Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mambo yafuatayo yazingatiwe hasa katika Mkoa wa Kigoma na Jimbo la Kasulu Mjini.:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umaliziaji wa nyumba za Polisi Kasulu Mjini zipo Blocks nne zinazohitajika kukamilishwa ujenzi wake. Nyumba hizi zina uwezo wa kuishi zaidi ya familia 20 za Askari Polisi. Tafadhali kamilisheni nyumba hizo kwani ni muhimu sana kwa utendaji kazi wa Jeshi la Polisi. Barua ya mchanganuo nimeiwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani kwa hatua zaidi tangu mwaka 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo umuhimu wa kuongeza idadi ya Askari katika Wilaya ya Kasulu ambayo ni kubwa na ina changamoto nyingi sana, pamoja na kuwa na Kambi kubwa ya Wakimbizi ya Nyarungusa. Wilaya inastahili kupewa kipaumbele cha Askari na vitendea kazi vingine kama magari ya doria na motisha kwa Askari hawa. Wilaya ya Kasulu ni tofauti kabisa na Wilaya nyingine kwa sababu zake za kijiografia na idadi kubwa ya watu. Kasulu pekee ina idadi ya wakazi zaidi ya 800,000 hadi milioni moja sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma ni Mkoa uliopo mpakani na nchi jirani za DRC, Burundi na Zambia kwa upande wa Kusini. Watu tumeingiliwa sana tangu miaka ya uhuru 1961, wakati idara ya uhamiaji wanafanya doria zao za kusaka wahamiaji haramu, wakimbizi wa wageni wakazi. Naomba sana yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Idara itumie weledi zaidi kuliko hisia, watu watambuliwe kwa hoja na siyo kwa sura zao au lugha zao za asili; Idara itumie viongozi wa Serikali waliopo katika maeneo na kamwe Maafisa hawa wasivamie watu barabarani, sokoni na kwenye nyumba za starehe; Wageni wakazi na wahamiaji haramu wanaweza kufichuliwa na viongozi wa Serikali za Mitaa katika sehemu zao;

Vizuizi barabarani siku za masoko na gulio siku ya minada kamwe zisitumike kunyanyasa raia halali wa Taifa hili kwa sababu tu wanaishi mpakani mwa nchi yetu;

Vitendo vya rushwa, uonevu na unyanyasaji kamwe visipewe nafasi katika misako ya Idara hii ya Uhamiaji;

Makamanda wa Wilaya na Vituo wawasimamie vijana wao kutenda haki na kwa mujibu wa sheria zetu; na Pia Idara ya Uhamiaji Kasulu wapewe vifaa vya kazi, mfano magari na vitendea kazi vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza linafanya kazi njema sana katika mazingira magumu. Jeshi hili kule Kasulu wapewe vitendea kazi ikiwemo nyumba za kuishi. Pia Wizara iboreshe makazi ya Askari wa Jeshi hili ili ubora wa Jeshi hili uonekane dhahiri mbele ya Jamii. Jengo la Magereza Wilaya ya Kasulu ni jengo la siku nyingi sana tangu Wakoloni wa Kijerumani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo hili lipo katika Mji wa Kasulu. Nashauri strongly Magereza haya yahamishiwe nje ya Mji wa Kasulu. Maeneo yapo mengi; maeneo ya Tarafa ya Makele yanafaa sana kujenga gereza la kisasa. Magereza ya sasa yaliyopo yanaweza kuendelea kutumika kwa ajili ya mahabusu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii.