Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Anthony Calist Komu (24 total)

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa swali la Mheshimiwa Raphael Japhary linafanana na hali ilivyo Moshi Vijijini, kuna kiwanda kilifunguliwa mwaka 1975 na Mwalimu Nyerere na kiwanda kile ni cha ngozi hakikupata mwekezaji mpaka leo, na kimepangishwa kwa shilingi 20,000 kwa mwezi. Naomba Waziri aniambie ni lini atakuwa tayari kwenda kuona hiyo hali nakuchukua hiyo hatua zinazoyostahiki?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Antony Komu, Waziri Kivuli wa Viwanda Biashara na Uwekezaji kuhusu kiwanda chake cha mwaka 1975 Moshi ambacho hakukitaja jina. Kwa kweli nitakudanganya nikisema ninakijua kwa sababu hukukitaja jina, niko tayari wewe unipeleke unionyeshe kiwanda tukitafutie majawabu.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri isipokuwa kwa mujibu wa Tume mbalimbali za Haki za Binadamu na hasa ile ya Umoja wa Mataifa ratio ya polisi na wananchi wanasema inapaswa kuwa 1:450 lakini katika nchi yetu ni 1:1300. Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wameamua kusitisha kwa muda ajira kutokana na mambo hayo mengine ambayo wanayafanya, naomba niulize haoni kwamba kufanya hivyo ni kuendelea kukuza lile tatizo la uwiano? Pia katika hiyo ratio ambayo nimeitaja, wanawake ni wachache kweli na ndiyo maana hata humu ndani ya Bunge ikitokea kitu chochote askari wa kiume wanakuja kuwakabili wanawake kwa sababu ya upungufu. Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, zipo taarifa kwamba katika jeshi letu wako watu wanaajiriwa na inachukua muda sana kwenda kwenye mafunzo ya msingi ya uaskari wakati jambo hili la uaskari linahitaji maadili ambayo ni maalum kwa sababu ni jambo nyeti. Siku zote kisingizio kimekuwa ni bajeti, sasa nataka kujua hali ikoje sasa hivi kama wameshakuwa na uwezo wa kumudu hali hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nirekebishe kidogo, uwiano wa askari kimataifa ni askari 1:400 na kwa upande wa Tanzania Bara ni askari 1:1200, kwa hiyo kidogo kuna utofauti na maelezo ambayo ametoa Mheshimiwa Mbunge. Niseme tu usitishaji huu hauathiri kwa sababu ni usitishaji wa muda mfupi sana, kuna mambo tu kidogo ambayo yanawekwa sawa, nadhani muda si mrefu tutaendelea na utaratibu wetu kama kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na swali lake la pili kwamba kuna upungufu wa wanawake katika Jeshi la Polisi, ni kweli na tunapoelekea kwenye fifty-fifty basi nitoe wito tu kwa wanawake kuhamasika zaidi ili kujiunga na vyombo vya ulinzi na usalama.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Nimesikia majibu ya Serikali kwa upande wa jinsi Serikali zitakavyoshughulika na hawa watu ambao wanaleta matatizo, lakini kuna matatizo ambayo yanasababishwa na Serikali. Kwa mfano kule Moshi Vijijini katika Kata ya TPC
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
17
watoto wa kike wanatembea kilometa kumi, saba kutoka eneo linaitwa Chemchem kwenda kutafuta shule iliko, na haya ni mashamba ya miwa ambapo kuna mambo membo mengi sana yanaweza kutokea hapo katikati, kuomba lift na vitu kama hivyo. Sasa Serikali inaweza kutuambia nini kuhusiana na hali kama hiyo; labda kujenga mabweni kwenye shule za aina hiyo ambazo ziko mbali kiasi hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA:Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya mwanza nilizungumzia suala ambalo Mheshimiwa Komu amelisema na hili linanipa faraja kubwa sana, kuona kila Mbunge hapa anasimama katika ajenda ya kumuokoa mtoto wa kike, hili naomba nishukuru sana. Na katika hili naomba niwaambie Wabunge tutaendelea kwa kadiri iwezekanavyo kuhakikisha kwamba tunasimika mabweni maeneo ya jirani, lakini sio mabweni peke yake, tutahakikisha kwamba jinsi gani tunafanya nguvu ya pamoja kwa ajili ya kuleta solidarity hata kwa wazazi; kwa sababu kuna maeneo mengine mabweni yamejengwa lakini watoto wanapenda kukaa uswahilini au kutembea mbali zaidi kwa sababu kuna mambo yao yale ya ku-discuss zaidi wanayoyapenda.
Kwa hiyo, sisi tutahakikisha kwamba tunasimamia na kuhamasisha wazazi wote; lakini kama Ofisi ya TAMISEMI inaliona hilo kwa sababu Wizara ya Afya imejielekeza vya kutosha katika kumuokoa mtoto wa kike na Wabunge wote, mimi naamini jambo hili tutafanikiwa kwa karibu zaidi.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba yake kwa sababu hayupo, yupo safari.
Pamoja na majibu ya Naibu Waziri; jambo hili limechukua muda mrefu na kama nchi ilivyokwishaamua kwamba inakwenda kwenye mpango wa viwanda na uchumi wa kati, jambo hili ni muhimu sana. Sasa nataka kujua:-
(i) Ni lini sasa huo mchakato utakamilika ili jambo hili liweze kuanza?
(ii) Napenda kujua vilevile kutoka kwenye Serikali, ni mambo gani hayo hasa ambayo yamepelekea huo mchakato kurejeshwa tena kwenye kufanyiwa marekebisho na vitu kama hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kama nilivyosema kwamba tukifanya rejea Bunge lililopita, nilisema kuna timu ya TAMISEMI itapita maeneo mbalimbali; na lengo kubwa ni kubaini kwamba yale maombi yaliyoletwa kutoka katika Ofisi za Mikoa baada ya vikao vya RCC kukaa, kwamba maombi yale sasa wataalam wakienda kufanya tathmini wataona jambo lipi limekamilika na jambo lipi halijakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri naomba nikujulishe kwamba ofisi yetu imeshatuma timu katika maeneo hayo yote na kazi hiyo wameshamaliza. Hivi sasa wana-compile ripoti yao baadaye kuweza kutushauri vizuri jinsi gani ya kufanya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Komu vuta subira jambo hili litaenda vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili kwamba mambo gani mwanzo yalikuwa hayajakamilika; ni kwamba ukiangalia Mji wa Moshi, square kilometer karibu 58 peke yake, yaani ni eneo dogo sana kuwa Jiji. Ndiyo maana walidhani kama ingewezekana ni kuongeza eneo lile la utawala na ndiyo maana nadhani wameona maeneo waliyokubaliana katika muhtasari wa mwisho, eneo limeongezeka mpaka maeneo ya Hai na maeneo mengine. Ina maana kwamba eneo limevuka kutoka zile square kilometer 58 imeenda mpaka karibu 142.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na mambo mengine hasa yanayohusu master plan. Kwa hiyo, vitu hivi vyote vilileta mrejesho, walipelekewa mrejesho watu wa Moshi kule kwenda kuvifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu ni kwamba marekebisho yale yameshafanyika, sasa wahakiki wetu walivyoenda kuangalia kule site, watajua ni jinsi gani vile vilivyoelekezwa vimeweza kufikiwa vizuri na baadaye Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana atafanya maamuzi. Naomba tusiwe na hofu, kila kitu kitaenda kwa utaratibu ambao umepangwa katika ofisi.
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Kwa kuwa, wananchi wa Moshi Vijijini kule Tarafa ya Kibosho katika Kata sita,
Kata ya Kirima, Kibosho Kati, Okaoni, Kibosho Magharibi na Kibosho Mashariki
wameshaitikia huu wito na kujenga chuo ambacho kwa kweli kina hadhi kubwa
sana na kinaweza hata kubeba Wilaya kama mbili, tatu. Waziri atakuwa tayari
kwenda na mimi kule kwenda kuona hiki chuo na kukiwekea utaratibu mzuri,
maana naamini akienda kule ataweza kukiwekea utaratibu mzuri wa kukipa
ruzuku kama Walimu na kadhalika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu
Spika, kwanza nawapongeza wananchi kwa kutambua umuhimu wa stadi za
kazi kwa wanafunzi wa vyuo hivyo.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa hali ya Momba ni sawa sawa na Moshi Vijijini, kwa sababu Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliahidi kujenga barabara ya Kibosho kwa Raphael kupitia central mpaka International School; na kazi hiyo ilianza lakini mkandarasi ameondoka site. Vilevile Rais wa Awamu ya Tano Mheshimiwa John Pombe Magufuli aliahidi kujenga barabara ya Mamboleo mpaka Uru Shimbwe kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nijue ni lini ahadi hizi zitatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Komu tuonane ili anipe taarifa za zaidi hasa ya huyo mkandarasi ambaye anasema ameondoka site. Njoo ili tuhakikishe huyo mkandarasi anarudi kwa sababu tulishatoa maelekezo wakandarasi wote ambao walikuwa wamesimama kwa sababu ya kutolipwa warudi site, sasa nashangaa leo naambiwa kuna mkandarasi huku tena kwenye barabara muhimu sana ya ndugu zangu kule wa Kilimanjaro. Hebu njoo ofisini tuongee kwa undani tulifanyie kazi na wataalam wetu wa Mikoa wa TANROADS au wa Halmashauri.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Kwa hali ilivyo sasa hivi Moshi Vijijini barabara nyingi hazipitiki na hali ni mbaya sana katika kata ya Mabogini barabara inayoanzia Bogini kwenda Chekereri mpaka kule Kahe na kule Uru Mashariki kata ya Uru Madukani, Mamboleo, Kishumundu mpaka kule Materuri. Hizi barabara zote zimeshaombewa kupandishwa daraja lakini hakuna kinachoeleweka. Sasa ninataka kufahamu kutoka kwa Waziri atakuwa tayari kutoa agizo kwa ajili ya kufanyika tathmini maalum ili hizi barabara tujue tatizo liko wapi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaamini Halmashauri iendelee kurekebisha hii barabara iweze kupitika muda wote, lakini wakati huo huo majibu ya barabara zipi tutapandisha hadhi yatakuja muda sio mrefu ujao.