Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Khamis Mtumwa Ali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiwengwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. KHAMIS MTUMWA ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuzungumza. Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kwanza kumshukuru kwanza Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na ardhi, kwa kutuwezesha kuwa wazima wa afya na kuweza kusimama katika Bunge lako hili Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri ambayo anafanya ya kutuletea maendeleo katika Taifa letu na kusimamia amani ya nchi yetu hii. Kwa kweli Mheshimiwa Rais anastahiki pongezi sana tena sana kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya za kuweza kuhakikisha Taifa letu hili linasimama kwa amani na Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake ipasavyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri na IGP na Makamishna wote, hongera sana kwa kazi ambayo wanaifanya ya kuhakikisha kwamba Taifa letu linakuwa na amani sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia sasa kuhusiana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani katika kipengele cha hali ya usalama nchini. Katika taarifa yake ukurasa wa tano, Mheshimiwa Waziri amesema matukio ya uhalifu yamepungua na kutoka mwaka 2017 kutoka matukio ya 56,913 yamepungua hadi kufikia matukio 47236 mwaka 2018. Hongera sana kazi nzuri ambayo wanaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kushauri zaidi kwamba ili matukio haya yapungue zaidi ni vyema sasa Mheshimiwa Waziri Wizara yake ikaendelea kuimarisha vifaa vya utendaji kazi katika Jeshi la Polisi na hasa kwenye kipengele cha mafuta ili kuhakikisha maeneo yote ambayo yanatokea matukio mbalimbali, Jeshi letu la askari la Polisi liweze kufika vizuri na kuweza kufanya kazi katika maeneo hayo ili kupunguza haya matukio yetu ya uhalifu ambayo yanaendelea kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kuchangia kuhusiana na suala la basic training za polisi. Hawa kuruta wanapofanya mazoezi wakati wapo katika training zao wanakimbia kwa kutumia viatu vya kiraia pamoja na tracksuit hizi za kiraia. Sasa unapofika wakati wa field yenyewe utamkuta askari amevaa lile bullet proof ambalo halipungui kilogramu 10 au amechukua mashine ya SMG isiyopungua kilogramu saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vyema hawa askari wakaweza ku-cope na haya mafunzo ambayo wanayapata. Kwenye mafunzo hawachukui hivi vifaa lakini kwenye field utakuta wanabeba hivi vifaa na utawakuta wamevaa mabuti na helment karibu masaa yote ya kazi wanatakiwa vifaa vile wawe navyo. Kwa kweli ili kuwajengea mazingira mazuri ya kuweza kupambana zaidi na kuweza kuzoea vile vifaa ambayo wanavitumia ni vyema wakati wa training vilevile waweze kupata hivyo vifaa ili waweze kufanya mazoezi vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naomba nichangia kuhusiana na suala la ujenzi wa nyumba za askari na vituo vya polisi. Mwaka jana tumemwambia Mheshimiwa Waziri kwamba hizi nyumba za askari hasa katika iji letu hili la Dodoma zimakaa kama incubator ambapo ukapeleka mayai yako pale baada ya muda utapata vifaranga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni aibu kweli kwa sababu askari wetu wanafanya kazi nzuri, lakini wanapoenda kulala siku za joto inakuwa balaa, siku za baridi inakuwa balaa, maana yake juu kuna bati, pembeni kuna bati na chini kuna bati. Sasa kama mtu ana mke ana watoto sijui wanaishi katika mazingira gani katika nyumba zile ni vyema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vema nyumba hizi tukazifanyia ukarabati zikaendana na hadhi ya Jiji la Dodoma. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kutenga zile bilioni 10 za kuhakikisha kwamba askari waweze kuishi vizuri na ningewaomba sana hizi nyumba 400 kila mkoa ambazo zimewekwa humu katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri ziweze kuonekana kwa vitendo. Kwa sababu mwaka huu umetuambia nyumba 400 kila mkoa ningeomba sana mwakani nyumba tusije tukazizungumza tena hasa katika hili Jiji la Dodoma askari wetu kukaa kwenye nyumba za incubator za kuzalishia vifaranga vya kuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, kuna suala la huduma za maji na umeme. Mwaka jana nilimshauri sana Mheshimiwa Waziri, hizi huduma ni bora wangekopi katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JW) wanafanyaje na wao wakachukua hizi wakafanya, kwa sababu huduma za maji na huduma za umeme kwa kweli ni gharama kwa askari mwenyewe kulipa. Imefika mahali miaka iliyopita wanafika askari wanastaafu wanakopesha pesa zao mfukoni kulipia huduma za maji na umeme katika vituo vya polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri askari wetu hawa pesa ambayo wanapata ni ndogo sana halafu pesa hiyo hiyo takribani huduma ya maji Mheshimiwa Waziri anaijua, haipungui shilingi 50,000 au 60,000 kwa mwezi na huduma ya umeme karibu 50,000 au 60,000. Ukiangalia mishahara yao ni midogo, kidogo linakuwa ni suala gumu zaidi kwa askari wetu hao. Naomba sana Mheshimiwa Waziri suala hili akalichukua akalifanyia kazi endapo mwakani akija atuambie kwamba amefanya kama JW wanavyofanya kuhusu suala la maji na suala la umeme kwenye huduma hizi za malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala pia la uniform, askari wetu wananunua wenyewe, ni nadra sana kupewa viatu bure kama ulivyokuwa unavaa wewe, ni nadra sana kupewa hizi uniform bure kama ambavyo wanavyopata kwa mgao ambao wanapopewa mara nyingi wanakuwa wanatumia pesa zao za mshahara sasa kujinunulia hivi vifaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amezungumza vizuri tu kwenye hotuba yake, kuna viwanda ambavyo vinatengeneza viatu na kuna viwanda ambavyo vinatengeneza nguo. Naomba sana Mheshimiwa Waziri hili alibebe ili sasa migao itakapotoka itoke kwa wakati na nguo hizi na vifaa wasiwe wananunua wenyewe waweze kununuliwa na jeshi letu la polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mishahara na posho za askari nalo hili imekuwa ni shida sana, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri aziangalie kama alivyosema kwenye maelezo yake wakati anahutubia hapa, kwamba yale masuala madogo madogo amezungumza nao. Mwakani naamini yale masuala madogomadogo hatosema amezungumza nao atakuja hapa atatuambia masuala madogo madogo tulishamalizana nao ili na wao waweze kufanya kazi vizuri kama Jeshi letu la Polisi ambao wanatulinda sisi tunalala kwa amani, wao wanapata shida, lakini mishahara yao bado na hali zao za mambo madogo madogo ambayo yapo zinakuwa vilevile zipo katika hali ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri suala hili alichukue serious kweli kwa sababu wenzetu hawa wanafanya kazi kubwa sana ya kulinda amani ya nchi yetu lakini posho zao na maslahi yao yanakuwa na shida. Hata wenzangu wamezungumza kuhusiana na suala la askari anapandishwa cheo anakaa miaka chungu mzima hapati matunda ya kile cheo ambacho anakipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri na namwelewa utendaji wake mzuri na Mheshimiwa Naibu Waziri watalizingatia hili, tuone sasa haya madeni ambayo askari anadaiwa yakamilike na hayo mambo mengine mazuri yapatikane vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala pia katika Kitengo cha Upelelezi, Mheshimiwa Waziri upelelezi hauwezi ukafanyika bila fedha, lazima zipatikane fedha, hawa askari wetu waweze kufanya upelelezi vizuri, vinginevyo kitengo hiki kitakufa kabisa. Information is money, huwezi ukaenda kwa mtu ukamwambia akupe taarifa au uka-collect information bila kuwa na fedha, lazima uwe na pesa kidogo umpatie maji ya kunywa kidogo, umpatie mtu kidogo vitu fulani ili aweze na yeye kumtengeneza ili akupe information Mheshimiwa Naibu Waziri anajua sana kazi hizi wameshazifanya sana wanazielewa. Kwa hiyo, nawauomba sana Kitengo hiki cha Upelelezi ili kiweze kufanya kazi vizuriā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.