Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Raphael Michael Japhary (18 total)

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa majibu ya namna hiyo kuhusu viwanda vya Moshi yamekuwa yakitolewa mara kwa mara katika Bunge lako Tukufu bila utekelezaji; na kwa kuwa ilikuwa ni moja wapo ya ahadi ya Mheshimiwa Rais kwamba kwa muda mfupi sana viwanda vile vingetwaliwa kwa waliovitumia bila utaratibu.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kutoa muda halisi kwa maana ya time frame ya lini viwanda hivyo vitatwaliwa kwa watu ambao wameshindwa kuvifanyia kazi katika malengo halisi yaliyokuwa yametarajiwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa majibu ya Serikali hayaakisi ukweli ulivyo kuhusu wafanyakazi, kwa sababu madai yao ni ya msingi na fedha wanazodai siyo za mikataba ya hiari na wamekuwa wakidai fedha hizo tangu mwaka 1998, na kwa kuwa Serikali haijataka kuwa karibu nao…
NAIBU SPIKA: Naomba uulize swali tafadhali!
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Je, ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kuanza kufuatilia ukweli wa madai hayo na kuwa karibu na hao wafanyakazi ili waweze kutoa ufafanuzi unaoridhisha wafanyakazi hao kuondoa manung’uniko yao? Ahsante sana.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na (b) suala la maslahi ya wafanyakazi ni lako wewe, ni langu mimi. Wewe kama Mwakilishi wao na mimi kama Kiongozi wa Serikali, mimi na wewe tuwasiliane tutakwenda wote mpaka Moshi tuwaone hao watu tuzungumze nao tutakwenda kwa Msajili wa Hazina, tutaweza kujua mbichi na mbivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali (a) Mheshimiwa Rais amezungumza bayana, na mimi nimekuwa nikizungumza mara nyingi kuhusu viwanda ambavyo havifanyi kazi. Jambo moja ambalo tunapaswa kulielewa kuna suala la kisheria kuhusu hivi viwanda vilivyobinafsishwa, kwa hiyo, tunajitahidi kufuata hizo sheria kusudi tuvitwae kisheria kusiwepo migongano. Nia yetu nikuona hivyo viwanda vinafanya kazi haraka sana, hatutaki kwenda mahakamani. Kwa hiyo, viwanda hivyo vitatwaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada za kuvitwaa tunawafuata wale watu ni Watanzania wenzetu tunawauliza kitu gani kilichowasibu? Sababu nyingine zina mantiki na kuna baadhi ya viwanda vimeshaleta proposal namna gani vitaweza kufufuliwa. Tumewapa wataalam watu, wataalam wa Wizara yangu wawasaidie hao waliovichukua, hasa wale Watanzania wazawa tuweze kuona wanatoa bidhaa tulizotegemea.
Moja ya sababu ni kwamba soko tulilokuwemo lilikuwa linaleta bidhaa ambazo lilikuwa linafanya viwanda vyetu nchini visiwe competitive hilo suala ni historia Mheshimiwa Rais na Waziri wa Fedha wamelisulihisha bidhaa zinaingia kwa kulipa kodi na bidhaa standard. Kwa hiyo, viwanda vya Watanzania waliopewa vitafanyakazi na hiyo ni kazi yangu tulishughulikie mnisaidie Waheshimiwa Wabunge.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tatizo lililojitokeza katika Jimbo la Chilonwa halitofautiani na hali iliyojitokeza katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kutokana na mvua iliyonyesha ambayo imeharibu miundombinu sana na sababu kubwa ya uharibifu huo ni kutokana na mwelekeo wa namna ambavyo TANROADS wameelekeza maji kwenye Kata za Msaranga, Shirimatunda na Ng‟ambo, kiasi kwamba madaraja yameharibika sana. Je, Serikali inatoa ahadi gani kwa wananchi wa Moshi kwamba itatoa maelekezo kwa TANROADS kuhakikisha wanarekebisha miundombinu iliyoharibika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutawasiliana na TANROADS ili wakayaangalie hayo maeneo ili hatimaye wajue nini cha kufanya katika kurekebisha mawasiliano. Kwa kweli mawasiliano yamekatika sehemu nyingi za nchi yetu na kama ambayo nimekuwa nikijibu hapa mara nyingi, tulitoa maelekezo maalum kwa TANROADS Mkoa kwamba sasa baada ya mvua kwisha tuelekeze nguvu zetu katika kurekebisha mawasiliano pale ambapo yamekatika.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa migogoro iliyozungumzwa katika hifadhi haitofautiani na malalamiko ya muda mrefu yanayotolewa na Jumuiya za Wapagazi, Waongoza Watalii na Wapishi katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na hifadhi nyingine za Taifa, wakigombana au wakilalamikia Tours Operators wao.