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kule Moshi Vijijini kuna vyanzo vingi vya kitalii ambazo havijatangazwa vizuri. Kwa mfano, kule Kata ya Uru Mashariki kuna maanguko ya maji ya ajabu sana yanaitwa Mnambeni na hivi karibuni katika Kata ya Mbokomu, kumevumbuliwa mti ambao unasemekana ni mrefu kuliko miti yote katika Bara la Afrika. Sasa nataka kufahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini Serikali itachukua hatua za makusudi kuweza kuvitambua hivi vyanzo na kuvitangaza inavyostahili ili tuweze kuvitumia kikamilifu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu hii ni tajiri sana ya vivutio vya utalii. Kama nafasi ingekuwepo, karibu kila Mbunge hapa angeweza kusimama na kueleza kwamba katika Halmashauri yake kuna kivutio hiki na kile; sasa suala la kuboresha utangazaji siyo suala la Serikali peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kuweza kuboresha matangaza ambayo sasa hivi tunafanya, nitoe wito sasa kwa Mbunge moja moja lakini kupitia Halmashauri zinazohusika kuanza kuvibainisha vivutio vilivyopo kwenye maeneo yao ili viweze kwenda mbele ya wataalam wa Idara ya Utalii katika Wizara ya Maliasili na Utalii tuweze kuviorodhesha kwa pamoja, halafu tukubaliane kama vinakidhi viwango vya Kimataifa kama vivutio, tuweze kuvifanyia grading, halafu baada ya pale tuendelee na utaratibu wa kutangaza tukitambua kwamba ni jukumu letu sote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 mwananchi mmoja wa Kenya alitamka maneno kwenye mkutano mmoja wa Kimataifa kwenye nchi mojawapo nje kule, kwa kurusha tu clip ndogo tu lakini ikatingisha dunia, lakini pia na sisi Watanzania tukaanza kusema kwa nini wanataka kuteka vivutio vyetu? Ule haukuwa mpango wa Serikali, ni mtu mmoja tu alifanya vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi wa Tanzania nasi kwanza tushiriki katika utalii wa ndani ili tuvifahamu vivutio vyetu na sifa zake halafu baada ya pale nasi tuweze kushiriki kama Watanzania kutangaza vivutio vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kushirikiana na wenzetu walioko nchi za nje kwa utaratibu wa diaspora ili tuweze kufanya nchi yetu ikapata kutangazwa sawa sawa kwa maana ya vivutio vya utalii. (Makofi)
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Kwa kuwa ugonjwa wa malaria ni ugonjwa ambao unaongoza kwa kuua katika nchi hii na ninaamini kwamba Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kupambana na malaria. Ni kwa nini Waziri asione kuna umuhimu wa fedha zote ambazo zimetengwa kwa ajili ya kupambana na malaria zikapelekwa kwenda kununua dawa za viuadudu Kibaha ili kupambana na malaria ikizingatiwa hicho kiwanda sasa hivi kimesimama kuzalisha kwa sababu ya kukosa soko la bidhaa zake?
NAIBU WAZIRI WA WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba kwa nini tusichukue fedha zote tukapeleka kwa ajili ya kununua biolarvicide pale Kibaha kwa ajili ya Halmashauri zetu nchini. Hatuwezi kufanya hivyo kwa sababu udhibiti wa malaria siyo kuua larva peke yake tunamu-attack adui mbu katika hatua nyingi tofauti tofauti, lakini pia tunamu-attack kile kijidudu chenyewe ambacho kinaambukiza malaria yaani plasmodium falciparum katika hatua nyingi tofauti. Kwa hivyo, mikakati ni mingi ambayo inamlenga adui mmoja kwamba yule vector ambaye ni mbu either wa aina ya anopheles ama tunamu-attack plasmodium mwenyewe akiishaingia kwenye damu ndiyo control inakuwa hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo hatuwezi kutumia njia moja kumu-attack adui kwamba tunaua tu mazalia yaani larvae halafu tunasema basi ndiyo tumemaliza, hapana! Lazima kuwe kuna tiba. Kwa hiyo, ndiyo maana tuna mkakati wa kusambaza ALU (Artemether na Lumefantrine combination) nchi nzima na tunagawa bure ili tuue plasmodium falciparum ambaye yumo kwenye damu. Ndiyo maana tuna mkakati wa wajawazito, tunatumia SP (Sulfadoxine Pyrimethamine) kwa ajili ya kumuua mdudu mbu ambaye anawa-attack akina mama wajawazito.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tuna net kwa ajili ya kuzuia mbu ambao wanapenda kuishi ndani ya nyumba na wanauma saa sita usiku kuambukiza malaria. Sasa tuna mikakati mingi, tunatumia IRS – Indoor Residual Spraying kwa ajili ya kumu-attack mbu ambaye anapenda kubaki ndani ya nyumba, mchana hatoki nje anabaki ndani ili asiwepo. Kuna mikakati ya kumuua mbu kama atakuwa nje kwenye mzingira. Sasa hii ya kwenye mazingira ndiyo tunaona teknolojia hii mpya ya biolarvicides itatusaidia. Vinginevyo tungetumia DDT. (Makofi)
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Moshi vijijini kuna mashamba ambayo toka mwaka 1968 yalitaifishwa na kimsingi ni mashamba ya umma, lakini baada ya kutaifishwa na kupewa Vyama vya Ushirika yamekuwa yakigawanywa kwa taasisi mbalimbali kwa ajili ya shughuli za wananchi. Sasa hizo taasisi zikitaka kupima hayo mashamba sasa kulingana na shughuli ambazo zinafanyika inakuwa vigumu kwa sababu tayari kuna hati ambazo zilikuwepo toka wakati huo, ikiwa ni pamoja na eneo kama la Uru Seminari ambalo nilishalifikisha kwa Mheshimiwa Waziri.
Naomba kujua kutoka kwenye Serikalini ni lini Serikali itakwenda kufanya upimaji upya ili kutoa hati kulingana na matumizi ambayo yapo sasa hivi katika yale mashamba katika Kata zote hizo?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mkoa wa Kilimanjaro na mashamba ya ushirika ni tatizo kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamna mashamba haya yalikuwa ni ya settlers, uamuzi wa Baba wa Taifa yalichukuliwa yakapewa Vyama vya Ushirika na mashamba haya ni mengi sana Mkoa wa Kilimanjaro ambayo yalimilikishwa Vyama vya Ushirika. Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo nimeshamwandikia lakini tunazungumza nia njema zaidi ya kuhakiki upya mashamba yanayomilikiwa na Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro hivi sasa. Ni kweli Vyama vya Ushirika zamani vilipewa, lakini leo matumizi yake ya vyama vya ushirika na ushirika wenyewe ni tofauti na madhumuni ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Mkoa wa Kilimanjaro maana hoja hii siyo ya Mheshimiwa Mbunge peke yake, Wabunge wote wa Kilimanjaro mashamba haya yanawahusu. Watuachie bado tuko kwenye mazungumzo na Wizara ya Kilimo ambaye ndiyo Msajili wa Vyama vya Ushirika ili tuone namna gani njema ya kuyahuisha mashamba yote ya ushirika ya Mkoa wa Kilimanjaro ili yawe na tija kwa wananchi wote kulingana na mazingira ya sasa. (Makofi)
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana kwa kuniona. Kwa kuwa, hivi karibuni Serikali kupitia Waziri Jafo ilitangaza kwamba au ilitoa agizo kila mkoa utengeneze viwanda 100 na kwa kuwa vyuo hivi vya ufundi ni muhimu sana. Je, ni lini Serikali itaanza kutoa ruzuku kama ilivyokuwa ikiahidi mara kwa mara kwenye vile vyuo ambavyo ni vya wananchi, kule kwangu kuna vyuo vya Mawelas, KVTC, Imani ili azma hiyo ya Serikali iweze kutimia haraka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika moja kati ya majibu yangu leo, kwa kuanzia tunaanza na ukarabati kabla hatujaanza kufikiria kutoa ruzuku tunaanza kwanza na ukarabati, kama nilivyosema tumepata Dola milioni 120 tunaanza kukarabati vyuo 30 kwanza kati ya 55.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Komu achukulie kama ni hatua mojawapo kufikia hicho anachotaka ili vyuo vyake viweze kushindania fursa hii ya kukarabatiwa; baadaye sasa vikishakuwa katika hali nzuri ya kuchukua wanafunzi ndiyo tuanze kufikiria masuala mengine kama ruzuku. Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa, Halmashauri ya Moshi imeshatenga bajeti kwa ajili ya kujinunulia mitambo, naomba niulize kama Serikali itakuwa tayari kuji-commit kushirikiana na sisi ili tuweze kufanya hizo njia mbadala za kupata mitambo kukwepa zile gharama za mara kwa mara za kukarabati barabara kutokana na ukosefu wa mitambo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Komu nadhani sitoweza kusema commitment kwa sababu lazima kama ofisi yetu ione andiko hilo linasemaje. Kwa sababu kama kuna andiko linakuja katika Ofisi ya Rais lazima tuliangalie, needs assessment inafanyika lakini hizo fedha zinapatikana wapi. Lengo kubwa ni mwisho wa siku baada ya kufanya hilo inawezekana tunaisaidia hata Halmashauri yenyewe kwa sababu unaweza ukafanya jambo ukaingia commitment hapa, baadaye linaweza likaleta athari kubwa sana kwa wananchi wa eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, imani yetu kubwa ni kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI itapokea mawazo mazuri yote na tutayafanyia kazi. Mambo kama hayo yakija kwetu maana yake tutafanya, kwa sababu ni sehemu ya utalii lazima miundombinu yake iwe rafiki. Kwa hiyo, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, mlango wake utakuwa wazi kujadiliana na kushauri vizuri, mwisho wa siku tupate mipango mizuri katika nchi yetu.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kule Moshi Vijijini kuna vyanzo vingi vya kitalii ambazo havijatangazwa vizuri. Kwa mfano, kule Kata ya Uru Mashariki kuna maanguko ya maji ya ajabu sana yanaitwa Mnambeni na hivi karibuni katika Kata ya Mbokomu, kumevumbuliwa mti ambao unasemekana ni mrefu kuliko miti yote katika Bara la Afrika. Sasa nataka kufahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini Serikali itachukua hatua za makusudi kuweza kuvitambua hivi vyanzo na kuvitangaza inavyostahili ili tuweze kuvitumia kikamilifu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu hii ni tajiri sana ya vivutio vya utalii. Kama nafasi ingekuwepo, karibu kila Mbunge hapa angeweza kusimama na kueleza kwamba katika Halmashauri yake kuna kivutio hiki na kile; sasa suala la kuboresha utangazaji siyo suala la Serikali peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Serikali inaendelea na utaratibu wa kuweza kuboresha matangaza ambayo sasa hivi tunafanya, nitoe wito sasa kwa Mbunge moja moja lakini kupitia Halmashauri zinazohusika kuanza kuvibainisha vivutio vilivyopo kwenye maeneo yao ili viweze kwenda mbele ya wataalam wa Idara ya Utalii katika Wizara ya Maliasili na Utalii tuweze kuviorodhesha kwa pamoja, halafu tukubaliane kama vinakidhi viwango vya Kimataifa kama vivutio, tuweze kuvifanyia grading, halafu baada ya pale tuendelee na utaratibu wa kutangaza tukitambua kwamba ni jukumu letu sote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 mwananchi mmoja wa Kenya alitamka maneno kwenye mkutano mmoja wa Kimataifa kwenye nchi mojawapo nje kule, kwa kurusha tu clip ndogo tu lakini ikatingisha dunia, lakini pia na sisi Watanzania tukaanza kusema kwa nini wanataka kuteka vivutio vyetu? Ule haukuwa mpango wa Serikali, ni mtu mmoja tu alifanya vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi wa Tanzania nasi kwanza tushiriki katika utalii wa ndani ili tuvifahamu vivutio vyetu na sifa zake halafu baada ya pale nasi tuweze kushiriki kama Watanzania kutangaza vivutio vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaweza kushirikiana na wenzetu walioko nchi za nje kwa utaratibu wa diaspora ili tuweze kufanya nchi yetu ikapata kutangazwa sawa sawa kwa maana ya vivutio vya utalii. (Makofi
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba bandari hii au mradi huu ni wa muhimu na utaleta nafuu kubwa sana kwa wananchi wa Kigoma, naomba Serikali iwaambie watu wa Kigoma, kwa kuwa mradi huu umeshachelewa sana, imetenga kiasi gani kwa bajeti inayokuja kwa ajili ya kuhakikisha sasa mradi huu unaanza mara moja? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kule Moshi tuna tatizo kama hili la Kigoma, tuna Stendi ya Kimataifa inapaswa kujengwa pale na Benki ya Dunia iko tayari kutoa fedha. Nataka nijue kutoka Serikalini, ni lini kibali kitatoka kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi hiyo li tuweze kunufaika na huo msaada kutoka World Bank?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kazi inayofanyika sasa hivi kama nilivyoeleza katika jibu la msingi ni kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kazi hiyo ikishakamilika wale ndiyo watatupa gharama zinazostahili kufanya kazi husika na ndipo tutakapojua tunatumia gharama gani katika ujenzi wa hiyo sehemu ambayo Mheshimiwa Mbunge anaifuatilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili kuhusu stendi, nikiri kwamba umuhimu wa kuwekwa stendi hiyo ni mkubwa sana kwa sababu ni kweli Benki ya Dunia imeonesha nia ya kufadhili. Hata hivyo, bado Serikali inaendelea na majadiliano na Benki ya Dunia kuangalia namna nzuri itakayofanya ili kuhakikisha ujenzi wa stendi hiyo unafanyika. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Moshi Vijijini hali iko kama Kondoa, miundombinu mingi imejengwa siku nyingi na imechakaa. Kwa kutambua hilo, Mamlaka ya Maji (MUWSA) imefanya kazi kubwa ya kukarabati miundombinu hiyo katika Kata mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana kulikuwepo na mradi mmoja katika Kata ya Mabogini ambao ilikuwa inahusu vijiji vinne na Wizara ilipokuja kuzindua kwa kuona kazi kubwa iliyofanywa na MUWSA katika Kata zingine iliahidi kutoa shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kuendelea kusambaza maji kwenye vijiji vingine vitano vya Mvulei, Muungano na Msarikia. Nataka kujua ni lini fedha hizo zitapelekwa MUWSA ili waweze kutekeleza ahadi hiyo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Komu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakubaliana na yeye kwamba MUWSA inafanya kazi nzuri na tunawapongeza sana na tumewapa miradi mingi kwa ajili ya Moshi Vijijini na wanafanya kazi kubwa. Serikali tuko tayari wakati wowote wakituletea, kwa sababu tumeshawapa kibali cha kupeleka mkandarasi kuanza kufanya kazi hiyo na wakati wowote watakapoleta certificate kwa ajili ya malipo ya mkandarasi sisi tumejipanga vizuri na tutaweza kuwalipa ili kazi hiyo iendelee. Mheshimiwa Mbunge naomba uwasiliane na MUWSA kujua wamefikia wapi lakini sisi tuko tayari fedha tunayo wakati wowote tutaweza kuwalipa waendelee na kufanya kazi hiyo.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kule Moshi Vijijini kuna mifereji ambayo ilikuwa ni ya asili na ya kwa kikubwa sana ndiyo ilikuwa ina support zao la kahawa na ilikuwa inatunzwa na KCU. Baada ya KCU kuyumba na zao la kahawa limeyumba.
