwa hiyo, masoko ya aina ya Kibaigwa Serikali ingeona uwezekano wa kufanya utafiti masoko haya yawepo katika maeneo mbalimbali kusaidia kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda vya kati kama ambavyo vilikuwepo hapo zamani. Nchi hii kuna maeneo ambayo kuna matunda mengi sana kwa mfano Muheza na Korogwe, machungwa ni mengi sana lakini wakulima wanaonewa kwa sababu yanakuja kwa wingi halafu hatuna hata viwanda vidogo vidogo vya kutengeneza concentrate za machungwa au kuhifadhi yale machungwa yaweze kutumika kipindi kingine ambacho siyo cha msimu. Hivi vitu hivi ndiyo vinakuza thamani ya yale mazao na wakulima wananufaika kutokana na mazao yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuongeze fedha kwenye taasisi za kilimo ili ziweze kufanya utafiti wa kutosha kuhusu mbegu bora kwa ajili ya wakulima, tuweze kupata mbegu zinazoweza kuendana na hali ya hewa. Vyuo vingi sasa hivi vinapata shida ya kufanya utafiti kwa sababu fedha zinazoingizwa kwenye utafiti wa kilimo vilevile zinakuwa za mashaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia tuanze kufikiria kuongeza pesa za kutosha kwenye kilimo cha umwagiliaji. Nchi hii ina maji mengi sana, mvua ikinyesha sote ni mashuhuda kwa mfano barabara hii ya Dodoma maji yamekuwa yanatoka Kiteto na maeneo mengine yanafunga kabisa barabara lakini tungeweza yale maji kuyahifadhi na kuyatumia kwa ajili ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Rombo kwa mfano mvua zikinyesha na sasa hivi Rombo tunapata mvua nyingi sana za vuli, maji yanateremka kutoka Kilimanjaro yanavuka kwenye mito yetu ya asili kule yanaenda Kenya na kule Kenya wameya-tape yale maji. Kuna eneo kule Kenya linaitwa Chumvini, wanalima mbogamboga, nyanya, vitunguu na kadhalika, wanakuja kutuuzia sisi ambao maji yanatoka kwetu. Kwa hiyo ilikuwa ni rahisi tungeweza kwenye makorongo ya ile mito ya misimu tukaiziba namna fulani na mawe yapo ya kutosha tukahifadhi yale maji, baadaye tukayatumia kwa ajili ya kilimo kuendelea kufikiria kuangalia anga mvua zitakuja lini na kadhalika, tutazidi kupata shida na kama nilivyosema nchi hii watu wetu walio wengi wamejiajiri katika kilimo na hakika kabisa kwamba kilimo kikiboreshwa kwa namna kubwa sana tutakuwa tumesaidia watu wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha mazao ya biashara kuna mazao mchanganyiko kama mbaazi, kunde, mahindi na kadhalika, tuimarishe pia masoko kwa ajili ya haya mazao, kwa sababu haya mazao yana masoko ndani, yana masoko nje na wakulima wetu wengi wanalima mazao ya namna hii. Kwa hiyo kuhusu kilimo nafikiri nimeongea vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ufugaji, ngombe wetu wanabaki ni ngombe wale wa asili na hapa Bungeni tumekuwa tukizungumza namna ya kubadilisha wale ngombe waweze kuwa bora zaidi na wakulima waweze kufuga ngombe wachache lakini wenye kipato cha kutosha. Sasa ni rai yangu kwamba Serikali iangalie namna sasa ya mawazo haya kutekelezwa. Zamani kulikuwa na vituo vya uhamilishaji katika baadhi ya vijiji, madume bora yalikuwa yanapatikana kwenye centre moja kwa ajili ya kubadilisha ile mbegu kwa ngombe na hata kwa mbuzi. Sasa baadhi ya hizi centre zimekufa na hatujui zimekufa namna gani. Kule kwetu Rombo centre kama hizi zilikuwa nyingi kabisa mimi nikiwa mdogo, nilikuwa naambiwa chukua ngombe peleka, napeleka, lakini sasa hivi vimekufa. Hivi ni vitu vya kawaida, lakini ni vitu muhimu sana kwa sababu ngombe hawa maziwa na mazao mengine ya maziwa yanasaidia sana katika kipato cha wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hawa ngombe wengi tunaopata Umasaini, Usukumani na kadhalika bado hatujafanya vya kutosha. Mazao yanayotokana na ngozi, mazao yanayotokana na pembe na kadhalika bado ni shida, wenzetu Kenya hapa wana Kiwanda cha Nyama cha Thika, ngombe wanatoroshwa kupitia mpaka wa Loliondo, wanaenda wanachinjwa Thika na matokeo yake nyama inabaki huko, ngozi inabaki huko na kadhalika. Kama nchi hatujashindwa kujenga kiwanda cha kisasa cha kimataifa kinachohusiana na mazao ya mifugo, tunaweza kwa sababu kama mengine yamewezekana kwa nini hili lishindikane na likifanyika ina maana tunawasaidia wakulima na wenyewe wanapata faida kutokana na kazi wanayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni uvuvi. Sasa hivi watu wamehamasika kufuga samaki na mimi nina diwani wangu mmoja ambaye amesoma hapo Sokoine anawafundisha watu namna ya kujenga mabwawa wanafuga samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua hata Waziri Mheshimiwa Mpango ana bwawa lake kubwa sana la samaki, ndiyo mimi najua hatujafahamiana barabarani na huyu mzee, ana bwawa kubwa sana la samaki. Sasa uangaliwe uwezekano wa Watanzania kufundishwa namna ya kufuga samaki kwa sababu watapata kipato kibiashara vilevile wataongeza afya zao, manaa yake tukizungumza samaki tunazungumza samaki wa baharini na kwenye maziwa yetu makubwa tu, lakini Watanzania wanaweza wakafuga samaki kama sehemu ya ajira na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo tuangalie uvuvi wa bahari kuu tumeiongela sana hili. Uvuvi wa bahari kuu unaweza ukatuletea kipato kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ambalo ningependa kuzungumza pia bajeti iongeze fedha za kutosha katika miradi ya maji. Huwezi kuamini sisi tuna ule mlima, chemichemi zilikuwa nyingi sana, lakini na vijiji karibu 41 havina hakika ya maji, yaani kilio cha maji ni kikubwa katika Jimbo langu la Rombo kuliko kitu kingine chochote. Nashukuru kuhusu umeme bado vitongoji kadhaa, lakini kuhusu maji shida ni kubwa sana naomba Mheshimiwa Mpango atakapokuja bajeti yake katika miradi ya maji iimarishwe kwa sababu kwa kweli maji ni uhai na kelele nyingi sana za Watanzania sasa hivi unaona hapa kila Mbunge akisimama anazungumza kuhusu maji katika eneo lake. Nadhani kama tukiweza kukazana kwenye maji kama tulivyokazana kwenye mambo mengine sasa watu wanaweza wakafikia mahali wakatulia na wakafanya mambo yao sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie katika muswada huu. Lakini kabla sijatoa mchango wangu ningependa nitoe ushauri kwa Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi ni ya Watanzania na hili Bunge ni Bunge la Watanzania wote. Ningependa kuliomba Bunge lako tukufu, sisi Wabunge tumepewa kazi ya kuishauri na kuisimamia Serikali, tuwe wakweli na ukweli utatuweka huru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba, tunajadili muswada huu tukiwa na kumbukumbu za kufungiwa kwa baadhi ya magazeti na vyombo kadhaa vya habari kama television pamoja na redio. Ni ukweli pia, kwamba, tunaujadili muswada huu tukijua kabisa kwamba, wanasiasa karibu wote tumefungwa midomo kwa dhana ya hapa kazi tu, lakini kila mmoja wetu anajua kwamba, kazi ya wanasiasa ni kitu gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasiasa kazi yao ni kufanya mikutano na uhamasishaji. Kwa hiyo, kila mmoja wetu anaifahamu hii contradiction, kwamba, wakati tunahimiza kufanya kazi kuna kundi kubwa sana la Watanzania ambalo linazuiwa kufanya kazi. Sasa ni dhahiri kwamba, miongoni mwetu kuna uwoga wa kusema ukweli na wanasiasa wanazuiwa kufanya kazi yao kwa matakwa tu ya mtu fulani, lakini jambo hili ni jambo la Kisheria na jambo la Kikatiba. Ndio maana waliochangia jana waliishauri Serikali na walitushauri sisi Wabunge kwamba, sisi Wabunge tunao wajibu wa kufanya kazi zetu za Kibunge bila uwoga kwa sababu, sasahivi tumeingiwa hofu na uwoga, Sheria zinakanyagwa, Katiba inakanyagwa, tunakaa kimya na hakuna anayesema! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Waziri wa Sheria alishambuliwa sana, shemeji yangu Mheshimiwa Harison Mwakyembe, hata na Mwanasheria Mkuu vilevile. Na hofu ilioneshwa kwamba, tunapitisha Sheria, tunatunga Sheria, lakini Sheria hazifuatwi, hofu hiyo kila mtu anayo katika moyo wake.
Mheshimiwa mwenyekiti, ninaomba kwa masikitiko makubwa niseme jambo hili, hivi tunavyojadili hii sheria sijui kama Serikali inajua kuna vijana wameshikiliwa pale Central Police kuanzia tarehe 24.Mmoja amepigwa mpaka amevunjwa miguu yote miwili, hawajapelekwa Mahakamani!; Tarehe 24 hadi leo! Sijui tunapojadili muswada huu kama Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Sheria anajua kuna vijana zaidi ya 10 wanashikiliwa Oytser Bay Police hawajapelekwa Mahakamani hadi leo. Hivi sasa tutaacha kusema kwa sababu gani? Tutaacha kusema sisi Wabunge kwa sababu tunamuogopa nani wakati sisi tumeapa kuhakikisha kwamba, taifa hili linakwenda vizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nashauri hii mijadala tunayofanya hapa Bungeni tuondoe hofu ya kujiangalia kisiasa, kwa sababu Taifa hili litaharibika, hili ni Taifa letu wote. Wenzetu wa nje mtu mmoja pekee akipata matatizo Taifa linatetereka. Sasa leo hii tuna vijana wameshikiliwa Kituo cha Polisi kinyume cha Sheria kwa zaidi ya wiki mbili, hakuna mtu anayesema, hakuna Mahakama inayoangalia. Hivi ni nani katika nchi hii yuko juu ya Sheria anayeweza kuwanyanyasa Watanzania kiasi hicho? Halafu Waziri wa Sheria unasimama unatuletea muswada mwingine tunapitisha sheria hazitekelezwi, tunapitisha sheria mwingine anazikanyaga! Inatia aibu na kichefuchefu cha hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilitoka nje wakati unajadili huu muswada nikakutana na Mbunge mmoja rafiki yangu sana akaniambia ninyi mnashambulia Serikali, mnasema Katiba imekanyagwa, sijui nini na nini! Katiba-Katiba nini? Rais ndiye Katiba. Khaa! Nikashangaa! Leo Rais ndiye Katiba? Nikashangaa kweli kweli! Nikamwambia wewe Mheshimiwa Mbunge! Kauli yako hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nimefikia hatua ya kusema wako Wabunge tukichangia sasa tutawataja kwa majina; kwa sababu humu ndani CCM wanakunja mikono, wakiwa nje ni kitu kingine tofauti wanachokisema! Kwa hiyo, mimi nashauri sana tunapotunga hizi sheria tuzijue, wengine si zetu, kwa sababu umri wetu wa kuzitekeleza unakwenda, lakini tujue tunawatungia hizi sheria watoto wetu na kizazi kinachokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo hebu tuiangalie Ibara ya 6 ya Sheria hii. Hivi unaposema taarifa iliyoombwa chini ya sheria hii itachukuliwa kuwa imezuiwa kutolewa ikiwa mamlaka ya umma ambayo inasimamia taarifa hiyo inadai kuizuia kwa taarifa yoyote, au sehemu yoyote ya taarifa, chini ya Kifungu kidogo. Mimi nauliza ni nani katika sheria hii au ni chombo gani katika sheria hii kimewekwa ku-determine kwamba, taarifa hii inakwenda kuingilia usalama wa Taifa, ni nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, kama mimi ni Mkurugenzi, taarifa inaombwa kutoka kwangu. Na mimi naona hii taarifa inakwenda kuharibu kazi yangu ni rahisi kama Polisi wanavyosema sasahivi, taarifa za kiintelijensia zinasema kwamba, msifanye hivi na hivi. Ndiyo maana tunasema Kifungu hiki chote ni kifungu ambacho ninyi Serikali mnataka kutumia kama kichaka kuficha mambo yenu. Hivi ni nani atakaye-determine kwamba, mkataba huu wa kibiashara unakwenda kuingilia maslahi ya nchi? Kama sio ni kichaka tu cha kuficha mikataba ovu ya kifisadi ambayo imeingiwa na Serikali, ambayo hatima yake ni kulihujumu taifa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema wenzangu jana. Uko ufisadi mkubwa kabisa katika nchi hii ambao umeibuliwa na taarifa za kichunguzi. Leo hii tunataka kuzia wale wanaotusaidia kupata taarifa kwasababu tu Serikali inataka kutengeneza kichaka cha kwenda kujibania ili taarifa ambazo wananchi wanapaswa kuzipata wasizipate. Nasema kwamba taarifa inaombwa ndani ya siku 30. Taarifa haiwezi kuwa na maana kama haikutolewa wakati muafaka. Kwahiyo, mimi naungana na wenzangu wanaosema kwamba ibara hii ya sita ni ibara ambayo itaua ule moyo wa wananchi kutoa taarifa na kuisaidia Serikali kupata taarifa mbalimbali ambazo zitasaidia katika mambo ambayo yanaweza kuibua uchunguzi wa mambo mbalimbali katika Taasisi za Umma na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, mimi napendekeza kwamba kifungu hiki cha sita chote kiondolewe au kiandikwe upya kwasababu kina kila vipengele ambavyo ukiona kabisa kwa mantiki yake kinakwenda kuua uhuru wa vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tujue, haki ya kutoa taarifa na kupata taarifa ni haki ya kikatiba; ni haki ambayo wanayo wananchi wote. Leo tunapoweka sheria ya kuwabana wananchi kutoa taarifa maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba ile haki ambayo imetolewa kwenye katiba tunakwenda kuichukua, tunakwenda kuipoka. Kwahiyo, ni rai yangu kwamba muswada huu kwa maoni yangu ni muswada ambao kama kweli nia ni nzuri lazima tukae huu muswada uandikwe upya ili muswada huu uweze kuwa ni wa manufaa kwa taifa hili. Vinginevyo, mimi ninavyouona muswada huu ni muswada ambao unakwenda kuua uhuru wa vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, mimi nimesoma kwenye zile definition kwenye muswada huu. Moja kati ya jambo ambalo limekuwa defined ni kwamba mtu ni raia wa Jamhuri ya Muungano. Lakini sheria yenyewe inasema sheria hii itatumika Tanzania Bara; sasa mimi naungana na wenzangu wanaosema kwamba sasa hapa ule mgogoro ambao tumekuwa tukizungumza kila wakati; mgogoro wa muundo wa muungano hapa ndipo unapokalia. Tunazungumza sheria ya Tanzania Bara lakini Wazanzibar ndio wanatumika kututungia sheria sisi watu watu wa Bara; sheria ambayo wao hawataigusa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama hii sheria ni sheria ambayo tunafikiria kwamba ni nzuri, chukueni hii sheria muipeleke Baraza la Wawakilishi waijadili; ipitishwe kama sheria ya Jamhuri ya Muungano. Vinginevyo ni kitu cha ajabu tumekaa hapa Wazanzibar wanachangia sheria hii kwa nguvu zote na rafiki yangu namuona kule bado kidogo atapewa nafasi atujibu; atachangia kwa nguvu zote kuonesha kwamba hii sheria imepanda imeshuka, lakini haiwahusu, hii inatuhusu sisi. Ndiyo maana tunasema kwamba ile hoja ya muundo wa muungano hapa ndipo mmejikoki (mmejiweka) vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kusema kwamba naomba sana, sisi Wabunge ushabiki tunaoufanya kwa mambo ya msingi mbaya sana, hautatusaidia chochote. Jana liliulizwa swali hapa la kitaifa kabisa, ambalo lilikuwa linatafuta elimu kwa ajili ya watanzania wote lakini limejibiwa kwa ku-personalize yale majibu kulingana na muuliza swali; tunakwenda wapi? Na hata hii sheria sisi tunajua finally sheria hii itapita, itapita kwasababu ninyi mlio wengi mmeamua kwamba itapita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini huko mbele ya safari; jana kuna watu walikumbushwa hapa, walikumbushwa habari ya viongozi waliotoka huko wakaja huku. Nawakumbusha habari ya Chiluba; sheria alizounda baadae zikaja zikam-cost yeye mwenyewe. Tuangalie kwasababu hakuna mtu ambaye anajua kesho itakuwa namna gani. Tujadili tukijua kwamba tunajadili kwa manufaa ya nchi yetu, na hii nchi ni yetu wote, na sana sana sisi tuliopewa dhamana tumepewa dhamana hii kwa ajili ya watanzania wengi ambao hawakupata nafasi ya kufika humu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikushukuru na nikupongeze kwamba finally umekuja kutusaidia kukaa hapo kuongoza Bunge letu; tunajisikia vizuri sana, tunakupongeza sana. Asante sana!
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ninamshkuru sana na Mheshimiwa Gekul kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya maji ni mbaya, jana nilikuwa nasikiliza vyombo vya habari vya Kimataifa, watabiri wanasema Vita ya Tatu ya Dunia itatokana na upungufu wa maji katika dunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba pale Rombo Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu Waziri wa Maji mmekuwa maarufu sana kwa Warombo, sababu ni tamko lenu la kuifuta Kili water. Baada ya kutoa tamko la kuifuta Kili water iliyowanyanyasa Warombo kwa ajili ya maji kwa miaka mingi sana, walikuwa wana matumaini makubwa sana sasa kuna jambo litafanyika tuweze kuwa na mamlaka yetu ili tuweze kuratibu matumizi ya maji kidogo tuliyonayo pale Rombo. Mheshimiwa Waziri nawaombeni sana hili jambo liweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba shida ni kubwa kuliko miaka mingine yote. Hivi ninavyozungumza ukame umeleta athari kubwa sana, vyanzo vidogo vya maji ambavyo tulikuwa navyo sasa vinatoa maji asilimia ndogo kabisa. Mheshimiwa Waziri bahati mbaya sana visima ambavyo tulivipata kutokana na mradi ule wa visima kumi vya World Bank mpaka sasa hivi miundombinu yake bado haijakamilika kutokana na ukosefu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kisima kwa mfano cha Shimbi Mashariki, visima kwa mfano vya Leto na vinginevyo maji yamepatikana lakini usambazaji umekuwa shida kwa sababu fedha hazijapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna imani na nyinyi kama nilivyowaambia baada ya kuifinya Kili water tumejenga imani kubwa sana na ninyi tusaidieni, kwa sababu hata huu utaratibu wa Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia maji, own source ndogo haiwezi kufanya Halmashauri ikapata fedha ya kutenga kwa ajili ya kusaidia miradi ya maji. Kwa hiyo, ni matumaini yangu Mheshimiwa Waziri hilo utalichukulia kwa uzito mkubwa na pale Rombo pana Ziwa Chala ambalo lina maji, maji yale yanatumika na wenzetu Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliuliza swali hapa nikajibiwa wakati huo Waziri Maghembe akiwa Waziri wa Maji kwamba maji ya Ziwa Chala ni maji ya Kimataifa, kwa hiyo, kuna mikataba ambayo lazima iangaliwe. Tunachoshangaa watu wa Rombo maji ya Ziwa Chala yanatumika Kenya, kwa nini yasitumike Rombo? Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri muangalie uwezekano haya maziwa yaweze kutumika pia kusaidia watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ningependa kulizungumza ni kwa Waziri wa Mifugo na bahati nzuri amekaa jirani na Waziri wa Viwanda.
Nimesikia sana huku Bungeni kwamba wafugaji wapunguze mifugo na kadhalika, waipunguzie wapi? Kwa sababu hakuna viwanda vya nyama hapa nchini, ng’ombe jinsi alivyo nyama ni pesa, ngozi ni pesa, kwato ni pesa na mifupa ni pesa. Kwa nini tusianzie hapo? Mheshimiwa Waziri teta na mwenzako upo jirani naye hapo alete viwanda kwa ajili ya mazao ya mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mwijage kama alivyotueleza jana pale yuko sharp, ng’ombe zikiwa na afya huwa zinavuka Ngorongoro zinaenda kiwanda cha nyama Thika Kenya, huu ni ukweli kabisa, lakini sisi tumekaa hapa tunapiga hadithi tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tulivyounda ile Kamati ya Migogoro ya Wakulima na Wafugaji tulipita vijijini, wafugaji wanatuambia kuna shamba darasa la kilimo mbona hatujawahi kuona shamba darasa la mifugo? Kwa hiyo, mimi pamoja na kwamba siyo mfugaji kwa ile maana ya ufugaji tunayoijua, lakini naona migogoro mingine ya wafugaji na wakulima inatokana na kutofanya maamuzi ya kusaidia haya makundi ili yakafanya mambo kitaalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rai yangu juzi nilikuwa natoka kumzika Kaka yake na Mheshimiwa Cecilia Pareso. Pori hilo kutoka Minjingu mpaka Makuyuni ni harufu ya uvundo ng’ombe wamekufa, Simanjiro yote ni harufu ya mizoga ya ng’ombe. Kwa hiyo ni vizuri…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Selasini.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Rombo hatuna Hospitali ya Wilaya. Hata hivyo Kituo cha Afya cha Karume Usseri kinaandaliwa kwa ajili hiyo. Hivi sasa majengo yote muhimu yapo tayari kasoro jengo la OPD ambalo ujenzi wake uko ngazi ya msingi. Ujenzi umesimama kwa sababu ya deni tunalodaiwa na mkandarasi. Tunaiomba Serikali kutusaidia kumalizia deni hilo na kutoa pesa ili kuharakisha ujenzi wa jengo hilo ili hospitali ipate kufunguliwa na hatimaye kuondoa kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika wananchi wamejitahidi sana kujenga kwa kujitolea zahanati na vituo vya afya. Hata hivyo tunakabiliwa na matatizo mawili ambayo ni wataalamu, madaktari, wahudumu wengine wa afya pamoja na vitendea kazi. Tunaiomba Serikali katika mgao wa wahudumu na vitendea kazi itufikirie ili nguvu za wananchi walizojitolea katika kujenga ziwe na manufaa kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunacho Kituo cha Maendeleo ya Wananchi Mamtukuna. Chuo hiki ni muhimu sana lakini kunakwamishwa na matatizo ya uhaba wa wataalamu (wakufunzi), uchakavu wa majengo, maji pamoja na bajeti ndogo. Tunaiomba Serikali isikiache chuo hiki ikitengee fedha za kutosha walau kutatua kwa awamu matatizo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa kumezuka mtindo wa kuwadhalilisha sana watoto wa kike na wa kiume. Baadhi wanaingiliwa, wanaolewa wakiwa na umri mdogo na kufanyishwa kazi ambazo haziendani na umri wao. Imefikia wakati Serikali ichukue hatua thabiti kuzuia mateso haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni ujenzi wa jengo kwa ajili ya installation ya mashine za kansa katika Hopitali ya KCMC. Hospitali pamoja na wafadhili wameshafanya kazi kubwa sana, gharama ya ujenzi wa jengo hilo ni karibu bilioni sita. Kutokana na kuzidiwa kwa taasisi ya kansa Ocean Road na kutokana na wingi wa wagonjwa na mahitaji ya upimaji kwa wananchi, tunaiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kusaidia ujenzi wa jengo hili.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi nataka kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kumteua Kamishna wa Tume ya Kuzua Dawa za Kulevya. Hiki ndicho kilikuwa kilio cha Wabunge. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge walikuwa wanapiga kelele mambo ya nchi yaendeshwe kwa mujibu wa sheria na kwa sababu sisi ndiyo watunzi wa sheria ilikuwa ni muhimu kupiga kelele ili sheria iweze kufuata mkondo wake. Haikuwa dhamira ya Mbunge yeyote aliyesimama katika Bunge hili ku-challenge utaratibu uliokuwa unatumika na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, haikuwa dhamira ya Mbunge yoyote kubeza kazi ambayo ilikuwa inafanyika na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini dhamira ya Wabunge ilikuwa kilio cha kufuata taratibu ambazo nchi imejiwekea. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukiruhusu Nchi hii ikiendeshwa kwa viongozi wake kuvunja sheria tutaichana chana vipande vipande nchi yetu. Tunayo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambayo tunaamini viongozi wake. Waziri wa Mambo ya Ndani, Katibu Mkuu na wengine wote wanaendesha Wizara ile kwa taratibu ambazo zimewekwa. Kwa hiyo, lilikuwa ni jambo la kusikitisha kusikia Mkuu wa Mkoa anatamka kama vile yeye ni Arresting Officer, watu waende wakaripoti kwake. Kila mtu mwenye akili na fahamu sawasawa, lazima alikuwa anapaswa ashangae. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninachosema, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alichokifanya pamoja na kwamba dhamira yake pengine kwa viwango vyake ilikuwa sahihi, lakini viongozi wa nchi yetu wasipodhibiti vitendo vya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bwana Makonda na wengine wa aina hiyo, nchi hii inakwenda kupasuka. Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi ukasimama tu ukamtuhumu Askofu na Kanisa lake kwa sababu kumtuhumu Askofu ni kutuhumu Kanisa zima, ni kutuhumu wenye imani hiyo, ni kuleta fujo! Huwezi kumtuhumu mtu halafu ukasema kwamba tutampekua halafu tukigundua kwamba hana tatizo tutamuachia. Umeshamchafua, utamsafisha namna gani? DCI ndiyo ana mamlaka ya kufanya upelelezi katika Jeshi la Polisi na anasimamia makachero wote. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini vita ya madawa ya kulevya imekuwa ikiendelea kwa miongo yote ya utawala wa nchi hii kwa hatua mbalimbali. Alikuja Waziri Kitwanga hapa akatuambia ana majina 550, nina imani Mheshimiwa Mwigulu halali na hajalala anaendelea kufanya kazi hiyo, anaendelea kufanya shughuli hiyo. Isije ikajengwa hoja kwamba sasa Makonda anafanya kazi kuliko Waziri Mwigulu. Waziri Mwigulu anafanya kazi hiyo, DCI anafanya kazi hiyo lakini kiherehere cha baadhi ya viongozi vijana watafanya kazi hii isiendelee sawasawa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo makubwa sana ya kutia shaka. Iko tuhuma inajengwa na bila shaka mmekwishaisikia kwamba Mheshimiwa Makonda sasa ana utajiri mkubwa kuliko umri wa kukaa kwake madarakani. Tunasikia amenunua apartment pale Viva Tower ya shilingi milioni 600. Mheshimiwa Rais umeingia madarakani kwa ahadi ya kwamba unapiga vita rushwa, huyu anatuhumiwa kwa kununua apartment kwa shilingi milioni 600, siamini kama Rais utakaa kimya. Vilevile Makonda huyu huyu anatuhumiwa amempa zawadi ya birthday yake mke wake Benz ya dola 250,000 sawa na shilingi milioni 400, hatuwezi kukaa kimya lazima tuseme. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu huyu Makonda, Rais amezuia safari za Mawaziri, safari za Wabunge lakini amekwenda Ufaransa na mke wake, ameingia kwenye ndege daraja la business class dola 7,000, yeye na mke wake wamekaa siku 21. Kwa nini tusifikirie kwamba kitendo cha Makonda kutangaza hadharani watu ambao nafikiri anawatumia ilikuwa ni mkakati wa kufanya wauza madawa ya kulevya wakimbie ndani ya nchi? Kwa sababu sasa hivi ni muuza madawa gani mjinga ambaye amebaki katika nchi hii? Maana yake ni kwamba Makonda amesaidia wauza unga kuondoka katika nchi hii. Kwa sababu inawezekana Makonda anashirikiana nao na ndiyo maana sasa ana utajiri huu mkubwa kiasi hiki. (Makofi)
Mheshimiwa MWenyekiti, rai yangu ni kuwaomba viongozi wa Jeshi la Polisi, Kamishna Siro leo ameibuka anasema Mbowe asipokuja tutamfuata. Siro unamfuata kwa summons ipi uliyompa? Mpe summons kwa mujibu wa sheria ili aende. Kwa sababu sasa hivi kuna kiherehere tu, kila mtu anajifanya anafanya mambo sijui kwa namna gani anavizia uteuzi au Siro unataka u-IGP? Lazima tuseme kwa sababu hakuna mtu ambaye anaunga mkono madawa ya kulevya. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja niwaambie Waheshimiwa Wabunge, mimi nina mtoto muathirika. Kwa hiyo, kama kuna mwenye uchungu, mimi nina uchungu kweli kweli, tena tangu darasa la nne lakini Makonda asivuruge vita hii, sisi tunataka hawa watu wakamatwe. Watu hawa hawawezi kukamatwa kwa kuropoka, hawawezi kukamatwa kwa kujisifu, hawawezi kukamatwa kwa majigambo! (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa viongozi, sisi tunataka succession ya uongozi, watu wazima tunaondoka vijana waingie. Mimi namshauri Rais, vijana anaoingiza madarakani aangalie busara yao. Tulizungumza hapa juu ya DC Mnyeti yule wa Arumeru, lakini leo kwenye mtandao kuna habari DC alikaa hotelini na Afisa Sheria wa Arumeru anamwambia Rais, bwana mkubwa alinipigia simu ananiambia usiwe na wasiwasi fanya kazi, hawa Wabunge wajinga tu – hee! Hapo ndipo tulipofikia Waheshimiwa Wabunge. Makonda anaenda kwa wafanyabiashara, anampigia Rais simu halafu anaweka loud speaker ili wafanyabiashara wasikie Rais anavyowasiliana naye. Wale wote waliokuwa wanashughulikiwa kwa kukwepa kodi leo ndiyo marafiki wa Makonda. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Boniphace Getere alisema hapa, tuache mambo ya CHADEMA na CCM, tujenge nchi. Wabunge tuwe wakali kusimamia sheria za nchi hii, kusimamia principles, nchi yetu isonge mbele. Kama kuna ukweli tuseme kwa sababu matatizo yakitokea CCM haitapona wala CHADEMA hatutapona. Nchi hii ikipasuka CCM haitapona, CHADEMA haitapona. Nchi hii ina hierarchy ya uongozi, haiwezekani Siro am-supersede DCI, haiwezekani, iko wapi, kwa sababu Jeshi linaenda kwa command! Sasa DCI anachunguza madawa ya kulevya, Siro anachunguza madawa ya kulevya kwa amri ya Makonda, DCI anashirikiana na Waziri, fujo! Jeshi likiwa na fujo linasambaratika. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo niseme tu kwamba sisi Watanzania kwa ujumla wetu tunajua madhara ya madawa ya kulevya, hakuna asiyejua! CCM mnajua, CHADEMA mnajua, Watanzania wote mnajua. Watoto wetu wanaathirika, watoto wetu wanakuwa na tabia za ajabu ajabu. Tushirikiane ili vita hii iweze kufanikiwa lakini vita hii isiende kwa majigambo ya mtu mmoja ambaye anajifanya yeye ni bora na anaweza kupigana hii vita peke yake, hawezi! Atawaacha wale wanaohusika wakikimbia halafu matokeo yake vita itaishia njiani. Nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia, naomba nichukue nafasi hii kuwatakia Wakristo wote walio hapa Bungeni na kote Tanzania kila la kheri katika siku hizi kuu za Juma kuu zitakazoanza kesho ili ziwe kwao baraka na neema katika maisha na kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda kusema kwamba, mimi ni Mbunge wa Rombo na katika siku mbili, tatu zilizopita jina la Ben Sanane limetajwa sana hapa Bungeni. Ben Sanane ni mpiga kura wangu, amezaliwa Tarafa ya Mashati, Kata ya Katangara Mrere, Kijiji cha Mrere na Kitongoji cha Kilosanjo.
Baba yake ni Mzee Focus Benard Sanane na mama yake ni mama Arinata Ben Sanane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Rombo tuna uchungu wa hali ya juu sana kwa sababu tangu jambo hili liliporipotiwa watu wa Rombo hususan familia na ukoo wa Mzee Focus Ben Sanane umetahayari, hawajui wafanye matanga, hawajui wafanye nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea kusema ninachokusudia kusema kuhusu jambo hili, nichukue nafasi hii kwa niaba ya Mzee Focus Benard Sanane na Mama Arinata Benard Sanane kutoa shukrani za dhati kwa Wabunge wote, vyombo vya habari, viongozi wote na wote wenye mapenzi mema ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakiomba, wakishinikiza, wakishauri kwamba jambo hili lifanyiwe kazi na Serikali ili tujue mwisho wake. Waheshimiwa Wabunge sisi wote ni wazazi, akinamama mlio Wabunge mnajua uchungu wa uzazi…
Mnajua uchungu ambao mama Arinata Benard Sanane anaupata. Mheshimiwa Jenista Mhagama dada yangu, fikiria kwa mfano yule
mwanangu Victor angekuwa amekumbwa na sakata kama hili, ungekuwa katika hali gani, unatikisa kichwa kwa
uchungu kwa sababu huu ndiyo uchungu ambao watu wa Rombo wanao, huu ndiyo uchungu ambao mama Arinata anao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Oktoba mwaka jana, kuna mtu aliyejitambulisha kama Joackim, Afisa wa Takwimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo. Alikwenda kwenye Ofisi za CHADEMA pale Wilayani. Baada ya kujitambulisha, akaomba kujua kama Ben Sanane ni mwanachama wa CHADEMA. Akaomba kujua kama Ben Sanane huwa anafika maramara katika Ofisi za CHADEMA. Akaomba kujua nyumbani kwa Ben Sanane na baada kukusanya taarifa alizozitaka mwezi wa Novemba tukasikia kupotea kwake, tupo katika lindi kubwa la mashaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo, niishie tu kusema nawaomba Wabunge, naiomba Serikali, nawaomba na Watanzania wote msifanye jambo hili kuwa jambo la siasa. Jambo hili linaumiza watu, jambo hili lina machungu makubwa miongoni mwa mioyo ya watu.
Nawaomba na nawasihi na Warombo wenzangu wananisikia na familia ya Ben, Mzee Focus na Mama Arinata wananisikia, tunaomba sisi watu wa Rombo Serikali tuambieni chochote ambacho mnacho.
Tuambieni kama mmeshindwa tulie, yaishe. Tuambieni kwamba amekufa ili tujue tufanye matanga. Haiwezekani tukakaa kama familia kwenye suspense tu hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nirudi kwa Warombo wenzangu katika mambo mengine ya maendeleo yanayowahusu. Katika kipindi hiki cha mwaka, tulipata bahati ya kutembelewa na Waziri wa Mambo ya Ndani pamoja na Naibu wake, waliutembelea mpaka wa Rombo pamoja na shughuli zinazohusu Wizara ya Mambo ya Ndani. Nataka niwashukuru kwa sababu tuumeendelea kutekeleza yale waliyoshauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sababu ya urefu wa mpaka wa Rombo na Kenya, watu wa Rombo wameamua kujenga kwa namna ya kujitolea vituo vya polisi.
Kituo cha Ngoyoni, Mahida, Mengwe, Useri na Kirongo Chini. Wamejenga na wanaendelea kujenga kwa kuchangia ili waweze kukaa katika hali ya usalama kwa sababu mpaka unaingiza mambo mengi na unawahusu sana katika usalama wao. Naiomba Serikali katika bajeti hii iangalie namna ya kusaidia hizi nguvu za wananchi ili hivi vituo viweze kukamilika tuweze kupata huo msaada au tuweze kupata hiyo huduma
kutoka polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Naibu Waziri TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo pia alitembelea Rombo na tunamshukuru. Alitembelea miradi kadhaa, kati ya mradi uliotembelewa ni ujenzi wa jengo la halmashauri. Nimesikia Wabunge wenzangu ambao halmashauri zao ni mpya wakiomba
majengo ya halmashauri yajengwe na yakamilike. Rombo ni halmashauri ambayo ina umri zaidi ya miaka 30 lakini haina jengo la halmashauri. Jengo wanalotumia lilitaifishwa kutoka kwa Masista wa Shirika la Masista Kilimanjaro. Ujenzi unaendelea lakini umekwama kwa sababu mkandarasi amekosa fedha. Tunaomba fedha zipelekwe ili kuweza kukwamua ujenzi ambao unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni Hospitali ya Wilaya. Vilevile hatuna Hospitali ya Wilaya.
Hospitali ya Huruma ni Hospitali ya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi. Kituo cha afya cha Karume tuliamua kwa makusudi ijengwe hapo Hospitali ya Wilaya, ujenzi unaendelea nao umekwama kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Naomba sana jitihada zifanyike ili jengo hilo liweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maji. Waziri wa Maji ametusaidia kuifuta Kill Water. Namshukuru Waziri na nimpe taarifa tu kwamba wataalam kwa ajili ya kutusaidia kuanzisha mamlaka wameshafika Rombo wanaendelea na kazi. Naomba msukumo uweze kufanyika ili tupate hiyo
mamlaka, kwa Rombo kuna shida kubwa sana ya maji hasa ukanda wa chini. Mamlaka itatusaidia kwa sababu kuna chanzo cha Ziwa Chala, kuna vyanzo vingine kule Rongai ambavyo tunaambiwa vinapeleka maji Kenya ili kuweza kutatua tatizo la maji katika halmashauri yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu afya, ni wataalam katika vituo vya afya. Kwa sababu wananchi wa Rombo wamejitahidi kujenga zahanati na kadhalika tunaomba sana waungwe mkono katika hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, tuna uhaba mkubwa sana wa walimu wa sayansi. Rombo tuna shule za kata karibu 41 lakini tangu tumeanza shule za kata hatuwahi kupata mwalimu hata mmoja wa sayansi katika baadhi ya shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maliasili, tunavamiwa sana na nyani, ukanda wa juu. Nimesikia kuna utaratibu wa kuhamisha nyani na kuwapeleka mahali pengine. Tunaomba Serikali ione uwezekano wa kuwasaidia hawa wananchi ambao wanapambana na nyani kila kukicha, wanashindwa kufanya kazi zao kwa sababu ya kupambana na nyani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala la njaa. Rombo kwa kawaida tunapata chakula kutokana na mvua za vuli lakini mvua za vuli mwaka huu hazijanyesha. Kwa hiyo, ukanda wa chini wa Rombo sio siri wananchi wana shida kubwa sana ya chakula. Mimi sijatembelea mikoa
mingine Serikali inasema nchi ina chakula, naomba ufanyike utaratibu chakula kilicho katika maeneo mengine ya nchi kiweze kusambazwa ili kusaidia wananchi wa maeneo mengine hususan katika Jimbo langu la Rombo. Watu wa Rombo siyo wavivu, akinamama wanalima kila wanapopata fursa lakini jambo ambalo limetufanya tukaingia katika hali hiyo kwa Ukanda wa Chini ni kwa sababu ya hali ya ukame,
mvua hazikunyesha tukapata shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni zao la kahawa ambalo lilikuwa zao la biashara katika Wilaya ya Rombo. Chama cha Ushirika KNCU kilitusaidia sana, lakini kimeingiliwa na mafisadi, wanauza mali za KNCU, wameuza
magari, nyumba na rasilimali zote za KNCU hatimaye wameshindwa kulisaidia zao lile. Matokeo yake gharama za uzalishaji wa zao lile zimekuwa kubwa, kodi imekuwa kubwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti,
ahsante sana, naomba sana Serikali itusaidie katika hayo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JOSEPH R.SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Kilimo inaajiri
wananchi wengi katika nchi yetu. Vilevile katika azma ya Serikali ya kukuza viwanda ipo haja kubwa ya kuimarisha sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao mengi ya biashara yanaelekea kukosa msukumo na wakulima kuyaacha. Hali hii inatokana na Serikali kuweka bajeti ndogo katika kilimo na hivyo kuifanya sekta hii kushindwa kuhudumia kilimo chetu. Hivyo, naomba:-
(i) Taasisi za Kilimo za Utafiti wa Dawa, Pembejeo na Mbolea lazima ziimarishwe kwa kupewa fedha za kutosha.
(ii) Bodi za Mazao haya kama Kahawa, Tumbaku, Pamba na kadhalika ziimarishwe ili kuweza kusimamia vyema mazao haya.
(iii) Tafiti za masoko ambayo yatawanufaisha wakulima kwa kuwapatia bei nzuri zifanyike.
(iv) Uhamasishaji ufanyike ili wakulima waendelee kuzalisha mazao haya kwa kuwa maeneo mengi hasa yanayolima kahawa wananchi wanaelekea kukata tamaa.
(v) Kuhusu mazao mchanganyiko Bodi ya Mazao Mchanganyiko iimarishwe.
(vi) Uhamasishaji ufanyike ili mazao yetu yaongezewe thamani ili kuyaongezea bili na pia kuongeza ajira kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika ni vema sasa kama nchi tuachane na kilimo cha msimu kwa kutegemea mvua na badala yake tuimarishe kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Jimbo langu la Rombo wananchi wamekata tamaa sana katika kuzalisha zao la kahawa. Hii ni kutokana na gharama kubwa za
uzalishaji na bei kuwa ndogo; hali kadhalika kuyumba kwa Vyama vya Ushirika hasa KNCU. Mali na mashamba ya KNCU yameuzwa kiholela bila kuwashirikisha wanachama. Naiomba Serikali kuingilia kati ili kunusuru mali na mashamba
ya KNCU ili kuifanya iwe na nguvu na uwezo wa kulisimamia zao hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya maji nchini katika majimbo yote ni mbaya sana. Katika Jimbo langu la Rombo wananchi wanateseka sana na ukosefu wa maji. Vyanzo vingi vimekauka na maji yananunuliwa kwa sh. 1000 – 1500 kwa dumu la lita 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi iliyoanzishwa, mfano Mradi wa Shimbi Mashariki na Leto. Miradi hii inasuasua kwa sababu ya fedha kutopelekwa kwa wakati. Kama miradi hii ikikamilika itasaidia kwa kiwango fulani kuatua shida hii
katika maeneo ya mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa water table katika jimbo langu ni zaidi ya mita 300 na kuondoa uwezekano wa visima kuchimbwa katika maeneo mengi, hapa Bungeni Wabunge wote wa Rombo walionitangulia wameleta mapendekezo ya matumizi ya maji ya Ziwa Chala.
Tumekuwa tukipata matumaini miaka yote. Tunaomba sasa
suala hili lifikie mwisho. Ni lini maji ya Ziwa Chala yataanza
kutumika kwa ajili ya wananchi wa Rombo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kuhusu maji tuliomba ianzishwe Mamlaka ya Maji ya Wilaya ya Rombo.
Tunaomba kujua ni lini mchakato huu utakakamilka ili mgao wa maji kidogo tuliyonayo uwanufaishe wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu afya, hivi sasa tuna mchakato wa ujenzi wa jengo la OPD katika Kituo cha Afya Karume ili kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Hivi sasa ujenzi umesimama kutokana na Mkandarasi kutudai. Tunaiomba Serikali katika bajeti hii kutupatia fedha za kukamilisha ujenzi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuna Mradi wa Ujenzi wa jengo la Halmashauri. Hii ni halmashauri kongwe ambayo ina zaidi ya miaka 30, lakini hatuna jengo la halmashauri. Tunaomba katika bajeti fedha zipatikane ili ujenzi uendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu tuna uhaba mkubwa wa Walimu wa sayansi. Tunaiomba Serikali katika mgawo wote wa Walimu wa sayansi tupatiwe kiasi cha
kuweza kutusaidia. Zipo shule ambazo tangu zimeanzishwa hadi leo hazina Mwalimu hata mmoja wa somo lolote la sayansi.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie katika hoja hii iliyo mbele yetu. Kwanza kabisa ningependa kuzungumzia ujenzi wa Hospitali ya Serikali ya Wilaya ya Rombo. Wilaya ya Rombo ni Wilaya Kongwe lakini katika umri wake wote haijawahi kuwa na Hospitali ya Wilaya. Hospitali ambayo tunatumia ni Hospitali ya Huruma ambayo Meneja wake ni Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Moshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali inayojengwa sasa hivi katika Kituo cha Afya Karume tumejitahidi, tayari tumekamilisha wodi zote tuna Theater tuna Mochwari lakini tunasumbuliwa na fedha za kumalizia jengo la OPD. Ujenzi umeshaanza, msingi umeshakamilika, lakini sasa hivi mkandarasi amesimama kwa sababu tumeshindwa kumlipa. Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI alitembelea jengo hili na alitoa ahadi kutusaidia. Nataka tu ku-register maombi haya pia kwa Wizara ambayo ndiyo inasimamia sera, mtusaidie ili jengo hili liweze kumalizika tuweze kuwa na hospitali ambayo itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Huruma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambasamba na hilo ningepeda kuzungumzia hitaji la watumishi kama wenzangu walivyozungumza. Tuna matatizo makubwa sana ya watumishi katika sekta ya afya kwenye Jimbo la Rombo, kuanzia Madaktari, Manesi na watumishi wengine. Wananchi
wa Rombo wamejitahidi sana kwa nguvu zao kujenga zahanati katika vijiji mbalimbali, lakini sasa ujenzi wa zahanati hizi ambazo nyingine zimekamilika na nyingine zinaendelea na ujenzi, tunapata shida kwa sababu tunawahamasisha wajenge, lakini hakuna wataalam. Kwa hiyo, ningemwomba dada yangu Ummy atakapopata fursa pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Utumishi kwa ajili ya kuwaajiri watumishi wa sekta ya afya atukumbuke Jimbo la Rombo kwa ajili ya Madaktari na Manesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuzungumzia Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Mamtukuna, Mheshimiwa dada yangu Ummy alifika pale anakifahamu kile chuo, tunahitaji kubwa sana la watumishi Walimu na bajeti yake ni ndogo na kile Chuo kinasaidia sana. Tunaomba sana kama Wizara wanaweza wakaendelea kukitunza na kukiangalia kile chuo ili kuweza kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ningependa kuzungumzia ujenzi wa jengo kwa ajili ya vifaa vya kansa pale Hospitali ya KCMC. Jitihada zimefanywa na wafadhili, jitihada zimefanywa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, kwa ajili ya kuhakikisha kumekuwa na kituo ambacho kitasaidia pia kupunguza msongamano katika Taasisi ya Kansa ya Ocean Road.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana fedha ambazo zinahitajika kwa ajili ya lile jengo ni kama bilioni sita hivi, ambazo kwa kweli kwa hapo tulipofikia KCMC ina mzigo mkubwa sana na vifaa vimeshapatikana. Kwa hiyo ningeiomba Serikali, tusiache hivi vifaa mwishoni wafadhili wavitumie kwa namna nyingine, tungeomba sana muwasaidie jengo hili liweze kukamilika ili taasisi ile iweze kusaidia Taasisi ya Kansa ya Ocean road ili wananchi wenye matatizo ya kansa ambao sasa hivi ni wengi waweze kupata nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ambayo yameendelea kuzungumzwa ya unyanyasaji wa watoto, wazee na kadhalika, ningeomba sana Wizara iweke msisitizo kwa sababu hili na lenyewe ni tatizo ambalo ni cross cutting, liko karibu katika kila eneo. Ni kweli watoto wanadhalilishwa, ni ukweli kuna watu ambao wakishafanya mambo kama haya wanaachwa mitaani kiholela. Ningeomba sana Wizara iweke msisitizo katika jambo hili ili watoto wetu wawe salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, hayo ndiyo nilikuwa nayo.
Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa fursa hii ndogo ili na mimi nichangie hoja hii. Kama walivyofanya wenzangu, nampongeza Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kazi ambayo wamefanya katika Wizara, ni nzuri ndiyo maana wanapongezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hotuba ya Waziri ukurasa wa 34 kuna hoja hii inayohusu mipaka ya kimataifa, hili ndilo jambo lililonifanya nisimame. Kwanza nimshukuru sana Waziri kwa kuliongelea jambo hili kwa sababu jambo hili limeleta sintofahamu kubwa sana kwa wananchi wangu wa Rombo eneo la Kikelelwa mpaka Nayeme. Wananchi wamewekewa nyumba zao X kwa hoja kwamba wanahamishwa kutoka mpakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa sababu nimefuatilia jambo hili na Waziri ameniweka wazi, kwamba Serikali ya mkoa ina mipango yake ya ulinzi na usalama. Sikatai kuhusu hiyo mipango lakini linapokuja suala linalohusu ardhi ningeomba sana Serikali za Mikoa zihusishe Wizara, kwa sababu sasa hivi wananchi wa Kikelelwa, Tarakea na Nayeme wengine sasa hivi wanaanguka kwa presha, wengine wanawaza kwenda mahakamani kwa sababu ya tishio la kubomolewa nyumba zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri wananchi hawa wameishi katika haya maeneo kabla ya uhuru na kwa sababu hiyo kuwawekea X sasa hivi ni sawa sawa na kuwapa hukumu ya kifo. Naomba ieleweke Rombo hatuna ardhi, hivi sasa hivi tunawaza namna ya kujenga hata taasisi za umma hatuna ardhi, hatuna hata maeneo ya viwanja vya michezo. Kwa hiyo jambo linalohusu ardhi katika Wilaya ya Rombo lisichukuliwe tu kwa mihemko kwa sababu ni jambo hatari na linaweza likasababisha maumivu makubwa sana kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, Mheshimiwa Waziri nashukuru na nimwombe atakapohitimisha hoja yake aseme kitu ambacho kitawapa comfort wananchi wa Nayeme, Tarakea na Kikelelwa ili waweze kupata utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze jambo lingine linalohusu ardhi. Mheshimiwa Waziri pale Rombo kuna eneo la Chala. Lile eneo ni ardhi ambayo wazee wanaotoka Kata za Holili, Mahida, Chala, Mengwe, Mamsera na Kata ya Manda walipewa na Land Board zamani, wanazo risiti walikuwa wanalipia hiyo ardhi, lakini sasa hivi kuna watu wamepewa ile ardhi kinyemela. Kinachotokea wananchi hata wakiingia katika lile eneo wengine wanapigwa, wengine wanakamatwa na kadhalika. Namwomba Mheshimiwa Waziri aje Rombo tukatembelee lile eneo, aseme kitu cha kuwapa comfort wananchi wa maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba pamoja na uhaba wetu wa ardhi tuna Miji ya Tarakea, Mkuu pamoja na Mji wa Holili, ni miji ambayo inapanuka lakini inapanuka hovyo kwa sababu hatuna fedha kwa ajili ya kulipa fidia. Mnajua matatizo ya ardhi kwetu tunazika katika mashamba yetu humo humo, kwa hiyo ukiamua kumwondoa mtu fidia yake ni kubwa kwa sababu unafidia mpaka makaburi, sasa ile miji inadumaa. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, Halmashauri hawana uwezo lakini wameomba awasaidie bilioni moja kwenye ile taasisi yake wapime, wananchi wapo tayari kununua hivyo viwanja na kurejesha fedha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalize kwa kusema kuhusu migogoro hii ya ardhi. Sisi ambao hatuna ardhi tunaomba hii migogoro iishe kwa sababu tuna hakika ardhi hii ikipimwa kwa sababu na sisi ni Watanzania, vijana wetu wa Rombo nao wanaweza wakapata ardhi katika maeneo mengine. Nilikuwa katika Kamati ya Bunge iliyochunguza migogoro ya ardhi. Wako watu waliopewa mashamba makubwa kwa maana ya uwekezaji, wengine wameyakodisha. Tulienda Kilosa hapa tukakuta Mchina ana shamba anakodisha watu; tumemkuta Mwenyekiti wa Halmashauri hapo ana shamba, anakodisha watu

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa dakika tano na mimi niseme machache kuhusu Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutumia muda wangu vizuri, niseme tu kwamba naunga mkono kwa asilimia mia moja hotuba ya Kambi, hotuba ya Mheshimiwa Lema na hotuba ya Mheshimiwa Peter Serukamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme jambo ambalo kwa kweli ningelizungumza kwenye briefing wakati tukitengeneza ratiba ya Mkutano huu wa Bajeti. Bajeti ni kuhusu mapato na matumizi, kwa muda wa siku 90, Wabunge tunakaa hapa kupanga matumizi lakini tukimaliza hizo siku 90 tunapewa siku moja au mbili kuzungumza habari ya mapato. Kwa jinsi hii sioni ni namna gani sisi Wabunge tunaishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu wa Mabunge mengine ukienda Bunge la Kenya hapa, juzi Kamati ya Bajeti ilikuwa Finland, ukienda Bunge la Uingereza muda wa kujadili vyanzo vya mapato katika nchi ni mkubwa sana Bungeni kuliko muda wa kujadili matumizi. Sasa sisi tunajadili matumizi ambayo hatujui tutayapata wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama Makinda alianza vizuri na Bunge la Tano, aliunda Kamati ile tuliita Chenge One ilitoa mawazo, ilitoa mapendekezo namna ya kuongeza vyanzo vipya vya mapato lakini sisi kila mmoja wetu analalamika, kila mmoja wetu anataka mradi lakini ukweli ambao tunauona sasa hivi Mheshimiwa Mpango tunamwonea pesa zipo wapi? Kwa hiyo, lazima tuamue, Bunge litengeneze ratiba inayofaa tupate muda wa kutosha kuweza kuishauri Serikali kuhusu vyanzo vya mapato, hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ambalo napenda kulisema ni kuhusu vyanzo ambavyo tayari tunavyo. Bunge lililopita tulifanya uamuzi wa makusudi kunyang’anya property tax kwenye Halmashauri na kuwapa TRA. Kwa mfano Jiji la Dar es Salaam walikuwa wameweka maoteo ya Sh.33,100,000,000/=, lakini katika uhalisia wamekusanya shilingi bilioni 6.5 tu ina maana shilingi bilioni 26.59 hazikukusanywa na TRA, jambo ambalo Halmashauri na Majiji wangeachiwa kukusanya zile fedha pengine zingepatikana fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo Hazina imeendelea kutoa pesa kwa ajili ya Jiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tuufikirie huu uamuzi wa kuchukua chanzo hiki cha mapato kutoka Majiji na Halmashauri na kukipeleka TRA, tuwarudishie Majiji na Halmashauri ili fedha ambazo zingeenda kwenye miradi ya maendeleo kwenye Majiji na Halmashauri kutoka Hazina zisiende na pengine haya majiji yanaweza kusaidia Hazina katika mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo napenda kuchangia ni kuhusu Tume ya Mipango. Ni ushauri wa Kamati ya Bajeti, ni ushauri wa wengi hapa, Tume ya Mipango irudi Ofisi ya Rais au iundiwe Wizara. Sababu ni kwamba Tume ya Mipango imeenda imejificha pale Hazina hakuna anayeitambua sasa Waziri na Naibu Waziri na wengine wako busy kwa ajili ya kutafuta fedha kwa ajili ya mipango mingine kwa ajili ya kuhakikisha bajeti inaenda vizuri lakini Tume ya Mipango imesahauliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari za kwenye corridor Mheshimiwa Waziri ni kwamba Katibu Mkuu wa Hazina amekuwa so powerful kiasi kwamba hakuna mtu anayemsikiliza, kwa hiyo Tume imebaki inaeleaelea tu pale. Tume kama chombo cha kutunga sera za uchumi, kusimamia sera za uchumi, kusimamia hii miradi ya maendeleo kimebaki kinaelea pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ombi langu kwa Mheshimiwa Rais aone uwezekano wa kuitoa Tume ya Mipango Hazina, aiundie Wizara au airudishe kwenye Ofisi yake kama ilivyokuwa zamani ili Tume iwe huru katika kupanga sera za uchumi za nchi na kuzisimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nakushukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo ningependa nichangie ni kwamba kwenye hoja hii mwaka jana tulizungumza sana kuhusu uwezo wa baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri zetu. Tuliishauri Serikali kwa makusudi kabisa ijitahidi kufanya semina, warsha na mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo baadhi ya Wakurugenzi ambao wameingia katika kazi hii kutoka kwenye shughuli nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo ya utendaji wao umesababisha migogoro kati yao na baadhi ya Watendaji wa Halmashauri. Wakurugenzi wakifikiria kwamba kule kuwa wasimamizi wa Halmashauri basi wao ndiyo kila kitu, umesababisha migogoro kati yao na Madiwani na baadhi ya Halmashauri migogoro hii inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokwenda kwenye Halmashauri na kukuta Mkurugenzi hayupo katika maelewano mazuri na Watendaji pamoja na Madiwani, kwa vyovyote vile Halmashauri haiendi. Ikumbukwe kwamba, hizi Halmashauri ni za wananchi, kwa hiyo Mkurugenzi hawezi kusimama kwenye Halmashauri kana kwamba yeye ndiyo mwenye kujua kila kitu, yeye ndiye mamlaka ya kila kitu, akikataa ushauri na mambo kama hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa kwanza kabisa naiomba Serikali iendelee kupitia uwezo wa Wakurugenzi wake na isaidie kuwapa uwezo ili waweze kusimamia shughuli za Halmashauri vizuri, vinginevyo tutapata shida, kazi hazitaenda sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sambamba na hilo tumetembelea baadhi ya Halmashauri, miradi ya maendeleo haisimamiwi sawasawa. Unakuta kuna ile Idara ya Mipango ya Halmashauri ni kana kwamba inajiweka pembeni mambo yanakwenda yenyewe kwenye maeneo mbalimbali ya miradi, lakini unapohoji zile Idara utasikia kwamba ohoo, hili halikupitia kwetu na kadhalika. Ndio maana nasema kama Mkurugenzi yuko vizuri na Wakuu wake wa Idara mambo kama haya yasingeweza kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano tu wa Idara ya Elimu, hivi majuzi Mheshimiwa Rais kwa nia nzuri kabisa ametoa maagizo kwamba michango mbalimbali katika shule ambayo haina tija iondolewe, hiki ni kilio cha Watanzania, lakini sasa kutokana na uwezo mdogo wa Wakurugenzi lazima niseme na hili nawaomba Rais alisikie, uwezo mdogo wa Wakurugenzi umewafanya wakatafsiri lile agizo la Rais vibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu zipo Halmashauri, zipo Wilaya ambazo wazazi katika kila shule walishakubaliana utaratibu wao wa namna watoto wao, kwa mfano wanavyopata chakula mashuleni, utaratibu huo hauhusiani na Mkuu wa Shule, hauhusiani na Mkurugenzi, wazazi wana chama chao, wana bajeti zao, wao ndiyo wanaopanga watoto wale nini, wao ndiyo wanaopanga bajeti iwe namna gani, kuni zipatikane wapi, chakula kipatikane wapi, kwa hiyo watoto wamekuwa wakila shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naelewa upo uhusiano mkubwa kabisa kati ya tumbo na kichwa. Mtoto ambaye hajashiba hawezi hata siku moja akazingatia yale ambayo anaelekezwa shuleni. Sasa Wakurugenzi hawa baadhi yao wamekuwa kama robot, wamekwenda wametengeneza majedwali, wameandika barua, wamekwenda kuzuia wale wazazi ambao kwa nia nzuri kabisa walikuwa wanachanga chakula kwa ajili ya watoto wao. Sasa nashangaa hapa tunaisaidia nchi au tunaibomoa, mtoto anaamka saa 11 alfajiri nyumbani, hajanywa uji, hajanywa chai, anakwenda shuleni hakuna chochote, halafu unasema kwamba tunakuza elimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa Wakurugenzi walimtafsiri Rais vibaya, yako maeneo, kwa mfano katika Jimbo langu, tulikuwa hatuna tatizo kabisa lakini baada ya tangazo lile wamekwenda wale wazazi wamegawana chakula ambacho tayari walikuwa wamenunua, wamegawana kuni ambazo tayari zilikuwa shuleni, wamegawana pesa ambazo zilikuwa tayari zimeshakusanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa sababu Waziri wa Elimu yupo hapa, atusaidie hawa Wakurugenzi waweze kuelewa vizuri agizo la Serikali lilikuwa nini kwa sababu sisi hatuna shida. Rombo kwa mfano, shule zote za Sekondari na za Msingi watoto wanakula shule na huhitaji kabisa kauli ya Mkuu wa Shule wala Mkurugenzi wala nini, wazazi wana vyama vyao, wanaitana wanajichangisha wenyewe, wanatengeneza bajeti wenyewe, wanaajiri mpishi wenyewe, wananunua kuni wenyewe. Sasa leo Mkurugenzi ukifikia mahali ukasema Rais kasema, matokeo yake hata Rais atachukiwa! Kwa sababu Wazazi kule tafsiri ni kwamba anachokula mtoto mchana nyumbani ndicho hicho tunaamishia shuleni, kwa hiyo hakuna tatizo lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo narudia kusema la kwangu ni hilo kubwa kwamba, baadhi ya Wakurugenzi wasiwe wanapokea maagizo ya Serikali halafu wanakuwa kama robot, sijui wametiwa hofu ya namna gani! Bila hata maelezo bila hata nini wanaingia katika utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulisema, hapa tunafanya bajeti, kila Halmashauri inajua kwamba bajeti ya maendeleo katika Halmashauri ni kiasi fulani. Kinachotokea ni kwamba, Halmashauri nyingi ambazo tumezitembelea fedha za maendeleo hazifiki kwa wakati au hazifiki kabisa, matokeo yake ni kama vile Halmashauri zimefungwa mikono na miguu halafu zinaambiwa kimbia, haziwezi kukimbia haziwezi kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba fedha za miradi ya maendeleo katika Halmashauri ziende kwa wakati na kama hazijaenda basi utaratibu uelekezwe ili wajue watafanya nini, vinginevyo ziko Halmashauri ambazo zitaendelea kuachwa tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo ningependa kuchangia kwa sababu Mheshimiwa Gekul ameniomba dakika tano na nataka nimpatie ni kwamba Serikali imejitahidi sana kupeleka watumishi, lakini bado kuna Halmashauri ambazo Ikama haijakaa vizuri, bado kuna Halmashauri ambazo watumishi wengi wanakaimu. Mtu anayekaimu hana hakika na ile nafasi hawezi akatoa maamuzi, kwa hiyo bado tunasisitiza na tunaiomba Serikali kwamba, Wakuu wa Idara katika Halmashauri zetu ifanyike jitihada wale wanaokaimu waweze kuthibitishwa ili waweze kufanya kazi yao kwa uhakika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti ni hayo, naomba muda wangu uliobaki amalizie Mheshimiwa Gekul.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mara nyingi nimekuwa nikieleza hapa kwamba huduma ya simu katika Wilaya ya Rombo hasa maeneo ya Useri, Tarakea, Ukanda wa Chini na Mkuu kuna muingiliano mkubwa sana kati ya mitandao yetu na mitandao ya Kenya hususan Safaricom. Ukiwa Tarakea pale lazima uwe na laini ya huku kwetu Vodacom na uwe na Safaricom.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikijibiwa kwamba hii inatokana na mitandao yetu kuwa dhaifu. Sasa ni kwa nini Serikali isifanye mkakati wa makusudi wa kutatua tatizo hili kwa sababu wananchi wanajikuta wameingia kwenye utaratibu wa roaming bila wao kukusudia na matokeo yake wanatumia pesa nyingi sana. Naomba hili sasa lishughulikiwe nipate majibu kwamba tatizo hili litaisha lini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kuna barabara kutoka Mamsera - Mahida – KNCU - Abiola ambayo ilichukuliwa na TANROADS, ilifanyiwa kazi kwa miaka kama miwili, mitatu hivi, lakini tangu mwaka wa fedha 2014/2015 barabara ile imetelekezwa mpaka sasa haijafanyiwa kazi yoyote. Tunataka kujua TANROADS imeamua kuiachia halmashauri barabara ile au bado iko chini ya TANROADS? Kama bado iko chini ya TANROADS basi ile barabara ishughulikiwe kwa sababu sasa haipitiki hata kwa tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, mimi nilipongeza uanzishwaji wa TARURA kwa sababu nilisema zile barabara za Halmashauri wakati mwingine zilikuwa zinatengenezwa kisiasa kwa Madiwani kila mmoja kuvutia upande wake, lakini fedha zinazotengwa kwa ajili ya TARURA ni ndogo. Jana nilikuwa naongea na Engineer wa TARURA kule kwangu anasema pesa walizonazo wana mkakati wa kutengeneza barabara mbili tu. Sasa nashangaa barabara nyingine za Wilaya nzima zitajengwa namna gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilitaka kusema, sisi Wabunge kazi yetu ni kuisimamia na kuishauri Serikali. Nimekuwa nikisikia malumbano mengi kuhusu Taarifa ya CAG, shilingi trilioni 1.5 na kadhalika. (Makofi)

Mimi nilikuwa nawashauri Wabunge wenzangu tuwe tunasoma hivi vitabu. Mwaka wa fedha wa 2015/2016 CAG alikuja pia na vitabu hapa na akasema mapato ya Serikali yalikuwa ni shilingi trilioni 21.9, matumizi shilingi trilioni 20.2 na akaonesha kwamba kulikuwa na shilingi trilioni 1.088 ambazo zilikuwa zinahitaji maelezo, hayakutoka. Sasa hiki kinachoulizwa sasa hivi tunakijadili kisiasa wakati ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba fedha hizi zinaonekana ili hii miradi ya maendeleo ambayo tunapigia kelele hapa iweze kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hayo, hizi sio fedha zetu ni fedha za wananchi. Mimi nawaomba Wabunge wenzangu, tunapojaribu mambo ya kitaifa tuyajadili tukijua kwamba tunajadili kwa niaba ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho napenda kusema hakuna Mbunge yeyote wa upinzani ambaye anakataa ufufuaji wa ATCL, ambaye anakataa miradi inayojengwa ya reli, barabara na kadhalika kwa sababu ziko kwenye Ilani. Tunachokisema hapa ni kwamba tunashauri ufufuaji huu uende kwa namna ambayo baadae Taifa halitapata hasara. Kama ni ununuaji wa ndege basi taratibu zifuatwe, kama ni management, management ziangaliwe, kama ni utengenezaji wa route, route ziangaliwe, hicho ndicho tunachoshauri, lakini hakuna Mbunge yeyote wa upinzani ambaye anasema shirika lile lisifufuliwe au tusitengeneze reli au mradi mwingine wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, infact sisi tunataka maendeleo na hii miradi ikifanikiwa ni kwa faida ya Taifa hili. Moja tu tunalosema, tunatahadharisha miradi hii wataalam wasikilizwe, wataalam washauriwe, ushauri wa kitaalam ukubalike ili Taifa lisipoteze pesa kidogo za wananchi bila sababu yoyote ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana mimi namshauri Rais na namshauri tena kwamba Mheshimiwa Rais cha kufanya aagize wataalam wapeleke documents zote zitakazoonesha kwamba shilingi trilioni 1.5 zimetumika na siyo vinginevyo. Hapa hatusemi kwamba kuna mtu kaiba, tunachosema Afisa Masuuli abebe makabrasha yake aende nayo kwa CAG aseme kwamba fedha nimezitumia hivi, CAG afunge hoja, kama Afisa Masuuli atashindwa fukuza kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Jeshi letu ni zuri na Wizara iko vizuri. Uzuri huo unatokana na uongozi wa Wizara na Jeshi lenyewe. Kwa sababu hiyo nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri na kumpongeza Mkuu wa Majeshi. Vile vitengo vingine siwafahamu na sivifahamu vyote, kwa hiyo, wachukue tu kwamba ni pongezi zangu kwa wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanali Mabeyo namfahamu, ni mtu mpole na mnyeyekevu sana. Nilifanya naye kazi ya Kanisa, mimi nikiwa Mwenyekiti wa Wazee Walei wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, yeye alikuwa anaongoza kitengo kidogo sana cha ulinzi cha Parokia ya Segerea. Meja Jenerali anajishusha, anafanya kazi na watu wa kawaida hata kufagia Kanisa. Ni mtu mzuri sana, nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi nashauri tu mambo machache. Ushauri wa kwanza, Jeshi letu lina heshima katika Majeshi ya Afrika. Heshima yake inatokana na misingi yake. Hili ni Jeshi la Wananchi, ni jeshi letu. Kwa sababu hiyo, nawaomba wanasiasa na viongozi wa Taifa letu tusilichafue Jeshi hili kama tulivyolichafua Jeshi la Polisi. Leo katika Taifa letu ikitokea ajali inayohusu Polisi, watu wanauliza wamekufa wangapi? Tusilipeleke Jeshi letu huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu tarehe 3 Februari, 2018, wakati wa kutunuku Kamisheni kwa baadhi ya vijana wetu waliohitimu pale Arusha, shughuli hii ya Jeshi ambayo ni muhimu sana ilihusishwa na tukio la kisiasa la kupokea Madiwani waliojiuzulu kutoka chama fulani cha siasa kwenda kwenye chama kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo hiki kilipunguza kwa kiasi kikubwa sana heshima ya siku ile. Kwa sababu tuna matukio mengi sana ambayo tunaweza kufanya siasa, lakini siyo katika tukio muhimu kama hili. Huku ni kulinajisi jeshi letu. Kwa sababu hiyo, naomba wanasiasa wajiepushe kabisa na kuwafanya Watanzania ambao tuko kwenye vyama mbalimbali tukaonekana kwamba sisi hatuhusiki na Jeshi kwa sababu Jeshi lilisimama na wanasiasa wa chama fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika operation fulani iliyotangazwa na chama cha siasa (Operation UKUTA), Wanajeshi walionekana mtaani wakifanya mazoezi. Jeshi letu ni Jeshi linalolinda mipaka yetu, haya mambo ya ndani yanahusu Jeshi la Polisi. Kwa nini tunalihusisha jeshi letu na mambo ambayo yanaweza yakashughulikiwa na Jeshi la Polisi? Au ndiyo kusema kwamba sasa Jeshi linataka lionyeshe misuli yake kwa wananchi ili wananchi waliogope? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hatuliogopi Jeshi la Wananchi, kwa sababu ni Jeshi letu. Hawa ni watu wetu. Kwa sababu hiyo, narudia kuomba, heshima ya Jeshi la Wananchi iendelee kubaki, tunawaheshimu viongozi wake, tunawapenda viongozi wake, waendelee kutunza jeshi hili ili liwe Jeshi la Wananchi wa Tanzania na siyo vinginevyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ambao nangependa kutoa. Inaonesha kwamba katika nchi yetu kuna viashiria niseme vya kigaidi. Ninaliangalia tukio la Kibiti, matukio ya watu kupotezwa na watu wasiojulikana na matukio ya kupigwa risasi kwa watu mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni dalili kwamba kuna udhaifu mkubwa sana wa Kitengo cha Upelelezi katika Jeshi la Polisi. Kwa sababu hiyo, namwomba Mkuu wa Majeshi na Jeshi lenyewe kuangalia uwezekano wa kutumia Military Inteligence kusaidia Jeshi la Polisi ili matukio haya ya aibu katika nchi yetu yaweze kupunguzwa na kuondoshwa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko hofu. Ukisoma mitandao hata leo hii, watu wanasema kwamba kuna maeneo fulani fulani nyeti katika nchi yetu sasa yanalindwa na Askari kutoka nje, hususan Rwanda. Sasa katika hofu hiyo, inawezekana ikahusishwa pia na watu wasiojulikana. Kwa hiyo, naomba sana Kitengo cha Military Inteligence cha jeshi kiimarishwe ili kuweza kuangalia haya maeneo ambayo watu wana hofu nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaliamini jeshi letu pamoja na weledi wake. Hatuna sababu yoyote ya kufikiria kwamba kuna mahali popote katika nchi yetu tunaweza tukaazima watu kuja kutusaidia ulinzi. Wanajeshi wetu ni weledi na wanaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza ni ajira. Kuna utaratibu mzuri wa ajira ambao vijana wetu kutoka JKT wanachukuliwa na kuingizwa katika mfumo wa Jeshi. Sasa kuna manung’uniko ya vijana kwamba wale vijana waliomaliza JKT awamu ya nne, hawajaajiriwa na hawanufaiki na utaratibu huo. Sasa hawa vijana wamefunzwa silaha, wakiachwa hivi hivi na manung’uniko mitaani, tunaweza tukaja kutengeneza kitu kingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hata inanipa hofu kwamba kama tunafikiria hatuwezi kuwaajiri vijana wote, ni vizuri hawa vijana wa JKT pengine tukaangalia wale ambao wanafaa kuwapa mafunzo ya kijeshi na wale ambao pengine tunafikiria wataenda uraiani wapewe mafunzo ya aina nyingine. Vinginevyo kuwafundisha kijeshi na kuwaacha tu mtaani italeta athari kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa tunaowachukua Jeshini ningeomba wafanyiwe psychometric test ili tuweze kupata Wanajeshi kweli ambao wanafaa. Kwa sababu zipo tetesi za baadhi ya Wanajeshi kufanya vitendo vya uhalifu mitaani. Kwa mfano, siku za karibuni Meya wa Ubungo alivamiwa na vijana waliovaa nguo za Jeshi. Sasa hatujui kwamba ni Wanajeshi, hatujui kwamba ni vijana waliomaliza JKT wako mtaani wakapata hizo nguo, hatujui kwamba ni Polisi walipata hizo nguo? Kwa hiyo, hili ni jambo la kuangalia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho napenda kukichangia ni kuhusu Kitengo cha Utafiti Ndani ya Jeshi. Ukiangalia sasa hivi, Maprofesa wetu wameamua kufanya siasa, wameamua kuingia kwenye utawala. Ukiangalia majeshi makubwa duniani hata Jeshi la Marekani, limeingia katika utafiti wa masuala mbalimbali ya kijamii kwa mafanikio makubwa kabisa. Kwa hiyo, naomba ajira za jeshi zihusishe pia vijana wataalam katika fani mbalimbali waingizwe katika tafiti za Jeshi lenyewe, lakini tafiti nyingine za kiraia ambazo zinaweza zikasaidia nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyosema, leo hapa tunajadili nchi, Jeshi letu ni nchi. Kwa hiyo, Jeshi letu lijipanue, lijihusishe katika mambo mengine ya kitafiti ambayo yanaweza yakaja yakawa na manufaa katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano ambalo ningependa kulisemea ni kuhusu madeni ya Jeshi. Jeshi kudai ni jambo la fedheha. Jeshi kudai kwa ajili ya kukarabati vifaa vyake ni fedheha. Jeshi kuomba omba kwa sababu ya vifaa, ni fedheha. Nadhani mahali ambapo tungekuwa na jeuri kabisa ya kufanya investment ya uhakika ni hapa. Kwa hiyo, namwomba Waziri wa Fedha, fedha zote zinazolihusu Jeshi letu zitolewe, tena kwa wakati kwa sababu zinahitajika kwa ajili ya ulinzi wetu. Tusiwe na blah blah na maneno maneno kuhusu pesa ambazo zinahusu wanajeshi; ziwe za pension, ziwe za vifaa, ziwe za nini, lazima Jeshi liwe na morali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na Jeshi lenye wanajeshi wanaonung’unika, hali yetu ni mbaya sana. Sasa hivi tumshukuru Mungu kwamba jeshi letu liko pamoja, hakuna manung’uniko na nini; lakini huku kuwanyima fedha kwa wakati, kunaweza kukaja kutuletea manung’uniko huko baadaye na itakuwa ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo napenda kuchangia ni kuhusu SUMAJKT. Mimi nimetoka ziara Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kutembelea Sekondari ya Ihungo pamoja na Nyakato, zile zilizokumbwa na madhara ya tetemeko. Sasa Shule ya Ihungo mkandarasi aliyepewa kuijenga ni TBA na Nyakato ni SUMAJKT. Wanafanya vizuri sana chini ya Kanali Ngata. Kwa hiyo, hiki kitengo kiimarishwe, kinaweza kikatusaidia mambo mengi sana hapa nchini kuliko hata TBA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, mimi niendeleze alipoishia Mheshimiwa Bulembo. Hadithi iliyopo ni kwamba nyavu ziko za aina mbili; ya dagaa na ya sagara.