Je, Serikali kwa sababu, inalifahamu hili, ni lini itatatua migogoro hii ili maslahi na mazingira ya kikazi ya Jumuiya hizo za Wapagazi, Waongoza Watalii na Wapishi yaweze kuboreshwa, kama mabalozi wema wa kustawisha utalii katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri lenye mwelekeo wa kuboresha zaidi huduma kwenye sekta ya utalii huku tukitambua wote kwamba, utalii unaongoza katika kuliingizia Taifa hili fedha za kigeni. Si zaidi ya wiki mbili nilikuwa KINAPA pale Kilimanjaro National Park, lakini baada ya pale niliungana na Mheshimiwa Waziri, Arusha Mjini ambako tulikutana na Vyama vya Watoa Huduma wote kwenye Sekta ya Utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, zilijitokeza changamoto nyingi, mojawapo ilikuwa ni hiyo na kwamba, sasa Serikali tayari imeshaweka jedwali la changamoto zote hizo ambazo zimezungumziwa na sasa tumejipanga kuhesabu moja baada ya nyingine ili kuweza kupata majawabu na kuweza kutatua migogoro hiyo na matatizo hayo ili tuweze kuboresha Sekta ya Utalii.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza, uwanja wa ndege wa Moshi umeharibika sana na ni uwanja wa muda mrefu sana tangu wakati wa Muingereza; na ni uwanja muhimu sana na wenye faida sana kiuchumi hasa utalii, kama ilivyoonekena hapa. Na unawezekana kujiendesha wenyewe na ukaleta faida wala hautategemea viwanja vingine kujiendesha. Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, nilikuwa naomba time frame, je, ni lini Serikali sasa itapeleka hata hizi milioni 350 angalao basi kufanya huo ukarabati ili uwanja huo uweze kutumika? Kwa sababu hii inaonekana inaweza ikawa ni ahadi ya kibajeti, lakini fedha hii isiende kwa wakati; na labda bajeti iishe ikiwa haijapatikana. Naomba nipate uhakika ni lini fedha hii itaenda ili uwanja huo uweze kutumika na uweze kujengewa uzio wake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kulikuwa na mpango wa Serikali wa kuwa na chuo cha mambo ya anga (school of aviation). Naomba kujua kutoka Serikalini, ni lini chuo hicho kitaanza ili kuweza kusaidia watu wetu kupata utaalam wa mambo ya anga katika nchi hii? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo shilingi milioni 350 naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Kilimanjaro kwamba zitatumika katika mwaka huu wa fedha; na taratibu za kumpata mkandarasi wa kufanya hiyo kazi zimeshaanza. Kusema lini, kwa maana ya tarehe naomba unipe subira, wakati hiizi taratibu zitakapokamilika ndipo tutakapojua. Lakini kikubwa ni kwamba fedha hizi kwa vyovyote vile lazima zitatumika katika mwaka huu wa fedha kabla haujaisha. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu shule ya aviation, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna mipango hiyo katika viwanja vingi na hizi zote zinaunganika. Kwa sababu katika masuala ya kufundisha, kwa mfano wenzetu marubani wanahitaji kutumia viwanja vingi na kimoja kati ya viwanja hivi ni hiki cha Moshi. Tuna shule, NIT wameanzisha kwa ajili ya kufundisha marubani na ndege zitakuwa zinatumia viwanja hivyo vyote ambavyo viliainishwa toka mwanzo kama sehemu ya aviation school. MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa vile muda umekwenda itabidi sasa tuchukue swali moja la msingi na muuliza swali tu. Tunaendelea na Mheshimiwa Omary Ahmed Badwel ambaye atauliziwa kwa niaba na Mheshimiwa Daniel Mtuka.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la kukatika kwa umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara halitofautiani na tatizo la kukatika kwa umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro hasa Jimbo la Moshi Mjini. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu kuhakikisha kwamba
wanatatua tatizo la ukatikaji wa umeme katika Jimbo la Moshi Mjini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Arusha kulikuwa na tatizo la mara kwa mara la umeme. Lakini uko mradi mmoja unaoitwa Trade Up unaotekeleza ukarabati wa miundombinu katika mikoa hiyo mitatu. Mheshimiwa Japhary nikuambie tarehe 22 Mei taratibu kabisa za kukamilisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Mji wa Kilimanjaro utakamilika kupitia
mpango huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa hatua ya pili
tunajenga pia mradi wa kusafirisha umeme unaotoka Kinyerezi kwenda Tanga, unakwenda mpaka Namanga, lakini uko unaotoka hapa sasa kutoka SInginda kupita Manyara na kwenda mpaka Kilimanjaro wa kilovoti 400 ambao pia utaongeza nguvu ya umeme na kupunguza sasa
kukatika katika kwa umeme kwa sababu ya low voltage.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa
Japhary kuanzia mwezi Mei tunaweka kwamba kukatika umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro utapungua kwa kiasi kikubwa.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali nilikuwa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Kitengo cha Zimamoto kikiwa kipo kwenye Mamlaka za Halmashauri za
Miji na Manispaa, Manispaa ya Moshi ilikuwa ina uwezo wa kuhudumia magari makubwa mawili na gari moja dogo ambalo tuliazima kutoka Japan. Tangu magari yale yachukuliwe na Kitengo cha Zimamoto Mkoa wa Kilimanjaro, leo tunahudumia gari moja tena tunahudumia kwa taabu na hicho kigari kimoja tulichokiomba Japan ndicho kinachofanywa kama ndiyo gari wanalotembelea Maafisa wa Zimamoto.
Je, Serikali imetumia kigezo gani kuonesha kwamba ufanisi umeongezeka baada ya kuhamisha kitengo hiki
kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani tofauti na kilivyokuwa Halmashauri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba kama Serikali haioni kwamba kuna haja sasa ya kusaidia Mkoa wa
Kilimanjaro kwa kuazima gari moja ya zimamoto kutoka KIA kwa sababu KIA wanaonekana wana magari ya ziada ili iweze kusaidiana na gari lililopo sasa hivi Mkoa wa Kilimanjaro ili kutoa huduma ya zimamoto kwa watu wa Mkoa wa Kilimanjaro? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa jambo hili. Niseme tu kwamba vigezo vilivyotumika kwa sasa, moja tofauti na ilivyokuwa katika ngazi za Halmashauri, sasa hivi vipo dedicated kwa ajili ya masuala haya ya zimamoto na kutokuhudumia gari mbili ni kwa sababu tu gari yenyewe imeenda kwenye uchakavu. Ukipima kwa ujumla wake, ni kwamba ufanisi umeongezeka na utaona kwamba sasa kikosi kipo dedicated kwenye masuala ya zimamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili la kuazima gari; gari za zimamoto zipo kwa ajili ya matukio na mara zote
katika maeneo yote panapotokea tukio la moto, gari zilizo karibu za kuzimia moto huwa zinaenda kutumika. Kwa hiyo, hilo hatuna tatizo nalo, lakini tunapanga kuimarisha hasa katika Miji ikiwemo hiyo ya Moshi kwa ajili ya ukubwa wa miji pamoja na uwepo wa uwanja wa ndege.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Halmashauri ya Manispaa ya Moshi imekuwa na maombi ya muda mrefu ya Hospitali ya Wilaya na tulikuwa tayari na majibu ya Serikali kwamba wakati wowote watajibu maombi yetu, lakini mpaka sasa hatuoni mwelekeo wowote. Nini tamko la Wizara ya TAMISEMI katika suala hilo la Hospitali ya Wilaya ya Manispaa ya Moshi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kweli Halmashauri mbalimbali hazina Hospitali ya Wilaya na siyo Moshi peke yake. Ndiyo maana wakati fulani nilikuwa naongea na dada yangu Mheshimiwa Esther hapa, alileta special request na Mheshimiwa Mbunge najua tupo karibu sana. Tukaona kwamba basi angalau tuongeze suala zima la kimkakati la afya katika eneo hilo, japokuwa tuna hospitali yetu kubwa pale ambayo tunaitegemea, ipo chini ya Kanisa ya KCMC, lakini ni lazima tuboreshe huduma ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tukaona katika kipindi cha sasa tuboreshe kwanza Kituo cha Afya cha Uru Mashariki ambapo siyo muda mrefu, ndani ya miezi miwili tutapeleka fedha za kutosha pale kufanya marekebisho makubwa sana. Tutajenga theater na wodi nyingine pale na vifaa mbalimbali vitawekwa pale. Lengo kubwa ni kupunguza changamoto za wananchi katika eneo lile.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo Serengeti linafanana na tatizo lililopo Manispaa ya Moshi na ukizingatia kwamba Manispaa ya Moshi ndiyo Makao Makuu ya Mkoa wa Kilimanjaro na ndiyo eneo ambalo watalii wote wanaoenda mlima Kilimanjaro hupitia pale. Tumekuwa na ombi la muda mrefu la kuomba Hospitali ya Wilaya Serikalini kwa zaidi ya miaka sita au saba hapa. Swali langu, je, Serikali itatusaidia lini kutekeleza ombi letu maalum la kujenga Hospitali ya Wilaya katika Manispaa ya Moshi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli inawezekana kulikuwa na maombi maalum katika vipindi mbalimbali, lakini tufahamu kwamba haya maombi maalum mara nyingi sana siyo kama ile bajeti ya msingi. Kwa hiyo, inategemea kwamba ni jinsi gani Serikali kipindi hicho imepata fedha za kutosha ku-accommodate maombi maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, najua kwamba Moshi kweli hakuna Hospitali ya Wilaya, lakini ukiangalia vipaumbele vya Taifa hili hata ukiangalia katika maeneo mengine kwa mfano kama Serengeti alipokuwa anazungumza ndugu yangu Mheshimiwa Marwa pale, wako tofauti sana na Moshi. Angalau Moshi mna alternative pale, watu wanaweza wakaenda KCMC au sehemu nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaangalia jinsi tutakavyofanya. Ninyi kama Halmashauri ya Wilaya anzeni kufanya hiyo resource mobilization katika ground level na sisi tutaangalia jinsi gani tulifanye jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ndiyo maana katika kusaidia katika suala zima la Moshi kwa ujumla wake (Moshi Mjini na Vijijini) sasa hivi tunaenda kukiboresha kituo cha Uru Mashariki pale. Lengo kubwa ni kwamba kiweze kusaidiana na hospitali zile ambazo ziko pale kwa lengo kubwa lile lile la kuwasaidia wananchi wa Moshi waweze kupata huduma nzuri ya afya.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa kuwa suala la Kigoma – Uvinza lipo sawa la Kiwanda cha Magunia Moshi na Kiwanda cha Kiritimba ambapo nimeshauliza swali la msingi hapa Bungeni na Serikali ikajibu kwamba ipo tayari kwenda kuonana na wale wafanyakazi ambao hawakulipwa mafao yao ili waweze kuwaeleza, kwa nini hawakuwalipa na kama wamewalipa, waliwalipa kwa vipi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali inipe commitment kama ni lini itakwenda kuonana na wafanyakazi wa magunia waliostaafishwa na wafanyakazi wa Kiritimba wa Mkoa wa Kilimanjaro. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anahitaji commitment ya Serikali ya lini tutakwenda kuwaona na kusikiliza matatizo ambayo yanayowakabili wafanyakazi hawa, nimuahidi tu kwanza kwa kuanzia Jumatatu nitamuagiza Afisa Kazi aliopo pale Moshi aende kukutana na Wafanyakazi hao na baada ya hapo akishanipatia taarifa kama kuna haja ya Naibu Waziri ama Waziri kwenda kufanya kazi hiyo basi nimtoe hofu Mbunge kwamba tutakwenda kuonana nao na tutatatua matatizo ambayo yanawakabili wafanyakazi hao.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Gereza la Karanga lina tatizo kubwa sana la vyombo vya usafiri kwa maana ya magari. Naomba majibu ya Serikali kwamba ina mpango gani wa kununua gari ili kusaidia wafungwa wanaokata rufaa pamoja na askari ili kulinda usalama wa wafungwa kwa sababu gari lililopo ni chakavu sana na hata matairi halina?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Gereza la Karanga limekuwa na tatizo la madeni makubwa kwa matibabu ya wafungwa wanaotibiwa nje ya zahanati ya gereza hilo. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba madeni yanayodaiwa gereza yanalipwa ili wafungwa waendelee kupata huduma ya matibabu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tuna matatizo ya upungufu wa magari katika Jeshi la Magereza maeneo mbalimbali nchini ikiwemo kwenye Gereza la Karanga kiasi tumefikia hatua ya kuweza kufikiria uwezekano kuwapatia magari matano miongoni mwa magari 50 ambayo tunatarajia kuyapokea hivi karibuni kupitia Jeshi la Polisi. Tutalichukua hili suala la Gereza la Karanga tuone kama katika maeneo yaliyo na changamoto kubwa Karanga ni mojawapo ili tuweze kuangalia uwezekano wa kuwapatia gari yatakapokuwa yamewasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la zahanati, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunajitahidi kulipia madeni ya magereza ikiwemo zahanati kadri fedha zitakavyokuwa zinaingia. Pia nataka nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna uwekezaji mkubwa katika Gereza la Karanga wa kiwanda chini ya uwekezaji wa Shirika la PPF na moja katika mpango ambao tunataka kutekeleza ni ujenzi wa zahanati kubwa na ya kisasa katika gereza hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti,unaamini kwamba tutakapomaliza ujenzi huo, changamoto hii ya gharama ya matibabu kwa maeneo hayo itasaidia kupatiwa ufumbuzi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge aendelee kuvuta subira wakati matatizo haya tunayatatua kwa hatua za muda mfupi na muda mrefu.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Serikali kuhusu tatizo hilo, lakini bado tatizo hili ni kubwa na linaendelea. Mijadala juu ya wapagazi, waongoza watalii na wapishi imekuwa ya muda mrefu baina ya Serikali na waajiriwa hawa, lakini utekelezaji wa makubaliano umekuwa hafifu sana.
Swali la kwanza, je, Serikali haioni kwamba kuna haja kwa sasa kwenda kuonana na waajiriwa kuongea nao ana kwa ana, kujua ni kwa kiwango gani miongozo hii ambayo wameipeleka imetekelezwa na imekuwa na tija kwa hao watu ambao ndio waathirika wa tatizo hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na utaratibu kwamba wanaoshughulikia matatizo ya watalii imekuwa ni kampuni ya nje na sio watu wa ndani. Ni kwa nini Serikali haioni haja ya kushirikisha kampuni za ndani kuhakikisha kwamba inasimamia suala la porters na waongoza watalii na inaliacha katika kampuni za nje? Ahsante sana.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunakubaliana kabisa kwamba kuna haja ya kuonana na waajiriwa ili kuweza kubaini kama kweli yale makubaliano tuliyoyafikia pale Arusha yametekelezeka. Na mimi naomba kumwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kikao hiki cha Bunge tutapanga safari ya kwenda kuonana na wale ili tuweze kuangalia utekelezaji wa hayo mambo yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu matatizo ya hawa wapagazi kwamba yanatatuliwa na kampuni ya nje, hili ni suala ambalo nimelisia sasa hivi, lakini nadhani tutalichukulia hatua na tutahakikisha kwamba matatizo ya Watanzania yanashughulikiwa na Watanzania wenyewe kupitia mifumo iliyowekwa na makampuni yetu yako tayari kabisa kushughulikia hili tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge, hili tutalishughulikia na kulifanyia kazi.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, kupitia fedha ya Mfuko wa Barabara na fedha ya Benki ya Dunia mtandao wa barabara ya lami katika Manispaa ya Moshi unaridhisha kwa kiwango fulani, lakini kwa kuwa fedha hizi hazina mahusiano ya moja kwa moja na ahadi ya Rais ya kilometa 10 aliyoitoa siku tano kabla ya kufunga kampeni zake mwaka 2015. Je, Waziri haoni kwamba, kuna sababu ya kumkumbusha Rais huenda akawa na nafasi ya kukumbuka ile ahadi yake ya kilometa 10 katika Manispaa ya Moshi?
Mheshimiwa Spika, lakini la pili, tangu TARURA imeanza kazi Manispaa ya Moshi speed yake ya uwajibikaji haijaenda kwenye kasi ile ambayo Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ilikuwa inafanya wakati inasimamia barabara zake.
Je, Waziri haoni kwamba, kuna haja ya kuisukuma TARURA ili iweze kuongeza kasi ili kuhakikisha kwamba, barabara ambazo zimeharibiwa sana na mvua kipindi hiki cha mvua zinakarabatiwa, ili ziwe katika hali nzuri kama ilivyokuwa wakati Halmashauri ya Manispaa ya Moshi inasimamia yenyewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza anasema kwamba utekelezaji wa hizi barabara hauna uhusiano wa moja kwa moja na ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, ni vizuri tu akatambua kwamba fedha zote ambazo zimefanya kazi ya ujenzi wa barabara katika Mji wa Moshi ni utekelezaji na mwenye fedha ni Mheshimiwa Rais yeye mwenyewe. Najua ana kiu, angependa barabara nyingi zaidi zijengwe, lakini haiondoi ukweli kwamba tumefanya kazi kubwa sana katika ujenzi wa barabara katika Manispaa ya Moshi.
Mheshimiwa Spika, lakini katika swali lake la pili, anasema haridhishwi na kasi ya chombo hiki ambacho tumeanzisha, TARURA, ukilinganisha na hapo awali jinsi ambavyo wao halmashauri walikuwa wakifanya.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie, chombo hiki ni baada ya kilio cha Waheshimiwa Wabunge wengi ambao tulikuwa tunapenda barabara zetu zichukuliwe na TANROADS, TARURA katika maeneo mengi inafanya kazi vizuri na Moshi naamini nao watafanya kazi vizuri. Hebu tukilee na tuhakikishe kwamba tunakisukuma tunakipa nguvu kifanye kazi iliyotarajiwa. (Makofi)
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tatizo la Hospitali ya Wilaya lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ni sawa na tatizo la Hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi. Tayari Hospitali ya Mawenzi imezidiwa na wagonjwa kama Hospitali ya Mkoa na Manispaa ya Moshi kwa muda mrefu imekuwa na ombi hilo la Hospitali ya Wilaya ambalo tayari Serikali imeonekana imelikubali. Je, ni lini Serikali sasa italeta fedha ili hiyo Hospitali ya Wilaya ya Manispaa ya Moshi iweze kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo ambayo Hospitali za Wilaya hazipo zinaenda kujengwa na ndiyo maana tumeanza na hospitali 67. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya kwamba hizo 67 kukamilika hatutaishia hapo tutaenda maeneo mengine ambayo hakuna Hospitali za Wilaya ili tuweze kujenga.
MHE. JAPHARY R. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Singida halitofautiani sana na tatizo la hospitali ya Mawenzi ya Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo hospitali ile imezidiwa sana na wagonjwa.