Sasa nilitaka kumuomba Waziri anipe commitment kama anaweza akapeleka wataalam wakaenda wakakagua ile mifereji ya asili na vyanzo vyake kwa sababu kutokana na mabadiliko ya tabianchi vyanzo vingi vimeharibika na kwa sababu hiyo ile mifereji haifanyi kazi kwa ufanisi ambao unatakiwa.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari nimeshatuma wataalam wangu, nilimtuma Naibu Katibu Mkuu kwenda kule ili aniletee taarifa ya awali halafu baadae tuweke kikundi cha wataalam kiende kule. Lakini si kweli kwamba ile miundombinu haitoi maji kwa sababu imeharibika ni kwamba kilimo maeneo ya juu kimepanuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wale wanayatumia maji yote yanashindwa kufika huku chini. Lakini hilo suala tutalirekebisha ili kuhakikisha kwamba yale maji yatumike kwa watu wote. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge tutalifanyia kazi hilo suala.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kule Moshi kuna scheme ya umwagiliaji inaitwa Moshi Lower inayohudumia Kata za Mabogini, Arusha Chini na Kahe kwa wakulima wa mpunga na vitunguu. Wakati wa kiangazi, kutokana na uchakavu wa miundombinu na mabadiliko ya tabia ya nchi, kunakuwa na mgogoro mkubwa sana wa maji kwa sababu hayatoshi, lakini wakati wa mvua kunakuwepo na mafuriko ambayo yanaharibu vilevile miundombinu na hata hicho kilimo chenyewe. Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga kitu kama bwawa au miundombinu yoyote ya kuvuna hayo maji ili yaweze kutumika wakati wa kiangazi na kutatua mgogoro unaojitokeza wakati huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Serikali kwanza tunaona umuhimu wa ujenzi wa bwawa hilo kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua. Kwa hiyo, kwa niaba ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, tutatuma timu yetu ya Kanda ya Kilimanjaro kufika katika bwawa hilo kufanya tathmini ya awali, baadaye tutapanga pesa kutokana na uwezo wa kibajeti na upatikanaji wa fedha, ili kuweza kujenga bwawa hilo kwa ajili ya kuvuna maji ili yaweze kutumika wakati wa kiangazi.
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo moja la nyongeza. Kwa kutambua mahitaji makubwa ya walemavu wananchi wa Moshi Vijijini kwa kushirikiana na Padri Apolnarys Ngao ambaye anaishi Ujerumani na marafiki zake kule Ujerumani, tunajenga kituo kikubwa cha walemavu kule Parokia ya Mawela. Naomba kumuuliza Waziri kama atakuwa tayari kuja kuona hii jitihada, kuitambua na kuhamasisha michango zaidi ili kuweza kufanikishi hii nia njema?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anthony Komu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa ameomba niweze kwenda kwenye hicho kituo ambacho kinaandaliwa sasa hivi, kwanza niwapongeze kwa hilo wazo jema kwa kundi hili la watu wenye walemavu. Mimi nikiwa kama Naibu Waziri mwenye dhamana hiyo, naomba niseme kwamba niko tayari.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna hiyo haja ya kupima upya hayo mashamba yaliyotaifishwa na kwamba jukumu hilo lipo kwenye Halmashauri, lakini kama inavyofahamika, sasa hivi Halmashauri nyingi nchini zina hali mbaya sana ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini.

Je, Serikali iko tayari kutoa fedha kwa namna ya upendeleo, kama tutatenga fedha kwenye Halmashauri kwa ajili ya kuharakisha huo upimaji? Kwa sababu tatizo kule ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Katika hayo mashamba yaliyotaifishwa, yapo mashamba ambayo yamegawanywa kabisa kwa ujumla na matumizi yakabadilika, kwa hiyo, wamiliki ni wapya kabisa. Sasa kila wakijaribu kuomba kupimiwa upya inakuwa ni tatizo kwa sababu zile hati za awali hazijafutwa. Mfano hai ni shamba moja kule Uru lililokuwa chini ya Chama cha Msingi Uru Kati, shamba linaloitwa Kosata. Mfano Shule ya Sekondari ya Uru Seminari imeshaomba kwa zaidi ya miaka kumi kupimiwa lakini hati ile haijafutwa.

Je, Serikali itafuta lini hizo hati za mashamba ya aina hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anauliza kama Wizara ni lini itaweza kusaidia Halmashauri ambazo pengine zipo duni kiuchumi kwa ajili ya kuweza kuongeza kasi ya upimaji. Naomba niseme, jana wakati najibu swali moja hapa nadhani la Mheshimiwa Joyce, nilitoa kwa ufafanuzi mkubwa sana kwamba pamoja na kwamba mamlaka za upangaji miji ni Halmashauri zenyewe, lakini wizara imeweka juhudi kubwa kuhakikisha kwamba inazipa support kubwa ya kuwawezesha kuweza kupima maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi kubwa ya kwanza ambayo tulifanya ni kuweka vifaa vya upimaji katika kanda zote na vifaa vile vinatolewa bure katika Halmashauri na inasaidia katika kupima kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tulitoa pesa, shilingi bilioni 6.4 na nimesema jana, katika Halmashauri 25 ambazo tunawasaidia kwa ajili ya upimaji, wamechukua zile pesa ili kuweza kuongeza kasi ya upimaji. Kwa hiyo, Halmashauri yake kama nayo ni mhitaji, nadhani tutaangalia uwezekano kwa kipindi kinachokuja tuweze kuona ni jinsi gani tutawawezesha ili waweze kupima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe Halmashauri zote wanatakiwa kutenga bajeti kwenye bajeti zao kwa ajili ya kuongeza kasi ya upimaji kwenye maeneo yao ili kupunguza migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ameongelea suala la shamba lile la ushirika ambalo kuna maeneo yamegawiwa kwa taasisi nyingine kwa mfano Jimbo Katoliki la Moshi wamepewa eneo hilo, Uru Seminari ambayo ameisema wamepewa eneo hilo lakini hawajaweza kumilikishwa kwa sababu nyaraka zinasemekana kwenye kile Chama cha Ushirika zimepotea. Mwezi Februari mwaka 2019 wametoa taarifa rasmi Polisi kuonyesha kwamba zimepotea. Sasa huwezi kumilikisha mtu mwingine wakati ile hati nyingine iliyokuwepo bado haijafutwa na haijaweza kupatikana kiasi cha kuweza kuwapa hati wale wengine. Kwa hiyo, kinachofanyika sasa baada ya ule utaratibu wa kisheria kukamilika, basi na hawa wengine ambao wamepewa maeneo yale katika lile shamba lililokuwa awali lililobadilishiwa matumizi, nao watapata. Pia kwa sehemu kubwa inaweza ikafanyika kwenye zoezi la urasimishaji kwa sababu tayari kuna maeneo mengi yameshajengwa hospitali, shule na makazi. Kwa hiyo, hilo litafanyika kulingana na taratibu za kisheria mara taarifa zilizopelekwa Polisi zitakapokuwa zimefikia hatima yake. Ahsante.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunpa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kule Moshi Vijijini kwa asili kabisa hali ni mbaya sana wakati wa mvua kwa sababu ya aina ya udongo ambao uko kule, lakini hali ni mbaya zaidi katika Kata ya Arusha chini kule TPC katika kijiji cha Chemchem ambacho kimetengwa na Mto Kikavu ambao wakati wa mvua kunakuwa hakuna mawasiliano kabisa na sehemu nyingine zozote za Jimbo.

Mhshimiwa Mwenyekiti, toka mwaka 2012, daraja hilo la Chemchem la hapo kwenye kivuko cha Mto Kikavu limekuwa likitengewa fedha, lakini ujenzi mpaka kesho haujaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri, ni lini mtakuja kuwaunganisha watu wa Chemchem na wenzao wa huku Tanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji ambacho Mheshimiwa Mbunge anakitaja kwangu mimi ndiyo nakisikia. Katika swali la msingi sikutarajia swali la kutoka huko ambako Mheshimiwa Komu anasema. Ni vizuri sasa nimwambie Mheshimiwa Mbunge, baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu ni vizuri tukawasiliana tujue uhalisia ukoje ili tuweze kutatua tatizo ambalo lipo.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kama ilivyo kwenye swali la msingi, kule Moshi Vijijini katika Kata ya Mabogini iko barabara inayotoka Mabogini inakwenda Chekereni mpaka Kahe. Ile barabara huwa inakarabatiwa na wananchi na wakati mwingine na TARURA lakini kwa fedha kidogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kuuliza swali la msingi hapa, nikaahidiwa kwamba TARURA inao mpango mkubwa wa kuifanyia kazi hiyo barabara ili iweze kupitika katika kipindi chote cha mwaka. Sasa hivi tunavyoongea, ile barabara haipitiki kabisa kwa sababu imebadilika kuwa mfereji. Naomba …

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Komu, uliza swali tafadhali.

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumwuliza Naibu Waziri, ni lini hiyo kazi ya kuitengeneza hiyo barabara itaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni jana tu Mheshimiwa Komu aliuliza swali kuhusiana na barabara ya Jimboni kwake na tukakubaliana kwamba ni vizuri tukaenda kwenye uhalisia. Naamini na hili anaongezea ili wakati tutakavyokuwa tunaenda Moshi tukashughulikie barabara zote mbili, tukitizama tujue suluhu ipi ambayo inatakiwa? Tujue tukiwa site. Mheshimiwa Komu, naomba niipokee katika lile la jana na la leo, kwa hiyo, tunakuwa na barabara mbili.
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya Serikali skimu za asili ile mifereji ya asili haikutajwa hata moja na katika Jimbo la Moshi Vijijini ambalo lina Kata 16, Kata 14 zote za Kibosho, Uru, Old Moshi, Mbokomu na Kimochi zote zinategemea hizi skimu za asili; Je, mko tayari kutuma wataalamu katika Jimbo la Moshi Vijijini kwenda kuona hizo skimu ambazo nazizungumzia na kubainisha changamoto zilizopo na kupendekeza utatuzi mahsusi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika Kata ya Old Moshi Magharibi upo mfereji unaoitwa Makupa ambao kwa sasa hivi wananchi wanaoishi nje ya Moshi Vijijini wanachangisha fedha ili kuukarabati na fedha zinazohitajika ni kidogo sana. Upo mfereji mwingine unaoitwa mfereji wa Muo ambao uko katika Kata ya Old Moshi Mashariki na unahudumia Vijiji Nne, Kijiji cha Suduni, Kikarara na Tela.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufahamu kutoka Serikalini, mtakuwa tayari kuwaunga mkono wananchi wa Kata hizi mbili ili kukamilisha haya malengo ambayo kwa kweli ile mifereji pamoja na jitihada kubwa sana zilizokuwa zimeshafanywa na Serikali huko nyuma, sasa hivi hiyo mifereji haitumiki kabisa kutokana na kubomokabomoka.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, swali lake la kwanza anataka kujua kama Serikali tupo tayari kutuma wataalam kwenda katika Jimbo la Moshi Vijijini, ili kwenda kuangalia jitihada zilizofanywa na wakulima wa huko; Serikali tupo tayari na nichuku nafasi hii kuwaelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro kutuma timu pale, ili iende kuangalia uhakiki na kufanya tathmini tuone hitaji mahususi ni nini, ili tuweze kuwaunga mkono.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa taarifa tu Mheshimiwa Mbunge kwa sasa tumeshapitia muundo wote wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, sasahivi inaanzia mpaka ngazi ya wilaya, palepale kuna wataalam wa Tume ya Umwagiliaji Ngazi ya Mkoa wapo na Ngazi ya Kanda. Kwa hiyo, pia nichukue nafasi hii baada ya Bunge hili waone wale watu wa kanda ya umwagiliaji katika wilaya yako, ili watatoa ushirikiano mkubwa, ili kufanya tathmini ya kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili pia anataka kujua kama Serikali tuko tayari kuwaunga mkono kwa kiasi hiki kidogo ambacho kinahitajika kwenda kuwaunga mkono kuboresha miundombinu ya umwagiliaji katika skimu hizi za Makupa na Muo; Serikali tuko tayari, lakini kwanza hatuwezi kujua pamoja na kiasi hiki kidogo kinachohitajika ni vizuri kwanza tusubiri taarifa hawa wataalam waende wakajionee na kufanya tathmini tuone hitaji hasa linahitajika kiasi gani, baadaye tutapeleka fedha kama ulivyoomba Mheshimiwa Mbunge.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kama ilivyo katika Wilaya ya Momba, kule Moshi Vijijini katika Kata ya Uru Shimbwe Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli wakati anagombea alikuja pale akahutubia na akaahidi kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mamboleo mpaka Shimbwe. Kwa kweli ile barabara sasa hivi iko katika hali mbaya sana, sasa naomba kujua toka kwa Serikali ni lini ahadi hii ya Mheshimiwa Rais itatimizwa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Komu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni kuunganisha mikoa kwa barabara za lami, lakini na mipaka ya majirani zetu kuunganisha kwa lami halafu baadaye ndiyo tunaendelea na barabara nyingine.
MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, majibu ya Serikali kwa kweli ni majibu ambayo yamelenga kuuficha ukweli kwa sababu ukweli ni kwamba huo mradi baada ya kukabidhiwa ulianza matatizo hapo hapo na maji hayakutoka kabisa. Sasa baadaye Wizara ikaenda kule na ikabaini kwamba ule mradi ulijengwa chini ya kiwango na MUWASA wakakabidhiwa huo mradi wakaanza kuurekebisha na tunavyoongea sasa hivi, wameshapewa milioni 135 kwa ajili ya kuukarabati. Sasa nataka kujua hao waliofanya huo ujenzi below standard wamechukuliwa hatua gani? Hilo swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, MUWASA wamepewa mzigo mkubwa sana kule Moshi Vijijini wamekabidhiwa Kata kama 12 kwa ajili ya kuzihudumia na zina matatizo ya miradi kama hiyo ambayo ni michakavu, ambayo imejengwa chini ya kiwango n.k lakini MUWASA wanadia kwenye Taasisi za Serikali kama Chuo cha Polisi-Moshi zaidi ya bilioni moja kwa hiyo wana tatizo kubwa sana la fedha. Nataka kufahamu kutoka Serikalini kuna commitment gani juu ya kulipwa hilo deni la MUWASA ili waweze kutuhudumia vilivyo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anthony Komu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni kuhusu chanzo hicho kama kilijengwa chini ya viwango; ni ukweli usiopingika kwamba kuna miradi mingi Nchi hii ya maji hasa iliyojengwa kutoka mwaka 2010 mpaka 2015 imejengwa chini ya viwango na ipo miradi kama 88 Tanzania nzima lakini nia ya Serikali ni kuhakikisha Watanzania kwanza wapate maji. Kama mradi umejengwa chini ya kiwango au vipi nia yetu sisi ni kukarabati Watanzania wapate maji, hilo la kwanza na ndiyo muhimu. Kwa mtazamo huo ndiyo tukatoa milioni 135 kwa ajili ya kutarabati chanzo kile na hivi tunavyoongea kazi inaendelea vizuri isipokuwa kutokana na mvua zinazoendelea kidogo kazi imepungua lakini tunaamini wiki tatu zinazokuja chanzo kile kitakuwa kimekamilika na ndugu zetu wale Watanzania wanapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, hatua ya pili inayofuata sasa ni kufanya uchunguzi wa kina kuelewa kwanini vyanzo hivi vilijengwa chini ya kiwango. Uchunguzi huo tunaweza kuoina kama ilikuwa kwa bahati mbaya ama kwa nini baada ya hapo taratibu za Kisheria zitachukua mkondo wake. Hatutaki kumuhukumu sasa hivi kitu muhimu mtu yoyote ni muhimu kwanza tufanye uvchunguzi tujiridhishe.

Mheshimiwa Spika, swali la pili nasema kwamba mamlaka ya maji ya Moshi imepewa majukumu mengi ni kweli na inafanyakazi nzuri na kuna madeni ambayo idara kama za Polisi wanadaiwa na naomba nimhakikishie tu kwamba jambo hilo tunalichukua na Taasisi nyingi za Serikali zinaendelea kulipa ili kuhakikisha kwamba mamlaka hizi za maji zote zinaweza kujiendeleza au kufanyakazi kwa kiwango kinachotakiwa.