Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kuwapa fidia wananchi wangu wa Jimbo la Makambako. Nawashukuru sana, kwa dhati kabisa kwa sakafu ya moyo wangu, nawashukuru sana, wamefanya kazi nzuri. Kwa sababu fedha hizi wamezidai kwa muda mrefu, lakini kupitia ahadi ya Mheshimiwa Rais imetekelezwa. Narudia tena kuwashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaposhukuru, kuna ombi tena kuhusu fidia nyingine. Pale Makambako kupitia Wizara ya Ujenzi, wana eneo ambalo waliomba, tuwaombe wananchi kwa ajili ya kujenga One Stop Centre katika Kijiji cha Idofili, kilometa tano tu kuingia Mjini Makambako ukitokea barabara ya Iringa. Katika eneo hilo, vile vile kunatakiwa kulipwa fidia ili waanze kujenga One Stop Centre. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri katika hitimisho lake, basi aseme neno ili roho za wananchi wangu wa Jimbo la Makambako waweze kupona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu, tuna Liganga na Mchuchuma. Imezungumzwa kwa muda mrefu sana kuhusu uchumi wa Liganga na Mchuchuma. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Fedha, atuambie ni nini kinachokwamisha Liganga na Mchuchuma isitekelezwe au isianze? Kwa hiyo kwenye hitimisho pia nitaomba nipate majibu, tatizo ni kitu gani ambacho kinafanya isianze? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine tumejenga zahanati nyingi sana katika nchi yetu ambayo magofu haya ni mengi ikiwepo Jimbo la Makambako. Makambako tuna zahanati ya vijiji zaidi ya 13 ambazo wananchi, Waheshimiwa Madiwani, Serikali, Mfuko wa Jimbo pamoja na mimi Mbunge wao tumejenga zahanati hizi. Ombi langu kwa Wizara ya Fedha, tuone sasa ni namna gani kwa nchi nzima na kupitia hata Halmashauri yangu ya Makambako tuzimalize zahanati hizi ili zianze kufanya kazi kusogeza huduma kwa wananchi wetu na hasa akinamama na watoto.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine napenda sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha, nipate majibu hasa ya miradi ya maji 17 nchini ikiwepo na Makambako kwa fedha za kutoka Serikali ya India kwa mkopo nafuu. Maana mpaka sasa hatuelewi kazi hii inaanza lini. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri pia katika miradi hii 17, mmojawapo upo Njombe, Makambako, Wanging’ombe na mahali pengine Zanzibar kule kuna mradi mmoja nadhani. Basi ni vizuri Mheshimiwa Waziri atuambie ni lini miradi hii itaanza ili wananchi waweze kupata huduma hii ya maji kama ilivyokusudiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, katika Wizara mbalimbali ambazo tumekuwa tukichangia hapa ndani, Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema, nami naomba niseme Mheshimiwa Waziri. Namwomba Waziri wa Fedha, fedha hizi za miradi mbalimbali basi ziende kwa wakati ili shughuli zilizopangwa kule kwenye Halmashauri yetu ziweze kwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika na Mheshimiwa Waziri, kupanga ni kuchagua. Kuna watu walizungumzia habari ya kununua ndege, habari ya reli, habari ya huo umeme kwamba huo umeme wa kutoka Bonde la Rufiji hauna manufaa na reli haina manufaa. Niseme kwamba Bunge lililopita la mwaka 2010 - 2015, Waheshimiwa Wabunge walisema hapa, ni nchi ya ajabu hii kutokuwa na ndege zake yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Serikali imetii kupitia Mheshimiwa Rais wetu, maana alikuwepo Bungeni hapa wakati ule akiwa Waziri, leo ametii, amenunua ndege katika nchi yetu, tunasema kwa nini amenunua ndege, hazina manufaa. Tukiwa hapa Bunge la mwaka 2010/2015 tulizungumzia hapa, ni nchi gani haina reli? Reli hii ya kati ni reli ambayo imepitwa na wakati, tunataka standard gauge. Mheshimiwa Rais ametii, amekubali, sasa ametafuta fedha tunajenga reli ya standard gauge. Kupanga ni kuchagua ndugu zangu, ni lazima tusiwe vigeugeu, tuiunge mkono Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulizungumzia hapa kwamba wawekezaji wanashindwa kuja ni kwa sababu umeme hautoshi. Leo ufumbuzi umeme kutoka Bonde la Rufiji, tunasema ule mradi haufai. Sasa tunajikatisha tamaa wenyewe kwa wawekezaji wanaokuja kwamba kumbe umeme kule haupo. Tuunge mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano juu ya mipango mizuri ambayo ipo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mpango na Wizara yake na Watendaji wake, achape kazi asonge mbele. Mipango ni mizuri sana. Kwa hiyo, sisi tuko nyuma yako, tunamuunga mkono kupitia bajeti hii.

Mheshimiwa Spika, wenzangu wamesema hapa, Mheshimiwa Waziri amekuwa muwazi, ameeleza kila jambo; hili liko hapa, hili bado hivi, hili liko hivi. Tunamuunga mkono, achape kazi, asonge mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.