Mheshimiwa Spika, nyavu za dagaa kapewa mtu mmoja Arusha kwa njia ya ajabu ajabu. Nyavu hizo zikiingia majini mwezi mmoja, zinakatika. Matokeo yake wafanyabiashara wanaagiza nyavu kwa njia ya panya, Serikali inakosa mapato, Mheshimiwa Waziri anajua, lakini yuko kimya, hakuna hatua iliyochukuliwa.

Mheshimiwa Spika, nyavu za sangara zimechukuliwa madukani, zimechukuliwa kwa wavuvi, zimechomwa, nyavu zimeagizwa na wafanyabiashara bandarini, hairuhusiwi kutoka kwa sababu yuko mfanyabiashara amepewa ili yeye ndiyo auze hizo nyavu. (Makofi)


Mheshimiwa Spika, zaidi ya hayo, watu wanateseka, wananyang’anywa pesa zao, shilingi milioni 20, risiti inaandikwa shilingi milioni tano. Kwa hiyo, naungana na Mheshimiwa Bulembo kwamba lazima operation hii isimame na uchunguzi ufanyike kwa sababu kuna harufu ya rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Bulembo amesema vizuri, hii ni Wizara ya siasa kama ilivyo kilimo na maji, ni Wizara za siasa. Mheshimiwa Rais amenunua Bombadier, sawa; anajenga reli, sawa, lakini wananchi wa kawaida Wizara hizi zitawaondoa madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda kuzungumza ni kuhusu Vituo vya Uhamilishaji. Mwalimu Nyerere alianzisha Vituo vya Uhamilishaji hasa maeneo ambayo sisi tuna zero grazing. Vile vituo vimekufa sasa hivi na matokeo ya vile vituo kufa, in-breeding ni kubwa na in- breeding inasababisha magonjwa, inasababisha ukuaji mbaya wa mifugo na maziwa kupungua. Naiomba Wizara ieleze mkakati wa kurejesha vile vituo ili kupata madume bora ya ng’ombe na mbuzi ili kuongeza kipato cha wananchi kwa njia ya maziwa na nyama.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo napenda kulisemea kwa dakika zangu hizo ni kuku. Akina mama wengi wamesomesha watoto wa nchi hii kwa miradi ya kuku wa kienyeji na hao tunaoagiza, lakini hakuna chochote kilichosemwa na Wizara kuhusu mkakati uliopo wa kuendeleza ufugaji huu wa kuku.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba hata ulaji wa mayai katika nchi hii umepungua kuanzia kwa watoto mpaka watu wazima na kwa sababu hiyo, lishe hii ambayo inahitajika sana kwa vijana wetu imepungua. Naomba Wizara ikija hapa ieleze mkakati ambao itatumia kuendeleza kuku na hasa kuku wetu wa kienyeji ambao wanapotea kidogo kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri akija hapa vile vile atueleze, ule ukatili uliofanywa Namanga wa kuchoma


vie vifaranga vilivyotoka Nairobi ni kwa sababu gani? Maana tuna sheria inayolinda wanyama. Vifaranga wamechomwa hadharani, ni uharibifu wa mazingira, ni ukatili, ni kuhatarisha mahusiano na wenzetu wa kutoka nje na kadhalika. Mheshimiwa Waziri atueleze, waliofanya ukatili ule wamechukuliwa hatua gani? Ili jambo hili lisipite hivi hivi bila kusemewa.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ambalo ningependa kulizungumza ni kuhusu viwanda vya ngozi. Tulipandisha export levy hapa ya ngozi kwenda kwenye 8%, matokeo yake sasa hivi machinjio mengi wananchi wakipeleka ng’ombe zao wanaambiwa ondoka na ngozi; na pa kuipeleka ngozi hakujilikani. Ngozi zinaoza, zinanuka kwenye machinjio, Wizara ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba ngozi za nchi hii zimetumika kwa ajili ya kukuza uchumi katika Taifa letu?

Mheshimiwa Spika, kiwanda cha ngozi, kwa mfano Kanda ya Kaskazini, kile cha Himo pale hakitoshi kuchukua ngozi nyingine zote. Tumezungumza habari ya viwanda.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Wizara ilete mkakati wa namna ambavyo ngozi italiingizia hili Taifa pato na kuondoa adha ambayo wananchi wanapata kwa sababu ya ngozi.

Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kwa kusema kwamba kero hizi ambazo tunazizungumza ni kero za wananchi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kwa kusema kwamba tuko hapa Bungeni kwa ajili ya kumsaidia Rais. Hakuna Mbunge yeyote humu ndani ambaye lengo lake siyo kumsaidia Rais. Mawazo tunayotoa hapa lengo lake ni kusaidia ili nchi hii iweze kuongozwa vizuri. Kwa hiyo, Bunge lisipotoshwe kwamba kuna watu ambao wako hapa wanafanya hujuma dhidi ya uongozi wa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nataka nilishauri Bunge na Taifa acheni Mheshimiwa Lissu afanye anachofanya kwa utashi wake. Tunapoteza muda na nguvu kujadili habari ya Mheshimiwa Lissu. Nguvu hizi tungezitumia wakati alipopigwa risasi kama Wabunge ingeonekana tumefanya jambo la busara sana lakini alivyopigwa risasi, alivyokuwa hospitali, alivyokuwa anahangaika na matibabu tulikaa kimya. Sasa hivi Mungu amemjalia pumzi acheni aseme. Kama kuna jambo ambalo atakosea atakuja ahojiwe mbele ya safari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa hapa jambo la Uchaguzi Mkuu na Tume ya Uchaguzi. Pia Serikali wiki iliyopita ilijibu maswali kuhusu Tume ya Uchaguzi na maandalizi ya uchaguzi ujao kwamba imeanza taratibu za kuboresha daftari, hili ni jambo zuri. Mwenzangu amechangia juu ya kupitia hata Tume yenyewe na kuhakikisha kwamba watendaji wa Tume wanateuliwa watu huru na watakaosimamia uchaguzi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chaguzi katika nchi mbalimbali zimeleta fujo sana na zimesababisha mataifa mengi kuvurugika. Kwa hiyo, naikumbusha na kuiomba Serikali, uchaguzi wa 2020 ni wakufa na kupona, naomba sana maandalizi ambayo mmeamua kuanza kuyafanya yawe shirikishi, wananchi washirikishwe, vyama vishirikishwe na kila mdau ashirikishwe. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Uchaguzi Mkuu unatanguliwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Mwaka huu kila mmoja wetu alitegemea kwamba maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa yangeshaanza kufanyika. Kama tunavyojuwa maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa yanaanza na kanuni na kuwashirikisha wadau. Naomba sana maandalizi yawe wazi, wadau wote washirikishwe, kwa sababu uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita ulikuwa na fujo za hapa na pale.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu wamekuwa wanatukatia muda wetu na Kiti kimekuwa kikipunguza muda wetu. Hakuna mtu huku anachangia dakika kumi hata mmoja ni saba, nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba wahusika washirikishe wadau na wadau ni vyama vya siasa na kadhalika, tuweze kuzipitia hizo kanuni ili uchaguzi uweze kwenda vizuri, tuweze kupata viongozi wa kutuongoza sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hilo haraka haraka nizungumzie kuhusu yanayotokea katika nchi. Tutafika mahali nchi hii tutaingia kwenye matatizo makubwa. Yapo mauaji na vifo ambavyo hadi sasa hakuna matokeo ya uchunguzi wake na nitataja baadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, alichinjwa Mwenyekiti wa CHADEMA wa Arumeru, hakuna taarifa mpaka sasa hivi; Ben Saanane hakuna taarifa; Azori Gwanda hakuna taarifa; David John wa Ananasifu hakuna taarifa; Simon Kangoye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo kupitia Chama cha Mapinduzi hakuna taarifa; Akwilina Akwilini, Kamanda wa Kanda Maalum anasema faili limefungwa wakati anasema alikamata askari sita ambao walituhumiwa kumpiga risasi; Petro Shemasi wa Itigi ambaye baba yake anasema alishuhudia Mkurugenzi akimlenga risasi ya kichwa, leo Polisi wanaanza kusuasua na kuweka mambo ili kulinda wauwaji; yupo Alphonce Mawazo na Lwena wa huko Kilombero. Siyo hao tu, wapo Watanzania wengi ambao wamekwishauwawa kwa sababu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nchi hii tunauwana hovyo namna hii, tuna Polisi na vyombo vya dola lakini hakuna taarifa tunaona ni jambo la kawaida tu, tukumbuke kwamba familia za hawa waliouawa…

T A A R I F A

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mmoja akiuawa, ni jambo kubwa sana katika nchi na unachoniambia wewe Mbunge wa CCM ni kwamba Serikali imeshindwa kuchunguza haya mauaji kwa sababu mimi sitetei wauaji wa Kibiti, sitetei wauaji wa sehemu nyingine yoyote, nachosema ni kwamba wajibu namba moja wa Serikali ni kumlinda raia na mali zake, wauaji waue Kibiti…

T A A R I F A

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachosema na kuiomba Serikali, mauaji ya holela katika nchi hii itafute namna ya kuyakomesha. Mimi sizungumzi habari ya kauawa wa CCM au CHADEMA. Nachosema tukiendelea na huu mchezo ni kwamba itafika mahali kisasi kitalipwa. Nasikitika yakizungumzwa mambo kama haya Wabunge wazima wanapiga makofi, wanacheka, wanabeza, wanatoa miongozo na nini kama vile hakuna kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasihi Wabunge wa CCM shaurini Serikali tutafute namna ya kukomesha haya mauaji kwa sababu leo hii ukinigusa mimi, mimi nina watoto, nina ukoo usitegemee kwamba watoto na ukoo wangu utachekelea tu hivi hivi, pengine ukiniua kuna reaction itatokea huko. Ndiyo maana nasema chonde chonde, Waziri wa Sheria kaka yangu Mheshimiwa Kabudi, kaa na vyombo kwa utulivu na amani kabisa, kaa na DPP, IGP na wengine wote hii ni aibu nimetaja watu karibu 20 wameuawa lakini hakuna uchunguzi, hakuna chochote, ni kama mbuzi tu. Hata hawa wa Kibiti waliokamatwa, nasema lazima washughulikiwe vinginevyo tukienda hivi, nchi hii itafika mahali kisasi kitatembea barabarani na haitakuwa jambo la maana. Rwanda ilianza kidogo kidogo hivi ikachochewa na vyombo vya habari matokeo yake Rwanda ikalipuka, sisi hatuna tofauti na Rwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema, limezungumzwa hapa jambo la walio mahabusu. Hoja hapa ni kwamba walio mahabusu wanaweza kutafutiwa njia nyingine. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, ingawaje kwa kweli haukuwa mpango wangu hasa kuongea lakini imebidi niongee kwa sababu zifuatazo.

Mheshimiwa Spika, jana nilikuwa namtania Mama Makilagi hapa aliposema haongei na watoto na mimi nikasema mimi ndiyo baba yao na Bunge likacheka kidogo. Kwa muktadha huo nataka niseme hivi, imetokea lugha hapa kwamba kambi yetu hii hatuthamini kazi ambazo zinafanywa na Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka niseme kwamba hii si kweli. Nichukue fursa hii kwa niaba ya wenzangu kuwapongeza askari wote wa jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Uhamiaji, Jeshi la Zima Moto ambao wanafanya kazi yao vizuri. Rai yetu hapa ni mbili tu ya kwanza ni kulikumbusha na kuliomba Jeshi la Polisi kufanya kazi zake kwa kufuata sheria hiyo ndio rai yetu tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa hili hakuna anaweza kusema kwamba Jeshi la Polisi lifuata sheria mia kwa mia hakuna kwa sababu yapo matukio kadhaa katika nchi yetu ambayo yana-prove tofauti. Kwa mfano juzi, juzi kuna kijana alikamatwa Waziri Dhahiri pale Lembeli amekamatwa asubuhi saa mbili amepigwa na askari mpaka kafia kituoni. Sasa askari kama huyu ni moja kati maskari ambao hawafuati sheria, hawafuati taratibu na matukio kama haya yapo maeneo mengi. (Makofi)

Kwa hiyo sio sahihi kusema kwamba tunaosema Jeshi la Polisi lijirekebishe lifanye tathimni ya baadhi ya askari wake sio sawa sawa na kusema kwamba hatulipendi jeshi la polisi wala asitokee mtu akasema eti kwamba ikitokeo polisi wasiwepo kwa masaa machache itakuaje haitatokea mpaka dunia itakapokwisha.

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Selasini pokea taarifa Mheshimiwa Chief Whip.

T A A R I F A

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa mchangiaji anaochangia nimpende kumkumbusha kwamba moja ya mambo ambayo jana yalifanya kiasi kwamba Wabunge wa Chama cha Mapinduzi wakafikia kusema kwamba hawa hawawapendi polisi wetu ni kwamba mchangiaji wao mmoja alifikia kusema kwamba polisi ni kansa ya Taifa. Nakupa taarifa kwamba hilo neno sio nzuri na tunafahamu kabisa kwanza kansa hata nikisikia kansa naogopa polisi hao hao wanaolinda usalama wetu na sisi tupo salama hapa wanapotamkwa kwamba wao ni kansa la Taifa hilo neno linaukakasi nashukuru.

SPIKA: Mheshimiwa bado Mheshimiwa Selasini kidogo. Sikupata privilege ya kulifahamu hilo lakini kama limesemwa na Mbunge ningeomba nifahamu tu wala usifiche ni Mbunge nani?

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Sophia Mwakagenda wakati anachangia jana alisema kabisa wazi na Hansard zitaeleza kwamba polisi ni kansa ya Taifa.

SPIKA: Ahsante naomba mniletee hiyo hansard sijui kama Mheshimiwa Sophia yupo lakini kama Wabunge haya ni majeshi yetu, hata uwe na chuki kiasi fani kuna mstari ambao huwezi kuvuka. Kwa hiyo, ni vizuri Chief Whip unaongea basi endelea.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, ahsante natumai utanihifadhia muda wangu.

Mheshimiwa Spika, nilivyoanza kusema nimesema nasimama kama kiongozi wa kundi hili, na Mbunge aliyeongea angekuwa amesoma saikolojia angekuwa amesoma kitu kinaitwa furious of generation haiwezekani kauli ya mtu mmoja ikawa kauli ya wote, na Mbunge hili lina taratibu zake kama kuna mtu mmoja amezungumza Bunge hili lina namna ya kumdhibiti huyo aliyezungumza. Lakini kama kiongozi wa kundi hili nasema hatuna msimamo wowote wa kulidharau jeshi la polisi kwa namna yoyote ile na ninawapongeza polisi ambao wamekuwa wakifanya kazi vizuri full stop hakuna zaidi. (Makofi)

T A A R I F A

SPIKA: Almas Maige.

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, Msemaji wa Kambi ya Upinzani kutoka CHADEMA huko nje, huko nje amesema mambo mengi na kulikashifu Jeshi la Polisi na ndiye Msemaji wa Kambi ya Upinzani, sasa wanakanusha au wanakubali?

SPIKA: Mheshimiwa Selasini unaipokea taarifa?

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, ninampa pole rafiki yangu katika utu uzima huu alipaswa vilevile awe amezijua kanuni. Pamoja na hayo sote kwa pamoja kama Wabunge wajibu wetu ni kulisaidia Jeshi la Polisi. Tunasema kwa pamoja jeshi letu lina matatizo, askari wetu wanahitaji nyumba bora wote, wa polisi, wa magereza, wa uhamiaji hili sio suala la upinzani ni suala letu wote na kila Mbunge akisimama hapo anazungumza kuhusu nyumba za askari kwenye jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, tunazungumza juu ya vitendea kazi vya polisi, tunazungumza habari ya vituo bora vya polisi, jeshi letu kwa sasa ni jeshi ambalo unakwenda kituoni wanahangaika na makaratasi na mafaili na kadhalika. Watu wameshaenda sasa hivi kisasa watu wana komputa na kadhalika na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazungumza hayo, tunazungumza habari ya mishahara na posho za askari wetu. Tunazungumza habari ya uniform za askari wetu haya ndiyo mambo ya kuzungumza na Mheshimiwa Kangi Lugola Waziri ametuletea hotuba hapa tuijadili sisi kama Wabunge sio kumjadili Mheshimiwa Tundu Lissu hayumo humu kwenye hotuba ya Waziri. Kwa hiyo, wakati mwingine tunatumia muda Wabunge vibaya kugeuza kila jambo kuwa jambo la siasa wakati huu muda ni muda wa wanaotulipa mshahara, wanaotuliapa posho ambao ni wananchi wa Tanzania wanaolihitaji hili jeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema wako askari ambao wanalifedhehesha jeshi la polisi na ushahidi ni kwamba limekuwa likichukua hatua dhidi ya askari wa namna hiyo. Tunachosema kasi ya kuchukua hatua iendelee.

Mheshimiwa Spika, na wewe unakumbua hotuba za Mwalimu Nyerere, Mwalimu Nyerere alikwisha kusema kuna vyombo viwili tu sasa hivi tunavitegemea sana watanzania. Chombo cha kwanza ni mahakama, chombo cha pili ni polisi. Mwalimu alisema polisi na mahakama wakiingia kwenye rushwa au kutotenda haki itakuwa ni balaa. Tunazungumza habari ya mikutano hapa, kusumbuliwa hapa, pilipili usizozila haziwezi kukuwasha sisi tunazungumza kwa sababu tunajua kinachotokea lakini polisi hawa lazima wawe mfano katika kutekeleza sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati sheria ambayo wanapaswa watekeleze, polisi hawaruhusuwi kuingia kwenye active politics kwa sababu wao wanafanya maamuzi, jeshi hili ni la wote. Sasa polisi kuwa tamed na Watanzania kwamba ni la CCM na la Chadema watu wa upande mwingine hawatawapa ushirikiano na matokeo yake utendaji wa jeshi la polisi hautakuwa sawa. Kwa hiyo, ndugu zangu tunapozungumza habari ya kuriboresha jeshi la polisi hatuzungumzi kwa sababu ya chuki na jeshi la polisi. Tunazungumza kwa sababu tunalipenda na tunapenda lifanye kazi vizuri zaidi. Tunazungumza ili Waziri na Naibu wake wapate uwezo wa kulisaidia zaidi.

Mheshimiwa Spika, na mwisho pale kwangu Rombo lile ni jimbo ni jimbo la mpakani Mheshimwa Waziri angalia uwezekano wa kusaidia wale polisi ili ule mpaka uweze kufanya kazi vizuri. Na sisi watu wa Rombo tunashirikiana vizuri na Jeshi la Polisi tumejenga kituo pale Useri kwa nguvu zetu tumekabidhi Serikalini sasa hivi tuna msingi kwenye Kata ya Mahida unakwenda, tuna msingi umeshafika leta kwenye Kijiji cha Kilongo chini msingi wa kituo cha polisi na wa nyumba za polisi. Huo ni ushahidi kwamba tunasaidiana na jeshi lenyewe na Serikali katika kuliboresha.

Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kusema kama tunatendelea na vijembee katika hoja kubwa kama hii ya jeshi tunaiweka nchi yetu katika hatari kubwa sana kwa sababu tunaligawa jeshi tugawa na wananchi. Kwa hiyo, naomba tu ni rai yangu chukueni hoja ambazo zinaweza kusaidia jeshi upande huu zichukuliwe zinaweza kuisaidi jeshi upande tuweze kujenga jeshi bora kwa ajili ya nchi yetu. Ahsante sana nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi na kabla sijaanza kuchangia hoja hii, naomba nichukue nafasi kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niweze kutoa salamu za rambirambi kwa familia ya Marehemu Reginald Abraham Mengi, Wafanyakazi wote wa Makampuni ya IPP, Wanahabari wote Nchini na Afrika Mashairiki, Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Tanzania, Watanzania wote na wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa kifo hiki cha ghafla cha ndugu Mengi ambaye alikuwa mtu mkarimu, alisaidia Watanzania wengi, aliajiri wengi, alikuwa Baba mwenye huruma kwa watu wote hasa walemavu na aliwasaidia Watanzania kuwajengea ari ya kujitegemea. Tutakumbuka kitabu chake kile cha “I can, I will, I must” kimewasaidia Watanzania wengi sana kuwa na courage na moyo wa kufanya biashara. Kwa hiyo huu ni msiba mkubwa unatusikitisha wote, naomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, niseme tu kwamba Wizara hii ni Wizara nyeti, ni Wizara ambayo inategemewa na Watanzania lakini inategemewa na sekta zote hapa nchini; inategemewa na Kilimo, Afya, Viwanda na kila kitu. Kwa hiyo ni Wizara ambayo inahitaji ushauri mzuri na inahitaji msaada wa kutosha kwa kweli badala ya kulaumu tu. Kabla sijatoa ushauri, niseme tu kwamba Jimbo langu ya Rombo lina shida kubwa sana ya maji na utashangaa Rombo ndiko ambako Mlima Kilimanjaro upo. Zamani kulikuwa na mito mingi ikitoka pale mlimani na kugawa maji katika maeneo mengi ya Mkoa wa Kilimanjaro, lakini sasa nadhani Rombo ni Wilaya inayoongoza kwa uhaba wa maji pale mkoani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo niseme tu kwamba naishukuru Wizara, tuna mradi pale katika Vijiji vya Shimbi Mashariki, Ngareni na Ngoyoni ambavyo kwa jumla tulikuwa tunahitaji bilioni 1.33 ili kukamilisha ile miradi lakini Wizara imeshatupatia shilingi milioni 717.7 na sasa hivi tunaomba Wizara itukamilishie shilingi milioni 617 ili miradi hii ambayo ni ya siku nyingi ianze kufanya kazi. Ni matumaini yangu kwamba Wizara itatekeleza kwa sababu niliongea na Naibu Waziri, nimeongea na Katibu Mkuu kwa kweli ni watu ambao ni wasikivu, wanapenda kushirikiana, kwa hiyo nadhani kwamba hili lilatekelezwa, naomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ni vyema Serikali pamoja hata na wananchi wangu wa Rombo kufahamu kwamba changamoto ya maji Rombo ukubwa wake unatokana na kwamba hakujawahi kuwa na uwekezaji mkubwa wa maji katika Wilaya ya Rombo kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita. Kwa hivyo miundombinu na vyanzo vya maji vilivyopo kwa miaka 20 iliyopita havijawahi kuboreshwa. Hata hivyo, kwa sasa ninayo furaha kwamba Serikali imeridhia kuboresha huduma hiyo ya maji kwa vijiji 41 vya ukanda wa chini ambavyo ndiyo nina shida kubwa sana ya maji. Kuna usanifu umeshafanyika kutoka chanzo cha maji cha Ziwa Chala ambacho chanzo kile kilikuwa kidogo Wakenya wanasumbuasumbua lakini sasa hivi wameshakubali na Serikali imeshaanza usanifu, kwa hiyo nawaomba Warombo wenzangu wawe watulivu, kazi hiyo inafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna chanzo kingine cha Mto Njoro kule Tarakea vilevile Wizara kwa kutumia wataalam wake na wataalam wa kule Halmashauri wameshaanza uwezekano wa kupata maji katika chanzo kile na chanzo kingine cha Kinyasini, Mto Uwashi na Mbushi vyote hivyo katika Mwaka huu wa Fedha huenda kazi ikafanyika na nimeongea na Katibu Mkuu kwamba tayari fedha ambazo zimeshatengwa bilioni 10 huenda zikapatikana kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hayo Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri, tulishasema mara nyingi hapa Bungeni kwamba tunayo shida kubwa sana na Jumuiya ya maji inayosambaza maji kule Rombo. Hii Jumuiya inaitwa Kiliwater. Utashangaa mwezi uliopita, mimi binafsi nimepokea bili ya maji Sh.58,000 na kule nyumbani nimeacha watu wawili tu ndiyo wanaotumia maji, lakini imeingia bili ya Sh.58,000. Nimejaribu kulalamika wakaniambia iko sawasawa, haya ndiyo malalamiko ya wananchi kwamba hata maji kidogo yaliyopo yanagawanywa vibaya na wale wanaotaka wafungiwe maji, hawafungiwi kwa sababu ambazo wala hazieleweki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwanzo wakati Mzee Lwenge akiwa Waziri tulilalamika na tukaomba kwa sababu Halmashauri iliweka azimio kwamba tuombe tuanzishiwe Mamlaka ya Maji katika Halmashauri ya Rombo baada ya kuindoa hii Halmashauri na ombi hili lilikubalika sasa kama litatekelezwa au kama tutaanzisha ile Mamlaka ya Maji ile ya Kitaifa ambayo itasimamia maji kwa ujumla, lakini kwa wakati huu wa mpito ile Jumuiya inayogawa maji pale, ifanywe mikakati ya kuiangalia ili isiendelee kuumiza wananchi, wakifanya hivyo watakuwa wamewasaidia sana watu wa Rombo .

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo lingine ambalo nataka kusema, suala la maji ni kubwa na kama tusipokuwa makini suala hili linaweza likaja kusababisha hata vita ya tatu ya dunia kwa sababu vyanzo vingi vya maji vinakauka nchini na hata duniani kwa ujumla. Kwa hiyo, ningeishauri Serikali; kwanza tufanye mkakati wa kuanzisha mabwawa maalum ya kuhifadhi haya maji ya mvua ambayo yanapotea hovyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukivuna haya maji ya mvua yanaweza kutusaidia. Nilisema tena katika mchango wangu mwaka uliopita; ukiangalia hapa Kongwa mpaka Kibaigwa maji mengi yanamwagika hovyo kutoka Kiteto huko na nchi kama zile za Senegal, Siera Leone huko walianzisha kitu kinaitwa “man-made lakes”, wakachimba, wakakinga yale maji na sasa hivi wanayatumia, hiyo itatusaidia. Vilevile tuanze utaratibu wa kugawana pia hata maji haya tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, tuanzishe utaratibu wa makusudi kwa baadhi ya maeneo hata mjini kufanya recycling ya maji haya tunayotumia tunasema machafu, tunayatupa, kwa sababu haya maji yanaweza yakatusaidia kwa matumizi mbalimbali; kwa matumizi ya wanyama, yanaweza yakatusaidia kwa matumizi ya umwagiliaji na matumizi mengine hata matumizi ya majumbani ukiondoa matumizi ya chakula na kadhalika. Kwa hiyo, ninachokisema ni kwamba, inawezekana tumerdhika kwamba maji tunayo, mito ipo na kadhalika, lakini tunakokwenda maji yanapungua Kitaifa na Kimataifa, kwa hiyo Wizara ifanye mikakati ya namna ya kuhifadhi haya maji yaliyopo ili yaweze kutumika sawasawa. Pia watunze na haya mabwawa kwa sababu kuna mabwawa mengine yanapotea. Angalia kwa mfano, Ziwa hili la Babati; Ziwa la Babati sasa hivi linajifukia kwa sababu ya uchafu. Angalia Ziwa Jipe; na lenyewe linajifukia kwa sababu ya uchafu kwa sababu tusipofanya bidii wenyewe kile alichotupa Mwenyezi Mungu kinapotea

