Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, naomba nishukuru sana kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya Maji. Naomba niungane na waliotangulia kuwapongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na msaidizi wake, lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo amekuwa anaifanya katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma hii muhimu ya maji.

Mheshimiwa Spika, kipindi chote ambacho nimekuwa nasimama hapa nimekuwa ni mtu wa kuomba tu juu ya mahitaji ya jimbo ambalo ninaliongoza, lakini katika Wizara hii nitakuwa mtovu wa fadhila kama sitatoa neno la shukrani kwa Mheshimiwa Waziri, Mzee wangu Mheshimiwa Kamwelwe, kwa kweli, ametitendea haki watu wa Wilaya ya Nachingwea, mara zote ambazo tumemuomba mahitaji yetu amekuwa ni msikivu, lakini pia amekuwa ni mtu ambaye amejali sana kwa kufanya ziara si chini ya mara tatu katika Wilaya yangu ya Nachingwea kuja kuona hali ya upatikanaji wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika hili nilikuwa naomba kabisa nimpongeze na nimtakie kila la heri mzee wangu kwa kazi nzuri ambayo anaifanya na tunaendelea kumuombea mambo mazuri zaidi ya hapo alipo ili ikiwezekana basi mambo yakae sawa.

Mheshimiwa Spika, yako maeneo ambayo kimsingi tuliomba, moja ni eneo la utanuzi wa mtandao wa maji ya Mbwinji. Kwa mwaka jana alitutengea shilingi bilioni moja na katika fedha ile tulipata zaidi ya shilingi milioni 870 na hii imetuwezesha kutanua maji. Katika Wilaya yangu mimi viko vijiji takribani nane ambavyo toka uhuru wa nchi hii upatikane hawakuwahi kupata maji safi na salama, lakini sasahivi tunavyozungumza wananchi wa Kata za Naipanga, Rahaleo, Chiwindi, Nkotokuyana, Stesheni, Mtepeche, pamoja na maeneo yote yanayozunguka mradi huu sasa hivi wanapata maji safi na maji salama. Kwa hiyo, katika hili Mheshimiwa Waziri naomba upokee pongezi na salamu kutoka kwa wale wananchi ambao uliwatembelea mwaka jana na ukaenda kupanda kwenye yale matenki ya pale Chiumbati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nilitaka pia nione na nipongeze ni eneo la upatikanaji wa fedha abayo sasa hivi nafikiri wametutengea. Nimesoma katika kitabu hiki cha bajeti nimeona kuna shilingi bilioni mbili zimetengwa kwa ajili ya kuuendeleza mradi huu kwa ajili ya kuweka chujio ambalo litasaidia kupata maji mazuri zaidi. Kwa hiyo, sio fedha ndogo hii ni fedha kubwa na kwa uchapakazi ambao Mheshimiwa Mzee Kamwelwe ameendelea nao nina hakika fedha hii tutaipata kwa wakati, ili wananchi wa Masasi, Nachingwea, pamoja na Ruangwa ambao wananufaika na Mradi wa Mbwinji waweze kupata maji ambayo kimsingi ni mahitaji makubwa sana ambayo tumekuwa tunayahitaji.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo pia, nilitaka nilizungumzie, nimeangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, nimeangalia kwenye kitabu ukurasa namba 120, nimeona fedha ambayo Wilaya ya Nachingwea tumetengewa, shilingi bilioni moja karibu na milioni mia mbili kwa ajili ya maji vijijini. Tunavyo Vijiji vya Mtua ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vinakosa maji, lakiini pia tunacho kijiji cha Ndomoni, tunacho Kijiji cha Marambo pamoja na maeneo mengine, yote hayo yatapata maji. Ila wito wangu Mheshimiwa Waziri, Mzee wangu Mheshimiwa Kamwelwe naomba nikuombe, mpaka sasa hivi wakandarasi ambao wamepewa kufanya kazi katika maeneo haya tayari tender zilishatangazwa.

Mheshimiwa Spika, tunaomba msukumo wako, ili kazi ya kupeleka maji kwa sababu fedha tayari mmeshatutengea, naomba kwa heshima na taadhima ifanyike, ili wananchi hawa waweze sasa kwenda kupata maji ambayo fedha yake kimsingi tayari hata mkurugenzi wangu mlishamuita na mmeshampa maelekezo juu ya kwenda kusimamia zoezi la kuanza kazi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, mradi huu au miradi hii ni muhimu sana na itawasaidia wananchi wa maeneo haya kupata maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo nikuombe Mheshimiwa Waziri pale Nachingwea kuna eneo moja linaitwa Mnero Miembeni, kuna mradi mkubwa ambao mwaka jana ulikuwa unatengenezwa na mkandarasi mmoja ambaye kimsingi kazi yake mpaka sasa hivi bado haijakaa
sawa. Yapo maeneo ambayo amefunga solar ambazo haziwezi kusukuma maji na ule mradi ni mkubwa zaidi umetumia zaidi ya shilingi milioni 150, lakini mpaka sasahivi ninavyozungumza Mheshimiwa Waziri na ofisini kwako nilikuja, bado maji katika maeneo yale ya Mnero Miembeni ambayo yanahudumia vijiji karibu sita mpaka sasa hivi ninavyozungumza bado maji hayajaanza kutoka na yule mkandarasi ni kama tayari alishamaliza kazi.

Sasa tunaomba msukumo wako, tunaomba wataalam waje wachunguze ni sababu gani ambazo zimesababisha kufunga solar ambazo zinashindwa kufanya kazi tofauti na malengo ambayo yamkusudiwa.

Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ni njema, nia ya wizara yako ni njema ndio maana ulitoa fedha. Mradi ule ulikuwa umeenda pia na maendeo ya Nditi kule ambako kimsingi Nditi maji yanapatikana, lakini katika eneo la Mnero Miembeni bado kumekuwa na changamoto ambayo nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha hotuba yako basi utuahidi namna bora ambayo unaweza ukatusaidia, ili maeneo yale wananchi waweze kupata maji ambayo wewe mwenyewe umeyasimamia na mimi nashukuru sana umenipa ushirikiano katika kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka pia, niombe ni eneo la visima. Nilikuomba Mheshimiwa Kamwelwe visima na uliniahidi kwamba utatusadia tupate visima kwa baadhi ya vijiji ambavyo kwa muda mrefu tumekosa maji na uwezekano wa kupeleka maji haya Mbwinji utatuchukua muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, tunacho Kijiji cha Namanga, hali ni mbaya, wananchi wanatembea umbali wa kilometa karibu 40 kwenda kufuata maji. Hali ile kwa wale mama zetu kidogo imekuwa ni ya kukatisha tamaa. Nia yako ni njema na ulishaniahidi tangu mwaka jana kwamba utatusaidia. Nikuombe sana na ninaleta hili ombi tena, kwamba vile vijiji ambavyo uliniahidi kunipa visima angalao vinne, basi tutumie nafasi hii ili wale wananchi tuweze kuwasaidia na tuwatue mama zetu ndoo kichwani, ili waweze kufanya shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ambalo nilitaka nichangie ni eneo la mradi wa umwagiliaji. Ndani ya Wilaya ya Nachingwea tunayo miradi mikubwa miwili ya umwagiliaji, eneo mojawapo ni eneo la Matekwe. Mradi huu ni wa muda mrefu kwa kipindi cha nyuma tulishawahi kupata shilingi milioni 500, lakini mradi ulikoishia mpaka sasa hivi ni kama fedha imepotea. Pia pia Mheshimiwa Kamwelwe unakumbuka tulikupeleka eneo moja la Mitumbati pale ukatuahidi utatupa shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuukarabati na kuurejesha ule mradi katika hali yake ya kawaida, lakini mpaka sasa tunavyozungumza nimeangalia katika makabrasha yako sijaona kama umetukumbuka.

Mheshimiwa Spika, wale wananchi wamesimamisha shughuli zao za kilimo, lakini pia, tulikuwa tunatamani tuwarejeshe kwa sababu kipato chao kwa sehemu kubwa wanakipata kupitia maeneo yale. Mimi nikuombe sana mzee wangu na watu wa wizara muweze kuona namna ambavyo zile fedha ambazo tumeziomba zitakavyoweza kwenda kupatikana tuweze kurudisha ile miradi ya umwagiliaji ikae katika utaratibu ambao wananchi wetu wanaweza wakafanya shughuli zao za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, mimi naomba niunge mkono hoja na niwatakie kila la heri watu wa Wizara katika utekelezaji wa bajetio yao. Asante sana.