Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Omary Ahmad Badwel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara hizi mbili ambazo ziko mbele yetu. Kwanza naomba niwapongeze Mawaziri wote wawili kwa kazi nzuri pamoja na Naibu Mawaziri wao na wasaidizi wao mbalimbali ambao wamekuwa wakishirikiana nao katika kufanya kazi mbalimbali za maendeleo za nchi yetu kupitia Wizara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nichukue nafasi hii kuwapongeza watumishi ambao serikali baada ya kuwaondoa katika utumishi na baadaye imekubali kuwarudisha. Kwa kweli nawapongeza sana, lakini pia nawapa pole kwa madhira waliyoyapata katika kipindi kila cha miezi mitatu ambao hawakuwepo kazini. Kwa hiyo tunaipongeza sana Serikali kwa kusikia ushauri wa Wabunge na kuwarudisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri maamuzi magumu na yanayolenga maisha ya watu kama hivi wakati mwingine kwa kweli Serikali itafakari kwa kina kabla haijachukua maamuzi magumu kama haya. Pengine sisi Wabunge wakati mwingine isitoshe tu kuishauri Serikali kufanya maamuzi tofauti na waliyoyafanya awali, lakini pia wakati mwingine tuelekeze pia kuchukuliwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini viongozi waliohusika walishauriwa pia na watendaji ambao hawakuwashauri vizuri mpaka wakachukua maamuzi haya. Nao wawajibike wakati mwingine waone uchungu wa kutoka kazini na namna ambavyo walikuwa wakitegemewa na watu mbalimbali na dhoruba ambayo wanaipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, nashukuru mpango amaboa umeletwa na Wizara juu ya fedha za CDG kutumika katika miradi michache ambayo itaweza kukamilika kwa wakati na kuweza kutoa huduma tofauti na miradi ambayo tulikuwa tunafanya kidogo kidogo. Huo ni mpango mzuri na sisi Bahi tumeiga hata kwenye bajeti hii ambayo tumependekeza sasa kuwa na miradi michache lakini ambayo itaweza kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachokiomba Serikali izileta hzi fedha. Ukiangalia fedha hizi za CDG kwa mfano Wilaya ya Bahi tumepangiwa bilioni moja na milioni mia mbili, na sasa imebaki miezi mitatu muda wa mwaka kwisha, lakini hakuna hata senti tano ambayo imekuja. Kwa hiyo ni vizuri sasa hizo fedha zikaletwa, tukiwa bado tupo Bungeni hizi fedha tuzione zimekwenda kwenye Wilaya zianze kufanya kazi ambayo kwa kweli tulikuwa tumekusudia na kuipanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine tunakubali miradi mingine ya Kitaifa inakwenda. Ukiangalia kila mahali miradi ambayo inasimamiwa kitaifa inakwenda, lakini miradi ya halmashauri haiendi halmashauri hazina fedha. Tuna watumishi wengi kule mpaka unafika mahali nasema tunawalipa mishahara bure kwa sababu hakuna fedha ambazo wanaweza kuzisimamia kuleta maendeleo kwenye halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kweli imeweka watumishi wengi na ni wataalam na wana sifa mbalimbali na wakipewa fedha wanaweza kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo wakishirikiana na wananchi; basi fedha ziende pia kwenye halmashauri zetu. Isiwe baba tu sasa anaonekana Serikali Kuu anafanya kazi lakini halmashauri ambayo sasa inachukuliwa kama watoto hawafanyi kazi. Hata sisi wazazi tunakwenda kazini na watoto tunawapeleka shule, kwa hiyo pia wazazi na watoto wapewe haki sawa katika kuleta maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za bajeti katika maendeleo mbalimbali ukiacha hizi fedha za CDG nazo pia zinapashwa kwenda katika halmashauri zetu ili ziweze kufanya kazi ambayo imekusudiwa. Kuna miradi mingi ya wananchi ambayo wameifanya kule ya kujenga zahanati, nyumba za Walimu, madarasa na tuliwaaambia wajenge mpaka hatua fulani halafu Serikali itakwenda kuwasaidia. Tunasubiri fedha hizo wazipate ili waweze kufanya hiyo kaiz ya kumalizia majengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maboma haya yamekaa muda mrefu, mahali pengine hata sisi viongozi kama Wabunge tunaona hata aibu kwenda katika baadhi ya vijiji. Umewahaidi wananchi mwaka huu kwamba tutatenga fedha, tunatenga kweli halmashauri lakini fedha zile haziendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko mifano mimi kwangu kule Bahi kuna kujiji cha Mayamaya wamejenga zahanati mpaka wamefika hatua ya visusi huu mwaka wa tano. Kuna kijiji cha chonde wamejenga zahanati wamefika hatua ya visusi huu ni mwaka wa tano na Mbunge unakwenda kila mara unafanya mikutano unabaki na hadithi ile ile, mwaka huu tumewatengea fedha milioni arobaini, unakwenda mwakani tumewatengea fedha milioni arobaini. Mwisho wanatuona na sisi ni watu ambao tunawadanganya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Serikali ifanye tathimini, iwatake Wakurugenzi kufanya tathimini ya miradi yote ya wananchi ambayo imekwama kwa muda mrefu. Uandaliwe mpango kabambe wa kwenda kumalizia haya magofu, yatatuletea shida wakati tunakwenda kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa, lakini pia itatuletea shida kwenye uchaguzi tunaokwenda wa mwaka 2020. Ni vizuri Serikali ikachukua hatua madhubuti kama ambavyo inachukua ili kukamilisha hii miradi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Bahi imegawanywa miaka 10 iliyopita, lakini watumishi waliotoka hapa Dodoma wakati huo tunakaa hapa Dodoma kama Makao Makuu ya Wilaya ikiwa Dodoma Vijijini mpaka leo huu mwaka wa 10 wamehamia Bahi hawajalipwa mafao yao ya uhamisho. Kwa kweli ni kitu cha ajabu sana. Watu wanasubiri miaka 10, wako waliostaafu, wako waliokufa, wako waliohama kwenda wilaya nyingine, wako waliobaki pale Bahi mpaka leo hawajalipwa fedha zao za uhamisho, miaka 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na wakati wa kushika shilingi nitashika mshahara wa Mheshimiwa Waziri mpaka aniambaie ni lini atawalipa hawa watumishi wa Bahi milioni mia nane sabini wanazodai kwa kipindi cha miaka 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA. Tunaipongeza Serikali na sisi Wabunge wenyewe ndio tumetunga sheria ile ya TARURA hapa, lakini upo upungufu katika ufanyaji kazi wa TARURA. Ukiangalia katika mchango wa Waheshimiwa Wabunge hapa wako Waheshimiwa Wabunge ambao wameshukuru sana namna ambavyo unashirikiana vizuri na TARURA, lakini wako Waheshimiwa Wabunge wameonesha tu kasoro katika namna ambavyo TARURA inashirikiaa na halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahali pengine wako Mameneja wa TARURA wamejisifu wanasema sisi ni chombo pekee, sisi ni chombo maalum, lazima Mheshimiwa Waziri kauli hii waiondoe waelekeze kwamba wao ni wakala na mimi najua wakala yeyote anafanya kazi kwa niaba ya mtu fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hawa kama ni wakala ina maana wanafanya kazi kwa niaba ya halmashauri na ndio wenye barabara wanapashwa kuripoti, wanapashwa kushirikiana na Mkurugenzi, wanapashwa kuhudhuria vikao mbalimbali vya halmashauri ili Madiwani ambao ndio wenye hizo barabara, ndio wanatekeleza ilani, ndio waliowaahidi wananchi kutengeneza barabara nao waweze kutoa ushauri katika utengenezaji wa barabara na kusimamia katika utengenezaji wa barabara zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa mara ya kwanza kututengea fedha katika bajeti hii za hospitali ya wilaya, jambo hilo tunalishukuru sana. Hata hivyo, nashauri, kama ambavyo tumetumia force account kwenye miradi ya vituo vya afya ambavyo pia wametupatia pesa na tumeona ufanisi mkubwa katika kutumia force account kwenye ujengaji wa vituo vya afya. Hizi fedha Wizara ielekeze nazo pia zitumike kwa mtindo wa force account. Hizi bilioni moja na nusu zinaweza kufanya kazi kubwa na kama upungufu unaweza kuwa kidogo tu kabla ya kukamilisha hizi hospitali za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI wamekuwa wakitupangia watumishi na wamekuwa wakituletea watumishi, tunaomba waache kutupangia vituo, watuletee watumishi kwenye halmashauri, Mkurugenzi ndiye apange vituo vya hawa watumishi. Leo wanaleta Walimu 20 halafu wanawaandikia na majina ya shule wakati pengine shule ile wanayompelekea haina upungufu kama ambavyo shule ambayo hawakuitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vizuri katika maeneo ya watumishi Walimu, watumishi wa hospitali na watumishi wa kada zingine wamletee Mkurugenzi, wamwambieni hawa ni wataalam fulani, yeye atawapangia vituo vya kazi kulingana na yeye anavyoona wapi pana mahitaji muhimu, kuliko kutupangia moja kwa moja kutoka Wizarani. Kwa kweli wamekuwa hawatutendei haki na mara nyingine wanakwenda kurundika watumishi mahali ambapo tayari walikuwepo na shule ya pili au ya tatu inakuwa haina watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapongeza kwa kuondoa riba ya asilimia 10 kwa ajili ya mikopo ya akinamama na vijana, lakini wahakikishe inafika. Kuondoa riba tu peke yake bila fedha hizi kutengwa haiwezi kusaidia kwa sababu wako Wakurugenzi katika kutenga hizi fedha wanaamua wanavyotaka, akijisikia kutenga anatenga.