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni huizi certificates; ni kweli zinachelewa na zikichelewa zinapandisha gharama kwenye ile miradi na ni kweli vilevile kuna ufisadi kwenye hii miradi na ni ukweli vilevile kwamba baadhi ya Watumishi katika mamlaka zetu na kadhalika bado hawajaenda na kasi ambayo inazungumzwa. Sasa nifikie mahali niseme, kwa nini tuna mamlaka halafu tunalalamika? Yaani kwa nini tunalalamika kuhusu Watumishi wa Halmashauri sisi Bunge? Yaani tunakaa hapa Bungeni tunamjadili Injinia wa Maji wa Halmashauri fulani, hivi hii inawezekana kweli? Kwa hiyo, niseme kwamba labda pengine sisi tumekosea mahali fulani. Niishauri Wizara hao wanaolalamikiwa wachukue hatua ili Wizara iendelee na kazi yake nzuri ambayo inafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa na mimi nimeomba nafasi hii kwa sababu ya mambo madogo mawili tu ambayo nilifikiri ni muhimu niyazungumze katika hoja hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, asilimia 85 ya watu wa Rwanda ni wakristo, na kama mtakumbuka mauaji ya Kimbari yaliyotokea Rwanda wakristo hawa hususan Wakatoliki wenzangu walihusishwa sana na yale mauaji, na ni kweli kwa sababu kuna wahanga walikimbilia katika makanisa, lakini baadhi ya mapadre wakawatosa.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ili baadaye nieleze ninachotaka kusema ninakumbusha miaka ya 1980 kulikuwa na mihadhara inaendelea nchini kwetu, na mihadhara hii iliwahusu sana Wakristo na Waislam. Wakristo tulilalamika sana Waislam walipokuwa wanalitaja jina la Bwana Yesu na walikuwa wanasema kwao ni Nabii Issa Aleyhi-Salam, lakini mapambano yalikuwa makubwa matokeo yake mihadhara iliachwa. Hakuna asiyekumbuka kipindi kile hali ilivyokuwa mbaya.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalotaka kusema ili niweze kueleza vizuri hoja yangu, Mheshimiwa Rais, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli anahimiza Watanzania tufanye kazi ili kila mtu aweze kupata ujira wake na kipato chake kutokana na kufanya kazi, na hata vitabu vya dini vinahimiza kazi. Mtume Paulo kwa Wakristo mnajua anasema asiyefanya kazi na asile chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nayasema haya kwa sababu ya hoja ya ulinzi na usalama tunayojadili na sasa hapa nataka ku-refer Wizara ya Mambo ya Ndani. Wizara ya Mambo ya Ndani ndiyo inayosajili vikundi vya dini katika nchi yetu na kwa maoni yangu ni kwamba sheria iko wazi na kanuni zipo na Wizara inajiridhisha kabla ya kufanya huo usajili. Na niseme wazi mimi sina tatizo na kikundi chochote cha dini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini yapo matendo ambayo yanafanywa na baadhi ya vikundi vya dini yasipoangaliwa na nchi na wenye mamlaka yanaweza yakalitumbukiza Taifa hili mahali pabaya kwa sababu ya hofu ya kuingilia uhuru wa dini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama anasimama Mchungaji au Askofu anawaambia watu fungueni mapochi yenu hela ziingie na anatoa hotuba labda kuanzia asubuhi mpaka jioni, ni wazi vijana wataacha kufanya kazi, watakwenda kufungua mapochi yao wakisubiri fedha ziingie kwa upepo wa kisulisuli. Sasa hii si sahihi. Na ndiyo maana nasema kama Wizara inavijua vigezo vya kusajili haya makanisa, mambo kama haya Wizara inapaswa iingilie kati kwa sababu jambo kama hili likiendelezwa linaharibu nchi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, wako wengine anasajili kanisa, baba ni askofu, mama ni mchungaji, kijana anaokota sadaka wanaweka maturubai barabarani ndiyo kanisa, wanawadanganya wananchi kwa kuwapa maji wanasema ni ya upako, wala maji hayo hatujui kama yamepitia TBS, wanawapa mafuta wanasema ni ya upako, hatujui kama yamepitia TBS, halafu matokeo yake watu wanachukua wanabugia tu wanaokota sadaka. Kwangu mimi anapomtaja Bwana Yesu au Roho Mtakatifu katika hoja kama hiyo mimi naona ni kashfa kwa sababu huyo sio Roho Mtakatifu ni roho mtaka vitu. Na lazima Wakristo wanajua tofauti ya Roho Mtakatifu na roho mtaka vitu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yako mengi yanayoendelea, na wanaoumia ni akina mama. Sijui ni kwa sababu gani kwa sababu akina mama wengi ndio wanaoonekana kwenye makanisa hayo. Mtu anawaambia akina mama waondoe nguo za ndani wapunge hewani ili wapate ujauzito, tunaona tu na Serikali ina mkono mrefu nina imani hata kwenye haya makanisa Serikali ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa iko siku wanaoamini katika roho na kweli hao wakwelikweli wataamua kumtetea Yesu Kristo, bwana na mwokozi wa kweli baada ya kuchoka kashfa hizi na itakuwa mbaya. Sasa mimi naiomba Serikali isogope kupitia sheria inayosajili hivi vikundi vya dini. Kama kuna haja ya kuihuisha iihuishe ili iweze kuangalia ni vikundi gani kweli vya dini au ni vikundi gani vimekuja nchini kuja kufanya utapeli kwa ajili ya kuwaibia Watanzania. Serikali inao wajibu wa kulinda raia wake na kitu kidogo ambacho raia wanapata ili matapeli wasije wakaingia wakawapora.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ninapenda kulizungumza ni kwamba tunakwenda kwenye uchaguzi na Mheshimiwa Rais wiki iliyopita amesema kwamba atahakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki. Sasa uko ushauri amekuwa akipewa, wiki hii amepewa ushauri na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, nina hakika atauzingatia na ninamuomba auzingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini na mimi nataka nimpe ushauri ambao tumekuwa tukiusema mara nyingi, wapo Watanzania wengi wanaoishi nchi za nje wakifanya biashara au wapo katika balozi zetu, sasa hivi tunahuisha daftari la kupiga kura bado hakuna kauli ya wazi ni namna gani Watanzania hawa watapata nafasi ya kujiandikisha kupiga kura au ni namna gani watakavyopiga kura. (Makofi)

Kwa hiyo ninaomba wakati ushauri mbalimbali ukitolewa na kuzingatiwa basi jambo hili ambalo tumelizungumza muda mrefu kwa miaka mingi lizingatiwe kwa sababu ni haki ya Kikatiba ya kila Mtanzania kuchagua uongozi wa nchi, kuchagua viongozi wanaowataka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, ni kwamba mtu akiwa mfungwa au akiwa mahabusu hapokwi haki zake. Hata jana au juzi tulimsikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali akisema kuna haki ambazo wafungwa wamepewa na hazipaswi kuondolewa. Haki moja wapo ni hii ya kuchagua, wale wafungwa na wenyewe tunaomba wakati mazingatio yakifanyika ya namna tutakavyokwenda kwenye uchaguzi huru na wa haki, nao waweze kupewa nafasi ya namna ambavyo watajiandikisha na namna ya kupiga kura.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, ninawaomba Watanzania wa vyama vyote, wa taasisi zote, kwa kawaida tunapokwenda kwenye uchaguzi lazima mihemko inapanda kwa kila mtu. Juzi Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi aliwakemea wale vijana ambao walikuwa wanawaalika wenzao kwa ajili ya kuwadhibiti vijana wa vyama vingine, hili ni jambo zuri alilofanya na kwa kweli nampongeza kwa jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini twende mbele zaidi, ile ni jinai, watu wanaofanya jinai namna hiyo wasikemewe tu kwa sababu watazoea kukemewa, watazoea kudekezwa. Imani yangu ni kwamba kama Serikali watu wa namna hiyo isipoanza kuwadhibiti tangu mapema zikaanza kutolewa kauli za kutishana namna hii, matokeo yake tunaweza tukafika kwenye uchaguzi tukiwa hatuko salama, tukafika kwenye uchaguzi nchi ikiwa vipande vipande. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba sana sisi Wabunge, viongozi wa vyama, wa taasisi za vyama na mabaraza ya vyama tujiepushe na kutoa kauli za kuwachochea Watanzania, za kuwachochea vijana wetu katika muda huu kwa sababu uchochezi huu unaweza ukaligawa hili Taifa na hatuna nchi nyingine zaidi ya Tanzania na tunao wajibu wa kuilinda Tanzania kwa nguvu zetu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika wangu katika mambo ambayo utakumbukwa kuyafanya kwenye Bunge hili ni pamoja nakutengeneza Kamati ya iliyochunguza fujo zilizotokana na gesi kule kusini. Kamati iliyochunguza madini ya Tanzanite na kamati iliyochunguza madini ya Almasi.

Mheshimiwa Spika, nimetazama picha Mheshimiwa Rais akiwa ameshika paji la uso anaonyesha kutafakari sana. Picha ile inaonesha amezeeka kuliko alivyoapishwa. Inaonekana Mheshimiwa Rais ana mawazo mengi. Sasa kutokana na hiyo hilo nililosema kwanza na hili la Mheshimiwa Rais naomba niseme yafuatayo.

Mheshimiwa Spika, kazi ya Bunge hili kuishauri Serikali, kazi ya Bunge hili ni kuisimamia Serikali. Tunafanya makosa makubwa sana kufanya siasa ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, naomba pia niseme nimekuwa msafirishaji wa korosho kwa miaka mingi. Maana Wabunge hapa hawajaambiwa waeleze vitu wanvyofanya. Wapo watu wanasimama hapa wanatetea mambo mabaya yanayofanyika kwa sababu tu wanalima korosho. Mimi nimesafirisha korosho, na kutokana na hilo nataka niwambie, karosho inaoza kama vitungu. Korosho iliyooza maji maji yake yakigusa korosho nyingine inaoza.

Mheshimiwa Spika, nimetangulia kukusifu kwa kutengeneza hizi kamati kwa sababu nataka nikuombe; kama kuna ubishi ndani ya Bunge hili kwamba korosho zimeoza au hazijaoza tengeneza kamati ya watu wachache waeendee wakakague kwenye maghala. Nataka nikwambie korosho imeoza kwa asilimia 30, na hakuna ubishi. Narudia; kama kuna ubishi, Mheshimiwa Spika wetu, Mheshimiwa Spika wangu, sisi ndio tunaosimamia Serikali tengeneza watu waende wakaone wakuletee taarifa. Kwa sababu tukizubaa zikiendelea kuoza hata hizo zilizopo tutapata hasara kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Gazeti la Nation la Kenya la tarehe 12 Mei lilikuwa na kichwa cha habari kinachosema President Magufuli aingizwa chaka na lilikuwa tunazingumza juu ya hii kampuni ya Indo Power kwamba hii kampuni ni ya kitapeli sasa tunazungumza kampuni ambayo ilisimama kama middlemen ikaja ikaidanganya nchi, ikaidanganya Serikali yote kwamba ina uwezo; na Serikali yetu, ya nchi yetu ikaingia mikataba na kampuni ambayo kumbe haina uwezo ilikuwa inaenda kutafuta kampuni nyingine.

Mheshimiwa Spika, ulikuwepo wakati wa sakata la Richmond na Mheshimiwa Mwakyembe ndiye alikuwa Mwenyekiti katika kuchunguza sakata lile. Kampuni ya Richmond haikuzalisha umeme; ilionekana kwamba haina uwezo, viongozi waliwajibika hapa. Kampuni ya Indo Power imekuja kutudanganya hapa, tumeingia hasara, hapo ndipo inaingia hoja ya Mheshimiwa Mnyika. Hakuna sababu ya taarifa, hakuna sababu ya miongozo; sisi kama Wabunge tuna wajibu wa kuangalia ni wapi tulipokosea.

Mheshimiwa Spika, sakata la korosho litadumu kizazi hata kizazi kwa sababu maghala sasa yamejaa, msimu unakuja, hakuna maghala ya kuweka korosho, wakulima wanadai, kwa hiyo kutakuwa na hasara mfululizo katika jambo hili, na hii inaenda kuwa kashfa kama za EPA, ESCROW na Richmond. Ndiyo maana sisi tunasema, kwa unyenyekevu wote, suala hili la korosho kama tulijikwaa, kama tuliteleza tusiendee kuvutana bila sababu ya msingi taifa likaendelea kupata hasara na wananchi wakaendelea kupata hasara; kwa sababu ukweli wa tatizo upo. Ndiyo maana naungana na wanaosema Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kama Mheshimiwa Spika utaona haifai uchague watu wachache wakaangalie basi Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali aende akachunguze ili aje aliambie Bunge fedha zilizopelekwa kwenye utaratibu huo ni kiasi fulani zimetumika hivi watu fulani hawakutumia vizuri fedha zilitoka wapi na tumepata hasara kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninasikitika sana kuwa suala ambalo linahusu maslahi ya taifa kulifanyia siasa. Bunge linapotoka kabisa, na Spika una uwezo, na umeshafanya mambo mazuri nayakaleta matokeo mazuri. Hili lipo mikononi mwako tusiache wananchi wetu wakateseka tu na majibu kwa sababu watu tunataka kufanya siasa.

Mheshimiwa Spika, baada yakusema haya ninakuomba sana nizungumze pia habari ya kahawa. Zao la kahawa limefanya mambo mengi mazuri katika nchi hii. Wale mliosoma Sekondari ya Lyamungo ilijengwa na KNCU kwa sababu ya kahawa; wale ambao wanaosoma sasa Chuo cha Ushirikia Moshi na waliosoma Chuo cha Ushirika Moshi kilijengwa na wakulima wa kahawa; kilijengwa kutokana na mapato ya kahawa. Hoteli ya KNCU pale Moshi, Moshi Curing yote kahawa ilifanya kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini zao la kahawa Mkoa wa Kilamanjaro linakufa na linauawa kwa sababu ya ushirika. Ushirika wa KNCU uliingia kwenye kashfa ya namna mbalimbali. Mali za ushirika zilifujwa, mashamba ushirika yalifujwa, wananchi walidhurumiwa na kadhalika na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, lakini yapo matatizo mengine yanayotokana na kwanini zao la korosho linakufa. Bei ni ndogo kwa sababu hatuna masoko ya nje hatuna ya ndani mazuri, na kwa sababu hiyo wakulima wanakata tamaa. Katika Wilaya ya Rombo katika Jimbo langu la Rombo baadhi ya wakulima wamekataa tama. Wanang’oa ile mibuni wanapanda makabichii, nyanya na kadhalika; jambo ambalo si zuri kabisa kwa sababu hata mimi nimesoma kwa kahawa na jua thamani ya kahawa.

Mheshimiwa Spika, mimi ninaiomba Serikali, jinsi ilivyopeleka nguvu kwenye zao la korosho, jinsi inavyopeleka nguvu kwenye zao la pamba iwakumbuke wakulima wa kahawa wa Rombo na wa Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, tuna shida ya Maafisa Ugani; ni wachache na ajira zao zinatoka kwa kusua sua. Wapo wazee wetu ambao wamestaafu wapo kule vijiji ambao wanaweza wakaletwa sasa kwenye mfumo. Wapo vijana ambao wamemaliza shule ambao kwa bahati mbaya hawajaajiriwa bado pia wanaweza wakaletwa kwenye mfumo kwa kujitolea. Wakati mwingine wakulima wale wakiwalipa wao wenyewe; Serikali iangalie namna ya kutengeza progamu ili wawalete hawa watu ili waweze kulisaidi lile zao.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna hoja ya pembejeo kuwa ghali, madawa yako juu na kadhalika na kadhalika. Liangaliwe hilo ili Serikali isaidie pembejeo ziwe naafuu wananchi waweze kununua pembejeo vizuri waweze kuamsha lile zao la kahawa.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya mwisho ni kuhusu umwagiliaji. Tunapoteza maji mengi sana katika nchi hii. Mvua inayonyesha maji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Malizia Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: …maji yanapotea. Kwa hiyo nilikuwa naomba Serikali na Wizara ingalie uwezekano wa ku-tap haya maji ya mvua ili yaweze kuwasidia wananchi katika kilimo na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, ninakushuru, ahsante sana, na ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naona tofauti kubwa sana ya kazi zilizofanywa na Wizara hii katika kipindi hiki na kipindi kilichopita. Kwa hiyo si jambo baya kupongeza juhudi na kazi kubwa iliyofanywa na Wizara hii. Pamoja na hayo ni vyema Wizara ikapokea upungufu mchache ambao tunauleta ili ufanyiwe kazi ili kazi ya Wizara iwe bora zaidi ya hapa ilipofikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niseme mambo matatu tu. Jambo la kwanza, mdogo wangu Mheshimiwa Mnzava amezungumza habari ya Sera ya Nyumba na huu Wakala wa Taifa wa Utafiti wa Nyumba Bora lazima utusaidie, ni aibu kwa Taifa kuwa na nyumba za tembe. Ukiangalia wananchi sio kwamba wanashindwa kujenga, lakini wakipewa aina fulani ya mjengo wanaweza wakaujenga taratibu wakamaliza na vilevile katika miji yetu sasa hivi kuna kujengwa holela tu.

Mheshimiwa Spika, ukienda miji ya wenzetu, najua Mheshimiwa Lukuvi ametembea sana, unakuta kuna eneo mtaa fulani ni marufuku kujenga aina fulani ya nyumba, aina hii ya nyumba ijengwe mahali Fulani. Sasa ni lazima tu miji yetu tuiboreshe vinginevyo tukiachia kila mtu ana plan ramani yake anabuni kitu chake, matokeo yake makazi yetu yatakuwa hovyo hovyo. Kwa hiyo huu Wakala ufanye kazi yake sawasawa kuishauri Serikali kuhusu nyumba ambazo kwa wananchi zinaweza kuwa affordable na vilevile bei na vifaa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine tumesema hapa na nataka nirudie Kambi Rasmi ya Upinzani haipingani na uchukuaji wa mashamba pori, yaani lazima hili lieleweke, sisi tunaunga mkono mashamba ambayo hayajaendelezwa yachukuliwe, tunachosema Serikali sikivu ikikutana na mwananchi mmoja anayelalamika imsikilize kwa sababu kuna baadhi ya wananchi wanalalamika kwamba mashamba yetu yamechukuliwa, lakini ndani yake kuna nyumba, kuna mifugo, kuna mashine na kadhalika. Si jambo baya Serikali ikakaa na watu hawa, ikawasikiliza wakaridhika tu, manung’uniko yakaondoka ndani ya mioyo yao.