Sasa swali langu kwa Serikali, wako tayari kusaidia kuongeza Madaktari katika hospitali ile ya Mawenzi ili iweze kutoa huduma inayoridhisha kwa wagonjwa katika hospitali ile?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Japhary Michael, Mbunge wa Moshi, kama ifuatavyo:-

Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ni hospitali ya Mkoa katika Mkoa wa Kilimanjaro na bahati nzuri nimepata fursa ya kutembelea ile hospitali. Kwa maana ya kuwa na Madaktari tunao Madaktari wa kutosha, changamoto ambayo tunayo pale ni Madaktari Bingwa na hili tumeshaliona Mheshimiwa Mbunge. Juhudi ambazo tunazifanya sasa hivi ni kusomesha Madaktari wengi zaidi na kuanza kuwapanga katika idara mbalimbali ambazo nimezisema katika swali la msingi, kuhakikisha kwamba sasa zile huduma za kibingwa zinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunaboresha mnyororo wa rufaa kwa maana ya kuboresha vituo vya afya na ujenzi wa hospitali za wilaya mbili ambazo zinaendelea katika Mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha sasa ule mzigo ambao ulikuwa unakwenda pale katika hospitali ya mkoa, uweze sasa kuchukuliwa na hivi vituo vya afya pamoja na hospitali za wilaya.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa ya Moshi ilishaleta ombi Serikali Kuu la muda mrefu kidogo, zaidi ya miaka minne, mitano, kuomba kupandishwa hadhi kwa Zahanati za Kata za Longuo, Ng’ambo na Msaranga, lakini bahati mbaya mpaka leo Serikali haijatujibu na tuna tatizo la huduma ya miundombinu ya afya katika Manispaa ya Moshi kwa sababu hatuna hospitali ya wilaya na hospitali ya wilaya Serikali haikuwa tayari kutukubalia ombi letu. Je, ni lini hadhi ya vituo hivyo itapandishwa ili tuwe na vituo vya afya vya kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, uwepo wa zahanati umuhimu wake hauondoki kwa kuondoa zahanati kuifanya eti kituo cha afya, kwa hiyo msimamo wa Serikali kwanza ni suala la uwepo wa zahanati lakini pia na uwepo wa vituo vya afya. Pale ambapo inaonekana kwamba hakuna namna, baada ya kujiridhisha kwamba matakwa yote ya kutoka zahanati kwenda kituo cha afya, hapo ndipo Serikali tunafanya kupandisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sio rahisi kwa swali ambalo Mheshimiwa Mbunge ameuliza bila kujiridhisha kwamba yale matakwa ya kituo cha afya ambayo ni tofauti na zahanati yametimizwa. Inawezekana ndiyo maana na yeye mwenyewe anaridhika kwamba Serikali tunahakikisha tunajenga vituo vya afya tukizingatia ramani lakini pia na eneo ambalo zahanati zinatakiwa kuwepo na vituo vya afya vinatakiwa kuwepo.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa mpango huu wa Serikali wa kupandisha hadhi Kituo cha Afya cha Moshi Arusha, lakini nilikuwa naomba Serikali, kwa sababu tunaelekea kwenye bajeti; na kwa sababu mchakato huo wa kupandisha hadhi kituo cha afya ni wa muda mrefu kidogo; ni lini sasa mpango huo utakamilika ili bajeti ya kukarabati hiyo miundombinu kwa ajili ya kuwa Hospitali ya Wilaya iweze kuingizwa katika bajeti ya mwaka huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, bado Moshi tuna tatizo kubwa la Vituo vya Afya. Tuna Vituo vya Afya viwili tu ambavyo vimeshazidiwa tayari; Kituo cha Afya cha Pasua na Kituo cha Afya cha Majengo. Nami naishukuru Serikali kwa kutupa shilingi milioni 400. Tumeleta maombi ya muda mrefu Serikalini ya kutusaidia kupandisha hadhi Vituo vya Afya vya Shirimatunda, Longuo B na Msaranga.

Je, ni lini Serikali itakubaliana na ombi letu? Kama hilo ombi haliwezekani, ni lini sasa itatujengea kituo kingine kimoja cha afya katika Manispaa ya Moshi?

Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii nimwombe Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu yeye ni sehemu ya Madiwani na katika mchakato wa kuhakikisha kwamba tunabadilisha hicho Kituo cha Afya ni pamoja na wao kutekeleza wajibu wao. Atusaidie kusukuma Halmashauri yake kufanya taratibu zile ambazo anatakiwa kuzifanya halafu sisi tuweze kumalizia.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameongelea juu ya suala zima la kubadilisha Zahanati kuwa Vituo vya Afya, ametaja nyingi lakini pia akawa na ombi kuwa, kama hilo haliwezekani ni vizuri basi tukafikiria suala la kujenga Kituo cha Afya kingine. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba Zahanati zinaendelea kuwepo kama Zahanati kwa sababu Zahanati na Vituo vya Afya ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, siyo azma ya Serikali kubadilisha Zahanati kuwa Vituo vya Afya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, Zahanati zile zilizopo ziendelee kuwa Zahanati ila ombi la kuanzisha ujenzi wa Kituo cha Afya kipya, hilo tunaliweka katika matazamio ya siku za usoni.
MHE. RAPHAEL H. MICHAEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri ya Kikanuni, lakini kutokana na jiografia ya Manispaa ya Moshi, Kata ya Msaranga, Ng’ambo na Kibororoni zipo karibu na wananchi hawa wanashirikiana pamoja katika kutafuta huduma za afya. Sasa je, Serikali kwa maelekezo hayo kwamba wanahamasisha kujenga vituo vya afya, ni lini itatupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika Kata hiyo ya Msaranga ili tuweze kusaidia hizo Kata tatu kwa pamoja ili wananchi wapate huduma za afya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Manispaa ya Moshi tuna ombi la muda mrefu kwa Serikali kuhusiana na Hospitali ya Wilaya na kuna uhitaji mkubwa sana ili kusaidia wagonjwa ambao wamezidi Hospitali ya KCMC na Hospitali ya Mawenzi. Je, ni lini sasa ombi letu litakubaliwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya?

Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza anaongelea Kata mbili ambazo ziko tayari kushirikiana ili waweze kupata Kituo cha Afya. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali tuko tayari pale ambapo wazo limeanzia kwa wananchi na eneo linakuwepo na utayari wa wananchi katika kujenga Kituo cha Afya, nasi kama Serikali tunapeleka nguvu yetu.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili anaongelea juu ya suala zima la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya Manispaa ya Moshi. Katika jibu langu la msingi nimemwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba huduma kwa ajili ya sehemu ambazo hakuna Hospitali ya Wilaya zinapatikana na ndiyo maana sisi kama Serikali kwa kushirikiana na St. Joseph tumewapa hadhi ya kuwa kama Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya kutoa huduma hiyo, lakini itekelezwe kwa muda wa mpito pale ambapo Hospitali ya Wilaya haipo.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali tuko tayari kama ambavyo tumeanza maeneo mengine, tutahakikisha kwamba hata Manispaa ya Moshi nayo inapata Hospitali ya Wilaya.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuwa Halmashauri nyingi nchini zinalipa hiyo posho ya Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji kati ya shilingi 5,000 mpaka shilingi 10,000. Je, Serikali haioni sasa kwamba imefika wakati ambapo wanapaswa kutoa maelekezo viwango vya posho hizo kupanda na vikawa vinafanana kwa Halmashauri zote nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Moshi Mjini ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri Mstaafu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hoja ya nyongeza ya posho ya Wenyeviti wa Mitaa inategemea na uwezo wa Halmashauri, mimi nafahamu natoka katika Halmashauri ya Ilala. Ilala wanalipa posho kwa mwezi shilingi 100,000 Wenyeviti wa Mitaa na wanalipa kila baada ya miezi mitatu, mitatu, lakini hiyo inategemea na mapato makubwa ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Kinondoni na Temeke.

Kwa hiyo, kama Moshi na maeneo mengine yana uwezo kama nilivyosema hatujazuia kabisa, fedha inayokusanywa kwenye Halmashauri kuna maelekezo yametoka, kwa mfano asilimia 10 itaenda kwenye vijana, akinamama na watu wenye ulemavu. Fedha zingine kuna maelekezo mengine yametoka, lakini inayobaki fedha ya maendeleo itatengwa, lakini inapohusika na uendeshaji kama ni Halmashauri ngazi ya Kata, Vijiji na Vitongoji inahusika. Kwa hiyo Halmashauri yenye uwezo itaendelea kulipa posho kubwa kulingana na uwezo wake. H lo linaruhusiwa hatujazuia. Ahsante.