Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami nichangie Wizara hii ambayo kama itasimamiwa vizuri inaweza kuwa mhimili mmojawapo ambao utachangia katika uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi za dhati sana kwa Mheshimiwa Rais kwa kuona kwamba Wizara hii sasa iwe Wizara kamili na kama ilivyoundwa na Naibu Mawaziri wawili kaipa thamani kubwa. Niwaombe viongozi walioteuliwa katika nafasi hii, Waziri na Naibu Mawaziri waione thamani ya Wizara hii na waitendee haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na jambo moja ambalo hatulioni sana. Wabunge wenzangu wamezungumza mambo mengi lakini na Wizara wenyewe katika kitabu chao wamejielekeza katika mambo mengi na Kamati pia. Wizara hii inaweza ikafanya kitu kimoja ambacho mimi nakiona ni bora sana. Tumekuwa tunakwenda nchi kama Dubai tunaona uhuria uliopo wa biashara lakini Singapore na maeneo mengine ambayo wamekuwa katika uhuria wa biashara kwa maana ya kwamba unaweza kwenda na mzigo wako pale lakini usiulizwe ili mradi tu unalipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri Wizara hii waanzishe soko huria la dhahabu kwa maana wananchi wa ukanda huu wa nchi 10, 13 za nchi hizi za Afrika Mashariki na Kati zina dhahabu nyingi sana na wananchi wanatafuta mahali pa kuuza dhahabu lakini hawana. Matokeo yake sasa watu wamekuwa wanapitisha dhahabu kinyemela na kwenda kuuza Kenya kwa sababu ya ile fursa iliyopo ya kuuza dhahabu Kenya kuliko ukionekana na dhahabu Tanzania. Nashauri Wizara ije na mkakati ambao utakuwa na soko ambapo Tanzania itakuwa sehemu ambayo itapelekea watu wa nchi jirani kuleta dhahabu yao hapa na kufanya wananchi wa nchi mbalimbali za huko waje wanunue lakini pia itaongeza kwa upande mwingine suala la utalii. Kwa hiyo, itachochea biashara na utalii pia katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo taarifa mbalimbali katika Wizara ya Madini zikiwepo zile quarter degree sheet ambazo zipo zenye taarifa za madini, zile zina taarifa za muda mrefu sana. Naomba Wizara hii kwa kuwa sasa imekuwa Wizara kamili wajikite kuboresha taarifa ili tuwe na latest kiasi kwamba mtu ukichukua ile taarifa ya pale uweze kuiuza kwenye maeneo mengine na kufanya wawekezaji waje. Sisi tunakosa wawekezaji mpaka mtu awe na shimo, anatoa dhahabu au aina nyingine ya madini, hatuna taarifa kama zilizofanywa na geo-survey wakati ule na zilizofanywa na taasisi zingine. Tumefika mahali tumesahau kabisa kazi ya kuhuisha taarifa za maeneo ambayo madini yapo katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na masuala ambayo yalikuwepo hapo nyuma, nashukuru sana sasa hivi Serikali imeliona kwamba gemstone ni madini ambayo yanatakiwa yachimbwe na wazalendo tu kwa maana wananchi wa Tanzania. Suala hili lilikuwa linaleta kero kubwa hasa tanzanite pale walipoingia ubia na hawa watu wa Afrika Kusini. Hii ilituletea shida kwa sababu ni miongoni mwa rasilimali chache sana ambazo tunazo nchi ya Tanzania na zinapatikana Tanzania lakini nchi za India, Afrika Kusini na Kenya ndiyo walikuwa wanaongoza kuuza tanzanite katika masoko ya dunia. Kwa mpango huu ambao umefanywa na Serikali na hili pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wake mkubwa na wa makusudi kabisa kujenga ukuta pale, kwa maana hiyo sasa kama nchi tutanufaika na rasilimali hii ambayo ipo hapa Tanzania pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo nataka niombe Mheshimiwa Waziri na Wasaidizi wake walione, suala la masoko ya madini haya. Ni vizuri basi kama Serikali ikatangaza madini ambayo yapo katika maeneo yetu, hata hizo tanzanite na rubi na madini ambayo yalisemwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge masoko yake ni mpaka mtu tu a-penetrate mwenyewe kwenda kutafutia soko. Hatuna latest taarifa kama nilivyosema kwenye maeneo haya lakini pia ni kwa kiwango gani wazalishaji wetu wa migodi midogo wanatambuliwa na kujengewa uwezo wa kuuza katika soko la dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, naunga mkono hoja na nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia.