Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Zainab Mndolwa Amir

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (TAMISEMI) kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ipandishe madaraja Walimu waliofundisha kwa zaidi ya miaka mitatu ili kuweza kuwa- motivate na kufanya kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhamisho wa Walimu; kumekuwa na changamoto kwa Walimu pindi ambapo anataka kuhama kutoka eneo (Mkoa, Wilaya) kwenda sehemu nyingine. Aidha, kumfuata mwenza wake au kwa matatizo ya kiafya. Suala la Mwalimu husika kutafuta Mwalimu mwingine wa kubadilishana nae ni gumu. Hivyo, nashauri Serikali isimamie zoezi hilo na sio kuachiwa Mwalimu husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, posho ya mazingira magumu; kuna baadhi ya Walimu hususan wa vijijini, vituo vyao vya kazi vipo mbali sana na huduma za kijamii mfano mabenki na ofisi za Serikali hivyo hulazimika kutumia fedha nyingi kwa usafiri. Hivyo, naishauri Serikali itenge fungu maalum la posho kwa Walimu hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu kuongeza ujuzi (elimu); naishauri Serikali itenge fedha katika bajeti hii 2018/ 2019 ili iwasaidie Walimu ambao watahitaji kwenda kusimama katika vyuo vyetu. Maana elimu hiyo itasaidia kuwajengea uwezo zaidi wa kuwafundisha watoto wetu wa kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu wa madarasa na uhaba wa shule katika Wilaya ya Temeke, Mkoani Dar es Salaam. Hususan shule za sekondari kutokana na kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza mwaka 2018. Hivyo, naishauri Serikali itusaidie kutatua upungufu huo uliojitokeza ili kuondokana na wanafunzi hao kusoma kwa session yaani asubuhi na jioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa nyumba za Walimu katika sehemu mbalimbali katika nchi yetu. Naishauri Serikali iwajengee nyumba bora ambazo zitawekwa na umeme ili kumsaidia Mwalimu kuweza kuandaa andalio la somo, azimio la kazi na kusoma mada mbalimbali ambazo atawafundisha wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana kwa samani (meza, viti na kabati (shelves), katika Ofisi za Walimu. Katika Shule ya Msingi Yombo Dovya Kata ya Makangarawe, Jimbo la Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, katika ofisi za Walimu hakuna meza, makabati na viti. Hivyo, Walimu hulazimika kutumwa madawati kwa kukaa na kufanyia shughuli mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iweze kutenga fedha katika bajeti 2018/2019 kwa ajili ya kutengeneza samani hizo ili ziweze kutumika katika shule mbalimbali ikiwemo Shule ya Msingi Yombo Dovya. Pia shule hiyo ina uhaba wa vyoo vya Walimu, Walimu hulazimika kutumia vyoo vya wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, katika Shule ya Yombo Dovya kuna wanafunzi walemavu nao pia hawana choo ambacho kitawasaidia kulingana na walemavu. Hivyo basi kutokana na changamoto hizo, naishauri Serikali itenge fedha ambazo zitasaidia kutatua tatizo hilo la kujenga matundu ya vyoo vya Walimu na wanafunzi walemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kuwa Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI ushauri wangu atauzingatia.