Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza kabisa napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia kwa kutujalia uhai mpaka leo tumeweza kuwa humu ndani ya Bunge tunachangia Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia napenda kuwaambia Watanzania wote kwamba tuilinde amani tuliyonayo na tuilinde kwa bidii kwa sababu amani ikipotea haina cha Mkristu, Mpagani, Muislam wala mtu wa aina yoyote, wote tutazama kwenye hiyo bahari. Amani ikipotea ina maana Watanzania wote tutazama kwenye hiyo bahari. Naomba Watanzania wasisikilize maneno, waendelee kuilinda amani tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa kuchangia mjadala ulio mbele yetu. Napenda kumpongeza kwanza Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya. Napenda vile vile kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote kwa nafasi zao tofauti na Wizara zao tofauti kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Mwigulu na Naibu wake Mheshimiwa Masauni kwa kazi nzuri wanayoifanya. Napenda pia kupongeza Jeshi la Polisi kwa kulinda raia na mali zao au zetu kwa ujumla. Napenda vile vile kulipongeza Jeshi la Magereza kwa kuwalea wafungwa Magerezani na kuwafundisha tabia njema wanapotoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kulinda mipaka yetu ya Tanzania na kulinda wahamiaji wanaoingia ndani ya nchi yetu. Pia napenda kupongeza Jeshi la Zimamoto kwa kusaidia maafa ya moto yanapotokea nchini mwetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niende moja kwa moja kwenye kuchambua hoja moja moja za Idara hii. Nianze na Idara ya Uhamiaji. Naomba Idara ya Uhamiaji ifanye kazi kwa weledi. Ihakikishe nchi yetu ya Tanzania haiingiliwi na wahamiaji haramu, iwadhibiti wahamiaji haramu wote waaoingia ndani ya nchi hii. Ihakikishe nchi yetu ya Tanzania siyo kisiwa cha kupokea maharamia na Alkaida wanaotoka nchi nyingine. Ihakikishe nchi yetu ya Tanzania siyo kisiwa cha kupokea dawa za kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo, Idara ya Uhamiaji wafanye kazi kwa weledi kwa kuangalia mipaka yote na nawaomba wasifanye kazi kwa computer, waende field. Wasifanye kazi kwa kuingia ofisini na kucheki computer unaona kwamba kuna usalama. Waende field wakakague mipaka yetu. Wachukue ramani ya Tanzania na waangalie mipaka ya Tanzania yote imekaaje? Waitembelee kwa kuiona visible siyo kwa kukaa kuiangalia kwenye computer.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mkurugenzi wa Uhamiaji kwa sababu ni mama tumeona mabadiliko anayoyafanya, atendee haki kiti chake; atembelee mipaka ya nchi yake ya Tanzania aijue, asifanye kazi kwa computer pamoja na timu yake yote ili nchi yetu iweze kuendelea kuwa na amani hii Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, haiingii akilini; juzi juzi hapa kuna wananchi walishikwa pale Dar es Salaam wako kwenye nyumba, ina maana hawa Immigration na Polisi kulikuwa na uzembe fulani ndiyo maana hawa watu waliweza kupenyeza mpaka kuwa kwenye nyumba ya mtu, walishikwa wakiwa wanagombania chakula, ndiyo maana wakafahamika kwamba wako pale, ina maana hapa Jeshi la Polisi na Uhamiaji halikufanya kazi yake vizuri. Kwa hiyo, haiingii akilini kuona wahamiaji haramu wanashikwa Dar es Salaam. Wamepitaje Tanga, wamepitaje Moshi mpaka wanakwenda kufika Dar es Salaam? Naomba warekebishe hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nichangie suala la Polisi. Polisi wanafanya kazi yao vizuri, lakini naomba wajirekebishe wawe rafiki na raia. Naomba nichangie hasa upande wa traffic. Traffic wamekuwa wakiwa-harass sana hawa vijana wa bodaboda kiasi kwamba wanawakimbia mpaka wanaenda sehemu nyingine na kuweza kusababisha ajali. Vijana wale wanatafuta maisha, kwa hiyo, wanahitaji tu kupewa semina ili waweze kufanya kazi zao vizuri za bodaboda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kuhusu traffic, unaposhika gari njiani, mimi mwenyewe nimewahi kukamatwa, tumelipa fine ya Sh.30,000/= lakini hatukupewa receipt, tumepewa notification. Sasa tunajuaje hiyo hela kama imefika Wizara ya Mambo ya Ndani? Naomba Mheshimiwa Mwigulu wale traffic ambao wanakamata magari njiani, wapewe mashine wanapokamata magari watoe receipt. Wasitoe ile karatasi ya notification. Notification siyo receipt. Unapodai receipt wanakwambia kwamba receipts utaipata mbele ya safari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikamatwa hapa kutoka Chemba tukaambiwa tutakuta receipt Chemba, tumefika pale Chemba wala gari la Polisi lilikuwa halipo. Kama vitendea kazi hamna, naomba Mheshimiwa Mwigulu hawa traffic wasikamate magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.