Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuongelea kuhusu Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Majukumu ya jeshi hili ni kupambana na majanga ya moto pamoja na kufanya uokoaji pale inapotokea majanga. Jeshi hili umuhimu wake unaonekana zaidi pale panapotokea majanga, hata hivyo umuhimu wake haupewi uzito kutokana na kutopewa fedha za kutosha na vitendea kazi ili waweze kufanikisha majukumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ihakikishe inalisaidia au inalipatia Jeshi la Zimamoto na Ukoaji fedha za kutosha na vitendea kazi vya kisasa ili utekelezaji wa majukumu uwe na ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, vituo vya polisi nchini. Vituo vya polisi nchini vingi vina uchakavu wa kutisha. Vituo hivi vimekuwa vikihifadhi wahalifu pamoja na uchakavu huo jambo ambalo ni hatarishi kwa usalama. Umuhimu wa kukarabati vituo hivi ni jambo ambalo haliepukiki. Jeshi lipange kimkakati wa ukarabati wa vituo hivi kwa awamu ili kuwa na vitu bora na vinavyokidhi haja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Jeshi la Magereza. Jeshi hili lina jukumu la kuwahifadhi wafungwa na kutazama mahitaji yao kwa ujumla, lakini majukumu haya hayatekelezwi ipasavyo kwa ufinyu wa bajeti na vitendea kazi ili kufanikisha majukumu yake. Msongamano ni mkubwa katika magereza yetu, magari ya kupeleka wafungwa mahakamani ni machache na mabovu sana. Nashauri Serikali itenge fedha za kutosha ili kukabiliana na upungufu mkubwa uliopo katika hili Jeshi la Magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, vitambulisho vya uraia. Vitambulisho vya uraia ni haki ya kila Mtanzania kwa kuwa ndicho kinachomtambulisha. Zoezi hili licha ya kushushwa kwenye wilaya zetu limekuwa la kusuasua na kuleta usumbufu na urasimu usiokuwa na ulazima. Wananchi wametakiwa kuchangia fedha ili kupata vitambulisho hivyo. Kwa nini Serikali inachangisha wananchi wakati ni haki ya wananchi kupatiwa vitambulisho. Serikali inawajibika kuwapatia vitambulisho bila vikwazo kwa kuwa Serikali inakusanya kodi ambazo zinapaswa kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha.