Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nakushukuru nami kunipatia hii nafasi ya kuchangia hoja iliyokuwa mezani. Kwanza nakupongeza kwa kazi kubwa uliyoifanya kwa kuunda Tume ya Bunge kuangalia udhaifu uliojitokeza katika makinikia pamoja na uvuvi. Hii imeleta faraja kubwa katika Bunge letu, kuwa sasa hivi Bunge linafanya kazi.

Mheshimiwa Spika, mwanzo lilikuwa Bunge ambalo unaona kabisa lipo lipo lakini naona sasa hivi umeliamsha dude ndani ya Bunge na Bunge liko vizuri. Nakuomba tena, tunataka Bunge Live ili hayo unayoyaunda watu wayasikie kule mtaani. Wananchi, wapiga kura wanataka kusikia nini unazungumza, Wabunge wako wanafanya nini? Hii kazi itasaidia kuweza kuleta uelewa kwa wale watu, watakuwa wanajua kinachoendelea ndani ya Bunge. Hoja za Wabunge wao zinazungumzia nini? Tukikaa humu ndani wananchi hawaoni hayo unayoyafanya. Kwa hiyo, ningeshukuru sana na hilo nalo ungeliamsha ingeleta tija zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naona kuna hoja nzito ya wafanyabiashara, wakulima dhidi ya kuwa na mahusiano mabaya na mabenki. Benki zimeamua kuwakandamiza wafanyabiashara hasa wakulima. Tumeona katika miaka miwili wakulima wako katika hali ngumu sana, wamelima mazao, lakini baada ya kulima mazao Serikali imewasimamishia maendeleo yao kwa kutokununua mazao yao. Matokeo yake benki hazikai chini kuangalia nini tatizo la hawa wakulima? Matokeo yake sasa hivi kila benki inataka kuuza mali za wakulima, mali za wafanyabiashara. Nafikiri Mheshimiwa Waziri akae chini na watu wa benki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Benki Kuu imepunguza riba kubwa sana kwa benki nyingine, nafikiri ni kama 9%, lakini benki hizo badala na wao kupunguza riba, wameongeza riba imekuwa kubwa sana. Imekuwa kubwa kiasi kwamba hakuna mfanyabisahara wa kawaida ambaye anaweza kukidhi haja. Ukiweka pesa wanaweka percent, ukitoa pesa wanaweka percent na ndani yake kuna udhaifu mkubwa. Nafikiri hata na maeneo haya ya benki yaangaliwe kuna nini? Kama Benki Kuu imepunguza riba, kwa nini bado wao wanaongezea mzigo mkubwa kwa wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali hii inakatisha tamaa kwa wakulima. Nataka nikupe mfano, nachukua mfano wa wakulima wako wa Kibaigwa. Pale palikuwa na wafanyabiashara wakubwa wa mazao, miaka mitatu wamekutana na crisis za mvua na pametokea mafuriko makubwa, wao bado wanaendelea na interest, lakini hawaangalii kuwa je, wenzao ambao wamekutana na mafuriko ambayo siyo wao, ni mipango ya Mwenyezi Mungu, wangekaa chini wakapunguza riba ile ili na wao waweze kufanya biashara. Matokeo yake wanawakandamiza na kutaka kuuza mali zao bila kuangalia nini tatizo.

Mheshimiwa Spika, Kenya, Waziri wa Fedha na watu wa benki wamesimama na wanafanya biashara. Nami nina imani kuwa Mheshimiwa Waziri ananisikia, atasimama na benki na kuangalia wafanyabiashara wakubwa wanaathirika vipi na mikopo ya benki ili kuweza kuisaidia? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia TRA. Ukiona mahali ngoma inachezwa sana, basi haikawii kuharibika. TRA walileta EFD machine. Kuna siku nilifika katika petrol station karibu mara mbili, nikifika wananiambia mashine haifanyi kazi. Nikauliza kwa nini haifanyi kazi? Hela zinaendelea kuchukuliwa, lakini zile hela ambazo zinatakiwa ziingie katika Serikali haziingii. Nataka nijue idara ya ICT ya TRA inafanya kazi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama mpaka Mbunge amekuja kuliona hili suala humu ndani, baada ya siku ya pili tumeona mashine zinafanya kazi, hii ni hujuma. Hujuma kama hamuisimamii itakuwa ni hujuma kubwa sana. Kwa vile ICT Department ndiyo inaweza kuingiza data ndani ya program ya Serikali na kuingizia pato Serikali, lakini kama ICT Department ikicheza na ma-hackers kwa kufunga hizi EFD Machines hizi pesa zote badala ya kuingia katika Mfuko wa Serikali zitaingia katika mifuko ya watu wengine ambao sisi hatuwajui. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nijiulize swali, Mheshimiwa Waziri atakapokuja kumaliza ku-wind up aniambie Department yake ya ICT iko makini? Huwa ni network, maana katika ICT inabidi ianzie TRA, iende mpaka katika mabenki, iende mpaka TCRA kuona je, humo ndani yake kuna nini ili angalau huu uovu, utasema Serikali haipokei mapato, kumbe mapato yanaingia kwa watu binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia suala la miradi mbalimbali ambayo imesimama kwa muda mrefu. Nataka nitoe mfano wa LNG (Liquefied Natural Gas) ambao uko Lindi. Tulitegemea mradi ule ungekuwa tayari umeshaanza kazi, lakini pamesuasua kwa muda mrefu, hatuambiwi mpaka leo ule mradi umesimama wapi? Huu ni mwaka wa tano wananchi wamechukuliwa maeneo yao hawajalipwa, lakini kinachoendelea hakijulikani.

