Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. ELIBARIKI E. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa kwa heshima kabisa nianze kwa kuzishukuru Wizara zetu hizi mbili, TAMISEMI na Wizara hii inayoshughulikia mambo ya Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru sana kaka yangu na mzee wangu Mheshimiwa Mkuchika. Mzee Mkuchika nampongeza kwa sababu miongoni mwa Mawaziri wasikivu yeye ni miongoni mwa Mawaziri wasikivu sana. Nakumbuka lilipotokea tatizo la watumishi kuondolewa kazini mimi binafsi nilikwenda ofisini kwake na alipopata taarifa kupitia kwa aliyekuwa anakaimu kama Katibu Mkuu pale Wizarani ambaye pia alinihudumia niliona public service pale, Mheshimiwa Mkuchika nataka nimpongeze sana na watumishi wake wa Wizarani hakika ni watu ambao wana commitment ya kazi. Naomba hilo nilitambue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nimpongeze Mheshimiwa Jafo. Mheshimiwa Jafo nampongeza sana kwa sababu kwa muda mfupi katika Wizara ambayo Mheshimiwa Rais amemweka kuweza kulitumikia Taifa letu amekuja Jimboni kwangu na Wilaya yangu ya Ikungi zaidi ya mara mbili, Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu ni kwa Mheshimiwa Jafo naelekeza ushauri wangu kwa taasisi ambayo Rais amemweka kuiongoza. Taifa letu linakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa nyumba za Walimu wa shule za msingi na sekondari. Nataka nimshauri kaka yangu Mheshimiwa Jafo, kama tulivyofanya mikakati ya kulisaidia Taifa kuondokana na uhaba wa madawati nchi nzima, natoa rai ni wakati muafaka kwa Serikali yetu kuamua kwa makusudi kukomesha tatizo la ukosefu wa nyumba za Walimu nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Jimbo la Singida Magharibi. Kuna maeneo unakwenda Walimu wanatembea zaidi ya kilometa saba mpaka nane hawana mahali pa kukaa. Changamoto hii inapelekea utulivu wa Walimu ku-concentrate katika kuwafundisha watoto wetu kuwa mdogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tuliweza kutatua changamoto za madawati kwa kipindi kifupi namwomba Mheshimiwa Jafo, kaka yangu, nina imani na yeye bado ni kijana mwenzetu namwomba akae na Wizara yake, akae na watendaji, wafanye tathmini ya upungufu wa nyumba za Walimu nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kwa sababu ya uzalendo wetu na kulipenda Taifa letu tutakuja kumuunga mkono atakapoleta mapendekezo ya kujenga nyumba za Walimu nchi nzima hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niongelee suala zima la afya. Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilielekeza kujengwa kwa zahanati katika vijiji vyote na vituo vya afya katika kata zote katika Taifa letu. Mimi katika Jimbo langu nimeshaanza kujenga zahanati vijiji vyote kwa nguvu za wananchi na kwa kushiriki mimi Mbunge binafsi na kwa kutumia fedha za Jimbo. Mpaka sasa hivi tunavyoongea, kuna changamoto ya kumalizia pale ambapo wananchi wamefanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa Mheshimiwa Jafo, Jimbo la Singida Magharibi sasa hebu alitumie jimbo hili kama mfano wa majimbo katika Taifa hili kwa sababu sisi hapa tunapozungumza vijiji vyote vya jimbo tumeanza kujenga zahanati. Mimi juzi nimegawa zaidi ya vitanda 85 na nimevipeleka hata pale ambapo zahanati bado hazijakwisha lengo ni kuipa Serikali changamoto ili waone ya kwamba tuna kila sababu ya kuhakikisha wananchi hawa wanafikiwa na huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tuna maeneo ambapo wananchi wamemaliza kujenga maboma kwa zaidi ya miaka mitatu. Tuna kijiji cha Mnang’ana pale Sepuka wamejenga boma mpaka leo Serikali bado haijapeleka nguvu kwenda kumalizia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri na changamoto ambazo Mheshimiwa Jafo anakabiliana nazo katika sekta hii lakini bado kuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba zahanati ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi, mimi mpaka sasa hivi tuna maboma zaidi ya 17 ambayo tumeanza kuyajenga kipindi mimi nimeingia hapa kama Mbunge lakini bado msukumo wa halmashauri kwenda kumaliza ni mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mheshimiwa Waziri kaka yangu Mheshimiwa Jafo akitoka hapa leo, akifanya mawasiliano na Mkurugenzi wangu atamwambia ni maboma mangapi tumeyasimamisha. Mheshimiwa Naibu Spika anapiga makofi kwa sababu alikuja jimboni kwangu akajionea. Kwa hiyo namwomba kaka yangu Mheshimiwa Jafo maboma ambayo tumeshayasimamisha watuletee fedha tuweze kuyamaliza ili tuweze kuwaunga mkono na kuwatia moyo wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu, nakwenda kuzungumza habari ya vyumba vya madarasa. Nimpongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Jafo. Amefanya kazi kubwa ya kutuunga mkono pale ambapo wanafunzi wetu walikuwa wanatembea umbali mrefu, sisi tumeanzisha programu ya kuanzisha shule za msingi ikiwezekana hata shule tatu katika kijiji. Kwa mfano, Kata yangu ya Minyuge tumeanzisha shule mpya za msingi katika maeneo ya Mayaha, Minyughe na Misake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ni kwamba kuna baadhi ya maeneo watoto wanatembea kilometa 14 kwenda kutafuta shule katika makao makuu ya kijiji. Sasa maeneo ambayo tayari sisi kama Wabunge kwa kushirikiana na wananchi wetu tumeanzisha ujenzi wa shule mpya, tunaomba Serikali isichelewe kwenda kuweka nguvu kuhakikisha kwamba madarasa haya yanapauliwa na kumalizwa. Hilo ni la msingi sana katika kuwasaidia watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuna Kata moja inaitwa Mwaru, kuna eneo linaitwa Mtakuja, watoto wanatembea umbali wa kilometa 16 kipindi cha mvua mito inakuwepo, watoto hawawezi kwenda shule, lakini sisi tumejenga shule pale Mtakuja tumeshamaliza. Kwa kushirikiana na wananchi tumeshamaliza kuipaua. Namwomba Mheshimiwa Jafo anapofanya location ya Walimu Jimbo la Singida Magharibi aliangalie kwa jicho la karibu sana kwa sababu tumeweka commitment na tumeweza kuwasaidia watu wetu katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne, nizungumze kuhusiana na barabara. Ombi langu kwa Mheshimiwa Jafo na Serikali yangu kwa ujumla, Serikali yangu sikivu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi, naomba Mfuko wa TARURA ikiwezekana asilimia waliyoiweka waiongeze kwa sababu idadi kubwa ya barabara ambazo zinahudumiwa na halmashauri changamoto ya barabara bado ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nina barabara yangu ambayo haijafanyiwa ukarabati wa kutosha kwa takriban miaka miwili inayotoka Puma - Ihanja - Muintiri - Igeransoni. Halmashauri yangu ya Ikungi sehemu kubwa ya mapato inategemea kutoka katika hizi kata ambazo ziko mpakani wa Tabora ikiwemo Igaransoni. Kwa hiyo, naomba kaka yangu Mheshimiwa Jafo chonde chonde…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.