Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi kubwa ambazo zimefanywa lakini bado kuna mambo kadhaa yanahitaji umakini mkubwa wakati wa utekelezaji wake ili kuruhusu sekta hii kukua zaidi na kulipatia Taifa pato kubwa na stahiki. Naomba kushauri mambo muhimu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara iongeze bajeti katika Chuo chetu cha Madini pamoja na kuhakikisha kwamba kunakuwa na wataalam wa madini na wanaandaliwa kikamilifu ili kukidhi haja ya kupata pato la kutosha katika sekta ya madini hapa nchini. Je, Wizara inashindwa kuandaa wataalam wengi zaidi na kuwa na Maafisa wa Madini angalau kwenye kila tarafa katika nchi hii?

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imejaliwa kuwa na deposit ya kutosha ya madini, ukiacha yale ya vito vya thamani, lakini yapo pia madini ya chumvi, mchanga, gypsum ambayo yametapakaa kila sehemu ya nchi yetu. Namna bora ya kuwa na uratibu mzuri wa sekta hii ni kuwa na maafisa wake katika ngazi za chini za utawala. Sekta ya madini imekuwa centralised mno, ikiwa tatizo ni uchache wa wataalam basi dawa yake ni kuanda wataalam zaidi kupitia chuo chetu cha madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu utaratibu wa kukata madini hapa hapa nchini. Jambo hili ni jema sana na likifanywa kwa weledi mkubwa litaipatia nchi mapato makubwa sana. Tatizo ninaloliona hapa ni kwamba hizo mashine zenyewe za kukatia madini hapa nchini ni chache mno na bado zinatumia teknolojia ya zamani kidogo. Jambo hili linasababisha kuwa na foleni kubwa katika maeneo ya kukatia madini na kuongeza kasi ya utoroshaji wa madini hivyo Serikali kupoteza mapato yake mengi. Jambo hili ni jema, kama nilivyotangulia kusema hapo awali, lakini linahitaji perfect and gradual changes na si haraka haraka tu, bila kuimarisha mifumo yetu ya ndani katika kuliratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kutoipatia fedha za maendeleo Wizara hii. Kiwango cha asilimia 3 pekee cha fedha za maendeleo ni kidogo mno kwa mustakabali wa maendeleo ya sekta hii muhimu. Wizara inapaswa kuwa na mkakati maalum na mahsusi wa kuhakikisha kuwa fedha za bajeti zilizopitishwa na Bunge zinapatikana ili sekta hii ijikwamue. Wizara ishirikiane na halmashauri za wilaya nchini katika kuhakikisha kuwa machimbo yake ya madini na mchanga yanatambuliwa na kuratibiwa vizuri ili mapato yake yawe registered vizuri na yafike kila sehemu inayohusika kwa mujibu wa Sheria ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni kuhusu zoezi la utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini ya mchanga na gypsum. Madini haya yapo maeneo mengi ya nchi yetu, watu wengi wanatamani kufanya biashara ya madini haya, lakini utaratibu wa kupata leseni bado ni mrefu. Tunaomba leseni za uchimbaji wa madini haya ziwe zinapatikana katika ngazi ya halmashauri.