Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. SOPHIA. H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii. Kwanza kabisa nitazungumzia utawala bora kama wenzangu walivyosema. CAG mara nyingi alikuwa akitoa ripoti na ripoti zake nyingi sana zimeeleza ubadhirifu wa mali uliofanywa na Serikali ya CCM. Ninachotaka kushangaa kuna msemaji aliyepita amezungumzia habari ya Chama cha CHADEMA lakini nikaona huyu mwenzangu labda hajasoma kitabu chote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zetu wa Chama cha Mapinduzi wamechukua pesa za watu ambao walitakiwa walipwe pension kwa cheque number 156424 wakazitumia vibaya. Mpaka CAG anakagua hesabu mwezi wa Pili hizo pesa hazijarudishwa. Anazungumzia tujitoe boriti kwenye jicho letu, huwezi kuwa nyoka ukazaa mjusi. Ili uweze kuwa safi pia lazima uzae mtoto safi, makosa ni ya CCM, si ya CHADEMA.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia utawala bora wewe kama kweli ni chama tawala na uko vizuri na unafanya kazi sawasawa na ilani ya chama chako kwa nini unatumia nguvu ya kuzuia upinzani ambao tayari ulipita kihalali na uliusaini na ukakubalika? Huwezi kuwa mzazi, watoto wawili wanagombana mmoja umemshika mkono halafu unajiita wewe ni mshindi, hiyo siyo kweli. Tupewe uwanja sawa, twende viwanjani na sisi tukazungumze, tuone zile kule milioni sita feki mlizotupa kama hatujawapiga 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye Wizara sasa, maana na mimi nilikuwa najibu ndugu aliyezungumza. Soko la Kariakoo lilijengwa kwa makusudi ya kusaidia wakulima na kuuza vifaa na pembejeo kwa ajili ya wananchi. Najua ni miaka mingi imepita soko lile kuwa pale, lakini tuna Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inayozalisha mazao mengi; huu ni wakati sasa mngejenga masoko hayo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri, Mkoa wa Mbeya ni mkoa ambao uko katikati, una mazao mengi sana, tunashauri mtupatie masoko ya kimataifa yanayoweza kusaidia wanawake ambao wanalima kwa nguvu zao zote waweze kupata masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejiunga na Afrika Mashariki lakini cha kushangaza wenzetu wa Kenya, Waganda wanakuja hadi vijijini kununua maparachichi bila utaratibu unaokubalika. Tukiwa na masoko haya tunaweza tukafanya kazi nzuri na tukasaidia uchumi wa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nazungumzia habari ya masoko hayo hayo. Leo hii Mheshimiwa Jafo, Tunduma wamefunga masoko; sijaelewa wanaposema ninyi mnatetea wanyonge, mmepoteza hela ngapi kwa siku ya leo kufunga soko la Tunduma? Sijajua ni kwa nini tunawaachia Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa waamue mambo bila kutumia utaratibu na professionalism?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mheshimiwa Waziri kama kiongozi wa Wizara hiyo, tunaomba Soko la Tunduma lifunguliwe. Tunadaiwa madeni mengi, kwa sababu mwishowe wafanyabiashara wamesema wanatupeleka mahakamani; ni nani atalipa pesa hizo? Halmashauri hii wameifungia Madiwani, kazi haziendi kisa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya. Hapa ndipo ninapoushangaa huu utawala bora Mzee Mkuchika. Naomba ninyi wazee ambao bado mpo na mpo kwenye system shaurini Serikali ifanye kazi sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija upande wa mikopo, ilitengwa bilioni sitini na moja kwa ajili ya wanawake na vijana, lakini bilioni kumi na tano ndizo zilizotumika. Idadi ya wanawake ni wengi lakini pesa zilizotoka ni kidogo. Tunaomba waachilie vyanzo vya mapato kwenye halmashauri ili tuweze kukusanya pesa nyingi na kusaidia wanawake na vjiana kwa ajili ya ahadi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo ugawaji wa mikopo hii unakwenda kiitikadi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)