Mheshimiwa Spika, hii inawapa mwanya wawekezaji kuchukua ile miradi kuipeleka Mozambique. Sasa hivi kila mradi ambao tunaukataa Tanzania, wenzetu Mozambique wanauchukua, matokeo yake badala ya kwenda mbele itakuwa sisi tumesimama na miradi yetu tukiwa na urasimu ambao mimi sijajua, lakini naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu aniambie.

Mheshimiwa Spika, kuna kitengo ambacho ni Taasisi ya CAG ya Ukaguzi. Kwa kweli hapa pana mtihani mzito sana. Kuna maeneo ambayo Serikali imeyaachia yasikaguliwe. Kwa nini? Kama Jeshi linakaguliwa na Bunge linakaguliwa, maeneo hayo ndiyo mianya mikubwa ya kupoteza hela ambazo sisi hatuzijui.

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano. Wafanyakazi wote wa Serikali mishahara yao inapitia NMB. Madaktari mishahara yao inapitia NMB na taasisi zote za Serikali zinapitia NMB, lakini hapakaguliwi. Sasa hivi nataka kufikia mwisho mpaka binadamu yule au biashara yao imekufa unakwenda kufukua makaburi. Tuache biashara ya kufukua makaburi. Kama ni sheria, walete Bungeni, Bunge lipitie sheria, wakaguliwe NMB, NBC na taasisi zote ambazo inabidi zikaguliwe. Kama hawakagui ndiyo mianya inapita ya pesa kwenda nje. Kama hawaiangalii mianya hii, leo kama taaisisi kubwa, mikopo yote ya Serikali iwe ya wanafunzi, inapitia NMB, halafu wanasema hawaikagui, wanalionaje hili neno? Ni hatari kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni lazima CAG awe na meno. Sheria ya CAG iletwe irekebishwe, apate fedha za kutosha ili awe na uwezo wa kukagua. Ama la, CAG anakagua chini ya 40%, ina maana maeneo mengi anashindwa kukagua. Kama anashindwa kukagua, ni vipi wataweza kujua athari ambazo zinapatikana katika maeneo mbalimbali? Leo hii unamwona CAG anashindwa kukagua maeneo mengine. Hakuna haja ya kufichaficha, tuseme aah, hapa TAKUKURU tusikague.

Mheshimiwa Spika, kwa nini TAKUKURU isikaguliwe? Pesa zinazokwenda pale ni za Watanzania. Matumizi ya pale ni ya Watanzania. Kama watu hawa hawakaguliwi, ndiyo mianya hiyo, maana watu wanatumia pesa bila kukaguliwa. Maana Jeshi wanakagua, ndiyo ambapo nilitegemea ni sehemu nyeti sana, lakini anasema maeneo mengine hatukagui. Hiki ni kigugumizi ambacho hakina maana, naomba Mheshimiwa Waziri atakapoingia katiak ku-wind- up anipe majibu kwa nini maeneo mengine yameachwa yasikaguliwe, tunaachia watu tu wanatumia wanavyotaka wao, wanakuwa na viburi vya kutosha? Hivyo naiomba Serikali iifanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia suala la barabara. Leo hii Mikoa ya Lindi na Mtwara ndiyo kwenye uchumi. Tunaona uchumi wa Mkoa wa Lindi kwa ajili ya korosho imekuwa ni green gold kulinganisha hata na madini mengine, lakini hatuna barabara. Tumekuwa maskini watu wa Mkoa wa Lindi, hapapitiki leo kwenda Liwale, Liwale ina Selous, lakini hakuna barabara, Liwale ina korosho, hakuna maendeleo ya barabara, Nachingwea hakuna barabara, Kilwa hakuna barabara. Sasa wanapelekaje uchumi bila kupeleka na barabara? Uchumi utakwenda sambamba na miundombinu. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atuambie, bajeti iliyopelekwa katika maeneo yale yanayozalisha, Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma inakwendaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana.