Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Ruth Hiyob Mollel

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inapita katika kipindi kigumu sana kwa ongezeko la uhalifu hasa dhidi ya haki za binadamu. Yamekuwepo matukio mengi ya watu kutekwa, kupotezwa, kuuwawa na miili yao kuopolewa kutoka baharini na kwenye mito. Taharuki ni kubwa kwamba watu hawa wasiojulikana hawatambuliwi wala kukamatwa na vyombo vyetu vya usalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya matukio makubwa ni kama la Mheshimiwa Lissu kumiminiwa risasi hadi leo hakuna hata mtuhumiwa mmoja aliyekamatwa. Kibaya zaidi matukio haya yote yanayowapata wananchi hakuna hata siku moja mkuu wa nchi au Waziri wa Mambo ya Ndani amejitokeza na kuzungumza na wananchi kuhusu matatizo hayo na kuwapa a sense of comfort kuhusu usalama wao na mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda muafaka sasa kwa kiongozi wa juu kuzungumza na wananchi kuhusu usalama wa nchi. Ili haki ionekane kutendeka wananchi wapate taarifa mara kwa mara kuhusu kukamatwa kwa watu hao wasiojulikana wanaoharibu taswira ya Jeshi la Polisi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na mhimili wa Mahakama wawaachie wafungwa, mahabusu wanaotuhumiwa kwa makosa madogo madogo yanayodhaminika watumikie kifungo cha nje. Kwa kufanya hivyo itasaidia kupunguza msongamano mkubwa kwenye magereza na kupunguza gharama na kuepuka magonjwa ya maambukizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto liwezeshwe kwa kupatiwa rasilimali ya kutosha kama watumishi na zana za kazi ili kuwawezesha kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye Wizara, taasisi, majengo ya biashara na huduma kudhibiti majanga ya moto ambayo siku hizi yamekuwa yanatokea mara kwa mara. Kinga ni bora kuliko tiba, kuzuia majanga ya moto ni jambo muhimu sana kama hatua ya kulinda usalama wa wananchi na mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.