Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia kwenye bajeti ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba hali iliyopo sasa hivi kwenye nchi hii ni lazima tufike mahali Wabunge tukubaliane, kila mmoja anasema hapa kwamba hali ni mbaya sana katika jimbo lake, lakini wako watu wanapongeza baadae wanaanza kulalamika kwamba hali ni mbaya. Hiki kitu ndiyo kinachotuchelewesha sana kuleta maendeleo kwa sababu tunazungumza jambo ambalo hatuna uhakika nalo huku tukijua kwamba hali ni mbaya sana katika majimbo yetu.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2016/2017 kwenye bajeti iliyopita kulikuwa na mradi mkubwa ambao ulitaka kutekelezwa kwenye Mji wa Tunduma na kampuni kutoka Ubelgiji. Mradi huu ulikuwa na thamani ya Euro milioni 100. Mradi huu umeyeyuka na sasa hivi hata kwenye vitabu hivi vya Waziri huwezi kuuona mradi huo. Ukiangalia kwenye Mji wa Tunduma ambao uko mpakani mwa nchi nyingi ambazo zinapitia pale karibu nchi nane hakuna maji kabisa. Wananchi wangu ambao wamewekeza kwenye Mji wa Tunduma leo hii wanakosa maji, wageni wanaokuja kutembelea kwenye Mji wa Tunduma na kuingia kwenye nchi sasa wanalala Zambia. Kwa hiyo, tunakosa mapato na Serikali inakosa mapato kwa sababu hoteli nyingi pia zimeanza kufungwa kwenye Mji wetu wa Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nikuambie tu kwamba mimi wananchi wangu wameathirika sana, sasa hivi pale kwenye Mji wetu wa Tunduma na Wilaya nzima ya Mbozi pamoja na Momba tuna tatizo kubwa la typhoid kwa sababu ya kukosa maji. Watu wengi wanapoteza maisha kwa sababu ya kupata maji ambayo si safi na salama. Mimi jambo hili kwa kweli sitakubaliana nalo kabisa na nataka niseme Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi wafike mahali waelewe kwamba kipaumbele kikubwa ni kuhakikisha kwamba afya za Watanzania zinakuwa bora ili waweze kuzalisha na waishi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi hii ukizunguka maeneo yote kwenye Taifa hili, tumejaribu kuzunguka kila maeneo tukiwa na ziara ya Kamati ya Nishati na Madini wanafikiri sisi ni Kamati ya Maji, kila mtu anasema jamani maji huku hatuna. Nchi nzima hakuna maji, hali ni mbaya sana katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi Tunduma pale nahitaji miradi mikubwa ya maji. Juzi kulikuwa na miradi imekuja midogo sana ambayo haiwezi kutosheleza wakazi wa Mji wa Tunduma, tunahitaji maji ya kutosha kwenye Mji wa Tunduma ili wananchi wangu waweze kupona magonjwa ambayo wanaendelea kupambana nayo ya typhoid kwenye mji wetu. Tumepoteza watu wengi mno kwa sababu ya uzembe wa Serikali kuendelea kutokutoa fedha kwenye Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wengi sana wanawaangalia vibaya Waheshimiwa Mawaziri lakini ukweli ni kwamba Mawaziri hawa wafanye nini? Ukiangalia miaka mitatu kuanzia mwaka 2015/2016, 2016/2017, 2017/2018 huwezi kuamini utekelezaji wa bajeti ya maji ni asilimia 26 tu kwa miaka yote mitatu ukichukua uwiano. Kweli tunaweza tukasema kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ina lengo la kupunguza tatizo la maji kwa wananchi wa Tanzania kama kweli inatekeleza kwa asilimia 26 ndani ya miaka mitatu uwiano tumejaribu kuangalia. Wananchi wa Tanzania wameiamini Serikali hii na mkapigiwa kura halafu baadae mmeanza kuwababaisha wananchi wa Tanzania. Tunataka maji kwenye Taifa hili, tunataka kuondoa matizo kwenye Taifa hili yanayotokana na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii wameweka bajeti ya maji kidogo na utekelezaji wake kama tulivyozungumza lakini huwezi kuamini leo tunakwenda kununua ndege, tena juzi tumenunua ndege sita na juzi Mheshimiwa Rais anasema anaongeza ndege ya saba eti wanakwenda kuchukua tena cash hakuna kukopa. Hivi wananchi wa Tanzania asilimia tano wanaopanda ndege ndiyo waliomchagua Mheshimiwa Rais? Hivi asilimia tano wanaopanda ndege ndiyo waliowachagua Wabunge wa Chama cha Mapinduzi ambao ni wengi ndani ya Bunge hili wanashindwa kuona

huruma kwa wananchi wa Tanzania ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wanapata maji, afya nzuri na wanapunguza vifo ambavyo vinatokana na magonjwa ya maji? Mimi sikubaliani hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna mambo ya msingi, tulisema tunahitaji tuwe na kilimo cha umwagiliaji ili tuwe na kilimo bora ambacho kitakuwa kinazalisha chakula kwa muda wote. Huwezi kuamini mwaka 2016/2017 tulitenga bajeti ya shilingi bilioni 25 fedha iliyokwenda ni shilingi bilioni
1.2 peke yake. Mwaka 2017/2018 tumetenga shilingi bilioni 24 lakini fedha iliyokwenda ni shilingi bilioni mbili peke yake, tunafanya nini katika Taifa hili.