Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kama kuna wakati Serikali ya CCM imewahi kupigwa upofu na Mungu basi ni wakati huu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, maji ni siasa, maji ndiyo kila kitu nchi hii; na kama ukitaka uendelee kuwepo madarakani, hakikisha ya kwamba umewapelekea Watanzania maji. Ukienda vijijini wananchi wanalia, wanalalamika maji, ukienda mijini wananchi wanalia wanalalamika maji. Lakini unashangaa watu hawa hawaoni, hawasikii, hawaelewi! Fedha nyingi wamepeleka sijui wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitamani Waziri wa Fedha awepo hapa, naona hayupo, maana huyu ndiye tatizo. Nilikuwa Mjumbe wa Kamati ya Kilimo na Maji, kilio kilikuwa ni hiki hiki tangu niingie Bungeni mpaka leo, fedha haziendi.

Mheshimiwa Spika, walitenga zaidi ya shilingi bilioni mia sita haziendi, leo wanaleta tena. Shida si hawa Mawaziri waliokaa hapo, shida ni huyu Waziri wa Fedha na Naibu wake, hawa ndio tunatakiwa tuwasulubu kweli kweli. Kwa hiyo, mimi niwashukuru sana Waziri wa Maji na Naibu wake, wanajitahidi, wanafanya kazi nzuri ila wanaangushwa na huyu mtu huwa anakaa hapa. Sasa amekimbia ngoja nimuache. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alikuja Serengeti, akauona ule mradi wa maji pale Mugumu, una zaidi ya miaka mitano. Kama asingekuja kwenye mradi ule maana yake hakuna chochote ambacho kingekuwa kinaendelea pale, lakini ujio wake umesababisha mambo sasa yaende vizuri. Ni ushauri tu kwamba jitahidini, kwa sababu ninyi ndiyo mnatoa fedha, jitahidini iwezekanavyo, nendeni kwenye miradi yote nchi nzima. Ni bahati mbaya sana hamna chombo kinachosimamia kwa niaba yenu. Ulikuja Serengeti, ulienda kwenye ule Mradi wa Mugumu. Kuna Mradi wa Maji Nyagasense, ulitumia zaidi ya shilingi bilioni 500 mpaka ninavyoongea hakuna maji! Imetulazimu kama Halmashauri tuutangaze upya, lakini fedha za wananchi zilishatumika pale.

Mheshimiwa Spika, kuna Mradi wa Maji Kata ya Kibanchebanche, Kijiji cha Kibanchebanche, mradi ule umetumia shilingi milioni 557 na kampuni iliyokuwa inajenga mradi ule inaitwa Gross Investment Company, wamejenga DP, wamejenga tank, power house lakini chanzo cha maji hakuna, na mkandarasi alishatokomea na ndiyo maana nilikuwa nalia Mheshimiwa Waziri ungefika pale Serengeti nikakupeleka mwenyewe ukaona pesa zimechukuliwa, lakini chanzo cha kuleta maji kwenye tenki hakipo mpaka leo na hakuna chochote kinachoendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nikuombe wa hili Mheshimiwa Waziri, ama wewe ama naibu wako, naomba aje twende Serengeti akajionee mwenyewe, lakini wakati anakuja aje na wataalam wake na hatua ya nini kifanyike kwa ajili ya ku-rescue hizi shilingi milioni 557 ambazo zimetumika lakini hakuna maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, pia niombe wakati unapokuja kujibu, kuna zile fedha ambazo ni mkopo kutoka Serikali ya India, nataka kujua zimekwamia wapi? Maana tangu bajeti ya kwanza tulianza kuzungumzia fedha za mkopo kutoka Serikali ya India, imepita miaka hiyo mpaka leo hazijulikani. Kwa hiyo naomba unapokuja ku-wind up ueleze wananchi wa Mugumu ni lini watasambaziwa maji maana Mradi wa Maji Mugumu ni moja ya miradi ambayo ilikuwa inapata hizi fedha za kutoka India.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja pia aje na ufafanuzi. Mradi wa maji Mugumu uko class gani. Najua uko class C, je, unastahili kupewa ruzuku kwa ajili ya kulipia umeme? Na kama unastahili kupewa ruzuku, nani yuko responsible na kulipa hiyo fedha maana wananchi wanapata shida, kila siku tunachangishana tu kwa ajili ya kulipia maji lakini ni mradi ambao unastahili kupewa ruzuku na Serikali kwa ajili ya kulipia bill.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, mimi niwashukuru mnafanya kaz nzuri lakini mnatakiwa kwenda mradi mmoja baada ya mwingine. Ahsante sana nashukuru.