Mheshimiwa Spika, lingine…

SPIKA: Mheshimiwa Selasini kwani jamaa si ameenda mahakamani au, endelea kuchangia tu.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, simjui huyo jamaa. Lingine Mheshimiwa Lukuvi akiwa Moshi alitushauri sisi watu wa Kilimanjaro tuache kuzika kwenye mashamba yetu na tulipiga kelele sana kwa sababu sisi kwa mila zetu na desturi zetu hatuwezi kuacha, lakini mimi ningesema hivi watusaidie katika yale maeneo ambayo huo utaratibu bado haujaanzishwa ili yale maeneo yabaki salama kwa sababu najua eneo ambalo limezikiwa thamani yake inapungua. Sasa kuna maeneo mengine kwa mfano kule wilayani, kwenye miji ile ambayo inakua sasa hivi watusaidie ili watu wasije wakapeleka tena huko makaburi, halafu tukapata shida. Sisi hatuna ardhi na kama nilivyosema huu Wakala wa Utafiti wa Nyumba Bora ingetusaidia sana sisi kwa maana sasa hivi hata shule tunajenga za kwenda juu maghorofa lakini tupewe ramani ili ziweze kutusaidia. Kwa hiyo Mheshimiwa Lukuvi hili zoezi sijui kama tutaliacha, lakini anaweza kuendela kuzungumza labda wazee wa kimila tutamsikia.

Mheshimiwa Spika, lingine ni hili la upimaji; upimaji umekuwa ni tatizo kubwa na hizi halmashauri sijui kama zitaweza. Zamani kulikuwa na utaratibu halmashauri zinakopa Wizarani halafu zinalipa kidogo. Nina maeneo pale Holili watu wanatafuta viwanja tumeshindwa kupima, lakini kwa nini Serikali wasirudishe ule utaratibu wa kuzikopesha halmashauri, zikafanya upimaji, zikauza viwanja halafu ile pesa ya kuuza vile viwanja ikarejeshwa kwa kutokana na mkopo ambao watakuwa wamekopa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kwa kusema Mheshimiwa Lukuvi comment aliyotoa mwenzangu Mheshimiwa Devota Minja…

SPIKA: Malizia kwa dakika moja.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: …aliyotoa Mheshimiwa Devota Minja ilikuwa na kusudio la kusema tujenge taasisi, Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri, lakini lazima wale wa chini yake wajengwe ili hata akiondoka pale Wizarani, Wizara iendelee na kazi ambayo tunaona anafanya ni pamoja na restructuring na kuhakikisha wale ambao hawafanyi kazi sawasawa wameondoka, lakini ifike mahali hata akiwa hayupo capacity building, Wizara iendelee kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie kwenye bajeti hii ya Serikali. Ningetaka niseme tu tangu mwanzo kwamba hii siyo bajeti ya Mheshimiwa Dkt. Mpango na mtani wangu Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Ashatu, hii ni bajeti ya Serikali. Bahati mbaya sana Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa sababu ni Waziri anapokea hayo madongo na namjua ni mtu mnyenyekevu anayapokea pia kwa shukrani, kwa hiyo, mzee pokea tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, niseme ninaunga mkono sera ya Serikali ya viwanda na kama Mheshimiwa Mlinga angekuwepo aoneshe Ilani ya CHADEMA angeona kwamba vilevile hiyo sera ipo. Kwa sababu ni mapinduzi ya viwanda yatakayotusaidia kusonga mbele katika nchi hii. Ningependa nitoe ushauri kuhusiana na jambo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ningesema kwamba basi Serikali ijitahidi kabla haijahamasisha au sambamba na uhamasishaji wa viwanda vipya, ifufue vile viwanda vya zamani vilivyojengwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Nyerere na kama mtakumbuka, Mwalimu alijenga viwanda karibu katika kila mkoa, kanda na alijenga viwanda kwa ajili ya kuyapa mazao yetu thamani. Tanga alijenga viwanda vya nyuzi, nguo, katani na viwanda vya magunia na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda hivi vilikuwa vimesambaa maeneo mengi katika nchi yetu, kwa mfano, pale Moshi kulikuwa na Kiwanda cha Machine Tools, Kiwanda cha Magunia, Kiwanda cha Plywood, Kibo Match, Coffee Curing, Moshi Textile, Kiwanda cha Pipi, Kiwanda cha Dawa za Mimea, Pharmaceutical Industry, Plastic Court, ICC Meal Café, Kiwanda cha Bidhaa za Misitu na Kibo Paper, vyote hivi vimekufa. Sasa tunahangaika kufungua viwanda vingine lakini viwanda hivi ambavyo vilianzishwa vingine kwa kodi za wananchi na utaalam na wataalam wenyewe wapo tunaviacha tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nashauri hivi kwamba Serikali iamue kwa makusudi mazima kama ilivyoamua kuchukua mashamba pori vile viwanda ambavyo vilibinafsishwa na wale wawekezaji hawakuviendeleza kadri ya mkataba, Serikali ichukue vile viwanda, itafutie Vyama vya Ushirika au labda wananchi ambao wana uwezo wa kuendesha hivi viwanda waendeshe hivi viwanda kwa sababu hivi viwanda ni mali yetu na vilianzishwa kwa kodi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu vilevile napendekeza sambamba na hili tuhakikishe kwamba tunarejesha imani ya wawekezaji kwa sababu ni kujidanganya kusema kwamba sisi wenyewe tuna uwezo wa kuanzisha viwanda wenyewe tu hapa ndani. Sisi tuko katika dunia ambayo imegeuka kuwa kijiji. Sasa katika hilo ningependekeza sasa Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango hapa pamoja na timu yake waangalie kodi zetu katika mambo mbalimbali. Wizara ya Ardhi iangalie namna ambavyo wawekezaji wanakuja hapa kupata maeneo ya kuanzisha viwanda kwa urahisi. Halafu na hawa viongozi wetu watu wazima, waangalie namna ya kuongea, kuwapa semina hawa viongozi vijana ili waangalie lugha ya kuongea na wawekezaji, vinginevyo mwekezaji mmoja akisumbuliwa hapa, akienda nje matokeo yake anaenda kuharibu image ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, ningesema haiwezekani suala la uanzishaji wa viwanda likabaki kwenye Wizara ya Viwanda peke yake, vinginevyo mtawatumbua Mawaziri wa Viwanda kila uchao. Ningeshauri iundwe timu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda, Wizara ya Uwekezaji, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Ardhi na Wizara ya Mambo ya Nje kuangalia namna bora ya kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza. Wizara ya Mambo ya Nje ina mchango mkubwa sana kwa sababu yenyewe ndiyo inayoliuza Taifa nje. Sasa kama Wizara ya Mambo ya Nje haitachukua lead, tukasema tunaachia Wizara ya Viwanda, kuna mahali tutashindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kilimo sitazungumza mengi. Naomba ushauri unaotolewa na Wabunge kuhusu kilimo ufuatwe kwa sababu wananchi katika maeneo yote wanahangaika. Kilimanjaro ilikuwa mzalishaji mzuri sana wa kahawa aina ya arabica lakini sasa hivi imekwenda na maji. Wakulima wanang’oa kahawa, wanapanda vitu vingine. Sasa tujiulize tumekosea wapi, tuwasaidie, kama ni pembejeo, kama ni masoko, kama ni utafiti tuwasaidie kwa sababu asilimia 75 ya Watanzania ni wazi wamejiajiri katika kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza ni hili la pads. Nashangaa akisimama Mbunge mwanamke katika Bunge hili kuunga mkono hili pendekezo la Serikali halafu hatoi solution, nashangaa sana kwa sababu ni TWPG pamoja na wanawake wote humu ndani walileta hilo pendekezo katika Bunge lililopita. Sasa ni kweli hilo pendekezo halikuweza kuzaa matunda, lakini tuache hivi hivi na kama kuna mtu ana watoto wa kike na yuko karibu naye anafuatilia, atagundua mtoto wa kike akipewa mtihani wakati wa zile siku lazima atayumba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nasema hivi; sisi katika Kamati yetu ya Utawala tulishatoa agizo kwa Halmashauri zote kwamba hatuwezi tukaongea nao katika bajeti ijayo kama Mkurugenzi hatatuambia kwamba amenunua hizo pedi na kugawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuliwapa utaratibu, tulisema kwamba ni lazima kila shule iwe na choo kizuri, iwe na chumba ambacho kitakuwa na sehemu ya kuhifadhi hizo pedi, iwe na dustbin ya kutupia na kadhalika. Sasa Wabunge wanawake nendeni kwa mtindo huo, kwa sababu sisi hatuwezi, wale watoto wanateseka. Watoto katika karne hii wa Kitanzania wanatembea na makanga machafu, wanajihifadhi kwa majani na kadhalika, halafu mtu anasimama hapa anasema hakuna cha bure! Sisi hatusemi mtoto wa Selasini apewe, sisi tunasema watoto wa maskini wapewe na kwa sababu wote wapo kwenye shule moja, basi watoto wanazipata pale shuleni na wala sio nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshangaa mtu anasema kwamba anaweza akapewa akampelekea mama yake, kwanza akimpelekea mama yake so what? Si amesaidia, lakini vinginevyo, hili sio suala la kuzungumza. Naomba Mheshimiwa Waziri akae na Mwenyekiti wa Kamati ya TAMISEMI, sisi hili agizo tulishalitoa na katika Kamati yetu walipokuja katika Bunge hili kuna Halmashauri zilikuwa zinatupa ripoti kwamba sisi tumeshatekeleza by half, sisi tumeshatekeleza asilimia 100. Kwa hiyo kama hili la kodi linawashinda, tuchukue hili lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningetaka niliseme kwa haraka haraka ni kuhusu TARURA, uamuzi tuliofanya wa TARURA ulikuwa uamuzi mzuri, lakini TARURA haina pesa na kwa sababu hiyo haiwezi kutekelezea miradi yake vizuri. Mwaka 2018/2019 katika Jimbo langu bajeti ilikuwa shilingi milioni 850, zimeenda shilingi milioni 550, wameweza kufanya miradi minne tu. Safari hii wamewaambia ceiling ni shilingi milioni 700. Wameniambia hawawezi kumaliza miradi viporo na wakafanya hata mradi mmoja.

Kwa hiyo, pamoja na kwamba najua kuna mikoa ambayo haijaunganishwa bado na lami kwa mfano Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Katavi, hilo jambo linaweza likafanyika, lakini kwenye bajeti ijayo waangalie namna ile Road Fund kuigawa labda TARURA half na TANROADS half baada ya kumaliza kuunganisha ile mikoa mingine ambayo bado haijaunganishwa, kwa sababu kwa mfano jimbo langu, ukanda wa juu wote ambao una volcanic soil, una mawe makubwa sana, TARURA hawawezi kufanya hiyo kazi. Kwa hiyo naomba hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi barabara ni muhimu sana, tunaweza tukajenga reli, tukajenga barabara za lami, sasa hizi feeder roads kama hazitajengwa ni shida na tulishawaaminisha wananchi wetu kwamba halmashauri inajenga. Kwa hiyo Madiwani na Wabunge wanalalamikiwa kumbe kuna chombo kinaitwa TARURA ambacho kinajenga…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, wakati tunaelekea katika ukomo wa Bunge hili, napenda kuchukua fursa hii kukupongeza na kuwapongeza Wabunge wenzangu wote kwa kazi tuliyofanya hapa kwa muda wa miaka hii mitano.

Mheshimiwa Spika, tumepata changamoto kadhaa lakini sote tumshukuru Mungu na changamoto hizo zitumike katika kuboresha Bunge la Kumi na Mbili.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Waziri Mkuu kuna mambo mengi yaliyozungumzwa. Hata hivyo ningependa kuchangia yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kuhusu elimu kuna ongezeko kubwa la watoto wanaoingia katika shule za msingi na sekondari hasa baada ya Serikali kuondoa ada. Hata hivyo ongezeko hilo haliendani na hali halisi iliyopo katika shule zetu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu uhaba wa walimu, ili kuhakikisha dhamira ya Serikali kukuza elimu inafanikiwa, Serikali inao wajibu wa kuongeza ajira za walimu pamoja na uboreshaji stahiki zao yaani makazi yao, mishahara, posho na stahiki nyingine.

Mheshimiwa Spika, pili ni vyumba vya madarasa, kila mwanzo wa mwaka wa masomo katika kidato cha kwanza na cha sita kunakuwa na upungufu wa vyumba vya madarasa. Hali hii inaleta usumbufu mkubwa kwa wanafunzi kwa kuwa wengine huchelewa kuanza masomo. Kwa kuwa idadi ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na wale wanaomaliza kidato cha nne wanajulikana, wataalam wetu wanao wajibu wa kulishughulikia tatizo hili mapema ili kuondoa usumbufu.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo bado tuna upungufu mkubwa wa vyumba vya maabara na vifaa vya maabara, ni vema Serikali kuangalia katika bajeti hii uwezekano wa kukamilisha vyumba vya maabara ambavyo vilianzishwa.

Mheshimiwa Spika, shule nyingi za zamani za msingi zinaelekea kubomoka. Jimboni kwangu kuna shule nyingi zinabomoka na hazikaliki au zinapaswa kufungwa. Kama Serikali ilivyofanya jitihada ya kuboresha shule za sekondari za zamani ione uwezekano wa kuboresha shule za misingi pia.

Mheshimiwa Spika, tatu ni shule za ufundi; ni muhimu tuharakishe ujenzi wa shule za ufundi katika kila Wilaya hasa kipindi hiki ambacho tunahimiza uchumi wa viwanda na kuimarisha private sector ili vijana wetu baada ya kumaliza elimu yao katika ngazi mbalimbali waweze kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, mageuzi yaliyofanyika kuanzishwa kwa TARURA yameleta mafanikio makubwa sana katika Halmashauri zetu. Hata hivyo, TARURA inakumbwa na tatizo kubwa la kibajeti.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iangalie uwezekano wa fedha za Mfuko wa Barabara kugawanywa kwa kiwango sawa kati ya TANROADS na TARURA.

Mheshimiwa Spika, tatizo la maji ni kubwa sana nchi nzima. Katika jimbo langu limekuwa kubwa zaidi kwa sabubu ya mabadiliko ya tabianchi yaliyosababisha chemichemi nyingi kukauka, ongezeko la binadamu na wanyama na kadhalika. Pamoja na hayo yote chanzo cha maji kimekuwa kile kile tangu enzi za ukoloni.

Mheshimiwa Spika, napenda kuishukuru Serikali kwa dhamira yake ya kuanzisha chanzo kipya cha Ziwa Chala. Naiomba Serikali iharakishe utekelezaji wa mradi huu ili kupunguza tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo tunapoteza maji mengi sana kutokana na maji ya mvua. Wilaya ya Rombo tuna mito mingi sana ya msimu na inayopitisha maji mengi sana wakati wa mvua na ina makorongo ambayo yanaweza kuzuiwa ili kuhifadhi maji hayo sambamba na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kuhifadhi maji.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuporomoka kwa vyama vya ushirika Waziri Mkuu amefanya jitihada kubwa za kuufufua na kupambana na ufisadi ndani ya ushirika. Chama cha Ushirika cha KNCU ambacho nacho kiliingiliwa na ufisadi kilikuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa kahawa katika Wilaya ya Rombo na Mkoa wa Kilimanjaro kwa jumla. Hivi sasa wakulima wengi wameamua kuachana na kilimo cha kahawa na kupanda mbogamboga na migomba. Licha ya ushirika, pembejeo ni ghali sana, bei ni ndogo na hivyo kuwakatisha tamaa wakulima. Ni vema Serikali iingilie kati ili zao hilo lisije likatoweka maana lilikuwa chanzo kikubwa cha fedha za kigeni na uchumi wa wananchi.

Mheshimiwa Spika, umezuka ukatili wa kuwadhalilisha watoto katika jamii. Watoto wanaingiliwa kinyume na maumbile, wanaingiliana wenyewe kwa wenyewe na mimba za utotoni mashuleni. Wengi hawaongelei jambo hili kwa kuchelea aibu lakini kama Taifa tusipokuwa makini Taifa letu linaweza kuja kugeuka kuwa la mashoga. Serikali iondoe uoga, ichunguze na kushughulikia tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa nishati, kazi inayofanyika kupeleka umeme vijijini na REA ni nzuri na ya kupongeza. Naiomba Serikali kuendelea kumaliza maeneo yaliyobaki na hasa katika jimbo langu yapo maeneo yaliyobaki na yenye malalamiko yafanyiwe kazi ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa afya, katika awamu hii hospitali na vituo vingi vya afya vimejengwa nchi nzima. Katika Jimbo la Rombo ipo Hospitali ya Wilaya inajengwa na kituo cha afya. Hata hivyo Rombo tuna uhaba mkubwa wa watumishi wa idara ya afya. Ninaishauri sana Serikali kwamba sambamba na ujenzi wa hospitali na vituo hivi vya afya Serikali iajiri watumishi wa afya nchini kote.

Mheshimiwa Spika, mwisho mengi yamefanyika katika awamu hii. Katika miundombinu, sekta zote yaani barabara ingawa mvua zinazoendelea kunyesha imeleta athari kubwa lakini kazi inaendelea, usafiri wa anga na reli kazi zinaendelea, hali kadhalika meli na vivuko katika maziwa yetu yameboresha usafiri na sekta ya uvuvi. Kwa hali hiyo kama Watanzania tunao wajibu wa kupongeza jitihada hizi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kuwasilisha.