Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mungu ambaye ametupa uzima na uhai mpaka leo tuko mahali hapa. Naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi, naomba nimpongeze sana Waziri kwa kazi kubwa ambayo anaifanya pamoja na Naibu wake, wanafanya kazi kubwa sana kusema kweli. Lazima tuwape pongezi kwa sababu wamejitahidi kadiri ya uwezo wao, lakini Mungu ataendelea kuwasimamia kwa sababu kazi mnayofanya ni ngumu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara hii naye anajitahidi sana. Ni mama, naomba nikupongeze mama yetu, endelea kufanya kazi, Mungu ataendelea kukusimamia na kukupigania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Rais kwa kuona sasa jukumu la ardhi ni kubwa ameona kwenye manispaa, halmashauri, vile vitengo vyote vitoke viwe vinaripoti kwa Katibu Mkuu moja kwa moja ili kurahisisha kazi iweze kuwa nzuri zaidi. Naomba nimpongeze sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametufanyia kazi kubwa, sasa tunajua Wizara imekuwa Wizara kamili kwa ajili ya kazi ambayo inatakiwa kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Mkoa wetu wa Katavi; Katavi ni mkoa na pale Mpanda Mjini ni Manispaa. Tuna Maafisa wachache sana wa Ardhi na Mkoa wa Katavi unakua kwa kasi kubwa sana. Mkoa wetu wa Katavi maeneo mengi hayajapimwa, hususan Mji Mkongwe pale Mpanda Mjini, Kata ya Kashaulili; ule mji umepimwa lakini wananchi wale hawajapata hati mpaka leo. Tunajua hati ni muhimu sana ndani ya maisha yetu ya kifamilia maana hati ndio msingi wa maisha ya kila jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara ya Ardhi ndani ya Mkoa wetu wa Katavi kwa sababu sasa hivi imekuwa ni Wizara ya Ardhi, tunaomba watuongezee watumishi, hatuna watumishi kabisa. Ndiyo maana sasa hivi ukiangalia Mpanda migongano ya ardhi imekuwa ni mikubwa sana kutokana na kwamba watumishi hatuna na wananchi wanajenga kiholela. Sasa ukija upimaji inakuwa ni shughuli kwa sababu viwanja vile vinagongana na maeneo mengi yanakuwa kuna migongano ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Kata yetu ya Semulwa, Mtaa wa Kichangani, haujapimwa kabisa na ni ndani ya Manispaa ya Mpanda Mjini, haijapimwa kabisa. Naomba Wizara ya Ardhi sasa hivi kwa sababu, imeshakuwa Wizara kamili ndani ya maeneo yetu husika, tunaomba tuletewe Wilaya ya Mpanda wafanyakazi wa kutosha, ili migogoro ya ardhi Mpanda iweze kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Kata ya Mpanda Hoteli na Kata ya Ilembo. Wananchi wa Mpanda Hoteli na Kata ya Ilembo walikuwa wana mashamba walikuwa wanalima kwa muda mrefu, lakini sasa imekuja kuwa migongano na jeshi; jeshi wanasema ile ardhi ni ya kwao, wananchi wanasema ardhi ile ni ya kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara ya Ardhi, Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri pamoja na Wizara ya Ulinzi, tuje tutatue hili tatizo Mpanda. Ni tatizo kubwa mno kiasi ambacho ni mfarakano kusema kweli, naomba sana msaada wao, waje mtatue tatizo hili. Wananchi wanasema ardhi ni ya kwao na Jeshi wanasema ardhi ni ya kwao. Sasa migongano hii; na ukizingatia ndani ya Wilaya ya Mpanda imekuwa ni Mkoa, tunahitaji nafasi kubwa zaidi. Nashauri Jeshi waweze kutafutiwa sehemu nyingine, yale maeneo wapewe wananchi kwa sababu migongano yao haifurahishi kusema kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Wilaya yetu ya Mpanda tulijengewa nyumba za National Housing. Tunaishukuru sana Serikali pamoja na shirika lenyewe, limejenga nyumba nzuri sana lakini hapa kuna tatizo. Hizi nyumba zimejengwa kwa sasa hivi ni takriban miaka kama mitano iliyopita. Hizi nyumba hazina watu na zimekwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa kuna tatizo; wamepanga sijui, wamenunua watu takriban kama sita tu katika nyumba mia mbili na kitu. Sasa sielewi: Je, hizi nyumba bei yake ni kubwa au National Housing hawana mpango mkakati wa kuweka hizi nyumba ziweze kupangishika kwa bei nafuu, wakawapangisha wananchi? Sasa hapo sielewi, kwa sababu zile nyumba sasa hivi zinaishi nyoka, manyasi yamelundikana pale, hazifanyiwi ukarabati wa aina yoyote. Kwa kawaida ukijenga nyumba, kama haiishi binadamu nyumba ile inakuwa boma. Sasa nyumba hizi zimetumia pesa nyingi sana za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hizi nyumba, National Housing watafute jinsi ya kufanya; aidha, wapunguze bei wapangishe wafanyakazi ambao wako ndani ya Mkoa wa Katavi, kwa sababu Katavi sasa ni Mkoa. Wawapangishe wafanyakazi wa Mkoa wa Katavi au waende wawakopeshe wafanyakazi wa Serikali ndani ya Manispaa, Halmashauri ili zile nyumba ziweze ku-survive kwa sababu pesa nyingi zimetumika kujenga zile nyumba na ni nyumba nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali itumie hekima kwa hizi nyumba za National Housing zilizojengwa kwenye Wilaya. Walijenga kwa manufaa ya Watanzania ili kupitia Serikali yao waweze kupata nyumba hizo kwa bei nafuu. Sasa kutokana labda na kuuziwa viwanja vile kwa bei kubwa na wenyewe wanataka kuweka bei kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba niunge mkono hoja.