Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Willy Qulwi Qambalo (1 total)

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Kilimo. Nilikuwa na swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zao la mkonge ni moja ya mazao yanayoiingizia nchi yetu kipato, na kwa kuwa wakulima wa mkonge katika Jimbo la Korogwe Vijijini na hasa Mkoa wa Tanga wamekuwa wanajitahidi sana kulima mkonge ili wajinufaishe wao na familia zao na kuwasomesha watoto wao, je, Serikali itawasaidiaje ili wapate kulipwa haraka fedha walizokuwa wanadai kwenye Mamlaka ya Mkonge au Katani Limited ili ziweze kuwasaidia kuendesha na kustawisha zao la mkonge hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba zao la mkonge ni zao muhimu sana na linaloingizia wakulima pamoja na nchi fedha nyingi. Kwa taarifa tuilizonazo ni kwamba mwaka 2014/2015 mkonge uliingizia nchi dola za Kimarekani milioni 35.4 na kwa sasa uzalishaji umefikia kiwango cha tani 40,000. Kwa sasa sisi ni nchi ya pili baada ya Brazil inayozalisha tani 150,000 za mkonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itahakikisha kwamba wakulima wanaendelea kufaidika na kuinuka tena kwa zao la mkonge fahari ya watu wa Tanga ambapo kwa sasa tunafuatilia kuhakikisha kwamba wakulima wanalipwa fedha zao miezi mitatu na ndiyo maana nimemueleza Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zinategemewa kulipwa mwezi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nieleze tu kwamba kilio hiki cha wakulima kucheleweshewa fedha siyo cha Mheshimiwa Ngonyani peke yake, Wabunge karibu wote wa Mkoa wa Tanga wamekuwa wakiulizia kuhusu hizi fedha, na Mheshimiwa Mbunge wa Pangani amelalamika sana kuhusu hili na nimuahidi Mheshimiwa Nyonyani na Wabunge wote wa Tanga baada ya Bunge hili mimi mwenyewe naondoka naelekea Tanga kwenda kushughulikia kwa karibu zaidi kuhakikisha kwamba fedha za wakulima zinalipwa.