Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya tote ninampongeza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William V. Lukuvi pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Angelina S. Mabula, kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya wananchi hususani katika Mkoa wa Dar es Salaam hununua nyumba maeneo ya makazi ya watu kisha kubadilisha matumizi ya ardhi hiyo kwa kujenga karakana au viwanda vidogo. Naishauri Serikali iwachukulie hatua za kisheria wale wote wanaofanya ubadilishaji wa matumizi ya ardhi bila kuzingatia sheria zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, ili kupata wataalam wa ardhi wa kutosha Serikali ifanye mpango mkakati wa kudahili wanafunzi wengi katika vyuo vyetu hapa nchini katika fani mbalimbali zihusuzo mambo ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itenge maeneo ya ardhi na kuwamilikisha kisheria wafugaji wote nchini na wakulima ili kuondoa migogoro ambayo hutokea mara kwa mara katika sehemu mbalimbali hapa nchini mwetu. Kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili kuweza kujua sheria za ardhi na kupunguza migogoro katika sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kulipa fidia kwa wakati kwa wale wananchi ambao ardhi zao zimetwaliwa na Serikali kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Walipe fidi hizo ili wananchii waweze kutumia fidia hiyo kuweza kutafuta maeneo mengine ya makazi au mashamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuharakisha upatikanaji wa hati miliki za ardhi na pia vibali vya ujenzi kwa haraka maana katika maeneo mengi kuna urasimu wa upatikanaji wa hati miliki na building permit huchukua muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kurasimisha pia maeneo yaliyojengwa kiholela (squatters) hususani katika Mkoa wa Dar es Salaam; kwa mfano Manzese, Tandale na kadhalika ili wananchi waweze wapate hati ambazo zitawasaidia kuweza kupata mikopo benki na kuboresha nyumba zao, pamoja na shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itoe fedha zilizotengwa katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019 kwa wakati ili kuisaidia Wizara kutekeleza majukumu yake kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, namwomba Mungu awape afya njema na umri mrefu Mheshimiwa William
V. Lukuvi, pamoja na Naibu wako Mheshimiwa Angelina S. Mabula ili muweze kuwatumikia Watanzania katika Wizara hii muhimu ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa weledi.