Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Freeman Aikaeli Mbowe (8 total)

MHE. FREEMAN A. MBOWE: Nakushukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa majibu yako, lakini ningependa kuuliza maswali ya ziada kama ifuatavyo:-
Kauli yako Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba katika Jimbo lako la uchaguzi mmekubaliana muache siasa mfanye kazi, niliomba tu utambue kwamba siasa vilevile ni kazi. Vilevile kwa sababu kauli ya Waziri Mkuu ni agizo bila kujali umeitolea Jimboni kwako ama nyumbani kwako Mheshimiwa Waziri Mkuu, kauli yako unapoitoa mahali popote kama Kiongozi Mkuu ni agizo. Sasa kwa sababu Mahakama Kuu Mwanza wakati ikisikiliza kesi ya Alphonce Mawazo ilitoa hukumu kwamba Jeshi la Polisi halina mamlaka ya kisheria ya kuzuia mikutano ya Vyama vya Siasa yakiwemo maandamano kwa kisingizio cha...
Mheshimiwa Spika, narudia hapo kwa kisingizio cha wana taarifa za kiintelijensia na Mahakama Kuu ikaagiza Jeshi la Polisi kama mna taarifa za kiintelijensia ina maana mna msingi mzuri wa kulinda usalama. (Makofi)
Kwa hiyo solution siyo katazo, solution ni Jeshi la Polisi kuwasiliana na wahusika ili waweze kuwalinda vizuri kwa sababu tayari wana taarifa za uvunjifu wa amani.
Sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu uko tayari sasa kutoa tamko kwa Taifa na kwa kupitia Bunge hili, kwamba lile katazo la mikutano ya siasa ya vyama vya siasa, sasa unalisitisha rasmi?
La pili hapo hapo, je, kwa kutoa tamko lile vilevile uko tayari tena kulieleza Jeshi la Polisi, liheshimu mhimili wa tatu ambao ni Mahakama ambayo ime-declare kwamba hawana mamlaka ya kutoa katazo wakati wanapopata taarifa za kiintelijensia?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maswali mawili ya nyongeza ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Mheshimiwa Mbowe. Kama ambavyo nimeeleza awali kwamba Katiba inaeleza, lakini Sheria ndiyo inayoongoza nchi hii kuweka miongozo ya utaratibu. Siasa nchi hii haijaanza leo, upo utaratibu na zipo taratibu za kimsingi, kama chama kinahitaji kufanya mikutano lazima wafuate utaratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la Mahakama kuzuia Jeshi la Polisi kufanya kazi, hii ni mihimili miwili tofauti, Mahakama siwezi kuzungumzia habari za mhimili mwingine na kuutolea kauli.
MHE. FREEMAN A. MBOWE:
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu nakushukuru kwa ajibu yako na ninaomba nikuulize maswali mengine machache ya ziada.
Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na nia njema sana ya kulinda viwanda
vya ndani ni dhahiri kwamba maamuzi yote ya kiutawala lazima yafanyiwe kwanza utafiti. Na tunapozungumza ninahakika Serikali yako inatambua kwamba kuna mradi mkubwa wa uwekezaji wa kiwanda cha sukari uliokuwa umependekezwa katika eneo la Bagamoyo uliouzungumza ambao umeanza kuratibiwa tangu mwaka 2006 wenye capacity ya kuzalisha sukari tani 125,000 kwa mwaka, lakini Serikali mpaka dakika hii tunapozungumza urasimu unasababisha mradi huu haujapewa kibali cha kuanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu, pamoja na kwamba ulisema kuna bei ya
elekezi sukari ambayo ingehitaji soko la sukari liweze kuwa controlled na Serikali, jambo ambalo linaonekana kushindikana. Unatupa kauli gani Watanzania kuhusiana sasa na hatima ya hayo mambo niliyokuuliza?
WAZIRI MKUU:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali pana la Mheshimiwa Mbowe, Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kama ifuatavyo:-
Kwanza tuna hilo shamba la Bagamoyo ambalo umelisema ambalo
umesema kumekuwa na urasimu wa muda mrefu. Nataka nijibu hili vizuri kwa sababu pia Wabunge tumeshirikiana nao sana katika kufanya maamuzi ya shamba lile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shamba la Bagamoyo kwa ukubwa wake na
mategemeo yake kwa mipango ya kuzalisha sukari inategemea sana Mto Wami. Mpakani mwa Mto Wami tumepakana na Mbuga ya Saadani, Mbuga ya Saadani uwepo wake na sifa iliyonayo inategemea sana wanyama wale kunywa maji Mto Wami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, uwekezaji wa shamba la sukari unahitaji maji mengi nayo yanatakiwa yatoke Mto Wami. Bado kuna mgongano kidogo wa mpaka kati ya shamba letu hilo la sukari linalotegemewa kulima miwa na Mbuga ya Saadani. Kamati ya Kudumu ya Bunge imefanya ziara na imeishauri Serikali kuangalia vinginevyo na mimi nimepokea ushauri wao vizuri kwa sababu una mantiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kamati ya Bunge imeishauri Serikali kwamba ni vyema
tukahifadhi mbuga, tukatafuta maeneo mengine ya kilimo cha sukari ili kulinda Mto Wami ambao unatumiwa na wanyama wetu kwenye Mbuga ya Saadani kuliko kupeleka shamba tukatumia maji yale tukafukuza wanyama hakutakuwa na mbuga tena.
Mheshimiwa Spika, sisi bado tuna nafasi kubwa ya maeneo mengi ambayo yamefanyiwa utafiti ya kulima sukari, mbali ya eneo la Morogoro na kule Kigoma, lakini tuna eneo la shamba lililokuwa linamilikiwa na Bodi ya Sukari kule Kilombero, nalo pia lina nafasi nzuri tu tunaweza kuzungumza na wakulima wanaolima mashamba ya kawaida watuachie tuweze kuwekeza.
Mheshimiwa Spika, lakini tuna Mto Rufiji tuna bonde kubwa sana uliokuwa
unamilikiwa na watu wa Bonde la Rubada, wana eneo kubwa sana. Kwa hiyo, tuna maeneo hayo mengi, tutakapopata wawekezaji wengi tutaanza kupima viwanda vilivyopo na uzalishaji wake. Makubaliano ya kiwanda kipya na uzalishaji wake tukigundua kwamba, uzalishaji wake unatosha mahitaji ya nchi.
Tutaanza kuwakabidha Kigoma, tutawepeleka Morogoro kule Kilosa, tutawapeleka hapa Ngerengere na Bagamoyo iwe sehemu ya mwisho baada ya kuwa Kamati ya Bunge imetushauri vizuri juu ya kulinda Mbuga yetu ya Saadani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili, ambalo umelitaja ni hili la bei elekezi, kwa
nini tunatoa bei elekezi.
Mheshimiwa Spika, mara nyingi tunakaa sana na wazalishaji wa viwanda
wa sukari na kufanya mapitio na kwa mara ya mwisho tumekutana hata wale waagizaji wa muda mrefu na sasa tunajua kupitia mitandao tunajua bei wanayonunulia sukari huko ughaibuni. Brazil na kule Uarabuni tumeshafanya calculation za pamoja mpaka sukari inaingia nchini na kulipa kodi zake.
Mheshimiwa Spika, usafirishaji kutoka Dar es Salaam na kuipeleka mpaka
mkoa wa mwisho Kagera, Lindi, Ngara, tunajua kule Ngara itauzwa bei gani.
Kwa hiyo, wajibu wa Serikali kutoa bei dira ni kumlinda sasa mwananchi wa kawaida asije auziwe kwa gharama kubwa kwa kisingizio cha usafirishaji huku tukiwa tunajua usafirishaji kutoka Brazil mpaka Dar es Salaam, Dar es Salaam mpaka Ngara na mwananchi wa Ngara atanunua sukari kwa kiasi gani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo suala la bei elekezi litategemea linaweza
likabadilika kutegemea na gharama ya usafirishaji ambayo na sisi pia tunafuatilia kwa karibu kupitia Bodi yetu ya Sukari. Kwa hiyo, suala bei dira linaweza kubadilika na sisi tunatoa kauli kutegemea na uagizaji lakini lazima wananchi waamini kwamba Serikali hii inawalinda walaji wadogo ili wasinunue sukari kwa bei ya juu.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, haihitaji utafiti wa ziada kujua uchumi umeshuka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini tunatambua kwamba Benki Kuu ndiyo taasisi muhimu katika Taifa ambayo mara kwa mara kila baada miezi mitatu ina-release data fulani fulani kuonesha hali ya uchumi katika Taifa, na tayari hali ya uchumi katika Taifa imeshaelezwa kwenye Ripoti ya Benki Kuu ambayo inatoka quarterly, kila baada ya miezi mitatu kwamba kuna kushuka kwa hali ya juu katika importation, kuna kushuka katika exportation, kuna kushuka katika construction industry, kuna kushuka katika circulation ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu hivi majuzi tulimsikia Mheshimiwa Rais akisema kwamba watu wanaweka fedha nyumbani, wanahifadhi fedha na ndiyo sababu mzunguko wa fedha umepungua katika circulation, kitu ambacho mimi binafsi naamini si kweli, na sijui vyanzo vya Mheshimiwa Rais ni nini kama Serikali ilikuwa haijafanya utafiti wa kina kujua kweli hali hiyo ipo. Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kamati ya Bunge ya Biashara na Uwekezaji ilikwenda Bandarini na ilitoa ripoti ambayo ni dhahiri, ni Kamati ya Bunge imedhihirisha hilo. Hao wadau mnaosema mtawashirikisha tayari wanalalamika. TATOA wanalalamika kuhusu mizigo yao, mahoteli yanafungwa, makampuni yanafungwa, watalii wamepungua, utafiti gani bado mnahitaji mjue kwamba uchumi umeanguka? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilitegemea leo Waziri Mkuu ujue kabisa waziwazi kwamba uchumi unaanguka na uchumi umeanguka na utueleze measures ambazo mnachukua kurekebisha hali hii. Lakini it seems like the government haina uhakika ni nini kinaendelea. Waziri Mkuu unaonaje katika mazingira hayo, mka-declare kwamba mmeshindwa kuendesha Serikali hii? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbowe, Mbunge na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa kuanza kusema kwamba Serikali hiihaijashindwa kuongoza nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote, tutaongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa sana kwenye sekta zote. Kazi hiyo imeanza kwa kufanya marekebisho makubwa ya maeneo ambayo tunadhani yatafanya Taifa hili liweze kupata mafanikio makubwa vilevile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani umeeleza hasa juu ya bandari. Kwanza nieleze kwamba Serikali imekuwa ikifanya mawasiliano na mataifa mengine yanayoendesha shughuli za bandari. Mwezi mmoja uliopita nilipokea timu ya wafanyabiashara maarufu duniani kutoka Singapore akiwemo mfanyabiashara anayefanya biashara za meli duniani. Alinieleza kwamba suala la mdororo wa usafirishaji wa mizigo kwa njia ya meli imeshuka duniani kote.
Mheshimiwa Spika, suala la kupungua kwa mizigo maeneo yote ni kwa sababu ya hali ya kiuchumi duniani iliyotokana na kuporomoka kwa bei ya gesi na mafuta duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukanda huu wa kwetu wa Afrika Mashariki ambako bandari yetu inatumika sana, nataka nikuhakikishie, Tanzania kupitia bandari zetu tunategemea sana mizigo kutoka Congo, Rwanda, Burundi kidogo lakini pia na Zambia; na wote mnajua kwamba Congo na Zambia ni nchi ambazo zilikuwa zinaelekea kwenye uchaguzi na kulikuwa na migongano mingi ndani ya nchi na wafanyabiashara wengi walisimama kidogo kufanya biashara zao; na hiyo ikasababisha kupungua hata kwa kiasi cha mizigo. Sio tu kwa Bandari ya Dar es Salaam pia hata usafirishaji kwenda kwenye bandari nyingine kutoka kwenye nchi hizo ambazo nimezitaja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nataka nikupe faraja kwamba wiki moja iliyopita tumepata barua kutoka kwa timu ya wafanyabiashara wa Congo. Kutokana na hali iliyokuwepo awali na stabilization iliyopo sasa wametuhakikishia kwamba sasa usafirishaji wa mizigo yao yote utafanyika kupitia Bandari ya Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Rwanda wametuandikia barua kutuhakikishia kwamba kutokana na mdororo uliokuwepo awali wafanyabiashara wengine kuamua kupeleka maeneo mengine kwa sababu ya hali ya kiuchumi lakini sasa wameamua mizigo yote itapitia Bandari ya Dar es Salaam, hasa kwa mkakati wetu wa pamoja wa ujenzi wa reli ya standard gauge inayotoka Dar es Salaam - Tabora mpaka Bandari kavu ya Isaka, lakini tunaunganisha pia na reli hiyo standard gauge kwenda nchini Rwanda na kwa hiyo jitihada za kusafirisha mizigo sasa zitaimarishwa ili kuleta motisha ya ujenzi wa reli hiyo ili iendelee kusafirisha mizigo hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nataka nikuhakikishie, ni kwamba haya yote uliyoyaeleza kama kuna jambo ambalo tunahitaji kukaa pamoja ni jambo la uchumi na hili ni jambo endelevu na nataka nikuhakikishie kwamba tutalifanyia kazi kwa kiasi kikubwa ili sasa tujiridhishe kila eneo na yale ambayo yanatakiwa na kama kufanya kampeni zaidi ya kupata wafanyabiashara zaidi, Serikali itafanya hilo kwa lengo lile lile la kuhakikisha kwamba uchumi wa nchi yetu hauporomoki na wala hauwezi kuathiri mahusiano na nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hiyo ndiyo commitment ambayo naweza kukupatia kwa ajii ya maeneo haya. (Makofi)
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mambo ya Ndani inakabiliwa na upungufu mkubwa wa magari na ninamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kukiri kwamba wanapungukiwa sana magari, vitendea kazi pamoja na ofisi. Vilevile wana upungufu mkubwa wa rasilimali watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu, siku za karibuni, kwenye upande wa Jeshi la Polisi ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani pamejitiokeza utaratibu ambapo Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wanalitumia Jeshi la
Polisi kuwalinda wao binafsi wakati kuna matatizo makubwa ya kiulinzi katika Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu ni hili, nikitoa mifano halisi, katika Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha analindwa na section nzima ya Jeshi la Polisi, ana motorcade, ana ving‟ora asubuhi mpaka usiku. Sasa magari kama mawili au matatu yanamhudumia Mkuu wa Mkoa na section nzima ya Jeshi la Polisi ambayo ina askari tisa na ving‟ora na hata Wakuu wa Wilaya wamejipa utamaduni huo sasa.
Je, ni nini itifaki ya Kitaifa kuhusu ulinzi wa Viongozi kama hata hawa Mawaziri wenyewe hawalindwi na Askari, lakini Wakuu wa Mikoa leo wanajilundikia Askari badala ya Askari kwenda kwenye lindo, ma-OCD wote siku hizi hawafanyi kazi ya ulinzi wanafanya kazi ya kulindana na kufuatana na Wakuu wa Wilaya. Tunaomba Wizara watueleze leo, ni nini sera ya Serikali kuhusu itifaki hii na matumizi mabaya ya Jeshi la Polisi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwenye utendaji wa kazi kwenye ngazi za Mikoa na Wilaya, Mkuu wa Mkoa ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ni Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, panapokuwepo na jukumu hasa ambalo linapohusisha shughuli za kiulinzi na nje ya ofisi, ni sahihi Mkuu wa Mkoa ama Mkuu wa Wilaya kuambatana na timu yake kwenda katika eneo husika. Inapotokea Mkuu wa Mkoa anakwenda ofisini kwake ama Mkuu wa Wilaya anakwenda ofisini kwake, maana yake OCD ama RPC ama wengine na wenyewe watakuwa kwenye ofisi zao. (Makofi)
Kwa hiyo, mimi kwa mazingira ambayo nimekuwa nikipewa ni pale ambapo hawa viongozi wanakwenda katika eneo la tukio ambalo linahusisha ulinzi na usalama. Huo ndiyo muogozo kwamba kama wanaelekea katika eneo ambalo linahusisha ulinzi na usalama ni sahihi viongozi hawa kwenda na timu zao kwa sababu ni mambo ya kiusalama na sehemu ya kutolea maelekezo, lakini siyo wakati wa kwenda ofisini on daily routine, unless kama wanafanya hivyo itakuwa maeneo ambayo kila mmoja anaenda kwenye ofisi na ofisi hizo ziko katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, kwa maelekezo haya, ni kwamba viongozi hawa wanapokwenda kwenye majukumu ambayo yanahitaji maelekezo na ni ya kiulinzi na usalama na wao ndio Wenyeviti wa Ulinzi na Usalama itifaki inataka hawa watu wawe na hao viongozi kwa ajili ya maelekezo ya site, lakini wanapoenda kazini na hawa viongozi wengine nao wanaendelea na majukumu yao.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kukiri kwamba Taifa letu lina historia ya watu kuheshimiana, ni jambo jema na ni kweli tumekuwa na historia hiyo na hofu ninayoizungumza ndiyo hiyo hiyo kwamba ustaarabu na utamaduni huo unaonekana kupotea kwa kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kututaka tuiamini, tuipe muda lakini hapa tunazungumzia kifo au kupotea kwa mtu. Jambo hili linazua hofu kwa familia na kwa Watanzania wote katika ujumla wake. Nina hakika mtu yeyote mwenye mapenzi mema na nchi yetu anaona jambo hili linataharuki kubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni utamaduni wa nchi yetu kushirikiana na mataifa mbalimbali katika maeneo


mbalimbali na kwa sababu mataifa yanatofautiana katika uwezo wa kufanya tafiti, uwezo wa kufanya uchunguzi na kipekee nikizungumza Uingereza ambayo tuna mahusiano mazuri nao wametumika maeneo mbalimbali duniani pale ambapo panaonekana pana uzito wa kiuchunguzi, taasisi yao ya Scotland Yard ina uwezo wa kusadia. Kama ambapo ilifanyika Kenya wakati amepotea na ameuwawa katika mazingira ya kutatanisha Robert Ouko aliyekuwa Kiongozi katika Jamhuri ya Kenya watu wakaomba Serikali kama imeshindwa kuchunguza iombe Scotland Yard watoe msaada na wana utaalam mkubwa katika forensic investigation na waliweza kufanya hivyo na wakatoa taarifa yao iliyokuwa sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na mazingira hayo basi kwa nini Serikali isitoe kauli kwa sababu miezi sita ni mingi na hofu inazidi kuwa kubwa, kwa nini Serikali isione umuhimu wa ku-engage Scotland Yard iweze kuja kusaidiana na jeshi letu na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ili kuonyesha ile nia njema kujaribu kuchunguza jambo hili kwa haraka kwa sababu wenzetu tukiri wana teknolojia ya ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile Waziri Mkuu atakumbuka katika uhuru na haki niliyoizungumzia hapa hajatoa kauli yoyote kuhusu kurushwa kwa Bunge live. Hebu tupe kauli ya Serikali basi turejee utamaduni wetu wa Kitanzania Bunge hili lisikike kwa wananchi ambao wametutuma hapa ndani. Tunaomba kauli ya Serikali kwenye hilo vilevile.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, najua kuna maswali mawili, la kwanza ni lile la kwa nini Serikali isishirikiane na mataifa mengine katika kufanya uchunguzi wa matukio kadhaa ndani ya nchi. Kwanza, nataka nikuthibitishie kwamba Taifa letu linayo mahusiano na mataifa kadhaa ambayo tunashirikiana kwenye mambo mbalimbali ikiwemo na mambo ya kiulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na matukio haya yanayojitokeza huku ndani, nikuhakikishie pia Taifa letu lina uwezo wa ndani wa kufanya ufuatiliaji wa kutambua matukio haya ya awali ya mtu kufariki au kutoweka mahali. Baada ya familia husika kutoa taarifa tunaweza tukafanya uchunguzi huo na baadaye tukaweza kubaini vyanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nimesema yote haya lazima mtuamini Serikali kwamba tunayo nia njema kabisa ya kutambua vyanzo na namna ya kudhibiti uendelezaji wa matukio yote ambayo yamejitokeza nchini.
