Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

Hon. Ajali Rashid Akibar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

MHE. AJALI R. AKBAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii mpya ambayo Waheshimiwa Wabunge wake au Mawaziri wake ni vijana na wapo watatu. Hawa Mawaziri wapo watatu, kwa nini waliteuliwa kuwa watatu na hii Wizara ni nyeti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sidhani kama Mheshimiwa Rais amewapenda sana kwa kuwapendelea ili kuwapungunguzia kazi. Mheshimiwa Rais ameonesha wasiwasi wake kuhusu Wizara hii ambayo ni nyeti. Kwa sababu matarajio ya Mheshimiwa Rais ni mapato makubwa sana katika Wizara hii ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja tuliwahi kusikia kwamba mambo ya madini yanatokana na mashetani, sasa haya mashetani ndiyo yanafanya nchi hii isipate madini. Kama kweli sisi hatupati madini, basi namwomba Mheshimiwa Angellah aende South Africa akamlete Sangoma aje atuchinjie ili tuwezeshwe kupata madini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli madini yataendelea kuwa na unyeti na usiri mkubwa sana. Huyo aliyesababisha usiri mkubwa sana sio mtu mwingine isipokuwa ni STAMICO. STAMICO ni kubwa kuliko Wizara yako Mheshimiwa Waziri. Mawaziri lazima mfanye maamuzi magumu. Bila kuivunja STAMICO hamwezi kuleta mabadiliko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO ni mzigo mkubwa sana kwa sababu ni Shirika la Serikali. STAMICO leo imeingia mkataba na Tanzanite One, lakini ule mkataba wenyewe una utata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanasheria wa STAMIGOLD na STAMICO wameshindwa kuelewana. Wanaiomba Serikali ninyi mkae mwapatanishe, wakati tunategemea wataalam wetu wa madini wapo STAMICO. Hivi ninyi Serikali mtawapata wapi wataalam? Hebu angalia utata huo. Kwa hiyo, maana yake STAMICO ni mzigo kwenu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, STAMICO wamekuwa ni tatizo. Leo STAMICO walikuwa wanamiliki mradi wa makaa ya mawe. Katika mradi wa makaa ya mawe wamechimba yale makaa wamepata tani 8,000. Mradi wa Kiwira Kabulo. Wameuza wamepata shilingi milioni 500. Hebu angalia huo uwekezaji. Ukubwa wa STAMICO wanapata shilingi milioni 550 na kilo 2,200 wameweka stoo wanasema wanasubiri kuuza. Inavyosemekana ni kwamba yale makaa ya mawe siyo chochote ila ni uchafu. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba hii ni kampuni ambayo ipo kwa ajili ya kuleta hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Mawaziri, ningekuwa ninyi leo leo jioni hii STAMICO ninge-declare kuivunja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO ina madeni makubwa kuliko uzalishaji wake ambao wale watu wa Kiwira wanadai pale. Madeni yaliyoko pale ni makubwa sana, lakini wao wanaonesha kwamba production ni milioni 550. Kuna sababu gani ya kuendelea kuwa na Kiwira tena?
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo kama haitoshi, hawa watu tena wameingia na STAMIGOLD. Kule wameumiliki ule mgodi, wamezalisha madeni ya shilingi bilioni 60. Kwa kweli haiwezekani hawa watu kuendelea kuwa ndani ya Wizara hii ambayo ni mpya, tena ina Mawaziri vijana. Wakiendelea kuwa nao, wataondoka nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, STAMICO ina majukumu makubwa ikiwa ni pamoja na kuwasaidia vijana. Hivi kweli itaweza kuwasaidia vijana kama wao wenyewe hawajiwezi? Wameandika hapa kwamba ni kutoa ushauri na kutoa huduma kwa vijana. Naomba vijana nchi mzima, kama wanaenda kushauriwa na STAMICO watafilisika kama STAMICO ilivyofilisika. Wao wasiifuate STAMICO, kuna utafiti hapa umefanywa na Kampuni kutoka STAMICO, wameenda kule, watu wamechimba mita 100 kwenda chini madini hawakuyapata. Maana yake ni utata uliopo ndani ya STAMICO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifikiria mwanzoni kwamba kama wameshindwa kwenye madini, basi hawa watu waende kwenye kokoto kule Ubena Zomozi. Hata zile kokoto pale Ubena Zomozi zimewashinda. Kama wameshindwa kuchimba kokoto, mnategemea hii STAMICO kweli itatusaidia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile wameomba, wamesema kwamba sasa hivi tunatafuta mwekezaji. Hivi kwenye kokoto unatafuta mwekezaji? Kokoto, yaani mtu ukiwa na shilingi milioni hamsini tu, inatosha kwenda kuchimba zile kokoto. Naomba Mawaziri, kwa kweli hatuna sababu ya kutafuta. Wamesema wanaenda kutafuta fedha, hizo hela wanaenda kutafuta wapi badala ya kuleta hapa Bungeni ili tuwape fedha wakachimbe zile kokoto?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaotoa fedha ni sisi Waheshimiwa Wabunge, wao wanasema wanafanya mpango wa kutafuta fedha, hizo fedha wanaenda kuomba wapi? Nadhani wangeleta hapa bajeti yao, wakasema maadamu tumeshindwa madini sasa tunataka fedha, shilingi milioni 200 ili tukachimbe zile kokoto. Nadhani ndiyo kazi rahisi ambayo wanayoiweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni hizi zimekuwa ni mzigo kwetu sisi; na madini, karibu asilima 90 ya Watanzania hawayajui. Ajabu asilimia hata asilimia 75 ya hawa Wabunge hatuyajui. Hata mimi ukija kunishauri leo, ukaniambia niingine kwenye biashara ya madini sitayajua. Kwa hiyo, naomba Wizara hii mpya ifanye semina kwa Watanzania, wapate kuyajua haya madini ni nini? Madini, watu wengi hatuyajui na yataendelea kuwa na utata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nimeona ni huo, kwa kuwa Wizara hii ni mpya, lakini napongeza sana jitihada ambazo anachukua Mheshimiwa Rais na kuujenga ule ukuta. Anaonesha wasiwasi na bado ameteua Mawaziri wengi kwenye Wizara moja ambayo ni ndogo, lakini ni mpya, tena vijana; anaonesha kwamba bado ana wasiwasi lakini bado anaamini kwamba Wizara hii ikisimamiwa kwa dhati itatoa production zenye tija. Nawaomba hawa vijana wasimamie. Huo ndiyo ulikuwa mchango wangu leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa kuwa hii STAMICO itaendelea kuwa msiri na itakuwa mzigo kwetu sisi. Leo waivunje. Ahsante sana.