Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Catherine Nyakao Ruge

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuchangia kuhusu Jeshi la Polisi. Zamani wananchi waliamini Polisi ni sehemu salama lakini Awamu hii ya Tano mambo yamebadilika, Polisi siyo sehemu salama tena maana matukio mengi ya vifo yametokea mikononi mwa Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kuna kijana anaitwa Allen aliuawa akiwa mikononi mwa Polisi Mjini Mbeya. Pia hivi karibuni mdogo wake Mbunge wa Tarime Vijijini, Mheshimiwa John Heche pia amechomwa kisu akiwa mikononi mwa Polisi, tena akiwa amefungwa pingu. Matukio haya yanalidhalilisha Jeshi la Polisi kwa kukosa weledi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuzungumzia ukimya wa Jeshi la Polisi kuhusu matukio mbalimbali ambayo yametokea katika nchi yetu. Mfano, Mheshimiwa Nape Nnauye alitishiwa bastola mchana kweupe; Mheshimiwa Lissu alimiminiwa risasi 38 mchana kweupe Mjini Dodoma, kifo cha mwanafunzi wa NIT ambaye alipigwa risasi wakati wa kampeni za uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni, mauaji ya Kibiti, kupatikana kwa maiti katika fukwe za Coco Beach, lakini mpaka leo hakuna taarifa yoyote kuhusu matukio haya. Namwomba Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha hoja yake atolee ufafanuzi suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuzungumzia suala la Askari Polisi kuwashikilia watumishi zaidi ya saa 48 bila kuwapeleka Mahakamani. Ni kwa nini Jeshi la Polisi linafanya hivi? Namwomba Mheshimiwa Mwigulu akija atueleze ni sheria gani ambayo inaruhusu Jeshi la Polisi kuwa- detain watuhumiwa zaidi ya saa 48 bila kuwapeleka Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.