Mheshimiwa Spika, ni kwamba Serikali haina kikomo cha uchunguzi kutegemea na nature ya tatizo lenyewe. Familia ya mtajwa aliyetangulia mbele za haki au vinginevyo hata sina uhakika, tunaweza kusema kwamba uchunguzi huu utakapokamilika taarifa itatolewa. Ingawa umesema kwamba ni miezi sita lakini kama ambavyo nimesema kwenye jibu la msingi kwamba itategemea kama vyombo vyetu vinapata msaada kutoka kwenye jamii na vyanzo vingine


na teknolojia ambayo tunaitumia kuweza kufikia hatua ya kupata majibu ya uchunguzi ambao tunautoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado naendelea kutoa kauli ya kuwaomba Watanzania kuwa watulivu na kuamini jeshi letu kwamba linafanya kazi. Vilevile sisi Serikali jambo hili ni letu, Watanzania watupe ushirikiano wa kutuhabarisha vyanzo vya matukio haya ili tuweze kufikia hatua muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge alitaka pia kupata ufafanuzi wa jambo la pili ambalo lilishazungumzwa na Bunge lililopita na maamuzi yalishatolewa ya kwamba Bunge letu litakuwa limeweka utaratibu wa namna ya kuwafikishia matangazo Watanzania. Utaratibu huo unaendelea na Watanzania wanapata matangazo kupitia utaratibu ambao tumeuandaa. Kwa hiyo, tutaendelea kuboresha kadiri ambavyo tunaona inafaa ili kuweza kuwafikishia ujumbe Watanzania. Ahsante sana.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa majibu yake, ni ukweli usiopingika kwamba pale muda unapotumika au unapopita sana bila majibu hata status kutolewa katika Bunge, hoja hiyo huonekana kwamba imefifia umuhimu na ulazima wake.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na kwamba umetoa ahadi ya kwamba Wizara zitashughulikia, unaweza ukatoa a firm commitment kwamba katika Bunge hili, kabla Bunge hili la Bajeti halijaisha, Serikali itapitia Hansard na kumbukumbu zote zinazohusiana na Maazimio yaliyopita ya Bunge halafu Serikali itoe status report na naomba itambulike hapa kwamba status report siyo lazima ndiyo iwe ripoti ya uchunguzi ya mwisho, angalau ituambie jambo hili limefikia hapa, limefanyiwa kazi moja, mbili, tatu, bado tutaletewa katika hatua ya baadae.

Mheshimiwa Naibu Spika, angalau Bunge lipewe status ya Maazimio kadhaa ambayo ni mengi kwa kweli, ambayo yameshaazimiwa na Bunge hili, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa sababu ya hiyo nia njema ya Serikali, unaweza ukatoa commitment hiyo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimeeleza awali kwamba masuala yote haya yanagusa maeneo mengi sana ambayo yanatakiwa ufuatiliaji wa kina na baadae nilieleza kwamba kila tukio linagusa Wizara kadhaa, kwa hiyo siwezi kusema kwamba katika Bunge hili nitakuja kuleta taarifa hiyo mpaka pale ambako nitakutana na Wizara, nijue wamefikia hatua gani, pia tutakutana na Mheshimiwa Spika ili tujue utaratibu mzima wa namna ya kupata hizo Hansard na kufanya mapitio. Tukijiridhisha na tukiona kwamba jambo hilo sasa linafaa kuletwa Bungeni na kwa kuwa liliazimiwa na Bunge, basi tutafanya maamuzi ya pamoja ya kuleta Taarifa hiyo Bungeni.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, nakubaliana na wewe kwamba maisha ya kila Mtanzania yana thamani kubwa, lakini swali langu lilikuwa specific, sikuzungumza suala la Watanzania wote wanaoathirika kwa matukio mbalimbali. Swali langu lilikuwa very specific ya jambo linaloitwa political persecution, na ningeomba nieleweke hapo.

Mheshimiwa Spika, matukio ya kushambuliwa Mheshimiwa Lissu, lile tukio si la kawaida na naomba tusijaribu kuli-dilute kwa kuchanganya na matukio mengine mengi. Nimeuliza swali specific ambalo ninaomba specific answers. Na uonevu dhidi ya viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani nchini umekuwa ni utamaduni wa kawaida. Vyombo vya dola vinafanya, vinatesa watu na vinaumiza watu.

Mheshimiwa Spika, leo ninavyozungumza hivi ni siku ya tatu tangu Mbunge wangu wa Ndanda, Mheshimiwa Cecil Mwambe akamatwe na polisi Mtwara na yuko chini ya custody sasa hivi ni zaidi ya saa 48, kisa alikuwa anafanya mkutano wa kampeni ya uchaguzi katika kata mojawapo pale Mtwara Mjini, polisi wakamshika. Huyu ni Mbunge na Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini yenye Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, yuko ndani siku ya tatu sasa. Sasa matendo haya ya uonevu yanaendelea na hivi tunavyokwenda kwenye uchaguzi wa marudio katika hizi kata chache, viongozi wetu kadhaa wanakamatwa, wanawekwa ndani, wanapigwa na wanateswa.

Mheshimiwa Spika, sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu ninachouliza, mimi nilikuomba specific utuambie Serikali inaona shida gani? Kwa sababu si mara ya kwanza kwa Serikali hii kuomba msaada wa vyombo vya uchunguzi kutoka nchi za nje. Wakati Benki Kuu ilipoungua Scotland Yard walikuja hapa kufanya uchunguzi kuhusu jambo hili, ni mambo ya kawaida katika jamii ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika, na kwa sababu vyombo vya dola tumevi-suspect kwamba either havikuchukua tahadhari ya kulinda viongozi au havikuchukua hatua ya mapema kuzuia uharifu ule aidha kwa kutaka ama kwa kushiriki. Lakini ambacho napenda nikuambie Mheshimiwa Waziri Mkuu, mimi nina imani kabisa vyombo vyetu vya ndani vina uwezo wala sidharau, ila hakuna dhamira ya kuchunguza jambo hili, hapo ndio kwenye tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwa sababu hakuna dhamira na kwa sababu wanaoonekana wanaumia ni wa upande mmoja tunaitaka Serikali itoe hiyo clearance. Waje watu wafanye investigation kama ni ku-clear kila mtu anaehusika awe cleared ili jambo hili likomeshwe kwa sababu linaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni kwa nini sasa usikubali kwa niaba ya Serikali turuhusu vyombo vya uchunguzi vya kimataifa vije vikamilishe jambo hili ili tukate huu mshipa wa fitina?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbowe unaposema jambo hili nilijibu umeliuliza specific, naweza kusema kwamba unapotaka specific basi inabidi sasa vyombo vya usalama vikamilishe kazi yao ndio vije viseme hasa kwa tukio ambao umetaka lizungumzwe. Hakuna mtu yeyote aliyefurahishwa na tendo alilofanyiwa Mbunge mwenzetu. Hakuna mtu yeyote anayefurahishwa na matukio yanayojitokeza huko iwe ya mauaji au ya mashambulio au migongano inayoendelea kwenye jamii yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vyombo vya dola tumevipa jukumu la kusimamia na kuhakikisha kwamba tunalinda usalama wa raia na mali zao kwa kiwango kinachotakiwa. Na pale ambapo kunatokea tatizo, vyombo vya dola vina majukumu ya kuhakikisha kwamba vinafanya uchunguzi na kuwakamata wale wote ambao wamehusika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimeeleza hapa kwamba wakati wote watenda makosa ni watu ambao wanafanya matendo yale wakiwa wameshajiandaa pia kuweza uovu wao na kujificha dhidi ya vyombo vya dola. Wanapojificha sio kwamba vyombo vyetu vya dola havina uwezo wa kufanya kazi yake ya uchunguzi. Mimi nimekwambia haya matukio yote, wanayo matukio megi yamejitokeza katika kipindi kifupi, tumeanza hayo kama nilivyoeleza na huwa ninapozungumza Kibiti, Rufiji na Mkuranga sina maana ya kuficha au kulifanya jambo hili lisitambulike, hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunachukua mwenendo wa matukio, tunachukua uwezo wa vyombo vyetu na namna vinavyofanya kazi ili kuhakikisha kwamba tunabaini matukio haya na ndiyo sababu wakati wote Watanzania tumeendelea kuwaambia na kuwahamasisha kwamba ni lazima tushirikiane katika kuilinda nchi yetu na kila mmoja ashiriki katika kutoa taarifa. Sisi tunakaribisha mtu yeyote anayejua kama kuna mwelekeo wa jambo hili atusaidie ili
vyombo vya dola viweze kufanya kazi yake kwa urahisi zaidi.
(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, najua unazungumzia kwa upande wako kama Kiongozi wa Kambi ya Upinzani na yeye Mbunge mwenzetu ambaye ni Mheshimiwa Tundu Lissu anatoka kwenye upande wako, lakini utambue kwamba na sisi pia ni Mbunge mwenzetu na jambo hili ni letu pia, lazima tushirikiane kuhakikisha kwamba jambo hili linapata mwelekeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuhakikishie vyombo vyetu uwezo upo, lakini pale ambapo wataona kama kuna umuhimu huo, vyombo vyenyewe vitafikia hatua vinaweza vikalieleza, lakini mimi siwezi kuhakikishia Taifa kwamba tumekosa uwezo kwa sababu tunaamini vyombo vyetu vinao uwezo wa kufanya uchunguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Kiongozi mwenzangu wa Kambi ya Upinzani naomba uamini kabisa kwamba Serikali yetu inayo nia njema, familia za wale wote walioathirika akiwemo Mbunge mwenzetu, Mheshimiwa Tundu Lissu waamini kwamba Serikali yetu inayo nia njema ya kukamata, lakini pia ya kulinda amani ya nchi hii ili kila mmoja, hata sisi pia tuwe na uhakika wa shughuli tunazozifanya za kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaendelea kufanya hilo na tutaendelea kuwasiliana nawe kama kiongozi mwenzetu ili uweze kuona haya na namna ambavyo tunaweza tukatatua matatizo haya ya ndani, juu ya matatizo ambayo yanajitokeza kwenye maeneo yetu, ahsante sana.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu unajua vizuri sana, Serikali yako inajua vizuri sana, Watanzania wanajua vizuri sana kwamba vyama vya siasa vya upinzani vimezuiwa kwa miaka minne sasa kufanya kazi zake za siasa za uenezi. Na Mheshimiwa Waziri Mkuu unapotupa maelezo ndani ya Bunge ya kuhalalisha kilichofanyika na ukasema ni utaratibu ambao mmejiwekea mmejiwekea kwa sheria ipi. Najua yote hayo unajua vizuri sana, kwamba Tume ya Uchaguzi unayoiita ni huru kwa sababu imeandikwa kwenye katibu si huru na watendaji wake vilevile wamekuwa ni partisan sana na masuala haya yamejitokeza wazi na yanaonekana.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE.FREEMAN A. MBOWE: Weweee!!!

MHE. ESTER A. BULAYA: Naomba muwe na adabu.

MHE.FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu haya ni majibu mepesi ambayo kuna siku mtakuja kujuta katika nchi hii kwa majibu haya mepesi. Je…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. ESTER A. BULAYA: Keleleni huko!

MHE.FREEMAN A. MBOWE:… Mheshimiwa Waziri Mkuu, narudia kwa mara nyingine hamuoni ni muda mwafaka sasa Serikali ikaona umuhimu wa wadau mbalimbali ambao wanahusika na masuala ya uchaguzi katika nchi hii kukaa na kutafuta njia bora zaidi ya kwenda kwenye uchaguzi Oktoba kuliko kwenda kibabe kwa namna ambavyo tunataka kwenda?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbowe Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nikanushe kwamba Serikali inaongoza kibabe, haiongozi kibabe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbowe ni kiongozi tunazungumza, tunabadilishana mawazo; sote tunapobadilishana mawazo tunalenga kulifanya Taifa hili liwe na usalama, liwe tulivu ili shughuli zetu ziweze kwenda lakini muhimu zaidi Watanzania wanahijtai maendeleo. Kwa maana hiyo tunapoweka utaratibu wa namna ya kuwafikia wananchi na kupata maendeleo jambo hili si la chama kimoja ni kwa nchi nzima. Hakuna Mbunge wala Diwani aliyezuiliwa kwenye eneo lake kufanya siasa na watu wake. Kunaweza kuwa labda kama kuna tatizo mahali fulani kwa utaratibu ule tunaozungumza tunakutana tuambizane wapi kuna shida. Kama wiki iliyopita Mheshimiwa Sugu alieza kwamba kule Mbeya anazuio na OCD na mimi nilimuita hapa tumezungumza. Mkuu wa Mkoa ameungana naye, Mkuu wa Polisi Mkoa ameungana naye. Shida kama ziko kwenye ngazi ndogondogo huko ni suala kuzungumza kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani; tunakuheshimu sana, tunatambua una majukumu kwa chama chako lakini Serikali yetu inaendelea kushirikiana na Viongozi wote kwa Mamlaka zao ili kufanya taifa hili liendelee kuwa salama na tulivu, pale ambako kuna shida ya namna hiyo tuendelee kuwasiliana Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi za Upinzani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili suala la Tume hii kuonwa kwamba si huru ni mtizamo wa mtu lakini Kikatiba na utendaji wake uiko huru. Pale ambako panaonekana kuna shida basi kwa utaratibu ule paelezwe kwamba hapa kuna shida lakini hatujawahi kuona Rais akiingilia, chama cha siasa kikiinglia ile Tume iko huru na inafanya kazi yake kama ambavyo imetakiwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kukiwa na jambo lolote lile unao uhuru wa kubadilishana mawazo ili tuone wapi tusaidie katika kufanya jambo hilo liweze kwenda sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)